Primary Questions from Hon. Hassan Zidadu Kungu (16 total)
MHE. DAIMU I. MPAKATE K.n.y. MHE. HASSAN Z. KUNGU Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Umeme Wilayani Tunduru chenye uwezo wa kupokea 132 KV ambazo ni uhitaji halisi kwa Wilaya ya Tunduru, Nanyumbu na Masasi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO) inaendelea na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Songea hadi Masasi kupitia Namtumbo, Tunduru na Nanyumbu umbali wa kilometa 395.
Mheshimiwa Naibu Spika, (TANESCO) pia inaendelea na taratibu za ujenzi wa Vituo vya kupoza umeme vya msongo wa kilovoti 132 kwenda 33 vya Namtumbo na Tunduru Mkoa wa Ruvuma, pamoja na vituo vya Nanyumbu na Masasi Mkoa wa Mtwara. Ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza ifikapo Desemba, 2022 na kukamilika mwezi Desemba, 2023 na gharama ya mradi inakadiriwa kuwa shilingi bilioni 132.7.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya kuwapatia maji wananchi wa Kijiji cha Fundimbanga, Kata ya Matemanga katika Jimbo la Tunduru Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Tunduru ni wastani wa asilimia 69. Katika kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Tunduru, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 inaendelea kuboresha huduma ya maji safi na salama kwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Mradi wa Maji Muhuwesi, Semeni, Ndaje- Mbesa kwa awamu ya pili na ukarabati wa Mradi wa Maji Njenga na Misyaje, ukarabati wa Mradi wa Maji Nalasi na Namwinyu, ujenzi wa Mradi wa Maji Masuguru, upanuzi wa Mradi wa Maji Majimaji, Chalinze, Ligoma, Makoteni na Imani, Kazamoyo na Daraja Mbili.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Matemanga ina jumla ya vijiji vinne, ambavyo ni Milonde, Changarawe, Fundimbanga na Matemanga. Katika vijiji vitatu vinapata huduma ya majisafi na salama kupitia mradi mkubwa wa maji wa Matemanga. Vilevile Kijiji cha Fundimbanga kinapata huduma ya maji kupitia visima virefu viwili vya pampu za mkono, ambavyo havitoshelezi mahitaji kwa wananchi wa kijiji hicho.
Katika kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji kwenye Kijiji cha Fundimbanga, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 imekamilisha utafiti wa maji chini ya ardhi na uchimbaji wa kisima utafanyika mwezi Aprili, 2022. Ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji utafanyika katika mwaka wa fedha 2022/2023.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalinda watumiaji wa cyanide kama mbadala wa zebaki?
WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatumia njia mbalimbali kuwalinda watumiaji wa cyanide kuzuia athari za kiafya zisitokee wakati wa kutumia kemikali hizi ikiwa ni pamoja na: -
(a) Kuelimisha wachimbaji juu ya madhara yanayotokana na matumizi ya cyanide na namna ya kujikinga na madhara yake. Pia kuwaelimisha kufika vituo vya kutolea huduma za afya mapema kupata matibabu wanapopata madhara.
(b) Kufanya upimaji wa afya za wafanyakazi maeneo ya migodini.
(c) Kutumia njia nyingine katika uzalishaji wa dhahabu katika migodi iliyopo hapa nchini kama direct smelting na njia nyingine mbadala.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Wilayani Tunduru?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo, kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe.
Mheshimiwa Spika, Tunduru ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa vyuo vya ufundi stadi katika mwaka huu wa fedha. Nakushukuru sana.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafungua tawi la Chuo Kikuu cha Sokoine Wilayani Tunduru kwani majengo yamekamilika kwa asilimia 65?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, kilikabidhiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru majengo na ardhi kwenye eneo lililokuwa Kambi ya Mkandarasi wa ujenzi wa barabara katika Kijiji cha Darajambili tarehe 17 Agosti, 2018.
