Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Spika, kwa miaka mingi kumekuwa na changamoto nyingi sana kwenye suala la elimu nchini hasa katika vitendea kazi katika ufundishaji wa michepuo ya sayansi. Natoa rai kwa Serikali kutatua changamoto hii na kuweka vifaa vya laboratories katika shule za sekondari. Walimu wana changamoto kubwa sana mashuleni hasa kulingana na Serikali kutoajiri walimu kwa muda mrefu hii inafanya walimu kuelemewa mwalimu mmoja anafundisha madarasa matano. Tunaomba Serikali iaajiri walimu wapya ili wapunguze mzigo mkubwa wa vipindi kwa walimu wachache ambao hawakidhi mahitaji ukilinganisha na idadi ya wanafunzi.
Tunaomba Serikali iendelee kuwalipa walimu stahiki zao, wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu. Walimu wamekuwa na hali ngumu hasa wale wanaopangiwa shule za vijijini. Tunaomba Serikali iendelee kuwawekea mazingira bora walimu ili wafanye kazi zao kwa ufanisi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja hii iliyoko mezani.
Mheshimiwa Spika, nina mambo matatu; jambo la kwanza ni pongezi na Shukurani. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa maono na msukumo Mkubwa ambao ameuweka kwenye wizara ya kilimo. Pia tunampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi wananchi wa Mkoa wa Iringa, tunaishukuru Serikali sana kwa mpango wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata parachichi katika Wilaya ya Mufindi, Kata ya Nyororo. Tunamuomba Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha atuambie ni lini ujenzi wa kiwanda hicho utaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo langu la pili, ni ruzuku ya mbolea. Tunaishukuru sana Serikali kwa ruzuku ya mbolea, wananchi wanafurahia sana kwa jambo hilo. Tunaishukuru tena Serikali kwa sababu mwaka huu wametenga tena pesa kwa ajili ya mbolea ya ruzuku. Lakini msimu uliopita kulikuwa kuna changamoto nyingi ambazo zilitokea. Naomba kutoa mapendekezo yafuatayo ili kuweza kutatua changamoto hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, tunaomba mbolea zifike kwa wakati kabla ya msimu haujaanza. Kwa sababu mwaka jana mbolea ya kupandia ilichelewa hadi mahindi yamekwisha ota mbolea ya kupandia ndio inafika ambayo ilileta usumbufu mkubwa sana kwa wananchi na kero kubwa sana. Mheshimiwa Waziri tunaomba utusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, tunaomba ziwekwe center ambazo wakulima wataweza kupata m,bolea kwa wepesi. Kwa sababu kwa mfano kule kwetu Mkoa wa Iringa, mwananchi alikuwa anatoka Mauninga karibuni kilometa 100 anafuata mbolea Iringa Mjini, ni mateso makubwa sana. Mwananchi anatoka Maduma anakwenda mpaka Mafinga Mjini ndio apate mbolea, ni mateso makubwa sana. Tunaomba ziwekwe hizo center na pia Mheshimiwa Waziri, mfumo wa ugawaji wa mbolea uendane na uhalisia wa maisha ya watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mapendekezo mengine ni usajili wa wakulima. Mheshimiwa Waziri, tunakuomba uanze usajili wa wakulima mapema kwa sababu suala la usajili sio dharura. Unaweza kuanza kuwasajili sasa hivi ili kuondoa usumbufu ambao ulikuwa unajitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la nne; ni Mamlaka ya Mbolea Tanzania, Mfumo wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania, tunakuomba Mheshimiwa Waziri, ukaufanyie mapitio. Kwa sababu una mapungufu mengi ambayo mawakala wanalalamikia. Kwa hiyo, tunaomba ukafanye mapitio kwenye mfumo huo ili kutoa haya mapungufu na kuwaondolea mzigo mawakala. Mheshimiwa Bashe, tunaimani kubwa na wewe na tunaimani kwamba utatatua changamoto hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya tatu; ni stakabadhi ghalani, Serikali ina mpango wa kuingiza zao la mahindi kwenye mfumo wa stakabdhi ghalani katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Lakini Mheshimiwa Waziri anapohitimisha tunaomba atwambie amejipangaje? Kwa sababu tumeona kwamba kwenye zao la choroko na dengu kulikuwa kuna usumbufu mkubwa na changamoto nyingi. Je, amejipangaje kwenye huo mpango wake wa kuingiza zao la mahindi kwenye stakabadhi ghalani? Kwa sababu wakulima wana hofu na wanahitaji kuondolewa hofu hiyo ili waweze kupata faraja katika jitihada zao za uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri wanayoifanya na mikakati mizuri ambayo wameipanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza TANESCO kwa mfumo rahisi wa maombi ya huduma ya umeme kwa njia ya mtandao ambayo inamuwezesha mteja kupata huduma mbalimbali bila kufika katika ofisi za TANESCO. Natoa rai kwa Serikali kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili wauelewe mfumo huu ili kupunguza usumbufu na mazingira yote ya rushwa na kurahisisha upatikanaji wa huduma ya kuingiza umeme kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa hatua kubwa ya majadiliano kuhusu mradi wa LNG Lindi. Ni hatua gani majadiliano yamefikia mpaka sasa na lini mradi huu utaanza na kampuni zipi zinahusika na mradi huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anipe maelezo kama kuna National Fuel Reserve; kama ipo ni kiasi gani? Katika changamoto tunazopitia za upatikanaji wa mafuta kama nchi ni lazma tuwe na Strategic Fuel Reserve. Serikali ianzishe Fuel Price Stabilization Fund ambapo kukitokea kuvurugika kwa bei ya mafuta duniani Serikali iweze kuingilia kati na kutumia hii fund kutuliza bei za ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nawatakia utekelezaji mwema wa vipaumbele vya bajeti.