Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kasalali Emmanuel Mageni (24 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na afya njema na kuniwezesha kufika hapa nilipofika. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuzungumza kwenye Bunge hili, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Sumve kwa ushindi mkubwa waliokipatia Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi uliopita. Nikishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kunipitisha na kunisimamia na kuhakikisha nashinda kwa kishindo katika uchaguzi uliopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika hoja iliyoko Mezani. Katika Nchi ya Tanzania, baada ya mimi kuangalia hizi hotuba, hotuba ya Mheshimiwa Rais ya kulifungua Bunge na nimepitia hotuba ya mwaka 2015 aliyoitoa wakati akilifunga Bunge la Kumi na Moja, nimeona kwamba Nchi yetu ya Tanzania inayo bahati kubwa. Tumempata Rais ambaye anayo maono, tumempata Rais ambaye ana nia ya dhati ya kulitumikia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa la Tanzania ni moja ya mataifa machache yenye bahati ya kuwapata viongozi wa aina ya Dkt. John Pombe Magufuli. Ukiangalia mipango yote na namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga na ilivyokuwa imejipanga katika kipindi cha kwanza na ilivyojipanga katika kipindi cha pili, unayaona matumaini ya Tanzania itakayokuwa ni nchi yenye uchumi mkubwa. Kwa hiyo ninayo sababu ya msingi ya kujivunia kwamba Watanzania tunaye Rais mwema, mwenye maono na ambaye anataka kutuvusha, anataka twende sehemu ambayo wote tumekuwa tukitamani kufika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengi yamefanywa na Serikali yetu, tunaweza tukazungumza hapa lakini muda usitoshe. Nitajaribu kuzungumza machache ambayo yamefanyika na kushauri nini tufanye vizuri zaidi. Serikali ya Awamu ya Tano katika jambo kubwa ambalo imelifanya ambalo dunia nzima inaona na tunajivunia ni kuhakikisha inasimamia vizuri uzembe, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu imeweka utaratibu kuanzia Mheshimiwa Rais akisimama, ukiwaona Mawaziri wake wamesimama, wote wanakemea namna yoyote ya uzembe, namna yoyote ya ubadhirifu na ufisadi wa mali za umma. Serikali ya Awamu ya Tano imefanya vizuri sana kwenye jambo hilo; majizi, mafisadi wameshughulikiwa vizuri na kila namna ambayo Serikali imeona inaweza kufanya kuhakikisha mali zetu, mapato yetu tunayoyakusanya yanakuwa salama, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya vizuri sana na matunda tumeyaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye ukusanyaji wa mapato kupitia TRA na halmashauri zetu, tumefika kiwango cha kuongeza mapato ya mwezi kutoka bilioni 800 mpaka mwezi uliopita tumeweka rekodi ya kukusanya trilioni mbili, mwezi Desemba; Serikali imefanya vizuri sana kwenye hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini yapo mambo ambayo yanahitaji kuangaliwa kwa undani zaidi. Katika kusimamia ubadhirifu wa mali za umma na matumizi mabaya ya fedha za Serikali, Serikali yetu katika kiwango cha Kitaifa, katika taasisi zilizoko karibu na Serikali kama maeneo ya bandari na maeneo mengine tumefanya vizuri sana. Hata hivyo, kwenye maeneo ya chini, kama kwenye Halmashauri za Wilaya kazi kubwa inahitajika kufanyika. Fedha nyingi za matumizi zinazopelekwa kwenye Halmashauri zetu hazitumiki inavyotakiwa. Bado kuna miradi hewa, kuna usimamizi mbovu wa fedha na fedha nyingi zinapotea. Hata viwango vya majengo na miradi inayosimamiwa na Halmashauri zetu hazijafikia viwango vinavyotakiwa. Kwa hiyo, Wizara husika, ambayo ni TAMISEMI, wanatakiwa kuziangalia Halmashauri kwa jicho la pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya vizuri sana kwenye sekta ya kilimo kufufua ushirika na mambo mengine, lakini bado kuna mambo ya kufanya kwenye ushirika. Naweza nikakupa mfano, katika Wilaya yetu ya Kwimba kuna shida kubwa sana sasa hivi inaendelea. Kuna mazao ambayo Serikali imeyaweka kusimamiwa na ushirika ambayo kiuhalisia hayakupaswa kusimamiwa na ushirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna zao la choroko na mazao mengine kama ufuta, yamewekwa kwenye ushirika lakini mazao haya siyo kama mazao mengine yaliyoko kwenye ushirika kama pamba. Mazao haya ni ya chakula, ni mazao ambayo uuzaji na usimamizi wake unapaswa uwe wa kawaida na usitegemee AMCOS na ushirika. Katika Wilaya Kwimba, moja ya jambo ambalo linatutesa sasa hivi ni mazao yetu ya choroko kupelekwa kwenye ushirika na tunalazimishwa mazao ambayo ni ya chakula, mazao ambayo sisi muda wote tunayategemea, tukitaka kuuziana ni lazima twende kwenye AMCOS.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niiombe Serikali kwamba umefika wakati wa kuangalia ushirika wetu. Tumeuimarisha ushirika, unafanya vizuri lakini tunauongezea majukumu ambayo ni magumu kuyafanya. Moja ya jukumu ambalo ushirika unapata shida kulifanya ni hili la ununuzi wa choroko, dengu na mazao mengine ambayo ni mazao yetu ya chakula na biashara, kuna wakati tunahitaji kuyatumia kama mazao ya chakula. Mimi siwezi kuhitaji kununua choroko ikabidi niende kununua AMCOS, nitanunua kwa mtu mwenye choroko. Naomba sana katika suala hili Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ione namna ya kuhakikisha mazao yaliyoongezwa kwenye ushirika yanarudishwa, tunaanza kuyanunua kwa njia zetu za kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naomba niunge mkono hoja ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na afya. Pia nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia nafasi za ajiri zaidi ya 21,000 ni jambo jema na ni jambo la kupewa heshima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene kwa nafasi hii aliyopewa na kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika Wizara mbalimbali alizopita na ninaamini Wizara hii imepata mtu sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Naibu wa Waziri Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, amekuwa ni msaada na kiongozi wa kujituma. Hongera sana Mheshimiwa Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wengine walivyotangulia kumpongeza Mheshimiwa Jenista Mhagama, Seneta, Waziri mzoefu, mwenye heshima, na anayejituma kufanya kazi yake vizuri; Mheshimiwa Waziri, hongera sana kwa njia uliyoiacha kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kabla sijaenda mbali, naunga mkono bajeti, kwa sababu naamini watu ninaoenda kuwashauri, watanisikiliza na watafanyia kazi ushauri wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia, nataka nitoe takwimu halisi za upungufu wa watumishi kwenye Jimbo la Sumve. Jimbo la Sumve hivi ninavyozungumza ni moja ya majimbo ambayo yako vijijini kwa asilimia mia moja. Ni majimbo ambayo yanakumbana na watumishi kupangiwa kazi na kuanza kuomba uhamisho siku wameanza kazi. Majimbo haya yanatakiwa yaangaliwe kwa jicho la pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Sumve ninavyozungumza sasa hivi, tuna upungufu wa walimu wa shule za msingi zaidi ya 1,311, lakini walimu wa shule za sekondari zaidi ya 318. Kwenye Jimbo la Sumve, kuna shule kama Nyang’ingi, shule nzima ina walimu watano. Kuna shule kama Bukala, shule nzima ina walimu saba. Hali ya upatikanaji ya watumishi ni mbaya kwenye maeneo ya vijijini. Serikali bado ina kazi kubwa ya kufanya kwenye sekta hii ya utumishi. Bado tuna upungufu mkubwa wa watumishi, kwa hiyo tunaomba Wizara iliangalie hili kwa jicho la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichangie kama ambavyo wengi wamesema kuhusu mfumo wetu wa ajira. Niliwahi kusema hapa na wengine wamesema. Tunalo tatizo kubwa sasa hivi kwenye nchi yetu la wananchi kupoteza imani na mfumo wetu wa ajira Serikalini; na Wabunge wote wamesema humu. Tunazo meseji mpaka zimejaa kwenye simu, za watu kuomba tuwasaidie kupata kazi Serikalini. Watu wamehamisha imani kwa Wabunge, wameondoa imani kwenye Mfumo wa Serikali wa Ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi tunaowaongoza, wana akili na wanajiongeza. Wanajiongeza kutokana na wanayoyaona. Mfumo wetu wa ajira umekuwa ni mfumo wenye usiri mkubwa sana. Watu wanaomba kwenye Tume ya Ajira; sijui kuna kitu kinaitwa sijui kanzidata na story nyingine nyingi. Watu wanamwambia mtu ameomba, aliyekosa amewekwa kwenye kanzidata, mwingine amepewa ajira. Baadaye tena ajira ile ile hawatumii tena kanzidata kumpa ajira huyu waliyemweka, wanatangaza tena ajira nyingine kwenye jambo lile lile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamefika wakati wamegundua kwamba mfumo wa ajira ni wa dili. Sasa kama kweli mfumo wa ajira ni wa dili, ni hatari sana. Tutakuwa tunapokea Ripoti za CAG hapa, watu wametushangaza, kwa sababu wameingia kwa dili. Kwa hiyo, lazima mfumo huu wa ajira tuuangalie kwa namna nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatari kubwa sasa hivi, leo naongea kwa Wizara ya Utumishi, lakini imani ya wananchi mpaka kwenye mfumo wa ajira kwenye majeshi ni ndogo sana. Yaani wananchi wanatupa ujumbe kwamba huko tuna askari wa dili. Sasa nchi kama tunataka hivi ni lazima tujifikirie, yaani kuna kitu kwenye mfumo wa ajira wananchi wameshaondoa imani. Serikali lazima ijitazame na ijiangalie mara mbili. Wananchi bado hawatuamini. Sasa tunafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kushauri hapa, ajira zikishushwa chini ni rahisi zaidi watu kuwa na imani. Maana watu wamesema hapa, hata ajira hizi kuna maeneo, mimi Mbunge wa Sumve nikikwambia ni wangapi wameajiriwa Sumve, siwezi kusema, maana sijui. Kwa sababu mambo haya yanafanyika juu juu tu. Sasa lazima ifike wakati uwazi uongezeke ili kuwe na mambo yanayoeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira hii siyo kwamba tunafanyia tu siasa. Mfano, leo tunasema kuna mfumo ambao TAMISEMI wamesema hapa, ajira wataangalia watu wa 2015, wengine hawawaangalii. Mtu wa 2015 leo ana miaka minane hafanyi kazi yoyote. Hawana database ya watu wanaojitolea. Watu wanaojitolea wanachukuliwa kama vile hamna wanachokifanya. Sasa kama Serikali yetu haina database ya watu wanaofundisha watoto wetu, inafanya kazi gani? Yaani sisi tumepeleka watoto shuleni, ninyi hamjui wanafundishwa na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanajitolea huko, wanajiandikisha Walimu Wakuu, kila mwezi wanapeleka ripoti ya watu walioko kwenye shule, kwamba nina walimu kiasi kadhaa. Kumbe tunafanya formality, ni mazoea tu, mambo ya kishikaji. Lazima tufike wakati vitu vya msingi tulivyokubaliana vifuatwe. Watu wamejitolea na mnawajua, taarifa za watu wanaojitolea zinajulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishauri Serikali, hizi nafasi zilizotolewa 21,000 tusiwe na haraka nazo sana, ni nyingi sana, tuzitengenezee mfumo mzuri ili watu wote wapate wanaostahili na zije kuwa na tija. Kwani tuna haraka gani? Kwani lazima tuajiri sasa hivi, si Rais ameshatupa. Hebu tulieni, tusikilizeni tuwaambie, kwamba watu wanaojitolea wanajulikana. Story ya kwamba hawajulikani, ni kuidhalilisha Serikali. Walimu Wakuu wanajua hawa watu, na ripoti za kila mwezi kwa Maafisa Elimu zinapelekwa. Leo mnasimama hapa mnatuambia hamuwajui, mnafanya kazi gani sasa hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufike wakati tusimamishe hii ajira ya watu 21,000, tushauriane humu, wote ni watu wazima, tumetumwa na wananchi, tukubaliane nani anaajiriwa, na kwa sifa ipi? Kwa sababu tukiendelea na utaratibu huu, tutaendelea kuwa na watu tu tunaajiri, tunaajiri kwa ajili ya kujifurahisha, lakini watu bora tunawaacha nje, lakini na wananchi wanakosa imani na mfumo wetu wa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nishauri jambo lingine. Kuna jambo hapa linaitwa kikotoo. Serikali iwape watu fedha zao. Mtu amefanya kazi kwa muda mrefu, amepokea mshahara wake, mlikuwa hamumtunzii, ilikuwa hamhusiki chochote na mshahara wake, leo anastaafu zinakuja story kwamba hawezi kutunza hela yake. Wapeni watu hela zao. Wapeni watu hela zao wapambane nazo huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya huko. Kweli kabisa! Humu tunaweza tukakaa tukawa tunafikiri hali ni nzuri; kuhusu wastaafu, wastaafu masikini ni wazee wetu, nasi ni wastaafu watarajiwa, hawariziki na hela yao kutunziwa. Wakitunziwa, hatujui mtu kesho na keshokutwa hayupo, inalipwaje? Tufike wakati mtu apewa hela yake, amefanya kazi kwa heshima kwenye nchi hii, aende akafanye kazi yake vizuri. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kasalali Mageni, kuna taarifa kutoka kwa Waziri, Mheshimiwa Profesa Ndalichako.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nilikuwa naomba nimpe taarifa kaka yangu, Mheshimiwa Kasalali Mageni ambaye ninamheshimu sana, na anachangia mchango mzuri, lakini naomba tu hili jambo lisije likapotoshwa kwamba Serikali inaona watu hawawezi kutunza fedha zao. Fedha ambazo mtu analipwa za mkupuo; na nilishafanya semina hata kwa Wabunge; anapata fedha nyingi kuliko hata zile ambazo amechangia katika miaka yake yote ya utumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokizungumzia mafao ya mkupuo, ni ile pensheni ambayo mtu anaipata ambayo makisio ya umri wa kuishi baada ya kustaafu tumekadiria ni miaka 12 na nusu. Kwa hiyo, tunafanya makisio ya fedha yote ta mtu kustaafu halafu katika fedha ile ndiyo tunampa mkupuo wa asilimia 33. Ni tofauti na kile ambacho mtu anakuwa amechangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona tu kaka yangu amechangia vizuri, nimpe hiyo taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri kwa taarifa, na muda wa mchangiaji umekwisha.

Ninakuongezea dakika moja na nusu ili uweze kuhitimisha hoja yako Mheshimiwa.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Waziri,

Mwalimu wangu, nimepokea taarifa yako. Ila nataka tu kusema, hao wanaolalamika siyo kwamba vichwa vyao vimekatwa, wanaona kwamba jambo hili siyo sawa. Nasi kazi yetu ni kuwaambia kwamba wale wastaafu wanalalamika. Wanapolalamika, ni kwetu. Sasa kama mtu anapewa hela nyingi zaidi halafu bado analalamika, sijui, labda wastaafu wetu wana hali ngumu sana za kufikiri; lakini kama ni kweli zile walizotutumikia mpaka nchi yetu imefika hapa, ukweli ni kwamba wanalalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuone namna ya kuwapa hela zao wachukue wakapambane nazo. Tusiwakadirie umri wa kuishi, kila mmoja Mungu ndio anakadiria umri wetu wa kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninamshukuru Mwalimu wangu wa Measurement and Evaluation, Profesa, nakuheshimu sana, lakini wananchi wanasema kwamba hawaridhiki, wanaomba mbadilishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Kicheko/Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Seriakli za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na uzima, lakini kabla sijazungumza sana naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo anatupelekea pesa nyingi sana za miradi ya maendeleo kwenye majimbo yetu. Pia ninampongeza Rais kwa namna ambavyo amekuwa akipeleka miradi hii kwa asilimia kubwa bila kubagua, hata sasa hivi sisi wa vijijini tumeanza kupata miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaelezea mfano mmoja wa mradi wa ujenzi kwa Kiingereza au tuseme Kisukuma ni Construction of Sports Center of Excellence katika Mji wa Malya katika Jimbo la Sumve. Mheshimiwa Rais alitupatia shilingi bilioni 31 kwa ajili ya mradi huo, Mheshimiwa Rais akiwa anaipokea timu ya Yanga alisisitiza kuhusu mradi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba nimezungumza mradi huo kwa kusudi moja, kila tunapokutana hapa kujadili ripoti ya CAG kazi yetu sisi hapa mara nyingi tumejikuta tukijadili madudu ambayo yamefanywa na watu tuliowaamini kusimamia mambo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya madudu yaliyosemwa na Kamati zote tatu, huwa yanatokana na mchakato, yaani watu huwa wanaanza kuzembea siku ya kwanza, siku ya pili, siku ya tatu mpaka linakuwa dudu, mwisho wa siku inakuwa hoja ya CAG tunakuja kujadili hapa.
Mheshimiwa Spika, nilitamani leo nitumie mradi huu kutengeneza utaratibu na kutengeneza mstari wa kuzuia hoja mpya za CAG. Ninazo documents hapa ambazo nilitamani niziweke mezani ambazo zitasaidia mimi katika kuchangia.

Mheshimiwa Spika, tarehe 06 Julai, 2023 Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, alisaini mkataba na kampuni ya CRJE East Africa wenye thamani ya shilingi bilioni 31 kwa ajili ya kujenga hiyo inaitwa Proposed Construction of Sports Center of Excellence to be building on plot Number 30, 31 and 32 at Malya Kwimba District. Katibu Mkuu akiwa hajafungwa pingu, akiwa na akili timamu na baada ya Serikali kupitia organs zake zote kufanya kila kilichotakiwa kufanyika alisaini huu mkataba.

Mheshimiwa Spika, tarehe 27, siku 21 baada ya kusaini huu mkataba Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela ikamwandikia Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ikimwambia kwamba; “Tunajibu barua yako ya tarehe 02 Juni, 2023 ya kutuomba eneo kwa ajili ya ujenzi wa hii sports…” mimi Kiingereza nilisoma mpaka Chuo Kikuu lakini kinanisumbuwa, yaani hii... (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, elimu yetu huko sisi tumesoma shule za ngumbaru, kwa hiyo… (Makofi)

SPIKA: Sema tu mradi.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, huu mradi wakieleza kwamba tunajibu barua yako ya tarehe 02 Juni, 2023 ya kutuomba eneo kwa ajili ya ujenzi wa huu mradi ambao siku 21 zilizopita Katibu Mkuu ameusaini kuujenga Malya - Sumve na Mheshimiwa Rais aliusema unajengwa Malya Sumve, Mheshimiwa Waziri aliyekuwepo Mchengerwa aliusema na Katibu Mkuu aliyekuwepo Dkt. Abbas alisema, lakini siku 21 baada ya kusaini, Ilemela inajibu barua iliyoandikwa kabla mradi haujasainiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia milolongo hii baadaye kuna barua nimeiweka humu ya consultant, Kampuni ya ABE, akimuandikia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo akimwambia kwamba; Ninarejea barua yako ya Tarehe 07 Septemba ya kuniomba ushauri kuhusu kubadilisha eneo la mradi. Yaani wameomba eneo kabla hata consultant hawajamshirikisha. Baada ya kuomba eneo na wameshasaini mkataba, wanamuomba consultant sasa awashauri. Consultant yeye hakukaa muda na hiyo barua, alikaa nayo kama siku tano akawaambia hili jambo haliwezekani, hili jambo mnaenda kuongeza gharama ya mradi, kubadilisha site ni ku-complicate mradi.. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, movement zote hizi zisizofuata utaratibu ndizo huwa zinazaa hoja za CAG, watu wanawekwa kwenye ofisi za Serikali badala ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, alichowaambia wakafanye, wanaenda kufanya wanayofikiria kichwani kwao.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amewaambia wapiga kura wake wa Sumve kwenye TV live kwamba tunajenga Malya, Serikali imesaini, mradi umeanza, Wizara ipo serious kuhamisha mradi huu kuliko walivyo serious kuhakikisha tunashiriki Kombe la Afrika. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nimeongea na Mheshimiwa Waziri kwa simu, nimeongea na Naibu Waziri na Katibu Mkuu wababe vibaya, wanazingua. Watu wa Sumve wanataka kuhamishiwa mradi wao majibu yao ni kwamba eti sisi tunakaa kijijini, mradi kama huu hauwezi kwenda kijijini. Malya kuna Chuo cha Michezo cha muda mrefu, unajenga chuo cha michezo bila kuweka shule ya mazoezi, ile ni shule ya mazoezi na Mheshimiwa Rais alitumia akili kuweka ule mradi, lakini wapo busy kuuhamisha. Wanaangaika na consultant aongeze gharama za mradi ilimradi watu wa Sumve wakose mradi waupeleke Ilemela. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kule Sumve, mimi naingia kwenye kashfa kwa ajili ya hawa jamaa…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, ninaanza kuonekana kwamba lile eneo la Ilemela ni eneo la Kasalali, ameuza, anatafuta hela za kampeni! Watu lazima waseme pembeni, kwa nini mradi uhamishwe kihuni namna hii!

