Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma (21 total)

MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha jamii inarudi katika maadili mema kutokana na ongezeko la mmomonyoko wa maadili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu kujibu swali kama Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba dakika moja niweze kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii kwa uhai na kila kinachotokea kwenye maisha yangu likiwemo na hili. (Makofi)

Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama yangu Daktari Samia Suluhu Hassan kwa imani hii kubwa aliyonipa na nimuahidi ya kwamba nitatekeleza majukumu yangu kwa weledi tuwatendee haki wananchi tunao wahudumia. (Makofi)

Niwashukuru sana wananchi wa Muheza kwa kuendelea kuniunga mkono na ushirikiano mkubwa wanaonipa na niwahakikishie Muheza bado Mbunge mnaye na nitahakikisha nawaheshimisha. (Makofi)

Nikushukuru wewe Spika na Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania kwa miongozo na maelekezo ya kila mara, hili ni darasa kubwa na ninaendela kujifunza. Mwisho niishukuru familia yangu mke na watoto wangu kwa mapenzi mengi yanayofanya kichwa changu kiendelee kutulia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, nijibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inachukua hatua zifuatazo ili kukabiliana na hali hiyo: -

(i) Wizara imeaandaa mwongozo wa maadili na utamaduni wa Mtanzania uliozinduliwa Tarehe 02 Julai, 2022 ambao unaendelea kusambazwa;

(ii) Kutoa elimu ya maadili na kufanya uhamasishaji wa mabadiliko ya fikra na vitendo kwa jamii kupitia Vyombo vya Habari. Mathalani, katika kipindi cha Januari – Aprili, 2023 Wizara imefanya vipindi 11. Pia Maafisa Utamaduni kutoka Halmashauri 16 kati ya Halmashauri 184 nchini wamefanya vipindi 21 kupitia vyombo vya Habari;

(iii) Kutoa elimu ya maadili kwa wadau wa malezi na makuzi ikiwemo Viongozi wa Dini, wamiliki wa vituo vya malezi na shule za awali na Wasanii. Aidha Wizara inameandaa mdahalo na semina maalum kwa Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wakati wa Tamasha la Pili la Kitaifa la Utamaduni litakalofanyika Mkoani Njombe tarehe 19-21 Mei, 2023;

(iv) Wizara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Viongozi wa Dini, Machifu na Viongozi wa Kimila pamoja na Wizara zenye dhamana ya malezi na makuzi ya watoto na vijana pamoja na usimamizi wa maadili nchini katika kuandaa na kutekeleza mikakati ya pamoja, ahsante.
MHE. KASSIM HASSAN HAJI K.n.y. MHE. SALIM MUSSA OMAR aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuandaa Filamu zenye kueleza Historia ya Nchi?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salim Mussa Omar, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Filamu Tanzania kwa kushirikiana na wadau imewezesha uzalishaji wa filamu zinazohifadhi na kuelezea historia ya nchi yetu.

