Supplementary Questions from Hon. Masache Njelu Kasaka (38 total)
MHE. MASACHE N. KASAKA:Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini kwa kuwa mpango huu wa kutumia maji ya Ziwa Nyasa ni wa muda mrefu na Serikali imekuwa inatoa ahadi hii mara kwa mara na hata kwenye ziara yako Mheshimiwa Naibu Waziri ulipofika na ulituahidi mradi huu utaanza.
Je, ni lini mradi huu utaanza ili walau kata za Kajunjumele, Ipinda, Kasumulu pamoja na Kyela Mjini waweze kunufaika?
Swali la pili kwa Wilaya yangu Wilaya ya Chunya kwa mwaka huu wa fedha zilitengwa fedha kwa ajili ya kuhudumia miradi ya maji kwa vijiji vinane lakini mpaka sasa hivi fedha hizo hazijaweza kutoka.
Je, ni lini fedha hizo zinaweza zikatoka ili sasa watu wangu wa vijiji vya Sangambi, Shoga, Kambikatoto, Lualaje, Nkung’ungu, Soweto na Itumbi waweze kunufaika nahii miradi ya maji? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally, Mbunge wa Kyela nipende kusema kwamba upembuzi yakinifu unaendelea na muda wa kufika mwezi Mei utakamilika na tunatarajia mwaka mpya wa fedha 2021/2022 Serikali itakwenda kutekeleza mradi huo.
Kuhusiana na swali lake la nyongeza kwa Wilaya ya Chunya nipende kusema kwamba Serikali imeweka jicho la kipekee kabisa kwa Wilaya ya Chunya na Chunya ni moja ya ile miji 28 ambayo tunaitarajia kuja kuitekeleza kwa fedha ambazo tumezipata za mkopo kutoka Serikali ya India kupitia benki ya Exim. Kwa hiyo kuanzia mwezi huu Machi shughuli ya kazi katika vijiji vya Sangambi na vile vijiji vya jirani pia vinakuja kutekelezwa, ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pia naishukuru Serikali kwa kuweza kutekeleza Mradi wa Maji kwa Mji wa Chunya uliogharimu zaidi ya milioni 900 lakini mradi huu mpaka sasa hivi haujaweza kuwanufaisha wananchi wa Wilaya ya Chunya na hata kiwango cha upatikanaji wa maji bado kiko chini ya asilimia 30. Tatizo kubwa tukiuliza tunaambiwa mara umeme unakuwa ni mdogo, mara maji ni machache. Sasa Serikali itueleze, je, tatizo ni nini mpaka mradi huu uliotumia fedha nyingi za Serikali haujaweza kuwanufaisha watu wa Chunya?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwenye mradi mkubwa wa maji wa bwawa la Matwiga design ya mwanzo ilikuwa inasema itanufaisha vijiji 16, lakini kwenye review ilivyokuja utekelezaji wake ni vijiji nane. Je, Serikali haioni haja sasa kuweza kurudisha hii design ya mwanzo kurudisha vijiji 16 ili wananchi wa Tarafa ya Kipendao waweze kunufaika na mradi huu wa maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Masache Kasaka kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nia na lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata maji safi na salama na ya kutosheleza. Niseme tu msimamo wa Serikali ni kuona kwamba miradi iliyokamilika na matunda yale ya mwisho maji bombani yanapatikana. Kwa mradi huu wa Chunya Mjini nipende tu kusema kwamba Mheshimiwa Mbunge nilifika Chunya na tulitembea pamoja, mradi ule umekamilika tatizo ni hili la umeme ambalo linaendelea kushughulikiwa ili liweze ku-support ile pump maji yaweze kwenda ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa swali la Bwawa la Matwiga, niseme kwamba, katika miradi ambayo ilichukua muda mrefu kutekelezwa ni pamoja na huu, lakini kwa nia njema ya Serikali hii na mkakati mkubwa wa Wizara chini ya usimamizi wa Mheshimiwa Waziri mradi ule sasa hivi unatekelezwa vizuri na mimi pamoja na Mheshimiwa Mbunge tulifika pale tukiongozana na Mtendaji Mkuu wa RUWASA kwa maana ya Director General. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, yale maji ambayo tuliyaona pale kwa pamoja kwenye kile chanzo hayatatoa tu kwa vijiji vile nane, tayari kama Wizara tumekubaliana tutakuja kutoa maji katika vijiji vyote 16.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Tatizo ambalo linaikumba Njombe Mjini la uhaba wa walimu, ndilo tatizo hilohilo ambalo linaikumba Wilaya ya Chunya kwa uhaba wa walimu. Ajira mara ya mwisho iliyopita Wilaya ya Chunya tulipata takribani walimu 26 tu ambao ni idadi ndogo ukilinganisha na ukubwa wa Wilaya ya Chunya.
Je, Serikali inatuhakikishia vipi kwamba kwenye awamu hii ya ajira itakayokuja tutapata walimu wa kutosha, hasa maeneo ya vijijini, ili kuweza kukidhi mahitaji ya watu wa Wilaya ya Chunya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, moja, nikubaliane na yeye kwamba kweli hata Chunya nakufahamu vizuri. Eneo ni kubwa na kuna idadi ndogo sana ya walimu. Lakini kwa sababu ameleta hapa ombi na sisi kama Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumelipokea hilo ombi na katika mgawanyo wa walimu 6,000 tutalizingatia hilo. Ahsante sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza: Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inafanya utafiti kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo kwa maana ya PMI za wachimbaji wadogo wadogo ili ziweze kuwasaidia waachane na uchimbaji wa kubahatisha.
Mheshimiwa Spika, suala la pili hii Taasisi ya Jiolojia ina ofisi zake hapa Dodoma. Sasa je, kwa mikoa ya nyanda za juu Kusini, ina mkakati gani sasa wa kufungua ofisi kule kwa Mkoa wa Mbeya ili nasi tuweze kupata hii ofisi ili iweze kuwasaidia wachimbaji wetu wadogo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Njelu Kasaka Masache, Mbunge wa Jimbo la Lupa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu utafiti kwa wachimbaji wadogo, taasisi ambayo inapaswa kufanya utafiti ni taasisi yetu ya GST, lakini wao wanaweza kufanya utafiti kwa njia zile za kawaida za awali kwa maana ya jiolojia, jiofizikia na jiokemia. Ili utafiti uweze kuwa wa kufana, unahitajika kidogo uchimbaji (drilling). Sasa taasisi iliyo na vifaa vya drilling ni Shirika letu la Madini la STAMICO.
