Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jonas William Mbunda (26 total)

MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, naomba nimshukuru Naibu Waziri wa TAMISEMI kwa majibu mazuri, lakini vile vile niipongeze Serikali kwa kutoa huduma nzuri katika maeneo mbalimbali kwenye fani ya afya. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa hospitali hiyo ilijengwa mwaka 1970, jengo la OPD na jengo la upasuaji ni majengo ambayo yamepitwa na wakati na hayaendani na hadhi ya hospitali ya wilaya pamoja na jengo la wodi ya watoto ambao limekosekana kabisa.

Je, Serikali itaanza lini kushughulikia ujenzi wa majengo ya OPD, upasuaji na wodi ya Watoto?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika hospitali hiyo kuna uhaba wa watendaji, wafanyakazi, Madaktari na watendaji wasaidizi. Je, ni lini Serikali itachukua hatua ya kuhakikisha kwamba changamoto hiyo inatatuliwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jonas William, Mbunge wa Mbinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee pongezi za Mheshimiwa Mbunda na kwamba Serikali imeendelea kuboresha sana huduma za afya kwa kujenga miundombinu, lakini pia kuhakikisha vifaatiba na dawa zinapatikana. Kuhusiana na hospitali hii kuwa kongwe ni kweli. Hospitali hii imejengwa miaka ya 70 na ni hospitali ambayo kimsingi ni chakavu, inahitaji kuboreshewa miundombinu ili iweze kuendana na majengo ambayo yanaweza kutoa huduma bora za afya kwa ngazi ya hospitali ya halmashauri.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hayo, ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimeeleza kwamba Serikali imeanza kufanya tathmini ya uchakavu wa majengo yale na upungufu wa majengo ambayo yanahitajika katika hospitali ile ili sasa tuweze kuona namna ya kutenga fedha kwa ajili ya kuanza either, kukarabati majengo yale na kuongeza yale majengo yanayopungua au kuanza ujenzi wa hospitali mpya. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tathmini hiyo itakapokamilika tutakuja na jawabu la njia sahihi ya kwenda kutekeleza ili kuondokana na changamoto hiyo.

