Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Michael Constantino Mwakamo (20 total)

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Makofia kupitia Mlandizi hadi Vikumbulu Kisarawe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Makofia – Mlandizi – Vikumbulu yenye urefu wa kilometa 135.97 ni barabara ya mkoa inayounganisha Wilaya za Bagamoyo, Kibaha na Kisarawe. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na uhakiki wa mali zitakazoathiriwa na mradi sehemu ya Makofia – Mlandizi – Maneromango yenye urefu wa kilometa 100 umekamilika. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii utaanza baada ya kupata fedha ambazo Serikali inaendelea kutafuta.

Mheshimiwa Spika, wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha, Wizara yangu inaendelea kuihudumia barabara hiyo ili iweze kupitika majira yote ya mwaka ambapo katika Mwaka huu wa Fedha wa 2020/21 jumla ya shilingi 1,524.000.07 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA - K.n.y. MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua migogoro ya mipaka ya kiutawala baina ya Mikoa, Wilaya na Vijiji hapa nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Constantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua migogoro ya mipaka ya kiutawala baina ya Mikoa, Wilaya na Vijiji hapa nchini Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kusambaza Matangazo ya Serikali kwa maana ya Government Notices au GN yanayoonesha mipaka ya Wilaya na Mikoa kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini; kKuunda vikundi kazi na kuvipeleka kwenye maeneo yenye migogoro ya mipaka ili kutatua migogoro; kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Matumizi Bora ya Ardhi nchini kwa kuhakikisha Vijiji, Kata na Wilaya zinaandaa na kutekeleza Mipango ya matumizi ya ardhi, kutoa elimu kwa umma kuhusu Sera na Sheria za ardhi, kusimamia upimaji wa viwanja na mashamba katika Halmashauri, kurasimisha makazi na kumilikisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kutatua migogoro ya mipaka ya kiutawala baina ya Mikoa, Wilaya na Vijiji hapa nchini.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia watumishi waliostaafu kupata mafao yao kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ulianzishwa rasmi tarehe 1/ 8/2018 kwa Sheria Namba 2 ya Mwaka 2018. Mfuko huu ni matokeo ya kuunganisha mifuko minne ya awali (LAPF, GEPF, PPF na PSPF) ambayo ilikuwa ikihudumia watumishi mbalimbali wa Umma na kuufanya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kubaki ukihudumia sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati, mipango na utekelezaji wa Serikali katika kuhakikisha watumishi waliostaafu wanapata mafao yao kwa wakati ni kama ifuatayo: -

(i) Kutengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA ili kuweza kuwatambua wanachama wake na kulipa mafao stahiki pale wanapodai mafao;

(ii) Kulipa malimbikizo mbalimbali ya mafao ya wanachama yaliyopaswa kulipwa na mifuko iliyounganishwa na yale yaliyopokelewa kipindi ambacho mchakato wa kuunganisha mifuko huo ulikuwa unaendelea; na

(iii) Kuandaa ofisi mbalimbali nchini kote na kuweka misingi bora itakayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wanachama wake ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha wastaafu wanalipwa kwa wakati, waajiri wanakumbushwa kufuata kikamilifu utaratibu ulioainishwa katika Sheria namba 2 ya Mwaka 2018 ambapo inaelekeza ipasavyo maandalizi ya taarifa za wastaafu kabla ya malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mifuko imeendelea kuboresha mifumo yake ambapo matarajio ni kuwa waajiri nao wafuate vizuri utaratibu ulioainishwa kisheria ili kupunguza ucheleweshaji wa kulipa mafao kwa wastaafu.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, ni Ranchi ngapi nchini zimeshawapokea wafugaji na kuwapatia nafasi ya kufuga kwenye Ranchi hizo kama Serikali ilivyotoa maelekezo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo Mbunge wa Kibaha Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imetekeleza maelekezo ya Serikali kwa kutenga jumla ya vitalu vya muda mrefu 116 katika Ranchi 11 za NARCO na kuzikodisha kwa wafugaji wadogo 116. Ranchi hizo ni Kikulula (Kagera) vitalu 2, Mabale (Kagera) vitalu 7, Kagoma (Kagera) vitalu 18, Kitengule (Kagera) vitalu 10, Missenyi (Kagera) vitalu 11, Mkata (Morogoro) vitalu 7, Dakawa (Morogoro) vitalu 2, Mzeri Hill (Tanga) vitalu 9, Usangu (Mbeya) vitalu 16, Kalambo (Rukwa) vitalu 13 na Uvinza (Kigoma) vitalu 21. Jumla ya eneo la vitalu hivi ni hekta 322,525.

