Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MAULID SALEH ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai, afya njema kuweza kukutana hapa, lakini vilevile niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Welezo kwa kunichagua kwa wingi na kunipa imani kubwa ili niwe mtumishi wao, lakini vilevile nimshukuru sana na kumpongeza Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kutupa matumaini makubwa kabisa kuendeleza yale ambayo yameachwa na Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake wa bajeti yake hii nzuri. Nimpongeze Katibu Mkuu, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, lakini na Makamanda wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nianze kwa kuchangia bajeti hii kwanza kwa kuanza na ile dhimay a Wizara. Dhima ya Wizara hii ni kuendeleza juhudi, kulinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya adui na aina yoyote katika ndani na nje ya nchi yetu, lakini vilevile niwapongeze sana jeshi letu kwa kuwa makini na kuonesha umahiri makini katika kutekeleza majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimeona bajeti yao hii fedha zile ni kidogo. Niiombe Serikali iwaongezee fedha hizi kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao, lakini hasa kuweza kupata zana zile za kisasa, kuboresha maslahi yao na makazi. Kama wao wametuahidi kulinda na kuitetea nchi yetu kwa muda wote ule, basi na sisi lazima tuwatetee maslahi yao, ili kuwa na hamu ya kuweza kulinda nchi yetu kwa makini kabisa. Na hii inasababisha nchi yetu kupata maendeleo makubwa. Bila ya jeshi hili kulinda amani na mipaka yake basi hatuwezi kuleta maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitagusa kidogo kuna huduma zile za afya, bahati nzuri na mimi nimebahatika kule katika jimbo langu ninacho Kikosi cha 672 ambacho tuna hospitali, lakini hospitali ile kidogo haiko vizuri ingawa inatoa huduma, lakini niombe Serikali sana ipeleke dawa zile na kuboresha kile kituo maana hakiko katika hali nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nimeona na mavazi yao, kidogo; unajua wanafanya kazi ngumu sana, lakini ukiangalia yale mavazi yao kidogo yaani siku zote mimi siku hiyo nakwenda kule, basi tujitahidi kidogo Mheshimiwa Waziri angalau wawe na sare tatu, nne waweze kubadili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nitilie mkazo katika ujenzi na uboreshaji wa Hospitali ya kule Bububu. Ni kweli viongozi wetu endapo itatokea wamepata maradhi kidogo kwa kule kwetu shida, mpaka wasafirishwe waletwe Tanzania Bara. Niombe Serikali iboreshe, hususan Hospitali ile ya Bububu ili viongozi wetu hawa wanapokwenda pale wapate matibabu mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile niwapongeze sana vijana wa JKT kwa kupata mafunzo mazuri ili kuweza kupunguza ule ukali wa maisha na hii niombe Serikali iwape mitaji pale ambapo wanapomaliza tu kule basi wanapokuja uraiani huku wapate nyenzo ili waendelee na maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache niwapongeze sana kwa kuchapa kazi vizuri, kwa bidii, uvumilivu, uzalendo,uadilifu na utii na nidhamu ya hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MAULID SALEH ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia uhai na afya njema ya kuweza kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kuendeleza vyema vyombo vyetu hivi vya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)
Vilevile nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Lawrence Tax, kwa kazi nzuri anayofanya akishirikiana na Katibu Mkuu Dkt. Faraji Mnyepe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika lakini vilevile nimpongeze sana Mkuu wa Majeshi - Jenerali John Mkunda na nimpongeze msaidizi wake, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi - Luteni Jenerali Othman. Vilevile niwapongeze Makamanda, Wakuu wa Kamandi wote, maafisa wakubwa na maafisa wadogo wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuchangia na nitachangia mambo mawili; jambo la kwanza, kuhusu upatikanaji wa fedha za maendeleo katika jeshi letu hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika jeshi letu linafanya kazi kubwa na nzuri sana ya kulinda mipaka yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika fedha za maendeleo ya jeshi letu hili lililopo chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kiukweli fedha walizopokea ni kidogo sana...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge masuala ya pesa zote mwisho wa bajeti ya Serikali ni mwezi wa sita na hoja zote za mapato na maingizo ya pesa kwenye Wizara zipo kwenye Kamati ya Bajeti, naomba uchangie maeneo mengine, masuala yote ya pesa zitalipwa na zipo kwenye Kamati ya Bajeti. (Makofi)
MHE. MAULID SALEH ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, saw ana nikushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe Serikali ipeleke fedha kwa wakati ili watekeleze majukumu yao kwa muda waliyojiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine kuna madeni, niiombe Serikali iweke mpango mkakati wa kuyafuatilia madeni haya ili iweze kuyalipa kwa Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nilipongeze Shirika la Mzinga kwa uvumbuzi wa bomu hili baridi la kufukuza tembo. Tembo hawa wamekuwa wakiathiri sana uchumi wa maendeleo katika nchi yetu, lakini niipongeze tena Serikali hususani shirika hili kwa ubunifu wao na umahiri wao wa kuweza kuleta teknolojia hii ambayo nchi yetu itanufaika kwa maendeleo zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali hasa Wizara ya Fedha kuwa na mpango mzuri wa kupeleka fedha kwa wakati ili mashirika yetu haya yaweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru sana watendaji wote wa Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Ulinzi la Kujenga Taifa na nimpongeze sana Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa umahiri wake na umakini wake wa kuweza kuwa nchi yetu ipo salama zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)