SPIKA: Mheshimiwa Kasalali, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam.

TAARIFA

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nampa taarifa msemaji kwamba mradi huo kuhamishwa kwake tu, kupelekwa Ilemela unahitaji uongezewe shilingi bilioni 13! Yaani ni upigaji wa dhahiri wa mchana kweupe. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Kasalali Mageni, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa mikono miwili, na nilikuwa hapa busy natafuta ukubwa wa eneo la Malya.

Mheshimiwa Spika, eneo ambalo sasa mradi unatakiwa uhamishwe lina square meter zaidi ya 100,000, unakopelekwa ni square meter 67,000 yaani haliruhusu hata uendelezaji.

Mheshimiwa Spika, Kamati yako ya Bunge inayoshughulika na mambo haya ilikuja mpaka Sumve na ikaona mradi huu una maana na ikatuambia kwamba tuendelee, ikaiambia Serikali mnafanya vizuri endeleeni, leo Kamati ya Bunge inataka ionekane imesema uwongo kwa sababu kuna Waziri tu jeuri anataka awaoneshe yeye ni jeuri, anajua kufanya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuendelea namna hii, Kamati ya Bunge imekuja, Mheshimiwa Rais amesema, Mheshimiwa Waziri aliyekuwepo na Katibu Mkuu wamesema na sisi Wabunge tumezunguka tunawaambia watu kwamba hiki kinafanyika, halafu mtu mmoja anakuja anasema kule ni kijijini, hawawezi kuwekewa mradi, ifike wakati muelewe nchi hii tuna usawa, watu wa Sumve hatuna lami sawa, hatuna hata milimita moja ya lami sawa, tumekubali. Maji ya Ziwa Victoria yapo Mwanza lakini Sumve hayajafika, sawa tumekubali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna Kituo cha Michezo na chenyewe mnakipeleka Ilemela, this is not fair, haiwezekani! Kwa utashi wa mtu mmoja wanajifanya hapa wanashauriana na consultant, sijui kulikuwa kuna consultation team na nini, ni ujanja ujanja tu huu. Ndiyo mambo aliyokuwa anasema Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anapokea Ripoti ya Ardhi Mwanza. Barua zina backdate watu wana-backdate barua ili kuweka mambo yasiyoeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naunga mkono hoja za Kamati zote tatu na naomba niongeze Azimio la kwamba hawa wanaotaka kuhamisha miradi na kutengeneza hoja za CAG, washughulikiwe kama wahalifu wengine na nipo tayari kuonesha ushirikiano kwenye hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, naomba kushukuru. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. KASASALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na uzima. Niwashukuru vile vile wapiga kura wa Jimbo la Sumve kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakinionesha tangu nichaguliwe kuwa Mbunge wao katika kutekeleza majukumu ya kuleteana maendeleo na kuisimamia Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajielekeza katika hoja yangu, naomba nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa sana ambayo ameifanya na anaendelea kuifanya kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizi sisi watu wa Jimbo la Sumve, Mbunge wa Sumve anaposimama na kupongeza, anapongeza kwa mifano ambayo ipo bayana. Tangu Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, sisi watu wa Sumve alitukuta tunazo zahanati 21 tu, lakini leo ninapozungumza, zahanati 10 ndani ya mwaka mmoja, yaani ninapozungumza zahanati 21 nazungumza tangu uhuru, lakini ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan, watu wa Kijiji cha Mwashilalage, Zahanati; Kijiji cha Bung’egeja, zahanati; Kijiji cha Nyamikoma, Zahanati inaanza kujengwa; Kijiji cha Busule, Zahanati; na Kijiji cha Kinamweli, Zahanati. Naweza kuzungumza hapa vijiji vingi lakini ndani yam waka mmoja kwa hiyo tunaposema Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa nadhani ni kazi ambazo zinaonekana kwa urahisi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge wa wakulima na wafugaji, katika Jimbo la Sumve tunalima pamba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametukuta tunauza pamba kwa Shilingi 800 lakini mwaka jana tumeuza pamba kwa bei ya juu kabisa ya 1,500 lakini sasa hivi pamba tunaendelea kuiuza kwa bei ya Shilingi 2,000. Kwa hiyo tunaposema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imetusaidia wakulima mifano inaonekana na ni bayana, ndiyo maana naona kwamba nikisimama hapa nikaacha kupongeza nitakuwa sijawatendea haki watu wa Sumve. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba sasa na mimi nielekee kwenye kushauri katika bajeti ambayo Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ametusomea humu bajeti ya Serikali yetu pendwa ya CCM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tunatakiwa sisi ambao wenzetu hawa ambao mmepewa kazi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika Wizara mbalimbali mnatakiwa mtumie muda mwingi kujifunza namna ambavyo Mheshimiwa Rais anavyotaka nchi iende. Mheshimiwa Rais ametuonyesha kwenye TARURA kwamba anataka kila eneo lipate kwa usawa. Wabunge ni mashahidi kwenye Majimbo yetu, Mheshimiwa Rais alipoingia tu alitupatia Milioni 500 kila Jimbo akiwa na maana kwamba hii nchi ni moja, watu wote wapate maendeleo kwa usawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye fedha maarufu za Mama Samia ambazo tulikopa Mama ametupatia kwa usawa kila Jimbo linajenga madarasa watu wanaona, kwa hiyo tunatakiwa sasa na maeneo mengine mfahamu nia ya Mheshimiwa Rais kupitia mifano hii. Katika sekta ya umeme sote tunaona nchi nzima vijiji vyote vinawekewa umeme, Mama anataka nchi iende kwa usawa. Sasa ipo shida moja kwenye eneo la miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi hii kuna maeneo ambayo yanabandua lami yanaweka mpya na kuna maeneo ambayo hayana hata milimita moja ya lami. Katika jumbo la Sumve ambalo mimi ninatoka, ambalo ninadhani wote tukipitishana kwenye historia ya nchi yetu Jimbo la Sumve liko kwenye Wilaya ya Kwimba, Wilaya ya Kwimba ni moja ya Wilaya ambazo zimeachwa ni Wilaya ambazo zilianzishwa kabla hata hatujapata uhuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Nyanza Province kulikuwa na Wilaya ya Mwanza, Wilaya ya Kwimba, Wilaya ya Maswa, Wilaya ya Musoma, Wilaya ya Shinyanga, Wilaya ya Kahama na Wilaya ya Bukoba, baada ya Nyanza Province kutoka ukaja Mkoa wa Mwanza Wilaya Nne za kwanza Kwimba imo, Kwimba Mwanza Geita na Ukerewe lakini baada ya Geita kutoka Wilaya Kwimba bado ipo na Jimbo lake la Sumve imezaa Wilaya ya Misungwi, Wilaya ya Misungwi ina lami, imezaa Wilaya ya Magu, Makao Mkuu ya Magu na Mkoa wa Mwanza na Mikoa mingine imeunganishwa na lami, tukazaa mjukuu Busega ameunganishwa na lami. Sasa Kwimba tunashida gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri wa Fedha, naiomba sana Serikali ya CCM igawe maendeleo kwa usawa hasa kwenye sekta ya barabara. Haiwezekani kila siku tangu Rais Mkapa alisimama akatuahidi watu wa Kwimba na sisi tutapata lami haikufanikiwa, akaja Rais Kikwete akatuahidi haikufanikiwa, akaja Hayati Magufuli akatuahidi haikufanikiwa! Hapa sasa hivi tuna amani Rais Samia ameonesha dhahiri anataka nchi iende kwa usawa. Sasa nimepitia hii bajeti bado mnaonekana hamko serious kwenye jambo la barabara kwenye baadhi ya maeneo hasa Jimbo ninalotoka la Sumve.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Sumve tulikuwa tukiimba wimbo wetu hapa kuanzia bajeti iliyopita tunataka walau basi kwenye bajeti na sisi mtuone mtujengee barabara yetu ya kimkakati na ya muhimu inayoanzia Magu inapita Bukwimba inaenda Ngudu mpaka Hungumalwa, barabara yenye urefu wa kilimeta 71 katika bajeti iliyopita Serikali ikatupangia kutujengea kilomita 10 hawajajenga hata milimita moja, katika bajeti hii ndiyo sioni kabisa hata mwelekeo, sasa tukienda namna hii nchi yetu tutakuwa tunapendelea baadhi ya maeneo na kutekeleza baadhi ya maeneo,.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufike wakati tufahamu kwamba ili maendeleo yafaidishe watu wetu lazima kuwe na usawa kwenye ugawanaji wa keki ya Taifa, haiwezekani wenzetu wanabandua lami sisi hatuijui, ukichukua mtoto wa Sumve ukamwambia neno lami hajui! Ninaposema hapa mnaweza mkawa hamnielewi kwa sababu ninyi wengi mnalami kwenu lakini Sumve hatuna hata milimita moja ya lami. Baada ya miaka yote hii ya uhuru sasa tufike wakati tuweke mstari na sisi sasa muda wetu umefika, eleweni Mheshimiwa Rais anataka watu wote wapate haki, watu wote wagawiwe keki hii kwa usawa, twendeni mtugawie kwa usawa zipo barabara za muhimu sana kwenyeJimbo letu, katika Serengeti ya Kusini…

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

T A A R I F A

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri sana wa Mheshimiwa Mbunge makini, jambo hili ni jambo ambalo haliwezi kuachwa liendelee hivi. Wengine tulioko Kaskazini tunazungukwa na Wilaya zenye lami na zingine ndiyo hizo ambazo ni bandika bandua imefika wakati wale ambao wanapata barabara za lami sasa hata za zamani wasimame tupate lami wengine ili na wao waweze kupata na wale walipata kupitia TANROADS wasipewe barabara nyingine kupitia TARURA mpaka Watanzania wengine tuwe tumepata lami, tumeahidiwa haitekelezwi! Ahsante.(Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mageni taarifa hiyo unaipokea.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa naipokea kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema kwamba tugawiwe kwa usawa nafikiri tunatakiwa tufike wakati tuelewane, Mheshimiwa Mwigulu na wewe unatoka Iramba huko angalau labda ninyi mmeungwa kwa lami, lakini tuelewe kwamba watu wetu wanahitaji maendeleo, tunapotaka utalii ukue Serengeti Kusini kote mimi nilikuwa juzi Mwandoya wananchi wanachukia Tembo, wanachukia mbuga za Wanyama kuliko kitu chochote, kwa sababu hawafaidiki nazo. Barabara za msingi zinazotakiwa kupeleka watalii waende mpaka Meatu, waende kwenye maeneo ya utalii ya Serengeti ya Kusini zote ni za vumbi! Barabara inayotakiwa kutoka Mwanza ikaja ikapita Fulo, ikaenda ikapita Sumve, ikaenda ikapita Nyambiti, ikaenda Malya mpaka Maswa, barabara hii imekuwa ni story na barabara ya kujazwa ukurasa wa Ilani inaandikwa kila siku, haijengwi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tufike wakati jamani kama alivyosema Mheshimiwa Ole-Sendeka waliopata wasimame, Mheshimiwa Waziri angalia hii bajeti yako haiwezekani sisi watu wa Sumve tukawa tunakuja kukusindikiza humu, tunasindikiza wengine wanawekewa lami sisi tuko tu hapa tunapiga makofi, wananchi wa Sumve wameniambia nisipige makofi kwenye mambo ya hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitapiga makofi kwenye mambo ya hivi, haiwezekani sisi tukasindikiza watu tukabaki kuwa watazamaji wa lami za watu. Inafika wakati mimi wakati kwa historia mwaka 2000 kuna binti anatusaidia nyumbani, Mimi naenda Shinyanga nikapanda naye basi nilipofika eneo ambapo kuna lami, kwenye eneo la Mabuki pale, yule mtoto akaniambia Kaka hivi kumbe barabara za huku zimewekewa cement yaani haelewi lami na cement anaonaga ndani sasa ifike wakati muwakumbuke hawa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi ni ya kwetu sote tunataka maendeleo, msisitizo wangu ni kwamba maendeleo na keki ya Taifa tuigawane kwa usawa. Nakushukuru sana. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na uzima lakini pia nitumie fursa hii kutoa pole kwa Watanzania na mimi mwenyewe kufuatia kifo cha Rais wetu wa Awamu ya Tano Rais wetu aliyekuwa amejikita kwenye kuhakikisha anatuletea maendeleo ya kweli Watanzania Hayati Dkt John Pombe Magufuli tunamuombea huko aliko apate pumziko jema na sisi tulioko huku tuendelee kuchapa kazi ili kutimiza malengo waliyonayo Watanzania na matumaini waliyonayo na Serikali yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan na Makamu wake na Serikali yote na niwakaribishe katika kuchapa kazi sisi tupo tutaungana nao na tutawaunga mkono kuhakikisha kazi ina kwenda ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika mpango wa bajeti ambao umewasilishwa leo Bungeni hapa. Ukiangalia Mpango huu unaona yapo matumaini ndiyo maana naanza kwa kuunga mkono lakini yapo mambo ya kuzingatia ambayo nilitaka tuyazungumze kidogo kwenye Bunge lako.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusu mambo ya vijijini kwasababu ni moja ya Wabunge wenye Majimbo ya vijijini, huko vijijini asilimia kubwa ya watu ni wakulima na sekta ya kilimo imekuwa ni uti wa mgongo wa Taifa letu lakini sisi kule kijijini ndiyo Maisha yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupitia Bunge lako niiombe Serikali katika sekta ya kilimo mnatakiwa sasa ifike tuanze kuwekeza katika kuboresha sekta hii kuanzia kwenye uzalishaji. Kumekuwa na utaratibu ambao umekuwa ukinishtua nadhani kwenye kikao kilichopita nilisema wakulima wakati tunazalisha mazao yetu Serikali imekuwa ikikaa kimya ikituangalia inapofika wakati wa kuvuna mazao yetu unaanza kuona vitu vinaitwa AMCOS unaanza kuona vitu vinaitwa Stakabadhi Ghalani, unaanza kuona usimamizi ambao si rafiki kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo la Sumve tunalima mazao ya jamii ya kunde hizi choroko na dengu ni mazao ambayo sisi wakulima tunayalima kwa nguvu zetu wenyewe hatujawahi kuona mbegu kutoka Serikalini, hatujawahi kuona dawa kutoka Serikalini, hatujawahi kuona Afisa Ugani kutoka Serikalini lakini inapofika wakati wa kuyauza unaanza kuona kuna watu wanaitwa AMCOS, kuna watu wanaitwa Ushirika wanakuja kusimamia mazao ambayo tumeyalima sisi wenyewe kwa nguvu zetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zaidi wanaleta utaratibu wa hovyo utaratibu ambao hautusaidii bei zimeshuka sasa hivi ukienda kwenye maeneo ambayo yanalima hizi choroko na dengu tunakaribia kuanza kuuza choroko soko lake limeporomoka kwa wakulima. Wakulima wameshindwa kabisa kufaidika kwa hiyo, naomba Serikali muwekeze zaidi kwenye uzalishaji kabla hamjaamua kuwekeza kwenye kutupangia namna ya kuuza mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni lazima mliangalie kwa undani hamuwezi kuweka mazao yote kwenye kapu moja zao kama choroko na dengu huwezi kulifananisha na korosho. Dengu sisi na choroko Wasukuma ni zao la chakula na biashara kuna mtu anahitaji kwenda kununua dengu sokoni akapike atumie lakini wewe umemwambia ili aziuze lazima apeleke AMCOS.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu amezungumza hapa Mheshimiwa Tabasamu kuhusu zao la pamba, ni Mbunge ninayetoka kwenye jimbo la wakulima wa pamba. Wilaya ya Kwimba ni moja ya wilaya ambazo zinazalisha pamba kwa wingi kuliko zote kwenye Mkoa wa Mwanza zao la pamba niwaambie kabisa Serikali mmeshiriki kuliua na mnaendelea kushiriki kupitia namna ambavyo mnasimamia masoko yake. Wakulima wengi wa Tanzania tunalima hatujui hata kama tunapata faida au hasara huwa tunalima tu lakini ukifanya hesabu asilimia kubwa tunapata hasara. Lakini bado Serikali kwenye kusimamia bei za mazao bado haijaonekana kwamba tuko serious kwasababu tunapeleka watu kwenda kusimamia vitu wasivyovijua.

