Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. George Ranwell Mwenisongole (50 total)

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Mbozi napenda kuuliza swali kuhusu Barabara la Mloo – Kamsamba mpaka Kilimamatundu na kutoka Utambalila mpaka Makao Makuu ya Wilaya ya Momba, Chitete, kilometa 145. Kwa kuwa, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeshakamilika; na kwa kuwa nyaraka za tenda ziko tayari.

Je, ni lini barabara hii itatengewa fedha na kutangazwa ili ijengwe kwa kiwango cha lami kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi na kama Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi inavyoelekeza kwa mwaka 2020 - 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoisema ya Mbozi – Mtambalila mpaka Kamsamba ni barabara ambayo, kama alivyosema imeshafanyiwa usanifu na ni kati ya barabara ambazo zimeahidiwa kwanza kwa bajeti zinazokuja zitajengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mwenisongole kwamba, barabara yake iko kwenye mpango na zitaendelea kujengwa barabara kadiri ya fedha itakavyopatikana katika kipindi hiki cha kuanzia mwaka wa fedha wa 2021/2022 mpaka 2025/2026, asante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Matatizo yaliyoko Kasulu Vijijini yanafanana na matatizo yaliyoko kwenye Jimbo langu la Mbozi katika Kijiji cha Sasenga na Itewe, kuna mgogoro kati ya wananchi na Kambi ya Jeshi. Napenda kumuuliza Waziri wa Ulinzi. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua huo mgogoro ambao umekuwa ni wa muda mrefu kati ya hivyo vijiji na Kambi ya Jeshi 845KJ. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba katika Kambi ya Itaka kuna shida hiyo ya mgogoro. Niseme kwamba migogoro hii imesababishwa na mambo mengi ikiwemo lile suala tu la uzalendo, majeshi yetu, pale ambapo tulikuwa tunawaruhusu wananchi kufanya shughuli zao; na walipozoea kufanya shughuli zao wakaamua kuhamia katika maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, kwamba tunafanya utaratibu maeneo yote na tumeshatambua maeneo yote yenye mgogoro na kwa hiyo, tumejipanga kwa ajili ya kuitatua. Tumeanzisha kitengo maalum cha miliki kuhakikisha kwamba migogoro yote tunaimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mwenisongole kwamba tunafahamu shida ya Itaka na kuna hatua zinachukuliwa, tunakwenda kutatua shida ambayo iko kwa wananchi. Vilevile nawasihi sana wanasiasa na viongozi mbalimbali, kwamba kuna wakati mwingine tumetafuta kura Waheshimiwa Wabunge tukiahidi kwamba tutawasaidia wananchi kupata maeneo ambayo ni ya Jeshi. Niwahakikishie tu kwamba tutafuata taratibu kuhakikisha kwamba haki inatendeka, wananchi wanapata haki zao na Jeshi linaendelea kufanya shughuli zake bila kikwazo chochote. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Mimi ningependa kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Kwa nini Serikali isipunguze riba kwa hao wanaolipa deni lote kwa mkupuo kwa wakati mmoja ikatoka asilimia kumi au asilimia mbili au tatu au na vile vile kupunguza- retention fee ambayo ni kubwa na haipo kwenye mkataba wanaojaza wakati wa kukopa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika majibu yangu yaliyopita, kwamba tunaenda kufanya review ya tozo hizi pamoja na riba na kuweza kuangalia namna gani tunaweza tukazipunguza au kuziondoa kulingana na uhitaji kutokana na malalamiko yaliyopo.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Napenda kuuliza swali langu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Maji kusambaza maji zinaweza kuwa bure kama gharama za kuunganisha maji hazitashushwa. Swali langu ni hili, kwa nini Serikali isishushe gharama za kuunganisha maji, ikiwa ni pamoja na kuzuia wananchi kulazimishwa kununua vifaa vya kuunganisha maji kwenye Mamlaka za Maji na gharama zake zikawa kama umeme wa REA shilingi 27,000? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Sisi kama Wizara ya Maji jukumu letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji, si maji tu, lakini kwa gharama nafuu. Kwa hiyo, nikiwa Waziri wa Maji tumepokea ushauri, ahsante sana.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa niaba ya wananchi wa Mbozi napenda kuuliza swali langu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Hayati Rais Magufuli akiwa kwenye kampeni aliahidi wananchi wa Mji Mdogo wa Mlowo kwamba kutajengwa kituo cha afya kikubwa cha kisasa pale. Tayari wananchi wameshapeleka site matofali 150,000 na tayari heka 10 zimeshatengwa. Sasa ni lini Serikali itapeleka fedha kuanza ujenzi wa kituo hicho cha afya katika Mji Mdogo wa Mlowo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ahadi za Viongozi wetu wa Kitaifa ni ahadi ambazo lazima Serikali tutakwenda kuzitekeleza na hivyo tumeandaa mpango kabambe wa kuhakikisha kwamba tunaratibu utekelezaji wa ahadi zote zilizotolewa na Viongozi wetu wa Kitaifa ikiwemo Kituo cha Afya cha Mlowo katika Jimbo la Mbozi. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuweka mpango na kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mlowo, Mbozi.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa hii nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbozi lenye wakazi 300,000 halina hospitali, linategemea vituo viwili vya afya kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wake, lakini katika hivyo vituo viwili vya afya cha Itaka na Isansa havina vyumba vya kulaza wagonjwa, havina wodi za kulaza wagonjwa. Sasa pamoja na kwamba tuna madaktari wazuri wa kufanya upasuaji mkubwa katika hivyo vituo vya afya wananchi wanakosa huduma kwa sababu hawana vyumba vya kulaza wagonjwa.

