Supplementary Questions from Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma (11 total)
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo kwa Jimbo la Nkasi Kusini, hali ni hiyohiyo ama mbaya zaidi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza ambapo tuna kata 37 na vituo viwili tu vya afya. Sasa swali langu, Serikali ina mpango wowote wa kuongeza vituo vya afya Wilayani Muheza ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamis Mwinjuma, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Jimbo la Muheza lina kata 37 na vituo vya afya viwili tu na hali hii ipo katika karibu majimbo yote nchini. Tunafahamu tuna kata zaidi ya 3,900 na ndiyo maana Serikali imeweka mpango wa kujenga vituo vya afya kwa awamu. Ni kweli kwamba hatuwezi kukamilisha kujenga vituo katika kata zote ndani ya mwaka mmoja wa fedha, lakini Serikali imedhamiria na inatambua kwamba tuna kazi ya kufanya kwa awamu kwa kadri ya fedha zinavyopatikana na kuendelea kujenga vituo vya afya katika kata zetu na kujenga zahanati katika vijiji na hospitali za halmashauri katika ngazi za halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mwinjuma kwamba katika mipango ya Serikali inayokuja, tutaendelea kuomba kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya kuendelea kujenga vituo vya afya katika kata nchini kote zikiwemo kata katika katika Jimbo hili la Muheza.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Najua barabara yote kilometa 40 ina umuhimu mkubwa, lakini kipande katikati ya Kisiwani na Kibaoni ndiyo kipande hasa ambacho kina matatizo makubwa, Je, Serikali ina mpango wowote wa kukishughulikia kipande hiki kwa namna ya kidharula ili kuhakikisha kwamba kinapitika wakati wote wa mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwinjuma, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, barabara hii inaendelea kutengenezwa. Jana nimepita maeneo ya Tanga na nilikuwa na Meneja wa TANROADS na moja ya maelekezo ambayo tumempa ni kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo yana shida likiwepo hili la kati ya Kisiwani na Kibaoni wahakikishe kwamba wanapeleka nguvu zao ili pasije pakatokea tatizo la kutokuwa na mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu barabara hii ipo kwenye matengenezo ndiyo maana tumeendelea kutenga hizo shilingi milioni 600 kwa ajili ya kurekebisha sehemu zozote ambazo ni korofi ikiwemo pamoja na hili eneo kati ya Kisiwani na Kibaoni. Ahsante.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri kwa niaba ya Serikali na ambayo yananipeleka kwenye maswali mawili ya nyongeza. Miongoni mwa matatizo makubwa ya kilimo na biashara ya viungo Wilayani Muheza ni kukosekana kwa ardhi kubwa ya kulimia mazao hayo kule ambako yanastawi. Pia na viwanda vya kuyachakata kulekule kwenye Tarafa ya Amani, ili kuyaongezea thamani kwa vile kule hakuna kiwanda hata kimoja. Sasa kuna ekari 35,063 ambazo ziko chini ya Kampuni ya East Usambara Tea Company ambazo zilikuwa na viwanda viwili ambavyo kwa sasa ni magofu na zinazotumika ni ekari 4,909 tu kwa miaka mingi na viwanda hivi vimegeuka magofu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali haioni hivi sasa ni wakati wa kuvirudisha viwanda hivi kwenye umiliki wake, ili kuwasaidia wananchi ikiwa ni kwa kuwekeza yenyewe ama kwa kushirikiana na wawekezaji wapya serious ili wananchi wa Amani wapate kupata viwanda vya kuongeza thamani mazao yao ya viungo kule? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tatizo la aina hii, Waheshimiwa Wabunge wanaweza kuwa mashahidi, limekuwa likitokea sehemu nyingi ambapo wawekezaji wamekuwa wakiomba kumilikishwa viwanda hivi kwa ahadi ya kuvifufua na kuzalisha ajira pamoja na kuliongezea pato Taifa, lakini badala yake wamekuwa wanaviuwa na kuvigeuza kuwa magofu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuwa aidha na sheria kali zaidi ama kutunga sheria mpya ili tusiendelee kuchezewa na viwanda vyetu vifanye makusudio yaliyokuwepo wakati vinaanzishwa? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma, Mbunge wa Jimbo la Muheza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Hamis Mwinjuma kwa kufuatilia sana maendeleo, hasa sekta ya viwanda katika jimbo lake. Amenifuata mara nyingi kuhusiana na viwanda hivi, hasa vya chai hivi vya East Usambara Tea Company Limited, ambavyo viko pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu suala la ardhi. East Usambara Tea Company Limited ina ekari 35,000 kama alivyosema na katika ekari hizo ni ekari 2,027 tu ndio zimepandwa chai na ekari 600 zimepandwa miti, kwa maana ya miti ile inayotumika kama nishati, kuni kwa ajili ya kutumika katika viwanda hivyo. Pia eneo lingine maeneo yaliyobakia ambayo yanamilikiwa na kampuni hii yanatumika kwanza katika sehemu nyingine ni vyanzo vya maji, lakini maeneo mengine ni natural reserve kulingana na utaratibu wa UNESCO kwamba, huwezi kutumia mazingira yote kulima, kwa hiyo, maeneo mengine makubwa yako katika mazingira ya reserve.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na uhitaji wa wakulima katika Jimbo la Muheza, tutaona namna gani kushirikiana na wenye kampuni, ili tuone kama wanaweza kutoa sehemu kidogo ambayo inaweza kutumika na wakulima wadogowadogo kwa ajili ya kuzalisha viungo ambavyo vitatumika katika viwanda vya kuchakata viungo kama alivyoomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwekezaji katika viwanda hivyo. Nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na ufuatiliaji huo wote, lakini viwanda hivi sasa vinafanya kazi vizuri. Uwezo uliosimikwa kwa viwanda vile viwili ambavyo vinafanya kazi vya Bukwa na Kwamkoro vina uwezo wa kuchakata kilo 120 kwa siku, lakini sasa hivi vinaweza kupata raw material kwa maana ya malighafi zaidi ya kilo 90,000. Kwa hiyo, maana yake viwanda hivi vinafanya kazi vizuri, lakini kuna viwanda vile viwili ambavyo kutokana na mahitaji haya wenye viwanda, Kampuni ya East Usambara Tea Company Limited, walivigeuza kama ma-godown, ambavyo vilikuwa Viwanda vya Munga na Nderema, lakini pia baadaye, nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kampuni hii ina mpango sasa wa kuanza ku-pack kwa maana ya blending ya ile chai wanayozalisha pale badala ya kwenda kuuza kwenye minada ya Mombasa na kwingine, wataanza kufanya blending pale. Kwa hiyo, tuna mpango wa kuwasaidia ili wafufue viwanda hivi viwili viweze sasa kufanya blending badala ya kuwa store au magofu kama yalivyo sasa.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, na nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni kwamba, kwa vile imeshathibitika kwamba jambo hili halina madhara yoyote kimazingira na kwenye idadi ya vipepeo, na kwamba kwanza ukiachilia mbali kuongeza vipato vya wananchi lilikuwa linasaidia kwenye idadi ya vipepeo kwa vile kwa kawaida kipepeo anayetaga mayai mpaka 500 kwa njia zake za kwaida huweza kuzalisha vipepeo wawili, lakini kwa njia hii ya msaada wa wananchi huweza kuzalisha mpaka vipepeo 300.
