Primary Questions from hon Hassan Seleman Mtenga (18 total)
MHE. HASSAN S. MTENGA Aliuliza: -
Je, Serikali haioni sababu kwa sasa kutumia Bandari ya Mtwara kusafirisha korosho zinazolimwa Kusini badala ya kutumia njia ya magari ambayo yanasababisha uharibifu mkubwa wa barabara kwenda Bandari ya Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Selemani Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, wafanyabiashara wamekuwa wakitumia bandari ya Mtwara kusafirisha korosho zinazolimwa kusini mwa nchi kwa kuzingatia ushawishi wa Serikali wa kutumia zaidi bandari hiyo badala ya kutumia njia ya magari ambayo ni kweli inachangia uharibifu wa barabara na wakati mwingine ajali za mara kwa mara. Katika kufanikisha nia hii, Serikali imeendelea kufanya vikao na wadau mbalimbali ili waweze kutumia Bandari ya Mtwara na hasa baada ya kufanya maboresho makubwa katika bandari hiyo kwa kujenga gati jipya na kuongeza kina cha maji ili meli kubwa zaidi ziweze kutia nanga katika bandari hiyo ya Mtwara.
Mheshimiwa Spika, changamoto za Bandari ya Mtwara ni utegemezi wa shehena ya aina moja tu ya korosho inayotoka Mtwara na hakuna shehena nyingine inayoingia katika Bandari hiyo. Hali hiyo inasababisha gharama za usafirishaji kuwa juu kutokana na meli kuja zikiwa tupu bila mzigo ili kufuata shehena ya korosho Mtwara tofauti na Dar es Salaam.
Kufuatia kuwepo kwa changamoto hiyo Serikali inaendelea kuwashawishi wenye meli kupunguza gharama za usafirishaji ili kufidia gharama za kusafirisha korosho kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa njia ya barabara. Aidha, Serikali kupitia TPA (Mamlaka ya Bandari) inaendelea kuitangaza bandari ya Mtwara ili zipatikane shehena zinazoingia katika bandari hiyo, ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE K.n.y. MHE. HASSAN S. MTENGA Aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza ruzuku katika mpango wa utoaji bure Elimu ya Sekondari na Msingi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango wa Elimumsingi Bila Malipo nchini ulioanza kutekelezwa mwezi Desemba, 2015. Fedha zinazotolewa kupitia mpango huo zinahusisha fidia ya ada, shughuli za uendeshaji wa shule, fedha za chakula kwa shule za bweni na malipo ya posho za madaraka kwa Wakuu wa Shule na Maafisa Elimu Kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali inaomba kutengewa kiasi cha shilingi bilioni
312.09 kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Elimu Bila Malipo ambalo ni ongezeko la shilingi bilioni 13.96 ikilinganishwa na shilingi bilioni 298.13 zilizoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2020/2021. Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa Elimumsingi Bila Malipo kwa kadiri ya mahitaji na upatikanaji wa fedha. Aidha, kuanzia mwezi Desemba, 2015 hadi Februari mwaka 2021, Serikali imetoa kiasi cha shilingi trilioni 1.26 kwa ajili ya Elimumsingi Bila Malipo.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara za lami katika Kata za Ufukoni, Magomeni na shangani Manispaa ya Mtwara Mikindani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais–TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Selemani Mtenga Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujenga mundombinu ya barabara nakufanya matengenezo katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018 kupitia Miradi ya Uendelezaji Miji yaani Tanzania Strategic Cities Projects Serikali ili jenga barabara za lami zenye urefu wa kilomita 4.53 katika Kata ya Shangani Manispaa Mtwara Mikindani kwa gharama ya shilingi bilioni 7.09. Aidha, katika mwaka wa fedha 2019/ 2020 kupitiafedha za Mfuko wa Barabara Serikali imejenga barabara za lami zenye urefu wa kilomita 0.85 katika Kata ya Shangani kwa gharama ya shilingi milioni 232.98. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 117.38 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 0.55 kwa kiwango cha lami katika mtaa wa Maduka Makubwa ambapo mkandarasi anaendelea na ujenzi.