Answers to supplementary Questions by Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma (40 total)
MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali lakini nilikuwa nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itafanya tathmini ya tamaduni ambazo tunazo nchini ambazo haziendani na wakati huu na mila zetu na desturi ambazo zinakwenda kukwamisha?
Mheshimiwa Spika, swali la pili mna mkakati gani wa kuanzisha somo la maadili kwenye mtaala yetu ya elimu hapa nchini? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikibainisha mila na desturi zisizofaa nakuchukua hatua kadhaa, zikiwemo kutoa elimu kwa jamii pamoja na uhamasishaji wa mabadiliko ya fikra na vitendo kutekeleza sera ya utamaduni ya mwaka 1997 Sura ya Nane na kifungu 1.3.
Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, it takes a village to raise a child, kwa hiyo pamoja na wajibu wa Serikali kulinda mila na desturi zetu haiondoi wajibu wa moja kwa moja wa wazazi walezi na jamii kujenga misingi imara ya makuzi ya vijana wetu katika ngazi ya familia na kaya zetu kwa kushirikiana na viongozi wetu wa kimila na viongozi wetu wa dini nchini kote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Bahati, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kutakuwa na somo la maadili kwenye mitaala mipya na itakuwa ni lazima kila mwanafunzi kulisoma. Ahsante. (Makofi)
MHE. KASSIM HASSAN HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kuwa watu wengi ambao wameiona historia ya Tanzania na Zanzibar wameandika vitabu katika historia hii.
Je, ni lini vitabu vile vitatafsiriwa, Serikali itachukua maamuzi ya kutengeneza filamu ya vitabu vile ili kizazi kinachokuja kiweze kujivunia na kuona uhalisia wa historia ya Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kassim Hassan Haji, Mbunge wa Mwanakwerekwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa lengo la Serikali siyo tu kuhifadhi historia ya nchi na mashujaa wetu kwenye filamu, lakini ni kuhifadhi katika kiwango na hadhi inayotazamika kwenye majukwaa ya Kitaifa na ya kimataifa. Kwa hivyo Serikali kwa sasa inafanya juhudi kubwa kuhakikisha uwekezaji mkubwa unaongezwa kwenye tasnia ya filamu nchini kuhakikisha hilo linatokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kudhibitisha hilo, ni juma lililopita tu Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, mama yangu, Mheshimiwa Balozi Pindi Hazara Chana, alihudhuria utiaji saini mkataba wa makubaliano kati ya Bodi ya Filamu Tanzania na Taasisi ya Mashirikiano ya Kimataifa ya Korea Kusini (BFIC), makubaliano ambayo pamoja na mambo mengine yanakwenda kuona uwekezaji mkubwa ukiongezeka kwenye tasnia ya filamu nchini ambapo filamu ambazo unazizungumzia Mheshimiwa zitakwenda kufanywa kwenye kiwango na hadhi inayotazamika kwenye majukwaa ya Kitaifa na ya kimataifa, nashukuru.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara hii inaangalia sana suala la maslahi ya wasanii na michezo kwa ujumla; ni lini Serikali itapitia upya makato inayokata katika mambo ya michezo? Kwa mfano juzi Simba wamepata milioni 180 katika 450; ni lini itapitia makato haya ambayo ni kandamizi?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na swali la Mheshimiwa Mbunge Isack kuwa liko pembeni kabisa ya swali la msingi, lakini kimsingi tunaangalia utaratibu ambao utawezesha vilabu vyetu viweze kuendelea kufaidika zaidi. Lakini kuna gharama kubwa za uendeshaji wa michezo inayotajwa na taasisi zetu zinaingia gharama kubwa ambayo inatoka mifukoni kwao kuweza kuifanya michezo hii ifanikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo pamoja na lengo letu la kuhakikisha timu zetu zinafaidika, lakini kuna gharama kubwa ambazo taasisi zetu zitashindwa kujiendesha kama tutazizuia moja kwa moja kukata makato yale, ahsante.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Je, ni lini Serikali itawapa vitambulisho machifu wetu ili kuweza kuwatambua kwamba ni machifu wa nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Lukago Midimu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha tunawekeza nguvu nyingi kuhakikisha utamaduni wetu haupotei. Na miongoni mwa mambo ambayo yanafanyika ni kutambua uwepo wa machifu wetu. Na hilo limefanywa hata na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukaa kikao na machifu mbalimbali – siyo mara moja – na kuwatambua kwenye masuala mbalimbali ya sherehe za Kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, machifu bado wanatambulika na Serikali, lakini juhudi mbalimbali bado zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha kutambulika kwao kunafahamika Kitaifa na kimataifa. Ahsante. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, katika dhana ileile ya kuendelea kutangaza utalii wa Taifa letu, je, Serikali haioni ni wakati sahihi wa kutengeneza filamu maalum ya kueleza historia ya Ukoo wa Simba wa Bob Junior na namna ambavyo ilisisimua Taifa na dunia kuhusu kifo cha Bob Junior?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Hai, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazo zuri ambalo amelitoa, na sisi kwa kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii tunaomba tulichukue na tutalifanyia kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa nusu ya Jimbo la Kawe kwa maana ya Msasani, Masaki, Oysterbay, Kunduchi, Mbweni, Kawe, Bunju, Sea Cliff na Coco yote iko katika ufukwe wa Bahari ya Hindi. Je, Serikali ina mpango gani maalum wa kuendeleza hii michezo ya Bahari kwa ajili ya afya, burudani na kipato cha watu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri, je, utakubali Jumapili hii tuandamane pamoja tukafungue Ligi ya Rede kwa michezo inofanyika katika Jimbo la Kawe? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kuchukua nafasi hii ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, Josephat Gwajima kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpe pongezi Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kwa kuona fursa kubwa iliyopo katika mchezo wa soka la ufukweni.
