Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Innocent Edward Kalogeris (7 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Na mimi nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii kwanza kumshukuru Mungu kwa mema mengi ambayo analitendea Taifa letu la Tanzania. Vile vile nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wa awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa nchi hii katika kipindi cha miaka mitano. Amekuza uchumi wan chi, ametupa ujasiri Watanzania na kubwa zaidi ametufanya tujiamini na kujitambua kwamba sisi sio masikini ni Taifa tajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii vile vile kumpongeza aliyekuwa Makamu wa Rais na sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amirijeshi Mkuu wa Awamu ya Sita, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa wakati ule ya kumsaidia aliyekuwa mtangulizi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi nataka niwaambie Watanzania na wapenda maendeleo katika Taifa hili kwamba Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan anatosha kwa nafasi ambayo anayo kwa sasa na kubwa zaidi, tutarajia makubwa kwa maendeleo ya haraka na kwa kasi kubwa zaidi katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo sisi Wabunge na yeye mwenyewe na Hayati Dkt. Magufuli walipita kuwaahidi Watanzania na tukakipatia Chama cha Mapinduzi ushindi mkubwa wa kishindo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii vile vile kumpongeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye leo hii ametuletea bajeti na tunaijadili, kwa kazi kubwa ya usimamizi wa shughuli za Serikali katika Bunge na nje ya Bunge katika kipindi cha miaka mitano. Ndani ya hotuba yake kumejaa yale ambayo yametekelezeka katika kipindi cha miaka mitano na yale ambayo tunaenda kuyatekeleza ndani ya miaka mitano katika kipindi cha mwaka huu mmoja ambao tunao katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika na Spika ambaye hayupo, niwape pongezi nanyi kwa kazi kubwa ambayo mliifanya katika Bunge la Kumi katika kuisimamia Serikali na kutunga sheria ambazo zimesababisha leo tumefika tuko hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge wenzangu nawaomba niwakumbushe, kazi kubwa ambayo tunayo kwa sasa, hata Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipokuja kufungua Bunge hili aliambia jambo moja; ana imani kubwa na Bunge hili. Sasa Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, hayupo, ametangulia mbele ya haki, tuelekeze nguvu zetu na tuonyeshe imani hiyo ambayo Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alitupa Bunge hili tujielekeze kumpa nguvu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan aweze kutekeleza yale ambayo tumewaahidi wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nianze kuchangia hoja. La kwanza, nichangie katika mipango ya miradi mikakati. Tuna Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo kwa namna moja au nyingine liko katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini na liko katika Jimbo langu la Morogoro Kusini. Ni mradi mzuri na mradi ambao kwa kweli ukikamilika utaleta mafanikio makubwa ya kujenga uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuthibitisha hilo nataka niseme tu mimi mwenyewe, ndani ya Halmashauri yetu, ndani ya kipindi hiki kifupi tumepata shilingi bilioni moja na karibu milioni 100 kama Service Levy ambapo fedha hiyo tayari asilimia 10 imekwenda kwa vijana na asilimia 40 imekwenda kwenye miradi ya maendeleo ya Halmashauri na nyingine zimeenda kufanya shughuli nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali, CAG amezungumza. Kuna 4% kama huduma katika shughuli za kijamii (corporate responsibility), ambayo inatakiwa itoke katika mradi huo iende katika shughuli za wananchi. Naiomba Serikali ikasimamie hili ili kusudi tuweze kuipata fedha hii katika Halmashauri tuweze kufanya shughuli nyingi za maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna huu mradi wa Standard Gauge, ninaamini kabisa kwamba Wizara ya Ardhi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Uchukuzi na Ujenzi zikishirikiana kwa pamoja wanaweza kutoa fursa kwa wananchi ambapo mradi huu utapita wakaweza kufanya kazi za maendeleo ambazo zitawaongezea uchumi na wakati huo huo mradi huu ukafanya katika misingi hiyo. Naomba tuangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la utawala. Katika Halmashauri yetu ya Morogoro Vijijini tuna jengo la Halmashauri. Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika mwaka wa fedha uliokwisha tumepata shilingi milioni 700. Mkandarasi yuko site, kazi inaendelea. Naomba nijue, katika awamu hii ya mwaka huu wa fedha, Halmashauri yetu imetengewa shilingi ngapi ili mradi huo uende moja kwa moja, tusije tukasimama ili tuweze kufanya shughuli za kuleta maendeleo kama vile ilivyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni afya. Katika mwaka wa fedha uliokwisha tumepata shilingi bilioni 4.3 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ambayo imekamilika na ujenzi wa vituo sita vya afya ambavyo vimekamilika. Sasa hivi kuna suala la vifaa tiba, kuna suala la dawa, ambulance na matabibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji hospitali ile ianze kazi ikiwa imekamilika, pia tunahitaji vituo hivyo vya afya vifanye