Primary Questions from Hon. Nancy Hassan Nyalusi (9 total)
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA (K.n.y. MHE. NANCY H. NYALUSI) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama katika Tarafa ya Mahenge Wilayani Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kuwa Mahakama ya Tarafa ya Mahenge iliyopo Wilaya ya Kilolo ni miongoni mwa Mahakama za Mwanzo hapa nchini zitakazoanza kujengwa kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022.
Napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupitisha Wizara ya Katiba na Sheria ambayo ndiyo inayokwenda kutekeleza ujenzi wa Mahakama hiyo. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge avumilie kidogo kuanzia Julai, Mahenge wanakwenda kushuhudia kuanzwa kwa ujenzi huo. Ahsante.
MHE. DAVID M. KIHENZILE K.n.y. MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi na kuanza kutumia Hospitali ya Wilaya ya Mufindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu katika Hospitali ya Halmashauri. Hadi Aprili 2021, ujenzi wa majengo saba ambayo ni jengo la utawala, jengo la huduma kwa wagonjwa wa nje kwa maana ya OPD, jengo la maabara, jengo la mionzi, jengo la wazazi, jengo la kuhifadhia dawa, jengo la kufulia umekamilika na ujenzi wa wodi ya watoto na wodi ya magonjwa mchanganyiko kwa wanaume na wanawake upo katika hatua ya upandishaji wa ukuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Mufindi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti na wodi ya upasuaji kwa wanaume na wanawake. Hospitali ya Wilaya ya Mufindi imeanza kutoa huduma za wagonjwa wa nje na inatarajiwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2022 hospitali hiyo itaanza kutoa huduma kwa zaidi ya asilimia 90 ya huduma zote zinazotakiwa kutolewa katika ngazi ya Hospitali ya Halmashauri.
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza na kukamilisha ujenzi wa barabara ya Igowole – Nyigo kilomita 54 ambayo imetajwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara anayoizungumzia Mheshimiwa Mbunge ni barabara ya Mkoa ya Igowole - Kasanga – Nyigo yenye urefu wa kilometa 54.51, inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi sekta ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya Igowole – Kasanga – Nyigo yenye urefu wa kilomita 54.51 kwa Wananchi wa Wilaya ya Mafinga. Kwa sasa, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na hatimaye kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kutafuta fedha ili kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami, Wizara yangu kupitia TANROADS inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii, ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha shilingi milioni 66 kimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Ahsante.
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya uhaba wa madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa hadi sasa ina jumla ya madaktari bingwa kumi na moja. Madaktari bingwa wa afya ya akina mama na uzazi wanne, madaktari bingwa wa upasuaji wawili, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani mmoja, madaktari bingwa wa watoto wawili, daktari bingwa wa macho mmoja na daktari bingwa wa mionzi mmoja.
Mheshimiwa Spika, katika kuongeza idadi ya madaktari bingwa, Wizara imepeleka kusoma jumla ya madaktari kumi na mbili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Iringa, ambapo madaktari wawili wanasomea
kinywa, sikio na koo, madaktari bingwa wa mifupa wawili, daktari wa magonjwa ya dharura mmoja, madaktari bingwa wa watoto wawili, madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani wawili, daktari bingwa wa meno mmoja, daktari bingwa wa usingizi mmoja na daktari bingwa mbobezi wa masuala ya watoto mmoja. Ahsante.
MHE. NANCY H. NYALUSI atauliza: -
Je, ni lini Serikali itafunga Mtambo wa Mashine ya Oxygen katika Hospitali ya Rufaa ya Iringa ili kuhudumia wagonjwa wa dharura?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 599.3 kwa ajili ya manunuzi ya mtambo wa kuzalisha Hewa Tiba ya Oksijen na ujenzi wa chumba cha kuhifadhia mtambo huo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na tayari hatua za manunuzi zimeanza na mradi huu utakamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2022.
