Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from hon Hassan Seleman Mtenga (25 total)

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nataka niulize swali la nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo inawezekana nikayapokea au nisiyapokee.

Mheshimiwa Spika, Bandari ya Mtwara ambayo tulipokea takribani bilioni 153 kwa ajili ya matengenezo makubwa sana. Lakini cha kushangaza bandari hii kwa nini isitumike kwa meli kubwa ambazo zinaweza zikabeba mizigo? Kwa sasa hivi kuna kampuni moja ya meli ambayo kampuni hii inaitwa Sibatanza hawa watu ndiyo ambao wanaleta meli pale peke yao na kuja kufanya kazi ya uchukuzi.

Swali la pili kwa kuwa tumepoteza rasilimali nguvu kazi za watu takribani wachukuzi 6200 wamepoteza ajira kwenye Bandari ya Mtwara ni lini Naibu Waziri tutaongozana kwenda kuzungumza na wale wachukuzi ili waelewe hatma yao ya kazi zao za kila siku walizokuwa wanazifanya kwenye bandari ya Mtwara? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imewekeza shilingi bilioni si 153 lakini bilioni 157 kuboresha Bandari ya Mtwara kwa kujenga gati na kuwekeza fedha nyingi hizi ni ili kuhakikisha kwamba Bandari ya Mtwara inatumika kwa meli kubwa.

Sasa juhudi zinazofanyika mpaka sasa hivi kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, moja ni kwamba Serikali tayari imeshafanya usanifu kujenga chelezo kwa ajili ya kujenga meli yetu chini ya MSCL ambayo itakuwa na uwezo wa kufanya biashara kati ya bandari ya Mtwara na bandari zingine. Lakini tayari Serikali imeshamshawishi mfanyabiashara Dangote aweze kutumia Bandari ya Mtwara kuleta bidhaa zake lakini pia na kusafirisha bidhaa zake.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ushoroba wa Mtwara kuanzia Mtwara, Tunduru, Songea, Mbinga mpaka Mbambabay barabara hii imekamilika tayari Serikali imeshafanya mazungumzo na upande wa wafanyabiashara wa Malawi kwamba waweze kutumia Bandari hii ya Mtwara, lakini pia mazungumzo yapo na upande wa Msumbiji Kaskazini Magharibi ili waweze kutumia bandari hiyo. Kwa maana hiyo tuna uhakika kwamba bandari hii itaendelea kufanyakazi kama ilivyokuwa imekusudiwa ndiyo maana Serikali imewekeza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuongozana na Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga kwenda Mtwara mimi nasema hili halina shida naomba baada ya hapa tukubaliane lini tunakwenda lakini pia tunampongeza Mheshimiwa Mtenga kwa kuhakikisha kwamba bandari hii inafanyakazi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nitoe shukurani kwa majibu, lakini nataka niseme kwa mradi ambao unazungumzwa wa TACTIC mradi huu nadhani ulishapangiwa fedha, lakini mpaka sasa hivi jinsi ninavyozungumza kuhusu Kata ya Magomeni na Ufukoni bado hali ni mbaya. Je, Serikali ni lini ujenzi wa barabara hizi utakua tayari?

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili ni lini miundombinu ya mifereji ambayo tulikua tunaizungumza toka mwanzo Serikali itakua tayari kuweza kuboresha mifereji ambayo sasa hivi mara kwa mara kunapatikana mafuriko makubwa na wananchi inatokea hali sinto fahamu kwenye majumba ya watu na wengine kupoteza maisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ametaka kufahamu ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ambazo ameziainisha zilizopo katika mradi wa TACTIC kwa kifupi ni kwamba mradi wa TACTIC bado katika hatua za mwisho za makubaliano na mahafikiano na Serikali ili zianze kutekezwa.

Kwa hiyo, Mbunge nikuhakikishie kabisa kwamba mara baada ya huu mradi kuwa umekamilika na Serikali kumaliza hatua zote, barabara hizo ambazo umeziainisha zitaanza kujengwa kwa sababu ziko katika mradi wa TACTIC.

