Supplementary Questions from Hon. Agnes Elias Hokororo (51 total)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa suala la upatikanaji wa maji safi na salama bado ni tatizo sugu katika Mkoa wa Mtwara na hivyo kupelekea akina mama kutumia maji ya kuokota okota na hivyo kuongeza gharama za matibabu kwa sababu ya matazizo ya homa za matumbo na kadhalika.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba tunamaliza tatizo la kuongeza gharama za matibabu kwa sababu ya upatikanaji wa maji ya kuokota okota ambao unapelekea wananchi kuendelea kupata homa mbalimbali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hokororo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya umuhimu wa upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Mtwara, Serikali kwa kupitia Wizara ya Maji, tayari tumejipanga kuhakikisha tunakwenda kutumia maji ya Mto Ruvuma. Tutakapoweza kufanya mradi huu, adha ya maji katika Mji wa Mtwara, Nanyamba na maeneo yote ya mwambao ule yanakwenda kukoma kwa sababu itakuwa ni suluhisho la kudumu. Kwa hiyo, tunatarajia mwaka ujao wa fedha kutumia maji ya Mto Ruvuma.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuulizwa maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa barabara hiyo sasa inaitwa kwa jina la dhihaka kwamba ni barabara ya kuombea kura na kwamba katika jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri amesema jumla ya Shilingi Bilioni 10 zimetengwa kwa bajeti ya mwaka 2020/2021 na sasa imebaki miezi miwili, naomba kuuliza swali, ni lini hasa ujenzi huo unaanza na kukamilika kwa kuwa hata Mkandarasi na ukusanyaji wa vifaa haujaanza? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na ubovu wa barabara hiyo vyombo vya usafiri vimekuwa vikitoza nauli kubwa. Umbali wa kutoza Sh.750 unatozwa Sh.3,000 na kuendelea. Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Mtwara namna inavyoweza kukomesha ama kuwasaidia kumudu gharama za usafiri ili waweze kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinawahitaji kusafiri? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA
M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnes Hokororo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Mtwara kwa kuwasemea wananchi wake katika jambo muhimu sana la mawasiliano ya barabara. Kwenye swali lake la kwanza amesema ni kweli kwamba zimetengwa Shilingi Bilioni 10 na muda wa bajeti ya mwaka huu imeyoyoma sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya hapa tu baada ya maswali na majibu tutakaa naye kwa sababu hapa kuna mchakato fedha zipo zimetengwa kama kuna changamoto kama nilivyosema hakuna taarifa kule eneo la Mtwara hasa TANROADS tuwasiliane, tumpe majibu sahihi ili aweze kueleza wananchi wake ni lini barabara hii inaanza kutengenezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anasema nauli imepanda kwa sababu ya ubovu wa barabara kutoka 750 hadi 3,000 na nini kauli ya Serikali. Kauli ya Serikali ni kwamba, Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami kama ambavyo ilivyoahidi kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Naomba niwaambie wananchi wa Mtwara na maeneo ya jirani kwamba sasa barabara hii haitakuwa barabara ya kura itakuwa jambo halisi na litatekelezwa. Ahsante sana.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Kwa kuwa, uwepo wa viwanda visivyofanya kazi katika Mkoa wa Arusha inafanana kabisa na Mkoa wa Mtwara ambako kuna viwanda vya korosho ambavyo havifanyi kazi. Naomba kujua ni lini Serikali itahakikisha Viwanda vya Kubangua Korosho vilivyopo katika Mkoa wa Mtwara, Wilaya ya Masasi, Newala na Mtwara vinaanza kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hokororo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwa muda mrefu Viwanda vya Kubangua Korosho katika Mkoa wa Mtwara na maeneo ya Pwani vilisimama kufanya uzalishaji. Sababu ya msingi ilikuwa ni kwamba mfumo wa uuzaji wa korosho wa minada ulikuwa unawaweka kwenye disadvantage processors wa viwanda ndani ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hatua ya kwanza ambayo Serikali imechukua na marekebisho haya tumeyafanya mwaka jana ni kwamba, tumeruhusu mfumo wa primary market kwamba wenye viwanda vya kuzalisha korosho wanaainisha mahitaji yao ya awali na tunawaruhusu kwenda kununua moja kwa moja katika vyama vya msingi badala ya kusubiri kwenye mnada kwa sababu, kwenye mnada wanakuwa not competitive na matokeo yake gharama ya wao kuchakata korosho inakuwa kubwa. Mwaka huu vipo viwanda viwili ambavyo vimeanza kufanya hiyo process na tumevifanyia majaribio na tumeona manufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini changamoto ya pili inayowakabili wenye viwanda vya kuchakata korosho ni thamani ya mtaji unaotakiwa kununua sokoni ili aweze kuhifadhi kwa msimu mrefu kwa maana ya mwaka mzima.
Kwa hiyo, sasa hivi tunafanya mazungumzo na Tanzania Agricultural Development Bank ili tuanzishe mfumo wa Collateral Management System kwamba wenye viwanda wanapata raw material zinahifadhiwa katika maghala, wanakuwa wanachukua kidogokidogo kutokana na mahitaji yao ili waweze ku-sustain katika kipindi cha mwaka mzima. Msimu huu wa korosho utakaoanza mfumo wa primary market kwa viwanda kununua moja kwa moja katika vyama vya msingi tutawaruhusu ili viwanda vya Mkoa wa Mtwara na Lindi viweze kufanya kazi.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa katika majibu ya msingi Serikali imetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujenga kongano ya kubangua korosho katika eneo la Masasi, je, ni lini ujenzi huo utaanza? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, baadhi ya viwanda vya kubangua korosho vimekuwa vikinunua korosho katika minada ya awali ili kuwezesha viwanda hivyo kubangua korosho na kuongeza thamani. Hata hivyo, imeonekana pia vimekuwa vikibangua korosho kiasi kidogo na nyingine kuuzwa ghafi. Serikali ina utaratibu gani wa kudhibiti jambo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnes Hokororo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa mfuatiliaji sana kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya korosho na hasa katika uwekezaji kwenye viwanda vya kubangua korosho.
Mheshimiwa Spika, kama alivyosema ni kweli Wizara na jukumu la Serikali ni kuhakikisha mazao ya kilimo ikiwemo korosho yanapata soko lakini pia yanaongezewa thamani kwa kuchakatwa katika viwanda vyetu vya ndani.
Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto kubwa iliyokuwepo ni kuona korosho hizo zinapata wanunuzi na ndiyo maana tumeanzisha kongano au cluster ya korosho ili kuwahusisha pia na wajasiliamali wadogo waweze kushirikki katika kuongeza thamani ya zao la korosho.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilikuwa tumetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kongano hilo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka wa fedha ujao 2021/2022 kazi hii ya ujenzi itaanza kwa sababu tayari fedha hizo zimeshatengwa kwa ajili ya kujenga kongano hilo la wajasiliamali kwa ajili ya kubangua korosho kwenye maeneo ya Masasi na Mtwara.
Mheshimiwa Spika, kuhusu viwanda na kupata korosho katika minada ya awali, ni kweli ni utaratibu ambao Serikali imeuweka baada ya kuona viwanda vingi vinakosa malighafi ambayo ni korosho kwa ajili ya kubanguliwa katika viwanda hivyo. Kwa hiyo, utaratibu sasa kama alivyosema ni kweli kuna minada ya awali ili angalau viwanda hivi visikose kupata malighafi. Baada ya viwanda hivi kununua korosho hatua ya pili ni mnada ambao sasa unashirikisha na makampuni mengine.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kudhibiti viwanda hivi inategemea kwa sasabu kama kiwanda kimeshatosheka na malighafi inayohitajika katika kuchakata korosho basi wana uhuru wa kuuza nje. Kama tunavyojua Tanzania tuna competitive advantage kwa maana ya kuzalisha zaidi korosho kuliko maeneo mengine. Kwa hiyo, tukitosheka sasa katika viwanda vyetu then korosho inayobaki inaweza kuuzwa kwenye minada ya nje ambapo wanaweza kusafirisha nje kama ambavyo wanafanya sasa.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa kuwa katika swali la msingi majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ilikuwa kwamba lengo la Shamba la Nangaramo ni kusambaza mitamba, lakini katika maeneo mengi yenye mashamba haya mitamba hiyo imekuwa ndama wake wanauzwa kwa shilingi 1,500,000 na hivyo wananchi kushindwa kumudu gharama za kununua ndama.
