Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Charles John Mwijage (55 total)

MHE. DKT. CHRISTINA G. ISHENGOMA aliuliza:-
Wanawake wa Mkoa wa Morogoro wanaojishughulisha na usindikaji wa matunda wanakabiliwa na ukosefu wa soko na mikopo ya uhakika.
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wanawake hao kupata soko la uhakika?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia mikopo ya uhakika wanawake hao?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, lenye Sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kuwasaidia wanawake wasindikaji matunda na mboga mboga kupata soko la uhakika na kuhakikisha wanaondokana na tatizo la kutokuwa na uhakika wa masoko ya bidhaa zao, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwawezesha Wajasiriamali kushiriki kwenye maonesho ya kutangaza bidhaa zao kupitia maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Saba Saba, Maonesho ya Kikanda, Maonesho ya Juakali na Maonesho mengine ambayo huendeshwa na nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC.
Mheshimiwa Spika, pia wajasiriamali hao huhamasishwa kushiriki katika Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane na kuwapatia mafunzo ya ubora wa bidhaa na hatimaye kuhakikisha wanapatiwa alama ya ubora (TBS Mark), kwa kutambua umuhimu wa ubora kwa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali hao. TBS inatoa huduma ya kupima ubora wa bidhaa kwa wajasiriamali bure na wajasiriamali sasa hivi wanapata huduma ya mfumo wa ufuatiliaji (traceability) na alama za utambuzi (Bar Code), humu humu nchini kupitia GS 1 wakati zamani ilikuwa ni vigumu kuzipata kwa sababu zilikuwa zinapatikana nje ya nchi tu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu sehemu ya pili ya swali la Mheshimiwa Dkt. Ishengoma, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba mipango iliyopo ya kuwapatia mikopo ya uhakika wanawake wajasiriamali ni kama ifuatavyo:-
Mpango wa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Japan na Benki ya CRDB imeanzisha Mfuko wa Dhamana kwa Wajasiriamali Wadogo (SME Credit Guarantee Scheme), wenye thamani ya shilingi bilioni mbili. Dhumuni kubwa la mfuko huo ni kusaidia wajasiriamali wadogo wakiwemo wanawake, kupata mikopo yenye riba na masharti nafuu. Kwa kuanzia, Mfuko huu tayari umeanza kufanya kazi kwenye Mikoa saba ambayo ni Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Morogoro na Singida.
Kadiri Mfuko utakavyoimarika mikoa mingine itafikiwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuboresha Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Ujasiriamali Nchini (National Enterprenuership Development Fund) ili kuwawezesha kutoa huduma kwa wajasiriamali wadogo wengi zaidi. Hadi sasa Mfuko huo umeongeza kiwango cha mikopo kwa wajasiriamali wadogo ili kuwezesha kupanua biashara ndogo na viwanda vidogo kutoka shilingi 500,000/= hadi shilingi 2,500,000/= na shilingi 2,500,000/= hadi shilingi 5,000,000/= kwa kufuatana.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha mipango ya kuvisaidia vikundi au Vyama vya Ushirika vinavyojihusisha na usindikaji wa mazao ya kilimo kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania na kupitia mikopo rahisi itakayotolewa na Halmashauri, hasa kwa wanawake na vijana. Serikali kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) imeendelea kutoa elimu ya mafunzo ya ujasiriamali ili kuwawezesha wajasiriamali wadogo kupata mikopo ya kuendesha biashara zao kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na kuunda vikundi vya kufanya shughuli zao, kuandaa michanganuo ya biashara kwa mjasiriamali mmoja mmoja na katika vikundi.
Mheshimiwa Spika, ili wajasiriamali waweze kupata masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi, Serikali inasisitiza wazingatie mahitaji ya soko tarajiwa kujiunga katika vikundi au Vyama vya ushirika na waweze kutumia vizuri fursa ya kuwepo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Nchini.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Serikali ilichukua eneo kubwa kwa ajili ya kujenga Soko la Kimataifa, Makambako na iliahidi kulipa fidia wananchi waliopisha ujenzi huo; na Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliahidi kuwalipa fidia hiyo:-
Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hao?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa Makambako, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa mpango wa kujenga Soko la Kimataifa la Makambako ni wa muda mrefu na suala la wananchi kulipwa fidia limechukua muda mrefu pia. Sababu zilizosababisha kuchelewa ni ufinyu wa bajeti na hivyo kusababisha kurudia kufanya tathmini ya mali na mazao ya wananchi waliotoa maeneo ya kupisha mradi huu. Tathmini ya kwanza ilifanyika mwaka 2011 na kurudiwa mara ya pili mwaka 2015 baada ya muda wa kulipa fidia kisheria kupita.
Mheshimiwa Spika, tayari Mthamini Mkuu wa Serikali amepitisha tathmini hii mpya na hivyo, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Makambako itatenga fedha kwa ajili ya malipo ya fidia katika mwaka wa fedha 2016/2017. Kwa hiyo, wananchi waliotoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Kimataifa, Makambako watalipwa fidia katika mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. UPENDO F. PENEZA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha nia ya kutaka kuongeza mapato kwa ufuatiliaji na kuondokana na ukwepaji kodi bandarini, lakini kwa miaka mingi Serikali imekuwa ikikosa mapato kwa kutoa misamaha ya kodi kwa kampuni za uwekezaji katika sekta ya madini:-
Je, Serikali inachukua hatua gani ili kuondokana na misamaha ya kodi inayotolewa kwa kampuni ya uwekezaji?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitoa vivutio vya aina mbalimbali kwa wawekezaji ili kuvutia uwekezaji nchini. Misamaha ya kodi ni moja ya vivutio vinavyotolewa kama moja ya njia ya kuwahamasisha wawekezaji ili wachague nchi yetu badala ya kwenda nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, misamaha hii hutolewa kwa mujibu wa sheria na mara nyingi kwa kipindi cha awali cha uwekezaji. Misamaha hii kama alivyoeleza Mheshimiwa ni pamoja na inayotolewa kwa makampuni ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta, gesi na madini na misamaha inayotolewa kupitia maamuzi ya Kamati ya Uwekezaji ya Taifa (NISC) na kwa kutumia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua upungufu uliopo katika kutumia kodi kama kivutio cha uwekezaji. Tatizo kubwa ni wale wanaotumia fursa hii kuhujumu mapato ya Serikali au pale misamaha inaposababisha kutokuwepo ushindani sawa kati ya kampuni moja na nyingine katika sekta ile ile. Hata hivyo, kama nilivyoeleza awali, uwekezaji utakaolazimu kushindania wawekezaji na nchi nyingine duniani au kuhamasisha uzalishaji nchini wenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi walio wengi na kivutio cha kodi kikawa ndicho kigezo muhimu cha kufanya uamuzi tunalazimika kutoa misamaha ya kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kufanya mabadiliko katika sheria ili kupunguza misamaha ya kodi inayotolewa kwa ridhaa, yaani misamaha inayotolewa kwa kampuni moja moja kwa mikataba na kwa kupitia kwa mamlaka ya Waziri wa Fedha na Mipango. Ili kuboresha kivutio cha misamaha kwa wawekezaji, kodi imekuwa ikipunguzwa katika bidhaa na shughuli za jumla zinazo-cut across.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada za kuondoa upungufu unaoendana na misamaha ya kodi, napenda nikiri kuwa pamoja na vivutio vingine muhimu kwa kuvutia wawekezaji, misamaha ya kodi itatumika pale inapobidi. Aidha, tofauti na zamani tutaperemba misamaha hiyo mara kwa mara ili kuipima tija yake.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 imelenga kuanzisha Mfuko Mkubwa kwa ajili ya kutoa mkopo kwa wafanyakazi na wajasiriamali wadogo kwa masharti nafuu.
Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa jambo hilo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nianze kwa kunukuu Ibara ya 57(e)(v) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, inayosema; “Kuanzia Mfuko Mkubwa wa Kitaifa wa wajasiriamali wadogo na wakati kwa kushirikiana na Mifuko ya Jamii na Asasi nyingine za Kifedha. Hivyo ibara hiyo iliyorejewa imewalenga wajasiriamali wote bila kujali kama ni wafanyakazi au si wafanyakazi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutekeleza maelekezo ya Chama Tawala, chini ya Ibara ya 57(e)(v) Ilani ya Uchaguzi itawajengea wananchi uwezo wa kuanzisha, kuendesha na kukuza shughuli zao za kiuchumi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuendesha uchumi wa Tanzania. Serikali inategemea kuanza mazungumzo na wadau wa Mifuko ya Kijamii pamoja na asasi nyingine za kifedha mwezi Februari mwaka huu ili kujadili namna bora ya kuanzisha na kuendesha Mfuko huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inatarajiwa taratibu za kuanzisha Mfuko huo zitakamilika katika mwaka wa fedha 2016/2017 na kuweza kuanza kwa Mfuko huo katika mwaka wa fedha 2017/2018, baada ya Serikali kutenga fedha za kutosha.
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM aliuliza:- Ajira iliyotarajiwa kuongezeka kutokana na ukuaji wa sekta ya viwanda haijafikiwa hasa baada ya viwanda vingi kubinafsishwa na kuachwa bila kuendelezwa:-
Je, Serikali inasema nini kuhusu hili?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nia njema kabisa Serikali ilibinafsisha viwanda na mashirika ya umma ikiwa na matumaini kuwa sekta binafsi ingeliweza kuendesha taasisi hizo kwa faida na kulipa kodi kwa Serikali, kuzalisha bidhaa au huduma na kutoa ajira kwa wananchi. Pamoja na malengo hayo Serikali ililenga kuachana na shughuli za biashara ikielekeza nguvu zake katika shughuli zake za msingi za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Masoud, makampuni mengi yaliyobinafsishwa hayakufanya vizuri, ikiacha mfano wa makampuni machache yakiwemo Tanzania Breweries, Morogoro Polister ambayo inaitwa Twenty First Century na Tanzania Cigarette Company.
Mheshimiwa Naibu Spika, tathimini inayoendeshwa na Wizara yangu kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina juu ya viwanda, mashamba na mashirika ya Serikalil yaliyobinafsishwa kuanzia mwaka 1992 inadhihirisha ukweli tunaoujua kuwa wengi kati ya waliyopewa taasisi hizo hawakutekeleza mikataba ya mauziano kikamilifu. Hivyo tunawafuatilia kwa karibu wale wote waliopewa mashirika ya umma kwa utaratibu wa ubinafsishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu ni kuhakikisha makampuni yote haya yanazalisha kwa tija ili tupate bidhaa, kodi ya Serikali na ajira kwa wananchi wa Tanzania. Wale wote watakaobainika kukiuka makubaliano yaliyomo katika mikataba ya awali, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuvitwaa viwanda au mashirika hayo na kutafuta Wawekezaji mahiri wa kuviendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutimiza adhma ya kutoa ajira kwa Watanzania, Wizara inafanya yafuatayo chini ya viwanda vidogo na vya kati unaoshirikisha SIDO na Halmashauri za Wilaya na Mikoa tunahamasisha shughuli za ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani mazao na kilimo, uvuvi na ufugaji huku Mikoani.
Pia kupitia mamlaka zetu za EPZA, TIC na NDC tunakaribisha na kuwaongoza wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika shughuli za kutoa ajira zaidi. Serikali kupitia Wizara yetu inaboresha mazingira ya uwekezaji hali itakayowajenga imani wawekezaji na kupelekea kupanua shughuli zao zaidi za kibiashara kupitia njia hii ajira zaidi itaongezeka.
MHE. HASSAN E. MASALA (K.n.y. MHE. HAMIDA M. ABDALLAH) aliuliza:-
Vijana wengi wa Mkoa wa Lindi karibu 40% hawana ajira kutokana na ukosefu wa viwanda mkoani humo; na kwa kutambua kuwa sehemu kubwa ya uchumi wetu unategemea kilimo na Serikali ilitunga Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 1996 -2020 itakayosimamia maendeleo ya viwanda vya kusindika mazao ya kilimo ili kuongeza thamani ya mazao:-
Je, Sera hiyo imesimamiwa vipi katika kuvifanya viwanda vilivyopo vya usindikaji wa mazao viendelezwe ili kuongeza thamani ya mazao yetu na kukuza uchumi na hatimaye vijana kupata ajira katika Mkoa wa Lindi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuchochea maendeleo ya viwanda nchini, Serikali iliandaa na kuanza utekelezaji wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda (Sustainable Industrial Policy – (SIDP) 1996 -2020) na baadaye iliandaa Mkakati Unganishi wa Kuendeleza Sekta ya Viwanda (Integrated Industrial Development Strategy 2025) ili kuimarisha utekelezaji wa Sera hiyo. Moja ya vipaumbele vya Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ililenga katika kipindi cha muda mfupi kuendeleza viwanda vinavyoongeza thamani ya rasilimali zinazopatikana nchini ikiwemo mazao ya kilimo ili kukuza uchumi na kuongeza ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa utekelezaji wa Sera unaanza mwaka 1996, mkoa wa Lindi ulikuwa na viwanda vitano vinavyosindika mazao ya kilimo, vikiwepo viwanda vya kubangua korosho na viwanda vingine vidogo vidogo vya samani, kukamua mafuta ya ufuta, usindikaji nafaka na kadhalika. Aidha, viwanda hivyo vilibinafsishwa na kwa bahati mbaya havijawahi kufanya kazi hadi sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na utekelezaji wa Sera, ikijumuisha uhamasishaji wa sekta binafsi kuwekeza kwenye viwanda, upatikanaji wa miundombinu muhimu kama vile maji, umeme, mawasiliano, barabara na kuimarisha mazingira ya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu za sasa zinaonesha Mkoa wa Lindi una jumla ya viwanda vinavyosindika mazao pekee vipatavyo 329 vinavyoajiri watu 770 na kati ya hivyo viwanda vikubwa vinavyoajiri watu watano mpaka kumi vipo kumi. Kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina, sasa tunapitia vile Viwanda vya Korosho vilivyobinafsishwa ili viweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati unganishi wa kuendeleza Sekta ya viwanda umeibua mwambao wa Pwani kuwa kitovu cha kuendeleza viwanda na kuuza mauzo nje (Water Front Industrial and Export Frontiers). Lengo la mkakati ni pamoja na kukuza sekta ya viwanda vijijini itakayoongozwa na maendeleo ya kilimo na kutoa fursa ya ukuaji wa viwanda vidogo na vya kati kwa kuchukua hatua za makusudi za kuvisaidia katika ngazi zote za maendeleo ili viweze kukua.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafungua rasmi Kiwanda cha kutengeneza Matairi cha General Tyre ambacho kilikuwa ni mkombozi mkubwa kwa uchumi wa Taifa na ajira kwa wananchi wa Arusha?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Kutengeneza Matairi cha General Tyre Arusha kilisimamisha shughuli zake mwaka 2009 kutokana na Serikali kukosa fedha kwa ajili ya kukiendesha. Wakati huohuo, aliyekuwa mbia mwenza (Kampuni ya Continental AG) hakuwa tayari kuendelea kuwekeza katika kiwanda hiki.
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuona kiwanda hiki kinaanza kuzalisha matairi mapema iwezekanavyo. Hii inadhihirishwa wazi katika Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano 2016/2017-2020/2021 na tumepanga kuanza utekelezaji katika mwaka wa fedha unaoanza Julai 2016. Aidha, Serikali tayari imenunua hisa 26 zilizokuwa zinamilikiwa na mbia mwenza. Kiwanda hicho kwa sasa kinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Vile vile, Serikali imeamua kuweka dhamana ya kusimamia na kuendesha kiwanda hiki chini ya NDC na Tangazo la Serikali (GN) juu ya uamuzi huo litatolewa wakati wowote.
