Contributions by Hon. Eric James Shigongo (30 total)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge hili. Naishukuru familia yangu, Wajumbe wote na wananchi wote wa Buchosa walionipa nafasi ya kuwa hapa, Chama changu Cha Mapinduzi, Mwenyekiti, Katibu wa Chama chetu cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nachukua nafasi hii kuwashukuru sana viongozi wa nchi yetu waliotangulia ambao kwa uwepo wao, maisha yangu leo ni bora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi yetu leo hapa ni kujadili hotuba mbili za Mheshimiwa Rais. Nami nimepata bahati ya kuzisoma kama walivyozisoma wenzangu wote, nimezisoma na nimezielewa. Katika kuzisoma kuna kitu kimoja kikubwa nilichokigundua kwamba Mheshimiwa Rais anawaamini sana Wabunge wake na anaamini kwamba hakuna kiongozi duniani anayefanikiwa peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Musa alichagua wazee; Yesu Kristo alikuwa na wanafunzi wake 12; na Mtume Muhammad alikuwa na Maswahaba wake. Kwa hiyo, sisi hapa ndani ni Maswahaba wa Mheshimiwa Rais, ametuamini, amekuja kutusomea hotuba hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusoma, nimekumbuka kitabu kimoja nilikisoma kinaitwa Checklist Manifesto. Kwa wale ambao wamekisoma watagundua kwamba hotuba hizi mbili za Mheshimiwa Rais ni Checklist Manifesto mbili; ya kwanza ilikuwa ya 2015 – 2020 ambayo inaonyesha mambo ambayo Mheshimiwa Rais alitaka kuyafanya kwenye kipindi cha miaka mitano. Nikiwauliza kwenye Checklist Manifesto, kazi yako ni ku-list mambo yako, unatiki moja baada ya lingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikikuuliza wewe na Waheshimiwa Wabunge kwamba kwenye miundombinu, Mheshimiwa Rais ametiki au hajatiki?
WABUNGE FULANI: Ametiki! (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwauliza kwenye umeme, Mheshimiwa Rais ametiki, hajatiki? Kwenye barabara, ametiki hajatiki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mengi yametikika. Sasa tuna Cheklist Manifesto ya pili ya mwaka 2020 – 2025, ni checklist ngumu zaidi ya checklist tuliyomaliza. Ni ngumu kwa sababu nchi yetu iko kwenye uchumi wa kati. Ni checklist ambayo siyo rahisi kama iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuja kwenu na nazungumza mbele yako na mbele ya Watanzania wote kuwakumbusha kwamba kasi tuliyonayo ni kubwa. Mengi yamefanyika, kazi kubwa imefanyika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote, lakini nataka niwakumbushe kwamba kazi tuliyonayo mbele ni kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu mmoja aliwahi kusema kwamba the smallest of implementation is better than the biggest of intensions. Kama hatutatekeleza hotuba hii, tukabaki na mazungumzo ya hotuba nzuri, hakika hotuba hii ya Mheshimiwa Rais itabaki ni intensions peke yake, hakuna matokeo yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natokea private sector. Kwenye private sector hatuna hotuba nyingi sana, tuna utendaji peke yake. Nazungumza hapa nikiwaomba Waheshimiwa Wabunge, katika Checklist Manifesto ya pili 2025, tufanye kazi, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, tusimvunje moyo Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma katika hotuba yake, ukurasa siukumbuki vizuri, lakini amesema kwamba mazao ya bahari yangeweza kuiingizia nchi yetu shilingi bilioni 320 na kitu hivi kwa mwaka. Tunazozipata ni kidogo mno kwa sababu tulishindwa kudhibiti na kusimamia vizuri, (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia nyuma ya statement hiyo kwa mimi mwanafasihi, nagundua kwamba Mheshimiwa Rais alikuwa na manung’uniko, alikuwa na masikitiko. Nawaomba Waheshimiwa Mawaziri walioko hapa ambao mmepewa jukumu, mmefanya kazi nzuri sana kwenye checklist manifesto ya kwanza. Mmeaminiwa, fanyeni kazi, tumikeni, tengenezeni historia, tuko hapa kujenga historia yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wetu watakapokuja baada ya miaka 20 waseme maisha yao ni bora sana kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa kaka yangu Majaliwa. Watoto wetu wasimame waseme maisha yao ni bora kwa sababu sisi tulioko ndani ya ukumbi huu leo tutafanya maamuzi sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kuwaomba ndugu zangu, Watanzania wanatuamini, dunia inatutazama, tutakachokifanya hapa ndani katika kipindi cha 2025 ni kufanya maamuzi ambayo tutatekeleza ndoto ya Mheshimiwa Rais wetu. Viwanda ni ndoto ya Rais wetu lakini hakuna viwanda bila kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikomee hapo. Ahsanteni sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kusimama tena ndani ya Bunge hili Tukufu kutoa mchango wangu ndani kwa Taifa langu. Naomba tu niishukuru sana familia yangu, wapiga kura wangu kwa kazi kubwa waliyoifanya kunileta hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa matumaini. Najua nasikilizwa hap ana watu hapa ndani, lakini najua nasikilizwa na Watanzania sehemu mbalimbali ya nchi yetu. Naomba tu niseme hivi, nina matumaini makubwa kwa nchi yangu leo kuliko ilivyokuwa jana. My hope for this country is greater today than it was yesterday. Nataka niwaambie Watanzania wanaonisikiliza kwamba tunakokwenda ni kuzuri sana.
Sasa nina bahati ya kuwa hapa ndani leo, tangu nimeingia nasikiliza watu wanaongea, nasikiliza napata muda wa kujifunza. Namshukuru Mungu niko hapa ndani nashiriki, zamani nilikuwa nawaangalia mnaongea nikiwa nje. Najifunza kitu kimoja kikubwa sana. Ukiwa hapa ndani kuna wakati uweke fence kwenye akili yako, ujiwekee fence, useme hiki hakiwezi kuingia kwenye kichwa changu, hiki kinaweza kikaingia maana kuna mtu anaongea kitu halafu najiuliza hivi huyu hajui yanayoendelea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii inakua, tena inakua kwa kasi! Nani hajui tulipotoka? Nani hajui?
T A A R I F A
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe Taarifa Mheshimiwa Mbunge Eric Shigongo anayeongea kwamba katika Bunge hili sisi tuko kwa niaba ya wananchi tunatoa mawazo yetu na ya wananchi, kwa hiyo pana uhuru wa mawazo yote tunayoongea ni sahihi mahali hapa. Mwisho wa siku tunakuja na kitu kimoja. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shigongo hajamtaja mtu, endelea tu.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa hiyo sijaipokea kwa sababu sijamtaja mtu yeyote. Nataka niwaeleze Watanzania na niwaeleze watu wote walioko hapa ndani kwamba mnapoamua kujenga uchumi kuna transition period. Kuna kipindi cha mpito lazima mpite. Hata ukisoma historia ya China wakati wa Mao Tse Tung kulikuwa na kipindi kigumu sana walikipitia wale watu hatimae wakafika walipo leo. Yawezekana tunapita lakini tumeshaanza kupita kwenye transition hivi sasa mambo yanaenda kuwa safi. Nataka kuwaambia Watanzania wanaonisikiliza kwamba ya kwamba wawe na matumaini, wawe na imani na kiongozi wetu mkuu, wawe na Imani na Bunge hili ya kwamba tunakokwenda ni kuzuri na kazi inafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nichangie Mpango wa Mwaka mmoja na wa Miaka Mitano. Nasema hivi; nitachangia eneo la digital economy, uchumi wa kidijitali. Eneo la viwanda na nikipata nafasi nitachangia eneo la mitaala yetu ya elimu kwa ajili ya watoto wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia nizungumze mambo matatu tu ya muhimu kwamba we are a blessed country. Tanzania kama Tanzania ni nchi iliyobarikiwa sana. Kuna mtu alisema kwamba Mungu wakati anaumba dunia inawezekana siku ya saba alikuwa yuko Tanzania, maliasili zote aliziacha hapa wakati anakung’uta kung’uta mavazi yake ili arejee alikung’uta kila kitu akaacha hapa. Kaacha gesi, makaa ya mawe, almasi, dhahabu na kadhalika. Wakati anaondoka wanasema akadondosha handkerchief yake pale Arusha kadondosha Tanzanite pale haipo sehemu nyingine duniani. This is a blessed country, tukusanyikeni hapa tuzungumze namna ya kutumia utajiri wetu kupeleka Taifa letu mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kulizungumzia ni uchumi wa kati. Hatujafika kwenye uchumi wa kati accidentally, hatujafika kwa bahati mbaya. Kuna mambo tuliyafanya yametufikisha hapo. Mambo hayo tuliyoyafanya tunayajua, basi tukayafanye mara mbili zaidi tulivyokuwa tukifanya zamani. Tutapanda kutoka uchumi wa kati wa chini kwenda uchumi wa kati wa juu, hili linawezekana. Hilo ni jambo la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu linahusu kufanya kazi kwa juhudi kubwa. Haukuwepo Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza hapa nikawakumbusha Wabunge juu ya checklist manifesto, kuandaa mpango kama huu uliokuja halafu mnakuwa mna-tick kimoja kimoja mnachokifanya baadaye kwenye siku ya pili au mwaka wa pili mnahama na yale ambayo hamkuyatimiza huko nyuma. Lazima tuwe na checklist manifesto ya namna ya kutekeleza mambo yote tunayoyapanga kwenye mpango huu na tuanze moja baada ya lingine na tupange vipaumbele vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Afrika huwa inateseka na tatizo kubwa sana la kupanga priorities. Sisi tukatae, sisi tuwe watu tunapanga priorities zetu sawasawa, tunaanzia hapa kwa sababu ni muhimu, tunakuja hapa, tunakwenda hapa, tunakwenda pale. Watu tufanye kazi, Rais wetu anafanya kazi sana. Tuna Rais mchapa kazi, Rais visionary, lazima tumuunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais huyu hana maneno mengi na hazungumzi sana. Mfano, juzi alikuwa Mwanza akasema huko Dar-Es-Salaam nikija nikute shule imejengwa; imejengwa haijajengwa?
WABUNGE FULANI: Imejengwa.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo ndiye Rais tuliye naye tufananye nae Watanzania wote tufanye kazi kwa nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napenda kusoma vitabu. Kaka yangu Waziri wa Sheria aliwahi kuniambia msemo mmoja niurudie hapa, akasema ili ufanikiwe lazima uwe na kitu kinaitwa Bibliophilia, yaani usome sana vitabu. Sijasoma sana lakini napenda kusoma sana vitabu. Nimesoma kitabu cha Jack Welch, Jack Welch is a number one general manager in the history of the world. Huyu ndio aliyeitoa General Electric kwenye kufilisika mpaka kuwa number one company in America.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jack Welch alisema ili uongoze watu lazima ufanye mambo mawili. La kwanza uwaongoze kwa compassion, kwa kuwasukuma au uwaongoze kwa persuasion, kwa kuwasihi na kuwabembeleza wafanye kazi. Hapa Tanzania na Afrika Jack Walsh angekuja kufanya kazi hapa angefilisika. Kwa sababu hapa Tanzania ukitaka kuwapeleka watu kwa kuwabembeleza kazi haziendi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina kampuni binafsi; nilijaribu persuasion ikanishinda nikaamua kutumia compassion kwamba anayetaka kusukumwa anasukumwa anafanya kazi anayetaka kubembelezwa anabembelezwa anafanya kazi. Hapa Afrika mambo yote mawili yafanye kazi. Rais wetu anataka kazi. Ukipewa jukumu lifanye kwa nguvu zote ndiyo tunaweza kutoka hapa tulipo kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye digital economy. China wamegundua kwamba, manufacturing imeanza ku-decline, imeanza kushuka, ndiyo maana wakaamua sasa tuwekeze kwenye digital economy, uchumi wa kidigitali, ndio maana wanakimbia kwenye mambo ya 5G tunayaona. Sasa hivi duniani hapa China inaongoza katika mambo ya digital, kwa nini alifanya hivyo? Wanataka ku-cover lile gap ambalo litatokea manufacturing itakapo- fail.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hakuna ubaya kwa sisi kujikita kwenye kutengeneza viwanda, ni sawa kabisa, lakini hebu tuelekezeni na akili yetu upande wa pili kwenye digital economy. Kwa nini tunaacha nchi jirani hapa zinajivuna kama zenyewe ndiyo Silicon Valley ya East Africa? Tuna vijana wana akili hapa Tanzania sijawahi kuona. Wanagundua vitu vingi, lakini hawana mtaji hawa watoto, wanatoka UDOM hapo; wamejifunza mambo makubwa kabisa ya kuleta solution kwa changamoto tulizonazo lakini hawana capital na hawawezi wakaenda benki leo na idea akapewa mkopo, haiwezekani, benki zetu sio rafiki wa masikini. Sasa kama tunaweza kukopesha fedha kwa kijiji milioni 50, kama tunaweza kupeleka pesa kwenye halmashauri kuna shida gani hawa vijana wetu wakapewa guarantee ndogo tu kwa benki kwamba, you have the best idea, sisi tutaku-sponsor wewe utengeneze application yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-declare interest, mimi nina run media company. Pale kwetu tuna online radio, tulihangaika sana tulipopata kazi ya kuweka redio kwenye mabasi ya mwendokasi pale Dar-Es-Salaam, tulikosa technology. Tukapata South African partner halafu akajitoa, tukabaki tumekwama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini huwezi ukaamini waliotupa solution hiyo ni vijana wamemaliza UDOM hapa? Vijana wale wametengeneza king’amuzi cha kwao ambacho kinanasa matangazo kutoka ofisini kwetu mpaka kwenye mabasi yote ya mwendokasi. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Watanzania let us trust our children, tuwaamini na tuwawezeshe watoto wetu.
MWENYEKITI: Ahsante sana ni kengele ya pili.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekit, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu kwa Taifa langu katika bajeti hii ya mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijazungumza mengi, naomba nitoe shukrani nyingi sana kwa Serikali ya Awamu ya Sita; kwa Mheshimiwa Rais kwa mambo ambayo mimi peke yangu, sijui kwa wenzangu; amenitendea kwenye jimbo langu. Katika historia, tangu mwezi Januari mpaka Aprili, nimeshapokea karibu shilingi bilioni tatu za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo, mimi na Wabunge wenzangu tulipata nafasi ya kukutana na Mheshimiwa Rais kabla hajaja Mwanza kwenye kikao kidogo, nikawa nimeomba kupewa kituo cha afya kwenye Kisiwa cha Maisome. Ni jana Waziri wa TAMISEMI, dada yangu Mheshimiwa Ummy, alinipigia simu ya kwamba kituo hicho kitajengwa. Kwa hiyo, natumia nafasi hii kuishukuru sana Serikali hii kwa usikivu na namna ambavyo inafanya kazi kuwatumikia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango nitakaoutoa leo nilikuwa nimetarajia kuutoa wakati wa Wizara ya Afya, lakini bahati mbaya nafasi haikupatikana. Hata hivyo, kwa sababu tuna Wizara ya Fedha na Waziri wa Fedha yuko hapa na ndio mpangaji wa ceiling za kisekta na Wizara zote, ni vizuri nikazungumza suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna uhusiano mkubwa sana (correlation) kati ya afya za watu na maendeleo ya Taifa. Kuna uhusiano mkubwa sana. Wanasema there is a correlation between the wellbeing of the people and socio-economic development. Nchi yoyote ambayo watu wake hawana afya, haiwezi kuwa nchi yenye maendeleo. Nchi yoyote ambayo vijana wake ni wagonjwa, haiwezi kuwa nchi yenye maendeleo. Kwa hiyo, kuna umuhimu wa kuwa na Taifa lenye afya. Watu wenye afya wataleta maendeleo ya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama huo ni ukweli, nataka nikurejeshe wewe na Wabunge wenzangu kwenye Azimio la Abuja. Mwaka 2001 mwezi Aprili, nchi zote za Afrika ikiwemo Tanzania chini ya OAU, walikutana Abuja na zikakubaliana na wakaazimia ya kwamba fifteen percent ya annual budget itaelekezwa kwenye huduma za afya. Hayo yalikuwa ni makubaliano. Hayati Mzee Mkapa alikuwa pale na wote walikubaliana na nchi zote zikakubaliana kwamba kila tunapopanga bajeti yetu, asilimia 15 lazima iende kwenye afya kwa sababu tunataka kujenga Taifa la watu wenye afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, miaka 20 baadaye; nina habari ya kusikitisha kuhusu azimio hilo ya kwamba hatujaweza bado kutimiza suala hilo, nafahamu ya kwamba tuna matatizo ya bajeti, uchumi kwenda taratibu, lakini ipo sababu ya Wizara ya Fedha kutazama na kupanga jinsi ya kuiwezesha Wizara ya Afya iweze kutimiza majukumu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka 20 baadaye, nitakupa mfano wa mwaka 2017 na 2018 tulikuwa asilimia 7 tu, ya bajeti yetu kwa Wizara ya Afya na hiyo ilikuwa chini ya azimio la Abuja ambalo lilitaka asilimia 15. Mwaka 2018/2019 tulishuka na kwenda asilimia 6.7 inaendelea kushuka bajeti ambayo inatakiwa kuhudumia afya ya watu wetu. Mwaka 2021/2022 bajeti tunayoijadili hapa leo tumeshuka mpaka asilimia 2.7 maana yake nini, maana yake ni kwamba tuna bajeti ya trilioni 1 kwa afya, lakini tuna trilioni 36 annual budget hiyo peke yake inaashilia ya kwamba tumeshuka mpaka 2.72 percent hiyo ndiyo allocation yetu kwa afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina wasiwasi kama tunaweza kuwa na Taifa lenye afya kwa bajeti ambayo tumeipanga kwa mwaka huu. Nafahamu kabisa ya kwamba tuna matatizo kama nchi, nafahamu ya kwamba mnahitaji kufunga mkanda kama Taifa. Lakini afya za watu wetu ni kitu cha muhimu sana na kikubwa kabisa ambacho nataka nikizingumzie hata hiyo kidogo ambayo tunaipata, tunai-allocate yote huwa haiendi kwenye wizara. Tunawezaje kuwa na Taifa lenye afya linaloweza kujenga ustawi wa watu wake wakachangia utumishi wake, hatuwezi mpaka tuweze kuhakikisha ya kwamba hata kama hatuendi 15 percent, lakini lazima tuweze kupandisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna kodi hapa, kodi mpya tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri, tumekuja na kodi mpya, kodi ya simu, kodi ya majengo, kwenye mafuta tumeweka shilingi 100 na fedha hizi zimeelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu, kwenye elimu, kwenye maji na vilevile kwenye afya, ndiyo maana nazungumza hapa leo ya kwamba ipo sababu kubwa sana ya Mheshimiwa Waziri atakavyopata fedha hizi azielekeze kwenye afya za watu wetu ili bajeti iweze kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikupe mfano, mfano huu ni wabajeti ya Wizara ya Afya mwaka 2019, nitakueleza jinsi ilivyogawanywa, asilimia 41.9 kwa mujibu wa health forum chini ya UNICEF ilielekea Wizara ya Afya na nyingine asilimia 40.7 ilielekea kwenye TAMISEMI ambayo ndiyo watekelezaji wa Sera huo ndiyo ulikuwa mgawanyo, nyingine ikaenda NHIF asilimia 10, nyingine 0.4 ikaenda TACAIDS sasa tuachane na hizo zilizoenda TAMISEMI tuachane na hizo zilioenda NHIF na TACAIDS.
Mheshimiwa Naibu Spika, twende moja kwa moja kwenye iliyokwenda Wizara ya Afya, nionyeshe namna ambavyo fedha hiyo iliweza kutumika na nionyeshe ni kiasi gani kama Taifa hatupo serious kwenye suala la kuzuia magonjwa yasitokee.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya ni kama tunatamka hivi ugueni mkishaugua mje tutawatibu, kama Taifa nimeona hatuna capacity ya kuwatibu watu wote wanaougua ipo sababu ya kuyazuia magonjwa kabla hayajatokea. Leo hii wote tunafahamu ya kwamba kansa inatafuna Taifa letu, lakini wangapi wanafahamu ya kwamba kansa inayotusumbua inasababishwa na Aflatoxin sumu kuvu ambayo ipo kwenye mazao. Niishukuru sana Wizara ya Kilimo wanajenga ghala kwenye jimbo langu kwa ajili ya kuhifadhi mazao ili watu wasiweze kuhifadhi mazao vibaya hatimaye kukawa na sumu kuvu ikawasababishia kansa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo ni suala la elimu tu, ni elimu peke yake ikitolewa hapa nchini watu wataweza kuepuka kansa inayosumbua Taifa. Wizara ya Afya asilimia 41.6 inayokwenda kule 33.5 inalipa mishahara, asilimia 31.8 inakwenda kwenye capacity building mambo ya kuelimisha watu, kuelemisha watumishi wetu wa wizara ya afya ili waweze kufanya kazi vizuri, sina tatizo lolote na capacity building hata kidogo ni sawa, lakini asilimia 31.8 capacity building, asilimia 7.1 inakwenda kwenye tiba, sasa sikiliza hapa, asilimia ngapi inakwenda kwenye preventive medicine, asilimia inayokwenda kwenye preventive medicine ni asilimia 3.7, tunawezaje kuzuia watu wetu wasiugue kwa asilimia 3.7? Hiyo ndiyo hoja yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nazungumza hapa leo natoa mchango wangu kumkukumbusha Mheshimiwa Waziri na nimeikubali bajeti yake na haya kama hayatafanyiwa kazi hivi sasa, yafanyiwe kazi huko mbele tuongeze bajeti yetu kwenye preventive medicine asilimia 3.7 haitoshi kuzuia watu wetu wasiugue.
Mheshimiwa Naibu Spika, napozungumza hapa leo, tarehe hii ya leo infant mortality rate kwenye Taifa letu, watoto wanaokufa chini ya miaka mitano wanakufa watoto 60 katika kila watoto 1000, katika kila watoto 1000 watoto 60 wanakufa. Navyozungumza leo kwa mambo ambayo yangeweza kuzuiliwa kwa elimu peke yake, leo ninapozungumza hapa, leo siku ya leo, jioni ya leo mortality rate ya kinamama wanaojifungua ni wakina mama 558 katika kila vizazi 100,000, tunawapoteza wakina mama wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wiki mbili zilizopita mama kapoteza maisha akiwa ndani ya Mtumbwi anaenda hospitali mtoto katanguliza mkono, tutawazuiaje wakina mama wasiendelee kufa mpaka tutenge elimu, pesa ya kutosha, wakina mama wetu wasiendelee kuugua, inawezekana. Navyozungumza leo hapa hepatitis B, Homa ya Ini ni asilimia 6 watu wengi wana Homa ya Ini tunaweza kuwazuia kwa kuwachanja watu wetu kuna shida gani kama NHIF wakikubali Chanjo ya Homa ya Ini iingie kwenye Bima ya Afya?
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuendelea kupoteza maisha ya watu wetu ni lazima sasa Mheshimiwa Waziri akumbuke suala la muhimu sana kwenye Taifa hili preventive medicine tuzuie watu wetu wasiugue kwa kuongeza bajeti angalau kutii azimio ambalo tulilisaini wenyewe, Azimo la Abuja, Abuja declaration. Nchi yetu inapita kwenye wakati mgumu na ninafahamu nani wajibu wetu kama watanzania kujua tunawezaje kufunga mkanda ninachokiomba, Mheshimiwa Waziri nakusihi rafiki yangu wakumbuke Wizara ya Afya uokoe maisha ya watu ambao hawatakiwi kuugua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuunga mkono hoja na baada ya hapo nitoe shukrani nyingi sana kwa Serikali ya Awamu ya Sita, Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa mambo ambayo ameyafanya kwa ajili ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa ajili ya miundombinu, niendelee tu kukumbusha kwamba, barabara ya kutoka Sengerema kuelekea Nyehunge - Buchosa bado inahitaji kutiwa angalao lami ili wananchi wa Buchosa nao waweze kuona lami kwa mara ya kwanza katika maisha yao. kwa hiyo, nilitaka tu kukumbusha hilo kabla sijaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo nitazungumzia maeneo mawili. Eneo la kwanza kama walivyotangulia wenzangu nitazungumza juu ya kilimo cha nchi yetu na baada ya hapo nitazungumzia suala la uwezeshaji wa wazawa wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha nchi yetu kama ambavyo tumetangulia kusikia kinaajiri watu asilimia 65. Mchango wa kilimo kwa Taifa letu kama ambavyo tumesikia wote ni asilimia 26.9 ya pato la Taifa. Hii ni dalili kabisa ya kwamba, kilimo chetu kinatoa mchango mkubwa sana kwa Taifa letu. Sasa nimeusoma mpango, nimepitia ndani, sijaona mahali popote ambapo wamezungumza juu ya taasisi zifuatazo: Sijasikia wamezungumza juu ya TANTRADE, sijasikia wamezungumza juu ya TIRDO, sijasikia wamezungumza juu ya TEMDO, CAMARTEC na SIDO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nazitaja hizi taasisi? Nazitaja kwa sababu ya mfano wa nchi kama Taiwan, ninapozungumzia suala la maendeleo ya kilimo huwa napenda sana kuchukua mfano wa nchi ya Taiwan. Watu wa Taiwan mwaka 1950 walifikia uamuzi ya kwamba baada ya vita ya pili ya dunia walime na wakaamua kulima sana na wakawa wana-export mazao kwa wingi sana kwenda nchi za nje, lakini baadae wakasema haifai kuendelea ku- export mazao ghafi, badala yake ni bora waanze kutengeneza bidhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walichokifanya ndiyo hicho ambacho Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliki-copy na kukileta hapa nyumbani ya kwamba, tunalima halafu tunatengeneza bidhaa ndiyo tunazipeleka nje. Alipokuja hapa Mwalimu alikuja kuanza na taasisi ya kwanza ya Board of Internal Trade na baadaye akawa na Board of External Trade ambayo kwa sasa inaitwa TANTRADE ambayo kazi yake ni kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali. Kwa hiyo, tulikuwa tunaanzia sokoni kutafuta kwanza masoko halafu tukishapata masoko tunakuja hapa nyumbani tunawaambia sasa nyie watu wa Tanga mtalima katani, nyie watu wa Kilimanjaro mtalima kahawa, watu wa Mwanza mtalima pamba kwa sababu soko lipo, hilo ndilo lilikuwa likifanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo taasisi za utafiti kama TIRDO ilikuwa inafanya utafiti wa kutengeneza vifaa vya kiwandani, mashine za kiwandani kwa ajili ya kutengeneza bidhaa kutokana na kilimo tulichokuwa tunafanya. TEMDO walikuwa wanafanya pia na wenyewe utafiti na CAMARTEC wanatengeneza mashine za kutumia katika kilimo chetu huko vijijini. Sasa sijaona kiasi cha fedha ambacho kimetengwa kwa ajili ya taasisi hizi. Ndiyo ninataka kumkumbusha Mheshimiwa Waziri ni bora akalizingatia suala hili kwa sababu hatuwezi kunufaika na kilimo chetu kama tutaendelea tu ku-export raw mazao ambayo ni ghafi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo la muhimu sana ni kuhakikisha kwamba, tunatengeneza products na tunazi-export kwenda nje. Nilitaka kukumbusha kuhusiana na suala hilo ni la muhimu sana kwa ajili ya kilimo chetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia suala hilo nataka nizungumzie suala moja muhimu sana juu ya National Whisper, yaani mnong’ono wa Taifa. Sisi kama Taifa, kama Tanzania, tunanong’ona nini juu ya wafanyabiashara wetu? Tunanong’ona nini juu ya vijana wa Taifa hili? Tukiwa tumekaa peke yetu sisi wenyewe tunaongea nini juu ya maendeleo ya vijana wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasikitika tu ya kwamba, vijana wetu wa Tanzania walioko katika nchi hii hatuwapi kipaumbele kikubwa linapokuja suala la maendeleo ya Taifa lao. Nasema hivi kwa sababu, wote tunaona kwa macho na wote tunashuhudia kabisa kwamba, vijana wetu tunawapeleka shule, wanasoma, wanapata elimu, wakitoka shuleni wanakuwa hawana chakufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri ni kuanza kufikiria namna ya kuanzisha mfuko wa ubunifu wa Taifa ambao utakuwa na kiasi cha fedha cha kuwasaidia vijana wetu ili waweze kuwa na ubunifu na mfuko huo uwasaidie kuweza kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo zitaweza kuingia sokoni. Hilo ni jambo muhimu sana kwa ajili ya nchi yetu, hatuwezi kuwa na vijana ambao wamesoma, wana elimu, lakini elimu yao haitumiki kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. Kwa hiyo, ninaomba sana na ninaomba nisisitize kwa mara nyingine kwamba ni jambo muhimu sana kuhakikisha ya kwamba, kunakuwa na mnong’ono wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnong’ono wa Taifa namaanisha nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zote za nchi hii, utajiri wote wa nchi hii uko hapo chini kwenye hivyo viti vya hapo mbele vilivyokaa hapo. Utajiri wote wa Taifa hili uko hapo mbele, nikianzia huko kwa Mheshimiwa Mashimba nikaja mpaka huku kwa Mheshimiwa Kipanga, trilioni 33 za nchi hii ziko hapo chini, nani anazipata, ndiyo swali la kujiuliza, nani anazipata? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kunong’ona kama Taifa kwamba, tumeamua kama nchi tenda zote za kuanzia kiasi hiki cha fedha ziende kwa vijana wa Kitanzania? Hatuwezi kuongea kama Taifa ya kwamba, fedha hizi akija mwekezaji yeyote katika nchi hii lazima ashirikiane na Mheshimiwa Tale? Maana yake nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, kwa kufanya hivyo fedha hizi zitabaki kwa Watanzania wenyewe zinazunguka hapahapa nyumbani na tutatengeneza mabilionea wengi ambao unawaongelea hapa ndani. Tusipofanya hivyo watakuwa wanakuja hapa watu na begi baada ya miaka mitano ameshakuwa bilionea anaondoka zake sisi tunabaki tunashangaa. Matokeo yake vijana wetu wanajaa chuki ndani ya mioyo yao wanaanza kuchukia Serikali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu ni lazima itengeneze mazingira ya kuwawezesha vijana wa nchi hii kutajirika. The Government must create environment ambayo ina-foster development ya vijana wetu. Kama hatutengenezi mazingira ya vijana wetu kutajirika hakuna kijana wa nchi hii atakuwa bilionea na mabilionea wataendelea walewale kila mwaka, mwaka huu na mwaka ujao. Kama tuna nia ya kutengeneza mabilionea wengi ni lazima tuseme kwa nia moja kwamba, tumenong’ona kama Taifa ndani ya chumba ambacho hatuzungumzi wala hatuandiki gazetini wala mahali popote ya kwamba, tumeamua kama Taifa vijana wetu ni lazima watajirike. Kwa hiyo, ukiwa kama ni mradi, Rais wetu alizungumza juzi akasema nimeleta fedha hizi zisaidie wawekezaji wa ndani. Ile kauli tafsiri yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Buchosa kwenda Sengerema itengenezwe na mzawa. Tukifanya hivyo utajiri huu utazunguka kwa vijana wetu hawahawa ambao tunawatazama leo, mwisho wa siku nakuhakikishia mabilionea wataongezeka. Tusipofanya hivyo tutaendelea kushuhudia watu wanakuja hapa Tanzania baada ya muda mfupi ni mabilionea wanaondoka wanatuacha hapa tunalalamika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati umefika wa kuhakikisha kwamba, vijana wa nchi hii, vijana wa Taifa hili wananufaika na utajiri wa Taifa lao ili mwisho wa siku waweze kuanzisha viwanda wao wenyewe waajiri wenzao hapahapa nyumbani. Jambo hili linawezekana, South Africa walifanya, South Africa walikuja na utaratibu wa Black Empowerment. Black Empowerment ikawawezesha akina Motsepe na Rais wa South Africa wa sasa kuwa mabilionea mpaka leo. Sisi kama Taifa tunashindwa wapi? Tunashindwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kama Taifa kuamua kwa nia moja kwamba, tumeamua kutengeneza mabilonea 20 katika nchi hii, tukaenda TIRDO, TIRDO wanayo incubation center ambapo vijana wetu wana products nyingi wamebuni lakini hawana mitaji ya kufanyia biashara. Wakienda kwenye benki za biashara kukopa wanaombwa nyumba na kama kijana hana nyumba hawezi kutengeneza product yoyote ile. Hatuwezi kama Taifa kusema, Mheshimiwa Waziri unanisikia, sehemu ya tozo hii tuchukue pesa kidogo tuanzishe National Innovation Fund ambayo kijana akiwa na idea yake yuko COSTECH au yuko TIRDO awe supported atengeneze bidhaa hatimaye aje aajiri wenzake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yanawezekana. Nia ya wazee wetu wa mwanzo ilikuwa ni kuona Watanzania wanatajirika. Hatuwezi kuendelea kukaa hapa tunashuhudia wanatajirika watu, wanakuja wanatajirika wanaondoka, hatutakubali. Tukiendelea hivi baada ya muda utaanza kuona kutakuwa na chuki dhidi ya kundi fulani la watu. Tuwasaidie vijana wa nchi hii waweze kufanya vizuri maishani mwao na waweze kufanikiwa kwa sababu, hii ni nchi yao na wana haki ya kutajirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nianze kwa kukushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi ya kuzungumza ndani ya Bunge hili Tukufu. Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kunipa uhai. Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na ninampongeza sana kwa kazi kubwa anayoifanya.