Je, Serikali haioni haja ya kuondoa kabisa hayo mashamba na kwa vile lile lengo la msingi la kusambaza mitamba halijafanikiwa? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; kuhusiana na bei ya mitamba, hiyo ni biashara; na ndama au ng’ombe wanaouziwa wananchi bei yake inajumlisha gharama za kumtunza yule ng’ombe pamoja na gharama zingine zote.
Mheshimiwa Spika, sasa huwezi kumnunua ng’ombe ambaye Mheshimiwa Mbunge anamuita ni ndama, actually ni ng’ombe kwa sababu huyo ng’ombe anaponunuliwa kwetu anakuwa yupo tayari kubeba mimba ili aweze kuzaa. Sasa sio ndama kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amemuita na pengine tutaangalia utaratibu ambao unapelekea mpaka kufikia gharama za namna hiyo, tuone kama tunaweza taratibu za gharama zikapungua tuweze kuwauzia kwa bei ambayo ni reasonable. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitangaze tu kwamba kwa Shamba la Nangaramo tayari tumewauzia wananchi walio karibu na shamba hilo mitamba 14 wameweza kununua na shamba letu kwa sababu linazalisha sio mitamba mingi sana, inatafutwa na wana order kubwa mpaka sasa hivi wanasubiria. Sasa suala la bei tutaliangalia tuone ni kwa namna gani inaweza kupungua ili wananchi waweze kununua mitamba mingi zaidi. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante, lakini uzalishaji wa miche ya kahawa unafanana na uzalishaji wa miche ya mikorosho iliyopo Mkoani Mtwara. Vikundi vinavyozalisha miche ya korosho Mkoani Mtwara vinaidai Serikali tangu mwaka 2018 na hivi karibuni tulipata kauli ya Serikali kwamba hundi imeandikwa.
Mheshimiwa Spika, swali langu ni je, ni lini Serikali italipa vikundi hivyo vya uzalishaji wa miche ya korosho vilivyoko Mkoani Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hokororo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza, nitumie Bunge lako kuwaambia kwamba wakulima wadogo wote ambao walikuwa wanadai zaidi ya shilingi bilioni 1.8, tayari fedha hizi zimeshatoka na sasa tunafanya utaratibu ili Wizara ziweze kupelekwa Bodi ya Korosho na Bodi ya Korosho ianze kulipa wakulima. Anytime kuanzia sasa fedha hizo watakuwa wameanza kuzipata.
Mheshimiwa Spika, niwahakikishie tu kwamba kwa sababu utaratibu tuliokuwa tumejiwekea na ninashukuru Waziri wa Fedha hapa alisema kwamba taasisi yoyote ya Serikali itakayopokea fedha dakika za mwisho, hakutakuwa na ule utaratibu wa kuzirudisha, tunaamini kwamba kati ya wiki ijayo mpaka mwanzoni mwa mwezi Julai fedha hizi zitanza kulipwa kwa sababu tayari utaratibu wake umeshakamilika.
Mheshimiwa Spika, vilevile watumishi wa umma walioingia mikataba na Bodi ya Korosho, malipo yao na yenyewe kama Wizara sisi tumesha-compile na kuzipeleka Wizara ya Fedha ili na wao waweze kupata haki yao kwa sababu kuwa watumishi wa umma hakuwaondolei haki ya kulipwa kama ambavyo walitakiwa kulipwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Mbunge, tutaendelea kuwasiliana kwa karibu kuhakikisha kwamba mpaka Julai wakulima wote fedha zao wawe wameshazipata kwa sababu fedha hizo hata zikiingia kwetu tarehe 30 hazitarudi Hazina.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri yenye matumaini yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri kwa wananchi wa maeneo ambayo walikuwa na shida kubwa ya maji, lakini pamoja ma majibu hayo mazuri naomba kuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba kwa kuwa katika Kata za Mpanyani, Namatutwe, Msikisi, Namajani ambao pia Nambawala ipo katika Kata ya Mpanyani, wananchi hawa hawajawahi kuona maji salama kwa maana ya mabomba na naomba kuuliza; je, Serikali ina mpanga gani wa kuharakisha uchimbaji wa mabwawa katika kata hizo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Kijiji cha Mraushi na vitongoji vyake ambapo katika majibu ya msingi Serikali imethibitisha kwamba ujenzi wa mradi wa kuwapatia maji wananchi hao umeanza kwa bajeti ya mwaka 2021/2022. Ni lini mradi huo utakamilika ambapo pia nina uhakika Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuambatana na mimi kwenda kujionea kadhia ya hali ya maji katika maeneo hayo?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake mkubwa na si mara moja amekuja katika Wizara yetu ya Maji kuhakikisha wananchi wake kuwa wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, kwanza nilishukuru sana Bunge lako Tukufu sisi Wizara ya Maji kutuidhinishia zaidi ya shilingi bilioni 680. Lakini kwa namna ya kipekee Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake njema ya kuhakikisha kwamba anakwenda kumtua mwana mama ndoo kichwani ametupatia fedha ya nyongeza zaidi ya shilingi bilioni 207; haijawahi kutokea; nataka nimuhakikishie fedha zile moja ya mipango ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kununua vitendea kazi kwa maana ya magari ya kisasa kwa ajili ya ujengaji wa mabwawa pamoja na uchimbaji wa visima. Kata zake alizoainisha tutakwenda kuzipa kipaumbele katika kuhakikisha kwamba tunakwenda kutatua tatizo la maji. Ahsante sana.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimwulize maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri amezingatia eneo moja tu la uchimbaji wa dhahabu: Je, Serikali ina mpango gani wa kubadili matumizi ya zebaki inayotumika katika vifaa vya afya ikiwemo katika ujazaji wa jino?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Je, zebaki inayotumika katika huduma za afya kama vile kipima joto kwa maana ya thermometer ama wakati wa kujaza jino kwa maana ya amalgam, ina athari gani zinapotumiwa na binadamu; na je, athari hizo zinapatikana baada ya muda gani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili mazuri ya Mheshimiwa Mbunge mwenzangu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, matumizi ya vitu vyenye mercury kwenye kutibu meno; moja, kwa mercury ipo dozi maalum ambayo kuna mahali inapofikia ndiyo inaweza kuleta athari. Hata hivyo ni kweli kwamba kuna baadhi ya watu wakizibwa meno kwa kutumia amalgam hiyo yenye mercury, wengine wanapata allergy.