Sasa nini mkakati wa Serikali wa kujenga wodi za kulaza wagonjwa kwenye hivyo vituo vya afya viwili vya Itaka na Isansa ambavyo vinategemewa katika Jimbo la Mbozi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa Mheshimiwa Mbunge ni kweli kwenye Hospitali yake ya Wilaya ya Mbozi kwanza miundombinu ni michache, lakini sasa hivi ndio inatumika kama Hospitali ya Mkoa na sasa tumeshamalizia majengo ya Hospitali yao ya Mkoa. Kwa hiyo, mzigo ulioko kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mbozi ambao ilikuwa inaubeba kama Hospitali ya Mkoa sasa utahamia kwenye hospitali ya mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni kweli kwamba ili kuboresha huduma na kupunguza adha ya wananchi kufuata huduma mbali ni vizuri vituo vya afya viweze kusimamiwa. Kwa hiyo, mimi nafikiri Mheshimiwa Mbunge ni tukitoka hapa Bungeni tukae mimi na wewe, ili uweze kuleta vituo vya afya ambavyo umevifikiri tuangalie kama tayari tumeviingiza kwenye bajeti, kama hatujaingiza tutaweza kuingiza kupitia Global Fund ili viweze kufanyiwa utekelezaji.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Napenda kuuliza swali langu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na upungufu huo wa watumishi wa afya kwenye hivi vituo kwa nini Serikali isitoe vibali maalum kwa hizi zahanati na vituo vya afya kuajiri watumishi wa kujitolea kwa kutumia mapato yao ya ndani, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA(MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba pamoja na jitihada za Serikali Kuu kuajiri watumishi katika Sekta ya Afya lakini mamlaka za Serikali za Mitaa zina wajibu pia wa kuajiri watumishi hawa kwa mikataba kupitia mapato ya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hili naomba nimhakikishie kwamba Serikali ilikwishatoa kibali kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia zahanati, vituo vya afya na hospitali wale ambao mapato yao yanaruhusu kuajiri watumishi kwa mikataba, waajiri na Serikali imeendelea kufanya hivyo; kuna vituo vingi ambavyo vina watumishi wa mkataba wanaolipwa na Halmashauri ili kuboresha huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, naomba nimhakikishie kwamba suala hilo lipo hivyo na niwaelekeze Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa vile vituo ambavyo vina uwezo wa kuajiri watumishi wenye sifa kwa kufuata taratibu, waajiriwe kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma za afya katika vituo vyetu, ahsante sana.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili kuuliza swali. Napenda kuuliza swali; ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kutoka Igawa, Mbeya mpaka Tunduma, zikiwemo njia nne za Mbeya Bypass kwa ajili ya kupunguza msongamano uliopo pale Mbeya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja ni barabara muhimu sana na kwako Mbeya Mjini ni shida. Bahati nzuri mwezi uliopita tulikwenda kule Mbeya, kulikuwa na mgomo wa bajaji, pikipiki na daladala, shida ni kwamba kuna msongamano mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mpango mkubwa wa Serikali wa kujenga barabara ya njia nne. Tunafanya mpango na majadiliano na Benki ya Dunia, tukipata fedha hiyo wakati wowote kuanzia sasa, barabara hii itajengwa ili kuweza kupunguza msongamano katika Mji wa Mbeya na maeneo ya jirani. Ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa hii nafasi.

Mheshimiwa Spika, msongamano huu wa magari katika Mji wa Tuduma haujaathiri tu magari yanayopita mpakani, lakini umeathiri wananchi na usafiri wa daladala, na wananchi wote hata wanaokwenda mikoa ya jirani. Lakini Mheshimiwa Rais, Marehemu Dkt. Magufuli, alipofika wakati wa kampeni aliahidi kilometa 10 za lami kwa ajili ya kupunguza huu msongamano kwa ajili ya kujenga njia za pembezoni na za mchepuko. Sasa nini kauli ya Serikali kuhusu ahadi hii ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa ya kilometa kumi za lami ili kupunguza msongamano katika Mji wa Tunduma? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tunakubali kwamba ahadi hiyo ilitolewa na Mheshimiwa Rais. Lakini kwa kutambua changamoto ya msongamano ambayo ipo pale Tunduma, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ina mambo yafuatayo ili kuondoa hizo changamoto za msongamano.

Mheshimiwa Spika, kwanza, tunategemea kubadilisha mfumo wa mizani iliyopo iwe ni weigh in motion ambayo inachukua muda mfupi sana, pale Mpemba ambayo ni jirani, kama kilometa 10 pale Tunduma, ambayo inachukua takribani dakika moja mpaka mbili gari linakuwa limeshapita. Kwa hiyo, itakuwa ni moja ya njia za kuondoa msongamano.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, nitumie Bunge hili kusema kwamba Halmashauri ya Tunduma waweze kuongeza maegesho ili magari ambayo hayaendi kwenye Kituo cha Forodha yasiwe na sababu ya kukaa barabarani. Kwa hiyo, ni fursa kwa Halmashauri ya Tunduma kuongeza maegesho.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa tatu, ile barabara sasa hivi tunaifanyia utaratibu tuweze kupanua njia ili kuwe na lane badala kuwa na lane mbili ziwe walau ziwe hata lane nne, lakini mkakati wa nne ni kutengeneza bypass ya barabara ili magari yote ambayo yanakwenda ama yanatoka yaani yanakwenda Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Katavi hadi Kigoma yasiwe na sababu ya kupita Tunduma, kwa hiyo yapite pembeni ili kuruhusu hii barabara sasa iwe huru na tunaamini tukifanya hivyo tutakuwa tumepunguza sana msongamano katika njia hii. Ahsante. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika awamu hii ya REA kila kijiji kimepewa kilomita moja, nataka nifahamu hizi kilomita moja zinaanza kuhesabiwa wapi, ndani ya kijiji au nje kwa sababu kuna vijiji vingine vimeachana kilomita tatu, kutoka kijiji kimoja mpaka kufika kingine? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa katika swali la msingi na swali la nyongeza la Mheshimiwa Pallangyo. Vile vile nimpongeze Mheshimiwa Mwenisongole kuuliza swali la msingi ambalo kimsingi linawahusu Wabunge wote katika majimbo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumetoa utaratibu mkandarasi anapoingia katika kijiji angalau atumie umbali wa kilometa moja kusambaza umeme tofauti na ilivyokuwa huko zamani ambapo ilikuwa ni wateja wawili watatu wanne. Jambo la msingi hapa ni kwamba ile kilometa moja tunayoitaja ni ndani ya kijiji, sio kati ya kijiji kimoja na kingine, ndani ya kijiji akishafika. Hata hivyo, hao ni wateja wa awali, ataendelea kuunganisha wateja wengine kadri wateja wengine wanavyojitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, tusifungwe na kilometa moja, kilometa moja ni wateja wa kuanzia, badala ya kufunga transformer ukaiacha bila kuwa na mteja. Nimeona nitoe ufafanuzi wa jumla ili Waheshimiwa Wabunge wawe na imani na wateja wa kwanza wanaoanza na tuwaombe wananchi jirani na wateja wa kwanza wanaunganishwa waendelee kulipia umeme hili nao waendelee kuunganishiwa umeme. Ahsante sana.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa hii nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu bei ya umeme vijijini; kwa nini Serikali isitoe tamko hapa Bungeni ili wananchi wote wanaoishi vijijini waelewe bei ya umeme vijijini ni shingapi, ni shilingi 27,000 au ni hiyo 300,000? Ili kuondokana na sintofahamu inayowapata wananchi wa vijijiji.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mwenisongole kwa swali lake zuri na kwa ufuatiliaji wa mambo yanayowahusu wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshatoa tamko na mimi nilirudie; umeme vijijini ni shilingi 27,000 kwa njia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie tena; kwa single phase vijijini umeme ni shilingi 27,000. Ilikuwa jana na itakuwa leo na kwa hali ilivyo sasa na maelekezo tuliyonayo itakuwa hivyo kesho, shilingi 27,000. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa hii nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Barabara ya Mlowo – Utambalila – Kilyamatundu inaunganisha Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Katavi, na ni barabara ya pili kwa ukubwa ndani ya Mkoa wetu wa Songwe. Kwa sasa hii barabara maeneo ya Itewe pale Itaka pameharibika na imesababisha kero kubwa kwa wananchi wa Songwe, Mbozi na mikoa ya jirani. Ni nini kauli ya Serikali kuhusu matengenezo ya haraka yanayohitajika ili kuinusuru barabara hiyo na hizi mvua zinazoendelea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mlowo – Itaka – Kilyamatundu ni barabara muhimu sana kwa Mkoa wa Songwe ambayo inaunganisha na Mkoa wa Rukwa; na kwa kuwa hiki ni kipindi cha mvua, naomba pia nitumie nafasi hii kuwajulisha na kuwaelekeza Mameneja wote wa TANROADS kuhakikisha kwamba kila kunapotokea changamoto kwenye barabara ambazo tunazihudumia basi wazishughulikie mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nitumie nafasi hii kumuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe kesho afike eneo la Itaka, Kijiji cha Itewe kwenye changamoto ili aweze kutatua hiyo changamoto, na mimi mwenyewe binafsi na Mheshimiwa Mbunge tuweze kupata majawabu. Ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa hii nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali kwa kuweka bayana bei ya umeme vijijini ni shilingi 27,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni hili; hapa katikati kuomeongezwa bei ya umeme mijini kutoka shilingi 177,000 mpaka shilingi 320,000.

