Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Muharami Shabani Mkenge (23 total)

MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Maeneo ya wananchi wa Kata ya Zinga, Kitongoji cha Mlingotini na Pande, yalichukuliwa na Serikali ili kupisha Mradi wa EPZ lakini hawajalipwa fidia:-

Je, ni lini wananchi hao watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone ni moja ya miradi wa kielelezo na kimkakati ambao umepewa kipaumbele nchini na umeainishwa katika Mpango wa Miaka Mitano wa Kwanza, wa Pili na wa Tatu na katika Ilani ya CCM.

Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa mradi huo, Serikali ilichukua hatua mbalimbali za uendelezaji ikiwemo kulipa fidia kwa baadhi ya watu waliopisha mradi kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, eneo ambalo lilifanyiwa tathmini ni hekta 5,743 ambazo fidia ilikuwa ilipwe jumla ya bilioni 58.5 na katika hekta hizo zilizolipwa fidia ni hekta 2,339.6 ambazo jumla ya fidia iliyolipwa ni takriban bilioni 26.6. Serikali inatambua uwepo wa maeneo yanayodaiwa fidia katika eneo maalum la kiuchumi la Bagamoyo yakiwemo maeneo yaliyoko katika Vitongoji vya Mlingotini na Pande katika Kata ya Zinga, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza azma ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, Serikali inaendelea kuangalia namna bora zaidi ya utwaaji wa maeneo ya namna hii na kuweka utaratibu wa fidia wenye kuleta tija ya uwekezaji kwa Taifa kwa ujumla. Taratibu hizo zitahusisha ulipaji wa fidia kwa maeneo yaliyotathminiwa na Mthamini Mkuu wa Serikali na fidia hufanywa kwa mujibu wa Sheria. Pia utaratibu huo unalenga kuyamiliki na kuyaendeleza maeneo hayo ili yawe na tija kwa Taifa letu. Hivyo, fidia kwa wananchi ambao bado wanadai katika eneo hilo la Mlingotini na Pande itafanyika kwa kuzingatia utaratibu hu una Serikali italipa wadai hao haraka iwezekanavyo.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaandaa wakulima wadogo wa miwa (outgrowers) wa Bagamoyo ili kuwa na uzalishaji mkubwa na wenye tija?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo kimejiwekea mipango inayotekelezwa kwa awamu. Awamu ya Kwanza, kiwanda kinatarajia kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika hekta 2,050 za mashamba yake. Hadi kufika mwezi Desemba, 2020 jumla ya hekta 1,700 zimelimwa, kati ya hizo hekta 750 zimewekewa mfumo wa umwagiliaji wa matone.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wadogo wa miwa (outgrowers scheme) watahusishwa katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ambayo inatarajia kuanza mwaka 2022/ 2023. Katika awamu hiyo, Serikali kwa kushirikiana na mwekezaji imetenga eneo lenye hekta 3,600 kwa ajili ya wakulima wa miwa (outgrowers) ambao watazalisha na kuuza miwa yao katika Kiwanda cha Miwa cha Bagamoyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwanda unategemewa kukamilika ifikapo Juni, 2022 kwa hiyo miwa ya wakulima itakomaa wakati kiwanda kimeanza kufanya kazi. Hivyo, wakulima hao watakuwa na uhakika wa soko la miwa watakayozalisha.
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE K.n.y. MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapima eneo la mifugo la Ruvu na kulikabidhi kwa Halmashauri ya Chalinze?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete, Mbunge wa Chalinze kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshapima na kutoa kipande cha ardhi chenye ukubwa wa hekta 2,208 kutoka Ranchi ya Ruvu kwa ajili ya matumizi ya wananchi. Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ilikatiwa hekta 1,488 kwa ajili ya vijiji sita ambavyo ni Kijiji cha Ruvu Darajani hekta 200; Kijiji cha Kidogozero hekta 200; Kijiji cha Kitonga hekta 480; Kijiji cha Magulumatali hekta 200; Kijiji cha Vigwaza hekta nane; na Kijiji cha Milo-Kitongoji cha Kengeni hekta 400.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imepima na kutoa kipande cha ardhi chenye ukubwa wa hekta 120 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa ajili ya vijiji vitatu vya Kidomole hekta 40; Fukayosi hekta 40 na Mkenge hekta 40. Pia, Serikali imepima na kutoa ardhi yenye ukubwa wa hekta 600 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Vijijini kwa ajili ya Kijiji cha Mperamumbi Kitongoji cha Waya.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa Kilomita tano ndani ya Mji wa Bagamoyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza ahadi ya Rais ya ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 5 iliyotolewa katika mwaka wa fedha 2015 ambapo hadi mwaka 2019/2020 barabara zenye urefu wa kilomita 2.36 zimejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.37. Barabara hizo zinajumuisha Barabara ya Stendi ya Kongowe – Kwa Chambo kilomita 0.6, Mgonera – Forodhani kilomita 0.63, Rubeya kilomita 0.7 na Soko la Uhindini kilomita 0.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 375 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Bomani kipande chenye urefu wa kilomita 0.4 kwa kiwango cha lami. Tayari Mkandarasi ameshapatikana na yupo kwenye maandalizi ya kuanza kazi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 375 kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Kapala kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 0.45.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuvisaidia vikundi vya BMU ili kuendeleza kasi ya upandaji mikoko na kusafisha fukwe kuanzia Pwani ya Bagamoyo, Pangani hadi Tanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari ina mipango ya kuvijengea uwezo wa uelewa ili kujisimamia vikundi vyote vya BMUs katika kuendeleza kasi ya upandaji mikoko na kusafisha fukwe za bahari yetu. Jumla ya vikundi 18 vya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti vimepatiwa mafunzo ya kupanda, kuhifadhi na kusimamia mikoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, vikundi vya BMUs vya Mlingotini Bagamoyo vimewezeshwa kupanda miche 7,000 ya mikoko. Vilevile, vikundi vya BMUs vya vijiji vya Moa, Ndumbani na Mahandakini Wilayani Mkinga vimepatiwa mafunzo ya usimamizi wa mazingira ikiwemo upandaji wa mikoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kupitia mradi wa South West Indian Ocean Fisheries (SWIOfish) unaoratibiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Vikundi vya BMUs vya Bagamoyo na Pangani wamepata uelewa wa kukusanya maduhuli ambapo kiasi cha fedha kinachokusanywa kitatumika katika kuendeleza shughuli za upandaji wa mikoko na usafi wa mazingira. Ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je ni lini Serikali itakabidhi majengo yaliyokuwa ya Hospitali ya Muhimbili kwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ili kupunguza uhaba wa majengo katika Hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shaban Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba majengo hayo yanayomilikiwa na Chuo Kikuu cha Afya Kishiriki cha Muhimbili (MUHAS) na chuo kimekuwa kikiyatumia majengo hayo kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wake.

