Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jeremiah Mrimi Amsabi (35 total)

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Kwa kuwa, tatizo la maji katika Jimbo la Serengeti ni sawa kabisa na tatizo la maji kule Namtumbo. Naipongeza sana Wizara, rafiki yangu Mheshimiwa Jumaa amejitahidi sana kuhakikisha mradi wetu wa maji hasa ule wa chujio unakamilika hata hivyo mpaka sasa hivi mradi ule bado haujakamilika, lakini pia kupeleka maji katika vijiji vya Jirani. Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi yote hii miwili?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri wangu kwa namna bora na nzuri ya kujibu maswali. Kweli nimeamini mtoto wa samaki hafundishwi kuogelea, hongera sana Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa ambalo nataka niliseme ni kwamba Wizara ya Maji tumepokea miradi 177 ambayo ni kichefuchefu na ilikuwa ikichafua Wizara. Mkakati wa Wizara baada ya kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), tukasema miradi hii yote kichefuchefu ikiwemo mradi wa Mugumu ambao ulikuwa ukichafua, sasa hivi tunaukwamua. Katika wiki hii tunatoa fedha zaidi ya milioni 300 kuhakikisha tunakamilisha mradi ule na wananchi wa Mugumu waweze kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Takwimu mbalimbali za wataalam zimeonesha kama Uwanja wa Ndege wa Serengeti ukiboreshwa utakuwa uwanja pekee katika Kanda ya Ziwa utakaoleta tija kubwa kiuchumi, kiuhifadhi na kijamii kwa wananchi wa Serengeti na Tanzania kwa ujumla. Kwa kuwa mpaka sasa tayari wadau mbalimbali na wananchi wamekwishachangia ujenzi wa uwanja huu. Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa uwanja huu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli Uwanja wa Serengeti ni muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi ya nchi lakini pia katika eneo la Serengeti na Mkoa wa Mara kwa ujumla. Pia naomba nitambue kwamba ni kweli wananchi na Mheshimiwa Mbunge amejiunga, wametengeneza group la WhatsApp, wanachangisha fedha na Mheshimiwa Mbunge leo ameomba appointment watu wakija awapokee tuzungumze.

Mheshimiwa Spika, naomba nimwelekeze Mkurugenzi wa Viwanja vya Ndege atume watalaam wetu katika eneo hili ili juhudi nzuri za wananchi zisipotee, atuongezee utalaam wa Wizara yetu kazi hii ifanyike na uwanja ujengwe ili watalii wasizunguke Zaidi, washuke pale karibu na tutape huduma na fedha iongezeke.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Kufuatia mvua nyingi ambazo zimenyesha katika Jimbo la Serengeti, barabara nyingi zilizo chini ya TARURA sasa zimeharibika sana ikiwemo barabara ya kwenda Iselesele, barabara ya kwenda Mosongo lakini pia barabara ya kuzunguka stendi ile. Pia barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kuzunguka soko la Mji wa Mugumu nayo haijajengwa muda mrefu:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hizi na zile za kufanyiwa marekebisho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Jeremiah Amsabi Mrimi, ameainisha barabara kadhaa ambazo zinahitajika zitengenezwe; na kwa kuwa nafahamu changamoto za barabara kama ambavyo Wabunge wamekuwa waki- debate humu ndani ya Bunge; niseme tu, jambo hilo tumelipokea na sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika ule mchakato wetu wa pamoja, tunaandaa plan ambayo itahakikisha barabara zote nchini tunazipitia, tunafanya tathmini ya kutosha na kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha hizo barabara zinatengenezwa.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, awaambie tu wananchi wa Serengeti wakae mkao wa kula, hizi barabara tutazifanyia kazi na kazi yake mtaiona kabla ya miaka hii mitano kwisha.Ahsante. (Makofi)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu ambayo yametolewa na Serikali. Pengine niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ningemwomba Waziri wa Maliasili na Utalii akaambatana nami na kutembelea wananchi wa Jimbo la Serengeti kuona ni namna gani tatizo hili ni kubwa na mikakati iliyowekwa, je inaweza kweli kutekelezeka na kumaliza tatizo? Kwa sababu hivi ninavyozungumza kila mara tunapata ripoti za tembo, simba kuvamia wananchi. Pamoja na majibu haya yanayotolewa lakini bado hatuoni tatizo hili likiisha. Kwa hiyo niombe, kwa maana ya kwamba kwa majibu haya Waziri afike na yeye aona kama kweli haya yanaweza yakatosheleza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ukitoka katika eneo la mpaka wa hifadhi katika vijiji vingi unaingia kijijini moja kwa moja, hili ni tatizo kubwa sana. Serikali iliwahi kutoa mpango kwamba kutaongezwa buffer zone ambayo ni nusu kilomita kuingia ndani ya hifadhi, lakini mpaka leo bado hawajatekeleza. Sasa je, ni lini Serikali itatekeleza uamuzi huu wa kuongeza buffer zone kuingia ndani ya hifadhi ambayo ni moja ya jambo linaloweza likasaidia sana kupunguza mwingiliano huu wa wanyama na makazi ya watu?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Maliasili na Utalii na Naibu Waziri wake wako tayari kutembelea eneo hilo la Serengeti kama Mheshimiwa Mbunge alivyotaka. Na kwa sababu wako tayari kutembelea eneo hilo. Hata yale majibu yanayohusu buffer zone ambayo iliahidiwa napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba yatatolewa majibu wakati wa ziara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni sote tumeona jitihada kubwa sana za Rais Samia za kuvutia watalii katika nchi yetu, lakini pia sasa hivi tayari Mkuu wa Mkoa wa Mara Mheshimiwa Ally Hapi, pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii walianza jitihada za pamoja, wameanza vikao vya kuona namna ya kujenga uwanja ule. Hii ni kuzingatia pia kwamba kuna ushindani mkubwa kwa wenzetu, watu wa Masai Mara kule Kenya ambao wana-share ikolojia moja na Serengeti.

