Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Issa Ally Mchungahela (28 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru wewe; lakini pia niishukuru familia yangu; tatu nishukuru wananchi wa Jimbo langu la Lulindi walioniamini; nne nishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kuniamini kuwa naweza kufanya hizi kazi kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nataka nizungumzie suala la performance; nataka nijaribu kuweka wazi katika jambo hili. Wakati unapotaka kuchunguza performance ya mtu au kitu, cha msingi sana kinachohitajika kutumika pale sio percentage term, unatakiwa utumie an absolute term, maana yangu ni nini? Ni kwamba ukichukua bilioni moja ukazidisha kwa asilimia 10 unapata milioni 100, lakini ukichukua milioni 100 ukazidisha kwa asilimia 27 au asilimia 30 unapata milioni 30. Kwa hiyo, ukisema kwamba eti kwa sababu umetumia percentage kubwa wewe ume- perform, huo ni upotoshaji mkubwa, kwa hiyo nataka nieleweke hapo kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende katika utendaji wa Serikali. Hakuna hata mtu mmoja ambaye anasema kwa dhati kabisa kwamba, eti Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hakufanya vizuri kwa dhati kutoka rohoni kwake, atakuwa anatania tu. Kiuhalisia yaliyofanywa ni mengi sana, hatuwezi kuyamaliza hata tukisimulia wiki nzima maajabu hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kwamba suala la maendeleo ni mtambuka. Tunahitaji kuhusisha vitu vingi na sekta mbalimbali kwa ajili ya kutengeneza hayo maendeleo. Barabara za Dar-es-Salaam za mwendokasi, ni jambo zuri sana, lakini nashauri barabara hizi zizingatie pia na ukuaji wa miji ile. Nashauri kwamba barabara hizi ikiwezekana zifike hata Mkuranga kwa ajili ya ku-accommodate watu wanaoishi maeneo kama ya Mbagala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mradi wa bandari Mtwara umetumia pesa nyingi sana, takribani shilingi bilioni
157. Naomba mradi huu uunganishwe haraka sana na reli ya Standard Gauge ambayo itafika kwenye miradi mikakati ya Mchuchuma na Liganga. Tusiendelee tu kuongea mdomoni, tufanye kwa vitendo kama kweli tunataka maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine mradi huu pia uunganishwe na barabara zote za kimkakati zikiwepo barabara zile za ulinzi. Kwa mfano, barabara inayotoka Mtwara – Mtawanya - Mpilipili – Chikoropola - Nanyumbu. Barabara hii nafikiri ni muhimu sana kwa ku-boost maendeleo ya watu wa Kusini na viwanda vya Kusini, hasa kiwanda cha korosho ambacho nakitegemea mimi kama mmoja wa wahamasishaji kipatikane kule lakini kiwe ni kiwanda kikubwa kabisa cha kushawishi watu wengi sana kuuza pale, kusudi tuweze kupata bei nzuri. Hali ilivyo sasa hivi hatuwezi kupata bei nzuri kwa sababu tunauza raw material. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda EPZ iwe ndio msingi wa maendeleo kwa sababu ndiyo inaweza ikasababisha watu wengine wakawekeza kikamilifu. (Makofi)

(Hapa Kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mengi, lakini niseme naunga mkono hoja kwa sababu yaliyo ndani ya Mpango ni mazuri. Nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunilinda na kunipa ari ya kuifanya kazi hii muhimu kwa ustawi wa nchi, pia nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu unajikita katika kusisitiza utekelezaji wa yale ambayo Wizara imejipangia. Lakini pia kuiomba kutoa kipaumbele kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa wa maji. Mkoa wa Mtwara ni mfano wa maeneo yenye uhitaji mkubwa wa maji, mwaka jana Mheshimiwa Waziri alitembelea na kujionea yeye mwenyewe ambapo maeneo yote bei ya dumu la lita ishirini ilifika shilingi 2,500. Hali hii inajitokeza kila mwaka wakati wa kiangazi.

Naishauri Wizara kwamba Jimbo la Lulindi lina chanzo cha uhakika cha maji cha Mto Ruvuma, hivyo Mradi wa Mbangara - Mchoti naomba uwekewe pesa ya kutosha kwa sasa umepewa shilingi bilioni 1.3 pekee licha ya kuwa ni mradi unaoweza kutatua changamoto ya maji kwa karibu ya nusu ya jimbo; Kata za Lupaso, Lipumburu, Sindano, Mchauru, Mpeta na Chiungutwa na maeneo hayo yako ndani ya kilometa 50 kutoka kwenye chanzo hivyo kuwa ni mradi mkubwa wenye tija unaoweza kutekelezwa kwa gharama ndogo sana.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru lakini nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa uhai. Pia, niishukuru familia yangu kwa kunivumilia kuwa peke yao na mimi nikichapika na kazi huku za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote humu ndani ni viongozi. Familia zinatutegemea, taifa linatutegemea lakini vizazi vijavyo vinatutegemea sana. Kwa kadri tutakavyofanya vizuri sasa hivi, ndivyo tutakavyoweka mazingira mazuri ya vizazi vinavyokuja. Inashangaza katika level hii ya uongozi, sisi kwa maana ya Wabunge kufikiria katika level ya kifamilia kwa kweli tutakuwa hatuitendei haki nchi hii. Tunatakiwa kufikiria katika level ya kitaifa na kimataifa kwa ajili ya kuiwezesha nchi hii kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia na mimi hili jambo lilozungumziwa na wabunge wengi hapa la uuzwaji wa Tanga Cement. Kwa sababu gani? Lina masilahi ya nchi. Tunatamani kabisa kwamba Wabunge wote tukae hapa tukiwa na mtizamo huo kwamba hili jambo tukiliendea Kimasihala tutapata doa kubwa sana kwa kizazi kinachokuja kwa kuliingiza taifa hili katika janga. Tunayo kila sababu ya kufanya analysis ya kutosha kabisa na kufanya maamuzi ya kufanya jambo hili lakini pia Sheria zinatakiwa zifuatwe lakini pia wataalam waachwe huru wafanye kazi zao kitaalamu ili kusudi tuweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo dhana miongoni mwetu kusema kwamba linalofanyika sasa hivi la kuuzwa kwa Tanga cement kwamba ni jambo baya. Hata hivyo, nataka nikwambie kwamba ubaya au uzuri wa jambo hili tunaweza tukauangalia au tukaliona katika muktadha wa misukumo isiyopungua minne. Jambo hili liko katika misukumo minne kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, msukumo wa kwanza, nii msukumo wa muuzaji. Muuzaji amekuwa na changamoto ya uendeshaji wa Kampuni hii kwa takribani miaka minne au mitano tangu Mwaka 2016. Hivi sasa amekuwa akipata hasara hali ambayo iliyofikia mpaka sasa hivi tunavyokwambieni ni takribani miezi minne watu hawajalipwa mishahara yao. Jambo hili kwa namna yoyote ile hakuna mfanyabiashara ambae anaweza kulivumilia. Kwa sababu athari zake ni kubwa. Athari zake ni kwamba: -

(i) Serikali inakosa kupata kodi yake kwa maana ya corporate tax;

(ii) Kuna watu wamewekeza pale ambao walikuwa na matumaini ya kupata faida kwa maana ya dividends, hawapati kampuni inashindwa kuwalipa.

(iii) Pia huyu anahusiana na watu wengine kwa maana wanunuzi kwake lakini kwa anaowauzia (suppliers na customers).

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hali kama hiyo lazima kuna mazingira ambayo yanapelekea mahusiano yale yakawa sio mazuri. Tunasema kuna jeopardize uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kuna msukumo mwingine, huu ni msukumo wa mnunuzi. Kumekuwa na ongezeko kubwa sana la kasi sana la bidhaa hii ya cement. Tanzania imezalisha kiasi kikubwa sana cha cement mpaka kufikia mwaka 2022, kulikuwa na uzalishaji wa takribani tani zipatazo milioni 7.5. Pia, kumetokea ongezeko la soko la nje ambalo Tanzania kupitia viwanda vyake hivi vimelipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na ongezeko kubwa kiasi cha kwamba mpaka kufikia mwaka 2022, Tanzania iliweza kuuza nje kiasi cha dola milioni 147.6. Hata hivyo, pamoja kuuza nje hivyo, pia tuliweza kununua kutoka nchi za nje cement hiyo hiyo kwa thamani ya dola milioni 137.2. Sasa ukiangalia hapo kwa mtazamo huo unaweza ukakuta kabisa kwa mfanyabiashara yeyote yule mwenye jicho hawezi kuiachia hiyo fursa. Huo ni msukumo ambao mfanyabiashara unamsukuma aamue kuinunua hiyo kampuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika kuna msukumo wa Serikali. Serikali inatarajia kupata pesa kwa mtindo wa kodi kama nilivyowahi kusema hapo. Serikali inatagemea sana kuimarika kwa bidhaa hii ya Cement kwa ajili ya kuweza kukidhi haja ya mahitaji ya miradi yake ya kimkakati kama vile Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere lakini na mabwawa mengine ya umwagiliaji, Mradi wa Fly over, Mradi wa Reli na miradi mingine ambayo inatarajia kabisa kwamba kama atanunua kupitia soko hili la ndani kwa vyovyote vile watakuwa wamenunua kwa bei ya chini kabisa na hivyo kufanya miradi hii kuwa viable na kuleta tija mwishoni mwa safari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtazamo mwingine tena, huu ni mtazamo wa walaji. Walaji wanategemea kabisa kwamba bidhaa hii iwe ni ya bei ya chini lakini iwe ni bidhaa ya uhakika, kusiwe na bei za kubadilika badilika. Katika mazingira hayo kama nilivyojaribu kusema huko mwanzo unaona kabisa kwamba mazingira haya yote unapelekea uuzwaji wa Tanga cement kuwa hakuna njia lazima Tanga Cement iuzwe. Hii ina- justify kwamba Tanga cement iko katika mazingira ya kwamba lazima iuzwe kwa ajili ya masilahi mapana ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kinachotokea sasa hivi kumekuwa na madai ya hapa na pale kama nilivyosema watu wamekuwa wakidai kwamba jambo hili si zuri, ni masuala ya kufirika tu. Unavyozungumzia cartel kwamba Twiga Cement Ikinunua Tanga cement itasababisha cartel hilo ni jambo la kufikirika. Kwa sababu hakuna mazingira yoyote yale ya kibiashara kwamba yanaonesha cartel inaweza ikajitokeza. Kwa sababu gani? Kwa sababu cartel inakuja baada ya kuwa na stiff competition yaani ushindani uliokuwa mkubwa sana miongoni mwa makampuni yaliyoko kwenye participation ya biashara hiyo. Kiasi cha kutishiwa kuona kwamba kuendelea kuvutana inasababisha wao kuwa na cost ya production kuwa kubwa. Sasa kwa namna moja wanalazimika kwamba basi wapange bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira hayo hayapo hapa kwetu kwa sababu gani? Hapa kwetu sio tu bidhaa ya cement lakini bidhaa yoyote ile hakuna bidhaa ambayo ina meet competitive market. Masoko yetu yaliyoko hapa hapa nchini yana viashiria tu vya kuonesha kwamba kuna competition lakini is not competitive market na hivyo suala zima la kusema kwamba kuna cartel hili ni suala la kufikirika na tusiingie katika mtego huu. Tuiache Twiga cement ainunue Tanga Cement kwa sababu kutakuwa na tija kubwa, production itakuwa kubwa lakini pia atakuwa na ushindani na makampuni mengine ya nje.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA:…kutakuwa na uwezo wa kuwa na creativity katika kampuni lakini pia …

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mchungahela, kiti kikizungumza inabidi usubiri. Naomba upokee taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Timotheo Mnzava.

TAARIFA

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, sidhani kama kuna mtu ana shida ya nani kumnunua nani. Nataka nimpe tu taarifa kwamba kwenye kuangalia hili hatuangalii stiff competition peke yake, namna ya ku-measure iko nyingi. Hali ya soko, share markets, capacity ya viwanda kuzalisha na sababu nyingine. Ukisoma Major analysis and report ya FCC ukurasa wa 34, wenyewe wanakili kwamba hawa waki-major wakafika asilimia 42 na point ya share ya market, hiyo ndio changamoto iliyopo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, unapokea taarifa?

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa kwa muktadha kwamba market share sio inayosababisha cartel kwa kadili nilivyojaribu kuzungumza hapa. Kwa sababu sikuwa na muda tu, kama ningekuwa na muda ningeweza kumpa fact zote zinazosababisha cartel na miongoni mwake ni competition ya market na sio kuwa na wingi wa share. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano sasa hivi Dangote ana share takribani kwa mfano 20 percent lakini anaweza aka-inject capital kubwa pale kiasi cha yeye akawa na uwezo sasa wa kuwa na share asilimia 60 utamfukuza sokoni? (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, na muda wako umekwisha, hitimisha hoja yako. (Makofi)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nashukuru kwamba ninachotaka kuhitimisha ni kwamba tuynatakiwa tuwe makini kwamba Serikali yenyewe iwe makini katika utendaji wake kwa sababu shida iliyoko hapa siyo wafanyabiashara walioko sokoni shida inaweza ikapatikana kwa watendaji wa Serikali katika kutimiza majukumu yake; na kutokutimiza majukumu kwa Serikali isitupiwe kwamba hawa wafanyabiashara wanafanya kosa la jinai ambalo sisi nafikiri tunaweza pia tukaliona kwamba siyo kosa isipokuwa huu ni udhaifu wa upande mwingine. Mimi ninaomba tuwe serious biashara tunahitaji biashara kubwa wafanyabiashara wakubwa wakubwa ambao wataiondoa nchi hii hapa tulipo na kuwa katika viwango vya kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na afya kuweza kutekeleza majukumu yangu ya kila siku, pili nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii kulihutubia Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru mzalendo Namba Moja Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa uzalendo wake aliouonyesha ni uzalendo mkubwa sana, siku tulipoingia mkataba wa LNG ule hodhi, Mheshimiwa Rais alifanya kitu kikubwa sana ambacho aliitangazia Dunia kwamba yeye anafahamu sana diplomasia ya uchumi. Mheshimiwa Rais alisimama na kuwaambia wawekezaji kwamba wanapokuja Tanzania wahakikishe kwamba wanayo dhamira ya dhati ya kufanya biashara nasi na kwamba mkataba ule usije ukawa ni shere ya kutufanya sisi tuendelee na jitihada zetu zakutafuta mtu wa kutusaidia kushughulika na biashara ile. Ikawa wao wanaishikilia kwa maana waendelee kufanya biashara ile kwenye maeneo mengine walikowekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kauli hii imetoka mdomoni mwa Mheshimiwa Rais ni kauli nzito sana ile ni message ambayo inatakiwa watu wote tuzingatie kwa sababu ni message inayoonyesha uzalendo wa hali ya juu na kuonesha ni kwa jinsi gani yuko serious hasa katika suala hili la uwekezaji. Message kwa mtindo upi? Kwamba Tanzania kama nchi ni nchi tajiri sana na ina madini mengi lakini ina vitu vingi sana vitakavyoweza kutusaidia tukiamua kuvitendea kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lmessage ile ilikuja kwa Watendaji pia kuwa wakati wanatengeneza mikataba wawe makini sana kwa sababu failure inaleta hasara kubwa sana katika nchi, lakini message kwa dunia na wawekezaji kwamba wanapokuja Tanzania wajue kwamba biashara ya uwekezaji Tanzania ni very serious siyo kitu cha mchezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kauli ile ilinitia nguvu kama nilivyosema kuhutubia Taifa, dhana hii ya kuhutubia Taifa kuna baadhi hawaielewi lakini siwezi kuwalaumu kwa sababu ni dhana yenye maana pana sana pia ni mtambuka. Kwa kifupi tu ni kwamba ni dhana inayoendana na falsafa ya kuchunga fedha, falsafa ambayo inafanya kazi vizuri sana katika mazingira ya jamii yenye itikadi ya kizalendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema ni itikadi maana yake siyo wimbo wa kizalendo kwa maana itikadi ni dini na dini ni kuamini na kuabudu. Kwa hiyo, Watanzania lazima tuamini na kuabudu kwenye itikadi hii, tukifanya hivyo itatusaidia sisi kufanya yale tunayokusudia kuyafanya kwa maslahi ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tumepungukiwa sana na hii dhana ya uzalendo, tumekuwa hatuwezi kuweka maslahi ya Taifa mbele na hii imetokana na jinsi tulivyopita katika mapito mbalimbali kuelekea kutengeneza uchumi wa nchi hii, mapito ambayo yameleta athari mbalimbali ambazo hasi pamoja na athari chanya, sitazungumzia athari chanya kwa sababu zimegusa watu wachache lakini athari hasi zimegusa watu wengi kwa maana jamii nzima. Athari hasi zimetengeneza mitazamo hasi pia kwa jinsi tunavyoangalia mambo mbalimbali ya muhimu sana yanayohusu maendeleo ya nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tukiangalia dhana ya elimu, jamii ya nchi hii kutokana na athari zilizojitokeza inaiangalia elimu kuwa ni chombo cha kutengeneza fursa ya ajira ambayo itatengeneza fedha, kwamba mtu anayetafuta ajira ni lazima aje kuajiriwa baadaye lakini ajira hiyo impe fedha. Sasa mtizamo huu ukiuangalia umeleta msukumo ambao unaleta changamoto sana katika utendaji wa masuala mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, unakuta kwamba kila mtu anayetaka kusoma, anataka kusoma masomo ambayo anasema ni yenye mlengo wa deal, masomo yatakayo mpa ulaji na hata wazazi wamekuwa wakiwasukuma watoto wao kusomea masomo ya namna hiyo na kuacha masomo mengine, pia msukumo wa kikazi uko katika kutafuta fedha kwa maana mtu anahangaika kutafuta kwa njia yoyote ile, bila kujali hata kama fedha hiyo inapatikana kwa taratibu unaostahili au lah. Kwa hiyo, kumekuja na mtazamo kuwa mwajiriwa akimuibia mwajiri wake hata kama wizi huo utasababisha kufilisi kampuni au kama utasababisha kuyumbisha uchumi wa nchi, mtu huyo anaonekana kuwa ni mtu mjanja. Sasa suala hili ni baya sana ndugu zangu watanzania, tunatakiwa kwa makusudi kabisa tuwe na jitihada za kuepukana nalo jambo hili, tufanye jitihada kubwa sana kuwasomesha watoto wetu kuwaelimisha lakini kuwaelimisha kizazi chetu na jamii nyingine kwamba tunatakiwa tuifikirie nchi kwamba ndiyo pekee yenye maslahi, wewe usifikirie kwamba nchi itakufanyia nini lakini fikiria kwamba wewe utaifanyia nini nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwamba kumekuwa na mtizamo wa masuala tofauti tofauti, pia kumekuwa na changamoto sana katika usimamizi wa bajeti kwa mfano, Serikali kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi imelazimika kwa namna moja ama au nyingine kutekeleza miradi mkakati. Miradi hii kama tutaangalia mapato yetu ya ndani hatuwezi kuitekeleza au itachukua muda mrefu sana kuitekeleza, lakini kutokana na hiyo Serikali inalazimika kwenda kukopa. Mheshimiwa Rais kwa mfano, ameenda nje akajitahidi kukopa zile fedha zikija hapa ni fedha zinatakiwa ziende moja kwa moja katika miradi mkakati, kwa sababu kama hazitaenda huko zitatupa madeni makubwa ambayo itakuwa ni mzigo mkubwa kwa Serikali, nataka jambo hili lieleweke tukiangalia kwa mfano kwenye bajeti tunaweza tukalielewa jambo hili vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya Mwaka 2019 kwenda 2020 tulikuwa na bajeti ya kulipa Deni la Taifa takribani Trilioni 9.3 lakini bajeti ya Mwaka 2020 kwenda 2021tulikuwa na amount ya kulipa Deni la Taifa trilioni 10.4 bajeti ya mwaka 2021/2022 tulikuwa na bajeti ya kulipa Deni la Taifa shilingi trilioni 10.6 lakini kwenye bajeti ya mwaka huu kuna mapendekezo estimation ya kulipa Deni la Taifa takribani trilioni 9.093 ukijumlisha hii yote kwa miaka minne utakuta ni zaidi ya trilioni 39 fedha ambayo ni nyingi sana yaani ni bajeti nzima ya mwaka mzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unaweza ukaona kwa jinsi gani hapa fedha nyingi sana kama hii ingeweza ikatumika katika masuala mengine kwa mfano, tungekuwa tunatumia ile trilioni kumi ya kila mwaka kuchanganya na fedha nyingine ya maendeleo utaweza ukaona kwa jinsi gani fedha hii ingeleta tija kubwa sana, lakini kwa sasa hivi fedha hiyo tunalipa deni, hapo ndipo linapokuja umuhimu wa sisi kusimamia hii fedha ya madeni tunayoikopa kutoka nje ili kusudi ifanye kazi inayostahili pia kusimamia ni pamoja na kuhakikisha tunapunguza changamoto zozote zile za kuongeza riba katika madeni hayo, kama hatuwezi kufanya hivyo maana yake tunaingizia hasara nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye usimamizi, kuna suala la kwamba, Wabunge wanatakiwa kusimamia. Tukiangalia hapo kuna changamoto, changamoto ipo kwamba je, Mbunge anasimamiaje? Mipaka yake ya kusimamia ni nini, nini anatakiwa asimamie, nini hatakiwi kusimamia. Akienda kuangalia akakuta kuna changamoto anaziripoti kwa nani?

