Primary Questions from Hon. Eric James Shigongo (12 total)
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza:-
Je ni lini Serikali itaacha kuwatoza shilingi 600 wakati wa kuingia na kutoka Bandarini wananchi wa Visiwa vya Kasalazi, Yozu, Gembela na Soswa katika Jimbo la Buchosa kwa kisingizio cha uwekezaji?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kiwango cha tozo ya abiria wanaopita katika bandari ndogo zilizopo katika maeneo mbalimbali ya mwambao wa bahari na maziwa ni shilingi 600 kama ambavyo imeainishwa katika kitabu cha tozo cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA). Hata hivyo, TPA baada ya kupokea malalamiko ya wadau mbalimbali kuhusu tozo hizo, imeanza kuchukua hatua za kufanya marejeo ya tozo hizo kwa bandari zote ndogo nchini kwa kushirikisha wadau katika maeneo mbalimbali. Vikao vya wadau ikiwemo wananchi katika Visiwa vya Kasalazi, Yozu, Gembela na Soswa vitafanyika kwa lengo la kupokea maoni yao kabla ya kuidhinishwa kwa tozo mpya. Ahsante.
MHE. TUNZA I. MALAPO K.n.y. MHE. ERIC J. SHIGONGO Aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itarejesha Mamlaka kwa Madiwani ya kuzisimamia halmashauri zao pamoja na kuwaazimia Wakurugenzi wa Halmashauri pale linapotokea tatizo kwenye halmashauri husika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo, Mbunge wa Jimbo la Buchosa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mamlaka za ajira na nidhamu kwa Watumishi wa Halmashauri hutofautiana kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 8 ya mwaka 2002 na Kanuni zake za mwaka 2003. Kwa mujibu wa Sheria hii Mamlaka ya nidhamu ya Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji ni Katibu Mkuu Kiongozi na Mamlaka ya nidhamu ya Wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa, Miji na Wilaya ni Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, halmashauri kupitia Baraza la Madiwani imepewa Mamlaka ya kusimamia nidhamu ya watumishi wengine wote wa halmashauri wakiwemo Wakuu wa Idara kwa kuzingatia kifungu cha 6 (6) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 8 ya mwaka 2002 na Kanuni zake za Mwaka 2003.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia Sheria hizo Waheshimiwa Madiwani hawana Mamlaka ya kuwawajibisha Wakurugenzi, ikitokea tatizo katika utendaji wa Mkurugenzi wa Halmashauri wanapaswa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika. Ahsante.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Barabara ya Sengerema – Nyamazugo – Nyehunge na Nkome kwa kiwango cha lami ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa Kampeni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu Swali la Mheshimiwa Erick James Shigongo, Mbunge wa Buchosa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ipo katika hatua za Manunuzi ya kumpata Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Sengerema – Nyamazugo – Nyehunge yenye urefu wa kilometa 54.4. Zabuni zilifunguliwa mnamo tarehe 30 Agosti, 2022. Uchambuzi wa zabuni unaendelea na mkataba wa kazi za ujenzi unatarajiwa kuwa umesainiwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba, 2022.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itazuia Mamba wanaoua watu na kujenga uzio wa nondo maeneo ambayo watu huchota maji Jimboni Buchosa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo Mbunge wa Jimbo la Buchosa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na matukio mbalimbali ya wanyama wakali kujeruhi au kusababisha vifo vya watu pembezoni mwa maeneo yenye maziwa, mito na mabwawa hususani mamba. Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Migongano baina ya Binadamu na Wanyama wakali na waharibifu. Aidha, kuanzia kipindi cha Julai, 2021 hadi Aprili, 2022 jumla ya mamba wawili wamevunwa katika Kata ya Maisome Wilayani Buchosa. Vilevile, katika kipindi tajwa watu 992 wamepewa elimu kuhusu namna ya kuepuka madhara ya wanyama wakali na waharibifu. Hadi sasa kikosi cha Askari wa Uhifadhi watatu wapo uwandani wanaendelea na doria za kudhibiti mamba katika Wilaya ya Buchosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazishauri Mamlaka ya Serikali za Mtaa (Halmashauri) kuandaa mpango madhubuti wa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vizimba na Wizara ya Maliasili na Utalii itatoa wataalam.