Mheshimiwa Spika, sasa namwomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri nipate nafasi ya kukutana naye kwa mazungumzo maalumu kuona ni namna gani tutapata mwelekeo wa pamoja wa kuweza kujenga uwanja huu kwa viwango vikubwa kabisa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara hii ya Sanzate mpaka Natta, na ile ya Tarime – Mugumu – Natta, barabara hizi hazi-connect Makao Makuu ya Wilaya ya Serengeti pale Mugumu. Mwaka wa jana, 2020 aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano alitupa ahadi ya ujenzi wa kilometa 30. Kwa hiyo, namwomba sana…

SPIKA: Unasema Tarime – Mugumu – Natta, haifiki Mugumu tena!

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, Tarime – Mugumu – Natta halafu kuna ile ya Makutano na Sanzate – Natta. Sasa zote hizi kwa jinsi ya ule mpango wa ujenzi, zitachukua muda mrefu kuja kuunganisha Makao Makuu ya Wilaya. Kwa hiyo, tukawa tumemwomba aliyekuwa Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwamba kipande cha Natta – Mugumu kiweze kupewa fedha kijengwe haraka ili barabara ile ya Makutano – Sanzate – Natta sasa itoke pale Natta mpaka Mugumu. Halafu na ile inayotoka kule Tarime – Nyamwaga – Mugumu iweze kuungana nayo mapema zaidi.

Mheshimiwa Spika, sasa ni lini Wizara inaweza kutekeleza mpango huu na ile ahadi ya Rais? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Amsabi Jeremiah, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ameomba tufanye mazungumzo namna bora ya kupata fedha ya kujenga uwanja wa ndege wa Serengeti.

Mheshimiwa Spika, naomba tu nitumie nafasi hii kusema kwamba kwa sasa pia Mheshimiwa Rais ameshatoa fedha za kutosha za kuanzia ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma na mkandarasi ameshapatikana, yupo site anafanya kazi, lengo ni kuboresha huduma katika Hifadhi ya Serengeti.

Mheshimiwa Spika, tangu anazungumza Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, walifanya kazi nzuri sana pamoja na Wizara ya Maliasili ya kufanya mjadala. Sisi tunaona kwamba uwanja ambao walipendekeza kujenga ni uwanja ambao unamilikiwa na TANAPA na Halmashauri, ambao ni uwanja mdogo. Sisi tunataka tujenge uwanja mkubwa wa Kimataifa ili tushindane na wenzetu wa Kenya ambao wanajenga kule Masai Mara uwanja mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumewaelekeza watu wa Maliasili Uongozi wa Mkoa wa Mara watuletee andiko maalumu, tukae pamoja na Wizara ya Ujenzi, tujenge Uwanja wa Ndege wa Kimataifa ili tusigawane watalii wanaotaka kupata huduma katika mbuga yetu ya Serengeti. (Makofi)

SPIKA: Huo uwanja mnataka kujenga wapi?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, tunafikiria kujenga uwanja wa ndege Serengeti pale Mugumu, wanalo eneo pale la kutosha.

SPIKA: Haya endelea.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, sawa, ahsante.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kweli kwamba barabara ya Sanzatte inajengwa na ameleta ombi la kilometa 30, tumepokea ombi hilo na linafanyiwa kazi. Wakati huo huo, kilometa 25 zinajengwa kutoka eneo la Tarime kwenda Serengeti ili wananchi wa eneo hilo waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Spika, mawazo yote ni mazuri, lakini kupanga ni kuchagua. Kadri tunavyopata fedha za kutosha, barabara hizo zitakamilika kwa wakati ili huduma iweze kupatikana katika eneo la Serengeti. Ahsante. (Kicheko)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne pamoja na Rais wa Awamu ya Tano ya ukamilishaji wa ujenzi wa lami kipande cha Mnata -Mugumu mpaka Arusha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara ya Nata – Mugumu kwenda Arusha ni barabara ambayo inaanzia Makutano- Sanzate – Nata – Mugumu na kuelekea Arusha.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba hadi tunavyoongea mkandarasi yupo site kujenga kilometa 40 kuanzia Sanzate kwenda Nata na baada ya Nata tunafuata Nata kwenda Mugumu. Kwa hiyo, Serikali ina mpango wa kuhakikisha kwamba barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami kadri fedha itakavyoendelea kupatikana. Ahsante. (Makofi)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Pamoja na hayo niombe kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; katika bilioni 2.36 ambazo zilipelekwa Hospitali ya Wilaya, zilichukuliwa milioni 400 ambazo zilikuwa kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Iramba katika Jimbo langu la Serengeti na hali ya afya kule ni mbaya, ni kituo cha muda mrefu kimechakaa na kinahudumia watu wengi. Je, ni lini Serikali itapeleka tena hizo fedha milioni 400?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, hospitali ya Nyerere DDH inahudumia zaidi ya wakazi 100,000 katika Jimbo langu na idadi ya watumishi Saba iliyopelekwa bado kuna upungufu wa Madaktari 22, Wauguzi Wasaidizi 28 na Wauguzi wa kawaida 37.