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kutatua migogoro ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi nchini hasa baada ya wafugaji kuondolewa kwenye hifadhi za misitu na mapori ya akiba, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ilianzisha utaratibu wa kugawa vitalu vya muda mfupi ambapo jumla ya vitalu 128 vimekodishwa kwa wafugaji wadogo 128 kutoka katika Ranchi 10 za NARCO. Ahsante sana.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kutatua migogoro ya ardhi kati ya Wananchi na Wawekezaji wenye mashamba makubwa Kibaha Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendelo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 17 la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua jitihada za kutatua migogoro ya ardhi kati ya wananchi na wawekezaji katika maeneo mbalimbali hususan katika Jimbo la Kibaha Vijijini. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kufanya ukaguzi wa ardhi iliyomikishwa kwa wawekezaji ili kubaini iwapo masharti ya umiliki yanazingatiwa.

Pili, kuchukua hatua za ubatilisho kwa wawekezaji waliobainika kukiuka masharti ya uwezekezaji; na Tatu, kupanga upya ardhi iliyobatilishwa kwa kushirikiana na Mamlaka za Upangaji kulingana na mahitaji halisi ya sasa hususan hazina ya ardhi, huduma za kijamii na makazi. Aidha, Wizara inaendelea kutoa elimu kwa jamii na wawekezaji kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na miongozo ya sekta ya ardhi ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya mzunguko katika makutano ya Barabara ya Dar es Salaam, Morogoro na Bagamoyo kuelekea Mlandizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Constantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Makofia, Mlandisi hadi Mzenga kilomita 35, makutano ya barabara ya Dar es Salaam -Morogoro na Makofia- Mlandizi-Mzenga eneo la Mlandizi limesanifiwa kwa ajili ya kujenga barabara ya mzunguko yaani round about. Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuanza ujenzi wa barabara ya Makofia – Mlandizi hadi Mzenga utakaohusisha na ujenzi wa round about katika eneo la Mlandizi. Ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kudhibiti kuhama kwa Mto Ruvu-Kibaha ili kuzuia uharibifu wa mashamba na miundombinu ya Reli ya SGR?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo Mbunge wa Kibaha Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mto Ruvu eneo la Kibaha hadi Bagamoyo umekuwa na kawaida ya kuhamahama kwa vipindi tofauti tofauti kutokana na kuwa katika uwanda wa chini karibu na Bahari ya Hindi. Hali hii hupunguza kasi na kufanya udongo kutuwama ndani ya mto na kusababisha mto kuhama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea na kazi ya kunyoosha mto pamoja na kuimarisha kingo zilizoathiriwa kwa kuweka gabions na njia mbalimbali, ikiwemo upandaji wa miti pembezoni mwa mto na kwenye vyanzo vya maji, kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuhifadhi vyanzo vya maji, kuiwezesha jamii kutekeleza shughuli mbalimbali za kujipatia kipato ili kuondoka ndani ya vyanzo vya maji. Kuweka alama na mipaka na mabango ya makatazo ya kuzuia kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ya vyanzo vya maji ili kurudisha uoto wa asili na kupunguza athari za mmomonyoko. Jitihada hizi zitaepusha mashamba katika eneo hilo kuathiriwa na maji ya mto Ruvu.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuwawekea mazingira mazuri Wakulima wadogo wa kilimo cha Umwagiliaji katika Mto Ruvu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Constantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya kilimo kwa wakulima wadogo ndani ya Bonde la Mto Ruvu kwa kubaini maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa Skimu ya Kisere (Nyani), usanifu huu ukikamilika ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji utaanza katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kutoa mwongozo kwa wawekezaji kuchangia shughuli za maendeleo katika maeneo wanayowekeza?