Je, Serikali haioni kwamba, ilishauriwa tu vibaya kwenye suala hili kwa kutotenganisha kati ya wanyama wakubwa kama chui, twiga na swala na hawa vipepeo wetu na kwamba inatakiwa kurudi nyuma na kutenganisha sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa vile ni nchi chache sana duniani ambazo zinaweza kuzalisha vipepeo kama sisi, na ni biashara na utalii mkubwa duniani; Serikali haioni haja sasa ya kuwekeza kwenye kuanzisha utalii wa vipepeo, ili kuongeza vivutio vya utalii nchini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hamis Mwin’juma, Maarufu kama “Mwana FA”, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Hamis Mwin’juma, lakini pia nimpongeze sana kwa kuendelea kusimamia eneo hili la wanyamapori hai, lakini nimpongeze pia kwa kuendelea kupigania wananchi wa Muheza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo ameshauri Mheshimiwa Mwinjuma, kwamba Serikali inawezekana ilishauriwa vibaya. Nimtoe wasiwsi kwamba Serikali iko makini na Serikali iko kazini na ina wataalamu wa kutosha. Suala hili limekuwa likichunguzwa na wataalamu mbalimbali. Muhimu ni kuangalia kipi faida na hasara ambayo inaweza ikapata Serikali. Tunapoendelea kuhamisha wanyama mbalimbali kutoka ndani ya nchi kupeleka nje ya nchi ina maana tunazidi kuuwa utalii wa hapa Tanzania. Hata hivyo nimtoe wasiwasi, kwamba suala hili tunaendelea kulifanyia tathmini, tutachakata kuangalia faida na hasara ya eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze pia, kwa kuendelea kuhamasisha utalii kupitia vipepeo ambavyo amevitamka yeye mwenyewe. Kwa hiyo, kama kweli tutaanzisha utalii wa vipepeo haina haja sasa hata kuendelea kuvitoa hivi vipepeo viende nje ya nchi kwa sababu tunapoendelea kuvitoa tunauwa soko la utalii wa ndani.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, ripoti ya NEMC ya Oktoba, 2018 ambayo Mheshimiwa Waziri anaitaja, ilielezea wazi kwamba kinachokatazwa ni uchimbaji mdogo na inashauriwa ufanyike uchimbaji aidha wa kiwango cha kati ama mkubwa, kwa sababu hizo za kimazingira ambazo Mheshimiwa Waziri amezitaja. Sasa je, Serikali haioni kwamba kwa vile wananchi wa Sakale, Kata ya Mbomole, Wilaya ya Muheza, hawana uwezo wa kufanya uchimbaji wa kiwango cha kati ama mkubwa inafaa sasa iwasaidie kupata mwekezaji mwenye vigezo vinavyotajwa na ripoti hiyo ili uchimbaji ule uweze kufanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyikiti, la pili; ni ombi kwa Wizara, kwamba tuna maeneo kadhaa mengine katika Wilaya ya Muheza katika Kata ya Pande Darajani katika Kata ya Magila na katika Kata ya Magoroto hasa Kijiji cha Mwembeni ambayo yanaonyesha dalili za kuwa na madini. Je, Serikali inaweza kututumia watalaam wake ili wakafanye tathmini na kuona kama kuna uwezekano wa kuchimba katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda ujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge Hamis Mohamed Mwinjuma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla ya kutoa majibu ya Wizara, napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa mwelewa, kwa sababu tulipofanya ziara hii na kukubaliana kwamba uchimbaji mdogo utaleta athari kubwa za mazingira, mara nyingi watu wasingeweza kuamini kwamba mbona kuna mali, lakini tathmini ya kimazingira ilionyesha kwamba uchimbaji mdogo utaleta athari kubwa ambazo yawezekana zisiwe na faida hata kama uchimbaji unafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya kuelewa kwa Mheshimiwa Mbunge ndiyo maana hata wananchi wote wakaelewa kwamba huenda kama madini haya lazima yachimbwe basi iwe ni kwa uchimbaji wa kati ambao teknolojia yake inakuwa ni ya kuchukua udongo mahali pale na kuchenjulia sehemu nyingine ili kuendelea kulinda vyanzo vya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo, Wizara itatoa ushirikiano wote ambao wananchi wanauhitaji kwa sababu pale tulikwishatoa leseni za uchimbaji mdogo. Kwa hiyo tutawaomba tu wafuate utaratibu, wao watapata muwekezaji halafu watakuja Wizarani, watafanya amalgamation ya uchimbaji mdogo tutazi-upgrade kuwa za uchimbaji wa kati na tutawapa miongozo yote inayostahili ili waweze kufanya uchimbaji ambao bado utazingatia kutoathiri chanzo cha maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili; GST ndiyo taasisi yetu ambayo inakwenda kufanya utafiti wa awali na huwa tunapenda kuhimiza utafiti wa awali kwa sababu hautakuwa ule ambao unaleta na wingi wa mashapo kwa kule chini. Sasa hilo linawezekana, tutawaagiza waje. Mheshimiwa Mbunge hata baada ya hapa anaweza akaja pale ofisini kwetu tukaongea na watu wa GST na wakapanga namna ya kwenda nawe ili awaelekeze katika maeneo ambayo anataka waweze kufanya utafiti ili huo wa awali uweze kuonyesha kama uchimbaji unaweza kuendelea katika vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu ya Serikali kupitia kwa Naibu Waziri ambayo yananipeleka kwenye maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza, wakati huu ambao taratibu mbalimbali zinaendelea za kutafuta masoko kwa ajili ya machungwa, lakini pia kutafuta uwekezaji kwa ajili ya kutengeneza viwanda cha kuchakata matunda: Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kutengeneza vituo vya ukusanyaji, uhifadhi na uuzaji wa machungwa ili kuwapa uhakika wa sehemu ya kuuzia machungwa yao wananchi wa Wilaya ya Muheza na pia kuepusha idadi kubwa ya machungwa yanayoharibika kila mwaka kwa kukosa uhifadhi mzuri?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma, Mbunge wa Muheza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia sana kuhusiana na soko la machungwa katika Mkoa wa Tanga Wilayani Muheza. Niseme kweli, machungwa ya Muheza ni ya aina yake kwa maana ya ladha; ni matamu kuliko; kwa hiyo, unaweza ukayatenganisha kuliko ya maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imeanza mpango wa kujenga maghala ambayo yatakuwa kama vituo vya kukusanyia matunda ili kuhakikisha matunda hayapotei. Siyo maghala tu, yatakuwa ni maghala ambayo yatakuwa na vyumba vya ubaridi (cold rooms) ambavyo vitawasaidia wakulima kutunza mazao yao, yakae kwa muda mrefu wakati wanatafuta masoko.
