Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Muharami Shabani Mkenge (32 total)

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa kuzungumza kitu kimoja:-

Mheshimiwa Spika, sasa hivi ni mwaka wa 12 toka fidia ya mwanzo ilipofanyika na wengine mpaka sasa bado hawajafanyiwa fidia. Na lile eneo Serikali ilishatengeneza GN tayari kiasi kwamba, wananchi wanashindwa kufanya tena chochote katika maeneo yale. Na maeneo yamekuwa mapori, yamekuwa usumbufu, wafugaji wameingia pale inakuwa mgogoro kati ya wakulima na wafugaji. Je, Serikali inaweza ikafanya mpango wowote kuwarudishia maeneo yao hawa wahusika kama hawatakuwa tayari?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, kwa haya majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari mimi na yeye tuongozane bagamoyo tukafanye mkutano wa hadhara Mlingotini, ili awaridhishe wananchi wa kule kwa hili janga ambalo lilewapata kwa miaka 12 sasa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwanza fidia ya mwisho iliyolipwa kwa wananchi hao ilikuwa ni mwaka wa fedha 2017/2018 kwa hiyo, sio kweli kwamba, ni zaidi ya miaka 12 katika malipo ya mwisho yaliyolipwa fidia kwa wananchi hao.

Mheshimiwa Spika, maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya maendelezo, hasa kwa sekta ya viwanda na uwekezaji mwingine ni muhimu sana. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa mkenge kwamba, si vema maeneo ambayo yameashaainishwa kwa ajili ya maendeleo ya viwanda na uwekezaji mwingine kurudishwa kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali inaendelea kuona umuhimu wa kulipa fidia hizo haraka iwezekanavyo, ili uendelezwaji wa maeneo hayo uweze kufanyika. Lakini pili tunaendelea kushauri Serikali za Mikoa na halmashauri kuona namna bora ya kuyamiliki maeneo ambayo Serikali Kuu kwa maana ya kupitia EPZA tutakuwa bado tunashindwa kuyalipa, ili nia ya Serikali ya kuwa na maeneo maalum ya uwekezaji na hasa kwa ajili ya maendeleo ya viwanda yaendelee kuwepo kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mheshimiwa Mkenge niko tayari, tutaongozana na wewe na wataalamu wetu kutoka EPZA ili kuweza kuongea na wananchi wa Mlingotini kwa ajili ya kuona namna bora ya kuendeleza, hasa kulipa fidia maeneo haya ambayo yametwaliwa.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi huu ni mpya kabisa katika Ukanda wetu wa Pwani ya Bagamoyo na Kata za Yombo, Magomeni, Nia Njema, Makurunge pamoja Fukayosi, wamejiandaa kuupokea mradi huu kwa ajili ya kilimo cha miwa. Sasa, je, ni lini Serikali itawapa mafunzo hawa watu, ili waweze kuzalisha kilicho bora kwa ajili ya kupeleka kiwandani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali namba mbili; katika jibula msingi Serikali imetenga hekta 3,600 kwa ajili ya outgrowers. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza akanionesha hizo hekta kusudi nisikae katika mikutano ya watu nikawaambia kwamba tumetengewa hekta 3,600 wakati mimi mwenyewe Mbunge sijazijua bado? Yuko tayari kwenda kunionesha ili nikienda katika mikutano niwaambie wananchi wangu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu maswali ya nyongeza mawili ya Mheshimiwa Muharami, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mafunzo yataanza hivi karibuni ambayo tutashirikiana na mwekezaji katika wakulima wote watakaoingia katika hiyo scheme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuwa niko tayari kwenda, baada ya Bunge hili tutakwenda pamoja tutafanya ziara na tutaelekezana wapi hiyo scheme ya outgrowing itafanyika.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na maswali mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, tatizo lilolopo Chalinze ni sawa na tatizo lililopo Bagamoyo na hasa katika Vijiji vya Mkenge Kidomole pamoja na Vijiji vya Milo. Sasa swali langu ni kwamba, kutokana na tatizo la wakulima na wafugaji eneo lililotengwa halitoshi, ni dogo sana kwa vijiji hivyo. Ni lini Serikali itaongeza hili eneo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, Serikali inazingatia sana maoni na ndiyo maana hata maoni uliyoyatoa ni katika sehemu ya mpango wetu wa bajeti tunayokwenda ya kuboresha zaidi NARCO ili iweze kukidhi haja ya kuhakikisha kwamba wadau wetu mnafurahi na kuweza kutumia fursa ya ardhi hii kubwa na nzuri ya Serikali kuweza kufanya shughuli za uzalishaji kupitia mifugo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa hili la Bagamoyo Serikali iko tayari kupokea tena maombi ya wananchi na kuyafanyia kazi kwa ajili ya kuweza kuondoa kabisa migogoro ya wakulima na wafugaji.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa barabara hizi ahadi yake ni ya muda mrefu na zimetengewa kiasi kidogo sana cha pesa. Na tuna barabara nyingi sana ambazo katika Mji wa Bagamoyo zinahitaji kupata huduma ya lami, mfano.