Je, Mbunge kama kazi hii ya kusimamia anatakiwa kuisimamia, anawezeshwa, ana uwezo wa ku-move kutoka eneo moja kwenda lingine kusudi kuangalia miradi hii jinsi inavyofanyika?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia pia usimamizi unapwaya kwa wenzetu Madiwani ambao ni muhimu sana. Tukiangalia Madiwani wao ndiyo wana nafasi kubwa ya kusimamia kwa sababu miradi hii inafanyika katika maeneo yao. Lakini Diwani ndugu zangu yuko hohehahe. Tukiangalia kimshahara, Diwani ni kama hana mshahara. Hata posho anayopewa Diwani haitoshi kabisa, kiasi kwamba suala la usimamizi kwake yeye linakuwa ni suala nyeti kabisa kwa sababu kuna wakati anaweza akatishiwa hata na Mtendaji kwa sababu tu hana kipato kizuri kiasi cha kumfanya Mtendaji amshawishi Diwani kufanya kitendo kibaya cha kuweza kubadili fedha ambayo inatakiwa kusimamiwa ikatumika vinginevyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye hili, ninalo la kuishauri Serikali. Tujaribu kufumba macho tuweze kumwezesha Diwani, kwa sababu Madiwani katika halmashauri 185 za nchi hii, kuna Madiwani 5,774 kiasi kwamba tukiamua tukatoa shilingi milioni moja kama mshahara wa Diwani kwa mwezi, tuna uwezo wa kumpa... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante, kengele ya pili hiyo. Mheshimiwa Kengele ya pili hiyo, ahsante.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sekunde mbili, tatu nimalizie, kwamba tukiweza kumlipa Milioni moja kila Diwani, tuna uwezo wa kulipa…

NAIBU SPIKA: Ahsante, mengine utaandika. Unaruhusiwa kuandika. (Makofi)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Pia nitangulize pongezi zangu kwa watu wote waliopa bahati ya kuchaguliwa kuwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwenye nafasi zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nampongeza pia Mheshimiwa Rais, mama yetu kwa kuonyesha njia ya jinsi tutakavyoelekea Tanzania kwa kipindi hiki japo tulikuwa tunashaka kidogo tukifikiria kwamba itakuwaje baada ya kupata msiba mkubwa tulioupata angalau sasa hivi tunaona kidogo kuna hali tunaweza kuelekea sehemu. Nashukuru kwa hilo na tumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba ametuona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, kwanza pia niwapongeze wananchi wangu wa Jimbo la Lulindi kwa kunichagua nawahakikishia kwamba sitawaangusha hata mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kuangalia jinsi mwenendo mzima wa huu Mpango ulivyokwenda ni mpango mzuri sana ambao kwa muda mrefu sana tulikuwa tukiusubiri mpango wa namna hii. Kwa kweli hakuna shaka juu ya mpango huu, lakini nafikiri kwa namna moja au nyingine najielekeza katika kuchangia baadhi ya mambo katika mpango huu, hususani katika fursa ambazo kwa namna moja au nyingine tunaweza tukazitumia sisi kama Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa kusini kwa mfano, tuna fursa kubwa sana eneo lote la Mkoa wa Mtwara ni eneo la fursa ambalo tunaweza tukalitumia vizuri sana kujielekeza na kujikita kwenye biashara na nchi takribani tatu au nne. Hiyo ni advantage kubwa sana na mfano, ukiangalia kusini kule Mtwara tuna ukaribu kabisa moja kwa moja na Nchi ya South Afrika na Nchi ya Mozambique lakini pia tuna ukaribu na nchi ya Comoro, hali kadhalika tuna ukaribu na nchi ya Madagascar. Hizi nchi kwa namna moja au nyingine kama tutajikita kufanya nazo biashara, kwa sababu kwanza zenyewe zina mapungufu mengi sana ambayo wanayategema sana yanaweza yakasaidiwa na sisi uimara wetu katika kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tunayo bandari kubwa ambayo haina shida, mpaka sasa imetengenezwa kwa kiasi kikubwa kabisa lakini pale ni lango pia ambalo la kuweza kutokea nchi nyingi kwenye bandari hiyo. Kwa sababu kama unavyoangalia ile Bahari ya Hindi imeunganika moja kwa moja katika hizi nchi, lakini sisi tunazalisha vitu vingi hususani mazao ya kilimo ambayo kwa namna moja au nyingine wenzetu kule hawawezi kuzalisha kwa mfano Nchi ya Comoro. Pia tunazalisha mifugo ambayo Nchi ya Comoro hawawezi kuzalisha, sisi tunaweza kuitumia nafasi hii kwa kuwauzia kwa kiwango kikubwa kabisa tukapata pesa za kutosha. (Makofi.)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyosema Bandari ya Mtwara, moja kwa moja kwa makusudio yetu yale ya kuunganisha reli ya standard gauge kwenda Mbamba Bay lakini kupitia Mchuchuma na Liganga moja kwa moja, hapo tunaona kwa jinsi gani hizi products zinazozalishwa kwenye Liganga na Mchuchuma kwa mfano chuma na makaa ya mawe, tuna uwezo wa kuwauzia moja kwa moja nchi hizi ambazo nimeziataja hapa kirahisi kabisa. Kwa namna moja au nyingine pia bandari hii inaweza ikawa ni kiunganishi cha nchi nyingi sana hasa hasa zilizounganikaunganika kwa upande kwa kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naliona kwa sababu Mkoa wa Mtwara unazalisha zao kubwa la korosho ambalo kwa namna moja au nyingine siku zinavyokwenda limekuwa zao linalopendwa kwa matumizi na watu wengi sana inakuwa ni rahisi kwa namna moja au nyingine kuziuza korosho zetu katika nchi hizo ambazo nimezitaja. Kwa hiyo tunaweza kuona jinsi gani Mkoa wa Mtwara unaweza ukawa umetumika kwa namna moja au nyingine ikawa kama mkoa mkakati wakusambaza uchumi wetu, lakini na kuhakikisha kwamba uchumi wetu unakua kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Spika, naona kwamba, bado hatujachelewa, lakini kuna gesi ambayo Mtwara imekuwa ni kitovu kikubwa sana cha gesi ambayo mpaka sasa hivi haijatumika vya kutosha. Naomba Serikali ifanye jitihada ya kutosha kabisa kuhakikisha gesi Mtwara inatumika. Sijajua tatizo ni nini mpaka sasa hivi ambalo linatukwamisha. Ningeomba Wizara husika ifanye mkakati wa kutosha kabisa kuhakikisha kuona gesi hii inatumika kama vile tumetegemea itumike.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo la uzalishaji katika masuala ya kilimo, Mkoa wa Mtwara hauko nyuma pia katika uzalishaji wa mazao mengine ukiachia korosho ambao ni zao maarufu. Mkoa wa Mtwara ni maarufu pia katika kuzalisha ufuta ambao ni kigezo kikubwa kabisa cha kupunguza hili gap ya matatizo ya mafuta ya kupikia kama tutaweka nguvu za kutosha kidogo kwenye ufuta, lakini korosho na mazao mengine bila shaka Mtwara itakuwa ni sehemu mojawapo inatusaidia sana kupunguza shida hasa hasa katika suala zima la kupunguza matatizo ya mafuta yanayohitajika katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niweze kuzungumzia suala la miche ya korosho ambayo ilikuwa imelimwa na wajasiriamali wadogo wadogo kwa minajili ya kwamba ilikuwa ikatumike kwenda kuwekezwa katika maeneo mengine ambayo hayalimi hiyo miche. Wawekezaji wale mpaka sasa hivi wamekuwa wakilalamika kwamba hawajalipwa stahiki zao baada ya kuwa wametumia nguvu nyingi sana, lakini pia na kutumia pesa zao katika kuwekeza hiyo miche ambayo namna moja au nyingine ilizalishwa ikaiuzia Serikali kupitia Mamlaka ya Korosho lakini mpaka sasa hivi wananchi wale wanalalamika hawajalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kwa jicho la huruma kabisa iwasaidie hawa wawekezaji wadogowadogo kwa sababu wao ni sehemu kubwa kabisa ya maendeleo ya nchi hii kama vile ilivyokuwa wawekezaji wa maeneo mengine, hususani ukizingatia kwamba hawa ni wakulima ambao hutegemea kidogo sana wanachokuwa nacho waweze kukiwekeza sehemu nyingine wajipatie mkate wa siku zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna moja ama nyingine hapo ni kama nimchomekea tu maana yake nilijua sitapata nafasi ya kulizungumza hili, nimejaribu kulizungumza kwa mara mbili, mara ya tatu, sijalipatia jibu, naomba japo sio mahali pake hapa, lakini kwa taadhima Waziri husika atuonee huruma watu wa Mtwara, aweze kuwapa wale watu waliowekeza katika ile miche ya korosho wanachostahili angalau waweze kusukuma mbele kidogo maisha yao, japo najua sio mahali pake hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, najaribu kujielekeza pia katika suala zima la gesi kwa ujumla. Gesi kwa namna moja au nyingine imekuwa ni tegemeo kubwa katika eneo la Mtwara, lakini hata kwa Tanzania kwa ujumla, nafikiri itakuwa sehemu ya mojawapo itakayotusaidia kutatua baadhi ya changamoto ndogondogo ambazo kwa namna moja au nyingine tungeweza kushindwa kuzitatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo, naomba nishukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia. Ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema; lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Taarifa ya Kamati ya LAAC na taarifa zingine.

Mheshimiwa Spika, sitakuwa na shukrani kama sitaanza kwa kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu shupavu jemedari Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Kipekee nimpongeze yeye mwenyewe binafsi. Hii ni kwa sababu ya utashi wake na dhamira yake aliyokuwa nayo katika kutekeleza au kutatua changamoto za wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais Samia Hassan anafanya kazi kubwa sana, kazi ambayo hakuna mwananchi wa nchi hii hazioni. Amekuwa na dhamira njema kabisa ya kuhakikisha kwamba kila palipokuwa na changamoto, changamoto hiyo inatatuliwa. Pamoja na dhamira hii njema kumekuwa na changamoto kadhaa ambazo zinazoweza kupelekea matarajio haya ya Mheshimiwa Spika yasifikiwe.

Mheshimiwa Spika, kumeripotiwa makosa, changamoto mbalimbali au dosari mbalimbali na Mkaguzi Mkuu wa Serikali katika ripoti zake. Dosari hizi zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara, mwaka hadi mwaka hali ambayo imesababisha baadhi yetu kufikiri kwamba ripoti hizi hazina majibu au hazina suluhisho, jambo ambalo sio kweli.

Mheshimiwa Spika, changamoto hizi ukiziangalia kwa umakini kabisa unaweza ukakuta kwamba zinatatulika. Nataka niziangalie changamoto chache tu kama mfano.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa changamoto zilizokuwa zikiripotiwa mara kwa mara na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ni kama ifuatavyo: -

Kumekuwa na matumizi mabaya kwenye akaunti ya amana. Hapa pamekuwa na kizungumkuti kwa sababu akaunti ya amana si akaunti ya halmashauri. Akaunti hii ni imewekwa kwa ajili ya kutatua migogoro ya kimkataba wakati panapotokea changamoto; kwa hiyo pesa zinazowekwa kwenye akaunti hii zinaweza kutumika kutatua changamoto hizi.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na manunuzi yasiyozingatia taratibu. Hiki ni kichaka kikubwa sana kinachotumika kupoteza fedha za wananchi kwa makusudi kabisa. Hapa kuna mambo mengi sana. Kunakuwa na kutokushindanisha kandarasi, hali kadhalika kunaweza kukawa na mtu mmoja amekusanya document zote, akitaka kutengeneza kandarasi anajitengenezea mwenyewe lakini mtu huyu akapewa tender. Kwa maana hiyo mara zote yeye atakuwa ndio mpataji wa tender hizo. jambo hili limekuwa ni gumu sana hususan kwa watu ambao wako makini katika suala zima la manunuzi.

Mheshimiwa Spika, pia kumekuwa na changamoto katika uwekezaji wa mitaji ya umma. Fedha nyingi zimewekwa katika maeneo ambayo hayana tija. Mara nyingi watu wamekuwa wakijiamulia kutengeneza mradi pasipokufata taratibu kama vile kufanya visibility study; pia bila kujua hata breakeven point itafanyika kwa wakati gani au itatokea lini. Mambo mengine ni kama vile halmashauri kushindwa kukusanya madeni ya mikopo ya vikundi ambavyo imevikopesha. Kuna pesa nyingi sana zimekopeshwa na halmashauri kwenye vikundi vya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu lakini imekuwa ni shida sana urejeshaji wake.

Mheshimiwa Spika, kuna vitu vingine ambavyo vinaweza vikakushangaza zaidi, kama vile ujazaji wa fomu. Kama suala la kujaza fomu tu limekuwa ni changamoto ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa sana upotevu wa fedha katika halmashauri. Fedha nyingi sana zimekuwa hazipewi halmashauri kwa kisingizio hiki. Pia kuna tatizo hili la uteketezaji wa dawa. Nchi kama Tanzania yenye mahitaji makubwa sana ya dawa inashangaza sana inapofika wakati kwamba dawa zinateketezwa eti kwamba zime-expire.

Mheshimiwa Spika, sasa, haya yote ni matatizo ambayo kama tusipokuwa makini yataendelea kujitokeza na kuendelea kupoteza fedha za wananchi walipa kodi, wavuja jasho pasipokuwa na mafanikio yoyote wala kuwa na matumaini kwamba mambo haya yatarekebishwa.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema mwanzo, kwamba mambo haya yanaweza yakatekelezeka. Kutokana na taarifa za ripoti ya CAG kumekuwa na ushauri mara nyingi jinsi gani ya kuenenda kutatua changamoto mbalimbali nilizojaribu kuziorodhesha hapa.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kama halmashauri ikijielekeza katika kujengea uwezo kamati zake zile za halmashauri hapa patakuwa na tija. Shida iliyopo kamati hizi zimekuwa dhaifu kiasi kwamba panapohitajika kwenda kukagua miradi mbalimbali haziwezi kukagua miradi hiyo. Aidha ni kutokana na uelewa wa wanakamati au wakati mwingine vitendea kazi vya Kwenda kukaguliwa miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Ikage alipendekeza na mimi naendelea kusisitiza na kukumbusha kwamba kamati za halmashauri zitumike kikamilifu. Kwanza zijengewe uwezo wa kutosha kusudi waweze kuwa na uwezo wa Kwenda kukagua vizuri. Lakini kwa sababu Kamati ya Fedha na Kamati ya Ujenzi ni kamati ambazo zinahusika au zina mahusiano ya moja kwa moja na masuala ya pesa basi kamati hizi zitambuliwe kuwa ni kamati maalum za ukaguzi wa miradi na pesa za maendeleo katika halmashauri. Halmashauri iwajibike kwa namna yoyote kutenga pesa ambayo itaiwezesha kamati hizi kufanya kazi kikamilifu. Ikitokea kamati zimeshindwa kufanya kazi kutokana na upungufu au kutokana na uzembe wa halmashauri kuitengea fedha basi halmashauri inatakiwa iwajibike.

Mheshimiwa Spika, kamati hii ipewe jukumu la kutengeneza ripoti ya miradi ya maendeleo na pesa za maendeleo. Ripoti ieleze waziwazi kiasi gani cha pesa zimepokelewa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali. Kwa mfano vyanzo vya maendeleo kutoka Serikali Kuu, kutoka kwa wafadhili; lakini pia ieleze chanzo cha maendeleo kinachotokana na mapato yake yenyewe.

Mheshimiwa Spika, vilevile kamati hii katika ripoti hii iielezee waziwazi kila akaunti; kwamba akaunti hizi zilizopo zina bakaa ya kiasi gani. Hali kadhalika kamati hii ni lazima iweze kujadiliwa na Baraza la Halmashauri. Baada ya ripoti hii kujadiliwa iunganishwe pamoja na ripoti ya ukaguzi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kupelekwa kwenye vikao vya LAAC kwa ajili ya kuendelea kutumika katika matumizi ya vikao hivyo. Jambo hili litakuwa limetengeneza check and balance katika maeneo yote ya halmashauri.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo linaweza likainusuru halmashauri ni suala la ajira. Mapendekezo mengi sana yametolewa mara kwa mara pamoja na Khaji akipendekeza kwamba ajira katika halmashauri husika lazima zizingatie weledi. Watendaji katika idara mbalimbali, hali kadhalika katika vitengo na Mtendaji Mkuu lazima wawe na ueledi, kwamba lazima wawe na ujuzi wa vitengo ambavyo wanavyovisimamia, pia wawe na ujuzi husika wa idara wanazozisimamia.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mtendaji Mkuu lazima apimwe kutokana na performance kwa maana ya uwezo au kwa kile alichokitimiza katika eneo lake la kazi.

Mheshimiwa Spika, jambo hili litafanya kila mtu awajibike na pia awe na ajira ya mkataba pamoja na wale viongozi wa vitengo wawe na ajira za mikataba. Hii itasaidia sana kuwafanya wawajibike wakihofia kwamba kama hawatafanya vizuri watakatishiwa mkataba wao au hawatapewa mkataba mwingine.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine limejitokeza ambalo linahusiana moja kwa moja na Wizara ya TAMISEMI, halikadhalika Wizara inayoshughulika na masuala ya utoaji wa fedha. Kumekuwa na malalamiko mengi sana kwamba fedha zile za maendeleo haziendi kwa wakati. Jambo hili limeleta changamoto nyingi sana kwa sababu unakuta fedha zinaenda zikichelewa na wakati mwingine zinakuwa hazitoshi hali ambayo mipango iliyotarajiwa katika miradi ya maendeleo haifanikiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika kumekuwa na changamoto kwamba pesa ile ikienda imechelewa miradi haifanikiwi. Mfano mkubwa unaonekana hata sasa hivi, fedha yetu ya Majimbo haijaenda. Kwa hali ilivyo, kama itakwenda kwa kipindi hicho cha baadaye, maana yake, kwa vyovyote vile fedha hii itakuwa imechelewa na kushindwa kutekeleza mambo yaliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoanza kuzungumza kule mbele kwamba changamoto nyingi sana zinazoonekana katika level ya Halmashauri ni zile ambazo zinaweza zikatekelezeka lakini zikatibika pia. Hivyo tunayo kila sababu ya kumsaidia Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza yale anayodhamiria yatokee.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kuniwezesha kuwa hai hivi leo na kuchangia hoja hii ambayo ni hoja muhimu sana. Pia nawashukuru wale wote waliowezesha kwa namna moja ama nyingine kunifanya nikachangia hivi leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie hali halisi ya mazingira ambayo nafikiri kwa namna moja au nyingine Serikali haijafanya jitihada za kutosha sana kuangalia hiyo halisi na kuangalia jinsi gani ya kutatua tatizo hili la mazingira.

Mheshimiwa Spika, mfano katika mji wa Dar es Salaam, tafiti zinatuonyesha kwamba tani 5,600 za uchafu zinazalishwa; na uchafu wenyewe umejikita sana kwenye takataka za plastic. Pia tafiti hizo hizo hizo zinatuonyesha kwamba asilimia 30 mpaka 40 ya taka ngumu zinakuwa ndiyo peke yake zinaweza kupelekwa maeneo ya kutupa (dump) na dampo kwa Dar es Salaam liko moja tu, Pugu Kinyamwezi. Sasa ukiangalia asilimia iliyobakia ni takataka ambazo zenyewe hazina uhakika wa kwamba zinapelekwa wapi. Unaweza ukaona kwa jinsi gani hali ilivyokuwa ngumu hapo.

Mheshimiwa Spika, hali halisi pia inaonyesha kwamba kwenye beach za Mkoa wa Dar es Salaam kuna takataka takribani mifuko 150 mpaka mifuko 200 ambazo zinatolewa kila siku, yaani wale watu wanaojishughulisha na utoawaji wa taka, kila siku wanafanya kazi ya kutoa uchafu huo. Katika hali hiyo, tunahitaji kujielekeza sana kwenye jitihada ya kuzoa takataka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jitihada ambayo nayotaka ni-stick, ziko mbili ya kwanza kabisa ni kwenye suala la elimu. Tumejikita sana katika utatuzi wa kutengeneza miundombinu mikubwa mikubwa. Tnafikiria vitu vikubwa badala ya kufikiria vitu vidogo ambavyo vitatuwezesha kufanya suala hili kwa umakini kabisa. Kama tumeamua kutoa elimu, basi tuelekeze elimu yetu kwa sehemu kubwa kabisa kwa vijana, kwenye shule za msingi.

