Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. George Ranwell Mwenisongole (11 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwa sababu leo ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili Tukufu la Kumi na Mbili, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwanza kwa kutuwezesha kufika hapa salama na kutuwezesha sisi kushinda uchaguzi mgumu uliopita.

Mheshimiwa Spika, vile vile napenda niwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Mbozi Mkoa wa Songwe na Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuniamini na kunichagua mimi kuwa Mbunge. Nianze kwa kusema naunga mkono hoja. Hotuba hii ya Mheshimiwa Rais sio tu ni dira kwetu sisi Wabunge, nafikiri ni mwelekeo kwa miaka mitano ijayo kwa Taifa letu. Kuna jambo moja ambalo ningependa nijikite ambalo nikuhusu kilimo. Chama chetu Cha Mapinduzi kwa nia njema kabisa kilileta hii sera ya ushirika kwa nia ya kumsaidia mkulima mmoja mmoja ili awe na uhakika wa masoko na bei yake.

Mheshimiwa Spika, katika maeneo mengi vyama hivi vya ushirika nahisi sijui vina mapepo au vimevamiwa na majambazi, sielewi! Sijaona mahali ambako vyama vya ushirika vimefanya vizuri. Ukienda Kagera, ukija Mbozi, ukienda Mbinga kote ni malalamiko hayo hayo yanayofanana. Kwangu mimi kwenye Jimbo langu la Mbozi vyama hivi vya ushirika sisi kule tunaita AMCOS, huwa wakulima wanapeleka kahawa. Kule kwetu Mbozi, sisi kahawa ndiyo kama dhahabu, sisi hatuna zao lingine tunalotegemea zaidi ya kahawa. Sasa wakulima wakishapima kahawa yao, hawa viongozi wa AMCOS wanachofanya, wanakwenda benki kuchukua mkopo bila wale wakulima wengine kwenye vyama vile vya msingi kujua kwamba wale viongozi wamechukua mkopo. Matokeo yake sasa benki inapokuja kufanya malipo inafyeka yale malipo na kuwafanya wakulima waishi katika hali ya umaskini. Hii hali imeendelea kwa kipindi kirefu sana.

Mheshimiwa Spika, napenda nishukuru juhudi ambazo zimeanza kuchukuliwa sasahivi naOfisi ya TAKUKURU ya Mkoa, ingawa zimekuja kwa kuchelewa lakini bado hatua zaidi, ningependa tunapozidi kufikiria hili suala liingie kisheria. Hawa watu sio tu wafilisiwe nyumba zao, wafikishwe mahakamani na kufungwa. Nafikiri tukiamua kuwa wakali katika hili suala la ushirika na hawa viongozi ambao wanataka kuua ushirika, nafikiri tutakuwa tumemsaidia sana mkulima, kwa sababu kwa muda mrefu sana hawa viongozi wamekuwa wanaishia TAKUKURU tu, wanapewa ratiba ya kurudisha fedha zao, wengine wanahama miji, lakini bado hatujapata solution ya kudumu ya kuokoa maisha ya hawa wakulima ambao bado wanaishi katika hali ya umaskini. Kwa hiyo, napenda kuunga hoja hii ya hotuba ya Rais, lakini hili suala la viongozi waAMCOS ni lazima tuje na solution ya kudumu ili kuhakikisha kwamba wakulima wa chini wanalindwa kutokana na mazao yake.

Mheshimiwa Spika, kingine napenda sana kumshukuru Mheshimiwa Rais, wakati wakampeni alikuja kwenye Jimbo langu la Mbozi na mimi binafsi pamoja na watu wengine tulimweleza shida ya wafanyabiashara pale Mlowo, Vwawa na Tunduma wanavyopata shida na TRA. Rais alikuja tarehe Mosi Oktoba, siku ya Alhamisi. Siku ya Jumatatu yake tarehe 4 alimtuma Kamishna waTRA aje pale Mbozi. Kinachotokea, TRA badala ya kuwa rafiki wanachofanya wakikutana na mfanyabiashara wanamkadiria makadirio ya juu kwa mapato yake, kodi ya juu sana kuliko uwezo wake ili tu akae nao mezani waweze kupata kitu chochote.

Mheshimiwa Spika, matokeo yake ni kwamba TRA imekuwa kama ni fimbo kwa wafanyabiashara na hili ni suala ambalo limekuwa kinyume na maono ya Mheshimiwa Rais. Rais wakati anazindua hili Bunge alisema kwamba angependa TRA na wafanyabiashara wawe marafiki, lakini mahali popote unapokutana na mfanyabiashara, adui yake mkubwa ni TRA. Kwa kweli hili ni suala ambalo kama kweli unataka kumsaidia mfanyabiashara na kuinua mapato ni lazima hawa maafisa wasio waaminifu wa TRA, washughulikiwe.

Mheshimiwa Spika,kwa hiyo kwa kusema hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kuungana na Wabunge wenzangu kuipongeza sana Wizara ya Maji kwa juhudi kubwa walizozifanya kusambaza maji vijijini. Vilevile napenda niwapongeze RUWASA Mkoa wa Songwe hasa Meneja Injinia Charles Pambe kwa kazi kubwa anayoifanya, ingawa nasikitika kusema kwamba RUWASA, Mkoa wa Songwe hatuna gari, wamekuwa wakifanya kazi kwa kuazimaazima gari. Vilevile nimpongeze meneja wa RUWASA, Wilaya ya Mbozi Bw. Gratius Haule kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya Wilaya ya Mbozi. (Makofi)

Mheshiniwa Naibu Spika, pamoja na juhudi hizi kubwa za Wizara ya Maji kusambaza maji huko vijijini juhudi hizi zinaweza zikawa bure kama Serikali haitaingilia gharama za kuunganisha maji vijijini. Katika ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi inasema kwamba kufika mwaka 2025 asilimia 85 ya wakazi wetu vijijini lazima wapate maji, lakini kwa gharama hizi ya shilingi laki nne laki tano kuungainishiwa maji, hivi mwananchi maskini wa kijijini hizi laki nne laki tano anapata wapi? (Makofi).

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wakulima mwananchi ataamua ni bora anunue mifuko ya mbolea kuliko kuunganishiwa maji, lakini kama gharama hizi zikishushwa zikawa sawa kama umeme wa REA ambao kuungaishiwa ni Shilingi elfu 27 tunaweza tukafikia sio tena asilimia 85 itakuwa ni asilimia 100. Ushauri wangu Mheshimiwa Waziri ni huu, wananchi waunganishiwe bure halafu wakate gharama za kuunganisha bure wanapokuja kulipia gharama za maji kila mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo kama wananchi wote wataunganishwa bure maji, halafu wakaja kuwakata mwisho wa mwezi wanapolipa bili yao ya maji, tunaweza kufika sio tena asilimia 100 hata asilimia 150, lakini bila kufanya hivyo hizi juhudi zote zitakuwa bure kama hatutaweza kushusha gharama za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine Mheshimiwa Waziri kwa masikitiko makubwa wananchi vijijini wanalazimishwa kununua vifaa vya kuunganisha maji kwenye mamlaka za maji. Sasa nataka niulize hizi mamlaka za maji zina maduka ya kununulia vifaa vya kuunganisha maji? Kama sio udalali! Kwa sababu maduka hayo hayo wananchi ambao wangeenda kununua ndio hayo hayo ambayo hao Maafisa wa Maji ndio wanakwenda kununua hivyo vifaa. Sasa kuna sababu gani ya msingi kulazimisha wananchi kununua vifaa vya kuunganisha maji kwenye mamlaka za maji, kwa nini wasiende kununua kivyao wao wa-deal tu na gharama za kuunganisha maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ushauri wangu ni huu, kama kweli tuna nia yakutaka kusambaza maji na kuhakikisha maji yanafika kwa kila mwananchi ndani ya nchi yetu ya Tanzania, ni lazima gharama za kuunganisha maji ziwe ndogo. Kwa kufanya hivyo tutaweza kabisa kumaliza tatizo la maji ndani ya nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa hii nafasi muhimu sana ya kuchangia bajeti hii muhimu kwa Watanzania. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa fedha shilingi 100,000,000,000 alizotoa, imeonesha kabisa kwamba Rais wetu anajali maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa mara ya kwanza tangu niwe Mbunge nimeshuhudia Waziri anawasilisha hotuba yake ya Bajeti bila kumleta mke wake humu ndani, badala yake Mheshimiwa Waziri ametuletea hivi vipaumbele vya bajeti imeonesha kabisa huu Waziri yupo serious. Mambo ya kuja kuuza sura hapa yeye hana, yeye yupo serious na kazi. (Kicheko/Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri, nimesoma hotuba yake ya bajeti yote, jamani Wabunge naomba mnisikilize. (Kicheko/Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwenisongole wewe ndiye unayechangia, endelea kuchangia kiti kinakufuatilia.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, okay, ahsante.

