Primary Questions from Hon. Zaytun Seif Swai (19 total)
MHE. ZAYTUN S. SWAI Aliuliza:-
Kutokana na changamoto za vyanzo vya mapato hususan katika Halmashauri zilizo nje ya miji kumekuwa na uwiano usio sawa wa utoaji wa mikopo.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutafuta njia ya kuweka uwiano sawa wa mikopo hiyo bila kujali mapato ya Halmashauri husika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri hutolewa kwa kuzingatia kifungu cha 37A cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 na Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019. Halmashauri inatakiwa kutenga na kutoa asilimia 10 ya fedha za makusanyo ya ndani katika kipindi husika kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu baada ya kuondoa vyanzo lindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa sheria hii ni asilimia 10 ya mapato yanayokusanywa kwenye Halmashauri husika ambayo yanatofautiana kati ya halmashauri moja na nyingine kutokana na fursa zilizopo. Hivyo, kiwango cha mikopo inayotolewa kinategemea uwezo wa makusanyo wa Halmashauri husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka hususan baada ya kuwepo kwa sheria ambapo mikopo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 26.1 mwaka 2017/2018 hadi shilingi bilioni 42.06 mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio hayo Serikali inatambua changamoto zinazotokana na utaratibu huu na itaendelea kuuboresha ili kuongeza tija na kufikia malengo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo hii.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupima na kuchimba visima virefu Mkoani Arusha hasa Wilaya ya Longido katika Vijiji vya Noondoto, Matale, Wosiwosi na Ngereani ambapo kuna uhaba wa vyanzo vya maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kutokana na Wilaya ya Longido kuwa na uhaba wa vyanzo vya maji hasa chemichemi, Serikali imeendelea na jitihada mbalimbali ikiwemo kufanya utafiti wa maji chini ya ardhi na kuchimba visima virefu, ambapo katika Kijiji cha Matale B, uchimbaji wa kisima unaendelea kupitia Bajeti ya mwaka 2020/2021 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2021.
Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Noondoto, kinapata huduma ya maji kupitia mradi wa maji wa Kijiji cha Elang’atadabash unaohudumia vijiji vitano vya Elang’atadabash, Sokoni, Olchonyorokie, Noondoto, Losirwa na Naadare. Katika Kijiji cha Wosiwosi kisima kilichochimbwa, maji yake yalibainika kutofaa kwa matumizi ya binadamu kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha madini chumvi ukilinganisha na kiwango kinachokubalika.
Mheshimiwa Spika, hivyo, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali itatumia vyanzo vya Mto Engaresero kutekeleza mradi wa kufikisha maji Kijiji cha Matale na Wosiwosi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kijiji cha Wosiwosi, tumeweka bajeti ya kujenga bwawa litakalosaidia mifugo na wananchi.
Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Ngereani kinapata huduma ya maji kupitia Mradi wa Maji Tingatinga Ngereani. Serikali itaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Longido wanapata huduma ya maji safi na salama kwa kutumia vyanzo mbalimbali vitakavyoonekana vinafaa ikiwemo mito, visima na mabwawa.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani dhidi ya vitendo vya Ukatili vinavyofanywa kwa wanawake na watoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa tatizo la ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto na kuendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutokomeza ukatili huo. Moja ya hatua hizo ni pamoja na kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Mpango kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022. Mpango huu wa miaka mitano unalenga kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii yetu kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.