Mheshimiwa Naibu Spika, soka la ufukweni katika nchi hii limeanzishwa rasmi mwaka 2014 na ni kwa miaka tisa tu ambayo tumekuwa tukilifanya, lakini limeonyesha kuwa na mafanikio makubwa. Kwa sasa tuko Namba Tano kwa Bara la Afrika kwa soka la ufukweni na Namba 42 kwenye rank za FIFA za kidunia kwa soka la ufukweni, namba ambazo hili soka letu la kawaida hatujawahi kuzifikia na pengine itatuchukua muda mrefu kidogo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mafanikio haya yanatokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na TFF kwa kushirikiana na Serikali, kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunaweka mkazo kwenye michezo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TFF wanao mpango mkakati wa miaka mitano, ambao pamoja na mambo mengine unahakikisha kwamba soka la ufukweni linafundishwa mashuleni na vyuoni na kila Mkoa ambao una fukwe kuweza kuwa na ligi yake kwa ajili ya soka la ufukweni. Lengo ni katika kipindi cha miaka mitano hii inayofuata tuwe na wachezaji angalau 10,000 na kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali imeanzisha mazungumzo na JKT na wadau wengine kadhaa ili kuhakikisha tunaongeza uwekezaji kwa ajili ya soka la ufukweni. Pia, kumekuwa na mashindano ya Copa Dar es Salaam ambayo yanazishirikisha nchi mbalimbali kama Burundi, Uganda, Comoro, Ushelisheli na Malawi, mwaka huu tuna mpango wa kuwaalika Kenya, Oman, Morocco na Senegal. Kwa hiyo, tutakuwa na Ligi ya Soka la Ufukweni yenye nchi Tisa, ambapo ni wazi kabisa itaongeza Pato la Taifa lakini wachezaji wetu wengi watashiriki na itatoa ajira za moja kwa moja na ajira nyingi nyingine zinazozunguka mchezo huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, najua Askofu utakuwa na maono, umengundua kama Jumapili ninao muda na tutaambatana mimi na wewe kwa ajili ya kwenda kuanzisha Ligi yako ya rede pale Jimboni Kawe. Ahsante. (Makofi/Kicheko)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninashukuru Serikali kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, kuna academies za mchezo wa mpira wa miguu kama vile Kilombero Soccernet Academy ambazo zimesajiliwa rasmi na ziko pale Wilaya ya Kilombero, lakini zina uhaba mkubwa wa vifaa.
Je, kwa dharura, Wizara haioni kwamba inaweza ikachukua hatua za kutafuta vifaa, hata kama ni mipira, jersey, ikazipelekea hizi academies ambazo zimesajiliwa rasmi na TFF?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nilimwomba Mheshimiwa Naibu Wazri mipira 100 ya vijijini na aliniahidi atanipatia; je, lini tunakwenda kukabidhi mimi na yeye mipira hiyo Ifakara na kukiamsha pale Ifakara Mjini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kama nilivyosema kwa sasa Serikali inachoweza kufanya kutokana na upatikanaji wa fedha ni kupunguza kodi kwenye vifaa vya michezo kama vile nyasi bandia na viambata vyake. Haya mengine kwa kadri fedha zitakavyopatikana tutaendelea kuvi-support vituo hivi na kuhakikisha vinapata nguvu kupitia Serikalini vilevile, ahsante.
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuirejesha Ligi ya Muungano?
Swali langu la pili, je, ushirikiano wa ZFF na TFF unasaidia Soka la Zanzibar la Wanawake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha Ligi ya Muungano inaanzishwa upya na tunafahamu umuhimu wake kwenye kuimarisha ushirikiano hasa kwenye upande wa michezo. Kwa hivyo, kwa nyakati tofauti TFF na ZFF wamekuwa wakikaa kuangalia namna bora ya kuianzisha tena Ligi ya Muungano, japokuwa wanapata changamoto kwenye kupata udhamini wa kulifanya hili lakini nikuhakikishie dhamira ipo na tutahakikisha Ligi ya Muungano inaanza tena.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu Ligi ya Wanawake, TFF na ZFF zimekuwa zikiendesha program mbalimbali za kiutawala na makocha wanawake kwa Soka la Zanzibar na unaweza kuona miongoni mwa mafanikio ambayo yameshapatikana ni kwa timu za wanawake za Zanzibar kufanya vizuri kwenye mashindano ya CECAFA. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa Kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki na mnafahamu kamati za kitaifa nyingi ni za wazi. Kwa mfano, ile Kamati ya Makinikia mnaikumbuka, kamati ya hamasa ya Taifa Stars inafahamika. Kwa nini, kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki? Je, Serikali wako tayari kuitangaza ili tuwafahamu?
Swali la pili, mchakato ni wa muda mrefu sana nadhani unafahamu. Serikali inahitaji muda gani wa ziada ili kuhitimisha jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Antipas Mgungusi kwamba, Kamati hii haikuwa ya siri. Kamati hii ilitangazwa tarehe 20 Julai, 2022 baada ya kuteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo, Kaka yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa na Mwenyekiti, wake alikuwa Profesa Hermas Mwansoko na Katibu wake alikuwa Dkt. Emmanuel Temu, ikiwa na Wajumbe tisa, wakiwamo Masoud Ali Kipanya, Mrisho Mpoto, Ndugu Khadija Mwanamboka, Ndugu Mwanajuma Ali na wengineo. Kamati hii ilishakamilisha kazi yake kwa hiyo, hili jambo limerudi kwa Wizara kupitia Idara ya Maendeleo ya Utamaduni ndiyo inafanya hatua za mwishoni za kukamilisha mchakato huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni hamu yetu kwenye Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuona kwamba, mchakato huu unakamilika kama ambavyo ni hamu ya Mheshimiwa Mbunge Antipas. Kwa hivyo, mahali ilipofika sasa hivi ni mwishoni kabisa. Hivyo, Idara ya Maendeleo ya Utamaduni inafanya michakato wa kumalizia kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mwaka huu wa 2024 hautakwisha kabla hatujajipatia vazi la Taifa, ahsante. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Kalenga limekuwa kinara wa kuendeleza mila na tamaduni; je, Serikali haioni haja sasa ya kutujengea hata kituo cha utamaduni katika Jimbo hilo la Kalenga ili tuweze kuendeleza utamaduni wetu wa Kihehe? (Makofi)
Swali namba mbili, kwa kuwa Makumbusho ya Mkwawa ambayo ndiyo sehemu ya kuenzi mila na tamaduni zetu yako katika eneo la makaburi ya familia ya Mkwawa na Uchifu wa Mkwawa upo hai. Je, Serikali haioni haja sasa katika vile viingilio wakawa wanatupa hata asilimia moja au mbili ili kuendelea kuimarisha ule utamaduni wetu na uchifu wetu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza ni kuhusuana na kujenga kituo cha utamaduni pele Kalenga, namuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, inaendelea kufanya tathmini ya kutambua maeneo ya kiutamaduni ili kutoa maelekezo mahsusi kwa mamlaka husika za mikoa na wilaya, namna ya kuyaenzi na kuyahifadhi maeneo haya. Kwa hiyo, hili la kujenga kituo cha utamaduni pale Kalenga, namuahidi Mheshimiwa Mbunge ninalichukua na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo italifanyia kazi na muda utakaporuhusu tutaweza kufanya hivyo. (Makofi)
Swali lake la pili kuhusuana na sehemu ya malipo ya maonesho ya kaburi la Chifu Mkwawa kwenda kwa familia, namuahidi Mheshimiwa Mbunge pia nalichukua na tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya Makumbusho ya Taifa kuona namna ambavyo hili linaweza kufanyika na familia ya Chifu Mkwawa ikaweza kufaidika na sehemu ya kiingilio cha makumbusho yale, ahsante. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya utafiti gani ili kujua makabila yaliyoko nchini, kuweza kuyasaidia na kuyaendeleza kuwa kivutio ili kuweza kuiingiza Serikali Pato la Taifa na watalii zaidi ya Wamasai? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi, mpaka sasa tafiti 286 zimeshafanyika, tunachofanya ni mwendelezo wa tafiti hizo na kuona namna ambavyo tunaweza kutumia ufahamu tulioupata kupitia tafiti hizo ili kuyaenzi na kuhifadhi tamaduni za makabila mbalimbali zaidi ya Wamasai hapa nchini, ahsante. (Makofi)
MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa Kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki na mnafahamu kamati za kitaifa nyingi ni za wazi. Kwa mfano, ile Kamati ya Makinikia mnaikumbuka, kamati ya hamasa ya Taifa Stars inafahamika. Kwa nini, kamati hii ya vazi la Taifa haifahamiki? Je, Serikali wako tayari kuitangaza ili tuwafahamu?
