Supplementary Questions from Hon. Issa Ally Mchungahela (40 total)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ninayo maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikipoteza pesa nyingi sana, hasa kwenye miradi na miradi ya maji ikiwapo hasa huu mradi wa Chipingo. Hii imetokea mara nyingi kutokana na watendaji ambao sio waaminifu wakishirikiana na wakandarasi kuhujumu Taifa kwa kutotimiza majukumu ya mikataba yao. Je, Serikali ina tamko gani kuhusiana na suala hili? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, sina shaka na utendaji wa Wizara hii; Mheshimiwa Aweso pamoja na timu yake wanachapa kazi sana lakini wale watendaji wenu kule wanawaangusha. Je, Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri anakubali kuambatana na mimi kwenda kuangalia hali halisi mkajiridhisha kisha mkatatua changamoto hii kwa umakini kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Issa Mchungahela kutoka Jimbo la Lulindi, kama ifauatvyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara kwa sasa hivi tumekuwa tukifanya jitihada za kuona kwamba watendaji wanaendana na kasi ya hitaji la Wizara yetu kwa sababu, madeni yote na miradi ambayo imekuwa ya muda mrefu awamu hii tunaelekea kuikamilisha.
Mheshimiwa Spika, hivyo, napenda kumtoa hofu Mheshimiwa Mbunge kwa hawa watendaji ambao wanakiuka maadili yao ya kazi na kuweza kuwa wahujumu katika shughuli zao tayari tunawashughulikia na tayari tuna mkeka mpya wa Wahandisi ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao kadiri ambavyo tunahitaji watuvushe.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na suala la kuambatana, Mheshimiwa Mbunge aondoe hofu. Hiyo ndiyo moja ya majukumu yangu na ninamhakikishia baada ya kukamilisha ziara yangu kwenye maeneo mengine, basi na hata huko Masasi pia nitakuja na nitajitahidi kufika kwenye majimbo yote kuona suala la maji linakwenda kupata muarobaini.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Imekuwa ni changamoto kubwa sana kwenye masuala ya pembejeo hasa muda. Mara nyingi sana kwamfano jimboni kwangu kumekuwa na changamoto ya kuchelewa pembejeo kila muhula na hili jambo linajirudia mara kwa mara. Je, Serikali inaona jinsi gani ya kuweza kulitatua tatizo hili kwa haraka hasa hususan katiak msimu huu wa mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Mchungahela kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uchelewaji wa upatikanaji wa pembejeo una mahusiano ya moja kwa moja na upatikanaji wa fedha. Kw ahiyo tumebadili mifumo, sasa hivi tunatumia bulk procurement system ili tuweze kupata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu. Tunaamini kwamba kuanzia msimu unaokuja kwa maeneo ya Lindi, Mtwara wanaolima korosho mtaona mabadiliko ya upatikanaji wa pembejeo.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, naomba nijenge maswali yangu kupitia kwenye hoja tatu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara hii ni muhimu sana kwa ajili ya ulinzi wa nchi hii; pia barabara hii ni muhimu sana kwa usafirishaji wa mazao ya ufuta na korosho katika kata zilizopo pembezoni mwa Mkoa wa Mtwara; barabara hii ni muhimu vile vile kwa usafirishaji wa ufuta na korosho kutoka katika maeneo ya nchi jirani ambayo mazao hayo hayana masoko kule:-
(i) Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)
(ii) Je, Serikali ina commitment gani kwamba barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami na lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela yote mawili kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, naomba tu nitoe taarifa kwamba barabara hii ni barabara ambayo inafunguliwa. Kwa hiyo awamu ya kwanza ni kuifungua barabara hii yenye urefu wa kilometa 365 na ikishafunguliwa ndipo utaratibu wa kuijenga kwa kiwango cha lami utaanza kufanyika.
Mheshimiwa Spika, Serikali imetambua umuhimu wa barabara hii, kwanza ni barabara ambayo ni muhimu sana kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, lakini pia ni barabara muhimu sana kwani ikishafunguliwa itafungua uchumi na itaboresha maisha ya wananchi wengi ambao wanaishi katika kata ambazo amezitaja.
Mheshimiwa Spika, barabara hii inatoka Mtwara hadi Ruvuma na ni barabara ambayo inaambaaambaa na Mto Ruvuma. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya hatua ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha changarawe, hatua za ujenzi kwa kiwango cha lami zitafuata kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, hali inayoonekana Manispaa ya Iringa yaani inafanana moja kwa moja na hali iliyopo kwenye Halmashauri ya Masasi. Kwa sababu ni kata 18 kama ilivyo, lakini hali kadhalika vituo vya afya viwili na hali ni mbaya kabisa.
NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Mchungahela.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu je, ni lini Serikali itatuwezesha kuwa na vituo vya afya zaidi, maana yake vituo viwili vya afya ni vichache?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchungahela, Mbunge wa Jimbo la Lulindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Masasi Vijijini katika mwaka wa fedha kuna fedha ambazo zimetengwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kujenga vituo vya afya. Kwa hiyo, naomba nimuhakikishie kambwa pamoja na bajeti yetu 2021/2022 kutenga fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya afya kwa mapato ya ndani lakini pia kwa fedha za Serikali Kuu tutaendelea kutenga fedha kuhakikisha jimbo hilo pia linapata vituo vya afya.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikifuatilia suala hili kwa muda mrefu sana na majibu yamekuwa ni hivihivi. Naomba Serikali itoe commitment ni lini watalipa deni hili.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kutokuwa na umakini hasa hasa katika ulipaji wa madeni ya ndani, Serikali haioni sasa ni muda wa kulipa riba katika madeni haya ya ndani pia kama vile wanavyolipa madeni ya nje na riba.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mchungahela maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, suala la riba, mikataba ilikuwa haionyeshi kwamba kutakuwa na riba pale ambapo kunapokuwa kuna ucheleweshaji lakini siwezi kutoa commitment ya hilo jambo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu lini watalipwa nataka nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na kweli amekuwa akifuatilia yeye na Wabunge wa Mkoa wa Lindi na Mtwara na baadhi ya maeneo mengine ya nchi yetu kuhusu hawa waliogawa miche. Niwahakikishie kwamba mwaka ujao wa fedha watalipwa watu wote waliosambaza miche na sisi Wizara ya Kilimo tumeshamaliza zoezi hili na tumepeleka hazina.