Mheshimiwa Spika, jitihada nyingine ni pamoja na kuanzishwa kwa Kamati 16,343 za Ulinzi na usalama wa wanawake na watoto kwenye ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zina jukumu la kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Pia kuanzishwa kwa madawati 420 ya Jinsia na watoto katika vituo mbalimbali vya Polisi nchini ambayo huwezesha wahanga wa ukatili kuripoti aina mbalimbali ya ukatili wa kijinsia.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imewezesha kutungwa kwa Sheria za Msaada wa Kisheria Na.1 ya mwaka 2017. Sheria hii inatoa fursa kwa wanawake waliofanyiwa unyanyasaji au kudhulumiwa kupata haki zao kupitia vyombo vya usimamizi wa sheria.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha utekelezaji wenye ufanisi wa Mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili, sheria zilizopo pamoja na kuimarisha Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto. Ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka uwiano sawa wa mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani bila kujali mapato ya halmashauri husika ili kusaidia wanufaika wa mikopo wanaoishi nje ya miji wapate fursa sawa na wanufaika wa mijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura ya 290 kifungu cha 37(a) na Kanuni zake za mwaka 2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msingi wa Sheria ya mikopo ya asilimia 10 ya wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu ni asilimia 10 ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri baada ya kuondoa mapato lindwa. Hivyo kiwango cha mikopo kinatokana na uwezo wa makusanyo ya halmashauri husika. Halmashauri zimeelekezwa kutoa fursa sawa za mikopo kwa vikundi vyote vilivyokidhi vigezo vilivyopo ndani ya halmashauri husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo hii ni sehemu tu ya mifuko mbalimbali ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi iliyopo nchini, na Serikali itaendelea kuiboresha kadri itakavyohitajika.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, ni lini akina Mama zaidi ya 300 waliokuwa Wafanyakazi wa Kiwanda cha Kiliflora Wilayani Meru watalipwa stahiki zao baada ya Kiwanda hicho kufungwa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Zaytun Seif Swai, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mgogoro uliopo baina ya wafanyakazi na mwekezaji wa Kampuni ya Kiliflora Ltd. Hivyo, Serikali ilifuatilia mgogoro huo na kubaini kuwa Tanzania Investment Bank (TIB) ilirejesha fedha iliyokopesha kwa kuuza mali za Kiliflora Ltd zilizowekwa dhamana ili kulipa deni la mkopo uliochukuliwa na Kampuni. Hivyo, kisheria Wafanyakazi wanapaswa kulipwa na Kampuni ya Kiliflora kwa kuwa kilichofanyika ni ufilisi kabidhi na siyo kufunga kampuni. Mfilisi Kabidhi (Receiver and Manager) ni tofauti na Mfunga Kampuni (Liquidator).
Mheshimiwa Spika, aidha, wafanyakazi wa Kiliflora Ltd, Wilson Samwel na Wenzake 502 walifungua Kesi ya Labor Na. ARS/ARM/305/2020, 152/2020 dhidi ya Kampuni ya Kiliflora Ltd na Frank Mwalongo ambaye ni Mfilisi Kabidhi ambayo ilianza kusikilizwa tarehe 30/10/2020. Shauri hili lilikwishatolewa maamuzi na Mahakama kwamba, masuala ya madai ya wafanyakazi yanapaswa kufanyiwa kazi na Kampuni ya Kiliflora Ltd maana haijafilisiwa kama ilivyoonekana kwenye taarifa za BRELA kwamba, Kampuni bado ipo hai.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango inaendelea kuhimiza mmiliki wa shamba la Kiliflora kuwalipa akina mama hao. Nakushukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Viwanda vya Kusindika Maziwa katika Mkoa wa Arusha?