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wawekezaji wanachangia shughuli za maendeleo za jamii katika maeneo wanayowekeza, Serikali ina sheria za kisekta na miongozo inayosimamia wawekezaji katika sekta ya uziduaji ambayo ni mwongozo wa ushiriki wa Watanzania katika sekta ndogo ya mafuta 2019, mwongozo wa kuwasilisha mpango wa ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini wa mwaka 2018 na mwongozo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu uwajibikaji kwa jamii wa makampuni wa mwaka 2022. Aidha, Serikali iliandaa mwongozo wa Taifa wa ushiriki wa Watanzania katika sekta mbalimbali wa mwaka 2019 kwa ajili ya kusimamia masuala ya ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji. Utaratibu huo unaruhusu wawekezaji kuchangia sehemu ya mapato yake kwa jamii ikiwa ni sehemu ya uwajibikaji kwa jamii na kuchangia shughuli za maendeleo katika eneo la uwekezaji kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa. Nakushukuru.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, Serikali ina mipango gani ya kuliendeleza Bonde la Mto Ruvu kwa kushirikiana na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijiji kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Mpango wa Uhifadhi vidakio vya Maji wa mwaka 2021-2035 ambao unahusisha ushirikishwaji wa wadau mbalimbali ikiwemo wananchi. Kupitia mpango huo, jamii inaelimishwa kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji ambapo zimeundwa Jumuiya za Watumia Maji 11 na kupitia Jumuiya hizo, wananchi wanashiriki moja kwa moja kulinda na kutunza rasilimali za maji kwenye maeneo yao. Vilevile, kupitia mpango huo, Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu inaendelea kujenga miundombinu ya kunyweshea mifugo ili isiendelee kunywa maji kwenye vyanzo vya maji hasa mitoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kutafanyika uainishaji wa maeneo ya malisho na vivuko kwa ajili ya mifugo, na kuweka mipango ya pamoja ya matumizi bora ya ardhi hususani kwenye maeneo yanayohusisha vyanzo vya maji. Aidha, katika kuliendeleza Bonde la Wami Ruvu, kazi nyingine zinazotekelezwa kupitia mpango huo ni pamoja na kutambua maeneo ya uhifadhi wa vyanzo, kuyawekea mipaka na kuyatangaza kwenye Gazeti la Serikali kuwa maeneo tengefu ambapo hadi sasa maeneo 230 yametambuliwa, 13 yamewekewa mipaka na mawili yametangazwa kwenye Gazeti la Serikali.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, nini kauli ya Serikali juu ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanaozuiwa kufanya biashara na TFS?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Misitu Sura ya 323 na Kanuni zake za mwaka 2004 zimeelekeza utaratibu unaopaswa kufuatwa ili kuvuna, kusafirisha na kuuza mazao ya misitu kwa kuzingatia umiliki wa misitu au miti ambao ni ya watu binafsi, Serikali za vijiji, Serikali za mitaa au Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TFS haizuii kufanya biashara ya mazao ya misitu isipokuwa inasimamia sheria na kanuni ambazo zinahakikisha kunakuwa na usawa katika biashara hiyo pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu nchini. Natoa rai kwa wadau au wafanyabiashara wote wenye nia njema ya kuvuna au kufanya biashara ya mazao ya misitu wafuate sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kulinda misitu yetu ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa letu.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kuwaendeleza vijana wanaomaliza kidato cha nne na kupata daraja la nne au sifuri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetoa fursa kwa vijana wote hata wale waliomaliza darasa la saba kujiunga na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi na vyuo vya maendeleo ya wananchi vilivyo karibu na maeneo wanayoishi kwa lengo la kujiendeleza katika ujuzi na stadi mbalimbali za maisha. Vile vile vijana hao wanaweza kurudia mitihani yao kama watahiniwa wa kujitegemea iwapo wanahitaji kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu) inatekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi kwa kuwapatia vijana mafunzo ya uanagenzi na utambuzi wa ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, lini Serikali itawasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Wazee?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM, alijibu:-

Mheshmiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinisia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, napenda kulithibitishia Bunge lako tukufu kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wazee nchini. Sera ya Wazee ya mwaka 2003 iko katika hatua za mwisho za mapitio ili kujumuisha masuala mapya yanayojitokeza tangu kupitishwa kwa Sera hiyo iliyopo.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa mapitio ya Sera ya Wazee kutatoa fursa ya kutungwa Sheria ya Wazee na Serikali kuwakilisha Muswada huo wa Sheria ya Wazee Bungeni kwa hatua za sheria hiyo iliyotungwa, ahsante. (Makofi)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE K.n.y. MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya viwanja vilivyouzwa na Halmashauri ya Wilaya Kibaha eneo la Kisabi na baadae kuzuiwa kuviendeleza?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Kibaha ilisanifu na kutekeleza mradi wa upimaji viwanja katika Eneo la Kisabi mwaka, 2010. Jumla ya viwanja 262 vya matumizi mbalimbali ya ardhi vilipimwa na kusajiliwa kupitia ramani za upimaji namba E1359/378, E1359/379, E1359/382 na E1359/383. Viwanja hivyo viliuzwa na kugawiwa kwa waendelezaji mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021 Taasisi ya Taifa ya Kusimamia Mazingira (NEMC) ilisitisha uendelezaji wa viwanja hivyo kutokana na viwanja hivyo kupimwa kwenye Bonde la Mto Ruvu kwa kuwa uendelezaji wake ungeathiri bayoanuai katika eneo hilo. Kufuatia hali hiyo, Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira kupitia barua ya tarehe 18 Aprili, 2022 iliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kufanya Tathmini ya Mazingira ya Kimkakati ili kubaini athari za kimazingira zinazoweza kujitokeza kutokana na uendelezaji huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suluhisho la kudumu la suala hili litapatikana baada ya kufanyika kwa tathmini hiyo ambayo inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuepuka mzigo mkubwa wa ulipaji wa fidia wakati inapoongeza ukubwa wa barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007, iliongeza upana wa hifadhi ya barabara kutoka meta 45 hadi meta 60 kwa barabara kuu na za Mikoa ili kukidhi mahitaji ya uendeshaji wa miundombinu ya barabara kwa wakati huu na wakati wa baadaye, ili uendane na ongezeko la watu na ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupunguza ulipaji wa fidia Wizara, kupitia TANROADS, imefanya tathmini ya awali ya gharama inayohitajika kwa ajili ya kulipa fidia kwa mali zilizomo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara lililoongezeka la meta 7.5 kila upande na kuonesha kuwa, gharama kubwa za fidia ziko katika majiji na miji. Kutokana na hali hiyo, Serikali inaangalia uwezekano wa kuchepusha barabara kwenye maeneo hayo. Aidha, uchambuzi wa kina unafanyika, ili kubaini ni barabara zipi kweli zinahitaji upana wa eneo la hifadhi ya barabara wa meta 60 kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya hapo baadaye ya kuzipanua kulingana na ongezeko la wingi wa magari. Zoezi hili likikamilika taarifa kamili itatolewa, ahsante. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja ya kuanzisha vyuo vya mafunzo katika fani za kilimo, mifugo na ufundi ili kuwawezesha vijana kupata elimu ya ufundi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ili kutoa mafunzo kwa wananchi kwa lengo la kuwapatia ujuzi utakaowawezesha kutekeleza shughuli zao mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo pamoja na shughuli nyingine kulingana na fursa zinazopatikana katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutekeleza azma hiyo, Serikali kwa sasa inaendelea kutekeleza Mpango wa Kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 64, pamoja na Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe. Ujenzi wa vyuo hivi unaendelea kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo yatakayokuwa yanatolewa na vyuo hivi yamezingatia shughuli za kiuchumi katika maeneo husika ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, uchimbaji wa madini, utalii pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi, nakushukuru.
MHE. HAWA M. CHAKOMA K.n.y. MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kuwa na Ofisi ya NIDA na RITA katika kila halmashauri nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuwa na Ofisi za NIDA katika kila halmashauri nchini. Katika kutambua umuhimu huo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ina jumla ya majengo na Ofisi za Usajili 16 kati ya hizo 13 ni Ofisi za Usajili za Wilaya. Serikali katika kutambua uhitaji wa ofisi za usajili, katika mwaka wa fedha 2024/2025 NIDA imetenga jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo 35 yakiwemo ofisi 31 ya ofisi za usajili katika halmashauri nchini.