Mheshimiwa Spika, nimewahi kusema huko nyuma kwamba mwanadamu hupimwa kwa matendo yake, narudia tena kusema leo ya kwamba Tanzania ina Rais smart, Rais intelligent na Rais mwenye uwezo mkubwa sana wa kufanya kazi. Ushahidi wa jambo hili ni kwamba alichukua nchi hii ikiwa inakua kwa asilimia 2.2. Leo ninavyozungumza Tanzania inakua kwa asilimia 4.5, inaelekea Tano. Alichukua nchi hii ikiwa imeanza kupunguziwa misaada ya wahisani kwa sababu ilikuwa imeshatambuliwa kama nchi ya uchumi wa kati, wahisani walikuwa wanaondoa misaada kwa kuona kama vile mtoto sasa amekuwa anaweza kujitegemea. Alichukua nchi ikiwa kwenye ugumu wa uchumi lakini ameweza kudhibiti mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Spika, ninavyozungumza hapa leo unaweza kusema kwamba Tanzania ina bei mbaya ya bidhaa. Lakini wacha nikupe record kidogo. Mfumuko wa bei nchini Sudan ni asilimia 285; mfumuko wa bei Nchini Kenya ni asilimia 6.7; mfumuko wa bei Nchini Uganda ni asilimia 7; mfumuko wa bei Tanzania ni asilimia 4.4. Tanzania ni nchi yenye lowest inflation katika nchi za Afrika Mashariki. Naomba tumpongeze sana Rais wetu kwa sababu anatupeleka vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, asubuhi ya leo nilikuwa napiga hesabu ya saa ambazo Mheshimiwa Rais amekwenda nje ya nchi kuitafutia Tanzania riziki. Amesafiri nje ya nchi saa 263, hivi ninavyoongea, Rais wangu yuko China anatafuta riziki kwa ajili ya watu wake. Kwa wanaosafiri kwa ndege wanaelewa maana ya saa 263. Tunastahili kumpongeza sana Rais wetu, mimi binafsi niseme jukumu langu la kwanza litakuwa ni kumlinda na kumtetea Rais wa nchi yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niseme – na Mungu anisaidie – niseme yale ambayo naamini Mungu ametaka niseme. Nchi yangu inaumwa. Tulipoitwa na Rais Ikulu wakati ule nilisema Tanzania inaumwa widespread Institutional failure; mtakumbuka. Taasisi zimefeli. Nataka niseme leo ya kwamba Tanzania nchi yangu inaumwa magonjwa makubwa mawili; ugonjwa wa kwanza ni anemia ya integrity; ugonjwa wa pili ni anemia ya accountability. Tanzania inaumwa ukosefu wa uadilifu na pili ni ukosefu wa uwajibikaji. Magonjwa haya ndiyo yamesababisha tatizo tulilonalo leo la widespread institutional failure.
Mheshimiwa Spika, tangu nimekuwa Mbunge nikiingia hapa ndani ripoti ya CAG ikija ni watu wameiba. Nilizungumza hapa mara ya mwisho nikasema na iko siku mtakuja kukubaliana na mimi ya kwamba iko sababu kubwa sana ya kuanzisha taasisi ya monitoring and evaluation. Mheshimiwa Engineer Ulenge huwa anazungumzia suala hili sana, na mimi ninataka kusisitiza, watu wanaiba. Sasa siyo kwamba hatuna watu waaminifu, wapo! Lakini katika asilimia kubwa ya watu wetu uadilifu na uwajibikaji umemomonyoka sana.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi katika Taifa hili niseme bila kupindisha maneno, tumefika mahali inaanza kuaminika kwamba mtu asipokuwa mwadilifu ni hero. Tanzania mtu asipokuwa mwadilifu ameanza kutafsirika kama hero. Kwamba alikuwa Mtumishi wa Umma akajenga ghorofa Nane, akanunua mashamba makubwa, sasa ameacha kazi anaonekana alikuwa smart, na watoto wake wanasema Baba yetu alikuwa Kiongozi, alikuwa very smart. Kumbe mwizi! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yule aliyekuwa mwaminifu sana kwa Taifa lake, akaitumikia Tanzania kwa akili yake yote, kwa uaminifu, akaondoka kazini maskini, wakati mwingine amemwagiwa tindikali kwa sababu alikuwa TRA hataki kupokea rushwa, leo hii anateseka wanasema Baba yetu alikuwa Serikalini lakini alikuwa mjinga. Hatuwezi kuwa na Taifa ambalo wezi wanaonekana heroes. Hatuwezi! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nipongeze sana Bunge leo, tangu nimeingia hapa ndani Bunge la safari hii nimefurahi sana. Natamani Bunge hili liendelee kama lilivyo hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakumbuka huko nyuma nilikuwa nawaambia kuna na Bunge la Speed and Standards. Natamani Bunge hili liwe la Quality and Perfection, chini ya uongozi wako ujipatie sifa ya kuwa na Bunge la 12 la Quality na Perfection ambalo tunakuja hapa kusimamia mambo bila hofu wala woga, tumsaidie Rais wetu aweze kuongoza Taifa letu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima tutibu tatizo la integrity na uwajibikaji ndiyo maana tuko hapa, ndiyo maana tumeaminiwa na Watanzania wote tuje hapa tutibu tatizo hili. Taasisi za dini BAKWATA, Episcopal Conference na CCT, walim-hire marehemu Prof. Ngowi ili afanye utafiti kuonesha ni kiasi gani cha pesa kinapotea kila mwaka, ripoti hiyo nimeisoma ina kurasa 64.
Mheshimiwa Spika, Tanzania inapoteza karibu Dola Bilioni Moja kila mwaka kwenye mapato yake kwenye mikono na mifuko ya watu wasiokuwa waaminifu. Lazima tuzuie mambo ya namna hii. Sitaki kupita kwenye details za kwamba ripoti ikoje, yameshasemwa yote hapa, kila mtu anasema ni madudu, ni wizi na wizi zaidi.
Mheshimiwa Spika, nami naungana na wote waliozunguma. Nilimsikia Kaka yangu Mheshimiwa Tarimba akiongea jana kwa uchungu, nikamsikia Dada yangu Mheshimiwa Kapinga anaongea kwa uchungu; na wote wameongea kwa uchungu kwamba tunaibiwa. Nasi kazi yetu kama Wabunge ni kuisimamia Serikali yetu tuzuie fedha zisiibiwe ili ziende kwenye huduma za jamii yetu.
Mheshimiwa Spika, wewe ni Mwanasheria unafahamu Katiba yetu imetamka na mimi nitanukuu Katiba ilivyotamka. Katiba imesema: “We, The People of The United Republic of Tanzania, do sovereignly agree that we are going to build a country under the principles of freedom, justice, fraternity and concord.” Tumekubaliana kujenga Taifa ambalo litajengwa chini ya uhuru, haki, udugu na amani.
Mheshimiwa Spika, tukizungumzia haki, haki ya Watanzania kupata huduma za afya, haki ya Watanzania kupata elimu, haki ya Watanzania kupata maji. Hatuwezi kutimiza haki hii kama watu wanaiba kiasi hiki. Ni lazima tuzuie wizi, na tunaweza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa maslahi ya muda niseme nini kifanyike. Jambo la kwanza, kuna kitabu kimoja aliandika Jack Welch ambaye anaaminika kama the number one General Manager in the world, aliandika kitabu kinaitwa ‘‘Straight from the Gut’’, akasema kuna njia mbili za kuongoza watu, njia ya kwanza ni persuasion (kuwasihi) ili waweze kwenda na wewe au compassion kuwalazimisha waende. Watanzania kwa kuwasihi hawawezekani, tuwalazimishe kuwa waadilifu, walazimishwe kuwa waadilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, moja, tupandikize uadilifu kwenye mioyo ya watoto wetu. Watoto wetu wasione kwamba wezi ndiyo mashujaa wa Taifa letu, ifanyike kwenye mitaala yetu, wazazi nyumbani watimize wajibu wa kuongea na watoto wao ili ionekane ya kwamba uzalendo, uadilifu kiwe kitu cha kwanza kwa kila mtoto wa nchi hii. Hilo likiingia ndani ya mioyo ya watoto wetu nakuhakikishia tutajenga Taifa la watu ambao watalipeleka mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, tukimalizana na watoto, sisi watu wazima tulioshindikana – rafiki yangu, Mheshimiwa Dkt. Ntara, amenipa maneno hapa, yanasema hivi: Waarabu wanao msemo unasema: ‘Yamshillah Jabari illah jadhaa’ ikiwa na maana kwamba punda haendi bila bakora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ingekuwa ni maamuzi yangu Shigongo ningetangaza tuwe na siku ya uchapaji bakora Kitaifa. Fimbo zitoke Mbeya, wachapaji watoke Tarime halafu tukutane Uwanja wa Jamhuri siku ya uchapaji bakora Kitaifa. Unakuja pale na mke wako na watoto wako kama siku ile ulipokuwa unaapishwa, halafu unatajwa, Hamisi Taletale, unakwenda mbele, unachapwa, ili tujenge jamii ya watu wanaoogopa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama hatutaki kuwachapa watu wetu, tumepitisha Sheria Tano katika Bunge hili, sheria ya kwanza ni Sheria ya TAKUKURU; Pili, Sheria ya Fedha; Tatu, Sheria ya Manunuzi; Nne, ni Sheria ya Utakatishaji Fedha na Sheria ya Tano ni Sheria ya Uhujumu Uchumu. Bunge hili limepitisha sheria hizo zisimamiwe! Kuwe na law enforcement. Changamoto yetu ni law enforcement. Tunayo sheria nzuri lakini hatuzisimamii. Kuna watu wanaishi uraiani walitakiwa kuwa jela leo kwa sababu ya sheria hizi. Tuzisimamie sheria zetu, mwenye haki ya kuwa jela awe jela, mwenye haki ya kuwa uraiani awe uraiani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wa Jimbo langu la Buchosa pale, nimesoma ripoti hii wametajwa kabisa kwamba wamekula Milioni 94 za bakaa. Halafu mimi naona aibu, hela za amana wamekula bila wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema maneno machache tu. Kwanza, lazima sheria zisimamiwe. Mwisho Waheshimiwa Wabunge niwaombe, neno la Mungu linasema kwenye Mathayo 12.25 ya kwamba Taifa lolote linalopingana lililogawanyika, halidumu. Nyumba yoyote inayopingana na iliyogawanyika, hufa. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa umoja wetu tusimame pamoja kwenye suala hili, tupambane kukomesha wezi kwenye Taifa letu, inawezekana. Utakumbukwa mbele tunakokwenda, Watoto wetu na wajukuu zetu watasema Bunge la 12 chini ya Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu lilibadilisha Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mungu wa Mbinguni awabariki sana. Ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nasimama hapa jioni hii ya leo kutoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa msiba mkubwa ambao umelipata Taifa letu. Natoa pole kwako wewe mwenyewe Naibu Spika na Spika wa Bunge letu. Natoa pole kwa Wabunge na Watanzania wote kwa msiba huu uliotupata. Ni msiba mkubwa ambao kwa kweli umetutikisa, lakini nashukuru kwamba tunaendelea vizuri kama Taifa. Ni jambo la kumshukuru Mungu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, siku ya Ijumaa tarehe 26 nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu kutoka Australia. Alinipigia simu kutoka Australia akiniambia kwamba, ameshuhudia bendera katika taifa lile zikipepea nusu mlingoti. Nilifurahi sana moyoni mwangu nilipojua kwamba bendera ile ilikuwa inapepea nusu mlingoti kwa sababu ya rais wangu Hayati John Pombe Magufuli. Ni jambo la kujivunia sana na kwa kweli sio jambo dogo kijana kutoka Chato kufanya bendera za dunia hii zipepee nusu mlingoti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kama raia wa nchi hii ambaye nina kila sababu ya kujivuna kuwa na kiongozi kama Mheshimiwa Magufuli ambaye alijitoa sadaka, alijitoa uhai wake, alijitoa nafsi yake kwa ajili ya Watanzania masikini wa nchi hii. Amefanya mambo mengi ambayo siwezi kuyataja yote, wote mnayafahamu. Ameuthibitishia ulimwengu ya kwamba Tanzania inaweza kuendesha mambo yake bila kumtegemea mzungu. Tanzania inaweza kujenga reli yake yenyewe bila kutegemea mkopo. Tanzania inaweza kujenga bwawa la umeme bila kutegemea msaada wa mtu yeyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni jambo kubwa. Kwa miaka mingi sana tumeishi tukiamini ya kwamba sisi ni watu masikini, hatuwezi kufanya lolote bila msaada wa mzungu, lakini Mheshimiwa John Pombe Magufuli amezunguka nchi hii akiwaambia Watanzania nchi hii ni tajiri. Nimesimama hapa leo napeleka ujumbe kwa dunia nzima wapate kuelewa ya kwamba, mimi Erick Shigongo sitoki Taifa masikini, ninatoka Taifa tajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ilifika mahali anakuja mzungu hapa mbeba mizigo tu kule, lakini ukimuona unaona kwamba ni msaada. Sisi Watanzania, sisi waafrika, tunao uwezo wa kujiletea mabadiliko wenyewe bila kumtegemea mzungu wala mtu mwingine yeyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inakwenda kwa kasi. Nchi yetu leo iko kwenye uchumi wa kati. Ni kweli, ziko nchi zilizoingia uchumi wa kati, lakini baadaye zikarudi nyuma kuwa masikini tena. Kama Watanzania tunapaswa kujituma, kuteseka, kutimiza ndoto za Rais wetu, Hayati John Pombe Magufuli, ambaye ametangulia mbele za haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufikiria kwa dakika moja, wakati Mheshimiwa anatuacha alikuwa anafikiria nini akilini mwake. Najua alikuwa anafikiria angetamani kuona Daraja la Busisi magari yanapita, angetamani kuona treni inapita pale TAZARA, treni inaenda kwa kasi kwenda Morogoro, hayo yote hayakutokea. Mahali fulani naamini ya kwamba, alikuwa ana disappointment kwa sababu ameondoka mapema. Kazi yetu sisi tuliobaki ni kumpa furaha Rais wetu, ni kumpa furaha Hayati Magufuli huko aliko kwa kuyatimiza haya mambo aliyokuwa ameyaanzisha, na inawezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, azimio la pili ni la Mheshimiwa Rais Suluhu Hassan ambaye, kwa kweli nataka nikuhakikishie moyoni mwangu sina hofu hata kidogo wala sina wasiwasi. Matumaini yangu ni makubwa sana leo kwa sababu naamini uwezo wa mwanamke. Wanawake wana uwezo mkubwa sana, wanaume naomba tukubali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wanasayansi walifanya utafiti katika Chuo Kikuu cha Havard wakagundua ya kwamba, mwanamke ana-emotional intelligence kubwa kuliko mwanaume, na ndiyo maana anaweza kufanya kazi tano kwa wakati mmoja, mwanaume ukipewa kazi moja unateseka. Kama hiyo ni kweli nina uhakika nchi yangu iko katika mikono salama, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan atalivusha Taifa hili mpaka kwenye uchumi wa juu kabisa badala ya uchumi wa kati. Tumempata na Makamu wa Rais mtaratibu, mnyenyekevu, wote hapa tumetoa kura asilimia 100. Huyu mtu atamsaidia Rais wetu kutumiza ndoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisiongee mambo mengi. Nataka niwaombe wote pamoja tumuunge mkono Rais wetu kuipeleka nchi yetu mahali inapotakiwa kwenda. Ahsanteni kwa kunisikiliza, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninapenda niende moja kwa moja kwenye hoja kwasababu ya muda, lakini naomba tu kwanza kwa kusema kwamba ninatangaza mapema kabisa kabla ya wakati kwamba nitashika shilingi kwenye mshahara wa Waziri wakati utakapofika kwasababu ya suala zima la RPL- Recognition of Prior Learning ambayo Wizara iliifuta na hatimaye inawanyima watu ambao hawakupata nafasi ya kupata elimu ya Sekondari kuweza kupata elimu ya chuo kikuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaielezea baadaye vizuri zaidi wakati wa kushika shilingi utakapofika, naomba nizungumzie suala zima ambalo ninaliona kama changamoto kwenye Taifa langu, changamoto namba moja ninayoiona ni utekelezaji wa mambo tunayozungumza ndani ya Bunge, tangu nimefika hapa nikisikia michango inayotolewa hapa ndani najiuliza tatizo lipo wapi? Hapa ndani kuna michango very constructive watu wanaongea vitu vya maana tatizo kubwa kabisa ni utekelezaji na ninaomba namuomba Mheshimiwa Waziri haya yanayozungumzwa hata kama sio yote akayafanyie kazi ni kufanya kazi peke yake itatutoa tulipo kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tusijekuwa Taifa la watu tunaozungumza watu tumeacha shughuli zetu kuja hapa tunaongea alafu hayafanyiki, haya yanayosemwa hapa yakifanyika nchi hii inabadilika. Tatizo kubwa kabisa ninaloliona katika nchi hii na ambalo ninaamini ni solution la matatizo ya nchi zote za Afrika ikiwemo Tanzania ni mabadiliko ya mind set ni mabadiliko ya akili za watu namna wanavyotazama mambo, shinda kubwa kabisa tuliyonayo bado hatujabadilika jinsi tunavyotazama mambo na namna tunavyofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumnukuu Dkt. Gwajima mara ya mwisho alipozungumza aliongea suala la human resource is far better above natural resources. Alisisitiza kwamba kinachohitajika katika nchi yoyote duniani ni watu kuwa na akili. Watu wakiwa na akili wataweza kutafsiri Liganga na Mchuchuma kuwa barabara, watu wakiwa na akili wanaweza kutafsiri utajiri walionao uweze kuwa elimu au huduma za afya, changamoto yetu ndiyo iko hapo tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, elimu ya vyuo vikuu, shule za msingi inachangia kuweka akili kwenye vichwa vya watu. Kama siyo shule basi ni familia, kama siyo familia basi ni society tunazoishi ndani yake. Tunatia akili kwenye vichwa vya watu wetu ili waweze kutusaidia kutatua changamoto zetu. Ndiyo kazi ya shule, kazi ya vyuo vikuu ni kuweka akili na ufahamu kwenye vichwa vya watu ili waweze kuwa na uwezo wa kutatua changamoto zinazowazunguka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti na hapo hatutaweza kuhama mahali tulipo. Ndiyo maana leo nimesimama hapa kusema kwamba naona kuna tatizo kubwa sana kwenye mtaala wa elimu ya Tanzania. Hii ndiyo inasababisha nchi hii isiende mbele kwa kasi. Simaanishi kwamba hakuna kilichokwishafanyika, mambo mengi mazuri yamefanyika na yanaendelea kufanyika lakini mimi naomba mtaala huu ufumuliwe upya na kama ilivyoamuliwa uweze kupangwa upya ili uweze kupeleka Taifa letu mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano na mfano huu ni wangu mimi mwenyewe niliyesimama hapa. Mpaka mwaka 2017 nilikuwa darasa la saba, sikuwahi kusoma sekondari mahali popote kwenye nchi hii. Baadaye nikasema bora nirudi shule nikasome ili niweze kupata elimu ya kuniwezesha kufanya kazi zangu ofisini. Nikaenda TCU nikapeleka vitabu ambavyo nimeviandika nikawaonyesha walipoona vitabu vyangu wakasema unaweza kusoma chuo kikuu, nikapewa mtihani nikaufanya nikafaulu nikaingia degree ya kwanza Tumaini University, one of the best University in the country kutoka darasa la saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma pale miaka mitatu nimemaliza mwaka jana chuo kikuu, nina degree yangu safi, kutoka darasa la saba mpaka university na nimemaliza. Fuatilia pale utaambiwa nimemaliza na GPA 4.8 nikiwa best student katika chuo kile kutoka darasa la saba. Kilichonipeleka chuo kikuu mimi ni RPL lakini Mheshimiwa Waziri kaifuta. Kwa kuifuta anawanyima watu wengi sana fursa ya kupata elimu. Leo hii nimekaa hapa nasema kama RPL hairudishwi shilingi mimi sitaitoa, nataka kusema wazi hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme hapa mambo anayotakiwa kufanya Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya elimu ya nchi yetu, naomba Waheshimiwa Wabunge hapo mlipo muandike neno UKUTA kwenye karatasi zenu, nataka kusema nini kifanyike kama solution.
Kwanza, lazima mtaala utakaokuja ufundishe ujasiriamali na uzalendo kwa taifa letu. Watoto wetu wafundishwe uzalendo kwa Taifa na ujasiriamali, itawasaidia sana baadaye hata wakikosa kazi waweze kuajiri wenzao. Mimi nimeajiri watu katika taifa hili na elimu yangu ndogo niliyokuwa nayo nimefanikiwa kuajiri watu ofisini na wanafanya kazi mpaka leo, jambo hilo lazima liwefundishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, U tumeizungumzia K ni Komputa, lazima watoto wetu wafundishwe komputa tangu wadogo. Haiwezekani Taifa hili hatufundishi watoto wetu elimu ya computer. Kuna shida gani tukifundisha coding kwa watoto wetu ili waweze kuwa na uwezo wa kutengeneza software na application mbalimbali? Taifa letu linaenda kwenye digital economy, dunia imebadilika sasa hivi digital economy ndiyo inayotawala dunia bila kuwapa watoto wetu elimu ya computer watawezaje kushindana? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la tatu ni U, nimesema UKUTA, U inayofuata hapo ni uamuzi either Kiswahili au Kiingereza basi. Hatuwezi kuwafundisha watoto wetu Kiswahili mpaka darasa la saba halafu form one tunaanza Kiingereza, ni uongo. Wabunge wote walioko hapa ndani anyooshe mkono Mbunge yeyote ambaye mtoto wake anasoma Kiswahili, tunawadanganya wananchi wetu. Sisi hapa wote watoto wetu wanasoma international schools na shule ambazo zinatumia Kiingereza kufundisha; wakulima wetu tunawafundisha Kiswahili akifika form one wanafundishwa Kiingereza watoto wana-fail masomo, hatuwezi kuendelea namna hiyo.
Mheshimiwa Spika, jambo la nne ni T ambayo ni tuamue, practical ni lazima iwe 70% na theory iwe 30% ili watoto wetu waweze kuwa-competent. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naona muda haunitoshi lakini naomba niseme kwamba nitawasilisha mchango wangu kwa maandishi, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa rafiki yangu Mheshimiwa Condester umenichukua kidogo, nikawa nimepoteza kidogo direction.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuishukuru sana Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Makamu, Katibu Mkuu na ninawashukuru pia Wajumbe wenzangu wa Kamati ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu Tanzania miaka miwili iliyopita tulisherekea tukashangilia kwa pamoja kupanda mpaka uchumi wa kati. GDP ya Taifa ilikua, per capital income ikaongezeka, na hivyo tukasherekea kwamba nchi yetu inakwenda vizuri, lakini ninavyozungumza na wewe hivi sasa, nchi yetu imerudi ilipokuwa. Pato la Taifa (per capital income) la Mtanzania imeshuka mpaka 976. Ina maana tumeporomoka chini kwa sababu yoyote ile; iwe ni sababu ya COVID au ya kitu chochote, lakini ukweli ni kwamba tumeporomoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi yetu kama Wabunge, kama Watanzania ni kuhakikisha tunafanya kazi kwa nguvu tena kurudi tulipokuwa na kwenda mbele zaidi. Hili litawezekana kwa jambo moja kubwa, Agriculture. Kilimo peke yake; kilimo cha nchi yetu ndiyo kitatupeleka tena tulipokuwa na hata kuwa na per capital income ya dola 4,000 au 5,000 tuweze kukua zaidi. Kilimo peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia Kamati ya Viwanda na Biashara leo, sizungumzii Wizara ya Kilimo. Sasa hoja yangu iko wapi? Watanzania wanalima sana, lakini kinachowasumbua ni soko la mazao yao. Watanzania siyo masikini, ila wanakosa soko la mazao yao. Hili lazima nilizungumze kwa utaratibu na nieleweke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha nchi hii kinachangia asilimia 27 ya pato la Taifa. Maana yake ni kwamba kama tukiamua kulima kwa nguvu kubwa zaidi, tutaweza kuchangia hata asimilia 50 ya pato la Taifa. Ardhi tunayo, ardhi yetu ni square kilometer 940 arable land. Inayoweza kulimika ni square kilometer 345,000 hivi, lakini nchi kama Malawi inatuzidi kwenye pato la Taifa katika kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kuzungumza kitu kimoja, Wizara ya Viwanda na Biashara ina Kitengo kinachoshughulika na masoko, na Kitengo hiki ni TANTRADE, wapo hapa wananisikia. Nimeshawahi kukutana nao mpaka ofisini kwangu nimeongea nao, nimewaleza what to do? Tufanye nini kama Taifa ili tuweze kusaidia kilimo chetu? Mheshimiwa Bashe analima sana, lakini hauzi mazao. Kazi ya Bashe ni kulima, na kazi ya kuuza mazao ni ya dada yangu Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji. (Makofi)
Mheshimiwa Menyekiti, sasa TANTRADE hawa ninaowaongelea, nitumie neno hili; linaweza kuwa siyo zuri lakini naomba wanivumilie, wako ICU. TANTRADE wako ICU, hawana pesa za kutafuta masoko, wanawezaje kushindana na Kenya? Wanawezaje kushindana na Malawi? Hawana fedha halafu tunategemea Mheshimiwa Bashe alime, halafu atafute masoko. Watatafutaje masoko hawa? Hawana uwezo, hawana technology.