kazi vikiwa vimekamilika, kufikia lengo ambalo Serikali inataka kutoa huduma kwa wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini na Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliomba katika bajeti hii shilingi milioni 600 kwa ajili ya kujenga wodi tatu katika Kituo cha Afya cha Mikese, Kituo cha Afya Kisaki na Kituo cha Afya cha Kisemo. Tukipata fedha hizi ni kwamba tutakuwa na uwezo wa kujenga, kukamilisha na hivi vituo vya afya vitafanya kazi na wananchi watapata kile ambacho tunakihitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili, Halmashauri ya Morogoro Vijijini iko katika jiografia mbaya sana. Naiomba Serikali, pamoja na kwamba tumepata vituo vya afya sita, bado tuna uhitaji wa vituo vya afya tu. Tunahitaji Kituo cha Afya kwenye Kata ya Kasanga; Kata ya Bwakilajuu na Kata ya Singisa. Kata hizi ziko milimani na ni mbali kufikika, kwa hiyo, wananchi wetu wanapata wakati mgumu sana katika kupata huduma za afya. Tukiweza kuwafikishia huko, tutakuwa tumewasaidia sana. Naiomba Serikali ione ni jinsi gani ya kufanya na kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nizungumzie kidogo kilimo. Mkoa wa Morogoro ni mkoa ambao una ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo. Nimeona katika mpango ambao tumeletewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba kuna fedha zilikwenda Njage Wilaya ya Kilombero, kuna fedha zilikwenda Mvumi Wilaya ya Kilosa, kuna fedha zilikwenda Kigubu Mvomero na kuna fedha zilikwenda Kilangazi Kilosa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na fedha hizo kwenda, lakini Mkoa wa Morogoro bado una maeneo makubwa kwa ajili ya kufanikisha kilimo cha umwagiliaji na ambacho nina uhakika ndiyo kilimo cha uhakika na cha kutusaidia. Niombe sana kuna mradi wa Kongwaturo, mradi mkubwa sana unahitaji fedha…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Niendeleze hapo hapo alipozungumza dada yangu Mheshimiwa Munde Tambwe. Mkoa wa Morogoro tunaomba ukatwe ipatikane mikoa miwili. (Makofi/Kicheko)

MBUNGE FULANI: Ugawanywe.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Nimeelekezwa ni ugawanywe.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Morogoro ugawanywe ipatikane mikoa miwili ambapo kutakuwa na Wilaya ya Morogoro, Wilaya ya Mvomero, Wilaya ya Gairo na Wilaya ya Kilosa; na kwingine kutakuwa na Wilaya ya Ulanga, Wilaya ya Malinyi na Wilaya ya Kilombero. Tupate mikoa miwili ili kuweza kurahisisha kupata maendeleo katika Mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana dada yangu Mheshimiwa Ummy kwa uteuzi ambao ameupata katika Wizara hii mpya. Ni imani yangu kwamba yeye na wasaidizi wake; Manaibu wake watafanya kazi kubwa kama ile aliyoifanya akiwa Wizara ya Afya wakati wa mapambano ya Corona na tukashinda, naamini kabisa kwamba TAMISEMI atafanya vizuri zaidi. Hizi changamoto zote pamoja na mafanikio yote, lakini changamoto hizi tutakwenda kuzimaliza.

Mheshimiwa Spika, nianze na suala la barabara. Mimi ni Mkandarasi. Katika uhalisia, Wilaya ya Morogoro Halmashauri yetu ina eneo la square mita 11,731, ina barabara zenye urefu wa kilometa 750, ina madaraja makubwa 29, ina ma-box culvert 74, lakini mgao wake tunapata shilingi bilioni 1.1. Ni kwamba kwa namna moja au nyingine, tunatengeneza kilometa moja tu bila kugusa makalavati wala nini kwa shilingi milioni moja.

Mheshimiwa Spika, kama Mkandarasi, barabara ya changarawe ili iweze kupitika ikiwa na madaraja au box culvert, unahitaji kilometa moja kwa shilingi milioni 30. Sasa naomba tu, ndugu yangu Mheshimiwa Zungu amezungumza, Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Miundombinu Mheshimiwa Kakoso amezungumza, tuangalie jinsi gani tunaisaidia TARURA. Katika kuisaidia TARURA, naomba, hawa wenzetu wamekokotoa, wamechanganua, ni kwamba kutakuwa na uwezekano wa kila mwaka kupata shilingi milioni 500. Katika hilo suala la Mwenyekiti wangu ndugu yangu Mheshimiwa Kakoso, kila mwaka tutakuwa tunapata shilingi trilioni 2,160. Naomba Serikali ichukue mawazo haya na ikayafanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika shilingi trilioni 2,160 ukizigawa kwa Halmashauri zetu, tutakuwa na uhakika wa kila mwaka kupata kila Halmashauri shilingi bilioni 11. Shilingi bilioni 11 ukipeleka kwenye Halmashauri, ndani ya miaka mitano, tatizo la TARURA litakuwa halipo tena hapa Bungeni. Kwa hiyo, naiomba Serikali tu, mama yangu Mheshimiwa Ummy, Waziri wa Fedha na wengine wote wanaohusika, lisimamieni hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakupa kichekesho kimoja, lakini siyo kizuri. Juzi mliona katika mitandao, wale watu waliokuwa wanatembea uchi, wametoka jimboni kwangu. Kilichojitokeza, watu huwa wanavua nguo wanapopita kwenye barabara za umande, wanazihifadhi nguo zao. Kwa hiyo, naomba tu, tunadhalilika. Jimbo la Morogoro Kusini eneo kubwa ni milima, kwa hiyo, shida yetu kubwa ni barabara. Tunawaomba mtusaidie katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, kuna suala la maboma, ndani ya Halmashauri yetu tuna maboma 170 yanasubiri kumaliziwa, tunaiomba Serikali sijui dada yangu Mheshimiwa Ummy katika bajeti ya mwaka huu umetutengea kiasi gani? Tunaomba tufanya jambo hilo ili zile nguvu ambazo wananchi wamezitumia zikakamilike na waone faida yake. Tutaendelea kuwahamasisha kufanya mambo mengine, lakini kama haya hatujawakamilishia wataona kama vile tunawapotezea nguvu zao. Kwa hiyo, katika bajeti hii sijui Halmashauri yetu umetutengea kiasi gani, lakini tunaomba maboma yakamilike.