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa, karibu.

T A A R I F A

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, akinamama wanaoletwa hapa Bungeni wanakuja kwa heshima zote, ni walezi wa familia, wanajaliwa na hawa waume na hawa wanawake na ndio maana wanaletwa hapa, hawaji hapa na wala hawaletwi hapa kwa ajili ya kuuza sura. Haya ni matusi makubwa sana kwa wanawake, naomba arekebishe maneno yake, maneno ya hovyo kabisa haya. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lucy Mayenga, ni taarifa au unataka afute maneno yake.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, afute.

MWENYEKITI: Nazungumza na Mheshimiwa Lucy Mayenga, kiti kikizungumza unanyamaza.

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, arekebishe maneno yake Hansard ikae sawa, haiwezekani wanawake wanaokuja hapa Bungeni, ikaonekana wanakuja kuuza sura.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lucy Mayenga ulitumia taarifa, kwa hiyo Mheshimiwa Mwenisongole taarifa unapokea?

GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naona Mheshimiwa Lucy Mayenga hajanielewa, mimi nimempongeza January Makamba, yeye alichokisia…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Kuhusu Utaratibu

KUHUSU UTARATIBU

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama kufuatia kauli aliyotoa mchangiaji ambayo ni ya maudhi, wakati anachangia amempongeza Waziri wa Nishati, lakini ameenda mbele zaidi akadhihaki kwa kusema kwamba Mawaziri ambao wanawaleta wenza wao hapa wanawaleta kuja kuuza sura na hawapo serious. Sasa kanuni zetu zinakataza lugha za kuudhi kwa hiyo ningependa mzungumzaji afute kauli, hiyo kauli aliyotoa ambayo inaudhi na inakera. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Esther Matiko amesimama kwa kifungu cha Kuhusu Utaratibu, Kanuni ya 75 bila shaka inayotaka kufahamu ni kanuni gani ambayo imevunjwa maana ndio msingi wa kifungu hiki. Labda nikusomee: “Mbunge yeyote anaweza kusimama wakati wowote na kusema maneno “kuhusu utaratibu” ambapo Mbunge yeyote ambaye wakati huo atakuwa anasema atanyamaza na kukaa chini na Spika atamkata Mbunge aliyedai utaratibu ataje Kanuni au sehemu ya Kanuni iliyokiukwa”.

Mheshimiwa Esther Matiko ni kanuni gani imekiukwa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 71(1)(j).

MWENYEKITI: Kanuni ya 71(1)(j) inayosema lugha za kuudhi ni pamoja na hatatoa lugha ya matusi au ishara inayoashiria matusi au kumsema vibaya Mbunge au mtu mwingine. hatotumia lugha ya kuuzi au inayodhalilisha watu wengine.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, yes, 71(1) (j).

MWENYEKITI: Mheshimiwa George Mwenisongole amesimama Mheshimiwa Matiko hapa kukutaka ufute maneno uliyotumia ya kutambulisha kwa sababu tunao utaratibu Bungeni hapa wa kuruhusu wageni mbalimbali kuja wakiwemo viongozi pamoja na wanaoambatana na viongozi wenzetu. Kwa hiyo kuwaita waanauza sura ni maneno yasiyofaa, kwa hiyo futa maneno yako hapa ili uendelee kuzungumza. (Makofi)

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafuta kauli ya kuuza sura, lakini nabaki na msimamo wangu wa kumpongeza Mheshimiwa Waziri…

MWENYEKITI: Sasa sikiliza Mheshimiwa Mwenisongole, ukifuta ukasema lakini nitakukalisha usiendelee kuzungumza.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa nafuta kauli. (Makofi)

MWENYEKITI: Haya, endelea kuchangia.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

La pili nampongeza Mheshimiwa Waziri, nimesoma hotuba yake yote ya bajeti, katika hotuba yake ya bajeti kwa mara ya kwanza tangu nimekuwa Mbunge asilimia 99 ya fedha anazoomba zote zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo, sijawahi kuona hiki kitu, ni asilimia moja tu ya bajeti yote ya Wizara ya Nishati inakwenda kwenye matumizi ya kawaida. Hiki ndicho ambacho sisi na Watanzania tunataka kukiona, hiki ndio kilio cha Watanzania kuona fedha za wananchi nyingi zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kaka yangu January, Mheshimiwa Waziri nina mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana Serikali ili ilisaini mkataba wa REA na wakandarasi mwezi Juni, mkataba wa miezi 18 na sisi kama Wabunge na wananchi wote tulifurahi tukiamini kwamba vijiji 3,448 vilivyobaki kwenye mpango wa REA vinakwenda kumalizika na kwa mara ya kwanza umeme utafika katika vijiji vyote Tanzania. Hata hivyo, cha kusikitisha hawa wakandarasi hawa ambao kwa kweli sijui wamepata wapi hiyo jeuri, waliposaini mkataba wa miezi 18 walipewa miezi sita, hiki kipindi kinaitwa mobilization period na walilipwa 25 percent ya gharama yao, wakaambiwa mobilization period ni kipindi ambacho mkandarasi anatakiwa afikishe vifaa vyote site au ahakikishe vifaa na taratibu zote zimefika site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo vifaa ambavyo mkandarasi wa REA anavihitaji ni nguzo, transformer, LUKU na nyaya ambavyo vyote vinazalishwa hapa nchini. Kwa mshangao hawa wakandarasi mwaka huu mwezi Machi wanatuambia vifaa vimepanda, kwamba umeme wa REA hauwezi kuendelea kwa sababu gharama za vifaa zimepanda, lakini cha kushangaza hata Waziri naye anakubaliana na sababu hizi ambazo hazina mashiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walikuwa wapi katika kipindi cha mobilization period kupeleka vifaa kwanini wasiseme kipindi hicho, Miezi sita wao kupeleka vifaa site imefika, leo hawawezi kuja wakatuambia umeme wa REA umeshindwa kufika kwa sababu vifaa vimepanda, hivyo vifaa vimepanda mwaka huu. Kwa hiyo, ni kwamba maamuzi ya Waziri kukubaliana na hizi hoja za Wakandarasi si sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu ya CCM imeahidi umeme utafika vijijini kufikia Disemba, vilevile Mheshimiwa Waziri katika hotuba yako hujatuambia sasa umeme huu wa REA utaisha lini na hawa Wakandarasi wanadai kiasi gani sasa za kupanda. Pia katika majadiliano na Wakandarasi si kuna kitu kinaitwa variation ambayo mnaweza mkakaa na Wakandarasi mkajadiliana variation ambayo imepanda, hata ukiangalia bidhaa zote za hawa Wakandarasi wanazozihitaji zinazalishwa hapa nchini! Sasa transformer zipi, nyaya zipi, LUKU zipi au nguzo zipi zimepanda kiasi cha kusababisha huu mradi wa REA usiendelee? Kwa kweli ni jambo ambalo inabidi tuwe makini sana na Wakandarasi otherwise watatuletea historia ya mtu na Ngamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ngamia alikwenda kwa mtu mmoja akamuomba aingize mguu, yule mtu akamkubalia baadaye akasema naomba niingize na kichwa yule mtu akamkubalia, mwisho wake ngamia akaingia nyumba nzima akatoa! Tukiendelea kuwakubalia Wakandarasi kwa kila hoja wanayokuja hatutaweza kufanikisha kufikisha umeme vijijini, huu ni udhaifu ambao unataka kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine cha mwisho wananchi tunaotoka maeneo ya mpakani tunayo advantage ya kufaidika na bidhaa zinazouzwa bei ya chini upande wa pili wa mpaka. Kwa mfano, sukari imepanda Tanzania lakini ukienda Zambia ipo chini, mafuta ya kula yamepanda huku ukienda Zambia yapo chini na vitu vya namna hiyo, lakini cha kushangaza sasa gharama hizi za mafuta ambazo zimepanda Mkuu wangu wa Mkoa yeye ameunda taskforce kupambana na wananchi wanaokwenda Zambia kuchukua vitu kwa bei nafuu wanasema hao ni walanguzi, sasa mimi nilitegemea angeunda taskforce kupambana na wafanyabiashara wasiowaaminifu ambao wanapandisha vitu ambavyo havihusiani hata na bei ya mafuta. Mimi niiombe Serikali itoe kauli kwa Wakuu wa Mikoa wote ambao maeneo yao yanapakana na nchi za Jirani, wananchi wana-advantage ya kuishi maeneo ya mpakani waruhusiwe kwenda kufuata bidhaa nje kwa bei nafuu, hawa siyo walanguzi! Mtu akienda akichukua kilo kumi kwa sababu anachukua kilo kumi au ishirini kwa sababu hataki kwenda kila siku kununua sukari, kwa hiyo anachukua nyingi ili haifadhi na anamchukulia na jirani yake, lakini sasa tukisema kila mtu anayekwenda kufuata vitu vya bei nafuu ni walanguzi hii tutakuwa hatuwatendei sawa wananchi wanaoishi mipakani. Naomba Mheshimiwa Waziri uliangalie kwa sababu Nishati ya Mafuta imepanda na imesababisha vitu vingi kupanda. Kwa hiyo, niombe hili suala ambalo jingine ambalo wananchi tunaoishi maeneo ya mpakani tunahitaji kuwa na hiyo advantage. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo Mheshimiwa Waziri mimi nitaunga mkono hoja pale nitakapopata maelezo ya kutosha kwa nini tunawapa kichwa hawa Wakandarasi na sababu zao ambazo hazina msingi za kutuambia kwamba vifaa vya REA vimepanda wakati havijapanda na vyote vinapatikana hapa nchini. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Kusema kweli ninaongea kwa uchungu sana kwa sisi watu wa Mkoa wa Songwe na kwa ujumla na mikoa hii ya kusini. Kiuhalisia niungane na Mbunge wa Newala ambaye ameongea kwa uchungu sana na ninashangaa kuona hata Wabunge wenzangu sijui mnaogopa nini kuongea ukweli katika hili jambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge wa Mikoa hii ya Mbeya, Songwe, Liwale, Lindi tukiuliza hii barabara tunaambiwa barabara zenu zitajengwa kadri fedha zitakavyopatikana. Tukiuliza barabara, tunaambiwa barabara zenu Serikali inaendelea kutafuta fedha, lakini kuna baadhi ya mikoa hayo majibu hawayapati, wanaambiwa Mkandarasi amechelewa, barabara zenu hela ziko tayari, inakwenda kujengwa siku fulani. Sasa mimi nataka Waziri atuambie kuna kigezo gani mnatumia kugawa hizi fedha kwenye mikoa? Kwa nini mikoa mingine Wabunge tunapewa majibu kama haya? Hata sisi tunalipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya mambo ambayo amenifurahisha Mheshimiwa Rais Mama Samia, ni juzi alipofuta Sherehe za Muungano. Kwa mara ya kwanza aliamua kuzigawa zile hela za Muungano pasu kwa pasu; Bara na Visiwani. Sasa ninyi wasaidizi wake mjifunze kwamba hii keki ya Taifa hata mikoa yote igawanywe sawa. Ameshawapa somo! Sisi kwetu hii barabara ya Mloo - Utambalila mpaka Kamsamba upembuzi yakinifu uko tayari, usanifu wa kina uko tayari, nyaraka za tenda ziko tayari, lakini miaka yote kutenga fedha tenda itangazwe tunapigwa dana dana, lakini mikoa mingine barabara inatengewa usanifu wa kina, inatengenezwa kwa haraka kabisa. Hii siyo sawa mimi sioni kama sisi tunatendewa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hili naomba Waheshimiwa Wabunge tuungane, hii keki ya Taifa tugawane sawa mikoa yote. Hata huko nako kuna Watanzania. Kwako pale, kuna barabara ile ya Mbeya mpaka Tunduma tumeambiwa itajengwa njia nne za pembeni; ni stori tu, hakuna. Tusipoangalia mpaka 2025 haitajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge ambao mikoa yetu haipewi kipaumbele katika hii bajeti, tuungane tuhakikishe tunambana Waziri atuambie aje na majibu halisi, kwa sababu kule nako kuna Watanzania.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa. Nataka kumwongezea kaka yangu George anayeongea hapa…

