Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Maulid Saleh Ali (4 total)

MHE. MAULID SALEH ALI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzuia Hati za kusafiria kwa Wakandarasi wanaoingia nchini kutekeleza miradi mbalimbali?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Saleh Ali, Mbunge wa Welezo, kama ifuatavyo: -

Mheshimwa Spika, Serikali haina mkakati wa kuzuia hati za kusafiria kwa Wakandarasi wanaoingia nchini kutekeleza miradi mbalimbali isipokuwa inafanya hivyo kwa mujibu wa sheria pale inapohitajika. Serikali kupitia Sheria ya Uhamiaji Sura Na. 54 rejeo la mwaka 2016, imeipa mamlaka Idara ya Uhamiaji kuweza kushikilia au kuzuia kitu chochote ikiwa ni pamoja na nyaraka yoyote ambayo inaweza kuonyesha au kuthibitisha uvunjifu wa sheria.
MHE. MAULID SALEH ALI aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kudhibiti utapeli unaofanywa kwa kutumia namba za simu za nje?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Saleh Ali, Mbunge wa Jimbo la Welezo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, utapeli ama kwa lugha nyingine ni udanganyifu unaofanywa kwa kutumia simu za nje hudhibitiwa kwa kushirikisha Mamlaka za Udhibiti kwenye nchi ambako namba zinazotumika zimegawiwa. Mamlaka hizo huchukua hatua stahiki kwa kadri wanavyopokea taarifa zinazohusiana na utapeli huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni Mwanachama wa Jumuiya za Kikanda na Kimataifa kama vile ATU, EACO, CRASA, CTO, ITU, UPU, PAPU na kadhalika. Ushirikiano uliopo kupitia Jumuiya hizi husaidia sana kwenye utatuzi wa masuala mengi yakiwemo yanayohusu utapeli unaofanyika kwenye mitandao ya simu.
MHE. MAULID SALEH ALI aliuliza: -

Je, Serikali imefikia hatua gani ya kuziunganisha na Mfumo wa NIDA taasisi zote za umma na binafsi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Saleh Ali, Mbunge wa Jimbo la Welezo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya majukumu ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ni kuanzisha na kutunza kanzidata ya taarifa za watu na kushirikishana taarifa hizo na taasisi nyingine za umma na binafsi ili kutatua changamoto za utambuzi katika shughuli za kiuchumi, kijamii na kiusalama. Kuanzia mwezi Julai, 2020 NIDA ilipoanza kuunganisha taasisi na kanzidata yake hadi tarehe 6 Januari, 2024 jumla ya taasisi 96 za Serikali na Binafsi zimeunganishwa na kanzidata ya NIDA ambapo taasisi 44 ni za Serikali na taasisi 52 ni za binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa NIDA ni kuendelea kutoa elimu na kuunganisha taasisi 200 ifikapo mwezi Juni, 2026. Kasi ya uunganishaji inatarajiwa kuongezeka kufuatia utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya tarehe 10 Agosti, 2023 ya kutumika kwa namba moja (namba jamii) katika kumtambua mtu wakati wa kumpatia huduma, badala ya mtu mmoja kuwa na namba zaidi ya moja, ahsante.
MHE. ALI JUMA MOHAMED K.n.y. MHE. MAULID SALEH ALI aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kudhibiti mfumo wa makosa ya kimtandao (cyber crime) ili yasitokee nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, uhalifu wa makosa ya mtandaoni unasimamiwa na Sheria Na. 14 ya Mwaka 2015 na ndiyo Sheria inayodhibiti makosa haya. Sheria inaelekeza matumizi sahihi ya mtandao na imeainisha adhabu kwa makosa ya matumizi mabaya ya mtandao. Serikali katika kuimarisha udhibiti wa makosa ya mtandaoni imeanzisha mkakati wa Taifa wa udhibiti wa usalama mtandaoni wa kuanzia mwaka 2022 – 2027.

Mheshimiwa Spika, mkakati huu utawatumia wataalam mbalimbali katika kuratibu ugunduzi, kuzuia, kukataza, kufanya uchunguzi wa majibu na kuandaa mashitaka ya uhalifu. Pia, kuimarisha mazingira ya matumizi ya mtandao na kuboresha sheria iliyopo, kulinda huduma muhimu za habari, kuendeleza ujuzi kwa wafanyakazi na usalama mtandaoni, kutoa elimu kwa wadau na kuweka ushirikiano wa Serikali, wafanyabiashara na watu binafsi ili kudhibiti matukio ya uhalifu mtandaoni, ahsante.