Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo (30 total)

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa miaka mingi wananchi wa Jimbo la Handeni Mjini wamekuwa wakiishi katika dhiki kubwa ya maji. Ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji wa Handeni Trunk Main kutoka Mto Ruvu kwenda Handeni?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Napenda kumpongeza Naibu Waziri wangu kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, anayelala na mgonjwa ndiye anayejua mihemo ya mgonjwa. Mimi naishi Tanga, najua moja ya changamoto kubwa ni eneo la Handeni. Serikali imeainisha miji 28 na tumeshapata Dola milioni 500 kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa tuko katika hatua ya manunuzi. Ndani ya mwezi Aprili, Wakandarasi wote watakuwa site kuhakikisha tunajenga miradi mikubwa ya maji. Hii ni katika kutimiza azma ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ya kumtua mwanamama ndoo kichwani. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. REUBEN N. KWAGILWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza ili yaweze kupata majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa Wilaya ya Handeni ina majimbo mawili ya uchaguzi na mimi ni muwakilishi wa Jimbo la Handeni Mjini, je, Serikali haioni haja ya kuongeza wigo wa idadi ya viijiji ambavyo havijapata umeme upande wa Handeni Mjini hasa katika Kata ya Mlimani Konje, Kideleko kwa Magome, Kwenjugo, Kwadyamba, Malezi na Mabada?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kumekuwa na hali ya kukatika katika kwa umeme kila mara hali inayopelekea kuwapatia hasara wananchi kwa vyombo vyao vya umeme lakini vilevile kushindwa kufanya shughuli zao za kiuchumi za uzalishaji. Ni lini Serikali itakomesha tatizo hili wananchi wa Handeni Mjini washiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Reuben Mbunge wa Handeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya tatu, mzunguko wa pili wa REA unapeleka umeme katiika vijiji vyote Tanzania Bara ambavyo havikuwa na umeme ambavyo mpaka sasa havizidi 1974. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji vyake vyote ambavyo havikuwa na umeme vitapata umeme katika awamu hii ya tatu, mzunguko wa pili ambayo imeanza tayari mwezi wa nne huu na itakamilika kufikia Desemba, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo linaenda pia kwa Waheshimiwa Wabunge wengine wote wa Tanzania Bara, kwamba vijiji vyote ambavyo havikuwa vimepata umeme vimeingizwa katika awamu ya tatu, mzunguko wa pili na tutahakikisha tunapeleka umeme katika maeneo yote hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, ni kweli, Tanga kama Mkoa na Handeni ikiwemo imekuwa na matatizo ya kukatika kwa umeme ikiwemo Mikoa wa Mbeya Pamoja na Mkoa wa Kagera. Hata hivyo Wizara kwa kushirikiana na TANESCO imechukua juhudi mbalimbali kuhakikisha inamaliza tatizo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa Mkoa wa Tanga na hasa Handeni tatizo kubwa lilikuwa ni miundombinu chakavu ambayo ilikuwa inapelekea umeme katika maeneo hayo; na hivyo yamefanyika mambo mawili moja ni la sasa na lingine ni la muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, umeme unaokwenda Handeni unatokea katika kituo chetu cha Chalinze unakwenda kwenye substation ya Kasija, unatoka Kasija unakwenda Korogwe – Handeni – Kilindi, na njia ndefu sana ina km. zaidi ya 500. Kwa hiyo, tumebaini kuna nguzo zaidi ya 1300 ambazo zilikuwa zimeoza zimeanza kufanyiwa marekebisho na kuondolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka tunavyoongea sasa tayari nguzo zaidi ya 500 zimerekebishwa, na tumehakikisha kwamba kufikia mwishoni mwa mwezi wa nne, nguzo zote 1300 zitakuwa zimerekebishwa na kuhakikisha kwamba basi umeme haukatiki hovyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hatua ya pili ambayo ni ya kudumu na ya muda mrefu tumeshauriana na kukubaliana na wataalam, tumekubaliana tujenge kituo kidogo cha kupoza umeme pale Handeni. Kwa hiyo tutatoa umeme Kasija kwenye kituo cha kupoza umeme cha sasa tutapeleka Handeni, km. 81 kwa gharama ya shilingi bilioni 4nne. Tukishajenga kituo hicho cha kupoza umeme pale Handeni basi tutatoa line moja ya kuhudumia Handeni, tunatoa line moja kwenda Kilindi na line nyingine moja itaenda kwenye machimbo ambayo tumeambiwa itaanzishwa siku si nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo tunahakikisha kwamba basi tatizo la kukatika umeme Wilaya yetu ya Handeni na majimbo yote mawili litakuwa limefikia ukomo na tutakuwa tuna uhakika wa umeme.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri hapo umetoa maelezo marefu na mimi ninakupongeza sana. Sasa hapo umeitaja Mbeya halafu kule hujaeleza tatizo ni nini, maana huko kwingine umesema ni nguzo haya Mbeya unakatika katika kwa nini?