Mheshimiwa Mweneyekiti, ninachokizungumza na nieleweke, kama tumedhamiria kurudi tulipokuwa kiuchumi, pato la Taifa liongezeke, per capita income iongezeke, ni lazima kuanzia sasa tuamue kuwekeza. Hatuwezi kupeleka wanajeshi wetu vitani bila silaha. Tuna tabia ya kupeleka wapiganaji halafu hatuwapi silaha. Unategemeaje wewe Mheshimiwa Bashe unalima, halafu kesho unataka uongeze pato la Taifa, halafu hutafuti masoko?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtafuta masoko hana fedha anahangaika, kazi yake imebadilika kuwa kuandaa sabasaba kila mwaka; kazi ya TanTrade siyo kuandaa sabasaba, kazi ya TanTrade ni kutafuta masoko yenye mazao ya nchi yetu. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
T A A R I F A
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge Eric Shigongo kwamba amesema tuliingia uchumi wa kati lakini tena tumerudi tulipokuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumtaarifu ni kwamba, kilichotuingiza uchumi wa kati tumekiacha ndiyo maana tumerudi tulipokuwa; hii ni kwa sababu ya kukosa dira ya taifa na maono ya taifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shigongo taarifa hiyo unaipokea?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu, naweka sawa hiyo.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee au nikae kwanza?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri ulikuwa unasemaje.
KUHUSU UTARATIBU
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti nataka niweke kumbukumbu sawa; kwamba hatujarudi tulipokuwa; hii naomba isikike vizuri sana. Tulitoka uchumi wa chini, tukaenda uchumi wa kati wa chini, hatujawahi kurudi uchumi wa chini. Nchi yetu bado iko middle income. Tunachokiongelea ni ukuaji peke yake. Yaani hizi terminology za kiuchumi ni vizuri sana kuzisogelea kwa utaratibu. Kuta tofauti sana kati ya level of income ya nchi na growth rate.
Kwa hiyo sasa hivi ambacho kimeathiriwa na COVID pamoja na vitu vingine vyote ni growth rate tu; na yenyewe ni trend zinazobadilika kama mfumuko unavyobadilika. Kwa hiyo kilichobadilika tulishafika asilimia 7 tukashuka mpaka asilimia nne ya ukuaji wa uchumi ile ya annual growth rate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na sasa hivi tumeshapanda kutoka hiyo asilimia nne tumeshakwenda asilimia 4.9; na takwimu hizi zinapokamilika za 2021 likely ukichukua quoters ambazo zimekwishajumlishwa, ukijumlisha wastani unakwenda kwenye 5; na 2022 wastani unaotarajiwa ni 5.2…
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: …kwa maana hiyo; hata wenzetu wa Benki ya Dunia juzi walisema huenda tukaenda 5.5. Na kwa sasa hivi ambavyo tunategemea kuwekeza pakubwa kwenye bajeti inayokuja kwenye sekta za uzalishaji tunategemea tutakwenda kwenye hiyo saba. Kwa hiyo, hatuongelei level of income tunaongelea growth rate.
MWENYEKITI: Umeeleweka ahsante Mheshimiwa Waziri; Mheshimiwa Shigongo karibu umalizie.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee; na kama siendelei naomba muda wangu uhifadhi kwenye friji.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shigongo naomba usubiri kuhusu utaratibu. Msiwe mnahata nafasi mimi naangalia sauti yako huku kumbe upo huku. Mheshimiwa kuhusu utaratibu?
KUHUSU UTARATIBU
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu ulikuwa unakwenda kwa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Ulikuwa unatafakari sauti kabla hujaniona; lakini nimesimama kuhusu utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni kawaida ambayo inakwenda kinyume na Kanuni zetu. Kwanza tunatakiwa tunapotoa taarifa isizidi dakika mbili; lakini Mheshimiwa Mwigulu Nchemba akisimama anahutubia zaidi ya dakika mbili, kinyume kabisa na taratibu; na hii imeshawahi kutolewa angalizo na Mheshimiwa Spika hapa baada ya kuombewa mwongozo. Tunaomba tu-observe Kanuni zetu, kama Waziri umeshindwa kuvumilia uje kujibu mwishoni basi ukisimama ujihakikishe unaji-confine ndani ya dakika mbili unatoa ule taarifa yako watu wanaendelea siyo unaanza kuhutubia kabla ya muda wenyewe husika.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Easter tumepokea kuhusu huo utaratibu na naamini wenyewe wamesikia na kwa vile imeshatolewa mwongozo basi tunaomba wajirekebishe. Mheshimiwa Shigongo naomba uridhie.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu mimi kama mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi, mwaminifu, Mbunge wa Chama cha Mapinduzi siyo vizuri sana kupisha na Waziri wangu wa Fedha. Lakini document hapa inanionesha hivi; qualification of a country to become middle income is per capital income of USD133,000 to USD 445,000; yaani qualification ya nchi yoyote kuwa uchumi wa kati ni pato lake la mtu mmoja per capital kufikia dola 1036 sisi tulifikia Dola 1080; tuka-qualify kuwa uchumi wa Kati. Lakini hivi sasa record zilizopo hapa zinaonesha uchumi wetu sisi sasa hivi pato la mtu mmoja per capital imefikia 976. Ndiyo maana nasema tumerudi kwa sababu per capital income imeshuka.
Mheshimia Mwenyekiti, nchi hii imepiga hatua kubwa sana, kazi kubwa sana imefanyika; tulikotoka na hapa tulipo ni pazuri sana; lakini hoja yangu ilikuwa ni kwamba kurudi nyuma kwetu hapa sisi siyo sababu, kazi yetu ni kuwaomba Wabunge na watanzania tufanye kazi kwa juhudi kubwa turudi tulipokuwa. Sasa itawezekanaje hili; hili linawezekana kwa kilimo; na kilimo tuanzie sokoni, kwanza tutafute soko ndipo tuje tuwaambie wakulima walime nini, na hiyo kazi ni Tantrade. Kwahiyo Tamtrade TanTrade wawezeshwe, wapate fedha, watafute masoko halafu wakulima waambiwe walime nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wangu wa Buchosa wwaliambiwa walime maparachichi, lakini hivi sasa yanawaozea. Sasa watu wanalima miwa inawaozea, TanTrade wapewe fedha, TanTrade wapo ICU, tuwatoe ICU kwa kuwapa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuhakikishia, na kumbukumbu zikae sawasawa; kama tukiwa-impower watafuta masoko wetu; na wananchi wetu wakalima uchumi wanchi hii utakua, pato la taifa litaongezeka na watanzania watakuwa na fedha. Kwa hayo, ninayosema nakuona unagusa kengele bila shaka unataka kunisimamisha; ahsante naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kunipa nafasi ya kusimama tena ndani ya Bunge hili. Nikushukuru sana ingawa haupo kwenye kiti Mheshimiwa Spika kwa uongozi wako wa Bunge letu hili Tukufu. Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana sana, pia wananchi wangu wa Buchosa ambao nipo hapa Bungeni kuwawakilisha, nafanya kazi hii waliyonituma kwa uaminifu wote ili kero zao ziweze kuondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nianze kwa kusema, miezi 11 iliyopita nilisimama hapa Bungeni nikaeleza wasiwasi wangu. Ni kama nilikuwa na wasiwasi kwamba nchi yetu ingerejea ilikokuwa, kwa sababu tulikuwa tayari kwenye uchumi wa kati, pato la Mtanzania mmoja mmoja lilikuwa tayari limekwishafika dola 1,080, lakini kwa corona ilivyokuwepo, Ukraine vita na nini, nikahisi tungerudi tulikokuwa. Hata hivyo, kazi kubwa imefanyika na mtakumbuka niliwaomba hapa kwamba Watanzania tufanye kazi kubwa sana tumuunge mkono Rais wetu ili nchi yetu isirudi ilikokuwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo nina furaha sana moyoni mwangu kwa sababu taarifa nilizonazo ni kwamba nchi yetu imepenyeza na imezidi kwenda mbele pamoja na changamoto ilizokuwa nazo. GDP ya Taifa letu hivi sasa ni bilioni 85, wakati ule tunazungumza zilikuwa zinakadiriwa kuwa Dola za Kimarekani bilioni 67. Leo ninapozungumza ni bilioni 85, tumekuwa na pato la Mtanzania hivi sasa kutoka 1,080 tumefika 1,232. Pamoja na yote yaliyotokea. Kwa hiyo naomba nisimame hapa kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sana tu kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewahi kuzungumza hapa, nirudie tena na nitazungumza kila ninaposimama kwamba we have the most intelligent in Africa and in the world. Kuthibitisha hilo Tanzania image yake sasa hivi Kimataifa imebadilika kabisa. Sisi kukaa pamoja na dada zangu pale, kukaa pamoja, Rais amefanya image yetu imebadilika. Tanzania sasa hivi inajulikana kama one of the democratic country in the world, kwa sababu ya kuishi pamoja na ndugu zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi zangu hizi ziwaelekee Wabunge wote walioko hapa kwa namna wanavyotoa michango yao hapa Bungeni. Mimi hoja yangu ipo kwenye suala la umaskini wa Taifa letu. Najua wamezungumza juu ya viwanda, wamezungumzia Twiga, naomba nisiguse kabisa habari ya Kiwanda cha Twiga na Tanga Cement. Naungana na hoja ya dada yangu Tauhida pale alichokisema ndio ninachokisema mimi ya kwamba suala hili lina utata, limeleta kelele nyingi, turejee mezani tukaangalie tatizo liko wapi. Langu ni suala zima la umaskini wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maendeleo tuliyoyapiga nchi yetu ni tajiri lakini watu wake bado ni maskini. Bado ni maskini, watu wana shida nyingi sana huko mtaani, maisha ni magumu pamoja na pato letu kuongezeka mpaka dola bilioni 85, lakini watu bado wana shida nyingi sana, maisha ni magumu. Inavyoonekana ni kwamba hii bilioni 85 iko kwenye karatasi, lakini haipo mezani mwa Mtanzania wa kawaida. Hapo ndio nataka niongelee mimi hoja yangu ya leo kwamba, umaskini bado upo na ni lazima tutafute njia yoyote ile ya kuhakikisha hii 85 bilioni inaonekana kwenye maisha ya Mtanzania wa kawaida. Hoja yangu ipo hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale wasomaji wa vitabu bila shaka wamewahi kusoma kitabu cha Marehemu Profesa Mtulya aliandika kitabu kinaitwa Growth and Development. Kwamba kuna tofauti kubwa sana kati ya growth na development. Kukua ni ku-increase in size, tume-increase in size tuna pato kubwa la Taifa lakini development in increase in activities, kuongezeka kwa activities za Taifa. Kwamba ukuaji huu unaonekanaje kwenye maisha ya Shigongo, kwenye maisha ya Kingu, kwenye maisha ya mkulima wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado ukuaji huo haujaonekana kwenye maisha yetu. Ni kama jenereta liko nje, lakini ndani ya nyumba kuna giza na jenereta inawaka. Ina maana kinachokosekana hapa ni cable ya kutoa umeme nje kuingiza ndani, hakuna connection kubwa kati ya GDP na maisha ya Mtanzania wa kawaida. Sasa niliposimama hapa leo naongea na Wizara ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ni Wizara muhimu sana kwa Taifa letu. Wizara ya uratibu, Wizara hii ikisimama sawasawa kwenye uratibu itatuondolea umaskini wa nchi yetu. Nataka niseme mambo ambayo mimi naamini yakifanyika katika nchi yetu, umaskini wa Tanzania utaondoka au kupungua kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, naamini sana kwenye kilimo, naamini sana kwenye agriculture. Tulime na Serikali imeamua kulima kweli, Mheshimiwa Rais ameongeza fedha nyingi sana Wizara ya Kilimo ili tulime na kweli tunalima sana. Kilimo kitatutoa kwenye umaskini wetu, kimeajiri watu wengi katika nchi yetu, bahati mbaya sana kilimo chetu hiki, watu wengi wanatumia kilimo cha mkono, asilimia 70 ni jembe la mkono, asilimia 20 ni ng’ombe na asilimia 10 pekee yake ndio zimetumika zana za kilimo za kisasa kama trekta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme kitu kimoja kama Mheshimiwa Bashe analima, Mheshimiwa Ashatu ana mambo kadhaa ya kufanya. La kwanza, anatakiwa kuhakikisha mazao yetu yanatangazwa na masoko yanatafutwa, hiyo TanTrade anayo yeye kwenye Wizara yake. La pili, anatakiwa kuhakikisha mechanization ya kilimo inafanyika, zana za kisasa anayo TIRDO ofisini kwake anayo TIRDO na anayo TEMDO, lakini lingine ana CAMARTEC katika zana za kilimo ambazo zinatumika huko mashambani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba utusaidie Wizara hii ipewe pesa za kutosha kwenye hayo maeneo niliyoyasema, tofauti na hapo tutalima kweli mazao lakini post harvest loss yetu itakuwa kubwa, mazao mengi yatakuwa yanaharibika na hakuna masoko, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ambalo unatakiwa kulifanya ni innovation, utakumbuka nilishakuja hapa nikasema juu ya innovation ya kwamba ubunifu ni kitu cha muhimu sana kwenye Taifa letu. Tuna vijana wengi wamebuni vitu vingi sana, lakini hawana mitaji amezungumza dada yangu Tauhida hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshakuja hapa nikasema, narudia kusema tena na leo kwamba, kuna mtu mmoja kule Iringa aligundua umeme anasambaza kijiji kizima. Kuna kijana mmoja pale Mabibo alikuwa na redio yake anatangazia watu pale Mabibo lakini badala ya kusaidiwa katika nchi hii ukiwa mbunifu unajikuta unaingia kwenye matatizo. Hiyo sio jambo sahihi naomba tufanye kila kinachowezekana kuwasaidia wabunifu wa nchi yetu. Vijana wetu wanatoka vyuo vikuu na shahada wana ubunifu lakini hawana mitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishamshauri Mheshimiwa Waziri aanzishe National Innovation Fund. Aanzishe Mfuko wa Ubunifu wa Taifa na huu sio lazima akusanye pesa yeye, kuna Global Innovation Fund huko ina pesa nyingi tu. Tunaandika mradi tunapewa mabilioni ya pesa, tena sio mkopo ni grant. Nilishamwambia, tulishaongea nikiwa Kamati ya Viwanda na Biashara nilisema sana. Nasema tena leo na leo nitakuwa mkali kidogo, nitataka nipate maelezo kwamba nini kinaendelea kuhusu Global Innovation Fund. Hatuwezi kuwa na vijana wenye akili kiasi hiki kwenye Taifa letu, hawana mitaji wana ubunifu wao ndani ya nyumba, lakini wanakufa bila kufanya chochote. Hatuwezi kukubali Waheshimiwa Wabunge, ni lazima National Innovation Fund ianzishwe. Kenya wanayo, South Africa wanayo, Ethiopia wanayo, kwa nini sisi hatuanzishi? Naomba sasa tuwathamini wabunifu wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kuwawezesha Watanzania. Watanzania wanahitaji kuwezeshwa, China miaka 15 iliyopita iliamua kwa nia moja kwamba tunaenda kuweka watu wetu kwenye list ya makampuni 500 duniani haikuwepo hata kampuni moja ya Kichina. Leo ninapoongea hapa nusu ya ile list ni kampuni za Kichina. Kwa sababu nchi iliamua we need a political will to change mambo. Lazima tuamue kama Taifa ya kwamba ile list tuhakikishe tunafanya jambo wenyewe, watoto wetu waweze kuwa na pesa. Tuwape Watanzania uwezo wa kuwa na kipato waweze kushikilia uchumi wa nchi yao. Tumechoka kuwa watazamaji, wageni wanakuja hapa siku mbili, tatu wameshatajirika, wanaondoka hapa na mali zetu sisi tunaendelea kubaki maskini. Nataka majina mapya ya mabilionea kwenye nchi hii, majina mengi kwa muda mrefu ni yale yale tu. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kuwa miongoni mwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mema yote ambayo amelifanyia Jimbo la Buchosha kwa upande wa elimu. Ameleta fedha nyingi sana, tumejenga madarasa mengi, nina uhakika aliyoyafanya Wanabuchosha wote wanamshukuru wakiongozwa na mimi mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Elimu na najua anafahamu kabisa kwamba sina mashaka naye hata kidogo. Nimekwishazungumza naye mara nyingi kwamba uadilifu wake na uzalendo wake katika Taifa na namna anavyoipenda elimu, nina hakika kabisa elimu yetu iko kwenye mikono salama. Nimshukuru sana Naibu Waziri, rafiki yangu Kipanga ambaye mara kwa mara tunajadiliana kuhusu elimu ya nchi yetu, hakika anatumika vizuri sana kwa ajili ya Taifa lake, Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Mkuu na Watumishi wote wa Wizara ya Elimu ambao wako hapa nyuma wananisikiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajadili suala la elimu, nimekuwa mshabiki mkubwa wa elimu na jambo moja ambalo nimekuwa nikilizingumza sana hapa Bungeni ni kuhusu elimu, kitu ambacho mwenyewe nikiwa kijana mdogo mtoto mdogo nilikikosa. Sikufanikiwa kupata elimu ya kutosha na kwa sababu nimefika kwenye hatua hii na najua umuhimu wa elimu kwa watu wa nchi yangu, nasimama imara siku zote kuhakikisha kwamba elimu ya nchi yangu inakuwa elimu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Nelson Mandela aliwahi kusema na nitamnukuu alisema; “Education is the most powerful weapon you can use to change the world”. Kwamba elimu ni silaha yenye nguvu mtu yeyote anaweza kuitumia kuibadili dunia. Kwa hiyo tunapojadili elimu inatakiwa tuwe na umakini wa hali ya juu sana kwa sababu kuna uhusiano mkubwa sana kati ya maendeleo ya watu na elimu. Maendeleo ya watu yanategemeana sana na aina ya elimu ambayo nchi inatoa kwa watu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ya watu wenye akili sio wenye elimu pekee yake, haiwezi kuwa nyuma kimaendeleo. Ndio maana nasema na narudia kusema na nitaendelea kusema, tuna wajibu wa kuingiza maarifa kwenye akili za watoto wetu. Huo ni wajibu wa Serikali, Serikali ikitimiza wajibu wake sawasawa ika instill au kuingiza maarifa kwenye akili za watu wake, hatuna mashaka kuhusu maendeleo ya Taifa letu. Kwa hiyo Wizara ambayo Mheshimiwa Mkenda anaiongoza ni Wizara moja muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Kwa sababu kama hatutotimiza wajibu wetu tutakuwa na wananchi, tutakuwa na human capital ambayo haina elimu ya kutosha, haitoweza kusukuma maendeleo ya Taifa letu mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote zilizofanya vizuri katika ulimwengu huu watu wake wameelimika vya kutosha na aina ya elimu wanayopewa ndiyo jambo la muhimu zaidi. Sio tu kuwapeleka watoto shule wakasome, lakini aina ya elimu tunayotoa iwe ni elimu ambayo itasaidia kutatua changamoto zetu. Tunapeleka watoto shule tuwaelimishe ili watupe solution ya matatizo yetu, ndio lengo. Ninapopeleka mwanangu shule aweze kuja na solution kwa matatizo ya familia, solution kwa matatizo ya nchi na solution kwa matatizo ya dunia. Otherwise hapa hakuna sababu ya kupeleka mtoto shule kama tutapeleka watoto wetu shule wakasoma, lakini mwisho wa siku wasitupe solution ya matatizo yetu haina sababu ya kupeleka watoto shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lengo letu tunasomesha watoto watupe solution ya matatizo yetu. Inaniuma sana, inaniuma sana mara nyingi, ninapokutana na kijana amesoma, amemaliza chuo kikuu, ana masters, yuko mtaani hatupi solution yoyote kwa Taifa letu. Anazunguka huku na kule akiwa na bahasha, hana mchango wowote kwa Taifa anageuka mzigo kwa Taifa, mzigo kwa familia yake, sio lengo la elimu yetu, lengo liwe ni kuwaelimisha watu wetu. Sasa tujiulize sisi wenyewe hapa tulipo ni matokeo ya aina ya elimu tuliyopata. Je, tunafurahia tulipo? Je, tungetamani tuwe mahali tofauti? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo yangu mimi ni kwamba elimu iliyotufikisha hapa haiwezi kutupeleka tunapokwenda. Narudia, elimu iliyotuleta mpaka hapa tulipo, mimi sina furaha sana, nataka aina nyingine ya elimu itakayonitoa hapa kunipeleka kule ninapokwenda kwenye ulimwengu wa kidijitali. Internet of things, cloud computing mambo ya coding na namshukuru sana Mheshimiwa Waziri tulizungumza mambo ya coding hapa, nimeyakuta kwenye rasimu ya mtaala ambayo nimeisoma. Nimefurahi kwa sababu nina uhakika kwamba rasimu niliyoisoma, watoto tunaokwenda kuwatengeneza kwa rasimu hii watakuwa ni watoto ambao watatusaidia sana tunapokwenda. Kwa hiyo, ninao ushauri kwa Serikali, ushauri wangu kwa Serikali ni mambo yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wanaotoka kijijini kama mimi mnafahamu huwa tunafyatua matofali kwa kutumia kibao, kile kibao kinaitwa kifyatulio. Kwa hiyo kama kifyatulio ni cha duara matofali yatatoka ya duara, kama kifyatilio ni cha mstatili matofali yatatoka ya mstatili. Hauwezi ukawa na kifyatulio cha mstatili ukapata matofali ya duara. Maana yangu ni nini? Aina ya elimu tunayotoa tujiulize, tunatengeneza watoto wa aina gani huko mbele? Je, tunatengeneza watoto wanaofanya tushinde kwenye ulimwengu ujao? Hili ndilo swali langu la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakuja kwenye mambo yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kwangu mimi ni mtaala, mtaala wetu ni lazima uwe ni mtaala ambao utamwandaa mtoto wetu kushindana kwenye ulimwengu ujao. Tusiwajaze watoto wetu content pekee yake kichwani isipokuwa tuwape elimu ambayo itawafanya waweze kuwa na solution za matatizo. Kwa hiyo, tuupitie mtaala wetu, nimeuona mtaala huu ni mzuri, una maboresho kidogo lakini watoto watakaosomeshwa kwenye mtaala huu wawe majibu ya matatizo kwenye ulimwengu tunaokwenda mbele, sio hapa tulipo hivi leo. Kwa hiyo, mtaala uboreshwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu Mheshimiwa Waziri ni kwamba tusichukue muda mrefu sana kutekeleza mambo. Tunapojadiliana kuhusu mtaala tufanye mambo yetu haraka. Dunia inaenda kwa kasi, unaweza kuwa mjadiliana, mnajadiliana, mnajadiliana kuhusu mtaala, dunia itabadilikia ukajikuta mtaala wako umekwenda obsolete kabla hujautekeleza. Kwa hiyo hayo nayo Mheshimiwa Waziri wameshayajadili, wadau wameongea, tuyafanyie utekelezaji kwenye mtaala tuanze kuufanyia kazi mara moja. Kwa hiyo mtaala wetu uboreshwe, uende na ulimwengu ujao, sio ulimwengu tuliotoka wala ulimwengu tuliopo hivi sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu; Walimu wetu katika nchi hii wana matatizo sana. Walimu wetu wana shida; huwezi kuwa na elimu bora kwa Walimu wanaolalamika kila siku. Walimu wetu wamejaa mikopo, Walimu wetu wana kila aina ya dhiki, kama tumedhamiria kuboresha elimu ya nchi hii tuanze na Walimu wetu kuboresha maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kengele imelia niende katika jambo lingine la muhimu sana ambalo nataka kulisema, wazazi wa nchi hii watimize wajibu wao kwa watoto wao. Kuanzia kwa mama mjamzito, ahakikishe anakula chakula bora, mama mjamzito ajiepushe na matumizi ya dawa au vitu vinavyoathiri akili ya mtoto wake. Udumavu upigwe vita kwa sababu mtoto aliyedumaa hawezi kujifunza sawasawa tunakokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya vitendo; tupunguze nadharia tuongeze vitendo kwenye elimu yetu. Medium of instruction, nilishasema huko nyuma, sikatai kufundisha kwa Kiswahili, lakini wasiwasi wangu ni kwamba mtoto utakayemfundisha Kiswahili kwenye ulimwengu ujao itakuwaje? Asubuhi ya leo wakati nafanya mazoezi, nimekutana na watoto wawili, mmoja amesoma English medium, mwingine anasoma shule ya kawaida ya Serikali wote wapo sekondari moja. Nikamuuliza yule aliyetoka shule ya msingi ya kawaida, akaniambia nahangaika sana form two kwa sababu nimesoma Kiswahili mpaka darasa la saba, form one Kiingereza. Yule mwingine akaniambia mimi sipati shida yoyote kwa sababu nimesoma Kiingereza mwanzo mpaka mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu, tuamue kama ni Kiswahili, iwe ni Kiswahili, kama ni Kiingereza iwe ni Kiingereza na kama hilo hawalitaki, basi niwaombe wafundishe mpaka darasa la tatu au la nne Kiswahili, la tano mtu aanze Kiingereza kusudi wajiepushe na suala la mtoto form one, form two anajifunza Kiingereza hajakielewa vizuri form four umefika mtihani, anafeli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoteza watoto wengi sana. Naomba sana tuamue Wabunge sisi ndio wawakilishi wa wananchi, hebu tuchague tunataka nini, nani kati yetu hapa mtoto wake anasoma Mwananyamala Primary School? Nani? Napendekeza huko mbele ikiwezekana Waziri akiteuliwa tu iwe ni sharti kwamba mwanao asome shule ya kawaida. Tukifanya hivyo elimu yetu itabadilika. Sasa hivi tunawadanganya wananchi wetu kwamba tufundishe Kiswahili, watoto wetu hapa wote wanasoma international schools, that’s a lie, tusiendelee kuwadanganya wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na cheti cha form four; kansa ya cheti cha form four katika nchi yangu. Nilizungumza mara ya mwisho hapa narudia tena. Hivi sasa nina stori ya watoto wamesoma China medicine, wamesoma miaka mitano medicine China, wamekuja hapa wamekataliwa kufanya internship kwa sababu hawana cheti cha form five na six. Waliondoka hapa kwenda kusoma medicine China kwa elimu ya form four, hapa wamelazimika kufanya QT ya form five na six ndio wafanye intership, what is wrong with this? Hebu tufike mahali tuache watu wapate elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme mapema, issue yangu ya RPL, Recognition of Para Learning ambayo ikanifanya mimi nikapata elimu ya chuo kikuu kutoka darasa la saba. Naomba sana Mheshimiwa Waziri anipe majibu ya suala hili, ni lini RPL itaanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Eric.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge hili tukufu ili niweze kutoa mchango wangu wa mawazo ambao binafsi naamini unaweza kusaidia Taifa langu kwenda mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru awamu zote sita za Uongozi wa Taifa letu. Namshukuru Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mzee Mwinyi, Hayati Benjamin Mkapa, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Hayati Dkt. Magufuli na sasa tuna Mama Samia Suluhu Hassan. Watu wote hawa wanaendelea kupeleka Taifa letu mbele. Mimi kama Mtanzania nina kila sababu ya kuwashukuru kwa sababu wamefanya maisha yangu yamekuwa bora kwa mambo waliyoyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme ambacho nimezoea kukisema kila siku, na nitakirudia tena na tena kwamba tuna Rais smart, intelligent and clever, na nitatoa sababu. Huko nyuma niliwahi kusema, alipewa fedha za barakoa akajenga madarasa. Sasa nataka niwaambie kitu kingine leo. Tanzania inauza zaidi Kenya kuliko inavyonunua, la kwanza. La pili, uchumi wetu umekua ndani ya miaka miwili kutoka Dola bilioni 69 mpaka 85. La tatu, ndani ya muda mfupi amefanya kile ambacho wengine kiliwashinda kwa upande wa demokrasia. Amefanya jambo lililokuwa linamtia hofu kila mtu la kuruhusu mikutano ya hadhara ya wapinzani. Amefanya jambo kubwa sana la kwenda mpaka kwenye mkutano wa Umoja akina Mama wa CHADEMA. Maana yake nini? Maana yake ni kwamba amebadilisha taswira ya nchi yetu Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimwona Makamu wa Rais wa Marekani amekuja hapa akatamka, Marekani ikatamka ya kwamba Tanzania is a democratic country, tumemaliza. Ile peke yake ni smartness. Nataka niwaambie, hiyo ni smartness, subirini muone misaada itakavyomiminika kuja hapa nchini kwa sababu ya kitendo hicho kilichofanyika. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais na namtia moyo aendelee kufanya kazi. Aelewe ya kwamba watu wote hawatakubaliana na anachokifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimtie moyo sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Kazi yake ni ngumu. Anafanya kazi ngumu sana ambayo siyo rahisi kueleweka. Ila tukumbuke Henry Ford alipotengeneza gari, watu walikuwa wamezoea farasi, wakakataa gari, lakini baadaye walipozoea gari, wakakataa farasi. Kwa hiyo, yapo mambo ambayo siyo lazima sisi wote tukubali, ilimradi lina maslahi ya Taifa, ilimradi jambo hilo siyo maslahi ya mtu binafsi, lifanywe hata kama wengine hawakubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, nashukuru sana kwa jimbo langu. Jimbo langu mimi Shigongo Eric la Buchosa limepiga hatua kubwa ndani ya muda mfupi kuliko miaka kumi yote iliyopita. Barabara zinapitika, miradi mingi ya maji, tumejenga madarasa, tuna Chuo cha VETA, tuna kivuko kipya cha kwenda Kome cha shilingi bilioni nane, haijapata kutokea. Nisipomsifia Rais wangu, nimsifie nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, niwaambie kitu kimoja, hakuna jambo baya kama kumsifia mtu sifa za uongo. Ni sawa na mimi uniambie nina six packs na wakati nina kitambi, unapunguza heshima yako. Niseme ukweli, ukisifiwa sifa za uongo unamdharau anayekupa sifa. Nami natoa sifa hizi kwa Rais kwa sababu ni mambo ya ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niendelee. Nachangia mambo makubwa mawili tu. La kwanza, kukua kwa Taifa letu. Tanzania nchi yangu ninayoipenda inakua. Ni rahisi sana sasa hivi mtu kuzunguka huko akafanya mikutano yake ya hadhara, akawaaminisha watoto wetu kwamba hakuna kinachoendelea na watu wakaamini. Mimi ni wazamani kidogo, nimeshuhudia Marais wengi, lakini ngoja nitoe takwimu chache hapa kuonesha kwamba Taifa letu linakuwa ili kusudi tutembee kifua mbele, tusitembee kwa unyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1961 tulipopata uhuru barabara za lami zilikuwa kilometa 1,300. Leo ninavyoongea tuna kilometa 14,000. Mwaka 1961 life expectancy, umri wa Mtanzania kuishi ilikuwa miaka 38, leo tuna miaka 68. Tulikuwa tuna chuo chetu kimoja, leo tuna vyuo vikuu 47. Tulikuwa na hospitali za wilaya na mikoa 96, leo 1,030. Tulikuwa na vituo vya afya 22 nchi nzima, leo tuna vituo vya afya 4,030. Tulikuwa na zahanati 1,332 leo tuna zahanati 7,458. This country is growing. Hii nchi inakua. Tufike mahali tukubali kwamba nchi yetu inakua, asije mtu hapa kutuaminisha kwamba hakuna kinachoendelea, that is a lie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua tunaweza kutofautiana kuhusu speed, wengine wanaona tunaenda polepole, lakini this country is growing. Watoto wetu wanaonisikiliza huko nje, wasidanganywe na mtu yoyote, nchi yetu inakua tuendelee kufanya kazi, muda siyo mrefu tutakamata uchumi wa Afrika na hatimaye kuheshimiwa zaidi ya tunavyoheshimika hivi sasa. Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni umaskini wa kipato. Mimi nimetoka katika familia maskini sana, na kwa kweli nauchukia sana umaskini kwa sababu ulinitesa sana nikiwa mtoto. Mungu kanitoa huko, lakini mimi peke yangu kutoka siyo kwamba umeisha, kuna watu nimewaacha wengi huko nyuma. Ndiyo maana napambana na umaskini kila siku. Kwa miaka 23 nimezunguka nchi hii kwenye vyuo, kwenye Makanisa, napambana na umaskini, kuwaelimisha watu mbinu za kutoka kwenye umaskini. Nimeandika mpaka vitabu kwa sababu siupendi umaskini practically kwa sababu una mateso. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili ni Tajiri. Tanzania nchi yangu ni tajiri. Ngoja nikupe data kidogo. Tanzania kwa makaa ya mawe ni ya 87 duniani; Tanzania kwa gesi ni ya 82 duniani; Tanzania kwa Helium ni ya kwanza duniani; Tanzania kwa dhahabu ni ya 19 duniani; Tanzania nchi yangu kwa almasi, ni nchi ya 17. Nchi hii tajiri, hatutakiwi kuendelea na umaskini wa kipato. Ilitakiwa tuwasaidie watu wetu kubadilisha utajiri huu uweze kuwa pesa na maisha ya watu yabadilike. Tunahitaji pesa kwenye mifuko ya watu wetu. Unapowaambia Watanzania wanajilipia shilingi bilioni 85, wakati mchele ni shilingi 3,500 hawaelewi. Tufanye nini? Muda ni mchache. Tufanye nini kuwasaidia Watanzania wawe na kipato? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza, let us invest in agriculture. Nataka kumsifia sana Mheshimiwa Rais wangu, kumsifia Mheshimiwa wangu Waziri Bashe kwa jinsi ambavyo Tanzania imeamua kuwekeza kwenye kilimo. Ni kilimo pekee yake kitawasaidia Watanzania kutoka kwenye umaskini wa kipato. Naomba tuwekeze kwenye mbegu, tuwekeze kwenye masoko, tuwekeze kwenye teknolojia, watu wetu waweze kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme ya kwamba, tuwekeze kwenye kilimo hasa cha mazao ya chakula (food crops). Unaweza ukalima maparachichi, it is okay, ukilima pamba it is okay, ukalima chai it is okay, lakini Wazungu wanaweza wakaweka sera zao za ushoga hapa, ukakataa sera zao wakasema unajua maparachichi ya Tanzania yana Sodium Bicarbonate, wakasema hatuyanunui, lakini tukilima chakula na tukawa ni soko la chakula cha Afrika nzima, nataka kuwahakikishieni, hatuna sababu ya kufunga mipaka. Kwa nini tusiwe soko la chakula la Afrika nzima, watu waje wanunue chakula Tanzania? Tukifanya hivyo, watu wetu watakuwa na pesa mfukoni. Agriculture. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili la muhimu sana, nataka kuona Watanzania wazawa wanawezeshwa kiuchumi. Bajeti ya mwaka huu, shilingi trilioni 44, natamani fedha hizi zibaki kwa vijana wa Kitanzania. Nilishaongea mara nyingi, Watanzania wamechoka kuona wageni wakija hapa wanatajirika wao wanaendelea kubaki maskini, that is not right. Siwezi kwenda India leo nikapewa tenda ya kuchapa vitabu vya sekondari. That is a lie, lakini Wahindi watakuja hapa watachapa vitabu vya watoto wetu wa shule. Kwa nini? Nataka kuona wazawa wanawezeshwa kushikiklia uchumi wa nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo Sheria ya Manunuzi. Hebu sikiliza sasa uone. Sheria ya Manunuzi ambayo nailalamikia kila siku, inasema eti kwenye ku-supply tender ikifika shilingi bilioni moja, hiyo tender inabadilika inakuwa international. Hebu ona sheria hiyo. Mmetunga humu humu ndani kwamba tender ikifika Shilingi bilioni moja, inaenda international. Eti mimi nipambane na Mturuki, nipambane na Mchina, nipambane na Mwingireza, haiwezekani. Nataka hiyo sheria ibadilishwe. Watanzania hawawezi kushindana na watu wenye mikopo ya dola mbili, sisi tuna mikopo ya dola 22 ya CRBD. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie.
MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa, sekunde 30.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kuisaidia nchi yetu tuwasaidie Watanzania washike uchumi wa nchi yao. Mambo ya kuwa mashuhuda, wamechoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie jambo la mwisho kabisa kwa upendeleo ulionipa. Namwomba Mheshimiwa Waziri apanue wigo wa kodi. Naomba nikushauri, kutegemea kodi pekee yake kama chanzo cha mapato, haiwezekani. Nataka uwezeshe sekta zetu kwa pesa za kodi ili sekta ziingize fedha kwenye pato la Taifa. Kwa mfano,…
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Eric.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nianze na pongezi kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwenye Wizara hii. Nina siku mbili tu tangu nimerejea na Mheshimiwa Naibu Waziri kutoka Jimboni kwangu ambapo tumesafiri pamoja kwa mtumbwi mpaka kwenye visiwa ambako amekutana na wavuvi na kusikiliza kero zao; nampa pole sana kwa shida aliyoipata wakati tunapita ziwani kwani alijua asingeweza kurejea mahali hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa inafanyika katika nchi yetu kwenye suala zima la uvuvi ambalo nitachangia kwalo. Nataka nizungumzie sana suala la uvuvi kwa sababu eneo/Jimbo langu lina visiwa 32 na asilimia 35 ya watu wanaoishi eneo lile wameajiriwa kwenye uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kwanza kwa kusema kwamba kama kweli kama Taifa tuna dhamira ya dhati kabisa ya kukuza uchumi wa nchi yetu, ni lazima sasa tuanze kutumia zawadi ambazo Mungu ametupatia; zawadi mojawapo ni uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imebarikiwa kuwa na vitu vingi sana, ukienda huko Liganga kuna mlima wa chuma, kando yake kuna mlima wa mawe; vyote hivyo Mungu alitupatia. Ni wakati wetu sasa kuanza kuvitumia vitu hivi, hatukuvinunua, Mungu alitupatia kama zawadi na ile sisi maisha yetu yabadilike ni lazima sasa tuanze kuvitumia, hilo ni jambo la kwanza ambalo nilitaka kuwakumbusha Watanzania wenzangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja kubwa na kama hotuba yangu/mchango wangu huu ungepewa jina ungeitwa contribution of political will kwenye development. Tunazungumza mambo mengi sana mazuri, nakaa hapa ndani nasikia michango mizuri najiuliza what is wrong with us; watu wanajua jinsi ya kutoka mahali tulipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokikosa kabisa kwenye Taifa letu ni political will, utashi wa kisiasa. Bila utashi wa kisiasa hatutoki mahali tulipo na ndio maana nataka kusema ni lazima sasa tuanze kuwa na utashi wa kisiasa na determination na commitment ya kwamba ni lazima uvuvi ubadilishe maisha ya nchi yetu, ni lazima uvuvi utupandishe kutoka tulipo kwenda hatua ya juu zaidi; bila ya political will hatupigi hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kwa kusema kwamba zawadi tulizopewa na Mungu zipo underutilized, ziwa letu na bahari yetu vipo underutilized; ni wakati wa sisi kuanza kuvitumia hivi vitu kuleta maendeleo ya nchi yetu. Kwa mfano, nataka nikupe data ndogo tu, mchango wa uvuvi kwenye GDP yetu kwa mujibu wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri ni 1.7 percent, wakati huo tuna maziwa yote na bado kwenye bahari yetu tuna maili 200 kutoka ufukweni, zote ni za kwetu tunaweza kufanya chochote. Nchi ya Uganda ambayo ina asilimia 45 tu ya Ziwa Victoria na Tanzania ina asilimia 49, GDP yake ni asilimia 12 mchango wa uvuvi. Ukianza kuona hivyo lazima ujue hapa kuna tatizo/kasoro ndio maana nasema kuna mambo ambayo wenzetu wanayafanya sisi hatuyafanyi, tunahitaji political will. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma Sheria ya Uvuvi ya Uganda ya mwaka 2018 na Sheria ya Uvuvi ya Tanzania yam waka 2003 nimegundua kwamba sheria yetu sisi imejielekeza zaidi kwenye ku-control lakini sheria ya wenzetu imejielekeza kwenye ku-facilitate. Hivyo basi, kama sheria yetu inaelekea kwenye ku-control, kila siku tutakuwa tunakamatana na wavuvi wetu, kuwachomea nyavu zao; jambo hili sio sahihi hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tujielekeze kwenye sheria ambayo ita-facilitate wavuvi wetu kuweza kuvua na kujipatia kipato na kuchangia kwenye GDP ya nchi yetu. Kama mambo haya hayawezi kufanyika nataka nikuhakikishie kabisa mchango wa uvuvi utaendelea kuwa mdogo kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, samaki wanachangia asilimia 20 ya protini ya wanyama katika nchi yetu. Kwa Uganda natolea mfano, samaki wanachangia asilimia 50 ya protini ya wanyama. Matumizi ya samaki wa Tanzania kwa mwaka kila Mtanzania anatumia kilo 5.5 tu lakini wenzetu ni kilo 15 mpaka 20. Ni lazima tufike mahali sasa tuamue kwa dhamira moja kabisa ya kuhakikisha kwamba watu wetu wanatumia samaki. Jimboni kwangu samaki imekuwa kitu expensive, watu wa kawaida hawawezi kumudu samaki kwa sababu gharama yake imekuwa kubwa sana. Sasa tufanye nini? Ili uvuvi wetu uchangie kwenye pato la Taifa letu, ili uvuvi wetu uwe na impact kwenye uchumi wetu ni lazima kama nilivyosema tuanze kuhakikisha kwamba kuna political will (dhamira ya kisiasa), tusije hapa kuzungumza tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunatoa michango mizuri sana, lakini kama hakuna political will hatupigi hatua. Kama Mheshimiwa Waziri hapa hawataachana na hofu na kuanza kutenda, hatupigi hatua hata kidogo. Tutabaki nyuma, tutaendelea ku-lag behind hatuwezi kukuza uchumi wa nchi yetu. Hatuwezi kuendelea namna hii, ni lazima tubadilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya nchi hii TBS wana kipimo chao cha nyavu na Wizara ina kipimo chake cha nyavu. Lazima hawa watu wawili wakae pamoja na wakubaliane…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mungu muweza wa yote kwa kunipa nafasi ya kusimama jioni hii ndani ya Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo mengi ambayo amelitendea Jimbo langu la Buchosa. Wananchi wa Buchosa wote kwa ujumla wao wanamshukuru Mheshimiwa Rais wao kwa barabara, maji, vituo vya afya na mambo mengi na kwa kweli tunasubiri utekelezaji kulipa fadhila zetu mwaka 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa leo nizungumze kile ambacho mimi naamini kwamba ni ukweli wangu. Nafahamu katika nchi yenye watu milioni 60 hatuwezi kufanana Mawazo yetu wakati wote. Tunatofautiana Mawazo, huyu atakuwa na Mawazo haya, mwingine na Mawazo yale. Kwa hiyo, nimepewa nafasi hii niweze kusema kile ambacho mimi naamini kitaweza kulisaidia Taifa langu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkononi mwangu hapa nimeshika kitabu, kitabu hiki kinaitwa The Checklist Manifesto, How to Get Things Right. Kitabu hiki nilikisoma baada ya kuona kwamba sifanikiwi kwenye mambo mengi. Nilikuwa nikifanya mambo mengi lakini sipigi hatua na wala nikienda nasimama, nikienda nasimama nikalazimika kutafuta kitabu hiki nikakisoma. Baada ya kusoma kitabu hiki kimebadilisha kabisa maisha yangu na ninaamini kwamba kama nchi ya Tanzania ilivyo na ninawashauri Waheshimiwa Wabunge tutafute kitabu hiki tuweze kukisoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kama nchi inahitaji checklist manifesto, orodha ya mambo ambayo tunataka kuyafanya, wazee wetu mwaka 1961 walikuwa na Checklist Manifesto baada ya uhuru wakasema tunayo madini mengi ardhini lakini tunayatunza yatachimbwa na watoto wetu. Checklist Manifesto, wameyatunza madini yale tumekuja kuyachimba sisi. Kwa hiyo, leo tunapokaa hapa kukaa kuzungumza tunajadiliana checklist manifesto ya nchi yetu. Tunataka kufanya nini ndani ya miaka mitano, tunataka kufanya nini ndani ya miaka 20 checklist manifesto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila checklist manifesto hatuwezi ku-achieve kitu chochote. Binafsi sina mashaka yoyote na Mheshimiwa rafiki yangu Profesa Mkumbo kwa uwezo wake na kwa uzalendo wake, lakini lazima tupange nini tunataka tukifanye ndani ya muda gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa nikiamini ya kwamba tunayo kazi kubwa ya kubadilisha Taifa letu, lakini hatuwezi kubadilisha Taifa hili kwa wakati mmoja kwa mambo yote. Ningependa tujiulize leo tunataka Tanzania ya namna gani? Tunataka Tanzania yenye nini baada ya miaka 50 au miaka sitini ijayo? Hilo ndilo jambo la kujiuliza leo na tunaanza kufanya kazi moja baada ya nyingine kwenye checklist yetu tuna-tick kitu kimoja kimoja hatimaye tutimize vitu vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika checklist manifesto yetu sisi kama Watanzania tunataka kufanya nini ambacho watoto wetu watakaokuja watakuja kutusifia nacho, kwamba wazazi wetu walitangulia walifanya mambo haya ambayo yamekuwa na faida kwetu. Kwa hiyo, tumekutana hapa kujadili Mpango na Mpango nimeusona una mambo saba Mheshimiwa Mkumbo ameyaorodhesha pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza sisi kama Watanzania, sisi kama Wabunge, sisi kama watu waliotumwa tunataka ku-achieve kitu gani, tunataka tukumbukwe kwa jambo gani kama Bunge la Kumi na Mbili, tunataka Rais wetu wa Awamu hii ya Sita akumbukwe kwa kipi? Lazima tuwe na vipaumbele, hatuwezi kuyamaliza matatizo yote kwa wakati mmoja lazima tu-set priorities, kipi katika list yetu yote ile tunataka tuanze na kipi kifuate nini? Hilo ni jambo ambalo nimelikosa wakati nasoma Mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitaji tukubaliane tunataka tuanze na barabara, tunataka tuanze na maji, tunataka tuanze na umeme ili mwisho wa siku tumalize kimoja baada ya kingine. Tukifanya hivyo tutamaliza mwisho wa siku itajulikana kwamba Rais wa Awamu ya Sita alishughulika na healthcare, Rais wa Awamu ya Saba alishughulika na barabara, Rais wa Awamu ya Nane alishughulika na maisha ya watu, hiyo ndiyo checklist manifesto, nimefanya hivyo maishani mwangu na maisha yangu yamebadilika. Tunayo sababu ya kuwa na checklist manifesto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimeusoma Mpango huu na nimeuelewa ya kwamba tunatakiwa tupange kipaumbele ninachokitafuta tunaanza na nini, kinafuata nini, tunakuja nini na tunamalizia na nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ambalo nataka kuliongelea hapa leo ni suala zima la mapato, ukurasa wa 21 pameandikwa tutaongeza mapato katika Mpango huu. Ninao ushauri wa kutoa, jambo pekee litakaloongeza mapato katika nchi ni kuboresha sekta zetu. Sekta zetu zimeshindwa kuchangia vya kutosha kwenye Pato la Taifa. Nchi hii ni Tajiri sana na wote tunafahamu lakini sekta zetu zimeshindwa kabisa kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi huwa natoa mfano wa Venezuela nikiongea, Venezuela ni nchi tajiri sana ya mafuta namba moja Duniani inafuatiwa na Saudi Arabia lakini Venezuela ni nchi maskini kuliko Tanzania kwa sababu wameshindwa kutumia utajiri wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utajiri tuliopewa na Mungu tuutumie kuingiza fedha kwenye kapu la Taifa. Tukiingiza fedha kwenye kapu la Taifa nataka kukuhakikisha ya kwamba fedha zitakuwa nyingi na mwisho tutakuja kufikiri hata kupunguza kodi kwa wafanyabiashara wetu. Tuwapunguzie VAT tukipinguza VAT lazima tutaongeza compliance ya wafanyabiashara waweze kulipa kodi kwa wingi, tukifanya hivyo tutakuwa tumesaidia sana nchi yetu, (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwawezesha wazawa kiuchumi tuwawezesheni watu wetu washikilie uchumi wa nchi yao, nimeshaongea sana jambo hili mara nyingi, tuwapeni fursa Watanzania washiriki kwenye kukuza sekta binafsi tuwape mitaji, tuwape fursa mwisho wa siku wakipata fedha Watanzania wataitumia hapahapa nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongee jambo la mwisho, National Innovation Fund, nimeshazungumza sana hapa, kwamba tuna vijana wengi wabunifu kwenye Taifa letu hawana mitaji, kama tuna Mfuko wa Kilimo, tuna Mfuko wa Filamu, tunayo Mifuko kadhaa tumeanzisha, tunashindwaje kuanzisha National Innovation Fund? Tuwasaidie wabunifu wetu wanatoka Chuo Kikuu hawana mitaji, watengeneze products.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina vijana wengi sana wabuni. Kuna mtu ametengeneza mashine za kusaga, mtu wa Darasa la Saba. Leo hii huko Iringa hawanunui mashine za Kichina wananua mashine za mtu huyo. Asaidiwe. National Innovation Fund itakopa fedha kutoka Global Innovation Fund. Global Innovation Fund, ni mfuko wa dunia ambao matajiri wakubwa kama akina Bill Gates wanapeleka fedha pale. Fedha hizi siyo mkopo, unaandika tu barua, unapeleka maombi, unapewa grant, na unawapa watu wako bila riba yoyote. Naamini tukianzisha National Innovation Fund, tutawasaidia sana vijana wetu wa Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Profesa Mkumbo, tumekuamini, tumekupatia jukumu la kutuendeshea mipango ya ychi yetu. Nataka nikwambie kaka, fanya jambo hili kwa uaminifu wako wote, kwa akili zako zote. Kwa sababu tumekupa responsibility na authority, mwisho wa siku tutaku-hold accountable. Tukifeli kama Taifa tutakushika mkono wewe. Bahati nzuri uliwashawahi kuwemo ndani halafu ukatoka, tumekurudisha tena, ukituharibia tutakutoa tena. Tukikutoa safari hii hatukurudishi tena. Kwa hiyo, nataka nikwambie Mheshimiwa Prof. Mkumbo, fanya kazi yako kwa akili zako zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshatoa ushauri, Waziri aunde kitu kinachoitwa National Economic Planning Think Tank. Wako watu kwenye Taifa hili wana akili nyingi japo hawana certificate wala degree, wala Ph.D. Wachague hao watu wakuzunguke wawe wanakupa ushauri. Ninaamini kabisa ya kwamba ukifanya hivyo utapata mawazo mazuri sana kutoka kwa watu na utafanikiwa kwenye kazi yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ni wizi. Sikuchangia kwenye Ripoti ya CAG, niliamua niache kwa sababu mara ya mwisho niliongea sana kuhusu wizi, lakini ngoja niligusie tena leo. Tunakusanya fedha lakini zinaibiwa. Kwenye Taifa hili ni kama kuna pepo wa wizi anazunguka. Kila mtu anataka aibe, lazima mpango huu unioneshe ya kwamba wizi utadhibitiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hapa ni pen. Kwa watu wengi hii ni kalamu, lakini wasomi mtanisamehe, simaanishi wasomi wote. Kwa wasomi wengi hii siyo kalamu, hii SMG, hii AK-47
MBUNGE FULANI: Eeeh!
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Wanatumia hii kuiba fedha zetu. Ni lazima tuwathibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu utamke kwamba watu watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria tulizonazo. Tuna sheria tano tumetunga ndani ya Bunge hili; Sheria ya Fedha, Sheria ya TAKUKURU, Sheria ya Manunuzi, Sheria ya Watakatishaji Fedha, Sheria ya Uhujumu Uchumi na bado kuna Sheria ya Jinai. Tutumie sheria hizi kuwadhibiti watu wanaotuibia,
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha anisikilize. Nataka nimwambie jambo, kuna bomu linakuja mbele. Ndani ya Wizara yake kuna Kitengo kinaitwa TSA kama sikosei, watu hawa wanaiba fedha, wanazituma kwenye halmashauri, halafu zinatoka kwenye halmashauri zinarudi kwao. Naomba kaka yangu ninakupenda, nenda kawadhibiti Watu wa TSA watakuingiza kwenye matatizo. Wanatuma pesa kwenye halmashauri… (Makofi)
MWENYEKITI: Kengele ya pili, ahsante.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa nafasi ya kuwa ndani ya Bunge hili Tukufu, nafahamu dhahiri kabisa kwamba siko hapa kwa sababu nina akili nyingi na uwezo mkubwa, bali niko hapa kwa sababu Mwenyezi Mungu aliamua niwe mahali hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mabadiliko anayoyafanya katika Taifa letu, ukitembelea Buchosa leo utashangazwa na uzuri wa barabara, utashangazwa na miradi mingi ya maji yenye thamani yenye karibu Shilingi Bilioni 15, utashangazwa na madarasa mazuri vijana wetu wakisoma katika hali nzuri kabisa, napenda nimpongeze sana Rais wetu na ninaipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, mimi huwapima watu na uwezo wao wa akili kwa matendo, nirudie tena uwapima watu uwezo wao wa akili kwa matendo yao. Mara ya mwisho niliongea hapa nikasema tuna best President, intelligent President and clever President, nilisema! Narudia tena leo maneno haya leo kuyasema na nitatoa sababu mtu yeyote ambaye ana mashaka na uwezo wa Rais wetu anisikilize kwa makini.
Mheshimiwa Spika, Rais wetu amefanya jambo moja kubwa sana kuonesha kwamba ana uwezo mkubwa, jambo hilo niuwekaji wa post code bajeti ya post code ilikuwa Bilioni 720 samahani, lakini alivyopelekewa mezani bajeti ile alikatakata mpaka Bilioni 28, ni mtu mwenye akili peke yake anaweza akafanya jambo la namna hiyo. Katika hali ya kawaida ukiletewa ripoti mezani huwa tuna tabia ya kupitisha tu, lakini Rais wetu alikata mpaka ikabaki Bilioni 28.
Mheshimiwa Spika, ninapozungumza na wewe leo tayari mradi wa kuweka post code nchi nzima umekamilika kwa asilimia 95. Narudia tena kusema kwa matendo haya nina kila sababu ya kusema we have the best President, intelligent President, clever President na smart President. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa bajeti yake, nimeona ni bajeti ya kimapinduzi ameenda kuendelea kufanya mambo makubwa katika Taifa letu, nimuombe Mheshimiwa Waziri ajiepushe na kufanya vitu vinavyofanya awe popular badada ya kufanya vitu ambavyo vitamfanya vitu sahihi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Waziri asiguse kabisa ile asilimia 10 aiache kama ilivyo hilo la kwanza, asiguse kabisa asilimia 10 aiache kama ilivyo na ikiwezekana aiongezee. Jambo lingine la muhimu sana ambalo nataka nilichangie katika bajeti hii ya leo ni kwamba tunakusanya fedha nyingi sana tunakopa fedha tunakusanya fedha kwenye kodi tunapeleka kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, lakini kuna kitu kimoja muhimu sana ambacho mimi naona kama tunakisahau ni ufuatiliaji wa fedha zetu tunakozipeleka, monitoring and evaluation.
Mheshimiwa Spika, Dada yangu Mheshimiwa Eng. Ulenge aliwahi kuzungumza siku moja hapa ndani suala la monitoring and evaluation, ufuatiliaji na tathmini ni changamoto kwenye Taifa letu. Tunakusanya fedha nyingi tunapeleka huko kwenye Halmashauri zetu tunasahau kwamba kuna watu ambao hawaogopi fedha ya umma kabisa! Wanasubiri fedha ya umma ije waitafune. Niseme bila kupindisha maneno kwamba Halmashauri zetu ni mchwa wa fedha za umma narudia tena halmashauri zetu ni mchwa wa fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninawaomba kama Taifa ninawaomba Waheshimiwa Wabunge, tujue kabisa ya kwamba tunao wajibu wa kufuatilia fedha zetu ambazo tumezipeleka kwa wananchi, Rais wetu ana nia njema ya kuleta maendeleo lakini hatufuatilii fedha zetu. Mfano, mdogo wangu Mheshimiwa Aweso alienda Handeni, nikamsikia anasema nionyeshe bwawa akarudia nionyeshe bwawa hakuna bwawa akaoneshwa dimbwi Milioni 600 zimeliwa.
Mheshimiwa Spika, sijakaa sawa nikamuona Kaka yangu Mheshimiwa Prof. Mbarawa na yeye analalamika kwenye television ya kwamba nioneshe temporary office, temporary office imekuja kuonekana ya Milioni 100 ni kibanda cha mabati! Sijakaa sawa nikamuona ndugu yangu Mheshimiwa Musukuma Kaka yangu Kasheku analalamika kwamba kule kwake bati ya kununuliwa Shilingi 40,000 imenunuliwa Shilingi 72,000. Sijakaa sawa nikamuona Kaka yangu ambaye ninamheshimu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Kassim yuko MSD anasema vifaa vinavyotakiwa kununuliwa kama sijui ilikuwa Milioni 20 kimenunuliwa kwa Milioni 129.
Mheshimiwa Spika, hii ni mifano michache tu ambayo tumeiona kwenye television, iko mifano mingi sana ambayo hatuioni ya pesa za umma zinatafunwa na watu wenye nia mbaya na maendeleo ya nchi yetu! Monitoring na evaluation naungana na Dada yangu Mheshimiwa Ulenge leo hayupo kuiomba Serikali yangu iimarishe ufuatiliaji na tathmini ya pesa zinazoenda vijijini, tofauti na hapo tutakuwa tunapeleka fedha zinaishia mikononi mwa watu wachache, zinatafunwa, hakuna kinachofanyika. Hatuwezi kutimiza ndoto ya nchi yetu kama watu wachache wanatuvurugia movement yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilisoma ripoti moja na ilinisikitisha sana ripoti hiyo ya transparence international ambayo walisema dola bilioni 50 zinatoka Afrika kila siku kwenda mabenki ya Ulaya, nikasoma chini yake nikakuta wanatamka jambo la kusikitisha kabisa kwamba kiasi cha dola bilioni 4.5 zinapotea kama mapato katika Taifa la Tanzania, fedha ambazo zingethibitiwa zisipotee zingejenga Vituo vya Afya 1,730 kwa kituo kimoja milioni 600. Zingethibitiwa zisipotee zingeweza kujenga kilometa 5,300 za lami. Najenga hoja ya kwamba fedha zinazopotea zikidhibitiwa zisipotee maendeleo yetu yatakwenda kwa kasi kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa tunafanya nini kama Taifa; Kwanza, nilizungumza tulipoitwa Ikulu na Mheshimiwa Rais kule Chamwino, nikasema Tanzania kama mataifa mengine ya Afrika yalivyo yanasumbuliwa na ugonjwa mmoja mbaya unaitwa Institutional failure. Taasisi zetu zime-fail, zime-fail tafsiri yake ni lazima ziimarishwe, kama taasisi zinafanya kazi zinavyotakiwa Mheshimiwa Aweso – Waziri wa Maji asingeweza kulalamika pale kuhusu bwawa, pale alipolalamika Mheshimiwa Aweso hakuna Mkurugenzi? Hakuna DC? Hakuna TAKUKURU?