Kwa hiyo, wakati mwingine watu wanaweza wakafikiri ni madhara ya mercury, lakini ni allergy kwa sababu kuna watu wenye allergy na baadhi ya mambo. Mpaka sasa, kwa kutibu meno, inatumika na haijaonesha madhara ambayo unadhani yanatokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna options mbalimbali za kutumia na utafiti unaendelea kuona namna ya kupata kitu chenye strength ile ile ambayo amalgam ilikuwa inafanya ili waweze kuitoa, lakini kwa kweli mpaka sasa kitiba haina shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, amezungumzia thermometer na vifaa vingine vya tiba ambavyo vina mercury, tunafanyaje? Kikubwa ambacho mpaka sasa hata kwenye madini kinafanyika, kwenye vifaa vyote vya tiba na hata dawa, suala kubwa hapa, ni kwa namna gani unafanya disposing na control mechanism zinavyohaibika na zile thermometer unazi-dispose kwa namna gani? Ndiyo maana kuna utaratibu maalum wa namna ya ku-dispose vifaa tiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutaendelea na utaratibu wa kuhakikisha thermometer na vifaa vingine vyote vinavyotumia mercury vinakuwa under control na vikiharibika ile disposing mechanism inafuatwa ili kutunza mazingira na kutunza afya ya binadamu. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri. Je, ni lini Serikali itafikisha huduma ya majisafi na salama katika Wilaya za pembezoni katika Mkoa wa Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara imejipanga kutumia Mto Ruvuma kuona maeneo yote ya pembezoni yanaenda kupata maji na Wizara tunaendelea kutafuta fedha, naamini ndani ya mwaka ujao wa fedha maeneo mengi ya pembezoni mwa Mtwara yataenda kupata maji.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami kuunganisha barabara ya Mnivata – Tandahimba – Newala – Masasi kwa kuwa tulishaona kwenye vyombo vya habari upatikanaji wa fedha umekamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Agnes kwamba barabara ya Mnivata – Tandahimba- Newala hadi Masasi yenye urefu wa kilomita 210; kilomita 50 Mtwara hadi Mnivata imekamilika na tayari barabara hii ipo kwenye taratibu za manunuzi ambapo itafadhiliwa na Benki ya African Development kwa ajili ya ujenzi wa barabara yote. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya za Mkoa wa Mtwara takriban zote ziko mpakani. Je, Serikali iampango gani wa kujenga kituo cha Polisi katika Wilaya Masasi katika kata za mpakani kabisa za Mnadhira, Mchauru, Sindano na Chikoropola ambapo kwa sasa kunaonekana kuna vuguvugu za vurugu kati ya wakulima na wafugaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Hokororo Mbunge wa Viti maalum kutoka Mtwara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunapitisha ile bajeti yetu ya 2021/2022 moja ya miongoni mwa mambo ambayo tunakwenda kuyafanya katika bajeti ile ni kujenga vituo vingi vya Polisi na hasa yale maeneo ambayo yanautauta kiulinzi, maeneo ya mipakani na maeneo mengine ambayo tunahisi yana sababu za zaidi asilimia moja kuwepo kwa vituo vya Polisi kwa ajili ya kulinda Maisha ya wananchi na mali zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa kwamba awe na subra Serikali itahakikisha kwamba inajenga vituo vya Polisi maeneo mengi lakini hasa katika maeneo ambayo wameyataja ili liengi na madhumuni wananchi waweze kuishi katika Maisha ya ulinzi na usalama zaidi, Nashukuru.
MHE. AGNES J. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali madogo ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2022, idadi ya watu imeongezeka: Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza mawanda ya mradi huo ili kuongeza idadi ya watu watakaonufaika na mradi huo?
Mheshimiwa Spika, pili, chanzo cha maji cha Chiwambo na Maratu havitoi maji kwa sasa kutokana na deni kubwa la bili ya TANESCO. Serikali ina mpango gani wa kusimamia jambo hili ili kuwawezesha wananchi hao kupata maji safi na salama?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Hokororo kutokana na kazi kubwa anayoifanya hasa kupigania wananchi wake kwa ajili ya kupata huduma hii ya maji.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Wizara ya Maji kutokana na takwimu hii ya ongezeko la watu, tumejipanga kutumia kwanza vyanzo toshelevu kwa maana ya mito na maziwa ili kuhakikisha kwamba tunawafikia watu wengi ili kuendelea kutoa huduma ya maji. Mathalani, huu Mradi wa Nanyumbu, tunatoa maji ya Mto Ruvuma ili kuhakikisha wananchi wengi wanaenda kupata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; ipo mamlaka ambayo ina deni na TANESCO. Namwomba Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge tukae ili kuona namna gani tunaweza kuisaidia mamlaka hiyo kwa haraka ili huduma iendelee kwa ajili ya upatikanaji wa maji.
MHE. AGNESS E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante; ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami kipande cha barabara kutoka Masasi kwenda Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hokororo, Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Masasi - Nachingwea kilometa 45 imepangiwa bajeti kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami, lakini pia kipande cha Masasi - Nachingwea hadi Liwale pia kimeingizwa kwenye Mpango wa EPC+F ambapo wakandarasi tayari wameishaoneshwa barabara hiyo na tayari tunategemea pengine kufungua zabuni kipindi si kirefu, ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami, barabara inayounganisha Mkoa wa Lindi na Mtwara, RuangWa – Nachingwea - Masasi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hokororo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mpango wa Serikali kuijenga barabara ya Masasi -Nachingwea kwa kiwango cha lami, lakini itaanza tu pale ambapo Serikali itakuwa imeshapata fedha kwani tayari usanifu wa kina ulishakimilika, kwa hiyo kinachosubiriwa ni upatikana wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. naomba kuuliza swali dogo la nyongeza: -
Je, ni lini Serikali itaongeza majengo na kukarabati Kituo Polisi Masasi ambacho kilijengwa wakati wa ukoloni 1959?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongea la Mheshimiwa Hokororo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua vituo vilivyojengwa kabla ya uhuru kama hiki cha Masasi ni vya muda mrefu, vimechakaa, vinahitaji ukarabati. Kupitia Bunge hili namwomba IGP kupitia wasaidizi wake walioko mikoani waweze kufanya tathmini ya kiwango cha uchakavu wa Kituo cha Polisi ngazi ya Wilaya pale Masasi ili baada ya kubaini kiwango cha uchakavu kiweze kutengewa bajeti kwa ajili ya matengezo kulingana na mpango wetu wa matengezo na ujenzi wa vituo vyetu vya Polisi, nashukuru.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mhesimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba niulize maswali madogo mawili. Kwa kuwa katika majibu ya msingi amesema matibabu ya wototo njiti hayatozwi, lakini kwa kuwa mpaka sasa huduma hizo zinatozwa;
Je, Serikali iko tayari kurejesha fedha ambazo wazazi waliojifungua watoto njiti walizitoa?
Kwa sababu ninayo madai ya mama anayedaiwa milioni moja na laki nane katika Hospitali ya Muhimbili.
Mhesimiwa Naibu Spika, kwa kuwa watoto njiti wamekuwa na changamoto mbali mbali za kiafya zinazowakosesha pengine kuendelea kuishi vema sawa sawa na watoto wengine;
Je, Serikali iko tayari kufanya mapitio ya likizo ya uzazi kwa wazazi wanaojifungua watoto njiti?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mhesimiwa Naibu Spika, nijibu maswali yake mawili kama ifuatavyo: -
Mhesimiwa Naibu Spika, moja; nitoe agizo kwa hospitali zote lakini vile vile mfuko wetu wa bima ya afya, kwamba suala la watoto njiti kama ni mama amejifungua na mtoto njiti au wakati wowote bima ya afya iweze kumuhudimia kama ni mwenye bima ya afya. Kuhusu kwamba wakizaliwa kwenye hospitali zetu zote watibiwe bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Hokororo amesema je Serikali iko tayari kwa sababu ana ushahidi wa hospitali ambayo wanatoza. Ninakuomba Mheshimiwa Mbunge nikishakaa uje unionyeshe halafu tufuatilie nini kilichotokea. Siwezi kukuambia kwamba zitarudishwa lakini tutampata anayefanya hivyo na tuweze kumpa maelekezo mazuri, ili suala hilo lisijitokeze tena.