Je, Serikali haini kama hiyo bei kwa watu wanaoishi mijiji nao bado ni kubwa sana? Kwa nini isirudi bei ya awali ya shilingi 177,000 ili wananchi wa mijini nao kwa wingi wapate nafasi ya kuunganishiwa umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanisongole kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu niliyoyatoa kwenye swali la nyongeza la Mheshimiwa Cosato Chumi, kimsingi ndiyo yanayokwenda mpaka kwenye swali la Mheshimiwa Mwenisongole. Tunakwenda kuangalia kwa ujumla maeneo ni yapi na gharama ipi iweze kutumika katika maeneo hayo ili kuwahakikishia wananchi wote huduma hiyo kwa gharama nafuu ambayo wataiweza. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa hii nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Mbozi wakulima wetu wamefungiwa, hawawezi kwenda kukopa kwenye Mfuko wa Pembejeo na sababu ni hao wakulima 28 ambao hawajarejesha mikopo kwenye huo Mfuko wa Pembejeo.

Je, Serikali haioni kwamba haitendi haki kuwazuia wakulima wote wa Wilaya ya Mbozi, kutokupewa nafasi ya kukopa kwenye huu mfuko kwa ajili ya hao wakulima 28? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kilimo ndiyo uti wa mgongo kwenye Taifa letu. Kwa nini basi ni ngumu kwa mkulima hasa aliyepo vijijini kukopesheka ndani ya nchi hii? Nini mkakati wa Serikali kumwekea mazingira mazuri huyu mkulima aweze kukopa kwa urahisi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba tu kwamba baada ya Bunge aidha ni leo au kesho tuweze kukutana tujadili suala la wakulima wake wa Mbozi kama special case na tuweze kutafuta solution ya kudumu kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ambalo nataka niseme ni kweli mfumo wa fedha katika nchi yetu na mifumo ya kukopesha katika nchi yetu sio rafiki kwenye sekta ya Kilimo. Kwa hiyo, kama Wizara ya Kilimo hatua tuliyochukua sasa hivi tumeanza maongezi na wenzetu Wizara ya Fedha na vile vile kuwahusisha Banki Kuu ya Tanzania, ili tuwe na sera ya fedha ya kukopesha wakulima. Kwa sababu sera zetu za fedha na sheria zetu za mikopo zinazo guide financing kwenye uchumi na kutoa mikopo nyingi zimekaa kuitazama kama grocery ndio hivyo hivyo na sekta ya kilimo inavyotazamwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tumekubaliana na wenzetu Wizara ya Fedha ili kuja na financing na policy ya agriculture financing na SME ili iwe rafiki kuwakopesha wakulima wakati huo huo tayari tunayo instrument ya TADB, kwa sababu sasa hivi tunatumia kukopesha kutokana na case by case. Kwa hiyo, tunataka tuwe na legal frame work ili iweze kusimamia suala la ukopeshaji wa sekta ya kilimo na vile vile ukopeshaji wa value chain ya kilimo na tuwe na legal procedure ambayo inaweza kuzifanya taasisi za fedha ziweze kuifata na zisimtazame mkulima kama muuza duka wa kawaida. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza kuhusu suala la Mkandarasi wa REA katika Mkoa wetu wa Songwe. Nafikiri hili tatizo Waziri analifahamu na binafsi nimekwenda ofisini kwake mara kadhaa kuhusu huyo Mkandarasi. Kwa kifupi huyu mkandarasi ana kiburi, mpaka sasa hivi amewasha vijiji vitano tu mkoa mzima na ana majibu ya jeuri, Waziri mwenyewe ameshuhudia. Sasa nini mkakati wa Wizara au Waziri yuko tayari kwenda Songwe kuonana na huyu mkandarasi kuhusu tatizo la REA, Mkoa wa Songwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mkandarasi anayetekeleza mradi wa REA III, Round Two katika Mkoa wa Songwe, ni mkandarasi anayeitwa Derm Electric ambaye pia anafanya kazi hiyo katika Mkoa wa Dodoma. Mkandarasi huyu siyo hohehahe, siyo legelege, ni mojawapo ya wakandarasi ambao tunawatarajia wafanye kazi nzuri. Changamoto ambayo Mheshimiwa Mbunge ameisema tumeshaanza kuifanyia kazi na tutaendelea kusukumana na kusimamiana ili kazi hizo zote za maeneo husika ziweke kukamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, tayari tumeshapanga kikao na wakandarasi hawa, mwishoni mwa mwezi huu ili tuweze kwa pamoja changamoto ambazo zinatokea kwa upande wao ili tuweze kuzitatua na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa hii nafasi.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba hali ni mbaya katika Wilaya ya Mbozi hivi ninavyoongea Mkuu wa Polisi wa Wilaya hana gari hata la kutembelea. Kwa hiyo, katika hayo magari 78 Mheshimiwa Waziri naomba unihakikishie gari moja liende katika Wilaya ya Mbozi ili kumuokoa yule Mkuu wa Polisi wa Wilaya. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nitakuwa sijakosea nadhani Wilaya yake ndiyo ile ya Mheshimiwa Silinde, kama hivi ndivyo hivi karibuni tulipeleka gari huko ambalo halikuwa jipya, kwa hiyo litasaidia nadhani tatizo litakuwa limepata ufumbuzi kama itakuwa siyo Wilaya hiyo ni Wilaya nyingine basi tutalizingatia vilevile. (Kicheko)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nauliza hili swali hii ni mara ya nne, na kila ninapouliza napata majibu tofauti. Mgogoro huu hauwezi kwisha kwa Serikali kusema kwamba hakuna mgogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali la nyongeza: Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutuma timu ya Maafisa wa Wizara na mimi na yeye kuongozana kwenda kule kuongea na wananchi wa Itaka na Mbinzo na wa Kata ya Isalalo kujua nini kinachoendelea kwa wananchi wale ambao kwa miaka zaidi ya 50 wamekuwa wakilitumia eneo hilo kwa shughuli zao za kilimo? Ahsante (Makofi)

