Contributions by Hon. Saada Mansour Hussein (6 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. SAADA MONSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi kuchangia. Kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili tukufu, nakishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniteua. Pia nawashukuru Umoja wa Wanawake wa Tanzania Taifa (UWT) pamoja na wanawake wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kuniamini ili niwe mwakilishi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia umuhimu wa Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania iliyopo Bububu kuboreshwa. Hospitali hii ni muhimu kwa kuwa ndio hospitali kubwa ya jeshi ndani ya Zanzibar, hivyo ninashauri Wizara ya Ulinzi iongezewe fedha kwa ajili ya kuongeza majengo na vifaatiba.
Pia ninashauri Wizara hii ijengewe majengo maalum ya kutoa huduma kwa viongozi wetu wa Kitaifa pale wanapoumwa. Hospitali nyingi za binafsi za Zanzibar na za Serikali hazina faragha za kutosha kwa matibabu ya viongozi, hivyo majengo hayo yakiwepo yatarahisisha huduma na kuwa kimbilio kwa viongozi na wananchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, Wizara ya Ulinzi haina jengo la Wizara ndani ya Zanzibar, Wizara hii ni ya kimuungano, hivyo ninashauri iwe bajeti hii ama bajeti ijayo Serikali ianze mchakato wa kuanzisha ofisi ya jengo la Wizara ndani ya Zanzibar. Ofisi hiyo itasaidia shughuli za Wizara ndani ya Zanzibar ikiwemo kutoa huduma kwa urahisi kwa askari wetu wa JWTZ wanapotaka huduma za kiwizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. SAADA MANSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na Mawaziri wote kwa ushirikiano wao leo wameweza kupunguza kodi ya asilimia sita kwenye mkopo ya elimu ya juu, maana wazazi tumepata nafuu kwa msaada huu tuliopewa kwa watoto wetu kutoka kwa huruma na mapenzi ya mama yetu Mama Samia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia sisi Wabunge wote tumefarajika sana kuona Madiwani, Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kwa kupewa posho kila mwezi kupitia kwenye account zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la posho kwa watendaji wenzetu limetupa faraja sana sisi Wabunge maana kusema kweli walikuwa na hali ngumu sana ya utendaji wao wa majukumu yao wakati wao ndio wapo na wananchi muda mwingi kuliko sisi Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuwakumbuka wastaafu kulipwa kwa wakati, kwani wastaafu wengine wanafariki wakati haki yake hajaipata, anakuja kulipwa mrithi yeye aliyetumikia ajira hajaigusa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kupunguza muda wa mikataba ya Jeshi la Polisi kutoka miaka 12 hadi miaka sita, hii tutafanya askari wetu waendelee kuilinda amani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niaishukuru Serikali kwa kuamua sasa tozo ya viza ya wageni wanaoingia Zanzibar ibaki Zanzibar na Tanzania Bara ibaki Bara hii imepunguza kero za Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru viongozi wetu wote mama yetu kipenzi Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi, Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba na Mawaziri wote kwa kazi nzuri ya kutuogoza na kulitumikia Taifa letu na wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishukuru Serikali kwa kurejesha VAT kwenye bidhaa zinazonunuliwa Tanzania Bara na kutumika Tanzania Zanzibar. Pia naipongeza Serikali kwa kuondoa kero kwa vijana wetu waendesha pikipiki (bodaboda) kwa kupunguza faini ya makosa ya barabarani kutoka shilingi 30,000 hadi shilingi 10,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. SAADA MONSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi leo kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yangu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya kwa kuwatumikia wananchi wake wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi kwa kazi nzuri naye anazozifanya kule Zanzibar. Pia naipongeza Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi hoja yangu kuhusu vijana wanaokwenda JKT. Pamoja na kuwafunza uzalendo na mambo mbalimbali, niiombe Serikali iongezewe fedha Wizara hii ili iweze kuwaajiri vijana hawa katika vitengo mbalimbali. Tukifanya hivyo, tutaweza kuwanusuru vijana hawa wasirudi mitaani bila ya kuwa na shughuli rasmi ya kufanya, kwa kuwa vijana hawa wameshafundishwa hadi kushika silaha.
Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya pili, Mheshimiwa Waziri unapokuja hapa kujibu hoja ya bajeti yako, uniambie Serikali imefikia wapi kuhusu ujenzi wa jengo la Wizara ya Ulinzi ndani ya Zanzibar. Pia kuhusu majengo ya Hospitali ya Bububu kwa ajili ya faragha ya viongozi wetu wa Kitaifa pale wanapoumwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa haya machache naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. SAADA MONSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kuipongeza Wizara ya Nishati chini ya ndugu yangu Mheshimiwa January Makamba kwa kazi kubwa anazozifanya kwa kuhakikisha Taifa letu linaendelea kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ni kuhusu Bwawa la Mwalimu Nyerere lililopo Rufiji, napongeza ujenzi kufikia asilimia zaidi ya 60. Bwawa hili ni muhimu sana kwa maendeleo na pia tunalitegemea kuboresha hali ya umeme hadi Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mkoa wangu wa Kaskazini Unguja kuna uwekezaji mkubwa wa hoteli kubwa na ndogo ndogo, ujenzi wa hoteli hizi kwa kiwango kikubwa utakwenda kusaidia wananchi kwa kupata ajira na fursa za biashara. Aidha bwawa likikamilika uzalishaji ukianza hoteli zitapata umeme wa uhakika na wananchi wa Zanzibar watafaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ihakikishe fedha zinapatikana kwa miradi yote kutoka Hazina kwa wakati ili ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere usikwame na uende kwa muda. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SAADA MANSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu yake ya kazi iendelee.
Mheshimiwa Spika, Bwawa la Mwalimu Nyerere kazi imeendelea kutoka 32.82% hadi 97.43%; tunampongeza sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Mradi wa Umeme wa REA hivi sasa tumefikia zaidi ya vijiji 11,850 sawa na 96.2% na sasa hivi vimebakia vijiji 468.2. Mheshimiwa Rais anaupiga mwingi sana.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanikiwa sana kudhibiti mgao wa umeme nchini, pia Serikali imefanikiwa kuendelea na ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta, naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri zinazofanywa.
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia hasa mitungi ya gesi.
Mheshimiwa Spika, nishati safi itasaidia wanawake kuokoa muda wa kutafuta kuni porini na kuokoa misitu na pili nishati safi itasaidia kulinda afya za akinamama na watoto hasa kwa ugonjwa wa kansa unaotokana na moshi jikoni.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali iwekeze zaidi kwenye miundombinu ya umeme ambayo imechakaa. Hivi sasa uchakavu wa miundombinu ndiyo inayopelekea umeme kukatika.
Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Wizara hii ya Nishati na watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa na nzuri wanazozifanya kwa kuhakikisha Taifa letu linaendelea kupata umeme.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu; elimu kwa wananchi iendelee tolewa kuhusu matumizi ya gesi majumbani na pia Kikosi cha Zimamoto washirikishwe kwenye kutoa elimu hiyo kwa wananchi wajue matumizi ya kwamba hayana athari yoyote kwamba gesi ya sasa hivi ipo salama na haina madhara yoyote.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. SAADA MANSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya kwa kuwatumikia wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameingozea uweledi katika kazi na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi, kwa mfano, kusimamia maandamano ya vyama vya siasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali kwa ujenzi wa vituo vya polisi nchini, Serikali imejenga vituo vya polisi maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano jengo la polisi la Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kituo cha Polisi Tumbatu na hata Mkoa wa Kusini Unguja pia kumejengwa jengo la polisi la mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali na Wizara ya Mambo ya Ndani, changamoto iliyopo ni vituo vingi nchini Bara na Zanzibar vilijengwa muda mrefu hivyo vinahitaji ukarabati mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vituo vingine vimejengwa tangu ukoloni kwa mfano, Kituo cha Polisi Mahonda na Mfenesini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa vituo vya polisi katika mkoa wa Kaskazini Unguja, Wilaya ya Kaskazini B kuna maeneo muhimu kama Kichakani, Mwembemajogoo, Kichwele, Kichungwani, Mbaleni na Kitope Ndani. Wananchi wa maeneo haya wanapata tabu kufuata huduma ya Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.