Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Innocent Edward Kalogeris (3 total)

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvuna mamba katika Mto Ruvu hasa katika Vijiji vya Kigamila, Bwila juu, Magogoni, Bwila chini, Kongwa, Tulo, Lukuhinge, Kata za Mvuha na Serembala katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini, ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na mamba hao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Edward Kalogeris, Mbunge wa Morogoro Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya mamba katika mito iliyopo katika Mikoa ya Katavi, Rukwa na Morogoro. Baada ya tathmini hiyo kukamilika na kubainika kuwa idadi ya mamba waliopo ni kubwa, mamba hao watavunwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, endapo itabainika kuwa idadi ya mamba katika maeneo husika ni ndogo, Serikali itabaini mamba wanaosababisha adha kwa wananchi na kuwavuna ili wasiendelee kuleta madhara makubwa kwa wananchi. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza: -

Je, ni lini ahadi ya ujenzi wa uwanja wa mpira Dodoma iliyotolewa na Mfalme wa Morocco itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana na kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Edward Kalogeris, Mbunge wa Morogoro Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imefuatilia utekelezaji wa ahadi ya ujenzi wa uwanja wa mpira Dodoma iliyotolewa na Mfalme wa Morocco. Mawasiliano kuhusu utekelezaji wa mradi huo baina ya Serikali ya Tanzania na Morocco bado yanaendelea. Vilevile katika kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa Serikali imedhamiria kutafuta fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali vikiwemo sekta binafsi na wabia wa maendeleo.
MHE. DENNIS L. LONDO K.n.y. MHE. INNOCENT E. KALOGERIS aliuliza: -

Je, ni lini TFS itaanza kutoa vibali vya malisho kwa wafugaji kama inavyotoa vibali vya kuvuna mbao na mkaa ili Serikali ipate mapato?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Edward Kalogeris, Mbunge wa Morogoro Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Misitu, Sura ya 323, Kifungu cha 26(n) kinakataza kuingiza au kuchunga mifugo kwenye maeneo ya hifadhi. Aidha, Kanuni za Misitu za mwaka 2004, Kifungu cha 14(4) kimeweka katazo la kutoa vibali vya kuchunga au kulisha mifugo au kufanya shughuli za kilimo kwenye hifadhi za misitu.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa kuchunga, kulisha mifugo au kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo ya hifadhi za misitu ni kuvunja sheria. Hivyo, sheria zimewekwa ili kulinda rasilimali zilizomo hifadhini kwa matumizi endelevu ya rasilimali za misitu kwa kizazi cha sasa na vijavyo.