NAIBU SPIKA: Sasa umeuliza mambo mawili; atume timu au aende yeye?

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, yote mawili.
NAIBU SPIKA: Aje yeye, nafikiri ndiyo muhimu. Mheshimiwa Waziri utaambatana naye.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Lakini Wilaya ya Mbozi ina shule za sekondari 44, Serikali imepelekea vifaa vya maabara kwenye shule za sekondari 12 tu. Sasa je, nini commitment ya Serikali katika hizi bilioni tano ambazo zimetengwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kusaidia shule ambazo katika Wilaya ya Mbozi hususan Jimbo la Mbozi ambazo hazijapata vifaa vya maabara? Naomba kuuliza.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu
Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mbozi ni kwamba tutapeleka fedha kwa ajili ya shule za sekondari ambazo ameziainisha katika jimbo lake, zile zote ambazo zitakuwa zimemaliza maabara katika mwaka wa fedha unaokuja na zile nyingine ambazo tumeshanunua vifaa tunasubiri tu zile shule ambazo zitaleta taarifa tupeleke.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natambua kazi njema anayoifanya katika Jimbo la Mbozi na ninajua ameji-commit kwa kiwango gani kwa wananchi wake. Kwa hiyo, nimuondoe shaka kwenye hilo.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali langu la kwanza, hili swali nimeliuliza hii ni mara ya tano sasa ndani ya Bunge hili na kila wakati mnasema Serikali kwamba inatafuta fedha.

Sasa nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, je, hizo fedha zinatafutwa miaka yote hii au lini zitapatikana?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa sasa hiyo barabara ina hali mbaya sana kutoka Mlowo mpaka pale Igamba sehemu ya Zerezeta na Mheshimiwa Naibu Waziri umefika umetumiwa picha umeona uhalisia.

Nini kauli ya Serikali kwa wakazi wa Mbozi wanaopata tabu sana kipindi hiki cha masika kwa hiyo barabara ifanyiwe matengenezo ya haraka na kuondolewa vile vifusi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii anayoitaja ni muhimu sana ya kiuchumi na inayounganisha Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Rukwa na ndiko kunakotoa mpunga mwingi sana katika nchi ya Tanzania.

Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ndiyo maana Serikali kwanza iliona ijenge daraja la Mto Momba kurahisisha usafiri, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba matarajio ya Wizara kwamba tutaweka kwenye mapendekezo ya bajeti barabara hii iweze kuanza kujengwa.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili, ni kweli kati ya Mlowo na Igamba eneo linaloitwa Zerezeta pamekuwa na changamoto na tulishamuagiza Meneja wa Mkoa aweze kuhakikisha kwamba anafanya marekebisho na kuweka changarawe ambazo ni imara ambazo haziwezi kuteleza ili shughuli za kiuchumi kwenye barabara hiyo ziendelee.

Kwa hiyo, nachukua pia nafasi hii kupitia Bunge kumuagiza Meneja wa Mkoa kuhakikisha kwamba anachukua jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba eneo hilo la Mlowo - Igamba eneo la Zerezeta linafanyiwa matengenezo haraka, ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa hii nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyoko kwenye hili Pori la Wamembiki yanafanana na matatizo yaliyoko katika Wilaya yangu ya Mbozi kwenye Pori la Isalalo kati ya wananchi wa Kata ya Isalalo na Mbinzo na Itaka na TFS.

Je, ni lini Serikali itatatua huu mgogoro wa Pori la Isalalo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George, Mbunge wa Mbozi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote niwaombe wananchi wafahamu kwamba migogoro mingi ambayo inasemekana kuwa ni migogoro ni migogoro ambayo ni nani amemkuta mwenzie? Pori analoliongea Mheshimiwa George ni eneo ambalo lina GN ambayo GN ni ya miaka ya nyuma na wananchi wamesogea katika maeneo hayo. Kwa bahati mbaya kabisa Kamati ya Mawaziri Nane haikuweza kupita katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuombe kwa kuwa huu ni mgogoro mpya, Serikali itaenda kuhakiki yale maeneo na kuyaangalia umuhimu, kwanza tunaangalia umuhimu wa eneo lile kama ni vyanzo vya maji na kuna wanyamapori na mazalia ya wanyamapori yako katika maeneo hayo, tunaendelea kuwashauri wananchi kuyaachia yale maeneo pamoja na kuwa tunawaita sisi ni wavamizi. Linapoonekana eneo halina umuhimu sana basi Serikali inapitia na kumega yale maeneo nakuwaachia wananchi.