Mheshimiwa Spka, vilevile waliokuwa watumishi wa umma kwa maana ya Wakurugenzi na Madiwani kwa kuwa kulikuwa na mikataba halali, haki zao zitalipwa na haziwezi kudhulumiwa kwa kuwa tu ni mtumishi wa umma. (Makofi)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara ya Tandahimba ni barabara ya muda mrefu sana imeahidiwa kwa muda mrefu sana tangu wakati wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Serikali itakuwa imeamua lini kufanya kwa vitendo kutimiza ahadi zake kwa sababu barabara hii ni ya muda mrefu sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mchungahela Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii imeahidiwa muda mrefu lakini Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba barabara hii tayari Serikali imeshaanza kutekeleza kwa vitendo ambapo kilometa 50 zimeshajengwa na katika bajeti tunayoenda, bado tunaendelea tumetenga Billioni tatu kwa ajili ya kuanza barabara hii ya Mnivata kwenda Tandahimba. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara bajeti itakapoanza kutekelezwa barabara hii itatangazwa na itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, hali ya kufunga mpaka huu kwa muda mrefu imesababisha mkwamo mkubwa wa kiuchumi kwa wananchi katika eneo hili.
Je, hivi Serikali haioni sababu ya kufungua mpaka huu kusudi wananchi wanufaike na zile fursa zilizoko katika eneo lile? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge kama ataangalia zaidi katika jibu langu la msingi nimesema kwamba, ufunguaji wa kituo hiki unategemea zaidi makubaliano ya nchi mbili baada ya kukaa na kuangalia namna ya kuweza kufungua kituo hiki kwa ajili ya kuwapatia huduma wananchi. Nimesema Serikali inaendelea kufuatilia hali hii ili kuona namna bora ya kuweza kukaa na jirani zetu, ili kuweza kuwafungulia.
Mheshimiwa Spika, kikubwa afahamu tu kwamba, lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma katika mpaka huu katika hatua za uingiaji na utokaji na hali ya ulinzi na usalama inaendelea. Hivi tunavyozungumza vipo vikosi vyetu ambavyo vinaweka amani na utulivu katika eneo hilo na huduma nyingine zinapatikana. Ninakushukuru.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona lakini kumekuwa na ucheleweshaji wa mara kwa mara wa kusaini document za kuendeleza mradi. Je, Serikali inachukua hatua gani za kuharakisha mradi huu kusudi uende sambamba na maendeleo ya mradi wa bandari.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge swali lake la nyongeza kama ifuatavyo. Nia ya Serikali si kuchelewesha mradi Serikali siku zote tunataka mradi uanze mara moja lakini kuna matatizo ambayo baadhi ya wakati hayawezi kuepukika. Kwa mfano sasa hivi kulikuwa na shida ya ugonjwa wa corona na vifaa vingi hasa vile vya taa vilikuwa vinatoka nje kwa vile hiyo ilisababisha mradi uweze kuchelewa kidogo.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa sababu mazingira ya ukamilishaji wa vituo hivi umechangiwa kwa namna moja au nyingine kuonekana kwamba kuna maeneo ambayo bado hayajakamilika, kwa mfano Nagaga, Mnavira pamoja na Chiungutwa kuna fedha ambazo hazijatimia pale, kwa sababu bajeti nzima ilikuwa shilingi milioni 500 lakini wamepewa shilingi milioni 400 na hivyo kusababisha baadhi ya majengo kama vile wodi ya akinamama pamoja na majengo ya ultrasound kutokamilika.
Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha majengo haya yaliyokosekana? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa vituo vya afya nchini kote unakwenda kwa awamu. Tunapeleka fedha awamu ya kwanza, tunajenga majengo ya kipaumbele ili kuwezesha vituo kuanza kutoa huduma za msingi, lakini tunatafuta fedha kwa ajili ya awamu ya pili ili kukamilisha majengo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo fedha ambazo zilipelekwa Nagaga na Mnavira zilikamilisha sehemu ya kwanza ya majengo, lakini milioni 100 ambayo inabaki itapelekwa ili kukamilisha wodi ya wanawake pamoja na jengo hilo la ultrasound. Ahsante sana.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante, ni miradi mingapi ya uwekezaji kati ya hiyo 294 imeanza?