Je, ni lini Serikali itatusaidia kuhakikisha tuna Madaktari wa kutosha na Wauguzi wengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Jimbo la Serengeti kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilipeleka Shilingi Bilioni 2.36 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Serengeti, kati ya fedha hizo, Shilingi Milioni 400 ilipelekwa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Iramba. Sasa kwa sababu Halmashauri walitumia fedha ile kujenga majengo ya hospitali ya Wilaya, kwanza naomba nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Serengeti kuhakikisha wanazingatia maelekezo ya Serikali. Fedha inapopelekwa kwa ajili ya kujenga vituo vya afya ijenge vituo vya afya kama ni zahanati ijenge zahanati, kama ni hospitali ijenge hospitali badala ya kuhamisha matumizi bila kibali maalum.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natoa maelekezo katika mapato yao ndani watenge kwa awamu Shilingi Milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Iramba.

Mheshimiwa Spika, kuhusina na Hospitali ya Nyerere DDH, ni kweli kwamba ina upungufu wa watumishi lakini Serikali imeendelea kupeleka watumishi, katika mwaka huu wafedha imetengewa ajira Saba kwa ajili ya kuonesha kwamba tunaendelea kupunguza upungufu wa watumishi katika hospitali hiyo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, awali ya yote ninaishukuru sana Serikali na kipekee kabisa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa VETA Wilayani Serengeti.

Mheshimiwa Spika, watu wa Serengeti wamekuwa na uhitaji wa chuo hiki kwa muda mrefu sana jambo ambalo lilipelekea kumfuata mara kwa mara Waziri, Naibu Waziri kuwataka kutusaidia kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki.

Sasa niiombe Serikali itoe kauli ya ni lini chuo hiki wataanza ujenzi wake pamoja na maandalizi yote yanayoendelea, lakini tunataka kujua ni lini ujenzi utaanza? Hilo ni swalila kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na changamoto za kijiografia pamoja na mahitaji maalumu ya Serengeti, niliiandikia Wizara proposal ndogo ya kuboresha kile chuo ambacho watajenga Serengeti.

Sasa je, Waziri au Naibu Waziri pamoja na wataalam wake wapo tayari kuja Serengeti kuona mazingira na kufanya need assessment kwa sababu proposal hii itahitaji nyongeza ya fedha kidogo na hivyo watapata uelewa mpana na kutusaidia katika proposal hii? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jeremiah Mrimi, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri ni kweli Mheshimiwa Mbunge toka mwaka 2021 amekuwa akifika ofisini mara kwa mara, lakini hata hapa Bungeni tukionana mara kwa mara alikuwa akinikumbusha jambo hili, lakini mara kadhaa nadhani amefika kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na kupiga simu kufuatilia jambo hili.

Kwanza nikushukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji huo wa karibu kwa kuwafuatilia wananchi wa Serengeti tunakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kipekee nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, siyo kwa kutenga tu fedha.

Mheshimiwa Spika, naomba nikuhakikishie kwamba hii shilingi bilioni 100 tayari Mheshimiwa Rais ameshaitoa, kwa hiyo, ni jukumu letu sisi kama Wizara sasa kusimamia kwa karibu.

Kwa hiyo, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge hivi sasa tuko kwenye maandalizi, hauwezi ukasema tu kwamba utaanza kesho kwa sababu kuna taratibu ambazo lazima tuzifanye. Nimesema hapa maeneo tayari tumeshapata, tumebainisha maeneo yale na hivi sasa tunafanya topographical survey, lakini vilevile lazima tufanye geo-technical survey, lakini vilevile lazima tufanye environment impact assessment ili wakati tunapoanza tusiweze tena kupata changamoto.