Swali la pili, mchakato ni wa muda mrefu sana nadhani unafahamu. Serikali inahitaji muda gani wa ziada ili kuhitimisha jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Antipas Mgungusi kwamba, Kamati hii haikuwa ya siri. Kamati hii ilitangazwa tarehe 20 Julai, 2022 baada ya kuteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo, Kaka yangu Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa na Mwenyekiti, wake alikuwa Profesa Hermas Mwansoko na Katibu wake alikuwa Dkt. Emmanuel Temu, ikiwa na Wajumbe tisa, wakiwamo Masoud Ali Kipanya, Mrisho Mpoto, Ndugu Khadija Mwanamboka, Ndugu Mwanajuma Ali na wengineo. Kamati hii ilishakamilisha kazi yake kwa hiyo, hili jambo limerudi kwa Wizara kupitia Idara ya Maendeleo ya Utamaduni ndiyo inafanya hatua za mwishoni za kukamilisha mchakato huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni hamu yetu kwenye Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuona kwamba, mchakato huu unakamilika kama ambavyo ni hamu ya Mheshimiwa Mbunge Antipas. Kwa hivyo, mahali ilipofika sasa hivi ni mwishoni kabisa. Hivyo, Idara ya Maendeleo ya Utamaduni inafanya michakato wa kumalizia kama nilivyojibu kwenye jibu la msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mwaka huu wa 2024 hautakwisha kabla hatujajipatia vazi la Taifa, ahsante. (Makofi)
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ningeomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza ya ziada na kiada kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Lugha ya Kiswahili imekua kimawanda na kwa upana wake, mwaka 2004 kimeanza kutumika katika mikutano rasmi ya Bunge la Afrika pia Bunge la Afrika Mashariki, Bunge la SADC na pia Kiswahili kimetangazwa siku adhimu duniani kila mwaka tunakiadhimisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko haya makubwa ya kijamii ya Lugha ya Kiswahili, kiuchumi, kiteknolojia na kisayansi hatuoni kwamba sasa imefika wakati kuwe na sera inayojitosheleza ya Lugha ya Kiswahili, badala ya ile Sera ambayo imeegemea ndani ya Sera ya Utamaduni? (Makofi)
Swali langu la pili ni kwamba, Kiswahili hivi sasa tumekibidhaisha ni mikakati gani ya hivi sasa na baadaye ambayo itatumika kukifanya Kiswahili kuwa ni bidhaa bora yenye viwango kifasaha na kiusanifu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la nyongeza la Mheshimiwa Ameir Abdalla Ameir ni kwamba kweli kulionekana kuna haja ya kuwa na Sera inayojitegemea ya Kiswahili badala ya kukiacha Kiswahili kisimamiwe na Sera Mama ya Utamaduni. Majadiliano yalikuwa yanaendelea hata miongoni mwetu wenyewe, pamoja na kuonekana kwamba Kiswahili kinahitaji kusimamiwa na Sera yake binafsi pia kukaonekana kwamba kuna uwezekano Sera Mama ya Utamaduni itapwaya sana kama Kiswahili kitaondolewa kusimamiwa na Sera hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge majadiliano hayo hayajafa yanaendelea na pengine hivi karibuni tutaoa mwongozo wa namna ambavyo tunataka kulifanya jambo hili na pengine Kiswahili kitapata Sera yake binafsi ya kukisimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusiana na kubidhaisha Kiswahili. Ni kweli baada ya Kiswahili kutangazwa kuwa miongoni mwa lugha za kazi, mahitaji ya vitabu, machapisho na magazeti yameongezeka sana na hivyo wigo wa soko la Waandishi wa Kiswahili umepanuka sana nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia BAKITA na BAKIZA tunahakikisha ya kwamba Kiswahili kinabidhaishwa kwa kupelekwa sehemu mbalimbali Duniani na hivi navyoongea vipo vituo 43 kwa ajili ya kufundishia Kiswahili Dunia. Vituo 16 kati ya hivyo vikiwa nje ya nchi na 11 vikiwa katika Balozi zetu mbalimbali Duniani kama Ufaransa, Uturuki, Uholanzi, Italia, Korea Kusini, Umoja wa Falme za Kiarabu, Mauritius, Sudan, Nigeria, Cuba na Zimbabwe. Hali kadhalika kwa sasa BAKITA na BAKIZA wameendelea kuadhimisha siku ya Kiswahili Duniani ambayo ni tarehe 07 Julai ya kila mwaka na mwaka jana ilifanyika Zanzibar, pia hiyo ni kutii wito wa UNESCO ambao walipitisha siku hiyo kuwa siku ya Kiswahili Duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ya kwamba tunafanya kila ambalo lipo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha Kiswahili kinasambaa zaidi na mikakati tuliyonayo ni kuhakikisha tunakuwa na vituo vingi zaidi vya kufundishia Kiswahili katika nchi mbalimbali Duniani, ahsante.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, inaonekana kwamba Serikali haina mkakati madhubuti wa kujenga viwanja kwenye maeneo ya vijiji na maeneo mengine nchini. Naomba niulize maswali mawili mengine ya zaida.
Swali la kwanza, je, endapo tutaweza kuhamasisha wananchi wetu pale Himo ambapo kusema kweli kwenye Jimbo letu hatuna kiwanja chochote tukasawazisha, Serikali itakuwa tayari kutupa support ya nyasi bandia?
Swali la Pili, ni kwamba tunajua Serikali sasa inaingia kwenye mitaala mipya ya elimu ambapo tunahamasisha mkondo wa amali na michezo ni mmojawapo, hili halitafanikiwa kama kwenye maeneo tunayoishi hakuna sehemu za kufanyia michezo ya aina mbalimbali na kukuza stadi zetu.