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA K.n.y. MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga chuo cha VETA Wilaya ya Buchosa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila mkoa na wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Tayari Serikali imeshakamilisha kuandaa michoro na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Sengerema eneo lililotengwa kujengwa Chuo cha Ufundi Stadi ni katika Kijiji cha Kayenze Kata ya Nyehunge na tayari kiasi cha shilingi million 45 kimetolewa mwezi Machi, 2023 kwa ajili ya shughuli za awali za ujenzi wa chuo hicho, nashukuru.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -
Je, lini vifaatiba vya Hospitali ya Wilaya ya Buchosa vitanunuliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo, Mbunge wa Jimbo la Buchosa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2020/2021 ilipeleka Bohari Kuu ya Dawa fedha shilingi bilioni 34 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba kwa hospitali za halmashauri 67 zilizoanza ujenzi mwaka wa fedha 2019/2020 ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Buchosa ambapo kila hospitali ilitengewa shilingi milioni 500.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023 Hospitali ya Wilaya ya Buchosa imepokea fedha za ruzuku kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba shilingi milioni 800 pamoja na vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 596.
Mheshimiwa Spika, taratibu za kusimika vifaatiba vilivyopokelewa unaendelea kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Buchosa. X–Ray mashine tayari imefungwa tangu mwezi Aprili 2023. Tunsubiri wataalamu wa mionzi kutoka Tume ya Nguvu za Atomic Tanzania kukagua na kutoa kibali ili utoaji wa huduma uweze kuanza.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Zahanati ya Maisome kuwa Kituo cha Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo, Mbunge wa Jimbo la Buchosa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa miongozo ukubwa wa eneo la kituo cha afya linatakiwa kuwa na angalau ekari nne katika maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Spika, Serikali haikuipandisha hadhi Zahanati ya Maisome iliyopo Kijiji cha Kanoni kuwa Kituo cha Afya kwa sababu ya kukosa eneo la ujenzi. Aidha, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 imepeleka shilingi milioni 500 kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya kwenye Kata ya Maisome, Kijiji cha Kanoni. Ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje na jengo la maabara upo katika hatua ya ukamilishaji na ujenzi wa majengo ya wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la kufulia na kichomea taka upo hatua ya awali, ahsante.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha uchimbaji wa visima vya maji vilivyoanza kuchimbwa katika Jimbo la Buchosa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo, Mbunge wa Jimbo la Buchosa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa 2023/2024 Serikali inaendelea na zoezi la utafiti wa maji chini ya ardhi pamoja na uchimbaji wa visima 13 katika Jimbo la Buchosa Wilayani Sengerema. Hadi sasa jumla ya visima sita vimechimbwa, ambapo kati ya visima hivyo tulivyopata maji ni visima vinne vilivyochimbwa katika vijiji vya Bulolo, Nyonga, Bulyahilu na Izindabo. Aidha, kazi ya utafiti wa maji ardhini na uchimbaji wa visima inaendelea katika Vijiji vya Kisaba, Busikimbi, Kasalaji, Nyamiswi, Luharanyonga, Irenza na Bugoro ambapo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -
Je, lini Serikali itawamegea eneo Wananchi wa Visiwa vya Maisome katika Hifadhi ya Kisiwa cha Maisome?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mhehimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eric James Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo: -