Kwa hiyo, nikuhakikishie tu kwamba taratibu hizi zitakapo kamilika ujenzi huu utaanza mara moja.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la pili, kwa upande wa kuja sisi aidha mimi au Waziri na wataalam, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge tupo tayari kwenda Serengeti ili kuweza kuona changamoto na namna gani tunaweza kuzifanyia kazi, nashukuru sana.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Hata hivyo, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza: Vijiji vya Borenga, Nyiboko, Buchanchali, Nyasulimunti na Gantamome ambavyo vipo kando kando ya Mto Mara kwa muda mrefu sasa vimeendelea kupata adha kubwa na hasara ya mafuriko katika mashamba, na tunaona mpango huu wa Serikali wa miaka kumi: Je, ni lini mpango huu utaanza ili kuondoa hadha hii inayoendelea katika maeneo hayo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kumekuwepo na mpango mzuri na maarufu kabisa wa Serikali uliojulikana kama Nile Basin Initiative ambao unahusisha maeneo haya ya Mto Mara kujengewa mabwawa makubwa, scheme za umwagiliaji na kudhibiti mafuriko haya: Je, mpango huu sasa wenyewe umefikia wapi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jeremiah Amsabi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika Serikali hasa kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira tunayo nia ya kuhakikisha kwamba tunafanya huo mradi ambao Mheshimiwa ameupendekeza ama ameutaja. Kikubwa nimwambie Mheshimiwa awe na subira kwa sababu miradi hii kwanza lazima tufanye utafiti, tuone namna itakavyowezekana lakini lazima kuna Wizara tukae, kwa sababu kama tunavyoona hili jambo lina Wizara za kisekta lazima tukae Wizara ya Maji, tukae Wizara ya masuala ya Kilimo pia na sisi tukae pamoja, lakini kubwa zaidi atupe muda kidogo tutafute fedha kwa ajili ya kurekebisha ama kukamilisha mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili nimwambie kwamba Wizara hii ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira tumekuwa tuna utaratibu wa kutembelea miradi takribani yote ambayo inasimamiwa na Ofisi yetu. Kila tunapokwenda tunatoa maelekezo kwamba kwanza miradi ikamilike kwa wakati, pili, miradi iwe ya kiwango, lakini tatu, miradi hii ihakikishe kwamba inanufaisha walengwa. Nimwambie tu kwamba miradi yote iliyo katika eneo lake ama jimbo lake tutaifuatilia na tutatoa maelekezo na itakamilika kwa wakati, nakushukuru.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Vikao vya DCC na RCC wakati mwingine majibu yake yanachelewa kutoka Serikalini: Je, ni lini Serikali itatupatia majibu ya mabadiliko ya jina la Mji wa Mugumu kuwa Mji wa Serengeti kama lilivyopitishwa na vikao vya DCC na RCC? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amsabi Mrimi, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa maelekezo na utaratibu wa taarifa na maamuzi na mapendekezo ya DCC na RCC kuletwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI yako wazi. Nisisitize kwamba baada ya vikao hivyo, Makatibu Tawala wa Mikoa wahakikishe kwamba taarifa zinafika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu jina la Mugumu kwenda kuwa Serengeti, naomba tulichukue hili tukatazame limefikia hatua gani, tuone maoni ya wadau na baadaye Serikali itatoa maamuzi lipi linakwenda kufanyika? Ahsante sana.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Tunaishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kusukuma sana ujenzi wa barabara ya Sanzate – Nata; je, ni lini kipande cha Nata mpaka Mugumu ujenzi wake utaanza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Nata kwenda Mugumu ni barabara ambayo tutakuwa tunakamilisha barabara ya makutano Nata hadi Mugumu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti ambayo tunaiendea, tumeipanga ili iweze kukamilika na hivyo kukamilisha mzunguko wa Nata – Mugumu; Mugumu hadi Tarinya kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari Ngoreme Wilayani Serengeti kumekuwepo na jitihada nyingi za wananchi na wadau mbalimbali za kujenga miundombinu kwa lengo la kuifanya kuwa shule ya Kidato cha Tano na cha Sita. Yamekuwepo maombi yangu mbalimbali mara kadhaa kwa TAMISEMI.

Je, ni lini sasa TAMISEMI mtaipandisha hadhi shule hii kuwa ya Kidato cha Tano na cha Sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Amsabi Mrimi kwa jitihada zake za kuhakikisha shule hii ya Ngoreme inapandishwa hadhi. Kwa sasa walikuwa wanamalizia ujenzi wa mabweni ili kuweza kuhakikisha kwamba shule hii inakidhi vigezo vya kuwa A level na baada ya hapo Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Elimu zitafanya jitihada za kuhakikisha shule hii inasajiliwa kuwa na mkondo wa Kidato cha Tano na Sita.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mji wa Mugumu kama unakuwa kwa kasi na shuguli za maendeleo wakati wote zinaendelea.

Je, ni lini sasa Serikali itatusaidia kuhakikisha tunapata taa za barabarani katika mji wa Mugumu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kuweka taa katika mji wa Mugumu kwenye barabara zinazokamilika. Mheshimiwa Mbunge ni shahidi kuna barabara inayozunguka Soko kuu la Mugumu ambayo inakamilika muda si mrefu na barabara ile itakapokamilika taa zile zitafungwa kama nilivyosema awali kwamba sasa TARURA katika barabara zote zinazojengwa katikati ya miji ni lazima ziwekewe taa.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kutokana na umuhimu mkubwa wa kiuchumi na shughuli za kijamii kwa wananchi wa Ngoreme hasa upande ule wa Majimoto, Busawe na Iramba. Ni lini sasa barabara ya Musoma kutoka pale makutano ya Nyakanga mpaka Sirori Simba kupitia Iramba - Majimoto mpaka Nyasirori itajengwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jeremiah, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitamka Mheshimiwa Mbunge, ni barabara ambayo katika mwaka huu wa fedha tulikuwa tumeifanyia upembuzi yakinifu wa awali na katika mwaka wa fedha ujao tutaifanyia upembuzi yakinifu wa kina kama maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kuna jitihada nyingi katika Jimbo la Serengeti Kijiji cha Nyamatale pale Nyirongwa wamejenga boma, pale Kitalahota Kitongoji katika Kijiji cha Nyamakobiti, pia wamejenga boma kwa jajili ya zahanati, Kijiji cha Bisalala, Ngalawani na Kenokwi.