Mheshimiwa Spika, aidha, Chuo kikuu MUHAS bado kina mipango ya uendelezaji na upanuzi wa eneo hilo ili kutimiza majukumu yake, katika kuzalisha wataalam wa afya nchini.

Mheshimiwa Spika: Serikali tayari imepeleka fedha shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la huduma za dharura kwenye Hospitali ya Bagamoyo na hivyo naomba majengo ya Chuo Kikuu MUHAS yaendelee kutumika kwa shughuli za ufundishaji na utafiti kwa wanafunzi wa Chuo cha MUHAS. Hata hivyo uwepo wa Chuo cha MUHAS ni fursa kwa ukuaji wa Hospitali ya Bagamoyo na ni fursa kwa watu wa bagamoyo kitiba na kiuchumi. Ahsante sana.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, ni lini wananchi wa Kata ya Makurunge watapatiwa eneo la makazi la Razaba baada ya maeneo yao kuchukuliwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 147 la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wakati eneo hili linachukuliwa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji wananchi waliokuwa wakazi wa eneo hilo walilipwa fidia stahiki kwa mujibu wa sheria. Aidha, tunatambua uwepo wa wananchi 16 ambao wamekuwa wakidai kulipwa fidia zao, Serikali inaendelea kushughulikia madai hayo na yatakapokuwa tayari tutawapa taarifa.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO K.n.y. MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuboresha minara ya mawasiliano ya simu katika Kata za Makurunge na Fukayosi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imezijumuisha Kata za Makurunge na Fukayosi katika Mradi wa Tanzania ya Kidigitali unaotekelezwa kwa fedha kutoka Benki ya Dunia ambapo zabuni ya mradi huo imeshatangazwa tarehe 24 Oktoba, 2022.