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la pamba asilimia kubwa linasimamiwa na watu wasiolijua na limeingiliwa amesema Mheshimiwa Tabasamu hapa hawa siyo wawekezaji ni mabeberu ni watu ambao wanakwenda kumdidimiza mkulima. Kwa hiyo, ni lazima Serikali muangalie Mheshimiwa Waziri wa Fedha muone namna ambavyo mtalifufua zao la pamba kwasababu tunataka viwanda, viwanda vinatoka wapi kama mazao tunayaua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini huko vijijini kwetu ambako ndiko tunakozalisha mazao haya ya chakula ambayo watu wa mjini wanatumia lakini ndiko nguvu kazi nyingi iko kule, bado tunazo changamoto za miundombinu. Katika mpango wa bajeti nimeona tunazungumza kuhusu miundombinu mikubwa mikubwa kama reli ya kati tunazungumza madaraja lakini pia sisi kule site vijijini kuna miundombinu ya kwetu ya kawaida kabisa mabarabara ya vijijini kupitia TARURA bado hali vijijini si nzuri barabara za Dar es Salaam zisipopitika utaona watu wamepiga picha zimeonekana kwenye mitandao Serikali imeenda kurekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini barabara za Sumve asilimia kubwa hazipitiki vijijini kuna kata zingine kama Kata ya Mwabomba ikinyesha mvua ikakukuta uko kule kama una pikipiki unaacha unatembea kwa mguu. Kwa hiyo, bado kabisa tunatakiwa tuwekeze pesa kwenye miundombinu ya vijijini ili wakulima wetu waweze kusafiri waweze kusafirisha mazao lakini pia ipo miundombinu ya kimkakati ambayo inawezekana hatujaiona sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ambayo imekuwa ikiongelewa sana tangu mimi nimekuwa chaguzi zote za Chama cha Mapinduzi za vyama vingi imekuwa ikitajwa barabara yenye urefu wa kilometa 71 inayotokea Hungumarwa kupita Ngudu kwenda mpaka Magu. Barabara hii ni barabara ya kimkakati ambayo imesahaulika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mpango huu pia nimeiona imezungumzwa lakini imezungumzwa katika ile stori ya kutenga pesa na mipango ya baadaye. Lakini imeanza kuzungumzwa niko darasa la tatu. Sasa barabara hizi za kimkakati kwasababu barabara hii ikijengwa kwa kiwango cha lami inapunguza umbali wa mtu anayesafiri kutokea Shinyanga kwenda nchi Jirani ya Kenya au Mkoa wa Mara au Wilaya ya Magu kwa kilometa zaidi ya 83. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ukiijenga unakuwa umeokoa uchumi tunaposema kukuza uchumi barabara za kimkakati ndiyo hizi. Hii ni barabara ambayo inaweza ikafungua mbali na kufungua wilaya ya Kwimba kuongeza mapato kuongeza mzunguko kwasababu Wilaya ya Kwimba ni wilaya pekee ambayo kwenye Mkoa wa Mwanza haijui maana ya lami kwenye Makao Makuu yake kwa hiyo, barabara hii ikipita itafungua uchumi wa Wilaya ya Kwimba. Lakini siyo tu uchumi wa Wilaya ya Kwimba itafungua uchumi wa kanda ya Ziwa na uchumi wa Taifa kwasababu tunahitaji mizigo inayopelekwa nchi jirani ya Kenya iende kwa urahisi zaidi, tunapunguza uhai lakini tunafungua uchumi wa wilaya husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika mpango huu wa kiuchumi; Mpango Mkakati wa Maendeleo ambao tumeletewa leo, ni lazima tuangalie pia maeneo ya vijijini. Sisi tunaotoka vijijini, bado tumesahaulika. Hii miundombinu yote tunayoisema inazungumza mambo mengi ya mjini, lakini sisi ambao wakati mwingine hata mawasiliano ya simu siyo mazuri, hatuzungumzwi humu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kupitia Bunge lako, Wizara na Serikali katika Mpango wao huu wahakikishe wanazingatia maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi hii, lakini pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na uzima.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuchangia hii hotuba ya bajeti ya Wizara muhimu kabisa ya TAMISEMI, naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Waziri, Dada yangu Ummy, hongera kwa kupewa hili jukumu zito. Sisemi kwamba, mwanzo alikuwa una majukumu mepesi, lakini kila mara amekuwa akipewa majukumu mazito anafanya vizuri. Nategemea kwa usaidizi alionao wa Manaibu Mawaziri kazi ataifanya vizuri; ndugu yangu Mheshimiwa Silinde, Mheshimiwa Ndugange, najua kazi yenu mlivyokuwa mnafanya na sasa mnalo jukumu la kusaidiana na Waziri Ummy kufanya vizuri zidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe ushauri katika Wizara hii. Mheshimiwa Waziri na Manaibu wako mnaweza mkawa na mipango mizuri sana ya kufanya kwenye Wizara hii, lakini sisi sote Wabunge humu ni mashahidi kwamba Wizara ya TAMISEMI imekuwa na shida kubwa sana kwenye usimamizi wa pesa zinazopelekwa kwenye halmashauri zetu. Nimeona hapa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuna kama shilingi trilioni 2.9 karibu shilingi trilioni tatu zinaenda kwenye miradi ya maendeleo. Hizi pesa ndizo pesa watu kule kwenye halmashauri wamejipanga kuzipiga. Hizi pesa asilimia kubwa zinaenda kufanya kazi ambazo sio zenyewe. Ili tuweze kufanikiwa kwenye halmashauri zetu hizi pesa zinazotumwa kwenda kule na pesa zinazokusanywa kule ni lazima tuziimarishe halmashsuri zetu. Kwenye kuimarisha halmashauri zetu ni lazima tufahamu nani hasa ni msimamizi wa hizi halmashauri na kama zinafeli yeye anasababisha kwa kiwango gani?

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tunakimbilia kushughulika na watumishi wa halmashauri, simamisha Mkurugenzi na Mkuu wa Idara, kabla hatujaangalia msingi hasa wa usimamizi mbovu wa pesa za halmashauri. Kwenye halmashauri zetu na sheria zinavyoonesha wasimamizi wakuu wa halmashauri ni Baraza la Madiwani. Mimi ni ni-declare interest nilikuwa Diwani wa Kata ya Lyoma kabla ya kuwa Mbunge wa Sumve. Kwa hiyo, ninao uzoefu kidogo wa kukaa kwenye Baraza la Madiwani nikiwa Diwani wa Kata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Mabaraza ya Madiwani ndiko huu mwanya wa upotevu wa pesa unaanzia. Hauwezi kumwambia Diwani akasimamie Wakuu wa Idara wanaomzidi malipo mara kumi. Tumewahi kuangalia maslahi ya wasimamizi wa halmashauri zetu? Hawa Madiwani wanaosimamia halmashauri, je, wanazo nyenzo za kusimamia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kinachoangaliwa hapa ni upotevu wa mapato. Diwani anaambiwa asimamie shilingi bilioni 30, hela anazolipwa ni kidogo sana. Malipo ya Madiwani ni lazima tuyaangalie, hawa wasimamizi wa halmashauri; watumishi tunawalipa pesa ili wasimamie vizuri kazi zao, lakini Madiwani kwanza malipo yao yamekuwa ya hisani, wanalipwa kutokana na mapato ya ndani. Mkurugenzi akijifikiria ndio anawalipa kama hisani halafu haohao wakamsimamie. Kwa hiyo, mwisho wa siku tunatengeneza mwanya wa hawa watumishi kutumia uwezo wao wa kipesa kuwarubuni hawa Madiwani wasisimamie mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni lazima Serikali irudi iangalie kwanza, hata kwa hii pesa ndogo ya posho ya mwezi mnayowalipa Madiwani haitakiwi kulipwa kwa hisani ya Wakurugenzi iwe inalipwa kutoka TAMISEMI ili huyu mtu awe na nguvu ya kumsimamia Mkurugenzi. Kwa sababu siwezi kuomba hisani nasimama namshukuru Mkurugenzi, mimi nimehudhuria vikao vya Baraza la Madiwani, Diwani akisimama kwanza anamshukuru Mkurugenzi. Unamshukuru nini wakati wanaenda kumsimamia? Wanashukuru kwa sababu ili awe kwenye mgawo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pesa za marupurupu ya Madiwani ya ulipaji wa vikao na nini, ninyi Wabunge ni mashahidi kwa vile ni Madiwani, halmashauri nyingi wanadai. Pesa za bima za afya za madiwani hazipelekwi zinakusanywa, inaonekana ile mikopo ya benki haipelekwi kwa sababu hakuna utaratibu maalum wa usimamizi wa suala hili. Sasa kama hatuwezi kusimamia maslahi ya Madiwani nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri TAMISEMI hutaisimamia vizuri, lazima utaratibu wa wasimamizi walioko kwenye halmashauri ubadilishwe. (Makofi)

T A A R I F A

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mbunge wa wapi? Ndiyo nakuruhusu endelea.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, naomba tu nimpe Taarifa mzungumzaji anayeendelea kwamba, baadhi ya halmashauri, mfano Halmashauri kama kule Korogwe ambayo Madiwani waliomaliza udiwani wao mwaka 2020 mpaka leo wanaidai halmashauri. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Kasalali unapokea Taarifa hiyo?

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, naipokea hiyo Taarifa na kuongeza kwamba kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kuna Madiwani ambao wamefariki mpaka leo hata mafao yao familia hazijalipwa, akiwepo Marehemu Diwani wa Kata ya Lyoma ambayo mimi niliingia baada ya yeye kufariki na wengine. Kwa hiyo, bado tunayo kazi kubwa kwenye kusimamia maslahi ya Madiwani hawa ndiyo wanasimamia halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, niende mbele zaidi nikaangaliue jambo ambalo watu wengi wameliongelea hapa la TARURA. TARURA ni tatizo kubwa sana ndiyo maana Wabunge wengi wameliongelea hapa. TARURA ndiyo inahudumia watu wetu kule vijijini na mimi sielewi sababu za kutoa ujenzi Halmashauri tukapeleka TARURA, labda tuangalie kuna ufanisi gani upo kwa kufanya hivyo kwa sababu barabara bado hazipitiki.

Mheshimiwa Spika, nikienda Jimbo la Sumve kuna Kata kama ya Mwandu sasa hivi mvua zikinyesha huwezi kwenda, haipitiki kata nzima. Ukienda Kata ya Mwabomba haipitiki kata nzima. Nikisema nitoke Bungulwa niende Ng’undya kwenye kata hiyohiyo kuna Kijiji cha Ng’unduya huwezi kwenda kabisa, lakini tatizo kubwa TARURA uwezo wao wa kujenga madaraja ni mdogo sana. Barabara za vijijini kinachokwamisha sanasana ni madaraja, kuna madaraja sugu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kwimba hatuna Hospitali ya Wilaya, tuna Hospitali Teule ya Wilaya ambayo iko Sumve, kutokea Ngudu kwenda Sumve kuna mito mitatu ambayo mvua ikinyesha haupiti hata kama una mgonjwa na barabara ile iko TARURA. TARURA hawana hela za kujenga haya madaraja na hawana uwezo wa kujenga madaraja. Kwa hiyo, ni lazima muwaongezee uwezo na pesa ili tuweze kurahisisha maisha ya watu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja lakini naomba Mheshimiwa Waziri apokee ushauri wangu wa kuongeza ufanisi wa Mabaraza ya Madiwani kwa kusimamia malipo ya Madiwani, lakini pia kwa kuhakikisha TARURA inapatiwa pesa za kutosha. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru sana kwa nafasi hii. Kabla sijaongea sana niseme tu naunga mkono hoja. Pia nimpongeze ndugu yangu Waziri wa Maji, Mheshimiwa Aweso na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya kwenye sekta ya maji. Wanafanya kazi nzuri ya heshima na sisi hatuwezi kuwalipa kwa maneno yetu haya lakini Mwenyezi Mungu atawalipa vile wanavyostahili. Naomba waendelee kuchapa kazi na Mungu na Watanzania wanawaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Sumve wanalo jambo lao ambalo wameniomba nije nimwambie Mheshimiwa Waziri kuhusu mambo ya maji. Katika Jimbo la Sumve lililoko kwenye Wilaya ya Kwimba nadhani katika Mkoa wa Mwanza ambao ukilitaja Ziwa Victoria unaongelea Mkoa wa Mwanza kwa kiasi kikubwa ni jimbo pekee ambalo halijui utamu wa maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria. Mheshimiwa Naibu Waziri nikiangalia katika bajeti zilizopita kila mara mradi nafikiri namba 3403 ambao unahusisha kupeleka maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria katika Miji ya Sumve, Malya pamoja na Malampaka iliyoko kwenye Jimbo la Maswa Magharibi kwa Mheshimiwa Mashimba umekuwa unatajwa kila bajeti, unatengewa hii shilingi milioni 600 lakini haufanyiki. Mpaka umekutwa na miradi mingine, naanza kuona Busega ambaye ni mjukuu wa Kwimba tumemzaa sisi anapangiwa mabilioni ya fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Kwimba hasa Jimbo la Sumve kijiografia, hali ya hewa inafanana. Mradi huu wa Kuokoa Mazingira wa Simiyu, unapokwenda Simiyu unaiacha Sumve inakuwa sio sawa, watu wa Sumve tuna matatizo makubwa ya maji. Tunaomba mradi huu katika bajeti hii muweke fedha ambayo watu wa Sumve na sisi tutajiona ni sehemu ya Watanzania kwa sababu tupo kwenye Wilaya ya Kwimba lakini Jimbo la Kwimba lina maji ya bomba kutoka ziwa Victoria lakini Jimbo la Sumve hakuna.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri aliwahi kuja kwenye ziara Wiayani Kwimba nikamwomba walau utengenezwe usanifu yale maji ya bomba katika tenki la lita milioni mbili waliloliweka kwenye Mji wa Ngudu yaende walau kwenye Kata za Lyoma, Malya, Wala ili kata zilizo karibu na mji wa Ngudu zipate maji kutoka Ziwa Victoria. Hata hivyo, naona bado usanifu ni wa kupeleka kata zilizo kwenye Jimbo la Kwimba lakini Jimbo la Sumve tumeachwa. Kwa niaba wa watu wa Sumve naomba kusema kwamba maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria ndiyo yatatuokoa na matatizo ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Sumve hata uchimbaji wa visima wamekuwa wakichimba wanakosa maji chini. Tuna shida visima havijawahi kutusaidia kutatua tatizo hili. Tunapata visima vichache lakini na vyenyewe havijengewi mfumo wa maji ambao utawafikia watu wote. Naomba katika jambo hili la maji kwenye Jimbo la Sumve mtuangalie kwa jicho la pekee. Naunga mkono hoja kama nilivyosema lakini nahitaji sana tupate majibu yanayoeleweka hasa kwenye mradi wa maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria kwenda kwenye Mji wa Malya, Sumve na Malampaka ambao utalisha vijiji vingi vya Jimbo la Sumve na kuwa limepunguza tatizo la maji kwa kiasi kikubwa kwa watu wa Sumve. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo la Sumve pia ipo miradi nimeona nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri miradi ya visima katika vijiji vya …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Nasisitiza maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria kwenda Jimbo la Sumve hayaepukiki, naomba mtusaidie. (Makofi)


Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, kabla sichangia sana nataka nitende haki kwa Wizara hii na wasimamizi wake kwa kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya. Mheshimiwa Waziri Masauni kazi yako ni nzuri, umekuwa msikivu, umekuwa muungwana, Naibu Waziri Sagini wewe ni Ndugu yetu sisi watu wa Sumve, tumekuwa tukileta shida zetu mnatusikiliza na mnazitatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nichangie kidogo katika Wizara hii hasa katika vitu viwili. Katika Jeshi letu la Polisi ambalo linafanya kazi nzuri sana chini ya usimamizi wa IGP, wanafanya kazi nzuri sana ya kutulinda, lakini sijaelewa kuna shida gani kwa muda mrefu nimekuwa shahidi wa kuona mazingira magumu sana ya Askari wetu ya kufanya kazi, hasa vituo vyao vya Polisi na nyumba zao za kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Askari wetu asilimia kubwa hawana makazi yanayofanana na kazi wanayoifanya, nadhani umefika wakati sasa Serikali kupitia Wizara hii tuende na jambo la dharura la msingi la kuhakikisha Askari wetu wanapata makazi ambayo yatawafanya wafanye kazi zao vizuri. Hao Askari tunaowazungumzia ndiyo watu ambao tukisikia kuna panya road tunawafuata wao, kukiwa kuna wezi tunawauliza wao! Lakini hawa Askari ambao ndiyo wanatulinda suala la kuwatafutia makazi limekuwa likiimbwa kila siku Bungeni lakini hatua hazichukuliwi! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hao Askari tunaowazungumzia ndiyo watu ambao tukisikia kuna panya road tunawafuata wao, kukiwa kuna wezi tunawauliza wao, lakini hawa askari ambao ndiyo wanatulinda suala la kuwatafutia makazi limekuwa likiimbwa kila siku Bungeni humu, lakini hatua hazichukuliwi. Sasa nafikiri umefika wakati Serikali hatuwezi kuwa tuna jenga nyumba 20 za askari tunazungumza hapa, wakati tumejaza askari huko kwenye vituo wanatulinda. Suala la nyumba za askari liwe ni jambo la kipaumbele, watu wanatulinda, tunataka watulinde, unajua inawezekana tunachukulia poa kwa sababu askari hawana tabia ya kulalamika, wao wakikutana na sisi wanapiga saluti, basi, lakini jamani tuangalie watu kama ndugu zetu. Mazingira wanayoishi ni magumu, kwa hiyo kuna haja kabisa ya kulichukulia suala la nyumba za askari kama jambo la msingi.

Mheshimiwa Spika, magari wanayotumia, kwenye Wilaya ya Kwimba, hapa ninavyozungumza kuna gari moja tu la askari lakini nalo ni bovu; na juzi kama wiki moja imepita kulitokea ajali pale Sengerema gari la Mwanza ya Askari steering road zilichomoka tu, yaani gari ambazo hazina service, sasa hata namna tu ya kutafuta vyombo vizuri vya kufanyia kazi hawa askari wetu kweli ndugu yangu tumeshindwa. Lazima tufika wakati tuamue kuliboresha Jeshi la Polisi, tusing’ang’anie tu kuwa tunalalamika barabarani askari wanafanya nini wanafanya nini, lakini na sisi tuangalie namna ya kuboresha Jeshi la Polisi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele imeshagonga.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii adhimu. Kwanza kabla sijazungumza naomba niunge mkono hoja ili nisije nikasahau. Siungi tu mkono hoja, ninayo sababu. Sababu ya msingi kabisa ni kwamba ile barabara ambayo nilikuwa ninasema, leo ni mara ya nne naizungumzia hapa Bungeni. Barabara inayotokea Magu – Bukwimba – Ngudu mpaka Nhungumalwa yenye urefu wa kilometa 71 sasa nimeona kwenye Vote namba 4162 imepangiwa kujengwa kilometa 10. Hiyo ndiyo sababu nimeunga mkono kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu tunaheshimiana sana, wewe ni kama kaka yangu na watu wa Kwimba wanakushukuru kwa hili. Lakini, wanao ushauri kwako. Katika Vote hii namba 4162 ambayo tumehangaika mimi na wewe mpaka naiona hapa umetupangia bilioni 1.5 nadhani mimi na wewe ni mashahidi kwamba bilioni 1.5 haiwezi kutosha kuanza kutujengea kilometa 10 kwenye hizi kilometa 71. Sisi tunataka kwa kweli tumeshaomba sana, sasa sasahivi tunataka mtujengee, msikomee kutuandikia hapa kwamba mnajenga kilometa na mmetenga bilioni 1.5 halafu ujenzi usitokee katika Mwaka huu wa Fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo wazungumzaji wa mwanzo wamesema, ni lazima ifike wakati sasa vipaumbele hivi vitolewe kwa maeneo yote. Tumekuwa tukiona maeneo ya mjini ambayo yanaonekana kwa urahisi, ikitokea foleni kidogo tu naona zinajengwa ring roads, fly overs, lakini sisi watu wa vijijini inawezekana foleni zetu Mheshimiwa Waziti hauzioni, foleni zetu ni za mazao yanayoharibikia shambani kwa kushindwa kusafirishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, foleni zetu sisi ni watu wanaolala njiani siku mbili kwa barabara kuharibika. Hamyaoni haya, lakini nchi hii ili uchumi uende vizuri na watu waache kuhamia mijini wabaki vijijini wazalishe ni lazima na vijijini huduma ziende. Barabara za vijijini zipitike, kule ndiko tunakolima mazao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo la Sumve mazao yakilimwa mfano kwenye Kata kama ya Mwandu, ukilima mazao wakati wa mvua ni mpaka usubiri kiangazi uje uyasafirishe na tela ya ng’ombe. Mkokoteni ule ndiyo unasafirisha. Sasa, na sisi tunayo haki kama watu wengine wanaobanduliwa lami na kuwekewa lami mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano natoa barabara ambayo haipitiki kabisa iko kichwani tu lakini haipitiki. Yaani ukitokea Goroma unaenda Shushi, unaenda Mwakaluto, uende mpaka Ngudu kupitia Ilumba, ile barabara ni ya kichwani, haipitiki wakati wa mvua lakini kule ndiko tunakozalisha mazao mengi ya mpunga. Ukitaka kwenda kutokea kwenye mnada mkubwa kabisa kwenye Wilaya ya Kwimba Wabungurwa, unaenda Ng’undya, barabara ile haipitiki lakini kule ndiko mazao yanazalishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa waziri, tufike wakati uangalie hii barabara ya kwetu ya msingi kabisa ambayo inatokea Magu kwenda Ngudu mpaka Nhungumalwa kupitia stesheni ya Bukwimba ni lazima sasa muijenge kwa kiwango cha lami. Maombi tumeomba sana. Tunaomba sasa hizi kilometa 10 zilizoandikwa kwenye bajeti tuzione. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini iko barabara ambayo ndugu yangu Mheshimiwa Flatei Massay alitaka kupiga sarakasi hapa. Barabara hii inaanzia, yeye aliishia Maswa lakini ukitoka Maswa inakwenda mpaka Malya. Kutokea Malya inaenda mpaka Nyambiti. Kutokea Nyambiti inaenda mpaka Fulo, barabara hii imeahidiwa kwenye ukurasa wa 77 wa Ilani ya CCM kwamba itafanyiwa upembuzi yakinifu na kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii itamsaidia mtu anayetoka Mwanza akapita Jimbo la Sumve akaenda mpaka Maswa – Meatu, akaenda mpaka Hydom Mbulu akasafirisha mazao yake na inarahisisha sana usafiri. Barabara hii ni ya kimkakati kwenye kuinua utalii wa Serengeti. Sasa barabara hii imekuwa ikiandikwa na kuachwa na kwenye bajeti sijaona ule upembuzi yakinifu niliuona kwenye Ilani kwenye bajeti sijaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa waziri, naomba sasa Wizara iipe kipaumbele barabara hii. Ijengwe kwa kiwango cha lami ili na sisi tupate kama wanavyopata wengine. Nakushukuru sana. (Makofi)


Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Pia nitumie nafasi hii kuwapongeza viongozi wa Wizara ya Kilimo, Waziri na Naibu; na mahususi kabisa nampongeza na kumshukuru Naibu Waziri wa Kilimo, kaka yangu Mheshimiwa Hussein Bashe. Wakati sisi watu wa Sumve na Kwimba tulipokuwa tuna kilio chetu cha kupangiwa namna ya kuuza choroko, zao ambalo tulikuwa tunalilima bila usaidizi wa Serikali kwa asilimia 100, alilia pamoja na sisi. Namshukuru kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kusema kwamba, sisi watu wa Sumve bado tunacho kilio chetu kikubwa katika Wizara hii ya Kilimo. Shida yetu kubwa…

SPIKA: Kwa hiyo, Mheshimiwa Kasalali Serikali iliingia hata kwenye choroko?