Mheshimiwa Spika, vile vile, katika sehumu ya ule mradi wa TACTIC miongoni mwa component ambazo ziko ndani yake ni pamoja na ujenzi wa mifereji kwa hiyo, mradi huu utakapokua umefikia hatua za mwisho na ninaamini Serikali ipo katika mazungumzo na ninahuhakika kabisa mara itakavyokamilia basi barabara zako pamoja na mifereji ya wananchi wa Mtwara Mjini itajengwa kama ambavyo imeainishwa katika huo mradi ahsante sana.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini nina swali la nyongeza.

Kwa kuwa hospitali ile ni kongwe na mpaka sasa hivi kwenye Hospitali ya Ligula Mtwara haina x-ray machine, lakini katika suala hilo la kutokuwa na x-ray machine huduma za theatre kwa ujumla wake hazipo.

Je, ni lini Serikali sasa itaamua kututengenezea masuala mazima ambayo yanahusu package hiyo ya x-ray machine pamoja na jengo la theatre? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, je, ni lini Serikali itaratibu suala zima la kutuletea Madaktari Bingwa ambapo tunashida ya Madaktari Bingwa wa Watoto, Madaktari Bingwa wa Koo ambao vifo vinasababisha kuwa vikubwa sana kwenye hospitali yetu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Hassan Tenga kwa ufuatiliaji wake wa kina sana kwa suala zima la Hospitali ya Mkoa, lakini sio tu Hospitali ya Mkoa, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kwenye Wilaya yake.

Swali lake la kwanza ni lini hospitali hiyo itapata x-ray, lakini pamoja na vifaa vya theatre. Kama ambavyo nimekuwa nikisema hapa Rais wetu miezi michache iliyopita alitoa shilingi bilioni 123 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa na hospitali yake hiyo ipo kwenye bajeti kwa ajili ya vifaa husika ambavyo ameulizia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili analoulizia ni suala ambalo mimi na yeye kama ambavyo nimemuomba la madaktari kupelekwa kwenye hospitali yake; na ni ukweli kwamba kuna tatizo la madaktari kwenye maeneo mengi tu sio eneo la kwake na kuna makakati huo sasa wa ajira mpya ambazo zinakuja tunamfikiria lakini mimi na yeye kama tulivyopanga tutakwenda kwenye hospitali yake kufuatilia Hospitali ya Mkoa tutakwenda pamoja tutaona tatizo ni kubwa kiasi gani tuone tunafanya nini kuhamisha sehemu nyingine ili madaktari waweze kusaidia eneo hilo.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa shauri hili lilizungumzwa toka mwaka 2018 na Ofisi ya Msajili Hazina wakapewa jukumu la kulisimamia tuna miaka zaidi ya mitatu sasa hivi imeshapita: Je, ni lini tutaelezwa kwamba shughuli hii itakuwa imemalizika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Wananchi wa Mtwara ambao wanadai zaidi ya shilingi milioni 250: Ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja kuzungumza na wananchi wa Mtwara ili waelewe mustakabali mzima wa fedha zao ambazo zimepotea mpaka sasa hivi haijulikani watalipwaje? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mtenga kwa kufuatilia sana masuala ya wananchi wake wa Jimbo la Mtwara. Mara kwa mara akija ofisini anafuatilia masuala yanayohusu wananchi wa Mtwara katika sekta mbalimbali na anatumia vizuri uzoefu wake wa kuwa Katibu wa Mkoa wa Chama na maeneo tofauti tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kwanza kwamba jambo hili limechukua muda, ni kweli lilichukua muda kwenye hatua za awali kwa sababu lilipokuwa kwenye ngazi za kimahakama, hatua nyingine hizi zisingeweza kufanyika, lakini baada ya kuwa shauri hilo limeshaamuliwa na Mahakama, kwenye hizi hatua nyingine, zinaweza zikafanyika kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba wananchi wake watapata uhakika haraka tu. Naamini nami nitapata uhakika kutoka kwa Msajili wa Hazina ili niweze kumuarifu makadirio hasa ya muda aliyokuwa anataka aujue kuwa ni lini?