NAIBU SPIKA: Subiri kwanza, huongei kabla hujatambuliwa na Kiti. Haya sasa unaweza kusimama. Mheshimiwa Condester Sichalwe.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. nataka kumwongezea taarifa Mheshimiwa

Mbunge wa Jimbo la Mbozi kwamba barabara pia anayoiongelea ya Mloo – Kamsamba – Chitete - Utambalila yenye kilometa 145.14 ni miongoni mwa barabara ya kimkakati kabisa katika mkoa wetu wa Songwe. Kwa hiyo, tunashangaa ni kwa nini Serikali haijatuingizia kwenye bajeti?

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni miongoni mwa barabara ambayo itatusaidia kuinua kipato sana kwenye mkoa wetu wa Songwe na ukitegemea ndiyo barabara ambayo inatoa mazao kupeleka nchi za jirani na kusambaza mkoa wote wa Songwe na sehemu nyingine.

NAIBU SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa. Mheshimwa George Mwenisongole unapokea taarifa hiyo?

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kichwa na miguu na mikono naipokea hii taarifa. Hii barabara ndiyo uhai wa mkoa wetu. Kahawa yote inayolimwa Mbozi inapita kwenye hii barabara. Mchele wote, mpunga wote wa Kamsamba unapita kwenye hii barabara na ni kiunganishi kati ya mkoa wetu, Mkoa wa Katavi mpaka Tabora. Kama hii barabara itawekewa lami, malori hayana haja ya kupita Iringa kwenda Dodoma au Tabora, yote yatakuwa yanapita njia ya huku.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nashindwa kuelewa, kila kitu kiko tayari; nyaraka za tender ziko tayari, usanifu wa kina uko tayari, upembuzi yakinifu uko tayari, shida nini Mheshimiwa Waziri kututengea fedha? Kwa kweli tunahitaji majibu katika hili suala.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kusema hayo, mimi nikushukuru sana. Niungane na Mbunge wa Newala aliyesema anaunga hoja mkono kwa shingo upande, tusubiri majibu ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Nianze mchango wangu kwenye hii Wizara kwa kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, nimeingiwa na hofu sana baada ya kuisoma hii bajeti. Nimeingiwa na hofu kwa sababu hii ni bajeti ya kwanza tangu tutoke kuinadi Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2020 kwenye Uchaguzi ambao ulitupa ushindi wa kishindo sana kutoka kwa wananchi. Tuliwajaza matumaini makubwa sana wakulima na Watanzania masikini waishio vijijini kuhusu bei za mbolea na uhakika wa masoko; lakini katika hii bajeti ambayo nimeisoma zaidi ya mara tatu, sijaona hata mstari mmoja ambao unasisitiza kwamba Serikali itaweka mkazo kupunguza bei za mazao ya mahindi au kahawa. Sijaona mkazo wowote katika hii bajeti kuelezea uhakika wa soko la mahindi.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi kule kwetu Mbozi, debe la mahindi ni shilingi 3,000/=, gunia ni shilingi 18,000/= lakini mfuko wa mbolea ni shilingi 70,000/=. Sasa unategemea hawa wakulima ambao tumetoka tu kwenye uchaguzi wakatupa kura, watatuelewa vipi? Tunarudi tena mtaani hakuna solution ya bei za mbolea! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kati ya vitu ambavyo Bunge hili linaweza kufanya ni kuishinikiza Serikali at least kutoa bei elekezi za mbolea. Shilingi 70,000/= kwa mfuko wa mbolea ni kubwa mno, huwezi kulia eka. Tutakuwa hatuwatendei haki wakulima masikini ambao wametuamini wakatupa kura zao, lakini miezi sita baadaye, Bajeti ya Kilimo ambayo walikuwa wakiisubiri, haina majibu ya matatizo yao. Kwa kweli hili ni suala ambalo ni lazima Mheshimiwa Waziri aliingilie na kulitilia mkazo sana kuhakikisha bei ya mbolea na uhakika wa haya masoko unakwenda kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine, nimpe pole Mheshimiwa Waziri, kwa sababu kama Wabunge wenzangu walivyoongea, uzoefu unaonyesha fedha za bajeti ya maendeleo zinatengwa nyingi, lakini zinazokuja ni chache. Sasa sijui kuna miujiza gani ya hizo baiskeli na pikipiki alizowaahidi Maafisa Ugani? Sijui atazipata vipi wakati fedha za maendeleo hazipati? Sijui atajigawa vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli hili ni suala ambalo kama kuna kitu ambacho Bunge hili linaweza kufanya, shilingi bilioni 200 ambazo ni bajeti nzima ya hii Wizara, ni hela ndogo sana kwa Serikali ambayo inakusanya zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwezi. Sasa kuna ugumu gani kupeleka hizo hela zote? Kwa nini kila mwaka hii Wizara hela inazoomba kwa maendeleo huwa hazikidhi vigezo vyao? Kwa nini hawapelekewi hela zao zote wanazoomba? What is billioni 200 kwa hii Serikali ambayo inakusanya zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwezi? Kwa nini wasipelekewe zote? Ugumu uko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima tuje na jawabu kuhakikisha hii bajeti, fedha zote walizoomba wanapelekewa kama kweli tuna nia ya kutaka kumsaidia mkulima masikini wa kule kijijini.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, nataka niongelee hivi vyama vya msingi, AMCOS. Ni kweli kabisa kwamba vyama vya AMCOS ni Sera ya CCM na vilikuja kwa nia nzuri ya kutaka kumsaidia mkulima, especially wa kahawa kule kwetu Mbozi. Kwetu Mbozi hivi vyama vya ushirika vimegeuka kuwa kaburi kwa wakulima. Kwanza vinachukua mikopo benki bila wanachama wao kujua, unapofika wakati wa malipo, benki inakuja inakata hela zao na kuwafanya wakulima wale masikini kushindwa kupata malipo yao.