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilipoitaja Mbeya nikaitaja Kagera kwasababu na mimi natokea Kagera ili utakaponipa nafasi ya kuzungumzia Mbeya basi na Kagera nipitie humo humo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbeya tunayo matatizo makubwa mawili, tatizo moja kubwa ni radi ambazo zimekuwa zikisumbua mifumo yetu ya umeme kwenye transfoma. Tatizo hilo pia liko Mkoa wa Kagera. Tulichokifanya katika mikoa hii miwili tumeanza kufunga vifaa vinaitwa auto recloser circuit breaker ambayo vinazuia radi isirudi kwenye maeneo mengine ambayo hayajaathirika hilo ni tatizo moja kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tatizo la pili lilikuwa ni uchakavu wa miundombinu kwenye maeneo hayo. Tumeunda vikosi kazi maalum katika mikoa hiyo mitatu, Mbeya, Tanga na Kagera ya kuhakikisha kwamba kinapitia kila eneo na kubaini tatizo kubwa ni nini ili iiweze kurekebisha. Vikosi kazi hivyo viko kazini, vinafanya kazi; na tunahakikisha kufikia mwezi wa sita, maeneo yote ambayo yalikuwa yana matatizo sugu yatakuwa yamefanyiwa kazi na kurekebishwa.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali moja la nyongeza. Changamoto ya mawasiliano iliyopo katika Jimbo la Kilolo inafanana kabisa na changamoto ya mawasiliano ambayo tunayo katika Jimbo la Handeni Mjini, hasa maeneo ya Kwa Magome, Malezi, Mlimani, Konje, Kwediyamba, Kwenjugo, Msasa, Kideleko na Mabanda. Je, ni lini, Serikali itapeleka mawasiliano katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema Serikali inabidi ifanye tathmini, ni kwa sababu tumekuwa na uelewa ambao unatofautiana kidogo. Kuna maeneo ambayo tayari unakuta kwamba kuna mnara mmoja, kuna minara miwili, lakini wananchi wetu wanatamani kuona kila kijiji kina minara mitatu au minne. Kazi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kupitia Serikali yetu, ni kuhakikisha pale ambapo hakuna kabisa mawasiliano na ndipo Serikali inapokwenda kufikisha mawasiliano kwa wananchi. Ndio maana tunasisitiza sana, Serikali tutaendelea kuhakikisha kwamba tunafika katika maeneo husika na kufanya tathmini na kujiridhisha kama tatizo ni kwamba hakuna mawasiliano ama mawasiliano yaliyopo hayana ubora unaotakiwa na kama hayana ubora unaotakiwa basi tutaelekeza TCRA kuhakikisha kwamba inawawajibisha watoa huduma katika maeneo husika kulingana na makubaliano ya utoaji wa huduma nchini. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Ndani ya Mkutano huu wa Tatu Serikali ilikuja hapa ikatoa majibu kwamba mradi huu wa HTM utaanza mwezi wa Aprili. Wananchi wamekuwa wakiniuliza mara kwa mara mwezi Aprili umepita na mradi haujaanza. Sasa kwenye majibu ya Serikali wanadai kwamba mradi utaanza kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha. Mwaka wa fedha unaisha mwezi mmoja mbele, naomba nijue ni lini hasa mradi huu utaanza kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Handeni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, wananchi wa Jimbo la Handeni tuna dhiki kubwa ya maji na tumekuwa tukinywa maji kwenye mabwawa kwa miaka mingi lakini mabwawa haya pia yamebebwa na mvua katika misimu iliyopita. Bwawa la Kwimkambala pale Kwendyamba, Kumkole pale Mabanda pamoja na Bwana la Mandela pale Kwenjugo; yote haya yamebebwa na mvua.

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa mabwawa haya ili wananchi angalau tuendelee kunywa maji tukisubiria Mradi huu wa HTM. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru lakini nimpongeze Naibu wangu kwa namna anavyojibu maswali. Kubwa nimpongeze sana kaka yangu Reuben amekuwa amefuatilia mradi huu mkubwa wa miji 28.

Mheshimiwa Spika, kesho nimewaalika Wabunge wote wanaohusiana na mradi huu wa miji 28 tuwape commitment na uelekeo mzima wa mradi huu. Kwa hiyo nimwombe sana kesho katika kikao ambacho tutakachokaa tutatoa commitment ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kubwa tunatambua kabisa kwa eneo la Handeni palitokea mafuriko yale mabawa yalikwenda na maji, Mheshimiwa Mbunge kwa udharura huo na sisi tuna pesa za dharura, naomba saa saba tukutane tuone namna ya kuweza kusaidia wananchi wake waweze kupata huduma ya maji. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; Tokyo International Conference on African Development (TICAD) pamoja na mambo mengine inahusisha nchi zote za Afrika kupeleka vijana kwenda kusoma katika vyuo nchini Japan na kupata uzoefu kwenye kampuni kubwa za nchini Japan kwa lengo kwamba wanapotoka huko waje kufanya uwekezaji hapa nchini kwa kushirikiana na kampuni hizo za Japan. (Makofi)