Mheshimiwa Spika, hili la pili kwa ridhaa yako, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tukishamaliza Bunge tutapanga utaratibu ili tuweze kuwaandaa wahusika hao, nami niweze kufanya ziara kuweza kuwaelimisha nikiwa tayari na majibu ya uhakika kutoka kwa Msajili wa Hazina kuhusu kipindi ambacho kitatumika kuweza kuhakikisha kwamba hatua hizo za kiutawala zitakuwa zimekamilika.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba nataka nielewe sisi kule kwetu Mtwara nimechimbiwa visima vitatu katika Jimbo langu, lakini takriban mpaka sasa hivi karibu miezi minne inakimbilia na mvua zinaanza kunyesha na visima vile tayari vimeshaanza kuziba.

Ni lini sasa visima vile vitamaliziwa kwa taratibu zingine za upatikanaji wa maji? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mwenyezi Mungu; Mheshimiwa Rais alitupatia fedha na visima vimechimbwa, kinachofuata ni mtandao wa usambazaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninatoa agizo kwa Mameneja wa Mtwara wafanye kazi haraka iwezekanavyo ndani ya mwezi mmoja, waweze kuona kwamba utaratibu wa mwendelezo wa visima hivi inaweza kufanyika. (Makofi)
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mtwara Mjini ni jimbo ambalo kwa sasa linaongoza kwa ukatikaji wa umeme kwa kila siku, mikatiko inaweza ikafika zaidi ya 30 kwa siku. Je, ni lini Serikali itaiingiza Mtwara na Lindi kwenye gridi ya Taifa na sisi tukafaidika na umeme wa gesi ambayo inatoka Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwashukuru wana- Mtwara kwa kuwa, sehemu kubwa sana ya umeme ambayo inalisha nchi hii kwenye gridi ya Taifa inatokea katika Mkoa wa Mtwara. Na nimuahidi kwamba, katika mipango ambayo Serikali ikonayo ni kuhakikisha kwamba, sasa umeme ambao unazalishwa tayari kwenye gridi ya Taifa na kwenyewe uweze kufika. Niseme kwenye mipango tuliyokuwanayo kufikia 2025 itakuwa imefikia hatua sasa ya kuamua ni lini gridi ya Taifa itafika katika Mkoa wa Mtwara na Mkoa wa Lindi kwa ajili ya kufikisha huduma nzuri zaidi.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri niliongozana naye mwaka jana kwenda Mtwara kuangalia maeneo ambayo yana matatizo ya mawasiliano ikiwepo bandarini pale Mtwara, pale Mitengo kwenye Hospitali ya Rufaa.

Sasa nahitaji commitment ya Serikali, kwa kuwa tulishawahi kwenda na mwenyewe ukaangalia uhalisia. Ni lini sasa minara hii itapatikana kwenye maeneo husika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa tuliongozana na Mheshimiwa Mbunge kuangalia changamoto ya mawasiliano katika maeneo haya. Lakini tulitoa maelekezo kwa operator wote ambao wanatoa huduma ya mawasiliano katika maeneo haya ili kuweza kufanya optimization ili kutatua changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, kwa vile Mheshimiwa Mbunge bado anaonesha kuna changamoto pale, basi tutatuma wataalam wetu ili waweze kufanya tathimini ili tujirizishe kama kuna uhitaji wa ujenzi wa minara katika maeneo hayo. Nakushukuru sana.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Jimbo la Mtwara Mjini ni jimbo ambalo kidogo lina shida ya maji, lakini niishukuru Serikali kwa kutuletea bilioni 19 kwa ajili ya usambazaji wa maji kwenye Jimbo la Mtwara Mjini. Hata hivyo, tumechimba visima toka mwaka jana na vile visima vitatu mpaka sasa hivi havina mwelekeo wowote. Je, ni lini Serikali itamaliza visima hivi ili wananchi wapate maji kwenye Jimbo la Mtwara Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nnaomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nipende kupokea pongezi zake kwa Serikali kwa kazi kubwa ambayo imeshafanyika Mtwara. Kupitia visima hivi hata jana tumeongea na Mheshimiwa Mbunge, tayari nimeshawaagiza wale watendaji wetu pale Mtwara wanakwenda kulifanyia kazi na hili ni agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu, maeneo yote ambayo visima vilishachimbwa sasa hivi watendaji ni lazima kuvipa vipaumbele ili kuhakikisha vinasambaza maji kwenye maeneo yote ya wananchi.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa barabara ya kutoka Mtwara mpaka Msimbati, ambayo takribani sasa ina zaidi ya miaka 15, barabara hii inajengwa kwa vipande vipande? Sasa hivi wamejenga kilometa tano tu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtenga, Mbunge wa Mtwara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii tunajenga kwa awamu kadiri fedha inavyopatikana. Azma ya Serikali ni kujenga barabara yote. Kwa hiyo Serikali inatafuta fedha ili zikikamilika basi tuweze kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Naibu Waziri kwa kunipa majibu yake mazuri sana ambayo nimeyapokea.

