Supplementary Questions from Hon. Joseph Zacharius Kamonga (29 total)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ina uhaba mkubwa wa walimu kwenye shule zake za msingi, jambo linalosababisha wazazi kuchangishwa kati ya 15,000 mpaka 20,000 kwa ajili ya kuajiri walimu wa kujitolea kwenye Kata ya Mlangali, Mavanga na Lugarawa. Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kutosha kwenye shule za msingi za Wilaya ya Ludewa ikiwa ni pamoja na kuwaajiri wale walimu waliojitolea kwa muda mrefu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, shule 23 za sekondari zilizopo Jimboni Ludewa hazijafanyiwa ukaguzi muda mrefu. Je, ni lini Wizara itatoa maelekezo kwa wadhibiti ubora wa elimu walioko pale Ludewa waweze kufanya ukaguzi huo kuliko kuendelea kusubiri wakaguzi kutoka kanda? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna changamoto ya uhaba wa walimu katika maeneo mbalimbali nchini. Na kama mnavyofahamu hivi punde tu Mheshimiwa Rais aliagiza kwamba, wale walimu 6,000 ambao wa kuziba nafasi utaratibu wake uweze kufanyika mapema. Lakini kama mnavyofahamu mwaka jana mwezi wa Novemba Serikali ilitoa kibali cha kuajiri walimu zaidi ya 13,000. Tunaamini kati ya wale 13,000 walimu karibu elfu nane walikuwa tayari wameshasambazwa shuleni na walimu 5,000 walikuwa wanaendelea na mchakato.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika magawanyo huu sasa na hawa 6,000 watakaopatikana hivi punde watakwenda kutatua tatizo lile la upungufu wa walimu katika Halmashauri zetu ikiwemo na Halmashauri au Wilaya ya Ludewa.
Mheshimiwa Spika, hili la wazazi kuchangishwa, naomba tulibebe. Tutashirikana na wenzetu wa TAMISEMI tuweze kuangalia namna gani jambo hii linaweza likachukuliwa hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili amezungumzia suala la ukaguzi wa shule, Wizara inaendelea na kuimarisha Kitengo hiki cha Wadhibiti Ubora, ambapo hatua tofauti zimeweza kuchukuliwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2018/2019 mpaka hii 2020/2021. Wizara imeweza kufanya mambo yafuatayo; kwanza, tumeweza kusambaza Wadhibiti Ubora 400 katika Halmashauri zote nchini.
Pia katika kipindi cha mwaka 2018/2019 hadi 2020/ 2021 jumla ya ofisi za Wadhibiti Ubora 100 katika Halmashauri zetu zimeweza kujengwa na mpaka hivi navyozungumza tunaendelea na ujenzi wa ofisi 55 na ukarabati wa ofisi 31. Sambamba na hilo, Wizara yangu tumeweza kununua na kusambaza magari 83 kwenye Halmashauri tofauti tofauti.
Mheshimiwa Spika, lengo la kufanya hayo yote ni ili kuimarisha Kitengo chetu hiki cha Udhibiti Ubora hasa katika Halmashauri zetu. Kwa kufanya hivyo, tunaamini kutokana na ongezeko la shule nyingi ambazo zinahitaji kukaguliwa za msingi na sekondari tutaweza sasa kuzifikia shule hizo kwa umakini mkubwa.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sasa Wadhibiti wetu wa Ubora hawa wa Wilaya watakwenda kufanya ukaguzi katika shule hizi za msingi na sekondari katika maeneo waliopo badala ya kutumia wale Wadhibiti Ubora wa Kanda ambao walikuwa wanakagua hizi shule katika kipindi kilichopita. Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Ziwa Nyasa lina Kata zisizopungua nane; Kata ya Ruhuhu, Manda, Iwela, Lupingu, Lifuma, Makonde, Kilondo na Ruhila. Je, ni lini Serikali inakusudia kupeleka vifaa vya uvuvi kama engine za maboti kwa vikundi vya wavuvi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ningetamani kufahamu ni lini Serikali itapeleka kituo cha kufanya utafiti wa samaki na viumbe maji huko Wilayani Ludewa maana kata hizi zina wakazi wasiopungua 28,000 ambao wanatumia ziwa hili kama swimming pool na njia tu ya usafiri. Ningependa kufahamu commitment ya Serikali juu ya kupeleka kituo cha utafiti wa samaki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kamonga, Mbunge wa Ludewa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, juu ya kupatikana kwa vifaa vya uvuvi katika makundi ya vijana kwenye Kata za Ruhuhu, Manda, Makonde na kwingineko katika Jimbo lake la Ludewa naomba nimhakikishie kwamba katika mwaka wa fedha huu ambao leo tunaendelea kujadili bajeti yake, Serikali imejipanga kuhakikisha vijana wote waliopo katika maeneo hayo na wenyewe wanaweza kuwezeshwa kupata vifaa vya kufanyia shughuli zao za uvuvi.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kituo cha utafiti; Ziwa Nyasa ni katika maeneo ambayo Shirika letu la Utafiti la Uvuvi (TAFIRI) litakwenda kufanya utafiti kule na uwezekano wa kuweza kupata kituo kidogo pale kwa ajili ya utafiti kwenye eneo la Ziwa Nyasa upo na naomba nichukue jambo hili nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itafanya jitihada ya kuhakikisha kituo kinapatikana pale ili na Ziwa Nyasa wakati wote liwe linatazamwa na kuangaliwa kwa karibu. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; wananchi wa Ludewa wangependa kufahamu kwa kuwa wamesubiria fidia hizi kwa muda mrefu. Je, kwa nini Serikali isitenganishe majadiliano na mwekezaji na suala la fidia ili wananchi wa Jimbo la Ludewa waweze kulipwa fidia mapema?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ningependa kufahamu ni lini Serikali itaanza kutoa elimu ya kuandaa wananchi wanaoathirika na miradi ili waweze kunufaika na miradi hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Jimbo la Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika mradi huu fidia kwa wananchi iliyothaminiwa jumla ya bilioni 11.037 katika majadiliano au katika mkataba ambao tuliingia na kampuni hii Situan Honda ilikuwa yeye kama mwekezaji atakuwa na wajibu wa kulipa fidia eneo hilo ambalo atakuwa analitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama nilivyosema baada ya majadiliano na mwekezaji huyu tutaangalia sasa kama tutafikia muafaka maana yake yeye atakubaliana kulipa fidia, lakini utekelezaji wa mradi huu lazima uanze mwaka 2021/2022, aidha tumekubaliana na mwekezaji huyu au hatujakubaliana lakini mradi huu lazima uanze kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshaeleleza na ni utekelezaji ambao unaenda kufanyika katika mwaka wa fedha ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu katika eneo hili, ni kweli Serikali imekuwa ikiweka fedha kwa ajili ya kuelimisha wananchi namna ambavyo watashiriki katika ujenzi wa mradi huu kwa maana ya local content kwamba wao watafanya nini au watashiriki vipi katika mradi huu mkubwa wa Mchuchuma na Liganga. Kwa hiyo fedha zinatengwa kila mwaka na elimu inaendelea kutolewa kwamba sasa mradi huu ukianza naamini elimu zaidi itatolewa ili wananchi wa eneo hili waweze kushiriki katika utekelezaji wa mradi huu kikamilifu.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Moja, namwomba Mheshimiwa Waziri aweze kutupa Mpango wa Serikali: Ni kwa muda gani chuo hiki kitakuwa kimekamilika na kuanza kutoa mafunzo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Ludewa kwa umoja wao wamechangia fedha na nguvu zao kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya wanafunzi watakaokuwa na ufaulu mkubwa wa Darasa la Saba.
Je, ni lini Serikali katika kutambua jitihada za wananchi na kuunga mkono juhudi zao? Ni lini Wizara itatuma watalaamu kwa ajili ya kwenda kusajili shule ile ili watoto waweze kuanza kusoma pale?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; naomba sasa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kamonga Mbunge wa Ludewa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Kamonga pamoja na wananchi wa Ludewa na vilevile Watanzania wengine walioko kwenye Mikoa ya Rukwa, Geita pamoja na Simiyu, kwa sababu katika maeneo ambayo vyuo vya mikoa vinaenda kujengwa ni pamoja na maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la muda, tunatarajia ndani ya miezi minane kutoka leo vyuo hivi vinakwenda kukamilika kwa sababu fedha hizi zina muda maalumu wa utekelezaji kuhakikisha kwamba miradi hii inafanyiwa kazi sawa sawa. Kwa hiyo, niwahakikishie tu, Mheshimiwa Rais ametoa fedha hizi kwa kuhakikisha katika kipindi hiki kifupi huduma hizi zinaweza kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili, anazungumzia Shule ya Sekondari; nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Ludewa kwamba taratibu za kufuata zipo wakati wa kufanya ukaguzi na kusajili shule hizi. Namshauri Mheshimiwa Mbunge kupitia Mkurugenzi wa Halmashauri kuweza kuandika barua kupeleka kwenye idara yetu ya Udhibiti Ubora iliyokuwepo katika Wilaya ile ya Ludewa na wataalamu wetu wale wakishapata tu barua na maombi hayo, mara moja wanatakiwa kwenda kwa ajili ya kufanya ukaguzi ili kutengeneza ithibati iwapo viwango vile vimethibitika kuwepo, basi usajili huo utapatikana. Ila kwa vile amelizungumza suala hili hapa Bungeni, tutakwenda kulifanyia kazi kuhakikisha kwamba wiki ijayo wataalamu hao waweze kwenda kwenye eneo hilo la shule ili kuweza kupata usajili ili vijana wetu kama Januari shule hii inaweza kufunguliwa, iweze kufunguliwa na wanafunzi waweze kupata huduma. Ahsante. (Makofi)
MHE. JULIUS KAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Utaratibu wa ruzuku ulitoa nafuu kubwa sana wa bei za mbolea wakati huo. Hivi tunavyozungumza, bei za mbolea bado ziko juu na hii changamoto bado haijatatuliwa: Je, Serikali inasema nini kwa Watanzania kuhusu bei za mbolea ambapo hadi sasa wanashindwa kuzimudu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, bei ya mbolea ipo juu tofauti na bei ambazo wakulima walinunua katika misimu miwili au mitatu iliyopita. Hata hivyo, Serikali imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha kwamba tunampunguzia maumivu mkulima.
