Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo (18 total)

MHE. REUBEN N. KWAGILWA Aliuliza:-

Je, ni lini wananchi katika mitaa 30 isiyo na umeme Wilayani Handenni watapatiwa umeme kulipia mradi wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Reubne Nhamanilo Kwagilwa Mbunge wa Handeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika vijiji, mitaa na vitongoji visivyokuwa na umeme kupiitia miradi mbalimbali. Kwa sasa mkandarasi Kampuni ya M/S Sengerema Engineering Ltd. amepewa kazi ya kupeleka umeme katika vijiji 15 na mitaa vitongoji zaidi ya 30 katika Wilaya ya Handeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hizo zinajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa KV 0.4 umbali wa km. 27.5, ufungaji wa transfoma 11 za 50 kVA na 100 kVA; pamoja na kuwaunganisha wateja wa awali 669. Mradi unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 3.36. Utekelezaji wa mradi umeanza mwezi Februari, 2020 na utakamilika ifikapo Disemba, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, TANESCO inaendelea kuunganisha umeme kwa wateja ambao hawajaunganishiwa umeme katika mitaa na vitongoji vya Tanzania Bara ikiwemo Wilaya ya Handeni kupitia majukumu yake ya kila siku.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji Handeni Trunk Main (HTM)?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilipata mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India kupitia Benki ya Exim, jumla ya Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika miji 28 nchini ukiwemo Mradi wa Maji wa Kitaifa Handeni (Handeni Trunk Main) utakaohudumia vijiji 84 katika Wilaya ya Handeni pamoja na Miji Midogo ya Mkata, Komkonga, Kabuku, Michungwani,Segera pamoja na Mji wa Handeni.

Mheshimiwa Spika, taratibu za kupatikana kwa wakandarasi watakaotekeleza mradi huu zimekamilika na unatarajiwa kuanza wakati wowote katika mwaka wa fedha 2020/2021 na ujenzi wa mradi umepangwa kutekelezwa miezi 24.
MHE. REUBEN N. KWAGILWA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Handeni, Mziha hadi Turiani, Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Handeni – Mziha – Turiani yenye urefu wa kilometa 109.36, inahudumiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Handeni – Mziha – Turiani umekamilika. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetengwa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kulipa sehemu ya madai ya mkandarasi wa barabara ya Magole – Turiani yenye urefu wa kilometa 45.2 na kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Turiani – Mziha – Handeni yenye urefu wa kilometa 104.0 kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Handeni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mpango wa kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi ikiwa na lengo la kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi katika kila ngazi ya Mkoa na Wilaya. Tangu mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga zaidi ya shilingi bilioni 76 kwa ajili ya kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi 33, ambapo vyuo 29 ni vya ngazi ya Wilaya na vyuo vinne ni vya ngazi ya Mkoa. Mpaka sasa vyuo hivyo viko katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Handeni kuna Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Handeni ambacho pia kinatoa mafunzo ya ufundi stadi. Katika chuo hiki Serikali ilifanya ukarabati na ujenzi wa miundombinu uliogharimu jumla ya shilingi milioni 599.6 na kwa sasa Chuo kinaendelea kutoa mafunzo ya ufundi stadi.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA wilayani humo, nashauri wananchi wa Handeni kuendelea kutumia vyuo vilivyopo nchini, ikiwa ni pamoja na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi wa Handeni. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. REUBEN N. KWAGILWA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga miundombinu ya kisasa katika mnada wa Nderema?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ilitenga kiasi cha Shilingi 287,194,890 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi na uboreshaji wa miundombinu katika mnada wa mifugo wa Nderema uliyopo Halmashauri ya Mji wa Handeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mzabuni ameshapatikana na ameshakabidhiwa mradi mwezi Januari, 2022 na sasa ujenzi umeshaanza. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2022 kwa mujibu wa mkataba.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE K.n.y. MHE. REUBEN N. KWAGILWA
aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme mitaa 28 ya Jimbo la Handeni Mjini ambayo bado haijapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Handeni Mjini lina jumla ya mitaa 60. Kati ya mitaa hiyo 32 ina umeme sawa na asilimia 53.3 na mitaa 28 haina umeme sawa asilimia 46.7.