Mheshimiwa Spika, pili, ni kweli kuna changamoto ya upungufu wa watumishi katika kada mbalimbali katika hospitali hiyo na nchini kote kwa ujumla. Katika bajeti yetu tumeeleza mipango kwamba baada ya kukamilisha miundombinu ya majengo, tutakwenda kuhakikisha tunaboresha upatikanaji wa vifaatiba, lakini suala linalofuata muhimu na linapewa kipaumbele cha hali ya juu ni kuhakikisha sasa tunakwenda kuomba vibali vya kuajiri watumishi wa afya katika ngazi zote za vituo vya afya, zahanati na hospitali ili tuweze kutoa huduma bora zaidi. Kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunda kwamba, katika Hospitali hii ya Mji wa Mbinga pia tutaweka kipaumbele katika kuajiri watumishi ili kuendelea kuboresha huduma za afya.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, Mji wa Mbinga unakua kwa kasi na kipindi cha mvua barabara nyingi ambazo zimejengwa kwa kiwango cha changarawe huwa zinaharibika. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuongeza kiasi kilichotengwa katika msimu wa 2020/2021 na 2021/2022 ili kuhakikisha kwamba angalau kipande kirefu kijengwe ili kukidhi matakwa ya wananchi wa Jimbo la Mbinga Mjini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Serikali imefanya vizuri sana katika program ya ULGSP na TSCP na kuna uwezekano mradi wa TACTIC, je, Halmashauri ya Mbinga Mjini itakuwepo katika programu hii ya TACTIC?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipate majibu ya Serikali. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaomba tu kwamba katika bajeti ya mwaka 2021/ 2022 Serikali iweze kuongeza fedha katika Mji wa Mbinga Mjini ili angalau Serikali iendelee kujenga barabara nyingi za kutosha. Kwa sababu bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilishapitishwa na kiwango tulichokitenga kwa ajili ya fedha kipo kulingana na ukomo, lakini katika majibu yetu ya msingi tumeainisha hapo kwamba kwa kadri fedha zitakavyoendelea kupatikana, udharura na kadhalika, tutaendelea kupeleka fedha katika Halmashauri ya Mji Mbinga ili wananchi wake waweze kupata barabara nzuri na zinazopitika wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ameuliza kama Mji wa Mbinga upo katika ule mradi wa TACTIC. Nimwambie tu kabisa kwamba katika ule mradi, Halmashauri ya Mji Mbinga ipo. Ni sehemu ya ile miji 45 ambayo imeainishwa.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina swali moja la nyongeza. Barabara hiyo ili iweze kukamilika inatakiwa yajengwe madaraja mawili; je, Serikali haioni kwamba kiasi cha fedha cha shilingi milioni 10 kilichotengwa hakitatosheleza kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameuliza, kwa nini Serikali isijenge pamoja na daraja lingine kwa sababu hiyo barabara ina madaraja mawili na fedha tuliyotenga ni ndogo kukamilisha hiyo barabara. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda kufanya tathmini na baada ya hiyo tathmini tutatafuta fedha ili tuweze kumalizia na hilo daraja lingine ili liweze kukamilika. Ahsante sana.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Vile vile naomba niishukuru Serikali kwa kutekeleza miradi ya Lusaka, Mradi wa Mpepai na mradi wa Lifakara. Mwaka 2020 Serikali ilianza kutekeleza mradi katika Kata ya Myangayanga na Kata ya Ruahita, miradi hiyo miwili hadi sasa bado haijatekelezwa. Kwa hiyo nataka nijue, je, Serikali ina mpango gani wa kutekeleza miradi katika hizo kata mbili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jonas Mbunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hizi kata alizozitaja ziko kwenye mpango wa utekelezaji na kwa Mbinga Mjini tunatarajia hadi kufika 2023 Disemba, labda vitabaki kama vijiji viwili tu ambavyo vitakuwa bado havijapata maji. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwa namna ambavyo tunashirikiana nampongeza sana na nimhakikishie maji Mbinga yanakwenda kupatikana.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nishukuru sana kwa majibu ya Serikali lakini nilikuwa na ombi. Naiomba Serikali kuhakikisha kwamba mradi huu unatekelezwa mapema kwa sababu ni barabara muhimu sana kwa wananchi wa kata ya Luwaita kwa ajili ya kusafirisha mazo yao kwenda kwenye maeneo ya soko, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Mbinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea tutafanya hivyo, kwa sababu awamu ya kwanza na ya pili ziko katika utekelezaji kwa hito na hii ya tatu tutaitekeleza, ahsante.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Mbinga, Litembo, Kili ilitolewa ahadi na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nilitaka nijue je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFRY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunda Mbunge wa Mbinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ahadi zote ambazo zimetolewa na Waheshimiwa viongozi wakuu wa nchi, ni ahadi ambazo tunazitekeleza. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunda, Mbunge wa Mbinga, kwamba barabara hii ipo kwenye mpango kwa ajili ya kuijenga kama ambavyo viongozi wetu walioahidi na sisi tutamhakikishia kwamba ahadi hiyo tutaitekeleza.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali naomba kuuliza swali la nyongeza. Hospitali ya Wilaya ya Mbinga Halmashauri ya Mbinga Mji ilijengwa mwaka 1970, na mpaka sasa hivi majengo yake yamechakaa. Sasa hivi Serikali ina mpango mkakati wa kuhakikisha hospitali hizo zilizochakaa majengo zinajengwa upya.

