Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Vita Rashid Kawawa (18 total)

MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza:-

Kumekuwa na ongezeko la wanyamapori katika Hifadhi ya Mbuga ya Selous na sasa tembo na nyati wanavamia mashamba pamoja na makazi ya wanavijiji na kuleta taharuki:-

Je, Serikali inaweza kuwarudisha wanyama hao porini mbali zaidi na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mali asili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa na inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya binadamu na wanyamapori.

Aidha, Wizara inaendelea kukamilisha utaratibu wa kuweka alama katika shoroba na mapito ya wanyamapori ili kuimarisha uhifadhi wake na kuendelea kufanya utafiti na kueneza matumizi ya mbinu mbadala za kujikinga na wanyamapori waharibifu hasa tembo. Baadhi ya mbinu hizo ni: Matumizi ya pilipili, mafuta machafu (oil) na mizinga ya nyuki; na kutoa mafunzo kwa askari wa wanyamapori wa vijiji. Katika Wilaya ya Namtumbo, jumla ya askari wa wanyamapori wa vijiji 198 wamepewa mafunzo.

Mheshimiwa Spika, Wizara imekuwa ikiendelea kufanya doria za msako kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ambapo katika kipindi cha Julai hadi Disemba, 2020 zilifanyika doria za msako zenye jumla ya sikuwatu 133 katika vijiji vya Wilaya ya Namtumbo; kutoa elimu kwa wananchi juu ya mbinu za kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu ambapo jumla ya wananchi 2,303 walipata elimu katika vijiji 42 vya Wilaya za Namtumbo na Tunduru; kuimarisha vituo maalum vya doria za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika Kanda za Kalulu na Likuyu- Sekamaganga.
MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza umeme wa REA kwenye baadhi ya vitongoji vya vijiji vya Namtumbo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kupeleka umeme katika vijiji na vitongoji nchini. Vijiji vyote 14 vilivyobaki katika Wilaya ya Namtumnbo vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaotarajiwa kuanza mwezi Februari, 2021 na kukamilika mwezi Septemba, 2022. Mradi huu utahusisha pia kupelekea umeme vitongoji vya vijiji vitakavyopelekewa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa vitongoji vyote nchini vikiwemo vya Wilaya ya Namtumbo vitaendelea kupelekewa umeme kupitia miradi ya umeme vijijini kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. VITA R. KAWAWA Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukifufua Kituo cha Utafiti na Uzalishaji Mbegu cha SKU – Suluti cha Shirika la Kilimo Uyole kilichopo Wilayani Namtumbo ambacho kwa sasa hakifanyi kazi na majengo yake yameharibika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Suluti chenye jumla ya hekta 378 ni miongoni mwa vituo vidogo vilivyo chini ya Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI – Uyole) vinavyofanya utafiti na uzalishaji wa mbegu kwa kufuata ikolojia. Kwa muda mrefu kituo hiki kimekuwa kikizalisha chini ya uwezo na hivyo kusababisha maeneo ya mashamba kutotumika kikamilifu na miundombinu mingine ikiwemo nyumba, maghala na baadhi ya mashine kuharibika kwa uchakavu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ikolojia ya Suluti, TARI, Serikali katika Mwaka wa Fedha wa 2021/2022 ina mpango wa kumaliza mgogoro wa ardhi katika eneo la hekta 100 zilizovamiwa, kupeleka kiasi cha fedha shilingi milioni 200 kwa ajili ya kulima mbegu za alizeti, mahindi na soya. Kati ya hizo, milioni 70 zitatumika katika kilimo cha alizeti, milioni 100 zitatumika katika kilimo cha mahindi na milioni 30 zitatumika kwa kilimo cha soya.

Mheshimiwa Spika, vilevile Wizara ina mpango wa kukarabati majengo na kuongeza watumishi kutoka watumishi wawili kwenye kituo hicho na kufikia watumishi wanne. Mpango wa Wizara katika msimu wa Fedha 2021/ 2022 ni kuiwezesha TARI kuongeza uzalishaji wa mbegu mama za mahindi na soya. Vilevile TARI inatarajia kulima hekta 200 za alizeti ambapo mbegu hizo zitawafikia wakulima ili kuzalisha alizeti na kupunguza uhaba wa mafuta ya kula nchini.
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:-