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, iliingia.

SPIKA: Umesikia hayo maneno! (Kicheko)

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, ni jambo la aibu kulisema hapa kwenye Bunge Tukufu namna hii kwa sababu, sisi Wasukuma tunalima choroko. Kwetu choroko ni kama benki. Yaani familia ambayo haina choroko ni familia ambayo haiheshimiki. Yaani tunamaanisha kwamba choroko ni kama benki zetu kwa sababu hatuko karibu na mabenki, sisi bado kule ni washamba, ni vijijini. Sasa mtoto anapougua, mimi nachukua kilo moja ya choroko naenda kwa mtu ambaye anajulikana kwamba huwa ananunua, ninampa napata pesa, naenda kununua dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali bila aibu, wakaweka choroko kwenye Stakabadhi Ghalani.

SPIKA: Aah, kwa hiyo, ni kangomba.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, mwaka 2020 watu wa Sumve wameteseka. Ninasema Mheshimiwa Bashe tumelianaye kwa sababu nimehangaikanaye kwenye kiti chake pale nikijitahidi kujieleza. Nimeeleza, lakini naye akichukua hatua, kuna mtu anaitwa mrajisi, sijui hawa watu wanatoka wapi? Nikafikiri labda mrajisi huyu inawezekana amezaliwa India au Denmark. Kama angekuwa amezaliwa kwetu, angeshangaa kama ulivyoshangaa wewe kuona choroko inaingizwa kwenye Stakabadhi Ghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakulima wamenyanyasika, wanalazimishwa wapeleke hizo kilo moja moja…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Tabasam.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, namwambia tu mzungumzaji kwamba choroko ili uipeleke katika Stakabadahi Ghalani, mtu analima eka moja anapata debe moja. Ili kujaa tani 10 mpaka uwe na wakulima 1,000. Sasa hii ni hatari sana na hao walioko kule au wale AMCOS na wenyewe ni majambazi hawana hata mtaji wa 2,000/=. (Makofi)

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, taarifa hii ya heshima kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam naipokea. Nasisitiza kwamba mimi nilikuwa natamani kumwona Mrajisi. Wakati unatambulisha wageni wa Wizara ya Kilimo, nilikuwa nime-concentrate, lakini inaonekana ulimjumuisha kwenye Maafisa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hawa watu wanafikiria kama wako nje ya nchi. Aling’ang’ana, Mheshimiwa Naibu Waziri anatoa maelekezo mpaka akaandika barua, hawataki kuifuata. Tunalazimishwa; mwaka 2020 watu wa Sumve wamepata hasara ya mamilioni ya pesa. Kuna watu wamekamatwa, wamelipishwa fine zisizoelezeka.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Kilimo nitawaunga mkono bajeti yao tu endapo watakuja na maelezo ya kutosha ya kurudisha pesa zilizoibiwa kwa kutumia mgongo wa Serikali kwa wakulima wa choroko kwenye Jimbo la Sumve. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kitu kinaitwa sijui TMX, sijui wanaita kitu gani. Mtu anakuja anaambiwa, kwamba sasa mwishoni waliposumbua sana; na ninamshukuru sana Mkuu wa Mkoa wa sasa wa Dodoma alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, kidogo alifanya ubunifu ambao ulirahisisha hili tatizo ingawaje lilibaki kuwa tatizo, lakini alilirahisisha akasema, sasa kwa sababu mnawalazimisha wakulima wote wakusanye mazao yao wakakopwe, yeye akasema wanunuzi nunueni, mkishanunua, basi hiyo sijui malipo yao ya TMX na nini na nini wachukue Serikali. Yaani wale Ushirika, zile AMCOS zilikuwa zinachukua pesa ambayo hazijaifanyia kazi. Huu ni ujambazi kama ujambazi mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa watu wanatakiwa warudishe hela. Mheshimiwa Waziri tunataka hela za watu wa Sumve…

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Getere nimekuona, taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Wakati naendelea kumpa Taarifa mzungumzaji anayezungumza saa hizi, nikuombe hiyo sura uliyoingianayo asubuhi, uendelee kuwanayo hivyo hivyo. Mungu akusaidie hivyo hivyo; ya kukemea mambo ambayo yanaenda ovyo ovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, AMCOS katika nchi yetu, mimi sielewi. Mama mmoja ana miaka karibu 75 alinihoji siku moja. Wewe ni Mbunge wa nini? Kama mnakuwepo Bungeni miaka yote, sisi wakulima wa pamba kuna kitu kinaitwa AMCOS, hawana hela, wanachukua hela ya pamba ya mkulima wanakula; wanachukua ushuru wanakula; hawana hela ya kununua pamba. Ananiuliza ninyi ni Wabunge wa nini? Mbona mnazungumza mambo hayaishi?

Mheshimiwa Spika, ndiyo anayozungumza mzungumzaji hapa.

SPIKA: Taarifa hiyo Mheshimiwa Kasalali.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, naipokea na ninasisitiza, Mheshimiwa Waziri mimi sitaunga mkono hii bajeti, urudishe pesa. Hawa watu wanaitwa TMX na nani waliokuwa wanachukua pesa kwa wakulima wa Sumve bila kufanya chochote na kuwasababishia matatizo kwenye uuzaji wa choroko, pesa zirudi. Halafu pili, hiki kitu kinaitwa ushirika kwenye choroko kisije kikajirudia tena. Hatuwezi kuendelea namna hii, mnaleta vitu ambavyo havipo katika hali ya kawaida na bado sasa hivi tunavuna dengu, nasikia mna mpango huo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Sumve huo mpango hatuutaki. Tunataka tuuze tunavyotaka kwa sababu wakati wa kulima hamtuletei chochote. Tunaanza kulima wenyewe, tunahangaika; sijawahi kuona Afisa Ugani anashauri kuhusu choroko. (Kicheko/Makofi)

SPIKA: Yaani Mheshimiwa Kasalali Serikali ina mpango wa kuingia kwenye dengu pia! (Kicheko/Makofi)

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, wapo wamejipanga. Hawa watu wakati mwingine tuwe tunaona hata aibu, kwa sababu sisi ni viongozi na hawa wataalamu walioko huko, wanatushauri ovyo. Kwa sababu, hamwezi kushauri Serikali iweke Stakabadhi Ghalani choroko, kama kweli nyie ni watafiti. Kwa sababu, kuna wengine ni maprofesa, madokta, hizo elimu za Ph.D ni utafiti, sasa mnaingiaje kwenye jambo bila kulifanyia utafiti? Kwa sababu, wangefanya utafiti wasingetuletea hili tatizo. Sasa hivi wakulima wamefilisiwa, watu kule Sumve kwa kweli uchumi wetu umeyumba hapa katikati kwa sababu ya haya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nimalizie kwa suala la pamba. Mheshimiwa Waziri Bodi ya Pamba sisi wakulima wa pamba hatuitaki. Wewe ndio unaitaka. Sasa itaanza kushughulika na pamba ya Wizarani. Kwa sababu, hii bodi imeshindwa kabisa kuwasaidia wakulima wa pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamba imeshuka, bado tuna bodi na bado tuna wataalamu. Sasa hawa wataalamu ni wa nini? Tunaendelea kuwanao wa nini? Kwa sababu, hamji na mbinu za kumsaidia mkulima wa pamba apende kulima pamba. Wakulima wa pamba wakiniuliza jimboni kwangu nawaambia waache, kwa sababu, mwisho wa siku zinaniletea matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna wakulima kwenye AMCOS kama za Kiminza, Lyoma, nakumbuka nikiwa Diwani, mpaka leo wanadai kuna hela; mpaka kuna wahasibu wamejinyonga. Sasa mnaendelea kuwa na Bodi ya Pamba ya nini? Hata hizi AMCOS, ni za nini? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nafikiri kesho tutazungumza vizuri kama nitaunga mkono hoja au la, lakini haya mambo lazima yabadilishwe. Sisi watu wa Sumve kwa kweli hamjatutendea haki. (Kicheko/Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia katika bajeti yetu nzuri ya Serikali ambayo kwa kweli ni bajeti imeakisi mahitaji halisi ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijazungumza sana naomba nianze kwa kuunga mkono bajeti hii nzuri inayotia matumaini. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, kaka yangu Mheshimiwa Engineer Masauni, lakini na Katibu Mkuu kaka yangu Tutuba kwa kazi nzuri mliyofanya ya kutuandalia kitu ambacho hata tukikipeleka site kinakubalika. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nitumie nafasi hii kumpongeza sana, sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Tumetoka Mwanza Wabunge wa Mwanza tulikuwa na ziara na Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Rais na sisi tulikuwa tuna jambo letu Mwanza, amefanya kazi kubwa nadhani watu wote mmeiona. Ameionesha dunia kwamba Tanzania kazi inaendelea, ametia saini ujenzi wa meli tano mpya hii ni historia kubwa kwenye maendeleo ya nchi yetu, kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii yapo mambo ambayo nafikiria niishauri na mimi kwa Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi. Suala la kwanza niipongeze Serikali kwa juhudi ilizozifanya katika kuimarisha utendaji kwenye Serikali za Mitaa juhudi hizi zimeonekana bayana kwa Serikali kuamua kuanza kuwalipa Madiwani kutoka Serikali kuu, hiyo ni hatua muhimu sana kwenye kuimarisha utendaji kwenye Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali hiyo haijawaangalia Madiwani tu imewaangalia na Watendaji ikawawekea posho za kuwaongeza morali kufanya kazi ni jambo jema sana linahitaji pongezi, lakini na mimi ninayo maboresho ambayo nataka nishauri. Madiwani tumeamua kuwalipa kutoka Serikali Kuu, mimi pia nimewahi kuwa Diwani wa Kata, kazi za Diwani wakati mwingine kwenye Kata zinakuwa ni kazi za moja kwa moja za kushughulika na wapiga kura kwa sababu ndiyo mtu anayeishi nao muda wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali yangu ya CCM itoke kwenye kuhakikisha Madiwani inawalipa posho kutoka Serikali Kuu lakini na posho hizi ziongezwe zifanane na majukumu ya Madiwani. Madiwani bado wanachokichukua ni kidogo kulingana na majukumu yao, tumeongeza kwa Watendaji tukasahau Madiwani, kuwalipa kutoka Serikali Kuu ni hatua mojawapo nzuri, lakini ni lazima tuwaongeze kipato chao ili wakasimamie vizuri shughuli za maendeleo. Nikuambie kumuongeza posho Diwani ni kuiongeza posho jamii anayotoka Diwani, kwa sababu yeye ndiye anayeshughulika na shughuli za kwenye lile eneo muda wote, kwa hiyo hilo naomba niishauri Serikali iliangalie kwa jicho la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimetoka kwenye Jimbo la Sumve, Jimbo la Sumve ni jimbo la wakulima na wafugaji, nilizungumza hapa kuhusu mazao ya chakula kama choroko na dengu kuwekwa kwenye stakabadhi ghalani, kiti kilielekeza wakati wa kujadili Wizara ya Kilimo, kwamba Wizara ya Kilimo sasa kutokana na yale waliyoyakubali kwamba wanayaondoa choroko na dengu na ufuta kwenye stakabadhi ghalani waandike barua kwenda chini kuelekeza waliokuwa wamewaandikia barua kuyaweka mazao hayo kuyatoa, lakini mpaka sasa hiyo waraka haujaandikwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huko bado kuna usumbufu wa stakabadhi ghalani ninaomba sasa Serikali kwa sababu tunataka bajeti yetu hii iakisi mahitaji ya wananchi iende ikaondoe migogoro na vikwazo vya ukusanyaji wa kodi kwa sababu moja ya kitu ambacho kilipoteza mapato ya Halmashauri ikiwepo Halmashauri ya Kwimba ni kuyaweka mazao haya kwenye stakabadhi ghalani. Jambo hili lichukuliwe kipaumbe ili barua ile itoke iende ikabadilishe hili jambo ili tuweze kukusanya mapato tuweze kutekeleza hii mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali sana imeleta pesa kwenye TARURA sasa hivi matatizo hayajaisha lakini walau yamepungua, hata sisi kwenye jimbo la Sumve kuna barabara ambazo zilikuwa hazipitiki sasa kupitia hii milioni 500 tuliyopewa tumeanza kuzitengeneza zinapitika sasa hii ni jambo jema lakini ili tuongeze mapato lazima vikwazo hivi tuvishughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la watu wa Sumve nimekuwa nikilisema kila mara na nilipata matumaini makubwa Mheshimiwa Rais akiwa Mwanza alielekeza kwamba Serikali sasa inapanga kuijenga kwa lami barabara yetu inayotokea Magu kupitia Bukwimba, Ngudu mpaka Hungumarwa kwa kiwango cha lami. Nilipata matumaini makubwa sana na wakati tunajadili bajeti ya Wizara ya Ujenzi na wenyewe walikuwa wamesha tupangia pesa na kusema wanaanza kujenga kilometa 10, sasa jambo hili naomba nisisitize kupitia mchango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi hii tumekuwa tukiaahidiwa muda mrefu na imekuwepo hii vote muda mrefu, sasa nadhani kupitia bajeti hii imefika sasa wakati huu mpango ambao tumekuwa tukipangiwa kwa muda mrefu sasa na sisi watu wa Kwimba tuonewe huruma tujengewe barabara yetu hii kwa kiwango cha lami kwa mujibu wa ahadi iliyotolewa ili na sisi tufanane na maeneo mengine. Kwa sababu katika bajeti nzuri kama hii, itakuwa si vema kama bajeti hii itaisha itafika kikomo hatujapata jambo hili nasi walau tuweze kusimama kifua mbele tukisema bajeti ya 2021/2022 ilituangalia kwa jicho la tatu watu wa Sumve tukapata barabara hii. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, sijui ni kengele ya ngapi?...

NAIBU SPIKA: Muda wetu umeisha Mheshimiwa malizia.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, muda wangu umeisha. Nakushukuru sana kama nilivyosema tangu awali naunga mkono hoja na naomba yale yaliyoahidiwa kwenye bajeti hii yakatekelezwe nasi tutakuwa pamoja na ninyi kwenye kutenda kazi. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na uzima, lakini pia nikushukuru wewe, kwanza kwa nafasi hii uliyonipatia ya kuchangia hoja hii ambayo imewasilishwa kwa umaridadi mkubwa na Makamu Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete. Lakini pia nikushukuru kwa kuamua kiniteua kuhudumu katika hii Kamati ya Sheria Ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama wenzangu waliotangulia, mimi pia kwa taaluma yangu ni mwalimu, nilipoona nimepelekwa kwenye Kamati ya Sheria Ndogo nilishtuka kidogo nikasema sasa huku Mheshimiwa Spika amenipeleka nikafanye nini?

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya kuanza kufanya kazi mule niligundua ulinipa jukumu nyeti, kubwa na ambalo linahitaji umakini na muda. Kwa sababu mambo mengi yanayoendeshwa kwenye nchi hii yanaendeshwa kwa utaratibu wa kanuni na sheria ndogo ambazo sisi kwenye Kamati yetu ndiko tunakozipitia. Kwa hiyo nakushukuru sana kwa nafasi hii na ninakuahidi nitafanya kazi kwa nguvu zote na weledi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda kwenye vitu mahususi, niliomba kushauri kidogo, nadhani katika uwasilishaji tumeona katika muda huu mfupi tu kuna sheria ndogo zaidi ya 915. Hizi sheria ndogo zote zinaathiri maisha ya watu wa chini huko, zinapitishwa na mamlaka mbalimbali zilizokasimiwa na Bunge kufanya kazi hii.

Mheshimiwa Spika, lakini katika sheria chache ambazo tumezipitia tumegundua mapungufu makubwa sana. Kuna mapungufu ambayo ukiyaangalia tu unasema hawa watu wakati wanatengeneza hizi sheria walikuwa wamejifungia wapi.

Kwa hiyo, kama alivyomalizia Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda wakati anamaliza mchango wake, mimi mwenyewe nimeona lipo hitaji la Kamati ya Sheria Ndogo kupata muda zaidi wa kupitisha sheria ili kupunguza kero tunazokutana nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naamini kama sheria iliyopeleka zao la choroko na dengu kwenye Stakabadhi Ghalani ingeanzia kwenye Kamati ya Sheria Ndogo, wala tusingekuja kutoa maelekezo hapa Bungeni kuwaambia Wizara kwamba waandike waraka mwingine wa kwenda kuviondoa kwenye Stakabadhi Ghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ambacho mimi nimekigundua katika muda mfupi kwenye Kamati hii, inawezekana kwenye maeneo mengi tunapeleka watu ambao hawayajui hayo maeneo kwenda kuyatengenezea sheria ndogo. Kwa sababu ninaamini, kwenye maeneo kama ya – tulikuwa tunaangalia hapa Sheria ya Bodi ya Filamu, kwamba mtu anakwenda kutengeneza kanuni za filamu, mtu ambaye kwenye maisha yake hata filamu kuiangalia huwa haiangalii, lakini anakwenda kuwatengenezea watu wanaoangalia filamu na watu wanaofanya maigizo kanuni pale.