Mheshimiwa Spika, hivyo nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaenda kuyahakiki hayo maeneo na kama yanaendelea kuwa yanafaa katika uhifadhi basi tutawashauri wananchi lakini kama yatakuwa yaruhusu kumegwa basi tutayaachia. Ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada kubwa za Serikali kusambaza maji vijijini jitihada hizi zinaweza kuwa bure iwapo gharama ya kuunganishiwa maji kwenye nyumba za wananchi hazitashuka. Je, Serikali haioni sasa ni wakati umefika wa kuangalia hizi gharama za kuunganishiwa maji kwa wananchi, especially wananchi wa vijijini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, gharama za uunganishi Wizara tunaendelea kuzipunguza kwa kuzisogeza bomba kuu ambalo litambunguza umbali wa kutoka kwenye main line kwenda kwa watumiaji, na tayari kazi hii imeanza katika maeneo mbalimbali. Hivyo, ninatarajia kuwa hata katika jimbo lake pia huduma hii itamfikia.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa hii nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Napenda kuuliza swali kuhusu barabara ya Mlowo – Kamsamba mpaka Utambalila; barabara hii upembuzi yakinifu na usanifu wa kina vimeshakamilika, na mwaka jana nilipouliza swali kuhusu hii barabara Mheshimiwa Naibu Waziri aliniambia kwamba Serikali inatafuta fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu ni hili; je, Serikali bado inaendelea kutafuta fedha au mpango umeishia vipi? Kwa sababu wananchi wa Mbozi wanasubiri kwa hamu sana hii barabara.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa ustawi wa Mkoa wa Songwe. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii baada ya kukamilika kwa usanifu wa kina Serikali inatafuta fedha ili ianze kuijenga kwa kiwango cha lami barabara yote ya kutoka Mlowo hadi Kamsamba, ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nilitaka kujua ni vigezo vipi vinatumika katika kugawa hizo fedha za umaliziaji wa maboma ya zahanati kwani Jimbo la Mbozi tuna maboma zaidi ya 20 lakini kiasi kinachokuja ni kidogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vigezo ambavyo vinatumika kupeleka fedha ni idadi ya watu, umbali wa kijiji hicho kwenda kwenye kijiji chenye zahanati cha jirani zaidi. Lakini katika Jimbo la Mbozi pia Serikali imeendelea kupeleka fedha na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kupeleka fedha pia.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri matatizo ya mkandarasi wa REA aliyepewa tender ya kusambaza umeme kwenye Mkoa wa Songwe unayafahamu. Mpaka sasa hivi katika ya vijiji 127 amepeleka umeme kwenye vijiji 48 tu: Sasa hamwoni wakati umefika wa kuvunja naye mkataba kunusuru Mkoa wa Songwe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Songwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna baadhi ya maeneo ambapo Wakandarasi wetu hawajafanya vizuri. Tunachokifanya kikubwa ni kuhakikisha tunawasimamia kwa karibu kuhakikisha kwamba kazi zao zinakamilika kwa wakati. Katika eneo la Songwe, tumekuwa tukilifuatilia kwa karibu na Mheshimiwa Mwenisongole na tunamhakikishia kwamba ndani ya muda stahiki mradi huo utakamilika.

Mheshimiwa Spika, katika wale Wakandarasi ambao wako nyuma sana na hatuna namna, tutavunja mikataba yao, lakini wale ambao wanaweza kufanya kazi na kuikamilisha kwa wakati, tutasimamia vizuri ili tuweze kuikamilisha kwa wakati kwa sababu kuvunja mkataba pia siyo option nzuri ya kukamilisha mradi kwa wakati.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; tatizo ni muda, mwezi Juni na mwezi Mei mwishoni wakulima wa kahawa wanaanza kuvuna kahawa yao kupeleka kwenye hivyo Vyama vya Msingi, sasa Waziri anaposema mwezi ujao, kwa nini hili suala lisifanyike mapema kabla ya msimu wa kuuza haujaanza ili hayo makato yaondolewe na wakulima wapate chao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; niipongeze Serikali kwa uamuzi wa kuwafutia leseni mawakala wa mbolea 700. Kwa kweli hii ni hatua nzuri na naomba wasirudi nyuma wakaze buti, hatuwezi kutishwa na watu wasiokuwa waaminifu, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri wakati naingia hapa Bungeni taarifa imekwishafika Wizarani, kwa hivyo tutaanza kulifanyia kazi mwezi huu ili kuuwahi msimu.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ambayo yanatia moyo, kuna barabara nyingine ndani ya Mkoa wetu wa Songwe ambazo zimekwama, kwa mfano barabara ya kutoka Mlowo – Itaka – Kamsamba na Barabara ya Mbalizi – Utengule mpaka Mkwajuni kule kwa Mheshimiwa Mulugo, zote hizo zina ahadi nyingi na ninaomba Serikali itilie mkazo zipate kutekelezwa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga barabara hizi, hasa hizi alizozitaja Mheshimiwa Mbunge kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha. Katika mwaka huu wa fedha tunaokwenda wa 2023/2024, Bunge lako tukufu limeiidhinishia TARURA zaidi ya shilingi bilioni 772 kwa ajili ya kutengeneza barabara mbalimbali hapa nchini, na ninaamini katika hizi barabara za Mlowo ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge nazo zitawekwa katika kipaumbele cha mwaka huu wa fedha tunaokwenda kuutekeleza.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mlowo – Utambalila mpaka Kamsamba kila kitu kiko tayari, nyaraka za tender, usanifu wa kina. Sasa nilitaka nijue, ni lini Serikali itapeleka barabara hii kwa Mheshimiwa Rais kuombewa kibali cha kujengwa kwa njia ya lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mlowo – Utambalila hadi Kamsamba ni barabara ambayo tayari Serikali imeshajenga Daraja la Mto Momba na kumekuwa na maelekezo ya viongozi mbalimbali wa Kitaifa akiwepo Waziri Mkuu, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaiweka kwenye mapendekezo kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa bajeti ambayo tunaiendea mbele.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Mlowo – Utambalila mpaka Kamsamba, nyaraka za tenda, usanifu wa kina, kila kitu kipo tayari, na ipo ndani ya mpango wa bajeti: Je, ni lini Serikali itatoa fedha ili ujenzi wa kiwango wa cha lami uanze kwenye hiyo barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Mlowo - Utambalila hadi Kamsamba, barabara ambayo Mheshimiwa Mbunge amekuwa anaiulizia mara kwa mara, tumemhakikishia kwamba hiyo barabara ambayo inaunga Mkoa wa Songwe na Rukwa, tumeiweka kwenye mapendekezo, na tuliagizwa pia na viongozi kwamba barabara hiyo sasa tuanze kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tusubiri bajeti kama itapitishwa, barabara hiyo tutaanza kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnada wa Kahawa wa Songwe ni tofauti kabisa na mnada wa kahawa uliopo kule Kagera. Mazingira ya pale Songwe siyo rafiki, hauko wazi na kuna uhuni mwingi unaofanywa na baadhi ya wanunuzi kwa kushirikiana na watu wa bodi kuchezesha bei ya kahawa kwenye mnada ili wakulima wasipate bei inayostahili.