Mhshimiwa Spika, Jimbo la Mtwara Mjini ndiyo Jimbo ambalo linazungukwa na bahari. Kwa namna moja au nyingine, vijana wengi wa Mtwara Mjini shughuli zao zinahusika kwenye bahari: Je, ni lini Serikali itanihakikishia kwenye vikundi zaidi ya 30 ambavyo tuliahidiwa kwamba vitapata vitendea kazi, nyavu na vitu vingine, vitasaidiwa? Nipate majibu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Tunazungumzia bahari kama bahari: Ni lini Serikali itatuletea meli ya uvuvi ili vijana hawa waweze kupata ajira na samaki ambao wanapotea kwa njia bahari tuweze kunufaika sasa Tanzania kama nchi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kwanza naomba radhi kwa kutokupata majibu haya kwa ufasaha katika meza yako. Naomba nikuahidi kwamba tutafanya marekebisho ya utaratibu huu usirejee tena.

Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hassan Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini kwanza kwa kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya hasa ile niliyotangulia kuijibu katika jibu la msingi la kuwavuta wawekezaji na kukubali kuwasaidia wana- Mtwara.

Mheshimiwa Spika, kuhusu tutawasaidiaje vijana katika vikundi hivi 30 alivyovitaja waweze kununua nyavu na injini; matarajio yetu katika bajeti inayokuja ya 2022/2023, tunao utaratibu mzuri ambao tutakaposoma bajeti yetu, nataka niwaahidi Waheshimiwa Wabunge wengi, wataona matumaini makubwa ambayo yataenda kujibu swali hili la Mheshimiwa Mtenga. Kwa hiyo, ni matarajio yetu katika mwaka ujao wa fedha, viko vikundi vya vijana vitakavyopata fursa ya kwenda kupata mikopo nafuu ambapo wataweza kununua nyavu na injini.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni juu ya ununuzi wa meli ambazo zitatoa pia ajira kwa vijana. Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ina mkakati mzuri wa kwanza kwa kujenga Bandari ya Uvuvi. Bandari ambayo itajengwa katika Mji wa Kilwa Masoko. Vilevile tunayo bajeti ya kwenda kununua meli za uvuvi zipatazo nne. Meli hizi zitakwenda kuajiri vijana wa Kitanzania wakiwemo vijana kutoka katika Jimbo la Mheshimiwa Hassan Mtenga, kwa maana ya pale Mtwara Mikindani. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina swali moja la nyongeza. Iliundwa tume ya kuja kuangalia jengo lile la Mtwara tangu mwaka 2020 na tume ile ikapendekeza kwamba jengo lile lisitumike;

