Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Nicholaus George Ngassa (18 total)

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa eneo la Hifadhi ya Bonde la Wembere kwa Wananchi wa Igunga kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo na ufugaji ili kumaliza mgogoro wa muda mrefu katika eneo hilo kwa kuwa Bonde hilo limepoteza sifa ya kuwa Hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Jimbo la Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Bonde la Wembere ni ardhi oevu inayofahamika Kitaifa na Kimataifa kwa kuhifadhi ndege wa aina mbalimbali ambao huishi na kuzaliana kwa wingi. Eneo hili ni dakio na chujio la maji ya Ziwa Kitangiri na Eyasi, pia ni mapito, mazalia na malisho ya wanyamapori linalounganisha mifumo ya ikolojia ya ukanda wa Kaskazini, Kati, Magharibi na Kusini mwa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na umuhimu wa eneo hilo, wananchi wameendelea kuvamia eneo la ardhi oevu la Wembere kwa ajili ya shughuli za kilimo, malisho na ukataji miti. Hali hiyo inasababisha mwingiliano wa shughuli hizo na kusababisha migogoro kati ya wakulima, wafugaji na wahifadhi. Pamoja na uvamizi huo, eneo hilo bado lina umuhimu katika shughuli za uhifadhi hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa eneo hili la ardhi oevu la Bonde la Wembere na kwa kuzingatia kuwa ni chanzo muhimu cha maji kwa wananchi wa mikoa ya Tabora, Singida na Simiyu, Serikali itafanya tathmini na kutambua mipaka ya ardhi oevu kwa njia shirikishi ya wananchi na Serikali. Na lengo ni kupanga matumizi ya ardhi kwa vijiji vinavyopakana na eneo hilo kwa ajili ya matumizi ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kutoa ushirikiano kwa Serikali na wananchi katika kushughulikia suala hili ili kupata suluhisho la kudumu. Naomba kuwasilisha.
MHE. NICHOLAS G. NGASSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaipatia Hospitali ya Wilaya ya Igunga gari la kubebea wagonjwa kwa kuwa lililopo limechakaa sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholas George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, gari la wagonjwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ni chakavu na halifai kuendelea kutumika. Kwa sasa Hospitali ya Halmashauri ya Igunga imepatiwa gari la Kituo cha Afya kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kutoka katika Kituo cha Afya cha Choma ambalo linatoa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto za uchakavu wa magari ya kubebea wagonjwa katika Hospitali na Vituo vya Afya nchini. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kununua magari ya kubebea wagonjwa na itatoa kipaumbele kwa Hospitali na Vituo vya Afya vyenye uhitaji mkubwa wa magari ya kubebea wagonjwa.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Chuo cha VETA Igunga?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Igunga kama ifuatavyo: -

Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Igunga ni miongoni mwa vyuo 29 ambavyo vinaendelea kujengwa. Ujenzi wa Chuo hiki unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai, 2021. Aidha, mchakato wa ununuzi wa mitambo na zana za kufundishia unaendelea sambamba na ukamilishwaji wa chuo hiki. Ujenzi wa chuo hiki utakapokamilika udahili wa wanafunzi wa kozi fupi utaanza mara moja wakati ule wa kozi ndefu unatarajia kutafanyika ifikapo Januari, 2022. Ahsante.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaipandisha hadhi barabara ya Igurubi – Mbutu – Igunga hadi Itumba yenye zaidi ya km 140 kuwa chini ya TANROADS ili ijengwe kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, taratibu za kupandisha hadhi barabara ni kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007 na Kanuni za Menejimenti ya Barabara za Mwaka 2009. Kwa vile suala hili ni la kisheria, ninamshauri Mheshimiwa Mbunge awasilishe maombi yake ya kupandisha hadhi Barabara ya Igurubi – Mbutu – Igunga – Itumba, yenye kilometa 102.8 kwenye Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Tabora. Bodi ya Barabara ya Mkoa itajadili maombi hayo na ikiridhia itawasilisha maombi kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ambaye ndiye mwenye dhamana ya kupandisha hadhi ya barabara nchini. Ahsante.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je ni lini Serikali itafanya ukarabati wa nyumba za makazi ya askari wa Jeshi la Polisi kwenye Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Igunga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba nyumba za makazi ya askari Kituo cha Polisi Wilaya ya Igunga ambazo ni nyumba nne zenye kuishi familia 20 zimechakaa. Tathmini kwa ajili ya kubaini kiwango cha uchakavu na gharama za ukarabati imefanyika na kubaini kuwa kiasi cha shilingi 165,000,000.00 zitahitajika. Serikali imepanga kuanza kufanya ukarabati wa vituo na makazi chakavu ya askari wa jeshi la polisi, yakiwemo ya kituo cha polisi Wilaya ya Igunga kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaweka Kituo cha kupoza umeme Igunga?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO imebaini uhitaji wa vituo vya kupoza umeme katika Wilaya zote Tanzania Bara zenye uhitaji huo. Aidha, imeweka mpango wa ujenzi wa vituo hivyo kulingana na uhitaji kuanzia mwaka huu wa fedha 2022/2023. Kituo cha Kupoza umeme cha Igunga kitawekwa katika mpango wa ujenzi wa mwaka ujao.

Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha huduma ya umeme katika maeneo ya Wilaya ya Igunga na Nzega, Serikali inaendelea na mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Lusu kilichopo Wilayani Nzega kutoka MVA 15 132/33kV hadi MVA 60 132/33kV. Upanuzi huu, utakamilika ndani ya mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Skimu ya Umwagiliaji ya Igurubi katika Jimbo la Igunga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya umwagiliaji imepanga kufanya mapitio, upembuzi yakinifu na usanifu kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji katka Skimu ya Igurubi. Aidha, mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu na gharama ya ujenzi kujulikana, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itatenga fedha katika bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je, ni lini Kata za Mtungulu, Mwamashiga, Isakamaliwa, Kining’inila na Kinungu zitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Mtungulu, Mwamashiga, Isakamaliwa, Kining’inila na Kinungu zote zipo kwenye Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unaoendelea. Mkandarasi anayetekeleza mradi huo anaitwa M/S CEYLEX ameshafika kwenye maeneo hayo. Kwa Kata ya Mtunguli, katika vijiji viwili kati ya vijiji vitatu ambavyo ni Maguguni na Mtungulu, kazi ya kusambaza umeme imekamilika na umeme umeshawashwa, isipokua Kijiji cha Mwajijambo ambacho kazi ya kuvuta nyaya inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa Kata za Mwamashiga, Isakamaliwa, Kining’inila na Kinungu kazi ya uchimbaji mashimo na usimikaji nguzo inaendelea. Utekelezaji wa miradi hii yote unategemewa kukamilika ndani ya kipindi cha mkataba ambacho kinaishia mwezi Aprili, 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafikisha mawasiliano ya simu katika Kata ya Kinungu, Isakamaliwa, Mtungulu, Kining’inila na Itumba?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafikisha huduma za mawasiliano ya simu katika Kata za Kinungu, Isakamaliwa, Mtungulu, Kining’inila na Itumba katika Jimbo la Igunga mwaka wa fedha 2022/2023 kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.

Mheshimiwa Spika, Zabuni ya miradi hii itatangazwa kabla ya mwaka wa fedha wa 2021/2022 kukamilika. Ahsante.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaipatia gari Ofisi ya Zimamoto ya Wilaya ya Igunga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa Mbunge wa Igunga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya magari kwa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Nchini. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga bajeti ya jumla ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa magari matano ya kuzima moto ambayo yatasambazwa katika mikoa na wilaya zenye upungufu wa magari ya zimamoto na uokoaji nchini ikiwemo Wilaya ya Igunga. Kwa sasa Wilaya ya Igunga inahudumiwa na gari la zimamoto lililopo Mkoani Tabora.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuliongezea wataalam na vitendea kazi ikiwemo magari ya kuzimia moto na uokoaji kwa ajili ya kuzifikia wilaya zote nchini kutegemea upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je, nini kauli ya Serikali juu ya wateja waliolipia shilingi 27,000 ambao wanatakiwa kulipa fedha zaidi ili kuunganishiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA MADINI K.n.y. WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa uunganishaji umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 kwa maeneo yote ya mjini na vijijini, wateja wengi sana walijitokeza na bei ziliporudi za awali, wateja takribani 80,000 walibaki bila kuunganishiwa umeme na walikwishalipia huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, msimamo wa Serikali uliotekelezwa na TANESCO ulikuwa ni kuwaunganishia umeme wateja wote waliolipia shilingi 27,000 bila kuongeza malipo yoyote. Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2023, wateja wote waliolipia shilingi 27,000 kabla ya Januari, 2022 walikwishaunganishiwa umeme bila kulipa gharama za ziada, ahsante sana.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza kutekeleza mradi wa maji wa Ziwa Victoria kwenda vijiji na vitongoji vya Kata za Nguvumoja, Lugubu na Itumba – Igunga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu spika, katika jitihada za kuboresha huduma ya maji safi na salama kwenye Kata za Nguvumoja, Lugubu na Itumba zilizopo Wilaya ya Igunga, Serikali inatekeleza mipango ya muda mfupi na muda mrefu, ambapo katika mpango wa muda mfupi kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itafunga pampu za kutumia Nishati ya umeme jua katika visima virefu vya Vijiji vya Nguvumoja, Mwanshoma, Lugubu na Itumba ili kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji na kupunguza gharama za uendeshaji wa miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Serikali imepanga kufanya utafiti wa maji ardhini na kuchimba kisima kirefu katika Kijiji cha Chagana kilichopo Kata ya Lubugu katika kipindi cha Mwezi Desemba, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa muda mrefu, Serikali itaboresha huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza katika Kata za Nguvumoja, Lugubu na Itumba – Igunga kwa kutumia mradi wa maji wa Ziwa Victoria ambapo upembuzi yakinifu na usanifu wake wa kina umekamilika na utaanza utekelezaji mara fedha zitakapopatikana.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaweka taa za kuongoza magari Igunga Mjini kwenye makutano ya barabara kuu ya Singida – Mwanza ili kuepusha ajali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2022/23, imepanga kuweka taa za kuongozea magari katika Mji wa Igunga sehemu tatu tofauti kulingana na uhitaji wa sehemu hiyo. Mkandarasi wa kufanya kazi hiyo amepatikana na kukabidhiwa kazi tangu tarehe 01 Aprili, 2023, ahsante. (Makofi)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-

