Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Deodatus Philip Mwanyika (22 total)

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA Aliuliza:-

Je, ni lini mradi wa kusambaza maji Mji wa Njombe kutoka Mto Hagafilo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilipata mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim India jumla ya Dola za Marekani millioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika miji 28 Tanzania Bara na Zanzibar. Moja ya miji itakayonufaika na mkopo huo ni Mji wa Njombe, kwa sasa mradi upo katika hatua za manunuzi na tunatarajia Wakandarasi watakuwepo eneo la mradi kwa ajili ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi ifikapo mwezi Aprili, 2021 na ujenzi wa mradi utachukua miezi 24.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA Aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kumaliza tatizo la upungufu wa Walimu nchini, hasa shule zilizopo maeneo ya vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu katika shule za msingi na sekondari, kuanzia Disemba 2015 hadi Septemba 2020, Serikali imeajiri walimu 10,666 wa shule za msingi na walimu 7,515 wa shule za sekondari na kuwapanga kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa. Aidha, kuanzia mwezi Desemba 2015 hadi Septemba 2020, Halmashauri ya Mji Njombe imeajiri walimu 21 wa shule za msingi na walimu 111 wa shule za sekondari. Vilevile Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaajiri walimu wapya 6,000 wa shule za msingi na sekondari ifikapo Juni 2021 ili kujaza nafasi zilizoachwa na walimu waliofariki ama kustaafu kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kupitia ofisi za wakuu wa mikoa imekuwa ikifanya uhamisho wa ndani kwa kuwahamisha walimu waliozidi hasa kwenye maeneo ya mijini na kuwapanga kwenye shule zenye uhaba mkubwa wa walimu ambazo nyingi zipo maeneo ya vijijini. Serikali itaendelea kuajiri na kuwapanga walimu kwenye shule za msingi na sekondari hasa zenye mahitaji makubwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, ni lini Vijiji na Vitongoji nchini ambavyo havijapatiwa umeme vitapatiwa huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) inaendelea kutekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini Awamu ya III mzunguko wa pili. Mradi huu unatarajiwa kufikisha miundombinu ya umeme katika vijiji vyote 1,974 ambavyo havijapata umeme kati ya vijiji 12,268 vya Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika, mradi huu pia utafikisha umeme katika vitongoji 1,474 ambavyo havijafikiwa na umeme. Mradi ulianza mwezi Machi, 2021 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba, 2022. Gharama ya mradi ni takriban bilioni 1,176.

Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme katika vitongoji ni endelevu. Serikali kupitia REA na TANESCO itaendelea kupeleka umeme katika vitongoji vyote mwaka hadi mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa uwanja mpya wa ndege katika Mji wa Njombe utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): alijibu

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanja cha ndege cha Njombe ni miongoni mwa viwanja 11 vya ndege vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Transport Sector Support Project (TSSP). Viwanja hivyo 11 ni pamoja na Lake Manyara, Musoma, Songea, Kilwa Masoko, Tanga, Iringa, Lindi, Moshi, Singida, Njombe na Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hatua ya awali ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika, Serikali imejipanga kuanza ujenzi kwa hatua mbalimbali kwa awamu kwa kutumia fedha za ndani, lakini kutokana na ukweli kwamba gharama za ujenzi wa viwanja hivyo ni kubwa ukilinganisha na bajeti inayotolewa kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia bajeti, Serikali kupitia TANROADS imejipanga kuanza na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Iringa na Songea. Ujenzi wa viwanja vilivyobaki kikiwemo cha Njombe utaanza mara Serikali itakapopata fedha. Aidha, kwa sasa Serikali inaendelea kuwasiliana na washirika wa maendeleo ili kuweza kupata fedha za kujenga viwanja hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maelezo hayo hapo juu, namuomba Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika pamoja na wananchi wa Njombe Mjini waendelee kuvuta subira kwani Serikali ina nia ya dhati ya kujenga kiwanja hicho.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Zahanati ya Ihalula kuwa Kituo cha Afya baada ya kukidhi vigezo vyote kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali iliipandisha hadhi zahanati ya Ihalula kuwa Kituo cha Afya mwaka 2018/2019 na kupewa namba ya utambulisho 101604-7. Aidha, Serikali katika mwaka wa fedha 2017/2018 ilipeleka Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ukarabati wa majengo mengine likiwemo jengo la upasuaji ambalo sasa linatoa huduma.

