Supplementary Questions from Hon. Nancy Hassan Nyalusi (11 total)
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Spika, katika ukanda huu kuna barabara tatu ambazo ni Gohole, Nyigu, Mtwango, Nyololo na Mafinga Mgololo.
Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba barabara hizo zitapitika katika kipindi hiki cha mvua ambazo zinaanza? Kwa sababu hazipitiki. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nancy Nyalusi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo hili Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ameshaji-commit. Tulikubaliana kwamba mwaka wa fedha unaofuata 2022/2023 tutaanza kujenga eneo hili kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili naomba nitumie nafasi hii kutoa maelekezo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa, atembelee maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. Afanye tathmini na kama kuna shida basi matengenezo yafanyike, wananchi wapate huduma ya usafiri wa miundombinu wakati wote wa mvua. Ahsante.
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali, lakini hali bado ni mbaya.
Je, Serikali ina mkakati gani wa dharura wa kutatua changamoto hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Afya alieleza juzi hapa Bungeni, ni kwamba tunaendelea kuangalia sasa ikama ya madaktari kwenye hospitali zote za mikoa kwenye nchi yetu na kuwaangalia mabingwa kote waliko, tukiona na kuangalia hali ilivyo pale Hospitali ya Mkoa wa Iringa ili kuweza kuwahamisha maeneo mengine ambayo yamezidi na kupeleka kule Iringa.
Mheshimiwa Spika, lakini kuna masomo yanayoendelea miezi mitatu mitatu kwa ajili ya super specialists kwa hiyo tutawaondoa nao kwenye eneo hili na kuwasomesha kwa muda mfupi na kuwarudisha kwenye eneo hilo.
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Spika, skimu ya umwagiliaji ya Mgololo ambayo ina hekta 700 ilijengwa na Serikali kwa shilingi bilioni 1.9 ambayo ilikamilika mwaka 2012, mwaka 2013 ikaanza kutumika na mwaka 2013 hiyo hiyo mifereji ikaanza kuvujisha maji kwa sababu ilikuwa ni mibovu.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza kujenga mifereji hiyo ili kuokoa pesa yake iliyotolewa, lakini pia kwa sababu mradi huo haujakamilika na haujawanufaisha wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nancy Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli Skimu hii ya Mgololo ni muhimu kwa sababu inahusisha Kata mbili za Makungu na Kiyowela na humo ndani kuna vijiji zaidi ya tisa ambavyo vinanufaika na mradi huu. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti yetu inayokuja tutauingiza mradi huu kwa ajili ya utekelezaji ili kuweza kurekebisha mapungufu yote na uweze kuwanufaisha wananchi, hasa wa Vijiji vya Lugolofu, Kitasengwa, Lugema, Mabaoni, Makungu na Lole.
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Je, ni lini Serikali itapeleka mashine ya kupimia saratani ya matiti katika hospitali ya rufaa Mkoa wa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nafikiri Mheshimiwa Mbunge hilo ni hitaji la msingi kwa sababu mashine hiyo iko kwenye Hospitali ya Kanda ya Mbeya, lakini ni vizuri ikapatikana kwenye hospitali ya Mkoa wa Iringa. Basi mimi na wewe tuje tukae tushirikiane na wenzetu ili tuone ni namna gani tunaweza tukaweka utaratibu wa mashine hiyo kupatikana kwa sababu fedha zipo.
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante; je, ni lini Serikali itajenga mtambo wa kusafisha na kutibu maji katika Chanzo cha Mgombezi - Ilula?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nyalusi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chanzo cha Mgombezi ni moja ya vyanzo muhimu sana katika eneo la Iringa. Katika mwaka ujao wa fedha tuna mradi mkubwa sana wa USD Million 88.4. Kupitia mradi huu tunatarajia chanzo kile pia kiwe sehemui ya wanufaika kwa kupata eneo la treatment plant, lakini vilevile maeneo ya Kilolo pia yatapata kunufaika na tunatarajia pia kuwa na uboreshaji wa huduma ya maji safi na maji taka katika eneo la Iringa.