Je, kwa nini Serikali isiboreshe mazingira ya mnada wa kahawa wa Songwe ufanane kama mnada wa kahawa wa Kagera ambao uko wazi fair na hakuna uhuni wowote unaoweza kufanyika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge George Mwenisongole, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kagera inalimwa robusta, Songwe inalimwa arabica. Haya ni variety mbili tofauti. Ukienda kwenye soko ili uweze kuuza kahawa ya arabica lazima pia ionjwe ndio unapata radha na quality inayokwenda ku-determine bei. Tumesikia hoja ya Mheshimiwa Mbunge naelekeza bodo ya kahawa kuhakikisha kwamba wanaweka mazingira wezeshi ili pia mkulima wa Songwe aweze kunufaika na bei ya kahawa.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la madawa nchini linaweza kwisha iwapo tu Serikali itaamua kutoa fedha za mtaji ambazo Bohari Kuu ya Dawa Nchini (MSD) wameomba. Wameomba takribani shilingi bilioni 200.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, anaweza kutuhakikishia Wabunge kwamba Serikali ipo tayari kutoa hizo fedha za mtaji ili kumaliza tatizo la usambazaji wa dawa hapa nchini kwenye vituo vyetu vya afya na zahanati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, hilo lilikuwa ni mjadala mkubwa sana hapa ndani ya Bunge wakati wa bajeti. Nawashukuru ninyi Wabunge kwamba mlilipitisha hilo na Serikali ipo tayari, ndiyo maana wakati wa bajeti, Waziri wa Afya na Waziri wa Fedha walikiri kwamba hilo litaenda kufanyiwa kazi.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kata ya Igamba katika Wilaya ya Mbozi ni moja ya kata ambazo zimeahidiwa kupelekewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya. Je, ni lini sasa hizo fedha zitaenda ili ujenzi uanze?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kata hii ya Igamba itapelekewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kama ambavyo Serikali imeahidi, ahsante.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba mradi wa kutoa maji kutoka Mto Mafumbo kwenda kwenye Mji wa Mlowo na Vwawa unatekelezwa kwa haraka, ili kuondoa adha ya wakazi wa Mlowo na Vwawa wanaokabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mto Mafumbo ni moja ya chanzo kilichogunduliwa na Ofisi yetu ya Bonde la Ziwa Tanganyika na tayari Ofisi ya Vwawa - Mlowo wanashughulika na chanzo hiki kuhakikisha kiweze kutumika. Wameshaandika proposal imekuja Wizarani, ninaahidi tutafanyia kazi kwa sababu ya umuhimu wake. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nataka nimwombe Mheshimiwa Naibu Waziri, Je, yupo tayari kuongozana na mimi Mbunge wa Jimbo la Mbozi kwenye mji wa Mlowo kuangalia hivyo vyanzo vya maji na kuhakikisha kwamba yote aliyosema yataenda kutekelezwa kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole Mbunge wa Jimbo. Awali ya yote nipokee pongezi lakini Mheshimiwa Mbunge na wewe nakupongeza na ninakusihi tuendelee kushirikiana. Ufuatiliaji wako wa karibu ndio matunda ya miradi hii kufika hatua hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuongozana Mheshimiwa Mbunge, kama tulivyoongea ulipokuja Wizarani kufuatilia miradi hii, niko tayari na tutakwenda kuhakikisha miradi hii inatekelezwa kwa wakati.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza naishukuru Serikali, imesikia kilio cha wananchi wa Mbozi na Momba kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.

Swali langu la kwanza; je, ni kilomita ngapi sasa Serikali itaanza kwa awamu hii?

Mheshimiwa Spika, pili; je, ni lini mchakato wa kumpata mkandarasi utaanza ili ujenzi uanze? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 147 kwa mwaka ujao wa fedha tumepanga kuanza kuijenga kilometa 50.

Swali lake la pili kuhusu ni lini tutaanza, barabara hii tutaanza kuijenga ama kutafuta mkandarasi tutakapoanza utekelezaji wa bajeti wa 2023/2024, na ndipo tutakapoanza kutekeleza mpango huu wa kuanza kuijenga hii barabara kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Serikali imeweka zuio la kuu za mahindi nje ya nchi. Hali hiyo imesababisha bei ya mahindi kushuka. Kwa mfano, kwenye Jimbo langu la Mbozi debe sasa hivi ni shilingi 8,000 na bei inazidi kushuka; nini kauli ya Serikali ili kuwaokoa hawa wakulima ambao kwa sasa wamevunjika moyo na kuporomoka kwa hii bei?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya changamoto kubwa ambayo tunaipata katika biashara ya mazao ni uholela. Serikali ilichokifanya siyo kuzuia moja kwa moja. Imetoa mwongozo na kuweka utaratibu wa namna ya kufanya biashara ya mazao nchini Tanzania ambapo tumeelekeza kwamba, hivi sasa kila mfanyabiashara wa mazao, ahakikishe kwanza kabisa anapata Business License; pili, awe ana TIN; na tatu, kabla hajaenda mpakani kusafirisha mazao, ahakikishe kwamba ameshapata kibali cha kusafirisha mazao nje ya nchi (Export Permit).

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kufanya hivi ni kuweka takwimu sawa, kwa sababu kumekuwepo na wafanyabiashara ambao wanakwenda mashambani moja kwa moja kwa wakulima kwenda kununua mazao na hivyo Serikali kupoteza mapato mengi sana. Serikali ipo kwa ajili ya kuwalinda wakulima na kuhakikisha kwamba wakulima wanapata bei bora tukishawasimamia, kwa sababu ndiyo azma ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba mkulima ananufaika na kilimo chake. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri kidogo yanatia moyo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza wezi wa kuku, wezi wa ng’ombe na mbuzi wakikamatwa wanafikishwa mahakamani, na kufungwa jela, lakini hawa wa Vyama vya Ushirika wanaambiwa tu warudishe fedha na ndio sababu hili tatizo limeota usugu sana Wilayani Mbozi. (Makofi)

Sasa ni lini hawa viongozi watafikishwa mahakamani na kuchukuliwa hatua za kisheria? Swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Afisa Ushirika ambaye ametajwa kwenye hii tuhuma kwamba alishirikiana na hawa viongozi wa Vyama vya Ushirika nashangaa mpaka sasa hivi bado yuko kazini, sasa ni lini na yeye hatua hii itamchukulia? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, baada ya kufanya uchunguzi taarifa hii imekabidhiwa kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na vyombo vingine vya kisheria kwa ajili ya kuweza kuchukua hatua na ninavyozungumza hivi sasa tayari zaidi ya shilingi milioni 77.6 zimerejeshwa na baadhi ya viongozi wameondolewa na wengine tumewakabidhi TAKUKURU kwa ajili ya hatua za kijinai.