Je, ni lini sasa Seriali itaamua kutuletea fedha ili tuweze kupanga sehemu nyingine kwa sababu jengo lile haliko salama sasa kwa wafanyakazi waliopo mule ndani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua kwamba jengo lile ni la siku nyingi na ni chakavu na kwa kweli halina sifa ya kuendelea kutumika kama jengo la halmashauri. Hivyo, Serikali imeweka kipaumbele baada ya kukamilisha majengo haya ambayo mengi yako katika hatua za ukamilishaji katika halmashauri zile mpya, tutakwenda kwenye halmashauri kongwe ikiwepo Halmashauri ya Mtwara Mikindani na nimwakikishie kwamba tutahakikisha kwamba Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo hilo, ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru, nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna barabara ambayo inatoka Mtwara Mnivata inayojengwa kwa kiwango cha lami kuelekea Newala mpaka Masasi. Kwa taratibu ambazo zinaendelea sasa hivi kuanzia Mnivata – Newala – Masasi wapo kwenye hatua za kulipa malipo kwenye zile nyumba ambazo zimeondolewa na miche. Lakini kipande cha kilometa 50 ambacho tayari kimejengwa barabara ya lami mpaka leo wananchi hawajalipwa fedha zao kama fidia. Je, ni lini Serikali itarudi kuwalipa fidia wananchi wale?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi barabara Mtwara – Mnivata imetekelezwa kwa fedha ya Serikali ya Tanzania na Barabara ya kuanzia Mnivata – Newala kwenda Masasi itatekelezwa kwa kusaidiana na wahisani ambao ni African Development Bank.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwamba kama kuna wananchi ambao katika eneo la Mtwara Mnivata bado wana changamoto ikiwa ni nje ya zile kilometa 45 tuweze kuonana nae ili niweze kupata taarifa kamili kwa wananchi ambao bado wanadai fidia eneo hili la Mtwara – Mnivata kilometa 50.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mtwara Mjini ndio kwenye Kituo Kikuu cha Polisi. Kituo hicho kilijengwa toka mwaka 1962, kwa sasa kituo hicho ni chakavu mno na inapelekea Askari kufanyia kazi kwenye mwembe. Je, ni lini Serikali itakwenda kufanya ukarabati kwenye kituo hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, tunatambua hali ya uchakavu wa Kituo cha Polisi ngazi ya Wilaya Mtwara. Hata hivyo, katika bajeti yetu ya mwaka 2023/2024, fedha zimetengwa za kuanza kufanya ukarabati kwenye kituo hicho. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na matumaini kwamba mwaka 2023/2024 kituo hicho kitakarabatiwa, nashukuru.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimshukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini swali la kwanza; ni lini upembuzi yakinifu na usanifu wa kina utafanyika kwenye daraja hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali ya Mozambique iko tayari kutoa ushirikiano wa ujenzi wa daraja hilo, ni lini mazungumzo haya yatakuwa yanaendelea kwa kina? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kwa pamoja, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kutambua umuhimu wa barabara hii kwa upande wa Tanzania, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi upande wa Tanzania tuko tayari kuijenga hiyo barabara na katika mwaka huu wa fedha ambao tunakwenda kuleta bajeti, tumeweka fedha kwa ajili ya kuanza kufanya maandalizi ya kufanya usanifu na kufanya upembuzi na usanifu wa kina, lakini kama nilivyosema kazi hiyo itaanza tu pale ambapo tutakuwa tumekamilisha na wenzetu wa Msumbiji kwa sababu ni daraja la pamoja, ahsante. (Makofi)
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana Mheshimiwa Waziri aliahidi kuja Mtwara kuzungumza na wadeni hao. Je, Mheshimiwa Waziri upo tayari kuja Mtwara kuja kuzungumza na hawa ambao wana wadai? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wananchi wa Jimbo la Mtwara wameahidiwa mara kwa mara juu ya majibu ya Mheshimiwa Waziri. Sasa ni lini sasa mtakuja kuwapa fedha zao hao wananchi wa Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hassan Mtenga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mimi niko tayari kabisa kwenda kuwasikiliza na kukaa na wananchi wa Mtwara Mjini kuhusu madai yao mara tu baada ya Bunge kumalizika tutakaa na Mheshimiwa Mtenga tuende kukutana na wananchi hao.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kama nilivyojibu katika swali la msingi kwamba taratibu za ufilisi zinaendelea na kuanzia Julai mwaka wa fedha unaokuja tunaenda kuwalipa wananchi kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa uwanja wa Mtwara inawezekana tukauita international airport kwa sasa package yake ya mradi ule ulikuwa ni kuwepo na gari ya zimamoto nikimaanisha fire. Je, ni lini sasa Wizara itahakikisha kwamba mkandarasi anatuletea gari ya zimamoto pale airport?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili uwanja wa airport umepakana na maeneo ya wananchi, lakini baadhi ya maeneo ya wananchi lilipita bomba la gesi na wananchi wale wakalipwa. Sasa ni lini Serikali itaamua kuwalipa wananchi ambao bado hawajalipwa ili waondokane na adha hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini kama ifuatavyo:-

Naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ukarabati na upanuzi wa uwanja huu suala la gari la zimamoto ni sehemu ya mradi huu na tayari mkandarasi ameshatoa order gari itanunuliwa kutoka Ujerumani na thamani yake itakuwa ni bilioni 1.4. Kwa hiyo tayari gari limeshaanza kutengenezwa kwa ajilli ya uwanja wa Mtwara, ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; naomba commitment ya Serikali, ni lini ujenzi huo wa daraja utaanza?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni lini Mheshimiwa Waziri tutaongozana nami ili twende kwenye eneo husika ambalo tunalizungumzia la kujenga daraja apate ufumbuzi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hassan Selemani Mtenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza anataka commitment ya Serikali kwamba, lini ujenzi huu hasa utaanza katika daraja hili la Mto Ruvuma, eneo la Kilambo. Nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amekuwa akifuatilia suala zima la daraja hili katika Mto huu Ruvuma, sababu tunatambua kwamba, daraja hili ni kiungo muhimu kati ya Nchi yetu ya Tanzania na Nchi ya Msumbiji. Kwa maana hiyo, mazungumzo ambayo tutayaanza hivi karibuni pamoja na Nchi ya Msumbiji kupitia Wizara yetu ya Mambo ya Nje, tutafanya commitment kupitia pia Wakala wetu wa Barabara Nchini (TANROADS) ili tuanze sasa mchakato mzima wa kuanza kujenga daraja hili, maana daraja hili lazima lijengwe na nchi mbili kati ya Tanzania na Msumbiji.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kwenda naye kuona hili eneo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mara baada ya Bunge hili la Bajeti, mwezi Julai nitakuwa na ziara, hivyo nitakwenda kwa Mheshimiwa Mbunge kutembelea eneo hili. (Makofi)
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna agenda ya Mtwara Corridor na tunapozungumza Mtwara Corridor tunazungumza bandari, tunazungumza Airport pia tunazungumza reli ya Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umekuwa ni wimbo toka mwaka 2020 mpaka leo hii Serikali kila ikija hapa wanasema ipo kwenye mpango. Tunataka sasa tufahamu ni lini sasa ujenzi wa reli hii ya Liganga na Mchuchuma.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimwa Mwenyekiti, nafikiri Mheshimiwa Mtenga anataka kupata pengine ufafanuzi wa ziada. Nimekwishasema na naomba nirejee. Tulishaanza SGR ya kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Isaka, tumekwishaenda na SGR kutoka Dar es Salaam tumekwenda mpaka Kigoma sasa tunakwenda mpaka Msongati Burundi. Awamu inayofuatia Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua na imejiwekea malengo ya kwenda SGR Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe mashaka uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita unakwenda kujenga reli ya SGR ya kusini ambayo ni Mtwara Corridor kama nilivyosema. Hii inakwenda kuungana pamoja na uboreshaji mkubwa wa Airport kama nilivyosema sambamba na uboreshaji mkubwa wa maeneo ambayo nimeyaeleza pale awali, kwa hiyo, nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna agenda ya Mtwara Corridor na tunapozungumza Mtwara Corridor tunazungumza bandari, tunazungumza Airport pia tunazungumza reli ya Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umekuwa ni wimbo toka mwaka 2020 mpaka leo hii Serikali kila ikija hapa wanasema ipo kwenye mpango. Tunataka sasa tufahamu ni lini sasa ujenzi wa reli hii ya Liganga na Mchuchuma.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimwa Mwenyekiti, nafikiri Mheshimiwa Mtenga anataka kupata pengine ufafanuzi wa ziada. Nimekwishasema na naomba nirejee. Tulishaanza SGR ya kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Isaka, tumekwishaenda na SGR kutoka Dar es Salaam tumekwenda mpaka Kigoma sasa tunakwenda mpaka Msongati Burundi. Awamu inayofuatia Serikali ya Awamu ya Sita imejipambanua na imejiwekea malengo ya kwenda SGR Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe mashaka uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita unakwenda kujenga reli ya SGR ya kusini ambayo ni Mtwara Corridor kama nilivyosema. Hii inakwenda kuungana pamoja na uboreshaji mkubwa wa Airport kama nilivyosema sambamba na uboreshaji mkubwa wa maeneo ambayo nimeyaeleza pale awali, kwa hiyo, nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nina swali moja la nyongeza;