Mheshimiwa Spika, kata hizo zitapata huduma za mawasiliano kwa teknolojia za 2G, 3G na 4G. Ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga gati ya kuegesha boti na vyombo vya usafiri Bagamoyo ili kuvutia watalii kutembelea Mbuga ya Saadan?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza miundombinu ya kisasa ya kuegesha vyombo vya usafiri katika pwani ya Wilaya ya Bagamoyo ili kuvutia watalii kutumia miundombinu hiyo kwenda kutembelea vivutio vya utalii katika mbuga ya Saadan pamoja na Visiwa vya jirani.

Mheshimiwa Spika, katika kutimiza azma hii, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchi kwa maana ya TPA iko katika hatua za mwisho za kuhuisha mpango kabambe wa kuendeleza miundombinu ya bandari nchini ambao utaainisha mahitaji sahihi ya miundombinu ya gati zinazotakiwa kujengwa kwa ajili ya kuegesha boti na vyombo mbalimbali vya usafiri katika Bandari ya Bagamoyo. Maandalizi ya Mpango Kabambe yanatarajiwa kukamilika Juni, 2022 na kufuatiwa na usanifu wa kina ili kupata taarifa za msingi ikiwa ni pamoja na gharama za utekelezaji wa mradi huo. Kazi hii itafanyika katika Mwaka wa Fedha 2022/2023. Ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, kwa mwaka 2020/2021 na 2021/2022 ni kiasi gani cha gawio kimetolewa na eneo la Utalii Kaole kwa Halmashauri ya Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Magofu ya Kaole kilianza kutambuliwa na kuhifadhiwa kisheria mwaka 1937 ilipoanzishwa Sheria ya Uhifadhi wa Majengo ya Kihistoria, kipindi cha utawala wa Mwingereza na kwa sasa yanalindwa kwa Sheria ya Mambo ya Kale, Sura 333. Hapo awali vituo vya mambo ya kale vilitumika zaidi katika masuala ya tafiti na elimu hivyo kutembelewa zaidi na wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na miongozo iliyopo hakuna gawio lolote linalotolewa kwa Halmashauri kutokana na mapato ya vituo vya malikale. Aidha, Magofu ya Kaole yanatoa fursa kwa wananchi wa Halmashauri ya Bagamoyo kunufaika kiutalii kwa kuuza bidhaa mbalimbali kwa watalii kama vile vitu vya kiutamaduni, vyakula na kutoa huduma ya malazi. Kwa kufanya hivyo, halmashauri hunufaika kupitia tozo mbalimbali kwa wafanyabiashara hao.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga jengo jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uhitaji wa Jengo jipya la Utawala katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Hivyo, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ipo katika maandalizi ya kuanza ujenzi wa Jengo hilo kupitia fedha za Mapato ya Ndani ya Halmashauri ambapo katika mwaka wa Fedha wa 2022/2023 jumla ya Shilingi milioni 500 zimetengwa.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imekamilisha maandalizi ya nyaraka za ujenzi wa jengo hilo na kuwasilisha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuidhinishwa ili ujenzi uweze kuanza kwa kuwa Halmashauri hiyo imepanga kutumia mchoro wao badala ya mchoro ulioandaliwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imetenga pia Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa jengo hilo.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaongeza eneo na kuboresha Skimu ya Umwagiliaji ya Mto Ruvu – Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Skimu ya Kisere ambayo ni miongoni mwa skimu katika bonde la mto Ruvu. Aidha, Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kubaini maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa mabwawa ili kuhudumia skimu zilizopo katika bonde hili, kwani hii itaepusha changamoto ya ukosefu wa maji kwa wakulima kwa kuwa Mto Ruvu unategemewa kwa matumizi mbalimbali ikiwemo matumizi ya majumbani kwa wakazi wa ukanda wa Pwani na Dar es Salaam.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamalizia fedha za ujenzi wa Soko la samaki Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu : -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo n Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Soko la Samaki Bagamoyo limejengwa kwa fedha za Serikali kupitia Halmashauri ya Bagamoyo na limeshaanza kutumiwa na wadau wa uvuvi. Kwa sasa soko hili lina miundombinu ya jengo la mnada, jengo la kuhifadhia samaki, jengo la maliwato, jengo la kuhifadhia taka, kibanda cha askari/mlinzi na jengo la kukaangia samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukamilisha soko hili kuendana na michoro iliyopo, inahitajika kuongezewa jengo moja la kukaangia samaki, jengo la mama lishe, jengo la maduka na jengo la ofisi. Aidha, katika mwaka 2024/2025, Serikali imepanga kujenga miundombinu hiyo iliyosalia katika soko hilo kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (Agriculture and Fisheries Development Programme - AFDP).