Mheshimiwa Spika, hivyo kazi yetu ilikuwa uchunguzi tumekamilisha, tunasubiri vyombo vingine vya Serikali na vyenyewe vifanye kazi, lakini tu niseme katika hili tumekuwa tukitoa maelekezo mbalimbali, hatutamvumilia mtu yeyote ambaye atafanya ubadhirifu katika Vyama vya Ushirika na kuwakosesha wakulima mapato yao, Serikali ipo macho tutachukua hatua na hakuna ambaye atapona. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge taarifa iko pale, vyombo vitafanya kazi yake.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Afisa Ushirika ambaye yuko chini yetu kwa sababu hii taarifa imeshawasilishwa ili kuendana na uwezo wetu tutachukua hatua stahiki pale ambapo itabainika kupitia taarifa ambayo imewasilishwa kwamba ni mhusika moja kwa moja huyu yuko ndani ya uwezo wetu tutachukua hatua stahiki juu yake.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Mbozi ni moja ya Wilaya inayoongoza kuwa na shule nyingi za msingi, shule 179, lakini kiasi cha fedha za miundombinu na ukarabati zinazotoka Serikali Kuu kuja Wilaya ya Mbozi ni kidogo sana ukilinganisha na idadi ya shule 179. Sasa kwa nini Serikali isiangalie Wilaya ya Mbozi kwa jicho la tatu na kuangalia idadi ya hizi shule nyingi za msingi na kuongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya miundombinu na ukarabati kwa ajili ya shule hizi za msingi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba Jimbo la Mbozi lina shule nyingi na lina majengo mengi ambayo bado hayajakamilika. Nimhakikishie Mbunge tu kwamba moja ya vigezo ambavyo tutavitumia sasa hivi ni kuhakikisha yale maeneo yenye uhitaji mkubwa tunayapa kipaumbele ikiwemo Jimbo la Mbozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nataka nimuulize swali Naibu Waziri, kuna Halmashauri zingine zina Majimbo zaidi ya mawili au matatu, sasa kama mtapeleka gari moja, hilo gari litaenda kwenye Jimbo gani? Kwa nini usiweke wazi, kwa nini isiwe kwa Majimbo badala ya kuwa Halmashauri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa kupeleka magari ya wagonjwa kwenye Halmashauri unazingatia vigezo, kigezo cha kwanza ni idadi ni ya watu katika Halmashauri, kigezo cha pili ni idadi ya wagonjwa kwa maana ya burden of disease katika Halmashauri husika. Utaratibu huu hauzingatii Majimbo kwa sababu Majimbo pia yanatofautiana na idadi ya wananchi ukilinganisha na Halmashauri. Kwa hiyo, tutakwenda kupeleka magari haya, kwa kigezo cha Halmashauri na idadi ya watu na burden of disease. Pale ambapo itahitajika kwa Majimbo mawili kupata gari tutafanya hivyo. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa mfano jimbo lake lile la Tunduma, linaingia mara sita kwa jimbo langu, lakini wote tunapata fedha sawa za mgao wa barabara, sasa haoni kama hiyo siyo sawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli ukichukulia Jimbo la Mbozi, ukifananisha na Jimbo la Tunduma, Jimbo la Mbozi ni kubwa zaidi kuliko Jimbo la Tunduma na utaratibu ambao ulikuwa unatumika mwaka uliopita ni utaratibu ambao tulikubaliana wote Wabunge humu ndani na ndiyo maana sasa hivi tunarekebisho hiyo formula ili majimbo yote yapate kulingana na ukubwa wa eneo na mahitaji ya eneo husika. Ahsante sana.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nataka nimuulize swali Naibu Waziri, kuna Halmashauri zingine zina Majimbo zaidi ya mawili au matatu, sasa kama mtapeleka gari moja, hilo gari litaenda kwenye Jimbo gani? Kwa nini usiweke wazi, kwa nini isiwe kwa Majimbo badala ya kuwa Halmashauri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mpango wa kupeleka magari ya wagonjwa kwenye Halmashauri unazingatia vigezo, kigezo cha kwanza ni idadi ni ya watu katika Halmashauri, kigezo cha pili ni idadi ya wagonjwa kwa maana ya burden of disease katika Halmashauri husika. Utaratibu huu hauzingatii Majimbo kwa sababu Majimbo pia yanatofautiana na idadi ya wananchi ukilinganisha na Halmashauri. Kwa hiyo, tutakwenda kupeleka magari haya, kwa kigezo cha Halmashauri na idadi ya watu na burden of disease. Pale ambapo itahitajika kwa Majimbo mawili kupata gari tutafanya hivyo. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri na niko tayari kuvuta subira kusubiri hiyo tume itakayotuletea majibu ila nilikuwa nina ombi moja kwa Mheshimiwa Waziri, je, tume hiyo itakapomaliza kazi, yuko tayari kwenda na mimi Mbozi kuzungumza na wananchi wa hivyo vijiji na kutoa majibu kwa wananchi hao? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kama nilivyokwishamuahidi Mheshimiwa Mbunge, tumeshazungumza suala hili mara nyingi na nathibitisha tu kwamba, niko tayari kwenda kuongea na wananchi wake. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Wananchi wa Isansa wamehamasisha kwa kutumia mapato ya ndani ya kituo cha afya wamechanga milioni 56 pamoja na matofali na mchanga; wameanza ujenzi wa wodi ya kinamama na wazazi katika kituo cha afya. Nini kauli ya Serikali katika kuwaunga mkono wananchi hawa Kata ya Insasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuendelea kukamilisha majengo ya zahanati na vituo vya afya, hospitali za halmashauri kwa awamu. Kwa hivyo, katika mipango hii tutaendelea pia kuhakikisha tunatambua maeneo haya ya Mbozi ili nayo yaweze kuingia kwenye bajeti kwa awamu kwa ajili ya ukamilishaji wake. Ahsante.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa, Mheshimiwa Waziri wakati akihitimisha bajeti hapa alisema kwamba hiyo tozo atakuwa analipa mnunuzi, na kwa hiyo wakulima wa arabica nchini hawatalazimika kulipa shilingi 200.

(a) Je, kwa nini bodi bado inaendelea kuwatoza?

(b) Je, kwa nini basi mnunuzi asiambiwe rasmi kwamba awe analipa hiyo, na ijulikane kwenye Hansard?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli Mheshimiwa Waziri alipokuwa anazungumza hapa wakati wa Bunge alilitolea ufafanuzi, na ndiyo maana hii bei ya shilingi 200 ikawa inawekwa katika bei ile ya jumla ya soko, kwa maana mnunuzi analipa moja kwa moja na katika ile sehemu mkulima anakatwa. Hata hivyo, mapendekezo yake sisi tunayapokea na tutayapitia upya ili tuone namna bora ambayo mkulima ataona athari za moja kwa mojo za makato hayo ya shilingi 200. Ahsante sana.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini naomba commitment ya Mheshimiwa Waziri.