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Arusha ni moja ya mikoa yenye uzalishaji mkubwa wa maziwa ambapo unazalisha takriban lita 30,550,500 kwa mwaka. Mkoa wa Arusha una jumla ya viwanda 18 viwanda ambavyo ni vikubwa na vidogo vya kusindika maziwa vilivyosajiliwa na Bodi ya Maziwa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo uliosimikwa wa kusindika maziwa kwa viwanda tajwa ni kiasi cha takriban lita 43,789,200 kwa mwaka. Lakini hata hivyo, usindikaji halisi ni lita 6,315,400 kwa mwaka. Maziwa mengi hayaingii kwenye soko rasmi na kushindwa kupelekwa viwandani kwa ajili ya kuchakatwa, kutokana na ukusanyaji mdogo wa maziwa yanayozalishwa na wafugaji katika maeneo hayo. Jambo linaloathiriwa na ukosefu wa mifumo mizuri ya ukusanyaji wa maziwa (collection centres).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ni kushirikiana na sekta binafsi kuendelea kuhamasisha ujenzi wa miundombinu ya kukusanyia maziwa ili viwanda vyote vipate maziwa ya kutosha katika mkoa wa Arusha na mikoa mingine nchini, yenye uzalishaji mkubwa wa maziwa. Hii itasaidia kuongeza tija kwenye mnyororo wa thamani wa maziwa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya sintofahamu ya utaratibu wa kuwapata wanafunzi wanaorudishwa masomoni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa Mwongozo wa Februari, 2022 wa kuwarejesha wanafunzi waliokatisha masomo katika elimu ya msingi na sekondari kwa sababu mbalimbali ili waweze kukamilisha mzunguko wa elimu katika ngazi husika.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kusafisha maji kabla ya kusambazwa ili kuondoa Floride ambayo huleta ulemavu kwa Wakazi wa Arumeru?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati ya kuondoa madini ya fluoride kwenye maji ya kunywa na kupikia katika maeneo mbalimbali yaliyoathirika na madini hayo. Mikakati hiyo ni pamoja na kujenga Miradi ya Kusambaza Maji Safi na Salama kutoka kwenye vyanzo vya maji vya uhakika ambavyo havijaathirika na madini ya fluoride; kusambaza teknolojia ya kuondoa madini ya fluoride kwa kutumia chengachenga za mkaa wa mifupa ya ng’ombe; na kuweka mitambo ya reverse osmosis kwa ajili ya kusafisha maji ikiwa ni pamoja na kuondoa madini ya fluoride kwenye maji ya kunywa na kupikia katika Kata za Oldonyosambu, Ngaramtoni, Embasenyi katika Wilaya za Arumeru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Wizara kupitia Kituo cha Utafiti cha Kuondoa Madini ya Fluoride cha Ngurdoto imeendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya kiwango kikubwa cha madini ya fluoride katika maji ya kunywa na matumizi sahihi ya teknolojia ya kuondoa madini hayo kupitia vyombo vya habari, mikutano na makongamano mbalimbali.
MHE. MUSSA R. SIMA K.n.y MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma za Afya kwa Wazee hasa wa Mkoa wa Arusha kwa kuwapatia dawa kupitia mfumo wa bima tofauti na iliyopo sasa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekwishatoa maelekezo kwa wasimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya kuwa wazee wasio na uwezo na waliotimiza vigezo wapewe huduma za Afya wakiwa nje na ndani ya mikoa yao. Aidha, Serikali ipo kwenye hatua ya ukamilishaji wa Muswada wa Bima ya Afya kwa wote utakaowezesha makundi yote kupata huduma za afya.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI K.n.y. MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha Wanawake wanashiriki kikamilifu kwenye mnyororo wa madini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Wazari wa Madini, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wamekuwa wakishiriki kwa kiasi kikubwa kwenye sekta ya madini kupitia vyama mbalimbali ikiwemo Shirikisho la wachimbaji wadogo nchini (FEMATA) lenye lengo la kuwaunganisha wachimbaji wadogo wa madini wakiwemo wanawake pia Umoja wa Wanawake Wachimbaji Madini (TAWOMA) ambao unajumuisha wanawake wote wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji na utengenezaji bidhaa mbalimbali zinazotokana na madini. Pia wako Muungano wa Wanawake Wanaouza Bidhaa Mbalimbali Migodini (WIMO) na Chama cha Tanzania Women in Mining and Mineral Industry (TWIMMI) ambacho kimeundwa kwa lengo la kuwaweka pamoja wachimbaji wa madini wanawake na wote walioko kwenye sekta ya madini ili kuweka mazingira bora ya kuwawezesha wanawake na ustawi wa sekta ya madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na uwepo wa vyama hivyo Wizara imekuwa ikisaidia wanawake kwenye sekta ya madini katika mnyororo mzima kwa kuwapa leseni za uchimbaji, uongezaji thamani na uuzaji madini, ahsante sana.