Mheshimiwa Spika, nashauri moja kwa moja tuwe na somo la mazingira. Lichukuliwe kama ni somo linafundishwa kuanzia Darasa la Kwanza, kwa sababu tunajua vijana wadogo ndio wanaoweza ku-pick suala lolote kwa uharaka zaidi. Wanajifunza kwa uharaka zaidi na kulitendea kazi; na kwa sababu wao ndio wenye nchi yao au dunia yao ya kesho; kwa sababu siyo dunia yetu, ni dunia yao wao, kwa hiyo, tukiwafundisha wao nafikiri itakuwa vizuri zaidi. Tutumie fedha nyingi katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine nashauri tuwamilikishe uchafu wale wanaotengeneza uchafu. Kama tutafanya jitihada hii, tutahakikisha kwamba mazingira yanakuwa safi. Hapa najaribu kuzungumzia kitu gani? Kwa mfano, tunajua kuna watu wanatengeneza maji, wanatengeneza juice, lakini kiuhalisia siyo kwamba wanatengeneza maji, isipokuwa wanatengeneza uchafu wa plastic, vile vifaa wanavyovitumia katika kuweka hayo maji au kuweka hivyo vitu vingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lazima tufanye jitihada kuwamilikisha uchafu. Katika njia gani? Kuwaambia kwamba uchafu ule ni mali yao, wahakikishe kwamba kwa namna moja au nyingine, uchafu wowote utakaonekana sehemu yoyote ile unawahusu wao. Nao lazima wawajibike katika kuhakikisha uchafu ule wanauondoa. Kwa hiyo, njia mojawapo ni kuweka bei, kwa mfano bei ya maji shilingi 600, lakini iwekwe kama shilingi 100 iwe ni pesa ku-retain ule uchafu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mtu anayekuja kununua maji, ananunua kwa shilingi 600 lakini shilingi 100 ni gharama ya kutolea uchafu pale. Kwa hiyo, nafikiri kwa namna hiyo tunaweza kuwa na uhakika wa kuondoa uchafu ambao unazagaa kiholela.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalotaka kuzungumza ni kuhusu sera. Sera zetu lazima zihakikishe zinaangalia ajira za watu wa kutoa uchafu zinathaminiwa. Tuhakikishe kwamba kwa namna moja ama nyingine watoa uchafu wanaajiriwa kwa kuwawezesha kwenye miradi midogo midogo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, Wizara ijielekeze katika kujenga uwezo wa kutimiza wajibu wa kutekeleza majukumu yake kwa kadri ya kiwango cha matarajio yaliyo wengi. Wizara hii ya TAMISEMI ni miongoni mwa Wizara kubwa, muhimu na mtambuka, lakini inakumbwa na changamoto ya kiutendaji.

Kwanza, Wizara inakabiliwa na ufinyu wa nguvu kazi, eneo muhimu katika kutekeleza majukumu; watendaji hawatoshi kwa idadi na yao na ubora na pia watendaji hawatoshi kiuweledi (professionalism). Aidha, majukumu muhimu yanatekelezwa na watendaji wasio na sifa za elimu na uelewa wa kazi husika (elimu na uelewa duni) mfano Halmashauri ya Mtama na Nanyamba, kazi za engineer zinatekelezwa na fundi wa cheti na kusababisha utekelezaji duni wa miradi ya hospitali kwenye maeneo hayo.

Pia watendaji kukosa maadili ya kazi hivyo hivyo kusababisha ubadhirifu mkubwa mahala pa kazi (upotevu wa pesa na mali).

Mheshimiwa Spika, pia watendaji wenye sifa kukaidi taratibu za kazi na maelekezo kutoka kwenye mamlaka zinazowatuma (Wizara yao) kwa mfano Masasi DC engineer alishindwa kutoa mchanganuo wa miradi aliyotekeleza baada ya kuamua kutozingatia BOQ iliyokuwa imuongoze kwenye utekelezaji wa vipengele vya mradi mkuu wa ujenzi wa A-Level ya Mpeta. Utaratibu aliouchukua baada ya kuachana na BOQ ulipelekea kupelea (deficit) ya shilingi 345,000,000; asilimia 34.5 zaidi ya pesa iliyokusudiwa kukamilisha mradi huo. Mradi ulipewa bilioni moja zikatumika zote hazikutosha.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya kiutendaji pia inajionesha kwenye mifumo; mifumo ni mingi lakini pia haisomani hivyo taarifa kuchelewa ama kuwa zisizo na uhalisia (potofu).

Mheshimiwa Spika, taarifa zinazotolewa kwa Wabunge kuhusu miradi na masuala ya ufuatiliaji zinachelewa, hongera Waziri kwa kuliona hilo naona ameanza kulifanyia kazi jambo hili.

Kuhusu mfumo wa udhibiti mahali pa kazi (internal control system) licha ya umuhimu wake umekuwa dhaifu kiasi cha kudhania kuma haupo. Shida kubwa inajionesha kwenye ukaguzi wa ndani. Eneo hili lingekuwa linafanya kazi zake vema, changamoto nyingi za ubadhirifu wa fedha zingepungua kama sio kwisha. Shida kubwa ya ubadhirifu inayoripotiwa mara kwa mara inatokana na ukosefu wa maadili uliokithiri.

Mheshimiwa Spika, kuhusu shida ya ajira kwa vijana; wahitimu wa vyuo (walimu) hasa wa sayansi waliohitimu miaka ya 2016, 2017 na 2018 wametuma maombi lakini mpaka sasa hawajapata kazi, wanaendelea kutuma mambo. Nashauri ajira zitolewe kwa kuzingatia majimbo ili kila jimbo lipate, hali ilivyo sasa inaonesha upendeleo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nikushukuru wewe mwenyewe binafsi, kwa kadri jinsi unavyoiendesha taasisi yako hii ya Bunge. Lakini nimshukuru pia Naibu Spika kwa kazi hiyo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze katika sekta hii ya kilimo, Sekta ya kilimo imekuwa ni sekta nzuri ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa sana uchumi wa nchi hii. Kwa muda wote sekta ya kilimo imekuwa namba moja katika uchangiaji katika uchumi wa nchi hii. Kwa mfano, mwaka 2018 sekta hii ilichangia kwa takribani asilimia 27.9 ya bajeti nzima. Lakini pia mwaka 2019 ilichangia kwa takribani asilimia 26.6 kwenye bajeti ya nchi nzima. Lakini imeendelea pia kuchangia sekta hii katika ajira, asilimia 58 ya ajira zinazopatikana katika nchi hii zinachangiwa na sekta ya kilimo. (Makofi)

Halikadhalika asilimia 65 ya malighafi (raw materials) inachangiwa na sekta ya kilimo. Baada ya kuona umuhimu wote huu bado Serikali imeendelea kuwa na kigugumizi kikubwa katika kuhakikisha kwamba sekta ya kilimo inapata haki inayostahili. Serikali imekuwa haioneshi weledi wake katika kuchangia sekta hii kikamilifu. Naomba kwa namna moja au nyingine, Serikali ioneshe nguvu zake zote kwenye sekta ya kilimo kusudi tuweze kufanya mapinduzi ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi tunatumia jembe la mkono, maeneo mengi sana jembe la mkono limekuwa siyo Rafiki. Hali hii imesababisha mpaka vijana ambao ndiyo wengi katika nchi hii kushindwa kujiingiza katika sekta ya kilimo kwa sababu ya ugumu wa matumizi ya hili jembe la mkono. Kwa hiyo, naiomba Serikali itilie mkazo kwa kiasi kikubwa kuiinua sekta hii ambayo inabeba ajira za wananchi walio wengi hasa wananchi walioko pembezoni vijijini huko.

Mheshimiwa Spika, lakini Serikali pia inaona shida gani kutumia sekta zake tofauti, kwa mfano sekta ya fedha kama benki, kuyaamrisha au kuyapa taarifa kwamba wawakopeshe wananchi. Kuna ugumu gani kwa sababu hii ni sekta muhimu na kilimo kinakopesheka. Wananchi wote ambao wanashughulika na kilimo wanakopesheka.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia mfano mdogo tu wa zao la korosho limetoa dola takriban bilioni 589. Hizi ni fedha nyingi sana, ni trilioni 1.3. Nashangaa kwa nini Serikali imekuwa na kigugumizi kuwekeza katika kilimo kwa sababu hii trilioni 1.3 ni takriban asilimia 4 ya bajeti nzima. Ukiangalia ni mchango mkubwa sana, sioni sababu kwa nini Serikali haijajielekeza kwenye sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, sisi pia tumejitambulisha kuwa tunataka kuendesha uchumi wa viwanda. Uchumi wa viwanda hauwezi kufanikiwa pasipokuwa na sekta ya kilimo. Kama tulivyoona pale kwamba asilimia 65 ndiyo inapeleka pale kama malighafi, sasa ugumu uko wapi?

SPIKA: Unajua Mheshimiwa Mchungahela, Waheshimiwa tuwe tunawasikiliza Wabunge wanaochangia. Huyu ni Mheshimiwa Issa Mchungahela wa Lulindi, unajua kule Kusini zamani neno mhasibu halikuwepo walikuwa wanaitwa wachungahela. (Kicheko)

Mpaka sasa hivi Mheshimiwa hueleweki kwa kweli, yaani hujajikita moja kwa moja kujaribu kueleza kitu chako, unapiga theory. Hebu endelea kidogo lakini shuka kwenye kitu ambacho unataka kifike.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nilitaka kujikita kwenye korosho. Korosho kwa namna moja au nyingine iko wazi kabisa kwamba inachangia kiasi kikubwa kwenye uchumi lakini pia kwenye ajira ya wananchi wa Kusini kwa sababu ni pesa nyingi sana ambazo Serikali inapata kupitia kwenye korosho.

SPIKA: Yaani mtu anaweza akakuuliza swali, haijajikita vizuri kivipi, unataka kusema nini? (Kicheko)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Ahaa.

T A A R I F A

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Ndiyo, taarifa, nimekusikia.

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mchungahela, anaposema Serikali haijajikita ipasavyo kwenye kulisaidia zao la korosho, hivi tunavyozungumza hata Bodi ya Korosho yenyewe haijaundwa. Bodi ile ya Korosho kwa sasa inakaimu Mkurugenzi hamna analolifanya. Kwa hiyo, napenda kumpa taarifa msemaji anaposema Serikali haijajikita alijumuishe na jambo hilo la Bodi ya Korosho. (Makofi)

SPIKA: Yaani anasema lilelile nililokuwa nakushauri mwanzoni, unaposema kitu hebu fika mwisho.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Yes! Napokea taarifa Mheshimiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nataka kusisitiza kwamba hata jitihada zinazofanyika sasa hivi za kupeleka pembejeo, hizo pembejeo mpaka sasa kuna maeneo ya Jimbo langu ambapo ndipo panapozalishwa korosho mapema sana, sasa ni kipindi cha maandalizi ambapo pembejeo zinahitajika lakini hazijafika. Kwa hiyo, nilikuwa najaribu kuonesha pia katika mazingira hayo kwamba kwa namna moja au nyingine umakini sana unatakiwa katika utekelezaji wa yale tunayoyazungumza.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Issa Mchungahela, bahati mbaya dakika zimeisha. Nakushukuru sana sana kwa mchango wako.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ameniweka hai na kuweza kuchangia bajeti hii ya viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kujielekeza kwenye bajeti hii kwa kuangalia baadhi ya vitu mimi sina shaka na mipango, mipango ya Chama chetu cha Mapinduzi lakini mipango pia ya Serikali sina shaka. Tumekuwa na mipango mizuri mingi sana tangu Serikali ilivyoanza kuundwa na mpaka hivi leo, ukiangalia bajeti za kila mwaka utathibitisha hilo. Kwa miaka mitano hii inayokuja mipango yetu imekuwa mikubwa na mizuri sana na kama tunavyojielekeza kwenye bajeti ya uchumi endelevu, lakini uchumi shindani pia hili ni jambo zuri kabisa na ni jambo jema lakini tunahitaji kujielekeza nguvu zetu katika utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tuna shida sehemu katika suala hasa la bajeti kuangalia vipaumbele. Tumekuwa hatujikiti sana katika vipaumbele vya bajeti zetu, tunaongea mambo mazuri, lakini katika utekelezaji nafikiri kumekuwa na changamoto, tuangalie mfano mdogo tu katika bajeti zetu, ukiangalia bajeti ya viwanda kwa mfano bajeti hii ndio mkombozi katika uchumi wa nchi hii kwa sababu kwa kutumia bajeti hii tungeweza kwa namna moja au nyingine kufikia malengo yale ya uchumi endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani kama tungeingia kwenye vipaumbele, lakini ukiangalia unakuta miradi ambayo tunajaribu kutaka kuitekeleza ambayo kwa hali halisi ndio miradi ya mkakati unakuta kitu tofauti kwa mfano Mradi wa Liganga na Mchuchuma ambao ni mradi mkakati kwa mwaka 2020/2021 ulitengewa takribani shilingi milioni 120 tu, mwaka 2021/2022 umetengewa shilingi milioni 25. Kwa kweli hatuko serious kabisa kama kweli tunataka kufanya yaani kwamba kama miradi hii ni mradi mkakati tofauti tunachoongea na kile tunachokifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia Mradi wa Mchuchuma tumetengewa takribani shilingi milioni 120 peke yake mwaka 2020/2021 lakini mradi huo huo pia tumetengewa takribani shilingi milioni 25 katika msimu wa mwaka 2021/2022 kwa kweli hatupo serious, hatupo serious kabisa, lakini mradi wa Ziwa Natron wenyewe ulitengewa shilingi milioni 50 peke yake, hali kadhalika kwenye mwaka 2021/2022 ulitengewa shilingi milioni 24 kwa kweli haioneshi kabisa kama sisi tupo serious katika huu uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu tukitaka tuendelee kwa umakini kabisa uchumi wa viwanda lazima tufanya seriousness, ionekane kabisa kwa sababu ukiangalia kiasi kilichotengwa kwa maendeleo kwa takribani kwa miaka hii miwili haizidi bilioni 30 sasa sijui kama kweli tunataka kutekeleza maendeleo ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuzungumza ni nini; kama tutajielekeza kweli kwenye uchumi wa viwanda kikweli kweli tunaweza tukaendelea vizuri sana na tukawa tumepata tija kubwa na mafanikio makubwa sana katika maendeleo na hatuwezi kujidanganya hatuwezi kuendelea pasipo kuendeleza viwanda, kwa sababu viwanda ndio vyenyewe vinakula material, material nyingi sana ambazo sisi tunatengeneza hapa ina maana kwamba kwenye kilimo kwa mfano, lakini kwenye maeneo mengine ya uchumi kwa mfano ya madini na hali kadhalika kwenye maeneo mengine ya uchumi kwa mfano yanayotokana na bahari yaani kwenye uchumi wa blue hivi vyote vinatumika na viwanda ndugu zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo bila viwanda hivi vitu vyote tunavyovizungumza haviwezi kufanikiwa na hatutaweza kuviendeleza, kama nilivyojaribu kuangalia kwa mfano tuchukulie mfano tuone muonekano halisi wa kadri jinsi haya mambo yanavyokwenda yanavyoweza yakatupatia tija. Tuna issue ya EPZ ambaye na yenyewe hatuoni kama tuna u- seriousness.

Mheshimiwa Mwenyekiti, EPZ kwa mfano pale Benjamin William Mkapa Serikali iliwekeza pale shilingi bilioni 36.4 kwa ajili ya kufidia na kuweka miundombinu, lakini ukiangalia pale kilichotokezea tulipata tija kubwa sana kutoka kwenye hiyo shilingi bilioni 36 tuliyowekeza tija tulizozipata pale tulipata uwekezaji wa mtaji yule mwekezaji aliweka mtaji wa shilingi bilioni 134; unaweza ukaona ni fedha nyingi kuliko tulizowekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa shilingi bilioni 36 tuliyowekeza tumepata shilingi bilioni 134 kama uwekezaji wa mtaji, lakini kampuni pia ilifanya mauzo ya shilingi bilioni 385.93 na kampuni hizo pia zilifanya matumizi ya fedha ambazo takribani shilingi bilioni 2019.184 lakini pia Serikali ilipata faida kupitia kodi ya shilingi bilioni 22.67 on top of that tulipata ajira ya watu 3,156.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaweza mkaona kwa jinsi gani tija kubwa ya shilingi bilioni 36 tu imezalisha haya yote haya tumepata Watanzania, kama tungewekeza vya kutosha Benjamin William Mkapa bila shaka mngeweza mkaona tija gani mngepata hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ukiangalia SEZ eneo na Bagamoyo Serikali iliwekeza shilingi bilioni 26 peke yake lakini katika kuwekeza shilingi bilioni 26 Serikali ilikuja ikapata tija kubwa sana kulikuwa na tija kwa mfano shilingi bilioni 4.8 ya uwekezaji; mwekezaji aliweka hizo fedha, lakini mwekezaji pia alifanya mauzo ya nje ya shilingi bilioni 56.2 lakini kama haitoshi kampuni pia ilipata kwa kulipa kodi shilingi bilioni 1.305. Kwa hiyo unaweza ukaangalia kwa kiasi kidogo tu cha shilingi bilioni 26 tulizowekeza Bagamoyo tumepata fedha nyingi hizi, lakini cha kushangaza hapo hapo Serikali inadai kujaribu kurudisha baadhi ya maeneo ambayo tungeendelea kuyawekeza ya SEZ kwa kweli hatupo serious na kama tupo serious kwa kweli tunatakiwa tuwekeza kikamilifu kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini naomba seriousness kwenye viwanda ifanyike, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa afya tele mpaka naweza kuchangia bajeti hii.