Je, uko tayari kuongozana na sisi kwenda Mbozi kuangalia hali ya vituo vya Polisi na kuhusu ujenzi wa hicho kituo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimepokea ombi lake na ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kujibu swali hili tutakaa tupange ratiba mimi na yeye ya kuweza kutembelea kwenye Jimbo lake ili kuweza kukagua maendeleo ya vyombo vyetu vya usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ujumla wake.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa taratibu zote zimeshakamilika kwa hiyo barabara ya Mlowo – Kamsamba, nilitaka kujua sasa, lini itatangazwa rasmi ili ianze kujengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyomjibu Mheshimiwa Condester Sichalwe, ndiyo barabara hiyo hiyo kwamba tutaitangaza muda wowote ili ianze kujengwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali kwa hatua hii ambayo tumefikia, lakini mpaka jana tunaongea, mkandarasi amepokea shilingi milioni 50 tu kati ya fedha zote hizo alizoomba. Sasa swali langu la kwanza ni hili; ni lini sasa Serikali itakuwa serious kuhakikisha kwamba, fedha zote anazohitaji mkandarasi zinaenda kwa sababu wananchi wa Igamba wanakisubiri kwa hamu sana chuo hiki?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yuko tayari sasa kuongozana na mimi kwenda Igamba, Mkoa wa Songwe, akaangalie kinachoendelea pale? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, sisi Wizara ya Mifugo tumetimiza wajibu wetu. Tumeomba fedha Wizara ya Fedha na tayari documents zote ziko Wizara ya Fedha na mara tutakapopata fedha, tutapeleka kwenye ujenzi wa chuo hicho. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, fedha zitakapokuwa tayari tutazipeleka kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho.

Mheshimiwa Spika, la pili la kutembelea chuo hiki; Wizara iko tayari, mimi au Mheshimiwa Waziri tuko tayari, kutembelea chuo hicho na kama kuna mapungufu ama changamoto zozote tuko tayari kwenda kuzitatua, ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, nataka kujua, ni lini Serikali itapeleka fedha kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kimkakati cha Igamba katika Tarafa ya Igamba, Wilaya ya Mbozi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, natumia nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kuanza kutenga fedha za mapato ya ndani, kwa ajili ya kuanza kujenga Kituo cha Afya cha Kata ya Igamba wakati Serikali pia inatafuta fedha kwa ajili ya kwenda kuwaunga mkono wananchi wa Kata hii, ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kituo hiki kinasubiriwa kwa hamu sana na wananchi wa Mkoa wa Songwe kutokana na matatizo ya umeme yaliyopo ndani ya Mkoa wa Songwe kwani itaondoa utegemezi wa Mkoa wa Songwe kutoka Kituo cha Mwakibete pale Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tangu kuwashwa kwa mtambo wa umeme Na.9 katika Bwawa la Mwalimu Nyerere, sisi Mkoa wa Songwe bado hatujafaidika na kuwashwa huko kwani bado tatizo la umeme limeendelea kuwa kubwa Mkoani Songwe especially line ya Mlowo-Kamsamba na line ya Tunduma. Nini hasa kinachosababisha matatizo ya umeme kuendelea katika Mkoa wa Songwe licha ya kuwashwa kwa mtambo Na.9 katika Bwawa la Mwalimu Nyerere?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia maendeleo ya watu wa Mbozi na Mkoa mzima wa Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na umeme kukatika katika line ya Mlowo-Kamsamba pamoja na Tunduma. Mkoa wa Songwe unapata umeme kutoka katika Kituo cha Kupoza Umeme cha Mwakibete kilichopo Mbeya. Line kutoka Mbeya mpaka Songwe ni ndefu sana na hivyo kupelekea tatizo la low voltage. Serikali tumeshaliona, kwa sasa kupitia Mradi wa Gridi Imara tunakwenda kujenga switching station pale Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kupitia Mradi wa Tanzania-Zambia Interconnector tunakwenda kujenga Kituo cha Kupoza Umeme Songwe kwa ajili sasa watu wa Songwe waweze kupata umeme kutoka Kituo cha Kupoza Umeme Songwe na switching station ambayo itakuwa Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Mkoa wa Songwe, tumeliona tatizo hili na tutalifanyia kazi kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Songwe, ahsante. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa nini kwenye hiki Kituo cha Afya cha Mlowo Serikali inakuwa na majibu mengi tofauti tofauti? La kwanza mlituambia kwamba mimi nilipouliza kama Mbunge wa Jimbo mlisema itajengwa kwa kutumia fedha za World Bank. Leo dada yangu Mheshimiwa Juliana Shonza ameuliza unatuambia kitajengwa 2026. Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja Mbozi alipiga simu TAMISEMI tukakubaliana kuna fedha zimekuja za ujenzi wa Serikali zitaenda kujenga kwenye hiki Kituo cha Afya cha Mlowo sasa kituo kimoja cha afya majibu matatu, sisi tushike lipi kwenye hili jibu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mwenisongole, amefuatilia kwa karibu sana kuhusiana na Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Mlowo na nimewasiliana naye mara kadhaa na nimemhakikishia tu kwamba Serikali ina vyanzo vingi na vyanzo mbalimbali vya ujenzi wa vituo vya afya.

Mheshimiwa Spika, tuna vyanzo vya World Bank ambavyo tunatarajia wakati wowote fedha zikipatikana zitakwenda kwenye vituo vilivyoainishwa, lakini tuna mipango ya Serikali kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya miaka inayofuata 2024/2025 na 2025/2026 na hata tukipeleka fedha za World Bank mwaka huu wa fedha ujao bado tuna awamu ya pili ya Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mlowo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mbunge hii ni faida kwake kwamba tuna mpango wa World Bank fedha zikipatikana kituo hiki kitaanza kujengwa wakati wowote kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi.

Mheshimiwa Spika, lakini tuna mpango wa 2025/2026 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa kituo hicho ili kiweze kuwa fully na kuweza kutoa huduma vizuri zaidi. Kwa hiyo, majibu ya Serikali ni yale yale, dhamira ni ile ile kujenga Kituo cha Afya cha Mlowo na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutakwenda kujenga Kituo hicho, ahsante. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. kwanza ninampongeza sana Mheshimiwa Rais, hii barabara ilikuwa ni kilio kikubwa sana cha Wananchi wa Mbozi na Mkoa mzima wa Songwe. Sasa Mheshimiwa Waziri unasema taratibu za manunuzi zinaendelea; sasa, ni lini hizo taratibu zitakamilika kwa sababu tunaelekea kwenye masika ili mkandarasi aanze kazi haraka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tender ilishatangazwa na zabuni zimeshafunguliwa na tunavyoongea sasa hivi wako kwenye tathmini (evaluation) ili kumpata mkandarasi ambaye atajenga hiyo barabara. Ahsante.