Kwa nini mpango huu kwa Tanzania umekoma ilhali nchi nyingine za Afrika zinzendelea kupeleka vijana Japan kujifunza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; vijana hawa ambao tayari tumebahatika kuwapeleka Japan na wamesharejea. Serikali imewatumiaje kwa kushirikiana na kampuni sasa walikopata uzoefu huko Japan kwa ajili ya uwekezaji hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Tanzania na Japan bado wanaendelea na mipango ya kuwapa mafunzo na pia kupata uzoefu wa kazi mbalimbali kupitia taasisi zake nyingi ikiwemo JICA, lakini pia kuna utaratibu maalum baina ya Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa vijana kwenda kupata mafunzo Japan. Kwa hiyo, sio kweli kwamba tumekoma au utaratibu huo umesitishwa kwa sababu hata mwaka 2019 ambayo ni TICAD ya mwisho iliyofanyika nchini Japan baadhi ya maeneo ambayo yaliongelewa ni kuendeleza au kukuza ushirikiano wetu ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, alikuwepo kule Tokyo moja ya maeneo yaliyoongelewa ni kuona namna gani kutumia vijana wetu katika miradi mbalimbali ikiwemo kuvutia kampuni mbalimbali za uwekezaji nchini kama vile TOSHIBA, ambayo yanaweza kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kielektronic, lakini kuhusu kuwatumia vijana ambao wamepata mafunzo au uzoefu mbalimbali nchini Japan.

Mheshimiwa Spika, Tanzania bado inaendelea kuwatumia vijana hao wengi, lakini pia kwa Taarifa yako na mimi ni mmoja wa vijana hao ambao nimeweza kupata mafunzo Japan na ninaendelea kutumikia Serikali ya Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika sekta ya viwanda. (Makofi)
MHE. REUBEN N. KWAGILWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali langu la msingi lilikuwa: Ni lini, Serikali kwa kiasi kikubwa inatoa maelezo ya kipande cha barabara cha Magole – Turiani badala ya Handeni – Mziha –Turiani. Naomba kurudia: Ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kipande hiki cha Handeni – Mziha – Turiani? La kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; tunayo barabara inayofanana na hiyo ya kutoka Handeni – Kibilashi – Kiteto – Kondoa – Singida, mikoa minne inaunganisha barabara ile; Na bomba la mafuta linalotoka Hoima mpaka Tanga linapita kwenye barabara hiyo: Ni lini Serikali pia itaanza ujenzi wa barabara hiyo muhimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati njema sana, kwenye bajeti ya Wizara hii tarehe 27, 28 mwezi uliopita Mheshimiwa Waziri alisimama hapa kwenye Bunge Tukufu akataja kwamba tumepata kibali cha barabara 16 kati ya barabara 29 na barabara hii ya Handeni – Kibilashi – Kiteto – Kondoa – Singida imetengewa kuanza ujenzi wa kilometa 25 na wakati wote kuanzia sasa itatangazwa, ipo kwenye mchakato mbalimbali wa kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Wabunge wa maeneo ya Mkoa wa Tanga, Dodoma, Manyara na Singida ni kwa sababu tumepata activation kubwa, bomba la mafuta linapita hapa na mmeshuhudia Mheshimiwa Rais Museveni amekuja hapa na Mheshimiwa Mama Samia walikuwa pamoja wameweka sahihi ya ujenzi wa bomba hili la mafuta. Maana yake ni kwamba barabara hii ni lazima ijengwe ikamilike ili huduma hii iweze kufanya vizuri. Kwa hiyo, msiwe na wasiwasi ujenzi wa barabara hiyo utakamilika mapema sana. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kuuliza swali moja la nyongeza; ni lini Serikali itapeleka umeme kwa vijiji 28 ambavyo viko katika Jimbo la Handeni Mjini havijapata umeme mpaka sasa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kwagilwa Mbunge wa Handeni Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimshukuru pia na yeye kwa kuendelea kufuatilia upelekaji wa umeme katika maeneo yake. Jimbo la Handeni Mjini halina tofauti na Jimbo la Bukoba Mjini ambao ni maeneo ambayo hayakuwa yananufaika na Mradi wa REA, lakini sisi tumeweka katika mradi wa peri urban ambao tunatarajia kuuanza mwezi wa tisa na hivyo maeneo yote ya mijini ambayo pengine bado yanaonekana yana nature ya vijiji; Jimbo la Bukoba Mjini, Handeni Mjini na maeneo mengine yakiwepo yatapelekewa umeme kuanzia mwezi wa tisa kupitia mradi wetu wa peri urban ikiwa ni pamoja na Ilemela, Mwanza na maeneo kama ya Geita ambayo yako mjini, lakini yana hadhi ambayo ya kijijini. Nashukuru.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kwenye swali langu la msingi. Kwa kuwa Serikali imewaelekeza wananchi wa Handeni kuendelea kutumia Chuo cha Wananchi cha Maendeleo kilichopo Handeni wakati tukingoja ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya yetu: Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa vya kufundishia kwenye chuo hiki cha FDC kwa maana ya vitabu, mitambo na mashine? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, Serikali haioni umuhimu wa kukiendeleza chuo hiki cha FDC kilichopo ili kifikie kuwa katika hadhi ya Chuo cha VETA? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjii kama ifuaavyo: -

Mheshimiwa Spika, tarehe 10/10/2021 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliubainishia Umma kwamba tumepata fedha zile ambazo zinatokana na namna gani tunaweza kuondoa changamoto ya Uviko 19.