Mhesimiwa Naibu Spika, lakini la pili, suala la sheria ya likizo, hilo sasa ni la kisheria sio suala la Wizara ya Afya, lakini nimeshasikia kuna harakati hizo zinaendelea na kuna majadiliano ndani ya Serikali kuona hilo linafanyikaje. Tungojee hayo majadiliano ndani ya Serikali halafu yakifikia muafaka tunaweza tukajua ni nini kitakachofanyika. Kwa sababu hilo si suala la Wizara ya Afya pekee yake, hilo linahitaji masuala mengi kama vile utumishi, Wizara ya Katiba na mambo mengine.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, je, ni lini ujenzi wa barabara ya kutoka Masasi kwenda Nachingwea utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ipo kwenye evaluation kupitia EPC+F. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Serikali ina mpango gani wa kupeleka watumishi katika kituo cha afya Lukuledi ambacho kinakamilika ambacho kitahudumia Kata zaidi ya Tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Hokororo Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kituo cha afya hiki cha Lukuledi ambacho amekitaja Mheshimiwa Mbunge ni miongoni mwa vituo ambavyo vitapelekewa watumishi ili viendelee kutoa huduma bora za afya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakipa kipaumbele kituo cha afya hiki?
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Je, ni lini Serikali itasafisha ili kuongeza kina cha Bwawa la Lukuledi ikiwa ni ahadi yake Mheshimiwa Waziri ya mwaka 2021, maji ambayo yanatumika katika Vijiji vya Lukuledi, Mwangawaleo, Ndomoni, Mraushi na Nambawala?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa moja ya changamoto kubwa katika utekelezaji wa mabwawa ilikuwa suala zima la vifaa. Lakini tumekwishapata fedha juu ya ununuzi wa vifaa hivi vya kisasa na moja ya maeneo ambayo tutayapa nguvu na ya kipaumbele ni kuhakikisha kwamba tunajenga mabwawa. Kwa hiyo, tutawapa kipaumbele katika kuhakikisha mabwawa ambayo yatakayokuwa yamejengwa na yeye jimboni kwake.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsane kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha vile vikundi vya wanawake na vijana ambao wanapata mikopo ili mikopo hiyo isipotee wafanyiwe tathmini ya kazi wanazokwenda kuzifanya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Hokororo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kabla ya vikundi hivi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu havijapewa mikopo, moja ya kigezo muhimu ni kufanya tathmini ya uwezo lakini na utayari wao wa kuanza kufanya shughuli hizo za ujasiliamali ili kuhakikisha zile fedha wanazokopeshwa zinaleta tija, lakini pia hazipotei. Tumeendelea kufanya hivyo na ndiyo maana tumeona matokeo mazuri ya urejeshaji ukiangalia kwa miaka inavyokwenda mpaka sasa kuna improvement kubwa na tutaendelea kufanya hivyo.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wakati Taasisi zisizo za Kiserikali zinahamasisha hedhi salama na kwamba kutakuwa na maadhimisho ya hedhi salama tarehe 28 ya mwezi huu, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba katika shule za msingi na sekondari na hasa tunaposema hedhi salama moja ya kikwazo ni ukosefu wa maji. Kwa nini Serikali isiweke kwenye mikakati yake kila mradi wa maji unapoenda mahali popote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ihakikishe maji hayo yanafika kwanza kwenye shule zetu za msingi na sekondari ili kuhakikisha changamoto hiyo ya hedhi salama inaondoka?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hokororo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji tayari tunahakikisha shule, vituo vya afya na zahanati zote zinapatiwa huduma ya maji safi na salama. Kwa kuzingatia hili la watoto wa kike tunapomtua mama ndoo kichwani tunahakikisha pia huyu mama ajaye pia anabaki na afya yake kwa kupata maji safi na salama. Hivyo watendaji wetu mikoa yote wanafahamu hili na wataendelea kulifanyia kazi.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Je, ni lini Serikali itaanza kutupa mrejesho wa vifo vya uzazi vinavyotokana na uzembe ili tuweze kuwa na imani kwamba Serikali inafuatilia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kila kifo kinachotokea cha mama anayejifungua huwa kinajadiliwa. Sasa, anasema kwamba ni lini wataanza kutupa mrejesho; kwakweli ni kazi yetu pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwetu Mheshimiwa Waziri wa Afya ameshaelekeza, na kwamba tumegundua watu kama Red Cross wana mtandao mkubwa sana kutoka taifa mpaka tunafika kwenye vitongoji vyetu na ni mtandao wa kijamii. Tunafikiri kwamba tukiwashirikisha hao, tunataka sasa, kama ilivyo elimu, kwenye vituo vyetu vya afya na zahanati zetu kuwepo na ownership wa kijamii, kwamba kila tatizo linapotokea liwepo wanajamii wanajadili inajulikana kwenye jamii na information zinaenda vizuri kwenye jamii. Kwa namna hiyo tutaweza kupunguza vifo vya akina mama
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile sisi wanaume tunahitaji kuwa na ownership ya ujauzito wa akina mama tangu mama anavyobeba mimba tuweze kushirikiana na mama mpaka siku anapojifungua. Tukifanya hivyo nayo itatusaidia vizuri sana kwasababu kila baba anapenda kujisifia mtoto wake ambaye anafaulu vizuri shuleni, lakini kufaulu kwa mtoto vizuri shuleni kunaendana vilevile na kuanza kutunza mimba toka siku mimba inavyobebwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo akinababa kama tunapenda watoto wafanya vizuri shuleni wawe brilliant kwenye maisha tuanze na mimba siku mama anapobeba ujauzito. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna hiyo suala la afya litakuwa sio suala la wataalam wa Afya peke yao, litakuwa suala la kijamii. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuuliza swali Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, ni kweli kwamba miradi ya barabara ile nane aliyoisema kwenye majibu yake ya msingi ikiwemo ya Masasi – Nachingwea itakayojengwa kwa program ya EPC + F ni kwamba haijulikani lini itaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hokororo, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda na barabara hizi zote kwa pamoja na kama Mheshimiwa Mbunge alinisikiliza, hizi ni hatua na ni mfumo mpya. Kwa hiyo, kusema ni lini tarehe itakuwa ngumu lakini tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Fedha sasa hivi inapitia kila barabara na kuona kwamba tunafanya tunavyotakiwa ili tutakapoanza kuzijenga hizo barabara tuwe na uhakika kwamba tulichofanya ni maamuzi sahihi na yatakwenda. Kwa hiyo, cha msingi tu ni kwamba ni hatua, ni process ambayo inaendelea lakini tutakapokuwa tumekamilisha upande huu tukishaanza kuitangaza sasa unaweza ukasema sasa baada ya kuitangaza tuna muda huu na huu.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itaweka kipaumbele kuajiri Maafisa Mipango na Maendeleo ya Jamii ili kupanga na kuchechemua maendeleo katika halmashauri zetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Hokororo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuajiri Maafisa Mipango na kada mbalimbali katika Serikali kama ambavyo imekuwa inaombwa vibali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Vile vile, katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetoa vibali 30,000 vya kuajiri kada mbalimbali. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama eneo hilo alilolieleza na uhitaji ambao tunaufahamu, nataka nimhakikishie kabla ya mwisho wa mwaka jambo hilo tutalifanyia kazi tuweze kuhakikisha kwamba hiyo kada imeenea kama ambavyo imeombwa. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza tija kwenye zao la korosho ambao kwa msimu uliopita imeuzwa kwa bei ya chini na ya kutupa na kuwaletea hasara wananchi wa Mtwara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sera yetu ya Kilimo ya mwaka 2013 kipengele cha pili (2)(3) likiwa ni lengo la pili la malengo 10 ya sera ya kilimo imeeleza kuhusu tija katika mazao yote ya kilimo hapa nchini. Yako mambo lazima tuyafanye kama Serikali ili wakulima wetu waweze kulima kwa tija. Jambo la kwanza ni kuhakikisha tunapima afya ya udongo kutambua virutubisho ndani ya udongo ili tuwashauri vizuri wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili ni kuimarisha utafiti na cha tatu ni huduma za ugani na ugawaji wa pembejeo. Nataka nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwenye korosho tunajua kuna changamoto nyingi na jana tulikuwa na kikao cha tathmini tumeyaona na tutayafanyia kazi ili wakulima wa korosho na wenyewe waweze kulima kwa tija tuweze kufikia malengo na matarajio ambayo tumejiwekea kama nchi.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, Je, ni lini Serikali itapeleka madaktari kwenye hospitali ya kanda iliyojengwa Mitengo Mkoani Mtwara.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tutashirikiana na Wizara ambayo ndio wasimamizi wa hospitali hizi za kanda kuhakikisha kwamba Hospitali hii ya Kanda ya Mtwara kule inapata madaktari katika ajira hizi kwa sababu Wizara ya Afya nao wametoa ajira hizi kupitia mfumo wao.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Je, ni lini Serikali itajenga karakana ngumu na mabweni katika Chuo cha VETA kilichopo Kitangali ili kuwezesha vija wengi kupata mafunzo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Hokororo Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli na mimi nilishawahi kufika pale Kitangali, majengo yale yaliyokuwepo ni machache. Nakumbuka tuliweka kwenye bajeti yetu ya mwaka huu kwamba tuongeze majengo, madarasa na karakana katika Chuo kile cha Kitangali. Namwomba Mheshimiwa Hokororo mara tu baada ya kipindi hiki cha maswali tuweze kuonana tuweze kuangalia kwa nini fedha zile zaidi ya milioni 200 ambazo tulizitenga katika bajeti yetu ya mwaka huu kwa ajili ya kwenda kuongeza miundombinu katika chuo kile cha Kitangali kama hazijakwenda tuweze kuzipeleka kwa haraka.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru lakini sio mwiki ni mvuke. Maswali mawili ya nyongeza: -
a) Je, kwa nini SIDO na TBS isijielekeze katika kuboresha teknolojia za asili za watengenezaji wa pombe ya mvuke ya mabibo badala ya kuendelea kutoa mafunzo?