Mheshimiwa Spika, aidha Serikali ina mpango wa kuziunganisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ili kuwa na taasisi moja itakayoshughurika na matukio muhimu maishani. Zoezi hilo linatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Juni, 2024, nakushukuru.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, nini mpango wa Serikali kujenga madampo Kibaha Vijijini kwani kuna viwanda vingi na uzalishaji wa taka ni mkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kibaha Vijijini kwa sasa ina viwanda 145. Kati ya hivyo, viwanda vikubwa ni 29 na vya kati na vidogo ni 116. Uwepo wa viwanda hivyo umeongeza uzalishaji wa taka katika eneo la Kibaha Vijijini hususan eneo la Kwala ambalo linatarajiwa kujengwa viwanda zaidi ya 200.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na ongezeko la uzalishaji wa taka, Serikali imeanza kuchukuwa hatua za awali za ujenzi wa madampo kwa kutenga eneo la viwanja namba mbili na namba tatu katika kitalu G eneo la Kwala vyenye jumla ya meter za mraba 124,901 maalumu kwa ajili ya kukabiliana na taka ngumu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mpango jumuishi katika eneo la Kwala kuwa mji wa viwanda na uwekezaji, Serikali imebainisha maeneo mengine ya ujenzi wa madampo yenye ukubwa wa hekta 142.8 ili kukidhi taka ngumu kutokana na viwanda. Maeneo hayo ni pamoja na Mizuguni hekta 39.5; Pingo hekta 32.2; Mihugwe hekta 35.6; na Madege hekta 35.5. Wakati wa utekelezaji wa mpango kabambe huo, maeneo hayo yatatwaliwa kwa ajili ya kujengwa madampo, ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya kuunganisha Kongani ya Viwanda ya Kwala na Stesheni ya SGR ya Ruvu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini imepanga kufanya usanifu wa kina wa barabara hii katika mwaka 2024/2025 kwa lengo la kutambua gharama halisi za mradi huu na ujenzi wake utategemea na upatikanaji wa fedha.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaipatia vitendea kazi kama magari, majengo na shajara Wilaya ya Kipolisi ya Mlandizi, Jimbo la Kibaha Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa spika, Serikali inatambua uhaba wa majengo ya ofisi, vitendea kazi na nyumba za makazi ya askari katika Kituo cha Polisi cha Mlandizi. Tathmini kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za uchunguzi wa kisayansi, intelijensia na upelelezi imeshakamilika na fedha kiasi cha shilingi 82,000,000 zinahitajika. Pia, kiasi cha fedha shilingi 232,590,000 zinahitajika, kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa nyumba mbili za makazi ya askari za familia sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha zote hizo kiasi cha jumla ya shilingi 314,590,000 zimetengwa kwenye Bajeti ya Serikali ya Mwaka wa Fedha wa 2024/2025. Kwa sasa kituo cha Polisi Mlandizi kina gari moja na pikipiki mbili, pindi magari 122 yaliyoagizwa na Serikali, kwa ajili ya Wakuu wa Polisi wa Wilaya yatakapowasili, Kituo cha Polisi Mlandizi pia, kitapatiwa gari. Ahsante. (Makofi)