Je, ni lini sasa Serikali itatoa mchango wake kusaidia jitihada hizi za wananchi kukamilisha zahanati hizi? ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amsabi la zahanati hizi za vijiji ambavyo amevitaja Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi hawa kadri ya upatikanaji wa fedha. Na tutajitahidi, kwa sababu ni adhma ya Serikali hii ya awamu ya sita kuhakikisha afya za Watanzania zinaimarika zaidi kwa kupata huduma iliyobora. Tutahakikisha kadri ya upatikanaji wa fedha tunachangia nguvu za wananchi wa pale.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya mwaka jana tulipata bahati ya kupita naye katika baadhi ya zahanati zetu Wilayani Serengeti alishuhudia upungufu mkubwa wa dawa na vifaa tiba. Sasa je, ni lini na kuna mpango gani wa kuhakikisha uwepo wa dawa na vifaa tiba vya kutosha katika zahanati ya Kemgesi, Maburi, Busawe, Nyansulula, Mbalibari, Koleli, Rubanda, Kituo cha Afya Nata na Zahanati ya Rigita? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tulikuwa naye pamoja Serengeti, tuliona hilo tatizo. Sasa namwagiza DMO wa Serengeti leo aandike mahitaji ya hiyo hospitali na wiki hii watapata dawa.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Tunaishukuru Serikali kwa kuanza ujenzi wa kilometa 600 za lami kutoka Benki ya CRDB pale Mjini Mugumu kuelekea Hospitali ya Wilaya. Pamoja na ujezni huu barabara hii imesimama sasa kwa muda, na kwa vile inaelekea hospitali ya wilaya, imekuwa na usumbufu mkubwa sana kwa wananchi. Pamoja na jitihada nyingi za mawasiliano na TARURA, wilaya na mkoa bado ujenzi huu hauendelei. Je, ni lini changamoto hizi zitatatuliwa na ujenzi ule ukamilike? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii anayozungumzia Mheshimiwa Mrimi ya CRDB – Hospitali katika Mji wa Mugumu imekuwa na changamoto ya mkandarasi mwenyewe kuwa anafanya kazi kwa taratibu sana. Mkandarasi huyu ameshaitwa kwenye Kamati mbalimbali za pale katika Wilaya ya Serengeti kuangalia ni namna gani anaweza akamaliza barabara hii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tukitoka hapa tutakaa naye tuweze kuona tunaweka mkakati gani na Meneja wa TARURA wa Mkoa wa Mara na Meneja wa TARURA wa Wilaya ya Serengeti kuona mkandarasi huyu anarudi site vipi kwa haraka sana kumalizia barabara hii.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Machwechwe pamoja na changamoto zingine ndogo ndogo nimewasilisha TAMISEMI mara kwa mara juu ya changamoto ya kukabiliana nayo ya gharama kubwa za vifaa vya ujenzi. Sasa je, ni lini Ofisi ya Rais, TAMISEMI watatuongezea fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kile Kituo cha Afya cha Machwechwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaangalia, tutakakaa na Mheshimiwa Amsabi Mrimi kuhakikisha tunaangalia katika mwaka wa fedha huu unaoenda kuanza wa 2023/2024, ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya kumalizia Kituo cha Afya cha Machwechwe kule Wilayani Serengeti na ikiwepo basi tutahakikisha fedha hizo zinaenda mara moja.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa ajili ya kuongeza idadi ya watalii na kuboresha uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti; je, ni lini ujenzi wa uwanja wa ndege wa Serengeti utaanza?

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba tu niwataarifu ndugu zangu wana-Serengeti, hususan Mugumu kwamba mchakato unaendelea na uko kwenye hatua za utekelezaji kwa maana ya kuanza. Tayari tulishaanza mchakato na namna ya ku-identify hayo maeneo na lengo ni kuhakikisha kwamba tunapunguza muingiliano wa shughuli za uhifadhi katika Hifadhi ya Serengeti, hivyo uwanja tutauhamisha usogee katika Eneo la Mugumu. Kwa hiyo, mchakato unaendelea.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mto Nyahende kule Nyansulula?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la Mheshimiwa Amsabi Mrimi la Mto Nyahende kule Wilayani Serengeti tutaangalia katika mwaka wa fedha huu ambao tumeidhinishiwa na Bunge lako tukufu wa 2023/2024 kuona kama fedha ilitengwa ya kuanza ujenzi wa daraja hili. Kama fedha hiyo haikutengwa tutaangalia katika kuitenga kwenye mwaka wa fedha wa 2024/2025.
MHE. JEREMIAH A. MRIMI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Afya Iramba kilichochakaa sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tutaangalia katika mwaka wa fedha unaofuata na kuipa kipaumbele kata hii na kuweza kupeleka fedha kadiri ya ilivyotengwa.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kemgesi pamoja na Ligicha Wilayani Serengeti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni majuzi tu ambapo tulikaa na Mheshimiwa Mrimi aliwasilisha maombi haya katika Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya kituo cha afya Kemgesi na kadiri ya upatikanaji wa fedha tutahakikisha Mheshimiwa Mrimi kule wanaserengeti wanapata kituo hichi cha afya.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itapeleka na kujenga minara ya simu katika kata zenye shida kubwa ya mawasiliano ya simu yaani Serengeti ikiwemo Busawe, Issenye, Kenyamonta, Manchira, Mbalibalim Nagusi, Natta, Nyamatare, Nyambureti, Nyamoko na Uwanja wa Ndege?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amsabi Mrimi, Mbunge wa Serengeti kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kbisa Mheshimiwa Mbunge ameshaleta changamoto ya maeneo ambayo yana changamoto ya mawasiliano, lakini katika kata ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge isipokuwa Kata ya Uwanja wa Ndege na ndio ambayo hatutaiingiza katika mpango huo wa utekelezaji. Zingine zote tutaziingiza katika utekelezaji, ahsante sana.

