Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jonas Van Zeeland (10 total)

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa tuna vijiji ambavyo vimepakana moja kwa moja na Hifadhi ya Mikumi. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuweka kila kijiji angalau kuwe na game ambaye ataweza kuzuia tembo mara tu anapotoka kwenye hifadhi na kutaka kuingia kwa wananchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, kwa kuwa tuna wananchi zaidi ya 28 wameshapoteza maisha kwa sababu ya tembo, lakini wananchi zaidi ya 2,000 mazao yao yameharibiwa na tembo.

Je, ni lini sasa Serikali itaenda angalau kuwafuta machozi na kuwafuta jasho kwa kupata uharibifu na tembo katika Wilaya yetu hii ya Mvomero? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Mvomero kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba kuwepo na askari maalum kwa ajili ya kuweka usalama wa wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi vikiwemo vijiji ambavyo amevielezea, nimuahidi tu Mbunge kwamba Serikali inatambua changamoto hii na ndio maana tumekuwa tukitoa ushirikiano wa karibu sana na wananchi kuhakikisha kwamba wananchi wanalindwa na mali zao pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba atuvumilie lakini tutaandaa eneo maalum kwa ajili ya kuweka askari game ambao watakuwa standby kwa ajili ya kufanya patrol katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tuna upungufu wa askari kwa maana ya kuweka kila Kijiji, nimuombe aendelee kutuvumilia, lakini tutahakikisha tunaimarisha eneo lile ili wanyama wakali na waharibifu wasiendelee kuvamia wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kifuta machozi nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili Tukufu nitazunguka kwenye maeneo yote ambayo hayajapata kifuta machozi. Nimuahidi kwamba nitalisimamia zoezi hili mimi mwenyewe kuhakikisha kwamba wananchi wanalipwa kwa wakati. Ahsante. (Makofi)
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nichukue nafasi hii niipongeze Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa changamoto ya barabara iliyopo Mzumbe kwenda Mgeta inafanana kabisa na changamoto ya barabara kutoka Turiani kwenda Mziha mpaka Handeni.

Je, ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami kutoka Turiani kwenda Mziha hadi Handeni?

Swali la pili, kwa kuwa tuna barabara ambayo ndiyo inasafirisha mazao ya wananchi wetu kutoka Kata ya Kibati, Pemba na Wilaya jirani ya Kilindi.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuiongezea bajeti hii barabara ili iweze kutengenezwa kwa kiwango cha kuridhisha na iweze kupitika nyakati zote, lakini pia na kujenga daraja ambalo ni muhimu sana linalounganisha Wilaya ya Kilindi na Wilaya ya Mvomero katika Kata ya Kibati na Kata ya Kinde? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE.ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee pongeze alizozitoa kwa Serikali kuendelea kufanya kazi katika barabara ambayo ameisema katika swali lake la msingi.

Mheshimiwa Spika, katika barabara aliyoisema ambayo inaanzia Magole – Turiani – Mziha, kipande cha Mziha - Handeni ambacho bado hakijajengwa barabara hii imetengewa bajeti katika mwaka huu wa fedha. Hivyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge awe na subira kadri fedha zitakapopatikana barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami ili kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Tanga - Turiani hadi Handeni.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara ya Kibiti ambayo inaenda Kilindi, Tuko kwenye kipindi cha bajeti, ameomba bajeti iongezwe ili tuweze kuijenga kwa kiwango kizuri zaidi. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ombi hilo tumelipokea na tutaangalia namna ya kulifanyia kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali la moja la nyongeza; kwanza nichukue nafasi hii nimshukuru sana kwa niaba ya Wananchi wa Jimbo la Mvomero, Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa kutupa fedha nje ya bajeti ya TARURA.

Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuiongezea TARURA bajeti ya matengenezo ya barabara, kwa kuwa barabara nyingi zilizoko vijijini ambako kule yanapotoka mazao ya wakulima wetu, barabara zile ni mbovu.