Je, ni lini mfuko wa pembejeo utarejeshwa ili Serikali iweze kumaliza haya matatizo yote ya ulipaji wa madeni ya watu ambao wanaleta mbolea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba, jambo hili liko katika mchakato na sisi kama Wizara ya Kilimo tunalipitia upya ili kuhakikisha tunaondokana na hizi changamoto, kwa hiyo tutakapolimaliza tu, tutalirudisha kwa wananchi mara moja kama ilivyokuwa hapo awali ili kuondokana na kero hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo jambo hili tumelipokea.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri, kwa majibu mazuri. Nina swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo tajwa, lina wanajeshi zaidi ya 10 wapo kwenye maeneo hayo na wamejenga nyumba na wana hatimiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu, ni lini Serikali itakwenda kufuta hati zile, kwa sababu wanajeshi wale wanakuwa wanawapiga wananchi kwenye maeneo mengine na kuwavunjia nyumba ambazo zimejengwa na wanajeshi pale ambazo zina hati kwenye eneo la Jeshi, bado wanaendelea kukaa?



Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni lini Mheshimiwa Waziri tutaongozana kwenda kwenye eneo husika na wewe ukajionee hali halisi ili tuweze kutatua mgogoro huo kidiplomasia. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa vile Mheshimiwa Mbunge ameomba tuongozane nikaone hali halisi basi haya yote nitayaona tutakapotembelea eneo hilo na nakubaliana kuongozana naye. (Makofi)
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri ya ujenzi huo wa ofisi.

Swali la nyongeza, kwa kuwa Serikali ilitoa fedha nyingi sana kwenye ujenzi huo na majibu ambayo nimeyapata ni mazuri, lakini niiombe Serikali kwa sasa bado hali haijawa nzuri kwenye miundombinu ambayo imebakia.

Je, ni lini Serikali mtaikamilisha ile miundombinu kwa sababu kituo kile tayari kimekwishaanza kutumika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imeamua kuleta huduma kule chini kwa wananchi, tunayo Kata moja ya Chikongola ambayo ina Kata moja ya Magomeni katika Jimbo la Mtwara mjini ina watu zaidi 29000.