b) Je, kwa nini Serikali, isipitie watengenezaji wote wa pombe ya mabibo, badala ya kusubiri waombaji wachache wenye uwezo wa kuagiza mitambo kwa ajili ya kupata hizo ithibati za TBS na SIDO?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni kweli kabisa kwanza nimpongeze Mheshimiwa Agnes Hokororo kwa kuleta tena hili swali ambalo ni hoja muhimu sana kwa Watanzania wengi ambao wengi tumeendesha shughuli zetu za kusoma shule na mambo mengine kupitia pombe hizi za kienyeji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kweli tunachofanya sasa ni kuboresha teknolojia zilizopo lakini pia kuna wakati mwingine tungependa kupata teknolojia rahisi lakini za kisasa zaidi. Ndiyo maana SIDO tunahakikisha tunawatembelea wazalishaji hawa na kuwasaidia. Kama ambavyo nimesema, tayari kuna haya maombi, maana yake hawa ni wale ambao wana uwezo wa kuomba; lakini ambao sasa hawana uwezo wa kuomba, kama ambavyo nimesema wale wazalishaji wa pombe hii ya mvuke kupitia mabibo, tumeshaamua sasa tutawatembelea wauzaji wote wa pombe za kienyeji ili tuwaelimishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, tutawaelimisha kuhusu mazingira sahihi ya kuzalishia, kwa maana ya kuzalisha pombe, ambapo itakuwa na mazingira sahihi mazuri. Pili tuwasaidie teknolojia rahisi na kuzihuisha zile zilizopo ili ziwe katika mazingira ambayo yatapelekea kupata viwango sahihi vya pombe. Tatu, tuwasaidie kuhakikisha wanapata teknolojia ya kutunza, packaging ili zile pombe zisiharibike mapema au zipate shida ambayo itapelekea kuwa sumu kwa walaji katika mazingira mabayo si sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza: -
Je, Serikali iko tayari kufanya tathmini kwa vijana hao ambao wamepatiwa mafunzo ya uanagenzi katika Mkoa wa Mtwara na nchi nzima ili kuona kama hiyo programu ina tija?
Swali la pili, hao vijana ambao hawajapatiwa vyeti kwa maana ya kutambuliwa ama kurasimishwa, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba vijana hao wamepatiwa vyeti na kutambulika katika elimu isiyo na mfumo rasmi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali iko tayari kufanya tathmini na siyo kwa Mkoa wa Mtwara pekee, ni nchi nzima kwa sababu sera hii ni kwa ajili ya wananchi wote.
Mheshimiwa Spika, kwa kipengele cha pili, wale ambao wamekidhi vigezo vya kupatiwa vyeti, utaratibu utafwatwa na watapatiwa vyeti vyao. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa tangu tathmini ya malipo ya fidia kwa wananchi wa Nanganga yamefanyika muda mrefu umepita.
Je, Serikali iko tayari kuongeza kiwango cha fidia kwa wananchi wale kwa sababu walisimama kabisa katika maendeleo yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni utaratibu wa Serikali kwamba kama fidia imefanyiwa tathmini ikapita miezi sita ni lazima turudi kuhuisha tena ile tathmini ili kupata thamani ya wakati huo. Kwa hiyo itafanyiwa tathmini mpya kama imepita miezi sita na watalipwa sasa fidia ya wakati huu, ahsante. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, je, Serikali haioni haja ya kuweka kipaumbele kuongeza watumishi wa afya kwenye Halmashauri mpya ikiwepo Halmashauri ya Mji wa Nanyamba pamoja na Newala Vijijijni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu swali la Mheshimiwa Hokororo, ni kweli tunaona haja ya kuongeza watumishi hasa katika Halmashauri hizi mpya kama ya Nanyamba na ndiyo maana Serikali ilitenga bajeti katika mwaka huu wa fedha kuajiri watumishi 21,390 nchi nzima katika sekta ya elimu na afya, kwa ajili ya kupeleka katika maeneo yenye uhitaji mkubwa kama Halmashauri ya Nanyamba.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na fedha za wastaafu lakini kumekuwa na changamoto kubwa kwa watumishi wanaofanya kwenye Wizara hiyo, wanapohama kutokulipwa madai yao ya uhamisho kwa wakati.
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuhakikisha inawalipa kwa haraka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ni kweli moja ya changamoto zinazotokea pale kunapokuwa na uhamisho ambao haukuwepo kwenye bajeti kwa mwaka husika. Nakuhakikishia kwamba, uhamisho wote ambao umefuata taratibu kamili, wote watalipwa na hasa hii inatakiwa baada ya kuhakiki gharama hizo na kuingiza kwenye bajeti ya mwaka husika, watumishi hawa wanaohama wanalipwa stahiki zao kama ambavyo wamestahili. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, sasa ni mwaka wa tano tangu 2018 maktaba ilipokamilika, thamani zake ziko wapi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, maabara ilipanga kukamilika Oktoba, 2022 na kwa sasa imefikia asilimia 35, nini tamko la Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwamba Wizara ilikuwa inasubiri ukamilishaji wa maktaba na maabara na baada na ukamilishaji huo, Serikali inakwenda kuweka samani zote. Kwa kuwa tayari maktaba imeshakamilika, bado maabara, Wizara ilikuwa inasubiri vyote vikamilike kwa pamoja ili samani hizo zote ziende kwa pamoja. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute Subira, jambo hili tunalifuatilia. Leo jioni tukutane mimi na yeye twende pale Wizarani tufuatilie tuone jambo hili linafika mwisho kwa kiwango hiki, ahsante. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Masasi – Nachingwea - Liwale itajengwa kwa utaratibu wa EPC + F tuliambiwa Mkandarasi amepatikana. Ni lini mkataba utatiwa saini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kama nilivyojibu katika swali ambalo nimeulizwa barabara hizi ziko saba na moja ya barabara hiyo ni ya Masasi – Nachingwea hadi Liwale. Mikataba ilishakamilika kinachosubiriwa ni muda na kwa sasa kwa sababu ni miradi mikubwa signing itafanyika muda wowote iko tayari kwa ajili ya signing na tunategemea kabla ya mwisho wa mwezi Juni barabara hii ya Masasi – Liwale – Nachingwea kilometa 175 itakuwa imesainiwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza ajira zaidi kwa wanawake kwa kuwa hawa 241 bado ni wachache katika zao la korosho Mkoani Mtwara? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Mtwara haujapata block farming katika zao la korosho; Serikali ina mkakati gani wa kuwatengenezea vijana programu mahsusi katika mnyororo wa thamani kwa zao la korosho ili vijana wa Mtawara waweze kunufaika na project za Wizara ya Kilimo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 zaidi ya asilimia 60 ya korosho inayozalishwa ndani iweze kubanguliwa na hivyo kutunza ajira zetu za akina mama na vijana kuliko ilivyo hivi sasa ambavyo ajira nyingi zinasafirishwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mkakati huo pia hivi sasa tunatazamia kuanza maandalizi ya ujenzi wa industrial park katika eneo la Nanyamba ambako tutajenga viwanda vya ubanguaji wa korosho na zaidi ya tani 300,000 zitabanguliwa na akina mama na vijana hawa wataunganishwa katika mfumo uliyosehemu pia ya ajira yao na kutatua changamoto hiyo ya korosho kutokubanguliwa.