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningependa kulizungumza ni kwenye masuala ya madeni ya watumishi. Katika Halmashauri yetu watumishi wanadai karibu shilingi bilioni mbili. Watu hawa wanajitoa kwa hali na mali katika kufanya kazi, inapofika mahali hatuwezi kuwapatia fedha ambayo ni stahiki yao, tunakuwa hatuwatendei haki. Nawaomba katika bajeti hii, fedha zitengwe watu wapate haki zao ili waweze kututumikia vizuri vile inavyopasa.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, namwomba dada yangu Mheshimiwa Ummy au wasaidizi wake, tukimaliza bajeti twende wote wakaone uhalisia wa Jimbo la Morogoro kusini na Halmshauri ya Morogoro jinsi gani ilivyo ili wakija katika bajeti ijayo wawe na mpango uliokuwa sahihi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii nyeti ambayo imegusa maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya katika Wizara lakini vilevile kuwapa pole kwa haya ambayo yanaendelea kutokea. Yote haya naamini kabisa yanatokana na ufinyu wa bajeti ambapo kwa namna moja au nyingine kama wangeweza kupata fedha nyingi haya yasingetokea.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi kubwa ambayo Wizara inafanya, naomba niseme bado kuna kazi kubwa ambayo Wizara inaifanya katika kuinua kilimo kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, mimi nijikite kwenye eneo moja tu; naamini kabisa kilimo chenye tija na cha uhakika kwa Mtanzania ni kilimo cha umwagiliaji. Hadi hivi sasa tunavyozungumza kupitia Tume ya Umwagiliaji, tunaambiwa kwamba kuna lengo la kulima hekta milioni moja na laki mbili na hadi hivi sasa tumefikia asilimia 58 ambayo ni hekta 695. Ombi langu na ushauri wangu kwa Serikali, naomba tujikite kwenye maeneo ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, nianze na moja tu, tunapoteza maji mengi ambayo yanakwenda baharini na Serikali imekaa hatuingii huko. Mfano, nataka nizungumzie kwenye Bonde la Kongwa unapoingia Kibaigwa, maji yanatiririka mwaka mzima, yanakokwenda hapajulikani lakini pale tungeweza kuchimba mabwawa watu wakafanya kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile Mto wa Dumila, mpaka tunaharibu barabara, zinakatika. Mimi niishauri Serikali katika maeneo kama yale ya Dumila, Ruvu, hebu tungechimba mabwawa watu waweze kufanya kilimo cha umwagiliaji ambacho kitaweza kuleta tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi Watanzania wanalima maeneo makubwa, dhamira kubwa ni kukusanya kidogokidogo kwenye kila hekta ili kuweza kupata tija. Nilipata nafasi ya kwenda China mara mbili, mtu analipa hekta tano, tatu analima mpunga mbili analima kilimo cha horticulture, ndani ya mwaka anapata tija kubwa kuliko Mtanzania ambaye analima hekta mia katika Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naamini kabisa kilimo cha umwagiliaji ndicho ambacho kitamkomboa Mtanzania. Mkoa wa Morogoro umeambiwa ni FAMOGATA – Fanya Mkoa wa Morogoro kuwa Ghala la Taifa la Chakula. Ndani ya Mkoa wa Morogoro tuna eneo ambalo linatosha kwa kulimwa kwa kilimo cha umwagiliaji hekta 230,000 lakini mpaka hivi sasa tumetumia hekta 28,000 tu. Kama kweli we are serious na kilimo hebu tu-inject hela katika kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo langu la Morogoro Kusini tuna mradi wa Kongwa Tulo ambao una uwezo wa kulima hekta 3,000. Hadi hivi sasa zimetumika hekta 200 tu. Kuna mradi wa Mbangarawe, kuna hekta 230 tumetumia hekta 200 tu bado 30. Kuna mradi wa Lubasazi, una uwezo wa kulima hekta 120, hadi hivi sasa kuna shilingi milioni 800 imewekwa pale lakini bado mradi haujaendelea, maana yake tumeweka fedha ambazo hazitumiki. Kuna mradi wa Kirokwa ambao una hekta 105, mpaka dakika hii tunatumia hekta 40.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukijaribu kuangalia, tuna-ijnect fedha kwenye miradi lakini haifanyi kazi. Tumeomba katika mradi wa Kongwa Tulo ili tuweze kuendelea mwaka karibu wa pili huu sasa, nilikuwa Mbunge miaka mitano iliyokwisha, miaka mitano nimekwenda likizo, hakuna kilichowekwa. Sasa hivi tumeomba tena shilingi bilioni 1.4; Mbarangwe shilingi bilioni 1.5; Lubasazi shilingi bilioni 1.5; Kiroka shilingi bilioni 3, ukijumlisha ni shilingi bilioni 7. Fedha hizi tukipeleka pale nina uhakika tutanyanyua kilimo cha Watanzania na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nizungumzie suala la masoko. Kwa kweli watu wengi wamezungumzia suala la masoko; ni kero kwa wakulima wetu. Hivi ninavyozungumza kuna wakulima wangu kule mazao yako ndani na wanakaribia kuuza nyumba zao kama hatutaweza kuwasaidia kuwapatia masoko.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu ya wataalam ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Kwa kuwa muda ni mchache, niombe nijikite katika maeneo kama mawili, matatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, niiombe Wizara kuna mbuga mpya ambayo imetangazwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo zamani ilikuwa ni pori la hifadhi. Niombe Wizara mbuga hii ni kubwa ina wanyama wengi, ina wanyama wakubwa na wazuri ambao inaweza kuwa ni kivutio kikubwa kwa watalii katika nchi.