SPIKA: Sasa ngoja Mheshimiwa nilikuwa nimekuacha ili uende na huo mtiririko lakini sasa wacha nikuongoze kidogo, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aweso ni Mheshimiwa Aweso awe shemeji yako, kaka yako humu ndani ni Mheshimiwa, kwa sababu la sivyo tutafika mahali watu wanaanza kama mke wangu alivyosema. Sasa ngoja tuite kwa kadri Kanuni zinavyotuongoza humu ndani wote ni Waheshimiwa kwa sababu ukisema tu neno Aweso bila Mheshimiwa Baba yake anaitwa Aweso, sasa tunakuwa hatujui unamuongelea yupi unamuongelea huyu Waziri au yule mwingine. Ahsante sana.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naomba nimuombe sana radhi mdogo wangu Mheshimiwa sana Jumaa Aweso kwa kumtaja tu kama Aweso na Mheshimiwa Spika nimeyapokea maelekezo yako vizuri kabisa.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba niseme what do we do? Nilizungumza alipotuita Mheshimiwa Rais Ikulu kwamba, tatizo kubwa la Tanzania na nchi za Afrika ni Institutional failure, taasisi zimeferi taasisi zingefanya kazi yake zisingemsubiri Mheshimiwa Aweso- Waziri wa Maji, zisingemsubiri Mheshimiwa Waziri Mkuu, palepale kuna DC, Mkurugenzi, kuna watu wa TAKUKURU wangefanya kazi yao sawasawa wasingemsubiri Mheshimiwa Waziri Mkuu au Mheshimiwa Waziri wa Maji aje.
Mheshimiwa Spika, naomba sana tuimarishe taasisi zetu zitimize wajibu wake kule chin,i tunafanyaje kwenye suala zima la mapato ya umma? Kwenye mapato ya umma tuimarishe TAKUKURU. Nilikaa wiki mbili zilizopita na Mkurugenzi wa PCCB ofisini kwake nikawa nazungumza naye nabadilishana naye mawazo, tunafanyaje tuweze ku-control tuweze kudhibiti rushwa katika Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, tulipoanzisha TAKUKURU ilianza mwaka 1974 lakini hata 1991 ilikuwa inaitwa (PCB) Prevention of Corruption Bureau, kazi yake ya kwanza TAKUKURU kabisa ya mwanzo kabisa ilikuwa ni kuzuia rushwa mwaka 2007 tukabili sheria tukaita Prevention and Combating of Corruption Bureau (PCCB). Tukaongeza suala la combating maana yake sasa ni kuzuia na kupambana na rushwa, TAKUKURU wamesahau suala zima la prevention wamejielekeza kwenye combating kwenye kupambana, wanazo kesi nyingi sana hivi sasa lakini bado kuna kesi nyingi zinatokea.
Mheshimiwa Spika, nataka TAKUKURU wawezeshwe, tuwawezeshe kufanya suala la prevention kuzuia rushwa wamelisahau hiyo task. Mheshimiwa Waziri amezungumza juzi hapa, akasema amewawezesha CAG kwa kuwapa fedha nyingi, namuomba Mheshimiwa Waziri hizo fedha badala ya kuzipeleka CAG awapelekee PCCB ili wawezeshwe kwa mafunzo, kwa idadi kubwa ya watu wa kufanya kazi maana yake labor force, mwisho wa siku tuweke sheria ya kwamba fedha inapokwenda kwenye Halmashauri yoyote iwe mandatory iwe ni lazima PCCB wapate kopi kwa ajili ya ufuatiliaji. Narudia tena iwe ni lazima PCCB kupata copy kwamba tumepeleka fedha Milioni 600 na isome ya Kituo cha Afya kwa hiyo TAKUKURU wapokee kwa ajili ya ufuatiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi sasa ninavyozungumza ni hiyari kuwapelekea TAKUKURU. Naomba niunge mkono hoja ahsante kunisikiliza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai ambayo ameniwezesha kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu leo kuweza kuzungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa mambo mema anayolifanyia Taifa letu. Kama sijakosea hesabu zangu sawasawa, leo ninapozungumza, amesafiri angani masaa 402, akienda huku na kule kutafutia riziki Watanzania na kuiunganisha Tanzania na nchi za nje katika kutengeneza mahusiano. Hakika anafanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Buchosa, nasimama hapa kumpongeza sana Rais wangu kwa kazi nzuri anayoifanya. Kwa wanaoelewa maana ya kusafiri kwa ndege masaa yote hayo angani ni jambo linalochosha sana, lakini hivi ninavyoongea, anatarajia kurejea nchini kutoka Uturuki. Kwa hiyo, nina kila sababu ya kumpongeza Rais wangu kwa kazi njema anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu. Pia nampongeze sana Spika wetu wa Bunge kwa mambo mema na anavyotuwakilisha kila kona ya dunia. Ametuletea heshima kubwa sana. Mara kwa mara huwa namwambia binti yangu, anasema yeye ni role model wake. Kwa hiyo, kama mwanangu anaangalia hivi sasa, basi ajue ya kwamba anatakiwa awe kama Spika. Nitakuwa mzazi mwenye kujivunia sana nikiwa na mtoto kama yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nina mambo mawili tu leo na ninaomba niongee kwa utaratibu na nimemwomba Mungu anisaidie niweze kueleweka. La kwanza ni upande wa wafanyakazi wa nchi hii kwa sababu leo tunajadili Bajeti ya Utumishi, na la pili ni suala la rushwa na ufisadi katika Taifa letu kwa sababu tunazungumzia watu wa TAKUKURU.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la TAKUKURU, muda ukitosha kule mbele nitakuja kwenye suala la watumishi, maana limeshaongelewa na watu wengi. Nilisimama hapa wakati fulani akiwa anawasilisha rafiki yangu Mheshimiwa Ndumbaro akiwa Waziri wa Sheria, nikazungumza juu ya TAKUKURU ambao wanafanya kazi kubwa sana. Kazi yao ni njema, nimesoma ripoti leo ya Transparency International, wamepanda kidogo kutoka nafasi ya 38 mpaka nafasi ya 40.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi duniani TAKUKURU ina nafasi ya 87 kwenye ubora wa kujiepusha na masuala ya rushwa. Kwa kweli nina kila sababu ya kuwapongeza. Katika Afrika Mashariki, Tanzania ni nchi ya pili ikiongozwa na Rwanda. Kwa hiyo nataka niwapongeze sana TAKUKURU kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, leo nina jambo linaloitwa Security of Tenure. Nilizungumza mara ya mwisho hapa nikasema, tunahitaji kum-protect, tunahitaji kumkinga Mkurugenzi wa TAKUKURU kwa maana ya Security of Tenure. Jambo hili linafanyika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kulinda ajira yake, ajira ya Majaji na ajira ya CAG, kwamba ukishamteua CAG huwezi kumwondoa, labda kuwe na sababu ambayo imetajwa katika Katiba. Hata Rais akimteua CAG hawezi kumwondoa tu hivi akaamka asubuhi akaamua kumtoa. Kwa nini waliamua kufanya hivyo kwa CAG? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yao ilikuwa ni kumpa uhuru (Independence) wa kufanya kazi yake bila kuingiliwa. Ndiyo ilikuwa sababu tumpe nafasi, tuilinde ajira yake. Ukimteua leo, huwezi kumtoa kesho asubuhi. Kuna mchakato mrefu sana mpaka utengeneze tribunal ndiyo uweze kumwondoa na ushauriwe kama Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini jambo hili halifanyiki kwa Mkurugenzi wa TAKUKURU? Nataka Mheshimiwa Waziri ukija hapa unijibu, kwa nini hutaki kum-protect Mkurugenzi wa TAKUKURU? Kwa nini Wabunge hatuitishi sheria ije hapa Bungeni tuweze kufanya marekebisho ya sheria tuweze kum-protect? Kwa nini ni muhimu kum-protect? Kwa nini ni muhimu kulinda ajira ya Mkurugenzi wa TAKUKURU? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano, umemkamata leo mtu kwenye halmashauri yako, amekuja CAG amekagua ambaye ana-deal na wanasheria, halafu unamwita mtu wa TAKUKURU amkamate akamhoji amfikishe Mahakamani. CAG ana protection analindwa, akishatoka pale huyu mtu anakabidhiwa kwa mtu ambaye halindwi na sheria ambaye ni Mkurugenzi wa TAKUKURU.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna uwezekano na simaanishi katika nchi yangu, kuna uwezekano katika nchi nyingine wakubwa au watu wenye ushawishi kupiga simu na kumwambia achana na hiyo kesi, lakini huwezi kumwambia hivyo CAG kwa sababu analindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni rahisi sana kumpigia Mkurugenzi wa TAKUKURU na kumwambia achana na hiyo kesi. Mkubwa ametuma ki-memo kimekuja, anatetemeka, anakuwa na hofu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nani asiyependa maisha mazuri? Ukishateuliwa tu Mkurugenzi wa TAKURURU, heshima inaanza siku ile ile, Land Cruiser V8, ofisi nzuri mpaka mjukuu wako kijijini anaitwa huyu ni mjukuu wa Mkurugenzi wa TAKUKURU. Nani yuko tayari kupoteza hadhi hiyo? Ikija memo mtu anasema aah, bwana ee, bora mimi nibaki na familia yangu. Ndiyo maana nasema kama CAG ambaye anafanya kazi similar kabisa na anayofanya Mkurugenzi wa TAKUKURU, ni lazima tum-protect, ni lazima tuilinde ajira yake kwa sheria na kwa Katiba yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili siyo geni. Nitakusomea hapa baadhi ya nchi ambazo zimefanya hivyo. Kabla sijasoma hizo nchi nikusomee Azimio la Umoja wa Mataifa Ibara ya 6 ambayo imetamka katika Ibara ya 6 (2) inasema; “Each state shall grant the body or bodies referred to in paragraph one of this article the necessary independence, in accordance with fundamental principles of its legal system, to enable the body or bodies to carry out its or their functions effectively and free from any undue influence.” Umoja wa Mataifa wamesema, kuwe na chombo ambacho kinalindwa na sheria ambacho ni TAKUKURU, ifanye kazi yake vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuachane na Umoja wa Mataifa, twende moja kwa moja Ghana. Ghana sheria yao Kifungu cha 4 na 5 wametamka hivi, “The procedure for removal of commissioner and deputy commissioners shall be the same as that provided for the removal of a Justice of the Court of Appeal and a Justice of the High Court respectively.” Ghana wamesema kumwondoa Mkurugenzi wa TAKUKURU iwe sawasawa na mchakato ule wa kumwondoa Jaji. Hao ni Ghana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Seychelles sheria yao inatamka hivyo hivyo. Senegal sheria yao inatakamka hivyo, kwamba kumwondoa Mkurugenzi wa TAKUKURU iwe ni mchakato mrefu. Kwa nini wanamlinda? Ili asiingliwe na mwenye mamlaka ili asiingiliwe na wenye ushawishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huko kote ni mbali, hebu twende kwa jirani zetu Zanzibar. Naomba univumilie kidogo. Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria yao inatamka katika article ya 5 Kifungu cha 5, mimi siyo Mwanasheria, najua kupita pita kidogo inasema, “In order to protect the integrity and independence of the authority, the Director General shall not be removed…”
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudie. “…shall not be removed from office, except for reasons and procedures laid down for the removal of the High Court Judge according to the article 95 of the constitution.” Hapo ni Zanzibar, ni sehemu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo sawa kutokum-protect Mkurugenzi wa TAKUKURU, ni kama vile tumejitengenezea kamlango kwamba tunabana hapa kwa CAG halafu tukibanwa sana tunaenda tunachomokea kwa Mkurugenzi wa TAKUKURU, haitakiwi, haiwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, nawaomba, tumeaminiwa na Watanzania na wizi, ubadhirifu, rushwa zimechelewesha maendeleo ya Taifa letu, zimechelewesha maendeleo ya Afrika. Tuhakikisheni tunapambana na adui rushwa kwa nguvu zote na tuanze na sheria. Kazi yetu sisi Wabunge tumeletwa hapa kutunga sheria na kuishauri Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sheria hii irejeshwe na sisi tuweke kipengele kama walichoweka ndugu zetu wa Zanzibar ili tum-protect Mkurugenzi wa TAKUKURU.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili. Maneno yako mengine ni ya muhimu yaandike mpe Waziri sasa hivi.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa Kuchunguza Mgogoro wa Ardhi kati ya Mwekezaji kwenye Shamba la Malonje na Vijiji Vinavyolizunguka Shamba hilo Kikiwemo Kijiji cha Sikaungu katika Jimbo la Kwela
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nikiri kwamba kuzungumza baada ya wazungumzaji wazuri kama hawa huwa ni changamoto kidogo, lakini najua Roho Mtakatifu atanisimamia na nitasema kile ambacho nataka kusema.
Mheshimiwa Spika, kwanza naanza kukushukuru wewe mwenyewe kwa uamuzi wako wa kuona nafaa kuwemo kwenye hii Kamati. Kwangu mimi hii ni privilege, ni heshima kubwa na nataka nikuhakikishie kwamba kazi yako imefanyika vizuri, imani yako haijapotea bure, nimekuwakilisha nilivyotakiwa, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nianze kwa kuunga mkono yote ambayo yamesemwa na Mwenyekiti wangu pamoja na wajumbe wengine wote. Nilichokikuta kule ni kwamba wananchi wa vijiji vile hawana ardhi ya kulima, huo ni ukweli wa kwanza ambao nimeukuta. Sehemu kubwa ya ardhi yao imechukuliwa na mwekezaji. Sasa kwa sababu hiyo, nakubali kabisa shamba hili libatilishwe na shamba hili liweze kugawanywa tena upya na wananchi wapate sehemu kubwa zaidi ya mwekezaji kama atapata.
Mheshimiwa Spika, naomba nikiri kwamba huwa ni mtetezi sana wa wawekezaji wa ndani, nimeshasimama mara nyingi hapa nikasema nitawatetea sana wawekezaji wa ndani ili waweze kumiliki uchumi wa nchi yao. Wajumbe wa Kamati watakumbuka, nilipokuwa natoa mchango wangu mwanzoni nilikuwa nasema, bwana huyu ni mwekezaji wa ndani lazima tumsaidie na yeye aweze kukua. Tukafunga safari kwenda Sumbawanga, kilomita nyingi.
Mheshimiwa Spika, nilipofika kule, niliyoyakuta, niliyoyaona nilibadilisha mtazamo wangu kuhusu wawekezaji wa ndani. Nimekuta umaskini uliopindukia wa watu wa vijiji vile. Hawana mahali pa kulima. Watu wa Sikaungu mwaka huu hawajalima kabisa, hata chakula kinakuwa tabu kukipata.
Mheshimiwa Spika, nimekutana na watu wamekatwa masikio, nimekutana na akinamama wengine wenye umri mkubwa kabisa wamebakwa. Nimekutana na kijana amepigwa risasi ziko kichwani.
Naomba nikiri nimeokoka na nampenda Yesu, lakini nilipoyaona yale nilijiuliza swali moja, huyu Mwingira, naomba niseme jina, huyu Askofu, na najua ananitazama hivi sasa, hivi huyu ni Askofu kweli? Haya mambo yanaweza yakafanywa na mtumishi wa Mungu kweli? Neno la Mungu kwenye Mithali 14:30 linasema, amuoneaye maskini amdharau Mungu na amhurumiaye maskini amheshimisha Mungu. (Makofi) [Maneno Haya Si Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Spika, baada ya haya niliyoyashuhudia, nilibadili msimamo wangu kabisa…
SPIKA: Mheshimiwa Shigongo, ngoja tuliweke sawa, jambo hili.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, tuliweke sawa.
SPIKA: Kwa sababu katika wale wawekezaji, zimetajwa kama taasisi. Kwa hiyo, Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Efatha nadhani na Efatha Foundation na kuna mahali nafikiri imetajwa Efatha Heritage. Sasa akitajwa mtu mmoja kwa jina lake atakuwa hajatendewa haki na Bunge kwa sababu zimetajwa taasisi. Yeye anaweza kuwa ni mkuu wa mojawapo ya taasisi hizo, lakini kwa maana ya hapa, mwekezaji ni hizo taasisi. Kwa hiyo, yeye kuwa kiongozi wa dini na hiyo nafasi yake ya uaskofu lazima somewhere atakuwa anaitendea haki hiyo nafasi ya uaskofu, kwa sababu kilichofanya uwekezaji sio Askofu, aliyefanya uwekezaji ni taasisi. Sasa huenda taasisi ziko chini yake, yeye ndiye Mwenyekiti na mambo kama hayo, mimi sijui kwa sababu sijazipitia. Sasa ili twende vizuri kwenye hoja hii, haya maneno hapa tunayaondoa ili yasilete mkanganyiko baadaye ili sisi tushughulike na mwekezaji. Wewe nenda na mwekezaji na hayo makampuni ambayo ndiyo yametajwa kama wawekezaji. Huyu aliyetajwa jina hapa kwa maana ya Askofu hajatajwa yeye kama ndiye mwekezaji. Ahsante sana Mheshimiwa Shigongo.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naomba nikubali, lakini sasa nirekebishe kauli yangu iwe hivi, hivi huyu Efatha kweli huyu Efatha, Huyu Efatha kweli ni mwakilishi wa Mungu duniani? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nimeondoa jina la mtu, huyu Efatha. Huyu Efatha amenibadilisha kabisa mtazamo wangu. Nimeokoka nasema nampenda Yesu na Biblia imetamka wazi ya kwamba amuoneaye maskini amdharau Mungu. Kwa matendo haya yaliyofanywa kama kweli ni maelekezo ya huyu Efatha image ya kanisa langu inaingia kwenye utata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ngoja nielekee kwenye hoja, wananchi hawa ni maskini. Mimi nimezaliwa familia maskini sana na kuingia hapa ndani ya Bunge ni privilege. Mimi peke yangu kufika hapa kuna maskini wengine wengi sana wako nyuma wanaohitaji ardhi iwatoe kwenye umaskini wao.
Mheshimiwa Spika, sio mimi tu miongoni mwa wanasheria wako mmojawapo anaitwa Praisegod Lukio anatoka huko Sumbawanga, jirani kabisa na maeneo yale, amesoma shule kimaskini. Elimu imemsaidia kuwa mwanasheria. Tunahitaji kuwasaidia wananchi wa vijiji hivi ili wapate ardhi hii iweze kuwasaidia kusomesha watoto wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haitawezekana katika Taifa hili ninalolifahamu mimi kukaa na watu ambao wako juu ya sheria. Hakuna mtu ambaye yuko above the law; wote tunaheshimu Katiba ya nchi yetu, tunaheshimu sheria ya nchi yetu. Haiwezekani mtu mmoja anafanya vitendo vya kinyama kiasi hiki, taasisi moja inafanya vitendo vya kinyama kiasi hiki halafu hakuna hatua inayochukuliwa.
Mheshimiwa Spika, wananchi wanafanyiwa yote haya, mtu hafikishwi hata polisi. Mimi kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nitasimama na wananchi wa nchi hii, nitasimama na upande wa haki siku zote za maisha yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme, shamba hili ni kubwa sana. Nilitembea shamba lile unaenda umbali mrefu sana uko ndani ya shamba moja. Naomba sana Waheshimiwa Wabunge. Namwomba sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, Taarifa, hapa Mheshimiwa Jacqueline.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kabla sijamsimamisha anayekuwa anazungumza ni kwamba sentensi yake anakuwa hajamaliza. Kwa hiyo na akirejea kwenye kuzungumza hataweza kumaliza ile sentensi yake. Kwa hiyo, ukisema taarifa, nakuwa nimeshasikia, akimaliza akifika mahali nakunyanyua, usiwe na wasiwasi.
Mheshimiwa Shigongo, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani.
TAARIFA
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa mchango mzuri wa Mheshimiwa Shigongo.
Mheshimiwa Spika, nataka niseme tu kwamba kutokana na hoja nzuri ambayo anaizungumza kwamba hakuna sheria yoyote wala hatua zozote zinazochukuliwa dhidi ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia unaofanyika, maana tumesikia kuna kubakwa, kuna watu kulawitiwa, kuna kukatwa masikio. Sasa naomba kwa niaba ya Serikali Waziri mwenye dhamana ya ukatili wa kijinsia Mheshimiwa Gwajima akaishtaki Efatha kwa niaba ya Serikali. Ahsante.
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, ili kesi iweze kufika Mahakamani ni lazima uchunguzi ufanyike na nadhani kwenye mapendekezo ambayo Kamati Maalum imeyaleta mbele ya Bunge hiyo ni sehemu kwamba uchunguzi wa kina ukafanyike ili ikijulikana hayo matendo yamefanywa na watu fulani basi watu hao wachukuliwe hatua za kisheria. Kwa hiyo, Mheshimiwa Gwajima yeye hawezi kwenda kushtaki lazima ule utaratibu wa kisheria tuliouweka ufuatwe.
Mheshimiwa Eric Shigongo.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa ya dada yangu Mheshimiwa Jacqueline Msongozi. Sasa nimalizie kwa kusema yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, nafahamu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Rais mwenye huruma, ni Rais ambaye anafikiria sana maisha ya watu wake. Katika hili naomba sana aliunge mkono Bunge lake Tukufu na kama ni kubadilisha hati ibadilishwe hati mara moja na wananchi waweze kupata maeneo ya kulima.
Mheshimiwa Spika, umaskini ni kitu kibaya sana. Naongea habari ya mwanasheria wako Lukio, anatoka maeneo yale yale, amekulia kwenye umaskini ule ule. Wazazi wake wameuza mahindi wamempeleka shule, leo ni mwanasheria. Tunahitaji watu wengine wengi katika nchi hii watoke familia maskini wawe kama sisi. Hawawezi kufika tukiendelea kuwanyang’anya ardhi na kumpa mtu mmoja.
Mheshimiwa Spika, nisiseme mengi sana, naomba niunge mkono hoja na ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama katika Bunge hili Tukufu ili niweze kutoa mchango wangu kwa Taifa langu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Buchosa. Sisi Buchosa tunahitaji barabara yetu ya lami kutoka Sengerema hadi Nyehunge ijengwe. Kwa hiyo, nimetumwa na wananchi wangu, kwamba fedha zitengwe ili barabara ile iweze kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili nataka nizungumzie Taifa langu Tanzania. naipenda sana nchi hii, na ushahidi wa uoendo wangu kwa nchi yangu ni uamuzi wangu wa kumwita binti yangu jina Tanzania. Kwa hiyo hayapo mashaka ya kwamba mimi ninaipenda nchi yangu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii, nisome data kidogo tu, kwa utalii Duniani ni ya pili, Afrika ni ya kwanza kwa utalii. Nchi yangu kwa makaa ya mawe ni ya 50 Duniani, kwa gesi asilia ni ya 82 Duniani, Tanzania kwa dhahabu ni ya 22 Duniani, kwa Helium ni ya kwanza Duniani, kwa almasi ni ya 10 Duniani, kwa Tanzanite ni ya kwanza Duniani, Tanzania ni nchi tajiri sana hatuwezi kuwa maskini hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaposikia mtu anasema nchi yangu maskini, mimi huwa sikubaliani na hilo jambo na sitaki watoto wa nchi hii waelewe nchi yao ni masikini, nchi yetu ni tajiri sana hatuwezi kuwa jinsi tulivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Venezuela ni nchi ya kwanza Duniani kwa mafuta, inafuatiwa na Saudi Arabia, na Urusi ya tatu lakini Venezuela ni nchi masikini sana kuliko Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka nimpongeze Rais wetu wa Awamu ya Sita kwa uamuzi wake wa kutumia sekta za uchumi kuongeza Pato la Taifa huo ni uamuzi wa Rais wetu kwamba amaeamua sekta zote za uchumi zichangie Pato la Taifa ili pato la Mtanzania mmoja mmoja liweze kuongezeka nampongeza sana Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Wabunge na Mawaziri niwaombe tumuunge mkono Rais ili sekta zote za uchumi ziweze kuchangia Pato la Taifa hatuwezi kuwa maskini kwa utajri tulionao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwapongeze Wabunge na nikupongeze wewe kwa uamuzi wa Bunge hili kupambana kubadilisha Sheria ya Manunuzi. Tumebadilisha Sheria ya Manunuzi na Kanuni zimebadilika kwamba kuanzia tarehe 01, Julai hakuna mgeni yeyoye anayefanya biashara ya bilioni 50 kushuka chini kwenye nchi hii. Tumefanya jambo jema sana tutakumbukwa kwa uamuzi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumedalili Sheria ya Manunuzi, Kanuni lakini kuna jambo moja tusipolifanya mabadiliko haya hayatatusaidia chochote. Benki zetu za Tanzania zibadilishe mtazamo wake kwa wafanyabishara wazawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi hii benki zetu hazitaki kuwekeza sana kwenye biashara zinataka kuwekeza kwenye mikopo ya wafanyakazi na watu wadogowadogo. Hauwezi kutajirika kwa fedha yako mwenyewe kuitoa laki moja kwenda milioni moja ni rahisi. Ila kuitoa bilioni moja mpaka bilioni 100 ni kitu kimoja kigumu sana you have to use the bank, lazima tutumie fedha za watu wengine. Kanuni ya utajiri inasema hivi use other people’s money sasa wenye pesa ni benki, kama benki zetu hazitabadilisha mtazamo wake kuwasaidia wazawa wa nchi hii waweze kuchukua fedha na kufanya biashara mabadiliko haya ya sheria tuliyoyafanya hayatasaidia chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba leo nitoe elimu kidogo, naomba nitoe elimu ndogo tu ya kitu kinachoitwa triangle of money ambayo matajiri wote wa nchi hii wanaitumia pembe tatu ya pesa upande mmoja ni A, upande wa pili ni B na upande wa tatu ni C iko chini, naomba nisikilizwe vizuri A ni mtengenezaji wa bidhaa B ni mnunuzi na C hapa chini ni mfanyabiashara. Sasa mfanyabiashara anaingia mkataba na TFC kwa kuiuzia labda mbolea, watakubaliana kwamba tutanunua nao mbolea tutalipa kwa siku tisini, mfanyabiashara huyo anaenda kuongea na mtengezaji wa mbolea yuko China au Urusi wanakubaliana atalipa kwa siku 120 anadaiwa kwa siku 120 analipa kwa siku 90. Matokeo yake hapa ni kwamba kama mbolea ni ya milioni 100 mimi sina milioni 100 nitaenda benki. Benki inatengeneza back-to-back LC yaani back-to-back LC ni kwamba inaingia mkataba na mnunuzi atalipa kwa siku 90 benki inaingia mkataba na muuzaji wa mbolea atalipa basi 120, maana yake ni nini? Nitalipwa na Serikali siku 90 kabla sijadaiwa na mtengenezaji wa mbolea maana yake hapo ni nini? Unatengeneza pesa bila kutumia pesa lakini benki lazima ikae nyuma yangu kunisaidia, benki zetu haziko tayari kufanya jambo hilo ni waoga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba CRDB wamejitahidi lazima niwapongeze na Mheshimiwa Bashe nimpongeze sana amewasaidia sana wafanyabiashara kwenye korosho kule kutumia mfumo huu Mtanzania anafanya biashara ya bilioni 100 anasaidiwa na benki tutumie mfumo huu kuwatajirisha Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wamechoka kuwa masikini, mimi mwenyewe nimechoka kuwa masikini. Nataka Watanzania watajirike kwa sheria hii kwa sababu hawana mtaji benki ziwe tayari kufungua back-to-back LC kuwasaidia ili huu mfumo wa pembe tatu ya fedha niliousema uweze kusaidia, hauhitaji pesa kupata pesa na hili jambo lazima lieleweke. Kama benki zinaogopa basi Serikali iwe tayari kutoa government guarantee kwamba kwenye korosho unahitaji bilioni 300 Serikali itoe karatasi peke yake government guarantee kuzipa benki ili ziwakopeshe Watanzania waweze kufanya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hilo lieleweke na kama jambo hili likifanyika nakuhakikishia Watanzania watabadilika, tumechoka kuwa maskini lazima jambo hili lifanyike tusaidie tuweze kutoka hapa tulipo. Kwa hiyo, kuendelea kuona wageni wanakuja hapa kila siku wanatajirika sisi tunaendelea kuwa maskini hatutaki na sisi hatutaki kuchukia siku moja tuweze kuwa kama nchi nyingine, tunataka amani ya nchi yetu iendelee kuwepo na Watanzania waendelee kunufaika na nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema hivi mambo manne ya kufanya kuisaidia nchi yangu la kwanza Sekta za Uchumi zichangie Pato la Taifa. Lazima tuhakikishe jambo hili linafanyika kama utalii umechangia Mheshimiwa Rais amecheza sinema mapato yameongezeka kutoka Dola milioni 900 mpaka Dola bilioni tatu ndani ya miaka mitatu iwe hivyo kwenye uvuvi, madini na kilimo nakuhakikishia tukifanya hivi iko siku tutapunguza mikopo tunayokopa, tutapunguza budget deficit na kesi ya bajeti inapungua tutatumia fedha zetu kujiletea maendeleo wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala zima la Sheria, Sheria zetu tulizonazo ziwe zinatoa fursa kwa Watanzania wazawa kufanikiwa, Sera zetu za Uchumi tuzipitie upya. Inawezekanaje mfanyabiashara wa Kitanzania akafungue duka Zambia? Inawezekanje mfanyabiashara wa Kitanzania akasajiri malori yake Rwanda? Kuna shida mahali fulani hapa ndani lazima tupitie upya tariff zetu ziwe za ushindani inawezekanaje ukanunie mashuka Kenya? inawezekanaje ukanunue mashuka Uganda? Kuna nini hapa kwetu ambacho kinakosewa? Tutazame upya sera zetu za Uchumi na sheria zetu ziwe ni zinazoshindana na nchi jirani tunapigwa bao tukiwa tunaona? Haiwezekani tukaendelea namna hiyo kama kweli tuna nia njema ya kuendeleza nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni upendo kati yetu sisi wenyewe Watanzania tupendane, Watanzania tubebane haiwezekani akaja mtu kutoka China akafanikiwa mimi Mtanzania nikabaki chini. Nchi yetu imefika mahali ukitaka kazi mahali fulani unalazimika kumkodisha mzungu wa kukodisha. Wako wazungu wanakaa Serena pale wanalipwa Dola 500 kwa saa, akaonekane mzungu ili wewe Mtanzania upate kazi, naomba Watanzania tupendane tushirikiane sisi kwa sisi ili tuweze kuinuka kwa pamoja katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni law enforcement, Sheria tunatunga, tuzisimamie ili kwamba sheria hizi wanaozivunja wapate adhabu inayowastahili. Haiwezekani watu unakusanya fedha zinaliwa watu wanaiba halafu bado hawawezi kidhibitiwa na sheria zetu. Tuna sheria nzuri sana, tuna Sheria ya Manunuzi nilishaisema, tuna Sheria ya Utakatishaji Fedha, Sheria ya Fedha, Sheria ya TAKUKURU, sheria hizi zote zikisimamiwa sawasawa tutawadhibiti wote wanaoiba fedha zetu kutakakuwa na hofu na woga kwenye fedha za umma hatuwezi kwenda hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma niliwahi kushauri kwamba tutafute utaratibu wa kuwachapa watu wanaoiba fedha za umma. Sasa mimi ninashauri tuongeze idadi ya magereza kwa watu wanaoiba fedha za nchi yetu…
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Eric.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Ununuzi wa Umma wa Mwaka 2023.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kipekee mchana huu wa leo kuwa mzungumzaji wa kwanza kwenye mjadala huu wa Sheria ya Ununuzi.
Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Kamati kwa kazi nzuri ambayo wameifanya ya kupitia sheria hii na kufanya mabadiliko ya muhimu kabisa ambayo mimi nimeyaona.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sana nimekuwa nikilalamika kuhusiana na Sheria ya Ununuzi, kwamba sheria hii imetumika sana kuwafanya Watanzania washindwe kuwa na kasi ya kukua kiuchumi. Nilikuwa na mjadala mrefu sana na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha, baadaye nikapata mjadala mrefu sana na Mkurugenzi wa Sheria wa Bunge, baadaye nikapata nafasi ya kukutana na watu wa PPRA kujadiliana kuhusu sheria hii.
Mheshimiwa Spika, najua waliokuwepo kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara watakumbuka kwamba nimewahi kuzungumzia huko nyuma ya kwamba iko sababu ya kuzipitia baadhi ya sheria zetu ili ziweze kutengeneza mazingira ya Watanzania kushikilia uchumi wa nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Taifa hili ni tajiri sana, nimeshazungumza na leo nasema na kesho nitasema na wiki ijayo nitasema, Taifa hili ni tajiri sana; kwa historia ndogo tu; Pato la Taifa letu ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan limeongezeka kwa takribani dola za Kimarekani bilioni 20, ndani ya miaka miwili. Hii ni ishara ya kwamba Taifa hili likitumika vizuri hakika hakuna sababu ya Watanzania kuendelea kuwa maskini, lakini tunazo changamoto kubwa sana za sheria zetu.
Mheshimiwa Spika, sheria zetu mara nyingi zimefanya ukuaji wetu uwe kidogo kidogo au utajiri wetu usionekane kwenye maisha yetu. Nchi tajiri lakini watu wake wanakuwa maskini na hii ni kwa sababu ya sheria ambazo tumezitunga. Sasa najisikia mwenye bahati sana leo kupata nafasi ya kushiriki kutunga upya Sheria hii ya Ununuzi. Kwa utajiri tulionao hatutakiwi kuwa jinsi tulivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa naelewa nia ya Rais wetu ambayo ni kuona nchi hii tunapiga hatua kwa kasi, kuona Watanzania vijana wa nchi hii wanafanikiwa kushikilia uchumi wa nchi, ndiyo nia ya Rais wetu. Hili lengo haliwezi likatimia kama hatujapitia sheria kama hii ya ununuzi. Kuna msemo unasema no one gets rich until the government decides (hakuna mtu anaweza kutajirika mpaka Serikali yake iamue) kwa kutengeneza mazingira ya mtu kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimewahi kuzungumza nyuma na ninarudia tena, miaka 15 iliyopita hapakuwa na bilionea hata mmoja kwenye list ya mabilionea duniani, na katika list ya mamilionea 500 wa dunia hapakuwa na Mchina hata mmoja, lakini Rais wa China aliamua miaka 10 iliyopita kwamba nataka niweke watu wangu kwenye hiyo list. Leo ninavyozungumza nusu ya ile list ni Wachina kwa sababu nchi iliamua kuwafanya watu wake watajirike.
Mheshimiwa Spika, ongelea Huawei, WeChat, Oppo, kampuni zote za Kichina ambazo zimefanya vizuri kwa sababu nchi iliamua. Sasa kazi yetu kama Bunge ni kutunga sheria ili Serikali iendeshwe kwa sheria hizo. Nataka niseme kwa nia moja thabiti ya kwamba lazima kama Bunge na kama nchi tuamue kwamba tunataka vijana wetu wafanikiwe na washikilie uchumi wa nchi.
Mheshimiwa Spika, vijana wetu wamechoka kutazama, wanakuja watu hapa kutoka nchi mbalimbali, sheria zetu zinaruhusu, wanafanya biashara na baada ya miaka mitano wakishakuwa mabilionea wanaenda kwenye mitandao wanaanza ku-brag kwamba I came to your country, I earn a lot of money, nawafahamu watu, ni marafiki zangu kabisa, ametoka nje amekuja Tanzania ame-tender vitabu vya shule ya sekondari halafu baadae ananipigia simu ananiambia nimekushinda kwenye ile tender, ananicheka, kwa sababu ya sheria zetu.
Mheshimiwa Spika, tumesaini mkataba hapa wa African Continental Free Trade, mkataba mzuri tu wa kufanya Afrika iwe soko moja. Mimi nilikuwepo na rafiki yangu Mheshimiwa Mkumbo alikuwepo, tukapitisha ile sheria lakini unajua ya kwamba kwa sheria hii tusipowalinda watu wetu, tutaenda kuua viwanda vyetu. Hivi tunajua kwamba tusipowalinda watu wetu kwa sheria hii tuliyosaini sisi wenyewe tunaenda kuua biashara za watoto wetu. Nilikuwepo kwenye Kamati na Mheshimiwa Mkumbo shahidi, nilisema napitisha sheria hii lakini naomba watu wetu walindwe. Atakumbuka na hata leo narudia, kwa sheria hii tuliyosaini kama hatuwezi kuwa-protect watu wetu tutaua biashara za watu wetu na tutawatia umaskini watu wetu. Ni sheria nzuri tu, lakini hakuna nchi isiyowalinda watu wao, haipo. Nakumbuka niliwahi kuzungumza mtu mmoja akaniambia protection is over, kwamba mambo ya kulinda watu yalishapita, hapana, kila nchi inalinda watu wake na inasaidia watu wake waweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumetunga Sheria ya Uwekezaji nzuri tu, nilikuwepo kwenye Kamati ya Viwanda, tumetunga sheria nzuri kabisa na tunawapa wawekezaji incentives nyingi waje nyumbani wawekeze. Sipingi foreign direct investment hata kidogo, sikatai. Nataka mitaji ije waanzishe biashara watu ili wetu waajiriwe, lakini bado naomba tuwalinde watu wetu kwa sheria zetu. Tusipofanya hivyo tutalaumiwa, watu watafilisika, biashara zitakufa kwa sababu tunawa-expose watu wetu kwenye ushindani ambao hawawezi kuuhimili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanakuja tunawapa incentives, good, hamna shida, watu wao tunawapa incentives bado wanatudanganya, wanafanya transfer pricing, wanatudanyanya mambo mengi wana-declare loss, they don’t pay tax most of them, huo ndio ukweli. Lakini tunafanya ili kuwasaidia akina Taletale? Tunafanya ili kumsaidia Taletale aweze kukua na kuweza kushindana na hawa wageni wanaokuja? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ununuzi hii ya mwaka 2011 na marekebisho yake yote 12, 13, 14 mpaka 18; naipongeza Kamati ya Bajeti na nimezungumza sana nao mmoja mmoja, nimefanya kazi nzuri, nimeona preference, ni upendeleo umewekwa mle. Lakini mimi sina amani na Ibara ya 57. Hii naomba niiseme Ibara ya 57 sina amani nayo kabisa na kama kuna kitu cha kukijadili kwa kirefu leo ni Ibara ya 57.
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 57, naomba kwa idhini yako noisome, inasema; “Endapo rasilimali fedha zimetolewa na taasisi ya umma ya Kitanzania pekee, kila ununuzi wa kazi za ujenzi bidhaa na huduma zenye thamani isiyozidi ukomo ulioainishwa kwenye kanuni utatengwa kwa ajili ya watu wa kampuni za ndani.” Imetamka hivyo kwamba kitakuwepo kiwango cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya kampuni za ndani. Sasa ukienda kwenye kanuni kwa sheria hii tunayobadilisha kiwango kilichowekwa ni bilioni tano. Kampuni ikiwa na bilioni tano inakuwa hiyo tender ni national tender, ikifika bilioni sita inakuwa international tender, ina maana niki-tender tender ya bilioni 10 lazima nitakutana na mchina, nitakutana na mhindi; sasa nitamshindaje kwenye tender? Nawezaje kumshinda mtu amekuja hapa na mkopo wa asilimia mbili ilhali mimi nina asilimia 18 za CRDB, inawezekanaje? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huyu mtu akienda kufanya biashara nje ya nchi anapewa incentives ya 20 percent na nchi yake kwa sababu anakwenda kufanya biashara nje ya nchi. Mimi naweza tender nikamshinda huyu, matokeo yake akinishinda bei yake itakuwa ndogo kuliko mimi. Nataka sheria hii imsaidie Mtanzania kushinda kwenye biashara hizi.
Mheshimiwa Spika, mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge, Watanzania wanatutazama, wamechoka kuona utajiri wa nchi yao unaenda nje, wamechoka, wamechoka; tunapitisha bajeti hapa ya trilioni arobaini na kitu wanataka kujua fedha ngapi zinabaki nyumbani? (Makofi)
Mheshimwa Spika, tunao uwezo wa kutengeneza mabilionea 10 kila mwaka kwenye taifa hili, tunaweza sisi, kwa mnong’ono wa Taifa, taifa linong’one tu, kwamba biashara fulani bwana tutawapa wakina Kingu, basi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi siwezi kwenda India leo nikapewa kazi ya kuchapa vitabu, ni uongo, hata kama nime-tender kuna namna fulani watafanya kazi iende kwa watu wao. Sheria hii hasa kipengele hiki nataka kitamke, kwenye sheria na si kwenye kanuni, kitamke kwamba limit iwe angalau bilioni 50 angalau tutoke tano mpaka bilioni 50, hiyo hiyo national tender, baada ya hapo twende international hapo sawa, baada ya muda tutakua, na sisi tutawafata Wachina huko huko juu kwenye bilioni 60 kwenda juu.
Mheshimiwa Spika, hili si jambo la ajabu, Kenya jirani yetu sheria yake ya ununuzi inatamka kwamba unit ya national tender ni shilingi za Kenya milioni 500 ambazo ni sawasawa na bilioni 10 za Kitanzania. Wiki iliyopita wamepeleka tena muswada Bungeni wanaipandisha kutoka milioni 500 mpaka bilioni tano ambayo ni sawasawa na bilioni 100 za Kitanzania. Hao ni jirani zetu tu hapo wamepandisha mpaka bilioni 100 za Kitanzania, hiyo kazi haifanywi na mgeni, wanafanya Wakenya wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ombi langu na ninaomba mnisikilize na Waheshimiwa Wabunge mniunge mkono, hii limit ihame kwenye bilioni tano iende angalau kwenye bilioni 50 angalau; hata 100 twende ili tuweze kuwalinda watu wetu waweze kutajirika.
Mheshimiwa Spika, umaskini ni kitu kibaya, hawa watoto wanamaliza vyuo vikuu wanakaa hapa hawana cha kufanya wanauza njugu, halafu anakuja Mchina anauza karanga Kariakoo, hawapendi, tunawafanya wanakuwa na chuki na wageni, tunasababisha xenophobia bila sababu ya msingi, tuwape nafasi vijana wetu ili wakue kwa kubadilisha hicho kipengele kwenye sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema haka kakipengele kasipo badilika leo moto utawaka…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Mbunge kengele ya pili ilishagonga.
MHE. ERIC J. SHIGINGO: Mheshimiwa Spika kwa haya machache naomba kuunga mkono hoja, ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa kwa sababu ya ufinyu wa muda, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuzungumzia moja kwa moja mambo yanayohusu jimbo langu. Nimeshazungumza mara kwa mara na Mheshimiwa Waziri kuhusu tatizo kwenye Visiwa vya Zilagula pamoja na Maisome ambako wananchi wale wanategemea umeme kutoka kwa watu binafsi. Hivi ninavyozungumza wananunua unit moja kwa Sh.2,400. Huyu ni mwananchi wa kawaida, maskini, nimeshazungumza na Mheshimiwa Waziri naomba atakapokuwa anafunga hotuba yake hapa awaeleze wale wanaitwa Jumeme na PowerGen, alishatoa maelekezo wauze umeme kwa Sh.100 lakini baada tu ya Hayati kupumzika wamepandisha bei. Kuna maneno wanayasema kwamba aliyekuwa anatusumbua ameondoka, hawajui kama mama Samia ni moto wa kuotea mbali. Kwa hiyo, mimi nina nia ya kushika shilingi ya Mheshimiwa Waziri kama hatakuwa na maelezo ya kutosheleza kwenye eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nizungumzie maeneo ambayo bado kuna matatizo makubwa sana ya umeme kwenye jimbo langu katika Kijiji cha Itabagumba, Makafunzo, Bupandwa, Nyehunge, Kanyala, bado kuna shida kubwa sana ya umeme. Umeme uko kwenye center tu, ukizama huko ndani kuna nguzo na maeneo mengine hakuna nyaya. REA Mkurugenzi yuko hapa, Mheshimiwa Waziri na Naibu mko hapa mhakikishe sasa umeme unakwenda moja kwa moja mpaka kwenye maeneo ya ndani kabisa ili lawama hizi ziweze kupungua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda niongelee kuhusu suala la nishati, kuna uhusiano mkubwa sana kati ya nishati na maendeleo ya watu. Taasisi moja inaitwa MDI ilifanya utafiti wakasema unapoongeza matumizi ya umeme kwa asilimia moja, unaongeza pato la Taifa kwa asilimia 1.72. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maana yangu hapa ni nini? Naomba kwanza nipongeze sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhakikisha kwamba umeme unapatikana kwa asilimia kubwa. Hii imewezesha pato la nchi yetu kukua. Naomba kabisa tuendelee kutafuta nishati kwa gharama yoyote ili nchi yetu iweze kuwa Africa Power House. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo hili likifanyika, hata kama tunapingwa, mimi nakumbuka wakati tunaanza ujenzi wa Bwawa la Nyerere tulipingwa, walisema kwamba kuna masuala ya mazingira. Namshukuru sana Hayati, namshukuru mama Samia, walisema hata kama kuna issue ya mazingira bwawa litajengwa na bwawa limejengwa. Jana nimesikia wameanza tena Wazungu kusema bomba la mafuta lina issue ya mazingira kwa hiyo hatutapewa mkopo; tusiwasikilize Wazungu, wanajua kwamba tukishakuwa na nishati tutakuwa na nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Baba wa Taifa, Mwalimu J. K. Nyerere alijua kwamba ili tukue kiuchumi tunahitaji nishati. Rais wetu, Hayati, alikuja hapa ametekeleza ndoto ya Baba yetu wa Taifa. Kweli tutakuwa na umeme wa kutosha katika Taifa letu na umeme utakuwa ni wa bei rahisi kuliko wakati mwingine wowote, wawekezaji watakuja na biashara zitaongezeka. Unapoongeza umeme, unaongeza production na GDP ya Taifa lako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri na Waheshimiwa Wabunge tulioko hapa leo, tuna bahati ya kuwa ndani ya Bunge hili, wazee wetu waliotangulia wamefanya maamuzi mazuri sana sisi leo ni Taifa bora na sisi tuliopo hapa ndani tufanye maamuzi bora kwa ajili ya watoto wetu watakaokuja baada ya sisi. Nataka Bunge la Kumi na Mbili likumbukwe kama Bunge lililohakikisha Tanzania inakuwa Africa Power House kwa kuwa na energy ya kutosha ili tuweze kukua na uwezo huo tunao. I don’t care where the source is, as long as ni power, leta power, hata kama ni nuclear power leta nuclear power ili tuweze kuwa na nguvu kama Taifa. Tukiwa na nishati hakuna atakayetutisha, uchumi wetu utakuwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu wake na moyo wa kujituma. Nampongeza sana Naibu wake, TANESCO na REA. Ninachowaomba sasa wakachape kazi zaidi ili Taifa letu liweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kama hakutakuwa na majibu ya suala la umeme unit moja Sh.2,400 nitashikilia shilingi. Naomba niishie hapo, Mungu ibariki Tanzania, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu katika kupitisha Azimio hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ni-declare interest kwamba ni makamu mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara na nilikuwepo kwenye mjadala mrefu sana kuhusiana na mkataba huu. Cha kwanza niliposoma mkataba huu mambo mawili yalinikuta la kwanza niliingia hofu, hofu yangu ya kwanza kabisa ilikuwa ni kwamba mkataba huu utaua viwanda vyetu, mkataba huu utaondoa ajira zetu, huo ni upande mmoja, lakini kuna upande mwingine mzuri sana wa mkataba huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ambao ulikuwa ni kwamba Afrika sasa inakwenda kufanya integration, Afrika inaanza kuuziana Afrika kwa Afrika, Afrika inaanza kufanya biashara Afrika kwa Afrika jambo ambalo huko nyuma lilikuwa halifanyiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipofika hapo nikaamua kuchagua upande wa uzuri wa mkataba, nikaamua kabisa kuachana na hofu ambayo ilikuwa imenikamata na hivi sasa nimesimama hapa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla wetu tuweze kuridhia Azimio hili nchi yetu ikaweze kuingia katika mkataba huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale waliowahi kusoma kitabu cha Walter Rodney how Europe underdeveloped Africa, alisema Walter Rodney ukitaka kuichezesha Afrika isababishie tu iwe na disintegration yaani tu tuwe hatuna ushirikiano na wakoloni walifanya jambo hili kwa umakini kabisa na wakatugawa wakaweka mipaka ardhini baadaye mipaka hiyo ikaamia kwenye vichwa vyetu. Kwa hiyo, tunatembea hapa Watanzania nikivuka tu pale Namanga kuingia upande wa Kenya hofu inaniingia. Na wakati narudi nyumbani nikivuka Namanga nikiingia upande wa Arusha kiburi kinaanza. Kwa hiyo, kuna mipaka tunayo ndani ya vichwa vyetu hiyo ndiyo itakayotuchelewesha kuweza kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba huu au Azimio hili linakwenda kuondosha barrier zote ambazo zilikuwepo ili sasa Afrika ifanye biashara Afrika kwa Afrika, ukijaribu kuangalia data ambazo zipo Afrika kwa Afrika kwenye Intra business, biashara ya ndani ya Afrika kwa Afrika ni asilimia 17, lakini ukiangalia Asia ni asilimia 69, ukiangalia North America ni asilimia 31. Kwa hiyo, ninachojifunza hapa ni kwamba tunafanya hii biashara sisi kwa sisi kidogo sana hatuwezi kukua mpaka tuweze kuondoa barriers, tuanze ku-trade kati ya Taifa na Taifa. Hapa tunazungumza tuna mahindi si ajabu kuna nchi haina mahindi, inahitaji mahindi lakini unaweza ukashangaa ikaagiza mahindi Brazil badala kuagiza mahindi Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naunga mkono Mkataba huu na ninaomba kabisa Waheshimiwa Wabunge wote turidhie kwa nia moja tuachane na hofu, tukubali kwenda kujifunza tukiwa tunafanya kuna learning unapokuwa unafanya na kuna kujifunza kwanza ndiyo ufanye. Ninawaomba tukubali nchi yetu iingie tukajifunze tukiwa tunatenda, tutarekebisha huko ndani kwa ndani, tutabadilisha mikakati tukiwa tunavyozidi kwenda tuta-change strategies, hatimaye tutaweza kuweza tutaweza kufanya vizuri hatutaweza kupata faidia kwenye mwaka wa kwanza au mwaka wa pili lakini nina uhakika kabisa baada ya muda si mrefu tutafanya vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la muhimu sana ni capacity building ni lazima nchi yetu iwawezeshe wafanyabiashara wetu. Ni lazima wapewe mikopo yenye riba ndogo, ni lazima tutambue ya kwamba Nigeria uchumi wake ni mkubwa sana kuliko uchumi wetu sisi. Ukinipambanisha mimi na Okwonko sasa hivi kuna uwezekano wa ku-fail, lakini kama nimewezeshwa na nchi yangu kama nchi yangu inadhamira ya kweli political will kwamba tunawapeleka hawa watu vitani wakapambane tutahakikisha kwamba wanashinda lazima tutashinda vita hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, South Africa ilifanya hivyo wakapatikana wakina Patrick Motsepe ni wakati wa nchi yetu tutengeneze mabilionea wengine wapya. Tumekuwa na mabilionea wale wale miaka hiyo tangu tukiwa watoto ni wakati sasa tuanze kusikia majina ya Aweso, tuanze kusikia majina ya kina Kigwangalla wakiwa mabilionea tumechoshwa na majina yale yale kila mwaka. Kwa mkataba huu nina uhakika wakiwezeshwa vijana wa kitanzania tutasikia majina mapya, kuna uwezekano kabisa wa kutengeneza wakina MO wengine, kutengeneza wanakina Bakharessa wengine kwa mkataba kama huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niseme kwamba tariff za kodi; tariff za kodi tusipoziangalia vizuri zitatuumiza. Nitatoa mfano mmoja hai nilitembelea kiwanda kimoja cha mapipa pale Mbagala, Mhindi anatengeneza mapipa mazuri tu lakini anashindwa kuuza Kenya, kwa sababu gani anashindwa kuuza kenya Kodi, Wakenya wanapoagiza sheet za chuma pale kwao hawatozwi kodi kwa sababu wananunua kwenye COMESA, wananunua Egypt. kwa sababu wako ndani ya COMESA hawalipi kodi asilimia 10, lakini yeye anapoagiza hapa analipa ten percent na Wakenya wakitengeneza mapipa yao pale kwa sababu ni EAC wanauza soko la Tanzania. Kwa hiyo matokeo yake mapipa yale yanakuwa chini kwa asilimia 10 upande wa bei lakini mapipa ya Mbagala yanakuwa juu, hawezi kuuza Kenya, hawezi kuuza hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kodi zetu tuzitazame vizuri wenzetu tunapotoa tariff ya kodi wanaziangalia hivi Tanzania import duty wameweka shilingi ngapi, wao wanapunguza kidogo ili waweze kushinda kwenye soko/wawe competitive kwenye soko. Ombi langu tariff za kodi tuwe smart kwenye eneo hilo, tuzipitie tuziangalie na tuwe smart kuwashinda wenzetu. Kwa nini mtu anatoka hapa anaenda kununua masharti Kampala anakuja kuyauza Dar es Salaam anapata faida, hapo kuna tatizo kwenye types za kodi kama mnataka bidhaa zetu ziweze kushinda kwenye soko tuziangalie types za kodi na ziweze kupunguzwa kushindana na wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono Azimio. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, kwa sababu ya ufinyu wa muda nianze kwa kukupongeza wewe kwa kupata nafasi ya kuwa Naibu Spika wetu, lakini nichukue nafasi hii poa kumpongeza sana Jirani yangu, dada yangu, Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu kwa nafasi hii ambayo ameteuliwa kuliongoza Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumpongeza pia Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa inayoendelea hapa nchini; kwenye miundombinu, afya, kwa kweli mimi binafsi ninaridhika kabisa kwamba kazi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 8(1) (a) inasema;Lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi. Hapa inamaana kazi kubwa ya Serikali ni kuhakikisha kwamba wananchi wake wanaustawi katika afya, katika uchumi, katika miundombinu, katika elimu na mambo mengine yote. Ni kazi ya Serikali nadhani nizungumzie suala moja juu ya uwezeshaji wa wazawa kiuchumi katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hili kwa sababu sisi tulioko hapa ndani tumebahatika kuwa Wabunge, tumebahatika kuwa na Maisha tulioyonayo lakini wako watu wenzetu wengi sana huko nje bado wanaishi Maisha duni na kwenye umasikini mkubwa. Bajeti ya Taifa letu kwa mwaka ni tirioni 34.88 najiuliza swali kila siku, tirioni 34.88 ngapi zimerudi kwa wananchi na ngapi zinaenda nje ya nchi yetu. Nimesimama hapa kuzungumza kwa niaba ya watanzania wazawa na ninaposema wazawa simaanishi rangi namaanisha watu wenye asili ya Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watanzania wanatakiwa wanastahili kunufaika kabisa na fedha hizi tirioni 34.8 inakuwaje fedha hizi sehemu kubwa zinaenda nje ya nchi badala ya kuwasaidia wazawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kwa sababu Bunge lako tukufu mwaka 1994 lilitunga Sheria ya uwezeshaji wazawa kiuchumi na ilisainiwa na Marehemu Rais Benjamini William Mkapa tarehe 19 Januari, 2005 ya kwamba nchi hii itawawezesha wazawa weweze kushikilia vyanzo vya uchumi vya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo ninaposimama hapa bajeti ya miundombinu ya Taifa hili ni tirion 3 nataka nijiulize tirioni 3 hizi za kutengeneza barabara ya miundombinu gapi zinabaki kwa watanzania bajeti hii ya miundombinu peke yake ni trioni 3 ni ngapi zinabaki kwetu sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wengi wanaendelea masikini mabilionea ni wale wale toka miaka ile na wajibu wa Serikali ni ustawi wa wananchi wake. Napenda kuona wazawa wengi wanafanikiwa kiuchumi katika Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani na sitaki kutaja nchi yoyote kama alivyozungumza Rafiki yangu Mpina haiwezekani tirioni 3 za barabara fedha inayoenda kwa wazawa ni asilimia 20 peke yake nyingi zinaenda kwa wageni wanaokuja hapa na magegi peke yake baada ya miaka mitano wamekuwa mabilionea na wanatuona sisi wazawa hatuna akili haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kukuomba wewe na kuomba Bunge hili tukufu kwa sheria hii ya Mwaka 1994 ya kuwawezesha wazawa kiuchumi, wazawa wapewe kipaumbele ni nchi gani duniani ambayo hakuna mnong’ono wa Taifa ni lazima Taifa hili linong’one na kusema ya kwamba biashara ya kiwango hiki itaenda kwa wazawa, barabara ya kilomita hizi zitaenda kwa wazawa, haiwezekani tukawaachia wageni kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayasema hayo siyo kwamba nachukia wageni nchi yangu inahitaji sana mitaji kutoka nje, lakini pamoja na kuhitaji mitaji kutoka nje bado tuwe na uwezo wa kuwa- protect watu wetu na kuwapa watu wetu kipaumbele ya kwamba tumezungumza hapa ndani nataka haya mambo yaende nje ya kwamba tender za aina fulani zitaenda kwa watu wetu hata kama hatuzungumzi, hata kama hatuandiki kwenye magazeti, hatakama hatusemi huko nje tunajua nitakapo tenda mimi na akatenda na huyu kutoka nje nitapewa mimi kwa sababu fedha hizo zitazunguka hapa hapa nchini kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili lizingatiwe kwa sababu watanzania wamechoka kuona wageni wanaendelea kutajirika wao wanaendelea kuwa maskini. Ni lazima wao wapewe nafasi ya kutajirika kwenye nchi yao nah ii nchi ni ya kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaandika kwa maandishi mambo yote ninayoyazungumza ahsante kwa kunipa nafasi nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataallah kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu, nimshukuru sana Jehova kwa upendeleo alionipa kuwa mmoja wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana wewe kunipa nafasi ya kusimama lakini niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Buchosa kwa kunituma hapa Bungeni kuwawakilisha, nataka niendelee kuwaahidi ya kwamba nitakuwa mwakilishi bora nitakaye wawakilisha wao hapa Bungeni na sitajiwakilisha mwenyewe hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda mbele sana naomba kwanza niunge mkono hoja, lakini niongee mambo matatu au manne hivi kabla sijazungumza hasa jambo nataka kuchangia.