Mheshimiwa Spika, katika hatua ya awali kabisa ambayo tumeanza nayo ni kwamba, hivi sasa tumeanza mazungumzo Pamoja na zile kampuni za usambazaji wa mbolea kutoka katika source yenyewe badala ya kuwatumia watu wa katikati, Mheshimiwa Waziri alifanya kikao na Makampuni kutoka Saud Arabia, China Pamoja na Urusi. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunaipata mbolea moja kwa moja kutoka kwenye source kuja katika nchi yetu ya Tanzania ili tusiwape nafasi katikati hapa watu ambao wamekuwa wakiongeza bei.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika bajeti inayokuja tumejiandaa kutenga fedha kwa ajili ya stabilization fund kuhakikisha kwamba tuna-control bei ya mbolea ili wakulima wasipate taabu.
Mheshimiwa Spika, la mwisho, tumeendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya mbolea. Ninavyozungumza hivi sasa, kiwanda cha ETRACOM pale Nala Dodoma, kinakamilika mwezi Julai. Kikikamilika kiwanda hiki kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 600,000 za mbolea kwa mwaka na hivyo tutakuwa tumeondoa changamoto hii ya bei ya mbolea kwa wakulima wetu. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ninapenda kufahamu ni lini Serikali itapeleka maji Vijiji vya Kipingu na Kiogo ili kunusuru akina mama wanaoliwa sana na mamba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kamonga kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali tayari tunao utaratibu wa kwenda kuhakikisha maeneo ya Kiogo na maeneo yote kandokando ya Ziwa yanapata huduma ya maji safi na salama bombani ili kunusuru wananchi ambao wanaliwa na mamba. Tayari nimeshamuagiza Meneja wa Mkoa wa Njombe na ameshaniahidi ndani ya muda mfupi atahakikisha eneo ambalo mradi ulikuwa haujafika unakwenda kukamilika. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Ningependa kufahamu, ni lini Serikali inatarajia kujenga vituo vya kupumzikia abiria na mageti ya kushushia abiria kwenye vituo vya Kilondo, Lupingu na Manda?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ziwa Nyasa tumeshafanya upembuzi yakinifu katika Bandari za Nyasa pamoja na Mbamba Bay. Kwa hiyo katika mwaka huu wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza kujenga katika maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Ninaomba tu kufahamu kwa kuwa nilishamwandikia barua na tumezungumza, ni lini sasa atakuja Ludewa ili aweze kupokea shukrani za wananchi wa Ludewa kwa Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Kamonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita ni sikivu na ombi la Mheshimiwa Mbunge tunalipokea na mimi nitaongoozana nae kwenda kuangalia changamoto za wananchi wa Ludewa. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, ila napenda kufahamu kwamba: Je, Mheshimiwa Waziri haoni sasa ni muda muafaka wa kufanya ziara Ludewa kwenda kutembelea hizo kazi na kugawa hati zile za mwanzo kwa wananchi ili kuongeza hamasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumhakikishia Mbunge kwamba umuhimu huo tunauona ndani ya Wizara na niko tayari sasa kuongozana naye baada ya Bunge kwenda kukabidhi ardhi zilizogaiwa ili kutengeneza hamasa kwa wengine waweze kujitokeza kwa wingi.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, ningependa kujua mpango wa Serikali kutumia chanzo cha maji ya Ziwa Nyasa kuhudumia wananchi wa Kata ya Ruhuhu na Manda kwa sababu wananchi hawa wanaliwa sana na mamba hasa Kitongoji cha Panton?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Joseph Kamonga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, matumizi ya Ziwa Nyasa kama chanzo endelevu tayari tuna miradi ambayo tumeanza kuitekeleza ukanda wa Nyasa pamoja na Ruhuhu. Tunafahamu eneo ambalo wananchi walikuwa wakiliwa na mamba na tayari tulishaagiza RM Njombe ameanza usanifu na anakuja kutekeleza.
MHE. JOSEPH L. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, ningependa kufahamu ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa kipande cha barabara kutoka Mawengi mpaka Makao Makuu ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kati ya hicho kipande. (Makofi/Vigelegele)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri yaliyotolewa na Serikali, ila nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imekuwa na dhamira ya kutengeneza ajira maeneo haya yenye uwekezaji kwa kutenga vitalu vya wachimbaji wadogo; na kwa kuwa katika eneo lile la Mkomang’ombe, eneo lote lenye makaa ya mawe limeshikiliwa na Serikali kupitia Wizara hii: Je, Serikali haioni haja ya kukaa na wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakiomba muda mrefu kugaiwa maeneo ya kuchimba makaa ya mawe ili nao waweze kutengeneza ajira?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Zachariuz Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Zacharius kwa ufuatiliaji kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu katika Jimbolake la Ludewa. Ni kweli dhamira ya Serikali ni kuona sasa tunashirikisha wachimbaji wadogo katika maeneo yote au katika biashara zote ambazo zinafanyika kwenye maeneo husika.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, kwa sababu mradi huu ni mkubwa, kwa sasa bado tunakamilisha majadiliano na huyu mwekezaji mkubwa. Kwa hiyo, naamini atakapoanza kutekeleza na hao wengine wachimbaji wadogo nao naamini watashiriki katika kuhakikisha wanafaidika na uwepo wa mali asili au madini haya katika maeneo hayo ya ludewa.