Je, Serikali inaweza kutoa kauli gani kuhusiana na suala hili zima la kusaidia kukuza stadi za michezo mbalimbali kwenye maeneo yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge Dkt. Charles Kimei kwa swali ambalo halina maslahi na manufaa kwa vijana na wanamichezo kwa ujumla wa Jimbo la Vunjo na Mkoa wa Kilimanjaro pekee yake bali kwa nchi nzima. Namshukuru kwa moyo huo wa kiuanamichezo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inayo nia thabiti ya kujenga, kukarabati na kuboresha miundombinu mbalimbali ya michezo. Mheshimiwa Mbunge atakuwa anafahamu mipaka mizito ya kibajeti ambayo Wizara yetu inayo lakini tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha kuona namna ambavyo tunaweza kuongezewa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hii.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali ina mpango wa kukarabati viwanja saba vikubwa vya michezo nchini vikiwemo viwanja vya Jamhuri wa Morogoro, Jamhuri wa Dodoma, Sokoine wa Mbeya, Majimaji wa Songea, Mkwakwani Tanga na vinginevyo ili kuhakikisha tunakuwa na maeneo thabiti kabisa ya kufanya shughuli za michezo katika Mikoa husika.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika, kwa sasa Serikali imechagua shule 56, shule mbili katika kila Mkoa wa Tanzania Bara kwa ajili ya kuzitengeneza kuwa shule maalum za michezo na kwa kuanzia tunaanza na shule tisa kwa sasa. Hii itasaidia kuongeza miundombinu ya michezo mashuleni na tunashirikiana kwa ukaribu na Wizara ambayo ina dhamana ya Elimu na wenzetu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika kuhakikisha hili linatendeka.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba wakisawazisha uwanja kama tunaweza kuwapatia nyasi bandia. Kama nilivyojibu tatizo letu kubwa ni mipaka ya kibajeti ambayo tunayo lakini nitahakikisha nashirikiana na Mheshimiwa Mbunge na Wananchi wa Vunjo kupata wadau kwa ajili ya kuwatafutia nyasi bandia wananchi hao kama watasawazisha uwanja wao, ahsante. Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alielekeza Serikali na Chama cha Mapinduzi mkae kwa ajili ya kurekebisa viwanja saba vya michezo; je, mmefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu kwenye swali la nyongeza la Dkt. Kimei, viwanja hivi viko katika mipango yetu na sasa hivi tuko katika hatua ya kutafuta wakandarasi kwa ajili ya kukarabati viwanja hivi saba.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ni kwa nini Wizara hii isishirikiane na TAMISEMI kuhakikisha inaboresha na kujenga miundombinu ya michezo kwenye shule zote za sekondari na msingi nchini kwa sababu kuna shule zingine hazina miundombinu hii?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu pia, mpango wetu ni kutengeneza viwanja vya michezo yote ya kipaumbele kwenye shule 56, shule mbili kwenye kila Mkoa wa Tanzania Bara kwa Mikoa 28 kwa sasa, kwa hiyo tunaendelea kushirikiana na wenzetu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kufanya jambo ambalo Mheshimiwa Mbunge analisema.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa kuanza kufikiria kuuboresha Uwanja wa Jamhuri wa Morogoro kwa sababu ni uwanja wa Kimataifa na wanachezea michezo ya Kitaifa. Je, ni lini mtaanza kuuboresha uwanja huu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi rasilimali fedha itakapokuwa imekaa sawasawa kwenye Wizara yetu tutaanza kuukarabati Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kumekuwa na taarifa mbalimbali kwamba kuna viwanja ambavyo vitakwenda kufanyiwa ukarabati na Serikali. Je, kiwanja cha Ali Hassan Mwinyi kilichopo Tabora ni moja kati ya viwanja vitakavyofanyiwa ukarabati huo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kutokana na Serikali kutokuwa na viwanja vingi vya michezo nchini, Serikali ina mkakati gani wa kukaa na Chama Cha Mapinduzi, kuzungumza nao na kuona namna bora ya kuchukua viwanja hivi vya michezo ambavyo wanavyo ili viweze kwenda Serikalini na viweze kufanyiwa ukarabati ili tuweze kukuza michezo nchini? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi, kwa sasa Serikali inaweka mkazo kwenye kumalizia miundombinu ya viwanja vya michezo vitakavyotumika kwa ajili ya AFCON 2027. Aidha, kwa kujenga miundombinu mipya kama tunavyofanya kwenye uwanja wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Arusha, ama kukarabati kama ilivyofanyika kwa uwanja wa Amani na uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo ukarabati unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo Serikali inaendelea na mpango wa kukarabati kwa awamu viwanja mbalimbali vilivyopo katika majiji, mikoa, halmashauri na manispaa kote nchini na uwanja wa Ali Hassan Mwinyi utakuwepo katika awamu zitakazofuata. Kwa sasa Serikali imeanza na viwanja vitano ambavyo ni Uhuru uliopo Dar es Salaam, Mkwakwani uliopo Tanga, Jamhuri uliopo Morogoro, Maji Maji uliopo Songea na Sheikh Amir Abed uliopo Arusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili, mazungumzo kati ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi kuhusiana na kukabidhiwa viwanja vyake ili vifanyiwe ukarabati viweze kutumika katika matukio mbalimbali yanaendelea na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, yanaendelea vizuri na hivi karibuni Serikali itatoa tamko kuhusiana na uwezekano wa Serikali kuvichukua viwanja ambavyo vipo chini ya Chama Cha Mapinduzi na kuvifanyia ukarabati kwa ajili ya matumizi. Ahsante. (Makofi)
MHE. NORAH W. MZERU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kujenga na kuboresha viwanja vya michezo nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu je, Serikali imejipangaje kuendeleza vipaji vya vijana hao? (Makofi)
Swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga na kuboresha viwanja vya michezo mashuleni na kwenye vyuo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Norah kwa maswali yake mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, mpango wa Serikali kuendeleza vipaji, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali kwa kushirikiana na TFF tunaandaa mashindano mbalimbali ya vijana ili vipaji ambavyo vimeweza kupatikana viweze kukuzwa na kuendelezwa kupitia mashindano hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kuna ligi ya under 17, lengo ni kuonesha vipaji hivyo vinakuwa vipi, tuna UMISETA na UMITASHUMTA ambayo kesho Mheshimiwa Waziri Mkuu ataenda kufungua kule Tabora. Mashindano hayo yote yana lengo la kuhakikisha kwamba vipaji vinavyopatikana vinaweza kuendelezwa. Katika kituo cha TFF Tanga na Dar es salaam mafunzo ya kuendeleza vipaji hivyo yanaendelea na hata hivi sasa ninavyoongea wataalamu wapo wanatoa mafunzo hayo. Kwa hiyo, tunahakikisha vipaji hivyo vitaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, katika bajeti tuliyopitisha mwaka huu tarehe 23 Mei, tulisema Serikali ina mpango wa kujenga shule 56 ili kuzibadilisha kuwa shule za michezo. Shule hizo 56 ambazo zitakuwa ni shule mbili katika kila mkoa Tanzania Bara na Visiwani zitakuwa ni mahususi kwa kuchukua vipaji hivyo na kuviendeleza, lakini kuendeleza miundombinu ya michezo katika mashule hayo. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, moja kati ya wadau wakubwa wa michezo ni Serikali na Serikali ina shule zake za sekondari na za msingi wanafunzi wengi hawana vifaa vya michezo.