Mheshimiwa Spika, mradi wa Kiwanda cha Matairi, Arusha una maslahi mengi kwa Taifa kuanzia wakulima wa mpira, wafanyakazi kiwandani na maduka ya bidhaa hiyo, usalama wa vyombo vya usafiri vitumiavyo matairi, kodi kwa mamlaka mbalimbali na kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza matairi nje ya nchi. Kwa kuzingatia umuhimu wa mradi huo, Wizara imeiagiza NDC kuandaa andiko la kitaalam ambalo pamoja na kujibu masuala ya kiuchumi, kiufundi, kijamii, lazima lizingatie maoni ya wadau wa sekta.
Mheshimiwa Spika, mradi huo ambao ni kielelezi tunataka ujiendeshe kwa kuwa na menejimenti huru yenye watu wenye weledi katika shughuli na bila kutegemea ruzuku ya Serikali.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:-
Viwanda vingi vya Moshi vilibinafsishwa havifanyi kazi, badala yake vimegeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhia bidhaa mbalimbali na vimechakaa sana; aidha mafao ya wafanyakazi waliostaafishwa katika Kiwanda cha Magunia na Kilimanjaro Timber Utilization hayakulipwa inavyostahili na hivyo kuwepo kwa malalamiko ya muda mrefu ya madai yao bila mafanikio:-
(a) Je, kwa nini Serikali isivikabidhi viwanda hivyo kwa kampuni nyingine zenye uwezo wa kuviendeleza na hivyo kupunguza tatizo la ajira katika Mji wa Moshi?
(b) Je, ni lini madai ya mafao ya wafanyakazi waliostaafishwa katika viwanda hivyo yatalipwa?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na zoezi la kufanya Ufuatilliaji na tathmini katika viwanda na mashirika ya umma yaliyobinafsishwa ili kubaini kama masharti ya vipengele vya Mikataba ya mauzo iliyoingiwa kati ya Serikali na wawekezaji yametekelezwa ili kuchukua hatua stahiki. Katika utekelezaji wa zoezi hilo, pamoja na mambo mengine mikataba yote ya mauzo inapitiwa na endapo itagundulika kuwa masharti ya mikataba husika yamekiukwa, hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwemo Serikali kuvirejesha viwanda hivyo. Pia wawekezaji mahiri wenye nia ya kuwekeza nchini watatafutwa. Vilevile viwanda ambavyo vitaonekana wamiliki wana nia na uwezo wa kuvifufua, makubaliano mapya yatafikiwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyakazi wote katika viwanda vilivyotajwa walilipwa stahiki zao. Hata hivyo, baada ya malipo hayo kutolewa wafanyakazi waliendelea kudai zaidi madai yanayotokana na Mikataba ya Hiari. Serikali ilishatolea ufafanuzi suala hili kuwa madai yanayotokana na Mkataba wa Hiari yanapaswa kulipwa kutokana na hali ya uzalishaji wa kiwanda au kampuni kwani yanalenga kugawana ziada ambayo kiwanda kama cha Magunia (Tanzania Bag Corporation –TBCL) hakikuwa nayo, wakati kile cha Kilimanjaro Timber Utilization kiliuzwa kwa ufilisi.
Aidha, wakati zoezi la ubinafsishaji linatekelezwa, kiwanda cha Magunia cha Moshi kilikuwa na malimbikizo ya mishahara ya Wafanyakazi wake kwa zaidi ya miezi 18 hivyo hakikuwa hata na uwezo wa kulipa malipo ya kisheria, hivyo madai ya nyongeza hayakuwa na msingi. Serikali haiwajibiki kulipa mafao yoyote kwa wafanyakazi waliokuwa katika viwanda vya Magunia na Kilimanjaro Timber Utilization.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE (K.n.y. MHE. TASKA R. MBOGO) aliuliza:-
Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa Mikoa ambayo haina kiwanda hata kimoja;
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga viwanda katika Mkoa wa Katavi?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake na vijana wa mkoa huo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na taarifa ya sensa ya viwanda iliyofanyika mwaka 2015 ni kweli kuwa Mkoa wa Katavi hauna viwanda vikubwa. Hata hivyo, Mkoa huo una jumla ya viwanda vidogo 221 ambapo kila kiwanda kina uwezo wa kuajiri wafanyakazi wasiozidi 10. Aidha, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) linatoa huduma katika viwanda vidogo vya usindikaji wa vyakula na asali vipatavyo 26, viwanda vidogo vya kukoboa mpunga tisa, viwanda vya kusaga unga 11 na viwanda vidogo vya kubangua karanga saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na juhudi za Serikali za kuhamasisha na kuboresha mazingira yanayovutia wawekezaji wa ndani na nje, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Katavi kuwa, tutaongeza juhudi za kutekeleza jukumu la kuhamasisha viwanda kwenda Katavi. Aidha, nimwombe Mheshimiwa Mbunge na wadau wote wa maendeleo kusaidiana na Serikali kuhamasisha ujenzi wa viwanda Mkoa wa Katavi kwa kulenga malighafi zinazopatikana sehemu hiyo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia SIDO imeendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi wakiwemo wanawake na vijana. Kati ya mwaka 2007 mpaka 2015 SIDO ilitoa mafunzo yenye nia ya kutoa maarifa na kujenga uwezo wa stadi kwa wajasiriamali wapatao 520. Mafunzo hayo yalitolewa katika nyanja zifutazo:-
Utengenezaji wa mizinga ya nyuki ya kisasa, usindikaji wa vyakula, utengenezaji wa sabuni, utengenezaji wa chaki, mafunzo juu ya ujasiriamali, utengenezaji wa majiko ya kisasa yanayotumia nishati ndogo, mfumo wa ufuatiliaji bidhaa za asali, utengenezaji wa mitambo ya kukausha mazao ya kilimo yanayotumia nishati ya jua na usimamizi wa masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, SIDO imekwishapata ofisi ya kufanyia kazi katika Mkoa wa Katavi kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi. Hatua hiyo itapanua wigo wa utoaji mafunzo ya ujasiriamali na usindikaji wa vyakula kwa wanawake na vijana katika Mkoa wa Katavi.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Ujenzi wa masoko ya Kimataifa yaliyokuwa yakijengwa huko Nkwenda na Murongo yamesimama kwa muda mrefu sana na wananchi wa Wilaya ya Kyerwa walitegemea masoko hayo kwa ajili ya kuuzia mazao yao mbalimbali:-
Je, ni nini kimesababisha kusitishwa kwa ujenzi wa masoko hayo? Na ni lini sasa ujenzi utafufuliwa na kukamilishwa ili kutoa fursa za kufanya biashara na kwa majirani zetu pia?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Omwanawumkazi, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa miundombinu ya masoko nchini hususan masoko ya mipakani, yakiwemo masoko ya Nkwenda na Murongo ni moja ya maeneo ya kipaumbele cha Serikali yetu. Masoko hayo yakikamilika yatakuwa ni kichocheo kwa wakulima kuzalisha zaidi na wafanyabiashara kuuza kwa uhakika, kutokana na kunufaika na soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Naibu Spika, masoko ya Kimataifa ya Nkwenda na Murongo ni kati ya masoko matano ambayo yalikuwa yanajengwa kwa kutumia fedha za mradi wa wawekezaji katika Sekta ya Kilimo Wilayani (District Agricultural Sector Investment Project - DASIP).
Mheshimiwa Naibu Spika, masoko mengine yaliyonufaika na mradi huo ni Kabanga - Ngara, Lemagwe - Tarime na Busoka - Kahama. Ujenzi wa Masoko hayo ulifikia kiwango cha kati ya asilimia 45 mpaka 65 kwa ujenzi na kusimama baada ya mradi wa DASIP I kufikia ukomo wake mwaka 2013 na Benki ya Maendeleo ya Afrika iliyokuwa ikifadhili ujenzi huo kusitisha utoaji wa fedha kwa ajili ya mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo jitihada zinafanyika ili kuendelea na mradi wa DASIP awamu ya pili ili pamoja na mambo mengine tuweze kukamilisha ujenzi wa masoko yote yaliyokusudiwa yakiwemo masoko ya Nkwenda na Murongo. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo vya ndani na wahisani wengine ili kumalizia ujenzi wa masoko hayo muhimu kwa uchumi wa nchi yetu. Kazi ya kuendeleza ujenzi na kukamilisha masoko hayo itaanza pindi Serikali itakapopata pesa hizo.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Wilaya ya Muheza ina utajiri wa uzalishaji wa matunda kama machungwa, maembe, machenza, mafenesi na kadhalika:-
Je, ni lini Serikali itajenga kiwanda Wilayani hapo cha kutengeneza juisi na kuwaondolea usumbufu wakulima hao wa kutafuta soko?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajabu, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri ya jukumu la Serikali katika kujenga viwanda ni kwa Serikali kuweka mazingira sahihi na wezeshi ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje wa sekta binafsi kujenga viwanda. Katika kutekeleza hilo, sera na mkakati mbalimbali shirikishi inatoa fursa kwa sekta binafsi na taasisi za uwekezaji kujenga viwanda na kunufaika na vivutio mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Tanga ikiwemo Wilaya ya Muheza wamejaliwa kuwa na utajiri wa matunda aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na machungwa, maembe, machenza, mafenesi, mananasi kwa kutaja baadhi. Kwa kutambua upatikanaji huo wa matunda, Wizara yangu inahimiza na kuhamasisha wawekezaji kutoka sekta binafsi wenye nia ya kufungua viwanda vya juisi Mkoani Tanga ikiwemo Wilaya ya Muheza kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa kampuni ya SASUMUA HOLDING imeanzisha mradi mkubwa wa kulima matunda katika utaratibu utakaoshirikisha wananchi (out grower). Mradi huo ulioko Kwamsisi – Handeni, Mkoani Tanga ni matengemeo yangu kama ukifanikiwa, wawekezaji wengine watavutiwa na kuweza kuwekeza eneo hilo la Tanga na sehemu nyingine za nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara kupitia Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) lina utaratibu wa kutoa ushauri jinsi ya kuanzisha mitaa ya viwanda kila mkoa ikiwa ni jitihada za kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuendeleza uzalishaji katika mikoa husika. Hivyo, ningependa kumshauri Mheshimiwa Mbunge tushirikiane kuhamasisha na kuwahimiza wadau wakiwemo wananchi na halmashauri mbalimbali nchini kutoa ushirikiano pindi wawekezaji wanapojitokeza.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE aliuliza:-
Viwanda vingi nchini vimekuwa vya kizamani, vingine vimetekelezwa na wawekezaji na baadhi hufanya kazi kwa kusuasua hasa katika Mkoa wa Kagera.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuviboresha viwanda hivyo ili viweze kufanya kazi vizuri kwa faida ya nchi yetu?
WAZIRI WAVIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vingi vinavyotumia teknolojia ya zamani ambavyo havifanyi kazi au kuzalisha kwa kusuasua vingi ni vile vilivyobinafsishwa. Tathmini iliyofanywa na Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina inaonesha kuwa kati ya viwanda vilivyobinafsishwa, viwanda 24 vinafanya kazi kwa kusuasua na viwanda 37 vimefungwa kote nchini.
Aidha, katika Mkoa wa Kagera kiwanda cha NMC Old Rice Milling kimefungwa wakati kiwanda cha Kagera Tea Co. Ltd (MARUKU) kinafanya kazi kwa kusuasua. Kusuasua kwa kiwanda hiki na vingine vyote nchini kutokana na uchakavu wa mitambo katika baadhi ya viwanda, ushindani katika soko, kupungua kwa mtaji na kutopatikana kwa malighafi nikizungumzia kiwanda changu cha MARUKU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inashauriana na wawekezaji wa viwanda vinavyofanya kazi kwa kusuasua na vile vilivyofungwa ili kuviwezesha viwanda hivi kufanyakazi. Aidha, majadiliano yanayoendelea pia tunawahimiza kutumia teknolojia ya kisasa katika uzalishaji ili kuongeza tija na kupunguza athari za mazingira zinazohusiana na uzalishaji viwandani. Vilevile tunawashauri wawekezaji walioshindwa kuendesha ipasavyo viwanda vyao kuingia ubia na wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuviendesha kwa tija ili tuongeze ajira, tuzalishe bidhaa kwa ajili ya soko la ndani lakini na zaidi walipe kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine itaendelea kulinda viwanda vya ndani kwa kuhakikisha bidhaa zote ziingiazo zinakidhi viwango na zinatozwa tozo stahiki. Aidha, tutahakikisha tunaboresha wepesi wa kufanya biashara kwa kuondoa tozo kero na kuhakikisha kuna umeme wa uhakika kama alivyosema Naibu Waziri wa Nishati.
MHE. JOHN P. KADUTU (K. n. y. MHE. MAGDALENA H. SAKAYA) aliuliza:-
Njia pekee ya kuinua uchumi wa Taifa linalotegemea kilimo kwa sehemu kubwa ni pamoja na kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo na mifugo;
(a) Serikali ina Mkakati gani wa kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo kwenye Mikoa yote ya kilimo na yenye mifugo mingi nchini;
(b) Wafanyabiashara wa mazao ya kilimo na mifugo wanafanya udanganyifu mkubwa wa kujaza magunia lumbesa, kutanua madebe, pia kupima mifugo kwa macho na kwa kupapasa hali inayowaumiza na kuwapa hasara kubwa wakulima. Je, kwa nini Serikali inashindwa kuweka matumizi ya mizani rasmi kwa mazao hapa nchini?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya Mbunge wa Kaliua lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, na Serikali ya India kupitia Mradi wa Supporting India Trade and Investment for Africa (SITA) imefanya juhudi kubwa kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya nguo na mavazi, ngozi, mafuta ya alizeti na mazao jamii ya kunde. Tayari mikakati ya jinsi ya kuendeleza sekta hizo yenye mipango kamili ya utekelezaji imekwisha andaliwa na utekelezaji wake utaanza mwaka 2016/2017. Aidha, Wizara inapanga kuanzisha makongano ya viwanda katika mikoa ili kuwezesha uzalishaji wa bidhaa. Wizara inahimiza kila Wilaya kuanzisha mitaa ya viwanda vitakavyotumia malighafi zinazopatikana katika maeneo hayo ili kuhamashisha uongezaji thamani katika mazao hivyo kuinua kipato cha wananchi na kukuza ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha mapitio ya Sheria ya Vipimo, Sura ya 340 ili iendeane na mazingira ya sasa. Lengo la Serikali ni kumlinda muuzaji kwa kuwadhibiti wanunuzi wanaotumia njia za udanganyifu. Wizara yangu itawasilisha mabadiliko hayo Bungeni mara taratibu zitakapokamilika. Pamoja na marekebisho ya sheria ya vipimo niliyoitaja hapa juu, wakala wa Vipimo imewasilisha mapendekezo Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ya kutungwa kwa sheria ndogo (By- Laws) katika Mamlaka za Serikali za Mitaaa zitakazowaongoza wakulima na wafanyabiashara kufungasha mazao yao kwa mujibu wa sheria ya vipimo na kanuni zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kurahisisha usimamizi wa matumizi ya vipimo rasmi katika ununuzi wa mazao, Mamlaka za Serikali za Mitaa zitaainisha vituo maalum (Buying centers) katika vitongoji nchi nzima na kwa mazao yote na hivyo hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kusafirisha mazao ambayo yamefungashwa kinyume na sheria ya vipimo. Aidha, Wakala wa Vipimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa itaanzisha vituo maalum vya ukaguzi bila kusababisha usumbufu kwa wafanyabiashara. Maafisa Ugani walioko vijijini watumike kusimamia matumizi ya vipimo rasmi katika vituo hivyo na kutoa taarifa zote muhimu kwa wakala wa vipimo.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza.