Je, lini Serikali itatenga fedha kuhakikisha kwamba majengo mapya yanajengwa katika hospitali ya Mji wa Mbinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunda Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa fedha 2022/23 jumla ya shilingi bilioni 16 zimetengwa kwa ajili ya ukarabati au ujenzi wa Hospitali za Halmashauri kongwe na chakavu, ambapo mpango ni kujenga hospitali 19. Kwa hivyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaangalia kama hospitali hiyo ipo kwenye orodha hiyo lakini kama haipo kwenye orodha hiyo tutafanya tathmini ili tuweze kuweka mpango wa kuikarabati hospitali hiyo. Ahsante.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia unaendelea katika nchi yetu, kuna umuhimu mkubwa wa Serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba vituo hivyo vinajengwa kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, jengo la dawati la jinsia lililoanza kujengwa katika Wilaya ya Mbinga sehemu kubwa limejengwa kupitia michango ya wadau mbalimbali. Swali langu: Je, Serikali ni lini italeta fedha kuhakikisha kwamba inakamilisha ujenzi wa jengo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi, vyanzo vya fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Polisi vikiwemo maeneo ya jinsia na watoto zinatoka Serikalini, kwa wadau wa ndani na wa nje na mashirika mbalimbali. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Mbunda kwa wadau wake kushiriki, lakini tumesema pale ambapo watakuwa wamefika kiwango cha umaliziaji kupitia Mfuko wa Tuzo na Tozo ya Jeshi la Polisi, tutasaidia kukamilisha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niko tayari kuwasiliana nawe ili kuona nini kinahitajika kukamilisha kituo hicho alichokirejea.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Mbinga – Litembo – Nkili ni barabara muhimu sana kwa wakulima wa kahawa. Nataka nipate majibu ya Serikali ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunda, Mbunge wa Mbinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyotaja itaanza kujengwa mara tu tutakapokuwa tumefanya review ama kukamilisha usanifu wa kina ikiwa sasa tutakuwa tumepata gharama ya hiyo barabara kuijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza naishukuru Serikali kwa kuanza kutekeleza mradi wa kujenga mnara katika Kata ya Kitanda, kupitia mradi wa Tanzania ya Kidigitali. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali imetoa maelezo kwamba, Kata za Kikolo, Mbangamao na Kagugu zitafanyiwa tathmini; na maeneo hayo watu wakati mwingine wanapanda kwenye miti kutafuta mawasiliano: Nataka nijue sasa ni lini tathmini hiyo itaanza kufanyika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika Kata ya Mpepai ulijengwa mnara ambao unaendeshwa na Kampuni ya Airtel, na wakati mwingine kunakuwa na changamoto ya mawasiliano, mtandao huwa haupatikani. Ninataka nijue ni lini sasa Serikali itafanya marekebisho katika eneo hilo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa fedha kwa ajili ya kufanya tathmini katika vijiji 2,116. Na katika upande wa Mbinga, Vijiji vya Luanda, Muhongozi, Matili na Kitanda zilifanyiwa tathmini hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini katika mwaka wa fedha huu wa 2023/2024, Kata za Kikolo na Kagugu zitaingizwa katika utaratibu wa kufanyiwa tathmini na baada ya hapo fedha zitakapopatikana zitaweza kufikishiwa huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, kwa kipengele cha pili kuhusu mnara wa Airtel uliopo katika Kata ya Mpepai; changamoto ya mnara huu ni kwamba unatumia nguvu ya jua (solar energy) na tumeshakubaliana na watoa huduma kufanya mambo mawili yafuatayo; la kwanza ni kwamba pale ambapo umeme wa Gridi ya Taifa umeshafika wafanye juhudi za kuhakikisha kwamba wanaunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, na pale ambapo umeme wa Gridi ya Taifa haujafika basi wahakikishe kwamba wanaweka jenereta ili iwe njia mbadala pale ambapo solar inakuwa imezidiwa. Na hayo tayari tumeshakubaliana na hatua zimeshaanza kuchukuliwa, ni pamoja na katika eneo hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitaja. Ahsante.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto ya upatikanaji wa maji katika Kata ya Kikolo na Kilimani pia Vijiji vya Mtama, Tukuzi, Masmeli na Mateka. Ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kujenga miradi katika maeneo hayo? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge, Jumatano kwa maana ya Tarehe 10 nawasilisha Bajeti yetu ya Wizara ya Maji kwa hiyo mambo yatakuwa ni fire, mambo ni moto. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafsi ya kuuliza swali la nyongeza. Lakini pia nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa utekelezaji wa hiyo miradi. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi zake nzuri. Alifika Mbinga, na wakati huo amekuja kukagua vyanzo vya maji aliona hali halisi ya mahitaji ya maji katika Mji wa Mbinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja la nyongeza. Pamoja na Serikali kusema kwamba imeanza kufanya ukarabati kilometa 21 na kununua dira za maji 2,500 kiwango hiki bado ni kidogo. Nilitaka nijue, sasa Serikali ina mpango gani wa kuongeza fedha ili kuhakikisha kwamba ukarabati ule unaendelea katika Mji wa Mbinga? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Mbinga kwa kazi kubwa na namna ambavyo anawapigania wananchi wake. Nataka nimhakikishie na ukisoma maandiko ya dini kwa maana ya Mathayo 7:7 yanasema: “Ombeni nanyi mtapewa, bisheni hodi nanyi mtafunguliwa.”

Nataka nimhakikishie tutaiangalia Mbinga kwa namna ya pekee ili kuhakikisha wananchi wake wanapata maji. Ahsante sana.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali inaendelea kujenga majengo mapya katika maeneo mbalimbali.