Mfano Makala ya Uzalendo iliyoandaliwa na Bodi ya Filamu mwaka 2021 kupitia muandaaji filamu Bwana Adam Juma inaelezea historia ya viongozi wetu na ushujaa wao katika kuipambania nchi. Pia, mwaka 2022 Bodi kupitia Studio za Wanene iliandaa makala inayotangaza mandhari ya kupiga picha za filamu na kuelezea maeneo ya kihistoria yaliyopo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Bodi ya Filamu inaendelea na maandalizi ya filamu inayohusu maisha ya Chifu Mkwawa iitwayo Mkwavinyika. Pia kwa kushirikiana na wadau wa filamu, Bodi inaratibu mpango mahsusi wa uandaaji wa filamu zinazohusu maisha ya viongozi wetu, ambapo itaanza na filamu ya Bibi Titi Mohammed, ikifuatiwa na ya Chifu Kingalu, Mtemi Mirambo pamoja na Mwalimu Nyerere.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakuja na mpango wa kuitumia Bahari kwa michezo mbalimbali ya majini ili kuongeza kipato cha wananchi wa Jimbo la Kawe?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Taifa ya mwaka 1995, Ibara ya 7(i) hadi (vi), jukumu la ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya michezo ni jukumu la Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa pamoja na wadau wa sekta ya michezo zikiwemo taasisi, mashirika na watu binafsi. Hata hivyo, Wizara kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wako katika mkakati wa kuziendeleza fukwe za Kunduchi na Kigamboni katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kukuza mchezo wa Soka la Ufukweni ambao tayari TFF wameshaanzisha Ligi yake ambayo ilianza tangu Tarehe 19/08/2023 na inafanyika kwa siku za Jumamosi na Jumapili katika fukwe za Koko, na jumla ya Timu 16 zinashiriki Ligi hiyo. Aidha, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kuwa mwezi Julai, 2023, Timu ya Taifa ya Soka la Ufukweni ilishiriki mashindano ya mchezo huo Barani Afrika yaliyofanyika Nchini Tunisia na kushika nafasi ya tatu, nyuma ya Morocco na Senegal.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa rai kwa wadau wa michezo mingine kama Mitumbwi na Ngalawa, Kuogelea, Mpira wa Kikapu na Wavu kuwekeza katika michezo hii ya ufukweni na kuziendeleza fukwe tulizonazo ili kukidhi matakwa ya michezo yao, kwani pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi, michezo hii pia inasaidia kuimarisha afya na kutoa burudani kwa wananchi.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA K.n.y. MHE. NORAH W. MZERU aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kuwawezesha wadau wa michezo kuwekeza katika kuzalisha vipaji vya michezo hasa mpira wa miguu?

NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, na kwa ridhaa yako, naomba nitumie sekunde chache kuwapongeza vijana wetu wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa ushindi wa goli moja kwa bila walioupata dhidi ya Niger jana, ushindi ambao unatuweka katika nafasi nzuri na uwezekano mkubwa wa kuweza kupata nafasi ya kushiriki katika Fainali za Mataifa ya Afrika zitakazochezwa mwakani kule Senegal. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo niliwaahidi jana ile milioni 10 yao ya goli la mama kutoka kwa shabiki na mwezeshaji namba moja wa timu ya Taifa itawafikia leo kwa sababu mama hana kona kona, akishaahidi lazima litekelezwe, ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, Mbunge wa Viti Maalum lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Abubakari Asenga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali katika kuwezesha wadau kuwekeza kwenye uzalishaji wa vipaji vya michezo hasa mpira wa miguu imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuweka miongozo mahususi ya uanzishwaji na uendeleshaji wa shule maalum za kuibua; kukuza na kuendeleza vipaji (sports academies); kuweka mfumo madhubuti wa usajili wa academia na vituo vya michezo; kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo kama vile nyasi bandia na viambata vyake; kutoa utaalamu na ushauri katika ujenzi wa miundombinu ya michezo; na kuandaa mashindano ya UMISETA kwa shule za sekondari na UMITASHUMITA kwa shule za msingi ili kuwashindanisha, kuibua na kuendeleza vipaji vyao, ahsante.
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID aliuliza:-