Je, Serikali ni lini itaongeza fedha za bajeti ya TARURA ili barabara hizi ziweze kutengenezwa vizuri na kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jonas Van Zeeland, Mbunge wa Jimbo la Mvomero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ofisi ya Rais – TAMISEMI, tunapokea pongezi kwa niaba ya Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini suala la pili la msingi ni kwamba nimhakikishie tu kwamba Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais wetu kipenzi, Mama yetu Samia Suluhu Hassan inazingatia jambo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amezungumza hapa la kuongeza bajeti kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, nimuondoe shaka tu kwamba fedha bahati nzuri iliyopo ipo na tutaendelea kuifanyia kazi na nyongeza yoyote tutaendelea kuileta kwa wananchi.
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Kwa kuwa Mvomero ni miongoni mwa Wiliya ambazo bado zina changamoto ya migogoro ya wakulima na wafugaji: Je, Serikali inamkakati gani wa kuendelea kuyafuta mashambapori yaliyopo Mvomero ili muweze kuwagawia wananchi na kupunguza tatizo hili la migogoro ya wakulima na wafugaji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Mvomero bado tuna migogoro ya ardhi pamoja na kwamba imepungua.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kuongozana nami baada ya Bunge hili kwenda kutatua migogoro hii Mvomero? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Zeeland Mbunge wa Mvomero, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na jambo la mashamba, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ilishakagua mashamba 75 na katika hayo, mashamba 15 yalishatolewa ilani ya kuendelea kufuatiliwa katika maana ya kufutwa au kuona utaratibu mwingine wowote, utakaofanyika. Katika hatua hizo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pale tutakapokuwa tumekamilisha taratibu nyingine zote tutamjulisha kwa niaba ya wananchi wake ili aweze kujua hatua Serikali ilizochukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kuongozana mimi naye kwenda Jimboni kwa ajili ya kutatua migogoro hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari baada ya hapa, kwa sababu ni njia ya kwenda Jimboni kwangu, nami nitasimama Mvomero pale tuweze kutengeneza mambo mazuri ili kuweka hali ya usalama na watu wetu wakae vizuri.
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa, hili zoezi ambalo linaendelea sasa hivi la kuweka mipaka ndiyo limeenda kuchochea kabisa mgogoro uliopo kati ya vijiji hivi 24 na Hifadhi ya Wamembiki. Na kwa kuwa Mheshimiwa Rais anazamira ya dhati kabisa kumaliza huu mgogoro uliopo pale. Je, Serikali haioni kuna haja ya kwenda kuhakiki upya hii mipaka kwa kufuata mipaka ile waliyokubaliana wananchi mwaka 97 kati ya wananchi na Hifadhi ya Wamembiki? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili Mheshimiwa Waziri kwa kuwa wananchi wanayozunguka Hifadhi ya Wamembiki wana changamoto nyingi sana. Uko tayari kuongozana nami baada ya Bunge hili la Bajeti kwenda kuzungumza na hawa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jonas Zeeland, Mbunge wa Mvomero kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mvomero kwa kukubali kuruhusu pori hili ambalo lilikuwa ni Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori (WMA) kuwa Pori la Akiba ambalo kwa kusema ukweli Serikali inawashukuru sana wananchi hawa. Kwa sababu umuhimu wa eneo hili kwanza ni mapito ya wananyama wengi wakiwemo wanyama wakali na ni ushoroba ambao unapita katika maeneo ya Hifadhi ya Selou, Mikumi, Tarangile na Saadan. Lakini pia katika maeneo haya kuna umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo nimhakikishie tu Mbunge kwamba wananchi hawakukosea kukubali kupandisha eneo hili kuwa Pori la Akiba. Sasa ile changamoto ambayo inaonekana kwamba tumeenda kuibua migogoro mipya niwahakikishie tu wananchi wa Mvomero kwamba tutaenda kuishughulikia na kwa kuwa wataalam wako uwandani basi tutahakikisha hii migogoro inakoma na wananchi waendelee kuishi maisha yao vizuri na wakati huo huo pori hili tunalihifadhi kwa faida ya wananchi wanayozunguka maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili niko tayari tu kuambatana na Mheshimiwa Mbunge pia kwenda kuwaona wananchi, kutatua na kuelezeana namna ya umuhimu wa kutunza maeneo haya kwa ajili ya vizazi vinavyokuja. (Makofi)