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Kwa kuwa mgogoro huu umekuwa ni wa muda mrefu na ni kero kubwa kwa wananchi wa Ng’ang’ange; je, Mheshimiwa Waziri upo tayari kufanya ziara katika kijiji hicho ili kuweza kutatua hiyo kero kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza linaloulizwa kwa niaba ya Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumhakikishia Mbunge kwamba kwa kuwa tumepanga ziara ya Mkoa wa Iringa, ambayo tutataka tutembelee majimbo yote na Halmashauri zote za Iringa, niko tayari pia kufika Halmashauri ya Kilolo ili kwenda kukutana na wananchi tuzungumze na kumaliza mgogoro huu. (Makofi)
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tunaishukuru Serikali kwa utekelezaji, hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itakamilisha kupeleka umeme katika Kijiji cha Idunda na Funuti, Kata ya Kimara katika Wilaya ya Kilolo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, ni lini Serikali itaanza kusambaza umeme katika Vitongoji Mkoani Iringa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili nyongeza la Mheshimiwa Nancy Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika jibu la msingi Vijiji vya Mufindi vitakamilika mwezi wa Sita mwaka huu kwa mujibu wa Mkataba, lakini vijiji vingine vyote nchini kama alivyovitaja yeye vya Kilolo kabla ya Desemba mwaka huu vitakuwa vimefikishiwa umeme kwa mujibu wa mkataba wetu tuliokuwa nao kwenye REA three, round two. Kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Nyalusi pamoja na Waheshimiwa wengine, kwamba jambo hili tunalisimamia kwa karibu zaidi kuhakikisha kwamba umeme unafika katika Vijiji vyote kabla ya mwaka huu kuisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la pili, tunaendelea kutafuta pesa ambayo itatuwezesha kupeleka umeme katika vitongoji vyote karibu 36,000 tulivyokuwa navyo nchi nzima katika miaka minne, mitano inayokuja kwa gharama ya Sh.6,500,000,000,000. Taratibu za kutafuta fedha hizi zinaendelea na zitakapokuwa tayari, basi zitaletwa kwa umma hili kazi hii iweze kufanyika na kuhakikisha vitongoji vyote vinapata umeme. (Makofi)
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru Serikali kwa utekelezaji ambao unaendelea. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa vyuo vingi vya VETA vina uhaba wa walimu na vifaa vya kujifunzia;
a) Je, Serikali ina mpamngo gani wa haraka wa kutatua changamoto hiyo?
b) Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba mitaala ya VETA inaendana na shughuli za kiuchumi katika maeneo husika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nancy, Mbunge Viti Maalum kutoka Iringa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali lake la kwanza, anataka kufahamu kuhusu mkakati wa Serikali kwa upande wa walimu na vifaa. Naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu pamoja na Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeshapata kibali kwa ajili ya kuajiri waalimu 514; na mpaka hivi sasa walimu 151 tayari wameshaajiriwa na kuripoti kwenye vile vyuo ambavyo vilikuwa vinaendesha mafunzo na hivi vyuo vipya; na tutaendelea na mkakati na mchakato huo wa kuajiri walimu kwa kadri fedha zitakavyoruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika swali lake la pili kuhusiana na suala la vifaa vya kufundishia na kujifunzia, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, kwamba Serikali tayari ilishatoa jumla ya shilingi bilioni 8.6 kwa ajili ya ununuzi wa samani kwenye vyuo vile 25 pamoja na vile vya mikoa na vifaa hivyo tayari vimeshanunuliwa na kupelekwa kwenye maeneo hayo. Lakini kwa upande wa vifaa vya kufundishia naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, tarehe 22 mwezi wa nne mpaka tarehe 30 mwezi wa nne, timu yetu ya wataalamu kutoka Wizara ya Elimu ikiongozwa na mimi mwenyewe pamoja na watu wa NACTVET pamoja na VETA tulifanya ziara katika nchi ya China kwa ajili ya kufanya venting ya vifaa vya kujifunzia na kufundishia, na Serikali tayari imetenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili kuhusiana na suala la mitaala, naomba nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge tunaendelea