Lakini pili, je, Serikali haioni sababu ya kuanzisha Idara au Kitengo Maalum cha Ufuatiliaji na Ushawishi?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kweli katika miradi hii 294 sababu ni swali la takwimu naomba tutafute takwimu zaidi za uhakika na nitampa Mheshimiwa Mbunge ni miradi mingapi ambayo imetekelezwa kati ya hii 294.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili tayari tuna vitengo vya ufuatiliaji kwa maana ya Monitoring and Evaluation katika Wizara, lakini pia hata katika taasisi zetu ikiwemo Kituo cha Uwekezaji cha TIC; na kwa taarifa tu katika miradi ambayo imetekelezwa mwaka 2021/2022 miradi zaidi ya 1,200 imeshafanyiwa ufuatiliaji kwa maana ya kuhakikisha kujua kama inatekelezwa na kwa kiwango gani. Nakushukuru sana.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ni lini barabara ya Mnivata kwenda Masasi itajengwa ni kwa nini haijengwi wakati pesa bado ipo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchungahela, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote ambao barabara hii inapita Mnivata - Newala hadi Masasi yenye urefu wa kilometa 160 kwamba tayari taratibu zote zimeshakamilika kwa maana ya maandalizi ya zabuni na barabara itakuwa na loti mbili na katika ujenzi huu pia Daraja la Mwiti limeunganishwa na tayari tunachosubiri ni wenzetu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika watupe no objection kwa sababu ndiyo wanaoijenga hii barabara. Kwa hiyo, muda si mrefu barabara hii itatangazwa kwa ajili ya kuijenga yote kilometa 160. Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Naomba Serikali ituambie hususani Wizara ya Nishati, kuna kigugumizi gani hasa katika suala la REA? Maana yake kumekuwa na changamoto kubwa sana kwa hawa Wakandarasi hawatoi ushirikiano, lakini hawashughuliki kabisa na miradi ile inayotakiwa ifanyike kule. Mfano kwenye jimbo langu ule mkataba uliopita haujatekelezwa hata katika kijiji kimoja. Sasa Serikali ina kigugumizi gani katika jambo hili, ituambie ukweli?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mchungahela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, niombe kupata ushirikiano wa Waheshimiwa Wabunge kwa sababu ni case by case kwamba Mkandarasi hana ushirikiano mzuri na Mbunge. Wako Waheshimiwa Wabunge wengine ambao wanatoa sifa nzuri na recommendation nzuri kwa wakandarasi waliokuwa nao kwamba wanatoa ushirikiano. Kwa hiyo, naomba kwa wale ambao wanapata changamoto ya ushirikiano, basi tuwasiliane ili tuweze kutatua changamoto hizo katika maeneo yao ili tuweze kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo lingine, tuwasiliane pia na kupeana taarifa na updates sahihi za ni lini umeme umewaka wapi na utawashwa wapi na pale ambapo tunaona kuna changamoto za ucheleweshaji usiokuwa na sababu kwa pamoja tuweze kushirikiana na kuchukua hatua ili tufikie azma ya kuwasha umeme katika vijiji vyetu vyote kwa kadri ya mikataba, lakini na lengo la Serikali Awamu ya Sita inaongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Barabara ya kutoka Newala kuelekea Masasi kupitia Mitesa imechukua muda mrefu sana kuanza licha ya kwamba fedha ipo, kwa nini barabara hii imechukua muda mrefu kiasi hiki? Lini barabara hii itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchungahela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nimemsikia vizuri, anaongelea barabara ya Newala kwenda Masasi kuanzia Munivata. Barabara hii ilishapatiwa fedha na ipo kwenye maandalizi ya kuanza ujenzi wa kiwango cha lami. Kwa hiyo, suala tu ni kwamba, mikataba tayari inaandaliwa kwa ajili ya kuanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kuanzia Mnivata, Newala hadi Masasi yenye urefu wa kilometa 160 kama nimemwelewa vizuri.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri. Wananchi wangu wa Mitesa Namalenga, Mdibwa, Nagaga, Chungutwa pamoja na Mpeta, wote hawa wamekuwa wakitarajia ujenzi. Sasa, kwa niaba yao nauliza, ni lini ujenzi huu utaanza?
Mheshimiwa Spika, lakini pili, kuhusu fidia, nimemsikia amejibu kwamba fidia imeanza, namuomba Waziri anijibu kwa asilimia ngapi jibu hili lina ukweli? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lindi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa vijiji vyote alivyovitaja kwamba barabara hii itajengwa. Tulishatangaza na tumesema tumefungua; na kwa kuwa inafadhiliwa na African Development Bank, mchakato wa manunuzi tuna uhakika by March barabara hii itaanza kujengwa, japo sisi tunasema tayari tumeshaanza kulipa fidia mchakato unaendelea.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa swali lake la pili, kwa asilimia ngapi, nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwenye jimbo lake, jumatatu watakuwa hapo wanalipa fidia kwani tayari Mnivata hadi Chikwaya Wilaya ya Mtwara tayari tumeshalipa, baada ya Tandahimba itakwenda Newala na Masasi na fedha ipo tayari, ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, sisi tuliomba tangu mwaka jana kwenye Shule ya Makong’onda hatujajua mpaka sasa hivi hali ikoje?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mchungahela, Mbunge wa Masasi Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, shule zote ambazo zipo katika maombi ndio tunazifanyia kazi. Tutakapopata hiyo hela maana yake kuna baadhi ya miundombinu ambayo tunatakiwa tukamilishe ili sasa ziweze kupandishwa. Ahsante sana.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kumekuwa na mkanganyiko kwa hizo pesa zilizopelekwa katika halmashauri kwa sababu wengine hawajui kama ziende kwenye vituo vya afya au kwenye zahanati.
Sasa Serikali haioni sababu ya kuweka maelekezo maalum kabisa kwamba hizi pesa either ziende kwenye kituo cha afya na hizi ziende kwenye zahanati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchungahela, Mbunge wa Jimbo la Lulindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inapopeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa zahanati au vituo vya afya au hospitali za halmashauri inapeleka na barua ya maelekezo kwa Mkurugenzi kwamba fedha zilizoletwa ni kwa ajili ya kujenga kituo cha afya eneo gani au zahanati eneo gani au hospitali ya halmashauri eneo gani?
Kwa hiyo, naomba nirudie kusisitiza kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kwamba wazingatie maelekezo yanayotolea na Ofisi ya Rais, TAMISEMI mara fedha zinapopelekwa katika ujenzi wa vituo hivi, ili kuepuka mkanganyiko ambao Mhehimiwa Mbunge ameusema, ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Nina swali linalofanana na hilo. Kule Lupaso kwenye Kijiji cha Matemwe, kunafanyika uchimbaji: Je, Serikali inafahamu kwamba kuna uchimbaji unaendelea pale?