Mheshimiwa Spika, tunalichukua hili kwa uzito wake ili kuhakikisha local content nayo inachukua nafasi yake.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Mpina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa tumbaku? Hilo swali la kwanza. Swali la pili: Je, Serikali inajipangaje kuhakikisha wakulima wanapata mbolea mapema ili kuweza kuwaruhusu mazao yote yale ya umwagiliaji yaweze kupata mbole kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika mpango wa msimu uliomalizika, wakulima wa zao la tumbaku hawakuwepo katika mpango wa ruzuku kwa sababu katika utaratibu wa manunuzi ya pembejeo kwenye sekta hii ya tasnia ya tumbaku wamekuwa na utaratibu maalum ambao ulianza kabla ya mfumo wa ruzuku. Hata hivyo, tumeendelea kukaa nao kuangalia pia utaratibu bora ili na wao waweze kunufaika na utaratibu wa ruzuku ambao unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili la kuhusu mbolea kupatikana mapema; tumeshakaa na waagizaji na wazalishaji wa mbolea wote hapa nchini kuhakikisha kwamba kuanzia mwezi wa Saba mbolea ianze kuingizwa nchini ambayo itawakuta wakulima wakiwa bado na uwezo wa kununua kwa kuwa watakuwa wamevuna ili wakulima wetu itakapofika kipindi cha kuanza msimu mbolea iwepo yote hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumebaini upungufu katika msimu uliopita, tumeyarekebisha, tutahakikisha kwamba wakulima wanapata mbolea kwa wakati katika msimu ujao.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri na pia atupelekee shukrani nyingi Serikalini kwa kutuletea milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Samaki pale Manda. Pamoja na Shukrani hizo naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kule Ludewa wananchi wana ng’ombe kama 33,871 wa kienyeji na 687 wa kisasa ambao sio bora sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa kutuletea madume bora kwa ajili ya kuboresha uzao wa ng’ombe kule Ludewa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ningependa kufahamu Serikali ina mkakati gani wa kurekebisha, Sheria Sera na Kanuni ili ziweze kusimamia Sekta ya Uvuvi ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili nyongeza ya Mheshimiwa Kamonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tunapokea shukrani na pili Program ya Uboreshaji wa Mifugo inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni program endelevu inayotumia njia ya madume bora na njia ya uhimilishaji. Yeye ameomba madume bora na katika mwaka huu wa fedha tunaoelekea 2023/2024, mkakati huu utaendelea na Ludewa tutaiweka kwenye eneo mojawapo la kunufaika na program hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya Sera, Sheria na Kanuni zetu tumekuwa tukifanya hivi na kila mara panapotokea hitaji, tutaendelea kuboresha Sheria na Kanuni zetu. Kwa hiyo kama Mheshimiwa Mbunge analo jambo mahususi tunamkaribisha kwa ajili ya kufanya maboresho hayo. Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, hasa kwenda kwenye chanzo cha uhakika. Pamoja na majibu hayo mazuri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Mlangali na Lugarawa ni kata ambazo zina ongezeko na kasi ya idadi ya watu tofauti na uwepo wa huduma za maji. Nini mpango wa Serikali kutenga fedha hizo kwenye bajeti ijayo ili kata hizo mbili ziweze kupata maji?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kitongoji cha Lutala la Kisaula, vina idadi kubwa ya wananchi na hadhi ya vijiji, lakini kwa muda mrefu vimekuwa na changamoto ya maji. Mheshimiwa Naibu Waziri, alishaelekeza wataalam wa-extend Mradi wa Iwela kuhudumia maeneo hayo...
SPIKA: Swali lako Mheshimiwa.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini maelekezo hayo ya Serikali yatatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kamonga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli Mlangali na Lugarawa Mheshimiwa Mbunge, tulikwenda na tumeshudia kwa pamoja, lakini tayari kama Wizara tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili tuweze kutumia vyanzo vile vya uhakika; ile mito yetu miwili, Mto Salali na Mto Mbiliwili. Tutahakikisha tunatumia mito hii pale ambapo usanifu utakapokamilika na kuonekana na maji ya kutosha, ndiyo mto ambao tutautumia. Hili Mheshimiwa Mbunge amefuatilia kwa muda mrefu na tulikwenda pamoja.
Mheshimiwa Spika, vile vile, masuala ya Kitongoji cha Kisaula na Lutala, wakati Mheshimiwa Waziri anahitimisha hapa hoja za bajeti yetu ya mwaka 2023/2024, tayari imeonesha tumetenga Shilingi milioni 20.7 kwa ajili ya kufanya upimaji, usanifu na kupanua mtandao wa maji kutoka Mradi wa Maji Iwela. Kwa hiyo, hili tayari tumeshalifanyia kazi. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, hata hivyo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kawaida ya Serikali kuwapangia watumishi Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa na kuwahamisha kabla hawajaripoti hasa madaktari, je, nini mpango wa Serikali kutoa ajira mbadala kwa nafasi hizo ambazo madaktari hawakuripoti?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kumekuwa na changamoto ya wananchi kulazimika kuajiri walinzi kwa ajili ya kulinda shule za sekondari na zahanati, je, nini mkakati wa Serikali kuajiri walinzi hawa ili waweze kulipwa na mafao yao ya uzeeni? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kwanza, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Kamonga, kwamba kwa utaratibu wa ajira ulioanza mwaka wa fedha 2021/2022. Kwanza ajira zinaombwa kwa njia ya mtandao kwa maana kwa njia ya kielektroniki. Kuna mfumo mahususi wa ajira lakini wanaoomba ajira wanaomba kituo mahsusi kwa maana ya ndani ya halmashauri husika na kituo husika.