Je, Wizara haioni sababu ya kuwa na mkakati wa makusudi wa kuwasiliana na Wizara ya Fedha mkashusha kodi kwenye vifaa vya michezo shuleni ili ku-support watoto wapate vifaa vya michezo kwa sababu imekuwa ni changamoto kubwa kwenye Taifa letu? (Makofi)
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na namshukuru Mheshimiwa Festo Sanga kwa ufuatiliaji mzuri wa maendeleo ya michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni Serikali kwa kushirikiana na TFF tumegawa mipira 1,000 kwa ajili ya wanafunzi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani. Tumepokea wazo lake, tutaongea na Wizara ya Fedha kuhakikisha kwamba tunatoa au kupunguza kodi katika vifaa vya michezo ili vijana hao wengi na Watanzania kwa ujumla waweze kumudu vifaa hivyo. (Makofi)
MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ingawa Serikali imetoa majibu mazuri sana, naomba niulize swali moja la nyongeza. Ni lini sasa viwanja vipya ambavyo Serikali ina mpango wa kuvijenga kwa ajili ya matayarisho ya AFCON vitakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa mujibu wa ratiba na mahitaji, viwanja hivi vinatakiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka ujao 2025 tayari kwa ajili ya ukaguzi wa kikanuni wa CAF ambao utafanyika ili kuhakikisha tuko tayari kuandaa michezo ya AFCON.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mara nyingi michezo huendana na mazoezi na wakati mwingine mazoezi husababisha injury. Katika kupambana, wanamichezo wengi hupata majeraha ambayo mengine ni ya muda mrefu. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha watu wote wanaojihusisha na elite sports (professionals) wanapata Bima ya Afya ili waweze kuendelea kufanya vizuri katika michezo, tofauti na ilivyo sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitilia mkazo mashindano yote ya ki-professional ambayo yanahusisha timu ziweke bima kwa ajili ya wachezaji wao na hata mahali ambapo wachezaji wanatumika kwa ajili ya Timu za Taifa, Serikali imekuwa ikihakikisha wachezaji hao wanakuwa wana bima ili kuhakikisha hawapati madhara ya kudumu na hata kama wakipata madhara ya kudumu Serikali inaweza kuwatibia kwa kutumia bima hizo.
MHE. DKT. ANGELINE S. L. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwuliza Naibu Waziri kwa sababu sasa hivi Mwanza imekuwa ikisahaulika sana kwenye michezo kwa kutokuwa na timu ambayo imeingia kwenye Premier League na sasa hivi Pamba FC Wanatipilindanda wako katika Premier League. Ni lini uwanja wa CCM Kirumba utakarabatiwa ikiwa ni pamoja na ule wa mazoezi ya AFCON wa Ilemela utakuwa tayari?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu kwenye jibu la msingi, kwa sasa mpango uliopo ni kuanza kujenga kiwanja kipya cha Ilemela lakini hata Uwanja wa CCM Kirumba uko katika viwanja vitano ambavyo tunaanza navyo kuvikarabati ambavyo viko chini ya Chama cha Mapinduzi kama ambavyo nilishasema. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, asiwe na wasiwasi Wanatipilindanda watakuwa na sehemu ya kuchezea michezo yao ya Ligi Kuu kuanzia msimu ujao ambapo kitakuwa kimekarabatiwa na kitakuwa katika kiwango cha kupendeza.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; pamoja na jitihada nzuri zinazofanywa na Serikali katika kulinda tamaduni za Kitanzania nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kwamba kuna baadhi ya filamu watoto wa kiume wana-act au wanaigiza kama watoto wa kike: Je, BASATA na Serikali hawaoni kwamba hili linaweza kuchochea watoto wetu wa kiume waone kwamba kuwa watoto wa kike ni jambo la kawaida? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kuhusu maudhui na miziki au filamu na mziki zilizomo ndani ya mabasi yaendayo mikoani. Mavazi yanayovaliwa na vijana wetu mle ndani hasa watoto wa kike ni nusu ya utupu. Je, Serikali au BASATA haioni kwamba hii ni kinyume cha sheria na kwamba ni tabia mbaya ambayo inaporomosha maadili ya nchi yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwenye swali la kwanza lina mtego kidogo kwa sababu kazi ya wasanii pamoja na mambo mengine ni kuburudisha. Sasa wasanii wanaweza wakavaa uhusika wa aina yoyote. Wasanii mara nyingi wameimba nyimbo wakiigiza kuwa madaktari, wakiigiza kuwa waganga wa kienyeji, wakiigiza kuwa walevi, walioathirika na kadhalika. Kwa hiyo, kuvaa uhusika ni jambo moja ambalo limekaa kimtego na namna ya Serikali kulishughulikia ni kuangalia tu namna ambavyo kama litakuwa limezidi na linaakisi kupelekea kwenye kuisukuma jamii kufanya vitendo visivyofaa hapo ni lazima tutachukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunaendelea kufuatilia kwa karibu kupitia Baraza la Sanaa la Taifa kuhakikisha kwamba maudhui yaliyopo katika filamu na nyimbo zetu hayakiuki misingi ya maadili ya Mtanzania na tunachukua hatua kila wakati inapofaa kufanya hivyo. Hata hivyo, tunaendelea kuwaelimisha wasanii kwa namna moja ama nyingine kuhusiana na jambo hili na kuhakikisha kama na wao wanabaki kwenye misingi na Maadili ya Kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, jibu hili pia linakwenda kwenye swali lake la pili kuhusiana na mavazi ambayo yanakuwa ni nusu uchi kwenye nyimbo zilizorekodiwa ama filamu ambazo zinaoneshwa kwenye mabasi. Tunachoendelea kukifanya ni kuhakikisha maudhui yote yaliyoko katika nyimbo ikiwemo video zake na filamu za Kitanzania hayakiuki maadili ya Kitanzania ili kuepusha tatizo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelisema, nakushukuru. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Je, ni upi mkakati wa Serikali kuanzisha kampeni maalum kuondoa kasumba ambayo imejengeka kwetu sisi Watanzania kwamba tunapotumia mambo ya kimagharibi sana ni tafsiri ya kuonesha kwamba tumestaarabika? Kwa mfano, mtu unapoonekana unaweza kuongea Kiswahili peke yake na huwezi kuongea Kiingereza wewe hujasoma, wakati Wachina na Wafaransa hawajui Kiingereza na bado wanaheshimika; au kuonekana ukiwa unatumia mvinyo ambao unatoka nchi za magharibi wewe umestaarabika na ni msomi, lakini ukitumia mivinyo yetu ya ndani ya nchi wewe ni mshamba…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sichalwe uliza swali lako. Mheshimiwa Waziri.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nimemwelewa vizuri ni kuhusu umagharibi kuingia kwenye tamaduni zetu na maisha yetu ya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, dunia imekuwa kama Kijiji, kwa hivyo ni suala la ridhaa ya mtu na namna ambavyo anataka kuendesha maisha yake, lakini sisi ambacho tunakifanya ni kuhakikisha tunaendelea kuelimisha. Pamoja na mambo mengine kwa sasa tunafanya filamu ambazo zina maudhui ambayo yanaonesha umuhimu wa kuweka mbele utamaduni wetu kuliko kuiga tamaduni za kimagharibi. Tunaendelea na suala hili kupitia Baraza la Sanaa la Taifa, Baraza la Kiswahili la Taifa na Bodi ya Filamu Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, hili jambo sisi tunaendelea kulifanya japo ni ridhaa ya mtu mwenyewe anaamua anavyotaka maisha yake yafanyike, lakini tutaiweka katika namna ambayo itaonesha kufuata utamaduni wa kimagharibi siyo ujanja wowote na unaweza kuendelea kufuata utamaduni wa Kitanzania na ukaonekana una class unayotaka ionekane unayo, ahsante.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Michezo.