Pili, niishukuru familia yangu, lakini kipekee kabisa nimshukuru mke wangu aliyenipa uwezo mkubwa sana wa kuwajibika na kuweza kutimiza majukumu yangu ya kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba, bajeti hii ni bajeti ambayo itaendelea kusomwa na kusifiwa kuwa ni bajeti nzuri kabisa katika bajeti zilizowahi kujadiliwa katika Bunge hili Tukufu. Siyo nasema hivyo kwa sababu tu ya kutaka kusifia, lakini ukiangalia jinsi hii bajeti ilivyotengenezwa, unaweza ukalithibitisha hilo nia ya bajeti ukiiangalia lakini pia ukiangalia dira lakini ukiangalia dhamira na pia ukiangalia pia utayari wa Mheshimiwa Jemedari wetu Mama Samia Suluhu Hassan, hiyo inakuashiria moja kwa moja kwamba hii bajeti itakuwa bajeti nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti yenyewe naanza kwa kusema kabisa kwamba itatekeleza na kusimamia mazuri yote ambayo awamu tofauti tofauti za uongozi imeyatekeleza. Mazuri katika awamu hizo yako mengi sana, kila awamu iliyopita imekuwa na jambo zuri sana la kuigwa na kulisimamia kwamba liendelee kuwepo. Hata hivyo, kwa hali jinsi ilivyo kutokana na ufinyu wa muda sitaweza kuzungumzia kila zuri la awamu iliyopita, lakini kipekee tu nitaweza kuzungumzia jinsi walivyoweza kusimamia yale waliyotaka kuyatekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, yeye aliamini katika Taifa lenye uchumi imara kupitia sera ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea lakini hali kadhalika nchi huru yenye fikra huru, yenye uchumi huru, yenye siasa huru bila kujifungamanisha na nchi yoyote ile. Hili lilikuwa ni jambo jema kabisa ambalo awamu hii pia italitekeleza kwa njia ya kipekee kupitia staili yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu iliyofuatia ilikuwa ni awamu ya Mheshimiwa Rais Ally Hassan Mwinyi na yenyewe ilikuwa na dhamira nzuri kabisa uchumi huria, lakini yenye watu ambao wako proactive, kukimbilia fursa ambazo zitawawezesha wao kuijenga nchi yao kikamilifu hasa katika masuala ya kibiashara. Fikra hii ililenga katika kuimarisha dhana ya kuwa uchumi au suala la biashara lishughulike na watu binafsi, lakini wakati huo huo Serikali ikijikita katika kutekeleza mambo ya msingi ya kijamii na kuendeleza miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Tatu, ya Mheshimiwa Benjamin William Mkapa na yenyewe ilikuja na fikra pevu, nzuri kabisa ambayo yenyewe ililenga kabisa katika utekelezaji wa uwazi, lakini seriousness katika utekelezaji huo. Lengo lilikuwa ni kuwajenga wananchi waweze kujitambua, lakini pia kuona kwamba kila wanachokifanya wanakifanya kwa ajili ya manufaa ya nchi yao na uzalendo wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia awamu iliyokuja, Awamu ya Nne ya Mheshimiwa JK. Awamu hii pia ililenga katika kutengeneza uchumi uliokuwa imara, bora kabisa, ilijihakikishia kwamba inaweka miundombinu yote ya kuchochea uchumi na maendeleo, ilijaribu kuweka mkakati pia wa mahusiano ya kimataifa ambayo yalikuwa mahusiano bora kabisa na nchi za nje. Hii yote ililenga katika kuweka uchumi uliokuwa imara uchumi endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Tano, awamu ya jembe, tuliona kabisa awamu hii ilikuja kwa kasi kubwa. Hii ilikuwa ni awamu ya kazi lakini hali kadhalika ilikuwa ni awamu ya viwanda ambavyo vimejielekeza katika kutekeleza uchumi wa nchi hii. Pia awamu hii ilikuwa awamu ya uwajibikaji lakini na u-champion katika kupambana dhidi ya rushwa na ufisadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia awamu hizi zote zilikuwa zimefanya vizuri na kama alivyosema Mheshimiwa jembe letu, mama yetu, jemedari wetu mkubwa, kwamba atajielekeza katika kutimiza mazuri yote, tunaona mazuri haya yanajenga msingi mkubwa na imara katika kutekeleza yale yote ambayo tunayategemea katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uzuri wa hayo yote, nina shaka kidogo hasa nikiangalia kwa kadri jinsi tulivyoweza kutekeleza bajeti zetu zilizopita. Ukiangalia bajeti zetu zilizopita unaweza katika hali ya ubinadamu ukaona kwamba kunaweza kuwa na shaka. Kwa mfano, kwenye kilimo kilitekelezwa kwa asilimia 13 tu ya bajeti nzima. Halikadhalika viwanda, ile dhamira ya kutekeleza uchumi wa viwanda, bajeti zilizopita zilitekeleza kwa takriban ya wastani wa asilimia 20. Kwenye mifugo, ilitekeleza kwa takriban ya asilimia 18.1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mazingira hayo yanaweza yakakupelekea ukawa na wasiwasi. Hata hivyo, wasiwasi huu unatoka moja kwa moja kwangu na imani niliyokuwa nayo ni kutokana na ile hali ya utayari wa mama yetu, hapo peke yake naamini kabisa kwamba hakutakuwa na wasiwasi kila kitu kitakwenda kama vile kilivyopangwa katika bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusisitiza kwenye hili ni nini? Nasisitiza katika utekelezaji. Naomba utekelezaji uwe wa umakini kabisa. Tukizungumzia utekelezaji hasa hasa unajikita katika maeneo matatu. Eneo la kwanza ni katika kutoa pesa inayohitajika, kusudi kila sekta ambayo imeomba pesa ipewe kwa kadri ya wakati na vile inavyohitajika na kwa kiwango kinachostahili. Awamu nyingine ni awamu ya utekelezaji, ambapo Wizara husika na watendaji kupitia sekta zake binafsi pamoja na halmashauri wawe wanawajibika kikamilifu kabisa kuhakikisha kila kitu wanachotakiwa kukifanya wanakifanya kama inavyostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo nataka kulizungumzia zaidi ni eneo la usimamiaji na hilo ndiyo jukumu letu sisi Wabunge pamoja na Madiwani. Sisi kisheria tumetambulika kwamba ni wasimamiaji ambao tunatakiwa tuisimamie Serikali kikamilifu kabisa. Kazi hii haiwezi kufanyika kikamilifu kama hatutapata taarifa zinazostahili katika kusimamia mambo haya. Kumekuwa na changamoto kubwa sana katika eneo la usimamiaji hasa hasa ukiangalia kwamba watendaji wameamua kupokonya kazi hii ya kusimamia. Mara nyingi wamekuwa hawatoi taarifa kwa Wabunge ambao ndiyo wanaostahili kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu haya wanajikabidhi wenyewe na wewe kama Mbunge ukijaribu kufuatilia kupata taarifa stahiki kutaka kujua ili uweze kusimamia, kunakuwa na changamoto ya usiri na unaonekana kama wewe ni kama vile kizabizabina, lakini halikadhalika unaonekana kama wewe unajipendekeza, lakini pia unaambiwa kama wewe unajipa madaraka ambayo hustahili wakati hili ni suala letu au ni kazi ambayo sisi tumeambiwa kisheria kabisa tunatakiwa tuifanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana Wizara, naomba sana na Mawaziri wafanye kazi ya kutupa taarifa kabla hawajapeleka pesa ya mradi wowote, sisi tunastahili kujua mapema kuliko mtu mwingine yeyote.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja, sina shaka bajeti hii itakuwa ni bajeti yenye kuzungumzwa na kutekelezwa, lakini na kusifiwa duniani kote na miaka yote. Ahsante. (Makofi)
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyeniweka hai na kuja kushiriki katika mjadala huu wa African Continental Free Trade Area.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni-declare kwamba mradi huu au itifaki hii ni itifaki nzuri ambayo itatuwezesha kufanikisha. Kwa hiyo, kwa mwanzo kabisa lazima niunge mkono hoja kwa sababu tunaenda kuliendea soko na takribani watu bilioni 1.2 ni watu wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini, baada ya kusema hivyo msimamo wangu mwingine wakutaka kuistua Serikali usichukulie kuwa kama nataka kuipinga Serikali au kutaka kuipinga hoja hii. Lakini ichukuliwe kwamba ni chachu ya kuisukuma Serikali kujielekeza katika kutatua changamoto muhimu hasa hizi za biashara ambazo zitatuwezesha sisi kunufaika sana na mkataba huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiniuliza kwamba, je? tumechelewa kwenye mkataba huu kama ambavyo watu wengine walivyojaribu kudai, ninaweza nikasema hapana hatujachelewa na hata wale waliokataa kusaini mwanzo mkataba huu walifanya jambo zuri kabisa kwa sababu gani? Kwa sababu Serikali iliweza kujiangalia kama Taifa na kuanza kutafakari njia bora za kuangalia changamoto ambazo zilitufanya tukaukataa mkakataba huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia sisi kama nchi tulijitutumua mbele za nchi nyingine duniani na kujionyesha kwamba sisi ni watu huru, lakini tunauwezo wa kujiamulia maamuzi yetu ambayo yenye maslahi na nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiniuliza kwamba, je, tuendelee kukataa mkataba huu? Nitakuambia hapana, hatuwezi kufanya hivyo kwa sababu mazingira ya sasa hivi yamekuwa ni mazingira bora kuliko yale mazingira ya zamani. Lakini hali kadhalika pia mkataba huu una content nyingi sana ambazo ni positive ambazo kama Serikali itafanya jitihada kwa umakini kabisa kufuatilia maslahi gani ambayo tunayoyapata humu, tutanufaika na huu mkataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa utendaji wa Serikali nianze kusema kwamba sina shaka kwa sababu kuna mambo mengi sana ambayo nafikiri kwa kukataa ule mkataba mwanzo kusaini Serikali ilienda ikajielekeza katika mazingira mazuri yakuanza kutafuta changamoto kama vile nilivyosema zile zilizosababisha watu kuukataa ule mkataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano ukiangalia, Serikali ilienda ikaweka mazingira mazuri ya mtandao wa barabara, imeweka mtandao mkubwa kabisa wa barabara ambao ni chachu kubwa katika suala la kiuchumi hasa hasa katika uzalishaji kule kwa mfano vijijini kwenye mazao ya kilimo. Mtandao wa barabara umekuwa ni muhimu sana naweza nikaishukuru sana Serikali na kuipongeza na kwamba iongeze bidii, iongeze zaidi ya hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ukiangalia Serikali ilifanya kazi kubwa pia ya kutengeneza mtandao wa nishati mpaka sasa hivi tunazungumzia kwamba nchi nzima tumekuwa na umeme takribani kila kijiji kasoro vijiji vichache. Hii pia ni sehemu kubwa sana Serikali ambayo iliifanya kazi hii kwa kuangalia changamoto zile ambazo zilipelekea sisi kuukataa ule mkataba kwa mara ya kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa namna moja au nyingine hatuna sababu ya sisi kujiona inferior kwa kukataa huu mkataba mwanzo haizidi haipungui ni kwamba tumepata nguvu sasa ya kuweza kupambana zaidi na wenzetu kwa sababu tayari tushapata vitu wezeshi vitakavyosaidia sisi kutusukuma kwenda mbele zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna kitu ambacho najaribu kutaka kusisitiza kwa Serikali pamoja na mazuri yote ambayo nimeyasema hapa na mengi ambayo nakusudia kuyafanya ukiangalia kuna mambo mengi sana kwa mfano, ujenzi wa Stigler’s gauge, lakini kuna pia ujenzi wa EPZ, lakini kuna mambo mengi sana yaani kama vile vyanzo vya nishati nakadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunaona kabisa kwamba Serikali ina nia nzuri, lakini pia nataka kuisisitizia Serikali kwamba iongeze kasi katika utekelezaji wa hizi adhima zake au nia zake, kwa sababu gani? Zenyewe ndizo zitakazotufanya sisi tuweze kuonekana mbele za wenzetu kwamba ni watu tupo superb na tuweze kuchangamkia hizi fursa tunazokwenda kuziendea vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho nilichotaka kusisitiza hapo ni kuiomba Serikali ifanye jitihada ya makusudi kabisa kuweka sub-seeds kwenye mazao au biashara mkakati vitu ambavyo tunaona sisi tunafanya vizuri zaidi basi tujaribu kuweka sub-seeds kuwezesha sisi kupata bei nzuri au kuwa na gharama ndogo ya uzalishaji, lakini wakati huo huo tukiweza kuweka bei nzuri ukilinganisha na bei za wenzetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine pia ni kuweza kutumia kodi au tariff vizuri katika maeneo ambayo tunaona kwamba tupo tunakaribia kupoteza, sehemu ambapo tukiona kwamba hapa tunakaribia kupoteza tunatakiwa tuweke tariff kwa ajili ya ku-protect. Kwa mfano, hizi product zetu tunazozalisha, lakini pia ku-protect wazalishaji wetu wa ndani na wafanyabiashara wa ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo tukijaribu kufanya hivyo nafikiri sisi tutakuwa ni miongoni mwa watu wenye manufaa makubwa sana na huu mkataba kwa sababu hiyo inajieleza mpaka sasa hivi ukizingatia tupo katika ndani ya watu au nchi kumi ambazo ni bora sasa hivi Afrika katika masuala ya kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo naomba kuunga mkono hoja asilimia mia moja. Ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kuniweka hai mpaka hivi leo na watu wa Lulindi wako wakinisikiliza kutaka kuwaongelea jambo lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti,kama muongeaji aliyepita natamani kuishauri Serikali kama itawapendeza basi waweze kuchukua na hiki ninachokusudia kuwashauri kukiweka katika mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejielekeza sana kwenye kilimo kama vile ambavyo wenzangu waliotangulia lakini nimejielekeza katika muonekano mmoja kwamba kama tutahangaika vizuri tu na kilimo biashara bila shaka matatizo makubwa ya kiuchumi lakini pia ya ajira yanaweza yakawa yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee eneo moja eneo ambalo linahusu maeneo ninayoishi kule kwetu Mtwara kwa maana ya Lulindi korosho. Korosho ni kitu ambacho inailetea pato nchi hii pesa nyingi sana nashindwa kuelewa kigugumizi kiko wapi kwamba Serikali bado haiweki juhudi ya kutosha kuhakikisha kwamba korosho zinapatikana kama vile ambavyo wao wanavyotarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, makusudio kwa mfano ya bajeti hii inayokaribia kuja Serikali ilijaribu kuelekeza kwamba korosho zipatikane takriban tani laki saba. Sasa tani laki saba ndugu zangu haziwezi kuja hivi hivi kwa maneno lazima tuwe tumejipanga vizuri na kwenye Mpango humu sioni wapi kwamba kuna kitu cha namna hii kitakachotuwezesha zao la korosho zipatikane tani laki saba, na kwa nini tani laki saba kwa sababu mpaka sasa hivi ambapo ni kiasi cha korosho kinapungua hakifiki hata tani laki tatu Serikali inapata pato la dollar takriban milioni 500 ambayo ni trilioni 1.3 kwa maana kama kweli lengo la tani 700,000 litafikiwa ina maana hapa ni zaidi ya dollar milioni moja ni kiasi cha trilioni tatu na zaidi mnaweza mkaona kwa jinsi gani hapa suala la kupata pesa ya kuingiza kwenye uchumi ilivyokuwa nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sisi hii dollar milioni 500 plus ambayo ni trilioni 1.3 mmeona athari yake kwenye uchumi nchi nzima kila mahali sasa hivi watu wanahangaika tunajenga kule tunajenga kule uchumi unaingia pale uchumi unaingia pale. Mnaweza mkaona hii dollar milioni moja ambayo Serikali ina i-target kupitia korosho tani laki saba inaweza ikawa ina athari kiasi gani? Sasa kwa hali hiyo hapa panahitajika kuwekeza kitu kidogo tu na chenyewe ni kitu kama hivi kwangu panahitajika kuingiza pembejeo za kutosha lakini mapema kabisa tena ambazo haziwezi zikazidi hata bilioni 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini halikadhalika kuwezesha jambo hilo pia liende vizuri tunahitaji pia ile barabara ya kutoka Mtwara kupitia Nanyamba kwenda Newala, kwenda Lulindi kwenda Masasi kwenda Nachingwea ambayo ni takriban kama bilioni 300 hivi. Hivi jamani hapa ukichukua hapo makadirio inaweza ikawa kama bilioni 400, bilioni 400 ukiwekeza ukapata takribani trilioni tatu hivyo jamani tunahitaji kitu gani? Shida ninayoona ninaona kwamba sisi tunafikiria sana vitu vikubwa mno baada ya kufikiria vitu vidogo vidogo ambavyo viko pale wala havihitaji kazi kubwa kuvitekeleza vikatupatia pesa. Kama tungekwenda kwa mtindo huu tukaenda kwenye eneo jingine la kilimo tukafikiria katika mtizamo huu bila shaka suala la kilimo kuwa uti wa mgongo lingekuwa lina maana sana na lenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya kutoa ushauri huo nataka niipongeze Serikali kwa kazi yake kubwa ambayo imejaribu kuionyesha katika maeneo yale muhimu ambayo yanaweza pia kusaidia kwa namna moja au nyingine kuleta matokeo ya uchumi ya haraka. Maeneo mengi ambayo watu wengi wameshaanza kuyasema huko mwanzo kama vile uwekezaji wa reli ya Standard Gauge ninaiomba Serikali kusisitiza kwamba hili suala la Standard Gauge katika eneo letu la Mtwara kutoka bandarini kwenda Mbamba Bay nakupitia katika maeneo yale mawili ya Mchuchuma na Liganga yaani tunasema kwenye matawi itawezesha sana bandari ya Mtwara kutumika na kuingiza uchumi mkubwa katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani sasa hivi tumetumia pale takriban bilioni 157 lakini ni kama zimelala tu bado hakujawa na kitu chochote cha maana cha kuifanya bandari ile ichangie kikamilifu kama vile tunavyotarajia na tunaweza tukaitumia bandari ile katika maeneo yote yale kule ya nchi za kusini kama vile Mozambique ambavyo kwa sasa hivi wanashida kwa sababu hawatumii bandari yao kutokana na hali yao ya matatizo ya migogoro yao lakini halikadhalika Malawi na Zambia wanaweza wakaitumia vizuri sana bandari ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali itumie nguvu nyingi sana kuhakikisha bandari ile inatumika kikamilifu, mambo haya yasiishie kwenye karatasi tu tumekuwa wepesi sana wa kuongea lakini kuthubutu kufanya maamuzi ya kutekeleza ni wagumu sana nashindwa kuelewa sababu za msingi sijui ni kwanini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti hizi tunazokaa hapa mara nyingi sana wengi wanaona kama ni sehemu tu ya kuja kuigiza tunakaa tunachangia na kutoka tukishatoka hapa utekelezaji unakuwa mgumu sana unakuta kiongozi ambaye muhusika msimamizi wa Wizara fulani unavyojaribu kumfuata kutaka kufuata utekelezaji wa jambo fulani ambalo mmelizungumza pale halitekelezwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mfano nataka nizungumzie suala la mawasiliano kule kwangu. Bajeti hii iliyoko sasa hivi nilihakikishiwa kwamba takriban kata nane katika kata 16 maana yake kata 16 katika jimbo langu hazina mawasiliano kabisa ya simu wala redio. Kwa hiyo nilihakikishiwa takriban kata nane kwamba nitapewa mawasiliano na sababu kubwa ni nini? Kwamba lile Jimbo liko mpakani kabisa wa Mozambique mpaka ambao una shida ndugu zangu na tujue kabisa mawasiliano ni njia pia mojawapo ya ulinzi ni ulinzi namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lakini mpaka sasa hivi hakuna chochote kinachofanyika kila ukiuliza wahusika hawana hata majibu yaani hata hawaelewi kitu gani wanaweza wakakwambia bwana kweli Mheshimiwa tulipanga hivyo lakini hili jambo halijatekelezwa kwa sababu gani sababu hazieleweki nashindwa kuelewa sasa hapa Bungeni tumekuja kuigiza au kweli tumekuja kufanya mambo kwa maana ya manufaa ya wananchi wetu?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mchungahela mwaka haujaisha.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Sawa lakini angalau hata dalili zionekane.

MWENYEKITI: Najua hasira yako lakini mwaka wa fedha bado haujaisha

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli naelewa lakini angalau dalili zionekane jambo tendering ifanyike uone kwamba kuna tender imefanyika hapa kwa ajili ya huu mradi hakuna, ushaona kuna sehemu nyingine kwa mfano kule kumejengwa mnara ule mnara ni mfupi yaani unakaribia yaani kama ufupi wangu ulivyo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unashindwa kuelewa hivi mnara…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mchungahela muda hauko upande wako.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ahsante naomba kuunga mkono hoja lakini nawaomba wahusika watekeleze haya yote ninayojaribu kuwakumbusha; ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunipa nafasi hii ya kupumua. Nakushukuru wewe pia kwa kunipa nafasi ya kuchangia mchango wa mapendekezo na bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kuwa, pato la Tanzania kwa maana ya pato la nchi limekuwa likiongezeka kwa wastani wa asilimia 4.9, wastani ambao ni pungufu kwa 1% ya wastani ule tuliokuwa tumeukusudia. Ongezeko hili limechangiwa na sekta mbalimbali. Sekta zilizosaidia kuchangia ongezeko hili ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Sanaa na Burudani imechangia kwa asilimia 19.4; Sekta ya Umeme imechangia asilimia10; Sekta ya Madini imechangia asilimia 9.6; halikadhalika Sekta ya Habari na Mawasiliano imechangia kwa asilimia 9.1. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango huo mzuri kwenye hizo sekta, bado kuna sekta muhimu sana za kiuchumi ambazo zenyewe zinategemewa kuwa ndiyo nyenzo za kufanya pato la Mtanzania au pato la nchi likue kwa haraka, lakini sekta hizi hazikukua katika kiwango kinachoridhisa. Sekta hizi zimechangia mchango kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Elimu ni asilimia 5.1; Sekta ya Viwanda imechangia kwa asilimia 4.8; halikadhalika Sekta ya Kilimo imechangia kwa asilimia 3.9; Sekta ya Biashara kwa asilimia 3.5; na Sekta ya Fedha na Bima imechangia kwa asilimia 4.9. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hizi ni muhimu sana kama nilivyosema kwa ajili ya ukuaji wa pato la Taifa. Kama kungekuwa na jitihada za kuhakikisha kwamba sekta hizi nilizozitaja hapo ambazo ni muhimu katika ukuaji wa pato la Taifa zingeangaliwa au kupewa attention ya kutosha, bila shaka hali ya uchumi ingekuwa imekua zaidi ya hali iliyoko sasa.