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kukomesha vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA). Ambapo, kamati za ulinzi wa wanawake na watoto zimeundwa kuanzia vijijini, mitaa hadi Taifa. Madawati ya jinsia na watoto sasa yako vituo vyote vya polisi. Madawati ya ulinzi na usalama wa watoto yanaendelea kuundwa ndani na nje ya shule zote za msingi na sekondari. Vyuo vyote vimeundwa madawati ya jinsia na mabaraza ya watoto 560 yameanzishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuimarisha utekelezaji wa MTAKUWWA, Serikali imeelekeza halmashauri zote kuhakikisha, ajenda ya kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto ni ya kudumu kwenye vikao ngazi zote, ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi katika Tarafa za Kitumbeine na Engarenaibor hususan kwenye migodi ya Rubi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali na Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa ya Kitumbeine na Engarenaibor zipo katika Wilaya ya Longido, Mkoa wa Arusha, Tarafa hizi hazina vituo vya Polisi vinavyofanya kazi. Huduma za Polisi hutolewa kwenye kituo cha Polisi cha Wilaya ya Longido kilichopo kilometa 54 toka Kitumbeine na kilometa 35 toka Engarenaibor. Serikali inatambua juhudi za wananchi wa Tarafa hizo mbili kuanza kujenga vituo vya Polisi viwili kwa nguvu zao na kwa kuwashirikisha wadau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Tarafa ya Kitumbeine jengo la Kituo cha Polisi limejengwa katika Kijiji cha Gelai Lumbwa, Kata ya Gelai Lumbwa lakini bado hawajaanza ujenzi wa nyumba za makazi ya Askari. Katika Tarafa ya Engarenaibor wananchi wamejenga Kituo cha Polisi katika kijiji cha Mundarara, Kata ya Mundarara na ujenzi umefikia kwenye hatua ya lintel.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawapongeza wananchi wa Tarafa ya Kitumbeine na Engarenaibor na itawaunga mkono katika kuchangia nguvu za wananchi ili kukamilisha ujenzi wa majengo hayo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 ili kutoa huduma za Polisi katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Shule ya Wasichana Arusha ambayo ilipangwa kujengwa katika Kata ya Enkikret - Longido?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia mradi wa kuboresha elimu ya sekondari imedhamiria kujenga shule za sekondari 26 za bweni za wasichana wanaosoma masomo ya sayansi kidato cha kwanza mpaka cha sita ambapo kila mkoa utajengewa shule moja. Ujenzi wa shule za bweni za wasichana za Mikoa unafanyika kwa awamu. Katika Awamu ya kwanza ya ujenzi Mikoa 10 imenufaika ambapo kiasi cha shilingi bilioni 30 zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo na ujenzi upo katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kuwa ujenzi wa Shule ya Mkoa wa Arusha utafanyika katika awamu inayofuata hivyo ombi lake lipo kwenye utaratibu wa utekelezaji, wakati wowote fedha zitakapokuwa tayari, zitapelekwa Halmashauri husika kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza vifo vya watoto wenye umri kati ya sifuri hadi mwaka mmoja?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeweka mipango ya kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa sifuri hadi mwaka mmoja kama ifuatavyo: -
Moja, kuongeza vituo vyenye vyumba maalumu kwa ajili ya kutoa huduma kwa watoto wachanga wenye hali mahututi (Neonatal Care Unit) kutoka 18 mwaka 2017 kufikia 175 mwaka 2023.
Pili, kutoa mafunzo kwa watoa huduma juu ya namna ya kutoa huduma jumuishi kwa watoto wachanga na watoto wakubwa (Integrated Management of Childhood Illness-IMCI).