Mheshimiwa Spika, kwanza; nataka nizungumze suala la uwezeshaji wa wazawa kiuchumi, nimezungumza hili suala mara kadhaa nataka nilizungumze tena leo. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 8 (1)(b) jukumu kubwa la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa ni kusimamia ustawi wa watu wake. Mwaka 2004 tukatunga sheria katika Bunge hili ya kuwawezesha wazawa wa nchi hii kushikilia uchumi wa nchi yao baada ya kuona kwamba uchumi ulikuwa mikononi mwa wageni, sheria hiyo ilisainiwa na Rais Mkapa Marehemu mwaka 2005 na ikaunda Baraza la Uwezeshaji wa Wazawa Kiuchumi ambalo lipo mpaka leo.
Mheshimiwa Spika, naomba sana bajeti tunayopitisha mwaka huu ya zaidi ya shilingi trilioni 40 hivi naomba iweze ku-consider sana wazawa wa nchi hii. Wazawa wa nchi hii wamechoka kuona sehemu ya bajeti kubwa kama hiyo inaishia kwenda nje na wao wanabaki na umaskini. Kwa hiyo, naomba hilo lizingatiwe kabla sijaenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili; nchi hii ina vijana wengi sana wabunifu. Nchi hii ina watu wengi sana wenye uwezo mkubwa wa kubuni solutions mbalimbali, lakini wengi wanaenda nazo kaburini kwa sababu ya ukosefu wa uwezo wa kuzalisha bidhaa au kuendelea mbele na ubunifu wao. Naiomba sana bajeti hii izingatie suala zima la kuanzisha National Innovation Fund, Mfuko wa kuwawezesha vijana wabunifu wa nchi hii waweze kwenda mbele na ubunifu wao na kutengeneza bidhaa. Hii ninaongea ni kama mara ya tatu ya nne hapa Bungeni kwa sababu wapo watu wengi sana wana ubunifu upo ndani ya kabati lakini hawana mtaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huko duniani kuna kitu kinaitwa Global Innovation Fund ambayo huwa inatoa fedha nyingi sana kwa mataifa mbalimbali kusaidia wabunifu wao. Ethiopia mwaka jana wamepewa Euro Milioni Sita na hizi zinakuja siyo mkopo zinatolewa kama grant kwa wabunifu wetu wanaotoka vyuo vikuu ambao hawana mtaji na hawakopesheki na benki zetu.
Mheshimiwa Spika, ninawaomba watalaam wetu, PhD ambazo tunazo katika nchi hii ziandike maandiko ili tuweze kupata sehemu ya fedha hizo ziwasaidie watu wetu.
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu; nataka kukumbusha kabla sijaenda mbele ni suala zima la kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mkataba au makubaliano ambayo iliingia na nchi za Uarabuni kuhusu mafuta. Waliingia makubaliano ya kwamba nchi za Uarabuni zitakuja hapa zitawekeza kwenye mafuta zitaweka matenki makubwa ili mafuta yawe yanawekwa hapa Tanzania igeuke kama Dubai au Gulf ya Afrika Mashariki na Kati. Naomba Serikali yangu itekeleza jambo hili mapema hizi deal na urasimu huu uondolewe ili jambo hili lingekuwa limeshafanyika mapema hakika tusingekuwa pengine tunapata changamoto tunayoipata leo. Kwa hiyo, naomba hilo lifanyike mapema sana.
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho na ninaomba niungane na Profesa Kitila Mkumbo ya kwamba ex-ordinary times require ex-ordinary decisions. Nchi yetu inapita kwenye wakati mgumu sana hivi sasa na siyo Tanzania peke yake ni dunia nzima inapita kwenye wakati usiokuwa wa kawaida, ninaiomba Serikali yangu Tukufu ifanye maamuzi magumu kwenye kipindi hiki.
Mheshimiwa Spika, mwaka 1979 baada ya vita ya Uganda nakumbuka Rais wetu Hayati Baba wa Taifa alisema tufunge mkanda kwa miezi 18, watanzania tunatakiwa kufunga mkanda kipindi hiki kwa sababu ni wakati mgumu kabisa na yafanyike maamuzi ambayo yatasaidia wananchi wawe na unafuu wa maisha. Huko vijijini kwa watu wa chini kabisa achana na sisi huku juu, ukienda watu wana malalamiko makubwa sana. Kila kitu kimepanda bei, mafuta ya kupikia, mafuta ya petrol, kila kitu kipo juu na wananchi wanashindwa hata ku-afford Maisha. Kwa hiyo, tufanye maamuzi ambayo yatakuwa na maslahi kwa Taifa.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nizungumzie suala la umaskini wa Taifa hili. Mwaka jana tumesherehekea uhuru wa nchi yetu mwezi wa 12, ni kweli Taifa hili limepiga hatua kubwa sana na mimi nakubali, lakini umaskini bado upo na umaskini unawasumbua sana watu wa nchi hii. Sisi wote hapa tunatoka vijijini na wengi wetu hapa tunatoka katika familia maskini tunaelewa madhara ya umaskini.
Mheshimiwa Spika, Taifa hili umaskini mkubwa unawakabili wakulima wa nchi yetu. Nchi hii wakulima wanapata shida na ndiyo mafukara namba moja, kilimo kimeajiri asilimia 65 ya watu. Naomba nizungumzie suala la kilimo kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, ili nchi hii iondoke kwenye umaskini unaotukabili ni lazima tuwekeze sana kwenye kilimo chetu, hatuwekezi vya kutosha kwenye kilimo. Nchi hii wakulima wanazidi kuwa maskini kila siku, tumeshakuja na mipango mingi sana, siasa ni kilimo, kilimo cha kufa na kupona, kilimo kwanza, mambo mengi tuna-fail wakati umefika tujiulize ni kwa nini tuna-fail. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Taifa hili lina ardhi kubwa sana square kilometer Laki Tisa hivi, na ardhi ambayo inaweza kulimwa ni kama square kilometer za miraba Laki Nne hivi. Lakini nchi ya Malawi ni ndogo, ardhi yao ambayo inaweza ikalimwa ni square kilometer kama 50,000 hivi, lakini wanazalisha soya bean tani 230 kwa mwaka sisi tunazalisha tani 6,000 mpaka 20,000 kwa mwaka na ukubwa wa hekta tunao na mchango wa kilimo kwenye pato la Taifa ni asilimia 26% lakini Malawi ina 42 % what is wrong with us. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka tujiulize kama Taifa nini shida yetu katika kilimo? Naomba uwekezaji kwenye kilimo ufanyike kwa nguvu kubwa sana kuwasaidia wakulima wanchi hii. Mazao ya nchi hii wakulima wetu wanalima lakini mwisho wa siku mazao yanaishia kuharibika, post-harvest loss kwenye Taifa hili ni asilimia 40, tafsiri yake ni kwamba unalima mazao lakini asilimia 40 yanaharibika.
Mheshimiwa Spika, miwa katika Taifa hili tunavuna tani Milioni Nane kwa mwaka, lakini tunatumia tani Milioni Nne peke yake na tani Milioni Nne zinaharibika. Naambiwa na wataalam wa kilimo kwamba tani Milioni Nne zinazoharibika zingeweza kuchakatwa kuwa sukari tusingeagiza sukari, hivyo, forex yetu tungeweza kuiokoa! Kwa nini hatuwekezi kwenye utengenezaji wa mitambo ya kuchakata sukari? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, TEMDO taasisi yetu ya Tanzania Engineering Manufacturing Development Organization wanatengeneza mitambo, wametengeneza mitambo, mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara wametengeneza mtambo wa kuchakata sukari ambao unaweza kusaidia wakulima wadogo wadogo wakikopeshwa na SIDO, SIDO kuna kitu wanaita NEDF wanakopeshwa wakawa wanatengeneza sukari hii miwa tutaiokoa. Kwa nini hatuwekezi sasa kwenye TEMDO?
Mheshimiwa Spika, kazi ya Mheshimiwa Bashe ni kulima, kazi ya Mheshimiwa Bashe siyo kuuza, kazi ya kuuza ni ya Mheshimiwa Dada yangu Dkt. Ashatu Kijaji, Wizara ya Viwanda na Biashara. Sasa najiuliza tunaweka bajeti kubwa kwenye kilimo lakini kwa nini hatuweki bajeti humu ya kutafuta masoko?
Mheshimiwa Spika, mimi ni Mwenyekiti ninakuambia TANTRADE hawana pesa watatafutaje masoko? Mheshimiwa Bashe atalima atauza wapi? Matokeo yake tutalima lakini mazao yataoza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana tubadilishe mtazamo wetu kwenye kilimo, ni kilimo peke yake kitaitoa nchi hii hapa ilipo kwenda mbele.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja tena. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyofanya kazi kubwa sana katika elimu ya Taifa hili. Mheshimiwa Rais alifanya jambo moja kubwa ambalo limemtengenezea heshima kubwa mno. Alichukuwa mkopo kwa ajili ya UVIKO (COVID 19) lakini akatumia fedha mkopo ule wa COVID 19 kujenga madarasa elfu 15 nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, that was the smart decision, katika Afrika hakuna kiongozi yeyote aliyechukuwa uamuzi wa namna ile. Alikuwa na uwezo wa kuamua anunue barakoa au anunue sanitizer lakini akaona jambo la maana sana kwa watu wake ni kujenga madarasa. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Buchosa namshukuru sana Mheshimiwa Rais na tumejenga madarasa 128, hivi ninavyozungumza watoto wanakaa kwenye madarasa mazuri yaliyotengenezwa vizuri. Ahsante sana Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Wabunge naomba tumuunge Rais wetu mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa kwa nini hampigi makofi ya kutosha kwa Mheshimiwa Rais. Nianze na kitu kinachoita form four certificate dilemma, dilemma ya cheti cha form four. Kabla sijakugusa cheti cha form four nisiache kumshukuru kwanza Profesa Mkenda kwa kazi kubwa ambayo ameanza nayo kwenye Wizara ya Elimu, Profesa namwamini sana, nilikuwa na mpango wa kushika shilingi lakini kwa mambo anayoyafanya sitashika shilingi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Naibu Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Kipanga, anazunguka Tanzania nzima kama pier kwenda kila wilaya kuangalia maendeleo ya elimu. Nampongeza sana Naibu Waziri kwa kazi nzuri. Nachukua nafasi hii pia kumpongeza sana Katibu Mkuu wa Wizara hii Profesa Eliamani Sedoyeka. Kwa kweli namfahamu Katibu Mkuu huyu tangu akiwa Chuo Cha Uhasibu Arusha kwa mambo aliyoyafanya pale Arusha. Aliingia Chuo Cha Uhasibu Arusha kikiwa kwenye hati ya kufungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, chuo hiki kilikuwa na wanafunzi kama sikosei 2,000, amekaa pale si zaidi ya miaka miwili, ameacha kina wanafunzi elfu 10 na kitu na tayari kina majengo ya ghorofa. Kwa hiyo naamini ujio wake kwenye Wizara ya Elimu, hatakubali hata siku moja kuharibu rekodi yake. Kwa hiyo rekodi yake iliyomsababisha akapewa Ukatibu Mkuu aendelee nayo na Watanzania wanufaike kwa kiasi kikubwa sana na umahiri wake. Niwashukuru Manaibu Makatibu Wakuu na pia niwashukuru watumishi wote wa Wizara ya Elimu, tuna kazi kubwa sana kwa ajili ya elimu ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumzie dilemma cheti cha form four. Wengi mnafahamu mimi sikupata nafasi ya kusoma elimu ya sekondari, lakini kwa neema ya Mwenyezi Mungu na kwa kipaji ambacho Mungu alinipa cha uandishi nilitathiminiwa na TCU nikakubaliwa kusoma Chuo Kikuu kwa mfumo uliokuwa unaitwa RPL Recognition of Prior Learning na nikamaliza Chuo Kikuu vizuri kabisa. Nilipotaka kufanya masters Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nikakataliwa nikaambiwa huna cheti cha form four na hayo ndio imekuwa vita yangu profesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshazungumza sana na Mheshimiwa Profesa na dada yangu Mheshimiwa Ndalichako anakumbuka vizuri sana kwa mapambano yangu mimi na yeye humu Bungeni, kwamba haiwezekani mtu nina shahada ya kwanza TCU wamenikubalia, halafu Chuo Kikuu wanakataa nisifanye masters kwa sababu sina cheti cha form four. Hii haiwezekani, wanawanyima watu haki ya elimu, kuna watu wengi nchi hii wamebuni vitu vingi, watu wametengeneza umeme bila elimu ya sekondari, wanajenga nyumba bila elimu ya sekondari, wanataka kusoma Chuo Kikuu wanakataliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Profesa Mkenda, aichukue kazi hii na kazi yangu hii aweze kulikamilisha jambo hili. Namwamini mno Mheshimiwa Profesa na tumeshazungumza mara nyingi sana kuhusu suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Profesa Ndekidemi anafahamu, kuna mtu mmoja kwenye Taifa hili lazima nimtolee mfano, alikuwa gardener kwenye chuo kimoja cha kilimo, akawa anatengeneza garden nzuri sana na kwa sababu hiyo Wazungu wakaona anafaa kusoma diploma, akapelekwa kusoma diploma, akamaliza best student kwa diploma kutunza gardener.
Mheshimiwa Naibu Spika, alipomaliza hiyo kozi ya gardener, wakasema aaa, umemaliza na distinction, basi distinction yako tunakupeleka kusoma Uingereza, akapelekwa Uingereza kusoma, from a gardener akaenda kufanya degree ya kwanza ya mambo ya kilimo na degree ile akarudi Tanzania baada ya miaka mitatu akarudi na masters, ndani ya miaka mitatu. Alipofika Tanzania, Tanzania yangu, nchi yangu, inayothamini cheti cha form four, alipotaka kufanya masters akaambiwa huwezi kufanya masters huna cheti cha form four.
Mheshimiwa Naibu Spika, huyu mtu yupo ukitaka nikuletee nakuletea na Profesa Ndekidemi yupo pale ni shahidi wangu. Yule mtu ikabidi aache kufundisha aende akasome QT Tanzania, Profesa Mkenda, akaenda kusoma QT miaka miwili, alipopata cheti cha form four ndiyo akafanya PhD na leo ni Profesa, the best professor in the country. Mimi binafsi siko tayari na nimesema sitashika shilingi, namwomba sana Waziri Profesa Mkenda hili jambo ni la kisheria, alete sheria Bungeni tubadilishe ili Watanzania wapate nafasi ya kusoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kengele ya kwanza kulia, sasa nitoe mchango wangu, nina mambo mawili tu. La kwanza medium of instruction, lugha ya kufundishia. Kwa muda mrefu sana nchi yangu imevutana tufundishe kwa Kiswahili, tufundishe kwa Kiingereza, mvutano huu mpaka lini?
Sasa ni wakati wa kufanya maamuzi, mwanangu anasoma darasa la kwanza kwa Kiswahili mpaka darasa la saba kwa Kiswahili. Akianza form one anaanza kwa Kiingereza. Ile transition ya kutoka Kiswahili kwenda kwenye Kiingereza tunapoteza watoto wengi wenye akili form one atakuwa anajifunza Kiingereza. Form two anajifunza Kiingereza form three kaanza kuelewa Kiingereza kidogo, mtihani wa form four umefika anapata division zero.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri na nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge kwa umoja wetu tuamueni tunataka tufundishe Kiingereza au Kiswahili.
WABUNGE FULANI: Kiingereza.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Kiingereza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili nisiliseme nimwombe Mheshimiwa Waziri, afanye utafiti aje na majibu ya watu wanataka tufundishe kwa lugha ipi, tuwe na lugha ya kufundishia ili tuwasaidie watoto wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala zima la mitaala ya elimu, limezungumzwa. Dunia inakwenda kwenye fourth industrial revolution, mapinduzi ya nne ya viwanda, lazima mitaala yetu ili-reflect kule tunakoelekea hatuwezi kuendelea kuwafundisha watoto wetu kwa mambo ya second industrial revolution kwa mambo ya third industrial revolution, hatuwezi kufanikiwa. Tutakapofika mapinduzi ya nne ya viwanda ambayo kutokana na mambo ya intelijensia ya bandia niseme hivyo, mambo ya five technology, cloud computing, lazima tuwaandae watoto wetu tuanze kuwafundisha kuanzia primary schools, kuna shida gani kumfundisha mwanangu coding akiwa primary school, kuna shida gani? Hatutaki kufanya maamuzi, matokeo yake shule za binafsi watoto wanaandaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotokea, huko mbele tunaandaa matabaka ya watu wawili; watoto wenu hapa watakuwa na nafasi kuliko watoto walioko vijijini, hatutaki Tanzania ya aina hiyo. Tunataka Tanzania yenye usawa, kwa hiyo naomba waache maandalizi mtaala huu, tufikirie sana kuwapa watoto wetu elimu ya computer toka Shule ya Msingi. Walimu tunao, hatuna sababu yeyote ile ya kutofanya jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ni suala la maslahi ya Walimu. Ukitaka kufanikiwa kwenye elimu mfurahishe Mwalimu, basi. Walimu lazima wawe na furaha katika nchi yetu, najua wananisikiliza, Walimu wanaouza visheti…
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Shigongo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mungu kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge hili nikiwa mtu wa kwanza kutoa mchango wangu kwa Taifa langu kuhusu idara hii ya afya.
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ninampongeza sana kwa niaba ya Watanzania kwa uamuzi wa kuongeza mishahara kwa asilimia 23.3. Nchi nzima imejaa shangwe kwa sababu ya jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi naomba nianze kwanza kwa kusema maneno yafuatayo: -
Mheshimiwa Spika, mwaka 2001 nchi za Afrika zilikutana kule Abuja-Nigeria na wakafikia uamuzi wa kwamba bajeti ya Taifa lolote la Afrika Marehemu Mzee Mkapa alikuwa pale ni lazima asilimia 15 ya bajeti ilielekezwe kwenye huduma za afya. Jambo hili halijaweza kutimia 2019 tulikuwa na asilimia Saba, Mwaka 2020 tulikuwa na asilimia 6.7 na ninavyotazama naona kama tunaendelea kushuka. Sasa mimi nilikuwa ninaushauri mmoja kabla sijaanza ni kwamba naomba Serikali yangu ifikirie kuongeza bajeti kwenye afya kwa sababu afya ya Mtanzania ni kitu cha muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la preventive medicine, suala la kuzuia magonjwa yasitokee, tumefanya kazi kubwa sana kama Taifa kutibu watu, tumefanya kazi kubwa sana kuwatibu watu wetu wanapougua lakini hatujawekeza kiasi kikubwa sana kwenye suala la kuzuia magonjwa yasitokee. Katika suala la kuzuia magonjwa yasitokee nitajikita moja kwa moja kwenye chanjo ya homa ya ini na homa ya ini yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 mimi na wenzangu katika Kampuni ya Global Publisher tuliamua kufanya kampeni nchi nzima kuwaelimisha watu kuhusiana na ugonjwa wa Homa ya Ini. Kilichotufanya tufanye kampeni ile ilikuwa ni data zilizokuwepo za Homa ya Ini zilitushtua, zilitutisha na tukaona kwamba ilikuwa sababu ya mimi na wenzangu kutoa mchango kwa nchi yetu ili kuweza kusaidia watu waweze kupata ufahamu.
Mheshimiwa Spika, wakati huo 2014 katika akina mama waliofanyiwa uchunguzi wa afya wajawazito asilimia tano ya akina mama wote walikuwa wanakutwa na Homa ya Ini. Damu iliyotolewa kwenye benki ya damu hapo Dar es Salaam na sehemu mbalimbali chupa 100 zilizochukuliwa chupa nne zilikutwa na homa ya ini na uwepo wa homa ya ini katika nchi ulikuwa ni asilimia tano data zile zilitutisha tukaanza kampeni ile, tumefanya kampeni kwa muda tu, wakati ule Waziri wa Afya alikuwa Rais wa Zanzibar sasa hivi Mheshimiwa Hussein Ally Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa Mheshimiwa Said Meck Sadiki, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa Dada yangu Grace Magembe na Meya wa Ilala alikuwa Mdogo wangu Mheshimiwa Jerry Silaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumefanya kampeni ile kwa muda mfupi nikaitwa nikaambiwa Eric kampeni yako ni nzuri lakini tunaomba uiache kwanza inasababisha hofu inaleta taharuki watu wanaogopa, tukakubali kuacha kampeni ile kwa shingo upande. Miaka nane baadaye nikiwa naongea leo naomba nikusomee data za homa ya ini nchini Tanzania. Kwa wajawazito 100 wanaopimwa leo kwenye antenatal clinic zetu asilimia Saba mpaka Nane wanakutwa na homa ya ini, imeongezeka. Benki ya damu wanapotoa damu watu 100 chupa sita zinakutwa na homa ya ini.
Mheshimiwa Spika, rate ya homa ya ini, uwepo wa homa ya ini kwenye Taifa letu sasa hivi ni asilimia mpaka 7.2 katika baadhi ya maeneo. Hii inatisha, hili siyo jambo la kukalia kimya, wala siyo jambo la kuacha kuliongelea.
Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa leo kuongea nikiamini ya kwamba tuna uwezo wa kuzuia ugonjwa huu, tuna uwezo wa kuokoa maisha ya watu wetu kwa sababu chanjo ipo na mimi nafahamu Waheshimiwa Wabunge humu ndani mnaonisikiliza wengi mmechanjwa kwa sababu chanjo ililetwa hapa hapa Bungeni, lakini huko nje watu wetu wanashindwa kuimudu hii chanjo, kwa bei ya Serikali ni Shilingi 10,000 kwa chanjo moja mtu anahitaji chanjo tatu na kabla hajachanjwa lazima afanyiwe rapid test kuona kama ameambukizwa au hapana Shilingi Elfu Arobaini, Elfu Arobaini ni nyingi kwa mwananchi wa kawaida. Wananchi wanauliza kama chanjo ya COVID tumechanjwa bure kwa nini chanjo ya homa ya ini tunaombwa pesa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wanakufa, maisha ya watu yanapotea, watu wengi wameambukizwa. Hapa ndani mnaonisikiliza kama haujafiwa, kama humjui mtu aliyekufa basi wewe mwenyewe jipeleleze. Ugonjwa huu unazidi kuenea, kasi ya kuenea ni mara 100 zaidi ya UKIMWI. Tuna sababu ya kuchukua hatua kuokoa maisha ya watu wetu. Tuna kila sababu ya kuchukua hatua kuokoa maisha ya watu wetu, watu wanakufa. Hatuwezi kunyamaza, hatuwezi kujifanya hatuoni, lazima tuchukue hatua tuokoe maisha ya watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuko hapa Bungeni Waheshimiwa Wabunge kwa ajili ya watu waliotuchagua. Tuko hapa Bungeni kama hatuwezi kutetea maisha ya watu wetu waishi hatuna sababu ya kuwa Wabunge. Najiuliza kila siku kwanini hatuchanji? Kuna mtu akaniambia nchi yetu ni maskini na hatuna uwezo. Nikakataa, nikamwambia ukiniambia nchi ni maskini niletee report ya CAG nitakuonesha fedha zinapotelea wapi. Mabilioni ya fedha yanapotea mikononi mwa watu wasiokuwa waaminifu. Tungeokoa fedha zetu kwenye report ya CAG katika nchi hii tungeweza kuwachanja watu wetu wote na chenji ikabaki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiachana na hilo, naomba niongee jambo moja la msingi sana na bahati nzuri wataalam wako hapa wananisikiliza. Umuhimu wa kumchanja mtu badala ya kumtibu ni jambo la maana mno. Kansa ya Ini, the Hepatocellular Carcinoma gharama ya kumtibu hapa Tanzania ni Shilingi Milioni 16 mtu mmoja. (Makofi)
SPIKA: Sekunde 30 malizia.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, sasa kama gharama ya kumtibu mtu mmoja hapa Tanzania ni Shilingi Milioni 15 mwenye Kansa ya Ini inayosababishwa na Homa ya Ini. Ni kwanini tusiwachanje watu kuokoa maisha yao? Fedha zipo, tuwachanjeni watu wetu tuweze kuokoa maisha yao. (Makofi)
SPIKA: Haya ahsante sana. Ahsante sana.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niamini kwamba tunachangia kwa dakika 10 na ninataka nizitumie dakika 10 hizi kwa kutoa mchango wangu kwa kifupi tu na ninaomba Wabunge mnisikilize kwa makini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 144 imetamka juu ya Security of Tenure. Security of tenure ya kwamba ziko nyadhifa katika taifa hili lazima watu walindwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitasoma kidogo Ibara ya 144(1); Bila kuathiri masharti mengine yaliyomo katika ibara hii, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Jamhuri ya Muungano atalazimika kuacha kazi yake atakapotimiza umri wa miaka sitini au umri mwingine wowote utakaotajwa na Sheria iliyotungwa na Bunge.
(2) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu aweza tu kuondolewa katika madaraka ya kazi yake kwa sababu ya kushindwa kutekeleza kazi zake (ama kutokana na maradhi au sababu nyingine yeyote).