Je, ni lini Serikali itachukulia umuhimu Barabara ya Makofia – Mlandizi kwa sababu ni barabara muhimu sana ambayo inapita katika chanzo cha maji ambayo wanakunywa watu wa Dar-es-Salaam pamoja na pwani ambapo panaitwa bomu. Ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami hii njia ili kunusuru magari yanayonasa kupeleka dawa wananchi waweze kunusurika afya zao katika mikoa hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, kama ifuatatvyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameainisha hapa, moja kwamba hizi barabara imekuwa ni ahadi ya muda mrefu na fedha inayotengwa ni ndogo, lakini pili ameanisha Barabara ya Kofia – Mlandizi ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wake wa Jimbo la Bagamoyo kwamba, ni lini sasa Serikali tutatenga fedha:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kama nilivyojibu katika majibu ya awali kwamba, moja ya wajibu wetu sisi ni kupokea mapendekezo yanayoletwa na Wabunge, lakini la pili ni kuhakikisha kwamba, zile ahadi zote ambazo viongozi wetu wakuu walizitoa zinatekelezwa. Na tutaendelea kuzitekeleza kwa kadiri ya upatiakanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndio maana katika jibu langu la msingi nikasema niwaombe Wabunge wote wapitishe Bajeti Kuu ya Serikali ili kile chanzo kilichokuwa kimetengwa zile fedha maana yake zitaongeza kuna kitu tutakwenda kukifanya. Na haya maombi mnayoleta maana yake tutayatekeleza. Hakuna barabara yoyote inaweza kutekelezeka bila kuwa na fedha. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge muweze kufanya hivyo, ili tuweze kufanya kazi nzuri ya kuwasaidia wananchi wetu. Kwa hiyo, tunayapokea hayo tutayafanyia tathmini na tutayaweka katika mipango yetu, ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Waziri anaweza kutueleza ni mafanikio yapi yamepatikana katika mpango huo toka umeanza kutekelezwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Bagamoyo imekumbwa na changamoto kubwa sasa hivi ya kumegwa ardhi na maji ya bahari na hasa katika Chuo cha Sanaa Bagamoyo na maeneo mengineyo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inadhibiti hali hiyo isiweze kuendelea.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Muharami kwa juhudi yake ya ufuatiliaji wa mazingira lakini na mabadiliko ya tabianchi katika Jimbo lake la Bagamoyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio ambayo yamepatikana katika miradi hii, moja; ofisi tano za BMUs tumejenga katika Wilaya za Bagamoyo na Pangani. Sehemu ambazo zimejengewa ofisi hizo na kuzipatia samani ni pamoja na Saadani, Chalinze; Zingibari, Mkinga; Kipumbwi, Pangani; Dunda, Bagamoyo; na Sudimtama na tumewanunulia viatu na makato kwa ajili ya kusimamia usafi huu wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni kweli kwamba Bagamoyo ni moja ya kati ya sehemu ambazo zina changamoto kubwa za mabadiliko ya tabianchi, lakini tayari ofisi yetu imeshapeleka watalaam kufanya upembuzi yakinifu na kufanya survey ambayo ni sahihi na watalaam hawa wameshaleta majibu, siku za karibuni hivi basi mradi utaanza kutekelezwa katika eneo hilo. Ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini majengo yale ni zaidi ya miaka 10 sasa yamekaa hayana matumizi yo yote. Swali la kwanza; je, MUHAS lini wanaanza huo upanuzi wao wa hayo maeneo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa nini wasiwaazime Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo yale majengo yakatumika kwa Hospitali ya Wilaya ili mradi majengo yale yapate kutumika, yasiendelee kuharibika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anawakilisha wananchi wa Bagamoyo. Ameuliza swali ni lini wataanza kufanya upanuzi na kuyatumia, nafikiri yanatumika wakati wote lakini nitakwenda tutembelee mimi na yeye na tuweze kuwasiliana na utawala wa MUHAS ili tuweke mkakati mzuri wa kuhakikisha wanashirikiana ofisi ya Mbunge na wananchi wa Bagamoyo na Chuo cha MUHAS.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ninachoweza kumwambia ndugu yangu ni kwamba, kikubwa kwa wananchi wa Bagamoyo, Chuo Kikuu kila Mbunge hapa angetamani Chuo Kikuu kiwepo ndani ya Jimbo lake. Chuo Kikuu kuwepo ndani ya Jimbo lako ni fursa kubwa sana. Kwa hiyo, kikubwa mimi na yeye tutakachokifanya ni kujenga uhusiano na Hospitali ya Wilaya na Chuo Kikuu cha MUHAS ili waweze kushirikiana na kufanya kazi pamoja na kufufua yale majengo ili hospitali ya Mheshimiwa iweze kupanuka, lakini manufaa ya watumishi yapatikane. Kwa upande wa hospitali ya wilaya lakini manufaa yanayotokana na Chuo Kikuu yapatikane kwa watu wa Bagamoyo. Tutakwenda kusisita umuhimu wa mahusiano. Ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo inadaiwa viwanja takribani 1,000 na pia hao wananchi wa Makurunge hawana sehemu ya kukaa ambayo ipo sahihi.

