Primary Questions from Hon. Kasalali Emmanuel Mageni (10 total)
MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza: -
Je, ni lini barabara ya kutoka Magu – Bukwimba hadi Ngudu itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuu nganisha Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba na Makao Makuu ya Mkoa wa Mwanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu Swali la Mheshimiwa Emmanuel Mageni Kasalali, Mbunge wa Sumve ,kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya kutoka Magu – Bukwimba hadi Ngudu ni sehemu ya barabara ya Mkoa yenye urefu wa kilomita 71 inayoanzia Magu – Bukwimba – Ngudu hadi Hungumalwa. Barabara hii nikiunganisha muhimu kati ya Wilaya ya Magu na Kwimba kupitia Isandula (Magu) – Bukwimba – Ngudu – Nyamilama hadi Hungumalwa.
Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha kazi ya Upembuzi yakinifu na Usanifu wa Kina kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Magu – Bukwimba –Ngudu hadi Hungumalwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 71. Kazi hii ilifanywa na Mhandisi Mshauri M/s Advanced Engineering Solution kwa gharama ya shilingi milioni 638.486 na kukamilika mwaka 2019. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha za kugharamia ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha, Wizara yangu kupitia TANROADS inaendelea kuihudumia barabara hiyo ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2020/ 2021 jumla ya Shilingi milioni 475.551 zilitengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii.
MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Jimbo la Sumve?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kasalali Emmanuel Mageni, Mbunge wa Sumve kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, huduma ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Kwimba kwa kutegemea visima virefu ni asilimia 72 ambapo Vijiji vya Mwabaratulu, Nyashana na Sumve Mantare, Ishingisha, Mwabilanda, Nyambiti, Isunga, Kadashi na Malya vinapata huduma ya maji kutoka kwenye vituo 122 vya kuchotea maji na wateja wa majumbani ni 1,208.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali itakamilisha usanifu wa kina wa mradi wa maji kwa ajili ya kuhudumia Miji Midogo ya Malampaka, Malya na Sumve na vijiji katika maeneo hayo ambavyo huduma ya maji haitoshelezi. Usanifu huu unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Desemba, 2021 na utekelezaji wa mradi utaanza kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Jimbo la Sumve?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kasalali Emmanuel Mageni, Mbunge wa Sumve kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, huduma ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Kwimba kwa kutegemea visima virefu ni asilimia 72 ambapo Vijiji vya Mwabaratulu, Nyashana na Sumve Mantare, Ishingisha, Mwabilanda, Nyambiti, Isunga, Kadashi na Malya vinapata huduma ya maji kutoka kwenye vituo 122 vya kuchotea maji na wateja wa majumbani ni 1,208.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali itakamilisha usanifu wa kina wa mradi wa maji kwa ajili ya kuhudumia Miji Midogo ya Malampaka, Malya na Sumve na vijiji katika maeneo hayo ambavyo huduma ya maji haitoshelezi. Usanifu huu unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Desemba, 2021 na utekelezaji wa mradi utaanza kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza: -
Je, ni lini barabara ya kutoka Magu – Bukwimba hadi Ngudu itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ili kuunganisha Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba na Makao Makuu ya Mkoa wa Mwanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Mageni Kasalali, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Magu – Bukwimba hadi Ngudu ni sehemu ya Barabara ya Magu – Bukwimba – Ngudu hadi Hungumalwa yenye urefu wa kilometa 71. Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii tangu mwaka 2019. Baada ya kukamilika kwa usanifu Serikali inaendelea kutafuta fedha za kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya Shilingi milioni 596.576 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali. Ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza: -
Je, ni lini barabara ya Fulo kupitia Nyambiti hadi Malya itafanyiwa upembuzi yakinifu na kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kasalali Emmanuel Mageni, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha za kuifanyia Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina barabara ya Fulo – Sumve – Nyambiti hadi Malya kwa lengo la kuijenga kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikitafuta fedha za Usanifu, Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili kuhakikisha kuwa inapitika vizuri majira yote. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya shilingi milioni 668.345 zimetengwa kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hiyo. Ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza: -
Je, ni lini barabara ya kilometa 73 kutoka Fulo – Nyambiti – Malya itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kasalali Emmanuel Mageni, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara ya Fulo – Nyambiti – Malya yenye urefu wa kilometa 73 wakati wowote pindi fedha itakapopatikana. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kazi hii. Ahsante.
MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza: -
Je, lini Serikali itahakikisha tatizo la kutokuwepo mawasiliano ya simu ya uhakika katika maeneo mengi ya Jimbo la Sumve linatatuliwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kasasali Emmanuel Mageni, Mbunge wa Jimbo la Sumve kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imefikisha huduma za mawasiliano katika Kata za Bugando, Lyoma, Mwandu, Ngulla na Sumve.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itafanya tathmini katika Jimbo la Sumve ili kubaini maeneo ambayo bado yana changamoto za upatikanaji wa huduma za mawasiliano ili yatafutiwe fedha kwa ajili ya kutatua changamoto hizo.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA K.n.y. MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza: -
Je, ni kwa nini Serikali isiyaondoe mazao ya choroko na dengu kwenye utaratibu wa stakabadhi ghalani kwani utaratibu huo umekuwa kero kwa wakulima na wanunuzi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Mageni Kasalali, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unawezesha uuzaji wa mazao kwa ubora na bei ya ushindani, kupata takwimu sahihi za uzalishaji za mauzo na kuchochea uzalishaji. Mathalani, katika msimu wa mwaka 2020/2021 jumla ya kilo 14,394,077 za choroko zenye thamani ya shilingi bilioni 18.7 ziliuzwa kwa mfumo wa Stakabadhi za Ghala ikilinganishwa na kilo 1,130,453 zilizouzwa katika msimu wa mwaka 2019/2020 katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Singida.
Mheshimiwa Spika, zao la choroko, dengu na mazao mengine yataingizwa kwenye mfumo wa stakabadhi kwa kuzingatia vigezo muhimu vya uwepo wa ghala, waendesha ghala, elimu kwa wadau wa mfumo na mazingira ya soko kwa wakati husika.
MHE. SUMA I. FYANDOMO K.n.y. MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha mchakato wa kuanzisha Halmashauri ya Wilaya ya Sumve ili kusogeza huduma kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kasalali Emmanuel Mageni, Mbunge wa Jimbo la Sumve, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala upo kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa Sura ya 287 na 288 pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa Mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, maombi ya kuanzisha Halmashauri mpya yanatakiwa kujadiliwa, kuridhiwa na kupitishwa kwenye vikao vya kisheria ngazi ya Vijiji, Kata, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Kamati ya Ushauri ya Mkoa kisha kuwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa tathmini ya vigezo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika kuboresha na kukamilisha miundombinu msingi kwenye maeneo ya kiutawala yaliyopo ili yaweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na baadaye kuendelea na maeneo mengine kwa kufuata taratibu na vigezo vilivyoainishwa, ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA K.n.y. MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Shule ya Sekondari Kata ya Malya, Kitongoji cha Mwashilibwa ili kuongeza huduma Vijiji vya Mwitemba, Talaga na Kitunga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) inaendelea na ujenzi wa shule za sekondari kwenye maeneo ya kata yasiyo na shule na maeneo yenye msongamano wa wanafunzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa shule ya sekondari ya mikondo miwili kupitia Mradi wa SEQUIP awamu ya tatu katika Jimbo la Sumve unatekelezwa katika Kata ya Malya, Kijiji cha Kitunga. Serikali itaendelea kujenga shule katika maeneo yasiyo na shule ili kuwarahisishia wanafunzi kupata elimu katika mazingira ya karibu na nyumbani kwao. (Makofi)