Katika fedha hizo, jumla ya shilingi bilioni 6.8 zimetengwa kwa ajili ya kupeleka vifaa pamoja na mitambo ikiwemo na vitabu katika vyuo 34 vya FDC. Miongoni mwa vyuo hivyo 34, kimojawapo ni hiki chuo cha Handeni.

Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi kwanza Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga vizuri, tunakwenda kupeleka vifaa pale ili kuhakikisha tunaboresha mazingira ya ufundishaji pamoja na vifaa ili vijana wetu waweze kupata taaluma yao katika eneo lile. (Makofi)

Katika eneo la pili anazungumzia namna gani tunaweza kuboresha chuo kile labda kiweze kuwa na hadhi ya VETA. Vyuo hivi vya FDC vilianzishwa kwa mkakati maalum wa kuhakikisha tunapeleka maendeleo katika maeneo yale. Hatuna sababu ya kuvibadilisha vyuo hivi kwenda kuwa VETA, ingawa bado vinatoa mafunzo haya ya VETA.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa vile Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba tunakwenda kujenga VETA katika kila Wilaya katika mipango yetu ya baadaye, chuo hiki tutaendelea kukiimarisha ili kiweze kutoa mafunzo na tija katika eneo hili ambalo limekusudiwa na Serikali wakati Serikali inajipanga kutafuta Chuo cha VETA katika eneo hilo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. kama ilivyo kwa Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Tanga haujaunganishwa na Mikoa miwili; Morogoro na Manyara. Barabara ya Handeni – Mziha – Turiani na barabara ya Handeni – Kiberashi – Kiteto – Kondoa – Singida; ni lini Serikali itakamilisha taratibu za kuanza ujenzi wa barabara hizi mbili?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayoanza Handeni kwenda Kiberashi hadi Kwamtoro taratibu zipo zinaendelea kwa kuanza na kilometa 50 na ziko kwenye hatua ya manunuzi; na barabara ya Handeni – Turiani upande wa kwenda Turiani barabara inaendelea kujengwa na bado hatujakamilisha kwa sababu ya upatikanaji wa fedha, lakini tayari nayo tumeshaanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, ni matumaini ya Serikali kwamba barabara zote ziko kwenye mpango na zitakamilishwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. REUBEN N. KWAGILWA: Mheshimwa Naibu Spika ahsante sana, naomba niulize swali moja la nyongeza kutokana na majibu ya swali langu la msingi. Mkataba aliopewa mkandarasi ambaye yupo site sasa kuujenga mnada wa Nderema, pamoja na kwamba unajenga miundombinu ya muhimu, bado kuna miundombinu ya msingi ambayo haijaainishwa kwenye mkataba na haimo kwenye mkataba, lakini miundombinu hii ni muhimu sana kwa mnada ule. Mathalani vibanda vya kupumzikia, mahali pa kupandishia ng’ombe kwenye magari pamoja na machinjio.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haifikirii pana umuhimu sasa wa kwenda kufanya marekebisho kwenye mkataba ule ili miundombinu hii iweze kuingizwa kwenye mkataba huu wa mkandarasi aliyepo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepeleka milioni 287 na mkandarasi atajenga miundombinu ikiwemo uzio, ofisi, mazizi manne, maeneo ya kushushia mifugo, lakini pia vyoo na miundombinu mengine. Hii ni hatua ya kwanza, hatua ya pili tutakwenda ku-consider miundombinu ambayo Mheshimiwa Mbunge ameisema ili tutenge bajeti kuhakikisha mnada ule unakuwa na miundombinu yote muhimu. Nakushukuru.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, ni hatua zipi zimefikiwa katika ujenzi wa njia ya msongo wa Kilovoti 132 inayotokea Mkata kupita Handeni Mjini kwenda Kilindi?

Swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuwa kukatikakatika kwa umeme na kutokuwa na umeme unaokidhi ndani ya Wilaya ya Handeni kumesababisha shughuli za uzalishaji kusimama na hasa kwenye migodi mikubwa iliyopo ndani ya Wilaya.