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha usambazaji wa umeme katika Vijiji Nane vya Wilaya ya Mufindi ambavyo havijapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mufindi ina jumla ya vijiji kumi tu ambavyo havina umeme na vinapatiwa umeme kupitia Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, kupitia Mkandarasi anayeitwa OK Electrical Services Limited. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2023 vijiji vinane vilikuwa vimeshapatiwa umeme na vijiji viwili (2) vijulikanavyo kwa majina ya Itika na Mpangatazara bado havijapatiwa umeme. Vijiji vyote vinatarajiwa kupatiwa umeme ifikapo mwezi Juni, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Wilaya ya Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge Viti Maalum kutoka Iringa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kujenga chuo cha ufundi stadi katika kila mkoa na wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kujenga vyuo vya ufundi stadi katika wilaya 64 ambazo zilikuwa hazijajengewa vyuo hivyo. Tayari Serikali imeshakamilisha kuandaa michoro na upatikanaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Kilolo eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha ufundi stadi ni katika Kijiji cha Luhindo Kata ya Mtitu. Aidha, pamoja na kiasi cha shilingi milioni 45 kilichotolewa awali kwa ajili ya shughuli za maandalizi, tayari Serikali imetuma kiasi cha shilingi milioni 228 kwa kila chuo kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza:-
Je, lini Serikali itaboresha mafao ya Wastaafu kwa kuongeza kiwango cha pensheni anayopata Mstaafu kwa mwezi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA. VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii huongeza kiwango cha pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu mara baada ya kufanya tathmini na kujua uendelevu na uwezo wa kulipa mafao kwa wanachama wake. Tathmini hiyo hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kipindi kifupi, miaka mitano kwa kipindi cha kati na tathmini ya kipindi kirefu kwa miaka kumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni za ulipaji mafao Namba 11(1) za mwaka 2018, zinaelekeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuongeza pensheni kwa kuzingatia mfumuko wa bei na uendelevu wa Mfuko kila baada ya miaka mitatu. Hata hivyo, ninayo furaha kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa hadi sasa wastaafu wa Serikali waliboreshewa pensheni zao za kila mwezi ambapo imefikia kiwango cha chini cha shilingi laki moja na kuendelea, tofauti na hapo awali, ahsante.
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza:-
Je, Serikali inachukua hatua gani za kukabiliana na athari mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na hali ya kisiasa duniani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, na kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inafuatilia kwa karibu athari na fursa za kiuchumi na kijamii zinazosababishwa na hali ya kisiasa duniani ikiwemo vita kati ya Urusi na Ukraine. Aidha, hatua zilizochukuliwa ni pamoja na: -
(i) Kufanya tathmini ya athari za kiuchumi na jamii zinazotokana na vita ya Urusi na Ukraine kwa Tanzania;
(ii) Serikali kutoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kupunguza bei ya mafuta kwa kipindi cha kuanzia Juni 1, 2022;
(iii) Kuruhusu wafanyabiashara wenye uwezo wa kuleta mafuta kwa bei nafuu ili kuhakikisha uwepo wa mafuta nchini. Mpango huu unatarajiwa kupunguza bei ya mafuta kuanzia mwezi Agosti 2022;
(iv) Kuhamasisha wafanyabiashara kuagiza ngano kutoka nchi nyingine zinazozalisha ngano ikiwemo Afrika Kusini, Canada, Australia, Uswiss na Ujerumani;
(v) Kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya kuzalisha mbolea nchini ambapo kutokana na uhamasishaji huo, kampuni ya Itracom Fertilizers Limited kutoka Burundi inaendelea na ujenzi wa kiwanda mkoani Dodoma. Kiwanda hicho kitakapokamilika kinatarajiwa kuzalisha tani 500,000 kwa mwaka.
(vi) Serikali kuendelea kutekeleza mikakati mahususi ya kukuza utalii wa ndani na kikanda kupitia fursa za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na Kamisheni ya Utalii ya Shirika la Utalii Duniani kwa Kanda ya Afrika.
(vii) Kuimarisha sekta ya uzalishaji ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na tathmini ya hatua mbalimbali zinazopaswa kuchukuliwa kwa kila sekta ili kukabiliana na athari za kiuchumi na kijamii zinazotokana na hali ya kisiasa duniani ikiwemo vita ya Urusi na Ukraine, ahsante.