Je, TFF inashirikianaje na ZFF kupandisha hadhi Ligi ya Zanzibar na kuendeleza vipaji vya wachezaji wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, Mbunge wa Jimbo la Magomeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) chini ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imekuwa ikishirikiana na ZFF katika mipango mbalimbali kwa lengo la kuendeleza Soka la Tanzania. Kwa sasa Bodi ya Ligi ipo katika mchakato wa kuandaa mafunzo ya uendeshaji wa Bodi ya Ligi ya Zanzibar ambayo kimsingi yatalenga namna ya uendeshaji wa Bodi ya Ligi katika masuala ya menejimenti, ligi na masuala ya uwekezaji, udhamini na masoko.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kuibua vipaji, TFF imekua ikishirikiana na ZFF katika uteuzi wa wachezaji katika timu za Taifa za Vijana, ambapo vijana kutoka Zanzibar wamekuwa wakiitwa katika vikosi vya timu ya Taifa ya vijana na hatimaye kucheza katika timu ya Taifa ya wakubwa (Taifa Stars), ahsante.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, mchakato wa kuwa na Vazi la Taifa umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iliunda Kamati ya Kitaifa ya kuratibu upatikanaji wa Vazi la Taifa. Kamati hiyo imefanikiwa kukusanya maoni kutoka kwa wadau na wananchi 2,452 kutoka Mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kuwa, Kamati itakutana ili kuwashindanisha wabunifu wa mavazi (designers), kutoka pande zote mbili za Muungano ili wale watakaokuwa washindi kwa upande wa wanaume na wanawake mavazi yao ndiyo yatakayopendekezwa kuwa vazi la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wabunifu hao watafanya kazi kwa kutumia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau pamoja na wananchi ili kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa vazi la Taifa kwa ufanisi na haraka zaidi. Aidha, tumeamua kutumia njia hii ili kuharakisha mchakato na kupunguza uhitaji wa matumizi ya fedha nyingi za uratibu wa upatikanaji wa vazi la Taifa. Ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaenzi Tamaduni za Makabila ili kulinda maadili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha tunaenzi tamaduni za makabila kwa lengo la kulinda maadili ya Mtanzania Serikali inafanya yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamza ni kuendesha Tamasha la Kitaifa la Utamaduni ambalo hufanyika kila mwaka. Tamsha hilo linashirikisha vikundi vya utamaduni kutoka Mikoa yote ya Tanzania bara na Visiwani, ambalo linahusisha shughuli mbalimbali za kiutamaduni, kama vile maonesho ya vyakula vya asili, urembo na utanashati, michezo ya jadi, teknolojia na sayansi jadia. Pia, Tamasha hilo linahusisha mashindano ya ngoma za asili, upishi na uandaaji wa vyakula vya asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sambamba na hayo, Tamasha hilo huambatana na mdahalo wa namna ya kupambana na mmomonyoko wa maadili. Hivyo kupitia tamasha hilo, wananchi wanasherehekea, wanaenzi, wanatunza na kuendeleza tamaduni zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili Serikali inaendelea kutumia majukwaa mbalimbali kama vile makongamano, semina, mikutano na warsha kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuthamini utamaduni na maadili ya Mtanzania

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, inaendelea kufanya Tafiti mbalimbali ili kubaini mila na desturi zinazo kubalika katika jamii ili ziendelezwe na zisizofaa waachane nazo, ambapo hadi sasa jumla ya tafiti 286 kuhusu mila na desturi za maeneo ya Kihistoria zimefanyika;

Mheshimiwa Mwenyekiti na mwisho inaendelea kushirikiana na wadau na kuwahimiza kufanya matamasha mbalimbali ya utamaduni nchini kote, ili kuhakikisha mila, desturi na tamaduni zetu zinalindwa na kuendelezwa.
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -

Je, mchakato wa kuwa na Vazi la Taifa umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo iliunda Kamati ya Kitaifa ya kuratibu upatikanaji wa Vazi la Taifa. Kamati hiyo imefanikiwa kukusanya maoni kutoka kwa wadau na wananchi 2,452 kutoka Mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kuwa, Kamati itakutana ili kuwashindanisha wabunifu wa mavazi (designers), kutoka pande zote mbili za Muungano ili wale watakaokuwa washindi kwa upande wa wanaume na wanawake mavazi yao ndiyo yatakayopendekezwa kuwa vazi la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wabunifu hao watafanya kazi kwa kutumia maoni na mapendekezo yaliyotolewa na wadau pamoja na wananchi ili kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa vazi la Taifa kwa ufanisi na haraka zaidi. Aidha, tumeamua kutumia njia hii ili kuharakisha mchakato na kupunguza uhitaji wa matumizi ya fedha nyingi za uratibu wa upatikanaji wa vazi la Taifa. Ahsante.
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR aliuliza: -