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa yapo malalamiko kwa baadhi ya askari wako kutotenda haki ikiwemo kuchukua rushwa na kuziharibu hizi kesi za migogoro ya wakulima na wafugaji, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuongozana nami baada ya Bunge hili la Bajeti kwenda kuwasikiliza wananchi wa Mvomero? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kutokana na jiografia yetu ya Mvomero, tuna uhaba mkubwa wa vituo vya polisi. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutuongezea Vituo vya Polisi lakini pia kuvimalizia Vituo vya Polisi vilivyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi kikiwemo Kituo cha Polisi Turiani na Kituo cha Polisi Mvomero? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwepo wa madai ya rushwa na kwamba Mheshimiwa amependekeza niende Mvomero pamoja naye kuwasilikiliza wananchi, hilo halina shida Mheshimiwa tutaongozana. Hata hivyo pale zinapokuwepo tuhuma za rushwa ushauri wangu wananchi waelekezwe kwenda kwenye vyombo vinavyosimamia sekta hiyo. Tunayo TAKUKURU kila Wilaya, kila Mkoa na Taifa, lakini kama inashindikana kuna Kamati ya Usalama inayoongozwa na Mkuu wa Mkuu wa Wilaya wanaweza wakapeleka manung’uniko huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wapo Wakuu wa Mapolisi hawa wadogo wanaokuwa kwenye site kama OCD wanaweza pia kuwasikiliza, lakini nipo tayari kuungana naye kwenda kuwasikiliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya swali la pili la kuongeza Vituo vya Polisi kwa sababu Wilaya ni pana, nitakapokwenda kwenye kikao hicho tutaweza kuviangalia vituo viwili vinavyoendelea kujengwa na kupata mapendekezo yako ni wapi kwingine wanapenda viongezwe ili viweze kuingizwa kwenye mipango yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa Mvomero ni miongoni mwa Wilaya ambazo ziko vijijini; na kwa kuwa, Kijiji cha Madizini, Lusanga, Manyinga, Turiani, Kilimanjaro na Kichangani, havikuwahi kupata hadhi ya kisheria kuwa miji midogo; Mheshimiwa Naibu Waziri, huoni sasa kuna haja ya kutoa maelekezo wananchi wa vijiji hivi walipie umeme kwa shilingi 27,000 badala ya kulipia umeme kwa shilingi 321,000? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Wananchi wa Tarafa ya Turiani wamekuwa wanapata adha kubwa sana ya kukatika kwa umeme: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, huoni sasa ni wakati muafaka kutenga bajeti ya kwenda kuboresha miundombinu hii inayotoka Morogoro kuelekea Turiani ya kupeleka umeme kwa sababu miundombinu hii ni ya muda mrefu na imechakaa kwa kiwango kikubwa sana? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jonas Zeeland, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Vijiji vya Madizini, Lusanga, Manyinga, Kilimanjaro, Kichangani na Turiani, vilitolewa tangazo, lakini havijaidhinishwa kama miji midogo. Kwa hiyo, niwaelekeze TANESCO Mkoa wa Morogoro kuendelea kuwa-charge wananchi 27,000 kwa maeneo haya yote ambayo hayajaidhinishwa kama miji kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la pili la line ya umeme inayotoka Turiani kwenda Kilosa na Gairo, mwaka huu wa fedha tumetenga bajeti ya matengenezo. Nikuahidi, kama matengenezo hayatakamilika, mwaka ujao wa fedha tutaendelea kutenga bajeti ili kuhakikisha tunaboresha miundombinu hii ili wananchi waendelee kupata umeme wa uhakika, ahsante. (Makofi)