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama katika Wilaya ya Mbinga na Songea?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha nimesema kwamba tuna Mahakama 24 tumeziitenga kuzijenga na Wilaya yake ni miongozni mwa wilaya hizo mabazo tutajengea Mahakama. Ahsante.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kuanza kutekeleza miradi katika Vijiji vya Sepukila na Kitelea pia kuandaa kutekeleza miradi ya maji katika Vijiji vya Tukuzi na Mateka. Vijiji vya Nzokai, Kilimani, Rudisha, Mikolola na Njomlole vina changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji. Nataka nijue sasa ni lini Serikali itaandaa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi kwenye maeneo haya. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nipokee shukrani zake kwa Serikali, lakini zote ni jitihada zake za ufuatiliaji wa karibu na ushirikiano wake mzuri ndani ya Wizara yetu ta Maji. Mheshimiwa Mbunge, nawe tunakupongeza katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji hivi alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge tayari vipo katika hatua mbalimbali za kuona kwamba na vyenyewe tunavifikishia maji safi na salama bombani. Hivyo, katika mwaka ujao wa fedha, vijiji hivi navyo tutavigusa katika namna ya kuona huduma inapelekwa.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika mpango wa Serikali wa kujenga vituo vya afya vya kimakakati, Kata ya Utiri Halmashauri ya Mji wa Mbinga ni moja ya kata ambazo ziliainishwa kujenga kituo hicho. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki cha afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hiki Kituo cha Afya cha Utiri, Wilayani Mbinga, kama nilivyosema hapo awali Serikali ilitenga zaidi ya bilioni 117 kwa ajili ya ukamilishaji wa vitu vya afya vya kimkakati hapa nchini. Tutaangalia kwamba kituo hiki kama kimetengewa fedha, basi fedha hizo ziweze kwenda mara moja na kuanza kufanya ujenzi ili kutoa huduma kwa wananchi wa Utiri na kama fedha hiyo haijatengwa tutahakikisha bajeti inayokuja nayo, tutakitengea fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa kituo hiki.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali ina mpango wa kujenga miradi ya kimkakati katika halmashauri mbalimbali, Halmashauri ya Mji wa Mbinga ni moja ya halmashauri ambayo inatakiwa ipate miradi hiyo ya kimkakati, nataka nijue kupitia mradi wa TACTIC ni lini serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kujenga mradi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ya kimkakati upatikanaji wake unaendana sambamba na tutakavyopokea maandiko kutoka kwa wataalam wetu kwenye halmashauri mbalimbali nchini ikiwemo Halmashauri ya Mbinga na Mradi wa TACTIC alioutaja upo unaratibiwa na Taasisi ya TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuona kama TACTIC phase one mradi wa mkakati wote upo katika halmashauri ile, kama haupo tuone ni phase two, kama haupo tuone kama ni phase three, lakini nitumie jukwaa hili la Bunge lako Tukufu kusema tu kwamba kuwaasa wataalam wetu Maafisa Mipango na Wakurugenzi wa Halmashauri kuwa wabunifu wanapofanya maandiko haya ya miradi ya kimkakati. Lengo la Serikali kutoa miradi hii ya kimkakati ni ili halmashauri ziweze kupata uwezo wa kimapato, wasibuni tu mradi ili mradi halmashauri fulani imefanya na wao wakataka, waangalie jiografia yao, eneo lao, ni mambo gani ambayo wakiyafanya basi miradi hii itawaingizia kipato.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pia naomba niipongeze Serikali kwa kuchukua jitihada kuhakikisha kwamba shirika hili linafanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa shirika hili muda mrefu halijafanya kazi, ni wazi kwamba kuna upungufu mkubwa sana wa wafanyakazi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inaongeza wafanyakazi katika shirika hilo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kama nilivyosema awali kwamba ni muda mrefu TFC haijafanya kazi, ni obvious kwamba miundombinu ya maghala ambayo yalikuwa yanatumika kuhifadhia mbolea yana hali mbaya: Serikali imeandaa mpango gani kuhakikisha kwamba maghala haya yanakarabatiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la wafanyakazi, ni kweli kampuni hii inahitaji wafanyakazi. Wiki iliyopita, management yote ilikuwa hapa kwa ajili ya kwenda kuutetea muundo kwa ajili ya kuanza kuboresha eneo hili na kupata wafanyakazi wapya. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii inaendelea ya kupata wafanyakazi wengine wa kusaidia kuendesha Kampuni yetu ya TFC.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusu maghala, ni kweli tunayo maghala ambayo yamekuwa na changamoto kwa kiwango kikubwa sana, lakini hivi sasa tunashirikiana na Halmashauri za wilaya husika kwa ajili ya maghala yale ambayo yapo katika maeneo yao tuweze kuyatumia. Pia sisi tunayo maghala yetu ambayo tunayaboresha hivi sasa ili yaanze kufanya kazi hii. Katika fedha ambayo tumeipanga mwaka ujao wa bajeti, pia tumeongeza eneo la kuboresha maghala yetu ili yaweze kutumika vizuri.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Naomba nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa jinsi inavyoweka mikakati mizuri ya kufanya ukarabati wa miundombinu katika shule zetu za msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mbinga Mjini lina Kata 19 na Kata nane ziko mjini, Kata 11 ziko vijijini lakini bado kuna changamoto kubwa sana ya Walimu katika eneo hili la Jimbo la Mbinga Mjini. Katika mgao wa Walimu ambao wameajiriwa hivi karibuni Jimbo la Mbinga Mjini halijapata Mwalimu hata mmoja. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inamaliza changamoto hii katika Jimbo la Mbinga Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kumwelekeza Katibu Tawala, Mkoa wa Ruvuma kuhakikisha anafanya msawazo ndani ya Mkoa wake kwa maeneo ambayo yana upungufu wa watumishi. Kuna maeneo ambayo yatakuwa na watumishi au Walimu wengi zaidi na yale ambayo bado hayajapata watumishi, basi Katibu Tawala wa Mkoa aweze kuhakikisha anapeleka watumishi ikiwemo katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunda la Mbinga Mjini.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, lakini pia niishukuru Serikali kwa kuendelea kufanya ukarabati wa barabara hiyo mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, kama alivyoeleza Naibu Waziri kwamba ni kilometa 14 tu za barabara hizo zimewekwa changarawe na maeneo ya Mbinga ni maeneo ya mteremko na milima, naomba kujua sasa Serikali ina mpango gani wa kuendelea kuweka changarawe katika kilometa zilizobaki pamoja na kuhakikisha kwamba mitaro imetengenezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Barabara ya kutoka Mbinga – Kitanda – Miembeni – Lupilo – Mpepai na Mtua iliharibika sana hasa katika kipindi cha mvua, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba barabara hiyo inatengenezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza, hii barabara ambayo ni Kitanda Road yenye urefu jumla ya kilometa 32. Serikali katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga fedha kwa ajili ya kutengeneza kilometa sita kwa kiwango cha kifusi. Kama nilivyosema awali tayari ilikuwa imeshatengenezwa kilometa 14 na katika mwaka wa fedha unaofuata Serikali itatengeneza kilometa sita na kuweka mifereji katika maeneo ambayo huwa maji yanajaa.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la barabara hii ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie kwamba katika mwaka wa fedha huu unaoanza 2023/2024, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuweka concrete (zege) katika yale maeneo korofi ya milimani kwa sababu jiografia ya kwa Mheshimiwa Mbunda kule ni ya vilima vingi. Kwa hiyo tutaweka concrete katika maeneo korofi na vilevile nimpe taarifa tu Mheshimiwa Mbunda kwamba ana Barabara hii ya Utili – Mahande ambayo ina kilometa 14 inaenda kuwekewa lami kama ambavyo aliomba yeye kwenye Mradi ule wa Agri–connect.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Mbinga Mjini mahitaji ya walimu kwenye shule za sekondari ni idadi ya 370 lakini waliopo ni 279 kuna upungufu wa walimu 91 hasa kwenye masomo ya sayansi na hesabu. Shule za msingi mahitaji ni 1,026 waliopo ni 605 upungufu 421 na ikama ya wafanyakazi katika afya wanaohitajika ni 725 waliopo ni 294 upungufu ni 431. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na upungufu huu mkubwa na kwa sababu Serikali imeahidi kwamba inafanya ajira, nilitaka nijue, je, Naibu Waziri ananihakikishia kwamba katika mgao huo wa watumishi, jimbo langu litapata watumishi wa kutosha ili kuweza kuziba hilo pengo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika maelezo ya Serikali na mkakati uliopo ni kujenga vituo vingi vya afya nchini. Lakini Serikali haijaonesha kwamba kuna mkakati gani wa dharura wa kuajiri watumishi ili kuhakikisha kwamba tunaziba hili pengo la wafanyakazi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jonas William Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na upungufu wa watumishi wa sekta zote, sekta ya elimu na sekta ya afya naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeweka mikakati ya dhati na inatekelezwa ya kuajiri watumishi wa elimu na watumishi wa afya na ndiyo maana hivi sasa tunapoongea tunaajira ambazo zinaendelea kuchakatwa za maombi ya watumishi ambao watapelekwa kwenye vituo vyetu vya afya lakini pia kwenye elimu na tutaendelea kufanya hivyo. Ahsante.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Jimbo la Mbinga Mjini, Kata ya Kitanda, Kikolo na Kagugu hakuna miundombinu ya mawasiliano. Je, lini Serikali itajenga miundombinu ya mawasiliano ili kuwarahisishia wananchi kupata mawasiliano?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maeneo aliyoyataja naamini yako kwenye orodha ya kata ambazo mwaka ujao wa fedha tunapeleka minara ya simu, lakini kama kata zote hazikuingia kama nilivyosema, baadhi ya hizo kata zitakuwa zimeingia, zilizobaki tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kufanya tathmini ya mahitaji yaliyopo, tuangalie uwezo wa bajeti yetu hasa kwenye maeneo yale ambayo yanahitaji huduma maalum na tutafikiria kuona namna ya kupeleka huduma kwenye maeneo aliyoyataja.

MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Changamoto iliyopo katika Wilaya ya Chemba inafafana sawa na changamoto zilipo katika Jimbo la Mbinga Mjini. Kuna zahanati katika vijiji vya Mzopai, Mundeki, Mikolola, Maande na Rudisha nguvu za wananchi zimewekezwa pale. Kwa hiyo, nilitaka nijue ni lini Serikali itafanya mkakati kuhakikisha kwamba inakamilisha ujenzi wa zahanati ile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, majengo haya ya maboma ya zahanati katika Jimbo la Mbinga Mjini, kwanza tunawapongeza wananchi kwa kutoa nguvu zao kwa sababu huu ndiyo mpango wa maendeleo ya afya ya msingi kuchangia nguvu za wananchi katika ujenzi wa vituo hivi, lakini nimuhakikishie kama ambavyo Serikali imeendelea kukamilisha maboma katika mwaka huu zaidi ya maboma 900 ya zahanati na mwaka ujao 300; tutaendelea pia kutoa kipaumbele katika maboma haya ya Mbinga Mjini ili yaanze kukamilishwa kwa awamu. Ahsante.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Mbinga – Muyangayanga – Mahenge – Litembo ina urefu wa kilometa 25. Ninaishukuru Serikali imejenga vipande vya lami kwenye maeneo korofi.

Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema tumeanza kujenga maeneo korofi. Nimhakikishie kwamba kadri fedha zitakapokuwa zinapatikana tutaendelea kuboresha maeneo ambayo yanahitaji kudhibitiwa, ahsante sana.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza, naomba niishukuru Serikali kwa kuweka mpango wa kufanya usanifu pamoja na kujenga miundombinu katika skimu ya umwagiliaji kwenye eneo la Kata ya Kihungu kwa Mwaka 2024/2025. Nina swali moja la nyongeza. Katika Kata ya Mpepai eneo la Mtuwa na Ruvuma Chini nayo ni maeneo ambayo yanafaa kwa ajili ya kujenga za umwagiliaji;

Je, Serikali inampango gani wa kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanajengewa skimu za umwagiliaji?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Moja, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba kilimo tunachokipeleka sasa ni kile ambacho kitakuwa kinategemea maji badala ya mvua. Yaani tunataka Mtanzania alime katika misimu yote, yaani kwa maana kipindi cha kiangazi awe na shughuli ya kufanya ya kilimo lakini na kipindi cha msimu wa mvua afanye hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo haya maeneo ambayo ameyaainisha Mheshimiwa Mbunge ni maeneo yote ambayo Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inayapitia ili kuhakikisha kwamba yote tunayatafutia fedha na yanaingia katika mpango ili yaweze kutekelezeka, ahsante sana.

MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Mbinga – Muyangayanga – Mahenge – Litembo ina urefu wa kilometa 25. Ninaishukuru Serikali imejenga vipande vya lami kwenye maeneo korofi.

Je, ni lini Serikali itajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema tumeanza kujenga maeneo korofi. Nimhakikishie kwamba kadri fedha zitakapokuwa zinapatikana tutaendelea kuboresha maeneo ambayo yanahitaji kudhibitiwa, ahsante sana.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kata ya Kikolo katika Jimbo la Mbinga Mjini ina changamoto kubwa sana ya mawasiliano: Ni lini Serikali itapeleka huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilipokee na nilichukue kama changamoto ambayo tutaenda kuifanyia kazi, ahsante.