SPIKA: Sasa hiyo ambayo hamuiingizi ni kwamba mnao mpango wa baadaye ama? Maana wananchi sasa wakisikia kwamba hii ndio haiingizwi kwenye mpango?

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ameshaleta changamoto hizo na tayari tulizipokea, ametaja hizo Kata nazikumbuka isipokuwa ya Uwanja wa Ndege ambayo hakuileta, sasa hiyo itabidi isubiri mpango wa awamu ijayo ili iweze kuingizwa, ahsante sana.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara nyingi za ndani ya Mji wa Mugumu kule Wilayani Serengeti zina hali mbaya sana na haziwezi kupitika; je, ni lini sasa Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amsabi Mrimi la lini Serikali itaongeza ukarabati wa barabara zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti?

Mheshimiwa Naibu Spika, nilijulishe Bunge lako tukufu kwamba hivi tunavyoongea hivi sasa kuna barabara ambayo inazunguka Soko Kuu la Mji wa Mugumu ambayo inatengenezwa kwa kiwango cha lami kupitia Wakala wetu wa TARURA na tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha mazingira ya Mji wa Mugumu kwa sababu ndiyo Makao Makuu ya Wilaya ya Serengeti. Lakini vilevile kupitia Wilaya nzima ya Serengeti barabara za changarawe vilevile tutaendelea kuhakikisha fedha inatengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara zake na nyingine Mheshimiwa Mbunge Mrimi amekuwa akija kwa ajili ya kuzielezea na kusema barabara zipi ziweze kutengewa fedha kwa ajili ya kuzifungua.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali hili hili ambalo limeulizwa na Mheshimiwa Mbunge wa Tarime Vijijini, nimeuliza mara nyingi na ni mara nyingi nimeongea na Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu barabara hii ya Nyamongo mpaka Mugumu: Sasa tunaomba kujua ni lini hasa kwa maana ya tarehe, utakaposainiwa huo mkataba na kuanza ujenzi wa barabara ya Nyamongo – Mugumu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda tu niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge, na hasa Mbunge wa Tarime na Mbunge wa Serengeti, hii barabara inaunganisha Serengeti na Tarime, lakini kutoka Serengeti pia inategemea kwenda Nata. Naomba wawe na Subira. Taratibu zote za manunuzi zimeshakamilika, tunachosubiri ni kutafuta siku maalum ya kufanya signing.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuna hakika, kama utaratibu utakwenda kama tulivyopanga ni kuisaini hiyo barabara kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha. Kwa hiyo, siku itakapokuwa tayari, tutawajulisha Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Mbunge wa Serengeti na Mheshimiwa Mbunge wa Tarime Vijijini, ahsante.
MHE. JEREMIAH A. MRIMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni lini, sasa Serikali itatusaidia fedha ya nyongeza kwa ajili ya ukamilishaji ujenzi kituo cha afya Machochwe kama tulivyoomba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Mheshimiwa Mrimi amekuwa akilifuatilia sana kuhusu fedha hizi za Kituo cha Afya Machochwe na tutaendelea kama ambavyo nimeonana naye ofisini mara kadhaa kumueleza kwamba, tunaangalia namna gani bora tutapata fedha ya kumalizia kituo hiki cha afya na pale ambapo Serikali itapata fedha basi tutapeleka katika kituo hiki cha afya cha Machochwe ili kiweze kukamilika. (Makofi)

