Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mohamed Suleiman Omar (4 total)

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH (K.n.y. MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR) aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Askari wapya Pamoja na kuleta vitendea kazi vya kutosha kwa Polisi Zanzibar inayokabiliwa na upungufu mkubwa wa Askari kutokana na wengi kufikia umri wa kustaafu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Suleiman Omar, Mbunge wa Malindi kutoka Zanzibar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mgawanyo wa rasilimali watu na vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi pamoja na mambo mengine huzingatia hali ya uhalifu wa eneo husika, jiografia ya eneo, idadi ya watu wanaohudumiwa na Jeshi la Polisi na ikama ya watumishi sambamba na upatikanaji wa vitendea kazi kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Spika, uwiano wa askari wa Jeshi la Polisi kwa Raia kimataifa ni askari mmoja kwa raia mia nne hamsini (1:450) hata hivyo kwa upande wa Zanzibar takwimu zinaonesha kuwa uwiano ni askari mmoja kwa raia mia tatu na tisini na mbili (1:392). Kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2012 hii inamaanisha kuwa idadi ya Polisi Zanzibar ni wengi ukilinganisha na mahitaji katika kuhudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vitendea kazi, napenda kukiri kuwa kama ilivyo maeneo mengine ya nchi, kuna uhaba wa vitendea kazi. Serikali itaendelea kuongeza ikama ya watumishi na vitendea kazi kadri nafasi za ajira na fedha zitakavyokuwa zinapatikana. Nakushukuru.
MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR aliuliza:-

(a) Je, ni hatua gani zilizofikiwa kwenye mapambano dhidi ya madawa ya kulevya nchini?

(b) Je, ni watu wangapi wamekamatwa kuanzia mwaka 2019 – 2020 na wangapi wamehukumiwa kifungo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Suleiman Omar, Mbunge wa Malindi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, Katika kukabiliana na changamoto ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini, hadi sasa Serikali imechukua hatua zifuatazo;

Mheshimiwa Spika, kwanza imetungwa kwa sheria mpya ambayo ilipitishwa na Bunge lako Tukufu, Sheria ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Na.5 ya mwaka 2015. Sheria hiyo, ilianzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kama chombo maalum chenye nguvu ya kisheria ya kukamata, kupekua, kuzuia na kupeleleza makosa yote yanayohusiana na dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika, pili; kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kama vile Jeshi la Wananchi wa Tanzania kitengo cha Wanamaji na Jeshi la Polisi, Serikali imeimarishaji operesheni za nchi kavu, anga na majini hasa katika viwanja vya ndege, maziwa na Bahari ya Hindi, ikiwa ni mkakati kwa kudhibiti njia na vipenyo vyote. Pamoja na kuendelea kutoa elimu ya athari za matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali kupitia mamlaka imetambua mitandao mikubwa ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini na kubaini njia mbalimbali za usafirishaji. Mkakati huo, umechangia kwa kiasi kikubwa kuziba mianya ya uingizaji wa dawa za kulevya na ukamataji wa dawa hizo.

Mheshimiwa Spika, kwa majibu ya swali (b) kutokana na hatua hizi zilizochukuliwa na Serikali, katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2020, jumla ya dawa za viwandani (Cocaine na Heroin) zilizokamatwa ni kilo 426 na gramu 363. Jumla ya dawa za asili bangi na mirungi zilizokamatwa ni tani 28 na kilo 34. Aidha, katika kipindi cha Januari - Desemba 2020, na Januari - Mei 2021, jumla ya watuhumiwa 124 walikamatwa, kati yao 23 wametiwa hatiani na usikilizaji wa mashauri 40 unaohusisha watuhumiwa 83 unaendelea.
MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR aliuliza: -

Je, ni kwa nini wananchi wa Tanzania Bara wanatozwa na polisi faini za papo kwa papo kwa kutotumia mashine za EFD wakati Polisi wa Zanzibar hawatozi faini za papo kwa papo kwa wananchi wasiotumia mashine hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Suleiman Omar, Mbunge wa Jimbo la Malindi kutoka Mkoa wa Mjini Zanzibar kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, sheria zinazotawala sekta ya usafiri wa barabarani nchini zipo chini ya mamlaka mbili tofauti huku msimamizi wa sheria zake ni Jeshi la Polisi Tanzania. Kwa upande wa Tanzania Bara sheria inayosimamia masuala ya barabarani ni Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 ya mwaka 1973 iliyorejewa mwaka 2002 na kanuni zake, na kwa upande wa Tanzania Visiwani sheria inayosimamia masuala ya barabarani ni Sheria ya Usafiri Barabarani Sura ya 7 ya mwaka 2003 na kanuni zake.

Mheshimiwa Spika, sheria zote mbili zinatambua adhabu ya tozo ya papo kwa papo kwa Tanzania Bara kifungu kinachotumika ni cha 95 Sura ya 168 ya 1973 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na kanuni namba 30 ya mwaka 2015 na kwa Tanzania Visiwani kifungu kinachotumika ni cha 183 Sura ya 7 ya mwaka 2003 na kanuni namba 64 ya mwaka 2014.

Mheshimiwa Spika, katika kudhibiti makosa ya usalama barabarani ambayo yanasababisha ajali zinazoleta vifo, ulemavu, majeraha na uharibifu wa mali. Serikali kupitia Jeshi la Polisi linahimiza sheria na kanuni zilizowekwa zifuatwe kama zilivyoelezwa kwa mamlaka zote zinazosimamia usalama barabarani na usafiri wa barabarani ili kuzuia ajali barabarani zisitokee. Nakushukuru.
MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR aliuliza:-

Je Serikali ina mpango gani wa kupitia upya fedha za Mfuko wa Vichocheo vya Maendeleo ya Majimbo na kuziongeza fedha kwa upande wa Zanzibar?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Suleiman Omar, Mbunge wa Jibo la Malindi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kifungu cha 5(3) cha Sheria ya Mfuko wa Jimbo kimefafanua vigezo vinavyotumika kugawa fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo kama ifuatavyo:-

(a) Mgao sawa kwa kila jimbo asilimia 25;
(b) Idadi ya watu katika jimbo asilimia 45;
(c) Kiwango cha umaskini katika Jimbo 20; na
(d) Ukubwa wa eneo katika Jimbo 10.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuangalia uwezekano wa kuboresha mgao wa fedha za Zanzibar kulingana na upatikanaji wa mgao. Ahsante.