Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Alex Raphael Gashaza (5 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kwa mara ya kwanza ili niweze kutoa mchango wangu katika Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ameniwezesha kuwepo katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge la Kumi na Moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukue nafasi hii pia kwa sababu nimesimama kwa mara ya kwanza kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Ngara ambao wameniamini na kunipa nafasi hii; kwani hii ni mara ya nne nagombea; na wananchi wa Ngara wamekuwa na imani, Jimbo la Ngara limeshinda kwa kishindo; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepata kura nyingi, Mbunge wa CCM amepata kura nyingi tofauti ya kura 18,000 dhidi ya Mpinzani wa CHADEMA, lakini pia Madiwani wote wa Kata 22 ni wa CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuonyeshe ni jinsi gani ambavyo wananchi wa Jimbo la Ngara lakini na Watanzania kwa ujumla walivyo na imani na Chama cha Mapinduzi na Serikali yake. Nachukua nafasi hii pia kupongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais. Sikupata nafasi ya kuchangia, lakini ni hotuba ambayo ilijaa weledi ambayo ilileta matumaini mapya kwa Watanzania.
Nachukua nafasi hii pia Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa Mpango huu ambao mmeuleta mbele yetu ambao pia unaleta matumaini. Ndugu zangu mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa nje ya Bunge hili nilikuwa nikiangalia yaliyokuwa yakiendelea, wakati mwingine nilikuwa nachelea kujua kwamba ni nini, hususan upande mwingine. Ndungu zangu, ninajua kwamba maendeleo ni mchakato. Miaka 54 inayotajwa kwamba ni miaka 54 ya Uhuru ni muda mrefu, naamini ukilinganisha na yaliyofanyika ni mambo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanasahau kwamba tayari wanayo zaidi ya miaka 29 tangu mwaka 1992, lakini mpaka leo huwezi ukapima. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika kuchangia mpango huu. Vipo vipaumbele ambavyo vimeainishwa katika Mpango huu ikiwa ni pamoja na kipaumbele cha kilimo, kipaumbele katika Sekta ya Madini. Naomba niwarejeshe katika Mpango huu hususan katika ukurasa ule wa 34. Naanza kuchangia upande wa Utawala Bora. Nina uhakika kwamba huu nao ni msingi katika kutekeleza Mpango huu na msingi ambao unaweza ukatupeleka katika mafanikio katika Mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua zimekuwepo jitihada kubwa na ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais alijaribu kuangalia akaona kwamba upande huu ni lazima tuushughulikie, ndiyo maana ameanza kuboresha sekta hii upande wa TAKUKURU kama chombo ambacho kinaweza kikasimamia na kuhakikisha kwamba pia utawala bora unafanyika, Mahakama na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze dhahiri kwamba pale ambapo Serikali itaweza kwenda sawasawa na kusimamia Mipango hii kwa umakini kwa kuzingatia Utawala Bora nina uhakika kwamba tunaweza kufanikiwa. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais kwa kutambua kwamba ipo mianya ambayo inasababisha tusiweze kupata mapato vizuri, lakini kwa lengo la kutaka kuimarisha utawala bora kwa maana ya kuziba mianya ya rushwa, kwa makusudi na kwa dhamira ya dhati akasema kwamba lazima sasa aanzishe Mahakama ya Mafisadi ya kushughulikia mafisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mkakati mahususi ambao utakapoenda kutekelezwa tuna uhakika kwamba Tanzania mpya itaonekana na Mpango huu utaweza kutekelezwa kwa umakini. Kwa sababu kwa kuziba mianya ya rushwa maana yake ni kwamba pia makusanyo ya Serikali yataweza kuongezeka. Makusanyo yatakapoongezeka, maana yake ni kwamba mipango hii itaweza kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaaminishe Watanzania na ninyi mtakubaliana na mimi kwamba kazi ya kiongozi ni kuonyesha njia na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli tayari ameonyesha njia kwamba anayo dhamira ya dhati ya kuonyesha kwamba makusanyo yanapatikana, anayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba mipango hii inatekelezeka. Tunaongelea siku 100 za utendaji kazi wake, lakini matokeo tumeyaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naongeze Baraza la Mawaziri ambalo ameliunda, kwa sababu kwa kipindi hiki kifupi cha miezi miwili, mitatu tumeona matokeo ya kazi wanayoifanya Mawaziri hawa. Kwa hiyo, tuna kila sababu ya kuwapongeza kwa sababu hii inaonyesha mwelekeo tunakokwenda kwamba itaweza kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika suala zima la madini. Tunajua kwamba eneo hili ni eneo ambalo ni nyeti na ambalo tuna uhakika na kuamini kwamba likisimamiwa vizuri linaweza likaendelea kuboresha na kuinua uchumi wa Tanzania.