Je, uchimbaji ule unanufaisha vipi Halmashauri na Serikali kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba nikiri kwamba sina hakika na tuko tayari baada ya Bunge hili nikutane na Mheshimiwa Mbunge na watendaji wetu tuweze kujua na kufuatilia kuhusu machimbo hayo. (Makofi)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Majimbo ya Vijijini yana maeneo makubwa sana ya kiutawala lakini yana mahitaji makubwa ya elimu ya VETA.
Je, Serikali haioni sababu ya kuowandolea adha wananchi wa vijijini kutafuta elimu hii kwa umbali mrefu?
Mheshimiwa Spika, kutokana na hoja za swali nililouliza hapo juu, Serikali ni lini itajenga chuo cha VETA angalau kimoja kwenye Jimbo la Lulindi.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Mchungahela kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, lengo la ujenzi wa vyuo hivi katika ngazi za Wilaya ni kusogeza huduma hizi karibu kule Wilaya. Tunafahamu kweli zipo Wilaya ambazo zina maeneo makubwa ya kiutawala, lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati tunajenga vyuo hivi, tunaweka vilevile na huduma ya mabweni. Lengo la huduma za mabweni ni kuhakikisha wanafunzi wote ambao wanatoka mbali kuweza kukaa pale pale chuoni na kuweza kupata huduma hii kwa karibu zaidi. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi, bado tunaweza tukawahudumia wale ambao wametoka mbali kwa sababu watakuwa wanakaa pale pale chuoni.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, anazungumzia suala la ujenzi kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya swali la msingi, kwamba kwa sasa tunakamilisha kwanza ujenzi wa vyuo hivi katika wilaya hizi, halafu tutaangalia sasa yale majimbo yenye changamoto ikiwemo labda na jimbo lake pamoja na Jimbo la Nanyamba kule nako kuna malalamiko makubwa sana. Hii itategemea sasa vile vile na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, kumekuwa na idadi ndogo sana ya wanafunzi wanaosoma katika A-level Mkoani Mtwara. Je, Serikali haioni sababu ya kutoa motisha kwa kutenga kiasi kikubwa cha wanafunzi wanaotakiwa kusoma sekondari za A-level ambazo ziko katika Mkoa wa Mtwara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mchungahela kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ina mkakati huo anaouzungumza yeye na ndio maana tayari imetengwa fedha ya kujenga shule za sekondari za mikoa kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaotoka kwenye maeneo husika wanabaki katika maeneo hayo hasa wasichana. Pia tayari Serikali imekwishatenga Shingi Bilioni tatu kwa mikoa 10 ya mwanzo na sasa itakwenda tena kwenye awamu ya pili kwenye mikoa mitano, halafu itakuja kumalizika katika mikoa mingine, hii ni kuwabakiza.
Mheshimiwa Spika, vile vile kuna shule zile za A - level ambazo zilijengwa na wananchi kule na Serikali ikaja kumalizia, huwa zile zinatoa kipaumbele kwa wanafunzi wa maeneo yale kasoro zile shule maalumu tu za kitaifa ndio zinachukua wanafunzi kutoka katika kila eneo la Taifa letu. Naomba kuwasilisha.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri ametamka uhaba wa shule za A-Level na jambo hilo limejityokeza katika jimbo langu. Mpaka sasa hivi kuna A- Level mbili tu zinazofanya kazi wakati kuna kata 18 na tulishaomba kupandisha hadhi Shule ya Makong’onda kuwa A- Level; mchakato huu wa kupandisha hadhi utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato wa kupandisha hadhi shule kuwa na mkondo wa kidato cha tano na sita ni upo chini ya Wizara ya Elimu, maombi yale yanapelekwa Wizara ya Elimu. Nitakaa na Mheshimiwa Mchungahela kuona mchakato huu umefikia wapi na kuweza kumpa majibu hayo.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Naibu kwa kutupatia baadhi ya shule chache, kama alivyosema, miongoni mwao zikiwepo Rivango, Chikolopola pamoja na Lulindi Maalum, lakini kama Waziri anavyoona shule zilizokuwa mbovu au chakavu ni nyingi sana kwenye majimbo hayo mawili, hususan kwenye Jimbo la Lulindi anaweza akaona, ziko zaidi ya 20 na kitu. Ni lini atafanya jitihada kwa ajili ya kumalizia hizo shule nyingine chakavu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe. Serikali inatambua kwamba, shule nyingi za msingi nchini ni chakavu na tayari tumeona jitihada kubwa za Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutafuta fedha kwa ajili ya kupunguza uchakavu huu katika shule zetu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ambayo ina Jimbo la Mheshimiwa Mchungahela na Mheshimiwa Mwambe, Shule ya Chikolopa imepokea shilingi milioni 331, Shule ya Rivango imepokea shilingi milioni 101, Shule ya Mkalapa imepokea milioni 120, Shule ya Mwena milioni120 na Shule ya Lulindi Maalum imepokea milioni 54. Fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa na ukarabati katika shule hizi. Hizi ni jitihada za wazi za Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha upungufu huu wa majengo katika shule za msingi na uchakavu unakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatoe mashaka Waheshimiwa Wabunge, Serikali itaendelea kujitahidi kutafuta fedha hizi kwa ajili ya kukarabati shule nyingi zaidi.