Mheshimiwa Spika, hii ni habari njema kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wengine wote kwamba wiki iliyopita taasisi yetu ya GST pamoja na STAMICO waliingia makubaliano ya ushirika ili waweze kufanya kazi Pamoja. Kwa maana aliyepewa jukumu la kutafiti, lakini hana vifaa vya drilling na mwingine aliyepewa kulea wachimbaji ana vifaa, basi washirikiane ili kwa pamoja waweze kuwa wa msaada.
Mheshimiwa Spika, sisi tunaamini kama Wizara kwamba ushirika wao huo ambao waliuingia wiki iliyopita, unakuja kuwa msaada mkubwa kwa sababu taasisi mbili chini ya Wizara zimeungana ili mmoja aweze kutafiti akiwa anatumia njia za kawaida, asaidiwe na yule ambaye ana vifaa vinavyoweza ku-drill, lakini itakuwa ni kwa gharama angalau iliyopunguzwa, siyo kama ile kwa wachimbaji wakubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pamoja na kwamba ni habari njema, wachimbaji wadogo wajue kwamba tutakapofanya drilling haitakuwa free, badala yake itakuwa kwa gharama iliyopunguzwa tukilinganisha na wale wachimbaji wakubwa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili; ni kweli kwamba GST Makao yake Makuu yapo Dodoma, lakini maelekezo ya Wizara ni kwamba kazi zake hizi zifanywe pia mikoani. Habari njema ni kwamba mwaka unaokwisha huu tulifungua ofisi Geita na lengo ni kwamba tuendelee kufungua katika kanda ili kurahisisha hasa zile kazi za maabara kwa kutumia ofisi zetu za Tume ya Madini zilizoko mikoani. Kwa hiyo, kwa kuanzia tutazitumi zile na maelekezo yetu ni kwamba shughuli zote zifikishwe kwa ofisi za RMO halafu ziletwe Dodoma na kisha waweze kuhudumiwa kwa jinsi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kadri tutakavyokuwa tunapanua shughuli na kupata watumishi wengi zaidi, tunatamani kwamba tufungue matawi kila kanda katika nchi ya Tanzania ili kurahisisha utendaji kazi wa GST.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kuniona. Nami pia niungane na swali la msingi kama ilivyo Wilaya ya Geita Mjini, kulikuwa na matatizo ya barabara zilizo chini ya TARURA. Wilaya yetu ya Chunya pia ina matatizo mengi ya barabara zilizo chini ya TARURA zilizoharibika vibaya kutokana na mvua zilizonyesha mwaka huu.
Mheshimwa Naibu Spika, barabara ya kuanzia Lupa kwenda Nkunungu – Lupa - Lwalaje zimeharibika vibaya na kwenye fedha zilizokuwa zimetengwa, zilitengwa maeneo korofi:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za dharura ili barabara hizo ziwewe kutengenezwa ikizingatiwa kuwa maeneo haya zinalimwa Tumbaku na msimu wa soko la Tumbaku unaanza wiki ijayo kwa hiyo, itashindwa kutoka kule? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Masache ameainisha baadhi ya barabara ambazo zimeharibika sana wakati wa mvua yakiwemo madaraja; na sehemu ya hizo barabara TARURA walipeleka fedha kwa ajili ya kutatua hizo changamoto za udharura kwa maana ya uharibifu wa hizo barabara. Sasa hivi ameomba tu kwamba Serikali ni lini tutatenga fedha kuhakikisha hizo barabara zinapitika?
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu la msingi ni kwamba kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyokuwa tutazitengeneza na bahati nzuri maeneo hayo mimi nayafahamu na nimeahidi kufika kujionea mwenyewe hali halisi. Nitakwenda na Mheshimiwa Mbunge na tutazungumza na wananchi. Ninaamini kabisa kwamba kutokana na bajeti ambayo Bunge lilipiga kelele na Serikali ikaongeza, tutafikia maeneo mengi sana mwaka huu wa fedha kuhakikisha tunapunguza hizo changamoto ambazo zinawakabili wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri. Naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali ilitenga fedha kujenga visima nane vya maji katika Wilaya ya Chunya katika Kata za Sangambi, Shoga, Matunda, Skambikatoto, Rualaje, Nkung’ungu na Soweto mpaka Itumbi, lakini mpaka sasa hivi fedha hizo hazijatoka.
Je, ni lini fedha hizi zitatoka ikiwa imebakia takribani siku 40 mwaka huu wa fedha uishe?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwenye chanzo cha maji cha Chunya Mjini kuna takribani visima nane vilichimbwa, lakini visima viwili pekee ndivyo vinavyofanya kazi.
Je, ni kwa nini visima hivi vingine, takribani sita, havifanyi kazi?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Mbarali kuwa miongoni mwa Wabunge ambao wamepitisha bajeti yetu na kutupatia fedha zaidi ya shilingi bilioni 680. Kwa hiyo, jukumu letu sisi kama Wizara ni kuhakikisha tunakwenda kutatua tatizo la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu fedha ambazo kwa ajili ya uchimbaji wa hivyo visima; nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya Saa 07:00 naomba tukutane ili tuweke commitment ya Wizara tuweze kuku-support kuhakikisha wananchi wako wanapata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu suala zima la visima pale katika eneo la Chunya Mjini, kuna visima nane, viwili vinafanya kazi. Nimetoa maelekezo mahususi. Wizara ya Maji inafanya mageuzi makubwa katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama kama Mheshimiwa Rais maelekezo yake ametupatia sisi Wizara ya Maji. (Makofi)
Kwa hiyo, maelekezo ambayo tumeyatoa kwamba, kwa wataalam wetu wote kusimamia na kufuatilia, hususan aidha visima ama miradi ya maji, kuhakikisha vyote vinafanya kazi na wananchi waende kupata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Nchi yetu hii imezungukwa sana na wachimbaji wadogo wadogo hasa kwenye maeneo mengi yenye uchimbaji wa madini. Je, ni lini sasa Serikali itarudisha utaratibu uliokuwepo mwanzo wa kutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo hawa ili kuweza kuwasaidia waweze kupata vifaa na baadaye waweze kufanya uchimbaji wao uwe mzuri zaidi, tuweze kuwapata walipa kodi wazuri zaidi. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kujibu swali la Mheshimiwa Masache, Mbunge wa Chunya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wakati wa nyuma Serikali ilitoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo, lakini nipende kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba utaratibu ule wa ruzuku ama haukueleweka vizuri watu walipokuwa wanachukua na haukuwa na tija yoyote katika kufanikisha malengo yaliyokuwa yamepangwa. Kwa msingi huo Wizara inaendelea kutathimini kuona kama kuna sababu ya kufanya hivyo tena iwe ni wachimbaji wetu wameelewa ili makusudi ya kutoa ruzuku hizo yaweze kufikiwa. Wakati Wizara inafikiria namna ya kufanya hivyo tena tumeona kwamba njia nyingine ambayo inaweza ikawa ni nyepesi ni ya kuyaona mabenki yetu ya ndani, ambapo Mheshimiwa Mbunge ana taarifa kwamba baadhi ya wachimbaji wadogo wadogo katika Jimbo lake la Chunya wamekwishapokea fedha kutoka kwenye mabenki yetu ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo huo ni utaratibu ambao tunadhani kwamba in the interim kabla ya kufikiria kwamba tunaweza tukawa na wakati mwingine wa ruzuku, basi twende na njia hii ambayo nayo imeanza kuonyesha dalili za kufanikiwa katika kuwasaidia wachimbaji wetu wadogo. Nakushukuru.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona changamoto ya Jimbo la Singida ziko sambamba kabisa na changamoto ambazo zinaikabili wilaya ya Chunya kwenye umaliziaji wa maboma; kuna boma lililojengwa kwa nguvu ya wananchi kwenye kata ya Ifumbo lina zaidi takribani miaka minne halijakamilika.
Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha ili ukamilishaji wa boma hili kwenye kata ya Ifumbo iweze kukamilika ilihali ukijua kata hii iko mbali sana na Makao Makuu ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu la Mheshimiwa Kasaka, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo: -
Mheshimwia Mwenyekiti, katika ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati tumeainisha maeneo ya kimkakati, na tuliwaomba Waheshimiwa Wabunge kuwasilisha vipaumbele. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge, kama Kituo cha Afya katika Kata ya Ifuko ni kipaumbele basi tupate taarifa hiyo rasmi ili tuweze kuweka mpango wa kuhakikisha kwamba tunakamilisha ili wananchi wapate huduma. Ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Changamoto ya maji Wilaya ya Chunya ni kubwa sana. Sasa naomba nimuulize swali Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Mradi wa Maji wa Kiwira umekuwa unatajwa muda mrefu na mpaka sasa utekelezaji wake haujaanza na mradi huu utafaidisha Wilaya ya Chunya pamoja na Mbeya Mjini. e, ni lini sasa Serikali itatoa fedha mradi huu uanze kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masache Kasaka, Mbunge kutoka Chunya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kumpongeza Mbunge Kasaka kwa kazi nzuri aliyoifanya Chunya, miradi ambayo ilikuwa kichefuchefu toka mwaka 2012, Mradi wa Matwiga sasa hivi upo kwenye hatua nzuri na tayari tumeshampata mkandarasi anakuja kule kwa ajili ya usambazaji wa vijiji vinne vya awali na huu Mradi wa Kiwira wiki ijayo tunakwenda kusaini mkataba ili mradi uanze utekelezaji. Hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana na kwa kazi nzuri anayoifanya Wanachunya wanakwenda kufaidika. (Makofi)
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake hayo. Nami nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Wilaya ya Chunya katika REA Awamu ya Pili tumepata vijiji 12; lakini katika vijiji 12, vijiji 10 vinapita kwenye misitu ambayo iko chini ya TFS. Sasa mradi huu unapopita, TFS imekwamisha huu mradi inasubiri mpaka iweze kupata malipo ya fidia ili mradi uweze kuendelea, kitu ambacho kinashangaza sana.
Je, ni lini sasa Serikali itakaa na taasisi nyingine ya Serikali TFS waweze kujadiliana ili malipo yaweze kufanyika na mradi huu uweze kutekelezeka na wananchi waweze kunufaika kama ambavyo wanategemea? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwenye kila kijiji kitapata transfomer ya KVA 50 ambapo usambazaji wake wake wa umeme ni wastani wa kilometa moja ambayo inahudumia takribani watu 68: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza transfomer yenye ukubwa zaidi ya KVA 50 ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na huduma hii ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia masuala ya wananchi na hasa kwenye hili eneo la fidia. Kwanza naishukuru Serikali kwamba ilishirikiana na wananchi na kuwaomba miradi yote ya REA isiwe miradi inayohitaji fidia katika maeneo ambayo miradi inapita. Nawashukuru wananchi kwa niaba ya Serikali walikubali ombi hilo kwa sababu umeme ni kwa mahitaji yetu sote.
Mheshimiwa Spika, kwanza niseme kwamba mradi wa REA hauna fidia kwa wananchi. Ila kwa wenzetu wa TFS wamekuwa wanazo kanuni ambazo zinaelekeza kwamba maeneo yao yakitaka kutumika kwa shughuli nyingine, basi fidia itolewe. Nasi mara kadhaa tumefanya mazungumzo nao ili eneo hili liondoke na kikao cha mwisho kimefanyika wiki hii na tunatarajia kabla ya mwezi huu tutakuwa tumekamilisha jambo hili, ili sasa kama ambavyo tunapeleka miradi ya umeme katika maeneo ya wananchi bila kuwafidia na TFS ambayo ni taasisi ya Serikali pia, isifidiwe kwa kutumia eneo kwa ajili ya shughuli za wananchi. Tuna uhakika jambo hili litakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika awamu hii ya pili eneo la Mbeya lakini pia Katavi, Simiyu na Morogoro yapo maeneo yanahitaji attention ya namna hiyo na tayari tunayafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye jambo la pili, ni kweli kwamba wateja ambao wamefikishiwa umeme kwa kipindi hiki, siyo wote wanaouhitaji, lakini Serikali imejitahidi sana kwa hizo shilingi trilioni moja na bilioni 250 kupeleka angalau kwa wateja wa awali katika maeneo ya mijini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wengine wote kwamba Serikali inayo mradi mwingine wa densification ambayo ni jazilizi; inayo mradi mwingine wa Peri-Urban wa kupeleka miradi ya umeme huko na pia TANESCO wanaendelea, kila mtu atapata umeme kwa kadiri Serikali inavyojitahidi kufikisha umeme katika maeneo hayo. (Makofi)
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona, Kituo cha Afya cha Mtanila, pamoja na Kituo cha Afya cha Kata ya Lupa ni vituo vya afya vya muda mrefu na vimechakaa sana. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kukarabati vituo hivi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Lupa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilifanya tathmini ya vituo vya afya, hospitali na zahanati zote chakavu sana nchini kote na tumeweka mpango wa kuanza kukarabati kwa awamu. Kwa mfano kwa mwaka huu tutakarabati hospitali 19 chakavu za wilaya, lakini tutakwenda pia kukarabati vituo vya afya chakavu na zahanati chakavu kwa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya vituo hivyo vya afya.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuweza kuniona.