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi hasa kwenye vituo vya afya na zahanati zilizopo pembezoni, je, lini Serikali itatuongeza watumishi ili kuweza kupunguza kero hii ya watumishi iliyopo sasa hivi katika vituo vyetu na zahanati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sera ya afya imeweka wazi kwamba kila kijiji lazima kiwe na zahanati na kila kata lazima kuwe na kituo cha afya. Mimi pamoja na wananchi wangu wa Mvomero tumeshajenga maboma zaidi ya kumi, je, lini Serikali itatupatia fedha kwa ajili ya kumalizia haya maboma ambayo tumejenga wenyewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa watumishi wa kada ya afya katika kuhakikisha huduma bora inawafikia wananchi katika vituo vya kutoa huduma ya afya msingi, tayari Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuajiri watumishi wa kada ya afya na katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali iliajiri watumishi wa kada ya afya 33, mwaka 2022/2023 Serikali iliajiri watumishi wa kada ya afya 36 na mwaka 2023/2024 Serikali imeajiri watumishi wa kada ya afya 48 katika Jimbo la Mvomero.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha inaajiri na kunakuwa na watumishi wa kada ya afya ili waweze kutoa huduma zilizo bora katika vituo vyetu vya kutolea afya msingi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili ambalo anaeleza kwamba ameweza kuwashirikisha wanchi wake katika kujenga maboma ya zahanati, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali inatambua jitihada kubwa ambayo imefanyika katika ujenzi wa maboma haya na tayari Serikali imefanya tathmini na kubaini kwamba kuna maboma ya zahanati 1,265 ambayo yatahitaji jumla ya shilingi bilioni 75.9 kuyakamilisha.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imeweka mikakati ya kutafuta na kupata fedha kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za wananchi. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali ipo kazini na itahakikisha inatafute fedha ili kujenga maboma hayo uliyoyataja ambayo yako katika jimbo lako.
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa tuna skimu za umwagiliaji ambazo ujenzi wake ulianza muda mrefu sana na skimu hizi hazifanyi kazi ikiwemo Skimu ya Lukenge ambayo ina wakulima zaidi ya 3,000 na Skimu ya Luhindo ina wakulima zaidi ya 2,400; tarehe 25 Machi, mlitangaza tender ya kumpata mzabuni wa kununua pampu mbili kwa ajili ya kwenda kufunga kwenye hizi skimu. Je, ni lini Serikali itakamilisha kazi ya kutafuta hizi pampu na kwenda kufunga ili skimu hizi ziweze kufanya kazi na kuwasaidia wakulima wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kata ya Mlali, Kijiji cha Mlali tuna skimu ambayo inajiendesha kienyeji, ina wakulima zaidi ya 400 na ni skimu ambayo ina hekta zaidi ya 500. Je, Serikali haioni sasa ni wakati mwafaka wa kuwatuma wataalamu wa umwagiliaji kwenda kufanya tathmini ili skimu hii iweze kupanda hadhi na iweze kupangiwa bajeti ili kuiboresha hii skimu.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba katika Skimu za Lukenge na Ludigo ambapo tuliweka pampu katika tenda na zimeshafika mkoani, ninachomwagiza tu RM wa Mkoa wa Morogoro ni kuzipeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ambayo ilichelewesha ni hizi mvua zilizokuwa zimezidi sana, ndiyo maana walishindwa kupeleka, kwa sababu unaweza kupeleka halafu vikaharibika tena. Kwa hiyo, kwa sababu mvua zinaendelea kupungua, maana yake tutaendelea kuzikamilisha ili wananchi waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Skimu ya Mlali, tutawatuma wataalamu ili waende pale wakafanye tathmini na upembuzi yakinifu ili watuletee gharama halisi na kuijenga kisasa ili mradi uweze kutumika kwa wananchi wote, ahsante. (Makofi)
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza.

Katika Kata ya Mkindo tuna mradi wa umwagiliaji wenye thamani ya shilingi bilioni 5.6, mkandarasi toka amepewa kazi mwaka juzi mpaka sasa hivi hajafika hata 50%. Je, lini atakamilisha ili mradi huu uweze kuwasaidia wakulima wetu wa Mkindo? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mkandarasi amekuwa akisuasua na amekuwa akitafuta sababu za kuhalalisha kuchelewesha utekelezaji wa mradi. Nataka tu nimhakikishie kuwa Wizara tumekuwa very close na yeye na si muda mrefu tuta-unlock matatizo yaliyopo kati ya sisi na yeye na ikishindikana tutatafuta njia sahihi ya kuachana ili hiyo ndoa ife, tutafute mkandarasi mwingine.