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/21 barabara zenye urefu wa kilomita 22.37 zimefanyiwa matengenezo na kilomita 1.3 zinaendelea na matengenezo kwa gharama ya shilingi milioni 74.19 katika Kata za Ufukoni na Magomeni. Serikali inatambua ukuaji wa haraka wa Mji wa Mtwara naitaendelea kuupa kipaumbele cha barabara za lami na mifereji ya maji ya mvua kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. MWANTUMU M. ZODO K.n.y. MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mtwara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2018/2019 hadi Mei, 2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Hospitali hiyo inajengwa katika Kituo cha Afya Nanguruwe ambacho kitapandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Halmashauri baada ya kuongeza miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Mei, 2021 ujenzi wa majengo matano umekamilika. Ujenzi wa wodi tatu za kulaza wagonjwa unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2021. Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba katika Hospitali ya Halmashauri. Vilevile katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara. Ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -
Majengo mengi katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara yamechakaa; je, ni lini Serikali itaanza ukarabati wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara - Ligula ni moja kati ya Hospitali za muda mrefu hapa nchini ambazo miundombinu yake imechakaa sana. Katika jitihada za kuboresha miundombinu ya Hospitali hiyo, kwenye bajeti ya 2020/2021 kiasi cha shilingi milioni 201 kimetolewa kwa ajili ya ukamilishwaji wa jengo la kuhifadhia maiti ambalo ujenzi wake umekamilika na vifaa vimenunuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha shilingi bilioni moja kimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa Majengo ya Wagonjwa wa Nje (OPD), wodi za wanaume na wanawake, upasuaji, wodi ya uangalizi maalum na kichomea taka. Ukarabati huo unatarajiwa kukamilika Machi, 2022. Ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itashughulikia urejeshwaji wa Fedha za Wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini ambao walijiunga na Pride kwa ajili ya kupata mkopo?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama inavyokumbukwa kuwa kulikuwa na shauri mahakamani lililofunguliwa mwaka 2016 kuhusu umiliki wa Kampuni ya Pride; baada ya kukamilika kwa shauri hilo na kutolewa hukumu tarehe 11 Novemba, 2018 kuwa Kampuni ya Pride Tanzania ni mali ya Serikali, Serikali ilifanya tathmini ya hali ya kampuni na kufuatiwa kwa ukaguzi maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kutambua kuwa mali na madeni ya Kampuni hiyo ambapo taarifa ilionesha kuwa Kampuni hiyo ina madeni makubwa kuliko mali zilizopo.
Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa hiyo, Wizara ya Fedha na Mipango imeielekeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kusimamia ufilisi wa Kampuni hiyo kwa kufuata taratibu za ufilisi wa Makampuni. Hivyo, kwa sasa Kampuni ya Pride ipo katika hatua za ufilisi. Madai yote yanayohusu Kampuni hiyo yatashughulikiwa kwa kufuata taratibu za ufilisi.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu Kata ya Jangwani na Mtawanya Manispaa ya Mtwara Mikindani?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Selemani Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kata ya Jangwani iliyopo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani inapata huduma za mawasiliano kutoka kwa Kampuni za Tigo, Airtel na Vodacom. Vile vile maeneo ya Kata ya Mtawanya yanapata huduma hafifu za mawasiliano kutoka kwa watoa huduma wa Airtel, Vodacom na Tigo kupitia minara iliyojengwa katika Kata ya Likombe juu ya Mlima wa Lilungu.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote itavifanyia tathmini na uhakiki wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano maeneo yote yaliyopo katika Kata za Jangwani na Mtawanya na kuchukua hatua stahiki mara moja ili kuimarisha na kuboresha huduma endapo utatuzi hautahitaji ujenzi wa minara mipya.