Kijiji cha Shoga kilichopo Kata ya Sangambi, Kijiji cha Sipa Kata ya Kambekatoto na maeneo karibu yote ya Kata ya Upendo yana changamoto kubwa sana ya mawasiliano ya simu za mkononi; je, ni lini sasa Serikali itapeleka minara ili kumaliza changamoto hii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika majibu yangu ya msingi ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya mawasiliano ili Watanzania waendelee kutumia huduma ya mawasiliano katika biashara na mambo mengine.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maeneo ya Mheshimiwa Masache ni kwamba yameingizwa pia katika utekelezaji wa Tanzania Kidigitali katika miradi 763. Nakushukuru.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana; nimeyapokea majibu ya Serikali. Kwa kuwa kwenye jibu la msingi amesema Serikali inaruhusu shughuli za kiuchumi kuweza kufanyika kwenye eneo la misitu zikifuata sheria, lakini sheria hizi zimekuwa ngumu sana kwa wachimbahi wadogo hawa kuweza kuzi-meet ili waweze kupata hivi vibali. Je, serikali haioni haja sasa kuweza kupunguza masharti ya kutoa vibali vya kuingia ndani ya misitu ili wananchi wetu hawa waweze kupata vibali hivyo waweze kufanya shughuli zao za uchumi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali imekuwa inaendesha zoezi la kuweka beacon katika mipaka kati ya vijiji pamoja na hifadhi. Zoezi hili limeweza kufanyika katika Kata za Mafyeko, Kambikatoto pamoja na Matwiga. Zoezi hili limeweza kufanyika bila kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika.
Je Serikali haioni haja sasa kuweza kuweka bikon zile upya katika maeneo yale ya mipaka ya asili ili wananchi hawa waweze kufanya shughuli zao vizuri bila kuleta taharuki?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masache N. Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza aliloliongelea Mheshimiwa Mbunge, kuhusu kupunguza masharti ili kuruhusu wachimbaji wadogowadogo waweze kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa. Nimtaarifu tu Mbunge kwamba, masharti haya tuliyoyaweka, yanazingatia pia kuhifadhi maeneo ya misitu na masharti haya kwa wachimbaji wadogowadogo tumeyaweka ni machache sana.
Mheshimiwa spika, kwa mfano, kwa ridhaa yako napenda tu nielezee kuhusu suala la masharti ya wachimbaji wadogowadogo ambao wanapaswa kupata leseni. Pia wanatakiwa kufanya Environmental Protection Plan (EPP), ambayo huwa haifanani na EIA, ni masharti madogo ambayo yanamfanya mchimbaji aweze kufuzu ili aweze kupata kibali cha kuingia kuchimba. Kwa hiyo sisi tunaona masharti haya ni nafuu sana na tunaendelea kuhamasisha wananchi kwamba tunapohifadhi ni kwa ajili ya uhifadi endelevu na wakati huo huo tunaruhusu shughuli za uchimbaji ndani ya hifadhi.
Mheshimiwa Spika, kwenye hili zoezi la beacon, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunapokuwa tunaweka mipaka, tunashirikisha pia Wizara ya Ardhi, ambapo wanakuwepo wapima ardhi ambao wanazisoma na kutafasiri ramani ambazo zinaonyesha ramani kamili ya hifadhi husika. Endapo kama kuna mgogoro uliojitokeza, basi nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba tutawashirikisha tena Wizara ya Ardhi ili tujiridhishe na wananchi kwamba mipaka hii ni sahihi ama siyo sahihi. Kama itaonekana bikon zimewekwa nje ya mipaka hiyo, basi tutafanya marekebisho. Ahsante sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi: Kituo cha afya cha Lupa Tingatinga ndiyo kituo cha afya kikubwa zaidi kwenye Tarafa ya Kipembawe, lakini kituo hiki hakina wodi yoyote kwenye Tarafa hii. Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kujenga wodi kwenye Kituo cha Afya cha Lupa Tingatinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa kwamba, kwenye Kituo cha Afya cha Lupa Tingatinga, na bahati nzuri hili eneo nalifahamu na changamoto zake nazijua, ninajua kazi ambayo Mheshimiwa Mbunge amekuwa akipambania pale ni wananchi wake kupata wodi. Nimhakikishie tu kwamba, tutaliweka katika mipango ya Serikali ili tuhakikishe wanapata wodi na hicho kituo kiendelee kutoa huduma. Ahsante sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona. Mradi wa maji wa Matwiga phase one ni wa muda mrefu na unakwenda kwa kusuasua. Je, ni lini Serikali sasa itaukamilisha mradi huu ili wananchi wa Kipembawe waweze kunufaika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masache Kasaka, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mradi huu unafanyiwa kazi kwa jitihada kubwa sana, Mheshimiwa Mbunge naomba uendelee kuwa na subira kidogo, mambo mazuri yanafika pale.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali pamoja na kuwa imeweka utaratibu wa kutoa mikopo kupitia taasisi za kifedha, lakini mikopo hii imekuwa na masharti magumu amabyo wachimbaji wetu wadogo wengi wameshindwa kuweza kuyafikia.
Je, Serikali haioni haja sasa ya kupunguza masharti na ikiwezekana iweze kutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo ili tuweze kuwasaidia katika uchumi wa madini.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kasaka, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, masharti ya kibenki yanaonekana kuwa ni magumu kwa sababu wachimbaji wadogo hawajapata uelewa mzuri wa namna ya kujipanga kupata mikopo hii. Kazi yetu kama Wizara imekuwa ni kutoa elimu ya vigezo muhimu ambavyo wanatakiwa wazingatie ili waweze kukopeshwa au waweze kukopesheka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Wizara tutaendelea kujadiliana na mabenki na kuona namna ya kutengeneza masharti rafiki na rahisi kueleweka ili wachimbaji hawa waweze kupata mikopo bila usumbufu. (Makofi)
Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, swali la nyongeza.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Msitu wa Mbiwe ilianza rasmi mwaka 1995, wakati shughuli za kibinadamu za kiuchumi katika mamlaka ya Mji Mdogo Makongolosi hasa kilimo zilikuwa zinafanyika: -
Je, Serikali haioni haja sasa kwa kipindi hiki kuweza kuweka utaratibu maalum kama ilivyofanya kwenye uchimbaji wa madini ili na hawa wananchi wanaoshughulika na shughuli za kilimo waweze kufuata hizo taratibu waweze kufanya shughuli zao za kilimo kwenye maeneo yanayofaa kwa kilimo?