Jimbo la Namtumbo lina tatizo la maji karibu maeneo yote ya Vijijini pamoja na Makao Makuu ya Wilaya: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo hili katika bajeti ya mwaka 2020/2021?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa Mbunge wa Namtumbo kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya Maji vijijini Wilayani Namtumbo ni asilimia 69. Katika kutatua tatizo la maji Jimbo la Namtumbo, Serikali Katika mwaka wa fedha 2020/2021 kupitia RUWASA imekamilisha miradi miwili, ambayo ni mradi wa maji Mkongogulioni - Nahimba na mradi wa maji Mtakuja. Miradi hiyo itahudumia jumla ya wananchi 9,683 katika vijiji vya Mkongogulioni, Nahimba na Mtakuja. Utekelezaji wa miradi ya maji ya Likuyusekamaganga, Njoomlole, Ligunga, Lusewa na Kanjele unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2021 na miradi ya Litola – Kumbura, Luhimbalilo – Naikesi, inatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mji wa Namtumbo Serikali inaendelea na mipango ya muda mfupi na muda mrefu. Kwa muda mfupi utekelezaji wa mradi wa uboreshaji, ambapo bomba kuu na mabomba kwa ajili ya usambazaji yamelazwa umbali wa kilometa 31.92 na umegharimu Shilingi milioni 653.2. Pia, kazi ya kuunga wateja 1500 katika urefu wa bomba kilometa 24 inaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mpango wa muda mrefu, Serikali imepanga kutekeleza mradi mkubwa kwa ajili ya maji kutoka vyanzo vya maji vya Likiwigi na Libula vyenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya Lita Milioni Nne kwa siku. Usanifu wa mradi umekamilika na ujenzi unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2021/2022.
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwarudishia wamiliki halali silaha zao ambazo zilichukuliwa na Serikali wakati wa zoezi la Operesheni Tokomeza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Jimbo la Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo mwaka 2013, Serikali baada ya kuona matukio ya ujangili na uwindaji haramu umeongezeka hapa nchini, hasa kwenye hifadhi za Taifa na mapori tengefu, iliendesha Operesheni Tokomeza na lengo lake lilikuwa kuwasaka na kuwakamata majangili pamoja na silaha walizokuwa wakizitumia. Operesheni hiyo ilishirikisha TAWA pamoja na vikosi vya ulinzi na usalama na jumla ya silaha 1,579 zilikamatwa na mpaka sasa zinashikiliwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 7 Januari, 2017 Serikali kupitia Wizara za Kisekta ambazo ni Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Katiba na Sheria, walikubaliana kwa pamoja silaha hizo zisirudishwe kwa wamiliki mpaka itakapofanyika tathmini ya hitaji la kuwarejeshea wamiliki wa silaha hizo. Nakushukuru.
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, Serikali inachukua hatua gani kudhibiti kuongezeka kwa bei ya mbolea nchini hasa Mkoani Ruvuma?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei za mbolea duniani imekuwa ikiongezeka kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji na mahitaji hususan kwenye nchi zenye watumiaji wakubwa wa mbolea kama vile China na India. Ongezeko hilo kwa msimu wa 2021/2022 limechangiwa na athari za UVIKO- 19 na vita kati ya Nchi ya Urusi na Ukraine ambao ni wazalishaji wa malighafi zinazotumika katika utengenezaji wa mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka utaratibu wa kudhibiti upandishaji holela wa bei za mbolea kwa kuhusisha Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini, inafanya tathmini ya gharama halisi ya mbolea na kutoa bei elekezi. Mwezi Machi, 2022 Serikali kupitia TFRA imetoa bei elekezi za mbolea za DAP, UREA, CAN na SA katika Mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuondokana na utegemezi wa uagizaji wa mbolea nje ya nchi, Serikali inaendelela kuvutia uwekazaji wa viwanda vya mbolea hapa nchini. Baadhi ya wawekezaji waliojitokeza ni pamoja na kampuni Itracom inayojenga kiwanda cha mbolea Jijini Dodoma chenye uwezo wa kuzalisha tani 600,000 na Kiwanda cha Minjingu kuendelea na kuongeza uzalishaji kutoka uwezo wa tani 100,000 za sasa hadi kufikia tani 500,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako Tukufu Serikali inasisitiza viongozi wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa bei elekezi zinazotolewa zinazingatiwa katika vituo vyote vya mauzo ya mbolea. (Makofi)
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatoa Shilingi Milioni 100 kumalizia Kituo cha Afya Mchomoro zilizoahidiwa na Rais wa Awamu ya Tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa Mbunge wa Jimbo la Namtumbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Mchomoro kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo kimejengwa kwa nguvu za Wananchi, fedha za Halmashauri, Mfuko wa Jimbo, pamoja na wadau. Ujenzi wake ulianza mwaka 2019 na kiasi cha Shilingi Milioni 52.5 zimetumika, kujenga jengo la wagonjwa wa nje ambalo limekamilika na linatoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kituo hiki hakina miundombinu muhimu ya kukiwezesha kutoa huduma za ngazi ya kituo cha afya, Serikali katika mwaka wa fedha 2023/2024, itatenga Shilingi Milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo. Ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, mpango wa ujenzi wa reli ya Kusini kutoka Mtwara hadi Ruvuma na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa njia ya reli ya Mtwara-Mbambabay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma kilomita 1,000. Upembuzi uliofanyika ulipendekeza kuwa utekelezaji wa mradi huo ushirikishe sekta binafsi. Kwa sasa Serikali inaendelea na taratibu za kumwajiri Mshauri Elekezi (Transaction Advisor) kwa ajili ya kuandaa Andiko, makabrasha ya zabuni ili kumpata mwekezaji kwa utaratibu wa ubia baina ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).