Mheshimiwa Spika, endapo tathmini hiyo itabaini utatuzi wa changamoto zilizopo unahitaji ujenzi wa minara mipya, maeneo husika katika kata hizi yataainishwa na kuingizwa katika zabuni za kufikisha huduma ya mawasiliano zitakazotangazwa katika mwaka wa fedha 2023/2024. Ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itasaidia vikundi vya Uvuvi katika Jimbo la Mtwara Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhamasisha wavuvi kuunda vyama vya ushirika pamoja na kuviunganisha na taasisi mbalimbali za fedha kwa ajili ya kupata mikopo ya kuboresha shughuli zao za uvuvi, kukuza uchumi wao binafsi na Taifa ambapo hadi sasa kuna jumla ya vyama vya ushirika 170 nchi nzima. Kati ya vyama hivyo, vitatu viko katika Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara imetoa mkopo wa shilingi milioni nane kwa Kikundi cha Uvuvi cha Kaza Moyo Mtwara kwa ajili ya kununua injini na nyavu. Aidha, kupitia mradi wa unaoratibiwa na Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi kwa maana ya FETA, ufadhili wa UNDP Kikundi cha NASARC cha Mtwara Mjini na Kikundi cha wanawake cha Umoja ni Nguvu na chenyewe ni cha Mtwara Vijijini, vimejengewa jumla ya mabwawa 13 ya kufugia samaki wa maji baridi. Jumla ya wanufaika wa mradi huu ni wananchi 140 kutoka katika Vijiji vya Msanga Mkuu, Kijiji cha Mtawanya, Msijute na Mikindani. Mradi huu una thamani ya bilioni moja. Vilevile mradi umelipia gharama zote muhimu za uzalishaji ikiwemo kununua vifaranga na chakula cha samaki hadi kuvuna.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -
Je, ni lini jengo la Manispaa ya Mtwara Mikindani litajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jengo la Utawala la Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara – Mikindani lilijengwa mwaka 1948. Hivyo, jengo hilo limechakaa na halitoshelezi mahitaji ya Ofisi. Serikali inatambua umuhimu wa Halmashauri hiyo kujengewa jengo jipya kwa matumizi ya Ofisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Novemba, 2022 Halmashauri iliwasilisha maombi ya kutengewa bajeti katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala na nyumba ya Mkurugenzi. Serikali itatenga bajeti ya shilingi milioni 180 katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba ya Mkurugenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele cha kukamilisha majengo ya utawala yaliyoanza kujengwa kisha itaendelea na ujenzi wa majengo mapya ya utawala likiwemo jengo la Halmashauri ya Mtwara Mikindani. Ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Daraja la Kilambo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hasan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Daraja la Kilambo linalopendekezwa kujenga litaunganisha Nchi ya Tanzania na Msumbiji katika Barabara ya Mangamba – Madimba – Tangazo – Kilambo yenye kilometa 36.8 Mkoani Mtwara. Kwa kuwa ujenzi wa daraja hili utahusisha Nchi mbili za Tanzania na Msumbiji, Serikali tayari imeanza mazungumzo ya awali na Nchi ya Msumbiji ili ziweze kukubaliana kuhusu ujenzi wa daraja hilo, ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itawasaidia Wananchi wa Mtwara Mjini waliojiunga na PRIDE kurejeshewa fedha zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya tathmini ya hali ya Kampuni ya PRIDE na kufuatiwa na ukaguzi maalum uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu kutambua mali na madeni ya kampuni hiyo. Kufuatia tathmini hiyo, Serikali inaendelea na taratibu za kisheria za kuifilisi PRIDE.