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nisikitike sana kutokana na majibu ya Naibu Waziri, haya majibu sidhani kama wanafanya research. Manati, watoto wanapiga vikombe kweli? Ni kitu cha kushangaza sana, lakini sasa kinachonishangaza zaidi kwenye chanzo cha umeme ndiko kwenye shida kubwa ya umeme. Je, ni lini Serikali itatuhakikishia kwamba huku tunapata umeme wa uhakika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikilalamika hapa kila siku kuhusiana na Jimboni kwangu Lulindi. Mkandarasi alipewa vijiji takribani 30 kushughulika na umeme kwa maana ya viunganishi, hakushughulikia hata kijiji kimoja, nimekuwa nikiimba kama wimbo. Je, ni lini nitaacha kuja hapa kulalamika kuhusiana na suala la umeme jimboni kwangu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyomalizia paragraph ya mwisho; upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Mkoa wa Mtwara utatokana na kukamilisha hizi njia mbili ambazo zinaleta umeme wa gridi ya Taifa kutoka katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna tatizo kwenye njia ya umeme, hata kama ni kwenye eneo la chanzo umeme utakatika. Kwa hiyo, azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha kwamba, miundombinu yote hii inarekebishwa na kuimarishwa, ili iweze kusafirisha umeme kwa wakati wote na kuwafikia wale walengwa ambao wanatakiwa kuutumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la pili; mkandarasi anayetekeleza miradi ya REA katika eneo la Lulindi ambalo ni Masasi, ana Wilaya ya Masasi na Nanyumbu, anaitwa Namis, alikuwa katika wale wakandarasi wenye lot zile saba ambazo zilikuwa zinasuasua, lakini tumesukumana naye na kuwekeana masharti na tunaamini kufikia Disemba na yeye atakuwa amekamilisha kazi yake. Kwa Lulindi alishawasha vijiji kama sita au saba kutoka kwenye vile alivyokuwanavyo na tunaamini kabla mkataba haujaisha atakamilisha kazi kwa sababu, tunasimamiana naye kwa karibu sana.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, sababu kubwa ya kutokushiriki kikamilifu kwa vijana na wanawake katika shughuli hii ya madini ni mikopo kwa maana ya capital.
Je, Serikali haioni sababu ya kuwapa vijana mitaji ili kusudi washiriki kikamilifu katika sekta hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Mchungahela mtetezi makini wa watu Jimbo la Lulindi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli changamoto kubwa ya vijana, wanawake na wachimbaji mbalimbali ni ukosefu wa mitaji. Katika kutanzua changamoto hii Wizara ya Madini kupitia Shirika lake la Taifa la Madini (STAMICO) wamewaweka wakfu walezi wakuu wa wachimbaji wadogo na hatua za awali za kuwasaidia zimehusisha kutoa elimu ili wafahamu namna ya kufanya uchimbaji wa tija, Sheria ya Madini, pia kuingia katika makubaliano na taasisi za kifedha hapa nchini zikiwemo Benki za NMB, CRDB na Azania ili waweze kuwakopesha wale ambao wamekidhi vigezo.
Mheshimiwa Spika, ili waweze kusaidiwa, wananchi wa Jimbo lake na Watanzania wote ambao wamepata hamasa ya kujihusisha na biashara ya madini ni vizuri waunde vikundi ili kuwa rahisi kuwafikia na kuwasaidia kupitia vikundi na wajiunge na Chama cha Wachimbaji wadogo wa Madini Tanzania ambao sasa hivi wapo kwenye mchakato wa kuanzisha benki yao ili waweze kupata mitaji na waweze kuchimba kwa wakati kwa tija zaidi na wa ufanisi.
MHE. ISSA ALLY MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hali hiyo inafanana pia katika Kata za Lipumbulu, Sinano, Lupaso na Mchauru katika Jimbo la Lulindi, ni lini zitapatiwa minara?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANONA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mchungahela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mheshimiwa Mchungahela pamoja na Kata ambazo amezitaja, zipo katika minara 758 ambayo tayari utekelezaji wake umeshaanza, ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu lakini ninayo maswali mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Lulindi ni mzalishaji mkubwa wa malighafi hya hivyo viwanda wanavyoahidi kuvijenga. Je, Serikali itajenga viwanda vingapi kwenye Jimbo la Lulindi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha korosho, zao hili pekee yake ndiyo linalochangia mfuko wa kilimo. Je, Serikali haioni sababu ya kutumia kiasi cha pesa zilizoko katika mfuko huu kwa ajili ya kutengenezea bima ya bei ya korosho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza nataka nikiri ni kweli eneo la Lulindi ni kati ya wazalishaji wakubwa wa korosho. Kwa kutambua hilo Serikali pamoja na sekta binafsi itaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kubangua korosho katika eneo hili la Lulindi ili wakulima wengi zaidi waweze kunufaika na hatua hii ya uchakataji wa korosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu bima, tumeshafanya mazungumzo na Shirika la Bima la Taifa kwa ajili ya kuhakikisha ya kwamba wanaingia katika zao hili la korosho ili tuweze kumlinda mkulima pale bei inapoporomoka. Hivi sasa tupo katika hatua nzuri na baadhi ya maeneo tumeanza majaribio naamini itawafikia wakulima wengi zaidi na itakuwa ni mkombozi mkubwa kwa wakulima wa korosho nchini Tanzania.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika vijiji 15 alivyovitaja vya vitongoji kumekuwa na changamoto kidogo kwa sababu, tulishapeleka vijiji 15 wakasema kwamba vijiji hivyo havitambuliki na TAMISEMI, lakini pia wakatoa condition nyingine kwamba vijiji hivyo lazima vipitiwe na mkondo mkuu wa waya.