Ombi langu kwa Wizara ni kwamba utangazaji wa mbuga hii bado haujakuwa mkubwa kiasi cha kuwafanya watalii wengi wafike kule. Ukiangalia bado tunatangaza mbuga ambazo ziko kaskazini wakati mbuga hii ni kubwa inaweza ikaongezea mapato makubwa Serikali na kufanya kwamba mambo yawe mazuri katika pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naamini kabisa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo linajengwa kule nalo linaweza likawa ni moja ya kivutio kikubwa cha watalii. Kwa hivyo niombe sana Wizara iangalie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo ningependa kuchangia na sisi Morogoro kule kuna eneo linaitwa Kisaki majimoto. Kuna maji ambayo yanachemka na mayai yanachemshwa. Niombe nacho ni kivutio ambayo Wizara kwa namna moja au nyingine watume wataalam wakaangalie jinsi gani wanaweza wakakitumia kivutio hicho kuongeza mapato kwenye Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo ningependa kuchangia katika Wizara hii, kati ya mwaka 2016 na mwaka 2021, kuna watu 46 wameuawa na mamba, kuna watu 15 katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini wamepata vilema vya kudumu kutokana na ongezeko kubwa la mamba katika Mto Ruvu na Mto Mvuha ambao unapita katika Vijiji vya Tununguo, Mkulazi, Selembala pamoja na Kijiji cha Mvuha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu ni kwamba, idadi kubwa ambayo imetokea katika vifo kutokana na mamba imetokea katika Kata ya Selembala. Mwaka 2016 kumetokea vifo vya watu watatu; mwaka 2017 kumetokea vifo vya watu tisa; mwaka 2018 watu watano; mwaka 2019 watu sita; mwaka 2020 watu 14 na hadi Mei mwaka huu, watu tisa wameshakufa katika Kata ya Selembala. Kuna taharuki kubwa kwa watu na hasa ukitilia maanani watu wengi vijijini wanatumia maji ya mto wanashindwa kwenda kuchota kwa sababu wakienda wanakumbana na vifo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali, naamini kwamba mamba wamekuwa wengi na naamini kwamba ni wakati muafaka kwa sasa kwenda kuvuna mamba hao ili tuepushe vifo vya watu, lakini wakati huo huo tukapata fedha katika kuuza ngozi za mamba hao. Sambamba na hili vile vile nikuombe kupitia Wizara kwamba, tunaomba vifuta jasho kwa watu hawa ambao wamepoteza maisha kwa mujibu wa taratibu na sheria za maliasili.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe vile vile kupitia Bunge lako Tukufu, kwa Wizara ya Maliasili na Utalii isaidie Halmashauri ya Morogoro Vijijini kwa vitendea kazi vya magari, lakini vile vile Askari wa Wanyamapori ili waweze kwenda kutusaidia ongezeko la wanyama ambao wamefanya uharibifu mkubwa kwenye Kata ya Kisaki, Kata ya Bwakila Chini, kata ya Serembala, Kata ya Mvuha. Nashukuru na naipongeza Wizara katika mwaka 2019 tumelipwa kifuta jasho kwa wakulima ambao waliharibiwa mazao na wengine ambao wamepoteza maisha wamepata kifuta jasho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado katika mwaka 2020 hatujapata kifuta jasho kwa wakulima ambao ekari 572 zimeathiriwa na ongezeko la wanyama hao waharibifu na wengine ambao wameshambulia watu. Ombi langu kwa Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, muda wako umeisha Mheshimiwa.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo ipo mbele yetu, lakini kubwa zaidi nikupongeze wewe binafsi kwa kazi kubwa ambayo unaifanya hapo katika kiti katika kutuongoza. Hakika wewe ni mtoto wa nyoka na kama sio wa nyoka basi ni mjukuu wa nyoka, maana yake damu ya ukoo wa Adam Sapi Mkwawa inaonekana inafanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Naibu wake na timu nzima ya wataalam kwa kutuletea bajeti ambayo kiuhakika imebeba dhana ya maelekezo ya mama yetu Samia Suluhu Hassan, lakini kubwa zaidi Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi katika kumsaidia Mtanzania kusonga mbele kutoka hapa tulipo na kwenda mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni uthibitisho tosha umeona kila Mbunge aliyesimama anapongeza, lakini sio Mbunge kwa sababu sisi Wabunge tulichangia katika bajeti katika Wizara mbalimbali, tukieleza zile kero za wananchi wetu na wananchi wetu huko nje vile vile wamepata faraja kubwa na wanaendelea kuipongeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa hongera sana kwa mdogo wangu Mheshimiwa Mwigulu na timu yake kwa kufuata maelekezo ya mama, lakini kwa kufuata maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Chetu Cha Mapinduzi. Ni imani yangu kabisa tukienda hivi ndani ya miaka mitano hii tutafanya mambo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kumpongeza Mama yetu Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jemedari mkuu katika nchi yetu, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya ndani ya kipindi cha siku 100 anakoelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika mama huyu ni Mama shujaa, mama shupavu ambaye kwa uhakika niwaambie Watanzania na naendelea kusema mama huyu anatosha, anatosha na atatuvusha salama Watanzania kule tunapotarajia kwenda. Hata hivyo, nitumie nafasi hii…