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, katika mwaka 2023/2024, Serikali kupitia programu ya kuendeleza kilimo na uvuvi itaweka vichanja kumi (10) vya kuanikia dagaa, mahema mawili (2) ya kukaushia samaki kwa kutumia nguvu ya jua na mtambo mmoja wa kuzalisha barafu katika eneo la karibu na soko hilo.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, lini Seriikali itafanya ukarabati wa majengo ya magofu ya Bagamoyo ili yasianguke na kuleta madhara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umiliki wa majengo mengi katika eneo la Bagamoyo kuwa chini ya usimamizi na umiliki wa mamlaka mbalimbali ikiwemo watu na taasisi binafsi, Wizara imeendelea kuwahamasisha wadau wote kufanya ukarabati usioathiri mwonekano au kuharibu historia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa tayari wadau wanne wamepewa vibali vya kufanya ukarabati wa majengo yao ndani ya Mji Mkongwe wa Bagamoyo. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ipo katika mpango wa kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la Ngome Kongwe baada ya kufanyiwa uokoaji kwa kuliimarisha jengo hilo.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, lini barabara ya Makofia - Mlandizi itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza maandalizi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Makofia - Mlandizi, kilomita 35 ambapo kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina imekamilika. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imepanga kujenga daraja dogo (box culvert) katika eneo la Mbwawa. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa barabara hii, ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kusamehe gharama za matibabu kwa marehemu ili kupunguza maumivu kwa wafiwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilishatoa maelekezo kwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kupitia Waraka Na. 1 wa 2021, wa kutozuia maiti na kuweka utaratibu wa kulipia gharama za matibabu na madeni ya miili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwa Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Wilaya pamoja na Waganga Wafawidhi wa hospitali kwa ngazi zote nchini, kuzingatia maelekezo ya mwongozo huu na kuhakikisha wananchi wanapata huduma pasipo kuwepo kwa vikwazo vya kuchelewesha marehemu kuzikwa.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE K.n.y. MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, lini Serikali itaachia maeneo yaliyotwaliwa na EPZA ambayo hayapo kwenye mipango ya matumizi ili wananchi wayatumie?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya EPZA imetwaa maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuanzisha Kanda Maalum za Kiuchumi. Maeneo hayo yapo katika hatua mbalimbali za utwaaji na uendelezaji. Katika kuendeleza maeneo hayo Mamlaka huandaa Mpango Kabambe ili kuainisha matumizi mbalimbali ya maeneo hayo. Hivyo, maeneo yaliyotwaliwa na EPZA bado yapo kwenye mpango wa matumizi yaliyokusudiwa.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE K.n.y. MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itaachia maeneo yaliyotwaliwa na EPZA ambayo hayapo kwenye mipango ya matumizi ili wananchi wayatumie?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya EPZA imetwaa maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuanzisha Kanda Maalum za Kiuchumi. Maeneo hayo yapo katika hatua mbalimbali za utwaaji na uendelezaji. Katika kuendeleza maeneo hayo Mamlaka huandaa Mpango Kabambe ili kuainisha matumizi mbalimbali ya maeneo hayo. Hivyo, maeneo yaliyotwaliwa na EPZA bado yapo kwenye mpango wa matumizi yaliyokusudiwa.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kufufua zao la nazi katika Ukanda wa Pwani hususan Bagamoyo ili kuleta tija kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati iliyopo sasa katika kufufua zao la nazi ni Wizara kupitia Kituo cha Utafiti cha TARI Mikocheni, imeanza kutekeleza mpango wa awamu ya kwanza wa kuzalisha miche bora ya nazi, ambapo hadi sasa miche 140,000 imezalishwa na itasambazwa kwa wakulima kabla ya Desemba, 2024. Aidha, utekelezaji wa mpango huo unahusisha wadau wenye teknolojia za kisasa za uzalishaji wa nazi, ikiwemo Kampuni ya Deejay Coconut Farm ya Nchini India ambayo imeonesha nia ya kuingia makubaliano ya ushirikiano na TARI.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia Msimu wa 2024/2025 Wizara kwa kushirikiana na wabia wa maendeleo itaendelea na programu ya uzalishaji wa miche bora kutoa mafunzo ya kilimo bora cha nazi kwa Maafisa Ugani na Wakulima katika maeneo ya uzalishaji wa nazi, ikiwemo Bagamoyo, sambamba na kuwaunganisha wakulima na masoko. Vilevile Wizara ipo katika jitihada za kutafuta wawekezaji, kwa ajili ya kuongeza mnyororo wa thamani wa zao la nazi ambao watakuwa tayari kujenga viwanda nchini.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Halmashauri ya Bagamoyo kwa kuwa imekamilisha vigezo vyote muhimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa inaendelea kutekeleza azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 64 ikiwemo chuo cha VETA cha Wilaya ya Bagamoyo kinachojengwa katika Halamshauri ya Mji wa Chalinze. Ujenzi huo unaendelea kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, sambamba na kutekeleza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali imeanza kutekeleza mpango wa ujenzi wa Shule za Sekondari za ufundi 100 ambazo zitajengwa katika Halmashauri ambazo hazina Vyuo vya VETA pamoja na maeneo mengine yenye uhitaji wa Vyuo vya Ufundi Stadi. Halmashauri ya Bagamoyo ni miongoni mwa Halmashauri zitakazojengewa Sekondari ya Ufundi. Nakushukuru.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, lini Vitongoji vya Kimele, Kilemela na Nyakahamba katika Kata za Mapinga na Kerege vitapata maji ya uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vitongoji vya Kimele, Kilemela na Nyakahamba ni kati ya vitongoji 15 vya Kata ya Mapinga na Kerege zinazopata huduma ya maji safi na salama kutoka chanzo cha Mtambo wa Ruvu nchini. Katika kuhakikisha huduma ya maji inakua ya uhakika katika vitongoji hivyo, Serikali kupitia programu ya WSSP II imetekeleza mradi uliohusisha miundombinu ya ulazaji bomba umbali wa kilometa 111.8 na ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 6,000,000 katika eneo la Vikawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huo umeongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Kata za Mapinga na Kerege hususani katika Vitongoji vya Kimele, Kilemela na Nyakahamba. Hata hivyo, kwa baadhi ya maeneo ya Kitongoji cha Kilemela kumekuwa na changamoto za kijiografia na kusababisha kutofikiwa na huduma ya uhakika. Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali inatekeleza mradi wa kuongeza msukumo wa maji ili kupanua mtandao wa upatikanaji wa huduma ya maji katika kitongoji hicho, ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -

Je, lini mradi wa umeme katika eneo la Kitume Kata ya Makurunge - Bagamoyo utaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini yaani REA imeendelea kutekeleza miradi ya kupeleka umeme katika maeneo ya Bagamoyo ambapo katika Kata ya Makurunge eneo la Kitume, REA inatekeleza mradi uitwao Electrification of Small-Scale Mining, Industries and Agricultural Areas in Mainland Tanzania kupitia mkandarasi aitwae M/s Dieynem Company Limited.

Mheshimiwa Spika, mradi huu ulioanza mwezi Machi 2023, umefikia asilimia 57 ambapo kwa sasa mkandarasi amekwisha simika nguzo kwa umbali wa kilometa 9. Mkandarasi anaendelea na kazi iliyobaki baada ya kusimama kutokana na maji ya mvua kujaa katika eneo kubwa ambalo mkandarasi anafanyia kazi. Mradi unategemea kukamilika mwishoni mwezi Desemba, 2024. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza:-

Je, lini Serikali itafanyia ukarabati nyumba chakavu za TBA zilizopo Bagamoyo na kujenga nyingine mpya, ili watumishi na wateja waishi vizuri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ulifanya ukarabati kwa kujenga upya mifumo ya majitaka kwenye nyumba zote 52 za makazi zilizopo Bagamoyo. Kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, Wizara ya Ujenzi, kupitia TBA, imetenga kiasi cha Shilingi 450,000,000.00 kutoka kwenye Bajeti ya Fedha za Ruzuku ya Serikali, kwa ajili ya ukarabati wa nyumba zilizorejeshwa TBA kutoka TAMISEMI katika Mikoa 20, zikiwemo nyumba zilizopo Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani. Aidha, Serikali imeandaa Mpango wa Ujenzi wa Nyumba za Makazi kwenye maeneo yaliyorejeshwa kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ikiwemo Bagamoyo na utekelezaji wa mpango huo tayari umeanza katika maeneo mbalimbali. Ahsante.