Primary Questions from Hon. Vincent Paul Mbogo (18 total)
MHE. VICENT P. MBOGO aliuliza:-
Jimbo la Nkasi Kusini lina Kata 11 na Kituo cha Afya kimoja pekee:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Vituo vya Afya hasa katika Tarafa ya Chala, Kate, Myula, Sintali na Ninde?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018 hadi mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imejenga na kukarabati Vituo vya Afya vya Nkomolo na Kirando kwa gharama ya shilingi milioni 900. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. Vilevile, Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma matatu ya zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kusogeza zaidi huduma za afya kwa wananchi, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi inakamilisha utaratibu wa kuingia makubaliano ya utoaji wa huduma za afya (service agreement) na Kituo cha Afya cha Mzimwa kinachomilikiwa na Taasisi ya Kikatoliki Abei kwa ajili ya wananchi kupata huduma za afya ikiwemo upasuaji wa dharura ambapo wananchi kutoka Tarafa za Myula na Sintali ni miongoni mwa watakaonufaika na mpango huo. Aidha, Halmashauri imetenga eneo katika Tarafa ya Chala kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya kupitia fedha za mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kujenga na kupanua vituo vya kutolea huduma za afya katika Jimbo la Nkasi na nchini kote kwa awamu kwa kuwa shughuli hizi ni endelevu.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro kati ya Hifadhi ya Lwafi iliyopo Nkasi Kusini na wananchi wa Vijiji vya Mlambo, King’ombe, Tundu na Kata ya Wampembe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba la Lwafi liliwahi kuwa na mgogoro wa Kijiji cha King’ombe ambapo baadhi ya wananchi wake walivamia eneo la hifadhi kwa ajili ya shughuli za kilimo. Hata hivyo, mgogoro huo ulitatuliwa na Serikali baada ya kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo wananchi kupewa elimu na kuonyeshwa mipaka halisi.
Mheshimiwa Spika, aidha, mgogoro huo ulikwisha, lakini kuna mgogoro mwingine kwa sasa ambao ni kati ya Msitu wa Hifadhi ya Loasi yaani Loasi River Forest Reserve na Vijiji vya Mlambo, King’ombe na Tundu, ambapo wananchi walivamia msitu huo kwa ajili ya makazi na shughuli za kilimo. Serikali imefanyia kazi mgogoro huo kupitia mapendekezo ya Kamati ya Mawaziri Nane ambapo maamuzi ya mgogoro huo yameshatolewa na utekelezaji wake utafanyika katika bajeti ya mwaka 2021/2022.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa rai kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wanaozunguka eneo hilo kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhimiza, kulinda na kutatua migogoro hiyo inayohatarisha uwepo wa maliasili zinazowazunguka.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa maji wa Mji Mdogo wa Chala ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni za mwaka 2020?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vicent Paul Mbogo Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji mdogo wa Chala unapata maji kutoka Mto Kauzike na Bwawa la Ntanganyika na hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Mji huo ni asilimia 56. Aidha, katika kuhakikisha huduma ya maji katika mji wa Chala inaboreshwa mwaka 2020/2021 ulitekelezwa mradi wa maji ambao umehusisha kuchimba kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 153,600 kwa siku na kiasi hiki kimeongeza upatikanaji wa maji zaidi ya lita 300,000 kwa siku. Hivyo kazi itakayofanyika kuanzia mwezi Julai, 2021 ni ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji, ujenzi wa nyumba ya mtambo wa maji, ufungaji wa pampu na ulazaji wa bomba mita 500 kwenda kwenye tanki lililopo la lita 150,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji wakati wote, hivyo mpango wa muda mrefu katika mji wa Chala ni kutumia mabwawa madogo na ya ukubwa wa kati ambapo kwa sasa utafiti wa kubainisha maeneo yanayofaa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa mawili (2) katika Mji Mdogo wa Chala unaendelea na unatarajiwa kukamilika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga masoko