Mhehimiwa Mwenyekiti, katika kutatua changamoto ya mwingiliano wa shughuli za uhifadhi na zile za kibinadamu, Serikali iliwasilisha taarifa ya umuhimu wa kumega hifadhi hiyo kama sehemu ya utatuzi wa migogoro ya Vijiji 975. Katika maelekezo ya Baraza la Mawaziri; Baraza liliridhia hifadhi imegwe na vijiji kupatiwa maeneo ya kuendeshea shughuli zao kwa uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshachukua hatua katika kutekeleza maelekezo ya Baraza la Mawaziri kwa kufanya mapitio ya mpaka wa msitu wa Hifadhi ya Maisome ambapo hekta 2,943.8 zimetolewa kwa wananchi na eneo hilo na kubakiwa na hekta 9,319.2. Kwa sasa taratibu za kubadili mpaka kisheria na kupata ramani mpya zinaendelea. Mara zoezi hilo litakapokamilika, Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi watajulishwa ambapo watakuwa na muda wa siku 90 kutoa maoni yao kabla ya tangazo rasmi la kutangaza eneo jipya la hifadhi baada ya mabadiliko niliyoyasema hapo juu.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itarejesha utaratibu wa Recognition of Prior Learning?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeandaa Mwongozo wa Kutathmini na Kutambua Maarifa yaliyopatikana Nje ya Mfumo Rasmi (Recognition of Prior Learning). Mwongozo unaweka utaratibu wa utambuzi na urasimishaji wa maarifa yaliyopatikana nje ya mfumo wa shule katika fani mbalimbali za amali kwa lengo la kuwawezesha walengwa kushiriki kikamilifu katika ulimwengu wa kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelekezo ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la mwaka 2023 mfumo wa kutambua na kurasimisha ujuzi na stadi zinazopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo umepewa kipaumbele. Serikali itatekeleza afua za kuimarisha utaratibu wa utambuzi na urasimishaji wa maarifa, ujuzi na stadi zinazopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo. Aidha, elimu nje ya mfumo rasmi itatambuliwa na watakaopitia mfumo huo watakuwa na fursa ya kujiunga na mfumo rasmi wa elimu kulingana na vigezo vitakavyowekwa, nakushukuru.
MHE. ERIC J. SHIGONGO aliuliza:-
Je, lini Serikali itatimiza ahadi ya kuwakatia eneo la Hifadhi Wananchi wa Kisiwa cha Maisome kwa kuwa idadi ya wakazi imeongezeka?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Msitu wa Maisome ilianzishwa mwaka 1955 kupitia Tangazo la Serikali Na. 355, ikiwa na ukubwa wa hekta 12,191.02. Kufuatia wananchi wa Kisiwa cha Maisome wanaoishi ndani ya hifadhi kuwa na uhitaji wa eneo, kwa ajili ya matumizi kwa shughuli mbalimbali za kijamii, Kisiwa cha Maisome kiliingizwa kuwa sehemu ya utatuzi wa migogoro ya vijiji 975 ambapo Baraza la Mawaziri liliridhia jumla ya hekta 2,871.782 zimegwe kutoka kwenye hekta 12,191.02 za eneo la hifadhi na hivyo, kufanya hifadhi kubakiwa na hekta 9,319.238.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tayari Wizara imekamilisha zoezi la kupitia mpaka wa hifadhi na kupima upya eneo lililobaki na tayari ramani mpya ya eneo hilo imeandaliwa. Aidha, Wizara imewasilisha Rasimu ya Tangazo la Serikali (Notisi ya Kusudio la Kutangaza Mabadiliko ya Eneo la Msitu wa Hifadhi wa Taifa Maisome ya Mwaka 2024) kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa ajili ya upekuzi ili kukamilisha taratibu za Kisheria za mabadiliko hayo.
MHE. ERICK J. SHIGONGO aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Soko la Samaki la Nyakarilo – Buchosa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa soko hilo la samaki, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara inaendelea na jitihada za kujenga, kuboresha na kukamilisha masoko mbalimbali ya samaki hapa nchini likiwemo soko la Samaki la Nyakarilo kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, ninaielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa kuweka ujenzi wa masoko ya samaki kwenye miradi yake ya kimkakati kwa kutenga fedha kupitia mapato yake ya ndani.