Mheshimiwa Spika, tumeshaweka utaratibu kwamba, lazima waripoti na hawawezi kuhamishwa ndani ya miaka mitatu ya kwanza katika maeneo yao. Naomba kuchukua suala hili la Ludewa, tulifanyie ufuatiliaji kama kuna madaktari walipangiwa na kabla hawajaripoti walihamishwa, tuone ni kwa sababu gani hatua hizo zilichukuliwa kinyume na taratibu za ajira ambazo zimewekwa kwenye mfumo wa ajira kukaa angalau miaka mitatu.
Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuhakikisha kwamba halmashauri zote za pembezoni, zinapangiwa watumishi zaidi kuliko za mijini kwa sababu za pembezoni zina upungufu mkubwa. Tutahakikisha kwamba hatuhamishi bila sababu za msingi kwa watumishi kutoka halmashauri za pembezoni.
Mheshimiwa Spika, kuhusu wananchi kuajiri walinzi katika shule na maeneo mengine kama zahanati. Tulielekeza kwamba Serikali za Vijiji ziweke utaratibu rafiki kwa wananchi kuona uwezekano wa kulinda rasilimali za shule. Lakini zahanati na vituo vingine vya huduma bila kuwaumiza wale walinzi kwa maana kuwalipa posho zao na kuhakikisha kwamba wanawekewa fedha kwa ajili ya kiinua mgongo pale wanapostaafu kwa taratibu zile za ajira za mikataba, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani nyingi kwa Serikali kwa kukamilisha kipande cha Lusitu - Mawengi na kuanza kipande cha Itoni – Lusitu ambapo kipande kile cha mwanzo kilitumia bilioni 179 cha pili bilioni 90 bado ninaomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, pale Mawengi wakati wanajenga ile barabara kuna wananchi wachache ambao hawakulipwa fidia wamekuwa wakihangaika sana;
Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wale ili waache kuhangaika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ningepena kufahamu Serikali imejenga barabara nyingi Ludewa lakini haijaweka taa za barabarani;
Je, ni lini Serikali itakwenda kuweka taa za barabarani hasa maeneo yenye miji ambayo yana wananchi, ili mji wetu uweze kuonekana wa kisasa zaidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kamonga Mbunge wa Ludewa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia; wananchi hawa ni kweli walikuwa hawajalipwa na ni kwa sababu zoezi wakati la ulipaji linaendelea hawa wananchi hawakuwepo. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge na wananchi hao waweze kumuona Meneja wa Mkoa wa Njombe ili aweze kuwapa taratibu zitakazofanyika namna ya kuwalipa wananchi hawa ambao walipisha ujenzi wakati wa mradi huu, hawa wananchi wa Mawengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu taa za barabarani. Kama tulivyosema sehemu zote za wilayani na kwenye miji ama center kubwa ni mpango sasa wa Serikali kuhakikisha kwamba tunaweka taa za barabarani. Na katika mwaka wa fedha ujao nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge moja ya eneo ambalo litafaidika kuwekewa taa ni pamoja na mji wa Ludewa, ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na ningependa kuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza; kwa kutambua umuhimu wa ulinzi na usalama wa mpaka ule wa Ziwa Nyasa na vivutio vya utalii, nini mkakati wa Serikali kuongeza fedha ili kasi ya ufunguaji wa barabara hii iongozeke?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; nini mpango wa Serikali kuongeza fedha kwenye barabara inayoanzia Mlangali – Lupila – Makete ili vikwazo vya eneo la Lusala na Ng’elamo viweze kuondolewa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba umuhimu wa barabara hii ukiachilia mbali kwamba ni barabara ya ulinzi, lakini pia wananchi wanaoishi kando kando ya ziwa hawana namna nyingine ya kuwasiliana panapokuwa kuna changamoto ya usafiri wa majini, ndiyo maana Serikali imeanza kwa awamu. Hata hivyo, mpango wa Serikali ni kutafuta fedha ambayo itaifungua hii barabara yote ambayo nimeielezea kwamba ni barabara ambayo inapita kwenye milima na mabonde makubwa sana. Kwa hiyo mpango huo upo ndiyo maana tumeanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu hii Barabara ya Mlangali kwenda Ikonda najua ni muhimu sana kuunganisha Ludewa na Makete na hasa Hospitali ya Ikonda. Serikali imetenga fedha mwaka huu kuhakikisha kwamba maeneo yote yale korofi inakarabatiwa ili iweze kupitika kwa kipindi chote, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, pamoja na hivyo naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Ludewa wamevuja jasho sana kuanza ujenzi kwenye Kata 12, Je, ni lini Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi ili kwenda kushuhudia jinsi wananchi walivyojitoa kutoa kujenga vituo vya afya na havijamaliziwa na Serikali?
Swali la pili, kwa kuwa Tarafa ya Mwambao haina usafiri wa magari na meli kwa muda mrefu haipo. Je, ni kwanini Serikali isitafute boti moja ya mwendokasi ambayo itasaidia wagonjwa kuanzia Lumbila, Kilondo, Makonde, Lifuma, Mkali mpaka Manda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Jimbo la Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kamonga, amekuwa akifuatilia sana miradi ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Ludewa, ikiwemo vituo vya afya na magari ya magonjwa. Kwa kweli katika Kata hizi 12 ambazo wananchi wamechangia nguvu zao kujenga vituo vya afya, nimhakikishie kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi kukamilisha vituo hivi.