Mheshimiwa Spika, mpaka dakika hii ninapoongea hapa ndani ya Bunge lako Tukufu, kuna AMCOS zaidi ya tisa ndani ya Wilaya ya Mbozi hazijalipa wakulima wao. Watu wameshindwa kupeleka watoto wao shule, wameshindwa kulima, wametiwa umasikini wa ajabu na Serikali ipo, inaona.

Mheshimiwa Spika, siku moja nilishangaa hapa, posho zetu sisi Wabunge zilichelewa kwa siku mbili tatu, kulikuwa hakukaliki humu ndani. (Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge)

Mheshimiwa Spika, lakini wakulima wangu mimi Mbozi hawajalipwa mwaka sasa fedha zao za AMCOS na hakuna anayeshtuka.

SPIKA: Mheshimiwa Mwenisongole, hapo unamchokoza Spika. Unajaribu kuonesha kama kuna inefficiency hapa ndani, kitu ambacho siyo kweli. Futa hiyo kauli yako.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, okay, nafuta, lakini msisitizo wangu…

SPIKA: Hakuna cha lakini, unafuta halafu unaendelea kuchangia.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, okay, nafuta.

SPIKA: Eeh, endelea.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, point yangu ninayotaka kusema ni kwamba, suala hili la wakulima wa AMCOS kutokulipwa, nataka nitilie mkazo, kwa sababu hawa ni watu ambao wamepeleka mazao yao, wamepima, lakini mpaka leo hii hawajalipwa. Katika hali hiyo, suala hili hatuwezi kumsaidia yule mkulima.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, ninachoomba ni kwamba utakapokuja kuhitimisha bajeti, uje na majibu ya kuhakikisha kwa nini hawa AMCOS mpaka sasa hivi bado hawajalipa fedha zao?

Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi muhimu sana ya kuchangia taarifa hizi za Kamati hizi tatu PAC, PIC na LAAC.

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujaalia afya na siku njema lakini kipekee niwashukuru sana Wabunge wenzangu. Nirudie tena; kipekee niwashukuru sana Wabunge wenzangu ambao kwa kweli kwa hizi siku mbili nimelala vizuri. Mimi sikuweza kutathmini wingi wa Wabunge ambao wamejitokeza kuongea kwa hisia kuhusu kupinga ufisadi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Biblia, Eliya siku moja alilalamika kwa Mungu kwamba yuko peke yake ambaye haabudu sanamu lakini Mungu alimwambia hauko peke yako wako zaidi ya 7,000. Na leo nimetambua ndani ya hili Bunge kumbe kuna watu 7,000 ambao tunapinga kwa dhati ubadhirifu, ufisadi na wizi. Kwa kweli Wabunge najisikia fahari sana kuwa sehemu ya hili Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze mchango wangu kwa kueleza masikitiko. Mwaka jana Bunge hili lilitoa Maazimio lakini leo ni asilimia 47 tu ya Maazimio yaliyoazimiwa na Bunge kwenye taarifa hii ya CAG yametekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mwaka huu tunakwenda tena kutoa maazimio wakati tuna asilimia 50 ya maazimio tuliyotoa mwaka jana hayajatekelezwa. Kwa mfano, Wabunge wenzangu niwarudishe nyuma, kuna hii Kampuni ya KADCO ambayo ilianzishwa na watu binafsi wawili kwa kushirikiana na Serikali kwa ajili ya kuendesha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa KIA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2009 Baraza la Mawaziri lilitoa agizo kwamba hisa zote za KADCO zinunuliwe na zikanunuliwa kwa thamani ya Dola za Kimarekani milioni tano, karibu bilioni sita za Tanzania, lakini mpaka leo uwanja huo bado haujarudi na KADCO wanaendelea kuuendesha licha ya maagizo ya Bunge hili tuliagiza mwaka jana. Nashukuru Mungu Waziri wa mwaka jana bado anaendelea na nafasi yake, bado anaendelea na hiyo nafasi yake na Bunge liliagiza na yeye akatuahidi kwamba, muda siyo mrefu TAA itachukua Uwanja wa Ndege wa KIA na kuundesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nimhoji Mheshimiwa Waziri hivi nani yuko nyuma ya KADCO? Hili ni lazima Wabunge tusiliache, tunataka tumjue nani yupo nyuma ya KADCO ambaye anakiuka maagizo ya hili Bunge na Serikali inaogopa kuurudisha ule uwanja ambao tayari ilishaununua na kulipa hisa zake. Hivi kweli Wabunge tufumbie macho na hilo? Tufumbie macho na hilo? hivi Watanzania watatuelewaje? Leo tena tutoe agizo lingine kusema Uwanja wa Ndege wa KIA urudishwe Serikalini wakati tayari maagizo yalishatolewa na hela ilishalipwa. Hivi tunaipeleka wapi nchi hii na nani huyo ambaye anamiliki hiyo KADCO mpaka ana kiburi cha kukataa Maazimio rasmi ya Bunge, Serikali na Baraza la Mawaziri ambayo vyote viliagiza?... (Makofi)

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa naomba taarifa yako iwe ya afya maana yake nahutubia Taifa…

SPIKA: Mheshimiwa George Mwenisongole, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest…

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa naomba taarifa yako iwe na afya maana yake nahutubia Taifa hapa. (Kicheko)

TAARIFA

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba, hiyo KADCO inayoendesha Uwanja wa Ndege wa KIA, inaendesha bila hata Mkataba, kinyume na Sheria za Nchi na bado inaendesha huo uwanja na siyo hiyo tu bado imeisababishia Serikali hasara ya kutosha…

SPIKA: Mheshimiwa taarifa ni moja…

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo taarifa yangu.

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa George Mwenisongole unaipokea taarifa hiyo?

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, kwa kichwa, mikono na miguu naipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli kama hili Bunge litashindwa kuchukua hatua kuhusu KADCO, hakuna maana basi ya Taarifa ya CAG kuletwa Bungeni, hakuna maana. Hili liko dhahiri kabisa, liko dhahiri kabisa na hata tukisema kwamba, Mheshimiwa Waziri ambaye alituhaidi kwamba KADCO itarudishwa Serikalini mpaka sasa hivi bado yupo kwenye nafasi yake kwa kweli mimi nashindwa kuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge, tumetumia hizi siku mbili kulalamika, lakini niwaulize Sheria za Nchi anatunga nani, si sisi? Naomba tufanye maamuzi magumu na nikushukuru Mheshimiwa Maganga, naomba uingize jina langu katika orodha ya Wabunge wanaotaka Sheria ya Watu Kunyongwa wanaofanya ufisadi, George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, hakikisha unaandika jina langu leo, sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa sababu sisi ndiyo tunatunga sheria, naomba kabla ya Bunge hili kwisha tujitolee Wabunge tulete Muswada binafsi kwamba, taarifa ya CAG inapotoka tutunge sheria Serikali ilete taarifa ya utekelezaji wa Maagizo ya CAG na Maamuzi ya Kamati na Maazimio ya Wabunge ndani ya miezi mitatu baada ya taarifa ile kutoka. Kama Serikali haitaleta maazimio ya kuonesha utekelezaji wa hizi taarifa tutakuwa tunafanya kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, naomba Wabunge mniunge mkono na Watanzania wote wananisikia. Naomba tutoe azimio wezi wote wa kuku, wezi wote waliopora simu waachiwe. Kama hatuwezi kuwafunga watu wanaoibia ushirika, kama hatuwezi kuwafunga Wakurugenzi wanaotafuna fedha, kama hawa watu wa KADCO wanaiibia Serikali mchana kweupe hatuwezi kuwafunga, kwa nini tuwaonee wezi wa kuku? Kwa nini tuwaonee hawa wezi, hawa wezi tuwaachie. Kuna sababu gani ya kuwakamata watu wa hao wezi, wakati majizi makubwa wanaoitia hasara Serikali wanaachia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili Bunge litaingia katika historia kati ya Mabunge bora duniani kama tutatoa azimio la kuwaachia wezi wote wa kuku. Hakuna sababu ya kuwaweka ndani wakati wezi wakubwa tunashindwa kuwachukulia hatua, kuna maana gani basi ya sisi kuwa Wabunge? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tumechoka, kule kwetu Mbozi kinachoendelea ni vichekesho, kinachoendelea ni vichekesho. Watu wamekamatwa, Viongozi wa Vyama vya AMCOS wamekatwa na wamekiri kwamba wameiba hela, eti wameambiwa rudisheni hela halafu wakaachiwa. Waliyofikishwa Mahakamani ni wale ambao waligoma kurudisha hela hivi kweli mtu ameiba, amekiri…

MHE. ALLY M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: …kwamba ameiba halafu wanawaachia, hivi hii nchi tunaipeleka wapi?

