Primary Questions from Hon. Jonas Van Zeeland (12 total)
MHE. JONAS V. ZEELAND: Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaondoa wanyama wakali hasa tembo katika Tarafa ya Mlali na kuwarudisha kwenye Hifadhi ya Taifa Mikumi kwa kuwa wamekuwa kero kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa pole kwa wananchi wote wanaokutana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo. Wizara imeendelea kudhibiti wanyamapori hawa katika Wilaya ya Mvomero, Mkoani Morogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada za kukabiliana na matukio haya, Wizara kwa kushirikiana na viongozi wa Mkoa iliweka mkakati wa pamoja ambapo kutakuwa na vikosi maalum vya kudhibiti tembo. Vikosi hivyo vimeendelea kutoa msaada wa haraka pale inapotokea tatizo katika Mkoa wa Morogoro na maeneo mengine ikiwemo Wilaya ya Mvomero. Vikosi hivyo vimewezeshwa kwa kupatiwa vitendea kazi muhimu vinavyohitajika katika zoezi la kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu. Vifaa hivyo ni pamoja na magari, risasi za moto, risasi baridi na mabomu maalum ya kufukuzia wanyamapori hususan tembo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na jitihada hizo, Wizara imenunua na kusambaza simu zenye namba maalum katika maeneo 14 nchini kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wanatoa taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu, kwa haraka bila malipo na kwa wakati ili ziweze kushughulikiwa mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne ya ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mzumbe hadi Mgeta?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo: -
Barabara ya Mzumbe – Mgeta yenye urefu wa kilometa 26 ni sehemu ya barabara ya Mkoa ya Sangasanga – Langali – Luale hadi Kikeo yenye urefu wa kilometa 59.16 na inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Mheshimiwa Spika, Ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mzumbe - Mgeta yenye urefu wa kilometa 26 imeanza kutekelezwa kwa awamu ambapo mwaka 2020 Serikali ilikamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami wa kipande cha mita 400 kuanzia Mzumbe na katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali inaendelea na ujenzi wa kipande kingine cha mita 700 kwa shilingi 216,800,000 na kazi ilianza Novemba, 2021 na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2022. Sehemu iliyobaki itaendelea kujengwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha shilingi 664,557,000 kimetengwa kwa kazi hiyo. Ahsante.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kumaliza barabara ya Manyinga hadi Madizini kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland Mbunge wa Jimbo la Mvomero, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 500.00 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwa urefu wa kilomita 0.54 ambapo ujenzi huo umekamilika.
Mheshimiwa Spika, TARURA itaendelea na ukamilishaji wa kipande kilichobaki kulingana na upatikanaji wa fedha ili wananchi wa eneo la Madizini na sehemu zingine katika tarafa ya Turiani waweze kufanya shughuli zao za kijamii na kiuchumi kwa ufanisi.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatatua migogoro ya Wakulima na Wafugaji Kata za Hembeti, Mkindo, Sungaji, Mtibwa, Kanga, Mziha na Doma?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi naomba kujibu swali Na. 63 la Mbunge wa Mvomero kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa migogoro ya wakulima na wafugaji katika Kata za Hembeti, Mkindo, Sungaji, Mtibwa, Kanga, Mziha na Doma Wilayani Mvomero. Kwa kutambua hilo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo hatua ya mwaka 2013 ya kutenga kwa kutumia fedha za ndani kwenda kutatua migogoro katika jumla ya vijiji 72 kati ya vijiji 130 vilivyomo katika Wilaya hiyo ambavyo vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Wamembiki na Wananchi wa Vijiji vinavyopakana na Hifadhi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba Wami-Mbiki linapakana na vijiji 24 ambapo vijiji Nane vipo upande wa Wilaya ya Mvomero na vijiji Vitatu vipo upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Aidha, vijiji 13 vipo upande wa Wilaya ya Chalinze, Mkoani Pwani.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa migogoro hii iliwahi kupitiwa na Kamati ya Mawaziri Nane, Serikali kupitia maamuzi ya Baraza la Mawaziri imeshaanza kutatua migogoro hiyo. Utekelezaji wa uamuzi wa Baraza la Mawaziri ulianza tarehe 05 Oktoba, 2021 kwa Mawaziri wa Kisekta na wataalam kupita katika Mikoa yenye migogoro ikiwemo Mkoa wa Morogoro. Aidha, wataalam kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa na Wilaya husika wamepita katika vijiji vyote 24 vinavyopakana na Pori la Akiba la Wamembiki. Baadhi ya mipaka ya vijiji imeonekana kuwa na muingiliano na Mipaka ya Pori la Akiba la Wamembiki. Kwa kuwa watalaam wa Kamati ya Kitaifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi bado wako uwandani Mkoani Morogoro suala hilo litapatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa na Wilaya husika.
Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa wananchi wa Wilaya ya Mvomero hususani katika vijiji vinavyopakana na Pori la Akiba Wamembiki kuwa wavumilivu na kuheshimu mipaka iliyopo wakati Serikali ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa migogoro hiyo.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuiliza: -
Je, ni kesi ngapi za Wakulima kulishiwa mazao yao zimeripotiwa na ngapi zimepelekwa Mahakamani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mashauri ya kesi za wakulima kulishiwa mazao yao zilizoripotiwa Vituo vya Polisi katika Wilaya ya Mvomero kuanzia Januari, 2022 hadi Machi, 2023, ni jumla ya Mashauri 343. Kesi zilizofikishwa mahakamani ni
184. Kati ya hizo kesi 119 zimehukumiwa, kesi 65 zinaendelea kusikilizwa mahakamani na kesi 159 zipo kwenye hatua mbalimbali za uchunguzi na upelelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO K.n.y. MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza ujenzi wa Kituo cha Polisi Turiani kilichojengwa kwa nguvu za wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa kupitia michango mbalimbali ya wananchi inayofikia shilingi milioni 36, Kituo cha Polisi Turiani kimefikia hatua ya lenta. Katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imepanga kutumia fedha toka Mfuko wa Tuzo na Tozo ili kuendeleza ujenzi wa kituo hicho ambacho hadi kukamilika kitakuwa kimegharimu shilingi milioni 110, ahsante.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO K.n.y. MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Turiani hadi Mziha kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Turiani hadi Mziha, yenye urefu wa kilometa 35.5 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami imekamilika. Serikali imepanga kujenga ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu katika mwaka wa fedha 2023/2024. Ahsante.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha kusambaza umeme kwenye Kata za Kikeo, Kinda na MaskatI – Mvomero?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mvomero ina jumla ya vijiji 129 ambapo kati ya hivyo, vijiji 92 tayari vimeshapatiwa umeme. Vijiji 37 vilivyosalia ambavyo baadhi vinapatikana katika Kata ya Kikeko, Kinda na Maskati vitapatiwa umeme na mkandarasi ambaye yupo maeneo ya mradi anaendelea na kazi za ujenzi wa miundombinu. Mkandarasi huyu anatarajia kukamilisha kazi ifikapo mwezi Juni, 2024, ahsante.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Boma, Kijiji cha Doma, Wilayani Mvomero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu;-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Doma kipo Kata ya Doma, Kijiji cha Doma katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero. Ujenzi wa kituo hiki ulianza mwaka 2021/2022 kwa wananchi kuanza ujenzi wa jengo la huduma za wagonjwa wa nje (OPD) ambalo limefikia hatua ya kupandisha kuta.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero imetenga shilingi milioni 40 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo hilo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati kote nchini kikiwemo Kituo cha Afya cha Doma.
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -
Je, lini Serikali itamaliza ujenzi wa Mradi wa Umwagiliaji katika Kijiji cha Msufini Kata ya Hembeti Mvomero?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Umwagiliaji ya Msufini yenye jumla ya hekta 1,000 iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero inakabiliwa na changamoto ya banio kuachwa na mto ambao ndiyo chanzo chake kikuu cha maji sambamba na mchanga kujaa kwenye mto huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika Mradi wa Msufini ili kujua gharama halisi za utekelezaji wa mradi huu na miundombinu sahihi itakayohitajika ili kukabiliana na changamoto zilizopo sasa. Aidha, kukamilika kwa ujenzi wa skimu hii utanufaisha wakulima 320
MHE. JONAS V. ZEELAND aliuliza: -
Je, lini Serikali itamaliza ujenzi wa Mradi wa Umwagiliaji katika Kijiji cha Msufini Kata ya Hembeti Mvomero?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Umwagiliaji ya Msufini yenye jumla ya hekta 1,000 iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero inakabiliwa na changamoto ya banio kuachwa na mto ambao ndiyo chanzo chake kikuu cha maji sambamba na mchanga kujaa kwenye mto huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika Mradi wa Msufini ili kujua gharama halisi za utekelezaji wa mradi huu na miundombinu sahihi itakayohitajika ili kukabiliana na changamoto zilizopo sasa. Aidha, kukamilika kwa ujenzi wa skimu hii utanufaisha wakulima 320