Mheshimiwa Spika, ili tuendelee tunahitaji sekta hizi zikue zaidi kiasi cha kuwezesha wastani mzima wa pato la Taifa kukua kwa angalau 8% na kuendelea. Hivyo ndiyo hali halisi ilivyojitokeza katika nchi nyingi sana zilizoendelea au zinazoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufanikiwa au kutokufanikiwa kunatokana na sababu, na sababu hii ni jinsi tafsiri iliyopatikana kwenye sekta hizi nilizozitaja kwenye mpango ule: Je, mpango ule umetafsiri nini katika sekta hizi? Kwamba inajua kitu gani kuhusiana na hizi sekta? Kwa mfano, ukuaji wa elimu, tafsiri sahihi ya ukuaji wa elimu, lazima iwe kama ifuatavyo: Kwamba nchi yenye ukuaji wa elimu basi itakuwa na rasilimali watu bora ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji; pia itakuwa na watu wenye fikra pevu; na halikadhalika ina watu wastaarabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri ya ukuaji wa viwanda ni nini hasa? Soko la uzalishaji linaonekana hapo katika tafsiri ya ukuaji wa viwanda. Ukuaji wa viwanda pia unatafsiriwa na ukuaji wa vitu vilivyozalishwa kama vile madini, mazao ya kilimo, mazao ya misitu, mazao ya uchumi, mazao ya uchumi wa bluu na mazao ya mifugo. Pia sekta hii ukuaji wake unatafsiri kodi iliyokuwa rafiki kwa maana kama kodi ni rafiki, inaweza ikaonekana waziwazi katika ukuaji wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa biashara pia unachangia sana katika kuenenda, yaani kuonesha jinsi gani uchumi unatakiwa uwe. Tafsiri sahihi ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa biashara pia unachangia sana katika kuenenda, yaani kuonesha jinsi gani uchumi unatakiwa uwe. Hapa tafsiri sahihi ni nini? Tafsiri inaonyesha kwamba, kama biashara imekuwa hapa kuna suala la ukuaji wa uwekezaji. Hali kadhalika, kuna ukuaji wa pato la Serikali kupitia vyanzo vya kodi ikiwa ni pamoja na leseni pamoja na tozo. Vilevile pato la mtu mmoja mmoja linakuwa linajionyesha hapa, hii ndio tafsiri inayopatikana katika ukuaji wa biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna uwezo wa mtu mmoja mmoja katika kufanya manunuzi yaani purchasing power, inaonekana hapa. Halikadhalika, ongezeko la bidhaa bora, ambazo zenye kuweza kuleta ushindani, mnunuzi ana uwezo wa kuchagua bidhaa anayojisikia. Haya yote yanatokana na ukuaji uliokuwa bora wa biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa fedha na bima tafsiri yake ni nini pia? Tafsiri yake ni kwamba, kuna ongezeko kubwa la mtaji, lakini kuna kuimarika kwa biashara pia na uwekezaji. Vilevile inaonesha hapa kuna mikopo shindani ambapo benki zinashindana kuweka riba ya chini kabisa ya mkopo, kiasi kwamba mlaji au mtumiaji wa mkopo ule anachagua wapi aende akachukue. Hali hii inaleta athari kubwa katika pale ambapo yeye atawekeza, halikadhalika ni kuwezesha uchumi wote wa nchi hii kwa ujumla au nchi husika kukua kwa kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa kilimo na wenyewe una athari zake ambazo una tafsiri sahihi, ambazo tafsiri hizi zinatakiwa pia zionekane wakati tunatengeneza plan au tuna-plan bajeti. Ongezeko la uzalishaji linaonekana pale, pia bei nzuri ya bidhaa zile zilizozalishwa. Pia kuna kinga ya bidhaa na bei, hapa kinga ni nini? Maana yake kwamba kile kilichozalishwa, kama kunatokea changamoto ya uzalishaji, kwa mfano, mvua, maana yake changamoto hii inaweza ikafidiwa kwa ile kinga iliyowekwa pale kwa maana ya bima. Vile vile hata kama bei itashuka, pia bei ile itafidiwa na bima ile, kwa maana hiyo kinga hii itakuwa imesaidia. Hizi ndio tafsiri za msingi kabisa ambazo zinatakiwa zi-reflect katika mipango yetu. Kama mpango wowote ule hauwezi ku- reflect tafsiri ya mambo haya basi ni kiasi kidogo sana tutaona kuna ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja, lakini na pato la Taifa ukuaji wake utakuwa mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojaribu kuanza kusema kule mwanzo, tafsiri hizi lazima zionekane katika mpango na mpango ambao utazalisha bajeti. Kwa sababu hiyo Mpango lazima uzungumze waziwazi products zote zile zinazotengenezwa soko lake liko wapi. Kama mpango hauonyeshi soko basi ni kama vile mpango huu umefeli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta mbalimbali za habari na mawasiliano ambazo zimeonyeshwa pale katika zile sekta zilizochangia maendeleo au ukuaji wa pato la Taifa, zilionyesha kama kwamba zimekua kwa kiasi kikubwa. Pamoja na ukuaji ule kwa sababu Sekta hii ya Habari na Mawasiliano ni sekta unganishi tu, ni sekta ambayo haiwezi kutoa athari yake moja kwa moja katika pato, kwa maana vile vyanzo ambavyo ni muhimu nilivyovitaja vinaunganishwa na sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumeonekana pia ongezeko la madini, lakini athari ya madini haiwezi kujionyesha moja kwa moja kutokana na hali ya sasa ya uchumi ulivyo, kwa sababu madini haya tunauza ghafi. Kama tungekuwa tumeyauza yakishakuwa processed bila shaka hali ya uchumi wa sasa hivi au ongezeko la pato la Taifa ingekuwa ni kubwa kuliko hali ilivyo sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojaribu kuzungumza pale, mpango huu wa sasa hivi kwa mfano, umeonesha changamoto nyingi. Changamoto mojawapo ni kutokuonesha masoko ya product ambazo zinatokana na uzalishaji. Mfano ni uzalishaji wa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, kengele ya pili.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma kwa kutuweka hai, lakini nikushukuru wewe kwa kunipa fursa hii ya kuchangia pia naomba nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniamini, naomba pia niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Lulindi kwa kuniombea dua kuniwezesha kutimiza malengo yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote niseme kwamba sina deni kwa Wizara yoyote ile, nasema hivi kwa sababu kwa kadri jinsi walivyokuwa wananipa ushirikiano mara zote nilipokuwa nikihitaji chochote mara zote nilivyoomba msaada wamenipa ushirikiano wa kutosha na ninauhakika kwamba wataendelea kunihakikishia kwamba nitakwenda kuwaomba misaada pale nitakapohitaji kwa maana hiyo ndio maana ninasema sina deni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo sina maana ya kwamba hawataniona, wataniona sana kwa sababu jukumu nililopewa na wana Lulindi ni kuhakikisha kwamba ninawaletea maendeleo pale kwao na maendeleo hayawezi kuja hivi hivi kwa mimi kusimama tu, ina maana kwamba lazima niende kila Wizara kuwaomba hayo maendeleo. Nawaomba msinifukuze, nikija mnikaribishe ndugu zangu, ninyi ndio wenye kunisaidia jukumu hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi Jimbo langu lina uhitaji mkubwa sana kwanini ni Jimbo lina historia na viongozi wakubwa kabisa wa nchi hii, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa aliyekuwa Rais wa nchi hii ndiye nyumbani kwake kwenye Jimbo hili na usingizi wake wa milele umelala pale Lupaso. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuna kila sababu ya kufanya eneo hili liwe na hadhi inayostahili, mimi peke yangu kama Mchungahela sitaweza ndugu zangu naomba ndugu zangu mnisaidie kuhakikisha kwamba Mkapa anapata stahiki yake, lakini Mheshimiwa Anna Abdallah mwanamke shupavu kabisa katika hii nchi amepigania nchi hii, amejitoa kwa nguvu zake, amelitumikia Taifa hili kwa uzalendo mkubwa kabisa, nyumbani kwake ni Jimbo la Lulindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba sana ndugu zangu mumpe heshima Mama Anna Abdallah kwa kumwezesha kila kitu ambacho kinaweza kikaonekana pale watu wakaona kwamba hapa ni nyumbani kwa Anna Abdallah. Ninayo kila sababu ya kuwaomba ndugu zangu Wabunge kuna baadhi yenu hapa mmejinasibu sana kwamba mmefanikiwa kupata miradi mingi sana katika maeneo yetu basi mkimuona Mchungahela anapewa miradi mingi msiwe na jealous ya namna yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba sana sana sana mniunge mkono kwa sababu kuna kila sababu sisi tunahitaji upendeleo na upendeleo huu ni wa umuhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine sababu iliyotufanya tumechelewa na mpaka kuhitaji upendeleo ni kwamba eneo letu limejishughulisha sana na shughuli ya kuwasaidia wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika, baada ya kutumia muda mwingi sisi kujishughulisha na masuala yetu ya kimaendeleo kulijenga jimbo lakini shughuli zetu za kawaida tulijishughulisha sana kuwasaidia sana hawa ndugu zetu wakati tukifanya hivyo tumechelewa kupata maendeleo ya kutosha, kwa hiyo, jamani tunayo kila sababu ya kuonewa jicho la huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hapo kama nilivyosema TAMISEMI ni Wizara muhimu sana, mara nyingi sana tunaweza tukasema kama ni engine ya bajeti zote ikitumika vizuri tunaweza tukawa na mafanikio makubwa sana kwenye hii nchi na hali hiyo imejitokeza mwaka jana kwa kadri tulivyoona tuliwekewa miradi mingi sana katika maeneo yetu halikadhalika bajeti hii ya mwaka huu inaelekea mwelekeo huo huo, kitu kimoja tu ninawaomba ndugu zangu ambalo tuna jukumu la kufanya kuisimamia hii miradi katika kiwango kinachostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado hatujafanya vya kutosha kusimamia hii miradi, tunalo jukumu la kuhakikisha miradi hii inasimamiwa na ikaweza kunufaisha wananchi kizazi chetu kinachokuja huko mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia elimu ambayo ndio msingi wa Maisha kwa kiwango kikubwa kabisa unatekelezwa na TAMISEMI, lakini utekelezaji wake kwa hali ya sasa ilivyo kwamba kuna baadhi ya maeneo kuna malalamiko mengi sana kwamba utekelezaji unachelewa. Ninaomba kutumia vyombo vyetu husika ambavyo vinaweza kutusaidia kwa namna moja au nyingine kwa mfano TAKUKURU iweze kuweka jicho katika miradi hii, TAKUKURU isisubiri mpaka waambiwe na mama kwamba jamani kuna suala la kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawomba sana, sana, sana waweke jicho, lakini chombo kingine cha audit unit ninaomba sana sana mara hii ilikuwa ni kipindi cha kutengeneza audit specials nyingi sana katika maeneo yetu huko kusudi angalau kuwatisha hawa watendaji ambao wenye nia tofauti na mahitaji hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hapo nizungumzie suala la Afya kwenye Jimbo langu nina Kata 18, lakini kituo cha afya kinachofanya kazi vizuri katika jimbo zima ni kimoja tu, kuna vituo vingine viwili ambavyo vilishajengwa havijaisha, lakini pia kuna Kituo cha Nagaga ambacho kinahitaji fedha kumalizia. Katika fedha shilingi 500,000,000 zilizotolewa kituo hiki kilipewa shilingi 400,000,000 peke yake na Kituo cha Chungutwa pia kilipewa shilingi 400,000,000 peke yake hivyo kufanya baadhi ya maeneo au baadhi ya miundombinu inayotakiwa katika hivi Vituo vya Afya kutokukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, alivyopita Makamu wa Rais alituahidi kwamba tushirikiane na TAMISEMI kuhakikisha kwamba tunaangalia ile fedha iliyopungua shilingi 100,000,000 kwa Nagaga na shilingi 100,000,000 kwa Chungutwa inapatikana kwa ajili ya kukamilisha Vituo vya Afya, nasikitika mpaka sasa hivi Mheshimiwa Waziri fedha hii bado haijapatikana licha ya kuwa tumewasiliana mara kwa mara na Wizara yako, sikulaumu lakini najaribu kukumbushia naomba hii shilingi 100,000,000 ya Nagaga ipatikane na shilingi 100,000,000 ya Chungutwa kusudi tuweze kufanikisha ukamilishaji wa Vituo vya Afya hivi, angalau Lulindi na yenyewe ionekane kwamba imepata vituo vya afya vya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo mengi sana ya kuzungumza, lakini nikijaribu kuangalia sana naona kama yataingia kwenye lawama wakati mimi nilishajielekeza kusifia Wizara zote katika nchi hii na Mawaziri wote, kitu ninachoweza kusema kwa sasa hivi naomba ushirikiano kwa Wabunge wote pale nitakapokuja kwa namna moja au nyingine kuomba msaada wa kunishauri jambo au kunisaidia jambo mnisaidie…

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kuunga mkono hoja asilimia moa moja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Pia nikushukuru wewe kwa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze moja kwa moja kwa kusema kwamba Maafisa Maduhuli kwa maana ya Wakurugenzi wanalo jukumu kubwa sana la kuhakikisha kwamba kila senti inayopitia katika mikono yao kwa maana ya halmashauri iko katika mikono salama. Jukumu hili ni la kisheria na linawataka wao kuhakikisha kwamba wanafanya kila kinachowezekana kuhakikisha kwamba fedha ya Mtanzania au kwa maana ya fedha ya wananchi inalindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu gani? Mimi kama Mjumbe katika Kamati ya LAAC, tumekuwa tukihojiana na halmashauri mbalimbali. Katika halmashauri 34, tuliweza kuhojiana na Kamati nne ambazo zilifanyiwa ukaguzi maalum kwa maana ya special audit. Tulivyohojiana na Kamati hizi, tulikuta kwamba kuna upotevu wa fedha nyingi sana ya Serikali. Kwa mfano, katika halmashauri nne, moja wapo ikiwa ya Dar es Salaam kwa maana ya Ubungo, Kigamboni, Ilemela pamoja na Iringa. Halmashauri hizi kwa pamoja zilipoteza takriban shilingi bilioni 9.055 kama ifuatavyo: -

(a) Halmashauri ya Ubungo ilipoteza takribani shilingi bilioni 4.9;

(b) Halmashauri ya Kigamboni ilipoteza shilingi bilioni 1.1;

(c) Halmashauri ya Ilemela ilipoteza shilingi bilioni 2.9; na

(d) Halmashauri ya Iringa ilipoteza takribani shilingi milioni 124.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla ndiyo kama hiyo amount niliyoisema hapo. Fedha hizi zimekuwa zikipotea vipi kwa namna moja au nyingine, kunakuwa na njama zinazofanyika kuhakikisha hizi fedha zinapotea. Njia mojawapo ni ya kurekebisha au kubadilisha miamala pamoja na tarakimu za ankara. Njia nyingine ni ya kufuta ankara pamoja na miamala hiyo na njia nyingine pia ni ya kuweka miamala ambayo haistahili maana yake miamala ambayo siyo sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa ni nini? Kwa kufuta miamala hiyo lakini pia na kurekebisha tarakimu za miamala pamoja na ankara kunakusudia wao kupata kiasi kidogo kwenye ripoti, kwamba ionekane kuna fedha ndogo kwenye ripoti lakini wakiwa wana fedha nyingi mkononi, hivyo kuwafanya waweze kutumia fedha hii kwa makusudio ambayo hayakukusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye hilo, ni kwamba ile ya kuweka miamala isiyostahiki, lengo ni kufanya financial statement kwa maana ya ripoti iwe impaired, yaani ionekane kwamba haina sifa ya kuweza kutumika wakati ikihitajika, kama mtu anashtakiwa. Kwa hiyo hayo yote tunaona kwamba ni makusudio ovu ambayo yanatokana na watendaji ambao siyo waaminifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha hilo, kuna jambo lingine ambalo limeashiria pia upotevu mkubwa wa fedha. Zile pale zilikuwa tayari zishapotea lakini hizi ni kiashirio cha upoteaji. Kwa mfano, ukienda moja kwa moja kwenye halmashauri ambazo nimezitaja, kwa Halmashauri ya Ubungo kwa mfano. Kumekuwa na ubadilishaji wa miamala yenye thamani ya takribani shilingi milioni 156. Halikadhalika kumeripotiwa madeni hewa kwa maana ya madeni ya uongo ya takribani shilingi milioni 976. Vilev vile kumeripotiwa pia madeni yasiyokuwa na viambatanisho au madeni yasiyokuwa na justification takribani ya shilingi bilioni 1.076.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mweka Hazina wa Halmashauri ya Ubungo kwa wakati huo, jina tunamhifadhi yeye alimdanganya Auditor kwa kusema kwamba amekusanya takriban shilingi bilioni 33.4, lakini kiuhalisia baada ya kufanya reconciliation ikaonekana kwamba ameweka benki kiasi cha shilingi bilioni 31.4 pekee, hivyo ni kwamba kuna kiasi cha takribani shilingi bilioni mbili ambacho kilikuwa hakieleweki, kimepotea. Inawezekana kwamba kweli alikusanya lakini fedha hii ikawa imetumika isivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika ripoti hiyo hiyo kwenye Halmashauri ya Ubungo ambapo iliripotiwa kiasi cha takribani shilingi milioni 829 ambayo mdaiwa wa halmashauri alikwenda akailipa benki moja kwa moja. Kitu cha kushangaza fedha hii ilitolewa siku hiyo hiyo kwa mfumo wa cash, kwa maana ya fedha taslimu. Sasa hapo unaweza ukaona jinsi gani mambo hayo yanavyokwenda. Kuliripotiwa pia kiasi cha mapato ambacho kilikuwa ni takribani shilingi milioni 623. Fedha hii ilikuwa ni mapato ya halmashauri lakini haikuripotiwa, yaani ilikuwa imeripotiwa pungufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala lingine la adjustment imefanyika, kwa maana ya marekebisho ya miamala. Kwenye Halmashauri ya Kigamboni kulikuwa na marekebisho ya takribani shilingi bilioni 10.8. Kwenye Halmashauri ya Ilemela kulikuwa na marekebisho yanayofanana na hayo ya takribani shilingi bilioni 8.7. Kulikuwa na fedha ambayo imeripotiwa ambayo yenyewe ilikuwa imefutwa kwenye POS kwa maana ya system za ukusanyaji takribani shilingi milioni 554. Halikadhalika kulikuwa na fedha pia imeripotiwa kwamba fedha hiyo haikupelekwa benki, takribani shilingi milioni 627. Kwa ushahidi huu unaweza ukaona ni kwa jinsi gani fedha za Serikali zinavyopotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, nini kifanyike? Kwa hali ya sasa hivi jinsi ilivyo inaonekana kabisa utaratibu unaofanyika kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa maana ya Auditor, jinsi anavyoripoti haioneshi kama kutakuwa na dalili ya tatizo hili kwisha. Kwa sababu gani? Yeye anavyokwenda kukagua anaenda moja kwa moja kukagua halmashauri, akishakagua yeye anaripoti kwa Bunge kwa maana ya Kamati ya LAAC na Kamati zingine. Akisharipoti pale, anatoa copy kwa Serikali akiiambia Serikali mambo ambayo amekutana nayo lakini kwa kuishauri marekebisho yafanyike wapi na wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, akisharipoti huku LAAC, sisi kama wasimamizi wa Serikali tunafanya majadiliano kama hivi na mwisho wa siku hatuna maamuzi ya kufanya ya kumchukulia mtu hatua. Yaani tumekuwa hatuna meno. Kinachofanyika sasa, sisi tunaishauri tena Serikali, tunawaambia kwamba fanyeni marekebisho, chukueni hapa, fanyeni hapa. Jambo ambalo ni kama vile mtoto aliyekosea, jirani amekosewa halafu anamwambia mwenye mtoto amuadhibu mtoto wake kwa kosa alilolifanya. Sidhani kama kitu kama hicho kinaweza kikafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa hali hiyo, tatizo ni nini? Nashauri kama tatizo ni sheria, naiomba Serikali kufanya jitihada ya kuileta hiyo sheria hapa kusudi tufanye mchakato wa kuirekebisha, kusudi Bunge liwe lina maamuzi sahihi ya kuweza kumwajibisha mtu yeyote yule au chombo chochote kile ambacho kimekutwa na ubadhirifu wa fedha za umma, la sivyo tutakuwa tukiongea hapa kwa mtindo huu na ndivyo ilivyo miaka nenda, rudi tunakuwa tukisema hapa fedha zinapotea, fedha zinapotea, hakuna action yoyote inayochukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, unasema kwamba TAKUKURU waende kufanya uchunguzi, wanaenda kufanya uchunguzi vipi wakati tayari uchunguzi ulishafanyika. Kwa mfano, uchunguzi uliofanyika wa special audit. Ule ni uchunguzi sahihi ambao una ushahidi wa kuweza kumpeleka mtu mahakamani. Inakuwaje uchunguzi unaostahili kumpeleka mtu…

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mchungahela kwa mchango mzuri.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma ambaye ametusaidia mpaka hivi sasa tumekuwa tukitimiza majukumu yetu. Lakini pia niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Lulindi kama nilivyowahi kufanya siku zote kwa kuweza kunisaidia kuniombea dua hivyo kuhakikisha kwamba matarajio yao tunayatimiza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba Wizara hii ni Wizara muhimu sana katika nchi hii, lakini hata nchi yoyote ile duniani, kama haujajipanga vizuri kwenye Wizara hii ya muundo huu yenye viwanda basi wewe upange kwamba unakaribia kufeli. Nashukuru kwamba kwa namna moja ama nyingine kumekuwa na uthubutu mkubwa sana kutaka Wizara hii ifanye kazi kwa kadri tunavyotarajia, lakini bahati mbaya tumekuwa na mtazamo ambao sio sahihi katika kuhakikisha kwamba Wizara hii inapewa uhalisia au inapewa hadhi inayostahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu gani, ukiangalia bajeti ya Wizara hii ni bajeti finyu sana, lakini ukiangalia umuhimu wake utakuta kwamba hii Wizara ina umuhimu mkubwa kwa sababu biashara ipo kwenye Wizara hii, sekta ya uzalishaji mali nyingine kwa maana ya viwanda ipo katika Wizara hiyo, lakini sekta ya ujasiriamali pia inashughulikiwa kikamilifu katika Wizara hiyo na sekta ya uwekezaji pia. Sasa ukiangalia sekta ya biashara, uwekezaji, ujasiriamali, na viwanda ni kama vile ni Wizara nne tofauti ambazo zimewekwa katika Wizara moja kwa maana hii unaweza ukaona kwa jinsi gani Wizara hii ni muhimu sana katika mhimili wa uchumi lakini uzalishaji na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama nilivyotangulia ukiangalia majukumu ambayo Wizara hii imepewa yameji- limit kwenye uratibu tu yaani Wizara hii haijajielekeza katika utekelezaji, kuna mambo mengi sana ambayo ni ya msingi sana katika kuhakikisha nchi inakwenda ambapo kama Wizara hii ingepewa jukumu hilo hayajapewa na hasa hasa tukiangalia kwa mtazamo huo inakuwa ni vigumu sana kwa Wizara hii kujiendesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninachoomba kwa ujumla tunatakiwa wote sisi kwa maana ya Wabunge tukae pamoja na hii Wizara tuisaidie, itazame katika mtazamo sahihi, iwe ni Wizara sahihi ya uzalishaji lakini ni Wizara ya kibiashara lakini ni Wizara ya kiuwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali iliyopo sasa hivi imekuwa kama na Wizara inayojishughulisha na masuala ya uchuuzi tu, jitihada kubwa ambazo zinafanywa na Mheshimiwa Rais kwa namna moja ama nyingine zinaonekana, lakini ninahofia kwamba hivi jitihada zinaweza zisifike popote kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ya Wizara hii, lakini ufinyu wa utendaji kazi kwenye hii Wizara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninawaomba sana ndugu zangu watu wa Wizara, lakini wadau wengine naomba tuishughulikie hii Wizara iwe na muonekano sahihi wa Wizara ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo nilitaka kulizungumzia hapa linahusiana na vikwazo vya Wizara hii kuna nyenzo muhimu sana ambayo Wizara hii kama kweli tunataka ifanye kazi nayo ni blueprint. Blueprint ni assurance kwa wafanyabiashara au wawekezaji kuja kuwekeza, hatuwezi kuwaambia tu kwa maneno kwamba mje muwekeze wakati hakuna sheria zinazo wa-assure kwamba wakija hapa mali zao zitakuwa guided, lakini pia uwekezaji wao utakuwa ni wenye tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kuna changamoto nyingi sana kwenye blueprint ukiangalia kwa mfano masuala ya kodi, kodi kwa mfano ya VAT ukiangalia unaona kwa jinsi gani inavyoathiri na kuwafanya wawekezaji washindwe kuweka fedha zao, tulipotembea kwenye shughuli za kikamati kwa mfano Dar es Salaam kwenye Kampuni ya ALAF na ile kampuni nyingine sikumbuki vizuri ambayo wanajishughulisha sana masuala ya uzalishaji wa mabati na aluminum kwa ujumla wanalalamika kwamba wanaidai Serikali VAT kwa takribani shilingi bilioni 20 ambazo zilitakiwa zirudishwe…

(Hapa kengele ililia kushiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: ...kwa makampuni hayo mawili tu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mchungahela, ahsante sana.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahante naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia kupitia njia hii ya mchango wa maandishi kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita kwenye maeneo mawili yanayoambatana pamoja na utalii wa tiba (medical tourism) na utalii wa kibiashara (business tourism).