T A A R I F A

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa tu ndugu mzungumzaji kwamba mama huyu sio tu anatosha bali anatosha na chenji inabaki. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kalogeris, endelea na kuchangia.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nimeipokea taarifa. Ni kweli chenji bado inabaki na itatosha kufanyia mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii vile vile kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, ndugu yetu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ndani na nje ya Bunge katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, lakini kuwa kama kiungo kati ya Mama Baraza la Mawaziri lakini na sisi Wabunge katika kuona kipi kifanyike. Ni imani yangu kwamba hata haya yaliyokuja kuna majumuisho makubwa ambayo yamefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii vile vile kutoa pongeza za dhati kwa Serikali yangu. Hakika kauli yake Mama, anatusalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sisi tunatakiwa kujibu kazi iendelee, kazi inaendelea tena kwa kasi kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona tumepata milioni 500 kila Jimbo kwa ajili ya TARURA. Wabunge tumepiga kelele kwamba barabara mbaya, barabara mbovu, lakini mama ametusikia ametupa. Pia nimpongeze ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu na naamini hayo ni maelekezo ya Mama kwa kubuni vyanzo mbalimbali ambavyo tunaamini kwa mwaka huu wa fedha tutakwenda kutengeneza bilioni 300 ambayo inaonekana inakwenda TARURA. Ombi langu kwa Serikali, Halmashauri, Majiji na Manispaa tumetengwa katika fedha za Mfuko wa Barabara, wamependelewa wenzetu wa Majiji na Manispaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu fedha hizi katika mgao wake uende kwa majimbo bila kujali la Manispaa au la Jiji na kadhalika ili na sisi Halmashauri twende tukajenge barabara ambayo ukitilia maanani mtandao wa barabara kwenye halmashauri ni mkubwa kuliko kwenye majiji au manispaa. Kwa hivyo niwaombe Wabunge wenzangu katika hili tuwe pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha TAMISEMI mgao wa fedha hizi bilioni 300, zigawiwe katika majimbo, nikiamini kila Jimbo litapata karibu millioni 800 na tutaenda kufanya kazi kubwa ya barabara. Ndani ya miaka mitano nataka nithibitishe katika Bunge hili kwamba suala la barabara litakuwa ni historia katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii vile vile kutoa pongezi za dhati kwa Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi tuliahidi na bahati nzuri nilikuwa ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa mpaka naingia hapa Bungeni. Nilipita Mkoa mzima wa Morogoro tukiahidi kila kitu tutafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la REA, walipotuambia umeme tulisema mpaka kufikia 2023 tutakuwa tumekamilisha kabisa. Nataka nitoe taarifa na shukrani za dhati kwa wananchi wa Jimbo la Morogoro Kusini na Mkoa wa Morogoro. Jana Mkoa wa Morogoro tumezindua rasmi REA III mzunguko wa II, vijiji vyote vinapata umeme. Hongera sana kwa Serikali yangu ya Chama Cha Mpinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru leo asubuhi katika kuuliza swali imeonekana vijiji vile ambavyo vimepungua, Wizara imesema kwamba navyo vitaingia hata kama havipo. Kwangu vimebaki vijiji vitano tu, ahsanteni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile niishukuru Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi kwa kazi kubwa ambayo imeifanya, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alipokuwa katika ziara yake katika siku zake za mwisho katika dunia hii, alisimama Morogoro na akasema atatoa kilometa 40 kujengwa kwa lami kutoka Mjini Morogoro mpaka tutakapoishia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru katika bajeti hii tumetengewa kilometa 15 na tayari imeshatangazwa maana yake kazi inaenda kufanywa, nina kila sababu ya kuipongeza Serikali, lakini niiombe Serikali barabara hii inakwenda mpaka kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere inakwenda mpaka kwenye Hifadhi ya Mwalimu Nyerere tuendelee kutenga fedha ili tufike huko, utalii ukaendelee kuwepo kwenye Hifadhi, lakini vile vile katika hilo bwawa la Mwalimu Nyerere. Naamini bwawa hili likikamilika utakuwa ni utalii mkubwa ambao utaingiza fedha nyingi kwenye Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, naomba nichangie kwenye maeneo mawili. Eneo la kwanza ni kwenye kodi; ni imani yangu hakuna Mtanzania ambaye hataki kulipa kodi, ila lipo jambo ambalo Serikali inatakiwa kufanya kupitia TRA kwamba kodi inayokadiriwa iwe na uhalisia na inayolipika. Katika maeneo mengi wafanyabiashara wanalia na ukweli usiofichika wanalia, kuna kama dhuluma ambayo inatendeka. Sasa katika hili, Mama yetu amesema hataki dhuluma, anataka watu walipe kodi kwa hiyari, naomba Mheshimiwa Waziri akasimamie hili TRA, kodi ikawe ya uwazi na iwe inayolipika kulingana na mwananchi alivyopata kipato chake, failure to that, ni kwamba watu watakwepa au tunatengeneza mianya ya rushwa kati ya watu wa TRA na walipakodi, mwisho wake kodi itakuwa haiwezi kulipika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho ambalo ningependa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja ili kazi iendelee, haya yote niliyosema yakamilike. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaitenda akiwa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nakumbuka katika Bunge lililopita nilisema kwamba mama huyu anatosha, na ni kielelezo tosha kwamba tumeshuhudia utendaji wake wa kazi uliotukuka. Sasa hivi majimboni mambo mazuri, sisi Wabunge tuko vizuri tukiamini kabisa kwamba utendaji wake wa kazi unatusaidia katika kutekeleza majukumu yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo anaitenda ndani na nje ya Bunge, akiwa kama Mtendaji Mkuu wa shughuli za Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Na nimpongeze kwa bajeti nzuri ambayo ameileta imesheheni katika kila sehemu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaamini ikipita na tunaamini itapita, na kwamba italeta matokeo mazuri katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama changu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi nijikite moja kwa moja katika kuchangia hoja. Cha kwanza, nichangie hoja katika hotuba yake namba 57 ukurasa wa 33 ambayo inaonekana itakuwa mwarobaini wa migogoro ya wakulima na wafugaji. Tumeona hapa Serikali imepanga katika mwaka huu wa fedha kutengeneza mashamba darasa katika Wilaya ya Handeni na Longido. Niiombe Serikali, Mkoa wa Morogoro vile vile ni Mkoa ambao una migogoro mikubwa ya wakulima na wafugaji, lakini una ardhi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba katika mwaka ujao wa fedha au mwaka huu wa fedha wangeweka utaratibu wa kutengeneza mashamba darasa katika Mkoa mzima wa Morogoro na ikiwezekana Mkoa wa Pwani ili wale wafugaji wenyeji walioko pale wapate utaalamu wa kutengeneza haya mashamba darasa, ili wawe na utaratibu kwamba, Januari atalisha hapa, Februari atalisha hapa, Machi atalisha hapa, mpaka mwaka mzima unapita na kuacha kwenda kuzurura ovyo kuchunga na kuingia katika migogoro ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kukupongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo uliifanya katika utunzaji wa mazingira Kitaifa katika Mbuga ya Ngorongoro. Ninaamini kabisa Ngorongoro ni urithi katika Taifa hili, kuendelea kuiachia watu wakaivamia, tutakuwa tunapoteza urithi huo, lakini kubwa zaidi tutapoteza fedha nyingi za kigeni ambazo zinasaidia katika kuendesha nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hili alilolifanya kama Waziri Mkuu, na ninaamini alishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Mazingira, sasa hivi tujielekeze katika kukabiliana na janga lingine la migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali katika mkoa huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kama tumeweza kupata hekta 500,000 ambazo Serikali imezipata Handeni, Tanzania bado ina maeneo makubwa ambayo tunaweza kwenda kuyapima na kuwapeleka wafugaji wakakaa huko wakanusuru mifugo yao katika kipindi cha kiangazi na tukaondokana na migogoro mikubwa ya wakulima ambayo haina sababu. Hili ni janga kubwa huko tuendako kama Serikali haitalisimamia na kulichukulia kwa umakini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini Mheshimiwa Waziri Mkuu akiamua na timu yake; Wizara ya Mifugo, Wizara ya Ardhi, wanaweza waka-allocate maeneo mbalimbali katika Tanzania yetu kama vile tulivyofanya Handeni tukapeleka huko nako wafugaji wengine wakakaa wakajengewa miundombinu ya barabara, maji na nyumba. Leo hii tunaambiwa kwamba tumepata ardhi, tumepata nyumba na tayari 101 zimeshajengwa kati ya nyumba 300; visima vinne vimeshachimbwa kati ya visima 13. Naamini Serikali ikiamua inaweza. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kama watu walivyokuwa wanapiga kelele kwamba tunafanyaje katika kunusuru mifugo? Tunafanyaje katika kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji? Naamini kama hii Serikali itashughulikia hili, itakuwa imetusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikwambie, kuwaachia Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji, haitawezekana kabisa kwa sababu hili tayari limeshakuwa janga kubwa na hawana uwezo nalo. Kinachotokea sasa hivi, tutakuja kufika mahali tutagombana kati ya wachuguliwa na watendaji wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala la barabara. Tumefanya mambo mengi, naipongeza Serikali yangu kwa kazi kubwa iliyoifanya. Kuna suala la TARURA, tulipata shilingi bilioni 1.5. Naomba na ninaielekeza Serikali, ikiwezekaa TARURA waongezewe fedha ili waweze kujenga madaraja huko vijijini. Kwa baadaye, naiomba Serikali ikiwezekana kuwe na special program kwa majimbo na wilaya zilizokuwa pembezoni ili ziongezewe fedha zaidi katika kutekeleza majukumu yake ya kutengeneza barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naipongeza Serikali kwa suala la TANROADS. Tumepata lami katika Barabara ya Bigwa – Kisaki yenye kilometa 15, tunasubiri mkandarasi tu, muda wowote aanze kazi. Pia kuna barabara yenye kilometa