Tatu, kuimarisha huduma za kukinga na kuzuia magonjwa yanayozuilika kwa chanjo kama vile surua, nimonia, kuharisha, donda koo, kifaduro, pepo punda na polio kwa kuongeza utoaji wa chanjo za watoto chini ya mwaka mmoja kufikia kiwango cha zaidi ya asilimia 98 ya utoaji wa chanjo ya Penta 3.
Nne, Serikali imeongeza vituo vinavyotoa huduma kwa watoto waliozaliwa wakiwa na uzito pungufu (Kangaroo Mother Care) ambapo kwa sasa vituo 72 na Hospitali 175 zinatoa huduma hizi. Aidha, kwa mwaka 2023/2024 Serikali imepanga kuongeza vituo 100 ili kufikia vituo 275 ifikapo mwezi Juni, 2024.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-
Je, ni lini Daraja la Mto Nduruma litakalounganisha Kata za Mlangarini, Nduruma na Bwawani Wilayani Arumeru litajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga Shilingi Milioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la mawe katika Mto Nduruma ili kuunganisha Kata za Mlangarini, Nduruma na Bwawani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TARURA itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara hii ili kuboresha mawasiliano ya Kata za Mlangarini, Nduruma na Bwawani.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Jengo la Mama na Mtoto kwenye Kituo cha Afya – Loliondo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Loliondo ni moja ya Vituo vya Afya chakavu 199 vilivyoainishwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa ajili ya upanuzi. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati pamoja na kuongeza miundombinu mbalimbali ikiwemo majengo ya Mama na Mtoto yenye uwezo wa kutoa huduma ya upasuaji wa dharura. Ahsante.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya maziwa Mkoa wa Arusha?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa za ujenzi wa viwanda vya maziwa katika Mkoa wa Arusha hutangazwa kupitia makongamano ya uwekezaji yanayoratibiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Vilevile, Kituo hiki huandaa safari na mikutano ya uwekezaji nje ya nchi ambapo hutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini ikiwa ni pamoja na fursa za uwekezaji wa viwanda vya kusindika maziwa katika Mkoa wa Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji nchini, Watanzania wanahimizwa kuendelea kuwekeza nchini kwa kutumia malighafi zilizopo katika maeneo yetu husika, nakushukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya maziwa Mkoa wa Arusha?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa za ujenzi wa viwanda vya maziwa katika Mkoa wa Arusha hutangazwa kupitia makongamano ya uwekezaji yanayoratibiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Vilevile, Kituo hiki huandaa safari na mikutano ya uwekezaji nje ya nchi ambapo hutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini ikiwa ni pamoja na fursa za uwekezaji wa viwanda vya kusindika maziwa katika Mkoa wa Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji nchini, Watanzania wanahimizwa kuendelea kuwekeza nchini kwa kutumia malighafi zilizopo katika maeneo yetu husika, nakushukuru.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI K.n.y. MHE. ZAYTUN S. SWAI aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Shule ya Wasichana Arusha ambayo ilipangwa kujengwa katika Kata ya Enkikret – Longido?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia mradi wa kuboresha elimu ya sekondari ilipanga kujenga shule 26 za bweni za wasichana za kitaifa katika mikoa yote nchini. Lengo la shule hizi ni kuongeza fursa kwa wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi na kuwaepusha na vishawishi vinavyosababisha kukatisha masomo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa shule hizi umefanyika katika mikoa yote kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilianza kwa mikoa ya Kagera, Shinyanga, Mwanza, Singida, Pwani, Songwe, Lindi, Dar es Salaam, Njombe na Ruvuma. Aidha, awamu ya pili imefanyika katika mikoa iliyobaki na kufanya mikoa yote kuwa imepokea fedha za ujenzi wa shule za bweni za wasichana za mikoa ikiwemo Mkoa wa Arusha ambapo ujenzi unafanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido na umefikia 85%. (Makofi)