Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Innocent Edward Kalogeris (2 total)

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na idadi kubwa ya vifo ya karibu watu 60 ndani ya mwaka mmoja na watu 30 kupata vilema vya kudumu, Serikali inakuja na majibu ya kusema kwamba inafanya tathmini. Ni tathmini gani ambayo inataka kuifanya ili kujiridhisha ili waende wakavune na ni lini watakamilisha hiyo tathmini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, ni lini Serikali itatoa kifuta machozi kwa watu ambao ndugu zao wamefiwa au wameliwa na mamba na wengine wamepata majeruhi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Edward Kalogeris, Mbunge wa Morogoro Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe ufafanuzi katika eneo la kufanya tathmini. Maeneo ambayo anayaongelea Mheshimiwa Mbunge ni maeneo ambayo kiuhalisia, ni maeneo ya Mito na maeneo mengi ya Mito mamba wengi wanapenda kuishi maeneo hayo. Sekta ya Maliasili na Utalii tunahifadhi maeneo mbalimbali ambayo yanakuwa yamehifadhiwa. Lakini maeneo ya Mito ni maeneo ya mtiririko ambapo ukiangalia Mto kutoka eneo moja kwenda lingine ni eneo refu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunafanya tathmini kuangalia namna ya hawa mamba wanavyoishi majini kwa sababu, wanasafiri wanatoka njia moja kwenda njia nyingine. Unaweza ukamuona mamba yuko Morogoro lakini baada ya muda fulani ukamkuta yuko Pwani au yuko Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa hiyo, tunafanya tathmini kuangalia hii namba ya hawa mamba ni kubwa kiasi gani. Kwa sababu, nao wana umuhimu fulani ambao katika maeneo hayo wanapaswa kuwepo sio kuwaondoa kabisa, kwa sababu vile vile, hiyo tunatambua kwamba ni moja ya maliasili ambayo inapaswa kuhifadhiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo, tukishakamilisha tathmini tutaangalia kama idadi ni kubwa basi tutawavuna. Swali la kwamba ni lini ni pale ambapo tutakamilisha tathmini ambayo sasa hivi mchakato wake tumeshaanza na kama ambavyo nimesema ni Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Katavi na Rukwa ambako ndio inasemekana kuna mamba ambao wanasumbua sana. Ikishakamilika tu ndani ya mwaka huu wa fedha tutawavuna ama kuwapunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine ameongelea kuhusu kifuta machozi nimtoe wasiwasi tu Mbunge kwamba, suala la kulipa kifuta machozi tumelianza toka mwaka wa fedha ulioisha na sasa hivi kuna maeneo yanaendelea kulipwa. Kwa hiyo, hata kwenye eneo lake kama wananchi hawajapata kifuta machozi basi ninawaelekeza Idara ya Wanyama Pori, wataenda katika eneo hili na wataenda kulipa wale wananchi ambao wameathirika na tatizo hili. Ahsante. (Makofi)
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiofichika kwamba ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo na shughuli za Serikali kwa Makao Makuu ya Dodoma haukwepeki. (Makofi)

Je, Serikali pamoja na majibu ya kusema kutafuta wabia, wadau mbalimbali wa michezo, kwa nini Serikali isiwe na commitment kwamba mwakani katika bajeti tunatenga fedha ili ujenzi huo uanze, ukitilia maanani uwanja hauwezi kujengwa kwa mwaka mmoja?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Innocent kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekwisha kujipanga na ndio maana tumeshafanya upembuzi yakinifu kujua kwamba huu uwanja tunaujenga wapi, lakini kwa gharama gani. Huu uwanja unahitaji zaidi ya shilingi bilioni 420 na Serikali tuko kwenye hizo hatua pamoja na maongezi yanayoendelea lakini ndani ya Serikali tunaendelea kutafuta fedha.

Mheshimiwa Spika, nihakikishie Bunge hili tukufu huu uwanja pia ni ahadi ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 na lazima tutaujenga.