Je, Serikali inatoa maelezo gani ya msingi kwa sababu inaonekana kule wale watendaji hawana uhakika wa kitu gani cha kutekeleza? (Makofi)
SPIKA: Nilikuwa najaribu kusikiliza kama swali lako linahusiana na swali la msingi au Hapana? Maana umetoa maelezo ya ziada hapo mwanzo yanayokuondoa kwenye swali la msingi. Swali lako ni nini? Uliza swali bila maelezo, itakusaidia kuwa kwenye swali la msingi
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, vitongoji 15 alivyovitaja kwamba ndiyo vinatakiwa vipitiwe kwa ¬level hii ya umeme aliyoisema sasa hivi kunakuwa na mkanganyiko, wale watekelezaji hawajui kwamba watekeleze vipi? Kwa sababu, ukiwapelekea vitongoji wanasema ah, ah, vitongoji hivi havistahili kwa sababu, hakuna umeme. Sasa je, kuna condition ya vitongoji au hakuna condition kwamba, vitongoji vyovyote vinaweza kuwekewa au kuna condition fulani lazima ndiyo vipelekewe huo umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, katika vitongoji 15 ambavyo tumepata fedha ya kuvipelekea umeme katika mradi huu utakaotekelezwa mwaka 2023/2024 nieleze wazi kwamba ni vitongiji ambavyo tunaviita underline. Ni vitongoji ambavyo tayari miundombinu ya umeme mkubwa ilishapita katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, unakuta kwenye kijiji kimoja chenye vitongoji labda vitano, vitongoji viwili vimefikiwa na miundombinu kwa maana ya kuwashwa, kitongoji kimoja miundombinu imepita kwa juu haijashuka kwenye kile kitongoji na labda vitongoji vingine viwili havijafikiwa kabisa na umeme mkubwa na havijafikiwa na umeme mdogo.
Mheshimiwa Spika, fedha hii ndogo tuliyoipata Shilingi bilioni 379 inatosha kwa kupeleka miundombinu ya umeme mdogo tu katika yale maeneo ambayo tayari miundombinu ya umeme mkubwa ilishapita. Kwa hiyo, wale watendaji wenzetu kule chini wanayo maelekezo haya na wanajua namna ya kuwasilisha maelezo haya. Wataleta vile vitongoji ambavyo vilishapitiwa na line kubwa, sasa tunashusha umeme kwa ajili ya kujazia katika maeneo hayo. Pia mwaka 2024/2025 kwenye mradi wetu mkubwa wa HEP wa shilingi trilioni sita hapo tutakwenda kumaliza vitongoji vyote ambavyo vilishafikiwa na ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, katika vijiji ambavyo vilipatwa na changamoto ya umeme kutokukamilika ni vijiji takribani vyote vya kata kama tatu hivi katika Jimbo la Lulindi; Kata ya Mchauru kulikuwa na hiyo; Kata ya Sindano, Kata ya Luatala.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha vijiji hivi vilivyokosa umeme mpaka sasa hivi katika kata hizo na maeneo mengine ya Lulindi vinapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchungahela kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nikwamba ifikapo Desemba, 2022 Serikali imeji-commit kuhakikisha inafikisha miundombinu ya umeme katika vijiji vyote Tanzania Bara ambavyo havijafikiwa na umeme na kazi zinaendelea katika maeneo mbalimbali, wakandarasi wako site wanaendelea.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ofisi ya jimbo ni nyenzo muhimu sana katika utekelezaji majukumu ya jimbo. Ofisi nyingi sana za jimbo zimekuwa hazina samani wala vitendea kazi vya ofisi. (Makofi)
Je, Serikali haioni sababu ya kuimarisha ofisi kusudi iwe inafanya kazi zake kikamilifu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini Serikali itatoa fedha ya kutosha kuhakikisha Mfuko wa Jimbo unafanya kazi inayostahili jimboni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Jimbo la Lulindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, natambua kwamba ofisi nyingi za Wabunge katika majimbo yao hazina samani na tunaziagiza Halmashauri zote nchini kupitia kwa Wakurugenzi kutenga fedha na kuzikamilisha ofisi hizo ili Wabunge waweze kuzitumia. Kwa hiyo, hilo ni agizo kwa Halmashauri na wakurugenzi wote.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili amezungumzia kuhusu ongezeko la fedha katika Mfuko wa Jimbo. Nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiyo anasimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kwa kuongeza fedha za Mfuko wa Jimbo kwa mwaka huu kutoka shilingi bilioni 11 ambazo zilitumika mpaka shilingi bilioni 15.99 kwa hiyo ni ongezeko kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika mwaka unaouja huu kutakuwa na ongezeko la fedha za Mfuko wa Jimbo katika majimbo yote nchini. Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi sana kununua viuatilifu hasa vinavyotumika katika zao la korosho, na mnunuzi mkubwa ni maeneo yote ya Mtwara na Lindi: Je, Serikali haioni sasa ni wakati muhimu wa kujenga viwanda vya viuatilifu ambavyo vinaendana na material hii ya gesi?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchungahela Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna changamoto kama ilivyo kwenye mbolea, lakini pia kwenye viuatilifu ambavyo kwa kiasi kikubwa tunaingiza kutoka nje. Serikali imeshaanza mipango hiyo ikiwemo kuzalisha kupitia kile kiwanda chetu cha viuwadudu pale Kibaha, lakini tutaona pia namna ya kutumia gesi kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, ambapo nayo ikianza kuchakatwa inaweza kuzalisha viuatilifu mbalimbali ambavyo vinaweza kutumika katika sekta hii ya kilimo hasa kwenye mikorosho na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kituo cha Afya cha Chikolopola kina mtumishi mmoja tu. Lakini pia Zahanati ya Mputeni na zahanati ya Makanyama haina watumishi kabisa. Ni lini Serikali itapeleka watumishi katika maeneo haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama ambavyo katika mwaka wa fedha uliopita halmashauri hii ya Masasi vijijini walipata watumishi. Nafahamu kwamba bado wanaupungufu mkubwa katika Kituo cha Afya cha Chikolopola. Nimhakikishie kwamba tutatoa kipaumbele kwenye ajira zitakazofuata ili waweze kupata watumishi wa kutosha katika eneo hilo. ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Makamu wa Rais alipokuja Chiungutwa alitoa ahadi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya kumalizia Kituo cha Afya cha Chiungutwa na pia shilingi milioni 100 pia kwa Kituo cha Afya cha…
SPIKA: Mheshimiwa swali la nyongeza huwa ni moja.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, lini…
SPIKA: Subiri, subiri. Kwanza huwezi kwenda mbili; pili, kwa sababu ni swali la nyongeza huwezi kuweka maswali mawili katika swali moja. Chagua kimojawapo kati ya hivyo umwulize Mheshimiwa Naibu Waziri ili akujibu.