Je, ni kwa kiasi gani BAKITA na BAKIZA zinaondoa changamoto za matumizi ya Lugha ya Kiswahili Kitaaluma na kijamii?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdalla Ameir, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Kiswahili BAKITA na BAKIZA yameendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto za matumizi sahihi ya Kiswahili kitaaluma na kijamii zikiwemo, kuandaa semina za ukalimani; kusanifisha maneno mara tu yanapoibuka kutokana na maendeleo ya Sayansi na teknolojia na ongezeko la matumizi ya mitandao ya kijamii, kutoa elimu ya matumizi fasaha na sanifu ya Lugha kupitia vipindi vya redio na televisheni, kuandaa makongamano ya Idhaa za Kiswahili Duniani kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya Lugha, kupitia vitabu mbalimbali vilivyoandikwa kwa Kiswahili kwa lengo la kuhakiki usahihi wa Lugha na kutoa ithibati, kuwapiga msasa wataalam wa Kiswahili na kuwapatia mbinu za kufundisha Kiswahili kwa wageni na kusambaza msamiati wa Kiswahili kupitia mitandao ya kijamii.
MHE. DKT.CHARLES S. KIMEI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaboresha uwanja wa michezo katika eneo la Polisi Himo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Charles Stephen Kimei, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inayo nia ya dhati kuhakikisha kwamba uboreshaji wa miundombinu ya michezo nchini unafanikiwa ili kukuza ushiriki wa michezo na kuibua vipaji. Katika kufanikisha suala hili, Serikali imekuwa ikiwahimiza wamiliki wa viwanja na wadau mbalimbali wa michezo kushiriki katika kujenga na kuboresha miundombinu ya michezo katika maeneo mbalimbali nchini kama Sera ya michezo inavyoelekeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali inahimiza wamiliki wa uwanja wa michezo wa Polisi Himo kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta binafsi katika kuboresha uwanja huo. Aidha, Wizara ipo tayari kutoa ushauri wa kitaalam kwa wamiliki na wadau wanaokusudia kujenga ama kuboresha miundombinu ya michezo nchini.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itafanya ukarabati mkubwa wa Uwanja wa Mpira wa Ali Hassan Mwinyi - Tabora ili utumike AFCON 2027?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa ukarabati wa Uwanja wa Mpira wa Ali Hassan Mwinyi uliopo Tabora pamoja na viwanja vingine hapa nchini na imeendelea kusisitiza wadau na wamiliki wa viwanja kujenga na kutunza miundombinu hiyo sawa na maelekezo ya Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995 sehemu ya 7(1)-(6).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivi sasa Serikali inajenga na kukarabati viwanja vitakavyotumika katika mashindano ya AFCON 2027 ambavyo ni Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam, Amaan Zanzibar na Uwanja mpya wa Dkt. Samia Suluhu Hassan unaojengwa katika Jiji la Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ipo tayari kutoa ushauri wa kitaalam wa namna bora ya kujenga, kukarabati na kuhudumia miundombinu mbalimbali ya michezo kulingana na mahitaji.
MHE. NORAH W. MZERU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wadau wa michezo kuwekeza katika kuzalisha vipaji vya michezo mbalimbali hasa mpira wa miguu?
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Norah Waziri Mzeru, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inayo mikakati mbalimbali ya kuwawezesha wadau wake kuwekeza katika kuzalisha vipaji vya michezo hususan mpira wa miguu ikiwemo kuandaa miongozo na kanuni mahususi zinazowalinda wadau wanaoanzisha shule maalumu za kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo (sports academies) ili kuhakikisha wananufaishwa na uwekezaji wanaoufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua kadhaa nyingine, Serikali inawaunganisha wadau hao na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania kupitia programu kadhaa za kuibua na kuendeleza vipaji zikiwemo UMITASHUMTA, UMISETA na UMISAVUTA. Aidha, Serikali imeanzisha mafunzo ya elimu ya michezo ngazi za Astashahada na Stashahada katika vyuo sita nchini vikiwemo Vyuo vya Ualimu Butimba, Korogwe, Mpwapwa, Monduli na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya. Hali kadhalika, Serikali inaendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo ya shahada ya kwanza katika elimu ya michezo kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza idadi ya wataalamu wa kufundisha michezo ili kupunguza gharama za uwekezaji.
MHE. RAMADHANI SULEIMAN RAMADHANI K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaamua kuwekeza kwa nguvu katika Viwanja, Walimu na Mawakala wa michezo inayoonekana kuleta tija kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, ambalo limeulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan, Mbunge wa Chakechake, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza ujenzi wa viwanja vya mpira wa miguu vya Arusha, Dodoma, Fumba-Zanzibar, Ilemela Jijini Mwanza pamoja na Akademia na Hosteli katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya. Vilevile, Serikali inaendelea na ukarabati wa Viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru – Dar es Salaam, Amani na Gombani vya Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya CHAN 2023 na AFCON 2024. Aidha, Serikali inaendelea na mpango wa ukarabati wa miundombinu ya shule 56 za michezo pamoja na viwanja vitano vya mpira wa miguu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kuwa kuna walimu wa kutosha wa michezo, Serikali imekuwa ikiongeza udahili katika vyuo vinavyotoa mafunzo ya walimu wa michezo, hususan Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hadi kufikia mwaka 2023/2024 jumla ya wanafunzi 812 wamehitimu katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa imeendelea kusajili Mawakala wa Michezo mbalimbali, ambapo jumla ya mawakala 233 walisajiliwa kuanzia mwaka 2018 hadi mwezi Desemba, 2023, ahsante.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA aliuliza: -