Mheshimiwa Spika, moja ya jitihada kama nilivyosema ni kujenga viwanda vya kuchakata matunda ya machungwa, lakini tunavutia viwanda vidogo na vikubwa. Tumeshaanza kujenga viwanda vidogo kupitia vikundi vidogo vidogo ambavyo vitaongeza thamani. Pia tumeshaanza kuongea na wawekezaji wakubwa ambao wataenda kuwekeza kwenye eneo la Muheza kwa kuwapa vivutio maalum maana wengi wanataka kuwekeza mjini badala ya mashambani ambako ndiko kwenye machungwa. Kwa hiyo, tutaweka mkakati maalum wa kuwavutia ili wapate vivutio vya kuwekeza katika Mkoa wa Tanga hususan Muheza. Nakushukuru.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na ninashukuru kwa majibu yanayotia moyo ya Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza: -
Kwanza; kwa muda mrefu kilimo cha muhogo kimekuwa kikifanywa kienyeji na kwa vile kwa sasa soko lake ni kubwa na la uhakika ni lini Serikali itaanza kuwekeza kwenye utafiti hasa kupitia kwenye kituo chetu cha TARI Mlengano ili kuongeza tija kwenye uzalishaji wa zao hili?
Swali la pili; kutokana na uwezo mdogo wa kipato kwa wananchi wengi wa vijijini Muheza, hali inayokwamisha ushiriki wao kwenye kilimo chochote kinachohitaji muda mrefu na uwekezaji mkubwa.
Je, kwa vile nimeshasema kwamba soko la muhogo sasa hivi ni kubwa na la uhakika. Serikali haioni haja ya kuhimiza kilimo cha muhogo ambacho inachukua Miezi Tisa tu kuwa tayari ili kuongeza kipato cha wananchi hawa wa vijijini? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mwinjuma kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwanza kama nchi tuna- import wanga zaidi ya tani 8,000 kwa mwaka, pamoja na tunatumia muhogo kwa ajili ya chakula vilevile tunatumia wanga kwa ajili ya viwanda hasa kwenye maeneo ya pharmaceutical, matumizi ya nguo na viwanda vya karatasi.
Mheshimiwa Spika, nataka nimwambie kuhusu varieties sasa hivi tumeshatambua variety 10 katika utafiti ambazo zina uwezo wa kutuzalishia mpaka tani 20 mpaka 40 ambazo zimegundulika na watafiti wetu wa TARI. Hatua ya pili kumpelekea mkulima variety azalishe halafu hakuna uhakika wa soko ni jambo la hatari zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumechukua hatua kama Wizara tumeshaanza vikao na viwanda vyote vinavyotumia wanga kuweza kutambua ubora wa wanga wanaoutaka ili tuweze kuwapelekea wakulima na tutengeneze mfumo wa contract farming ili yale yaliyotokea Muheza mwaka jana na mwaka juzi yasiweze kujitokeza tena.
Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mwelekeo wa Serikali kuhusu muhogo ni mwelekeo wa industrial pamoja na matumizi ya chakula ndani zaidi tunataka ku-push mwelekeo wa industrial na tumeanza kuchukua hatua hizo. (Makofi)
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Tatizo la upatikanaji wa maji katika Mji wa Muheza bado ni kubwa pamoja na juhudi nyingi zinazofanywa na Serikali.