Je, ni lini Serikali au Wizara itawapatia Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo mashamba mawili ambayo ni Greenwood na Jeneta ambayo umiliki wake ni wa utata ili kuweza kuwasidia wananchi hawa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri ni lini anaweza akaja Bagamoyo ili kuja kuyaangalia yale mashamba ya Greenwood na Jeneta ili atoe tamko la Serikali kuhusu umiliki wake yale mashamba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, juu ya shamba la Greenwood na Jeneta nadhani taratibu za kisheria zinaeleza na wananchi wa Bagamoyo wanatakiwa wafuate hizo taratibu kama kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo ili kama Serikali itajiridhisha juu ya maombi yao na kama ninavyosema kwamba kutakuwa na utata wowote basi tutaangalia kuona jinsi gani tunaweza kuliamua.

Mheshimiwa Spika, juu ya suala la pili, Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie tutakamaliza Bunge hili katika kipindi nitakachokuwa kwenye ziara katika Jimbo langu litakuja Bagamoyo ili tuweze kushughulikia kero hiyo. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Bagamoyo Kata ya Zinga, Kijiji cha Mlingotini, kuna wakulima mahiri kabisa wa mwani.

Je, ni lini Serikali itawapatia vifaa hususan boti ili waweze kufika katika maeneo ya uzalishaji kwa urahisi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Muharami Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna chama kikubwa na cha mfano cha ukulima na uchakataji wa mazao yatokanayo na mwani, kinaitwa Chama cha Ushirika cha Msichoke kilichopo Mlingotini – Bagamoyo kimeomba jumla ya fedha shilingi milioni 40. Chama hiki kitapata fedha hizi hapa karibuni kwa lengo la kununua boti itakayowawezesha kina mama wale kuingia baharini kwenda kuchukua mazao yale na vile vile kamba na taitai na zana zingine. Hongera sana Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Bagamoyo, ahsante sana.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Zanzibar inatembelewa na watalii wengi sana kwa kipindi cha mwaka mzima na wengi wanatamani kuja Bagamoyo kuja kuangalia vivutio vilivyopo pamoja na kutembelea Mbuga ya Wanyama ya Saadan, lakini kikwazo kikubwa wanachokipata ni sehemu ya kupaki boti kwa ajili ya kushuka ili waweze kufanya utalii. Je, Serikali ina mpango gani kuliingiza suala hili katika bajeti ya mwaka ujao ili kuunga mkono juhudi za Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan katika suala zima la Royal Tour?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa shughuli nyingi sana za usafiri kati ya Bagamoyo na Zanzibar za mizigo pamoja na abiria zinafanyika kwa boti za kawaida na majahazi ya kawaida. Je Waziri yuko tayari kutembelea Bagamoyo ili aone shughuli zinazoendelea pale ili alitilie umuhimu suala hili?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo.

Sasa napenda kujibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza anataka kujua nini committent ya Serikali katika bajeti ijayo kwa ajili ya ujenzi wa haya magati. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumekuwa na mpango kabambe wa kuainisha bandari zote nchini ikiwemo na Bandari ya Bagamoyo katika ujenzi wa hizi gati na nimhakikishie kwamba tayari kwenye mwaka wa fedha ujao, ambako tutasoma bajeti yetu, tumetenga fedha kwa ajili ya kujenga gati katika Bandari hii ya Bagamoyo.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, kwa mwaka huu wa fedha ambao unaendelea, tayari tumetenga kiasi cha Shilingi milioni 68 kwa kushirikiana na wenzetu wa Maliasili na Utalii ambapo tumeweka front dock yard kwa ajili ya kupokea majahazi, lakini pamoja na boti kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anataka kujua ama anaomba nitembelee Bandari ya Bagamoyo na nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na yeye mara baada ya Bunge la Bajeti, nitafika Bandari ya Bagamoyo kujiridhisha. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je Serikali haioni iko haja sasa ya kuondoa hizo sheria, miongozo na kanuni ili wananchi wa Kaole waweze kupatiwa gawio kwa kile ambacho kipo katika mji wao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je ni lini Serikali sasa ina mpango wa kuwatumia wazee wa Kaole kuelezea historia ya magofu ya kale pamoja na kaole kwa wageni wanaokuja badala ya kuwatumia waajiriwa ambao historia hiyo wameisoma kwenye vitabu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mharami Shabani, Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa namna ambavyo sasa hivi Wizara ya Maliasili na Utalii makusanyo yake yanaenda Mfuko Mkuu hatuoni haja ya kurekebisha sheria hii kwa sababu makusanyo yote yanayokusanywa yanaenda Mfuko Mkuu na yanapofika kwenye Mfuko Mkuu, halmashauri zinapokea ruzuku mbalimbali ambazo zinatoka katika Mfuko Mkuu. Kwa hiyo fedha yote inayokusanywa katika maeneo haya tuna uhakika kwamba inaenda kulenga wananchi wa Tanzania nzima kutokana na masuala mazima ya utalii.

Mheshimiwa Spika, hili lingine alilosema la kutumia wazee tunalipokea, tutawashirikisha wazee wa Bagamoyo pamoja na maeneo mengine zilipo malikale ili tuweze kuipata historia kamili ya Tanzania pamoja na wazee wetu waliotutangulia, ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya muuliza swali.

Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itakamilisha Barabara ya zamani kutoka Picha ya Ndege mpaka Mlandizi ili kupunguza foleni katika Barabara ya Morogoro?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Barabara ya Makofia - Mlandizi ni barabara ambayo ipo katika Ilani ya Chama kwa miaka mingi Je, ni lini Serikali itaanza kulipa fidia kwa wananchi wanaoishi katika maeneo haya kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa hiyo barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mpango ni kuiboresha na kuipanua barabara mpya ambayo tunayo, kwa sasa tutaanza kufanya hiyo kazi ya kujenga barabara hizo nne badala ya kuanza na ile barabara ya zamani aliyotaja Mheshimiwa Mbunge. Nadhani kwa kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza msongamano ambao upo na ndiyo lengo kubwa kuijenga ile barabara kwa njia nne zinazokwenda, zinazorudi lakini pia na zile zilizopo zitaendelea kuwepo.

Mheshimiwa Spika, suala la pili la Barabara ya Makofia – Mlandizi, Serikali sasa hivi inatafuta fidia ili kuwafidia wale wananchi ambao walishatathminiwa ambapo tuta-review tathmini na kuanza kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Benki ya Kilimo Tanzania imekasimu madaraka yake kwa Benki mbalimbali ikiwemo CRDB pamoja na NMB kwa ajili ya utoaji mikopo, lakini masharti yaliyokuwepo katika ukopaji huo ni magumu sana ikiwepo na kutoa asilimia ishirini na tano ya kile unachotaka kukopa, kutoa dhamana ya nyumba pamoja na cash flow ambayo inaelea katika benki ya mwaka mmoja. Je, ni lini sasa Serikali itapunguza masharti haya ili wakulima wapate nafuu kwa ajili ya kilimo na hasa wakulima wangu wa Bagamoyo ambao ni maskini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikiri ni kweli kumekuwa na changamoto ya wakulima wetu kukopesheka kirahisi na ndiyo maana Serikali tumechukua hatua madhubuti za kuhakikisha kwamba tunakaa na taasisi za fedha waelewe mfumo wa ukopeshaji katika kilimo ambao ni tofauti na maeneo mengine. Kwa hivi sasa tumekuja na mfumo mzuri ambao tumeu–design mikataba ya utatu ambayo imetusaidia sana kupunguza masharti mengi ambapo anakaa mkulima, anakaa off taker, anakaa na benki kwa upande mmoja ili mkulima aweze kukopesheka kutumia mikataba aliyonayo pasipo kutumia hati za nyumba na sababu zingine ambazo zinamfanya asiweze kufikia kwenye ukopeshwaji huo. Kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kama Serikali tumeliona hilo na tunaendelea na mikakati hii kuhakikisha kwamba mkulima wetu anakopesheka kirahisi. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika Jimbo la Bagamoyo, Kata ya Magomeni, maeneo ya Sanzale, Kata ya Makurunge, Kamata ya Fukayosi maeneo ya Kijiji cha Mkenge, hakuna kabisa mawasiliano, ni ya shida sana. Ni lini sasa Serikali itapeleka wataalam kule kwenda kuweka minara mawasiliano yapatikane?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Muharami Mkenge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema kwamba tulianza na vijiji 2,116 ambapo ni katika mwaka wa fedha 2022/2023 na sasa katika awamu inayofwatia ambayo ni 2023/2024 vijiji na kata za Jimbo la Bagamoyo zitaingizwa katika utaratibu wa kufanyiwa tathmini na baadaye Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kwenda kufikisha huduma ya mawasiliano, ahsante sana.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nina swali moja la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa jengo hili la Halmashauri ya Bagamoyo limejengwa toka miaka ya 1970, na sasa hivi linavuja, nyaraka nyingi zinaloa na Mkurugenzi anapata shida kufanya kazi na wafanyakazi wake ambao wako katika maeneo tofauti tofauti: Je, Serikali haioni umuhimu katika bajeti ya mwaka huu kutuongezea pesa kuanza ujenzi huo mara moja, kwa sababu, mapato yetu ya Halmashauri ni madogo sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, ni kweli jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo linalotumika sasa ni la muda mrefu. Kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, wao wenyewe Halmashauri walitenga fedha, shilingi milioni 500 kwenye mapato yao ya ndani na katika bajeti ya mwaka wa fedha unaokuja vilevile wametenga tena shilingi milioni 500.

Mheshimiwa Spika, vilevile wao wameenda na mchoro ambao utatumia zaidi ya shilingi bilioni 5.34, lakini mchoro ule uliotolewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ulikuwa una gharama ya shlingi bilioni 2.7 tu. Kwa hiyo, inaonesha wao walikuwa wana uwezo wa kujijengea jengo lao wenyewe na kutenga hizi fedha kwa sababu walichagua mchoro wa ghorofa mbili badala ya ghorofa moja, naomba kuwasilisha.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza. Bonde la Mto Ruvu katika sehemu ya Bagamoyo lina wakulima wengi sana ambao wanatokea Kata za Yombo, Magomeni na Makurunge: Je, ni lini sasa Serikali itawaombea wananchi hawa kupata eneo la Magereza ambalo ni kubwa na halina kazi yoyote inayoendelea ili waweze kufanya kilimo na kupata mahitaji yao?