Ni lini Serikali itatuletea kituo cha afya ili kuboresha huduma za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imefanya tathmini na kubaini kwamba zinahitajika shilingi milioni 883.7 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la utawala, lakini inahitaji milioni 176 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la hospitali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imetengeneza mikakati na ukamilishaji wa majengo hayo yapo katika mpango wa Serikali na Serikali itaendelea kutenga fedha kuhakikisha inakamilisha majengo haya muhimu.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge linahusu uhitaji wa kituo cha afya kuhudumia idadi kubwa ya wananchi 29,000 nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake hili la Mtwara Mjini tayari Serikali imepokea maombi ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati na Mheshimiwa Mbunge na yeye ameleta eneo lake mahsusi ambalo anaona kwamba linahitaji ujenzi wa kituo cha afya na bila shaka eneo hilo kwa kauli ya Mheshimiwa Mbunge ndio hili aliloliombea hapa fedha.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mipango ya upatikanaji wa fedha wa kujenga vituo vya afya vya kimkakati tutazingatia maombi yake ili kituo cha afya kiweze kujengwa.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini kwa kuwa, wenzetu wa Mozambique wameanza kutengeneza barabara ya lami karibu kilometa 20 kutoka Mozambique kuja Mto Kilambo. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali na wao wataanza kujiandaa kutengeneza barabara ya lami ambayo itatoka kwenye Kata ya Ziwani kuelekea kwenye eneo la Daraja?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni eneo tunalozungumza la Daraja. Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari tukaongozana na wataalamu wako wa Wizara kwenda kuona eneo ambalo ninalizungumzia mimi kwa takribani miaka mitatu mfululizo sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, naomba tu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunatambua kwamba daraja hili ni muhimu. Ndiyo maana tumekuwa tukitenga kiasi kidogo cha fedha, kwa ajili ya kuweza kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Mheshimiwa Spika, hili pia ni daraja ambalo linaunganisha nchi yetu ya Tanzania na Msumbiji kupitia Mtwara. Pia, ili Daraja hili kubwa ambalo pengine litakuwa na urefu si chini ya kilometa tatu, tuna taasisi mbalimbali ambazo ni lazima zihusike; sisi, kama Wizara ni wajenzi tu, lakini Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje kwa sababu, inahusisha nchi na nchi na pia, wenzetu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, wenzetu wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa sababu, ni Daraja ambalo linaunganisha nchi na nchi, tuweze kufikia maamuzi. Pia, tayari kuna mazungumzo ambayo yapo yanaendelea, yakishakamilika na sisi Wizara tukiambiwa tuanze, tutaanza kulijenga hilo daraja.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kwenda kulitembelea, niko tayari muda wowote tutakapopanga na Mheshimiwa Mbunge. Ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini kwa kuwa, wenzetu wa Mozambique wameanza kutengeneza barabara ya lami karibu kilometa 20 kutoka Mozambique kuja Mto Kilambo. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali na wao wataanza kujiandaa kutengeneza barabara ya lami ambayo itatoka kwenye Kata ya Ziwani kuelekea kwenye eneo la Daraja?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni eneo tunalozungumza la Daraja. Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari tukaongozana na wataalamu wako wa Wizara kwenda kuona eneo ambalo ninalizungumzia mimi kwa takribani miaka mitatu mfululizo sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, naomba tu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunatambua kwamba daraja hili ni muhimu. Ndiyo maana tumekuwa tukitenga kiasi kidogo cha fedha, kwa ajili ya kuweza kuanza upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

Mheshimiwa Spika, hili pia ni daraja ambalo linaunganisha nchi yetu ya Tanzania na Msumbiji kupitia Mtwara. Pia, ili Daraja hili kubwa ambalo pengine litakuwa na urefu si chini ya kilometa tatu, tuna taasisi mbalimbali ambazo ni lazima zihusike; sisi, kama Wizara ni wajenzi tu, lakini Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje kwa sababu, inahusisha nchi na nchi na pia, wenzetu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, wenzetu wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa sababu, ni Daraja ambalo linaunganisha nchi na nchi, tuweze kufikia maamuzi. Pia, tayari kuna mazungumzo ambayo yapo yanaendelea, yakishakamilika na sisi Wizara tukiambiwa tuanze, tutaanza kulijenga hilo daraja.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kwenda kulitembelea, niko tayari muda wowote tutakapopanga na Mheshimiwa Mbunge. Ahsante.
MHE. HASSAN SELEMAN MTENGA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itatupa fedha za kujenga jengo la Manispaa ya Mtwara Mjini ambalo limejengwa takriban miaka ya 60 iliyopita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA – (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, jengo la Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani ni kongwe na tayari Mheshimiwa Mbunge alishaleta taarifa hiyo na halmashauri walishawasilisha gharama zinazohitajika kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo. Namhakikishia tu Mheshimiwa Mbunge, kwenye bajeti ambazo tunaendelea kutenga kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutatoa kipaumbele, kwa ajili ya jengo la Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani. Ahsante.