Katika jimbo langu la Ngara yako madini adimu, madini ya Nickel, madini ambayo yanaifanya Tanzania iingie kwenye ramani ya dunia kuwa na deposit kubwa ya Nickel duniani kama siyo ya kwanza itakuwa ni ya pili. Ndiyo maana naunga mkono ujenzi wa reli ya kati pamoja na reli inayotoka Dar es Salaam kuja Isaka, kwenda Mwanza, Tabora, Kigoma, lakini pia mchepuko wa kutoka Isaka kuja Ngara ili kusudi mradi huu uweze kutekelezeka na nickel hii iweze kusafirishwa kwa ajili ya kupelekwa sokoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu tunategemea kwamba ni mkubwa lakini ambao wananchi wa Ngara kwa muda mrefu wamekuwa wakiuangalia kama tumaini lao kwa ajili ya kusababisha ajira. Tangu mwaka 1973/1974 exploration ilianza. Tulitegemea miaka ya 2010/2012 kwamba mradi huu ungeanza lakini mpaka sasa hivi haujaanza. Kulikuwepo na excuse ya kwamba hakuna umeme. Nampongaza Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Profesa Muhongo, na timu yake akiwemo Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo wamejitahidi kuhakikisha kwamba sasa umeme unasambazwa katika Wilaya ya Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naongea na Meneja wa Kanda, TANESCO mchana huu akahiadi kwamba tayari Ngara inaunganishwa kwenye grid ya Taifa na bahati nzuri kwa Mpango ambao unaanza Januari mwaka huu, Ngara imepewa kipaumbele kwenye kuunganishwa kwenye grid ya Taifa. Bado pia tuna mradi mkubwa wa umeme katika maporomoko ya Rusumo, mradi ambao unashirikisha nchi tatu; Rwanda, Tanzania na Burundi. Kwa hiyo, naamini kwamba Ngara itaweza kupata umeme wa kutosha na ni eneo ambalo linaweza likawekezwa. Naomba mgodi huu wa Kabanga Nickel uangaliwe na uweze kuanza mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye suala la afya. Tuna hospitali moja tu ya Wilaya ambayo inahudumia zaidi ya watu takriban 400,000 lakini kipo Kituo cha Afya ambacho tangu mwaka 2006 Halmashauri yangu ya Wilaya ya Ngara iliweza kuomba kupandishwa kuwa hospitali na Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, mwaka 2008 alitangaza kiwa hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeandika barua mara kadhaa kwa ajili ya kuomba usajili wa kituo hiki kiweze kuwa hospitali; ni hospitali inayotegemewa kwa sababu ina vigezo vyote vya kuitwa Hospitali na barua ya mwisho ilikuwa ni ya mwaka 2013. Nimebahatika kukutana na Naibu Waziri wa Afya na amekubali kulishughulikia hili, naomba liweze kushughulikiwa haraka iwezekanavyo ili kuweza kunusuru afya za wana-Ngara ili Hospitali hii ya Nyamiaga iweze kutambulika kama hospitali na iweze kupata mgao ili iingizwe kwenye bajeti kwa ajili ya kuhudumia wananchi hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni pamoja na Kituo cha Murusagamba ambacho Mheshimiwa Rais alishatangaza rasmi kwamba sasa kianze kupanuliwa kwa ajili ya kuwa hospitali kulingana na jiografia ya Jimbo la Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze pia katika suala la maliasili. Tunajua kwamba Halmashauri zina vyanzo vyao vya mapato. Kwa mujibu wa Sheria ya Maliasili, Jimbo la Ngara lina hifadhi mbili; Hifadhi ya Burigi na Hifadhi ya Kimisi. Hifadhi ya Burigi imeingizwa kwenye gazette la Serikali tangu mwaka 