Je, kwa nini Tamaduni za kigeni zimetawala sanaa zetu kuliko utamaduni wetu wakati BASATA ipo kuhimiza na kukuza utamaduni wetu?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kuu zinazosababisha tamaduni za kigeni kutawala kwenye sanaa zetu ni utandawazi pamoja na ukuaji wa teknolojia. Sababu hizi zimesababisha dunia kuwa kijiji hali inayotoa fursa kwa wasanii kupitia majukwaa ya kidigitali kuona mambo mbalimbali yanayofanyika duniani na kuyaiga na hivyo, kuathiri sanaa ya kitanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linafanya kazi ya kufufua, kukuza na kuendeleza sanaa zenye asili ya Kitanzania kupitia program mbalimbali mfano: Sanaa Mtaa kwa Mtaa na BASATA Vibes ili kutoa elimu kwa wasanii kuhusu umuhimu wa kuzienzi tamaduni zetu kupitia kazi za sanaa, kushirikiana na wadau wa sanaa kuandaa matamasha mbalimbali yanayolenga kutangaza utamaduni wetu. Hata hivyo, BASATA inaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wadau wa sanaa wanaokiuka kanuni za maadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, BASATA kwa kushirikiana na Kamati Maalum imetengeneza Kivunge cha Mtozi (Producers Kit) chenye vionjo zaidi ya 400 vya midundo ya makabila ya Kitanzania kitakachowezesha wasanii wa muziki kutumia midundo na vionjo vyenye asili ya Tanzania.
MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. AZIZA S. ALLY aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kuanzisha Kombe Maalum la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa anajitoa sana kwenye Sekta ya Michezo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Watanzania wanatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta ya michezo nchini. Katika kuenzi mchango huo, tayari tumeelekeza vyama na mashirikisho ya michezo nchini kuona namna bora ya kuwa na kombe maalum la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ukubwa zaidi kwa michezo wanayoisimamia, lengo likiwa ni kuwa na mashindano makubwa ya Kitaifa yatakayohusisha michezo mbalimbali yatakayofahamika kama Samia Taifa Cup kuanzia ngazi za chini na tayari Wizara imegawa vifaa katika mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa wadau tofauti wameanzisha mashindano mbalimbali yanayotumia jina la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo ni pamoja na Ligi ya Mama Samia Mshikamano Cup (Mbeya Mjini); Dr. Samia Katambi Cup (Shinyanga); Simiyu Samia Marathon; Dkt. Samia Cup (Same); Chato Samia Cup (Chato); na Samia Afya Cup ambayo ni mashindano yanayoandaliwa na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma na binafsi na mashindano mengine mengi.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kiwanja cha michezo cha Kisasa Mkoani Njombe?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali ipo kwenye ukarabati wa viwanja vya Uhuru na Benjamin Mkapa, ujenzi wa uwanja wa Arusha (Arusha Stadium) na kukarabati viwanja vingine vitano (5) vya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2024 na AFCON 2027. Kama sera ya michezo inavyoelekeza, ujenzi wa miundombinu ya michezo ikiwemo viwanja ni jukumu la Serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Baada ya kukamilisha ujenzi wa viwanja kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2024 na AFCON 2027, Serikali itatoa maelekezo kwa uongozi wa Mikoa yote ili kutekeleza mkakati wa ujenzi wa miundombinu ya michezo katika Mikoa yote. nakushukuru.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Viwanja vya Michezo nchini katika ngazi ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la ujenzi wa miundombinu ya michezo ni la Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Michezo zikiwemo taasisi, mashirika, watu binafsi na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Katika kuhakikisha kuwa kila Wilaya inakuwa na viwanja vya michezo, hivi karibuni Serikali itazielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga mafungu katika bajeti zao ili kutekeleza miradi ya ujenzi wa viwanja vya michezo kwa maeneo yao. Tayari kuna halmashauri zimeanza utekelezaji huu ambazo ni:-

