Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mohamed Suleiman Omar (3 total)

MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri, ningeomba tu niwe na swali moja tu la nyongeza kwa sababu majibu yake kwa kweli yamekamilika lakini ninalo swali moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nimepata malalamiko kutoka kwa wananchi wanapokwenda kutoa mashirikiano kwenye kitengo hiki cha madawa ya kulevya kwa kuwataja wanaohusika, baadhi ya maofisa hutoa taarifa zao za siri na kuwafikia wenyewe. Je, ni hatua gani mtakazozichukua endapo mtawabaini maofisa hawa ambao sio waaminifu ili wananchi warejeshe imani ya kwenda kusaidia Serikali? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, najua ni miongoni mwa Wabunge ambao wamekuwa mstari wa mbele kushughulikia tatizo hili la dawa za kulevya nchini na hasa kwa pande zote mbili za muungano, nakushukuru na nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya uongozi wa Mamlaka na kama mlivyoshuhudia kilogramu takribani kama 895 kwa mara ya kwanza mzigo mkubwa umekamatwa mwaka huu kwenye Pwani ya Mkoa wa Mtwara ambayo ilikuwa inatoka Mashariki ya Mbali huko kwa hiyo ninawapongeza wote na Rais wetu tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa tumekuwa na tatizo kubwa, baadhi ya watendaji na maafisa ndani ya Mamlaka lakini na vyombo vingine wamekuwa wakitoa siri, sio za watoa habari tu, hata siri ya mipango na mikakati ya kwenda kudhibiti na kuzuia matumizi na biashara hii na matumizi ya dawa za kulevya. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge mara zote tunapowabaini tumekuwa tukichukua hatua kali na wakati mwingine kuwafungulia mashtaka na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili waweze kuondoa kabisa tatizo hilo la ufichaji wa mianya ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.

Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa onyo kwa watendaji wote wa Mamlaka na watendaji wengine wote kutokuthubutu kabisa kuwa ni sehemu ya biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya nchini kwa ustawi wa vijana wetu na Taifa letu kwa ujumla. (Makofi)
MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza nashukuru majibu ya Serikali kwa kufuatia maswali yangu haya; lakini swali langu la kwanza katika maswali yangu ya nyongeza kwamba kama kwa mujibu wa majibu aliyonipa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba inakiri kwamba Mamlaka ya kule Zanzibar pia inayo sheria yake ambayo inatambua hizi sheria za faini za papo kwa papo; je, ni kwa nini Jeshi la Polisi sasa limeshindwa kusimamia sheria hizi za papo kwa papo pale barabarani kwa kutumia hizi mashine za EFD? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwamba ni lini sasa Wizara ya Mambo ya Ndani itakaa na mamlaka husika za kule Zanzibar ili kuona Jeshi la Polisi zinaanza kutumia mashine hizi na ukizingatia kwamba itapunguza malalamiko ya wananchi na itapunguza masuala ya rushwa lakini pia itapunguza zile ajali ambazo zitaweza kuepukika? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, naomba ama napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Malindi Mheshimiwa Mohamed Suleiman Omar maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, je, kwa nini Jeshi la polisi limeshindwa? Jeshi la polisi halijashindwa kusimamia taratibu, kanuni na sheria za usalama barabarani katika hili suala la kutumia mashine hizi hapa kuja jambo kidogo, Zanzibar kuna mamlaka inaitwa Mamlaka ya Usafirishaji au Mamlaka ya Usalama Barabarani ambayo ina sheria yake sheria namba saba na Bara kuna Baraza la Taifa la kusimamia usalama barabarani ambalo nalo lina sheria yake kama tulivyoeleza, lakini kama hilo halitoshi mamlaka hivi zote zina utaratibu wake na kanuni zake ambazo zinasimamia pamoja na kwamba Jeshi la Polisi ndio muhimili mkubwa ambao unasimamia mamlaka hizi.

Kwa hiyo, haijashindwa kusimamia tatizo lililokuwepo ni changamoto ya sheria kwamba hawa wanasheria yao, wana kanuni yao, hawa wana mamlaka yao pamoja na kwamba Jeshi la polisi ndio hilo. Kwa hiyo jeshi la polisi halijashindwa kusimamia sheria hii.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili; je, ni lini sasa Serikali hasa kule Zanzibar itaruhusu matumizi ya hizi mashine? Nimwambie tu kwamba kwa kuwa sheria ipo na mamlaka inayosimamia usalama barabarani ipo na sheria yake ipo kikubwa ni kwamba sasa hivi tupo katika harakati za kukamilisha kanuni itakayokuja kusimamia sheria hizi ili sasa hii sheria ya kutumia hizo mashine kwa ajili ya kukinga hizo ajali na mambo mengine zianze kutumika.

Mheshimiwa Spika, kubwa nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge awe na subira kidogo sana ili tumalize hizo kanuni na sheria zianze kutumika kote kote.
MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili nyongeza. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majawabu yake haya mazuri.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza ningeomba tu kuuliza katika asilimia hizi alizozotaja karibu majimbo mengi ya Zanzibar tayari yameongezwa ukubwa wa eneo na kwa maana hiyo idadi ya watu pia imeongezeka, lakini hata ile hali ya uchumi ya wananchi kwenye majimbo hayo pia hayako vizuri.

Je, Serikali haioni sasa ndio muda muafaka wa kupitia upya vigezo hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni ushauri tu kwamba kiongezwe kifungu cha kuangalia gharama ya matumizi ya hizi fedha kwenye maeneo husika kwa sababu sisi kwa kule Zanzibar kama hizi fedha zinatumika kwenye miradi labda ya shule au madarasa vifaa vya ujenzi viko juu sana katika manunuzi yake. Kwa hiyo tungeomba kigezo hiki pia kiongezwe. Nashukuru sana. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la ndugu yangu Mohamed Suleiman Omar kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kweli majimbo mengi sasa hivi idadi ya watu imeongezeka na hili si kwa upande wa Zanzibar peke yake isipokuwa kwa nchi nzima na ndio maana mwaka huu kuna umuhimu mkubwa sana. Katika sensa yetu ya watu na makazi, ni vyema watu wakajitokeza tukapata idadi halisi ya wananchi katika maeneo husika, hata projection zozote za masuala ya miradi ya maendeleo iweze kuakisi uhalisia wa watu. Kwa hiyo jambo hilo ni jambo la msingi sana, ni imani yangu kubwa baada ya sensa yam waka huu tutapata takwimu halisi ya kila eneo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo ndio maana pale Naibu Waziri hapa alizungumza katika bajeti yetu ya mwaka huu wa fedha tumeona ongezeko hili sasa limeongezeka kutoka shilingi bilioni 11 kwa majimbo yote mpaka shilingi bilioni 15.99, hay ani mafanikio makubwa na tuna kila sababu kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa utashi wake wa kuona majimbo haya lazima yaongezewe fedha.

Katika suala lingine la kuangalia au utaratibu mwingine wa kuboresha hili ni jukumu letu kama Serikali na hasa kuangalia masuala ya mipaka na mambo mengine. Naomba nikuahidi Mheshimiwa Mbunge na kama unavyofahamu kwamba jukumu langu kubwa hata nikija kule Zanzibar kwa kuchechua issue mbalimbali za kuhusu maeneo ya Zanzibar ambayo mimi nimepewa jukumu la kulisimamia, lengo letu ni kwamba wananchi wanaotarajia katika Mfuko wa Jimbo waweze kunufaika katika miradi ile inayogusa katika maeneo ya majimbo yao, ahsante sana.