Je, uko tayari kuambatana na mimi baada ya Bunge hili ukaione hali halisi ya jinsi ambavyo uzalishaji umesimama kwenye viwanda vyetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua iliyofikiwa sasa katika utaratibu wa kujenga njia ya Mkata kwenda Kilindi kupitia Kwambwembwele, Handeni Mjini ipo katika utaratibu wa zabuni. Tunatarajia mwishoni mwa mwaka huu mkandarasi wa eneo hili na maeneo mengine ambapo tutajenga vituo vya kupooza umeme na line za kusafirisha umeme watakuwa wamepatikana. kwa hiyo saa hivi hatua ni ya zabuni na tayari maombi yameshafanyika inaendelea evaluation kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili, nipo tayari kabisa kuambatana na Mheshimiwa Mbunge kwenda Handeni Mjini lakini pia na maeneo mengine yenye matatizo ya namna hii ili tujionee na tuweze kuweka msukumo katika utekelezaji wa maelekezo na ahadi za Serikali kwa wananchi. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii. Mkoa wa Tanga haujaunganishwa na Mkoa wa Manyara pamoja na Mkoa wa Morogoro kwa barabara ya lami. Ni lini Serikali itajenga barabara Handeni – Kibilashi – Kiteto – Kondoa - Singida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niseme Serikali imepokea ushauri ulioutoa. Nikuhakikishie kwamba katika bajeti ijayo limezingatiwa na tutaendelea kuzingatia zaidi ili kuokoa hizi barabara ambazo tayari zimeshajengwa.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali la nyongeza la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa Mbunge, nataka nikuhakikishie kwamba barabara hii ambayo tumeitaja kutoka Handeni - Kiberashi kwenda Kibaya ni barabara ya changarawe na tayari tupo kwenye hatua za manunuzi, kilometa 50 kuanzia Handeni kuja Kiberashi kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami; na kama taratibu zote zitakamilika, barabara hii itaanza kujengwa mwaka huu wa fedha. Ahsante. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; ni lini Serikali itatenga na kupeleka fedha kwa ajili ya kujenga majengo tisa muhimu ya kutolea huduma za afya katika Hospitali yetu ya Halmashauri ya Handeni Mjini, ili kuipa hadhi iwe sawa na Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali imeshapeleka shilingi milioni 900 katika Halmashauri ya Handeni Mjini, kwa ajili ya kuanza upanuzi wa Hospitali hiyo. Nimuhakikishie kwamba zoezi hilo ni endelevu ili tuhakikishe majengo yote tisa yanajengwa na huduma bora zinatolewa kwa wananchi wa Handeni Mjini.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa niulize swali moja la nyongeza. Korogwe Vijijini inazo Tarafa tatu ambazo zina jiografia ngumu sana, Tarafa ya Magoma, Mombo na Bungu. Mheshimiwa Mbunge Mnzava anataka kujua kwa nini Serikali isiweke kituo kingine cha pili katika eneo la Makuyuni ambako ndio Makao Makuu ya Halmashauri ili iweze kuhudumia Tarafa zilizobaki za Mombo na Mashewa.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo la Makuyuni tutaipeleka hii selling point yetu na niwaondoe hofu wananchi wa Korogwe Vijijini watanunua mahindi kupitia eneo hilo la Makuyuni.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Handeni – Mziha - Turiani hasa ukizingatia kwamba barabara hii ndiyo barabara pekee inayounganisha Mkoa wa Tanga na Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Handeni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii tulishaanza kuijenga mpaka Turiani na katika mwaka huu tulitenga kiasi cha Bajeti, lakini barabara hii haikupata kibali cha kuanza kujengwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama alivyosema inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Tanga kupitia Handeni, tutaiweka tena kwenye mapendekezo ya bajeti ya mwaka huu ili tuweze kuunganisha Mkoa wa Morogor na Tanga kupitia Turiani - Mziha hadi Handeni.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; hivi sasa ipo mitambo ya Serikali kupitia DDCA inayochimba Bwawa la Kwenkambala na kwa Mahizi. Kwa nini Serikali isiibakishe mitambo hii ndani ya Wilaya ya Handeni itakapokamilisha Kwenkambala na kwa Mahizi ili iendelee kuchimba mabwawa hayo mawili ambayo unayazungumzia Mheshimiwa Naibu Waziri?

Mheshimiwa Spika, swali la pili mradi wa HTM mkandarasi tayari amekwishapewa msamaha wa kodi na alikwishakamilisha usanifu. Ni lini mkandarasi huyu atakuwa site kuanza ujenzi mara moja kwa mradi huu mkubwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilwa Mbunge wa Handeni Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mitambo kubaki Handeni hakuna tatizo tutahakikisha inabaki mpaka imalize kazi. Kuhusu mradi wa HTM lini utaanza tayari, mkandarasi anapaswa kuwa site; kwa hiyo baada ya hapa Mheshimiwa Mbunge tuonane ili tufatilie kwa pamoja kuhakikisha mkandarasi anakuwepo site.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara hii iliyotajwa na Mheshimiwa Mnzava lini Serikali wataanza kuiwekea changarawe ili angalau ianze kupitika wakati wote maana kwa sasa kuna maeneo mengi hayapitiki.
NAIBU WAZIRI, 0FISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi ni barabara ambayo ipo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, na inaunganisha pia wilaya mbili. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 barabara hii ilitengewa shilingi milioni 230 kwa ajili ya ukarabati wa kiwango cha changarawe, na Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara hii kuhakikisha makalavati yanapitika lakini pia na ule upembuzi yakunifu kwa ajili ya kuwa barabara ya lami.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana; kwa nini ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Magole – Turiani – Mziha – Handeni umeanzia Magole na kuishia Turiani na kuacha kipande cha Handeni – Mziha – Turiani?