Mheshimiwa Spika, la pili la kuhusu mashamba makubwa ya pamoja, utaratibu huo chini ya Bodi ya Korosho umekwisha kuanza na umeanza kuwapanga wakulima katika mashamba makubwa na ninaamini kabisa kwamba wakulima wa Mtwara wakiwemo akina mama na vijana watanufaika na mpango huo mkubwa sambamba na mkakati mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya skimu za umwagiliaji katika mabonde ambayo pia tutayaweka maeneo kwa ajili ya umwagiliaji wa kilimo cha korosho na hakika pia kupitia utaratibu huu akina mama na vijana wa Mkoa wa Mtwara watanufaika katika mfumo wa mashamba makubwa ya pamoja.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, ni lini visima vilivyochimbwa katika majimbo ya Ndanda, Nanyumbu na Tandahimba wananchi wake wataanza kuyatumia maji hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Hokororo, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Hokororo naye pia ameshafika ofisini na tumeweza kujadiliana masuala ya visima vyote vilivyochimbwa kwenye haya majimbo aliyoyataja. Mheshimiwa Mbunge baada ya hapa tuonane ili tuweze kupanga mkakati baada ya Bunge hili twende kule site tutaangalia namna gani ya kuona tunatekeleza kwa pamoja.
MHE: AGNES HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu ya Serikali naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Je, ni sheria ipi kati ya hizo sheria 30 inayosimamia wanawake wajawazito wakati wa kujifungua wanaopata huduma zisizoridhisha? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na swali la pili; je, sheria hizo zinaruhusu malipo ya fidia kwa wagonjwa wanaopata huduma zisizoridhisha au zisizo na ubora zinazopelekea athari za kiafya au hata kifo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nijibu swali la Mheshimiwa Agness Hokororo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa namna ambavyo anafuatilia namna wananchi wanavyotolewa huduma za afya katika eneo lake. Ni kweli kwamba kumekuwepo na mambo anayoyasema kwa maana ya huduma ya mama na mtoto lakini si tu sheria, sheria za nchi yetu, utaratibu wa nchi yetu na kanuni za Wizara ya Afya zinataka mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano wapate huduma bure lakini sasa tunapokuja kujibiwa vibaya, kujibiwa kwa masuala ya fedheha maana yake kuna sheria za kiutumishi ambazo zipo zimeonyesha watu wanaofanya mambo yanayofanana na hayo lakini kuna sheria za maadili ya kitaaluma ambayo mara nyingi anapopatikana mtu ambaye amekuwa akijibu vibaya akifanya nini wakati mwingine anapitishwa kwanza kwenye sheria za maadili ya kitaaluma anawajibika lakini anaachiwa vilevile sheria za kiutumishi zichukue mkondo wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kama mdau mkubwa kwenye eneo hilo endelea kutusaidia na kutusaidia kutengeneza ushahidi wa kutosha kuwapata watu wa namna hiyo ili waweze kushughulikiwa kulingana na taratibu na sheria, ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Likombe kilichopo Mtwara ndicho pia kinatumika kama hospitali ya Wilaya kwa sababu katika Wilaya hiyo hakuna hpspitali ya Wilaya;
Je, ni lini Serikali itapeleka gari la wagonjwa kwa sababu kuna wagonjwa wengi hasa akinamama wanaotaka kujifungua?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, Kituo cha Afya cha Likombe kina-serve kama hospitali ya halmashauri kwa sababu hatuna hospitali ya manispaa. Hata hivyo, nimhakikishie kwamba Manispaa ya Mtwara ni moja ya halmashauri zitakazopata gari la wagonjwa. Kwa hiyo nimuelekeze mkurugenzi kuhakikisha unazingatia vigezo ikiwezekana wapeleke gari hili katika kituo hiki kwa kadiri ya vigezo ambavyo vimewekwa na Serikali. ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya vyuo katika taasisi hizo kama vile Mtwara–Mikindani, Kibirizi–Kigoma, Gabimori–Rorya mameneja wake wamekaimu kwa kipindi kirefu sana kuanzia miaka saba mpaka kumi na moja;
i. Je, Serikali haioni inafifisha malengo ama maelekezo ya Chama cha Mapinduzi katika vyuo hivyo kutoa mafunzo kwa sababu havina mameneja wa kudumu?
ii. Je, Serikali itakapokamilisha mchakato huo wa kujaza hizo nafasi kwa muundo uliokamilika tangu Novemba 2022, iko tayari kuwalipa mameneja hao wanaokaimu akiwemo meneja wa Mtwara-Mikindani aliyokaimu kwa miaka 11 kwa nafasi hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza nampongeza sana dada yangu Agnes kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia sana chuo hiki na kwa kweli kama Wizara tunatumia nafasi hii kumpongeza sana kwa jinsi ambavyo anafuatilia habari hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni kweli kwamba kuna makaimu katika vyuo vingi vinavyohusiana na masuala ya uvuvi. Napenda kutumia nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba makaimu hao sasa watakwenda kuthibitishwa, wale wenye vigezo. Jambo hili liko kwenye upekuzi na upekuzi upo katika hatua za mwisho namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba linakwenda kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili alilosema kuhusu mameneja waliokaimu kwa muda mrefu taratibu za kiutumishi zinafahamika. Kama watakuwa na sifa za kulipwa basi watalipwa, Serikali iko tayari kuwalipa na kama watakuwa hawana sifa za kulipwa basi hawatalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itachimba visima kwenye maeneo ambayo hakuna vyanzo vya maji katika Mkoa wa Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Hokororo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Agnes Hokororo, ameshafuatilia mara nyingi na kuelezea namna wanawake wa Mkoa wa Mtwara, baadhi ya maeneo wanavyopata shida, lakini tumeshaanza kuchimba visima. Maeneo mengine ambayo bado yana uhitaji wa kuchimbiwa visima yapo kwenye mkakati. Nimwambie Mheshimiwa Hokororo, tutakutana na kuona kwamba tunapanga ratiba nzuri ya kuweza kufika maeneo haya. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na kazi nzuri inayofanywa katika Mradi wa Makonde, katika bajeti ya mwa 2022/2023 Wizara ilipanga kujenga mabwawa kumi kwa kutumia force account nchini.