Halmashauri za Wilaya za Kinondoni (Uwanja wa KMC), Bukoba Mjini (Uwanja wa Kaitaba), Nyamagana (Uwanja wa Nyamagana) na Namungo (Majaliwa Stadium). Aidha, Halmashauri ya Wang’ing’ombe inajenga Kijiji cha Michezo ambacho kitakapokamilika kitakuwa na viwanja vya michezo ya soka, volleyball, Netball na Basketball. Pia, Halmashauri ya Sengerema, Mkoani Geita imeandaa ‘Concept Design’ kwa ajili ya kituo cha michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali ipo kwenye ukarabati mkubwa wa viwanja vya Uhuru na Benjamin Mkapa. Hata hivyo, Serikali inaendelea na ujenzi wa Uwanja wa Arusha (Arusha Stadium) na ukarabati wa viwanja vingine vitano vya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2024 na AFCON 2027. Hivyo basi, nitoe rai kwa halmashauri, wilaya na mikoa ambayo haijaguswa na miradi ya AFCON 2027 kuanza kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kujenga viwanja vya kisasa vya michezo ili pia wapate vyanzo vipya vya makusanyo ya maduhuli katika maeneo yao. Nashukuru. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kiwanja cha michezo cha Kisasa Mkoani Njombe?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali ipo kwenye ukarabati wa viwanja vya Uhuru na Benjamin Mkapa, ujenzi wa uwanja wa Arusha (Arusha Stadium) na kukarabati viwanja vingine vitano (5) vya mazoezi kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2024 na AFCON 2027. Kama sera ya michezo inavyoelekeza, ujenzi wa miundombinu ya michezo ikiwemo viwanja ni jukumu la Serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Baada ya kukamilisha ujenzi wa viwanja kwa ajili ya mashindano ya CHAN 2024 na AFCON 2027, Serikali itatoa maelekezo kwa uongozi wa Mikoa yote ili kutekeleza mkakati wa ujenzi wa miundombinu ya michezo katika Mikoa yote. nakushukuru.
MHE. ABDUL YUSSUF MAALIM aliuliza:-

Je, tathmini ipoje juu ya utatuzi wa changamoto zitokanazo na Mashirikiano yaliyopo kati ya ZFF na TFF?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa sasa mashirikiano kati ya ZFF na TFF hayana changamoto zozote kwani kazi zinaendelea kwa pamoja kwa manufaa ya pande zote za Muungano kwa maendeleo ya mpira wetu. Mathalani mashirikisho haya yanashirikiana katika kuendesha soka la vijana, mashindano yote ya kitaifa ya vijana under 15 na under 17. Aidha, katika mashindano ya CAF na FIFA wawakilishi wetu Taifa Stars, Twiga Stars, na Serengeti Boys hushirikisha wachezaji kutoka katika pande zote mbili za Muungano kulingana na vigezo vya Mwalimu katika uteuzi wa wachezaji husika.

TFF na ZFF pia wamekuwa wakishirikiana vema katika kuendesha mafunzo ya waamuzi pamoja na walimu wa soka kwa kozi zote za CAF na FIFA zinazoendeshwa ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo.

Mheshimiwa Spika, fauka ya hayo, mashirikisho haya yameendelea katika uandaaji wa mashindano ya kimataifa mathalani mashindano ya African Schools Football Championship ambayo yalifanyika mwezi Mei mwaka 2024 katika uwanja wa Amaan Complex, Visiwani Zanzibar na timu ya wavulana ya Taifa kuchukua ubingwa.