Mheshimiwa Spika, aidha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika -SADC imeahidi kutoa kiasi cha Dola za Marekani 6,000,000 kwa lengo la kumgharamia Mshauri Elekezi. Utaratibu wa kupata fedha hizi unaendelea na kazi hii inatarajiwa kufanyika Mwaka wa Fedha 2022/2023, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, ni kwa nini skimu za umwagiliaji za Liyuni na Limamu – Namtumbo hazijakamiliki ingawa Serikali imetumia fedha nyingi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu ya umwagiliaji ya Mtakuja iliyopo katika Kata ya Limamu yenye ukubwa wa eneo la hekta 350 na Liyuni iliyopo katika Kata ya Mchomoro yenye ukubwa wa hekta 140 ni miongoni mwa skimu zilizopo katika Wilaya ya Namtumbo. Katika mwaka 2006/2007 hadi 2012/2013, Serikali iliwekeza kiasi cha shilingi bilioni 1.260 kwa ajili ya ujenzi wa mfereji mkuu mita 3,950, vivuko viwili, daraja moja, kalvati na barabara yenye urefu wa kilomita 25 katika mradi wa Liyuni na ujenzi wa banio, mfereji mkuu mita 3,000 vivuko katika skimu ya Mtakuja kupitia fedha za DADPs, DIDF na MIVARF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa usanifu wa skimu hizi ulifanyika muda mrefu, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mwaka wa fedha 2023/2024 imepanga kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kubaini gharama halisi za kukamilisha miundombinu ya umwagiliaji na kuhakikisha skimu hiyo inakamiliaka na kuleta tija ya kilimo cha umwagiliaji katika kata za Limamu na Mchomoro.
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:-

Je, kwa nini viongozi wastaafu wa vitongoji na vijiji wenye sifa siyo wanufaika wa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa uratibu wa awamu ya kwanza ya mpango wa kunusuru walengwa wa kaya maskini ulipoanza, taratibu zilibainisha kuondoa baadhi ya makundi wakiwemo watumishi wastaafu wanaopokea pensheni, watu walioajiriwa na kuwa na kipato cha uhakika, Viongozi wa Vijiji na Wajumbe wa Kamati za Usimamizi za Jamii miongoni mwao ni Viongozi wa CCM katika ngazi za Kata na vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia maboresho ya taratibu za utambuzi na uandikishaji wa walengwa ya mwaka 2021, Kaya za Viongozi wa kisiasa wakiwemo Mabalozi wa Nyumba Kumi na Viongozi waliopo na wastaafu wa vijiji na vitongoji zinazokidhi vigezo zilipewa fursa ya kutambuliwa na kuandikishwa kwenye mpango huo wakati wa zoezi la utambuzi na uandikishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa viongozi wastaafu wa vijiji na vitongoji ambao kipindi cha zoezi la utambuzi wa walengwa linafanyika walikubalika na jamii kuorodheshwa awali kuwa katika kaya maskini wajiandishe ili nao waweze kuingia katika mpango huo.
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:-

Je, mpango wa ujenzi wa Reli ya Kusini umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Standard Gauge ya Mtwara - Mbamba Bay na matawi yake ya kuelekea Liganga na Mchuchuma. Aidha, taarifa hiyo ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali, ilionyesha kuwa mradi huu unaweza pia kutekelezwa kwa uratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership - PPP).

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kumwajiri Mshauri wa Kifedha (Transaction Adviser) ili aweze kufanya mapitio ya Upembuzi uliokamilika mwaka 2016 kwa lengo la kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mwekezaji kwa utaratibu wa ubia (PPP – Public Private Partnership), ahsante.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa barabara ya Mtwara Pachani – Nalasi hadi Tunduru utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara ya Mtwara Pachani – Nalasi hadi Tunduru yenye urefu wa kilometa 300. Katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali imepanga kuendelea na ujenzi wa kilometa mbili katika Mji wa Tunduru. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa sehemu iliyobaki, ahsante.
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka Walimu kukidhi mahitaji katika Shule za Sekondari na Msingi Wilayani Namtumbo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Jimbo la Namtumbo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiajiri walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kwa awamu kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 na 2021/2022, Serikali iliajiri walimu 22,930 ambapo walimu 111 walipangiwa katika shule zilizopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kupeleka walimu kwenye Shule za Msingi na Sekondari zikiwemo zilizopo katika Wilaya ya Namtumbo kulingana na uhitaji lakini pia kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.

MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa majengo ya Chuo cha VETA Namtumbo yakiwemo mabweni, bwalo la chakula pamoja na Lecture Hall?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitenga na kupeleka shilingi milioni 600 katika Chuo cha VETA cha Namtumbo ikiwa ni bajeti ya awali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mabweni mawili moja la wanafunzi wa kiume na moja la wanafunzi wa kike, bwalo la chakula na jiko pamoja na nyumba za watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo unatekelezwa kwa awamu ambapo kwa awamu ya kwanza ujenzi wa mabweni mawili umefikia hatua ya kuezeka na unatarajiwa kukamilika mwaka huu wa fedha 2023/2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali itatenga bajeti kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu iliyosalia ambayo inajumuisha ujenzi wa nyumba za watumishi, jiko pamoja na bwalo la chakula ambalo litatumika kwa matumizi mbalimbali ikiwamo shughuli za mihadhara, nakushukuru.
MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, mpango wa ujenzi wa reli ya Kusini umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TRC imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa reli ya Standard Gauge kutoka Mtwara – Mbamba Bay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma yenye jumla ya kilometa 1,000. Aidha, mradi huu ni mmoja wa mradi unaopendekezwa kupatiwa ufadhili wa fedha za maandalizi ya mradi kupitia Mfuko wa Miradi wa Nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC-PPDFA) ambapo kwa sasa timu kutoka Benki ya Afrika Kusini (DBSA) ilikuja Tanzania kwa ajili ya kufanya uthibitisho wa nyaraka (due diligence) za mradi ili kuendelea na hatua zingine za upatikanaji wa ufadhili wa fedha zitakazotumika kumnunua mshauri elekezi atakayekuwa na jukumu la kupitia andiko, kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kumpata mwekezaji kwa utaratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na binafsi.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, ni kwa nini wanufaika wa TASAF wanalazimika kufuata fedha benki hata fedha hiyo ikiwa ni kidogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa malipo kwa wanufaika wa TASAF unafanyika kwa njia kuu tatu: kwanza, kupitia akaunti ya Benki; pili, kupitia akaunti ya simu ya mkononi; na tatu, kwa malipo taslimu kupitia kwa wakala au katika kituo cha malipo. Uamuzi wa njia gani ambayo mlengwa atapenda kulipwa, unabaki kuwa wa kwake mwenyewe mlengwa ambaye anatambulika wakati wa uandikishaji wa daftari la walengwa.
MHE. MWITA M. WAITARA K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa nyumba za walimu wa Sekondari nchini na kukarabati zilizochakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya upungufu wa nyumba za walimu wa Shule za msingi na Sekondari nchini ambapo inatakiwa kutatuliwa. Katika mwaka 2022/2023 na 2023/2024, Serikali kupitia fedha za programu za kuimarisha elimu ya awali na msingi (BOOST) na sekondari (SEQUIP) pamoja na fedha za Serikali Kuu, imejenga nyumba 860 za walimu wa shule za msingi na sekondari zitakazochukua familia 2,018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2024/2025, Serikali itajenga jumla ya nyumba za walimu 562 zitakazochukua familia 1,124. Serikali itaendelea kutenga fedha kupitia programu za miradi mbalimbali na Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu ili walimu wetu wapate mahali bora pa kuishi.
MHE. YAHYA A. MHATA K.n.y. MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -

Je, mpango wa ujenzi wa reli ya Kusini umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TRC imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa reli ya Standard Gauge kutoka Mtwara – Mbamba Bay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma yenye jumla ya kilometa 1,000. Aidha, mradi huu ni mmoja wa mradi unaopendekezwa kupatiwa ufadhili wa fedha za maandalizi ya mradi kupitia Mfuko wa Miradi wa Nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC-PPDFA) ambapo kwa sasa timu kutoka Benki ya Afrika Kusini (DBSA) ilikuja Tanzania kwa ajili ya kufanya uthibitisho wa nyaraka (due diligence) za mradi ili kuendelea na hatua zingine za upatikanaji wa ufadhili wa fedha zitakazotumika kumnunua mshauri elekezi atakayekuwa na jukumu la kupitia andiko, kuandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kumpata mwekezaji kwa utaratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na binafsi.