Je, Serikali inatoa tamko gani kwa mabasi yasiyoingia stendi na ambayo hushusha abiria nje ya stendi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mabasi yote ya masafa marefu hupangiwa ratiba na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ambazo huonyesha stendi za kupakia na kushusha abiria pamoja na muda wa kusimama kwenye stendi hizo. Aidha, mabasi ya masafa marefu yamepangiwa kusimama katika stendi moja tu kwa kila Mkoa isipokuwa pale ambapo basi hilo lina abiria anayeshuka katika stendi ya Wilaya. Utaratibu huo umepangwa ili kuondoa usumbufu na ucheleweshaji wa abiria wa masafa marefu kwa kuwalazimisha kuingia kwenye stendi hata kama hawana abiria wa kupanda au kushuka.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Ngassa anatoka Igunga, naomba kumtaarifu kuwa, Stendi ya Igunga haimo kwenye stendi ambazo mabasi ya masafa marefu hulazimika kuingia ama kusimama isipokuwa kama yana abiria wa kupanda au kushuka kwenye stendi hiyo. Hata hivyo, stendi hiyo hutumika kwa magari yote yanayotoa huduma ndani ya Mkoa wa Tabora na Mikoa jirani.

Mheshimiwa Spika, kwa madereva wanaokaidi kuingia stendi na kushushia abiria nje ya stendi hususan barabarani, madereva hao wanakiuka maelekezo ya Kifungu cha 50(1) cha Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 kinachomzuia mtu yeyote kuegesha au kusimamisha gari barabarani bila kujali watumiaji wengine wa barabara, hivyo, huvunja Sheria. Ahsante.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Gereza la Wilaya ya Igunga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Gereza la Igunga lilianza kujengwa mwaka 2004 na lilifunguliwa rasmi mwaka 2006. Hadi sasa mabweni mawili ya wanaume yenye uwezo wa kulala wafungwa 51 kila moja yamekamilika na ujenzi wa jengo la utawala sambamba na nyumba za askari unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi za kukamilisha ujenzi wa Gereza hili zinaendelea na fedha kiasi cha shilingi 77,694,000 zimetengwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya umaliziaji wa jengo la utawala. Nashukuru.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Shule ya Sekondari ya Igurubi iliyopo katika Wilaya ya Igunga kuwa ya kidato cha tano na cha sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, Mbunge wa Jimbo la Igunga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya shule zilizopendekezwa katika Tarafa ya Igurubi kuwa shule za A level ni Igurubi Sekondari na Mwamakona Sekondari. Suala lililokwamisha shule ya Igurubi kutosajiliwa ni kutokuwa na miundombinu Kama bweni, bwalo na miundombinu mingine wezeshi. Hivyo shule ikikidhi vigezo kwa mujibu wa miongozo na taratibu, itasajiliwa kuwa ya Kidato cha Tano na Sita.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa Kituo cha Polisi Tarafa ya Igurubi - Igunga utakamilika?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kituo cha Polisi Igurubi ulianza mwaka 2018 kwa kushirikisha nguvu za wananchi na ulisimama mwaka 2020 baada ya kukosa fedha. Tathmini kwa ajili ya kumaliza ujenzi ili kuunga mkono jitihada za wananchi imeshafanyika ambapo kiasi cha fedha shilingi 53,000,000 zinahitajika. Fedha hizo zinatarajiwa kutengwa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2024/2025, ahsante.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA K.n.y. MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa uzio katika Shule ya Sekondari ya Igunga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023/2024 Serikali imepeleka shilingi milioni 58 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili na matundu matano ya vyoo katika Shule ya Sekondari Igunga kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita. Mwaka 2024/2025 Halmashauri ya Igunga kupitia mapato ya ndani imetenga shilingi milioni 55 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa uzio katika Shule ya Sekondari Igunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa uzio kwa ajili ya ulinzi wa mali na wanafunzi wa bweni, hata hivyo, kwa sasa kipaumbele cha Serikali Kuu ni ujenzi wa miundombinu ya msingi inayowezesha kuongeza nafasi za udahili wa wanafunzi.