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma ibara hii kuonyesha ya kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kwamba CAG awe protected na hiyo security of tenure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko katika vita dhidi ya rushwa kwenye Taifa letu. Mara ya mwisho niliposimama hapa nilisema kwamba watu wanaiba, wanaiba, wanaib. CAG ameleta ripoti tena hapa bado wizi unaendelea na unazidi kuongezeka. Sasa, kwa nini nimesimama kuzungumza, nimesimama hapa kwa sababu ya mtu mmoja ambaye ninamwona ni wa muhimu sana kwenye vita dhidi ya rushwa kwenye Taifa langu; mtu huyu ni Mkurugenzi wa TAKUKURU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkurugenzi wa TAKUKURU ambaye CAG akikamilisha kazi yake anamkabidhi mafaili yote anapata kibali cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anaenda kufungua kesi mahakamani kuwashitaki watu lakini hawi protected na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kazi yake ni kubwa anashughulika na watu wakubwa, watu wenye uwezo lakini hana protection yoyote kama mwenzake CAG.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza, kwamba jambo hili lilifanyika kwa bahati mbaya au lilifanyika kwa lengo gani? Kwamba yule anayechukua kazi kwa CAG na kupeleka mahakamani na kupata kibali cha mwendesha mashtaka na kushitaki watu hawi protected. Ukienda upande wa pili wa Tanzania Zanzibar iko protected, Kenya yuko protected, Sierra Leone yuko protected, analindwa. Naongea hapa kwa sababu ya confidence, mtu huyu anahitaji confidence, awe na uhakika wa kazi yake alindwe na sheria ili iweze kutimiza majukumu yake sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukatae tukubali wako watu kwa simu moja tu mambo yanaweza yakabadilika, ushahidi unaweza ukabadilishwa na vitu vikabadilika kabisa na kesi isifike hata mahakamani, kwa simu moja tu. Nitatoa mfano mmoja mfupi tu, Yesu alipokufa siku ya Ijumaa, Maria alipoenda kuomba mwili wake kwa Pilato, Pilato alikataa kutoa ule mwili. Mtu mmoja aitwaye Joseph Halimataya mtu mwenye nguvu na ushawishi, Maria alipoenda kwake kulia akamwambia twende, walipofika ofisini kwa Pilato akauliza mzee yupo akaambiwa yupo lakini ana mgeni, akasema ngoja nichungulie kidogo tu anione, alipofungua mlango hivi Pilato alivyomwona akasimama akamwambia karibu mzee, mgeni aliyekuwepo ndani akaambiwa subiri kwanza niongee na Joseph wewe usubiri. Kwa nini natoa huu mfano, wako watu wana nguvu, wako watu wana ushawishi, wanaweza kumpigia simu moja tu Mkurugenzi wa TAKUKURU na mambo yakabadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tumpe uhakika Mkurugenzi wa TAKUKURU ili afanye kazi zake kwa confidence, afanye kazi yake vizuri bila hofu ya kwamba nitafukuzwa kazi kesho, ukishamteua iwe kazi kumwondoa. Maana yangu ni nini, mimi mwenyewe hapa namkumbuka kaka yangu mmoja, sitaki kumtaja jina hapa, aliwahi kusema msinitilie kitumbua changu mchanga. Hata yeye Mkurugenzi wa TAKUKURU ana watoto, ana familia kuna mambo mengine anaweza akaacha kuyashughulikia kwa sababu tu anaogopa kazi yake inaweza ikapotea. Nani hataki heshima, nani hataki kutembea kwenye hiyo shangingi kila mtu anataka hata mimi nataka. Niko tayari ku-compromise wakati mwingine ili nibaki ofisini. Wako watu wamedhurika kwa sababu walishindwa kutekeleza maelekezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachokiomba wakati umefika wa sisi kufikiria sasa jinsi ya kum-protect Mkurugenzi wa TAKUKURU. Jambo hili si geni, Zanzibar inafanyika nimesema, Sierra Leone wanafanya na Kenya wanafanya kwa nini Tanzania hatuwezi kum-protect mtu huyu? Umem-protect CAG, anafanya vizuri, lakini Mkurugenzi wa TAKUKURU hana
protection.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapo niunge mkono hoja, ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kushukuru sana kwa microphone kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rasi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mema ambayo anaifanyia Taifa langu upande wa mawasiliano. Tanzania imeshuhudia maendeleo makubwa sana upande wa teknolojia kwenye kipindi hiki cha Awamu ya Sita. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu, rafiki yangu kwa kazi kubwa anayoifanya. Nakupongeza sana kwa sababu kumekuwa na uhuru mkubwa sana wa kujieleza kwenye kipindi cha Rais wa Awamu ya Sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii naisema niki-declare interest kwamba mimi ni mdau wa habari. Nimekuwepo Awamu ya Tano, na Awamu ya Nne nikifanya kazi ya habari. Kwa hiyo, ninaposema kwamba Awamu ya Sita tuna uhuru zaidi ya tulikotoka, iko sababu kubwa sana ya kumpongeza Mheshimiwa Rais na wewe Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana mdogo wangu Kundo kwa kufika mpaka jimboni kwangu na kujionea hali halisi ilivyo. Sasa wananchi wa Buchosa wamenituma. Buchosa ni jimbo kubwa, lina visiwa vingi sana. Watu wa visiwani hawana minara. Mawasiliano kwao ni magumu, na kuna wakati wanakuwa kwenye hatari ya kuzama, wanashindwa kuwasiliana. Kwa hiyo, naomba mwakumbuke sana watu wa visiwa vya Sosswa, Simbaya, na kwingineko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema maisha ya vyombo vya habari ni magumu. Media houses zina-suffer. Sasa ombi langu kabla sijaenda mbali ni kumwomba Mheshimiwa Waziri, msiwapatie ruzuku vyombo vya Habari. Ruzuku wapeni TSN, Uhuru na wengineo. Sisi tunachokitaka na wengine huko, vyombo vya habari vya Serikali vijitoe kwenye matangazo. Yaani ITV wasigombanie matangazo na TBC. BBC hawachukui matangazo, Voice of America hawachukui matangazo, vyombo vya Serikali, visigombanie matangazo na vyombo binafsi. Hiyo peke yake inatosha kuwasaidia vyombo vya habari viweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zetu za bajeti hapa zikienda kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya promotion na matangazo vyombo vitaweza kulipa wafanyakazi wake. Nami namshukuru sana dada yangu, Mheshimiwa Esther ameongea mambo mazuri kabisa hapa. Ahsante, Mungu akubariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, uongozi ni kutatua tatizo kabla halijatokea. Yaani uwe na uwezo wa kusema mwakani kutakuwa na njaa, kwa hiyo, unaweka chakula. Dunia imebadilika sana. Tanzania imebadilika sana. Mtu yeyote anaweza akashangaa kwamba zamani tulikuwa tunapiga picha; tunaweka filamu kwenye camera, lakini leo hii hamna. Tulikuwa tunatumia diskette, leo hii hazipo. Dunia inabadilika kwa kasi mno, lazima tubadilike nayo. Tusipobadilika sisi leo, utakuta tumechelewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaposimama hapa leo, nataka kusema hivi, huko tunakokwenda mambo yatabadilika. Sisi kama Taifa tufanye nini? Narudia yale yale ninayoyasema kila siku. Sisi kama Taifa tuelimishe watoto wetu, tuwekeze kwa kuelimisha watoto wetu. Katika hili, Mheshimiwa Waziri ni kweli wewe sio Wizara ya Elimu, lakini unashughulikia masuala ya TEHAMA. Naomba na ninasisitiza computer zisambazwe mashuleni, watoto wetu wafundishwe computer kuanzia primary schools ili matatizo yanayokuja huko mbele tuweze kukabiliana nayo. Tusipofanya jambo hilo, nataka niwahakikishie tutaachwa na hatutaweza kushindana na wenzetu kwenye ulimwengu unaokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aelewe kwamba suala la ubunifu na innovation ni jambo la muhimu sana. Wasaidie wabunifu wa Taifa hili. kuna vijana wengi sana wana ubunifu, nawe unawafahamu, lakini hawana mitaji, na wameshindwa kupiga hatua mbele. Benjamin Fernandes alianzisha mnara, kijana wa kitanzania, ameanzia hapa na matokeo yake amehamia nchi nyingine kwa sababu hapa nyumbani alikosa support.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna kijana anaitwa Magila Tech wote tunamfahamu, ame-invent mifumo mingi sana nyumbani. Ni kijana wa kitanzania, ana akili nyingi Mungu kamjalia, anafanya mambo mengi, lakini hapati support ya Serikali. Mabenki hayamtumii kutengeneza mifumo. Wanatoa kazi kwa mataifa ya nje, baadaye inaonekana kama mifumo waliyoiweka haifanyi kazi, wanamfuata Magila Tech huyo huyo aje atengeneze mfumo. Kwa hiyo, naomba tuwaelimishe sana watoto wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, na la umuhimu na la kusikitisha ni kwamba, Rais wetu alikwenda Dubai akakutana na Mwenyekiti wa Makampuni ya Airtel akaahidi yule tajiri ya kwamba ataisaidia Tanzania kwenye mambo ya technology. Mheshimiwa Waziri kama hujui sasa unisikilize vizuri. Yule bwana ameamuru kampuni yake iliyoko hapa itoe data bure kwenye shule za msingi na sekondari katika nchi hii ambapo thamani yake ni Dola 830,000, lakini eti TRA wamekataa kutoa exemption ya VAT pamoja excise duty. Are we serious?
MBUNGE FULANI: We are not. (Makofi)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashindwa kuelewa. Nakuomba Mheshimiwa Waziri kutana na Mheshimiwa Mkenda, kutana na Mheshimiwa Mwigulu mjadiliane suala hili. Baadaye mimi nitakamata shilingi yako kwenye hili. Hatuwezi kukubali tunapewa fedha zote hizi zisaidie walimu wetu tumewagawia vishikwambi huko vijijini, lakini hawana internet. Halafu mtu amekataa kutoa exemption ya VAT na excise duty.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili nitalisimamia na nitapambana na Waheshimiwa Wabunge naomba mniunge mkono nitakaposhika shilingi leo jioni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mengi ya kusema sana sina. Nakupongeza sana Waziri Nape na Makamu wako. Nakuamini sana na unajua. Nawe ni kijana mwenye akili, huwezi kushindwa kutatua matatizo yetu. Hakikisha kwamba Tanzania inakwenda mbele kiteknolojia. Jambo hilo linawezekana.
Mheshimiwa Spika, leo hii kwenye global innovation index, Tanzania ni ya 90 Duniani, Kenya ni ya 89, lakini Mauritius ni ya 35. Sisi tunashindwa nini? Akili tunazo, tutumieni akili zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nije kwenye suala la pongezi. Pongezi nyingi sana kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi aliyoionesha na dhamira ya dhati kabisa ya kuutangaza utalii wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara. Lakini kwa niaba ya wananchi wa Buchosa naomba nitoe shukrani sana kwa Wizara kwa kutujengea vizimba viwili kuzuia wananchi wetu wasiliwe na mamba.
Mheshimiwa Spika, hapa ndani leo imekuwa ni suala la ndovu kila kona, lakini napenda niwaongezee suala la mamba. Kule ninapotoka mimi wananchi, hasa akina mama, wanaliwa sana na mamba, na kimekuwa kilio changu sana kwenye Wizara. Ombi langu kwa Wizara ituongezee vizimba vingine vya kuzuia watu wasiliwe na mamba hasa maeneo ya kuchota maji na maeneo ambayo watu wetu wengi wanakwenda kuoga nyakati za jioni. Hayo ndiyo mambo ambayo wananchi wa Buchosa wamenituma.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni maeneo ya hifadhi. Tunacho Kisiwa cha Maisome ambacho wananchi walikuwepo baadaye tukaja kupima eneo tukasema hii ni hifadhi, idadi ya watu imeongezeka, wananchi wanaomba kukatiwa kipande kidogo kwenye eneo la hifadhi ili waweze kupata maeneo ya kufuga mifugo yao na hata maeneo ya kuishi.
Mheshimiwa Spika, vivyo hivyo kwenye Kisiwa cha Kome, na kwenyewe kuna tatizo hilo. Wananchi wanalalamika eneo la hifadhi lipo, idadi ya watu imeongezeka lakini hawana sehemu ya kujenga na pia kulisha mifugo yao. Kwa hiyo kila siku ng’ombe wanakamatwa wanapigwa faini 100,000 kwa ng’ombe, kwa hiyo naiomba Serikali hii sikivu, Mheshimiwa Waziri tulishazungumza, nikuombe sana suala hili uzingatie na ninakukaribisha Buchosa uje ujionee mwenyewe, umeniahidi kuja wananchi wanasikia, nakukaribisha sana Buchosa uje ujionee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la Wizara hii ni suala la biashara kabisa asilimia 100. Uhifadhi, lakini tunawezaje kupata fedha kutoka kwenye uhifadhi, tunawezaje kugeuza Hifadhi zetu za Serengeti, Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, wanyama kama tembo, simba waweze kuwa fedha. Hilo ndilo jambo ninalotamani kuliona. Nataka kuona fedha katika nchi hii ili ziweze kusaidia juhudi za maendeleo kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nimefanya utafiti kidogo na nimegundua kabisa ya kwamba kila unapo-double juhudi za kutangaza biashara ya utalii mapato yanaongezeka. Sasa, nimesoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri nikakutana na maandishi yanasema kama ifuatavyo: -
“Bila kutangaza sana bado tumeweza kufikia kiasi cha pato la Taifa asilimia 21 kutokana na utalii.” Bila kutangaza sana, bila promotion hii ni bahati kubwa sana, haitokei mahali popote duniani, yaani kwenye ulimwengu huu tulio nao wa leo unasema bila kutangaza sana tumefanikiwa. Tafsiri yake ni nini? Tafsiri yake ni kwamba kama Waziri angetangaza sana, mapato yangeweza kuongezeka na hicho ndio kimenisimamisha hapa kuongea leo.
Mheshimiwa Spika, ni kwamba siridhishwi kabisa na investment iliyofanyika kwenye suala zima la kutangaza utalii wetu. Tanzania katika dunia ni Nchi ya pili kwa vivutio vya asili ikiongozwa na Brazil. Tanzania ni Nchi ya kwanza Afrika kwa vivutio vya kiasili, nchi ya kwanza lakini angalia mapato yake. Mapato yake ni kidogo sana. Kama Taifa tunaweza kusema bado GDP ratio inaturuhusu kukopa. Tuna asilimia 40 tu, wenzetu wana asilimia 77, lakini je, tutegemee mikopo kila mara na utajiri huu tulionao? Ningetamani siku moja nchi yangu isikope, iweze kutumia zawadi ambazo Mungu ametupa kuendesha nchi yetu na inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikusomee data moja hapa, data moja rahisi tu. Baraza la Utalii Duniani (WTTC) mwaka 2019 lilisema maneno yafuatayo, Idara ya Utalii Tanzania iliingiza dola bilioni 6.7 mwaka 2019, bila kutangaza tunaingiza fedha hizi tuki-double itakuwa bilioni 13. Fedha hizo ukizijumlisha kwa ujumla wake ni trilioni 16. Shilingi trilioni 16 hiyo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, namalizia. Shilingi trilioni 16 hiyo deficit kwenye bajeti yetu sisi ni shilingi trilioni 10 ingeweza kuziba debt…tusikope. Ombi langu juhudi za kutangaza ziongezeke, tusiridhike na mambo ya bila kutangaza tumefanikiwa.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 4) ACT, 2021
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nianze kwa kumshukuru Mungu kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge hili kuzungumza suala la marekebisho haya ya sheria.
Mheshimiwa Spika, nitoe shukrani nyingi sana kwa Kamati kwa kutambua jambo ambalo nilizungumza wakati wa bajeti ya Wizara ya Elimu, suala la RPL (Recognition of Prior Learning) nimelikuta na limejadiliwa. Napongeza sana Kamati nzima, Mwenyekiti na Wajumbe wote kwa kutambua jambo hili. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri dada yangu Ndalichako hatimaye kuona kuna umuhimu wa kuanza kuliona jambo la RPL kama ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, sina mambo mengi sana ya kusema zaidi ya pongezi hizo. Isipokuwa, ukienda kwenye ukurasa wa 12 pameandikwa amendment of Section 2(31) naomba niisome, inasema “The principal Act is amended in Section 2 by inserting in their appropriate alphabetical order the following new definitions. Recognition of Prior learning means the process of evaluating skills and knowledge acquired outside the classroom for the purpose of recognizing competence against a given set of standards, competence or learning outcome”.
Mheshimiwa Spika, jambo hili nililizungumza wakati ule, wakati wa bajeti na nakumbuka kama nilishikilia shilingi ya Mheshimiwa Waziri. Wako watu katika Taifa hili ambao aidha kwa vipaji au kwa practical experience wameweza kufanya mambo makubwa sana. Nitatoa mfano wa mtu mmoja kule Iringa alifanikiwa kuzalisha umeme na kusambaza kwenye kijiji chake bila elimu formal, bila kupita darasani. Nakumbuka aliitwa Ikulu wakati ule na Hayati na kuzawadiwa.
Mheshimiwa Spika, lakini nitoe mfano wa mtoto mmoja hapa wa kidato cha nne ambaye ametengeneza bulb yake ambayo ameweza kuiamuru kwa maneno ikazima au kuwaka. Hapa ndani ya Bunge lako tukufu wako watu ambao wanaweza kukutajia mpaka mifano, hawana hiyo elimu kubwa lakini wanafanya mambo makubwa sana.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Mheshimiwa Kibajaji kwa uwezo wake wa ku-present mada hapa Bungeni angeweza kusomea public speaking na akatambuliwa na akasoma na akapata shahada kabisa ya mawasiliano ya Umma bila shida yoyote kwa uwezo tu wa kuzungumza alionao.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jumanne Kishimba kwa namna alivyofanya toka zero mpaka ku-own companies na elimu yake ya darasa la saba angeweza kabisa kwa utaratibu huu kuruhusiwa kusoma hata business administration.
Mheshimiwa Spika, wewe ni Mgogo unamkumbuka Ukwe Zawose. Ukwe Zawose alikuwa ni kipofu mtaalam wa kupiga ngoma lakini alikwenda Finland akapiga ngoma kwenye chuo kikuu kimoja kwa sababu ya utaalam wake wa kupiga ngoma wakamu-award PHD. Kwa hiyo, ninapoona mambo haya yanaanza kutambuliwa naanza kuona sasa tunaanza kuelekea mahali pazuri kielimu kwenye Taifa langu. Nataka nchi yangu isifunge ilango kwa watu ambao hawakupita kwenye formal education kuweza kupata elimu ya juu. Hiyo ndiyo hoja yangu na hilo ndiyo jambo ambalo nimeliongelea sana kwamba ninapozungumza hapa simaanishi ku-challenge legal framework. Isipokuwa namaanisha kufungua milango kama ulivyofunguliwa kwangu.
Mheshimiwa Spika, ushuhuda wangu sitaki kuurudia tena leo wote mnaufahamu nilishauzungumza Bungeni hapa. Elimu yangu ya darasa la saba kwa kipaji cha kuandika nikapelekwa Chuo Kikuu nikafauli na nikamaliza. Nilipokwenda University of Dar es Salaam ku-apply for masters nikakataliwa kwa sababu sina cheti cha form four. Sasa hii form four hii ndiyo ninayoiongelea leo. Lakini nimeenda Open University nimekuwa accepted, sasa hivi nafanya Masters ya Mass Communication hawajaniuliza cheti cha form four.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa kipengele hiki nilichokisoma kimetambua kwamba wako watu wenye elimu ya vitendo lakini hawama elimu formal…
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, nimalizie kidogo tu. Ukienda kwenye sehemu ya 35 hapa mwisho nilikuwa na mapendekezo ambayo baadaye…
SPIKA: 31…
MHE. ERIC J. SHIGONGO: …31 hapo nilikuwa nasoma lakini ukija 35 amendment Section 24 ukienda hapo kuna kipengele M. Ningependekeza, wameandika hivi “prescribing procedures for recognition of prior learning and…” hapo ningeomba tuongeze kipengele ambacho kinamtaka mtu ambaye ametambuliwa na aidha TCU au NACTE akasome popote pale bila kuuliza cheti cha Form Four. Ndiyo hoja yangu. Naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru sana kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu mchana huu wa leo. Hoja yangu kubwa itakuwa kwenye suala zima la Transfer Pricing. Jana suala hili limenifanya sikulala vizuri usiku. Nimelala natafakari, nafikiria namna ambavyo nchi yangu inaibiwa fedha nyingi na wajanja wachache.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilifanya utafiti kidogo, kwanza nilitaka nijielimishe hivi hawa watu wanatuibiaje? Nikaja kugundua kwamba hawa watu wanatuibia kwa namna mbili, kama ambavyo ametangulia kuzungumza Mheshimiwa Yahya ni kwamba kampuni inakuwepo hapa Tanzania labda ni Geita kunakuwa na kampuni nyingine Dubai na kampuni nyingine Mauritius. Kwa mfano kama ni dhahabu inayochimbwa na Shigongo ambayo ni kampuni iko Tanzania anamuuzia aliyeko Dubai, ili kuikosesha Tanzania mapato anauza kwa bei ya chini, badala ya Sh.100/= anauza kwa Sh.10/= ili awaoneshe kwamba aliuza kwa hasara. Anapotaka kununua spare parts zake ananunua kwa kampuni yake nyingine iko Mauritius inamuuzia spare parts kwa bei ya juu ili kusudi aonekane gharama zake za uendeshaji zilikuwa kubwa aoneshe hasara ili Serikali isiweze kupata kodi. Huu ni wizi na wizi wa namna hii hauwezi kuvumiliwa, nchi yetu haiwezi kuendelea kupoteza mapato. Wenzetu wazungu wanaandaa utaratibu huu kwa nia moja tu ya kuziibia nchi za Afrika ziendelee kuwa masikini nao waendelee kujitajirisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taifa hatuwezi kuruhusu mambo haya yaendelee na nataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa sheria ambayo ameileta hapa Bungeni. Ameleta hapa kipengele ambacho kinataka kufanya adjustment kidogo kwenye sheria yetu. Kinasema kwamba tukishamkamata huyu mtu katuibia asilimia 30 yetu kama kodi atulipe, akishatulipa asilimia 30 tumpige asilimia 100 kwenye zote alizokuwa ametuibia. Sasa hatuwezi kuondoa 100 ambayo ni fine kwa lengo tu la kuwaita eti waje kuwekeza nyumbani kwetu, hawa sio wawekezaji hawa ni wezi; hawa ni wezi hatuwataki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kimoja ambacho najua kimempa changamoto Mheshimiwa Waziri ni kwamba wakati anatakiwa kuwabana wawekezaji wakati huohuo anatakiwa aboreshe mazingira wawekezaji waje, kwa hiyo, amejikuta yupo njia panda. Akaja na solution ya kwamba kwa sababu niko njia panda nifanyeje wawekezaji waje ili niweze kupata kodi, uchumi wetu unakua kwa asilimia 4.5 kwa sasa, akajikuta anasema nipunguze angalau tutoke asilimia 100 ya penalty iwe asilimia 75. Mimi nakubaliana na asilimia 75 ambayo Mheshimiwa Waziri ameona inafaa na naomba kabisa kama lengo ni ku-attract investors tuwapige asilimia 75 na wakati uleule tuwapige asilimia 30 ya kodi waliyokuwa wanatuibia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba Kitengo chetu cha International Tax Unit cha TRA hakina uwezo wa kuwakagua wafanyabiashara wote. Hakina uwezo wa kuzikagua hizi multinational zote zilizoko hapa nchini, hakina uwezo, kina wafanyakazi 18 tu mpaka ninavyozungumza hivi sasa. Wafanyakazi 18 hawana uwezo wa kukagua kampuni zote hizi.
Ombi langu mimi kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba waki-strengthen Kitengo hiki kiwe na nguvu, wafanye capacity building ya kutosha watu hawa wawe na uwezo wa kukagua kampuni zote zilizoko hapa nchini ambazo ni multinational ili tuweze kugundua matatizo yote ambayo yanafanyika na wizi wote ambao unatokea. Tukishawakamata hatuna huruma, ni kodi yetu asilimia 30 na asilimia 75 yetu tuwatoze. Watakaotaka kufanya biashara wafanye ambao hawataki kufanya biashara na sisi waondoke. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nikukumbushe jambo moja la muhimu sana ya kwamba viwanda vyetu vya alizeti vya kukamua mafuta vikumbukwe. Viwanda vikubwa vinapata zero eighteen percent ya VAT, viwanda vidogovidogo vinapigwa asilimia 18. Naomba Mheshimiwa Waziri awakumbuke wafanyabiashara wadogowadogo wenye viwanda hivi nao pia waweze kupatiwa zero eighteen percent nao waweze kufaidi soko letu la alizeti hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushukuru sana na baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote wa Mwaka 2022
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kulitendea mema Taifa lake. Mara kadhaa nimezungumza, na leo tena nitasema na nitarudia kusema kila siku, we have the most intelligent, most smart President in Africa. Kwa hiyo, nimesimama hapa kukushukuru wewe pia kwa namna unavyoliongoza Bunge letu Tukufu, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa namna tunavyofanya kazi yetu kwa uadilifu wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli tunaisimamia Serikali yetu vizuri sana. Mtakumbuka tulifanya kazi nzuri sana kwenye Mkataba wa DP World, tumefanya vizuri sana kwenye mkataba huu pia, tuendelee kulitumikia vizuri Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka mmoja uliopita nilimtembelea mtu mmoja amekaa hapa nyuma ofisini kwake, na hii ilikuja baada ya kuuguliwa na mama yangu. Nikampeleka hospitali moja pale Dar es Salaam, sitaki kuitaja jina, akapimwa kipimo kinaitwa MRI, baadaye tukapewa referral ya kwenda Muhimbili. Tulivyofika Muhimbili, akapimwa kipimo kile kile tena kwa sababu hawakuweza kupata majibu ya hospitali tuliyotoka. Kwa hiyo, ikawa vipimo mara mbili.
Mheshimiwa Spika, hiyo inaitwa duplication of care. Kwa sababu hiyo NHIF ikalazimika kulipa mara mbili kwenye kipimo hicho hicho kimoja. Nilipotoka hapo, nilimfuata huyo mtu ofisini kwake, yupo hapa nyuma ananisikiliza. Nikapata muda wa kujadiliana naye ofisini kwake. Nikamwambia, ninauona Mfuko wa Bima ya Afya unakwenda kufa kwa sababu ya matibabu kufanyika mara mbili mbili. Tulizungumza pale akanipa document moja nikaenda kuisoma, ilikuwa ni ya actuarial study iliyofanyika na ILO, ikiwa inatabiri kwamba Bima ya Afya ingeendelea hivyo 2026 ingekufa. Sikuwa tayari ife, nikaanza safari ya kutaka kuuokoa huu mfuko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mara kadhaa nimekutana na Mheshimiwa Waziri, nikamwambia ipo sababu ya kufanya kila tunachoweza kuuokoa mfuko huu kwani unasaidia Watanzania maskini. Mheshimiwa Waziri ni shahidi. Sasa katika hilo, naunga mkono kabisa sheria hii ipite, kabisa asilimia mia moja. Sina cha kusema marekebisho yamefanyika, nimeridhika kwa niaba ya wananchi wa Buchosa, sheria hii ipite. Hata hivyo nina mabo matatu ya kutoa angalizo.
Mheshimiwa Spika, la kwanza, ni mifumo. Mifumo haisomani. Hospitali moja hadi nyingine unarudia vipimo. Muhimbili pale pale, ndani ya Muhimbili kuna MNH na kuna MOI. Ukitoka MNH kwenda MOI mifumo haisomani. Hii inasababisha NHIF iingie hasara kubwa sana kwa kuwa na matibabu mara mbili mbili. Ikiendelea hivi, hata tukibadilisha sheria itakuja kufa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba mfumo wa kuendesha NHIF uboreshwe uwe ni mfumo unaosomana. Mheshimiwa Waziri ni shahidi, nilitafuta mpaka wawekezaji kutoka Marekani nikamletea ofisini kwake, wakakaa kikao, wakajadiliana wakakubaliana kwamba mfumo unaotumika unaitwa Electronic Medical Record ambao kila hospitali una mfumo wake. Ili tufanye vizuri tunahitaji mfumo unaoitwa Electronic Health Record System ambao unakusanya zile IMR zote pamoja zinakuwa zinasomana. Mgonjwa akitoka Buchosa leo akifika hapa, majibu ni kuyaita tu yanakuja na mnayaona. Kwa kufanya hivyo, tutaokoa fedha nyingi sana na mfuko wetu hautakuwa na hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hilo ni la kwanza. La pili, ni wizi (fraud), sina kumbukumbu vizuri kama kuna mfuko mwingine katika nchi hii unaibiwa kama NHIF, sina kumbukumbu. Ukweli ni kwamba kuna watu wamekuwa mabilionea kwenye Taifa hili kwa sababu ya NHIF, ninyi ni mashahidi. Lazima tupitishe sheria kifanyike kila kinachowezekana Mheshimiwa Waziri na wanao nisikiliza huku nyuma, kudhibiti fraud. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikupe mfano mmoja hai, huwezi kuamini. Kadi ya Bima ya Afya sikuhizi ni pesa. Mtu anaweza akaenda nayo mahali, akamwambia mwenye hospitali nipatie Shilingi 30,000/= hapo nikanunue chakula. Akampa Shilingi 30,000/=, aka-sign document akaondoka. Huku nyuma daktari anajaza anachotaka. Wanajua. Wiki iliyopita nimemkamata mtu Songea anafanya kitu cha namna hiyo hiyo. That for, hata kama tunapitisha sheria, lazima tu-control fraud. Tofauti na hapo, mfuko huu niliwahi kusema ulikuwa ICU wakati fulani, watu wakakasirika. Tofauti na hapo, utarudi ICU tena, sheria hii tuliyoileta inautoa mfuko huu ICU unauleta HDU, wodi ya kawaida. Baadaye itakwenda wodi ya kawaida atapata discharge, lakini kama hatuwezi ku-control fraud kwa vyovyote vile itakufa tena. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la mwisho, nimesikiliza sana na nimeusoma Muswada huu, nahitaji kuona tunawekeza sana kwenye preventive medicine. Tuzuie watu wetu wasiugue. Badala ya kusema watu wauguwe tutawatibu, hatuna uwezo wa kuwatibu. Huko nyuma nilisema, narudia tena leo, ipo siku mtanielewa. Tufanye kila kinachowezekana kuzuia watu wetu wasiugue. Sisi tumejielekeza kwenye kutibu.
Mheshimiwa Spika, hapa tutakuja kusema aah, bajeti yetu ya dawa imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 200 mpaka 700, siyo sifa. Sifa iwe ni kupunguza watu wasiugue. Ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana dada yangu, wekeza kwenye kuzuia watu wasiugue. Kuna shida gani NHIF wakichukua sehemu ya fedha zao, asilimia mbili, asilimia moja, wakaanzisha hata open gyms za bure watu wakawa wanafanya mazoezi? Wawekeze kwenye elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kinachotuua leo ni magonjwa ya mitindo ya maisha (life style diseases). Kisukari kimeongezeka nchi hii; watoto wa miaka miwili wanaugua kisukari, ilikuwa siyo jambo la kawaida zamani, lakini leo hii life style diseases zinatumaliza. Nataka Serikali yangu sikivu, Serikali hii ni sikivu sana, iwekeze fedha ya kutosha kwenye kuzuia magonjwa yasitokee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wanakufa na magonjwa ambayo tungeweza kuyazuia yasitokee. Kama tukifanya kampeni kubwa kabisa nchi hii, kama tulivyofanya kwenye sensa dhidi ya magonjwa haya, watu wataelewa na watu watakuwa salama. Zamani wakati mimi nakua, mtakumbuka wazee wenzangu mliopo hapa, ilikuwa ukifungua redio unasikia “kuleni chakula bora, mboga Samaki…” Mnakumbuka hizo nyimbo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, redio zilikuwa zinatangaza kuhimiza watu wale chakula bora na pa kulala pawe safi. Leo hii ukifungua redio unachokisikia Nyama Choma Festival ukifungua tena upande mwingine, watu wanahimizwa kunywa, starehe bila mazoezi. Lazima sehemu ya fedha zinazopatikana zipelekwe kwenye kuzuia magonjwa yasitokee. Magonjwa ya Afrika ni biashara ya viwanda vya madawa duniani. Wanataka tuendelee kuugua, tuendelee kununua madawa. Hatuwezi kukubali, ndiyo maana tuna kiwanda chetu pale Kibaha cha kuzuia Malaria kile cha viuadudu. Cuba hawana Malaria kwa sababu ya kiwanda hicho hicho, lakini kimekuja nyumbani hapa kinatengeneza dawa lakini dawa hizo hatuzinunui sisi wenyewe kuzuia watu wetu wasiugue Malaria. inasikitisha. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono sheria ipite, lakini maangalizo haya niliyoyasema yazingatiwe.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine natoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa namna anavyolitumikia Taifa lake. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, tukitoka hapa, twende kwenye majimbo yetu, (alizungumza Mheshimiwa Dkt. Mnzava asubuhi) tukatangaze mema ya Rais wetu, tukazungumzie huu mfuko wa huduma ya afya na mambo mengine.
Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kusema, ahsante kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. Mungu akubariki sana. (Makofi)