Swali la pili. Mheshimiwa Waziri ni lini atakuja Bagamoyo kutembelea skimu ya umwagiliaji Ruvu inayojulikana maarufu kama JICA ili kuweza kuja kuzungumza na wakulima pale na kutupa matumaini kwa ajili ya kutengeneza skimu ile? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli pale kwenye eneo la Gereza la Kigongoni tunazo hekta zaidi ya 1,350 na kumekuwa na changamoto juu ya matumizi ya wananchi katika ardhi ya eneo hilo. Nachukua fursa hii kumwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji waende kukaa na uongozi wa gereza ili waone namna ambavyo wananchi wa kata ulizozitaja wataweza kushiriki kilimo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili la kuhusu kutembelea Bagamoyo baada tu ya vikao vya Bunge la Bajeti, mimi na wewe tutakwenda kuzungumza na wakulima ili tuweze kusikiliza changamoto zao na tuweze kuwatatulia ili wafanye kilimo cha umwagiliaji.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa mamalishe wengi waliokuwepo katika soko la zamani wamekosa nafasi katika soko jipya. Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya ujenzi wa dharula katika jengo la mamalishe ili kuwanusuru mamalishe waweze kufanya shughuli zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Bagamoyo ina wavuvi wengi ambao wanavua bila kuwa na utaalam. Je, Serikali ina mpango gani wa kutuma watu kuja kutoa mafunzo ya ubora na dhana bora ili wavuvi wasiweze kugombana na Serikali mara nyingi katika uvuvi wao?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jambo la kwanza ni mpongeze vile vile Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo kwa kufatilia sana jambo hili na bahati nzuri katika soko analolieleza mimi binafsi nimefika na nimejionea hali halisi. Kwa hiyo, sisi kwa kushirikiana na Halmashauri yake tutazungumza na Halmashauri ili tuone namna bora ya kutekeleza huo udharura wa kuwasaidia wale mama lishe ambao walikosa nafasi katika soko la awali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuhusu wataalam, nimhakikishie tu kwamba wataalam tunao na tutawatuma ili waweze kupeleka elimu ya utaalam wa uvuvi kwa wananchi wake, ahsante sana.

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru, katika Kata za Fukayosi na Makurunge katika Jimbo la Bagamoyo, DAWASA Chalinze wamesambaza miundombinu ya maji mwaka wa pili sasa lakini maji hayatoki.

Je, ni lini sasa maji katika maeneo haya yatatoka?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba niwe nimelipokea, nikalifanyie ufuatiliaji kwa nini maji hayatoki na usambazaji umefanyika.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza pamoja na ombi moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali. Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Mji Mkongwe watafanya ukarabati wa lile Jengo la Ngome Kongwe ya Bagamoyo; je, ni lini kazi hiyo itaanza rasmi kufanyika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi. Wananchi wa Kaole na Wazee wa Kaole Bagamoyo wamenituma; wanashukuru sana kwa eneo lao kuwa eneo maarufu kwa utalii wa malikale, lakini ombi lao ni kwamba pale pana msikiti wa miaka mingi, kwa hiyo, wanaomba ule msikiti uhesabike kama misikiti mingine na watalii pamoja na watu wengine watakapokuja wavue viatu ili watakapoingia mle ndani ili kutunza mila na utamaduni wa misikiti katika Mji wa Kaole Bagamoyo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali nampongeza sana Mheshimiwa Muharami, Mbunge wa Bagamoyo kwa namna ambavyo anaendelea kutunza historia hususan ya malikale. Pia nawaomba wananchi wa Bagamoyo tuendelee kushirikiana kwa pamoja, kulinda na kuendeleza hizi malikale tulizoachiwa na waasisi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la lini kazi hii itafanyika kwa mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, niwaahidi tu wanachi wa Bagamoyo, kwa mwaka wa fedha unaokuja ambapo tayari bajeti tumeshapitishiwa, tutaanza ukarabati wa jengo hili. Kwa hili la msikiti natoa tu maelekezo hapa hapa kwamba Mkurugenzi wa Maliakale ashirikiane na viongozi walioko katika Wilaya ya Bagamoyo kuhakikisha anatoa maelekezo kwamba msikiti huu ni sawa na misikiti mingine na heshima zinazotakiwa kama msikiti watu waingie bila viatu, basi utekelezaji wake uanze mara moja, ahsante. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, Kata ya Mapinga katika Jimbo la Bagamoyo katika sensa ya mwaka huu ina watu 42,000 na haina kituo cha afya.