Kiwanda cha Nyuzi Tabora hakiendelezwi kwa muda mrefu sasa:-
Je, Serikali itasaidia vipi kumwajibisha mwekezaji wa kiwanda hicho kwa kushindwa kukiendeleza?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Tabotex kilichopo Mkoani Tabora kilikuwa kikifanya shughuli ya usokotaji nyuzi tangu mwaka 1978 chini ya umiliki wa Serikali. Ilipofika mwezi Aprili, 2004. Serikali ilikibinafsisha kiwanda hicho kwa Kampuni za Noble Azania Investments Ltd na Rajani Industries ltd.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa wamiliki, kiwanda hicho kimesimamisha uzalishaji mwaka 2015 kutokana na changamoto ya soko la uzi ndani na nje ya nchi. Aidha, kiwanda bado kina akiba (stock) kubwa ya uzi uliozalishwa mwaka 2013, ambao hadi sasa bado unaendelea kuuzwa. Kawaida wanunuzi wakubwa wa uzi ni viwanda vinavyofanya shughuli ya ufumaji vitambaa, lakini viwanda vyote inavyofanya kazi ya ufumaji vitambaa (weaving) nchini vikiwemo 21st Century, Sunflag (T) Ltd, Urafiki, NIDA, na Musoma Textile vina mitambo yake ya usokotaji nyuzi, hivyo soko la ndani la Tabotex limekuwa likitegemea wafumaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hilo, kiwanda hicho hivi sasa kinatafuta mwekezaji ambaye atakuwa tayari kuingia nacho ubia kwa kupanua wigo wa uzalishaji na kufanya shughuli za ufumaji vitambaa (weaving) hadi ushonaji (finishing). Wakati huo huo, kwa kuwa kiwanda hicho ni moja viwanda vilivyobinafsishwa, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na tathmini ya kiwanda hicho na pindi tathmini hiyo itakapokamilika na tukajiridhisha kuwa mwekezaji huyo hajatimiza matakwa ya mkataba wa Serikali, Serikali itachukua hatua stahiki ambayo itakuwa na faidia kwa Serikali na wananchi kwa ujumla.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:-
Mkoa wa Tabora hauna viwanda kabisa na kwa sababu mkoa huu hulima tumbaku kwa wingi:-
Je, Serikali inasaidiaje kupata Kiwanda cha Tumbaku mkoani humo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kupitia TAMISEMI na hata kwenye Bunge lako Tukufu, Serikali imetoa mwongozo juu ya uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda na bayana tumeeleza wajibu wa kila mdau. Nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mkoa una viwanda. Mkakati wa Serikali ni kuhamasisha uwekezaji katika viwanda kwa nia ya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo yanayopatikana katika maeneo husika. Lengo ni kuongeza tija kwenye shughuli za wakulima ili kuongeza ajira na kipato.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Mkoa wa Tabora hulima tumbaku na msimu wa mwaka 2015 Tabora ilizalisha tumbaku tani 39,502 ambayo yote ilipelekwa Mkoani Morogoro kwa ajili ya kusindikwa. Tumbaku hiyo pamoja na nyingine kutoka Mikoa ya Nyanda za Juu husindikwa katika Viwanda vya Tanzania Tobacco Processing Limited- TTPL kinachosindika tumbaku asilimia 50 na Alliance One Tanzania Tobacco-AOTT asilimia 40 ya tumbaku inayolimwa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na mazungumzo na wawekezaji mahiri katika sekta ya kusindika tumbaku na kuzalisha sigara. Nirudie kueleza kuwa mpaka sasa tunaendelea kufuatilia wawekezaji kutoka Vietnam na China ambao tutawashawishi waje kusindika tumbaku na au kutengeneza sigara. Lengo letu ni kupata mwekezaji anayeweza kutengeneza sigara Tabora kwa “brand maalum” duniani na kwenda kuuza sigara hizo nje ya nchi yetu.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itasimamia kwa dhati sheria zake na kuondosha unyonyaji na ukandamizaji unaofanywa na wachuuzi kwa kununua mazao ya wakulima kwa utaratibu wa kufunga lumbesa?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondokana na unyonyaji na ukandamizaji unaofanywa na wachuuzi, Serikali imeamua kufanya mapitio ya Sheria ya Vipimo, Sura ya 340 ili iendane na mazingira ya sasa. Lengo la Serikali ni kumlinda muuzaji kwa kuwadhibiti wanunuzi wanaotumia njia za udanganyifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapitio ya sheria tajwa kwetu ni suala la kipaumbele. Katika kipindi kifupi kadri iwezekanavyo Wizara yangu itawasilisha mabadiliko hayo Bungeni ili Bunge lako Tukufu lifanye marekebisho yanayostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na marekebisho ya Sheria ya Vipimo yaliyotajwa hapo juu, Wakala wa Vipimo imewasilisha kwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, mapendekezo ya kutungwa kwa sheria ndogo (by laws) katika Mamlaka za Serikali za Mitaa zitakazowaongoza wakulima na wafanyabiashara kufungasha mazao kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo na Kanuni zake. Ili kurahisisha usimamizi wa matumizi ya vipimo rasmi katika ununuzi wa mazao, Mamlaka za Serikali za Mitaa zitaainisha vituo maalum (buying and selling centre) katika vitongoji nchi nzima na kwa mazao yote na hivyo hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kusafirisha mazao ambayo yamefungashwa kinyume na Sheria ya Vipimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wakala wa Vipimo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa itaanzisha vituo maalumu vya ukaguzi bila kusababisha usumbufu katika ufanyaji biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuwatangazia Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuunga mkono juhudi za kupiga vita matumizi ya vipimo batili katika ununuzi wa mazao ya wakulima ikiwa ni pamoja na kutenga na kuyasimamia maeneo maalum ya kuzuia mazao (buying and selling centres). Maafisa Ugani walioko vijijini watumike kusimamia matumizi ya vipimo rasmi katika vituo hivyo na kutoa taarifa zote muhimu kwa Wakala wa Vipimo.
MHE. ESTHER L. MIDIMU aliuliza:-
Vijana wengi wa Mkoa wa Simiyu hawana ajira kutokana na ukosefu wa viwanda mkoani humo na Serikali ilitunga Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda vya kusindika mwaka 1996-2020 itakayosimamia maendeleo ya kusindika mazao ya kilimo ili kuongeza thamani ya mazao:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga viwanda vya kusindika mazao katika Mkoa wa Simiyu?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vipaumbele vya Serikali hadi mwaka 2020 ni kuhimiza wawekezaji kujenga viwanda vinavyotumia malighafi za ndani hususan kwenye Sekta ya Kilimo na Maliasili, viwanda vinavyozingatia fursa za kijiografia, viwanda vinavyotoa ajira kwa wingi na vile vinavyochochea ujenzi wa viwanda vingine. Kwa sasa Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika maeneo hayo. Aidha, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda kwa kuzingatia vipaumbele tajwa ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo malighafi ya kutosha inapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo hayo napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa, tushirikiane kubaini fursa za uwekezaji katika viwanda, tuhamasishe wawekezaji na tuweke mazingira mazuri kwa wawekezaji popote nchini ikiwemo Mkoani Simiyu. Uwekezaji tunaoulenga hasa ngazi za vijiji mpaka wilayani ni ujenzi wa viwanda vidogo sana, viwanda vidogo na viwanda vya kati. Hili ndilo tabaka la viwanda linalotoa ajira kwa wingi, lakini tabaka linaloweza kusambaa kwa urahisi toka mijini mpaka vijijini. Mafanikio ya jukumu hili yanahitaji ushirikiano mkubwa kuanzia ngazi ya vijiji mpaka mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Kurugenzi ya Viwanda na Biashara ndogo pamoja na Taasisi za SIDO, TANTRADE, TBS na EPZA tuko tayari kushirikiana na mamlaka za Mkoa wa Simiyu ili kuhamasisha na kuwezesha ujenzi wa viwanda watakavyobaini na vile vilivyoahidiwa na viongozi wakuu wa Taifa hili.
MHE. JAMES K. MILLYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza wazo la kuanzisha mradi wa EPZ ambao umetengewa eneo kwenye Mji mdogo wa Mererani ili kuwezesha kuwepo kwa soko la Tanzanite Wilayani Simanjiro ambalo linadhibiti utoroshwaji wa madini ya Tanzanite na kuwapatia vijana wetu ajira?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa James Millya Kinyasi, Mbunge wa Simanjiro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara umetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 530.87 kwa ajili ya matumizi ya EPZ katika Kijiji cha Kandasikra - Mererani, Wilayani Simanjiro. Pamoja na kwamba juhudi za kutenga eneo hilo zilianza mwaka 2007, bado halikuwa tayari kwa uendelezaji kutokana na taratibu za kuhamisha miliki ya ardhi kuchukua muda mrefu. Taratibu hizo zimekamilika mwezi Julai, 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ucheleweshaji pia ulichangiwa na kuchelewa kulipwa kwa fidia kwa wananchi sita ambao walikuwa hawajafanyiwa uthamini waliokuwa wanadai jumla ya shilingi milioni 15.05. Mamlaka ya EPZ kupitia Halmashauri ya Simanjiro ilifanikiwa kulipa fedha hizo tarehe 31 Machi, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa eneo hilo lipo huru na hivyo taratibu za uendelezaji, ikiwemo kuandaa mpango kabambe wa uendelezaji wa eneo hilo (Master Plan) na hatimaye kuanza ujenzi wa miundombinu wezeshi kama barabara, umeme, maji, mifumo ya maji machafu, majengo ya huduma zitafanyika. Maandalizi hayo ya ujenzi wa miundombinu yatafanyika sambamba na uhamasishaji wa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kuwekeza katika eneo hilo.
MHE. JOSEPHINE T. CHAGULA aliuliza:-
Vijana wengi wa Mkoa wa Geita hawana ajira kutokana na ukosefu wa viwanda na hasa ikizingatiwa kuwa sehemu kubwa ya uchumi wetu unategemea kilimo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga viwanda vya kusindika mazao katika Mkoa wa Geita?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI, alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Thabita Chagula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa viwanda katika kuchangia ukuaji wa nchi, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia mkakati unganishi wa maendeleo ya viwanda (Integrated industrial Development Strategy), lengo ni kuhamasisha wananchi na wadau kuwekeza katika kuanzisha viwanda. Viwanda hivyo ni pamoja na viwanda vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa vyenye lengo la kuzalisha bidhaa zinazotokana na rasilimali zinazopatikana hapa nchini zikiwemo zile za kilimo, mifugo, uvuvi, misitu na madini zitakazounganisha nchi nzima pamoja na Mkoa wa Geita.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati huo pia unazitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa na Miji kutenga maeneo ya uwekezaji katika viwanda hadi ngazi ya Kata ambayo itatumika kuanzisha Mitaa ya Viwanda kwa kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo husika. Wizara itakuwa na jukumu la kuwaelimisha, kuwahamasisha na kuwajengea uwezo wananchi ili waweze kuanzisha viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara inamfuatilia mwekezaji ambaye ni bingwa wa kutengeneza juice akichukua kati ya namba tano mpaka saba duniani ili ajenge kiwanda mkoani Geita. Ujenzi wa kiwanda hicho utaenda sambamba na uwekezaji katika kilimo cha kisasa ambapo makubaliano yatafikiwa kwa kuwa na nuclear farm na wakulima wanaomzunguka kuweza kupatiwa huduma (outgrowers). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Wizara kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) itaendelea kushirikiana na wadau Mkoani Geita kuibua miradi kupitia program ya Wilaya Moja, Bidhaa Moja, (One District One Product-ODOP) kwa lengo la kuanzisha na kukuza viwanda katika ngazi ya Wilaya na hivyo kuleta ajira kwa vijana vijijini. Hatua hiyo itasaidia kupunguza wimbi kubwa la sasa lililopo la vijana kukimbilia Mijini sambamba na kuongeza pato binafsi na pato la Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane katika kuhamasisha na kuvutia sekta binafsi kuwekeza na kutumia fursa zilizopo katika Mkoa wa Geita.
Ujenzi wa Soko la Kimataifa Mpaka wa Kagunga

Je, ni lini Serikali itajenga soko la Kimataifa Kagunga mpakani mwa Tanzania na Burundi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kujenga soko la kisasa la Kimataifa la Kagunga jirani na Mpaka wa nchi yetu na Burundi lenye ukubwa wa hekta 1.5. Tayari Manispaa ya Kigoma imetenga shilingi milioni 250 kwa bajeti yake ya mwaka 2015/2016 kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo, juhudi za kumpata mzabuni wa kujenga soko hilo zinaendelea. Pamoja na jitihada hizo, mwekezaji kutoka United Nations Capital Development Fund pia ameonyesha nia ya kuwekeza kwenye miundombinu ya masoko, ameanza ujenzi na anajiandaa kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na soko hilo, Serikali kupitia mamlaka ya EPZ, imetenga eneo la hekta 20,000 kwa ajili ya uwekezaji yakiwa ni maeneo ya viwanda, makazi, biashara pamoja na Mkoa wa Kigoma (Kigoma Special Economic Zone).Hadi sasa hekta 700 zimepimwa na wananchi 369 kati ya 360 wamelipwa fidia ya maeneo yao, jumla ya shilingi bilioni 1.03 ambayo ni sawa na asilimia 61 imetumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, upimaji na uandaaji wa michoro ya matumizi unaendelea na utengaji wa maeneo hayo karibu na miji utasaidia kasi ya kuleta maendeleo na ushindani kuinua uchumi wa wananchi wa Kigoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa wito kwa Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine, kuhamasisha wawekezaji na wadau wa maendeleo kufanikisha ujenzi wa masoko ya mipakani kwani ujenzi wa masoko hayo unahitaji sana nyongeza na nguvu za wananchi kuongeza jitihada za Serikali.
MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-
Halmashauri za Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na Kampuni ya HELM wanakusudia kujenga Kiwanda cha Mbolea huko Msanga Mkuu, Mtwara Vijijini.
Je, ni lini Serikali itaridhia mradi huo kuanza?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Awa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kiwanda cha mbolea na ni mshirika mkuu wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha mbolea huko Msanga Mkuu-Mtwara Vijijini. Baada ya kufanya tathmini ya kitaalamu juu ya mahitaji ya gesi kwa ajili ya kiwanda hicho na kwa kuzingatia matumizi ya gesi nchini (Gas Utilization Master Plan) pia kwa kuzingatia hazina ya gesi tuliyonayo kwa sasa katika visima vya nchi kavu na baharini, kampuni ya HELM imealikwa kuwasili nchini kwa ajili ya majadiliano ya utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Awa Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na nilihakikishie Bunge lako Tukufu na Watanzania wote kuwa kwa hazina ya gesi tuliyonayo sasa Tanzania ya TCF 57.25 tuna uwezo wa kuwapatia HELM kiasi cha million cubic fit 104 kiasi wanachohitaji kwa siku wamalizapo kujenga kiwanda hicho.