63 kutoka Kiloka kwenda Mvuha, tayari tunatarajia kuitangaza. Ombi langu kwa Serikali, barabara ya Bigwa – Kisaki yenye kilometa 140 kwenye mradi wa umeme, lakini vilevile kwenye hifadhi ya Mwalimu Nyerere, ni hifadhi ambayo utalii wake utaweza kuwa mkubwa kama tukifika katika kilometa zilizobakia 40. Naiomba Serikali kushughulikia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali katika suala la afya. Wilaya ya Morogoro Vijijini, hospitali yao imekamilika; vituo vya afya, sita vipo; changamoto zetu, nianze na kimkoa. Mheshimiwa Mbunge wa Morogoro Mjini amezungumzia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa; Morogoro ni katikati, lakini hakuna Hospitali ya Rufaa, tuna Hospitali ya Mkoa. Tunaiomba Serikali itujengee Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro ili tuweze kunusuru maisha ya watu katika ajali za barabarani zinazotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna changamoto ya uhitaji wa vifaa tiba na dawa na majengo ya OPD katika Halmashauri ya Morogoro vijijini…

(Hapa, kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa kwa mchango mzuri wa Morogoro na maeneo mengine.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi ys kuchangia Mpango wa Taifa wa maendeleo. Nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mama yetu, Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuiendeleza nchi yetu. Nitumie nafasi hii na mimi nitoe mchango wangu kwa Taifa kwenye sekta ya utalii. Sisi wote ni mashuhuda, Mama amefanya kazi kubwa kupitia Royal Tour, watalii wamekuwa wengi na kuna kila sababu ya sasa kuelekeza maeneo mengine yenye utalii ili kusudi tuweze kuongeza pato kwenye Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi utalii upo katika Nyanda ya Kaskazini, lakini nchi yetu imepata bahati ya kuwa na vivutio vingi vya kitalii hata katika sehemu zote za Tanzania. Kuna mradi mkubwa ambao unafanyika wa kuendeleza utalii na kuendeleza rasilimali kusini ya nchi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mbuga ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lakini kuna Mbuga ya Mikumi, kuna Mbuga ya Uduzungwa zipo katika Mkoa wa Morogoro. Vile vile kuna Mbuga ya Ruaha Mkoa wa Iringa na kuna Mbuga ya Katavi Mkoani Katavi. Katika mpango huu wa REGROW tuna kila sababu ya kudhani kwamba, kama Serikali itasimamia kikamilifu mpango huu tuna uhakika wa kupata mapato mengi kwenye mbuga katika Ukanda wa Kusini na kuongeza mapato makubwa katika Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe tu kupitia mpango huu Serikali isimame na ihakikishe kwamba kuna fedha nyingi, najua zimepelekwa, zikasimamiwe inavyopaswa ili ziweze kuleta matokeo chanya. Yakajengwe madaraja kwenye hifadhi zetu, zikajengwe barabara kwenye hifadhi zetu, lakini vile vile zikatumike kufanya promotion ya utalii ili kusudi tuongeze pesa katika sekta ya utalii na kuweza kupata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, sambamba na hilo katika mbuga ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo iko Wilayani Morogoro, niiombe Serikali, ili kuweza kuwafanya watalii waweze kufika kwa haraka lakini vile vile kwa wepesi na kwa wingi barabara ya Digwa-Kisaki iko katika mpango wa ujenzi. Bajeti iliyopita imetangazwa, tuliahidiwa mpaka kufikia Mwezi wa Tisa itakuwa tayari imeshatangazwa kwenye TANePS kwa ajili ya kumpata mkandarasi. Hata hivyo, mpaka muda huu tunaozungumza jambo hili halija-tick. Nikuombe tu Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya ujenzi lakini Waziri wa Fedha najua fedha ipo basi kazi hii ifanyike ili kusudi suala hili likamilike tuweze kuongeza utalii. Tukiweza kuongeza watalii kwa upande wa kusini ni imani yangu kwamba tutakuwa tumepata fedha nyingi za utalii na tutaweza kusaidia kusukuma maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, nitumie nafasi hii kuipongeza Kamati ya Bajeti, tumeona ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Bwawa la Mwalimu Nyerere lipo katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini, Jimbo la Morogoro Kusini ambalo mimi nipo kule, lakini vile vile lipo katika Halmashauri ya Rufiji. Bwawa hili likikamilika litaweza kuleta matokeo makubwa sana katika uchumi wa nchi yetu. Niombe Serikali ikasimame katika mazingira yanayotakiwa kuhakikisha kwamba linakwisha kwa muda na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bajeti imesema, mradi ulikuwa unatakiwa kukamilika tarehe 15 mwezi Juni mwaka huu, lakini wameongezewa mpaka tarehe 15 mwezi Juni mwaka unaokuja. Ombi langu kwa Serikali, wakandarasi, na mimi mwenyewe ni mkandarasi, kuna