Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mohammed Maulid Ali (3 total)

MHE. MOHAMMED MAULID ALI Aliuliza:-

(a) Je, Serikali inatambua mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na Kambi ya Jeshi la Wananchi iliyopo Chukwani Zanzibar?

(b) Je, Waziri yupo tayari kufuatana na Mbunge ili kukutana na wananchi na kufahamu hali halisi ya mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maulid Ali Mohammed, Mbunge wa Jimbo la Kiembe Samaki lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-


(a) Mheshimiwa Spika, Kambi ya Chukwani imepimwa na inatambuliwa kama Kiwanja Namba 787 na ramani yake imepata usajili Namba S.40/07. Eneo hili limepewa Hati Miliki Namba Z.20.2007. Hata hivyo, kuna wananchi wachache wanafanya shughuli za kibinadamu ndani ya eneo la kambi. Wananchi hawa sio wavamizi, wanatakiwa kulipwa fidia kwani ni maeneo yao ya siku nyingi kabla ya Jeshi kutwaa na kupima eneo hilo, pia ilikubalika waondoke baada ya kufanyiwa uthamini na kulipwa fidia.

Mheshimiwa Spika, Wizara inatambua mgogoro huo na hivi sasa ipo katika mpango wa miaka mitatu wa kuondoa migogoro yote iliyopo katika maeneo yake ikiwemo Kambi ya Jeshi ya Chukwani iliyopo Zanzibar. Mpango huo utajumuisha na kupatiwa Hati Miliki za maeneo yake yote.

(b) Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa alikuwa anauliza kwamba tupo tayari kwenda kuonana na wananchi. Nimwambie tu kwamba tupo tayari kwenda kuonana na wananchi ili tuweze kukaa nao, tujue sasa asili na chanzo cha mgogoro huo na tuwaeleze hatua ambayo tumefikia kama Serikali. Nakushukuru.
MHE. MOHAMED MAULID ALI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kujikita zaidi kwenye uchimbaji wa Malambo ya kuhifadhia maji ya mvua na kujenga mabomba ya kuchukua maji toka kwenye maziwa na mito yote kuliko kuendelea kutumia gharama kubwa za kuchimba visima bila mafanikio?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Maulid Ali, Mbunge wa Kiembe Samaki, kama Ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa uvunaji wa maji ya mvua kupitia mabwawa unatekelezwa kwenye maeneo mengi nchini ili kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, kazi ya ukarabati na ujenzi wa mabwawa na malambo inaendelea katika vijiji 20 vya Mlele, Kisarawe, Bunda, Kalambo, Mkinga, Handeni, Chalinze, Songwe, Chamwino, Chemba, Bahi, Kaliua, Kilindi, Itilima, Kishapu, Monduli, Kibaha na Kondoa. Aidha, kazi ya kuainisha maeneo 58 yanayofaa kujenga mabwawa madogo na malambo imefanyika na ujenzi utafanyika mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Serikali ni kuhakikisha miradi ya maji inajengwa kwa kutumia vyanzo vya uhakika ambavyo ni maziwa makuu na mito mikubwa. Mradi huo ni wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyapeleka Shinyanga, Kahama, Tabora, Igunga na Nzega Bukoba, Musoma, Misungwi na Magu. Vilevile, Utekelezaji wa miradi ya Mugango, Kiabakari, Butiama, Tinde, Shelui, na mradi wa maji katika miji ya Busega, Bariadi na Lagangabilili unaendelea kupitia Ziwa Victoria na mradi wa maji wa kutoa maji Ziwa Tanganyika kupeleka Kigoma Mjini, Kirando na Kabwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, Serikali imeanza mpango wa kutekeleza miradi kupitia maziwa makuu ili kunufaisha maeneo ya pembezoni mwa maziwa hayo; kwa upande wa mito; mradi wa maji wa Kyaka - Bunazi ambao unatumia maji ya mto Kagera.

Mheshmiwa Naibu Spika, huduma ya maji yanayotokana na maji ya chini ya ardhi ni katika maeneo kame ambayo hayana vyanzo vya uhakika vya maji juu ya ardhi. Haya maeneo ni kama vile Dodoma, Singida, Lindi, Simiyu, Kigoma na Katavi.
MHE. MAULID ALI MOHAMED aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakifanyia ukarabati Kituo cha polisi Mazizini pamoja na kukarabati nyumba za Askari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Maulid Ali Mohamed Mbunge wa Kiembe samaki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya tathmini ya uchakavu wa kituo na nyumba za makazi za askari polisi Mazizini na kubaini kuwa kiasi cha fedha shilingi 64,484,700 zinahitajika kugharamia ubadilishaji paa, dari, mfumo wa umeme, maji safi, maji taka na kupaka rangi. Ukarabati huo utafanyika kulingana na mpango wa ukarabati kutegemea na upatikanaji wa fedha.