MHE. STEPHEN J. MASELE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itataifisha Kiwanda cha Nyama Shinyanga Mjini baada ya mwekezaji kushindwa kukiendesha?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Julius Masele, Mbunge wa Shinyanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuvirudisha viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo havifanyi kazi ili vifanye kazi, viongeze ajira na kuchangia Pato la Taifa. Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina tunafuatilia mikataba ya viwanda vyote vilivyobinafsishwa na kufanya tathmini ya kina ili kujiridhisha kabla ya kuvirejesha Serikalini. Tathmini hiyo inaendelea nchi nzima ikihusisha wataalam kutembelea mikoa yote ya Tanzania ili kujua hali halisi ya viwanda hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Nyama Shinyanga ni kati ya viwanda 55 vilivyofanyiwa tathmini kwa lengo la kukagua ufanisi na kuhakiki utekelezaji wa masharti kulingana na mikataba ya ununuzi kwa mujibu wa agizo la Mheshimiwa Rais wakati wa ufunguzi wa Bunge la Kumi na Moja. Aidha, Wizara yangu kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina wameshakutana na mwekezaji wa Kiwanda cha Triple S Beef Ltd na Msajili wa Hazina amemtaka mwekezaji wa kiwanda hicho kuwasilisha mpango mkakati na andiko la biashara wa kuendeleza kiwanda hicho. Nia ya Serikali ni kumpa fursa ya kwanza mwekezaji huyo ili aendeleze kiwanda kama ilivyokubalika kwenye mkataba wa kuuziana. Endapo atashindwa kutumia fursa hii ya mwisho aliyopewa kiwanda kitatwaliwa wala siyo kwamba kitabinafsishwa.
MHE. JOHN P. KADUTU (K.n.y. MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA) aliuliza:-
Serikali ina mpango wa kujenga maabara ya kupima ubora na kiwango cha asali inayozalishwa hapa nchini.
Je, ni kwa nini Serikali isijenge maabara hiyo mkoani Tabora ambako ndipo kunazalishwa asali nyingi kuliko mkoa wowote nchini?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali namba 84, kwa ruhusa yako nilikuwa naomba uniruhusu niseme kidogo juu ya janga lililowapata wananchi wa Tanzania, hususan Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Kamati ya Uongozi ya Bunge na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa namna ambavyo kipekee mliguswa na tatizo la wananchi wenzetu wa Tanzania walioko mkoani Kagera. Lakini nichukue fursa hii kuwashukuru wananchi na wadau ambao waliitikia wito wa Mheshimiwa Waziri Mkuu jana na kufika kumuunga mkono na kuweza kukusanya bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 1.369.
Nichukue fursa hii Waheshimiwa Wabunge, tusaidiane na Serikali kuhamasisha njia hii. Kiasi kilichokusanywa jana tulijiandaa kwa saa 30, tukijiandaa wote kwa pamoja tutatunisha Mfuko wa Maafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nichukue fursa hii kuwapa pole wananchi wa Mkoa wa Kagera, hasa Wilaya za Muleba, Karagwe, Kyerwa, Bukoba Vijijini, Bukoba Mjini na Misenyi, watulie Serikali ipo na Serikali itahakikisha hali inarudi katika hali ya kawaida na kimsingi baada ya kujibu swali hili itabidi niondoke mwenyewe niende site. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijibu swali namba 84. Upimaji wa ubora na viwango vya bidhaa aina ya asali unafuata kiwango chenye namba 851 cha mwaka 2006. Chini ya kiwango hiki maelezo na vigezo vimetolewa ambavyo mzalishaji, mtunzaji, muuzaji na mpimaji wanapaswa kuzingatia ili asali iwe katika ubora unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wadau wote kwa kufuata vigezo na maelezo katika kiwango namba 851 wanaweza kupima asali; hata hivyo, maabara kuu inayopaswa kutoa uthibitisho ipo TBS Dar es Salaam. TBS Makao Makuu ndio wanaopaswa kisheria kutoa hati ya ubora chini ya utaratibu maalum. Tunapoendelea kuhimiza ujenzi wa viwanda, ikiwemo viwanda vya asali, tutahakikisha viwanda hivyo vinakuwa na maabara zinazoweza kupima viwango vya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa maabara Tabora, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, wawekezaji ambao wanafuatilia ujenzi wa viwanda vya asali mkoani Tabora, Wizara yetu itahakikisha wanakuwa na maabara za kupima viwango vya msingi na kuiachia TBS kuweka Viwango vya Kitaifa na kudhibiti viwango hivyo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliahidi kuvirudisha Serikalini viwanda vyote vilivyobinafsishwa, lakini havifanyi kazi.
Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa ahadi hiyo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa agizo la Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, la kuhakikisha viwanda vilivyobinafsishwa vinafanya kazi, lilianza kutekelezwa mwezi Novemba, 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya kwanza ilikuwa ni Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwataka wote waliopewa viwanda katika mtindo huo kutoa taarifa ya kina ya utendaji wa viwanda hivyo. Timu ya wataalam kutoka Wizara ya Viwanda na Ofisi ya Msajili wa Hazina walifuatilia na wanaendelea kutathmini kwa kutembelea kiwanda baada ya kiwanda, ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayosababisha kiwanda kutokufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya taratibu hizo hapo juu, Wizara yangu inaendelea na zoezi la kuchambua mikataba ya mauzo kwa viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo ama havifanyi vizuri au vimesimama uzalishaji kabisa. Uchambuzi huo unafanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na Wizara za kisekta ambazo ni Maliasili na Utalii, Nishati na Madini, Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Uchambuzi huo unaangalia hali ya umiliki, wajibu wa mwekezaji, wajibu wa Serikali, utekelezaji wa mkataba wa mauzo, hali ya sasa ya kiwanda na hivyo kutoa mapendekezo ya hatua stahiki. Zoezi hili linaenda sambamba na ulinganishaji wa taarifa za uwekezaji katika viwanda vilivyobinafsishwa zilizowasilishwa kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina na wamiliki wa viwanda hivyo kama nilivyoeleza hapo awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tathmini ya hali ya viwanda nayo inaendelea kufanyika kwa ushirikiano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ambapo viwanda 45 tayari vimefanyiwa tathmini. Kati ya viwanda hivyo, viwanda vinne vimeonesha dalili kuwa wawekezaji wa sasa hawana uwezo wa kuvifufua hivyo, kuwa na uwezekano wa Serikali kutafuta wawekezaji wengine. Taarifa ya tathmini itakapokamilika itawasilishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupata maoni ya kisheria katika njia muafaka ya kutwaa viwanda hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua nyingine ambayo tumeichukua katika kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ni Serikali kukitwaa kiwanda cha chai Mponde (Mponde Tea Estate Limited) kilichopo Lushoto – Tanga, ambacho mwekezaji amekiuka makubaliano ya kimkataba. Kiwanda hicho kilitwaliwa tarehe 29 Januari, 2016 na tayari mazungumzo kati ya Serikali na Mfuko ya Hifadhi ya Jamii wa Local Authority Provident Fund – LAPF yanaendelea. Mazungumzo hayo ni matokeo ya maagizo ya Mheshimiwa Rais kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza katika sekta ya viwanda.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
Tanzania tunalima pamba kwa wingi lakini bado tunaagiza Gauze toka Uganda ambao hawana zao la pamba, lakini pia tunaagiza Drip toka nje ya nchi wakati tuna maji ya kutosha ya kuweza kutengeneza Drip hizo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia malighafi hizo ili kuzalisha Gauze na Drip hapa nchini na kuacha kuagiza bidhaa hizo toka nje?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Khadija alivyotoa mfano wa gauze na Intravenous Fluid zinazotundikwa wagonjwa na kujulikana kama drip tumekuwa tukiagiza bidhaa toka nje ya nchi ambazo kimsingi zinaweza kutengenezwa kirahisi hapa nchini. Ukirejea mkakati unganishi wa maendeleo ya viwanda IIDS na Mpango wa Pili wa Miaka Mitano, lengo lake hasa ni kuondoa upungufu huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia mashirika ya MSD, TIRDO, NHIF, TIB, TFDA wamepewa jukumu la kuandaa mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza katika Sekta ya Madawa ya Binadamu na Vifaa Tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa bidhaa inayolengwa ni ya IV Fluids na gauze zitokanazo na pamba. Chini ya uhamasishaji wa Wizara yangu na Kituo cha Uwekezaji (TIC), wawekezaji wamejitokeza kuwekeza katika Sekta ya Madawa ya Binadamu na Vifaa Tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako nitaje baadhi ya makampuni ambayo yamejitokeza. JSN solution watakaojenga kiwanda cha IV Fluid, China Dalian International group watakaojenga kiwanda cha kutengeneza vifaa tiba, Zinga Pharmaceutical watakaotengeneza madawa mbalimbali ya binadam; Boryung Pharmaceutical kutoka Korea ambao watatengeneza Penicilin na Antibiotics za namna hiyo; Agakhan Foundation Network watakaoanzisha viwanda vya madawa mbalimbali na Hainan Hualon ambao watazalisha madawa mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu kuwa katika hiki kipindi kifupi, tutaweza kuwa na sekta ya madawa ya binadamu ambayo pamoja na kuzalisha madawa na vifaa tiba itatoa ajira kwa vijana wetu.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y MHE. GODBLESS J. LEMA) aliuliza:-
Mahitaji ya tairi za magari katika Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla ni makubwa. Mpango wa Serikali kufufua kiwanda cha tairi cha General Tyre unaonekana kwenda taratibu:-
(a) Je, ni lini Serikali itatambua umuhimu wa kiwanda hicho kuanza uzalishaji mapema;
(b) Wapo baadhi ya waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho bado hawajalipwa mafao tangu kiwanda kifungwe: Je, Serikali ina mpango gani wa kuwahakikisha wafanyakazi hao wanalipwa stahili zao?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inatambua na kuthamini uwepo wa kiwanda cha kutengeneza matairi nchini. Ili kutimiza azma hiyo, Wizara yangu kama tulivyoelekeza katika Bajeti ya Mwaka 2016/2017 tumeanza jukumu hilo kwa kubaini mambo ya msingi tunayopaswa kuzingatia katika kujenga kiwanda cha matairi ambacho imara na shindani. Baada ya taarifa ya kitaalam (Roadmap) ambayo itakamilika wakati wowote, kwa kushirikisha ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwepo Kamati ya Bunge inayosimamia Viwanda, Biashara na Mazingira, uamuzi juu ya uwekezaji utafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji kiwanda cha matairi ili kutekeleza dhima ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Kiwanda hiki kitatoa ajira, kitazalisha bidhaa bora, salama na imara na kwa kuzalisha tairi nyingi tutaokoa fedha za kigeni zinazotumika sana kuagiza matairi kutoka nje ya nchi. Pia uwepo wa kiwanda hicho ni kichocheo kwa soko la malighafi ya mpira ambalo tuna fursa ya kuzalisha kwa wingi hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, mtupe muda tusimamie kikamilifu utekelezaji wa jukumu hili muhimu.
MHE. GIBSON B. MEISEYEKI aliuliza:-
Wakulima na wafugaji wa Tanzania hawajawahi kuwa na uhakika wa bei ya mazao yao hasa katika msimu wa mavuno ya kutosha badala yake wanageuka watumwa wa mazao yao wenyewe kwa kukosa masoko, maghala na bei zuri ya mazao.
Je, ni lini tatizo hili litaisha ili kuwezesha Watanzania wengi zaidi kujiingiza kwenye kilimo na ufugaji?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Gibson Ole-Meiseyeki, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama alivyoeleza Mheshimiwa Gibson, uhakika wa bei na masoko ya mazao ya kilimo umekuwa ni changamoto kwa wakulima na wafugaji wetu. Kwa kutambua hilo Serikali ilibuni Sera ya Masoko ya Mazao ya Kilimo mwaka 2008 mahususi kwa kuimarisha mifumo ya masoko ya mazao nchini. Aidha, mkakati unganishi wa maendeleo ya viwanda wa mwaka 2020 (intergrated industrial development strategy 2020 – IIDS) na Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano wenye lengo la kujenga uchumi wa viwanda umezingatia kwa dhati uongezaji thamani wa malighafi za kilimo ili wakulima wapate masoko ya uhakika.
Mheshimiwa Spika, viwanda vya kipaumbele vinavyolengwa katika mkakati na mpango huo ni pamoja na viwanda vya kusindika mbegu za mafuta, kutengeneza nguo na mavazi, kubangua korosho, kutengeneza ngozi na bidhaa zitokanazo na ngozi, viwanda vya nyama, viwanda vya maziwa, uzalishaji wa sukari na usindikaji wa matunda na mboga mboga.
Mheshimiwa Spika, aidha, ili kufanikisha uhakika wa ubora, wingi wa malighafi na bei nzuri kwa wakulima, Serikali inaendelea kuimarisha Mfuko wa Stakabadhi za Ghala ambao unawezesha mazao kutunzwa na kupunguza uharibifu wa mazao baada ya kuvuna (post harvest loss).
Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mipango iliyotajwa hapo juu itatuwezesha kutengeneza masoko ya uhakika na bei nzuri kwa wakulima na wafugaji. Kama ambavyo tumekuwa tukihimiza mara kwa mara tutashirikiana na kuiwezesha sekta binafsi kujenga viwanda.
Mheshimiwa Spika, Maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya masoko kama vile maghala ya kuhafadhia mazao, barabara za vijijini na utoaji wa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa uzalishaji wa tija.
MHE.GIMBI D. MASABA aliuliza:-
Kutokana na mpango wa Serikali kuhakikisha ifikapo mwaka 2025, Tanzania inafikisha uchumi wa kati.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha na kuhalalisha viwanda vya kutengeneza pombe aina ya gongo ili kuchochea uchumi wa nchi?
(b) Pombe hii aina ya gongo inapendwa kunywewa zaidi na watu wa vijijini. Je, Serikali haioni kwamba umefika wakati wa kuwaendeleza kielimu zaidi wataalam hao wanaotengeneza pombe hiyo ili wapate ujuzi kwa maslahi ya Taifa?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, viwanda anavyosema Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba ni tabaka la viwanda vidogo sana na viwanda vidogo. Viwanda hivi ni fursa ya sekta ya binafsi kuwekeza. Serikali inalenga viwanda vikubwa sana na miradi ya kimkakati.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuhalalisha pombe aina ya gongo kama ilivyo sasa ni jambo ambalo haliwezekani, ila sekta binafsi inashauriwa kuanzisha viwanda vitakavyotumia malighafi zinazotengeneza kinywaji hicho kwa lengo la kuzalisha kinywaji kinachokidhi viwango vya usalama na ubora wa chakula.
Naomba nirudie, kinywaji hicho kwa kuzingatia ubora na usalama wa mnywaji.
Mheshimiwa Spika, moja ya kigezo muhimu cha kuanzisha kiwanda ni uwepo wa soko. Kutokana na wananchi kupendelea kinywaji hiki, nitumie fursa hii kuwashauri wadau wa sekta hii kuwasiliana na ofisi za SIDO ambazo zinapatikana mikoa yote ili kupata mwongozo juu ya uanzishaji viwanda bora na salama vya aina hii.
Kwa upande wa Makampuni makubwa ya pombe nawashauri wachangamkie fursa hii kwa kutengeneza pombe yenye ladha ya gongo kwani baadhi ya wateja ni ile ladha inayowavutia na kupendelea kinywaji hicho.
MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:-
Wananchi wengi katika Kijiji cha Guta na Tairo walitoa ardhi yao kwa ajili ya mradi wa EPZA, sasa ni takribani miaka saba tangu kufanyiwa tathmini, pia wananchi hao hawaruhusiwi kuendeleza maeneo hayo.
Je, ni lini wananchi wa vijiji hivyo watalipwa fidia halisi kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 5 ya mwaka 1999 Kifungu cha 3(1)(g)?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, taratibu za kutwaa eneo la EPZ/SEZ Mara zilianza mwaka 2007 kwa kutambua mipaka ya eneo. Eneo lililopendekezwa ni la Kijiji cha Tairo kilichopo Kata ya Guta, Wilayani Bunda na lilikuwa na ukubwa wa hekta 2,200 likijumisha vitongoji vya Kirumi, Mabatini A & B na Bushigwamala. Uthamini wa eneo la mradi ulikamilika mwezi Julai, 2009 na taarifa yake kuidhinishwa na Mthamini Mkuu wa Serikali mwezi Septemba, 2009. Kwa mujibu wa uthamini, fidia iliyotakiwa kulipwa kwa eneo lote ni shilingi bilioni 3.477.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ufinyu wa bajeti, Mamlaka ya EPZ iliamua kupunguza ukubwa wa eneo na hivyo kuendelea na utwaaji wa eneo la kitongoji kimoja cha Kirumi. Aidha, fidia iliyohitajika kufidia eneo hilo ilikuwa ni shilingi bilioni 2.143 zilizopaswa kulipwa ndani ya miezi sita bila riba. Tayari Mamlaka ya EPZ ilikwishapeleka jumla ya shilingi bilioni 2.358 kwa ajili ya malipo ya fidia ikijumuisha riba ya ucheleweshaji. Fedha hizo zililipwa kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2009 na 2012 kwa wadai wote, isipokuwa wananchi watatu ambao Ndugu Chacha M. Marwa, Ndugu Gati M. Marwa na Ndugu Juma W. Mgoba, ambao bado wanadai jumla ya shilingi milioni 21.943 licha ya EPZ kupeleka fedha zote kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuchelewa kwa malipo hayo, tarehe 20 Mei, 2016 aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara aliagiza TAKUKURU na CAG wafanye uchunguzi wa matumizi ya fedha zilizotolewa na EPZA. Taarifa hiyo inasubiriwa ikamilike na pindi itakapokamilika hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watumishi waliohusika na ubadhilifu wa fedha hizo.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:- Kumekuwa na bidhaa fake katika nchi yetu na zinagundulika zikiwa zimeingia nchini. Je, Serikali haioni kuwa kugundua bidhaa hizo zikiwa ndani ya nchi zinakuwa tayari zimewaathiri wananchi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge, kugunduliwa kwa bidhaa fake au bandia zikiwa ndani ya nchi zinakuwa tayari zimewaathiri wananchi. Ili kukabiliana na tatizo la bidhaa hizo kuingia nchini na kuleta madhara kwa watumiaji Serikali kupitia Tume ya Ushindani (Fair Competition Commission) kwa kushirikiana na wamiliki wa nembo za bidhaa mbalimbali imekuwa ikitekeleza mikakati ya kuhakikisha bidhaa fake haziingii nchini. Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kwa lengo la kuwafahamisha wananchi madhara ya bidhaa bandia kiafya, kiuchumi na kimazingira na jinsi ya kutambua bidhaa bandia. Elimu hiyo hutolewa kupitia warsha, makongamano, maonesho ya biashara, vyombo vya habari kama redio, luninga, mitandao ya computer na magazeti. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika njia za kuingizia bidhaa, ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Viwanja vya Ndege vya JK Nyerere, KIA na mipaka inayopitisha bidhaa kutoka nje ya nchi kwa wingi. Pia, kaguzi za kushitukiza hufanyika katika maduka na maghala yanayohisiwa kuhifadhi na kuuza bidhaa bandia kinyume na Sheria ya Alama za Bidhaa ya mwaka 1963 na marekebisho yake ya mwaka 2012. Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali inadhibiti uingizaji wa bidhaa bandia nchini kwa kuimarisha ukaguzi wa bidhaa nje ya nchi kabla ya kuingizwa nchini (Pre Shipment Verification of Conformity Standard). Kuendelea kuajiri wataalam zaidi na kufungua vituo vya ukaguzi wa ubora wa bidhaa katika mipaka zinapoingilia bidhaa kutoka nchi nyingine. Mipango hiyo inahusu mipaka ya Horohoro, Holili, Namanga, Sirari, Mutukula, Kabanga, Rusumo, Tunduma na Kasumulo. Aidha, Fair Competition Commission hushirikiana na taasisi za Serikali hususan Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), TBS, Jeshi la Polisi, Serikali za Mitaa na wananchi wenye mapenzi mema ili kufanikisha ukaguzi na uteketezaji wa bidhaa bandia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itaendelea kuwachukulia hatua wale wote watakaohusika na uingizaji wa bidhaa bandia, ikiwa ni pamoja na kuteketeza bidhaa hizo au kuzirejesha zilikotoka.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza:- Mkoa wa Iringa ulitenga eneo la EPZ katika Wilaya ya Kilolo. Je, ni lini eneo hilo litaanza kuendelezwa na ni nini faida ya EPZ?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Venance Methusalah Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni maagizo ya Serikali kwa mikoa yote nchini kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji kwa mfumo wa EPZ na SEZ. Baada ya Serikali katika ngazi ya Mikoa na Wilaya kutenga maeneo hayo inatoa taarifa kwa Mamlaka ya EPZ, ili maeneo hayo yaweze kutangazwa kama maeneo huru ya uwekezaji nchini chini ya Mamlaka ya EPZ. Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Mamlaka ya EPZ haijakabidhiwa eneo lililotengwa kwa ajili ya uzalishaji katika Wilaya ya Kilolo kama ilivyobainishwa. Hii inazingatia kuwa tangu kufutwa kwa umiliki wa kwanza wa shamba hilo, kupitia Tangazo la Serikali Namba 130 la tarehe 17 Februari, 2012 taratibu za kulitangaza kama EPZ zilikuwa hazijakamilika. Hata hivyo, Halmashauri imeanza hatua ya awali ili iweze kukamilisha taratibu za kukabidhi eneo la Ruhundamatwe lililotengwa kwa ajili ya uendelezaji wa viwanda. Michoro (master plan) ya eneo husika imekamilika na kazi inayoendelea sasa ni kupima eneo husika. Kazi hiyo ikikamilika Halmashauri hiyo itakabidhi rasmi eneo husika kwa Mamlaka ya EPZ kwa ajili ya uwekezaji. Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji chini ya Mamlaka ya EPZ una faida zifuatazo:- Mheshimiwa Spika, kwanza, kukuza mauzo nje ya nchi hivyo, kuongeza mapato ya fedha za kigeni; pili, kukuza sekta ya viwanda; tatu, kuongeza ajira na kufundisha stadi za uzalishaji viwandani; nne, kuendeleza uhawilishaji wa teknolojia ya viwanda; tano, kuhamasisha isindikaji wa mazao yetu na uchakataji wa malighafi ili kuongeza thamani; na ksita, uchangia katika kuongeza kipato kwa wananchi, hivyo kupunguza umaskini.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS Aliuliza:-
Biashara ya vyuma chakavu imeshamiri sana Tanzania Bara na Visiwani na imesababisha madhara ya kuharibiwa na kuibiwa kwa miundombinu yakiwemo mifuniko ya chemba na majitaka.
(a) Je, Serikali imejipangaje kupambana na wizi na uharibifu huo wa mali za Serikali na wakati walinzi wa maeneo husika wanashuhudia hayo?
(b) Je, Serikali haioni kwamba hata usalama wa raia na mali zao uko mashakani?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI
Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis kuwa biashara ya chuma chakavu imeshamiri hapa nchini na duniani kwa ujumla. Kuongezeka kwa mahitaji (demand) ya vyuma chakavu kulitumiwa na wahalifu kuharibu miundombinu iliyojengwa kwa vyuma kwa nia ya kupata chuma ili waiuze kama chuma chakavu. Maeneo yaliyoathirika sana ni mifumo ya kusafirisha umeme, reli, barabara kwa kutaja baadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na hujuma hizi mamlaka husika yaani TANESCO, TANROADS na RAHCO wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na Jeshi la Polisi ikiwemo kutumia walinzi wa taasisi husika kulinda rasilimali hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupata suluhu ya kudumu, Wizara yangu imekwishaandaa rasimu ya muswada wa sheria itakayoweka bayana taratibu na mfumo wa usimamizi na udhibiti wa biashara ya chuma chakavu katika hatua mbalimbali za uzalishaji, ukusanyaji, usambazaji, uuzaji na uyeyushaji wake kwa kuzingatia uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa manufaa ya Taifa. Aidha, muswada huo umeweka bayana adhabu itakayotolewa kwa mtu yeyote atakayebainika kuharibu miundombinu kwa sababu ya kuchukua chuma chakavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge na Watanzania kwa ujumla usalama wao na mali zao ziko salama. Aidha, nitumie fursa hii kuwaomba wananchi wote kutoa taarifa pindi wawaonapo mtu anayehujumu miundombinu kwa namna yoyote ile kwa lengo la kuchukua chuma chakavu au chuma. Kwa wenye viwanda na wafanyabiashara wa vyuma chakavu jiepusheni na ununuzi wa vyuma ambavyo asili yake inatia mashaka. Kama nilivyoeleza awali, tutaharakisha sheria ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kutatua tatizo hili.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-
Alizeti ndiyo zao kubwa la biashara na limekuwa kimbilio kubwa kwa maisha ya wananchi wa Mkoa wa Singida. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 Singida ilipatiwa mashine ndogo tisa za kukamulia alizeti ambazo hazikidhi matarajio ya wakulima katika kujikwamua kiuchumi na alizeti inayozalishwa mkoani humo ambayo ni bora Afrika ya Mashariki na Kati haijapatiwa soko la uhakika kwa maana ya kuwa na viwanda vya kutosha ili wakulima waweze kuuza zao hilo kwa urahisi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuanzisha viwanda vya kisasa vya kukamulia mafuta ya alizeti Mkoani Singida?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mkakati wa Fungamanisho la Maendeleo ya Viwanda la mpaka mwaka 2025, mkakati uliozinduliwa Desemba, 2011 na Mkakati Maalum wa Kuendeleza Sekta ya Alizeti, 2016 mpaka 2020 uliozinduliwa mwaka 2016, tunaendelea na uhamasishaji wa zao la alizeti nchini. Moja ya mpango wa kuendeleza sekta hii ni kuhamasisha uongezaji wa thamani hapa nchini kwa kutumia viwanda vya aina zote. Kwa Mkoa wa Singida, mpaka Desemba, 2016 tulikuwa na viwanda vidogo 126, viwanda vya kati viwili na kiwanda kimoja kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada nyingine za Serikali ni kuuweka Mkoa wa Singida katika kundi la mikoa inayonufaika na Mfuko wa SME Credit Guarantee Scheme unaoendeshwa kwa ubia kati ya SIDO na Benki ya CRDB. Pia ubunifu wa Shirika la TEMDO wa kuchonga vipuri vya mashine za kukamua alizeti na business-re-engineering ya mashine za alizeti unalenga kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda vya alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii ya swali hili kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kukamua na kuchuja alizeti. Kiwanda kidogo sana kinakadiriwa kuwa na gharama kati ya shilingi milioni 10 mpaka shilingi milioni 15; kiwanda kidogo kati ya shilingi milioni 16 mpaka 200 ambacho kina uwezo wa kukamua na kuchuja kwa kiwango kidogo. Kiwanda cha kati kinachoweza kukamua na kuchuja mara mbili (double refinery) kinagharimu kati ya shilingi milioni 200 mpaka milioni 500.
MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:-
Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa ambayo haina viwanda licha ya wananchi wake kuwa wakulima na wafugaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga viwanda vingi Mkoani Simiyu wikiwemo viwanda vya kusindika nyama, matunda, maziwa, ngozi, mafuta ya kula na nguo ili kuharakisha ukuaji wa uchumi na ongezeko la ajira kwa vijana?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, azma ya Serikali ya ujenzi wa uchumi wa viwanda imeainishwa vyema katika Mpango wa Pilli wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa mwaka 2016/2017 mpaka 2020/2021 wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Ili kufikia azma hiyo, ushiriki wa mchango wa mtu mmoja mmoja, makundi ya watu, taasisi za umma na taasisi binafsi unahitajika. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine tumeanza kutekeleza mikakati minne ya ngozi, mafuta ya kula, nguo na mazao jamii ya kunde. Wakati huo huo mapango wa wilaya moja, zao moja na uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda chini ya SIDO unaendelea nchini kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla kuwa Mkoa wa Simiyu chini ya uongozi wa Komredi Anthony Mtaka umekuwa kinara wa kutekeleza mpango wa one district one product. Wilaya
tano za Bariadi, Busega, Itilima, Maswa na Meatu katika Mkoa wa Simiyu zimepangiwa kuzalisha mafuta ya alizeti. Vilevile Mkoa wa Simiyu una viwanda ambavyo vinaanzishwa kwa kuzingatia upatikanaji wa malighafi, teknolojia na soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Maswa kimejengwa kiwanda cha chaki, Wilaya ya Bariadi na Itilima kitajengwa kiwandacha nyama na Wilaya ya Meatu kimejengwa kiwanda cha Maziwa. Hizi ni kazi ya mwaka mmoja na naweza kusema ni mwanzo mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa taasisi, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unakamilisha taratibu za kuwekeza kwenye kiwanda cha kuzalisha vifaa tiba vitokanavyo na pamba na bidhaa za maji (drip). Gharama za miradi hiyo inakadiriwa kufikia dola za kimarekani 36.5 na kutoa ajira za moja kwa moja 1,600 na zisizo kuwa moja kwa moja 5,000. Mradi huo unakadiriwa kutumia pamba tani 50,000 kwa mwaka. Aidha, Serikali ya Mkoa inaendelea na jitihada za kutenga maeneo ya uwekezaji kwa kuwalenga wajasiriamali wadogo, wa kati mpaka wakubwa bila kujali kwamba wanatoka ndani ya nchi au nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshauri Mheshimiwa Mbunge tushirikiane katika kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuanzisha viwanda na kusindika mazao ya kilimo katika Mkoa wa Simiyu ili kuhakikisha ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa vijana.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y. MHE. GODBLESS J. LEMA) aliuliza:-
Agizo la Mheshimiwa Rais la kufufua viwanda ni muhimu na la msingi kwa maendeleo ya Taifa:-
Je, Serikali haioni mradi wa Kurasini Logistic Centre unakwenda kinyume na fikra za Mheshimiwa Rais kuhusu viwanda?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimshukuru Mheshimiwa Godbless Lema kwa kutambua na kuthamini fikra za Mheshimiwa Rais juu ya azma ya kujenga Tanzania ya viwanda. Mchango wake na Wabunge wote katika kuhamasisha dhima ya Mpango wa Pili wa Miaka Mitano ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Mradi wa Kurasini Logistic Centre tunaouhamasisha sasa ni mchango na chachu ya maendeleo ya uchumi wa viwanda. Dhamira yetu ni kuona mradi huo unaendeshwa na sekta binafsi kwa misingi ya kibiashara. Serikali imefidia eneo hilo kwa takribani shilingi bilioni 101 hivyo kiasi hicho ni mtaji wa Serikali katika mbia atakayechaguliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Kurasini Logistic Centre mwekezaji atawajibika kufanya yafuatayo:-
(i) Kujenga miundombinu ya viwanda ikiwemo ma-
godown ya viwanda, barabara, mifumo ya nishati na maji;
(ii) Kutafuta wawekezaji (operators) ambao watanunua malighafi kutoka ndani na nje ya nchi na kuzalisha bidhaa katika industrial shed nilizozitaja hapo juu;
(iii) Kuwa na mchakato wa kuzalisha bidhaa katika maeneo hayo;
(iv) Kufundisha na kuajiri vijana wa Kitanzania na kutumia Kurasini kama kituo cha mauzo ya bidhaa zinazozalishwa viwandani ambapo ni mauzo ya jumla tu yatakayofanyika katika sehemu hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango huu unakwenda sawa na fikra za Mheshimiwa Rais za kujenga viwanda ili kutengeneza ajira kwa vijana na kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kukidhi mahitaji ya soko la ndani na soko la nje.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE aliuliza:-
Uzalishaji wa zao la ufuta limeongezeka kwa msimu wa mwaka 2015/2016 na kusababisha kushuka kwa bei ya ufuta sokoni:-
Je, ni lini Serikali itajenga kiwanda cha kukamulia ufuta Wilayani Liwale?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Hassan Chande, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa mavuno ya zao lolote yakiongezeka, bei yake sokoni inaweza kushuka. Sera ya Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi iweze kujenga viwanda na kuwekeza katika biashara. Kufuatia uhamasishaji huo, Mkoa wa Lindi una jumla ya viwanda 11 vya kukamua mafuta, viwili vikiwa mahususi kukamua mbegu za ufuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa jukumu la msingi la Serikali limebaki katika kuhamasisha sekta binafsi, Wizara itaendelea kuhamasisha wawekezaji ili kuwekeza katika usindikaji wa mafuta ya ufuta Wilayani Liwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nitamwomba Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Wizara yangu katika kuhamasisha wajasiriamali wa Wilaya ya Liwale waweze kuwekeza katika usindikaji wa mbegu za ufuta. Kiwango cha ufuta kinachozalishwa Wilaya ya Liwale kwa sasa kinakidhi uwekezaji mdogo na wa kati ambao wananchi na wajasiriamali waliopo wakihamasishwa wanaweza kuwekeza katika usindikaji wa mbegu za ufuta.