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini niongezee kwenye hoja kwamba ili kuhakikisha wasanii wetu wanazingatia Maadili ya Kitanzania, tumeenda kubadilisha kanuni pale BASATA, tumeingiza wadau wengine ambao wanahusika kwenye production ya hizo video na nyimbo, kwa sababu mwanzoni tulikuwa tunamwadhibu msanii wakati producer ndio anatengeneza ile content na ndio anamwambia msanii avae vipi na a-behave vipi? Sasa hata producer na wadau wengine wa kwenye production tumewaingiza katika mfumo wa kanuni na wanaadhibiwa ili kuhakikisha tunakomesha vitendo hivyo. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tunapambana sana na maadili ya watoto, Wizara haioni sasa ni wakati wa kuzuia ule uhusika ambao unapelekea kuchochea watoto kuingia kule kwenye tabia zile mbaya hasa wale wanaume ku-act kama wanawake na baadaye kupelekea watoto kuona tabia za kishoga ni za kawaida?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu wakati najibu moja ya maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Giga, jambo ni lile lile ambalo Wizara inalitilia mkazo na inalifanya kwa nguvu nyingi, kuhakikisha tunatoa elimu kwa wasanii wetu. Halikadhalika tunachukua hatua pale inapostahili kufanya hivyo kama ambavyo tunaona kwamba wanakiuka maadili ya kitanzania. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo tunaendelea kulifanya kwa nguvu nyingi na tunahitaji ushirikiano wa kila Mtanzania kuhakikisha tunakemea jambo hili, ahsante.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa michezo iko mingi na hivi juzi tumeshuhudia Yanga imechukua shilingi milioni 30 uwanjani, je, ni mchezo gani kati ya michezo hiyo hasa ambapo Kombe la Mama litakuwa limetengewa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mama Shally hakuwa na sababu ya kuitaja Yanga, angeuliza tu moja kwa moja, lakini siyo neno. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuko katika hatua za mwishoni za mazungumzo na Kampuni ya 1xBet ambapo tunakwenda kupata ufadhili kwa ajili ya mashindano na timu zetu mbalimbali zikiwemo Timu za Taifa. Miongoni mwa mambo ambayo tumeamua ni kwamba Ligi ya Taifa ya Netball, itakwenda kuitwa Ligi ya Mpira wa Pete ya Samia Suluhu Cup. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, ni kwa nini Serikali isianzishe kliniki za michezo mbalimbali ambazo zitafanyika kila mwaka kwenye wilaya zote nchini ili kuweza kuibua vipaji na kuviendeleza na kupata vijana mahiri ambao watashiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa kama vile Olympic? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, Serikali inazo namna kadhaa kwa ajili ya kupata vijana kwa ajili ya kuliwakilisha Taifa ikiwemo mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA, lakini wazo la Mheshimiwa Mbunge siyo baya, naomba nilichukue twende tukalifanyie kazi, ahsante. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na naipongeza sana Serikali kwa utaratibu wa kupata na kufanyisha mashindano ya AFCON 2025 na 2027. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, sielewi ni kwa nini Wizara kwa mikoa ambayo haipo kwenye AFCON watoe maelekezo baada ya michezo ya AFCON kufanyika au ujenzi wa viwanja vya AFCON kufanyika 2027. Nadhani kwamba wangeweza wakatoa maelekezo sasa hivi ili mikoa mingine na yenyewe iweze kuwa na mikakati ya kujenga viwanja hivyo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa michezo siyo afya tu na michezo siyo ajira tu, michezo katika ulimwengu wa sasa ni utalii. Serikali kupitia Wizara hii ina mkakati gani kwa kushirikiana na Wizara nyingine kuhakikisha sasa michezo kwenye maeneo yenye hali ya hewa nzuri kama Njombe inaleta michezo ya kiutalii kama golf?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwenye swali la kwanza la nyongeza la Mheshimiwa Mwanyika, ni kweli Mheshimiwa Mbunge ameliona sahihi. Ipo haja ya kuharakisha utaratibu wa kuzielekeza mamlaka za mikoa ambayo haitachezewa AFCON kuanza ujenzi wa miundombinu bora ya michezo hasa ile mikoa ambayo haina viwanja hivi. Kwa hiyo tumelichukua tutalifanyia kazi atupe muda.
Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili, tumeshaanza mikakati ya kuunganisha utalii na michezo kwenye hili la utalii wa kimichezo hasa wa golf. Moja ya mambo ambayo tumeyafanya sasa hivi, ni kufufua viwanja vya zamani ambavyo vilikuwa vimekufa (vimeuliwa). Kwa mfano pale Njombe kulikuwa na kiwanja kilikuwa na mashimo tisa cha golf cha kwenye Kibena Tea Estate na tumeanza utaratibu wa kukifufua. Moshi pia kulikuwa na uwanja pia wa mwaka 1922 wa golf ambao nao umekufa na tumeshaanza kuufanyia kazi ambapo Mheshimiwa Waziri alimpa maelekezo Mtendaji Mkuu wa BMT na uwanja ule umeshaanza kutengenezwa.