Mheshimiwa Spika, nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, kwa mwaka ujao wa fedha baada ya mwaka huu ambao tumeshaupangia bajeti atenge fedha kwa ajili ya kujenga maabara na kichomea taka kwenye vituo ambavyo wananchi wameshaweka nguvu zao, ili huduma za OPD zianze na Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha vituo hivyo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na ambulance, boti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafanya tathmini maeneo yote ambayo ni magumu kufikika ya visiwa na ambayo yanapitiwa na mikondo ya maji, tuangalie uwezekano wa kupata ambulance hizi za boti kwa kadri ya upatikanaji wa fedha na tutatoa kipaumbele kwenye Wilaya ya Ludewa.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, pamoja na hivyo naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Ludewa wamevuja jasho sana kuanza ujenzi kwenye Kata 12, Je, ni lini Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi ili kwenda kushuhudia jinsi wananchi walivyojitoa kutoa kujenga vituo vya afya na havijamaliziwa na Serikali?
Swali la pili, kwa kuwa Tarafa ya Mwambao haina usafiri wa magari na meli kwa muda mrefu haipo. Je, ni kwanini Serikali isitafute boti moja ya mwendokasi ambayo itasaidia wagonjwa kuanzia Lumbila, Kilondo, Makonde, Lifuma, Mkali mpaka Manda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Jimbo la Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kamonga, amekuwa akifuatilia sana miradi ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Ludewa, ikiwemo vituo vya afya na magari ya magonjwa. Kwa kweli katika Kata hizi 12 ambazo wananchi wamechangia nguvu zao kujenga vituo vya afya, nimhakikishie kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi kukamilisha vituo hivi.
Mheshimiwa Spika, nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, kwa mwaka ujao wa fedha baada ya mwaka huu ambao tumeshaupangia bajeti atenge fedha kwa ajili ya kujenga maabara na kichomea taka kwenye vituo ambavyo wananchi wameshaweka nguvu zao, ili huduma za OPD zianze na Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha vituo hivyo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na ambulance, boti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafanya tathmini maeneo yote ambayo ni magumu kufikika ya visiwa na ambayo yanapitiwa na mikondo ya maji, tuangalie uwezekano wa kupata ambulance hizi za boti kwa kadri ya upatikanaji wa fedha na tutatoa kipaumbele kwenye Wilaya ya Ludewa.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza; na nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na kawaida wakati fulani kuzuia mahindi ya Tanzania kuuzwa nje ya nchi, jambo ambalo linaadhiri sana bei ya zao hili la mahindi kwa wakulima.
Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba mahindi ya Tanzania yanaruhusiwa kwenda kuuzwa nje ya nchi ili wakulima wapate bei nzuri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; bei za mbegu za mazao mbalimbali zimekuwa zikipanda kwa kasi sana.
Je, Serikali ina mpango gani walao kwa kuanzia na zao la mbegu za mahindi, Serikali ina mpango gani wakuweka ruzuku kwenye bei ya mbegu ya mahindi ili wakulima waache kurudia mbegu au kutegemea mbegu za asili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jambo la kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake ya msingi. Nimuondoe shaka kwamba moja ya wajibu wetu sisi kama Wizara ya Kilimo tunapokuwa tunazuia wakati fulani mahindi kuuzwa nje ya nchi lengo letu linakuwa kwanza, kujiridhisha kupata tathmini halisi ya usalama wa chakula nchini; na tunafanya hivyo ikiwemo kwa kutumia wakala wetu wa hifadhi ya chakula nchini kununua. Tukishamaliza jambo hilo ndipo ambapo huwa tumekuwa tukiruhusu wananchi kufanya biashara. Kwa hiyo tunaendelea kulizingatia ili kuleta namna bora ambayo itasaidia soko kwa wakulima wa mahindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuweka ruzuku katika bei ya mahindi, kwa maana ya mbegu mbalimbali ikiwemo mahindi, jambo hilo tumelipokea. Ndiyo maana katika mipango yetu ya awali, mwazo tumeanza na ruzuku katika upande wa mbolea na pembejeo nyinginezo zikiwemo viuwatilifu; lakini next maana yake tutakuja katika pembejeo nyinginezo zikiwemo bei za mahindi. Kwa sasa tumeanza na hizo items mbili then tutakuja katika hilo jambo lingine. Kwa hiyo, hilo tumelipokea na lipo katika mipango yetu. Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na nimshukuru Mheshimiwa kwa majibu mazuri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 Kata hizo Nane zina jumla ya wananchi 26,582. Je, kwa idadi hiyo ya boti mbili Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba Serikali inatakiwa iongeze boti?