SPIKA: Mheshimiwa George Mwenisongole, kuna taarifa kutoka Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, nimesema taarifa naomba iwe ina afya maana yake nahutubia Taifa. (Kicheko)

TAARIFA

MHE. ALLY M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hata Kyela ni hivyo hivyo kwenye AMCOS, watu wameiba pesa lakini wanasema zichangwe kokoa ndiyo zilipe wakati aliyeiba yupo anaonekana.

MHE GEORGE R. MWENISONGOLE: Lakini…

SPIKA: Mheshimiwa George Mwenisongole muda wako ulikuwa umeisha, sekunde thelathini malizia.

MHE GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu. Niliomba ukaguzi maalum wa CAG na CAG ametoa taarifa yake. Nimemkabidhi Mheshimiwa Waziri Mkuu, ameniahidi ndani ya wiki mbili anakuja Mbozi.

Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru Waziri wa Kilimo ambaye alileta timu ya wakaguzi kule Mbozi, imeifanyia kazi na naamini Mheshimiwa Bashe ataongozana na Mheshimiwa Waziri Mkuu anapokuja Mbozi ndani ya wiki mbili tunataka tufanye mfano, tunataka tufanye Mbozi iwe pilot study, sisi hatutaki ufisadi Mbozi…

SPIKA: Haya ahsante sana…

MHE GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi muhimu sana ya kuchangia taarifa hizi za Kamati hizi tatu PAC, PIC na LAAC.

Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujaalia afya na siku njema lakini kipekee niwashukuru sana Wabunge wenzangu. Nirudie tena; kipekee niwashukuru sana Wabunge wenzangu ambao kwa kweli kwa hizi siku mbili nimelala vizuri. Mimi sikuweza kutathmini wingi wa Wabunge ambao wamejitokeza kuongea kwa hisia kuhusu kupinga ufisadi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Biblia, Eliya siku moja alilalamika kwa Mungu kwamba yuko peke yake ambaye haabudu sanamu lakini Mungu alimwambia hauko peke yako wako zaidi ya 7,000. Na leo nimetambua ndani ya hili Bunge kumbe kuna watu 7,000 ambao tunapinga kwa dhati ubadhirifu, ufisadi na wizi. Kwa kweli Wabunge najisikia fahari sana kuwa sehemu ya hili Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze mchango wangu kwa kueleza masikitiko. Mwaka jana Bunge hili lilitoa Maazimio lakini leo ni asilimia 47 tu ya Maazimio yaliyoazimiwa na Bunge kwenye taarifa hii ya CAG yametekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mwaka huu tunakwenda tena kutoa maazimio wakati tuna asilimia 50 ya maazimio tuliyotoa mwaka jana hayajatekelezwa. Kwa mfano, Wabunge wenzangu niwarudishe nyuma, kuna hii Kampuni ya KADCO ambayo ilianzishwa na watu binafsi wawili kwa kushirikiana na Serikali kwa ajili ya kuendesha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa KIA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2009 Baraza la Mawaziri lilitoa agizo kwamba hisa zote za KADCO zinunuliwe na zikanunuliwa kwa thamani ya Dola za Kimarekani milioni tano, karibu bilioni sita za Tanzania, lakini mpaka leo uwanja huo bado haujarudi na KADCO wanaendelea kuuendesha licha ya maagizo ya Bunge hili tuliagiza mwaka jana. Nashukuru Mungu Waziri wa mwaka jana bado anaendelea na nafasi yake, bado anaendelea na hiyo nafasi yake na Bunge liliagiza na yeye akatuahidi kwamba, muda siyo mrefu TAA itachukua Uwanja wa Ndege wa KIA na kuundesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nimhoji Mheshimiwa Waziri hivi nani yuko nyuma ya KADCO? Hili ni lazima Wabunge tusiliache, tunataka tumjue nani yupo nyuma ya KADCO ambaye anakiuka maagizo ya hili Bunge na Serikali inaogopa kuurudisha ule uwanja ambao tayari ilishaununua na kulipa hisa zake. Hivi kweli Wabunge tufumbie macho na hilo? Tufumbie macho na hilo? hivi Watanzania watatuelewaje? Leo tena tutoe agizo lingine kusema Uwanja wa Ndege wa KIA urudishwe Serikalini wakati tayari maagizo yalishatolewa na hela ilishalipwa. Hivi tunaipeleka wapi nchi hii na nani huyo ambaye anamiliki hiyo KADCO mpaka ana kiburi cha kukataa Maazimio rasmi ya Bunge, Serikali na Baraza la Mawaziri ambayo vyote viliagiza?... (Makofi)

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa naomba taarifa yako iwe ya afya maana yake nahutubia Taifa…

SPIKA: Mheshimiwa George Mwenisongole, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Anatropia Lwehikila Theonest…

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa naomba taarifa yako iwe na afya maana yake nahutubia Taifa hapa. (Kicheko)

TAARIFA

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba, hiyo KADCO inayoendesha Uwanja wa Ndege wa KIA, inaendesha bila hata Mkataba, kinyume na Sheria za Nchi na bado inaendesha huo uwanja na siyo hiyo tu bado imeisababishia Serikali hasara ya kutosha…

SPIKA: Mheshimiwa taarifa ni moja…

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo taarifa yangu.

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa George Mwenisongole unaipokea taarifa hiyo?

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, kwa kichwa, mikono na miguu naipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli kama hili Bunge litashindwa kuchukua hatua kuhusu KADCO, hakuna maana basi ya Taarifa ya CAG kuletwa Bungeni, hakuna maana. Hili liko dhahiri kabisa, liko dhahiri kabisa na hata tukisema kwamba, Mheshimiwa Waziri ambaye alituhaidi kwamba KADCO itarudishwa Serikalini mpaka sasa hivi bado yupo kwenye nafasi yake kwa kweli mimi nashindwa kuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge, tumetumia hizi siku mbili kulalamika, lakini niwaulize Sheria za Nchi anatunga nani, si sisi? Naomba tufanye maamuzi magumu na nikushukuru Mheshimiwa Maganga, naomba uingize jina langu katika orodha ya Wabunge wanaotaka Sheria ya Watu Kunyongwa wanaofanya ufisadi, George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, hakikisha unaandika jina langu leo, sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa sababu sisi ndiyo tunatunga sheria, naomba kabla ya Bunge hili kwisha tujitolee Wabunge tulete Muswada binafsi kwamba, taarifa ya CAG inapotoka tutunge sheria Serikali ilete taarifa ya utekelezaji wa Maagizo ya CAG na Maamuzi ya Kamati na Maazimio ya Wabunge ndani ya miezi mitatu baada ya taarifa ile kutoka. Kama Serikali haitaleta maazimio ya kuonesha utekelezaji wa hizi taarifa tutakuwa tunafanya kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, naomba Wabunge mniunge mkono na Watanzania wote wananisikia. Naomba tutoe azimio wezi wote wa kuku, wezi wote waliopora simu waachiwe. Kama hatuwezi kuwafunga watu wanaoibia ushirika, kama hatuwezi kuwafunga Wakurugenzi wanaotafuna fedha, kama hawa watu wa KADCO wanaiibia Serikali mchana kweupe hatuwezi kuwafunga, kwa nini tuwaonee wezi wa kuku? Kwa nini tuwaonee hawa wezi, hawa wezi tuwaachie. Kuna sababu gani ya kuwakamata watu wa hao wezi, wakati majizi makubwa wanaoitia hasara Serikali wanaachia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili Bunge litaingia katika historia kati ya Mabunge bora duniani kama tutatoa azimio la kuwaachia wezi wote wa kuku. Hakuna sababu ya kuwaweka ndani wakati wezi wakubwa tunashindwa kuwachukulia hatua, kuna maana gani basi ya sisi kuwa Wabunge? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tumechoka, kule kwetu Mbozi kinachoendelea ni vichekesho, kinachoendelea ni vichekesho. Watu wamekamatwa, Viongozi wa Vyama vya AMCOS wamekatwa na wamekiri kwamba wameiba hela, eti wameambiwa rudisheni hela halafu wakaachiwa. Waliyofikishwa Mahakamani ni wale ambao waligoma kurudisha hela hivi kweli mtu ameiba, amekiri…

MHE. ALLY M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: …kwamba ameiba halafu wanawaachia, hivi hii nchi tunaipeleka wapi?