Je, Serikali ina mpango gani kujenga kituo cha afya katika kata hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tutatuma timu katika Kata ya Mapinga kule Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuweza kufanya tathmini na kuona kama vigezo vimefikiwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, halafu tutatafuta fedha kwa ajili ya kujenga kituo hicho cha afya.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Wananchi wa Kiharata katika Kata ya Mapinga wamepambana wamepata kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi. Je, Serikali ipo tayari kutusaidia ili tuweze kukamilisha Kituo hicho mapema?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shabani Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tunafahamu juhudi za Mbunge na wananchi wa Jimbo lake katika kutunza usalama raia na mali zao na uwepo wa Vituo vya Polisi ni moja ya mahitaji ya kukamilisha jambo hilo. Ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutashirikiana nae mwenyewe, wadau wa Wilaya ya Bagamoyo pamoja na wananchi ili kujenga kwenye kiwanja hiki cha Mapinga ambacho wananchi wamejitolea kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Ni moja ya eneo tutakaloingia kwenye mipango yetu ya uendelezaji wa Vituo vya Polisi. Nashukuru.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumuuliza swali la nyongeza Mheshimiwa Waziri. Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, wafanyakazi wake wanakaa sehemu tofauti tofauti, kutokana na uchakavu wa jengo, na jengo kuwa na nafasi ndogo. Je, ni lini Serikali itatujengea jengo jipya na maombi tulishapeleka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Muharami, Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kujenga majengo haya ya utawala, mpaka sasa takribani jumla ya Bilioni 224.5 zimetumika kwa majengo ya Halmashauri 95, tunafahamu Bagamoyo mlileta maombi hayo, nikuhakikishie kwamba tunaendelea kutafuta fedha na baada ya hapo tutaanza shughuli za ujenzi wa jengo la Halmashauri. Ahsante. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itajenga daraja linalounganisha kati ya Mbweni na Mapinga, Bagamoyo ili kupunguza foleni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Kibaha kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, daraja alilolitaja pia ni barabara ambayo ipo kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami na tunapojenga barabara hizo ni pamoja na madaraja yanayohusika kwenye hizo barabara, ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Wananchi wa Kiharata katika Kata ya Mapinga wamepambana wamepata kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi. Je, Serikali ipo tayari kutusaidia ili tuweze kukamilisha Kituo hicho mapema?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shabani Mbunge wa Bagamoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunafahamu juhudi za Mbunge na wananchi wa Jimbo lake katika kutunza usalama raia na mali zao na uwepo wa Vituo vya Polisi ni moja ya mahitaji ya kukamilisha jambo hilo. Ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutashirikiana nae mwenyewe, wadau wa Wilaya ya Bagamoyo pamoja na wananchi ili kujenga kwenye kiwanja hiki cha Mapinga ambacho wananchi wamejitolea kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Ni moja ya eneo tutakaloingia kwenye mipango yetu ya uendelezaji wa Vituo vya Polisi. Nashukuru.

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; barabara hii iliyofanyiwa tathmini, je, ni lini wananchi wake watalipwa fidia zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; miezi miwili iliyopita, nilihudhuria utiaji saini Mkataba wa BRT, awamu ya tatu ambao umejumuisha ujenzi wa kipande kilichobakia cha Barabara kutoka Tamko kuja Mapinga Bagamoyo. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kipande hiki cha barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Barabara hii ya Makofia - Mlandizi tulishakamisha usanifu na tulifanya tathmini kwa maana kupata gharama ya fidia mwaka 2018, lakini hatukufika mpaka mwisho. Kwa hiyo zoezi hilo limerudiwa na Mheshimiwa Mbunge atakuwa shahidi kwamba tayari watu wameshapita na hatua ambayo tunayo sasa hivi, ni kupata uhakiki ili jedwali la malipo liende Hazina kwa ajili ya kuandaa malipo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, zoezi hilo linaendelea na watalipwa baada ya kuhakikiwa na kuridhika kwamba hiki ndio kiasi ambacho wanatakiwa walipwe hao ambao wataipisha hiyo barabara.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala lake la pili ni kweli Barabara ya Tamko – Mapinga tulishatia saini na nakiri kushiriki. Mheshimiwa Mbunge, atakubaliana nami kwamba, barabara hii haikuwa na hifadhi ya kama barabara. Sasa Mkandarasi kuna mambo ya kimkataba ambayo anakamilisha na sisi kama Serikali tuko tunamfuatilia kuona anakamilisha zile taratibu ili aanze kuijenga na tuko kwenye hatua za mwisho, barabara hiyo sasa itaanza kujengwa kwa sababu tayari tulishawekeana saini, ahsante.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wengi wanapata changamoto wakati wa kwenda kutoa miili ya marehemu kwa kuweka dhamana ya Vitambulisho vya Taifa na kusababisha kukosa vitambulisho hivyo kwa muda mrefu kwa kupata huduma za kijamii mtaani.