Swali la pili, Wilaya ya Chunya imekuwa muhanga wa kupokea wahamiaji wengi waliotoka maeneo mbalimbali walikofukuzwa huko hasa maeneo ya Usangu pamoja na Wilaya ya Songwe: -
Je, Serikali haioni haja sasa kuweza kuona utaratibu maalum hawa wananchi ambao wametoka kwenye maeneo hayo, wanafika Wilaya ya Chunya na kuharibu mazingira hasa na mifugo yao kuweza kuingia kwenye maeneo ya mashamba kuweza kutoa tamko rasmi ili wananchi wetu wale wasiweze kuathirika na mifugo hiyo inayoingia ndani ya Wilaya ya Chunya.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masanche Njeru Kasaka Mbunge wa Rupa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu wa kuruhusu shughuli za kilimo ndani ya hifadhi, taratibu na kanuni zinaelekeza kwenye uapnde wa misitu ya TFS kwamba kunapokuwa na uchimbaji wa madini basi wale wachimbaji wanaruhusiwa kuchimba na wakati huohuo kurudishia miti ili kuendelea kuhifadhi maeneo hayo. Kwa hiyo, sheria na taratibu zinazoongozwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ni kwamba hairuhusiwi kufanya shughuli za kilimo isipokuwa uchimbaji wa madini, ambalo ni eneo maalumu lililo ndani ya hifadhi ya misitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu wahamiaji, binadamu au wananchi kulingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haimzuii mwananchi yoyote kuishi eneo lolote analohitaji. Katiba inaruhusu mtu yoyote kuishi pale ambapo anaona panafaa, isipokuwa kwa wale ambao wanavamia maeneo ya hifadhi sheria na taratibu zitafuatwa ikiwemo kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nawaomba wananchi waheshimu maeneo ya hifadhi kwa mustakabali wa Taifa letu na kwa faida ya wananchi wenyewe.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, barabara ya Mokongorosi - Rungwa imeahidiwa kwa muda mrefu, je, ni lini Serikali itatoa fedha ili kipande cha Makongorosi kianze kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE: Mheshimiwa Spika, tumeshaanza upande wa Itigi na bajeti itakayofuata tukishapitishiwa tutaanza upande mwingine wa Makongorosi kwenda Itigi, ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kituo cha Afya cha Chalangwa kimekamilika muda mrefu pamoja na jengo la Mochwari limekamilika, lakini mpaka sasa hivi hakuna majokofu wala vifaa tiba: Je, Serikali inatuahidi nini kupeleka vifaa tiba hivi pamoja na jokofu kwenye Kituo cha Afya cha Chalangwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masache Kasaka Mbunge wa Jimbo la Lupa kama ifuatavyo: -
Ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Chalangwa kimekamilika na ni miongoni mwa vituo afya ambavyo vimetengewa fedha ya vifaa tiba mwaka ujao 2022/2023 ikiwemo jokofu kwa ajili ya chumba cha kuhifadhia maiti.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Na mimi napenda kuuliza swali moja la nyongeza; Shule ya Msingi Chunya Mjini pamoaja na Shule ya Msingi Chunya Kati ni shule kongwe ambazo zilikuwepo tangu kabla nchi yetu haijapata uhuru. Shule hizi zimechakaa sana baaddhi ya majengo yameanguka.
Je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha ili ukarabati wa majengo hayo uweze kufanyika na ziweze kurudi katika hali kama shule nyingine ambazo zinajengwa sasa hivi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masache Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Lupa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kitu kikubwa ambacho nikukuhakikishie tu kwamba miongoni mwa shule ambazo ziko katika mpango hizi ni mbili ambazo umezianisha Mheshimiwa Mbunge, na tutahakikisha baada ya tathmini tutazipa kipaumbele ili kuhakikisha kwamba zinajengwa. Ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuweza kuniona. Barabara ya kutoka Matundasi kuelekea Itumbi imeharibika sana baada ya mvua hizi ambazo zinazoendelea kunyesha.
Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha changarawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masache Kasaka, Mbunge wa Chunya, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara hii ya Matundasi mpaka Itumbi ni kweli ipo chini ukilinganisha na usawa wa barabara yenyewe na ardhi ya pembezoni, tayari katika mwaka huu wa fedha wa 2023/2024 barabara hii imeombewa fedha na ukarabati wake utaanza ili kuweza kuinyanyua.
MHE. MASACHE J. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kuniona. Barabara inayoanzia Chunya Mjini kupita Igundu mpaka Sangambia ambako itaunganisha na Mbarali kwa kipindi hiki imeharibika sana kutokana na changamoto za mvua. Je, ni Serikali itatenga fedha hili barabara hii ijengwe kwa kiwango cha changarawe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA ina bajeti ya bilioni 11 kwa ajili ya dharura na hivi sasa maombi tayari yamefanyika kwa ajili ya kuongeza bajeti hii kwenda bilioni 46 ili kuhakikisha wana fedha ya kutosha kuweza kutengeneza barabara hizi wakati wa dharura. Kwa sasa tutaangalia barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge kuona katika mwaka fedha unaoenda kuanza tarehe 1, Julai inapewa kipaumbele cha kutengenezwa.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini kiasi cha fedha ambacho kimetengwa takribani Milioni 50 tunashukuru, isipokuwa kiasi hiki ni kidogo sana kuweza kumaliza gereza hili. Swali la kwanza; kwa kuwa Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani bado haijasomwa, je, hatuwezi tukaongeza hizi fedha ili gereza hili liishe kwa wakati?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa gereza hili linakwenda kuisha, sasa ni muda muafaka kuweza kupata vitendea kazi vya ofisi pamoja na gari. Je, Serikali inatuahidi nini ili tuweze kupata vitendea kazi hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunatambua ni kiasi kidogo Mheshimiwa Mbunge, lakini tulisema pamoja na ufinyu wa bajeti angalau gereza lile uendelezaji wake usisimame. Hata hivyo, nimuahidi tu kwamba kipaumbele baada ya mwaka huu 2023/2024 mwaka unaofuata 2024/2025, tutaongeza fedha za kutosha ili angalau ujenzi wake uwe wa kasi kubwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umuhimu wa kuwepo vitendea kazi, ofisi tumesema inaendelea kujengwa na gari tutapeleka kutokana na bajeti yetu itakavyoruhusu, ahsante sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwanza niseme sijaridhishwa na majibu ya Serikali kwa namna ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyasema. Kwa sababu tarehe 17 mwezi huu, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi akiwa Singida akisaini mikataba aliitaja barabara yetu ya Makongolosi kuelekea Mkiwa kuwa na yenyewe itajengwa kwenye mradi huu wa barabara ambazo amezitaja hapa lakini majibu ya Serikali yanaonekana kugongana.