SPIKA: Mheshimiwa George Mwenisongole, kuna taarifa kutoka Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, nimesema taarifa naomba iwe ina afya maana yake nahutubia Taifa. (Kicheko)

TAARIFA

MHE. ALLY M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba hata Kyela ni hivyo hivyo kwenye AMCOS, watu wameiba pesa lakini wanasema zichangwe kokoa ndiyo zilipe wakati aliyeiba yupo anaonekana.

MHE GEORGE R. MWENISONGOLE: Lakini…

SPIKA: Mheshimiwa George Mwenisongole muda wako ulikuwa umeisha, sekunde thelathini malizia.

MHE GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu. Niliomba ukaguzi maalum wa CAG na CAG ametoa taarifa yake. Nimemkabidhi Mheshimiwa Waziri Mkuu, ameniahidi ndani ya wiki mbili anakuja Mbozi.

Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru Waziri wa Kilimo ambaye alileta timu ya wakaguzi kule Mbozi, imeifanyia kazi na naamini Mheshimiwa Bashe ataongozana na Mheshimiwa Waziri Mkuu anapokuja Mbozi ndani ya wiki mbili tunataka tufanye mfano, tunataka tufanye Mbozi iwe pilot study, sisi hatutaki ufisadi Mbozi…

SPIKA: Haya ahsante sana…

MHE GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii muhimu kwa wananchi wangu wa Jimbo la Mbozi. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa nafasi ya kusimama kwenye hili Bunge Tukufu kuchangia bajeti ya Wizara ya Kilimo. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa ruzuku aliyotoa kwa wakulima wa Mbozi na nchi nzima. Kusema ule ukweli isingelikuwa ruzuku ile sijui tungeficha wapi sura zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nimpongeze Mheshimiwa Bashe, Naibu wake na Maafisa wote wa Wizara wakiongozwa na Katibu Mkuu kwa kazi nzuri na utendaji mzuri wa kazi wanaofanya. Kipekee nimpongeze Kaka yangu Bashe kwa maamuzi ya kuwafungia wale mawakala wa mbolea. Kwa kweli vitu alivyofanya ni sahihi ingawa kuna baadhi ya watu wachache wanajaribu kumtikisa, mimi nasema akaze buti. Hatuwezi kuwavumilia mawakala wasio waaminifu, ambao wanashindwa kufuata taratibu na kanuni tulizoweka. Wako mawakala wengi nje ambao wanataka kuwemo katika huo mfumo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kueleza masikitiko makubwa kwa wakulima wangu wa kahawa wa Mbozi. Hivi tunavyozungumza huu mwezi Mei, kuna baadhi ya wakulima mpaka leo hawajalipwa kahawa waliyopeleka mwaka jana mwezi Julai, ile waliovuna. Shida hii ya wakulima wa kahawa Mheshimiwa Waziri anaifahamu. Amekuja Mbozi, Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuja Mbozi, matatizo yaliyoko kwenye vyama vile vya msingi vya AMCOS ni makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hapa hata malaika ashuke mbinguni aje kuongoza vile vyama bado wataiba tu na sielewi kwa nini Serikali inaona hivi vyama vya ushirika kama vile ni msahafu ambao hauwezi kubadilishwa. Kwani kuna ugumu gani kuleta soko huru, kuwaruhusu wanunuzi binafsi nao wachangie. Kuna ugumu gani kuwaruhusu wanunuzi binafsi kama vile ilivyo kwenye mchele au kwenye mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo vyama vya ushirika viwepo, lakini na wanunuzi binafsi wawepo. Kwa sababu ukiangalia, mkulima anapovuna kahawa yake anapeleka kwenye hivi Vyama vya Msingi vya Ushirika kuna makato yasiyo na kichwa wala miguu ambayo yamejaa pale. Sijui kuna makato ya gunia, sijui hela ya viburudisho, sijui hivi, kila aina ya takataka. Ikitoka pale kahawa inachukuliwa na hivi vyama vya AMCOS, inapelekwa kiwandani, bado kule nako kuna makato mengi. Sasa haiingii akilini kwa Serikali kuwalazimisha wakulima wapeleke kahawa yao kwenye hivi vyama vya msingi wakati huko kuna makato mengi yasiyo na kichwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa ambacho kinaumiza viongozi wengi wa vyama vya ushirika ni wezi. Tuna ushahidi wa kila kona, kesi ngapi ziko Mahakamani kuhusu viongozi wa vyama vya ushirika? Mheshimiwa Bashe mwenyewe ameleta timu Mbozi wamekagua, madudu waliyoyakuta yamefika ofisini kwa Waziri. Yanatisha na huo ukaguzi umefanyika kwenye vyama 20 tu vya AMCOS na kwenye kata nane. Sasa je angefanya kata zote 29 na vyama zaidi ya 100 ingekuwaje? Nimwombe Mheshimiwa Waziri sielewi kwa nini Serikali inaogopa kuruhusu soko huru la kahawa, kwa sababu vyama vya ushirika vime-prove failure kila kona. Hakuna justification hata mmoja ya kusema hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio huu ni mfumo mzuri wa wakulima kulinda masoko, lakini una makato mengi na wizi na Serikali imeshindwa kutatua hilo tatizo. Wakati umefika sasa wa kuwepo kwa serious debate ya kuhusu soko huru kwenye kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kuna hii tozo ya shilingi 200 ambayo wakulima wa arabika nchini wanatozwa na Bodi ya Kahawa. Bodi ya Kahawa wanatuambia hii ni kwa ajlili ya kuendeleza zao la kahawa. Nataka niwaulize Bodi ya Kahawa lini wameendeleza Bodi ya Kahawa? Wamemsaidia vipi mkulima wa kahawa Tanzania waseme. Kwenye kata zote za kahawa za Mbozi hawajawahi toa msaada wa aina yoyote wa kusema wanasaidia. Sasa logic ya kuchukua hii shilingi 200 ya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa robusta wanalipa shilingi 100 na sababu kubwa ni kwamba wameamua Taasisi ya Utafiti wa TaCRI na hii Bodi ijiendeshe yenyewe, iendeshwe na wadau kitu ambacho sio sahihi. Mbona TARI wanawatengea bilioni 40 za utafiti, kwa nini na TaCRI nao basi wasiwatengee fedha au bajeti kubwa. Ndio maana wanakuja na hizi idea ambazo hazina mashiko za kuchukua shilingi 200. Sasa wewe zidisha tani 80,000 zinazozalishwa za kahawa zidisha mara mia shilingi 200 ni shilingi ngapi, sio chini ya bilioni 16, za nini zote hizo? Utafiti gani wanaoufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni jamaa yangu, lakini nahitaji maelezo ya kutosha kuhusu hii shilingi 200 ambayo wakulima wa arabika wanatozwa nchini bila sababu yoyote ya msingi. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, kesho atakapokuja kuhitimisha hotuba yake naomba yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza, ili kuondoa kwa wakulima walioko Mbinga na walioko Mbozi ambao wanatulazimisha tupeleke kahawa yetu kwenye hivi vyama vyao vya AMCOS ambako huko kumejaa wezi na makato yasiyo na tija, ninachoomba kahawa inapofikishwa pale kwa AMCOS, mkulima apewe hela yake. Mambo ya kumcheleweshea mkulima aje asubiri sijui miezi, sijui iende huku, kikaenda kikarudi, huko ni kuwaonea wakulima na hakuna tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine hii Taasisi ya TaCRI ambayo inafanya kazi nzuri, lakini wameacha iendeshwe na wadau wa kahawa. Huko ni kumtelekeza mtoto uliyemzaa, kwa sababu TaCRI haina tofauti na TARI, majukumu yake. TARI wanawatengea bilioni 40, TaCRI kwa nini hawataki kuwapa hela na wanategemea watajiendesha vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, tuna hili suala la farm gate price ambao Bodi ya Kahawa ilikuwa inapaswa ku- meditate hii farm gate price, lakini kwa kipindi cha miaka mitatu tangu walipo-review hawajatoa hiyo hela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake mwaka jana Halmashauri ya Mbozi ililazimika kukaa na viongozi wa hivi vyama vya AMCOS kupanga ushuru wa kahawa ambao halmashauri itachukua, kitu ambacho sio sahihi. Hii inafanya Bodi inakwepa majukumu yake. Kwa hiyo imekuwa kwa Mbozi kazi ya Bodi ni kukusanya tu shilingi 200, lakini majukumu mengine inakwepa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa, nataka aje majibu rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa ile timu ambayo iliituma Mbozi na najua imeleta majibu ya ukweli. Naomba wale wote ambao wametajwa kwenye hiyo ripoti wachukuliwe hatua kali za kisheria.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mwenisongole muda wako umekwisha.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaunga hoja baada ya kupata majibu yangu. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii muhimu ya wananchi na wakulima wetu. Kwanza nianze kabisa kwa kumpongeza na kumshukuru sana Rais wetu, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuongeza bajeti hii ya kilimo kutoka Shilingi bilioni 294 mpaka Shilingi bilioni 751. Kwa kweli huu ni ushindi mkubwa sana kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kitu kimoja ambacho nataka Wabunge wenzangu tukione na kama tunaweza kusaidia kubadilisha. Mwaka jana bajeti ilikuwa Shilingi bilioni 294 na katika hizo fedha za maendeleo zilizochangiwa kwenye hiyo bajeti zilikuwa Shilingi bilioni 164, lakini ni asilimia 46 tu ya bajeti nzima ya maendeleo iliyotoka Serikalini kwenda kwenye Wizara ya Kilimo. Sasa mwaka huu bajeti imepanda zaidi imekuwa Shilingi 751 bilioni, na katika hizo bajeti zaidi ya Shilingi bilioni 630 zinakwenda kwenye maendeleo kwa mafungu yote mawili 43 na 05. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali la kuuliza. Je, hizo fedha zitatoka? Kwa sababu kupanga bajeti na hela kutoka ni vitu viwili tofauti. Kama tutakaa hapa tutaongea hata kwa wiki nzima nakushauri hiki, nakushauri kifanyike hiki au kipi tunataka lakini kama Serikali haitatoa fedha za bajeti ya maendeleo kwenye hii Wizara ya Kilimo itakuwa ni kazi bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nimuombe Waziri wa Fedha aiangalie bajeti hii ya Wizara ya Kilimo kwa jicho la tatu. Au ikiwezekana sisi Wabunge tufunge angalau kwa wiki moja tumuombe Mwenyezi Mungu awaguse Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuhakikisha bajeti ya Wizara hii ya Fedha fedha zote zilizoombwa zinakwenda kama zilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tangu uhuru haijawahi kutokea bajeti ya Wizara ya Kilimo ikazidi Shilingi bilioni 300; lakini mwaka huu bajeti imekuwa mpaka Shilingi bilioni 751. Na kama Mungu akitujalia hii bajeti yote ikapita kama ilivyo na fedha zote zikaenda, mimi naamini nchi yetu ya Tanzania itakuwa imepiga mageuzi makubwa sana kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ina maana bajeti zote za ushirika zitafanya kazi, miradi yote ya maendeleo itapata fedha, kila kitu kilichoombewa kitakuwa na fedha, na kaka yangu Bashe nafikiri utaongezeka at least kilo 10. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine nafikiri imefika sasa tuwe na sheria ya kilimo. Huko vijijini watu wanauza mbegu feki. AMCOS nyingi hazilipi wakulima zinachukua mazao zinalima. Hawa watu hata wakikamatwa wakipelekwa mahakamani inageuka kuwa ni kesi za madai. Sasa mtu umemuuzia mtu mbegu feki, mtu umekopa fedha zake hujalipa mazao yake itakuwaje kesi ya madai? Mimi naomba hii iingizwe iwe kesi ya uhujumu uchumi. Na mimi naomba Mheshimiwa Waziri kama hutaleta muswada kwenye bajeti ya mwezi wa tisa hawa watu tu-criminalize basi mimi nitaleta muswada binafsi na ninaomba Wabunge wenzangu mniunge mkono hii iingizwe iwe sheria ya uhujumu uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani watu wawauzie wakulima mbegu feki, vyama vya ushirika visilipe mapato yao kwa wakulima alafu iwe ni kesi ya madai. Hichi kitu hakiwezekani tunawatia umasikini. Kwa hiyo, kuna umuhimu mkubwa wa hii sheria ya kilimo ije.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha mwisho; mimi natoka Mkoa wa Songwe. Sisi tunalima sana mahindi lakini mbegu zetu bora tunazotumia zinatoka Zambia. Sasa mimi naomba, na ambacho ninachoomba Wizara kama basi tunashindwa kuwaruhusu watu wetu waende Zambia kuchukua mbegu basi tufanye mpango hizo mbegu bora za Zambia zije zizalishwe hapa Tanzania. Kwani kuna ubaya gani hizo mbegu za Zambia zikija zikazalishwa hapa? Kwa sababu mbegu zilizopo Tanzania hazikubali kwenye mikoa yetu…

