MHE. SAADA MONSOUR HUSSEIN Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawapatia Vitambulisho vya NIDA wananchi wote waliojiandikisha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Saada Monsour Hussein, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Serikali ni kuhakikisha watu wote waliosajiliwa na kupata namba za utambulisho wanazalishiwa na kugawiwa vitambulisho vya Taifa.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Agosti, 2021, Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imefanikiwa kuzalisha na kugawa kwa wananchi jumla ya vitambulisho 8,397,524. Aidha, Mamlaka inaendelea na mpango kazi wa uzalishaji ambapo wananchi wote wenye sifa watazalishiwa na kugawiwa vitambulisho vyao ifikapo tarehe 31 Desemba, 2021. Nakushukuru.
MHE. SAADA MONSOUR HUSSEIN aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kunusuru maisha ya vijana wa kike kwa kudhibiti wimbi la mauaji Visiwani Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saada Mansour Hussein, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kufuatilia kwa karibu matukio ya mauaji yanayotokea maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo Zanzibar. Matukio haya tumebaini yanasababishwa na migogoro ya ardhi, wivu wa kimapenzi na migogoro ya ndoa, imani za kishirikiana, wananchi kujichukulia sheria mikononi, ulevi, na matukio ya uhalifu.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba 2022 jumla ya matukio manne (4) ya mauaji ya wanawake yametokea Zanzibar. Matukio haya yamehusishwa na wivu wa mapenzi na migogoro katika ndoa.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi itaendelea kutoa elimu kwa jamii kufuata sheria za nchi na njia sahihi za kutatua migogoro ya aina hiyo. Tunawashauri wahusika kuzishirikisha familia zao, viongozi wa dini, viongozi wa jamii, viongozi wa siasa, wazee wa mila, watu maarufu na wenye ushawishi katika jamii pamoja na Ofisi za Serikali za Mitaa ili kupunguza athari za migogoro hiyo. Aidha, kwa migogoro inayoshindikana ifikishwe katika vyombo vya dola hususan Polisi na Mahakama ili kupata suluhisho la kisheria.