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi tena. Nishukuru majibu ya Serikali yaliyotolewa kwa swali, lakini niombe kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza jumla ya barabara ambazo zilijengwa 2021/2022 na zitakazojengwa mwaka wa kesho zinaonesha wastani wa kilomita 100 tu kwa mwaka. Sasa basi jumla ya barabara zinazohudumiwa na TARURA ni zaidi ya kilomita 900, hii maana yake ni kwamba itatuchukua zaidi ya miaka tisa kujenga barabara zote zilizo chini ya TARURA katika Jimbo la Serengeti. Sasa basi Serikali haioni haja ya kutafuta fedha za ziada kwa ajili ya kuongezea Jimbo la Serengeti kwa sababu barabara ni nyingi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tarehe 25 Julai, 2021, Naibu Waziri wa TAMISEMI aliwaahidi wananchi wa Serengeti kwamba barabara ya lami inayozunguka soko la Mugumu ingejengwa na kukamilishwa. Mpaka sasa hivi mkandarasi ameshasaini mkataba toka mwanzo wa mwaka huu lakini barabara ile haijengwi. Tunaomba commitment ya Serikali ya kujenga barabara ile ya lami ya kuzunguka soko la Mgumu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jeremiah Mrimi Amsabi, Mbunge wa Jimbo la Serengeti, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Msabi kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kuwakilisha ipasavyo wananchi wa Jimbo la Serengeti. Pili, kuhusiana na fedha ambazo zinatengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika Halmashauri ya Serengeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii imeendelea kuongeza fedha ambazo zinakwenda kufanya matengenezo na ujenzi wa barabara vijijini na mijini. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2020/2021, bajeti ya Serikali kupitia TARURA ilikuwa bilioni 255, lakini 2021/22 Serikali iliongeza kutoka 255 mpaka bilioni 722, zaidi ya mara tatu ya bajeti. Pia mwaka ujao wa fedha tumeongeza kutoka 722 mpaka bilioni 822 plus.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hii yenyewe inaonyesha namna Serikali ambavyo ina commitment kubwa ya kuongeza fedha kupitia TARURA ili barabara zetu ziendelee kujengwa. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hata wao mwaka 2020/2021, bajeti ilikuwa ndogo, lakini imeendelea kuongezeka na tutaendelea kuhakikisha tunaongeza bajeti ili barabara za Serengeti zijengwe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na barabara ya lami inayozunguka Soko la Mugumu, naomba nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi na Watendaji wote wa Mamlaka hii ya Barabara TARURA kuhakikisha mkandarasi huyu anaanza kazi haraka iwezekanavyo na vinginevyo tutachukua hatua mapema iwezekanavyo ili kuhakikisha barabara inakamilika mapema. Ahsante.
MHE. JEREMIAH A. MRIMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuja kwa timu ya Mawaziri nane ambayo ilitangaza kuongezwa kwa eneo la mita 500 eneo la Kinga katika vijiji vya Mbilikili, Bisarara, Tamkeri, Mbalibali, Gwikongo, Machochwe, Nyamakendo pamoja na Meringa. Pia katika nyakati tofauti mwaka 2008, 2010, 2013 mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vijiji hivyo imekuwa ikibadilishwa.

Sasa je, Waziri wa Maliasili pamoja na Waziri wa Ardhi wako tayari kuja Serengeti wakiambatana nami mapema iwezekanaavyo wakiwa na GN ya mwaka 1968 yenye ramani namba 14, 15, 4 ili kutatuza tatizo hili kwa sababu ni la muda mrefu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali namba mbili; mwaka 1994 Serikali ilipunguza eneo la Grumeti Game Reserve pamoja na Ikorongo Game Reserve kutoka kilometa za mraba 3,600 kuwa 993.4 lakini mpaka sasa kumbukumbu za Serikali bado hazijafanya mabadiliko hayo. Kwa hiyo, wananchi wa Makundusi, Pakinyigoti, Rwamchanga, Rwabando wamekuwa wakizuiwa kufanya shughuli zao. Je, ni lini mabadiliko hayo yatafanyika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jeremiah Amsabi Mrimi, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mipaka kama ambavyo timu ya Mawaziri nane ilipita kutoa ufafanuzi, lakini pia ikaacha watumishi ambao walikuwa wanafanya tathmini ya namna ya kuja kutoa ufafanuzi juu ya mipaka hiyo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Serengeti na wananchi wa Serengeti kwamba tathmini sasa hivi imeshakamilika na kinachofuata sasa ni kwenda kuonesha mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wizara ya Maliasili na Utalii tukishirikana na wizara ya Ardhi tutaenda kufafanua hii mipaka tukiwa na wananchi wa maeneo hayo na lengo ni kuondoa sasa ile vurugu au taharuki ya kutotambua mipaka kati ya hifadhi na wananchi.

Kwa hiyo, niwahakikishie hawa wananchi kwamba tathmini imeshakamilika tunakuja sasa kufafanua utambuzi wa mipaka ni ipi ya hifadhi ni ipi ya wananchi, hilo linaenda kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na swali lake la pili limehusiana na ufafanuzi wa GN baada ya kurekebishwa eneo la Hifadhi ya Ikorongo; Serikali italifanyia kazi eneo hili na tutapeleka waraka kwa wananchi kwa maandishi sasa kuonesha kwamba eneo hili litakuwa ni la hifadhi na lile ambalo limeachwa kwa wananchi ili wawe na uwezo sasa wa kufanya shughuli zao za kila siku, tutaenda kulifanyia kazi na tutatoa taarifa kwa wananchi wa Wilaya ya Serengeti.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa ajili ya kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii, je Serikali ina mpango gani wa kufanya marekebisho katika barabara za Kata ya Nyamoko, Kisangura, Tarafa ya Ngoreme na Tarafa ya Ikorongo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Dkt. Mrimi, kwanza kuhusu hili la marekebisho, kama ambavyo tulizungumza hapa awali katika Bunge hili ambalo linaendelea kwamba, Serikali ilikuwa katika mchakato wa kuhakikisha TARURA inaletewa fedha ya dharura haraka.