Mheshimiwa Spika, Mitaa yote 28 ya Handeni Mjini ipo katika mpango wa kupatiwa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini, awamu ya tatu, mzunguko wa pili, unaotekelezwa na mkandarasi kampuni ya Derm Electrics Tanzania ambaye yupo eneo la kazi na anaendelea na ujenzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Handeni.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huu utakamilika Mwezi Desemba, 2022.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo kikubwa cha kupozea umeme Kwambwembwele Vibaoni?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kwagilwa Reuben Nhamanilo, Mbunge wa Handeni, kwa niaba ya Mheshimwa Waziri wa Nishati, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza mpango wa kuimarisha Gridi ya Taifa uliopewa jina ‘Gridi Imara’ kwa kujenga miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme pamoja na vituo vya kupoza na kudhibiti umeme. Mpango huu una miradi zaidi ya 40 inayotekelezwa ndani ya miaka mitano kuanzia mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka 2022/2023 Serikali itajenga njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 132 kutoka Mkata kwenda Kilindi kupitia eneo la Kwambwembwele Vibaoni, Handeni Mjini. Katika mwaka wa fedha 2024/2025 kituo cha kupoza umeme kitajengwa na kupokea umeme kutoka katika njia ya Mkata/Kilindi itakayojengwa mwaka huu.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Bwawa la Mandela Kwenjugo na Kamkole Mabanda?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa Mbunge wa Handeni Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuboresha huduma ya maji Wilayani Handeni, Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za usanifu wa Mabwawa ya Mandela – Kwenjugo na Kamkole – Mabanda na usanifu huo utakamilika mwezi Juni, 2023. Ujenzi utaanza katika mwaka wa fedha 2023/2024. Kukamilika kwa ujenzi wa mabwawa hayo kutanufaisha wananchi wapatao 11,004 wa mitaa ya Mabanda, Komoza, Kwenjugo, Ngugwini, Bwila, Kwedisewa na Kwedigongo.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA K.n.y. MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Hospitali ya Halmashauri ya Mji Handeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 17.1 kwa ajili ya ukarabati wa Hospitali 19. Aidha, hadi kufikia mwezi Februari, 2023 kiasi cha shilingi bilioni 12.95 zimeshatolewa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya hospitali kongwe 14 ikiwemo Hospitali ya Mji wa Handeni iliyotengewa shilingi milioni 900.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itatenga shilingi bilioni 27.9 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe 31 zilizosalia.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Kwamagome?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kwagilwa Reuben Nhamanilo, Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2020/2021, Halmashauri ya Mji Handeni, ilitengewa shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati ya Kwamagome na mwaka wa fedha wa 2021/2022 shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati ya Kwaluwala katika Kata ya Kwamagome.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshatoa jumla ya Bilioni 117 kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya ya Msingi kwa ujenzi wa vituo vya afya kwenye Kata za kimkakati kote nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga pamoja na wataalam wa Ofisi ya Rais (TAMISEMI), watafanya tathmini ya kina kuhusu kata hii na mara fedha zitakapopatika Kituo cha Afya katika Kata ya Kwamagome kitajengwa.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Handeni – Kibirashi - Kondoa hadi Singida kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza ujenzi wa Barabara ya Handeni – Kibirashi – Kibaya – Chemba – Kwa Mtoro hadi Singida yenye urefu wa kilometa 424.24 kwa awamu. Ujenzi wa sehemu ya Handeni – Mafuleta kilometa 20 umefikia 11.61% na sehemu ya Mafuleta – Kileguru kilometa 30 mkataba umepelekwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mapitio (vetting).