Kwa hiyo, ipo haja ya Kamati hii kupata muda wa kutosha ili kuweza kuzipitia sheria hizi, naamini ofisi yako italiangalia hili.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi naomba nijikite kwenye baadhi ya mambo, lakini kitu cha msingi kabisa ambacho nataka nikiangalie, kuna sheria nyingi ndogo na kanuni ambazo zinatengenezwa zinakuwa hazikidhi uhaliasia wa mambo.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo wachangiaji awali wamechangia, unakuta sheria imetungwa lakini ukiangalia uhalisia wake, nilikuwa naangalia Sheria Ndogo ya Jiji la Mbeya ambayo naamini ilitungwa huko nyuma, sasa imekuja kuanza kazi sasa, iliyokuwa inasema kwamba kila bajaji ilipokuwa inatoka stand inatakiwa illipe shilingi 1,500. Unajiuliza huyu mtu aliyetunga hii sheria alikuwa amejifungia wapi? Yaani bajaji kila ikitoka stand shilingi 1,500. Yaani hii unakuta kabisa hawa watu ukiangalia, wakati huo kuna daladala wanalalamikia zile bajaji.

Kwa hiyo, mimi naamini wale daladala wanakwenda kuhonga wale au inawezekana kuna mtu aliyekuwa anatunga hizo sheria labda ana daladala ili afanye kabisa bajaji zisiingie stand, kwa sababu bajaji ikibeba watu labda wa shilingi 500 kila mtu kwa watu watatu ina maana yeye bajaji anakuwa kazi yake ni kulipwa na kulipa ushuru. Hakuna kinachofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ilinishtua lakini nilipofuatilia na kwa faida ya Bunge hili, kwa sababu Mheshimiwa Naibu Spika ni Mbunge wa Mbeya, lakini ukiangalia, hii sheria imetungwa bado Mheshimiwa Naibu Spika hajawa Mbunge wa Mbeya. Inawezekana walijua watashindwa, kwa hiyo wakaona watengeneze sheria ambayo itakuja imfanye Mbunge anayekuja afanye kazi kwa ugumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ukiangalia sheria hizi zinapotengenezwa, ni lazima watu wanaozitunga wawe wana…

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Kasalali, inaelekea ilitungwa wakati ule CHADEMA ndio wanaongoza Jiji, eh?

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa.

SPIKA: Mheshimiwa Cecilia nimekuona umesimama.

T A A R I F A

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba utungaji wa sheria haumlengi mtu, utungaji wa sheria yoyote, ama sheria mama au sheria ndogo, unalenga utekelezaji wa jambo fulani kwenye jamii uweze kufanikiwa. Kwa hiyo, jamii yoyote inayolengwa, haijalishi ni CHADEMA, CCM au asiyekuwa na chama, mkristo au mpagani, vyovyote vile, inalenga jamii kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na wanaoandaa sheria ndogo hizi wengi ni watendaji wetu kwenye ofisi zetu za Serikali. Kama mchakato unaanzia kwenye ngazi za kata, vijiji, inapanda kwa mfumo wa…

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninataka nimpe hiyo taarifa. (Makofi)

SPIKA: Yaani alichokuwa anasema ni kwamba sheria hii ilitungwa kipindi kile ambacho Meya na Madiwani wengi wa Jiji la Mbeya walikuwa ni wa CHADEMA; ndicho alichokuwa anasema. (Makofi)

Mheshimiwa Kasalali, sijui kama ulimaanisha hivyo?

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, hii taarifa niliyopewa ngoja niendelee kuwa nimepewa, lakini mimi kitu cha msingi ambacho nilikuwa nataka kukieleza ni kwamba Baraza la Madiwani lililopita la Halmashauri ya Jiji la Mbeya ndilo lililoshiriki kutengeneza sheria hii ndogo ambayo ilikuwa inawakandamiza waendesha bajaji na bodaboda wa Jiji la Mbeya ambayo sisi wakati tunajadili kwenye… (Makofi)

SPIKA: Bahati mbaya muda umekwisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya. Pia niwapongeze Wajumbe wa Kamati zote mbili kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ya kuleta mapendekezo na ushauri wa namna ya kufanya katika mambo haya ambayo tunayajadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nipongeze Wizara zinazohusika na mjadala tunaoujadili hapa, hususan Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa usimamizi mzuri wanaoufanya huko kwenye halmashauri zetu, lakini pia Wizara ya Utawala Bora kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kusimamia Utumishi na kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo kama sitampongeza Mheshimiwa Rais kwa pesa nyingi alizotuletea kwenye halmashauri zetu hususan pesa zilizotokana na mkopo nafuu maarufu kama pesa za Mama Samia ambazo zimefanya kazi kubwa ya maendeleo huko Wilayani kwenye elimu, afya na maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi hizi zinaendana na ushauri ambao nataka niutoe hasa kwenye Wizara ya TAMISEMI na Utawala Bora kwenye namna ya kufanya majukumu yaende vizuri huko kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyosemwa awali katika Ibara ya 145 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, majukumu ya usimamizi yameshushwa kwenda kwenye Serikali za Mitaa. Katika Serikali zetu za Mitaa zipo hizi halmashauri za Wilaya, Majiji na Manispaa, wasimamizi wakuu wa halmashauri hizi ni Mabaraza ya Madiwani. Mabaraza la Madiwani ndiyo yametamkwa kama wasimamizi wakuu wa halmashauri zetu na Serikali za Mitaa, lakini kwa jinsi hali inavyokwenda tunaweza tukajikuta tunatengeneza mipango huku juu tukiiteremsha huko chini haifanikiwa vizuri kwa sababu hawa wanaosimamia hizi halmashauri zetu bado hatujawawezesha kiasi cha kutosha ili waweze kusimamia vizuri halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka hapa kwenye Bunge la Bajeti tulizungumza kuhusu kuhamisha malipo ya Madiwani yatoke kwenye halmashauri kwa mapato ya ndani na yalipwe na Serikali Kuu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na Viongozi wa Serikali kwa kulikubali suala hili. Limesaidia kwa kiwango kikubwa sana ingawaje bado malipo yale ni madogo, lakini limesaidia sana. Sasa hivi kuna tatizo moja kwenye halmashauri huko kuhusu posho za vikao vya Madiwani, Wakurugenzi wengi wanafanya kazi hizo kwa kutumia vichwa vyao na siyo utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umefikia wakati nikitoa mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, sasa hivi viko vya Baraza la Madiwani, Madiwani wanaenda tu ili liende kwa sababu Madiwani wote wanaotoka Jimbo la Sumve ambalo halina hata Makao Makuu ya Wilaya hawalipwi pesa ya kulala, wanalipwa pesa anaambiwa Diwani aende kwenye kikao cha halmashauri amalize kikao arudi nyumbani, ukimuuliza Mkurugenzi anasema kuna wakara. Hizi nyaraka za Serikali zinazozungumza kuhusu posho za Madiwani, nimejaribu kuzipitia nimekuta zipo nyaraka karibu tisa na inaonekana nyingine sijaziona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tuwasaidie hawa Madiwani imefika wakati Bunge hili la Serikali tuamue kutoa utaratibu wa aina moja unaosimamia maslahi ya Madiwani ili halmashauri zetu ziweze kusimamiwa na watu ambao wana uhakika na wanachokifanya, vinginevyo sasa hivi Madiwani wanaenda kwenye vikao kutimiza wajibu tu wanawahi warudi nyumbani. Sasa wasimamizi wa halmashauri wasipokuwa na uhakika na wanachokifanya mwisho wa siku ndiyo mwanya wa wizi na ubadhirifu tunaendelea kuuona unaendelea kwenye halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kushauri, Serikali na Bunge tutoe maelekezo ya aina moja, yanayofanana nchi nzima ya namna ya kushughulikia maslahi ya Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa hii nafasi uliyonipatia. Awali ninaipongeza Wizara ya Fedha kwa huu mpango ambao wameuleta hapa, ni mpango ambao unaonesha matumaini kwenye uchumi wetu lakini kwa kuutazama na mimi nimeona walau niongeze mchango wangu ili kuboresha katika maeneo machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu na wachangiaji wa mwanzo wamechangia na kuzungumza kuhusu umuhimu wa Sekta ya Kilimo. Sekta ya kilimo, Watanzania tumekuwa tukisema ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu. Sekta ya Kilimo kwa taarifa ambazo zipo na zimeandikwa kwenye taarifa ya Waziri wakati anatoa mpango ni kwamba bajeti imepanda kutoka bilioni 254, mpaka zaidi ya bilioni 900. Sekta hii inatoa ajira asilimia 65 na zaidi ya Watanzania. Kwa hiyo sekta ya kilimo ni sekta ya muhimu sana na kama tunataka kutoka hapa tulipo twende pazuri zaidi ni lazima tuongeze nguvu kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo inayo maeneo mengi ya msingi lakini nitazungumzia eneo moja la usafirishaji wa mazao ya kilimo. Mazao yetu ya kilimo mengi yanatoka maeneo ya vijijini, wakulima wetu wanapolima mazao yao wanatumia gharama kubwa sana kuyasafirisha. Jambo ambalo limekuwa likisababisha bei ya mkulima kuwa chini lakini bei ya mazao kwa mlaji inakuwa juu. Naishauri Serikali kwamba iwekeze zaidi kwenye kuhakisha barabara zilizoko vijijini ambako ndiko kwa wakulima wenyewe zinaboreshwa ili ziweze ku- accommodate usafirishaji wa mazao haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza nikatoa mfano kwa sababu mimi pia ni Mbunge ambaye ninatoka kwenye Jimbo ambalo asilimia kubwa ni wakulima na wafugaji, Jimbo la Sumve. Katika Jimbo zima la Sumve hakuna barabara ambayo inaruhusu gari la zaidi ya tani kumi kupita. Ina maana ili ubebe mazao ya pamba kwa mujibu wa sheria za barabara zetu zilivyo unatakiwa utumie canter au magari mengine madogo madogo ukishatoka Sumve ndiyo utafute magari makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa utaratibu huu wa kuwa na barabara mbovu kwenye maeneo ya uzalishaji hatumsaidii mkulima, lazima Wizara ndugu yangu Mwigulu Nchemba Waziri tufikirie hili jambo kwa undani wake. Ndiyo maana kila muda tunaposimama tuataka kushauri kuhusu maendeleo ya nchi hii, tunaotoka huko vijijini tunalia na miundombinu ya usafirishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani umefika wakati sasa Serikali ichukue hatua kwa ajili ya kukuza uchumi wetu. Tunapata taabu sana kwa mazao yetu kufika Mjini yakiwa na bei kubwa na wakulima wetu kupata bei ndogo kwa sababu ya matatizo ya usafiri, halafu tunasema tunaboresha barabara za mijini wakati sisi wa vijijini kila siku tunazungumzia barabara zetu. Hili jambo nilitaka Serikali iliangalie kwa jicho la pili kwa ajili ya kukuza uchumi wa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa sana hapa na michango iliyopita ni kuhusu tunapanga Bajeti hapa, tunapeleka pesa kwenye Halmashauri zetu kwa ajili ya pesa zile kutumika kuleta maendeleo kule lakini pesa zile zimekuwa hazifanyi kazi iliyopangwa. Pesa hizo zinafika kule zinapotea mwisho wa siku unakuta Waziri wa Idara kama TAMISEMI, unakuta kazi yake yeye ni kutumbua kushughulika na wezi kutengeneza Tume za kuchunguza na mwisho wa siku badala ya ile pesa kufanya kazi tunahangaika kufunga watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nafikiri tunatakiwa mpango wetu wa maendeleo huu uangalie hilo kwa jicho la pili. Lazima tujiulize kwa nini pesa nyingi zinazopelekwa kwenye Halmashauri zinakwenda zinaibiwa? Kwa nini iko shida kule? Halmashauri mfumo wake ukiuangalia umewekwa vizuri sana kisheria, Halmashauri zinasimamiwa na Mabaraza ya Madiwani, hawa Madiwani kwa mujibu wa sheria ndiyo walinzi wa Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Halmashauri tunapeleka Mabilioni ya pesa halafu kwenye mpango huu tumepanga wale walinzi wetu tunawalipa kiduchu ndiyo walinde hizo pesa. Kila siku tutatengeneza tume tusipofahamu siri ya wizi. Kwenye Halmashauri imefika wakati sasa hivi Madiwani hawafanyi hata ziara, yaani wale Watumishi wanatumia loophole ya Madiwani kutokuenda, mipango yetu na nyaraka zetu na maelekezo ya Mawaziri imefika wakati Madiwani wale wanaolinda mali zetu tunazopeleka kule, wanakutana kwenye Kamati kujadili makabrasha makubwa ambayo hawajajua hata hiyo miradi ikoje. Ziara za Madiwani za Kamati, zimefutwa, wanasema ni maelekezo ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inafika wakati utendaji kule umekuwa chini, kwa hiyo hawa walinzi wetu hawafanyi kabisa kazi vizuri, kwa hiyo mwisho wa siku ukiwa na walinzi dhaifu wanashirikiana na mwizi kukuibia. Kwa hiyo, kila siku tutakuwa tunapeleka pesa kule, tutakuwa tunakaa hapa tunapanga mabilioni kama hatujaangalia namna gani tunalinda pesa tulizozipeleka kule. Tutaendelea kuwapa kazi Mawaziri ya kutumbua, kazi ya kusimamisha, TAKUKURU kagua, anafika Mheshimiwa Waziri Mkuu kule anakuta yaani miradi mpaka afike Waziri Mkuu ndiyo ionwe wakati huo kuna wasimamizi kule ambao ni Madiwani, nadhani hili jambo tunatakiwa tuliangalie kwa jicho la pili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi yetu itaendelea kuibiwa ni lazima Serikali ije na mpango wa kulinda mali tunazopeleka kwenye Halmashauri. Halmashauri ndiyo chanzo cha maendeleo ya watu wetu. Nadhani hata Wabunge ni mashahidi. Hapa Wizara zinazotembelewa mara nyingi na Wabunge ni TAMISEMI. Sasa TAMISEMI huko ndiko kapu la pesa zinazowahusu wananchi wetu zinaenda kule, huu mpango tunapanga pesa nyingi tunapeleka kule. Sasa kule hakuna walinzi tumeweka watu tu wa kushirikiana na wengine kuiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu unapompa pesa humwekei mlinzi unamshawishi kuziiba ni lazima tuwe na mpango wa kulinda hizi pesa zetu vinginevyo…

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji, ndani ya huu mwaka tu mmoja zipo Halmashauri ambazo zimepokea Nyaraka Mbili tofauti zinazotoka TAMISEMI, juu ya Madiwani. Mwanzo waliongezewa posho zao lakini ikatokea tena waraka ndani ya huu mwaka mmoja wamepunguziwa posho zao. Kwa hiyo naungana kabisa nahoja ya Mheshimiwa, hawa walinzi wetu wanakaa hawaelewi kesho wataamka wako katika hali gani.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii naipokea na ninasisitiza ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge Serikali hili jambo tulipeni umuhimu wake ili pesa tunazozipanga na kuzipeleka huko zitumike vizuri. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na afya njema. Kabla sijaenda mbali sana, naomba nitoe haki kwa viongozi wa Wizara ya TAMISEMI, nikimaanisha Waziri, Mheshimiwa Bashungwa, Manaibu wake, Mheshimiwa Dugange na Mheshimiwa Silinde. Kwa nini nimesema nitoe shukrani na pongezi kwa hawa watu?

Kwa uzoefu wangu nadhani na Wabunge wengine, hakuna Mawaziri rahisi kuwapata kama hawa jamaa. Ukiwa na shida yako ni rahisi sana kuwapata hawa Waheshimiwa (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niwapongeze sana. Wamekuwa ni watu, wasikivu na ni wepesi wa kujibu shida za Wabunge. Ninapoleta shida TAMISEMI nakuwa na amani kwa sababu ya watu wanaosimamia Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni wakati muafaka kwa watu wengine kujifunza pia. Kuna Waziri mmoja mpaka nilimwandikia message nikamwambia Mheshimiwa Waziri nikitaka kukupata ninafanyaje? Kwa sababu huwezi kumpata. Ndugu zangu, zichonganishi lakini ninasema ukweli, mmekuwa watu wema sana, mnatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze kwenye kuwashauri hawa ndugu zangu wema. Wizara ya TAMISEMI ni Wizara kubwa sana, inasimamia vitu vingi sana. Mheshimiwa Rais amewapa kazi kubwa sana ya kusukuma maendeleo. Mheshimiwa Rais anatafuta fedha, analeta kwenye maendeleo. Sisi sote ni mashahidi na nchi ni shahidi, kama kuna wakati miradi ya maendeleo imepelekwa vijijini kwa watu, ni wakati huu wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Sasa ninyi TAMISEMI ndiyo mna jukumu la kusimamia hizi fedha Mheshimiwa Rais anazotupelekea kwenye maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasimamizi wa hizi fedha, leo ninarudia, kwenye bajeti iliyopita nilisema, nashukuru Serikali sikivu ilinisikia, ikahamisha posho za Madiwani katoka kulipwa kwenye Halmashauri zikaanza kulipwa na Serikali Kuu; kwenye Bajeti iliyopita tulisema kuhusu Madiwani kutokulipiwa Bima zao za Afya, tunashukuru Serikali sikivu ya CCM imeamua sasa kuchangia Bima za Afya za Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kada ya Udiwani ni muhimu sana kwako. Naweza kukwambia, inawezekana hawa ndio walinzi wa nyumba yako. Fedha zote zinazopelekwa Halmashauri, wanaozilinda ni hao Madiwani lakini walinzi wako hawana vifaa vya kulindia fedha. Unapeleka mabilioni ya fedha kwenye Halmashauri, lakini unawalipa watu shilingi 300,000 walinde mabilioni, siyo sawa na tunajidanganya. Fedha zetu zitaendelea kuliwa na kuibiwa kwenye Halmashauri mpaka siku tutakapotambua umuhimu wa Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nichangie hili kwa uchungu kwa sababu wakati nipo Diwani, mfano nilipokuwa nikienda kwenye kikao, Halmashauri zetu hazifanani. Halmashauri ya Dar es Salaam na Ilala na Kwimba ni tofauti, inabidi mimi niende nikalale Ngudu kutoka Lyoma.