Je, ni lini sasa Serikali itapanga utaratibu mwingine wa dhamana ili kuwaacha wananchi wabaki na Vitambulisho vyao vya Taifa, waweze kuendelea kuvitumia katika huduma za kijamii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka kugawana gharama za matibabu nusu kwa nusu na wafiwa ili kuweza kuwasaidia watu wasio na uwezo kuondokana na mzigo wa madeni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia vizuri kwenye eneo hili ambalo limekuwa likiwatesa Wabunge walio wengi. Kupitia swali hili namhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kwamba, tutaongeza nguvu sana kwenye kuona ni namna gani tunasimamia eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kwa swali lake la kwanza, kwa maana ukichukua kadi ya mpiga kura unaweza ukamsababisha mwananchi huyu akakosa huduma nyingine wakati anaendelea kulipa deni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, tutaenda kutafuta njia nyingine. Waraka haujasema chukua kitambulisho cha mwanannchi ya Taifa. Waraka unasema uwekwe utaratibu ambao mwananchi anaweza, tuna communication nyingi na njia nyingi za kuwasiliana ambazo hazihitaji kuchukua ile kadi ya Taifa, Kitambulisho cha Taifa. Kwa hiyo, tutakwenda kulishughulikia Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, suala la kugawana; moja, kwanza kwa sasa gharama ambazo watu wanalipa kwenye hospitali za Serikali wanachangia, hawalipi package nzima ambayo inatakiwa kulipwa. Pia, tuna utaratibu ambao moja, huyo mwananchi akiufuata anasamehewa kabisa au kupunguziwa gharama kama hawezi kuzilipa zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna mifumo mingi ambayo inaweza ikafanya. Sisi ni kusimamia na kuhakikisha wale watendaji walioko kule hospitalini ambao wanatakiwa kuwafuatilia watu na kuona namna ya kusaidiwa wafanye kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ni kwamba, kuna baadhi ya watendaji wetu hawafanyi kazi zao kwa uadilifu. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, katika Jimbo la Bagamoyo, Kata ya Mapinga maeneo ya Mingoi, Msongola, Kialaka na Kiembeni yamepata changamoto kubwa ya kupanuka kwa Mto Mpiji na kusababisha makazi ya watu kubomoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali sasa itakuja kufanya tathimini, hatimaye kujenga kingo za mto huo ili maji yasiweze kuathiri nyumba za watu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu la msingi hili ambalo nimejibu sasa hivi hapa kwamba tayari tumeshatenga fedha shilingi bilioni moja, tunakwenda kuanza kufanya tathimini kwenye maeneo yote ambayo kwa namna moja ama nyingine yamepata athari ya mvua ama athari ya mabadiliko ya tabianchi ili tuone wapi tunahakikisha tunaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu Mheshimiwa baada ya Kawe tutakuja Bagamoyo kuja kuanza kufanya tathimini Mheshimiwa. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kituo cha TARI kilichopo Chambezi, Bagamoyo, ni wazalishaji wakubwa sana wa miche ya minazi. Je, Serikali ina mpango gani kwa hii miche inayozalishwa angalau kuwagawia Wanabagamoyo miche 10 kila kaya ili kuweza kufufua zao la minazi Bagamoyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Je, Wizara sasa haioni umefika wakati wa kuanza kufundisha makundi mbalimbali kuotesha miche ya minazi, kama wanavyofanya kwenye korosho, ili kuleta wingi na uharaka wa uzalishaji wa miche hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ombi la Mheshimiwa Mbunge la kugawa miche kwa kila Kaya, hilo linazungumzika na linawezekana kutekelezeka kulingana na idadi ya miche. Kwa hiyo, tutaanza kutekeleza hilo kwa kaya na kwa awamu. Kwa hiyo, nakuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakuja katika Halmashauri yako ya Bagamoyo na tutalitekeleza hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuwafundisha wakulima namna ya kupanda miche ya minazi, kwa maana ya kuzalisha miche. Tutaiagiza TARI, Chambezi iliyoko pale Bagamoyo ianze kufanya zoezi hilo ili kupunguza hii adha ya Serikali muda wote kupeleka nguvu kwa wananchi. Kwa hiyo, hilo tutalitekeleza.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Je, ni lini sasa Serikali itaanzisha mpango maalum wa usuluhishi baina ya mtu na mtu katika masuala ya ardhi ili kupunguza migogoro ya kesi za ardhi Mahakamani?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea na mikakati mbalimbali ikiwepo eneo moja ambalo tunalifanyia kazi kwa kasi kubwa sana linaloitwa Kliniki ya Ardhi ambapo wale wanaogombana tunawakutanisha, kuwaweka sawa na nia ya kuwapatanisha inakuwepo pale. Hata hivyo, kuhusu masuala ya kupelekana Mahakamani, nadhani watu wengine ni kwa sababu huko mwanzo tulikuwa hatujawa wazi sana juu ya hizi Kliniki na kwa sasa tumeacha mlango wazi na tunaendelea na zoezi hili.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; tunatambua kwamba Serikali ina mpango wa kujenga Shule za Ufundi katika Halmashauri zote ambazo hazijapata vyuo vya VETA. Je, ujenzi huu utaanza lini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Chuo cha VETA kinachojengwa katika Wilaya ya Bagamoyo Halmashauri ya Chalinze mpaka sasa kinasuasua ujenzi wake na hatujui hatma yake ni lini kitamalizika. Je, Serikali ina kauli gani kumaliza chuo hiki ili wananchi wa Bagamoyo na wananchi wa Chalinze, wanafunzi wetu na vijana wetu wapate kusoma katika vyuo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mkenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake muhimu kwa Wanabagamoyo na Chalinze kwa ujumla na naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 87 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa shule hizi za amali kwa awamu. Kwa hiyo, katika kipindi hiki kwanza katika mwaka huu wa fedha tutajenga shule hizo 100, lakini ujenzi huu utaanza kwa awamu. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge tayari hivi sasa tumeshaanza kupeleka fedha ambazo ni kati ya shilingi milioni mia tano na ishirini na nane plus katika kila Halmashauri ambayo inataka kujengewa shule hizo.