Mhesjhimiwa Mwenyekiti, mashine ndogo sana ya kukamua mafuta ya ufuta, inakadiriwa kuwa na gharama kati ya shilingi milioni 10 mpaka 15 na mashine ndogo ni kati ya shilingi milioni 16 mpaka 200. Mashine ya kati inayoweza kukamua na kuchuja mara mbili (double refinery) inagharimu kati ya shilingi milioni 200 mpaka 500.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hakika wananchi wakihamasishwa wanaweza kujiunga katika vikundi na kuweka mitaji yao pamoja na kuweza kununua mashine ambayo ina uwezo wa kuchuja mara mbili (double refinery) yenye kuzalisha mafuta yenye soko zuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai pia kwa Waheshimiwa Wabunge wawahamasishe wananchi walio katika Majimbo yenye kuzalisha mbegu za mafuta waweze kushiriki katika kuanzisha viwanda vya kukamua mafuta kwa viwango mbalimbali. Wizara itakuwa nyuma yao kutoa ushauri na mafunzo ya kiufundi pamoja na kuelekeza mahali mashine zinapopatikana kupitia Taasisi zake za SIDO, TEMDO na TIRDO.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Singida Mjini ni Mji unaokuwa kwa kasi sana na tumetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji:-
Je, Serikali iko tayari kuleta wawekezaji?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhamasishaji wa uvutiaji wa uwekezaji ni jukumu la msingi la Serikali. Katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa mwaka 2016/2017 –2020/2021 imeelezwa wazi kwamba malengo ya Serikali ni kuongeza kasi ya kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje katika sekta zenye tija kwa Taifa. Hivyo, Wizara yangu imekuwa ikihamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza nchini ikijumuisha Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya kivutio cha msingi
cha uwekezaji ni uwepo wa maeneo ya uwekezaji. Hivyo, Serikali imeendelea kuhamasisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Mikoa na Wilaya kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji. Kutokana na juhudi hizo, hadi kufikia Aprili, 2017, jumla ya Mikoa 13 imewasilisha taarifa ya utengaji wa maeneo katika mikoa yao. Napenda kuchukua fursa hii kuupongeza Mkoa wa Singida kwa kuitikia wito huo na tayari wametenga hekta 6,595.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na jitihada hizo, katika kipindi cha kuanzia mwaka 1996 hadi Aprili, 2017, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania, imefanikiwa kuandikisha miradi 33 kwa ajili ya Mkoa wa Singida yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 997.879. Kwa muhtasari huo, kazi iliyofanyika katika uhamasishaji uwekezaji Mkoani Singida, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Singida kuwa Serikali itaendelea kuvutia wawekezaji kuwekeza katika Mkoa wa Singida. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH (K.n.y. MHE. DKT. DALALY
P. KAFUMU) aliuliza:-
Wilaya ya Igunga ni miongoni mwa Wilaya zinazolima pamba kwa wingi nchini:-
Je, ni lini Serikali itajenga au kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchambua pamba, kutengeneza nyuzi na nguo na hata mafuta ili kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga nchi ya viwanda?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mweyekiti, Serikali imeweka kipaumbele kikubwa katika kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumiwa na watu wengi nchini (mass consumption), zinazotoa ajira kwa wingi na zinazotumia malighafi za ndani ya nchi kama inavyojieleza kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano. Bidhaa hizo ni pamoja na nguo zitokanazo na pamba inayolimwa maeneo mbalimbali nchini ikiwepo Igunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha uzalishaji katika mnyonyoro mzima wa thamani katika zao la pamba unaofanyika, Serikali iliandaa mkakati wa kuendeleza zao la Pamba, Nguo hadi Mavazi (Cotton to Clothing Strategy –C2C) uliozinduliwa mwezi Mei, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huo ambao utekelezaji wake unaendelea, unahamasisha uendelezaji wa zao la pamba na uongezaji wa thamani wa zao hilo kuanzia kuchambua pamba, kutengeneza nyuzi na nguo na hata kuongeza thamani ya mafuta ya kula yatokanayo na mbegu za pamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza kasi ya uwekezaji katika Sekta ya Viwanda, Wizara yetu imendaa mkakati wa kuharakisha ujenzi wa viwanda (Fast Tracking Industrialization in Tanzania) na imekamilisha utafiti juu ya vikwazo zinavyochelewesha uwekezaji nchini. Ni imani yangu kuwa utekelezaji wa maandiko tajwa hapo juu na juhudi za uongozi wa Mkoa wa Tabora zitatuwezesha kuvutia uwekezaji Wilaya ya Igunga.
MHE. MWITA M. WAITARA (K. n. y. MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-
Serikali imetangaza kukabidhi rasmi kazi ya kufufua kiwanda cha kutengeneza tairi cha Arusha kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) baada ya kusitisha rasmi uzalishaji mwaka 2009.
Je, mpaka sasa kazi ya kufufua kiwanda hicho imefikia wapi na inatarajiwa kugharimu fedha kiasi gani?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kiwanda cha kutengeneza matairi cha Arusha kilisimamisha uzalishaji mwaka 2009 kutokana na Serikali kukosa fedha kwa ajili ya kukiendesha na mbia mwenza (Kampuni ya Continental AG) hakuwa tayari kuendelea kuwekeza katika kiwanda hicho. Hivyo, Serikali iliweka dhamana ya kukisimamia kiwanda hicho chini ya NDC. Dhamira ya Serikali hivi sasa ni kuona kiwanda hicho kinaanza kuzalisha matairi mapema iwezekanavyo.
Mpaka sasa Serikali imenunua asilimia 26 ya hisa zilizokuwa zinamilikiwa na mbia mwenza na hivyo kukifanya kiwanda hicho kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Ili uwekezaji mpya katika kiwanda uwe wenye tija, katika mwaka 2016/2017 Serikali imefanya utafiti wa kubainisha aina ya teknolojia itakayotumika, uwezo wa uzalishaji, upatikanaji wa malighafi, upatikanaji wa soko na athari za mradi na teknolojia itakayotumika kwa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya awali imebaini kuwa kwanza, mitambo iliyopo ambayo ilifungwa kwenye miaka ya 1960 ikiwa imetumika haifai kwa uzalishaji wa kiushindani, pili, inatakiwa kufungwa mitambo inayotumika teknolojia ya kisasa itakayowezesha kiwanda kufanya kazi kwa ufanisi na kwa kuzingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira. Tatu, kiwanda kipanuliwe ili kiweze kuzalisha matairi ya aina mbalimbali na kwa wingi ili kupata faida ya uzalishaji kwa wingi (economies of scale). Nne, kiwanda hicho kiundeshwe na sekta binafsi, Serikali ikiwa mbia kwa hisa zinazolingana na rasilimali za kiwanda zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mpango wa Serikali kwa mwaka 2017/2018 kutafuta mbia atakayekidhi vigezo tajwa hapo juu ili uwekezaji uanze.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Huko Nachingwea kulikuwa na viwanda viwili vya kukamua ufuta na korosho ambavyo vimebinafsishwa kwa muda mrefu lakini wawekezaji hawajaviendeleza hadi sasa hivyo kupunguza ajira na mzunguko wa fedha:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani juu ya wawekezaji waliopewa viwanda hivyo viwili?
(b) Kama wawekezaji hao wameshindwa kuendeleza viwanda hivyo, je, Serikali ina mpango gani na viwanda hivyo hasa ikizingatiwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha nia ya kufufua viwanda nchini?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kuona kuwa viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinafanya kazi na kuchangia katika uchumi kupitia uongezaji thamani mazao ya kilimo, ajira na mapato ya Serikali. Katika kutekeleza azma hiyo, juhudi zimefanyika kuhamasisha wawekezaji ili kufufua viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo havifanyi kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Nachingwea, mafanikio yaliyopatikana kiwanda hicho kiliingia makubaliano ya awali (MoU) na Kampuni ya Sunshine Industry ya China mwezi Machi, 2017 ya kufufua kiwanda husika kwa utaratibu wa kujenga, kukimiliki, kuendesha na kuhamisha (Build Own Operate and Transfer). Usimikaji mitambo unaendelea na uzalishaji unatarajiwa kuanza mwezi Septemba 2017.
Mheshimiwa Spika, kiwanda cha kukamua ufuta au Kiwanda cha Mafuta ya Ilulu Nachingwea kilianza uzalishaji mwaka 1989 na mwaka mmoja baadaye kilisimamisha uzalishaji hadi kilipo binafsishwa kupitia ufilisi tarehe 14 Mei, 1997 kwa Kampuni ya Murzah Oil Mills iliyokuwa inamilikiwa na Marehemu Abbas Gulamali. Hati miliki ya Kiwanda alikabidhiwa mnunuzi mwaka 1999. Kufariki kwa Mheshimiwa Gulamali kuliathiri sana juhudi za kufufua kiwanda hicho.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo zoezi la ukarabati mitambo ili kuendelea na uzalishaji wa mafuta ya kula lilishindikana kutokana na uchakavu wa mitambo. Hivyo, mwaka 2009 familia ya marehemu Gulamali ilibadilisha shughuli ambapo kwa kushirikiana na Kampuni ya JAKAS Cashewnuts Factory ya Mtwara ilianza kubangua korosho hadi mwaka 2014 ubanguaji uliposimama kutokana na matatizo mbalimbali yakiwepo kujiondoa kwa Kampuni ya Olam kwenye shughuli za ubanguaji na biashara ya korosho kwa vile ndiyo ilikuwa ikigharamia shughuli za ubanguaji na kununua korosho zilizokuwa zikibanguliwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeipa Ofisi ya Msajili wa Hazina maelekezo ya kuchambua Mkataba wa Mauzo ya mali ya Kiwanda cha Mafuta ya Ilulu kwa Kampuni ya Murzah Oil Mills na kujadiliana na familia ya Marehemu Gulamali ili kukubaliana jinsi ya kuhakikisha mali za kiwanda hicho zinatumika kuchangia katika uchumi kupitia ajira na mapato ya Serikali. Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na jukumu hilo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Tanzania imejaaliwa kuwa na almasi na madini ya aina mbalimbali kwa wingi ikiwemo gypsum;
(a) Je, ni busara kwa viwanda vyetu humu nchini kuagiza gypsum kutoka nje ya nchi?
(b) Je, Serikali haioni kuwa huo ni ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za Watanzania?, na
(c) Serikali inachukua hatua gani kukomesha utaratibu huu ili kutunza fedha zetu chache za kigeni na kulazimisha ajira kwa Watanzania katika machimbo ya gypsum hususan Itigi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI, alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a), (b), na (c), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kujenga uchumi endelevu na hasa uchumi wa viwanda, ni busara viwanda vyetu kutumia malighafi zilizopo nchini tukilenga zaidi upatikanaji ajira kwa Watanzania, kuimarisha urari wa malipo (balance of payment) kupunguza mfumuko wa bei na uhifadhi wa fedha za kigeni (Foreign currency retention).
Mheshimiwa Spika, viwanda vyetu hapa nchini hutumia aina mbili ya jasi yaani anhydrate (calcium sulphate) inayotumika katika viwanda vya saruji na food grade calcium sulphate inayotumika katika viwanda vya vyakula na vinywaji. Madini ya jasi yanayotumika katika viwanda vya ujenzi hupatikana hapa nchini katika maeneo ya Kilwa (Rufiji), Makanya (Same), Tanga na Itigi wakati yanayotumika kwenye viwanda vya vyakula na vinywaji hayapatikani nchini hivyo kulazimika kuyaagiza kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inahimiza na kuhamasisha watumiaji wa malighafi za ndani ili kuzalisha bidhaa za viwandani na kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini. Ni kwa mtazamo huo Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imesitisha uingizwaji wa jasi itumikayo katika viwanda vya saruji kutoka nje ya nchi kuanzia tarehe 10 Agosti 2016.
Mheshimiwa Spika, vile vile Serikali inaendelea kufuatilia na kuhakikisha wachimbaji wanafuata masharti ya leseni walizopewa. Aidha, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kulinda viwanda vya ndani na hatimaye kutengeneza ajira nyingi kupitia sekta hii. Katika kufanya hivyo, Serikali pia inazingatia mahitaji na uwezo wa uzalishaji wa ndani ili kulinda walaji wa Tanzania na mitaji ya wawekezaji.
MHE. GEORGE H. MKUCHIKA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Kwanza ilijenga viwanda vikubwa viwili vya kubangua Korosho kwa lengo la kuongeza thamani ya korosho, kupanua ajira na kukuza uchumi. Viwanda hivi vilibinafsishwa na mpaka sasa ni kiwanda kimoja tu kinachofanya kazi kwa robo ya uwezo wake na kingine hakifanyi kazi kabisa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha viwanda hivyo vinafufuliwa na kufanya kazi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, Mbunge wa Newala Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 1992, Serikali ilitekeleza Sera ya Ubinafsishaji na kurekebisha mfumo wa uendeshaji wa Mashirika ya Umma vikiwemo viwanda. Katika kutekeleza sera hiyo, jumla ya viwanda 10 vya kubangua korosho nchini vikiwemo viwanda viwili vilivyoko Wilaya ya Newala (Newala I na Newala II) vilibinafsishwa.
Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinabangua korosho ili tupate ajira, tuongeze thamani na kuuza bidhaa yenye chapa ya Tanzania (brand) hatua itakayotupatia pato kubwa katika Shilingi za Kitanzania na fedha za kigeni. Zaidi ya uwepo wa viwanda, tunataka kuongeza wigo wa walipa kodi.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2005 Serikali iliuza asilimia 100 za hisa za kiwanda cha Newala I kwa kampuni ya M/S Agro Focus Limited kwa bei ya shilingi milioni 75 ambayo walilipa.
Mheshimiwa Spika, mwekezaji alifanya uwekezaji mkubwa ambao ulifanya kazi na kuzalisha mpaka mwaka 2013 alipofunga kiwanda. Chini ya operation inayosimamiwa na Wizara ya Viwanda na Wizara ya Fedha ambapo lengo lake ni kuhakikisha viwanda vinafanya kazi ili kupata manufaa yaliyobinafsishwa hapo juu, kiwanda cha Newala I kimehusika.
Mheshimiwa Spika, chini ya zoezi hili, mmiliki wa kiwanda amelipa deni la benki ambayo ni moja ya sababu zilizosababisha kiwanda kufungwa. Atafunga mitambo mipya na ataongeza mtaji katika shughuli za ubanguaji na biashara ya korosho.
Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Newala II chenye uwezo wa kubangua tani 3,500 kwa mwaka, kilibinafsishwa kwa kampuni ya Micronix Systems Limited kwa shilingi milioni 75 kwa mwaka 2004. Mwekezaji alifanya ukarabati kwa kuongeza mashine mpya, vyumba vya kukaushia korosho na jenereta la kuendesha kiwanda.
Mheshimiwa Spika, kutokana na ukarabati huo unaoendelea ubanguaji wa korosho umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka. Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2013 walibangua tani 1,500; mwaka 2014 tani 1,800; mwaka 2015 tani 2,500; mwaka 2016 tani 3,000; na mwaka huu tunategemea abangue tani 3,500.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA aliuliza:-
SIDO pamoja na majukumu mengine inatoa huduma kwa viwanda vidogo na vya kati kwa kutoa mikopo, mafunzo na vitendea kazi.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuiwezesha SIDO kutimiza majukumu yake?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa SIDO katika ujenzi wa uchumi wa Taifa letu imekuwa na mipango na mikakati mbalimbali ya kuliwezesha Shirika hili kutimiza majukumu yake. Kupitia Bajeti Kuu ya Serikali, SIDO inatengewa fungu kwa ajili ya kujenga miundombinu ya ofisi ya maghala ya viwanda (industrial sheds). Kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 7.04 kwa ajili ya kujenga miundombinu tajwa hapo juu katika Mikoa ya Katavi, Manyara, Kagera, Geita na Simiyu. Nafurahi kutamka kuwa tayari shilingi bilioni tano kati ya bilioni saba zilizopangwa kufanikisha jukumu hilo hapo juu zimeshatolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hutoa fedha za mitaji kwa SIDO kupitia Mfuko wa Kuendeleza Wajasiriamali (NEDF). Mfuko huu uliainzishwa mwaka 1994 kwa mtaji wa shilingi milioni 800 na mpaka sasa Serikali imechangia shilingi bilioni 5.5 ambazo zimezungushwa na wajasiriamali na kufikia shilingi bilioni 62.8 kwa mwaka wa fedha 2017/2018; na kwa mwaka huu sasa tumetenga shilingi bilioni 7.14 kwa ajili ya mfuko huu; na mahususi tutaelekeza juhudi zetu katika uanzishaji wa viwanda vidogo sana na viwanda vidogo chini ya mkakati wa Wilaya Moja, Bidhaa Moja (ODOP).
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia ina mkakati wa kuwatafutia SIDO wabia wa nje ili waweze kuwasaidia kufikisha huduma kwa wananchi hasa wafanyabiashara na wenye viwanda vidogo. SIDO inashirikina na Shirika la viwanda la India (National Small Industry Corporation of India) katika masuala ya kukuza teknolojia. Ushirikiano huo unahusisha uanzishwaji wa kiatamizi cha teknolojia za aina mbalimbali katika Mitaa ya Viwanda eneo la Vingunguti Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, SIDO imewezesha kuingia ubia na Shirika la maendeleo la Sweden na wamepatiwa shilingi bilioni 1.8 kuanzisha Kongano. Vilevile SIDO imewezeshwa kuingia Ubia na Shirika la Maendeleo ya Uchumi la Canada (Economic Development Associates) ambao unawezesha kutoa mafunzo ya kuimarisha na kuendesha biashara katika ukanda wa Mtwara na Lindi na ukanda wa Morogoro mpaka Arusha.
MHE. ANNE K. MALECELA atauliza:-
Watanzania wamehamasika sana na kilimo cha tangawizi na zao la tangawizi kwa sasa linalimwa siyo tu na wananchi wa Wilaya ya Same bali pia katika Mikoa kama Mbeya, Kigoma na Ruvuma.
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kulitafutia zao hilo soko la nje?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa tangawizi na viungo vingine katika sekta hii ambayo ni dhahiri mipango yetu ya kuvisimamia ikifanikiwa sekta hii itachangia sana uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, mipango na mikakati ya Serikali katika kutafuta soko la tangawizi pamoja na viungo vingine nje ya nchi ni pamoja na kuelimisha na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika sekta ya viungo ikiwemo tangawizi; kutafuta wateja wa zao hili kupitia Maonesho ya SIDO; Maonesho ya Kimataifa ya Julius Nyerere - Dar es Salaam na Maonesho ya Kiserikai tunayoyafanya nje ya nchi. Ili kudhibiti ubora wa viwango vya tangawizi, TIRDO imejenga maabara ya chakula yenye hadhi ya Kimataifa ili kuwawezesha wazalishaji wa tangawizi kufikia viwango vya masoko ya nje.
Mheshimiwa Spika, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kuwa mpaka sasa tunayo makampuni 21 ambayo yanajishughulisha na kuuza viungo nje ya nchi ikiwemo tangawizi. Juhudi za Serikali ni kuona makampuni haya yanaweza kupata soko la ndani na nje ili kuwa na uwezo wa kununua tangawizi yote inayozalishwa kwa wingi na kwa bei yenye faida kwa mkulima.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Wilaya ya Ileje ni kati ya Wilaya zinazozalisha sana mazao mbalimbali ya nafaka, pia ina fursa nyingi sana za kilimo cha cocoa, vanilla, tangawizi, iliki na pilipili manga lakini hakuna viwanda vidogo na vya kati ili kuongeza thamani ya mazao hayo.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha viwanda vidogo hivyo ili kuongeza ajira kwa wananchi na pia mapato ya Serikali?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutekeleza mkakati wa ujenzi wa viwanda, Mamlaka za Mikoa na Wilaya zimeelekezwa kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Pia katika maeneo hayo, Mamlaka za Wilaya zinapaswa kutenga sehemu za hifadhi ya mazao au bidhaa na sehemu za masoko pale inapohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri za Wilaya pamoja na kutenga maeneo, zimehimizwa katika mipango yao ya maendeleo kuhusisha ujenzi wa miundombinu wezeshi na miundombinu saidizi katika maeneo hayo ya ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa nilizonazo ni kwamba Halmashauri ya Ileje imetenga mita za mraba 9,832 sawa na hekta 0.98 katika eneo la Itumba na mita za mraba 43,615 sawa na hekta 4.36 katika eneo la Isongole ambazo ni kidogo sana. Pia tathmini ya Wilaya moja, bidhaa moja (ODOP), ilionesha Ileje inaweza kufanya vizuri zaidi katika zao la alizeti. Tathmini hiyo hiyo inaonesha Ileje haijafikia kiwango cha kuzalisha cocoa, vanilla, tangawizi, iliki na pilipili manga kwa kiasi cha kukidhi mahitaji ya viwanda vya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Ileje iko katika Mkoa mpya wa Songwe ambao kwa sasa hauna Meneja wa SIDO, Wizara imemwagiza Meneja wa SIDO Mbeya awasiliane na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ili watathmini fursa zilizopo na kusaidiana nao katika kuandaa mpango mkakati wa ujenzi wa viwanda vidogo ikiwa ni pamoja na mipango ya uzalishaji wa malighafi ya kutosha.
Aidha, Wizara inakamilisha mwongozo utakaotumika katika Mikoa na Wilaya katika kutenga maeneo, kuyaendeleza na kuhamasisha uwekezaji.
MHE. JAMAL KASSIM ALI aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani katika kuwasaidia wafanyabiashara wa Kitanzania kuwekeza kwenye viwanda nchini?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa viwanda nchini unategemea zaidi mazingira ya uwekezaji yaliyopo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa ardhi yenye miundombinu wezeshi, sera mbalimbali, mifumo ya kodi na mifumo ya upatikanaji wa vibali vinavyotakiwa kisheria ambayo ni majukumu ya Serikali. Baada ya kuwepo mazingira wezeshi, Serikali inabaki na majukumu ya kuhamasisha wawekezaji wakiwemo wa Kitanzania kuweza kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu ina mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara wa Kitanzania ili kuwekeza kwenye viwanda hapa nchini. Miongoni mwa mikakati hiyo ni mafunzo yanayotolewa kwa Watanzania wenye nia ya kuwekeza katika viwanda juu ya kuibua mawazo ya kibiashara, kuanzisha, kuendesha na kusimamia biashara kupitia SIDO, kutoa ushauri wa kitaalamu wa jinsi ya kuchagua teknolojia sahihi inayoendana na wazo la ujenzi wa kiwanda alilonalo Mtanzania kupitia TIRDO, TEMDO na CAMARTEC na namna ya kupata ama kukuza mtaji wa ujenzi wa viwanda kupitia NEDF, SIDO na TIB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha utendaji, Wizara imeanzisha Dawati la Wepesi wa Kufanya Biashara (Easy of Doing Business) ambalo lina jukumu la kuondoa ugumu wa kuanzisha na kuendesha biashara hapa nchini. Vilevile, imeandaa mwongozo kwa Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji kutenga maeneo, kusimamia sheria, kanuni, taratibu na kutoa maelekezo kwa wawekezaji. Aidha, Watanzania wanaotaka ama walio na mitaji mikubwa wanaweza kuwekeza kupitia maeneo ya EPZA ambayo yametengwa mahsusi kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi. Vilevile, wanaweza kuwasiliana na TIC kupata vivutio mbalimbali vilivyowekwa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji.
MHE. LUCIA M. MLOWE aliuliza:-
Mgogoro wa Kiwanda cha Chai Lupembe umewaathiri wakulima wa chai Lupembe na Wilaya nzima ya Njombe kutokana na kukosa soko la zao la chai.
Je, Serikali ipo tayari kujenga kiwanda kingine cha chai kunusuru uchumi wa wakulima wa chai katika Wilaya ya Njombe?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa migogoro inaathiri sana shughuli za uzalishaji viwandani pamoja na kuwaathiri wakulima ambao hukosa soko la malighafi zinazozalishwa. Kiwanda cha Chai Lupembe ambacho kilikumbwa na mgogoro wa muda mrefu uzalishaji ulisimama kwa miaka nane kati ya 2008 na 2015. Katika kipindi hicho na baada ya Serikali kuona wakulima wanakosa soko la majani ya chai, Serikali ilishawishi Kampuni ya Mufindi Tea and Coffee Ltd. kujenga kiwanda cha chai, katika tarafa ya Lupembe, Kijiji cha Ikanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hicho kilijengwa na kuanza usindikaji wa majani ya chai mwaka 2013. Hata hivyo, kufuatia hukumu ya Mahakama iliyompa ushindi mwekezaji wa kampuni ya Dhow Merchantile East Africa Ltd., na Lupembe Tea Estate Ltd. dhidi ya Muungano wa Vyama vya Ushirika vya Lupembe, mwezi Januari, 2016 uzalishaji katika kiwanda hicho ulianza na unaendelea. Kwa sasa kuna kesi mahakamani inayoendelea kusikilizwa kufuata rufaa ya MUVYULU dhidi ya ushindi aliopata mwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na viwanda vya kutosha ili kuchochea kilimo cha zao la chai na usindikaji wa majini ya chai katika Mkoa wa Njombe anakotoka Mheshimiwa Lucia Mlowe ambao una utajiri mkubwa wa zao hilo. Hivyo, Serikali imendelea kuhamasisha uwekezaji katika mkoa huo. Kampuni ya Unilever imeanza ujenzi wa kiwanda kipya cha chai. Kiwanda hicho kinatarajia kuanza uzalishaji mwaka 2018 na kitatoa ajira zipatazo 300.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwekezaji anatarajia kuanzisha mashamba ya chai yenye ukubwa wa Ekari, 1,000. Kati ya hizo ekari 200 zimeshapandwa mbegu za chai. Hivyo wakulima wa zao la chai wa Wilaya ya Njombe watapata fursa ya kuuza mazao katika kiwanda hicho kipya cha Unilever kitakapokamilisha ujenzi sambamba na viwanda vya Lupembe Tea Estate Ltd. na Ikanga chini ya Kampuni ya Mufindi Tea and Coffee Ltd.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka maeneo yanapolimwa majani ya chai kuwa Serikali inafuatilia kwa makini chanzo cha migogoro katika mashamba hayo na kuitatua na kuipatia suluhu ya kudumu.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA aliuliza:-
Miradi ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Liganga imekuwa ikiwekwa katika mipango ya Serikali katika Awamu karibu zote nne zilizopita, hata Awamu hii ya Tano bado miradi hii imewekwa.
(a) Je, ni lini wananchi walioachia maeneo yao ili kupisha miradi hii watalipwa fidia yao?
(b) Je, ni lini miradi hii itaanza kazi?
(c) Je, ni kweli Serikali imejipanga kuhakikisha miradi hii inaanza?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deogratias Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa, lenye sehemu (a), (b) na (c), kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Mchuchuma na Liganga umeainishwa katika Dira ya Taifa 2025; Mkakati wa Fungamanisho la Maendeleo ya Viwanda 2015; Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016-2021) na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2015 - 2020. Ni majukumu na wajibu wa Serikali kutekeleza maamuzi na maelekezo yaliyorejewa hapo juu. Ni kweli, Serikali imejipanga kuhakikisha miradi hii inaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naelewa tatizo la Mheshimiwa Mbunge ni kuchelewa kuanza kwa mradi na hasa malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha mradi. Kuchelewa kuanza kwa mradi kumetokana na nia nzuri ya Serikali ya kutaka kuhakikisha miradi inatekelezwa na wakati huo huo Taifa linapata manufaa stahiki kutokana na uwekezaji huo. Timu ya wataalamu imekamilisha kazi ya kupitia vipengele vyote vya vivutio na kuwasilisha taarifa yao Kamati ya Kitaifa ya Uwekezaji (NISC). Kamati hiyo imetoa maelekezo kwa timu ya wataalam kujadiliana na mwekezaji maeneo yenye mvutano. Ni imani yangu kuwa baada ya makubaliano kwenye maeneo hayo machache yaliyobaki, vikao husika vitatoa baraka za mwisho na mradi utaanza mara moja ikiwemo kulipa fidia kwa watu waliopisha mradi.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA aliuliza:-
Mkoa wa Tabora upo tayari kwa ajili ya uwekezaji wa EPZ uliotengewa eneo katika Wilaya ya Uyui.