Mheshimiwa Spika, maeneo haya mawili ya sekta ya utalii yanategemea sana jitihada kutoka kwenye sekta nyingine kama vile sekta za afya, sekta ya ujenzi, sekta ya ulinzi, na sekta ya biashara. Hivyo Wizara ni lazima iwe na mashirikiano na Wizara za Ujenzi, Afya, Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mambo ya Nje, Ulinzi na Mambo ya Ndani. Lengo ni kuona jinsi gani mipaka inatumika kama fursa, badala ya kuichukulia kama zao la laana na uadui.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka miundombinu ya Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda kuwezesha utekelezaji wa utalii wa tiba (medical tourism), lakini pia nchi yetu ina mipaka, mkakati inayozalisha majirani ambao ni soko kubwa kuwezesha utekelezaji wa utalii wa biashara (business tourism). Mipaka inaleta wateja wa maeneo hayo mawili ya utalii wa tiba na utalii wa biashara.

Mheshimiwa Spika, nchi kama vile Malawi, Mauritius, Mozambique, Comoro, Seychelles, Zambia, Congo, Rwanda, Burundi, Somalia, Uganda, Sudan, Somalia na Kenya ni muhimu katika utekelezaji wa utalii wa biashara.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nikushukuru, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunijalia afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu katika Wizara ya TAMISEMI utajikita sana katika mambo matano. Mambo ambayo nitajitahidi kuchangia kama muda utanifaa au ntapata muda wa kutosha nitachangia kuzungumzia ufinyu wa nguvu kazi, nitachangia kuhusiana na mifumo ya kazi, nitachangia pia kuhusiana na changamoto ya kimaadili, nitachangia pia kuhusiana na tatizo la ajira na jinsi ya kulitatua lakini pia nitazungumzia ushauri jinsi gani tunaweza tukatatua baadhi ya changamoto kama muda utanitosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba Wizara ya TAMISEMI ni Wizara kubwa lakini ni Wizara muhimu sana na Wizara hii ni mtambuka. Pamoja na umuhimu wake na ukubwa wa Wizara hii kama Wizara nyingine kwenye nchi hii zina changamoto. Changamoto kubwa iliyoko katika Wizara ya TAMISEMI iko katika ufinyu wa nguvukazi. Licha ya kwamba kuna changamoto nyingine lakini eneo hili naliona ni eneo ambalo lina sumbua sana kiasi cha kufanya kwamba hata utekelezaji wake wa majukumu ukawa hauwezi kwenda sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida iliyoko hapa kuna uchache wa watendaji lakini hata wale walioko baadhi yao ni wachache tu ambao ni bora kwa maana ya kwamba quality. Hata hao wenye quality bado baadhi yao wanakosa weledi. Hali hii inasababisha changamoto nyingi zikiwapo ni pamoja na hasara zinazojitokeza katika maeneo mbalimbali hususani katika maeneo ya walaji kwa maana ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi inayokwenda kule kutokana na changamoto nilizozigusia hapo zinasababisha kusimamiwa na watendaji ambao baadhi yao hawana weledi lakini wengine hawana sifa lakini hata ufahamu wa jinsi ya kufanya hiyo kazi aliyotumwa inakuwa shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na u-sensitivity wa taarifa ambazo nitazitoa sitataka kuzungumza in details hizi taarifa. Nitazungumza tu generally. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kuna watu wamepewa kazi ilikuwa ni ya injinia lakini amepewa mtu wa certificate na hana uelewa wa kufanya kazi hiyo, hali ambayo imepelekea kutokea na hasara kubwa katika usimamizi wa miradi hususan katika miradi ya elimu pamoja na miradi ya afya. Kama nilivyosema sitataka kwenda kuingia kwenye details ninazungumza tu generally ninafikiri hizi details nitazituma kupitia mchango wa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ya mifumo pia, mfumo unaotumika hapa TAMISEMI, mifumo ya kifedha kwa mfano haioani, hashirikiani, haisomani. Unaweza ukakuta kuna taarifa zinatakiwa zipelekwe zinakwenda taarifa ambazo si sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika kumekuwa na changamoto ya watendaji kukaidi taratibu za utekelezaji wa majukumu yao, pia kukaidi maelekezo kutoka kwenye mamlaka zinazowatuma. Pia, kama nilivyosema, kwamba nahitaji kuzungumzia kidogo kwenye tatizo la ajira. Hapa naomba kidogo kama ushauri. Kwa bahati nzuri tulikuwa na ajira mwaka jana au muhula uliopita, zile ajira kwa kweli zimetuletea changamoto kubwa sana Wabunge, zimetuletea changamoo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani? maeneo yote takribani ya vijijini kuna shida ya ajira; na ajira zimetangazwa na wengi wamekuwa na matumaini kwamba kwa namna moja au nyingine wanaweza wakazipata lakini kilichotokea ni kwamba kuna maeneo hawakupelekewa kabisa; yaani kwamba watu hawakuajiriwa lakini kuna maeneo mengine wameajiriwa idadi ya watu wengi. Hatutaki kuzungumza kwamba wapi ilikuwa vipi lakini kwa mfano tu mimi Jimboni kwangu katika ajira zote zilizotoka za elimu pamoja na shule ni watu wawili tu ndio walipata ajira ile, kwa kweli sio fair ilhali kuna idadi ya watu wengi sana ambao wamekosa ajira na lakini wamesoma na wanatarajia pia na wanaomba. Kwa hiyo unapopeleka watu wawili katika jimbo zima sidhani kama huu mgawanyo wa cake uko sawa, naliomba jambo hili tuliangalie kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri kwamba katika hizi ajira 21,000 basi tutenge ajira 5,000 zibaki kwenye wizara kama msawazo lakini zile ajira nyingine yaani kwamba 21,000 ukitoa 5000 hizo zitakazobaki tuzigawe kimajimbo. Tuangalie proportional amount ambayo kila jimbo inaweza ikapata, kila jimbo lipate kwa kiwango kadhaa, halafu zile zingine 5,000 ndizo ziende katika kufuata hizo taratibu ambazo mlizfanya huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia bajeti hii ya Uwekezaji, lakini kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake kubwa za kutengeneza ustawi wa nchi hii.

Mheshimiwa Spika, naomba niwaase wasaidizi wake kwenda na kasi yake, ni vyema wakajibidisha kumwelewa, kufahamu matamanio yake, maono yake na matokeo anayoyatarajia. Kwa jitihada zake binafsi amepandisha idadi ya watu/makampuni yenye nia ya kuwekeza na hivyo kufanya TIC kusajili wenye nia ya kuwekeza kufikia 1,282 kwa muda wa miaka mitatu pekee. Kama wenye nia hawa hawa wote wangefanikiwa kuwekeza wangeingiza kiasi cha mitaji cha Dola za Marekani bilioni 15, sawa na shilingi trilioni 36 za Kitanzania.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika kwa miaka 23 toka mwaka 1996 hadi sasa TIC iliweza kusajili jumla ya wawekezaji 12,381 ambao wangeweza kuingizia mtaji wa dola bilioni 117 sawa na shilingi trilioni 281. Kama angalau nusu ya wawekezaji hao wangewekeza, wangeweza kuchangia mitaji ya dola bilioni 59, sawa na shilingi trilioni 140 za Kitanzania.

Mheshimiwa Spika, hapa naeleweka ninakoelekea, maana yangu ni kwamba wawekezaji wanakuja na dola, hivyo tungekuwa na dollar reserve ya kutosha na haya malalamiko ya dola yasingekuwepo; shillingi yetu ingeimarika sana dhidi ya dola na pia multiplier effects ya mitaji hii mikubwa ingeonekana kila pahali (sekta) na kuwa na uchumi imara, kwa mfano kila shilingi moja inaongeza shilingi tano kwenye mzunguko wa matumizi (one shilling creates five shillings spending) hivyo uwekezaji wa mitaji ya shilingi trilioni 140 ingetengeneza shilingi trilioni 700 kwenye mzunguko wa matumizi.

Mheshimiwa Spika, kwa uoni wangu jitihada hizi kubwa za Mheshimiwa Rais zimekuwa zikikwamishwa na watendaji wasioelewa tafsiri sahihi ya maono ya Mheshimiwa Rais kisha kutafsiri maono hayo kwa vitendo na mara nyingi ni zao la uvivu, uzembe wa kutowajibika.

Mheshimiwa Spika, ubora wa mambo utaonekana kwenye matokeo, mipango yetu ya mwaka, miaka mitano, kumi na kadhalika haioneshi matokeo chanya na tafsiri yake ni kwamba watekelezaji hawaimbi wimbo mmoja na wapangaji.

Mheshimiwa Spika, naomba ieleweke kwamba mipango imekuwepo muda wote, either ikisimamiwa na Wizara ama ikisimamiwa na Tume, hivyo Tume ya Mipango sio jambo jipya kwani kuwa na matarajio mazuri kwa kigezo tu cha kubadilisha utaratibu wa nani asimamie mipango bila kubadilisha mindsets zetu huko ni kujidanganya, yatubidi sote wapangaji na watekelezaji tubadilishe mitazamo yetu ya jinsi ya kuwajibika. Kama tabia yetu ya kutofuatilia mipango yetu itaendelea, basi hakuna kitakachobadilika.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, lakini nikushukuru wewe pia kwa nafasi uliyonipa ya kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza mchango wangu ningependa pia kutoa shukrani kwa Wizara ya TAMISEMI kwa kunielewa baada ya kuwa nimelia muda mrefu humu ndani kutokana na changamoto za Halmashauri yangu. Namshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa kuniletea mtu makini sana pale wilayani kwangu. Ni makini sana huyu mtu, huyu ni Mkuu wa Wilaya anaitwa Mr. Kanuni, hapa ni kanuni kweli kweli, na nafikiri vilio vyangu vilivyokuwa vikifululiza hapa kuhusiana na changamoto zinazojitokeza katika halmashauri yangu zitapungua kwa muda mfupi tu aliokaa Mheshimiwa huyu nimeona matunda yake makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo nianze moja kwa moja na mchango wangu, na mchango wangu utajielekeza katika maeneo mawili; eneo la kwanza litahusiana na masuala ya Wizara ya kilimo, na hapa moja kwa moja nitajielekeza kwenye zao la korosho.

Mheshimiwa Spika, kwa nini ni zao la korosho? Ni kwa sababu zao la korosho limekuwa likituongezea sana pesa za kigeni ambazo ni muhimu sana katika muhimili wa uchumi wa nchi hii. Kwa mfano, mwaka 2017/2018 korosho ililiingizia pato la Taifa dola takribani milioni 500, pesa hizi ni pesa nyingi sana katika uchumi, na imekuwa ikifanya hivyo kwa wastani kiasi hicho hicho kama miaka mitatu minne mfululizo hivi, lakini ninazungumzia suala hili sasa hivi kwamba uzalishaji wa korosho umeshuka kwa kiasi kikubwa sana, jambo ambalo nafikiri tunahitaji kila sababu ya kujiuliza kwa nini kushuka kwa namna hii.

Mheshimiwa Spika, mwaka takribani 2017/2018 kulikuwa na uzalishaji wa korosho wa tani 313,000 hivi, lakini kutoka hapo mpaka kufikia mwaka 2022 kumekuwa uzalishaji ukishuka kwa kiwango kikubwa sana kufikia kutishia amani ya lengo letu tulilojiwekea la kuzalisha tani 700,000 kwa mwaka. Kutoka tani 313,000 mwaka 2022/2023 korosho zilizalishwa kwa tani 186,000 hivyo kufanya mchango wa zao hili kwenye pato la Taifa kushuka kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada kubwa anazozifanya Mheshimiwa Rais kutaka kuboresha zao hili, lakini kumekuwa na mambo ya makusudi kabisa yanayoonekana kuwa ni uzembe unaosababisha kushuka kwa zao hili. Kwa mfano, hivi ninavyokwambia tayari pembejeo zimeshafika ambazo Mheshimiwa Rais kwa jitihada yake kubwa sana aliifanya kuzileta hapa nchini. Nashukuru pia Wizara ya Kilimo, Mheshimiwa Bashe na wasaidizi wake wa karibu walifanya jitihada za kuhakikisha kwamba, pembejeo hizi zinaingia nchini, lakini cha kushanganza mpaka sasahivi hizi pembejeo bado hazijagawiwa. Jambo ambalo linatia shaka kwamba, ni kwa sababu gani hizi pembejeo hazigawiwi licha ya kuwa zimekuja hapa ni mwezi mzima sasa hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo yanatakiwa kutoa pembejeo hii ni maeneo ambayo kwa sasa hivi wanatakiwa wajiandae na masuala ya kupulizia, kwa mfano katika Wilaya ya Masasi, Jimbo la Lulindi, takribani kata zote sasa hivi zinahitaji pembejeo, lakini so far ni kata chache sana wamepewa pembejeo na kuna maeneo mengine tunashangaa unapeleka mfumo uliotumika sasa hivi ambao ni mfumo bora wa kupata idadi halisi ya wazalishaji, lakini coupon zinakwenda, zile coupon hazina idadi ya pembejeo inayotakiwa apewe mzalishaji. Unakuta umeambiwa fulani utapewa pembejeo, unapewa coupon, ukienda pale hakuna chochote. Kwa hiyo, sasa tunashangaa tatizo ni nini?

Mheshimiwa Spika, ni uzembe kama nilivyosema kwa kweli, na hali hii inafanya kuwakatisha tamaa viongozi wetu wakubwa kwa sababu wao wana ndoto ya kuona kwamba zao hili linakwenda vizuri, liendelee kuzalisha, lakini pia liendelee kutoa mchango mkubwa kama ilivyokuwa ikifanya hapo mwanzo kwenye uchumi wa nchi hii. Ni muhimu kwa sababu inapunguza urari, I mean ile deficit ya urari wa biashara. Sasa kama hali itaendelea kuwa hivi kwamba, inashuka kila siku bila shaka hata hiyo faida hatutaiona.