MHE. ISSA ALLY MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ni lini pesa hizi shilingi milioni 100 zitakwenda kwenye Kituo cha Afya cha Chiungutwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mchungahela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Makamu wa Rais aliahidi shilingi milioni 100 kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo cha Afya cha Chiungutwa na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha hiyo imeshatengwa kwenye bajeti ya mwaka huu 2023/2024 na fedha zitakapopatikana zitapelekwa katika kituo hiki kwa ajili ya ujenzi, ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na nia nzuri ya Serikali juu ya TASAF kumekuwa na changamoto nyingi sana, miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kwamba pesa wanazostahili kulipwa wasimamizi na waratibu hazipelekwi au hazipatikani, lakini pia hata kama zikienda zinaenda kwa muda uliochelewa, semina ambazo ndiyo stahiki zitakazowesha kufanyika kwa jambo hili hazifanyiki kabisa; je, ni lini Serikali itatatua changamoto hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto ambazo Mheshimiwa Mbunge amezieleza nataka kukuhakikishia kwamba kwangu mimi kama Waziri mhusika tunazichukua na kwenda kuzifanyia kazi, lakini nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako, miongozo iliyotolewa kwa ajili ya kufanyika kwa hizi zote ambazo amezisema Mheshimiwa Mbunge ipo wazi, kwa mfano, kwa upande wa semina, upande wa semina fedha zinafika ndani ya muda kama Lulindi au Wilayani kwao hazijafika fedha hizi, basi mimi naomba nizungumze na Mheshimiwa Mbunge ili anieleze, lakini sio yeye tu pamoja na Wabunge wengine ambao wana matatizo kama haya nao pia nitapenda wanifuate nipate taarifa zao ili sasa tuweze kuwasimamia wenzetu wa TASAF ili mambo hayo yaweze kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka nikuhakikishie kuwa Serikali imepeleka hela nyingi za kutosha, kama uzembe upo ni kwenye usimamizi ambao sisi kama Serikali hatutoufumbia macho.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Masasi imekuwa na elimu ndogo kuhusiana na jambo hili. Je, Serikali ina-commitment gani kuhakikisha inatupa elimu hii, hususani katika Jimbo langu la Lulindi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nimesema kuna gap kidogo, suala la uelewa na ndiyo maana Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, iliamua kutafuta fursa ya kutoka kwa wadau kwa ajili ya kufanya capacity building kwa wataalamu wetu. Ndiyo maana sasa hivi Serikali kupitia Shirika la UNEP tutaenda kufanya awareness na capacity building kwa wataalamu wetu wa mazingira katika halmashauri zetu, Lengo kubwa tuwe na uelewa mzuri katika suala zima la uwekezaji katika biashara ya carbon. Kwa hiyo, kwenye hilo ni kwamba hata wataalamu wa Lulindi watapata fursa hiyo kupitia uhusiano huu tuliokuwa nao na UNEP. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri. Kwa kuwa mafunzo ya VETA yamekuwa ni mkombozi kwa vijana waliokosa kuendelea na masomo ya juu na kwa wale wasikuwa na ajira, kwa nini, Serikali isiondoe mzigo huu wa ada kwa hawa wanyonge?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali imeweka utaratibu gani wa kuhakikisha kwamba, wenye nia ya kupata mafunzo haya wanapata mafunzo haya bila kubugudhiwa licha ya kuwa wamekosa ada?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Mchungahela kama nilivyoeleza kwenye majibu ya swali la msingi ni kwamba, tumeweza kutoa ruzuku kwenye mafunzo haya na kupunguza ada kwa kiasi kikubwa, lakini kwa vile Mheshimiwa Mbunge anatoa ushauri kwamba tuendelee kupunguza, basi kwanza nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, ukipitia rejea ya Bodi ya Mikopo ambayo mwanzoni ilikuwa inatoa tu kwa elimu ya juu, lakini kwa sasa tumeanza kushuka kwenda kwenye elimu ya kati, kwa hiyo, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata elimu kwa utaratibu wowote ule.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaangalia ushauri wake wa kwamba, je, ifutwe au tuipeleke kwenye ule utaratibu wa Bodi ya Mikopo na hawa wanafunzi wasiojiweza kwenye maeneo haya ya ufundi stadi, ili waweze kupata mikopo na waweze kuendelea na elimu yao. Nashukuru sana.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Masasi haina soko kabisa, ni lini Serikali itajenga soko katika Kijiji cha Mbuyuni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Lulindi kwamba Serikali ilikwishatoa maelekezo kwa Wakurugenzi wote kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanatenga maeneo mahsusi kwa ajili ya ujenzi wa masoko. Nampongeza Mheshimiwa Mbunge na Halmashauri hii ya Masasi Vijijini kwa kutenga eneo hilo, namwelekeza Mkurugenzi kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI aanze kutenga fedha kwa mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo wakati Serikali pia ikitafuta fedha kwa ajili ya kuunga mkono juhudi hizo. Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Vikundi vingi vya mazingira vimekuwa vikikosa motisha na uwezo. Je, Serikali inachukua hatua zipi kuvijengea uwezo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Comrade, Mheshimiwa Mchungahela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, kuna vikundi vingi ambavyo vimejihamasisha zaidi kuhakikisha vinashughulika na shughuli za kimazingira, lakini wakati mwingine vinakuwa na changamoto ya bajeti. Nachukua fursa hii kuomba Mamlaka za Serikali za Mitaa, kupitia dirisha la utoaji wa fedha kwa ajili ya vikundi, ziangalie kama kuna vikundi vya kimazingira ambavyo vinaweza kupatiwa mtaji wa uzalishaji wa miti waweze kufanya hivyo, kwa ajili ya kuvisaidia vikundi vyetu mbalimbali kuwa na nguvu na uwezo kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kimazingira.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, shule hii ina tatizo la walimu, kwa hivi sasa ina walimu sita tu; je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza idadi ya walimu kuondokana na changamoto iliyokuwepo?