Je, ni lini Serikali italeta wawekezaji katika Mkoa wa Tabora?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanne Ismail Mchemba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato wa kutenga eneo la uwekezaji Mkoa wa Tabora kwa ajili ya EPZA ulianza mwaka 2010 baada ya Wizara yangu kuelekeza uongozi wa Mkoa kutenga eneo lisilopungua ukubwa wa hekta 2000. Uongozi wa Mkoa ulipendekeza eneo ulipokuwa Mgodi wa Resolute lenye ukubwa wa hekta 866. Baada ya ukaguzi wa eneo hilo ilibainika kuwa sehemu kubwa ni mashimo yaliyofunikwa hivyo kutofaa kwa ajili ya miradi ya EPZA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa ushauri kwa Mkoa wa Tabora na kwa Mikoa mingine waendelee kubaini na kutenga maeneo ya uwekezaji. Watenge maeneo kwa malengo ya Special Economic Zone - SEZ au Export Processing Zone - EPZ kulingana na ushauri utakaotolewa na wataalamu wangu, lakini pia watenge maeneo kwa ajili ya uwekezaji usiokuwa wa SEZ wala wa EPZA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelekezo ya hapo juu, Wizara yangu inakamilisha uandaaji wa mwongozo utakaosaidia Mamlaka za Mikoa na Wilaya kutenga maeneo ya uwekezaji na namna ya kuvutia wawekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuleta wawekezaji Tabora, nitoe taarifa kuwa hivi sasa Mamlaka ya Biashara Tanzania (Tan Trade) kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Tabara wanaandaa kongamano la kutangaza vivutio vya Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti,niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Tabora kuwa Wizara na mimi mwenyewe tutaendelea kuitangaza Tabora kwa lengo la kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.
MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-
Serikali iliingia ubia na kampuni kutoka Jamhuri ya Watu wa China ya kumiliki na kuendesha Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kilichoko Ubungo Jijini Dar es Salaam lakini mbia huyo ameshindwa kutoa mtaji wa kuendesha kiwanda hicho.
(a) Je, Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha kuwa mbia huyo anaweka mtaji wa kutosha wa kukiendesha kiwanda hicho?
(b) Je, kwa nini Serikali inafikia maamuzi ya kukibinafsisha kiwanda cha umma kwa mtu ambaye hana mtaji?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sued Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango ya Serikali ni kukiendeleza Kiwanda cha Urafiki ili kizalisje nguo na mavazi ya aina mbalimbali. Kutokana na mwekezaji aliyepo kutozalisha kwa ufanisi, mazungumzo ya wanahisa yalifanyika mwezi Machi, 2017 ambapo mbia mwenza, Kampuni ya Changzhou State Owned Textile Assets Operations Limited imeonesha kuwa tayari kumiliki kiwanda kwa kupunguza hisa zake kutoka 51 za sasa na kuipatia Tanzania hisa nyingi zaidi. Katika mpangilio huo mpya, tutakuwa na uwezo mkubwa wa maamuzi ikiwemo kusimamia kampuni kimkakati na kuweka mtaji wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Nguo cha Urafiki ni kiwanda cha kihistoria kilichoanzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1966. Kutokana na historia ya kiwanda hicho wakati wa ubinafsishaji, Serikali ya Tanzania iliitaka Serikali ya China iliyotusaidia kujenga kiwanda hicho kutupa mbia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya China ilikasimu ombi hilo kwa Jimbo la Liangsu ambalo ni bingwa katika sekta ya nguo. Serikali ikateua Kampuni ya Dieqiu Textile Dyeng (DTD)na Printing Group Company ambayo haikufanya vizuri na ikaletwa Kampuni ya Changzhou State Owned Textile Limited tuliyonayo sasa. Kampuni hii nayo haifanyi vizuri hali iliyopelekea kushinikiza ongezeko la hisa za Serikali na mamlaka katika uendeshaji wa kiwanda kama nilivyoeleza hapo awali.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA aliuliza:-
Wananchi wapatao 1,025 wa Vijiji vya Kiromo, Zinga, Pande, Mlingotini na Kondo walifanyiwa uthamini wa mali zao tangu mwaka 2008 ili kupisha mradi wa EPZA Bagamoyo lakini hadi sasa hawajalipwa fidia:- Je, ni lini Serikali itawalipa wananchi hao fidia stahiki?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la ukanda maalum la kiuchumi la Bagamoyo (Bagamoyo Special Economic Zone) ni moja ya miradi ya kimkakati ya kitaifa. Awamu ya kwanza ya mradi huu inahusisha ujenzi wa bandari kubwa ya kisasa, eneo la viwanda kando ya bahari ambapo kwa kuanzia viwanda 190 vitajengwa na ujenzi wa miundombinu wezeshi na saidizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2008 mpaka mwaka 2010 Serikali ilifanya uthamini wa eneo lengwa lililokuwa na wananchi 2,273 na kubaini mahitaji ya fidia ya shilingi bilioni 58.771. Katika kipindi cha kati ya Agosti, 2012 na Februari, 2015 Serikali iliwalipa wananchi 1,155 jumla ya shilingi 26.66 kama fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kasi ndogo ya upatikanaji wa fedha ya fidia kutoka Bajeti Kuu ya Serikali mwaka 2017, Septemba, Serikali iliamua kubadilisha chanzo cha fedha za fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya utaratibu mpya wabia katika mradi wa Bagamoyo (China Merchant na State Reserve Fund SGRF) ya Oman watatoa fedha za fidia kwa makubaliano maalum na mbia mwenzao (Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwahakikishia wananchi wa vijiji vya Pande, Zinga, Kiromo, Mlingotini na Kondo kupitia kwa Mheshimiwa Mbunge wao, kuwa pindi majadiliano ya hawa wabia watatu yanayoendelea sasa yatakapokamilika watalipwa pesa zao mara moja.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA (K.n.y. MHE. ALBERT O. NTABALIBA) aliuliza:-
Katika jimbo la Buhigwe hususan eneo la Munzeze, soko la tangawizi limekuwa la shida sana na tangawizi huuzwa bei ya chini sana.
Je, Serikali inasaidiaje upatikanaji wa masoko ili wananchi wauze kwa bei ambayo itawafaidisha?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la tangawizi ni miongoni mwa viungo vyenye thamani kubwa na linalimwa kwa wingi katika Mikoa ya Kigoma, Ruvuma, Kilimanjaro, Morogoro, Tanga, Njombe, Songwe na Mbeya. Kama alivyosema Mheshimiwa Ntabaliba, zao hili limekuwa na tatizo la upatikanaji wa soko zuri na la uhakika. Ili kutatua tatizo hili, Wizara kupitia Mamlaka ya maendeleo ya biashara Tanzania Tantrade imeratibu jitihada za kupata soko katika nchi za Ulaya na Marekani. Wateja wa awali wamefurahia ubora wa tangawizi za Tanzania na wameomba watumiwe tani 25 kama sampuli ya kujaribu soko (market testing). (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninashauri Mheshimiwa Ntabaliba na wananchi wenye fursa ya kulima tangawizi katika maeneo yao wawasiliane na Wizara yangu au Taasisi ya SIDO pamoja na Mamlaka ya Tantrade. Soko la Ulaya na Marekani ambalo limevutiwa na ubora wa tangawizi yetu linahitaji takribani tani 750,000 za viungo kwa mwaka kama tukikidhi vigezo.
MHE. MWITA M. WAITARA (K. n. y. MHE. SAED A. KUBENEA) aliuliza:-
Serikali imetangaza kukabidhi rasmi kazi ya kufufua kiwanda cha kutengeneza tairi cha Arusha kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) baada ya kusitisha rasmi uzalishaji mwaka 2009.
Je, mpaka sasa kazi ya kufufua kiwanda hicho imefikia wapi na inatarajiwa kugharimu fedha kiasi gani?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, Mbunge wa Ubungo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kiwanda cha kutengeneza matairi cha Arusha kilisimamisha uzalishaji mwaka 2009 kutokana na Serikali kukosa fedha kwa ajili ya kukiendesha na mbia mwenza (Kampuni ya Continental AG) hakuwa tayari kuendelea kuwekeza katika kiwanda hicho. Hivyo, Serikali iliweka dhamana ya kukisimamia kiwanda hicho chini ya NDC. Dhamira ya Serikali hivi sasa ni kuona kiwanda hicho kinaanza kuzalisha matairi mapema iwezekanavyo.
Mpaka sasa Serikali imenunua asilimia 26 ya hisa zilizokuwa zinamilikiwa na mbia mwenza na hivyo kukifanya kiwanda hicho kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Ili uwekezaji mpya katika kiwanda uwe wenye tija, katika mwaka 2016/2017 Serikali imefanya utafiti wa kubainisha aina ya teknolojia itakayotumika, uwezo wa uzalishaji, upatikanaji wa malighafi, upatikanaji wa soko na athari za mradi na teknolojia itakayotumika kwa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya awali imebaini kuwa kwanza, mitambo iliyopo ambayo ilifungwa kwenye miaka ya 1960 ikiwa imetumika haifai kwa uzalishaji wa kiushindani, pili, inatakiwa kufungwa mitambo inayotumika teknolojia ya kisasa itakayowezesha kiwanda kufanya kazi kwa ufanisi na kwa kuzingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira. Tatu, kiwanda kipanuliwe ili kiweze kuzalisha matairi ya aina mbalimbali na kwa wingi ili kupata faida ya uzalishaji kwa wingi (economies of scale). Nne, kiwanda hicho kiundeshwe na sekta binafsi, Serikali ikiwa mbia kwa hisa zinazolingana na rasilimali za kiwanda zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mpango wa Serikali kwa mwaka 2017/2018 kutafuta mbia atakayekidhi vigezo tajwa hapo juu ili uwekezaji uanze.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. MARTHA J. UMBULLA) aliuliza:-
Mazao ya pareto na vitunguu saumu yanalimwa Wilaya ya Mbulu na yana thamani na faida kubwa kwa wananchi.
Je, Serikali itakubaliana na mimi kuwa kuna haja ya kuanzisha viwanda vya kusindika mazao haya Wilayani Mbulu ili kuhamasisha kilimo cha mazao hayo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli mazao ya pareto na vitunguu saumu yanayolimwa katika Wilaya ya Mbulu yana thamani na faida kubwa kwa wananchi. Hivyo, Serikali inakubaliana na Mheshimiwa Umbulla kuwa kuna haja ya kuendelea kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vya kusindika mazao hayo Wilayani Mbulu ili kuchochea zaidi kilimo cha pareto na vitunguu saumu.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua faida zitokanazo na zao la pareto, Serikali iliamua kuanzisha Bodi ya Pareto kwa lengo la kudhibiti uzalishaji, usindikaji na biashara ya pareto nchini. Hivyo, kupitia Bodi ya Pareto na Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Serikali itaendeleza juhudi za kuhamasisha uwekezaji kwenye viwanda vya kuengua na kuchuja pareto ili kuongeza thamani ya zao hilo na kuwanufaisha zaidi wananchi katika maeneo yanayolimwa pareto ikiwemo Mbulu.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa zao la vitunguu saumu, Wizara yangu kwa kupitia karakana za SIDO katika Mikoa ya Arusha na Kimlimanjaro zinatengeneza blenda ambayo inatumika kusaga zao hilo kuwa katika mfumo laini (garlic paste); teknolojia hii inapatikana kwa shilingi 1,800,000. Aidha, SIDO hutoa mafunzo kwa vikundi na watu binafsi juu ya usindikaji wa zao la vitunguu saumu katika mikoa inayolima zao hili.
Mheshimiwa Spika, hivyo, nashauri Mheshimiwa Mbunge afike ofisi za SIDO, Mkoa wa Manyara zilizoko Babati kwa ufafanuzi zaidi na hatimaye tuweze kushirikiana.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Pamoja na kuwepo viwanda vingi vya sukari hapa nchini bado kumekuwa na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo hususan kwa upande wa Tanzania Bara; mfano bei ya mfuko wa kilo 50 ni shilingi 65,000 kwa upande wa Zanzibar ambako kuna kiwanda kimoja tu cha sukari, lakini kwa Tanzania Bara mfuko huu wa kilo 50 huuzwa shilingi 120,000.
(a) Je, kuna tatizo gani linalofanya sukari iuzwe bei ya juu kiasi hicho kwa upande wa Tanzania Bara?
(b) Je, Serikali itachukua hatua gani ili kuweza kuwapatia wananchi unafuu katika upatikanaji wa bidhaa hiyo?
(c) Kwa upande wa Zanzibar katika kipindi ambacho matumizi ya sukari kwa wananchi yanaongezeka mfano, mwezi wa Ramadhani, Serikali inashusha ushuru wa kuingia sukari nchini. Je, kwa nini Serikali ya Muungano isizingatie utaratibu huu mzuri ili kuleta unafuu kwa Tanzania Bara?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge wa Buyuni, Zanzibar lenye sehemu (a) (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu kuwa kwa vigezo vyovyote vya kupima uwepo wa bidhaa sokoni Tanzania Bara hakuna uhaba wa sukari. Kuhusu tofauti ya bei kati ya pande mbili za Muungano ni kuwa zaidi ya asilimia 53 ya sukari itumikayo Zanzibar huagizwa kutoka nje kwenye vyanzo ambavyo gharama zake ni nafuu ukilinganisha na asilimia 29 zinazoagiwa upande wa Bara kujaza mapungufu ya uzalishaji. Lakini upande wa Bara na nchi nyingine za Afrika Mashariki bidhaa ya sukari kutoka nje hutozwa ushuru wa asilimia 100 ili kulinda viwanda vya ndani. Kutokana na sababu hizo bei huweza kutofautiana.
Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua uamuzi wa kuhamasisha kusimamia kampuni kubwa nne zinazozalisha sukari ili zipanue uwezo wa mashamba na viwanda vyao. Zoezi linakwenda vizuri ambapo Kilombero Sugar tayari inaongeza uwezo wa uzalishaji maradufu kwa kuwekeza dola milioni 200 za Kimarekani. Mtibwa Sugar kwa kuwekeza shilingi bilioni 75 za Kitanzania wataongeza uzalishaji katika kipindi cha miaka mitano na kufikia tani 100,000 kwa mwaka toka tani 30,000 za sasa. Kagera Sugar wanawekeza shilingi bilioni 360 za Kitanzania ili kwa kipindi hicho hicho cha miaka mitano waongeze uzalishaji mpaka tani 170,000 kwa mwaka kutoka 75,000 za sasa. Wakati huohuo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inawekeza katika mradi kapambe wa Mkulazi Namba Moja na Namba Mbili wakilenga kuzalisha tani 250,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, kutokana na uwekezaji huo na kwa kuzingatia kiteknolojia ya kisasa inayotumika bada ya miaka mitatu mpaka minne ijayo tutajitosheleza kwa sukari yenye bei nafuu na kuuza ziada nje ya nchi. Pamoja na faida hiyo sekta ya sukari itatuwezesha kutengeneza ajira zaidi ya 50,000.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikishusha ushuru au kuruhusu kuingiza sukari bila ushuru ili kutoa nafuu kwa bei kwa watumiaji wa sukari. Katika kipindi cha mwezi Machi mpaka Juni mwaka huu Serikali kwa kuzingatia maoni ya wadau imetoa vibali vya kuagiza sukari tani 135,610 kwa kutoa ushuru pungufu kwa kiwango cha asilimia 25 badala ya 100 ili kutoa nafuu kwa bei kwa wananchi pamoja na kuziba pengo la uagizwaji wa sukari kutoka nje.