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kwagilwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii aliyoitamka kwamba imeanzia sehemu hiyo kipande na kingine kimeachwa, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango wa Serikali ni kujenga yote. Kwa hiyo tumeanza hicho kipande, lakini hata kipande kingine pia tutakimalizia, ahsante.

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kwenye swali hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inaunganisha Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Morogoro pia imekuwepo kwenye Ilani za Uchaguzi za CCM tangu enzi za Mzee Mkapa, Mzee Kikwete, Hayati Magufuli na sasa Rais Samia. Je, kwa nini Serikali isiweke Wakandarasi Mwaka wa Fedha 2023/2024 kwa barabara nzima kilometa 104 yaani Turiani – Mziha – Handeni badala ya kuweka kipande hicho kidogo? (Makofi)

Swali la pili la nyongeza, kwenye bajeti za Wizara hii kwa mwaka wa fedha 2020/2021, 2021/2022, 2022/2023 na sasa 2023/2024 barabara hii imekuwa ikitengewa kiasi hiki cha fedha cha bilioni moja na majibu ya Serikali yamekuwa ni haya haya.

Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Morogoro kuhusu barabara hii na ahadi zake zisizotekelezeka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara aliyoitaja ipo kwenye Ilani na ni kweli kwamba inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Tanga, ni barabara ambayo kwa kweli ina historia yake na kwa maana hiyo Serikali ilishaanza kuijenga hadi Turiani, kwa sasa Serikali imedhamiria kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kuanzia Turiani, Mziha hadi Handeni, Kilometa 104, lakini kuweka Wakandarasi zaidi ya mmoja utaharakisha lakini kutategemea sana na upatikani wa fedha ili kuweza kuweka Wakandarasi zaidi ya mmoja kwa kipindi kimoja. Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba kwa mwaka ujao wa fedha tunaendelea pale tulipoishia kukamilisha barabara hii hadi Handeni. Ahsante. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kwenye swali langu la msingi. swali la kwanza ni lini sasa Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na hao wataalam wa TAMISEMI uliowasema watafanya tathmini hiyo ya kujenga kituo cha afya pale Kwamagome?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ahadi hii ya ujenzi wa kituo cha afya ilifanywa kwenye mkutano wa hadhara na Waziri wa TAMISEMI.

Je, uko tayari baada ya Bunge hili la bajeti tuambatane mpaka Kata ya Kwamagome ili ukawaeleze wananchi kwa nini ahadi hii haijatekelezwa kwa miaka miwili tangu imetolewa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kwagilwa hili la kwanza la Ofisi ya Mganga Mkuu lini itaenda na hii timu ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Naomba nitumie Bunge lako hili Tukufu kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga pamoja na timu yetu ya tathmini iliyopo Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha wanafika katika Halmashauri ya Mji Handeni na Kata ya Kwamagome kwa ajili ya kufanya tathmini na kuona kama idadi ya watu inayohitajika na ukubwa wa kata ile vinakidhi vigezo vya kupata kituo cha afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili naomba nisisitize wafanye hivyo mara moja huku wakiwasiliana vilevile na Mheshimiwa Kwagilwa ili aweze kuwepo kwa niaba ya wananchi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pii nipo tayari kuongozana na Mheshimiwa Kwagilwa kuweza kufika Kata ya Kwamagome.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Kampuni hii ya Henan Highway Engineering Group iliyopewa kipande cha Handeni – Mafuleta kilometa 20, umepita mwaka mzima sasa tangu kampuni hii ipewe kandarasi hiyo, lakini ujenzi unasuasua. Kwa nini ujenzi huu unasuasua na unaenda kwa kuchelewa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza; ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Turiani – Mziha – Handeni kilometa 104 kwa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli mkandarasi hajaenda kwa speed ama kwa kasi ambayo tulikuwa tunaitegemea na hii ni kutokana na sababu kadhaa. Moja ya sababu wakati amekabidhiwa barabara hii kulikuwa na changamoto kubwa sana ya mahali pa kutolea materials ambayo ilichukua muda mrefu sana mpaka ku-acquire hilo eneo kwa sababu lilikuwa na mgogoro. Kwa sasa suala hilo limeshakamilishwa na sasa anaendelea kupata yale material ambayo alikuwa anahitaji kutoka kwenye hiyo sehemu ya kutolea materials.