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hayo niweze kuuliza sasa. Kwa sababu Mheshimiwa Waziri, alikwishasema fedha zipo za kuweza kujenga zaidi ya kilometa 2300. Je, ni lini sasa Serikali itatoa pesa hizi ili barabara yetu ya Makongolosi kwenda kuunganishwa mpaka Mkiwa iweze kujengwa kwa kuwa barabara hii ni muhimu sana kiuchumi kuunganisha Mkoa wa Mbeya na Singida?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara ya kuanzia Makongolosi kupita mpaka Mkwajuni mpaka Mbalizi ni barabara ya vumbi na imeahidiwa muda mrefu kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami na tayari Serikali imeshatenga kilometa 50 kuweza kujengwa. Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kuanzia Makongolosi hadi Mkwajuni ili iweze kuunganishwa mpaka Mji mdogo wa Mbalizi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Njelu Kasasa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Lupa, kwa kufuatilia barabara hii ambayo ni shortcut ya kwenda katika Mkoa wa Mbeya kutokea Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara hii kama nilivyokwisha jibu kwenye majibu yangu ya awali yenye kilometa 503, tumekuwa tukijenga awamu kwa awamu. Pia hadi sasa tumesaini mkataba wa kipande hiki cha Noranga - Doroto kilometa sita na Itigi – Mkiwa kilometa 25.6. Maana yake nini? Maana yake tunaendelea na ujenzi mpaka Makongolosi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, nikuhakikishie ya kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi itaendelea kujenga barabara hii na katika mwaka wa fedha ujao pia tumetenga fedha kwa ajili ya kutoka Makongolosi kwenda Singida.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, barabara ya Makongolosi – Mbalizi. Barabara hii imekuwa ikitengewa fedha kila mwaka na mwaka huu imetengewa kilometa 50 na mwaka ujao pia tumewekea fedha za kuanza ujenzi wa barabara hii. Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba barabara hii katika mwaka ujao wa fedha itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kituo cha Afya cha Kata ya Ifumbo ni kituo cha afya cha muda mrefu na kinajengwa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri. Je, ni lini Serikali itatoa fedha ya kituo hiki kiweze kukamilika na Wananchi wa Ifumbo waweze kunufaika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masache Kasaka, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ina utaratibu wa ujenzi wa vituo vya afya kwa kutumia nguvu za wananchi. Niwapongeze Wananchi wa Kituo cha Afya cha Ifumbo lakini tunaendelea kusisitiza kwamba kupitia mapato ya ndani watenge ile asilimia 20, 40 na 60 kwa ajili ya kukamilisha vituo hivi. Endapo halmashauri haina uwezo huo walete andiko hilo ili Serikali iweze kuchangia fedha kwa ajili ya kukamilisha kituo hicho, ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona. Katika Wilaya ya Chunya zipo Kata chache za kimkakati ambazo hazina vituo vya afya. Je, ni lini Serikali itatenga na kupeleka fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya afya kwenye Kata za Luwalaje, Upendo na Kata ya Chokaa katika Kijiji cha Mapogoro? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Chunya kwa kuwa na taarifa ya vituo vyake vya kimkakati kama walivyo Waheshimiwa Wabunge wengine. Wameshazileta Ofisi ya Rais, TAMISEMI Serikali inaendelea kutafuta fedha ili ujenzi kwa awamu katika maeneo haya ufanyike. Tutatoa kipaumbele katika Kata ambazo umezitaja, ahsante. (Makofi)
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naishukuru Serikali kwa majibu mazuri na tunaona namna ambavyo wanatuunga mkono na sisi tunasema ahsante. Tunaiomba tu Serikali tuweze kupata hizi fedha kwa wakati ili hivi Vituo vya Polisi viweze kukamilika.
Nina maswali mawili madogo ya nyongeza; Kituo cha Polisi cha Chunya Mjini ni Kituo cha Polisi cha zamani toka ukoloni, kidogo na kiko ndani ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya; je, ni upi mpango wa Serikali kuwezesha kujengwa kituo kikubwa cha Polisi chenye hadhi ya wilaya katika Wilaya yetu ya Chunya?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Wilaya ya Chunya ina changamoto kubwa ya nyumba za askari; je, ni upi mpango wa Serikali kuweza kujenga nyumba za askari ili waondokane kuishi katika mazingira magumu katika Wilaya ya Chunya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni mpango wa Wizara kupitia Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba Wilaya zote nchini zinapata vituo vyenye hadhi ya Wilaya ambavyo vitakuwa na OCD, OC-CID, askari wa idara nyingine na askari wa kawaida ili kuwezesha ulinzi wa raia na mali zao. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali kulitekeleza hili bado ipo na nikuahidi kwamba katika mpango wake wa miaka 10 ambapo sasa hivi miaka miwili imepita ya ujenzi wa vituo hivi, tutahakikisha kituo cha wilaya yako kinaingia katika mpango angalau mwaka ujao.
Mheshimiwa Spika, kuhusu nyumba tumwombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunapojenga Kituo cha Polisi cha ngazi ya Wilaya au vituo vya Polisi daraja C ngazi ya kata na tarafa, tuhakikishe eneo linakuwa kubwa la kutosha kwa ajili ya kujenga kituo pia na makazi ya askari na viongozi wao. Kwa hiyo, wilaya ikituhakikishia uwepo wa viwanja hivyo tutaingiza kwenye mpango wa ujenzi wa kituo pamoja na nyumba, ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwa Mkoa wa Mbeya kuna shule nyingi kongwe ambazo zimechakaa sana zinahitaji ukarabati mkubwa. Je, lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule hizi ndani ya Mkoa wa Mbeya lakini na kwa Tanzania kwa ujumla?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ndani ya Wilaya ya Chunya tuna shule kongwe ambazo zipo toka enzi za mkoloni lakini Serikali ilisema itatoa fedha na mpaka sasa hivi haijatoa fedha kwa ajili ukarabati.