Swali la pili, wavuvi wa Jimbo lile wana changamoto nyingi na wana maoni mengi ambayo wangetamani wakae na Mheshimiwa Waziri. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari kutangulizana na mimi baada ya Bunge hili kwenda kukaa na wavuvi wa Jimbo la Ludewa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la ugawaji wa boti lilianza kwa zoezi la awali Mheshimiwa Rais amekwishatoa maelekezo kwamba tuangalie maeneo yote yenye uhitaji wa kuongeza boti hizo na tayari tumeshaainisha maeneo ambayo yana umuhimu wa kuongeza boti na sasa Wizara iko tayari kuongeza boti kulingana na mahitaji ya maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu kuwatembelea, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kamonga kwa jinsi ambavyo anafuatilia sana shida za wananchi wake na kuwatatulia, kwa kadri hiyo na sisi Wizara tuko tayari kufika katika eneo lake kwenda kuzungumza na wavuvi hao kuona namna sahihi ya kutatua changamoto wanazopitia wavuvi hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alishatoa taarifa kwa Umma kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeshatoa fedha zote kwa ajili ya kuwalipa wakulima wa zao la mahindi kule Ludewa. Je, nini maelekezo ya Serikali kwa watu wa NFRA kuwahisha malipo hayo ili wazazi waweze kupeleka watoto vyuo na kununua mbolea? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge ameeleza kwamba tuko katika hatua za mwisho kumalizia malipo kwa watu ambao wapo katika awamu ya mwisho. Kwa maelezo ambayo Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alikuwa amenipatia, ni kwamba baada ya kumaliza huu mchakato, Serikali itarudi kwa ajili ya kuendelea kununua mazao kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ni kwamba, kwa sababu fedha hizi ziko katika Taasisi za Kibenki, wanamalizia tu huu mchakato na naamini kabla ya mwisho wa mwezi huu wakulima wote nchini watakuwa wameshalipwa. Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa vijiji 29 vilivyopo Jimbo la Ludewa vinahudumiwa na mzalishaji binafsi wa umeme na vinakabiliwa na changamoto ya bajeti kwa wazalishaji binafsi; na kwa kuwa Serikali imeshafanya kazi kubwa ya kutambua gharama za kufikisha umeme kwenye vitongoji na kuwasha umeme Mawengi na Milo: Je, nini ahadi ya Serikali kwa wananchi wale ikizingatiwa sasa tunaenda kwenye bajeti?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali moja la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na uzalishaji wa umeme kwenye vijiji hivyo 29, nafahamu kuna changamoto ya umeme kwa sababu ya wazalishaji ni wawezeshaji binafsi, lakini Serikali kupitia REA tunao mpango wa kuwawezesha wazalishaji binafsi wa umeme na utaratibu upo. Vilevile, tutaendelea kushirikiana nao kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata umeme wa uhakika. Pia, tunao mkakati wa kuhakikisha wananchi hawa wanapata umeme kupitia miradi ya Serikali ambayo tunayo na tutahakikisha hilo linafanyika haraka iwezekanavyo ili wananchi waondokane na kadhia hiyo, ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu ya Serikali, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; wananchi wa Kijiji cha Chanjale kilichopo Kata ya Lumbila, baada ya kuona wanatembea kilometa 22 kufuata huduma za zahanati, mwaka 2014 walianza kujenga zahanati yao, lakini hadi leo haijakamilika. Je, ni ipi kauli ya matumaini kutoka kwa Serikali juu ya Zahanati hii ya Chanjale ili wananchi waweze kupata huduma?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wananchi wa Kata ya Madope ambao wako 9,000 wanakaribia 10,000 na wao walianza jitihada za kujenga kituo cha afya ambacho Serikali ilituma wataalam kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwenda kukagua, wakaahidi kuwa watapeleka fedha kutoka Benki ya Dunia, lakini mpaka leo ikiwa ni mwaka wa pili bado hiyo fedha haijaenda. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha hiyo ili kukamilisha Kituo cha Afya cha Kata ya Madilu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kutumia nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Kijiji cha Chanjale kwa kuchangia nguvu zao kwa ajili ya ujenzi wa zahanati. Naomba kuwapa habari njema kwamba, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesikia kilio chao kupitia kwa Mheshimiwa Mbunge wa jimbo hilo, Mheshimiwa Kamonga. Ifikapo tarehe 30 Aprili, ile fedha shilingi milioni 20, itakuwa imepelekwa katika Kijiji cha Chanjale kwa ajili ya kukamilisha ile zahanati.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Rais amepeleka shilingi milioni 50 katika Kijiji hicho cha Chanjale kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba ili zahanati hii ikikamilika ianze kutoa huduma kwa wananchi. Natumia nafasi hii kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ludewa kwamba, ifikapo tarehe 30 Juni, 2024 zahanati ile iwe imekamilika ili tarehe 1 Julai, 2024, wananchi wa Chanjale waanze kupata huduma za afya katika zahanati hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, ni kweli kwamba, wananchi wa Kata ya Madilu wanahitaji kituo cha afya na tayari Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imepeleka wataalam. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kituo kile kipo kwenye orodha ya vituo ambavyo vitapewa fedha kupitia Mfuko wa Benki ya Dunia ambapo tunaamini kabla ya Mwezi Juni mwaka huu fedha zitakuwa zimefika na kazi za ujenzi zitaanza kutekelezwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa soko la samaki pale Manda. Pamoja na hilo nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sasa Serikali imejenga soko hili la kisasa, je, ni lini Wizara itatuma wataalamu kwenda kutoa elimu ya ufugaji wa samaki kwa vizimba kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Serikali itakwenda kutoa elimu ya uhifadhi wa mazalia ya samaki kwa wananchi ili kuweza kuongeza idadi ya samaki kwenye Ziwa Nyasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na baada ya Bunge hili kuhitimishwa tutatuma wataalamu kwenda kutoa elimu ya vizimba ili wananchi wa eneo hilo waweze kupata elimu ya vizimba, lakini kwa taarifa tu ni kwamba baada ya mwezi wa tisa tayari utafiti wa namna gani vizimba vitakaa katika maeneo gani ya Ziwa Nyasa vitakuwa vimekamilika na wananchi wanaozunguka maeneo hayo wataruhusiwa sasa kuchukuwa vizimba kwa ajili ya kwenda kuweka katika Ziwa Nyasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili la pili la kutoa elimu, Wizara imeendelea kutoa elimu kwa wavuvi katika maeneo mbalimbali nchini na hususani katika eneo la Mheshimiwa Mbunge kule Ludewa tutatuma wataalamu wataenda kutoa elimu na baada ya Bunge hili Tukufu tuwasiliane Mheshimiwa Mbunge tuone wavuvi gani wanahitaji elimu ili waweze kupatiwa elimu katika maeneo hayo, ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa, Kituo cha Afya cha Kata ya Makonde ambacho kiko ziwani kinategemewa na kata tano na mawimbi yakitokea ziwani usafiri kwenye maji hauwezekani. Je, ni lini Serikali itapeleka gari, kwa ajili ya kusafirishia wagonjwa wa Kata hizi tano? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikinunua magari haya ya kusafirishia wagonjwa, kwa ajili ya kuyasambaza katika vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya ya msingi. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa kadiri ya fedha zinavyopatikana na magari haya yanavyonunuliwa na kwa kuzingatia vipaumbele, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, ataletewa magari haya, kwa ajili ya kutoa huduma.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri na hatua hiyo waliyofikia ni muhimu sana. Hata hivyo, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Swali la kwanza. Sasa hivi Ludewa inakwenda kuwa na viwanda vikubwa sana, lakini bado inategemea power station kutoka Wilaya ya jirani ya Madaba. Je, Serikali haioni haja ya kujenga kituo cha kupooza umeme pale Ludewa, ili kupunguza adha kwa wananchi ya kukatika kwa umeme mara kwa mara?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Ninapenda kufahamu iwapo Serikali ipo tayari kunipa wataalam kutoka TANESCO na REA niweze kwenda nao Kata za Lumbila na Kilondo ambako bado vijiji vingi havijapata umeme hadi sasa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninapongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Kuhusu kujenga kituo cha kupooza umeme Ludewa; tutaenda kulifanyia kazi kuona kama uwezekano upo na kama upo basi tutaweka. Kama haupo, kwenye ule mradi wa grid imara basi tutaona ni namna gani tutaweza kujenga kituo cha kupooza umeme pale Ludewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninafahamu Wananchi wa Ludewa ni wachapakazi sana kwa hiyo, wanahitaji umeme wa uhakika, kwa ajili ya viwanda vidogo na vikubwa. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge tumelipokea na tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kupewa TANESCO na REA, ili kuhakikisha kwamba, vijiji vya Nsele, Kilondo, Mkanda, Lumbila na Changali wanapata umeme kwa sababu, nafahamu vijiji hivi havina umeme; tulipata changamoto ya mkandarasi, kwa sababu vijiji hivi vipo Mwambao wa Ziwa Nyasa akaona ni vigumu katika utekelezaji, hivyo akaamua kuvirudisha REA. Hata hivyo, kwa sababu tulisaini naye mkataba na alifanya survey na akakubali mwenyewe kuvifanya, tumekataa yeye kuvirudisha vijiji hivi REA na tayari tumeshampa schedule, ili atuambie ni lini atapeleka umeme kule, otherwise tutamchukulia hatua kali za kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namuambia mkandarasi huyu ahakikishe anatekeleza mradi kwa wakati. Otherwise tutachukua taratibu za Kisheria kuhakikisha ya kwamba na sisi tunapata haki yetu kwa sababu, alisaini mkataba baada ya kufanya survey na akahakikisha kwamba, anaweza kupeleka umeme kwenye vijiji hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama mwishoni kabisa tutajiridhisha hawezi kupeleka umeme katika vijiji hivi kwa wakati, sisi kupitia TANESCO na REA, tuna uwezo wa kupeleka umeme kwenye vijiji hivi. Kwa hiyo, tutachukua hatua zote za kisheria kuhakikisha umeme unaenda, lakini kama hataweza kupeleka kwa wakati tutafanya wenyewe. Vilevile, tutamchukulia hatua kali za kisheria. Hatuwezi kukubaliana na wakandarasi wababaishaji. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tutalifanyia kazi kwa hakika, ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Ludewa kwenda Ibumi ilikuwa imefunga kutokana na mvua zilizozidi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ilituma wataalamu kuikagua hiyo pamoja na nyingine tatu na kuahidi zitapewa fedha kutoka World Bank.
Je, ni lini Serikali itatoa fedha hizo ili kabla ya mvua ziweze kufanyiwa matengenezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, hakika amekuwa akizisemea sana hizi barabara kwa kuwa anatambua na ana matamanio wananchi wake waweze kupata barabara nzuri zenye hadhi nzuri ambazo zitawezesha shughuli za kiuchumi na kijamii katika Jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha hizi kwa ajili ya dharura zimepatikana shilingi bilioni 170 na nimhakikishie kwamba hatua ambayo ipo sasa ni ya manunuzi, kupata wakandarasi ili waweze kuingia site. Nimhakikishie baada ya muda mfupi kutoka sasa tutawaona wakandarasi wako site kwa ajili ya kuanza kujenga barabara hizi.