Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Maulid Saleh Ali (3 total)

MHE. MAULID SALEH ALI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwa kuwa kumekuwa na wakandarasi wengi kutoka nje ambao wanatekeleza miradi yao nchini bila kutekeleza miradi hiyo kwa wakati; je, Serikali haioni haja sasa ya kuweza kudhibiti passport za Wakandarasi hao mpaka watakapomaliza miradi hiyo kwa wakati? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa maulid Saleh, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tatizo la Wakandarasi kutokutekeleza miradi ni la kimikataba na pia linahusisha mamlaka nje zaidi ya Uhamiaji. Kwa hiyo, hatua za kudhibiti zinaweza kuwa nyingi kulingana na mkataba husika. Hata hivyo, kama nilivyoeleza katika jibu langu katika swali la msingi, kwamba pale ambapo Jeshi la Uhamiaji linahitajika kutumia sheria hii ambayo nimeiorodhesha hapa ambayo inaipa mamlaka kufanya hivyo kwa ajili ya maslahi mapana ya Taifa, kwa misingi ya sheria hii ambayo nimeizungumza, ikihitajika kufanyiwa hivyo; na imeshafanya hivyo mara kadhaa, lakini haiwezi ikatoka ikasema kila mradi ambao haujakamilika, basi twende tukakamate passport bila kufuata utaratibu.
MHE. MAULID SALEH ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Nitakuwa na swali moja la nyongeza.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha mfumo wa TEHAMA na kudhibiti usalama wa mawasiliano nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maulid Saleh Ali, Mbunge wa Welezo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita inaongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari imeshatoa mkakati (National Cyber Security Strategy) ya mwaka 2018, mwaka 2023 ambao ni kuhakikisha kwamba kuna usalama katika huduma zote zinazofanyika katika mtandao. Vilevile tunayo timu ambayo inaitwa Mwitikio wa Kukabiliana na Majanga ya Kompyuta (TZ-CERT) ambayo yenyewe kazi yake ni kuhakikisha kwamba pale changamoto kama hizi zinapotokea basi tunahakikisha tunaenda kuchukua hatua ili kuzuia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine tunao mfumo wetu ambao unaitwa Tele Traffic Management System ambao kazi yake ni kuhakikisha kwamba inadhibiti mambo mawili, kwanza kabisa ni kufatilia miendendo ya mawasiliano yote yanayoingia ndani ya nchi, vilevile ni kuangalia namna mapato yanavyotokea na namna ambavyo tunaweza tukaya–contrive.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. MAULID SALEH ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Nataka nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; je, Serikali imejipangaje kuweka mahusiano mazuri katika ya NIDA na Jeshi la Polisi katika kutatua taarifa za haraka za mitandao ya kijamii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, Serikali ina uhusiano gani mzuri wa kuhakikisha inatatua matatizo yale ya upelelezi ambayo yanafanyiwa kazi na polisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kuhusu swali lake la mwanzo, uhusiano kati ya NIDA na Polisi umetengenezwa na tumshukuru Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba NIDA inakuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Polisi ipo chini ya Wizara ya Ndani ya Nchi, chini ya Waziri mmoja, Naibu Waziri mmoja, Katibu Mkuu mmoja. Kwa hiyo, hilo pekee linawakutanisha viongozi wa Taasisi hizi mbili; pale kunapokuwa na changamoto basi hushauriana na kuhakikisha suluhisho hupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pili la uhusiano wa kiupelelezi vilevile panapohitajika huduma za NIDA, kuliwezesha Jeshi la Polisi litimize wajibu wake hasa idara ya upelelezi, ushirikiano hufanyika na hatuishii hapo tu, tunahusiana pia na taasisi nyingine za kiserikali kwa mfano, TCRA ikihitajika pia tupate ushahidi kule kuwezesha Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)