Mheshimiwa Spika, Madeni yatalipwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za ufilisi na yanatarajiwa kukamilishwa ifikapo Julai 2023. Ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la abiria katika uwanja wa ndege Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Naibu Spika, jengo la abiria katika kiwanja cha ndege cha Mtwara litajengwa katika awamu ya pili ya ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho. Hivyo, fedha itatolewa baada ya kukamilika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Mradi huu, ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Daraja la Mto Ruvuma ili kufungua Shughuli za Kibiashara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Selemani Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali za Tanzania na Msumbiji zilijenga Daraja la Umoja (Mtambaswala) ili kufungua shughuli za kibiashara. Kwa sasa Serikali ya Tanzania inategemea kuanza kufanya mazungumzo na Serikali ya Msumbiji, ili kuanza taratibu za ujenzi wa Daraja la Kilambo, Mto Ruvuma.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itazilipa fedha Kampuni za Usambazaji wa Mbolea na Viuatilifu Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasan Seleman Mtenga, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kulipa madai ya Kampuni na Mawakala wa pembejeo yaliyotokana na usambazaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na viuatilifu kwa wakulima hapa nchini. Madai hayo ni pamoja na madai ya Kampuni na Mawakala waliosambaza pembejeo kwa mfumo wa ruzuku katika msimu wa 2015/2016 katika Mikoa 24 ya Tanzania Bara ukiwemo Mkoa wa Mtwara. Madai hayo yalifanyiwa uhakiki na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Hadi kufikia Septemba, 2023 kiasi cha shilingi 42,440,275,705.00 kimelipwa kwa Kampuni na Mawakala 307 wanaostahili kulipwa. Kati ya kiasi hicho, shilingi 679,750,000 zimelipwa kwa kampuni zinazohudumu Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa 2021/2022 na msimu wa 2022/2023, Serikali iliratibu usambazaji wa tani 28,576.70 za sulphur, lita 4,181,824.50 za viuatilifu vya maji na mabomba 1,337 yenye thamani ya shilingi 156,325,550,300.00 kwa ajili ya wakulima wa korosho katika maeneo ya uzalishaji ikiwemo Mtwara. Kati ya kiasi hicho, Serikali imewalipa wazabuni kiasi cha shilingi bilioni 112.7, na deni lililobaki ni shilingi bilioni 43.5. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha malipo ya madeni hayo.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi baina ya Jeshi la Wananchi na Wananchi California Mtaa wa Mbae Mashariki, Mkoani Mtwara?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo linalozungumziwa lipo katika Kikosi cha Jeshi cha 665 kilichopo Naliendele Mkoani Mtwara. Eneo hilo linalokizunguka Kikosi hicho lilivamiwa na wananchi na mwaka 2014 wananchi walifungua shauri Mahakamani wakidai kumiliki eneo hilo. Hukumu ya shauri hilo ilitolewa mwaka 2021 ambapo Mahakama ilitupilia mbali madai hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupitia Bunge lako Tukufu kuwaomba wananchi kuelewa umuhimu wa maeneo ya jeshi kwa maslahi mapana ya ulinzi na usalama wa Taifa na kutoa ushirikiano. Aidha, naomba wananchi walio ndani ya eneo hilo la jeshi waweze kuondoka kwa kuzingatia taratibu na sheria.
MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaongeza Walimu wa Masomo ya Sayansi kwa Shule za Sekondari Mtwara Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya jitihada kila mwaka kuajiri walimu wa masomo mbalimbali wakiwemo wa masomo ya Sayansi. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 hadi mwaka 2022/2023, Serikali iliajiri walimu wa masomo ya Sayansi 8,425 ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani ilipata walimu 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023/2024 Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 wa masomo mbalimbali wakiwemo wa sayansi ambao watapangiwa vituo vya kazi katika maeneo yenye upungufu mkubwa ikiwemo Manispaa ya Mtwara Mikindani.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Daraja la Kilambo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatafuta fedha ili iweze kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Daraja la Kilambo. Baada ya kufanyiwa usanifu na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha, kwa ajili ya ujenzi. Ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Daraja la Kilambo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatafuta fedha ili iweze kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Daraja la Kilambo. Baada ya kufanyiwa usanifu na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha, kwa ajili ya ujenzi. Ahsante.