Mheshimiwa Spika, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kilianza kutumia majengo ya kampasi ya Tunduru kama kituo cha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosoma Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Usimamizi wa Wanyamapori na Wanafunzi wa Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Misitu mwaka, 2018/2019.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na mpango wa kufanya ukarabati wa miundombinu na kuanzisha shughuli mbalimbali za kitaaluma, utafiti na ushauri wa kitaalam kwa lengo la kuiwezesha kampasi hiyo kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.(Makofi)
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -
Je, ni lini Mradi wa REA II utakamilika katika Vijiji 23 vilivyobaki vya Jimbo la Tunduru Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Pili ulitekelezwa na Mkandarasi LTL ambapo jumla ya vijiji 36 vya Wilaya ya Tunduru vilipatiwa umeme na mradi ulikamilika Mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika Jimbo la Tunduru Kaskazini ambapo unatekelezwa na Mkandarasi M/S JV Guangdong Jianneng Electric Power Engineering Co. Ltd. and White City International Contractors Ltd. unalenga kupeleka umeme katika vijiji 23.
Mheshimiwa Spika, Mkandarasi yupo katika maeneo mbalimbali ya mradi akiendelea na kazi za ujenzi wa miundombinu na kuunganisha wateja. Mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2023.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafunga taa za barabarani eneo la Tunduru Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Tunduru ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 1,200. Kati ya hizo, barabara za tabaka la lami ni kilometa 4.5, barabara zenye tabaka la changarawe ni kilometa 285 na barabara za tabaka la udongo ni kilometa 914.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia TARURA ilifunga taa za barabarani 16 kwa gharama ya shilingi milioni 72 katika barabara ya Bus Stand –Sinabei Guest House, TUDECO – Tunduru Sekondari – Borrow Pit, NMB – Ushirika na Nguzo Sita – Muungano – Camp David. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya taa 20 za barabarani zitafungwa kwa gharama ya shilingi milioni 90 katika barabara ya Isalmic Centre – Amazon – Mkunguni na Bus Stand – Mseto – Mkunguni baada ya kukamilishwa kwa ujenzi wa barabara. Mwaka wa fedha 2023/2024 TARURA imetenga shilingi milioni 270 kwa ajili ya kufunga taa 60.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini itaendelea kuhudumia miundombinu ya barabara ya Mji wa Tunduru kwa kuweka katika mipango yake ujenzi na matengenezo ya barabara ikiwemo ufungaji wa taa za barabarani kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga angalau kilometa tano kwa kiwango cha lami Barabara ya Tunduru - Mtwara Pachani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Mtwara Pachani – Lusewa – Lingusenguse – Nalasi hadi Tunduru yenye urefu wa kilometa 300 kwa awamu ambapo jumla ya kilometa 3.23 zimejengwa kwa lami nyepesi katika maeneo ya miji midogo ya Mkongo, Ligela, Lusewa na Sasawala. Aidha, mwezi Machi, 2023 Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imesaini mkataba kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa kipande cha mita 500 katika eneo la Tunduru Mjini. Vile vile, Serikali imekamilisha kazi ya Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii.
Mheshimiwa Spika, baada ya Usanifu kukamilika Serikali inaendelea kutafuta fedha za kuendelea na ujenzi, ahsante.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza:-
Je, lini Serikali itatoa fedha za ujenzi wa Kituo cha mabasi cha kisasa katika Halmashauri ya Wilaya Tunduru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru iliwasilisha andiko la mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi. Baada ya kuchambuliwa andiko hilo halikukidhi vigezo hivyo lilirejeshwa Halmashauri kwa ajili ya kufanya maboresho na kuanza kutenga fedha kupitia mapato ya ndani kwa awamu kwa ajili ya ujenzi wa stendi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa stendi hiyo ya mabasi limekodishwa kwa Kampuni ya Kalpataru Power Transmissions Ltd inayofanya kazi ya ujenzi wa gridi ya Taifa kwa miaka miwili, (2022/2023 na 2023/2024). Hivyo, Ofisi ya Rais TAMISEMI inaielekeza Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kukamilisha tathmini ya gharama za mradi na kuanza kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa stendi hiyo katika mwaka wa fedha 2024/2025, ahsante.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kuchukua hatua kwa Watumishi wanaoripoti na kuondoka bila kufanya kazi Wilayani Tunduru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikwishatoa waraka wa kusimamia masuala ya uhamisho wa watumishi kutoka mwajiri mmoja kwenda mwingine ikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa ambapo Waraka huo pamoja na mambo mengine, unaelekeza Mtumishi wa Umma kukaa kwenye kituo chake cha kazi kwa muda usiopungua miaka mitatu kabla ya kuomba kibali cha kuhama kwenda katika kituo kingine cha kazi.