Mheshimiwa Spika, Kituo hiki kimekuwa kikilipwa fedha za Mfuko wa Bima ya afya kama zahanati kutokana na baadhi ya taratibu ambazo zilikuwa hazijakamilika.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zimekwishalifanyia kazi na barua rasmi itapelekwa ndani ya mwezi huu. Ahsante.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza kuwasaidia Wachimbaji wadogo wa madini katika Mji wa Njombe kama inavyofanya kwenye maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuwasaidia wachimbaji wadogo Wizara kupitia Shirika la Madini la Taifa imeandaa mkakati maalumu kwa ajili ya kuwasaidia na kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini ikihusisha wachimbaji waliopo Mkoani Njombe, pia. Mkakati huo ambao umeanza kutekelezwa mwaka wa fedha 2021/2022 umejikita kwenye maeneo manne muhimu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ni Mpango wa Mafunzo (Training Calendar) kwa mwaka mzima ambao utafanyika nchi nzima. Mpango huo uliandaliwa kwa kushirikisha wachimbaji wadogo kupitia uwakilishi wa vyama vyao (FEMATA) na ambao kwa sasa upo tayari kwa utekelezaji. Mafunzo haya yatatotelewa kwa kuhusisha Taasisi mbalimbali zinazohusika na utozaji wa kodi na tozo mbalimbali kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Tume ya Madini pamoja na Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa pili ni Mpango wa kuwawezesha wachimbaji wadogo kukopesheka katika taasisi za fedha ambapo tayari Shirika limeishaingia makubaliano na Taasisi za fedha za ikijumuisha CRDB, NMB na KCB ambazo zipo tayari kuwakopesha wachimbaji hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Tatu ni Kuingia makubaliano na GST (Geological Survey of Tanzania) taasisi yetu ya jiolojia, ambayo itawasaidia wachimbaji wadogo kujua taarifa za mashapo katika maeneo yao kabla hawajaanza kuchimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Nne ni Kupata mitambo ya uchorongaji mahususi kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kwa kuanzia Shirika limeagiza mitambo 5 ya uchorongaji mahususi kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CHARLES M. KAJEGE K.n.y. MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, ni fedha kiasi gani zimerudishwa kwa wadai wa VAT wanaoidai Serikali kuishia mwaka wa fedha 2021/2022?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mwaka 2021/2022, jumla ya Shilingi bilioni 916.68 zililipwa kwa wadai wa VAT, sawa na ufanisi wa asilimia 431.7 ikilinganishwa na bajeti iliyotengwa. Ufanisi huu umetokana na hatua iliyochukuliwa na Serikali ya kuhakiki maombi ya wadai kwa kuzingatia viashiria hatarishi badala ya utaratibu wa awali wa kuhakiki maombi yote kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, utaratibu huo umeongeza kasi ya uhakiki na ulipaji wa madai ya marejesho ya VAT na kupunguza ucheleweshwaji kwa kuwa uhakiki unafanyika kwa wakati. Hatua na mafanikio hayo yanalenga kuchochea ukuaji wa uchumi, uwekezaji na kulinda mitaji ya wawekezaji na wafanyabiashara hapa nchini. Ahsante.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati reli ya TAZARA?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuboresha miundombinu ya reli ya TAZARA. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 13.1 kwa ajili ya ununuzi wa mataruma ya mbao kwa ajili ya kufanyia ukarabati madaraja 172 yaliyopo upande wa Tanzania, ununuzi wa mtambo wa kisasa wa kushindilia kokoto kwenye reli, na ununuzi wa mtambo wa kuvunjia kokoto (secondary crusher) kwa ajili ya kuongeza kokoto za aina mbalimbali zinazotumika katika kufanyia matengenezo ya njia ya reli kati ya Dar es Salaam – Tunduma na Msolwa - Kidatu. Aidha, fedha hizo pia zitatumika kukarabati mabehewa 21 ya treni za abiria za Udzungwa na treni za abiria za mjini (commuter) za Jijini Dar es salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mikakati ya muda wa kati na mrefu, Serikali za Tanzania na Zambia zimeandaa mpango wa biashara wa miaka mitano ambao unatarajiwa kupitishwa na Baraza la Mawaziri wa TAZARA mwishoni mwa Novemba, 2022. Aidha, Serikali za Tanzania, Zambia na China zimeunda timu ya pamoja kwa ajili ya kuandaa mkakati wa pamoja kwa kuishirikisha Serikali ya Watu wa China katika kugharamia maboresho ya TAZARA. Ahsante.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanzisha Wakala wa kudhibiti Mazao ya Mbogamboga na Matunda nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa, Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa kuwa na Mamlaka ya kusimamia na kuendeleza tasnia ya mazao ya bustani kutokana na mchango mkubwa wa tasnia hiyo kwenye mapato ya fedha za kigeni.

Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa mapendekezo ya kufanya marekebisho madogo Miscellaneous Amendment ya Sheria ya Usalama wa Chakula Na. 10 ya mwaka 1991 iliyoanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko - Cereal and Other Produce Regulatory Authority, ambapo pamoja na mambo mengine majukumu ya Mamlaka hiyo yatarekebishwa ili kuipa jukumu mahsusi la usimamizi na uendelezaji wa tasnia ya bustani.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanzisha Special Economic Zone ili kuchochea viwanda vya uchakataji Njombe Mjini?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Programu ya Special Economic Zones na Export Processing Zones ina jumla ya maeneo ishirini na nne ambayo yametangazwa kuwa Maeneo Maalum ya Uwekezaji (Special Economic Zones). Serikali imeendelea na jitihada za kuanzisha Kanda Maalum za Kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa uchumi. Katika kufanikisha azma hiyo, Mamlaka ya EPZ imekuwa ikizihamasisha Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutenga na kuwezesha uendelezaji wa maeneo ya Special Economic Zones.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya EPZA iko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge wa Njombe Mjini na Uongozi wa Mkoa wa Njombe kufanikisha uanzishaji wa Kanda Maalum ya Kiuchumi katika Mkoa huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, nini mpango wa Serikali kufufua Kiwanda cha Maziwa Njombe?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto za kiwanda cha maziwa Njombe Milk Factory Company Limited na Serikali kupitia uongozi wa mkoa imekwishaanza kuchukua hatua za kukikwamua kiwanda hicho. Hatua za awali zilizochukuliwa ni pamoja na kuwakutanisha wanahisa wa kiwanda na uongozi wa Mkoa wa Njombe.

Aidha, ninapenda kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kuwa, kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Njombe, Serikali itahakikisha kiwanda hicho kinaweza kufufuliwa kwa haraka ili sekta ya viwanda vya maziwa izidi kukua na kuleta manufaa kwa wafugaji na wanahisa, ninakushukuru.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itarejesha kwa wananchi wa Kata ya Luponde Ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya Kituo cha Utafiti wa Kilimo Igeri ambayo kwa miaka mingi imekuwa haitumiki?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haina mpango wa kurejesha shamba la Utafiti wa Kilimo Igeri kwa kuwa kama nchi kuna uhitaji mkubwa wa uzalishaji mbegu. Shamba hilo lina ukubwa wa hekta 816, kati ya hizo, hekta 350 ni misitu ya kiasili, hekta 450 ni eneo linalofaa kwa kilimo na hekta 16 ni eneo lenye barabara na nyumba. Kwa sasa shamba hilo linatumika kwa shughuli za utafiti na kuzalisha mbegu za mazao mbalimbali. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imelima hekta 400 za mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kusafisha, kuweka fensi, kuchimba visima na kulima shamba lote kwa kuzalisha mbegu za awali na za msingi za mazao ya ngano na pareto kwenye hekta 348 na utafiti hekta 88.8. Lengo ni kujitosheleza kwa mbegu za zao la ngano na pareto kwa wakulima wa Njombe, Makete na sehemu nyinginezo. Aidha, natoa rai kwa wananchi kuacha kuvamia mashamba ya utafiti na uzalishaji wa mbegu.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ukarabati mkubwa wa barabara kuu ya Makambako - Njombe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kuifanyia ukarabati barabara yote ya kutoka Makambako – Njombe – Songea yenye urefu wa kilometa 295. Sehemu ya Lutukila – Songea kilometa 95 ipo katika mpango wa ukarabati kupitia Mradi wa Tanzania Transport Integrated Project (TANTIP) ambapo Mkataba wa Mkopo nafuu kati ya Serikali na Benki ya Dunia umesainiwa na zabuni za kumpata Mkandarasi wa ujenzi zinatarajiwa kutangazwa mwezi Juni, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu iliyobaki ya Lutukila – Makambako ikiwemo na sehemu ya Makambako – Njombe urefu wa kilometa 59, Serikali inaendelea kutafuta fedha toka vyanzo mbalimbali vya ndani na nje kwa ajili ya ukarabati. Ahsante.