Mheshumiwa Mwenyekiti, tathmini imefanyika kote nchini, tathmini ile ilikamilika mwisho wa mwezi Januari mwaka huu wa 2024, ikiwemo kutoka kule kwa Mheshimiwa Mrimi, hivyo basi fedha ile ambayo itapatikana itaenda katika maeneo yale kuweza kuanza kurekebisha barabara zote korofi, ikiwemo kule Jimboni kwa Mheshimiwa Mrimi.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuwa Kituo cha Afya Iramba, Wilayani Serengeti ni cha muda mrefu na kimechakaa sana ni lini sasa Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amsabi Mrimi, Mbunge wa Jimbo la Serengeti kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumuelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Serengeti kufanya tathmini kwa maana ya gharama zinazohitajika kwa ajili ya ukarabati wa kituo hiki cha afya na kuwasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kufanya tathmini lakini pia kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho, ahsante.

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa mgogoro wa ardhi kati ya Kijiji cha Remung'orori Wilayani Serengeti na Kijiji cha Mekomariro Wilayani Bunda, umedumu kwa muda mrefu na umekuwa na athari nyingi mbaya kwa Wananchi wa Remung'orori Wilayani Serengeti. Sasa Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kumaliza mgogoro huu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Serikali imeendelea na mchakato wa kuhakikisha kwamba, maeneo haya yanafidiwa haraka kwa kadri itakavyowezekana. Kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili tutakaa na kuangalia ni uharaka gani tuutumie ili kukamilisha zoezi la eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, amekuwa mfuatiliaji wa mgogoro huu ambao kimsingi tutakapokutana na wenzetu wa maliasili tutaona namna gani twende kuumaliza ili wananchi waweze kwendelea na shughuli zao za kawaida…
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kutokana na mabadiliko ya tabianchi kumekuwa na mafuriko makubwa katika Mto Mara ambayo yamesababisha uharibifu wa mashamba katika Vijiji vya Nyiboko, Korenga, Nyasulumunti na Iselesele, Wilayani Serengeti, je, ni lini sasa Serikali itatekeleza mradi wake mkubwa uliopangwa wa kudhibiti mafuriko hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa aliwahi kuuliza swali hili na tuliona namna ambavyo tunaweza tukamsaidia na bahati nzuri tumeona athari kubwa ambayo inajitokeza huko na namna ambavyo wananchi wanaathirika kutokana na athari hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumemsikia na bado Serikali tunaendelea kutafuta fedha za kuona namna ambavyo tunaweza tukatengeneza mradi huu na kuweza kuwasaidia wananchi, ili wasiendelee kusumbuka na changamoto hiyo, nakushukuru. (Makofi)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, katika Wilaya ya Serengeti Miradi ya Maji ya Gesaria, Nyamitita, Rigicha na Nyiberekera imekwama kabisa. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Serengeti katika eneo la Nyamitita, tayari mkandarasi wetu yuko site, yuko kwenye utengenezaji wa line ya umeme ya kilometa sita. Pia katika eneo la Rigicha mkandarasi tayari yuko katika eneo na anaendelea kurekebisha line ya umeme, lakini katika kijiji ambacho amekitaja, jina lake naomba liingie kwenye Hansard kama alivyolitaja, kuna visima, vituo 30 vya kuchotea maji tayari vimekamilika na asubuhi hii DM alikuwa katika eneo hilo na amenipatia mrejesho wa kazi ambayo imeshafanyika.

Kwa hiyo, namtoa hofu Mheshimiwa Mbunge kazi inaendelea na tutahakikisha kwamba maji yanapatikana kwa usahihi zaidi, ahsante sana.
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kutokana na mabadiliko ya tabianchi kumekuwa na mafuriko makubwa katika Mto Mara ambayo yamesababisha uharibifu wa mashamba katika Vijiji vya Nyiboko, Korenga, Nyasulumunti na Iselesele, Wilayani Serengeti, je, ni lini sasa Serikali itatekeleza mradi wake mkubwa uliopangwa wa kudhibiti mafuriko hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa aliwahi kuuliza swali hili na tuliona namna ambavyo tunaweza tukamsaidia na bahati nzuri tumeona athari kubwa ambayo inajitokeza huko na namna ambavyo wananchi wanaathirika kutokana na athari hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumemsikia na bado Serikali tunaendelea kutafuta fedha za kuona namna ambavyo tunaweza tukatengeneza mradi huu na kuweza kuwasaidia wananchi, ili wasiendelee kusumbuka na changamoto hiyo, nakushukuru. (Makofi)
MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mvua nyingi zilizonyesha katika Jimbo la Serengeti, Barabara za Bwitengi – Miseke na Mugumu – Machochwe zimeharibika sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya marekebisho ya haraka? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua madhara makubwa ambayo yametokea kwenye barabara zetu hizi za wilaya ambayo yamesababishwa na mvua. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua na tayari inafanya jitihada kuhakikisha kwamba inarudisha mawasiliano maeneo ambayo mawasiliano yamekatika, lakini inaboresha na kufanya ukarabati wa barabara kwenye maeneo yale ambayo yameharibika na barabara hazipitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kuhakikisha kwamba barabara hizi, mtandao huu wa barabara za wilaya unakuwa ni mtandao wa barabara ambazo zinapitika mwaka mzima. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali ipo kazini na tutafanya jitihada zote ili kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu ya barabara hizi za wilaya.