Je, ni lini mradi wa miji 28 ambao tunaamini kwamba ndiyo suluhisho la kudumu la tatizo hili utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamis, Mbunge wa Muheza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mradi wa Miji 28; miradi hii yote imeshaanza kutekelezwa kwa hatua za awali za kukusanya taarifa na kukamilisha taratibu za kuanza ujenzi tayari zimeshaanza ni vile hamzioni wanakusanya taarifa. Mradi huu ni design and build, kwa hiyo mwezi huu wa tatu tunatarajia wakandarasi waanze kuonekana sasa site na kuanza kufanya ujenzi.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na nashukuru kwa majibu mazuri na ya kutia moyo ya Serikali hasa kuhusiana na bomba la kilomita 14.5 na tarehe yake ya kukamilika. Hili ni moja ya matatizo tu nataka kupata commitment ya Serikali kuhusiana na tarehe ya kukamilika kwa mfumo mzima wa usambazaji ukiachilia mbali kilomita 14.5? Hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kama muda utaruhusu naomba kuambatana na aidha Waziri au Mheshimiwa Naibu Waziri kwenda Muheza ili jibu atakalonipa kwenye swali langu la nyongeza akawape wananchi wa Muheza pamoja na kujionea mwenyewe jinsi miundombinu ya usambazaji wa maji Wilayani Muheza kwenye Kata hizi za Mbaramo, Genge, Masuguru, Tanganyika, Majengo na Kwemkabala vilivyokuwa hoi, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kukupongeza sana Mheshimiwa Mbunge jitihada zako za kuweza kushirikiana na Wizara zinafahamika, commitment ya Wizara ni kuhakikisha muda ambao usanifu unataka mradi kukamilika tutajitahidi kufanya hivyo hizi kilomita 14.5 kuhakikisha zinakamilika na maji yatoke bombani, wananchi waweze kufurahia fedha ambayo Mheshimiwa Rais ametaka iwafikie. Lengo ni kuwatua akina Mama ndoo kichwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuambatana ni moja ya taratibu zote mara baada ya Vikao vya Bunge aidha mimi ama Waziri ukinihitaji mimi hakuna neno tutakwenda tukafanye kazi. (Makofi)
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwenye Jimbo la Muheza, Serikali iliahidi kupeleka Shilingi Milioni 600 kwa ajili ya shule mbili za sekondari kwenye Kata mpya. Kata moja ya Makole haijapata hata shilingi moja mpaka hivi tunavyoongea na mwaka wa fedha unakaribia kuisha.
Je, Serikali ina mpango wowote wa kupeleka fedha hizi kama ilivyoahidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamis Mwinjuma, Mbunge wa Jimbo la Muheza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa sekondari mpya katika Kata ambazo hazina sekondari unaendelea na kwa awamu ya kwanza Serikali ilipeleka Shilingi Milioni 470 katika Kata hizo, na itakwenda kumalizia Shilingi Milioni 130 kukamilisha Milioni 600. Ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kama Kata hii ya Makole haipo kwenye orodha ya kupata Milioni 600 na haijapata, tutafuatilia tuone ni kwanini haijapata ili iweze kupata kama ipo kwenye orodha ya kupata shule hizo.(Makofi)
MHE. HAMISI M. MWINJUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu ya kutia moyo ya Serikali. Na nina swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa vile suala hili linakuja na maslahi makubwa ya kiuchumi na kuna Ushahidi wa migongano katika maeneo kadhaa ambayo CMOs zimewahi kuruhusiwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha migogoro miongoni mwa CMOs hizi binafsi haitakuwepo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Naomba nijibu swali la nyongeza moja la Mheshimiwa Hamisi Mwinjuma, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Sheria hii ilipoanza kutekelezwa kwenye nchi zingine kuna migogoro ilijitokeza baina ya wadau. Sisi tumejipanga baada ya hili kupitishwa na Bunge hili tutakaa na wadau wote wa tasnia mbalimbali katika sanaa, kama ni wanamuziki wa Injili, kama ni wanamuziki wa Kizazi Kipya tutakaa nao. Tutahakikisha Uongozi wao tunauimarisha, lakini pia wanafahamu kwa nini CMOs zikakusanye na COSOTA itasimamia suala zima, kuhakikisha kwamba hawa watu hawaingii kwenye mgogoro.