Kwa hiyo, siku ninapoenda kwenye kikao nilikuwa nalipwa night, nikiamka naenda kwenye kikao, kesho yake naenda kwenye kikao cha Kata, kesho yake kikao cha Full Council, siku inayofuata nitatoka jioni, nitalala, kesho yake naondoka. Nilikuwa nalipwa siku nne. Nashangaa sijui huu utaratibu umetoka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni utaratibu umebadilishwa, Diwani anaambiwa yule anayelala, alale siku mbili; haya makabrasha wanayapitia saa ngapi? Ndugu zangu kama mnahudhuria vikao vya Madiwani yanakuja mabuku makubwa hivi, yanahitaji muda wa kuyapitia. Sasa wanayapitia saa ngapi? Cha ajabu siku za karibuni, na nilikwenda kumwona Mheshimiwa Waziri pale nikamwambia; Madiwani wameanza kulipwa, lakini wengi hawalipwi fedha za kulala, wanaambiwa aende arudi. Huu uzoefu ni wa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo la Wilaya ya Kwimba kuna Kata ipo kilometa kama sita kutoka Halmashauri, inaitwa Kata ya Mwang’halanga, kuna mto pale wa Mahiga, ukijaa maji, Diwani kama kalala kwake, hahudhurii vikao. Kwenye Jimbo la Sumve, Kata ya Wala tunamshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu amejenga daraja baada ya kumeomba. Diwani akilala kwake, ni kilometa kumi tu, hawezi kuhudhuria kikao. Nyambiti kuna Mto Solwe haupitiki mvua ikinyesha, ndio maana Madiwani walikuwa wanatakiwa wakakae kwenye Halmashauri wamalize vikao halafu waondoke.? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii akili ya kuanza kuwaambia Madiwani wahudhurie vikao warudi nyumbani, mmeitoa wapi? Otherwise mmeamua Halmashauri iwe shamba la bibi. Tutaibiwa kweli kweli, nakuhakikishia Mheshimiwa Waziri. Utakuja na bajeti hapa, tutakuwa tumepigwa, mtafukuza watu, mtasimamisha watu, lakini kama hamwelewi kuwawezesha Madiwani posho yao ya mwezi, unamlipa mtu shilingi 300,000/= unasema asimamie mabilioni; Mheshimiwa Waziri naomba sana, wewe ni msikivu, ni wakati sasa umefika Serikali kuelewa umuhimu wa Madiwani. Kama hamtaki kuelewa, mtaendelea kuibiwa, tutaendelea kukamata watu, kufukuza watu na tutakuwa hatujaisaidia nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa msingi kabisa ulikuwa ni huu. Nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, lakini kabla sijachangia ninazipongeza Kamati zote mbili kwa uwasilishaji mzuri na ushauri mzuri kwa Bunge, nadhani imekuwa ni mwanga mzuri wa kutusaidia kulijadili jambo hili kwa upana wake.

Mheshimiwa Spika, nadhani sote ni mashahidi katika wakati huu wa Serikali ya Awamu ya Sita ni wakati pekee kwa uzoefu wangu mimi wa kuishi Tanzania ambapo nimeona pesa nyingi sana za miradi ya maendeleo zinapelekwa kwenye Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya. Pesa zinazohusu madarasa, pesa zinazohusu vituo vya afya, zahanati, zinapelekwa kwa wingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sote hapa ni mashahidi na ni Madiwani huko kwenye Halmashauri zetu, hata Watumishi wetu wameingiwa na ugumu kwenye kusimamia pesa hizo nyingi zinazokuja. Sasa mimi nimesimama kuchangia kwenye Kamati hii ya Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Huduma za Jamii, nataka kujikita kwenye kutoa ushauri wangu wa namna bora ya kusimamia pesa za maendeleo ambazo zinapelekwa kwenye Halmashauri zetu. Pesa nyingi ambazo zikisimamiwa vizuri zitaacha historia isiyosahaulika kwenye nchi yetu na zitampa heshima kubwa sana Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu binadamu yeyote anapopewa pesa hapendi sana kusimamiwa, anapenda aachwe afanye vile anavyoona yeye. Na pesa daima ni sabuni ya roho, kila mmoja akiona pesa anatamani kuitumia yeye ndio maana zikawekwa taratibu za usimamizi. Ndiyo maana kwenye level ya Serikali Kuu lipo Bunge tunaisimamia Serikali, lakini kwenye level ya Halmashauri yapo Mabaraza ya Madiwani yanasimamia zile Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema Mabaraza ya Madiwani hapa leo?

Mheshimiwa Spika, Mabaraza ya Madiwani kusimamia kwake Halmashauri wanasimamia kupitia ziara mbalimbali, kupitia vikao, miradi inapopelekwa kule inaenda kukaguliwa na Madiwani kwenye ziara. Hivi ninavyoongea kuna nafasi ambayo imetolewa na Wizara yetu pendwa ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kupitia maelekezo mbalimbali na nyaraka mbalimbali, Halmashauri za Wilaya badala ya kusimamiwa kwa nguvu zote na Madiwani utendaji wa Madiwani, Halmashauri za Wilaya sasa zinaendeshwa kwa hisani za Wakurugenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi Waheshimiwa Madiwani kwenye baadhi ya Halmashauri za Wilaya, ikiwepo ya Kwimba, Kamati ile ya Huduma ya Jamii ambayo ilikuwa Elimu, Afya na Maji na Kamati ya Uchumi hazifanyi kabisa ziara kwa sababu, Halmashauri zinasema kuna nafasi inatoka kwenye kanuni ya kuwafanya wao waamue kama Madiwani waende ziara au wasiende. Kwa hiyo, hela zote tunazopeleka zile Kamati za Madiwani hazikagui hizo pesa, sasa hii ni hatari kubwa kuacha pesa zetu zisisimamiwe huko vizuri! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbali na hayo Halmashauri zetu ili zisimamiwe vizuri, hapa nilishawahi kusema na leo ninarudia, ukiwa na mali yako unaweka mlinzi aliyeshiba. Ukiweka mlinzi mwenye njaa una hatari ya kuibiwa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na nafasi hii kwa ruhusa yako naomba nisome waraka ambao ulitoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwenda kwenye Halmashauri ambao unatoa loop. Unasema hivi, katika kipengele cha nne; “Posho za kujikimu za Waheshimiwa Madiwani zinapaswa kulipwa kwa kuzingatia mahali, sehemu na umbali Diwani anakotoka. Msingi mkubwa wa kuzingatiwa ni kuwa Diwani husika sharti awe amesafiri na kulala nje ya makazi yake ili aweze kuhudhuria kikao kinachofuata.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sharti hili limekuwa likitumika vibaya, yaani Mkurugenzi ndio anaamua Diwani amelala au hajalala. Mwisho wa siku sasa Mabaraza ya Madiwani, Madiwani wanapoenda kwenye vikao vyao wanalipwa kwa hisani, yaani kitu kinaitwa mahusiano. Wasipokuwa na mahusiano mazuri na Mkurugenzi hawalipwi vile inavyotakiwa. Zile per diem za Madiwani zinaamuliwa kwa mahusiano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba Bunge lako Tukufu kupitia Kamati hii tumuelekeze Mheshimiwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa atoe maelekezo mahsusi kuliko maelekezo kama haya yanayotoa loop hole ya watu kucheza na Mabaraza ya Madiwani yashindwe kusimamia Halmashauri zetu. Atoe maelekezo mahsusi yanayozielekeza Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Majiji kulipa pesa kwa Madiwani kwa kuzingatia uhalisia kwamba, Madiwani wengi wanapokuja, hasa kwenye Halmashauri za Wilaya, wengi wanalala.

Mheshimiwa Spika, huwezi kusema Diwani wa Sumve um-judge kwa umbali wakati miundombinu yake haimruhusu, hakuna daladala, akishatoka kule akamaliza kikao saa 12 lazima alale Ngudu. Sasa unapomwambia kwamba, umbali wake na Halmashauri zetu hizi tunaanza kuweka, yaani imekuwa ni kwamba, ni hisani za watu wanafikiria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Bunge lako lielekeze Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa itoe waraka mahsusi ambao unaondoa mkanganyiko wa ulipaji wa posho za kulala za Madiwani kwenye Halmashauri za Wilaya na Miji ambazo kwa asilimia kubwa Madiwani wanapoenda kwenye vikao wanaenda wanalala ili waweze kukaa kwenye vikao wakiwa na amani, wasimamie pesa zetu vizuri ili sisi tunapopeleka pesa kule ziwe salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani jambo hili tumekuwa tukilisema mara kwa mara kuhusu usimamizi wa Halmashauri kwa kuboresha maslahi ya Madiwani…

SPIKA: Sekunde 30, malizia.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, naomba sasa Bunge lako Tukufu litoe maelekezo mahsusi na tumuombe Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa atoe maelekezo mahsui kwenye Halmashauri ambayo yataondoa mkanganyiko wa ulipaji wa wasimamizi wetu wa Halmashauri. Nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na mimi naomba nijielekeze katika kuchangia hoja za Kamati mbili ambazo zimewasilishwa hapa; Kamati ya Katiba na Sheria na Kamati ya Sheria Ndogo ambayo mimi pia ni Mjumbe wa Kamati hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti,nizipongeze Kamati hizo kwa kazi nzuri sana ambazo zimefanya katika kupitia na kujadili kazi zake ambazo zinaonesha moja kwa moja Bunge liko serious katika kuisimamia Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye mjadala wa Kamati ambao mimi ninahudumu ya Sheria Ndogo. Kama ambavyo wazungumzaji wengi wamezungumza hapa, ukiangalia kwa undani nchi yetu na sheria za nchi yetu zinaeleza kwamba Bunge ndio chombo cha kutunga sheria, lakini utaratibu wa kutunga sheria nchini kwetu umepelekea Bunge kukasimisha kwenye mamlaka mbalimbali kwa ajili ya kulisaidia Bunge kutunga sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu ambao nimeuona kwenye sheria ndogo mbalimbali ni kwamba hawa wenzetu ambao tumewakasimisha kazi ya kutunga sheria na kanuni na miongozo mbalimbali kwa niaba ya Bunge wamekuwa wakifanya mambo haya kama vile hawako kwenye nchi hii hii ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia asilimia kubwa ya sheria ambazo tumekuwa tukikutana nazo kwenye Kamati ya Sheria Ndogo, ukiiangalia unajiuliza hii sheria wakati wanaitunga walishirikisha kweli wadau? Kwa sababu sheria kabla hujaitunga inayoenda kutumika kwa watu ni vizuri ukawashirikisha, kwa sababu haiwezekani kwamba watu wa Misungwi wawe wameshirikishwa kwenye sheria ndogo za Halmashauri ya Misungwi ambazo zinasema kwamba wafunge maduka kuanzia asubuhi mpaka saa tano siku ya Jumamosi. Unakuta Sheria hizi zinatengenezwa na watu wachache, wanajifungia, wanatengeneza vitu ambavyo vinaleta kero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo sababu ya msingi sana ya Bunge letu kama ambavyo baadhi ya wasemaji wameshauri, sheria hizi ndogo ambazo zinatungwa kabla hazijaanza kutumika na kuleta kero kwa wananchi na kuleta usumbufu lazima ziwe na baraka ya Bunge, kwa sababu sisi ndio tunaotunga hizi sheria. Haiwezekani katika uzoefu wangu wa kukaa kwenye Kamati ya Sheria Ndogo nilishakutana na Sheria ya LATRA ambayo ilielekeza kwamba bodaboda zifungwe ving’amuzi, nikawahi kujiuliza hivi aliyekuwa anafikiria kwamba ili kuleta usalama, kuondoa wizi kila bodaboda ifungwe king’amuzi na king’amuzi unakuta kinauzwa zaidi ya shilingi 200,000 alikuwa anafikiria, akifikiria bodaboda za Dar es Salaam peke yake au alikuwa anafikiria na bodaboda za Sumve. (Makofi)

Kwa hiyo, unakuta wenzetu wanafikiria katika wigo mdogo sana na wakati mwingine katika wigo wa upigaji wanatengeneza kanuni ambazo zinatuletea shida kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu mimi kwa Bunge, tuchukue nafasi yetu sisi kama watungaji sheria, tusiruhusu mamlaka yetu ya kutunga sheria yatumike kunyanyasa wananchi kwa sababu ya nafasi tuliyowatolea wenzetu ya kutunga sheria ndogo na kanuni. Mawaziri wanamamlaka ya kutunga sheria kwa kupitia Bunge. Tumewapa kazi yetu tu hawa watusaidie, sasa wanapotunga kanuni ambazo zinanyanyasa wapiga kura wetu ni lazima Bunge lichukue nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maazimio, azimio la kwamba sheria ndogo kabla hazijaanza kazi zije hapa Bungeni, naomba liongezwe ili kuwe kuna tija kwenye utekelezaji wa sheria tunazotunga humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia kidogo pia suala la ajira; nadhani sote hapa tunafahamu, Wabunge wenzangu ni mashahidi mimi nina makablasha na CV za watu wengi sana wanaomba wasaidiwe kupata kazi. Hii ni alama kwamba Watanzania wengi hawana imani na mfumo wa ajira wa nchi hii. Wangekuwa wana imani na mfumo huo wasingekuwa wanataka kupitia mlango wa nyuma kusaidiwa na Wabunge kupata ajira. (Makofi)

Kwa hiyo, Mwenyekiti nakurudisha...

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa tu mzungumzaji Sheria za Ajira katika nchi hii kupitia katika mfumo, siku ya kutangaza kwamba ajira zinatangazwa kwa siku 21 au siku 14; siku moja inakuwa wazi siku 14 zote mifumo inazimwa, halafu wanaajiriwa watu kutoka sehemu moja au watu wenye ndugu muhimu, haiwezekani katika nchi hii. Wabunge tusilikubali jambo hili ahsante, endelea na mchango wako. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mageni unaipokea taarifa hiyo? Sina hakika kama ina ukweli kiasi gani.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo naipokea na ninaomba unitunzie muda wangu, Mheshimiwa Tabasam ametoa taarifa moja nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mifumo ya ajira kama kuna wakati fulani hapa nilisikia Waziri wa Fedha anasema mifumo haina shida. Mfumo wa ajira una shida, watu wanapoomba kazi namna ya kuomba kazi ule mfumo wanasema umezidiwa, lakini wewe Mwenyekiti ni shahidi wote hapa tunatumia mitandao ya simu, inatumiwa na Watanzania wote, kwa nini mifumo ya mitandao ya simu haizidiwi, lakini mifumo ya ajira peke yake ndio inazidiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nafasi za ajira mfano zinaweza zikatangazwa 100; watakuja wanafanya interview, unakuta interview inafanyika kwa watu laki, watu wanakusanywa, wanapoteza muda wao, na baadae inapofika wakati wa kuajiri unakuta hata hizo nafasi 100, ukienda kuangalia kwenye tangazo unakuta wameajiri watu 60, lakini watu walioambiwa wanasifa ya kuajiriwa labda ni watu 300. Kwa hiyo, hapa kuna namna fulani ya upigaji deal kwenye mambo ya ajira. Wale wanaomba kazi wanaona huo upigaji deal, wanaona watu wengi wanapewa wengine hawapewi na hizi ajira kama alivyosema Mheshimiwa Tabasam zimekuwa ni watu fulani tu wa Dar es Salaam, Dar es Salaam hivi, sisi watu wa Bujingwa, wa Mwashilalage hatuhusiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili na sisi tuhusike rudisha kwenye halmashauri huko nafasi za ajira kila halmashauri ipewe, kwa nini majeshi yanaweza, wanaleta kwa mshauri wa mgambo kwenye Wilaya zetu…

MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Haya ya ajira yame…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kasalali hebu hitimisha hoja yako.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti okay.

Haya mambo ya ajira kwa nini yameng’ang’ania makao makuu? Ajira zinatolewa mikoani huko watu wa ku interview wanatoka huku kwenda kule wanaenda na majina yao. Watu wa Kwimba wanaomba kazi hawapewi wale wanaokuja kusimamia hizo ajira wanakuja na majina kutoka Dodoma na sisi watu wa Chanza tunataka ajira hatujaja kusindikiza kwenye hii nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba niunge mkono hoja za Kamati zote mbili na ninaomba maoni ya kwangu yazingatiwe kwenye…

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nami nianze kwa kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Kigua na nijielekeze moja kwa moja katika kuipongeza Serikali kwa hatua ambazo imeanza kuzichukua.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu amewaita watu, amewaita Viongozi wahusika na ametoa maelekezo ya Serikali, nami nishauri kwenye jambo hili la msingi ambalo linaathiri maisha ya watu kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, unapozungumzia suala la kupanda kwa bei za mafuta katika Jimbo la Sumve ni tofauti sana na unapozungumzia jambo hili na Dar es Salaam. Watu wa vijijini unaposema Mwanza mafuta yanauzwa diesel kwa Shilingi 3,300 Sumve ujue yanauzwa kwa shilingi 5,000. Kwa sababu watu wetu hawana vituo vya mafuta wanakwenda kununua kwenye vituo vya mafuta ndiyo wanakwenda kuuziwa huko vijijini, usafiri wetu mkubwa ni bodaboda, kwa hiyo, suala la mafuta sisi pia watu wa vijijini limetuathiri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana mchango wangu mimi wa moja kwa moja ninaiomba Serikali, katika hatua ambazo imeanza kuzichukua jambo la kuondoa tozo za Serikali kwenye mafuta ni jambo ambalo haliwezi kuepukwa. Umefika wakati ni lazima sasa tuacha kugeuza mafuta kuwa sehemu pekee ya kutafuta fedha. Ni lazima tufikirie njia nyingine kwa huu muda hali ya wananchi huko vijijini ni na mijini ni mbaya kwa sababu mafuta yapo juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo hapa nataka pia tuliangalia wakati Serikali inajadili na inafuatilia najua ina vyombo na ina taratibu zake, suala hili la mafuta mimi limenishtua kidogo, kuna bei ya diesel imeizidi bei ya petrol, lakini namna ilivyoizidi kwa Tanzania bei ya petrol nilikuwa naangalia kwa Dar es Salaam ni karibu Shilingi 110 tofauti ya bei diesel na petrol, lakini ukiangalia kwenye soko la dunia tofauti si kubwa kiasi hicho.

Mheshimiwa Spika, mimi ninaona bado kuna shida kwenye namna ya manunuzi ya hii bidhaa ya mafuta. Hili jambo linatakiwa liangaliwe kwa jicho la tatu, inawezekana tunazungumza bei kupanda lakini pia kukawa kunakuwepo bei kupandishwa. Inaweza ikapanda lakini ikapandishwa visivyo kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia Serikali iangalie na kwa kuanzia vigezo vya namna ambavyo hizi taratibu za manunuzi za kupata wazabuni wa kutuletea mafuta zinafanyika. Kwa sababu pia kuna sehemu zinalalamikiwa na humu tulishawahi kushauriwa na baadhi ya Wabunge kufikiria njia mbadala kuhusu namna ya kununua mafuta, tusilazimishe kiwepo chombo kimoja tu cha kununua mafuta. Haya ndiyo madhara na inafika wakati namna ya ku-control inakuwa vigumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo, nashauri kwamba namna ya mafuta haya tunayoyatumia, tunayoyalalamikia kupanda bei, upo umuhimu wa Serikali mbali na kujadili namna ya kupunguza tozo, iangalie namna ya kuona kama kulikuwa kuna utaratibu unaofaa uliotumika kwenye namna ya kupata watu wa kutuletea haya mafuta kwa sababu ya hizo bei ambazo zinamkanganyiko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu...

SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nitumie fursa hii kuwapongeza watu wa Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu moja kwa moja kwa kuwaletea kilio cha watu wa Wilaya ya Kwimba. Tangu mwaka 2019 Serikali ilianza mchakato wa kujenga Chuo cha VETA kwenye Wilaya ya Kwimba katika Mji wa Ngudu ambao ni Makao Makuu ya Wilaya. Ujenzi wa hiki chuo umechukua sasa miaka takribani mitatu na Mheshimiwa Waziri ulikuja ziara kwenye Wilaya yetu ya Kwimba; na alikuwepo pia Mkurugenzi wa VETA aliahidi kwamba watamaliza mapema na Serikali iliahidi watamaliza mapema hakijakwisha mpaka sasa. Sasa sisi watu wa Kwimba hatupendelei sana kuwa na magofu ya kujificha wezi kwa sababu kimekuwa cha muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashauri Wizara ya Elimu, nilifikiri matatizo ya usimamizi yamebaki Serikali za Mitaa, lakini naona na Wizara ya Elimu kwenye usimamizi wa miradi yenu hasa mimi naona mfano wa hiki Chuo cha VETA kilichoko Kwimba, yaani Chuo kinajengwa Kwimba anayesimamia ni Chuo cha VETA Kagera. Hapo unaona kwamba ni kutengeneza maigizo fulani na kukwamisha shughuli za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wanaojenga Chuo cha VETA kwenye Wilaya ya Kwimba badala ya kuwa neema wametuletea matatizo. Kuna wajasiriamali ambao nilisema wakati wa ziara ya Naibu Waziri wametumia fedha zao wameleta kokoto, wameleta mawe mpaka leo hawajalipwa na nilisema na Mkurugenzi wa VETA aliahidi mbele yangu kwamba watalishughulikia, watawalipa. Wamefilisi watu, yaani badala ya kuwa neema imekuwa ni laana. Sasa tuwe serious kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kabisa hawa watu wa Wizara ya Elimu jambo la kumalizia VETA ya Kwimba na jambo la kulipa watu walioshiriki kwenye ujenzi wa VETA hiyo, ambao niliahidiwa kama Mbunge wao siku ya ziara ya Wizara husika, mpaka leo hawajatekeleza, wanawatisha hao watu, wanaomba rushwa na vitu vingine. sasa naomba Wizara ya Elimu wawe serious, walimalize suala la VETA Kwimba watu waanze kusoma lakini, yalipwe madeni ya watu wote wazabuni wa Kwimba walioweka nguvu zao pale. Najua bajeti ilikuwepo, hawawezi kuitisha kokoto wakati hakuna bajeti, vinginevyo tunataka kufilisi watu wetu na kuleta vitu ambavyo havina msingi huko site.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nataka nichangie hapa ni kwamba Wizara ya Elimu ndio uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi yetu, ili nchi iendelee ni lazima fursa na matatizo na vitu vilivyopo kwenye nchi vifahamike. Sasa tunaweza kufahamu vipi matatizo yetu, tunaweza kufahamu vipi fursa zetu na tunaweza kuwa na mbinu gani za kutatua matatizo yetu, kuna kitu kinaitwa utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu ndio wanaosimamia Vyuo Vikuu na Vyuo vya Elimu ya Juu. Vyuo Vikuu ndio kitovu cha utafiti kwenye nchi yoyote inayotaka kuendelelea na nchi yoyote inayotaka kutatua matatizo ya watu wake.

Hata hivyo, nasimama hapa nikiwa na masikitiko, Serikali iliahidi kwamba asilimia moja ya GDP, tutakuwa tunapeleka kwenye utafiti, kitu ambacho hatujakifanya. Utafiti kwenye vyuo vyetu vya elimu ya juu umekuwa ukitegemea fedha za wafadhili, mfadhili hawezi kuleta fedha ambayo haisaidia jambo lake. (Makofi)

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ili sisi tutatue matatizo yetu tunahitaji kuwa na fedha zetu wenyewe.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

MHE. KASALALI E. MAGENI: …na tuziwekeze kwenye utafiti.

T A A R I F A

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba sio tu vyuo vyetu vinategemea fedha ya tafiti kwa fedha za nje, lakini tu hata mtoa fedha akitoa tafiti ili mwanachuo afanyie tafiti, Mwalimu huyo huyo aliyepewa fedha mwanachuo afanye tafiti anamshika hamalizi chuo miaka sita ya PhD. Naomba nitoe taarifa hiyo.

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Mageni.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naipokea hii taarifa. Kwa kuweka msisitizo ni kwamba, hawa wafadhili wanaofadhili utafiti wetu wanawatumia wasomi wetu kutatua matatizo yao. Sisi tunao hawa wasomi, lakini tumeshindwa kuwatumia kutatua matatizo yetu, kwa sababu nafikiri tumeshafikia wakati tumekosa vipaumbele kwenye elimu, kwamba, umefika wakati sasa hata watu wanaoweza kutushauri kufahamu matatizo yetu hatuwapi fedha za kufanya hiyo kazi. Badala yake hao Maprofesa wetu/Madaktari tuliowajaza kwenye Vyuo Vikuu wanatumika na nchi za nje, wanatumika na wafadhili kufanya utafiti kwa ajili ya hao wafadhili badala ya kufanya utafiti kwa ajili ya nchi yetu. Kwa hiyo, nataka niishauri Wizara kwamba nguvu kubwa iwekeze kwenye utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina matatizo mengi, kwa mfano, tatizo moja tu la wizi, ubadhirifu na kukosekana kwa uaminifu kwenye usimamizi wa mali za umma. Tumekuwa tukilalamika huko kwenye halmashauri, tumekuwa tukilalamika kila sehemu, je, tumewahi kuwekeza kwenye utafiti kujua chanzo cha hili tatizo? Kwa sababu, hawa wanaoiba kila siku tunatengeneza CAG nenda kakague, Waziri nenda katumbue, tunaowatumbua ni wasomi wetu, wanaoiba ni wasomi wetu, tumeshatafiti elimu yetu ina msaada gani kenye Taifa letu? Kama inatuzalishia wasomi wanakuwa wezi, wasomi ambao wanahitaji ziara za Waziri awatumbue ndio wafanye kazi, kwa hiyo, hatuwekezi kwenye kutatua matatizo yetu, tunawekeza kwenye vitu ambavyo havina msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumza Waheshimiwa Wabunge hapa kuhusu mfumo wetu wa elimu. Hata mimi ukiniuliza mimi mwenyewe ni mfano, nimesoma form four nafikiri nilisoma masomo 10, ukiniuliza hayo masomo niliyoyasoma kwanza hata nilishayasahau. Yaani tunapoteza muda mwingi kwenye mfumo wa elimu wa kikoloni kupotezea muda watoto wetu mashuleni, badala ya kuweka mfumo ambao unatatua matatizo yetu ya sasa na jibu la haya yote hatufanyi utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika,Nani amefanya utafiti nani amejiridhisha kwamba ni lazima mtoto wa shule ya msingi akae miaka saba shuleni? Atoke hapo aende sekondari miaka minne, aende A Level miaka miwili, halafu sasa hao watu wetu ambao tunawasomesha muda wote huo na wale wanaosoma miaka minne Kenya, tukiwaweka sokoni tunaona tofauti gani? Kwa hiyo ni lazima tufike wakati kama Waheshimiwa Wabunge walivyoshauri kwamba tufike wakati mfumo wetu wa elimu ya msingi na sekondari, tuuangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna sababu ya kuweka watoto shuleni muda wote huo, tunawapotezea muda wanakuja kumaliza vyuo vikuu ni wazee, wanakwenda kazini muda mfupi tu wameshastaafu, lakini muda mwingi wameupoteza wanasoma logarithm, wamesoma kipeuo cha nini, mtoto unakuta amerundikiwa masomo mpaka anachoka kusoma. Unakuta mimi niliyoyasoma O Level nimeshasahau, sina kazi nayo, nakumbuka tu labda niliyosoma Chuo Kikuu machache ambayo niliyafanyia kazi. Kwa hiyo, tutafute tu namna ya kuwapa watoto wetu package ambayo inawastahili kwa ajili ya kutatua matatizo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee pia suala la Bodi ya Mikopo, Waheshimiwa Wabunge hapa wamelizungumzia. Vigezo vya kutoa mikopo imekuwa ni kuangalia umaskini na uhitaji wa mtu. Hawa watu wetu waliopo Bodi wako kama wangapi wangapi hao wana uwezo wa kujua huyu ni maskini na huyu ni tajiri?

Nafikiri tufike wakati tunatengeneza tu utaratibu mwingine wa kuonea watu, mimi Mbunge wa Sumve, kuna watu wengi kule wananilalamikia na ukiwaangalia ni maskini wamenyimwa mkopo. Vigezo vinavyotumika sio rafiki na naamini hatuna nguvu kazi wala wataalam wa kutosha kutafiti na kujua huyu ni maskini, huyu sio masikini. Cha msingi hapa tutafuteni namna ya kusomesha watu wetu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na uzima lakini pia nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu wake, ndugu zangu Aweso na Injinia Maryprisca kwa kazi nzuri sana mnayoifanya kwenye Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Sumve tulikuwa tunahangaika kwa muda mrefu, na tulikuwa tuna kilio chetu, kwamba katika Mkoa wa Mwanza na Majimbo yake tisa, Jimbo la Sumve ndilo lilikuwa Jimbo pekee halina maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria; na kimekuwa ni kilio chetu humu. Tulikuwa kila mara tunajiuliza, hivi tatizo letu sisi ni nini? Hawa wenzetu kwa nini wanayo sisi hatuna mpaka yanataka kuletwa Dodoma? Kumbe tulikuwa hatufahamu siri ya urembo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siri ya urembo ni Mama Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais Samia Suluhu Hassan ndiye amekuja kutuletea maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria kwenye Jimbo la Sumve. Nafikiri ingekuwa tunaruhusiwa kujenga sanamu, alitakiwa ajengewe sanamu na watu wa Sumve. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa jambo hili lililofanyika ambalo nimeliona kwenye bajeti hii, kwa sababu tumeshajua siri ya kupata maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria. Tumeshajua siri ya maendeleo ya uhakika sisi watu wa vijijini, naamini wenzangu kule vijijini ikifika muda wanahitaji kuchagua, hawataacha kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Aweso mimi nimekuwa nikilalamika na Wizara ya Maji kuhusu vijiji vya Sumve kupata maji ya Ziwa Victoria lakini leo nikiangalia kwenye bajeti ninaona kwamba kuna maji yanatoka Hungumalwa yanapitia Mwankulwe yanaenda mpaka Malampaka kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mashimba Ndaki, halafu kutoka Malampaka yanakuja Malya yanaenda kwenye vijiji vyote vya Kata ya Malya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wa Talaga, Mwitambu, Kitunga, Mwamembo na watu wa Kijiji cha Kiminza kwenye Kata ya Lyomo wanapata haya maji. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Jimbo la Sumve maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria hayaishii hapo yanatokea Ukiliguru yanakuja kupita kwenye Kijiji maarufu cha Kolomije yanaenda kwenye Kijiji cha Mantale yanaenda kwenye Kijiji cha Ishingisha yanaenda kwenye Kijiji cha Sumve yanaenda kwenye Kijiji cha Bungulwa na Kijiji cha Isunga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili jambo kwa watu wa Sumve huu ni muujiza waliousubiri tangu dunia iumbwe. Kwa hiyo, nashukuru sana Serikali ya CCM kwa kazi kubwa walioifanya. Mheshimiwa Waziri amefikia kiwango akawaambia watu wa RUWASA wabadili design ili Jimbo la Sumve lipate maji. Walikuwa wanapeleka bomba lenye nchi nane lakini baada ya sisi kusema humu amewaambia wabadili design na tenda imecheleweshwa kutangazwa ili waweke bomba la nchi kumi na wiki ijayo Mheshimiwa Waziri wamesema wanatangaza hiyo tenda ili watu wa Sumve tupate maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria. Hii kwetu ni neema na ni jambo la kujivunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Lakini Mheshimiwa Waziri sisi watu wa Sumve bado tunakushukuru. Upo mpango pia wa kupeleka maji ya Ziwa Victoria kutokea Nyamilama kwenda kwenye Kata ya Lyoma kwenye vijiji vya kina Mweli, Kunguru, Lyoma na Busule. Hili ni jambo la heshima sana kwa wananchi wa Sumve. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiacha haya mambo, Jimbo la Sumve lina kata 15. Hizi kata tunazozizungumzia ni kata tano. Kata 10 ili zipate maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria inabidi yatokee Magu. Naomba Wizara isiusahau mradi wa maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria kuja kwenye kata 10 zilizobaki za Jimbo la Sumve kutokea Magu.

Mheshimiwa Spika, mbali na kuwakumbusha hilo bado tunashukuru. Mimi kwa kweli leo Mheshimiwa Waziri utanisamehe, itabidi leo niwe chawa, yaani nishukuru tuu kwa kiwango kikubwa kwa sababu umefanya kazi ambayo nilikuwa ninaililia kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna miradi kwenye karibu kila kata ya Jimbo la Sumve. Kuna mradi unaendelea kwenye Kijiji cha Ibindo Shilingi Milioni zaidi ya 500. Kuna mradi unaendelea kwenye Kijiji cha Mulya, kuna mradi umeshatangazwa tenda kwenye Kijiji cha Lyoma, kwenye Kijiji cha Wala, Kijiji cha Nkalalo, Kijiji cha Ligembe, Kijiji cha Mulula na Kijiji cha Ng’undya; vyote hivi vinaenda kutengenezewa mradi wa uhakika wa maji ya bomba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri watu wa Sumve umetupa heshima kubwa. Wewe ni Waziri pekee ambaye umekuja tumeanza kunywa na sisi maji ya kutoka Ziwani. Tunategemea tutaanza kuyanywa maana yake zamani ilikuwa ukitaka kuyanywa inabidi ubebe ndoo uende Mwaloni. Sasa hivi tutakuwa tunafungua kwenye mabomba yanatoka.

Mheshimiwa Spika, kitu ambacho nataka kukuomba Mheshimiwa Waziri. Uhakikisho wa hii miradi kufanyika na kusimamiwa vizuri. Tumekuwa tuna shida sana kwenye miradi ya maji. Sisi Sumve kuna mradi unaitwa Waisunga - kadashi na mwabalatulu. Mheshimiwa Naibu Waziri aliwahi kuja mwanzoni kabisa. Siku ile unakuja Mheshimiwa Naibu Waziri walifungua maji yakatoka, ulipoondoka wakafunga. Wakasema watamalizia kuweka mabomba kule Isunga ili yaanze kutoka, hawajamalizia Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa hiyo, bado kunashida. Kuna watu baadhi hawako serious.