MHE. JOSEPH A. TADAYO K.n.y. MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itarekebisha Sheria ya Utakatishaji Fedha inayozuia dhamana kwa Watuhumiwa hata kwa makosa ya kawaida?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 12 cha Sheria ya Kudhibiti Utakasishaji wa Fedha Haramu, Ufadhili wa Ugaidi na Ufadhili wa Silaha za Maangamizi, Sura 423, kinabainisha makosa ya utakasishaji wa fedha haramu pekee. Sheria hiyo haihusishi makosa mengine yoyote, hususan kuzuia au kutozuia dhamana kwa watuhumiwa wa makosa ya kawaida. Aidha, utaratibu wa dhamana kwa makosa mbalimbali, ikiwemo utakasishaji wa fedha haramu unasimamiwa na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura 20.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, hakuna sababu ya kurekebisha Sheria ya Kudhibiti Utakasishaji wa Fedha Haramu, Ufadhili wa Ugaidi na Ufadhili wa Silaha za Maangamizi, Sura 423 kwa kuwa haizuii dhamana kwa watuhumiwa wa makosa ya kawaida. Ahsante.
MHE. DEODATAUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, kwa nini Sheria za Ardhi zinazokusudiwa kutumika kwenye miji zinatumika maeneo ya vijijini?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa kisheria wa usimamizi wa ardhi nchini umegawa ardhi katika makundi matatu ambayo ni Ardhi ya Kijiji, Ardhi ya Hifadhi na Ardhi ya Jumla. Kwa kuzingatia mgawanyo huo, Ardhi ya Vijiji inasimamiwa na Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura 114 na maeneo ya miji yanasimamiwa na Sheria ya Ardhi, Sura 113. Hata hivyo, yapo baadhi ya maeneo ndani ya mipaka ya vijiji yanayosimamiwa na Sheria ya Ardhi, Sura 113 kutokana na kumilikishwa kabla ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura 114 au kuhawilishwa. Aidha, baadhi ya maeneo ya vijiji yametangazwa kuwa ya kuendelezwa kimji (Planning Area) na kuandaliwa Mpango Kabambe (Master Plan) na hivyo kuyafanya yasimamiwe na Sheria ya Ardhi, Sura 113.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatatua tatizo la usafiri kwa ajili ya kusafirisha mahabusu na wafungwa katika magereza nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto iliyopo ya magari ya kusafirisha mahabusu na wafungwa kwa kuwapeleka Mahakamani na kuwarudisha gerezani. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Jeshi la Magereza ilitenga kiasi cha shilingi 878,125,000.00 katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ununuzi wa magari matano ya kusafirishia mahabusu na wafungwa katika Magereza nchini. Aidha, katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga fedha, kiasi cha shilingi bilioni 1.93 kwa ajili ya ununuzi wa magari 14 kwa ajili ya kusafirisha mahabusu na wafungwa katika magereza nchini. Nashukuru.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -
Je, ni lini wananchi wa Kijiji cha Mtila Kata ya Matola Njombe Mjini watapelekewa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha huduma ya maji katika Kijiji cha Mtila Kata ya Matola Njombe Mjini, Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025 imetenga fedha kwa ajili ya kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi pamoja na kuchimba kisima kirefu ili kupata chanzo cha maji. Aidha, baada ya kupatikana kwa chanzo hicho cha maji Serikali itafanya usanifu wa miundombinu ya usambazaji maji kwa ajili ya kunufaisha wananchi wa Kijiji cha Mtila, ahsante.