Mheshimiwa Spika, TFF kwa kushirikiana na ZFF zimekuwa zikipeleka mashindano mbalimbali Visiwani Zanzibar. Pia fainali za kombe la Shirikisho (FA Cup) kati ya Yanga dhidi ya Azam FC na nusu fainali ya Kombe la Ngao ya Jamii mwaka 2024, mchezo kati ya Coastal Union dhidi ya Azam FC yote ilifanyika katika uwanja wa Amaan. Hali kadhalika, misafara mingi ya Timu ya Taifa ya Tanzania - Taifa Stars imekuwa ikiongozwa na Rais wa ZFF kama Mkuu wa msafara, kuonesha ushirikiano mkubwa uliopo kwa sasa baina ya TFF na ZFF.
MHE. FESTO R. SANGA aliuliza: -

Je, upi mkakati wa kuongeza thamani ya zawadi kutoka shilingi 150,000 hadi milioni kumi kwenye Tamasha la Utamaduni nchini?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tamasha la Utamaduni nchini ni tamasha ambalo limekuwa likisherehekewa na makabila mbalimbali kila moja kwa wakati wake hasa nyakati baada ya mavuno. Matamasha haya hayakuwa na zawadi maalumu zaidi ya kuwa na sherehe kubwa ya kiutamaduni ambayo inakutanisha watu wa kabila moja kula, kunywa na kusherehekea mafanikio ya mavuno yao mfano ikiwa ni Tamasha la Wasukuma la Bulabo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais iliona ni vema kuyaunganisha makabila hayo na kuwa na tamasha moja la kitaifa. Uratibu wa tamasha hili umekuwa ukifanyika na Wizara yetu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mkoa mwenyeji wa tamasha kwa mwaka husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati mkubwa uliofanyika tangu kuanzishwa kwake ni maboresho ya zawadi ambapo kwa tamasha la mwaka 2024 zawadi za fedha zilitolewa kwa vikundi, washindi wa kwanza katika mashindano ya ngoma za asili na uandaaji wa vyakula vya asili ilikuwa ni fedha taslimu shilingi milioni moja, kutoka katika shilingi 150,000 zilizotolewa mwaka kabla ya huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati uliopo hadi sasa pamoja na ukuaji mzuri wa tamasha hili, Wizara inaendelea na maandalizi ya kuwashirikisha wadau wa sekta binafsi ili kupata ufadhili zaidi na kuboresha zawadi ya tamasha lijalo ili tuendelee kulikuza Tamasha la Utamaduni wa Taifa. (Makofi)
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS aliuliza:-

Je, kuna mpango gani kuhakikisha wasanii wanafanya kazi zao kwa uhuru pasipo kuvunja sheria, kanuni na maadili ya Kitanzania?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Wizara yetu kupitia Baraza la Sanaa la Taifa iliandaa Mwongozo wa Uzingatiaji wa Maadili katika Uzalishaji wa Kazi za Sanaa, ambao ulizinduliwa rasmi tarehe 3 Novemba, 2023. Kwa sasa tunaendelea na maboresho ya Kanuni za BASATA za Mwaka 2018 na pia mwongozo wa uendeshaji matukio ya sanaa ili kuweka misingi thabiti ya usimamizi wa matukio hayo.

Mheshimiwa Spika, lengo kuu la maboresho haya ni kulinda maadili katika uzalishaji wa kazi za sanaa na kuwafanya wasanii wajitathmini wenyewe kabla hawajazalisha na kuzitoa kazi hizo kwa walaji. Aidha, BASATA inaendelea kutoa elimu kwa waandaaji wa kazi za sanaa kuzingatia miongozo iliyotolewa kabla ya kuzalisha kazi yoyote iwe ya sauti (muziki) ama ya kutengeneza maudhui mtandaoni.

Mheshimiwa Spika, ninapenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kuwa, BASATA inaendelea kuwaelimisha wasanii ili kuwajengea uelewa wa kulinda maadili ya Mtanzania katika uzalishaji wa kazi zao.