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa hii nafasi na mimi kuchangia kwenye hii Wizara muhimu sana katika maendeleo na ustawi wa nchi yetu. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma kwanza kwa anavyotujalia uhai na anavyoendelea kuibariki nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee nimshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyohangaika kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri kwamba anafahamu katika Tanzania kuna Mkoa unaitwa Mkoa wa Songwe? Labda nafikiri hajui katika huu mkoa kwa sababu nimesoma hotuba nzima ya Wizara hii ambayo Naibu wako naye anatoka kwenye huo huo mkoa. Tulichopewa sisi kule ni ahadi tu, lakini hakuna hata mradi mmoja wa barabara wa lami ambao utafanyika ndani ya huu mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri hivi mnavyokuwa mnapanga hizi barabara kujenga lami mnatumia kigezo gani kati ya Mikoa na Mikoa? Na kwanini Mkoa wa Songwe kila mwaka unarukwa? Kila wakati kila mwaka, mwaka jana wakati naingia hapa Bungeni niliuliza swali hili na mara nyingi nimeuliza sana barabara zetu, lakini ukiangalia Mkoa wa Mbeya na Mkoa wa Songwe inaachwa nyuma sana kwenye hizi bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nataka Mheshimiwa Waziri utakapokuja ku-windup hii hotuba yako utuambie vigezo gani vinatumika katika kuchagua barabara za kuwekewa lami. Maana yake sisi hatuelewi, sasa tusije tukaanza kuwa na fikra zingine ambazo ni za ajabu na siyo sahihi. Lakini mimi nataka nikufahamishe kule katika mkoa wetu wa Songwe ambao tunakukaribisha kwa hamu sana ambao ndio mkoa pekee bado haujautembelea, kuna barabara ya kutoka Mloo kwenda Makao Makuu ya Wilaya ya Momba, Chitete na kwenda mpaka Kamsamvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Mkoa wa Songwe hii ni barabara ya pili kwa ukubwa ukiacha hii barabara inayotoka Mbeya mpaka Tunduma. Barabara hii kilometa 145 upembuzi yakinifu umekwishakamilika, usanifu wa kina umekwishakamilika, ipo ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu cha Mapinduzi. Lakini ni ahadi ya Marais wote wa Awamu ya Tano na Awamu hii ya Sita kuhusu hiyo barabara. Lakini sasa hata kutengewa kiasi cha fedha hakuna, taratibu zote za tender zishakamilika. Kinachotakiwa ni kutengewa tu fedha, sasa shida nini Mheshimiwa Waziri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpunga wote unaolimwa kule Kamsamba hii ndiyo njia yake, na ile barabara ikifunguliwa ikijengwa kwa lami kutoka Mbozi mpaka Tabora itakuwa ni kilometa chini ya 700 tu, maana yake inakwenda mpaka Kiliamatundu kutoka pale unaenda Muze, Majiyamoto ushaingia Tabora, lakini sasa nashindwa kuelewa shida ni nini ambayo tunashindwa kutengewa hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukiacha hiyo barabara Mheshimiwa Waziri kuna barabara inayotoka Uyole inaanzia Igawa inakuja Uyole mpaka Tunduma, mwaka jana niliongea hapa na nilimwambia Naibu Spika kabla hajawa kuwa Spika; nikwamwambia hii wameweka kwenye bajeti ya mwaka huu lakini fedha haitatoka na kweli mwaka jana fedha haikutoka, mwaka huu mmeiingiza tena kwenye bajeti ya mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini mwaka huu vilevile fedha itatoka. Sasa Mheshimiwa Waziri shida nini? Sasa hivi ukitaka kutoka Tunduma kwenda mpaka Mbeya unatumia zaidi ya saa tatu; kwa sababu ukifika mahali unaambiwa simama, subiri nusu saa kwanza malori yapite. Unaenda tena unatembea kilometa kadhaa unaambiwa simama subiri kwanza nusu saa malori yapite. Sasa uchumi wa kwetu wa mikoa yetu hii miwili ya Mbeya na Songwe unadumaa kwa sababu ya hizi foleni ambazo hazina maana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Mbeya na Songwe wamesubiri vya kutosha hizi barabara ziwekewe lami zifanyiwe matengenezo na sielewi shida ni nini? Lakini tukiangalia vilevile ndani ya Mkoa wa Songwe katika bajeti ya TANROADS katika Mikoa yote Tanzania, Mkoa wetu wa Songwe ndiyo unaoongoza kupata bajeti ndogo ya TANROADS na sijui shida ni nini Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndio maana nimeuliza vigezo gani vinatumika kugawa hii keki ya Taifa kwa hii mikoa? Na hata ukiangalia bajeti inayotoka kwenye hizi fedha kwa Hazina mwaka huu tumetengewa shilingi milioni 100 tu. Sasa shilingi milioni 100 utakarabati nini kwenye barabara yenye urefu wa kilometa 145? (Makofi)

Mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri tunajua sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tunaowajibu kwa chama chetu na tunawajibu kwa Serikali kupitisha bajeti, lakini hiki kinachoendelea siyo sawa na kuna kipindi itafika mpaka uvumilivu sisi utatushinda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena itafika mahali uvumilivu sisi utatushinda kwa sababu hata kule sisi tunahitaji lami. Inanitia uchungu sana hii barabara ya kutoka kila siku ninaporudi Jimboni kwangu napita hii barabara ya Mtera hii, imewekewa lami sasa hivi inakwanguliwa tena, basi tupeni hata hiyo lami iliyokwanguliwa kwenye hiyo barabara mtupe sisi tuwekewe kule, kuna shida gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanawekewa lami baadae zinatolewa lami, zinakwanguliwa sisi hata hiyo lami iliyokwanguliwa hatuna. Mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri tunaomba sana wananchi wa Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Mbeya barabara zetu nazo zina thamani sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Hoja ya Kuazimia Kuwahamisha Maafisa Ushirika katika Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Maafisa Ugani chini ya Wizara ya Kilimo
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuja kuhitimisha hoja yangu. Moja ya urithi alioniachia marehemu baba yangu Askofu Mwenisongole alioniachia ni kusema ukweli hata kama huo ukweli unakuathiri. Leo hii tunaweza tukajibu hoja hii kwa ushabiki na tunaweza tukatoa hii hoja kama hatuoni tatizo lakini ukweli utabaki kama ukweli tuna matatizo makubwa ya ushirika nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ilikuwa ni ndogo, anayetoa maono, sera na mipango ni Wizara ya Kilimo lakini yule afisa wa chini ambaye anapaswa kutekeleza maono, mipango na yote yuko chini ya TAMISEMI. Iwapo mipango hiyo itaenda vyovyote Waziri wa Kilimo hana uwezo wa kumhoji au kumuwajibisha na mifano iko wazi kila mahali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Simiyu Afisa Ushirika alikamatwa anapora kwa bastola, lakini mpaka leo yupo kazini kwa sababu tu TAMISEMI wameshindwa kumshughulikia, licha ya Tume ya Ushirika kusema huyu mtu hatufai. Tukija Mbozi ni madudu matupu pale ushirika, ukienda Mbinga hivyo hivyo, Mwanza kila mahali na hatuoni huko TAMISEMI kuwachukulia hatua ndiyo maana tukaomba kwamba hawa Maafisa Ushirika warudi Wizarani ambayo inajua taaluma zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ilikuwa ni hiyo, siyo kwamba tulitaka kuharibu D by D bali tulitaka kuiimarisha kuwafanya hawa Maafisa Ushirika wawajibike kwa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge, wakati anahitimisha Bajeti, Waziri wa Kilimo alitoa agizo hapa Bungeni kuwazuia Vyama vya Msingi kukopa. Kwa masikitiko, Vyama vya Msingi bado vinachukua mikopo na Maafisa Ushirika wanawasainia hiyo mikopo na hiyo mikopo haiendi kwa washirika badala yake viongozi wa ushirika wanakula kwa kushirikiana na washirika na Mheshimiwa Bashe hana uwezo wa kuchukua hatua kwa sababu wale wako TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo uende kwa Mheshimiwa Mchengerwa uanze kumwambia habari za ushirika, haelewi kitu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, anayejua hayo ni Mheshimiwa Bashe. Kwa hiyo, hoja yangu ilikuwa hapo, kuwaomba hawa Maafisa Ushirika wawe chini ya Wizara ya Kilimo hata tunapozungumza Bajeti ya Kilimo tunajua hawa watu tumekukabidhi, Maafisa Kilimo, Maafisa Ushirika ambao unawasimamia. Hata hivyo, namshukuru Waziri kwamba ametambua changamoto na ametuomba tumpe muda aje na hiyo Sheria. Kwa hiyo usiku wa deni hauchelewi kuisha, sisi wakati wa Bajeti tutamkamata, ametuomba muda na mimi kama mtoa hoja nipo tayari kutoa muda kwa Serikali kulichakata hili suala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge wote tunajenga nyumba moja na wote tunataka mkulima wetu afaidike na mazao yake.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, hoja gani?

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, namalizia, naomba kutoa hoja kukubaliana na maombi ya Serikali kwamba tuipe muda itimize wajibu wake. (Makofi)

SPIKA: Ngoja kwanza, Waheshimiwa Wabunge. Subirini kwanza Waheshimiwa…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge hoja iliyoko mezani, kwa sababu ni lazima Taarifa zetu Rasmi za Bunge zikae sawa. Hoja iliyoko Mezani na ambayo iko mbele ya Bunge ni Hoja ya Kuwahamishia Maafisa Ushirika katika Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Maafisa Ugani chini ya Wizara ya Kilimo. Hiyo ndiyo hoja iliyoko mbele ya Bunge. Kama Mbunge nataka nikuongoze vizuri ili ujue ni hoja gani unaitoa.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, sawa.

SPIKA: Ukisema unatoa hoja na ulikuwa unasema unaungana na Mheshimiwa Bashe hiyo kutoa ina sura mbili. Moja, unaiondoa hii hoja yako?

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, hapana.

SPIKA: Ama unaitoa, yaani umebadilisha hii hoja yako tuichukue ile hoja ya Serikali ndiyo tuiweke, ndiyo unayotaka Bunge lihojiwe kwa hiyo. Kwa sababu kama unaiondoa hoja maana yake Bunge hatutalihoji. Kama hoja yako bado ipo hii ndiyo tuliyonayo hapa mezani…

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ndiyo hiyo ipo.

SPIKA: Kama unaibadilisha ndiyo useme sasa umebadilisha hii hoja kwa sababu…

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, hapana.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge tusikilizane kidogo kwa sababu mambo haya kama halijawahi kutokea siyo jambo rahisi sana kujua ule utaratibu. Sasa kama hoja yako hii unairekebisha ili uchukuliane na ile hoja iliyotoa Serikali ya kwenda kutengeneza sheria maana yake hapa hii ya kwako unaiondoa kwenye Taarifa Rasmi za Bunge hoja hii itakuwa ni ile pale, yaani ni ya kwako bado lakini umeibadilisha kwamba Serikali sasa ika…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane, nadhani Mheshimiwa Mbunge umenielewa ili ujue ninapoitoa kwa Wabunge kuwahoji ili hoja hii ifungwe, nataka nijue niwahoji hoja ipi? Hii uliyoleta mwanzo ama iliyorekebishwa na Serikali ambayo bado itakuwa ni ya kwako.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hoja yangu ni hii, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Kilimo amesema kwamba wanaandaa Sheria kwa kushirikiana na TAMISEMI kuweka mazingira mazuri ya kuwasimamia hawa Maaafisa Ushirika na hii ndiyo ilikuwa ndiyo lengo la msingi la hoja yangu kwamba hawa Maafisa Ushirika wawajibike rasmi kule chini. Kwa maana hiyo ni kwamba nipo tayari kuipa muda Serikali, hoja yangu ni hiyo, kukubaliana na hoja ya Serikali. (Makofi)

SPIKA: Haya, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge nitakapowahoji Mheshimiwa mtoa hoja ameirekebisha hoja yake ya mwanzo. Badala ya kuwa hoja ya kuwahamishia Maafisa Ushirika katika Tume ya Maendeleo ya Ushirika na Maafisa Ugani chini ya Wizara ya Kilimo, sasa hoja yake pamoja na kwamba maelezo ni haya haya, hoja yake iliyoko mezani ambayo inaletwa Bunge liamue ni hoja inayohusu Serikali kutunga Sheria ili kuleta ufanisi kwenye utendaji kazi wa Maafisa Ushirika. Ndiyo hoja itakayotolewa kwenu. Sasa Mheshimiwa Mbunge baada ya kusema hayo sema unatoa hoja. (Makofi)

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, naafiki.

SPIKA: Haya Waheshimiwa Wabunge hoja ya Mheshimiwa George Mwenisongole imeungwa mkono. Unaweza kurejea kuketi Mheshimiwa Mbunge, ahsante sana. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge sasa nitawahoji Wabunge kuhusu hoja iliyorekebishwa ya Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole. (Makofi)