Mheshimiwa Spika, tutakapomaliza kukarabati na kuvifungua viwanja hivi, jambo la kwanza tutakalofanya ni kuandaa mashindano mbalimbali ya Kitaifa na ya Kimataifa ya golf ili kuhakikisha kwamba tunaunganisha utalii na michezo kwa kutumia mchezo wa golf. Nakushukuru.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa uwanja wa memorial kama walivyoahidi katika kipindi cha mashindano ya Kilimanjaro Marathon ili uweze kutumika kama kambi katika mashindano ya AFCON? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu mwanzoni viwanja vyote ambavyo vitatumika kwa ajili ya AFCON ujenzi umeshaanza na vile ambavyo vitatumika kama sehemu ya viwanja vya mazoezi ujenzi wake utaanza hivi karibuni. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu Serikali ilishaahidi kuanza kukikarabati kiwanja cha memorial, ukarabati huo utaanza hivi karibuni na asiwe na wasiwasi akae kwa kutulia. (Makofi)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ipo tayari kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya Hanang ili kujenga uwanja wa kisasa wa michezo pale Hanang ambapo eneo tayari limetengwa?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu wakati najibu swali la msingi kwa sasa msisitizo upo kwenye viwanja ambavyo vitatumika kwa ajili ya mashindano ya AFCON. Pia kwenye swali la nyongeza la Mheshimiwa Deodatus Mwanyika aliuliza kama kwa nini tunasubiri mpaka AFCON ipite ndiyo tuzielekeze mamlaka za mikoa kuanza kutengeneza miundombinu ya michezo kwenye maeneo yao. Nimeahidi na inamuahidi tena Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutauharakisha utaratibu huo ili mamlaka za mikoa na wilaya zianze kufanya ujenzi huu wa miundombinu ya michezo kwenye maeneo husika.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; tuna taasisi kubwa ambayo imewekeza katika wilaya zote za nchi hii viwanja vizuri vya mpira lakini ni chakavu. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inashirikiana na taasisi hii ili kuboresha viwanja hivi hasa katika halmashauri ambazo hazina mapato ya kutosha?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; tuna wilaya 139 katika nchi hii na ambazo Waziri mejibu katika swali langu ambazo zimeanza kufanya marekebisho ni wilaya sita. Je, wameshafanya tathmini ya kuangalia bajeti ya Wilaya zote, ukarabati wa viwanja ni kiasi gani ili wanapoelekeza halmashauri ziweze kukusanya fedha kwa ajili ya ukarabati huu? Je, kila halmashauri inahitaji fedha kiasi gani hasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Urambo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kama ambavyo nilishajibu kipindi cha nyuma, bado Serikali inafanya majadiliano na taasisi husika ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja kuhusu namna ambavyo tunaweza kufanya ukarabati na namna fedha ambazo tutazitumia zitaweza kurudishwa kwenye mfuko wa umma ambao tutazitoa. Hata hivyo, lengo hasa ni kwa Serikali kuutumia Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ambao kwa sasa unapata asilimia tano ya mapato kutoka kwenye sports betting. Lengo letu ni kuutunisha Mfuko ule kwa kuuongezea vyanzo vipya vya mapato ili kuhakikisha unakwenda kuleta athari chanya hasa kwenye maendeleo ya michezo nchini ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya michezo. Kwa hiyo, tutakapokuwa tayari, hata majadiliano na taasisi ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja tutawapa taarifa na namna ambavyo tunakwenda kulitekeleza jambo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa sasa kwa mpango huu tulionao ambapo mamlaka husika tulizozitaja, mikoa, halmashauri na manispaa zinajenga viwanja vyake vya michezo, wajibu wa kupata gharama halisi ya kukarabati miundombinu hii bado unabaki kwa mamlaka husika. Kwa ufahamu wangu, gharama zinatofautiana kutoka mamlaka moja mpaka nyingine, lakini tutakapokuwa tayari na hasa tutakapotaka kuzisaidia halmashauri ambazo hazina uwezo mkubwa wa kifedha kutengeneza viwanja hivi, tutaingia moja kwa moja pamoja na mambo mengine, kufanya tathmini ya kiasi gani kinahitajika kwa kila miundombinu ya michezo. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Ikungi ni wilaya mpya kwa maana haina uwanja wa michezo na kwa sababu ni eneo ambalo linatoa wanamichezo wengi ikiwemo wanariadha na kwa sababu kulikuwa na mpango wa kujenga kiwanja cha ndege katika Kata ya Unyahati, Shule ya Sekondari Unyahati, ni lini sasa Serikali itatekeleza mpango huu wa kutujengea uwanja ambao mimi na wewe tulishawahi kufanya mazungumzo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimetangulia kujibu, kwa sasa hivi Serikali imejielekeza sana kwenye ujenzi wa miundombinu ambayo itatumika kwa ajili ya CHAN 2025 na AFCON 2027. Hata hivyo, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ametangulia kusema tumeshajadiliana mimi na yeye na miongoni mwa mipango ambayo Serikali inayo ni kuimarisha miundombinu ya michezo kila mahali. Hamu yangu ni kuona kwamba kila Wilaya, ikibidi kila Jimbo, liwe na miundombinu bora kabisa ya michezo, ni ile tu kwamba rasilimali fedha hairuhusu kwa sasa, lakini mipango bado ipo na kama ambavyo nimetangulia kusema huu Mfuko wa Maendeleo ya Michezo unaweza kutumika kutengeneza viwanja vingi nchini hasa kwenye halmashauri mpya na zisizo na uwezo kama ya Ikungi. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, swali langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwa nini Serikali isitoe maelekezo mahsusi kwa halmashauri za manispaa zote nchini kufikia mwaka 2027 ziwe zimejenga viwanja vya michezo ambavyo angalau vinabeba watu 5,000, 10,000 ili kuondokana na uhaba wa viwanja nchini?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu wakati najibu swali la msingi, ni kwamba nitazielekeza Mamlaka ya Serikali za Mitaa kutenga mafungu katika bajeti zao ili kuimarisha miundombinu ya michezo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, yuko mle mle ambako tulikuwa tumejibu kwenye swali la msingi kuhusiana na mpango wa Serikali kuzielekeza mamlaka hizi. Ni jambo ambalo linahitaji muda na kufuata utaratibu rasmi kabisa ili mamlaka hizi ziwe na wajibu wa kutekeleza wakati Serikali itakapotoa maelekezo haya. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Serikali siku zote yamekuwa ni mazuri, yanavutia, lakini utekelezaji umekuwa ni sifuri. Nataka kujua mkakati wa Serikali kujenga viwanja vizuri kwenye Mkoa wa Songwe kwa sababu changamoto imekuwa ni kubwa sana. Ni upi mpango wa Serikali ili tuone hiki inachokisema kinatekelezeka? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nitajibu jibu hili hili kwa kila swali ambalo linahusiana na ujenzi wa miundombinu ya michezo, kwa sababu ukweli ni kwamba kwa sasa tumejielekeza kwenye miundombinu ya michezo kwenye viwanja vitakavyotumika kwa CHAN 2025 na AFCON 2027. Hayo mengine ni kwamba tunajipanga kutoa maelekezo kwa mamlaka za mikoa, halmashauri na manispaa ili zianze kujenga viwanja na miundombinu mingine ya michezo kwenye maeneo yao kwa kadri ambavyo wataweza na Serikali itawasaidia hasa zile halmashauri ambazo hazitakuwa na uwezo mkubwa wa kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo nimejibu hapo awali ni kwamba lengo letu ni kutengeneza miundombinu ya michezo katika kila eneo, kila Jimbo, kila halmashauri na kila mkoa, lakini kwa sasa rasilimali fedha haituruhusu kufanya hivyo kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, tutakwenda taratibu kwa phases na tutafikia halmashauri ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na naipongeza sana Serikali kwa utaratibu wa kupata na kufanyisha mashindano ya AFCON 2025 na 2027. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, sielewi ni kwa nini Wizara kwa mikoa ambayo haipo kwenye AFCON watoe maelekezo baada ya michezo ya AFCON kufanyika au ujenzi wa viwanja vya AFCON kufanyika 2027. Nadhani kwamba wangeweza wakatoa maelekezo sasa hivi ili mikoa mingine na yenyewe iweze kuwa na mikakati ya kujenga viwanja hivyo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa michezo siyo afya tu na michezo siyo ajira tu, michezo katika ulimwengu wa sasa ni utalii. Serikali kupitia Wizara hii ina mkakati gani kwa kushirikiana na Wizara nyingine kuhakikisha sasa michezo kwenye maeneo yenye hali ya hewa nzuri kama Njombe inaleta michezo ya kiutalii kama golf?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwenye swali la kwanza la nyongeza la Mheshimiwa Mwanyika, ni kweli Mheshimiwa Mbunge ameliona sahihi. Ipo haja ya kuharakisha utaratibu wa kuzielekeza mamlaka za mikoa ambayo haitachezewa AFCON kuanza ujenzi wa miundombinu bora ya michezo hasa ile mikoa ambayo haina viwanja hivi. Kwa hiyo tumelichukua tutalifanyia kazi atupe muda.
Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili, tumeshaanza mikakati ya kuunganisha utalii na michezo kwenye hili la utalii wa kimichezo hasa wa golf. Moja ya mambo ambayo tumeyafanya sasa hivi, ni kufufua viwanja vya zamani ambavyo vilikuwa vimekufa (vimeuliwa). Kwa mfano pale Njombe kulikuwa na kiwanja kilikuwa na mashimo tisa cha golf cha kwenye Kibena Tea Estate na tumeanza utaratibu wa kukifufua. Moshi pia kulikuwa na uwanja pia wa mwaka 1922 wa golf ambao nao umekufa na tumeshaanza kuufanyia kazi ambapo Mheshimiwa Waziri alimpa maelekezo Mtendaji Mkuu wa BMT na uwanja ule umeshaanza kutengenezwa.
Mheshimiwa Spika, tutakapomaliza kukarabati na kuvifungua viwanja hivi, jambo la kwanza tutakalofanya ni kuandaa mashindano mbalimbali ya Kitaifa na ya Kimataifa ya golf ili kuhakikisha kwamba tunaunganisha utalii na michezo kwa kutumia mchezo wa golf. Nakushukuru.
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa uwanja wa memorial kama walivyoahidi katika kipindi cha mashindano ya Kilimanjaro Marathon ili uweze kutumika kama kambi katika mashindano ya AFCON? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu mwanzoni viwanja vyote ambavyo vitatumika kwa ajili ya AFCON ujenzi umeshaanza na vile ambavyo vitatumika kama sehemu ya viwanja vya mazoezi ujenzi wake utaanza hivi karibuni. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu Serikali ilishaahidi kuanza kukikarabati kiwanja cha memorial, ukarabati huo utaanza hivi karibuni na asiwe na wasiwasi akae kwa kutulia. (Makofi)
MHE. SAMWELI X. HHAYUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Je, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ipo tayari kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya Hanang ili kujenga uwanja wa kisasa wa michezo pale Hanang ambapo eneo tayari limetengwa?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu wakati najibu swali la msingi kwa sasa msisitizo upo kwenye viwanja ambavyo vitatumika kwa ajili ya mashindano ya AFCON. Pia kwenye swali la nyongeza la Mheshimiwa Deodatus Mwanyika aliuliza kama kwa nini tunasubiri mpaka AFCON ipite ndiyo tuzielekeze mamlaka za mikoa kuanza kutengeneza miundombinu ya michezo kwenye maeneo yao. Nimeahidi na inamuahidi tena Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutauharakisha utaratibu huo ili mamlaka za mikoa na wilaya zianze kufanya ujenzi huu wa miundombinu ya michezo kwenye maeneo husika.
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza ninachukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuona haja ya kuongeza zawadi hii kutoka shilingi laki moja hadi shilingi milioni moja kwa sasa. Niseme wazi kwamba mbali ya hizi zawadi Serikali imefanya kazi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaipongeza Wizara kwa maandalizi ya tamasha la ugawaji wa tuzo, kwa maana ya Tanzania Music Awards, mmefanya kazi nzuri sana, tunawapongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa hili tamasha la utamaduni ambalo amekuwa akifanya kila mwaka nchi nzima, limekuwa linaleta tija na kulinda maslahi ya tamaduni zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninatoa rai kwa Serikali, ipi ni kauli yenu kwa matamasha haya kufanyika kwenye kila wilaya na kwenye kila mkoa ili kuhakikisha kwamba tunalinda utamaduni wa nchi yetu hususani kwenye maeneo mbalimbali ya Taifa, ambapo utamaduni umekuwa ukipungua? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA, NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimetangulia kusema wakati ninajibu swali la msingi, matamasha haya yamekuwa yakifanyika katika maeneo mbalimbali, japo siyo kwa urasmi huu ambao umebebwa baada ya Serikali kuingilia kati na kulifanya tamasha la pamoja la utamaduni kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachukua fursa hii sasa kuwaagiza Maafisa Utamaduni wa Wilaya na Mikoa, kwanza kuhakikisha wanashiriki na kuhakikisha matamasha ambayo yanafanyika katika maeneo yao yanafanikiwa na kama kuna mahali watakuwa wamekwama, sisi kama Serikali tuko tayari kushirikiana nao ili kuhakikisha matamasha haya ya utamaduni yanafana nchi nzima kutoka kabila moja hadi linguine, ahsante. (Makofi)
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali moja la nyongeza. Ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanaendelea kutia matumaini ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, pamekuwepo na baadhi ya wasanii ambao wanawakilisha ndani ya mataifa mengine ya nje, lakini wasanii hao ni wazuri, hawana scandal ya aina yoyote. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaonaje kwa wakati huu achukue fursa ya kuwezesha wasanii hawa kupatiwa hata Passport za kihuduma ambazo zitawafanya wao waendelee kuitunza sana aa kuiwakilisha vizuri Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Serikali inatambua umuhimu wa wasanii katika kuitangaza nchi yetu, lakini pia katika kuchangia uchumi wetu. Ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, upo umuhimu wa kuendelea kuwarahisishia wakati wanavyofanya safari za kwenda kufanya kazi zao nje ya mipaka ya Tanzania ambako wanakwenda kuitangaza nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nchini mamlaka ambayo ina jukumu la kutoa Passport na hati nyingine za kusafiria ni Idara ya Uhamiaji ambayo iko chini ya Wizara ya Mambo ya Nchi. Kwa mujibu wa Sheria ya Passport na Hati Nyingine za Kusafiria ya Mwaka 2002, wasanii si miongoni mwa wanufaika wa Hati za Kidiplomasia ama Hati za Kihuduma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninamhaidi Mheshimiwa Mbunge, swali lake hili ambalo limekuja kama maoni na ushauri, tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani kuona namna ambavyo tunaweza kuendelea kuwarahisishia wasanii wetu wanaofanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi yetu nje ya mipaka yetu namna ya kusafiri ili waendelee kuifanya kazi hiyo kwa moyo mmoja. Ahsante.