Mheshimiwa Spika, lakini nilitaka niongelee pia kwamba zao hili limekuwa tegemezi sana kwa baadhi ya taasisi katika hii nchi. Ni kwamba pesa nyingi zimekuwa zikitoka kwa mfano, kila kilo moja ya korosho imekuwa ikikatwa pesa kadhaa kwa maana ya tozo kwa ajili ya kuhudumia hizo taasisi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Korosho wanapata shilingi 30 katika kila kilo; Halmashauri wanapata shilingi 65 kwenye kila kilo; Chuo cha Naliendele wanapata shilingi 15 kwenye kila kilo; Chama Kikuu cha Ushirika wanapata shilingi 30 kwenye kila kilo; Chama cha Msingi wanapata shilingi 25 katika kila kilo; Halmashauri inachangiwa pia elimu shilingi 30 katika kila kilo; lakini cha kushangaza hata mfanyabiashara yule anayenunua korosho anachangiwa kwa kusafirishiwab korosho zake mpaka kwenye eneo anakotaka kuzipeleka.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia hapa utakuta kwamba ni zao pekee lenye pesa nyingi sana za tozo, lakini licha ya umuhimu huu zao hili hawa wanaochangiwa wanalidharau kwa maana ya kwamba hawafanyi kazi inayostahili kuhakikisha kwamba zao hili linakuwa bora.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kuna shida hapo na uzalishaji imeshuka, lakini halikadhalika kuna shida ya bei. Mwaka jana ni mwaka ulikuwa very worse, bei ilishuka kwa kiwango cha ajabu kabisa na kama unakumbuka nilishauliza hapa kwamba taratibu gani zinafanyika na Serikali kuhakikisha ile bei inaimarika, lakini mpaka sasa hivi bado hakujawa na majibu yaliyokuwa yanaleta matumaini kwa wakulima kwamba, hizi bei zitapanda au huu uzalishaji utapanda. Kwa kweli ni jambo ambalo tunatakiwa tujitathmini sana kwa umakini kama kweli tunataka kuendeleza zao hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine nililotaka kulizungumzia kwa siku ya leo ni kuhusiana na udhibiti wa mifumo; kumekuwa na mifumo mbalimbali ambayo imetengenezwa so far, ni jambo jema sana kwa Serikali kwa sababu ya nia nzuri ya kutaka kudhibiti mapato ya Serikali kwa namna moja au nyingine katika level mbalimbali, level ya Halmashauri, lakini hadi kwenye Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, mifumo iliyowekwa ni mizuri japo kwa kiasi kikubwa kuna changamoto kwamba tulikuwa tunategemea sana katika suala la uboreshaji paboreshwe katika mfumo wa I mean internal control system, mfumo wa control system. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30, muda wako umekwisha.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, baada ya kusema hayo niunge mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nijielekeze moja kwa moja katika uchangiaji wa hotuba kutokana na ufinyu wa muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba, kilimo ni uti wa mgongo kama ilivyoanza kusemwa hapo mwanzo. Kilimo ni chakula, watu tunaishi kwa sababu ya chakula cha kilimo, lakini kilimo ni biashara. Takribani asilimia kubwa ya biashara yetu ya ndani na ya kimataifa inategemea sana kutoka kwenye mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni uchumi. Takribani asilimia 30 ya Pato la Taifa inachangiwa na mazao kutoka kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ni ajira. Takribani asilimia 70 ya ajira zote za Tanzania zinachangiwa na kilimo. Katika hali kama hii hakuna njia yoyoye tunaweza tukapishananacho kilimo. Tunatakiwa kwa nguvu zote tuwekeze kwenye kilimo ili kuhakikisha kwamba, uchumi wetu unakua, lakini unakuwa imara. Nchi zote zilizoendelea ni kwa sababu, zimefanya mapinduzi ya kilimo na kwa kupitia mapinduzi ya kilimo ndipo unaweza ukaenda kwenye mapinduzi ya viwanda kwa sababu, viwanda na kilimo vinategemeana; kwa nini? kilimo chenyewe kinakuwa ni malighafi ya kiwanda, kwa hiyo huwezi kuzungumzia suala la kiwanda kama kilimo hakiko imara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina shaka na mipango iliyowekwa kwenye kilimo na Mheshimiwa Waziri na timu yake, ameweka mipango mizuri kabisa. Shaka yangu ni jinsi mtiririko wa fedha kutoka kwenye vyanzo hivyo; kwa maana ya vyanzo vya bajeti kwenda katika maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano halisi, muhula uliopita wa bajeti kilimo katika eneo la umwagiliaji kwenye suala la maendeleo kiliwekewa kiasi cha takribani bilioni 46.5, lakini cha kushangaza mpaka Februari mwaka 2020/22 imepelekwa milioni 590 pekee, hivyo kufanya asilimia 1.27 pekee katika suala la maendeleo la umwagiliaji, hasa ukizingatia kwamba umwagiliaji ndilo dira na umwagiliaji ndiyo maamuzi sahihi ya kufufua kilimo na kufanya kiwe bora. Sasa kwa mtindo huo sioni kama kweli tunaweza tukafikia lengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hapo naomba nijielekeze mchango wangu katika kilimo cha nyumbani kwetu; kwa maana kilimo pendwa. Kilimo cha mazao pendwa, mazao ya korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hapo, naomba nielekeze mchango wangu katika kilimo cha nyumbani kwetu kwa maana ya kilimo pendwa, kilimo cha mazao pendwa cha mazao ya korosho. Korosho limekuwa ni zao pendwa, kadri siku zinavyoongezeka limekuwa zao mahsusi kabisa katika matumizi ya shughuli mbalimbali katika dhima za kitaifa na za Kimataifa. Kwa maana hiyo hata wanunuzi wa korosho wamekubali wenyewe kabisa kuwa na hiari kutoa bei nzuri kabisa katika korosho, lakini cha kushangaza ni kwamba bei hii haimfikii mkulima. Kwa maana hiyo Waziri pamoja na timu yake kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba bei halisi inamfikia mkulima ambaye ni mvuja jasho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojaribu kuzungumzia tatizo kubwa la bei linatokana sana katika maeneo mawili, eneo la kwanza ni kwa sababu korosho zinauzwa ghafi huko India pamoja na nchi nyingine za Mashariki. Pia korosho zimezingirwa na wadau waliokosa weledi. Wadau wengi waliozingira kwenye korosho wamekosa weledi kwa namna moja au nyingine. Wako kwa mfano wafanyabiashara ambao wao kwao faida ndiyo msukumo pekee kwenye biashara hii au kwenye sekta hii. Halikadhalika wapo madalali ambao wao wamekaa kwa ajili ya kuwanyonya wakulima na wala hafanyi jitihada kubwa ya kuhakikisha kwamba korosho zinakuwa zao lenye tija kwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango huo.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona na kunipa fursa hii. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kunipa fursa hii pia ya kuongea na nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nahutubia Taifa hapa. Kwa makofi haya naona kwamba Wabunge tuko tayari kusikiliza Hotuba ya Taifa ambayo itatufanya tuitekeleze kikamilifu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo jambo la kulizungumzia ambalo kama sitalisema naona nitakuwa sitaitendea haki nchi hii. Sisi Watanzania, lakini sisi Wabunge ambao tumepewa dhamana hii kubwa ya kutengeneza maono na kutengeneza mwenendo wa nchi hii kwa maana ya uchumi wake, lakini na mahusiano yetu na nchi zingine na ustawi wa nchi hii, kwa kweli tunalo jukumu la kusimamia sana haya tunayoongea na siyo kusema tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia jukumu tulilokuwa nalo, kumekuwa na manung’uniko mengi sana yakijitokeza kwamba hatuna usimamizi mzuri katika bajeti zetu na hiyo inapelekea utekelezaji wa maeneo mengi sana, siyo bajeti hii lakini takribani bajeti zote unasuasua. Sasa ndugu zangu nataka nikwambieni kwamba pesa tunazozitenga hapa, ni nyingi sana, ukichukulia mfano kwenye bajeti hii peke yake kuna takribani bilioni 2.7, hii ni pesa kubwa sana. Ukiangalia kwenye bajeti nzima ni zaidi ya asilimia tano ya bajeti, ni pesa nyingi sana. Kwa hiyo tunayo kila sababu ya kuisimamia pesa hii kuhakikisha kwamba inafanya kazi inayostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu haya tunayo Wabunge, Wabunge ndiyo tumepewa dhamana ya kusimamia pesa hii, wale ndugu zetu wengine kwa maana ya wananchi wa kawaida, hawana nafasi hata kama watataka kufanya hivyo, lakini wanaona kwamba sisi ndiyo watu thabiti ambao tunatakiwa tuifanye hii kazi kikamilifu. Kwa hiyo nawaomba ndugu zangu Wabunge kwa pamoja kabisa na ndugu zangu Mawaziri ambao ndiyo watekelezaji wa haya majukumu ya Wizara zao, tusimamie kikamilifu kabisa hizi bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano kwenye bajeti iliyotengwa mwaka jana, mwaka jana kwa ujumla tulitengewa takribani trioni 2.3 za bajeti hii ya Nishati. Katika kiasi hicho cha pesa kumekuwa na changamoto katika maeneo fulani ya utekelezaji, kwa mfano, Mradi wa Kinyerezi wa kufua umeme ulitengewa takribani bilioni 88.5, lakini katika kiasi hiki cha pesa kiasi kilichopokelewa ni sifuri. Mnaweza mkaona hapo, sasa hatujui ni kwa nini kiasi hiki hakikupokelewa, wakati kuna umuhimu sana wa kupata huu umeme ambao ungetakiwa kufuliwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa REA pia tulitengea bilioni 363, lakini katika kiasi hicho kilichotengwa mwaka jana ni asilimia 59 pekee ndicho kilichopokelewa, lakini utekelezaji wake sasa katika hizo pesa zilizopokelewa ni mdogo sana. Ukiangalia kwa mfano, Kamati inayohusika na masuala ya Nishati ilivyokwenda kutembelea baadhi ya miradi, ilikwenda ikakuta eneo la Pwani ambako kulikuwa kumetekelezwa mradi mmojawapo wa REA ulitekelezwa kwa asilimia 20 tu. Sasa kama utekelezaji ni asilimia 20 kwenye REA, hivi mnafikiria kwamba tunaweza tukaendelea kwa kiasi gani. Hapa tunaweza tukasema kwamba utekelezaji umekuwa ni finyu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukulie katika Mkoa wangu wa Mtwara, Mkoa huu umekuwa na changamoto kubwa sana ya umeme, ni katika Mikoa ambayo tunaweza tukasema ina shida kubwa ya umeme ukiondoa Mkoa wa Tabora. Utekelezaji wake ni mdogo kabisa, kumekuwa na shida ya kubwa sana ya kukatikatika kwa umeme kwa mfano Masasi ukatikaji wa umeme umekuwa takribani mara nne kwa siku. Jambo hili hatuwezi kulivumilia kama kweli tunataka maendeleo ya kweli katika masuala ya kiuchumi. Bajeti iliyopangwa katika Jimbo la Lindi kulikuwa na takribani vijiji 30 ambavyo vilitakiwa kufikiwa na Mradi huu wa REA, kitu cha kushangaza mpaka hivi ninavyosema hata kijiji kimoja hakijafanyiwa utekelezaji wa Mradi wa REA. Sasa ndugu zangu tunaweza kufika kwa mtindo huu kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kuna baadhi yetu tumekuja hapa tumepongeza sana katika hii Wizara. Siyo vibaya kupongeza, lakini je, tukienda katika uhalisia hizi pongezi hii Wizara inastahili kweli, kwa sababu nikiangalia ni katika Wizara ambazo performance yake iko chini kabisa chini ya kiwango. Tukiangalia kama kweli tunahitaji kuendelea na hii Wizara ina-perform chini kiasi hiki katika bajeti zake, nashindwa kuelewa kwa kiasi gani hii bajeti iliyoko sasa hivi itaweza kutekelezwa. Ndipo pale niliposema ndugu zangu Wabunge kwa pamoja, kwa umoja wetu, naomba sana tuisimamie hii Wizara kikamilifu kwa sababu hii Wizara imepewa pesa nyingi sana hatuwezi kuziacha hizi pesa zikapotea kwa mtindo kama huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mradi wa Julius Nyerere kwa mfano, kuna pesa nyingi pale zimewekwa kwa ajili ya utekelezaji, lakini mpaka sasa hivi kitu cha kushangaza ni kwamba mradi huu haujakamilika wakati ulitakiwa at least kwa asilimia 98 uwe umekamilika. Sasa hivi uko kwa takribani kwa asilimia kwa kama 56 hivi, yaani takribani asilimia kama 40 hivi na kitu uko nyuma. Kwa hiyo tunaweza kuona ni kwa jinsi gani najaribu kuzungumza kwamba performance ya Wizara hii siyo nzuri japo kama sisi baadhi yetu tunasifia. Sina nia kuvutana na mtu yoyote, nisije nikaeleweka vibaya. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Issa Mchungahela.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naam.

MWENYEKITI: Nilikuongeza dakika moja, nikifikiri ndiyo unahitimisha lakini naona bado unataka kuendelea kuhutubia Taifa. (Makofi/Kicheko)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekushukuru sana. Naomba sasa baada ya shukrani hiyo, niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, lakini pia nikushukuru wewe kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utakapoanza nimeamua moja kwa moja kuondoa takwimu, kwa maana ya kuhakikisha kwamba mchango huu unaishi kwa muda mrefu miongoni mwetu.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyowahi kuzungumza hapo mwanzo, siku za nyuma, kwamba Taifa hili linakosa uzalendo. Tatizo hili limekuwa ni changamoto kubwa ambayo nafikiri tunahitaji kujitathmini na kuangalia jinsi gani ya kuenenda ili kuhakikisha kwamba, uzalendo unapatikana na mambo yanakwenda kama vile tunavyotarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, licha ya kuaminiwa tulikoaminiwa na wananchi, lakini pia wale walioteuliwa na Mheshimiwa Rais au na watu mbalimbali bado kumekuwa na changamoto, kwamba hatuzitendei haki teuzi hizo, wala hatutendei haki kuchaguliwa huko. Kumekuwa na shida ambayo ni ya wazi inayoonesha upotevu wa maadili, hususan katika taasisi mbalimbali ambazo zinafanya kazi zilizopewa mamlaka ya kutenda kwa niaba ya wananchi au kutenda kwa ajili ya Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu itajielekeza katika taasisi mbalimbali, hizi zikiwapo pamoja na taasisi za halmashauri, lakini na taasisi nyingine za kiserikali. Lengo kubwa ni kuwagusa maafisa masuuli ambao wao ndio wamepewa jukumu la kuendesha taasisi hizi kwa ajili ya ustawi wa nchi na ustawi wa wananchi pia.

Mheshimiwa Spika, uzoefu wangu nilioupata baada ya kujadiliana na kuhoji taasisi mbalimbali, kwa maana ya halmashauri tulizohojiananazo katika kipindi hiki kumeonesha kwamba, maafisa masuuli walio wengi aidha hawajui majukumu yao au kwa makusudi kabisa wameamua kukaidi kutoyatekeleza. Hali hii inasababisha athari nyingi sana, athari ambazo zinajitokeza katika sekta nyingi zilizoko hapa nchini, lakini katika taasisi hizo.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa majukumu waliyopewa maafisa masuuli ambao wao ndio wanaendesha hizo taasisi, majukumu makubwa sana. Majukumu hayo mojawapo kwanza ni kutafuta fedha popote ilipo. Lakini jukumu jingine ambalo afisa masuuli analo ni kuhakikisha kuwa fedha hii aliyoitafuta kwa maana ya aliyoikusanya katika maeneo husika, lakini pia fedha ambayo ameipata kupitia Serikali Kuu na vyanzo vya wafadhili mbalimbali kwamba, fedha hizi zinatumika kama inavyostahiki na matarajio ya walio wengi.

Mheshimiwa Spika, lakini pia, afisa masuuli anahakikisha kuwa anapata mapato kwa kadiri ya jinsi alivyojipangia, kwa maana ya bajeti. Afisa masuuli ahakikishe kwamba, bajeti yake amepata kiasi kinachostahili kwa ajili ya kuiendesha halmashauri au taasisi yake kwa ajili ya ustawi wa wananchi na nchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, afisa masuuli yeye ni msimamizi wa fedha alizokasimiwa kutoka Serikali Kuu au wafadhili mbalimbali; kuhakikisha kwamba fedha hizi zinatumika ipasavyo, lakini pia hazitumiwi isivyokuwa sahihi. Kutokana na uhalisia ulioko sasahivi ni kwamba, maafisa masuuli walio wengi wanalipuuza jukumu hili au tuseme kwamba hawajui kabisa jukumu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maafisa masuuli wamepewa nyenzo nyingi sana, bora na muhimu sana katika kutekeleza majukumu yake. Hata hivyo, inashangaza kwa jinsi gani wanashindwa kutekeleza majukumu haya. Kwa mfano, maafisa masuuli wamepewa mitaji, kwa maana ya nguvu kazi na vyanzo vya kukusanyia mapato hayo. Maafisa masuuli pia wamepewa wasaidizi, kwa maana ya wakuu wa vitengo na wakuu wa idara.

Mheshimiwa Spika, lakini afisa masuuli pia, amepewa mifumo mbalimbali wezeshi ambayo itamuewezsha yeye kufanya kazi kwa umakini na kufanya kazi kwa jinsi anavyotakiwa. Afisa masuuli anacho kitengo cha ukaguzi wa ndani, pia kamati ya ukaguzi wa ndani, anayo pia bodi ambayo inampa ushauri jinsi gani ya kufanya kazi zake. Halikadhalika afisa masuuli kupitia RAS anacho kitengo cha ukaguzi, ufuatiliaji pamoja na tathmini.

Mheshimiwa Spika, hivi vyote vimewekwa kwa ajili ya kumuwezesha afisa masuuli kufanya kazi yake kwa weledi, kama nilivyosema hapo mwanzo. Hivyo, inashangaza kwa nini afisa masuuli anashindwa kuwajibika na kufanya kazi kwa weledi kama si kukosa uzalendo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi kama ni yule mwakilishi aliyepita, yule aliyetoa ushauri hapa, kwa maana ya mchangiaji aliyepita alivyouliza kwamba, kama ingekuwa ni biashara binafsi ambayo mtu anayo kwa resources hizi zote alizopewa afisa masuuli kweli angeweza kushindwa kuifaya kazi yake kwa kiwango hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa ndipo tunapozungumza kwamba, uzalendo katika nchi hii haupo. Sasa, tunayo kila sababu kuhakikisha kwamba tunapambana kurudisha uzalendo.

Mheshimiwa Spika, hali hii ipo katika kila mahali, miongoni mwa wengi waliochaguliwa wanahisi kwamba wakishachaguliwa tu basi kazi yao imekwisha. Wengi hawafikiri kwa niaba ya nchi hii au kwa maslahi ya nchi hii. Walio wengi wanafikiri juu ya maslahi yao binafsi. Wengi tunaendekeza matumbo yetu kwa kweli. kweli tunahitaji kujirekebisha na kubadilika kama kweli tunaitakia mema nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyowahi kusema huko nyuma kwamba, nchi bila wananchi walio bora haiwezi kwenda popote, nchi bila wafia nchi haiwezi kwenda popote. Basi sisi tuliopewa majukumu na madaraka kwa namna yoyote ile tunatakiwa tufikirie jinsi gani ya kufia nchi, na huo ndio uwananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, malalamiko ya ufujaji wa fedha ambazo zinatoka aidha kutoka Serikali Kuu au maafisa masuuli wanazikusanya wenyewe katika maduhuli yao ni mengi sana. Takribani kila halmashauri katika nchi hii ina changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano nilkitolea kwangu kabisa, kwenye halmashauri yangu maana mimi si Malaika na kwamba halmashauri yangu haina shida hiyo; nataka niseme kwamba, ni miongoni mwa halmashauri zenye shida hiyo, tena kubwa. Hivi ninavyosema Mkuu wa Wilaya ametoa maelekezo kwa TAKUKURU kuichunguza Halmashauri ya Masasi DC kwa madai na malalamiko mbalimbali ya ubadhirifu yanayohusiana na fedha za maendeleo ya walizozikusanya, halikadhalika fedha wanazozipata kutoka kwenye vyanzo vingine.

Mheshimiwa Spika, jambo hili si jema. Na ninafanya hivi kwa nia ya kufanya nini, kwamba, tujirekebishe na mimi nikiwapo miongoni mwa hao wanaotakiwa kujirekebisha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. Nakubaliana na maazimio yote ya kamati zote zilizokuja kuwasilisha hapa. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Pili, nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa uhai. Leo kama siku nyingine nilizopata kuchangia namshukuru kwa fursa hii. Pia, niwashukuru familia yangu kwa kunivumilia kwa muda mrefu nikifanya kazi hii ya kuwatumikia wananchi wa Jimbo langu lakini na wananchi wa nchi hii kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, binafsi nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ya kutengeneza ustawi wa nchi hii. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa kama nilivyosema hapo mwanzo kwa sababu kila tunachojaribu kukiongelea kuhusiana na jitihada zake alizozifanya zipo wazi.

Mheshimiwa Spika, mimi binafsi nawaasa wasaidizi wake kwenda na kasi yake. Mheshimiwa Rais amekuwa akienda kwa kasi kubwa kiasi cha kuwaacha baadhi ya watendaji wengine wakiwa wanatambaa. Sasa kama nilivyosema ni muhimu sana watendaji na wasaidizi wake kwa ujumla tukajitahidi kutaka kuangalia na kufahamu kwamba Mheshimiwa Rais ana maono gani na anatarajia nini kutoka kwao, hali kadhalika matokeo ya kile anachokitarajia huko mbeleni ni nini?

Mheshimiwa Spika, ukiangalia ni kama vile sehemu hizi mbili kuna nyimbo hizi mbili tofauti zinaimbwa. Upande huu huku inachezwa nyimbo hii lakini upande mwingine unacheza wimbo mwingine; hakuna correlation. Natofautiana kidogo na wenzangu kuhusiana na suala la Tume hii ya Mipango kwamba labda inaweza ikatutoa sana katika mazingira yetu tuliyokuwa nayo kama sisi hatutabadili mind set zetu; kwa sababu gani?

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kwamba mipango ilikuwepo muda wote, hakuna hata mwaka mmoja ambapo mipango ilisimama. Kilichobadilika ni kwamba mipango hii imebadilishwa katika utekelezaji kwamba nani anaisimamia. Kuna wakati mipango hii ilisimamiwa na Wizara ya Fedha, kwa hiyo Idara ikawa ndani ya Wizara. Kuna wakati pia mipango hii ilikuwa imesimamiwa yenyewe ikiwa na Wizara maalum kabisa ikijitegemea kufanya mipango.

Mheshimiwa Spika, muda huo wote tumeona kwa kadiri mambo yalivyokuwa. Hali kadhalika hivi sasa toka mwaka 2023 Tume ya Mipango pia imerudi ikijitegemea na kuwa ni Wizara kamili kabisa ambayo inashughulika na mipango hii. Kwa hiyo nyakati hizi zote mbili tumepitia, kipindi ambacho Wizara imeshughulika na mipango, lakini kipindi ambacho Tume imeshughulika na mipango. Bado kumekuwa na mapungufu kwa nyakati hizo tofauti, licha ya kama nilivyosema viongozi wetu wakubwa kwa maana ya Marais kwa muda tofauti tofauti, kujitahidi sana kuhakikisha kwamba ustawi wa nchi hii unakuja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo jitihada zao binafsi zilikuwa zikionekana, lakini mipango ile ilikuwa inashindwa kuunganika kutoka kwa wenzetu, watekelezaji. Kwa hiyo kama nilivyosema nafikiri mind set ni muhimu sana katika kuhakikisha tunavuka hapa tulipo. Kusema peke yake kwamba Tume ya Mipango imekuja, kwa hiyo tutakuwa na hali nzuri, huko ni kujidanganya. Tunahitaji ku-change mind set completely kutoka kwa watendaji na wale wanaopanga hii mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikisema kwamba ni kwa nini, ni jitihada binafsi? Ukiangalia kutoka mwaka 1996 mpaka kufikia hivi leo, TIC ilivyoanza kusajili wawekezaji ilisajili takribani watu au kampuni 12,381 zilizokuwa na nia ya kuja kuwekeza katika nchi hii. Tafsiri yake ni nini? Kampuni hizi au watu hawa kama wangekuwa wamekuja wote wangetuletea pesa za Kimarekani takribani bilioni 117. Hizi ukizibadilisha ni pesa nyingi sana. Ni kama shilingi trilioni mia mbili hivi na kitu, ni pesa nyingi mno.

Mheshimiwa Spika, sasa pesa hizi kama zingekuja maana yake nini? Zingeleta mtaji kutoka pesa ya kigeni kuja hapa kwa kiasi cha pesa nilichokitaja hapo. Impact ya hii ingekuwa ni nini? Kungekuwa na vitu mbalimbali vingejitokeza. Kwanza hawa wawekezaji wanakuja na pesa ya kigeni kama nilivyosema kwa maana kungekuwa na pesa ya kutosha kwenye reserve kwa maana ya dola ya kutosha kwenye reserve. Hii ingeimarisha Uchumi, kwa sababu gani? Kwa sababu pesa yetu ya Kitanzania ingeimarika, kwa maana mahitaji ya dola yangekuwa yanaenda proportional kabisa na uwepo wa pesa hiyo.