Mheshimiwa Spika, suala lingine kulikuwa na changamoto kwenye management ya kwake, lakini hilo suala pia limeshakamilishwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama alivyomsikia Waziri wa Fedha madai yale ya wakandarasi akiwepo huyu mkandarasi wa barabara hii ya Handeni – Mafuleta malipo yao yatatolewa ili waweze kuendelea, lakini pia wanapokuwa wanapewa kazi hawa wakandarasi moja ya sifa ni uwezo wao kifedha na hatutegemei akiwa 11% aweze kusimama, anatakiwa aendelee lakini pia vifaa ikiwa ni pamoja na management yake kwa kweli ndiyo maana wanafanyiwa due diligence. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili, nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti hii ambayo tunaendelea nayo tumetenga fedha kwa ajili ya kuanza ama kuendelea na ujenzi pale tulipoishia ya Turiani – Mziha hadi Handeni kwa mwaka ujao wa fedha, ahsante.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa magari ya wagonjwa yaliyoagizwa na Serikali yanakuja kwa awamu, je, Serikali haioni umuhimu kwa awamu ya kwanza kuanza na Hospitali ya Mji Handeni kwa sababu haina gari la wagonjwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, magari haya yanakuja kwa awamu kama ambovyo nimesema awali na kila Halmashauri ilikuwa tumepanga kupeleka magari mawili na gari lingine la tatu kwa ajili ya monitoring and evaluation katika Halmashauri hizi.

Mheshimiwa Spika, tunapokea ushauri ambao umeutoa wa kuangalia Halmashauri zile ambazo zitakuwa zina eneo dogo lakini lile gari la monitoring and evaluation, bado litakwenda kwa ajili ya kuhakikisha kwamba huduma za afya zinasimamiwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali la Mheshimiwa Kwagilwa, tutakaa naye na kuona katika awamu hii ya kwanza, Hospitali ya Mji pale Handeni inaweza kupata gari pia. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka mwaka jana kwenye bajeti majibu ya Serikali yamekuwa ni haya haya hayabadiliki. Hatua za mwisho za kusaini mkataba. Swali langu la msingi lilikuwa ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ipi Barabara ya Handeni - Kwa Magome, Nziha - Turiani. Ni lini Serikali pia itaanza kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Reuben kwa jinsi anavyofuatilia barabara ambazo zinaanzia katika Jimbo lake kwenda kwenye Majimbo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea nataka nimhakikishie Mheshimiwa Reuben kwamba tayari kazi ya ujenzi imeshaanza na hivi tunavyoingia huku Mkandarasi ameshapatikana na sasa ameanza mobilization kupeleka vifaa site kwa hizo kilomita 20 ambazo zilishatangazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ya kutoka Handeni Mjini kuja Turiani naomba tusubiri bajeti ipitishwe halafu tuone tutakachofanya katika hiyo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. REUBEN N. KWAGILWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kwenye swali hili.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; ni lini sasa Serikali itamkabidhi mkandarasi huyu site ili ujenzi uweze kuanza mara moja? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza; barabara ya Handeni – Mziha – Turiani ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka karibia 30.

Je, Serikali haioni kwamba inakikosea Chama cha Mapinduzi kwa kutotekeleza ahadi yake ambayo ipo kwenye Ilani kwa miaka 30 iliyopita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara hii kama nilivyosema kwenye jibu la msingi mkandarasi ameshasaini tangu tarehe 11 Aprili na anaitwa Hernan Highway Engineering Group Company Limited na sasa hivi anachofanya ni maandalizi kwa ajili ya kuanza ujenzi. Kwa hiyo, taratibu zitakapokamilika ili akamilishe site tutamkabidhi na tutapenda kwa kweli Mheshimiwa Mbunge aweze kuwepo wakati sasa anaanza kazi rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu barabara ya Magole – Mziha – Handeni; Serikali imeeshaanza kwa kipande cha Magole – Turiani na katika mwaka huu wa fedha, fedha imetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa barabara hii ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini pia kuhakikisha kwamba hii barabara tunaijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kupata maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, mara baada ya mgogoro huo kutatuliwa, Shule ya Msingi Bondo iliyokuwa Handeni Mjini tumeikabidhi Kilindi, na Shule ya Msingi Parakwiyo iliyokuwa Kilindi imekabidhiwa Handeni Mjini. Swali langu ni kwamba, ni lini sasa Sereikali itaweka utaratibu wa walimu wa shule hizi mbili kuhamishiwa kwenye halmashauri husika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi mara baada ya Bunge hili kwenda Kata ya Kwamagome kwenye eneo linaloitwa Kwaubaka ambako sasa baada ya kuikabidhi Shule ya Msingi Bondo kwenda Kilindi, tumeanza jitihada za kujenga shule nyingine ili akajionee jitihada za wananchi na waone namna gani Serikali watatusaidia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Kwagilwa, kama ifuatavyo; kwanza, niwapongeza Wananchi wa Halmashauti ya Handeni pamoja na Kilindi kwa kutatua mgogoro huu na nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kusimamia suala hilo kwa umakini mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie tu kwamba tumeshatoa maelekezo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, kuhakikisha ifikapo tarehe 30 Desemba mwaka huu Watumishi wote wa shule ya Bondo na Parakwiyo wawe wamepewa barua zao za uhamisho kulingana na eneo ambalo wanatakiwa kuwa katika halmashauri hiyo.

