MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri Mkuu kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro pamoja na Waheshimiwa Mawaziri ambao walitutembelea wakati tulipopata maafa.
Mheshimiwa Spika, katika taarifa aliyotoa Mheshimiwa Waziri Mkuu, hakutaja katika taarifa Mkoa mzima wa Morogoro ambao pia ulikumbwa na mafuriko, ikiwemo Wilaya ya Mvomero, Morogoro DC ambayo mimi natoka na Ulanga. Kwa mfano kwenye jimbo langu zaidi ya nyumba 300 na kitu zimevunjika na mashamba. Sasa swali, ni je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na mafuriko haya ambayo yanatokea kila mwaka hasa katika Mkoa wa Morogoro, katika suala la kuchimba mabwawa ili kuweza kupunguza kasi ya mito ambayo iko mingi katika Mkoa wa Morogoro na kuendelea kuleta maafa kwa wananchi wetu na Serikali kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kukabiliana na majanga haya? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Kalogeris, Mbunge wa Morogoro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nakiri kwamba tumesahau kuiweka Ulanga, lakini Ulanga pamoja na Malinyi ni miongoni mwa Wilaya ambazo zimeathirika. Kote huko Kamati zetu za Maafa za Wilaya na Mkoa pamoja na hawa Waheshimiwa Mawaziri Nane na Makatibu Wakuu wote wamepita kule na wameona hiyo hali. Pia nimepata nafasi, nimepita maeneo hayo kutoka kule Mlimba, nimekuja Ifakara Mjini. Nilipokuwa naenda Malinyi nilipitia Ulanga kuona hali hiyo. Hakika hali siyo shwari sana kwa sababu eneo lote limejaa maji; na bado nikapita juu ya Mto Rufiji mpaka Rufiji kwenye kuona hali hiyo na ujaaji wa maji. Ni kweli kwamba maeneo hayo yamepata athari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nini mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba bonde hili tunalitumia vizuri na hasa kwa kuelekeza maji kwenye maeneo yanayoweza kuleta manufaa kwa wananchi. Tayari Wizara zetu mbili, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zimeshaandaa mpango wa kuchimba mabwawa, yatakayoweza kukusanya maji haya kwa matumizi mbalimbali ikiwemo moja, umwagiliaji na mbili, kutakuwa na uvuvi mdogo mdogo kwa maeneo hayo yenye mabwawa pamoja na kunyweshea mifugo yetu. Tayari wataalamu wako Ifakara kuona maeneo sahihi ya kuchimba mabwawa hayo ili kuchepusha maji kutoka kwenye ule Mfereji Mkubwa wa Rufiji na kupeleka kwenye mabwawa hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkakati huu pia unaendelea mpaka uelekeo wa Mto Wami, ambako huko nako pia kupitia mfereji ule tunachimba Bwawa kubwa sana la Kidunda kwa ajili ya matumizi ya maji ambayo yataingia Jijini Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaendelea na mpango huu mpaka Bonde la Mto Rufiji, Maeneo ya Rufiji yenyewe nako pia tumeshatenga fedha kwa ajili ya kuchimba mabwawa ili tuelekeze maji yetu katika maeneo hayo, tuyahifadhi halafu tutakuwa tunayatumia kulingana na mahitaji kwenye maeneo yote matatu ya kilimo, mifugo pamoja na uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa namna hii hii tutaendelea na mabonde yote. Bonde la Mto Ruvuma tutafanya kazi hiyo; kule eneo la Nyasa tutafanya jambo hilo na Wizara zetu zimeendelea kuongezewa bajeti na wataendelea na kazi hiyo kadiri tunavyopata fedha. Ahsante sana. (Makofi)