Mheshimiwa Spika, ni matarajio yetu ndani ya quarter hii ya kwanza ya mwaka huu ujenzi huu wa shule hizi za sekondari za amali katika maeneo haya niliyoyataja uweze kuanza mara moja.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la pili, katika Chuo chetu cha VETA pale Chalinze na bahati nzuri na nilifanya ziara pale nimetembelea eneo lile kulikuwa na changamoto za design pamoja na wajenzi wetu wale tukajaribu kutatua. Nimwondoe hofu tayari tumeshazungumza na wenzetu wa Wizara ya Fedha, tulipokea mwanzoni shilingi bilioni 49 bado shilingi bilioni 51 hatujazipokea kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.

Mheshimiwa Spika, tumekubaliana na Wizara ya Fedha ndani ya quarter hii ya kwanza tutahakikisha kwamba fedha zile shilingi bilioni 51 tumezipata ili kuendelea na ujenzi katika maeneo yote ya Wilaya hizi 64 ili kuhakikisha kwamba ujenzi huu unakamilika ndani ya mwaka huu ili mwakani vijana wetu waanze kupata mafunzo katika maeneo haya.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru, nina maswali mawili tu ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyojibu kwenye jibu lake la msingi kwamba kuna mpango wa kuongeza usambazaji wa maji katika Kitongoji cha Kilemela, je, ni lini mpango huo utaanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kata ya Makulunge pamoja na Kata ya Fukayosi zinapata maji kutoka katika mtambo wa Wami. Vitongoji vya Engero, Mkwama, Kijiji cha Mkenge pamoja na Kitongoji cha Kalimeni wananchi wake hawajapata maji mwezi mmoja sasa, je, ni lini Serikali itarekebisha huo mtambo wa Wami ili wananchi hawa waweze kupata maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri sana ambayo anaendelea kuifanya katika jimbo lake na kwa kuwasemea wananchi wake hasa katika sekta ya maji ameendelea kutupatia ushirikiano mzuri sana pale ambapo changamoto zinapotokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa upande wa Kibaha na Bagamoyo tumetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kupanua wigo wa kufikisha huduma ya maji safi na salama katika vitongoji. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, vitongoji ambavyo amevileta tutavifanyia kazi na tutaangalia namna ambavyo tutaenda kuvifanyia utafiti na kupata gharama halisi ili mradi uweze kuwafikia wananchi wapate huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la mtambo ambao una changamoto, Serikali kupitia Wizara ya Maji tumeendelea kuhakikisha kwamba tunachukua hatua stahiki pale ambapo panatokea tatizo lolote lile katika mitambo yetu ili tuwe na uhakika wananchi wetu wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama na hayo ni maelekezo ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hayo ni maelekezo ya Ilani yetu ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha watu wanapata maji ya kutosha katika wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, katika Kitongoji cha Changwahela kilichopo katika Kata ya Mapinga, mradi kama huo wa kupeleka umeme katika migodi ya wazalishaji chumvi umefanyika lakini wananchi wa kitongoji hicho hawajapata umeme. Je, ni lini sasa Serikali itawapatia umeme wale wananchi walio katika kitongoji hicho ili na wao waweze kufaidika na huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Mbunge, katika hiki kitongoji ambacho kipo katika Kata ya Mapinga, Mheshimiwa Mbunge, tumepokea changamoto hiyo na tutaenda kufanya survey kuona ni namna gani tutaweza kufikisha umeme katika kitongoji hiki na wananchi hao waweze kupata umeme wa uhakika. (Makofi)
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, eneo hili lenye nyumba 52 mpaka sasa bado linajaa maji pale mvua zinaponyesha. Swali langu la kwanza; je, ni lini sasa Serikali itafanya maamuzi magumu ya kuwauzia hizi nyumba wananchi wanaoishi pale ili waweze kulipa malipo ya kidogo kidogo ili wazimiliki wao na waweze kuzikarabati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja kutembelea pale katika zile nyumba aone jinsi zilivyochakaa na kuthibitisha kwamba, hizo pesa ambazo ametenga, kwa ajili ukarabati hazitoshi kabisa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutembelea Bagamoyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni wajibu wetu na tukubaliane tu, baada ya kipindi hiki cha Bunge ni lini tuweze kwenda pamoja katika maeneo hayo ili twende tukaangale hali halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza alilouliza Mheshimiwa Mbunge kuhusu maji kujaa tumelipokea. Nawaagiza Mameneja wa Mkoa wa TBA, Mkoa wa Pwani pamoja na Mtendaji Mkuu waweze kuangalia changamoto ni nini kuhusu kujaa maeneo haya ya nyumba za Serikali kwa maana ya TBA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuuza hizo, nadhani tathmini itafanyika kuona kama Serikali kuna haja ya kuziuza ama kuendelea kuzibakiza. Kwa hiyo, namuagiza Mtendaji Mkuu aweze kwenda eneo hilo afanye tathmini na wao wataishauri Serikali kama kuna haja ya kuziuza ama ziendelee kuwa za umma, kwa ajili ya kusaidia watumishi wengine wa umma. Ahsante. (Makofi)