Je, ni lini ujenzi wa Bwawa la Lukuledi – Masasi ambalo lilipitishwa katika Bunge lako Tukufu ujenzi huo utaanza?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii kwa mara nyingine kumshukuru Mheshimiwa Agnes Hokororo, kwa kweli amekuwa mfuatiliaji mkubwa sana juu ya changamoto ya maji, hasa maeneo ya Mtwara, lakini juu ya ujenzi pia wa bwawa hili la Lukuledi. Nataka nimhakikishie, Wizara ya maji hatuna kisingizio, tumepata mitambo ya uchimbaji visima na mitambo ya ujenzi wa mabwawa. Nataka nimhakikishie hii kazi tutaianza kwa haraka, ili Bwawa hili la Lukuledi tunalianza na wananchi hawa waende kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi na naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Jimbo la Nachingwea ni kubwa sana na lina kata ambazo zinapakana na Mkoa wa Morogoro lakini na Mkoa wa Ruvuma, Serikali pamoja na huo utaratibu haioni sasa ipo haja ya kugawanya maeneo ya kiutawala ili angalau kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Jimbo la Ndanda, limetawanyika pia kuelekea Mkoa wa Ruvuma, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Ndanda, ina sababishia wananchi watembee zaidi ya kilometa 80 kufuata huduma za Serikali. Je, Serikali haioni haja pia ya kugawa Jimbo hilo na kupatia halmashauri nyingine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Agnes Hokororo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la kuongeza Maeneo ya Utawala nilikuwa namshauri Mheshimiwa Mbunge, aendelee kuwasiliana na wenzetu wa TAMISEMI, kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa, Mamlaka, Wilaya sura ya 287 na kifungu cha 87(a)(1)(2) cha Sheria za Mamlaka za Serikali za Mitaa, kama zilivyorekebishwa katika marekebisho ya Sheria mbalimbali ili waweze kufuata huo utaratibu wa kuanzia u-DC, DCC, RCC na baadaye kuja Taifa ili waweze kuona namna ya kuzingatiwa kipindi hiko ambacho TAMISEMI, watafanya jambo hilo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili. Kuhusu Jimbo la Ndanda, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi kwa mujibu wa Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume imepewa mamlaka. Kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Mbunge, muda utakapofika Tume itakapotangaza basi na yeye afuatae utaratibu huo ambao utawekwa na Tume ili kusudi kuona jambo hilo utekelezaji wake, ahsante.
MHE. AGNESS E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.
(a) Je, kwa nini Serikali haiwalipi Mameneja wanao kaimu katika Vyuo vya Uvuvi pamoja na Wakurugenzi ambao wamekaimu kwa miaka zaidi ya 12?
(b) Wizara haioni imedumaza maendeleo ya Vyuo vya Uvuvi nchini ikiwemo Mikindani Mtwara kwa kuwakaimisha mameneja wake na kutokuwa na taratibu za uendelezaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nianze na hili la kwanza kwamba haiwalipi makaimu; utaratibu wa Serikali uko wazi kwamba mtumishi yeyote anaweza akakaimishwa nafasi yoyote kama ana vigezo na upekuzi ukikamilika anataeuliwa kushika nafasi hiyo rasmi kulingana na maelekezo ya Serikali yalivyo.
Mheshimiwa Spika, kwa kesi hii ya Mikindani, tumekuwa tukifanya upekezi kwa muda mrefu wenye sifa wanakosekana lakini tumeendelea kutafuta watu wenye uwezo wa kushika nafasi hizo katika maeneo hayo na sasa Serikali inaelekea mwishoni kukamilisha taratibu za uteuzi ili apatikane Mkurugenzi atakayekuwa ameshika nafasi katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na kwamba anafuatilia sana kwa karibu jambo hili kwa muda mrefu, nimhakikishie kwamba ndani ya muda mfupi tutakwenda kukamilisha jambo hili. Lengo la Serikali ni kuweka watu wenye weledi, wenye uwezo wa kushika nafasi hizo na si lengo kudumaza vituo hivyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba kuwasilisha.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, nadhani kulikuwa na swali la pili linalohusu kudumaa kwa wale wanaokaimu, kwamba wanashindwa kuendelezwa.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumeendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa wataalam wetu, kwa hivyo wataalam wale wanapopata mafunzo wanaojiendeleza wanakuwa na sifa za kushika nafasi hizo, kwa hiyo tumekuwa tukiangalia katika hao tuliowapa mafunzo, Je, wapi wana uwezo wa kushika nafasi hizi za kukaimu nafasi za juu katika uongozi?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tumeendelea kutoa mafunzo, mafunzo hayo yamezidi kuwasaidia wataalam wetu kujipatia uwezo wa kushika nafasi hizi na lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba wale wote wenye uwezo wa kushika nafasi hizi wanapewa nafasi hizo.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Masasi – Nachingwea ilisainiwa mkataba kwa utaratibu wa EPC+F, ni lini itaanza kujengwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi la swali hili, barabara zote za EPC+F tunategemea zilishasainiwa na tumesema kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha itakuwa tayari wakandarasi wameshaanza kwenda site kwa ajili ya kuanza kuzijenga. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ahadi ya Mheshimiwa Waziri ilikuwa ni kuongeza milioni 500 kuwa bilioni moja katika Barabara za TARURA, je, ni lini fedha hizo zitatoka?
Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa barabara nyingi zimekatika kutokana na athari za mvua ikiwemo Chiwale, Masasi Mkoani Mtwara. Je, Serikali ina mpango gani kupitia TARURA wa kuhakikisha barabara hizo zinapitika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kweli kuongeza bajeti kutoka shilingi milioni 500 mpaka shilingi bilioni 1.5 na Serikali ina nia ya kutekeleza ahadi hiyo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, Serikali itaweza kutimiza ahadi hii na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitalifuatilia suala hili. Tukitoka hapa tunaweza tukakutana tukazungumza ili kujua mustakabali wa masuala ya wananchi wa Geita Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, Serikali imeendelea kutenga bajeti ya kutosha na hivi sasa bajeti ya TARURA imetoka shilingi bilioni 272 na imeongezwa mpaka shilingi bilioni 710. Ni ongezeko kubwa, lakini tunatambua kwamba bado kuna mahitaji zaidi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kadri pesa zinavyopatikana Serikali inatambua umuhimu wa barabara hizi za TARURA na hasa kwa sababu zinagusa ustawi wa wananchi lakini pia zinagusa ustawi wa uchumi. Kwa hiyo, kwa kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana Serikali ina nia ya kuhakikisha barabara hizi zinajengwa na zinafanyiwa ukarabati. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi huu ulikusudiwa uanze tangu mwaka 2016 lakini mpaka sasa hivi taratibu zimechelewa kama alivyojibu kwenye majibu ya msingi. Je, ni lini mradi huu utaanza? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, vijiji vinavyonufaika na mradi huo wa Mbunyu, Chiwata na Chidya, vitanufaikaje kutokana na mradi huo utakapoanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la kwanza, naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyosema katika majibu ya swali la msingi, sasa hivi off-takers wale wanunuzi wa hiyo graphite ambayo ni kati ya madini mkakati yanayohitajika sasa hivi duniani kwa utengenezaji wa battery na vifaa vya magari yasiyotumia mafuta, yanatumia umeme, ni kwamba wamepatikana wawekezaji hao kutoka Marekani na kutoka Ulaya na wako katika hatua za mwisho ili uzalishaji uendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa swali lake la pili, faida za mradi huu utakapoanza ni nyingi, kwanza ninawapongeza hawa ndugu zetu wa Volt Graphite kwa sababu hata kabla mradi huu haujaanza, katika upande wa kutoa mchango kwa jamii, wameshachangia fedha katika ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Kijiji cha Nangwale, lakini pia wanachangia posho za walimu wawili wa kujitolea katika shule iliyoko katika kijiji hicho kama sehemu ya kuonesha dhamira yao njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia wameanzisha ofisi mbili katika Kijiji hicho cha Nangwale na Chiwata ambazo zinadumisha mahusiano na jamii ile. Ila watakapoanza kanuni zetu zinawataka kupitia kanuni za uwajibikaji na ushiriki wa Watanzania (local content) watoe ajira na wawaruhusu wenyeji na Watanzania kutoa huduma zote muhimu ambazo wanaweza kuzitoa pamoja na CSR sasa ambao wameanza kutoa kabla ya mradi kuanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mradi huu utakuwa na manufaa makubwa na ninawaasa wananchi wa maeneo hayo ya Mradi wa Mbunyu wakae mkao wa kutoa ushirikiano katika kampuni hii ambapo itakapoanza uzalishaji, matunda yake yatasambaa katika jamii husika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwanza naomba kuishukuru sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa kulipa fidia wananchi wa Nanyamba, Maranje na pia kwa kupeleka fedha shilingi bilioni 7.5 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi. Nina swali dogo tu moja la nyongeza.