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la walimu limekuwa ni tatizo sugu Mkoani Mtwara kwa ujumla. Je, Serikali ni lini italichukulia tatizo hili kwa umuhimu unaostahili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mchungahela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tukiri kwamba kuna changamoto ya walimu katika Chuo hiki cha Kitangari na siyo chuo hiki tu bali karibu vyuo vyote kutokana na uongezekaji uliotokea baada ya kujenga vyuo vipya 25 vya wilaya na vile vinne vya mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tarehe 02/03/2024 tumepata kibali cha kuajiri jumla ya walimu 239. Kati ya hao, watumishi 72 ni watumishi mwega na watumishi 167 ni walimu. Tutahakikisha kwamba walimu hawa watakapopatikana tutakipa kipaumbele Chuo hiki cha Kitangari lakini tutawapa kipaumbele sana Mkoa wa Mtwara na vile vyuo vipya 25 vya wilaya na vile vinne vya mikoa, ninakushukuru.
MHE. ALLY I. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, jimboni kwangu kuna vitongoji vingi sana vyenye hadhi ya kuwa Kijiji, lakini havina umeme kabisa. Je, Wizara ina mpango gani wa kuviangalia vitongoji hivi kwa jicho la huruma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kama ambavyo nimeshasema, tayari Serikali tumeanza utekelezaji wa miradi kwenye vitongoji baada ya kufika karibia na mwisho kwa mradi mkubwa wa kupeleka umeme kwenye vijiji. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba dhamira yetu ni kuhakikisha tunaendelea kupeleka umeme kwenye vitongoji ikiwemo vitongoji katika Jimbo la Mheshimiwa Mchungahela.
Mheshimiwa Spika, tumeanza na vile vitongoji 15 na tuna miradi mingine ya vitongoji inakuja. Vilevile, katika Mkoa wake tuna mradi wa ujazilizi ambao pia umeanza. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, miradi ipo na wakandarasi wako site na tutaendelea kupeleka kwenye vitongoji kwa kadri miradi na upatikanaji wa fedha unavyoendelea, ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu, lakini hali halisi ni kwamba, wananchi wangu wa Jimbo la Lulindi wapo katika adha kubwa ya maji. Swali la kwanza; sasa, Naibu Waziri anasema nini kuhusiana na hali hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; upo tayari kuongozana na mimi kwenda kujionea hali halisi ilivyo kule kwa sababu hayo majibu pamoja na kwamba ni majibu sahihi, hayakidhi hali ya changamoto waliyonayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchungahela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakiri kwanza kabisa tumekuwa na mjadala mrefu na Mheshimiwa Mchungahela kuhusu mradi huu. Kwa kweli kati ya watu ambao wanaufuatilia kwa karibu sana, Mchungahela amekuwa kinara katika kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kauli ya Serikali ni kwamba, kwanza kabisa natumia fursa hii kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, Mheshimiwa Waziri ameandika special request ya mradi huu Wizara ya Fedha ili uweze kutangazwa na kuhakikisha kwamba mradi huu unaenda kuanza mara moja kwa ajili ya wananchi wa Lilindi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge mradi huu sisi kama Serikali tunafahamu kwamba, tunaendelea kuunga mkono kampeni ya Mheshimiwa Rais ya Kumtua Mama Ndoo Kichwani na tunafahamu kwamba, ahadi ni deni na Serikali itatimiza ahadi hiyo. Kwa hiyo, usiwe na wasiwasi Mheshimiwa Mbunge tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni majukumu yetu Serikali kuhakikisha kwamba, tunaitikia wito wa Waheshimiwa Wawakilishi wa Wananchi pale ambapo wanatuomba. Mheshimiwa Mchungahela nipo tayari kuongozana na wewe kwenda kujionea hali halisi ya upatikanaji wa maji ndani ya Jimbo la Lulindi. Ahsante sana.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hali ya sasa ilivyo uzalendo kwa wananchi tulio wengi ni changamoto na Serikali imesema kwamba imekuwa ikitoa elimu hii kwa wananchi. Je, haioni sasa ni wakati wa kuongeza juhudi kuhakikisha elimu hii inawapata watu wote kwa ufasaha na kuweza kuwa chachu kwa kuelimika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali dogo la Mheshimiwa Mchungahela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli jambo hili ni muhimu kwa wananchi wote, lakini nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, yeye ni Mbunge na vilevile ni Diwani kwenye halmashauri au jimbo lake, mambo haya yamekuwa ni ajenda muhimu hata katika Mabaraza yetu ya Madiwani. Kwa hiyo, tunachukua ushauri wake, vilevile tuweze kuhakikisha na sisi kama Wabunge kwenye Mabaraza yetu ya Madiwani kwamba elimu hii inawafikia Madiwani na wananchi wote katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)