Mheshimiwa Spika, Kuna mradi wa Mwabilanda maji yanatoka kwa msimu. Kuna Kamati za Usimamizi wa Maji wanaiba pesa kama hawana akili nzuri. Inafika wakati wanashindwa hata kulipia bili za umeme. Kwa hiyo, iko miradi chechefu ambayo mnatakiwa mtusaidie. Hata hii miradi inayokuja bila kuwa na usimamizi wa uhakika inaweza isiwe na tija.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri najua wewe ni mchapakazi, Jimbo la Sumve sisi tunataka tukuone tu, tukushukuru lakini tukuoneshe pia ambapo panavuja. Kwa hiyo, nikuombe sana ukipata nafasi uje Sumve tukushukuru, tukuoneshe panapovuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kama ambavyo wengi waliotangulia wamesema, kwamba mpango huu ni matokea ya kazi nzuri ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na mipango mingine. Kwa hiyo na mimi naomba niungane nao kwa kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo ameonyesha umahili mkubwa tangu alipoingia madarakani na kuwa na mipango mingi inayotekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuirudisha Tume ya Mipango. Hii ni dalili njema ya kuonyesha kwamba Watanzania tumeamua kupanga, na kupanga ni kuchangua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaona ndugu zangu wawili pale kutoka Iramba, wanaosimamia mpango huu. Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba. Nawapongeza kwa namna ambavyo mmeonyesha kwamba mmejipanga kupanga kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nishiriki kwenye kupanga kwa kuwashauri wapangaji wenzetu. Nadhani wote tunafahamu, ili nchi iendelee inahitaji kuwa na mipango thabiti na endelevu, mipango ambayo Watanzania wakilala wakati wanaamka wanajua nini kitatokea. Kwa hiyo, ninaomba sana Serikali, tunapokubaliana kwamba tumepanga jambo fulani basi sote kwa pamoja tutumie nguvu zetu kulitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutakuwa tunakutana hapa kupanga mipango mipya wakati mipango ya zamani hatujaitekeleza, tutakuwa hatutendi haki. Kwa hiyo, niaombe sana ambao mmepewa dhamani hii ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza maono yake kwenye taifa hili, mhakikishe kwamba kila tunachokipanga mnakisimamia kinatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nitoe mfano mdogo, kwa sababu mimi ni moja ya Wabunge wengi wanaotoka vijijini. Mazingira ya vijijini kidogo nayafahamu. Vijiji vyetu wakazi wake wengi ni wakulima na wafugaji. Wakulima wanalima mazao ambayo ni malighafi za viawanda na mazao mengine yanasafirishwa yakiwa ghafi hivyo hivyo kwenda nje ya nchi na kulipatia taifa fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vyetu vinapata malighafi kutoka mashambani kwa asilimia kubwa. Mazao ambayo yanaenda nje moja kwa moja bila kuchakatwa kama hii wanaita korosho, choroko, dengu na pamba inachakatwa kidogo inapelekwa nje; mazao yote haya ni chanzo kikubwa cha mapato ya nchi yetu. Kwa hiyo ni lazima wote tujipange katika mopango yetu kuhakikisha mazao haya yanakuwa na tija. Tija kwa Serikali kukusanya fedha lakini tija kwa wakulima wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tuna shida moja kwenye kupanga. Maeneo ya vijijini ambako mazao haya yanatoka tumekuwa tukiyasahau. Kwa hiyo nataka niwakumbushe wenzangu, na nitumie mfano huu kumkumbusha kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu; tangu niwe Mbunge wa Sumve na tangu awe Waziri wa Fedha kwenye kila mpango na bajeti tumekuwa tukizungumza kuhusu Miundombinu katika Jimbo la Sumve. Kaka yangu huyu amekuwa mtu mwema sana kwangu. Amekuwa ananiahidi na kuonyesha kwamba atafanya. Kwa kweli kwenye kuniahidi na kunionyesha kwamba utafanya, mimi nakupa big up kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi zimekuwepo za uhakika lakini hazitekelezwi. Kwa hiyo ndugu yangu ili twende pamoja na ili tuanzishe mpango mwingine ahadi yako uliyonipa hapa tarehe 22 Juni, 2022, ya kwamba utanijengea kilometa zangu 71 za kutokea Magu – Bukwimba – Ngudu mpaka Nhungumalwa, kwa kiwango cha lami na ukaniambia umepata na mkopo, jenga basi. Ili mpango huu uende uje na mwingine. Lakini kama tutakuwa na mpango ule ule hautekelezwi halafu Watanzania hawa hawa tunakata tena Wabunge wao wasimame wapange mipango mingine inakuwa siyo sawa. Naomba na ninasisitiza kwamba tilichokipanga tukitekeleze (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Kitila Mkumbo akiwa back bencher huku, aliwahi kusema hapa kuhusu Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Madiwani. Kwamba, wale ndio wanaosimamia fedha zetu kule vijijini. Mheshimiwa Ng’wasi Kamani amesisitiza hapa kuhusu Ripoti ya CAG, na kwa mfumo wetu wa Bunge kuna Kamati Maalum kabisa inakagua Hesabu za Serikali za Mitaa. Kwa nini Kamati hiyo inazikagua? Na kwa sababu fedha nyingi tunazipeleka kule na kwa mujibu wa mfumo wetu Waheshimiwa Madiwani ndiyo wasimamizi wa hizo fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiamua wenyewe kupiga mpira, tunajirudishia pasi na tunajipiga chenga wenyewe. Wale wanaotakiwa kusimamia fedha hizi hayujawawezesha. Kwa hiyo Mheshimiwa Halima Mdee na Kamati yake wataendelea kila siku kutuletea madudu hapa na Serikali itaendelea kulalamikia wizi na Waheshimiwa Mawaziri mtaendelea kupanga kupeleka fedha na kutumbua watu kama hamjajipanga kuweka walinzi halisi wa hizi fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia Taarifa za Serikali. Naona juzi kuna nyaraka ilitoka ambayo inawa-exclude Wenyeviti wa Halmashauri kwenye kusaini mikataba. Sijui tunaona shida gani kama Madiwani watasimamia ile mikataba. Yaani tunataka Wakurugenzi wetu hawa ambao wakati mwingine hawana uwezo wa kutosha kufanya kazi ya ukurugenzi kwa sababu hawana uzoefu, waende kwa kutumia vichwa vyao wasaini mikataba bila kusimamiwa na Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatengeneza mwanya wa fedha zetu tunazozipeleka huko, ziende zikapotee. Kwa hiyo, mimi naomba niishauri Serikali kwamba, baada ya kupanga kutafuta fedha na kupeleka maendeleo, pia tupange kulinda na kuzisimamia fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nataka kuzungumzia Sekta ya Utalii. Sekta ya Utalii ni sekta ambayo inatuingizia mapato mengi sana; na wote tunafahamu kwamba tuna mbuga nzuri kabisa ya Serengeti na mbuga zingine, lakini wote tunafahamu kutokea Mwanza kwenda Serengeti ni karibu zaidi kuliko popote pale katika viwanja vya ndege nchini. Uwanja wa Ndege wa Mwanza uko karibu zaidi na Serengeti, lakini kwa nini watu hawautumii? Kwa sababu Serikali haijapanga kuuboresha uwanja ule kuufanya uwe wa Kimataifa. Kwa hiyo, hautumiki na sekta yetu ya utalii inakuwa imeng’ang’ania eneo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitokea Mwanza, ukaenda kwenye Jimbo la Kisesa kwa kaka yangu Mheshimiwa Mpina, pale Mwandoya ukaongea na wananchi kuhusu wanyama pori, ni viumbe anaowachukia kuliko viumbe wowote. Wanajiuliza kwa nini tunafuga tembo ambao wanaharibu mazao yao na wanaua watu wao. Kwa sababu hawafaidiki kabisa na huu utalii, lakini Serikali imeamua kuyatelekeza maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupanga sekta ya utalii, wekeni miundombinu ya kiutalii Mwanza. Kuna barabara za msingi kabisa za kiutalii. kwa mfano ukitokea Bujingwa kupitia Nyambiti kwenda Malya, ukaenda Ngulyati, ukaenda Itilima, ukaenda Mwandoya mpaka Sakasaka kwenye geti lile la Maswa Game Reserve ni karibu zaidi kuliko mtu atokee KIA mpaka aje huku. Sasa kwa nini hizi barabara hamziboreshi, hamzijengi halafu tunakutana hapa tunapanga kuboresha sekta ya utalii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba niishauri Serikali kwamba, sasa imefika wakati Maeneo ya Kanda ya Ziwa nayo yaboreshwe ili kukuza sekta ya utalii na iwe na manufaa kwa Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na uzima. Pia nakupongeza wewe kwa namna ambavyo unakiongoza kikao hiki vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na njema, ya maana anayoifanya kwa Watanzania, kwa bajeti ambazo amekuwa anatuletea hapa na sisi tukizipitisha na namna ambavyo zinaonyesha matunda chanya kwa Watanzania wa mijini na vijijini. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye leo bajeti yake ndiyo tunaijadili hapa. Amekuwa ni mtu mwema, mchapakazi, msimamizi mwema na msaidizi mwema wa Mheshimiwa Rais na Watanzania wote. Nampongeza kwa jambo hilo na ninaomba nitumie nafasi hii kumtia moyo yeye na Waheshimiwa Mawaziri wanaofanyanao kazi ofisini kwake; Mama yangu Mheshimiwa Jenista na Manaibu wake wote, Mheshimiwa Deogratius na Naibu Mawaziri wengine wote kwa kazi nzuri wanayoifanya. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mniruhusu nizungumze maneno machache ya kushauri namna bora ya kuwahudumia Watanzania, na kwa sababu leo tunazungumza na Ofisi ya Msimamizi wa Mawaziri wote, naamini kupitia yeye watanielewa na kutekeleza yale ambayo nitayashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilichonileta humu ndani ni wananchi wa Sumve ambao walinipigia kura, na kuna mambo niliwaambia nitafanya kwa kushirikiana na Serikali kwa kuishauri. Sasa yale mambo ambayo tumekuwa tukiwashauri na kusimamia Serikali, tunashukuru yamefanyika mengi, lakini kuna jambo la msingi sana kwenye Jimbo la Sumve naliona kama vile haliko sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii ni ya kwetu sote. Watanzania wote tunalipa kodi na tunategemea maendeleo yanapokwenda kwa Watanzania yaende walau kwa kuangalia kila eneo linapata nini? Maendeleo yanapokuwa yanajazana labda Dar es Salaam, tunaona sijui trilioni ngapi zinajenga mwendokasi, halafu Sumve tangu niwe humu, leo ni mwaka wa nne huu Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waheshimiwa Mawaziri wake wamekuwa wakinisikia nikisema kwamba kuna Jimbo kule linaitwa Sumve halina hata milimita moja ya lami. Halafu nikimaliza kuongea hivyo, anatokea Mheshimiwa Waziri anayehusika anatoa ahadi lukuki na hatekelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeanza kuzungumzia suala la Wilaya yetu ya Kwimba kuunganishwa kwa lami na Mkoa wa Mwanza tangu nilipoingia humu, sioni utekelezaji, naona majibu yasiyotekelezwa. Nimeanza kuhangaika na Mheshimiwa Dkt. Chamuriho akiwa Waziri wa Ujenzi, akawa ananikalisha pale kwenye kiti chake kila siku ni ahadi lakini hakuna kitu. Nikaenda kwa Prof. Mbarawa, akapata hiyo nafasi, tena yeye tulikwenda ofisini kwake Wabunge wote wa Mwanza, tukaahidiwa, lakini hakuna kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi yupo kaka yangu Mheshimiwa Bashungwa, naye hakuna kitu. Nikiongea nao wananiambia michakato ya manunuzi, na kadhalika. Yaani wananchi wa Sumve na watu wa Kwimba hawajui hayo mambo ya upembuzi yakinifu na hayo manunuzi. Wanachojua ni lami itokee Magu ipite Bukwimba iende mpaka Hungumalwa, tuunganishwe na sisi. Wanachojua ni lami itokee Fukalo ije Nyambiti iende Malya ili iunganishe na mnyororo wa utalii wa Mbuga ya Maswa na Mbuga ya Serengeti tufaidike na utalii. Sasa hatuwezi kuendelea hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka nikichangia bajeti yangu ya pili, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, Waziri wa Fedha wakati ule aliniandikia mpaka memo ya kuniambia kwamba, tunajenga hivi na hivi. Baadaye tena wakasema sijui wanakopa nini? Yaani hawajengi, kila siku ni story tu. Sasa wananchi wa Sumve wameniambia hivi, ukifika Bungeni kwa heshima waliyonayo na Ofisi ya Waziri Mkuu na namna ambavyo mambo yanakwenda, wewe nenda ukaunge mkono bajeti ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama itafika bajeti ya ujenzi, halafu hakuna mambo yanayoeleweka, usiiunge mkono. Watu wa Ujenzi niko very serious kwenye hili. Very serious, na sitaki mchezo. Wananchi wa Sumve wanataka na wenyewe wawe na lami. Haiwezekani ninyi kwenye Majimbo yenu mna lami, sisi hatuna halafu bado tunakuja humu wote tunaitana Wabunge. Ni lazima tuheshimiane kabisa. Hatuwezi kuwa tunakuja hapa tunaahidiwa vitu ambavyo havitekelezwi. Haiwezekani. Ni bora sasa sisi watu wa Sumve tuambiwe hatuhusiki humu. Kitu cha msingi hapa tunataka lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu waambie Mawaziri wako wanaohusika, waache kuwapa ahadi hewa watu wa Sumve. Nami Mbunge wa Sumve sitaki ahadi hewa kwa niaba ya wananchi wangu. Tunataka na sisi tujengewe barabara ya lami, story za kilometa 10 mnazotuambia ambazo na zenyewe hamjengi, sisi hatuko interested na kilometa 10 za kulambishwa lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka lami ambayo itatufanya na sisi tuweze kwenda mjini na magari yetu mazuri, lakini hii namna ya kutufanya sisi tuwe tunatuma nginjanginja, ninyi mnatanua na magari mazuri mjini, haipo. Watu wa Sumve wameniambia kuhusu miundombinu mtatusamehe, tunataka barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hilo naomba nihamie kwenye suala lingine la ushauri tu. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa kuhusu suala la kikokotoo. Kwanza, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa hatua ambazo amezichukua na maelekezo ambayo amekuwa akiyatoa na kuonesha moyo na nia ya kutamani jambo hili liende na liishe vizuri ili watumishi wetu waishi kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kikokotoo linakuja kwenye hoja ya kwamba ukiliangalia kwa undani lina hoja, kwamba watumishi wetu uwezo wao wa kutunza pesa na kupanga matumizi ya pesa ni mdogo. Ndiyo hoja ya kikokotoo inakuja hapo. Yaani watu wakipewa hela zao hawataweza kuzitumia vizuri, hawatazitunza vizuri, kwa hiyo, sisi Serikali tuwatunzie, tutawapa kidogo kidogo. Ndiyo hoja yenyewe ukiiangalia ukubwa wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka tujadiliane hapa kwa kushauriana, hawa watumishi ndiyo leo wako kwenye maofisi, ndiyo leo wanatuletea makabrasha yote tunajadili bajeti hapa, ndiyo leo wamepanga kila kitu huko, ndiyo hao wanaolinda nchi yetu na ndiyo hao wanafanya kila kitu, lakini tukifika wakati wanastaafu sasa, maana unajua huwa tunasema kwenye utumishi tunataka experience. Hawa watu mpaka wamestaafu wana uzoefu na matumizi ya pesa, wana uzoefu na maisha na wanajua wanafanya nini. Eti sasa wakishazeeka tunawaona hawa hawawezi kutunza pesa zao, tuwatunzie tuwe tunawapa pole pole. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye logic inaonekana kwamba siyo jambo jema. Jambo hili sisi tunasema ni zuri. Kuna wakati niliambiwa hapa sijafanya utafiti, lakini ukweli ni kwamba huko site hili jambo halijaingia kwenye vichwa vya watumishi, yaani limefeli na hawalielewi na wale ambao wamelazimika kuingia kwenye kikokotoo, wengi imewa-frustrate, wengi wanakufa kabla ya muda.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kasalali, ahsante sana.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iliangalie jambo hili kwa jicho lingine. Nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na uzima, lakini nitumie fursa hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amir Jeshi Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya kwenye kuboresha vyombo vilivyochini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Pia, nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Waziri Kaka yangu Masauni kwa kazi nzuri anayoifanya akisaidiana na Mheshimiwa Sillo, Wizara inakwenda vizuri sana, nawapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiacha hayo naomba nitumie nafasi hii kushauri machache kwenye hii Wizara nyeti na hasa nitashauri kwenye Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Askari wetu Polisi na Vitengo vyao vyote wanafanya kazi nzuri sana. Mimi kama mdau wao kazi wanayoifanya ni nzuri sana inahitaji kupewa moyo na kusahihishwa pale wanapokosea kwa sababu nao ni binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama wahudumu wao kwenye maslahi yaani Serikali na Bunge tunaopitisha bajeti, naomba niishauri Wizara iangalie sana maslahi ya askari polisi, waangalie mishahara yao, waangalie allowance zao, kwa sababu tumekutana na changamoto huko wanasema ration allowance kuna wakati inalipwa tarehe 40 badala ya kulipwa tarehe 15 na nafikiri kuna mambo mengi kwenye maslahi ya askari ambayo Mheshimiwa Waziri naomba sana ayaangalie. Askari wetu wanafanya kazi nzuri na sisi tufanye kazi nzuri kuwapatia maslahi mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jeshi la Polisi nakumbuka Mheshimiwa Rais akiwa anazungumza nao pale Kilwa alizungumza kuhusu kero ya kikokotoo kwa askari wetu. Kikokotoo kipo cha aina mbili, kuna kikokotoo ambacho kiko kwa watumishi huku, lakini Mheshimiwa Rais alisema Jeshi la Polisi linatakiwa liwepo kwenye utaratibu wa majeshi mengine. Majeshi mengine hayaingii kwenye huu utaratibu wa kikokotoo wa utumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niiombe Wizara ifahamu kwamba maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Rais alielekeza yale maelekezo kama Amiri Jeshi Mkuu na maelekezo ya Amir Jeshi Mkuu yanatakiwa yatekelezwe sio yajadiliwe. Niwaombe Wizara na niwatake wakatekeleze maelekezo haya, wakaangalie namna bora ya kuliondoa Jeshi la Polisi kwenye mambo haya ya kikokotoo wakati tunashughulika na kuondoa watumishi, lakini askari polisi wanatakiwa waingie kwenye utaratibu wa majeshi ili waachane na hii kero ya kikokotoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunayo changamoto ya makazi ya askari polisi. Kwenye Wilaya ya Kwimba ambako mimi natoka, askari wana tatizo kubwa la makazi. Kwa hiyo, naomba Wizara watuongezee bajeti ya kujenga makazi ya Polisi kwenye Wilaya ya Kwimba, lakini na nchi nzima. Vitendea kazi kama magari Wilaya ya Kwimba ina majimbo mawili, lakini gari zima linalotembea tena kwa kusukumwa ni moja, sasa askari wetu watafanyaje kazi kwenye mazingira hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri ndugu yangu Masauni, najua ni msikivu, askari bado wanahitaji vitendea kazi. Askari kata wanahitaji pikipiki, askari polisi mbali na vitendea kazi tatizo la uniform ni kubwa. Wanajishonea uniform zao, sasa utaratibu wa kawaida unataka askari ajishonee uniform zake, unataka makazi yake yawe ya chumba kimoja na jiko halafu maslahi yake sio mazuri, mwisho wa siku tunawavutia hata kuingia kwenye hizo tunazozisema rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inafika wakati sisi tunalalamika tu wao wanakula rushwa, lakini hatuangalii mazingira wanayofanyia kazi. Ni wajibu wetu kama Serikali kuhakikisha askari wetu wanakuwa na mafuta ya kutosha kwenye vituo vya polisi ikitokea kuna mhalifu wanawasha gari wanaenda kukamata. Sasa mtu ameenda kushtaki kuna mhalifu, polisi wanamwomba mafuta kwa sababu hawana hayo mafuta. Sasa hayo mafuta ya kujaza kwenye gari yeye ayatoe wapi. Kwa hiyo kuna vitu lazima tuvichukulie very serious. Hizi rushwa na kero za vituoni wakati mwingine tunasababisha sisi kwa kutokuhudumia vizuri Jeshi letu la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mageni.

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi hii. Kabla sijaenda kwa undani zaidi nimshukuru Mwenyezi mungu kwa uhai na uzima. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na wasaidizi wake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya, kuanzia kwenye bajeti kuu walipotuwasilishia ilikuwa nzuri, ina mwelekeo wakutatua hoja na shida za Watanzania na kwenye hii Sheria ya Fedha pia imejielekeza katika kutengeneza mazingira ya kukusanya pesa kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hii sheria katika vifungu vingi na maelezo mengi na mabadiliko mengi, mabadiliko yaliyofanyika ni mabadiliko rafiki kwa maendeleo yetu na hoja ambazo zilikuwa zinatolewa na Wabunge tangu tuanze kujadili bajeti, tangu Bunge la Bajeti likae mambo mengi yamejibiwa hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nijielekeze kwenye jambo moja, kwa hiyo nitachangia mahususi kwenye hii Sura ya 220, vifungu vya 46 na 47. Hapa kuna hii Sheria ya Barabara na Fuel Toll, ambayo inazungumza kuhusu pesa Sh.363 ambazo zinakusanywa kwenye kila lita ya mafuta. Katika hizi pesa Sh.100 ambayo imeongezwa inakwenda moja kwa moja TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kushauri hapa, kwanza niishukuru Serikali kwa kui-ring fence hii Sh.100 kwamba hii moja kwa moja inakwenda TARURA, inamaana inabakia shilingi 263.09. Sasa hii shilingi 263 iliyobaki, kabla ilikuwa inakusanywa, kabla ya kuongezwa hii Sh.100, asilimia 30 ya hii pesa ilikuwa inakwenda TARURA, inaingia kwenye Mfuko wa Barabara inakwenda TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mazingira ambayo nayaona hii shilingi 78 ambayo ni asilimia 30 ya hii shilingi 263, tusipoiwekea utaratibu mzuri, tunaweza tukajikua tunatumia hii shilingi 100, na hii shilingi 78 ambayo tumeiwacha kwenye ule utaratibu wa asilimia 30 ambayo sheria katika kipengele “A” ambacho tumekirekebisha, imeeleza kwamba Waziri kwa kushauriana na Waziri wa TAMISEMI wataamua namna ya kutumia hii Sh.263, sisi tunasema ni 30 kwa 70, baina ya TANROADS na TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nina pendekezo, kwamba hii asilimia 30 na yenyewe ambayo ni Sh.78, tuijumlishe na Sh.100, ziwe Sh.178, tuzi-ring fence, tuzipeleke moja kwa moja kwenye Mfuko wa TARURA.

Kwa hiyo napendekeza badala ya kupeleka kwenye Mfuko wa Barabara, kama nafasi inaruhusu na mazingira yanaruhusu, tupate Mfuko wa Barabara Vijijini. Mfuko huu uwe unapelekewa hii pesa moja kwa moja, ili kuepuka matatizo yaliyokuwepo awali. Kwa sababu awali tulikuwa tunapanga bajeti za TARURA na hii ipo, lakini mara nyingi bajeti za TARURA zilikuwa hazifikii malengo. Mara nyingi pia tulikuwa tunaacha uwazi wa hii asilimia 30, hii Sh.78, tunakuwa hatuna uhakika kwa asilimia zote kama yote imekwenda TARURA. Sasa ili tuwe na uhakika kwamba tumeongeza Sh.100, tumeongeza na Sh.78, hizi Sh.178.09 zote zinaenda kwenye Mfuko wa Barabara Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la TARURA tulilipiga kelele sana kwa sababu ni swala ambalo linatoka kwa wananchi wa vijijini moja kwa moja, barabara za vijijini hazipitiki na bajeti hii ya TARURA ilikuwa haikidhi mahitaji. Sasa tumeongeza Sh.100 na hii 78 zote tuzipeleke kule. Mheshimiwa Waziri hizi pesa za TARURA tunashauri sasa ufike wakati tuwe tunazipeleka kwa asilimia mia moja. Leo ninavyozungumza kwenye Jimbo la Sumve, tumepokea asilimia 91, asilimia ile iliyobaki kuna barabara muhimu sana zimeshindwa kumaliziwa ambazo zilikuwa kwenye bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Barabara ya kutoka Nyambui kwenda Manda na Barabara ya kutoka Mwitambu kwenda Kiminza zilikuwa kwenye pesa milioni zaidi ya 77 zimebaki. Hili ni chomekeo kuonyesha ni kiasi gani fedha za TARURA, zisipowekewa utaratibu tutakuwa hatutekelezi yale matakwa ya kupeleka barabara vijijini zikapitike. Sasa tunaishukuru sana Serikali kwenye upande wa TARURA, kwa kweli mwaka huu mmetupa raha, kama ambavyo wengi wamesema milioni 500 tumeshapewa, tumeshaahidiwa bilioni moja huko mbele, mambo ni mazuri, lakini sasa kwenye hili naomba tuweke sheria na utaratibu ambao utaifanya hii pesa moja kwa moja iende TARURA ikatumike kujenga barabara za vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)