ya samaki katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika hususani Kata ya Kala Mpasa, Wampambe, Kizimbi na Naninde ili wavuvi wapate maeneo ya kuuzia samaki badala ya kulazimika kwenda kuuza nchi za jirani za Zambia, Congo na Burundi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga miundombinu ya uvuvi katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika. Miundombinu ya Mialo na Masoko ni muhimu katika kuhakikisha kuwa na mazao bora na salama, kupunguza upotevu wa mazao na kusaidia ukusanyaji wa taarifa na mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu huu, ujenzi wa masoko unahitaji rasilimali ikiwemo ardhi na fedha. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali ipo tayari kujenga Soko, katika Wilaya ya Nkasi kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kuandaa eneo katika Wilaya ya Nkasi, ili kuwezesha hatua za ujenzi wa soko kuanza pindi fedha itakapopatikana. Ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU K.n.y. MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka Boti ya kubebea Wagonjwa katika vijiji zaidi ya saba vilivyopo Mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika Jimbo la Nkasi Kusini ambavyo havina huduma ya Zahanati wala Kituo cha Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vicent Paul Mbogo, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti; Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetenga shilingi bilioni 35.1 kwa ajili ya ununuzi wa magari ya wagonjwa 195 ambayo yatapelekwa kwenye Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Nkasi Kusini. Aidha, Serikali imekwishapeleka fedha shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya King’ombe kwenye Kata ya Kala ambapo ujenzi unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Nkasi imetenga shilingi milioni 23 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya magari ya kubebea wagonjwa na Boti zinazotoa huduma ili kuboresha na kuimarisha huduma kwa wagonjwa. Ahsante.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa Mahakama ya Mwanzo Chala?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Tarafa ya Chala yenye Kata nne; za Chala, Nkadasi, Kipande na Mkwamba, ina Mahakama za mwanzo mbili za Chala na Kipande. Katika kuimarisha majengo ya Mahakama kwa kuzingatia mpango uliopo wa ujenzi na ukarabati wa Mahakama nchini, Mahakama ina mpango wa kukarabati jengo la Mahakama ya Mwanzo Chala katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha Polisi katika kata ya Kala Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetoa kiasi cha shilingi 115,809,000 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi Daraja C katika Kata ya Kala Tarafa ya Wampembe Wilaya ya Nkasi. Taratibu za ujenzi wa kituo tayari umeanza mwezi Machi, 2023. Kituo hiki kinajengwa eneo la Mpasa na kitahudumia vijiji vya Mpasa, Kala, Mlambo, Tundu, King’ombe na kilambo cha Mkolechi.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga malambo ya kunyweshea mifugo katika Kata ya Chala, Kate, Myula na Nkandasi Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto ya upungufu wa maji kwa ajili ya mifugo katika Kata za Chala, Kate, Myula na Nkandasi, Serikali katika mwaka wa fedha 2023/2024, imepanga kufanya tathmini ya miundombinu ya maji na usanifu utakaowezesha kujenga malambo au kuchimba visima virefu katika maeneo hayo. Matokeo ya tathmini hiyo yataiwezesha Serikali kujenga miundombinu hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuongezeka kwa changamoto ya uhaba wa maji kwa ajili ya mifugo, nazikumbusha Halmashauri za Wilaya nchini kutekeleza Waraka wa Rais Na.1 wa mwaka 2002 kuhusu kutenga asilimia 15 ya mapato yatokanayo na Sekta ya Mifugo ili kujenga na kukarabati miundombinu ya maji. Pia, nitoe wito kwa wafugaji na wadau wengine kuwekeza kwenye ujenzi wa malambo au kuchimbaji visima virefu.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka Mradi wa Maji katika Kijiji cha Nkundi – Nkasi Kusini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Nkundi kinapata huduma ya maji kupitia Mradi wa Maji wa Bwawa la Kawa uliojengwa mwaka 2016. Hata hivyo, huduma ya maji kwenye kijiji hicho ilisimama kutokana na changamoto za kiuendeshaji zilizosababishwa na gharama za kusukuma maji kulingana na uwezo wa wananchi. Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua ya kuunganisha Chombo cha Watumiaji Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) cha kijiji hicho na vijiji vingine viwili vya Kipande na Kantawa ili kumudu gharama za uendeshaji. Tayari maji yameanza kusukumwa na kazi inayoendelea sasa ni kukarabati mabomba kwenye maeneo yaliyopasuka. Baada ya kazi hiyo, wananchi 4,540 wa Kijiji cha Nkundi wataendelea kupata huduma ya maji.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga barabara ya Ninde, Masokolo hadi Lupata katika Kata ya Kuzumbi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ninde – Masokolo – Lupata yenye urefu wa kilometa 40 inahudumia vijiji vitatu ambavyo ni Ninde, Masokolo na Lupata. Barabara hii ipo mpakani mwa Tanzania na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo ni muhimu kwa shughuli za kufuatilia masuala ya kiusalama. Barabara hii haipo kwenye mtandao wa barabara za TARURA. Hivyo, barabara hiyo inahitaji kufunguliwa ili kuunganisha vijiji hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itafungua barabara hii kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuimarisha usafiri na usafirishaji.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Soko katika Mji Mdogo wa Chala Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ipo katika hatua za awali za kupata eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 12,140 kwenye eneo la gulio lililopo katikati ya Mashete na Namanyere na ambalo litatosheleza mahitaji ya ujenzi wa soko katika Mji Mdogo wa Chala.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri itakapokamilisha taratibu zote za kupata eneo hilo na kuandaa andiko na gharama za mradi huo itatenga fedha kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Masoko ya Kuuzia Samaki katika Kata za Ninde, Wampembe na Kala Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuboresha na kujenga miundombinu ya uvuvi katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika. Katika mwaka 2023/2024, Serikali inajenga masoko ya samaki saba na mialo mitatu ambapo Wilaya ya Nkasi imepangiwa kujengewa mwalo wa Karungu. Aidha, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeingia Mkataba na Mkarandarasi Nice Construction and General Supplies Ltd. wenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kujenga mwalo wa Karungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalo huo wa Karungu utakaojengwa utakuwa na miundombinu ya soko ikiwemo chumba cha ubaridi, mtambo wa kuzalisha barafu na sehemu ya kuuzia samaki. Aidha, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Nkasi kutumia miundombinu hiyo kwa pindi itakapokamilika wakati Serikali inatafuta fedha za kujenga masoko ya samaki katika kata zingine zilizosalia. Vilevile, Serikali itaendelea kujenga miundombinu ya uvuvi katika maeneo mbalimbali nchini kuendana na upatikanaji wa fedha na mahitaji ya maeneo husika.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka mradi wa maji katika Kata za Kizumbi na Wampembe – Nkasi Kusini ?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri ya Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023, imekamilisha usanifu wa Mradi wa Maji Wampembe utakaohudumia Kata mbili za Kizumbi na Wampembe. Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Januari, 2024 na kukamilika mwezi Desemba, 2024 ambapo utanufaisha wananchi wapatao 15,089 waishio kwenye vijiji sita vya Wampembe, Mwinzana, Kizumbi, Lyapinda, Ng’anga na Katenge.
Mheshimwa Mwenyekiti, mradi huo unatarajiwa kutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la USAID kupitia Mradi wa Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira (MUM), ambapo baadhi ya miundombinu inayotarajiwa kujengwa ni pamoja na matenki Manne (4) ya kuhifadhia maji yenye jumla ya lita 405,000, ujenzi wa vituo 39 vya kutolea huduma kwa wananchi sambamba na mtandao wa bomba kuu na mabomba ya usambazaji umbali wa Kilometa 41.