Je, lini Serikali itatoa fedha hizo ili ukarabati uweze kufanyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasaka, kwanza kuhusu shule kongwe lini Serikali itakarabati shule hizi Mkoani Mbeya. Niseme tu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitafuta fedha kwa ajili ya kuanza ukarabati wa shule kongwe na tayari shule kongwe 84 hapa nchini zimekwisha karabatiwa ikiwemo nyingine zilizo katika Mkoa wa Mbeya. Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ukarabati wa shule hizi kongwe hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maelezo yanaenda pia kwenye swali lake la pili la shule kongwe kule Wilayani Chunya, tutaangalia katika awamu inayofuata ya ukarabati wa shule kongwe tuweze kuweka kipaumbele vilevile katika shule kongwe ambazo zilijengwa na mkoloni kule Wilayani Chunya.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kituo cha Afya cha Matwiga, Isangawana na Mafyeko vilipata milioni mia tatu kila kituo na ujenzi wake ulishaanza;
Je, ni lini Serikali itatoa fedha ili vituo hivyo viweze kumalizika na baadaye wananchi waweze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masache Kasaka Mbunge wa Lupa; changamoto iliyojitokeza kule Wilayani Chunya ilikuwa kwamba fedha ilipelekwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya kimoja. Wao wenyewe walikaa kwenye Baraza la Madiwani wakaamua kugawanya fedha ile na kuanzisha ujenzi wa vituo vya afya viwili. Ni mategemeo yangu kwamba walipopitisha maamuzi yale walijua wana mapato ya kutosha kwa ajili ya kumalizia vituo vya Afya hivi vya Isangawana na Mpepo kule. Lakini nitakaa na Mheshimiwa Kasaka kuona ni namna gani tunaweza tukakaa, tukazungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ili waweze kumalizia maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro ule ulianzishwa na wao wenyewe Madiwani kwa kugawanya fedha iliyotolewa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kimoja.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini sisi tunapenda kujua kwamba Serikali mradi huu wa maji wa Skimu ya Kata ya Ifumbo ulianza toka mwaka 2006 ni mradi wa muda mrefu na umetumia fedha nyingi sana za Serikali na kila siku Serikali imesema itakuwa inatenga fedha.
Je, ni lini sasa Serikali itatenga fedha kwa ajili ya mradi huu uweze kuanza?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mto Lupa unaopita kwenye kata nyingi pamoja na vijiji vingi una maeneo mazuri sana yanayofaa kwa kilimo cha umwangiliaji.
Je, Serikali haioni haja sasa ya kutuma wataalamu wake waweze kulitembelea hili bonde na baadaye waweze kuweka kwenye mpango na baadaye skimu iweze kujengwa kwenye Kata ya Mto Lupa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Rukwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli tunatambua kwamba mradi huu ulikuwa ni wa muda mrefu na iko kazi ambayo inapaswa kufanyika ikiwemo ya ukarabati wa mfereji mkuu tumebakiza mita 750, lakini na mifereji ya shambani. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ya umuhimu wa mradi huu tutaangalia pia vyanzo vingine vya fedha kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji ili tuweze kukamilisha maeneo machache yaliyobaki ili wananchi waweze kutumia eneo hilo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji hasa hekta 141 ambazo zimebaki.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la kuhusu kuwatuma wataalam, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba ndani ya wiki hii watendaji wa Tume ya Umwagiliaji nchini watakwenda kuangalia eneo hilo ili pia waje watushauri namna ya kuweza ya kuweza kutekeleza skimu hiyo. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Vijiji vya Upendo, Kijiji cha Shoga pamoja na Sipa vina changamoto kubwa sana ya mawasiliano. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba, vijiji hivi vinaweza kupata mawasiliano katika mwaka wa fedha unaokuja?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasaka, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu niliyoanza nayo mwanzo, mwaka huu wa fedha tumetenga minara mingi kidogo, lakini kwa maana ya eneo maalum analotoka Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ya shughuli za kiuchumi zilizopo kwenye eneo hili tunazipa kipaumbele cha pekee. Kama katika orodha yetu tuliyoitoa wakati wa bajeti hizi kata na maeneo aliyoyataja hayamo, basi na yenyewe tutayaingiza kwenye orodha ya yale maeneo maalum, kwa sababu ya shughuli nyingi za kiuchumi ambazo zinafanyika kwenye eneo lake na sisi tuko tayari kushirikiana kusaidia katika ujenzi wa uchumi wa kidigitali, kwa maana ya kwamba, ule uchumi unaofanyika kwenye eneo lake uingie katika mfumo wa jumla wa uchumi wa kidigitali.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kuweza kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mbea ni miongoni mwa majiji makubwa katika nchi yetu ya Tanzania, lakini mapka sasa hatuna stendi yenye hadhi ya jiji.
Je, ni lini sasa Serikali itajenga stendi yenye hadhi ya jiji kwenye mkoa wetu wa Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kasaka, Mbunge wa Jimbo la Lupa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Jiji la Mbeya ni jiji kubwa, lakini bado tunachangamoto ya stendi inayofanana na hadhi ya Jiji la Mbeya, lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Tulia Ackson, Mbunge wa Mbeya Mjini pia amekuwa akifuatilia sana suala hilo nakushukuru sana kwa kumuunga mkono, lakini Serikali inafanya tathimini na tumeshaelekeza Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuleta andiko la mapendekezo ya kujenga stendi ili tuone kama wanaweza kujenga kwa mapato ya ndani au kama mradi wa kimkakati ili Serikali tutafute fedha kwa ajili ya ujenzi huo. Ahsante.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, tunaishukuru Serikali ndani ya muda mfupi imeweza kujenga maghala takribani kumi ndani ya Wilaya ya Chunya kwa ajili ya baruti. Lakini maghala haya yapo pale Chunya mjini na maeneo ya uchimbaji wa dhahabu yako kule vijijini.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba vibali hivi vinaweza kuwafikia wale wafanyabiashara wa baruti kwenye maeneo yale ya uchimbaji kule vijijini?
Swali la pili kwa mujibu wa majibu ya Mheshimiwa Waziri, Serikali imeshaingia Mkataba wa Minamata kwa ajili ya kupunguza matumizi ya zebaki na baadaye kuitokomeza kabisa. Lakini kwa kipindi hiki cha mpito matumizi ya kemikali hii ya zebaki bado inaendelea kutumika kwa ajili ya kuchenjua na ukamatishaji dhahabu.
Je, Serikali ina mpango gani kutoa elimu kwa wachimbaji hawa wadogo wa dhahabu ili madhara yasiendelee kutokea zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasaka kama ifuatavyo: -
Kwa upande wa swali lake la kwanza napenda kumfahamisha kwamba Serikali imeendelea kuboresha utaratibu wa kuweka urahisi wa upatikanaji na matumizi ya baruti katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kufikia mwaka huu mwezi huu wa sita Waziri wa Madini kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa kifungu cha (8) cha Sheria ya Baruti ya mwaka 1963 Sura ya 45 amepewa mamlaka ya kutoa leseni kwa viwanda vya kutengeneza baruti hapa nchini na tayari kuna viwanda vitatu vimeshapewa hiyo leseni ya kuzalisha baruti jambo ambalo limepelekea kuwepo kwa upatikanaji wa zebaki kwa wingi nchini, lakini sambamba na hilo kifungu Na. 4 cha Sheria ya baruti Sura ya 45 imempa Waziri mamlaka ya kuteua wakaguzi wa baruti na hao sasa wameshateuliwa na wako katika kila Ofisi ya Madini ya Mikoa yetu yote ya madini nchini na wanafanyakazi chini ya Kamishna wa Madini ambaye anawapa kibali cha kutoa leseni za store na masanduku ya kuhifadhia baruti.