na mchakato wa mapitio ya mitaala pamoja na sera yetu ya elimu katika ngazi zote ikiwemo na hii ya VETA. Basi ushauri wake huu wa kuona namna gani tunaweza kuhusisha shughuli za kiuchumi na mitaala yetu tutakwenda kulizingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni hatua gani Serikali imechukua kuhakikisha kwamba, inaondoa usumbufu kwa wanachama kupata mafao yao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, kwa nini Serikali imeamua kuunganisha Mifuko ya Pensheni, haioni kwamba, imechangia kuzaa changamoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA. VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Nancy, kama alivyouliza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wetu wa Hifadhi ya Jamii au Mifuko yote kwa pamoja PSSF na NSSF imeweza kwa sehemu kubwa sana kuondoa changamoto za ulipaji wa mafao kwa wakati. Kwa kufikia sasa tunalipa ndani ya siku 60 kama mfanyakazi atakuwa hana changamoto zozote za kitaarifa au kumbukumbu na hata wakati mwingine tunalipa hata chini ya siku saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine ambazo Serikali imechukua kupunguza usumbufu ni pamoja na kuweka Mfumo wa TEHAMA ambapo mwanachama anapata taarifa zake kupitia simu yake ya kiganjani na hatua nyingine mojawapo, pia ilikuwa ni hii ya kuunganisha Mifuko ili kuweza kutengeneza utaratibu wa uwiano katika malipo, lakini pia ulinganifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, lilikuwa ni katika kutoa usumbufu, kwa nini Mifuko iliunganishwa. Mifuko hii iliunganishwa, la kwanza kulikuwa kuna changamoto kubwa sana ya uwiano wa mafao. Mtu alikuwa PPF na aliyekuwa LAPF unakuta wote wamefanya kazi sawa na wamestaafu sawa na wametumikia Taifa sawa, lakini mmoja unaweza ukakuta katika pensheni yake mwishoni akalipwa milioni 40 na mwingine milioni 75 kwa sababu ya utofauti wa Mifuko, lakini kwa hiyo, kutengeneza ulinganifu wa mafao tukaona ni bora kuweza kuunganisha Mifuko hii baada ya kupata utafiti uliofanywa kama actuarial evaluation.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya pili, ilikuwa ni uendelevu wa Mifuko. Uendelevu wa Mifuko hii kwa sababu ya kuwa mingi ilikuwa inasuasua sana katika kujisimamia na kuwa na uendelevu wake. Mpaka sasa baada ya kuchukua hatua ya kuiunganisha thamani iliyokuwepo kwa PSSF ilikuwa ni trilioni tano, lakini sasa Mfuko umeweza kufika zaidi ya trilioni 8.1. Kwa hiyo, unaweza ukaona tofauti hiyo kubwa kama faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine ilikuwa ni kupunguza gharama za uendeshaji. Hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ilikuwa zaidi ya mitano, sasa unakuta yote ina Menejimenti, Bodi na huku kuna Menejimenti, lakini pia kuna Bodi, kuziendesha na kulipa mishahara, gharama za operational cost na kadhalika zote zilikuwa kubwa sana. Tumeweza kufanikiwa kwa Serikali hii ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kupunguza hasara hiyo ya gharama ya uendeshaji kutoka asilimia 12 mpaka asilimia tano.
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Sheria imeweka wazi na inakataza lumbesa, lakini lumbesa bado inaendelea: Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba inakomesha ujazo wa lumbesa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli lumbesa ni jambo ambalo siyo la kisheria. Nitoe wito tu kwa wasimamizi wa hizi biashara za vijijini hasa maeneo hayo ambayo wananchi wanakiuka utaratibu, hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wale ambao wanaweka nje ya kipimo halisi na hasa kwenye mamlaka hizo za Halmashauri ambako Maafisa Biashara wanasimamia mazoezi haya.
MHE. NANCY H. NYALUSI: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, kwenye tathmini ya Serikali kati ya bidhaa ambazo zimeathiriwa na vita ya Urusi ya Ukraine ni mafuta ya nishati, mbolea na ngano.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kufuta VAT kwa wazalishaji wa mafuta ya kula ndani ya nchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, suala hili limejadiliwa na suala hili ni ushauri, linahitaji wataalam, tutakaa pamoja tutatoa majibu. Nadhani pengine leo ama kesho tutatoa jibu la suala hilo.