Kwa kuwa sasa mradi huo umeanza kutekelezwa na wanawake wa Mkoa wa Mtwara wakiwemo wanawake wa Tandahimba, Newala na Mtwara Vijijini yenyewe ndio wanaobangua korosho kwa sasa kwa kutumia mashine ndogo ndogo.
Je, Serikali imeweka mpango gani wa kuhakikisha hao wanawake wabanguaji wanaotambulika tayari waingie kwenye huo mfumo mara hiyo kongani inapoanza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Agnes Hokororo kwa kuwatetea wanawake katika mkoa wake na hususani maeneo ya Tandahimba, Mtwara na Newala. Nimthibitishie tu kwamba wanawake wote wanaotokea maeneo yanayozalisha korosho ndio watakaokuwa sehemu ya wanufaika wa mradi huu. Katika mradi ule kuna maeneo ambayo tutatenga ili na wao waweze kuwa sehemu ya mradi huo kwa sababu tunahitaji na wao kuongezewa thamani ya korosho pamoja na kupata kipato, ahsante.(Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; kwa kuwa vituo vingi wa afya vinajengwa kwa shilingi milioni 500 na hapo inaonekana halmashauri imetenga shilingi milioni 250 ambayo haina uhakika. Je, ni nini commitment ya Serikali?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Kata ambazo zinazunguka hiyo Kata ya Namwanga ni Nanjota, Mijelejele, Mpindimbi na Mkululu ambavyo kwa sasa vinapata huduma kwenye Kituo cha Afya cha mbali takriban kilometa 40. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha wananchi wa kata hizo zote nne wanapata huduma za afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ujenzi wa vituo hivi unakwenda kwa awamu; tumeanza Awamu ya Kwanza kwa shilingi milioni 250 na commitment ya Serikali ni kwamba shilingi milioni 250 nyingine itapelekwa mapema baada ya ukamilishaji wa Awamu ya Kwanza shilingi milioni 250 ili kufanya Shilingi Milioni 500.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na Kata hizi za Nanjota na nyingine ambazo wananchi wanalazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma, Kituo hiki cha Afya kwanza kita-serve purpose kama Satellite Health Center kwenye maeneo hayo, lakini tutaendelea pia kufanya tathmini ya uwezekano wa kuongeza vituo vya afya kwenye maeneo yetu kimkakati kwa kadri ya mwongozo na Sera yetu. Ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa ujenzi wa bandari kavu ilikuwa ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Mheshimiwa Mkapa na kwa kuwa Serikali imesema haijakidhi vigezo, je, Serikali iko tayari kwenda kuwaelezea wananchi ili sasa wazo hilo lifutwe kwenye mawazo yao kwa sababu walikuwa wanasubiria?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, lengo hasa ilikuwa kuongeza uchumi kupitia shughuli za usafirishaji wa mizigo hasa kutoka Bandari ya Mtwara na kupitia Daraja la Mtambaswala lile la Umoja, je, Serikali inafikiria shughuli gani sasa ili kuweka shughuli mbadala katika lengo la awali?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mhata na Mheshimiwa Hokororo kwa maana ya swali lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapojenga bandari kavu vipo vitu unavyovitazama na kikubwa tunaangalia shehena na ndio maana kwa sasa hivi ninapozungumza, Serikali ya Awamu ya Sita inajenga reli kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma, inaunganisha mpaka Burundi, lakini pia inajenga reli kuelekea Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ushoroba huu kilometa 2,300 tunajenga Bandari Kavu ya Kurasini, Bandari Kavu ya hapa Ihumwa - Dodoma, Bandari Kavu ya Fela kule Mwanza na Katosho, Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua ya pili tukishatoka kwenye upande huu wa central corridor kwa maana ya CSGR Serikali inaendelea na mchakato kwa ajili ya kujenga reli ya kusini inayotoka kwenye bandari yetu ya Mtwara pamoja na Kisiwa Mgao, inaunganisha kwenda Liganga na Mchuchuma ambako kuna madini pamoja na makaa ya mawe, lakini inakwenda mpaka Mbamba Bay ambayo tayari ninavyozungumza mjenzi wa Bandari ya Bamba Bay yupo site. Sasa hii Bandari Kavu ya Nang’omba itakuwa ni bandari muhimu tukishafika hatua hiyo ili tutoe mzigo bandari tuupeleke Msumbiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutauingiza katika mchakato huu wa southern corridor kuhakikisha kwamba na yenyewe inakuwa sehemu ya mradi wetu wa reli hiyo.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, je, katika hayo mabwawa 100, upo uwezekano wa kujenga bwawa moja kubwa kutokana na Bonde la Mto Lukuledi ambalo pia limekuwa likisababisha madhara katika Mkoa wa Lindi na Mtwara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni kwamba Bonde la Mto Lukuledi ni miongoni mwa maeneo ambayo yapo katika mpango. Hayo mabwawa 100 ni mabwawa yote nchini katika maeneo yote nchi nzima, yaani hakuna mkoa ambao tumeuacha katika maelekezo haya ambayo tunakwenda kuyatekeleza. Ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kumwuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa, majengo hayo yameanza kutumika na amekiri kwamba chuo ni kipya, je, Wizara ina mpango gani wa kuongeza fani zinazofundishwa katika Chuo cha Ufundi VETA – Chikundi hasa zitakazowajumuisha vijana wa kike ikiwemo upishi na ushonaji?
(b) Wizara ina mpango gani wa kuongeza majengo kwa ajili ya watumishi ili iendane na mafunzo yanatolewa na idadi ya watumishi ili waweze kufanya kazi zao vizuri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hokororo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoshasema kwenye majibu ya swali la msingi kwamba Chuo hiki kimeishafunguliwa na majengo yote yanatumika, nianze kwanza na swali la fani. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu chuo hiki ndiyo kwanza tumefungua na tunajua kwamba kuna mahitaji ambayo yanahitajika yakiwemo walimu. Kwa hiyo, nimwondoe hofu kwamba fani hizi zitakuwa zinaendelea kuongezeka kwa kadri mahitaji ya vifaa pamoja na wataalamu kwa maana ya walimu tutakapokuwa tunawapeleka pale, basi fani zitakuwa zinaendelea kuongezeka na tumesema fani ziendane na shughuli za kiuchumi eneo lile ambalo chuo hiki kimejengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa eneo la pili kuhusiana na uongezaji wa miundombinu kwa maana ya majengo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba vyuo hivi vimejengwa 25 katika awamu ya kwanza katika Wilaya pamoja na Mikoa Minne na tunajenga kwa awamu. Kwa hiyo, awamu ya kwanza ilikuwa tujenge majengo ambayo yatawezesha chuo kuanza kutoa mafunzo, lakini awamu ya pili itakuwa sasa ni kuongeza miundombinu ikiwemo na nyumba za watumishi pamoja na miundombinu mingine ambayo itakuwa inahitajika kwa ajili ya kutoa mafunzo kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo niwaondoe wasiwasi, siyo tu hapa Chikundi lakini kwa vile vyuo vyote 25 ambavyo tumejenga na vile vinne vya mikoa na hivi sasa Mheshimiwa Rais ameishatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 64 katika Wilaya 64 na Chuo kimoja cha Mkoa kule Songwe, tunaendelea na ujenzi huo na unakwenda kwa awamu, nakushukuru.(Makofi)