Mheshimiwa Spika, kana kwamba hiyo haitoshi, pia anawapa kibali cha kuweza kutoa leseni na mpaka sasa hivi tuna leseni 256 za maghala yaani magazine, leseni 338 za store yaani store yenyewe na leseni 114 za masanduku (storage boxes) ya kuhifadhia baruti na Kamishna kwa kutumia hawa wakaguzi wa baruti amewapa mamlaka ya kushirikiana na ofisi zetu za madini kila mkoa kuhakikisha kwamba baruti zinawafikia wachimbaji wadogo kwa njia iliyo salama na kwa njia rahisi kabisa kupatikana karibu na maeneo ya migodi.
Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili ambalo anataka kujua kwamba hii zebaki sasa ambayo ni hatarishi kwa mazingira iko katika mikakati ya kwenda kuondolewa matumizi yake, lakini kwa kipindi hiki cha mpito kabla haijaondolewa matumizi yake Serikali inafanya nini kutoa elimu, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka sasa hivi Wizara imeshatoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo zaidi ya 600 na namna salama ya kutumia zebaki.
Katika Mkoa wa Shinyanga tumetoa elimu hiyo katika maeneo ya Mwimbe, Mwambomba, Kalole, Zambazare na Mwakitolyo na katika mwaka huu wa fedha ambayo bajeti yake inakwenda kusomwa leo Bungeni, tunategemea kuendelea kutoa elimu hiyo katika mikoa yote ya kimadini nchini ikiwemo Songea, ikiwemo Chunya, ikiwemo Songwe, Singida, Geita na maeneo mbalimbali ili wachimbaji wadogo waweze kutumia zebaki kwa makini mpaka hapo njia za mbadala zitakapopatikana, ahsante sana.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru; Wilaya ya Chunya ina changamoto ya upungufu mkubwa sana wa watumishi hasa kwenye sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya; je, ni lini Serikali itatupatia watumishi wa kutosha kwenye sekta hizi hasa kwenye ajira ambazo zinafuata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masache Kasaka. Tutaweka kipaumbele vilevile katika hizo ajira mpya zinazokuja katika maeneo kama vile Chunya anakotokea Mheshimiwa Kasaka.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu ya Serikali. Kwa kuwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia akiwa Mkoani Singida akizindua barababra alitoa maelekezo barabara hii ya kuanzia Makongolosi mpaka Mkiwa ianze kujengwa.
Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza maelekezo hayo barabara hii ianze kujengwa kuanzia makongolosi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Barabara ya kuanzia Makongolosi kupita Mkwajuni, Wilaya ya Songwe mpaka Mbalizi imekuwa inaahidiwa mara nyingi kuanza kujengwa.
Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kutosha barabara hii na yenyewe ianze kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyosema katika jibu la msingi, tunatambua kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Singida kwenye ziara alitoa maelekezo kwa Wizara ya Ujenzi kuhakikisha kwamba tunaijenga barabara hii yote kwa kiwango cha lami. Tunachofanya sasa hivi Serikali, barabara hii ilishakamilishwa usanifu. Tunaendelea kutafatuta fedha ili kutimiza hayo maelekezo ya Mheshimiwa Rais. Hata hivyo tulitenga kiasi cha fedha kwenye bajeti kwa ajili ya kuanza kwa awamu lakini sasa maelekezo ya Mheshimiwa Rais yatazingatiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake sehemu ya Makongolosi kwenda Mkwajuni, barabara hii imeshatengewa fedha kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi kwa kipande cha kutokea Mkwajuni kuja Makongolosi.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona, Kituo cha Afya cha Mji Mdogo wa Makongolosi kimekamilika na kimeanza kutoa huduma, lakini hakina nyumba za madaktari. Chama Cha Mapinduzi Kata ya Bwawani Makongolosi wameanzisha ujenzi wa nyumba za madaktari.
Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha ili nyumba hizi za madaktari ziweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuwapongeza wananchi kwa kushirikiana pamoja kuhakikisha kwamba wanaunga mkono jitihada za maendeleo na kwa kuanza ujenzi wa miundombinu hii muhimu.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama vile ambavyo Serikali imekuwa ikiunga mkono jitihada mbalimbali za kuboresha miundombinu na hasa katika sekta ya afya na kuunga mkono tafsiri yake ni kupitia miradi kutoka Serikali Kuu, lakini pia kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, nikuhakikishie Serikali kwa utaratibu huo huo itaendelea kuhakikisha kwamba fedha zinapatikana kwa ajili ya kuunga mkono miradi ambayo inaenda kugusa miundombinu muhimu ya afya.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Matwiga, awamu ya pili ambao ulianza toka 2012 unaenda kwa kusuasua sana. Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kutosha ili Vijiji vya Mazimbo, Mtanila, Ifuma na Lupa viweze kupata maji haya? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa mradi huu ulianza mwaka 2012, lakini unaenda kwa awamu. Awamu ya kwanza unahusisha vijiji viwili vya Matwiga pamoja na Isagawana na awamu hiyo ishakamilika tayari, wananchi wanapata maji. Awamu ya pili ambayo inahusisha vijiji sita, upo katika asilimia 90. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa na subira, mradi huu utakamilika mwaka huu wa fedha na wananchi watapata maji.
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji ya Chimala pamoja na Ruiwa, pamoja na kwamba utekelezaji wake umeanza, lakini unakwenda kwa kusuasua. Je, ni lini Serikali itatoa fedha ya kutosha ili miradi hii iweze kukamilika kwa wakati?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwenye Wilaya ya Chunya Serikali iliweza kuchimba visima 16 na tunashukuru kwa hilo. Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha kwenye Vijiji vya STAMICO, Upendo, Lualaje, Supermarket, Sipa na Nkwangu ili miradi hii iweze kutekelezeka na wananchi hawa waweze kunufaika na mradi wa maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Kasaka kwa swali ambalo ameuliza, lakini pia kuhusu upande wa Chunya amekuwa akifuatilia sana maeneo haya kuhakikisha kwamba katika vile visima 16, basi vinaendelea kutoa maji lakini katika vijiji ambavyo amevitaja, tunaendelea kuviweka katika mpango kuhakikisha kwamba vinapata huduma safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Chimala, kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, Serikali inaendelea kupeleka fedha kwa kadiri zinavyopatikana ili kuhakikisha kwamba miradi yote nchini ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji inakamilika na kuanza kutoa huduma ya maji safi na salama.