MHE. TUMAINI B. MAGESSA K.n.y. MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga miundombinu ya umwagiliaji kwenye maeneo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tarafa ya Igominyi – Njombe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeanzisha mkakati wa muda mrefu wa kuwawezesha wakulima wadogo wa chai katika Mkoa wa Njombe kwa kuwawekea miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba yao. Ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ndani ya Tarafa ya Igominyi yenye hekta 1,021.52 itanufaisha zaidi ya wakulima 934 kutoka katika Vijiji vya Iboya, Ihanga, Itipula, Mgala, Igoma, Iwungilo, Ngalanga, Uliwa, Kifanya, Lilombwi, Lwangu, Luponde na Utengule.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeanza utekelezaji kwa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika Mashamba ya Igoma, Lwangu, Iwungilo, Kifanya na IRECO ambapo ujenzi wa miundombinu yake utaanza katika mwaka wa fedha 2024/2025. Aidha, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina zitaendelea katika mashamba yaliyobaki kwa ajili ya kupata makadirio ya gharama za uwekaji wa miundombinu ya umwagiliaji.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kiwanja cha michezo cha Kisasa Mkoani Njombe?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali ipo kwenye ukarabati wa viwanja vya Uhuru na Benjamin Mkapa, ujenzi wa uwanja wa Arusha (Arusha Stadium) na kukarabati viwanja vingine vitano (5) vya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2024 na AFCON 2027. Kama sera ya michezo inavyoelekeza, ujenzi wa miundombinu ya michezo ikiwemo viwanja ni jukumu la Serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Baada ya kukamilisha ujenzi wa viwanja kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2024 na AFCON 2027, Serikali itatoa maelekezo kwa uongozi wa Mikoa yote ili kutekeleza mkakati wa ujenzi wa miundombinu ya michezo katika Mikoa yote. nakushukuru.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kiwanja cha michezo cha Kisasa Mkoani Njombe?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali ipo kwenye ukarabati wa viwanja vya Uhuru na Benjamin Mkapa, ujenzi wa uwanja wa Arusha (Arusha Stadium) na kukarabati viwanja vingine vitano (5) vya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2024 na AFCON 2027. Kama sera ya michezo inavyoelekeza, ujenzi wa miundombinu ya michezo ikiwemo viwanja ni jukumu la Serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Baada ya kukamilisha ujenzi wa viwanja kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2024 na AFCON 2027, Serikali itatoa maelekezo kwa uongozi wa Mikoa yote ili kutekeleza mkakati wa ujenzi wa miundombinu ya michezo katika Mikoa yote. nakushukuru.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba katika Vituo vya Afya vya Kifanya na Makowo vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2022/2023 na 2023/2024 Halmashauri ya Mji wa Njombe ilipokea shilingi milioni 450 ambayo ilitumika kununua vifaa tiba kwenye vituo vya afya vya Kifanya na Makowo. Vituo hivyo vimeshapokea vifaa tiba muhimu vinavyotoa huduma ikiwemo upasuaji wa dharura kwa akinamama wajawazito. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali inashughulikia upatikanaji wa generator kutoka Bohari Kuu ya Dawa kwa ajili ya vituo hivyo ambapo kiasi cha shilingi milioni 40 kimeshalipwa. Aidha, Serikali itaendelea kuratibu na kutenga bajeti ya ununuzi wa vifaa tiba ambavyo vitapelekwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini vikiwemo Vituo vya Afya vya Kifanya na Makowo. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa mnara wa mawasiliano katika Kijiji cha Uliwa - Njombe utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante! Kijiji cha Uliwa kipo katika Kata ya Iwungilo inayoundwa na vijiji vya Ngalanga, Iwungilo, Igoma na Uliwa, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliijumuisha Kata ya Iwungilo katika mradi wa mawasiliano wa awamu ya pili ‘A’ (2A) ambapo mtoa huduma HONORA (TIGO) alijenga minara katika vijiji vya Iwungilo na Ngalanga inaohudumia vijiji vya Ngalanga, Iwungilo, Igoma na Uliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia UCSAF ilifanya tathmini katika Kijiji cha Uliwa na kubaini kuwa kulingana na jiografia ya kijiji cha Uliwa ambacho kipo bondeni, minara iliyojengwa awali haifikishi mawasiliano katika kijiji hiki. Hivyo, UCSAF tayari imekijumuisha kijiji hiki katika orodha ya vijiji vitakavyonufaika kupitia mradi wa mawasiliano vijijini utakaotekelezwa katika mwaka wa fedha 2024/2025.