ujanja na ubabaishaji; wanaweza wakafika mahali wakataka kutucheleweshea mradi wetu ambao kwetu sisi tunauhitaji kwa kiasi kikubwa. Tuhakikishe kwamba muda huu waliopewa kwa mujibu wa utaratibu kazi iwe imekamilika; kwa sababu; moja, inaonekana, vile vile Kamati yetu imesema, wameongezewa mwaka mmoja lakini mpango kazi wa mkandarasi huyu unaonekana kwamba atamaliza kazi hiyo mwaka 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niombe, wenzetu ambao wanasimama TANESCO wakahakikishe kwamba wanasimama kikamilifu kuhakikisha mradi huu unakamilika ndani ya muda ili yale matumaini ya Watanzania kupata umeme wa uhakika lakini uliokuwa salama uwe umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, katika suala hili la mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kuna suala la CSR. Halmashauri ya Morogoro Vijijini na Halmashauri ya Rufiji mpaka tunafikia asilimia 75 ya ujenzi wa Bwawa hili bado hatujapata fedha yetu ya CSR kwa mujibu wa mkataba unavyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi napata mashaka, kupitia Kamati ya Bajeti, TANESCO kwa mara ya kwanza walipeleka kwa mkandarasi ujenzi wa uwanja wa michezo Dodoma. Mkandarasi akakataa kwa sababu haikidhi vigezo vinavyotakiwa. Lakini tayari katika Kamati ya Bajeti nimeona, safari hii TANESCO tena wamepeleka miradi ambayo haihusiani na wananchi wa Morogoro Vijiji na Halmashauri ya Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuhalisia kuna ujenzi ambao unaambiwa unataka kujenga chuo cha umeme na gesi asilia Lindi, sitaki wala sina mashaka na Serikali kufanya hivyo. Kuna ujenzi wa kituo cha TEHAMA – Kigoma, sina mashaka na Serikali kufanya hivyo, lakini kuna ujenzi wa kituo cha Afya au Zahanati Dodoma sina mashaka na hilo lakini vilevile Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Morogoro hata sisi Halmashauri ya Morogoro Vijijini wanahitaji huduma hizo. Kama ni suala la Chuo cha Umeme, gesi asilia, kwa nini kisijengwe Morogoro au kikajengwa Pwani? Ninaishukuru Kamati ya Bajeti imeliona hilo na imesema, tunaomba fedha ya CSR ambayo iko ndani ya Halmashauri mbili; ya Morogoro Vijijini na Halmashauri ya Rufiji ije kwetu wananchi wenye halmashauri hizo kama vile utaratibu wa mkataba unavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la kilimo. Kilimo ndiyo uti wa mgongo na katika hili umeshuhudia hapa mchana leo kutwa nzima Waheshimiwa Wabunge wakizungumza suala la upungufu wa chakula na tatizo la mvua. Tumefanya kazi kubwa kwenye mbolea, mbegu, viuatilifu na kila kitu. Nadhani ni wakati muafaka sasa hivi tukajipanga katika bajeti yetu ijayo katika kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina maeneo makubwa ya kulima kilimo cha umwagiliaji. Mfano katika Mkoa wetu wa Morogoro, tuna zaidi ya hekta 2,000,000 zinazofaa katika kilimo cha umwagiliaji, lakini kila mwaka Serikali inapokuja inaendelea kuleta bajeti kwenye maeneo ya miradi midogo midogo tu ya umwagiliaji. Nadhani ni wakati muafaka kwa Serikali katika bajeti ijayo, kuangalia miradi mikubwa ambayo italeta tija na wingi wa chakula katika nchi, kitoshe nchini na ikiwezekana tusambaze kwa kuuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, naiomba Serikali, katika mwaka unaokuja iangalie uwezekano wa kuvuna maji ya mvua. Nilishalizungumza katika bajeti karibu mbili. Kipindi cha mvua, pale Mbande, kuna eneo linaitwa Matoroli, maji yanavuka mpaka juu ya barabara. Pia kipindi cha mvua, pale Mtanana karibu na Kibaigwa, maji yanavuka hadi juu ya barabara. Dumila vile vile mpaka yanafanya uharibifu mkubwa kwenye miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuna mabwawa katika station ya reli Msaganza-Kidete. Nadhani ni wakati muafaka kwa Serikali katika bajeti inayokuja ikaelekeza kufukua mabwawa yale, lakini tukachimba mabwawa katika maeneo haya niliyoyasema ili tuvune maji ya mvua, tufanye kilimo cha umwagiliaji ambacho ndicho chenye uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la maji. Niendelee kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo inaifanya katika suala la maji. Karibu tumepata taarifa, maji yamefika vijijini kuna mahali asilimia 80, asilimia 75, lakini uhalisia ni kwamba bado changamoto ya maji ni kubwa katika nchi yetu. Naishauri Serikali yangu, katika bajeti inayokuja, hebu ijielekeze kwenye kufanya miradi mikubwa ya maji yenye uhakika ili iweze kusambaza maji katika maeneo mengi na tukaondokana na adha hii ya maji, kuliko hii miradi midogo midogo ya kuchimba visima, halafu ndani ya kipindi kifupi visima vimekauka; kuchukua maji kwenye mito midogo midogo wakati tuna maziwa makubwa katika nchi hii ambayo tukiyatumia yanaweza kupunguza kero ya maji nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naomba kwa Serikali yangu, ijitahidi kwa kiasi inachoweza kufanya kufanikisha haya yote ili kuleta tija na mafanikio kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Huo ndiyo ulikuwa mchango wangu. (Makofi)