Mheshimiwa Spika, Kwa sehemu iliyobaki ya Kibirashi – Kwa Mtoro – Singida (km 384.33) utekelezaji wake upo kwenye miradi itakayojengwa kwa utaratibu wa Engineering, Procurement, Construction and Financing EPC+F). Hadi sasa Mkandarasi wa kujenga barabara hii amepatikana na mkataba wa kuanza ujenzi umesainiwa tarehe 16 Juni, 2023. Ahsante. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Handeni Kibirashi, Kondoa hadi Singida kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza ujenzi wa Barabara ya Handeni – Kibirashi – Kijungu – Kibaya – Njoro – Olboloti – Mrijo Chini – Dalai – Bicha – Chambalo – Chemba – Kwa Mtoro hadi Singida kwa awamu. Taratibu za manunuzi za kumpata Mkandarasi kwa sehemu ya Handeni – Mafuleta (km 20) zipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba. Aidha, maandalizi ya kutangaza zabuni ya ujenzi kwa sehemu ya kutoka Mafuleta – Kwediboma yenye urefu wa kilometa 30 yanaendelea na zabuni itakuwa imetangazwa kabla ya mwezi Juni, 2022. Kwa sehemu iliyobaki Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Handeni Kibirashi, Kondoa hadi Singida kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Handeni – Kiberashi – Kibaya – Chemba – Farkwa – Kwa Mtoro hadi Kititimo Singida kwa awamu ambapo mkataba wa mkandarasi wa kujenga sehemu ya Handeni – Mafuleta kilometa 20 ulisainiwa tarehe 11 Aprili, 2022. Ahsante.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka kati ya Handeni na Kilindi katika eneo la Bondo?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kwagilwa Reuben Nhamanilo, Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilikwisha tatua mgogoro wa mpaka kati ya Halmashauri ya Mji wa Handeni na Kilindi katika eneo la Bondo kwa maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwenye kikao cha tarehe 25 Julai, 2023.

Mheshimiwa Spika, timu ya wataalam wa ardhi, Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama wa Wilaya na viongozi ngazi ya Tarafa, Kata na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi na Handeni walikutana tarehe 8 – 9 Oktoba, 2021 kwa ajili ya kupitia Tangazo la Serikali (GN), kuhakiki idadi ya watu, kuhakiki upatikanaji wa huduma za kijamii pamoja na kutoa ushauri wa kitaalam ambapo taarifa hiyo iliwasilishwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa utekelezaji.

Mheshimiwa Spika, Wakurugenzi wa halmashauri ya Kilindi na Handeni wameelekezwa kutekeleza masuala yafuatayo; kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi wa misitu, kuheshimu mpaka ulioainishwa kutokana na tafsiri sahihi ya matangazo ya Serikali, kurekebisha usajili wa shule za Msingi Bondo na Parakwiyo ili zisomeke ndani ya Wilaya husika, ahsante.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka Gari la Zimamoto Handeni Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na jitihada za kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga bajeti ya jumla ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa magari matano ya kuzima moto ambayo yatagawiwa katika Mikoa na Wilaya zenye upungufu wa magari ya Zimamoto na Uokoaji, ukiwemo Mkoa wa Tanga, hususan Wilaya ya Handeni, nashukuru.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka Gari la Zimamoto Handeni Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea na jitihada za kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga bajeti ya jumla ya shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ununuzi wa magari matano ya kuzima moto ambayo yatagawiwa katika Mikoa na Wilaya zenye upungufu wa magari ya Zimamoto na Uokoaji, ukiwemo Mkoa wa Tanga, hususan Wilaya ya Handeni, nashukuru.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaipatia Hospitali ya Wilaya ya Handeni Gari la kubebea Wagonjwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 itanunua magari 195 ya kubebea wagonjwa ambayo yatapelekwa kwenye Halmashauri 184 Nchini kote ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Handeni. Ahsante.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Kata ya Mabanda – Handeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Mabanda iliyopo Halmashauri ya Mji wa Handeni ni miongoni mwa Kata za kimkakati ambazo zimewekwa katika mpango wa kujengewa kituo cha afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kata hii imeingizwa kwenye orodha ya vituo vya afya vya kimkakati 214 vitakavyojengwa katika kila Jimbo ambapo inatarajiwa kuanza ujenzi katika mwaka wa fedha 2024/2025, ahsante.