Mheshimiwa Spika, si kama hali iliyopo sasa hivi kwamba tunatamani kuwa na matumizi ya dola kwa ajili ya kununua au kuingiza kutoka nje, lakini dola hizo hatuna tunalazimika sasa kuzinunua dola zile kwa kutumia pesa ya Kitanzania, pesa nyingi sana. Wakati ambapo ungeweza ukanunua kikombe kwa shillingi mbili unalazimika kununua kikombe hicho hicho kwa shillingi 100 na sababu ni tofauti ya dola (exchange) iliyotokea pale.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unaweza ukaona kwa kiasi gani athari inajitokeza kwa kuja na kiasi hicho kikubwa cha fedha. Maana yake tungekuwa na fedha nyingi kwenye uchumi na uchumi ungekua. Pamoja na hiyo hali jinsi ilivyo, kungekuwa na wawekezaji wengi, kiasi hicho kingi cha fedha kingeingia. Hatuoni na hiyo fedha haionekani wala wawekezaji hawajaja kwa kiwango hicho. Hii inaonekana kwa uhalisia wa hali ya malalamiko yaliyopo sasa hivi ya dola na ni tafsiri ya wazi kabisa kwamba hizi fedha za kigeni ambazo kupitia kwenye investors hawa, ambazo wangezileta kama miradi hazipo au kama zimekuja basi ni kiwango kidogo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalozungumzia kwamba hakuna correlation ya mipango ni pale ambapo tunatamani kabisa miradi mikubwa ya kimkakati, ambayo tungetamani tufahamu kama imeshaanza kufanya kazi, ni kama vile Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Mradi huu umezungumzwa tangu wengine sisi hatujazaliwa, lakini mpaka sasa hivi bado umebaki kuwa kwenye karatasi. Kila wakati wa mipango, iwe ni mipango ya kutoka kwenye Wizara au kutoka kwenye Tume yenyewe, bado mpango huu ulikuwepo na umeendelea kuwa kwenye mchakato.

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie kwamba, hili neno la mchakato ndilo neno gumu sana na tena linaleta ukakasi mkubwa, kwa sababu mara nyingi sana kila kinachoshindikana kufanyika kwa kifupi tu utapewa taarifa kwamba, bwana hili jambo liko kwenye mchakato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mradi mkubwa, kwa mfano Mradi wa Gesi Mtwara. Huu ni kati ya mradi ambao tungetegemea kwamba nchi hii isingekuwa hivi ilivyo. Tulipewa matarajio makubwa sana wakati ule mradi unaanza na kila mtu alielewa hivyo kwa sababu uhalisia ndivyo ulivyo. Nchi kubwa zilizoendelea zenye vyanzo vya gesi zimekuwa zikiendelea kwa kasi kubwa, lakini ule mradi bado umebakia kwenye mchakato. Ukiuliza utaambiwa kwamba hili jambo liko kwenye mchakato na kama kuna kiwango kimetumika au kimetusaidia ni kiwango kidogo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika Mradi wa Gesi ya LNG, ndugu zangu wa Likong’o pale kuna wakati nalazimika kuwakimbia, nikipita pale hata kusimama sisimami kwa sababu nikipita pale swali la kwanza kuulizwa ni kuhusiana na mradi huu, kwamba unakuwaje na utaanza lini.

Mheshimiwa Spika, kuna project pia ambazo tumeshawahi kuzizungumza hapa; mimi mwenyewe nilishawahi kuzizungumzia kama vile Mradi wa Magadi Soda, Engaruka. Mradi huu umeendelea kuwa kwenye karatasi kama miradi mingine. Kwa hiyo ukiangalia hapa ninachoweza kuzungumza ni kwamba Waziri aliye kwenye nafasi hii sasa achukue reference kwenye miradi ile yote ambayo iko kule nyuma na failures ambazo tumekutana nazo kusudi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa, dakika moja malizia.

MHE. ISSA ALLY MCHUNGAHELA: ... tuweze kujirekebisha, twende katika hali ile inayotarajiwa na watu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ninakushukuru na ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai. Kama siku nyingine, ninashukuru kwa Mwenyezi Mungu kunipa nafasi hii nami kuweza kuchangia chochote katika mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami ninatoka kidogo, siyo mbali sana na walivyochangia wenzangu, lakini ni kwa sababu ya kujenga. Kama tunavyojua sote tunajenga nyumba hii, hatuna sababu ya kugombea fito.

MWENYEKITI: Samahani, Mheshimiwa Mchungahela, baada ya Mheshimiwa Mchungahela atafuata Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege na Mheshimiwa Zaytun Seif Swai ajiandae. Mheshimiwa, ninaomba uendelee.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ninavyozungumza, kwamba nitajaribu kuchangia kwa lengo la kutengeneza mtangamano wa mpango huu, kwa sababu huu mpango ndiyo msingi mkubwa wa bajeti yetu inayokuja hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona mgonjwa anaendelea kuumwa licha ya kuwa amepewa dawa, tafsiri yake ni nini? Kwamba, dawa aliyopewa siyo sahihi, lakini hii inaashiria nini? Kuna mambo mawili yanaweza yakajitokeza hapo. Jambo la kwanza, inawezekana maabara haijafanya uchunguzi sahihi wa changamoto ya mgonjwa, pia inaweza ikawa daktari ameshindwa kupata tafsiri sahihi ya ripoti ya maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kesi yetu sisi hapa, ni moja kwa moja kwamba, maabara imeshindwa kutoa majibu sahihi ya tatizo la mgonjwa. Kwa nini? Kwa sababu, daktari wetu sisi ni mahiri sana, Daktari wetu kwa maana ya Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mahiri. Amefanya jitihada nyingi za kutaka kutibu mgonjwa huyu kwa kwenda huku na huku akijaribu kutafuta jinsi gani ya kumtibu. Ni vema kwamba tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa lakini bado pia tunahitaji kufanya zaidi kwa sababu tumechelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya fununu ya kushuka kwa mfumko wa bei, lakini bado taarifa hizi zimekuwa siyo njema au hazina tija katika uchumi wetu. Bado kumekuwa na changamoto ya shilingi yetu kuwa dhaifu dhidi ya pesa za kigeni na hali hii inasababisha deni letu la Serikali kuongezeka kwa kasi siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kuwa, tumekuwa na mkakati mzuri sana wa kukopa, kwa sababu mara kwa mara tumekuwa tukijielekeza kukopa katika kiwango ambacho kwamba deni hili liwe himilivu, lakini pamoja na mkakati na umahiri huo, bado deni hili limekuwa likiongezeka kwa kasi kubwa na sababu kubwa ni kwamba bado hatuja-interact baadhi ya factor ambazo ni muhimu kwa ajili ya kufanya pesa yetu iimarike, kwa nini? Kutokuimarika kwa pesa hii, kunasababisha impact kubwa sana ya exchange rate kwenye deni hili. Ukiangalia hili Deni la Taifa, Deni la Serikali utakuta kwamba eneo kubwa la kukua kwake kunategemeana na rate ya exchange na riba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichokikopa siyo kikubwa ukilinganisha na hali halisi ya deni lenyewe. Sasa kutokana na hali hiyo bado tumeona kwamba jitihada kubwa zinazofanyika hazina impact hasa katika eneo hili la kuimarisha pesa ya shilingi, kuimarisha uchumi kwa ujumla na kufanya uchumi wetu uwe wenye manufaa na tija kwa society yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia mjengeko wa riba kwenye mfumo wa pesa, unaweza ukakuta viashiria vya haya mambo ninayoyasema. Kwenye riba ya kibenki, imepungua riba kati ya benki na benki na riba ya kibiashara ni kama bado imebaki palepale, iko juu. Ukienda kwenye riba ya dhamana za Serikali unakuta imekwenda mara dufu, hali ambayo inasababisha na kushawishi wawekezaji kuacha kuwekeza katika production activities kwa maana uzalishaji wa bidhaa ambazo ndiyo muhimili mkubwa wa usafirishaji kwenda nje na wanafanya kazi ya kununua dhamana hizi kwa maana ya kuwekeza kusudi kuwapatia pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hata role ya benki ambayo inatakiwa ifanyike unakuta haifanyi sawasawa, benki nao wame-concentrate katika kukopesha Serikali, hali kadhalika, kukopesha wawekezaji au watu ambao tayari wamepevuka wana uwezo wa kupata capital kutoka katika vyanzo vingine. Unakuta benki imejielekeza huko haitaki yaani imekosa uthubutu kabisa, benki imekuwa na uwoga, benki imeshindwa hata kutoa fursa kwa wananchi wa kawaida katika ku-enjoy mikopo katika maeneo hayo kwa kisingizio cha risk (hatari).

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hali hii kwa sababu ukizingatia kwamba hawa wananchi ndio wengi lazima athari yake ya kiuchumi utaiona pale kwamba watakosa pesa za kuwekeza na mwisho wa siku hakutakuwa na kitu chochote ambacho kitakuwa kimefanyika kwa ubora wake. Mipango ambayo tunayo, mipango mingi sana imekuwa haiendani na uhalisia na changamoto tulizokuwa nazo kama nchi kwa uchumi wa nchi hii. Mipango mingi imekuwa ikienda nusunusu tunakwenda sehemu tunagota.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kwa hali jinsi ilivyo hii mikoa ya kusini hii mikoa imekaa kimkakati Mkoa wa Mtwara, Lindi, Ruvuma na Iringa ni mikoa ambayo imekaa kimkakati, lakini ni mikoa tajiri sana kwa uzalishaji wa chakula, pia ni tajiri katika masuala ya utalii, hali kadhalika ni tajiri kwa sababu ya mipaka iliyokuwa nayo. Inapakana na nchi ambapo nchi hizo ni tegemezi katika mikoa hii, lakini licha ya kuwa na hiyo hali bado hakuna mkakati mkubwa wa waziwazi kabisa wa kuonesha kwamba mikoa hii ina utajiri huo. Bado imeachiwa yenyewe ikihangaika katika kufanya uwekezaji mdogomdogo wa mtu binafsi. Tunahitaji uwekezaji mkakati katika mikoa hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninategemea katika Mpango huu nione Reli ya Standard Guage ikitoka Mtwara kuelekea Mchuchuma mpaka Mbamba Bay, kwa ajili ya nini? Maeneo hayo yana uzalishaji wa Chuma cha Liganga, lakini pia na makaa ya mawe ambayo ni muhimu sana katika uchumi wa Tanzania pamoja na uchumi wa dunia kwa sasa hivi kwa maana ya nishati ya makaa ya mawe. Hali kadhalika, chuma ambacho sasa hivi dunia nzima imekuwa kikipatikana kwa kiasi kidogo sana kwa hiyo kama tungejikita katika maeneo haya bila shaka hii gap inayotokana na masuala ya exchange rate, lakini na pia kutokukua kwa uchumi, yangepungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya muda ninaona niunge mkono hoja na ninashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ALLY I. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kunijalia uhai na afya njema. Nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Lulindi kwa kuniombea dua njema; mamshukuru mke wangu na wanangu kwa ujumla kwa kuniombea dua njema; na pia nawashukuru wananchi wote wema, kwa kuniombea dua njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, mchango wangu nitajikita katika eneo moja tu, hili litakuwa ni eneo la upimaji wa ardhi na mipango miji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi iliyopimwa inaweka mipango mizuri ya matumizi yake. Ardhi iliyopimwa inatuonesha waziwazi wapi pa kujenga nyumba za kuishi, kulima, kufuga, kujenga viwanda, kuweka miundombinu ya kupumzika na michezo (recreation centers). Pia inaweza kuweka wazi wazi wapi pa kujenga shule, hospitali, ofisi na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi iliyopimwa inaonesha waziwazi wapi ni maeneo ya akiba, na pia inaonesha kila kitu kinachohusiana na ardhi. Ardhi iliyopimwa ndugu zangu ni fedha, na ardhi iliyopimwa ni dhamana. Benki itakukopesha kirahisi ukiwa na ardhi iliyopimwa. Ardhi iliyopimwa ni kinga ya umaskini. Ukishakuwa na njaa utauza ardhi yako kirahisi lakini hali kadhalika unaweza ukaiwekeza kirahisi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi iliyopimwa ni kinga ya majanga. Kipindi cha mafuriko ardhi iliyopimwa inaonyesha miundombinu wapi pa kwenda kukabialiana na majanga hayo; ardhi iliyopimwa inatuonesha wazi wazi wapi tutapata maji kwa maana ya zimamoto, wanafahamu ni wapi tutaenda kuchukua maji kwa ajili ya kuzima moto, pia vifaa na vitendea kazi vitapita kwenye maeneo gani katika ardhi hiyo ili kufikia janga mahali lilipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi iliyopimwa ni kinga kwa tetemeko; ardhi hii imekuwa ni bora sana wakati wa matetemeko kwa sababu nyumba zimewekwa kwa mpangilio kiasi kwamba hata itakapoanguka nyumba moja kutakuwa na ugumu kwa nyumba nyingine kuathirika, kama kwa watu walioko kwenye nyumba za karibu karibu kama zile ambazo ardhi hazijapimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ardhi iliyopimwa ni njia na kinga ya kuondokana na magonjwa. Kipindi cha mvua maji hayawezi kutuama na kusababisha magonjwa yanayosababishwa na uchafu kama vile kipindupindu, malaria na magonjwa mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ardhi iliyopimwa ni kinga ya migogoro. Kukiwa na ardhi iliyopimwa aghalabu huwa inakuwa na migogoro. Pia ardhi iliyopimwa ni urithi thabiti na kizazi kinachokuja, kwa nini nimeongelea haya? Nimeongelea haya kwa sababu hakuna kitu chochote cha muhimu kama nchi hatujaweka mipango yetu vizuri kwenye ardhi. Ardhi ni urithi mkubwa wa asili kwa dunia ambao tumepewa kuliko maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijikite kwenye Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, inayoonyesha matumizi hafifu ya ardhi. Kwa ripoti ya mwaka 2023 inaonyesha kwamba, Tanzania kiasi cha ardhi kilichopimwa ni 25% pekee. Pia ripoti inaonesha kuwa, kuna makazi holela takribani 70%, kwa maana hiyo wananchi wa Tanzania 70% wanakaa katika makazi holela. Hili siyo jambo dogo hata kidogo. Nafikiri tunajua jinsi gani tunatakiwa tuanze kujielekeza katika eneo la kupima ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia utafiti uliofanyika katika halmashauri mbalimbali umeonesha, kumekuwa na uibukaji wa maeneo yasiyokuwa rasmi. Majengo yanayojengwa katika maeneo yasiyopimwa, kwa maana hiyo makazi holela, kwa mfano ripoti ya New Urban Agenda, inaonyesha kabisa kuna takribani nyumbani 1,444,000 kwa makazi holela. Sasa ukichukulia idadi ya nyumba ambazo tumezijenga, unaweza ukaona ni kwa kiasi gani tunaishi katika makazi holela. Hili siyo jambo jema, hususan wakati kunapotokea masuala ya majanga, kama nilivyozungumza hapo mwanzo, na mambo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Ripoti ya Utekelezaji wa Wizara imetuonesha kwamba, kwa miaka tofauti tofauti kumekuwa na nyumba zilizojengwa kwenye makazi holela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2019/2020 takribani nyumba au majengo 348,918; mwaka 2020/2021 kuna takribani nyumba 741,645 holela na mwaka 2022 takribani nyumba 452,806 ambazo ni holela. Kwa hali hii inaonesha wazi wazi kwamba, tatizo hili ni kubwa, kama nilivyoanza kulizungumza hapo mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, makazi holela yameonekana katika halmashauri zote. Halmashauri ya Arusha inaongoza. Ni kitu cha kushangaza sana, lakini ndiyo inayoongoza kwa makazi holela. Takribani 95% ya makazi yaliyopo ni holela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kuzungumza hayo niliyoyazungumza, kutokana na ufinyu wa muda, naishauri Wizara kujielekeza moja kwa moja katika kuharakisha upimaji wa maeneo ya nchi, ili kupata uhakika wa ardhi iliyopo kwa vizazi vinavyokuja hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
The Finance Bill, 2022
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pili, nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Pia niishukuru Serikali, naomba nianze kuishukuru na kuipongeza Serikali kwa dhamira yake njema kwa wakulima wa korosho.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeleta mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Korosho, sheria namba 203, Sheria hii kabla ya mabadiliko ilikuwa ikielekeza kwamba kiasi cha export levy asilimia 65 kilikuwa kinakwenda kwenye Mfuko wa Bodi ya Korosho na asilimia 35 ilikuwa ikienda kwenye Mfuko Mkuu. Mwaka 2017/2018 kulitokea mabadiliko ambayo ililazimisha kwamba fedha yote ya export levy iende ikatumike kwenye Mfuko Mkuu hali ambayo kwa namna moja kulikuwa na changamoto kiasi kwenye uzalishaji lakini na uendeshaji wa zao la korosho.

Mheshimiwa Spika, tunashukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mabadiliko haya kwenye sheria namba 203, sheria ya sasa hivi inayopendekezwa, inapendekezwa kwamba asilimia 50 ziende kwenye Mfuko wa Wizara kwa ajili ya maendeleo ya kilimo, lakini asilimia 50 ielekezwe kwenye Mfuko Mkuu. Sasa ninayo mapendekezo kwenye sheria hii ili yafanyike mabadiliko na mabadiliko ninayoyapendekeza ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, napendekeza asilimia 50 ipelekwe moja kwa moja katika Mfuko wa Bodi ya Korosho. Asilimia 15 ipelekwe kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo yaani kwenye Mfuko wa Wizara na asilimia 35 napendekeza ipelekwe kwenye Mfuko Mkuu. Kwa maana hivyo export levy itakuwa imefanya kazi nzuri sana ya kuchangia zao ambalo ndiyo linazalisha lakini pia itakuwa imefanya asilimia 15 kwenye mchango wa mazao mengine kwenye kilimo na halikadhalika itakuwa imeichangia Serikali. Hapa tunaweza tukaona mgawanyo huu utakuwa ni mgawanyo wenye tija.

Mheshimiwa Spika, najaribu kusema hivi kwa sababu gani? Kwa sababu kwanza korosho ni miongoni mwa zao mkakati ambayo inailetea Taifa hili fedha nyingi sana za kigeni, lakini pia hali ya sasa ilivyo mikorosho peke yake ndiyo inayotozwa export levy na kiuhalisia hilivyo ni kwamba pamoja na kwamba export levy inalipwa na mfanyabiashara lakini yeye mfanyabiashara anafidia kwa kuweka bei ndogo kwa mkulima. Kwa hiyo mkulima anapunjika, baada ya kupata bei kubwa anapata bei ndogo kwa sababu ya ile export levy. Kwa hiyo ni busara kwamba fedha hii sasa ya export levy imguse yeye kwa kiwango kikubwa na kuhakikisha kwamba baadaye ana uwezo wa kuzalisha zaidi.

Mheshimiwa Spika, sababu nyingine kubwa ni kwamba, tumewekewa lengo kubwa la uzalishaji wa korosho. Sasa hivi lengo lililopo ni tani laki saba mpaka kufikia mwaka 2020/2025. Lengo hili hatuwezi kulifikia kama hakutakuwa na mkakati madhubuti wa kuifanya korosho iendelee. Njia pekee ya kuifanya korosho ni njia ya kuiwezesha kimapato hasahasa pato linaloweza kushughulikia kufanya utafiti. Utafiti hapa nazungumzia utafiti wa mbegu, utafiti wa magonjwa ya korosho, hali kadhalika na utafiti wa masoko. Mambo haya yote yataiwezesha korosho kuendelea na kwa sababu mkulima atakuwa motivated kuweza kulima kwa nguvu, mpaka hiyo target ya tani 700,000 inaweza kufikiwa kwa sababu atakuwa na uwezo wa kupata tija kwenye ukulima wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimejaribu kuzungumzia pia suala zima la maendeleo kwenye korosho, hapa tunazungumzia viuatilifu. Kwa mfano, mahitaji halisi ya korosho kwenye viuatilifu ni tani 45,000, lakini mpaka sasa hivi commitment ya Serikali ni tani 25,000. Kwa bahati mbaya mpaka hivi tunavyoongea, hata nusu ya tani ambazo Serikali imetoa commitment bado hazijamfikia mkulima. Kipindi hiki ndicho kipindi halisi cha matumizi ya viatilifu sasa ndiyo kipindi ambacho mkulima anapuliza zile dawa kwa maana ya sulphur na dawa za maji.

Mheshimiwa Spika, sasa kama hata nusu ya dawa hizo hazijafika tunaweza tukaona hapo tatizo linaloweza likazalisha tatizo lingine. Kuepusha tatizo hili ndipo nilipopendekeza kwamba asilimia 50 iende moja kwa moja kwenye zao la korosho kupitia Mfuko wa Korosho iwe inashughulikia masuala haya ya viatilifu, lakini iwe inashughulikia na masuala mengine pia ya uendelezaji kama vile kuangalia jinsi gani labda tunaweza tukapata kuiongezea thamani korosho, lakini na shughuli nyingine zote zinazohusisha mnyororo mzima wa thamani ya korosho.

Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivi tutakuwa tumefanya jambo sahihi na tuna uhakika wa kupata mazao makubwa tuliyojipangia na maendeleo kwa ujumla kwa wakulima yatakuwa mazuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja. Ahsante. (Makofi)