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia utaratibu huu ili kuhakikisha kuwa watumishi wanaopangiwa vituo vya kazi ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru wanafanya kazi katika vituo vyao.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka shilingi milioni 500 ya ujenzi wa Kituo cha Afya Namiungo na shilingi milioni 200 ya Kituo cha Afya cha Nakayaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imetenga shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Nakayaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kujenga Vituo vya Afya kwenye Kata za kimkakati kwa awamu ikiwemo Kata ya Namiungo. Ahsante.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -
Je, lini ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji katika Kijiji cha Nambalapi, Kata ya Masunya – Tunduru utaanza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika Skimu ya Nambalapi yenye ukubwa wa hekta 300.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa skimu hii, umeingizwa kwenye mpango bajeti katika mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo taratibu za manunuzi za kumpata mkandarasi atakayejenga miundombinu ya umwagiliaji zinaendelea. Baada ya kukamilisha hatua za manunuzi ujenzi wa skimu hii utaanza mara moja. Kukamilika kwa ujenzi wa skimu hii, kutanufaisha zaidi ya wakulima 5,933 katika vijiji vya Masonya, Nakayaya Mashariki, Mkalekawana, Nambalapi na maeneo jirani ndani ya Wilaya ya Tunduru.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza: -
Je, lini Barabara ya Pacha ya Mindu – Ngapa hadi Nachingwea itajengwa kwa Kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, maandalizi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya kutoka Pacha ya Mindu – Ngapa hadi Nachingwea yenye urefu wa kilomita 153 yameanza, ambapo zabuni kwa ajili ya kumpata Mhandisi Mshauri wa kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ipo katika hatua ya tathmini (evaluation). Kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina zinatarajiwa kuchukua kipindi cha mwaka mmoja, hivyo zitakamilika mwezi Juni, 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi, ahsante. (Makofi)
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza:-
Je, kwa nini Kiwanda cha Kubangua Korosho Wilayani Tunduru kimeshindwa kufanya kazi kwa miaka saba mfululizo?
WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Tunduru kilijengwa na Serikali mwaka 1981. Kutokana na mabadiliko ya kisera, Serikali ilibinafsisha kiwanda hicho kwa Kampuni ya Korosho Africa Limited mwaka 2001. Kiwanda hicho chenye uwezo wa kubangua wastani wa tani 3,500 kiliendelea na shughuli za ubanguaji hadi msimu wa 2019/2020 kiliposimamisha ubanguaji kutokana na kiwanda kubangua korosho kwa hasara tofauti na matarajio ya mwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina imeanza kupitia upya hali ya uzalishaji wa viwanda vya korosho vilivyobinafsishwa kikiwemo kiwanda cha Tunduru ili kujadiliana na kuhakikisha kwamba wawekezaji waliopo wanavifufua viwanda hivyo kwa malengo yaliyokusudiwa.
MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza:
Je, kuna upungufu kiasi gani wa walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru na upi mpango wa kuondoa upungufu huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua upungufu wa walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru na halmashauri nyingine nchini na imekuwa ikiajiri walimu wa shule za msingi na sekondari ambapo katika kipindi cha mwaka 2020/2021 hadi 2022/2023 jumla ya walimu 29,879 waliajiriwa wakiwemo walimu 16,598 wa shule za msingi na walimu 13,281 wa shule za sekondari. Katika kipindi hicho, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ilipangiwa walimu 213 kati yao walimu 145 wa msingi na walimu 68 wa sekondari.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2023/2024 Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 ambao watapangiwa vituo vya kazi katika maeneo yenye upungufu ili kupunguza upungufu uliopo zikiwemo shule za Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.
MHE. DAIMU I. MPAKATE K.n.y. MHE. HASSAN Z. KUNGU aliuliza:-
Je, ni Miradi mingapi ya kimkakati imetekelezwa katika Wilaya ya Tunduru?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Hassan Zidadu Kungu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati katika Wilaya ya Tunduru kama ilivyo katika wilaya nyingine na miradi hiyo ipo katika sekta zote; sekta ya elimu, Sekta ya afya, nyumba na maeneo mengine. Kwa mfano, katika Wilaya ya Tunduru, anafahamu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea na ukarabati mkubwa wa ukarabati mkubwa wa hospitali ya wilaya, ujenzi wa vituo vya afya na kadhalika. Ahsante.