MHE. BENAYA L. KAPINGA K.n.y MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itazigawa Kata za Chala, Kala na Ninde Nkasi kwa kuwa ni kubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishwaji wa maeneo mapya ya utawala huzingatia Sheria ya Serikali za Mitaa, Mamlaka za Wilaya, Sura ya 287 na Mamlaka za Miji, Sura ya 288, pamoja na Mwongozo wa Uanzishwaji wa Maeneo ya Utawala wa Mwaka 2014.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uhitaji wa kugawa baadhi ya maeneo mapya ya utawala, lakini kwa sasa Serikali imetoa kipaumbele katika kuboresha na kukamilisha miundombinu kwenye maeneo ya kiutawala yaliyopo ili yaweze kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na baadaye kuendelea na maeneo mengine kwa kufuata taratibu na vigezo vilivyoainishwa. Ahsante.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga Mahakama mpya katika Kata za Chala na Kate Jimbo la Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania inaendelea kuboresha miundombinu ya majengo ya Mahakama hususan kwa ngazi ya Mahakama za Mwanzo ambako ndiko kwenye changamoto kubwa ya uhaba na uchakavu wa majengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kata za Kate na Chala wanapata huduma za Mahakama ndani ya kata zao katika Mahakama ya Kate na Chala japo majengo ya Mahakama hizi ni chakavu. Kulingana na mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama, katika mwaka wa fedha 2023/2024 tunajenga Mahakama ya Mwanzo Namanyere na katika mwaka wa fedha 2024/2025 tutajenga Mahakama ya Mwanzo Kate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha Mahakama ni kujenga majengo ya Mahakama za Mwanzo katika maeneo ambayo hakuna kabisa huduma za Mahakama ili kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kimahakama. Ahsante sana.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itasawazisha vilima vilivyopo kwenye Barabara ya Ninde, Kala na Wampembe ambavyo vimekuwa vyanzo vya ajali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, vilima vilivyopo katika barabara ya Namanyere – Kakoma – Ninde vimeanza kufanyiwa kazi kwa kupunguza miinuko mikali na kuweka tabaka la zege lenye urefu wa meta 150 kwa gharama ya shilingi milioni 84.75 katika mwaka 2022/2023. Aidha, katika mwaka 2023/2024 Serikali imetenga shilingi milioni 550 kwa ajili ya kupunguza vilima na kujenga tabaka la zege lenye urefu wa meta 700 katika Barabara ya Kitosi - Wampembe ili kuondoa maeneo yote korofi ambapo mkandarasi ameanza kazi.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2024/2025 shilingi milioni 475 imetengwa kupitia Mfuko wa Jimbo kwa lengo la kuvisawazisha vilima vilivyopo katika Barabara ya Nkana – Kala. Aidha, Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 180 katika bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa ajili ya kupunguza miinuko mikali iliyobaki kwa kujenga tabaka la zege lenye urefu wa meta 200 hivyo kumaliza kabisa tatizo lililopo kwenye vilima vya Barabara ya Namanyere – Kakoma – Ninde.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE K.n.y. MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -
Je, lini Serikali itaenda kutatua migogoro ya ardhi ya Kata ya Kala, Ninde na Wampembe - Nkasi Kusini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Nkasi Kusini ni moja ya majimbo yaliyonufaika na Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki za Ardhi nchini (Land Tenure Improvement Project - LTIP) unaotekelezwa na Wizara kupitia mkopo wa Benki ya Dunia, ambapo Kata ya Kala ni moja kati ya Kata nufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Kala awali ilikuwa na mgogoro na hifadhi ya msitu wa Loasi kutokana na vijiji vya Kilambo, Mlambo, King’ombe na Mpasa vilivyokuwa katika Kata hiyo kuanzishwa ndani ya Hifadhi. Migogoro ya vijiji hivyo ilitatuliwa kufuatia utekelezaji wa Uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro katika vijiji 975 ambapo vijiji husika vilimepewa ardhi yenye ukubwa wa jumla ya hekta 10,828 kutoka Hifadhi ya Msitu wa Loasi. Aidha, utekelezaji wa uamuzi wa Baraza la Mawaziri ulihusisha uundaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutatua migogoro yote iliyobaki katika Jimbo la Nkasi Kusini ili kuhakikisha kuwa wananchi wanafanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii kwa amani. Aidha, wananchi wanaombwa kuendelea kusimamia kikamilifu mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji iliyoandaliwa ili kuwa na matumizi endelevu ya ardhi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vizazi vijavyo.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaweka wavu maeneo ambayo wananchi wanapoteza maisha kwa kuliwa na Mamba wanapofuata maji katika Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na matukio ya mamba kujeruhi na kusababisha vifo vya watu hususan kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa maeneo yenye maziwa, mito na mabwawa. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau imeandaa na inaendelea kutekeleza mkakati wa Taifa wa kusimamia migongano baina ya binadamu na wanyamapori. moja ya malengo ya kimkakati ni kuwajengea uwezo wananchi kwa kuwapatia mafunzo ya mbinu za kujilinda na kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu ikiwemo mamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza mkakati huo, Serikali imekwishajenga vizimba vya mfano kwa ajili ya kuzuia mamba katika baadhi ya maeneo hapa nchini. Aidha, Serikali imeandaa mpango wa kuendeleza ujenzi wa vizimba vya mfano vya kuzuia mamba katika maeneo mengine nchini yenye changamoto hiyo yakiwemo maeneo ya Ziwa Tanganyika kadri ya upatikanaji wa fedha.