Mheshimiwa Spika, pili, niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kuona juhudi za wananchi na kuona namna gani Serikali itawaunga mkono. Ahsante.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, magari matano ni machache sana kwa mikoa yote na Wilaya zote zenye uhitaji, je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatuhakikishiaje wananchi wa Handeni Mjini, kwamba magari haya matano yatakapowasili moja litapelekwa Handeni Mjini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; mwaka wa fedha 2023/2024 umebakiza miezi minne tu kukamilika, je, Serikali ipo katika mchakato gani wa manunuzi kwa magari haya matano ya zimamoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshasema kwenye jibu la msingi katika haya magari pamoja na uchache wake, Handeni mtazingatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaeleze Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeridhia kupata mkopo wenye masharti nafuu wa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 100 zitakazowezesha kupata magari na vitendea kazi vingine kwa ajili ya kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Mara vifaa hivyo vitakapopatikana, mikoa yote na Wilaya zote ambazo hazina vitendea kazi hivyo watapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali la pili kuhusu mchakato wa manunuzi umefikia wapi, nataka nikuhakikishie, mchakato wa manunuzi uko hatua nzuri. Mara hizo fedha zitakapopatikana kutoka Hazina malipo yatafanyika ili tuweze kupata vifaa hivyo kabla mwaka wa fedha haujamalizika, nashukuru.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, magari matano ni machache sana kwa mikoa yote na Wilaya zote zenye uhitaji, je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatuhakikishiaje wananchi wa Handeni Mjini, kwamba magari haya matano yatakapowasili moja litapelekwa Handeni Mjini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; mwaka wa fedha 2023/2024 umebakiza miezi minne tu kukamilika, je, Serikali ipo katika mchakato gani wa manunuzi kwa magari haya matano ya zimamoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshasema kwenye jibu la msingi katika haya magari pamoja na uchache wake, Handeni mtazingatiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaeleze Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeridhia kupata mkopo wenye masharti nafuu wa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 100 zitakazowezesha kupata magari na vitendea kazi vingine kwa ajili ya kuliimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Mara vifaa hivyo vitakapopatikana, mikoa yote na Wilaya zote ambazo hazina vitendea kazi hivyo watapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali la pili kuhusu mchakato wa manunuzi umefikia wapi, nataka nikuhakikishie, mchakato wa manunuzi uko hatua nzuri. Mara hizo fedha zitakapopatikana kutoka Hazina malipo yatafanyika ili tuweze kupata vifaa hivyo kabla mwaka wa fedha haujamalizika, nashukuru.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii niulize swali moja la nyongeza. Kutokana na ugumu wa jiografia za halmashauri, majirani zetu, hospitali hii imekuwa ikihudumia wagonjwa kutoka Mvomero, Chalinze, Kilindi, Handeni DC pamoja na kwetu Handeni Mjini.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kutuongeza walau tuwe na ambulance mbili kwenye hospitali hii ili kuhudumia wagonjwa wa halmashauri hizi zinazotuzunguka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Reuben Kwagilwa, Mbunge wa Jimbo la Handeni Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kwagilwa kwa kazi kubwa anayoifanya kuwasemea wananchi wa Jimbo la Handeni Mjini. Nimhakikishie tulifanya ziara pamoja kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Handeni, tuliona mahitaji yale na nimwahidi kwamba kwenye magari haya ambayo yatanunuliwa kwanza moja lazima apate lakini tutafanya tathmini kuona uwezekano wa kupata gari lingine kwa ajili ya Halmashauri yake. (Makofi)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kwenye swali hili la msingi.

Swali la kwanza, je, ukiacha hii Sheria ya Milki anayoizungumzia ni lini Serikali kwa ujumla wake kabisa italeta sheria kubwa na pana itakayo govern sekta ya makazi na upangishaji kwa maana ya real estate?

Swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kanzidata ya nyumba za kupangisha kwenye Majiji, Manispaa na Miji ndani ya nchi yetu?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi tupo katika hatua za ndani za Serikali, kuandaa sheria itakayotoa mwongozo wa jinsi ya kuenenda kwenye soko la nyumba kwa maana ya real estate. Sheria hiyo pamoja na mambo mengine itaunda chombo ambacho kitasimamia mawakala wote wa upangishaji na upangaji wa nyumba.

Mheshimiwa Spika, swali pili Wizara inaendelea na mchakato na iko katika hatua za mwisho kabisa za kutengeneza mfumo mkubwa wa management ya ardhi nchini. Moja kati ya maeneo hayo unapotaja mfumo wa usimamizi wa ardhi, utataja nyumba zilizoko kwenye maeneo yetu vilevile itatoa matumizi ya nyumba ile ikiwa ni pamoja na matumizi ya ardhi ya kiwanja kile.

Mheshimiwa Spika, katika mfumo huo tutazingatia ushauri wa Mbunge kwa kuweka uwezo wa kujua nyumba za upangaji ziko ngapi na kuweza kutoa miongozo na kuweza kuzisimamia ili wananchi wasiweze kupata taabu zilizopo sasa.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itaifanya Zahanati ya Hedi kwa Magome kuwa kituo cha afya kama Waziri wa TAMISEMI alivyoahidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kadri ya ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuongeza miundombinu kutoka zahanati ili iweze kukidhi ngazi ya kuwa kituo cha afya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kulifanyia kazi jambo hilo.