1974; Kimisi imeingizwa kwenye gazette la Serikali mwaka 2005. Kwa mujibu wa sheria hiyo kuna tozo ya asilimia 25 ambayo inatakiwa ingie kwenye Halmashauri kama own source, lakini kwa miaka yote hiyo kwa hifadhi zote hizi mbili hakuna hata senti tano ambayo imeingia kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri husika kwamba tozo hii ya asilimia 25 ianze sasa kuingia kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, lakini pia hata arrears kwa miaka yote hiyo ambayo haikuweza kutolewa kama tozo kwa ajili ya kuimarisha Halmashauri ya Wilaya ya Ngara iweze kutolewa kwa ajili ya kuongeza pato la Wilaya ya Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nangana na waliotangulia, kwamba lazima retention hii iweze kukusanywa kwa ajili ya kuweka kwenye mfuko…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Gashaza, ahsante.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia afya na uzima kuwepo ndani ya jengo hili.
Pili, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi, kwa sababu tangu Mkutano wa Tatu umeanza nilikuwa sijapata nafasi ya kuchangia, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee, nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Nishati na Madini na Naibu wake na timu nzima kwa hotuba nzuri ambayo wameilata mbele yetu, hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mmoja anatambua umuhimu wa nishati hii ya umeme kwamba ni nyenzo muhimu katika maendeleo na mageuzi ya kiuchumi katika nchi yoyote ile. Kila Idara, kila sekta na kila Wizara inaguswa na Wizara hii, kwa maana hiyo ni cross-cutting Ministry. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na nishati ya umeme, katika Wilaya yangu ya Ngara Jimbo langu la Ngara, nina kila sababu ya kuipongeza Wizara hii na kumpongeza Mheshimiwa Profesa Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini na Naibu wake kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika Jimbo langu la Ngara. Amenitembelea Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo ametembelea Naibu Waziri, ametembelea Waziri Mkuu katika kuzindua Mradi wa Orion Holland ambao utazalisha megawatt 2.5 kitu ambacho nina amini kwamba kinafungua fursa kwa wananchi wa Jimbo la Ngara na kwa Taifa kwa ujumla kuleta maendeleo na hasa katika sekta ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima niendelee kukupongeza kwa jitihada zinazoendelea sasa kwamba kufikia mwezi wa nane mwaka huu Wilaya yetu ya Ngara itakuwa imeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, kwa hiyo, kuendelea kutupa fursa ya kuwa na umeme wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi, Wilaya ya Ngara ni Wilaya ambayo mradi mkubwa ambao ninaweza kusema ni mradi ambao upo kwenye zile miradi ya flagship project ya umeme wa maporomoko ya Rusumo ambapo umeme huo utazalisha takriban megawatt 80, kati ya hizo megawatt 27 zitakuwa upande wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo kwamba wananchi wa Jimbo la Ngara wanafurahi na wanakupongeza kwa jitihada hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kwamba sasa tutakuwa na umeme wa kutosha ndani ya Jimbo la Ngara, kwa kuzingatia kwamba kwa sehemu kubwa tuna vijiji takribani 49 ambavyo mpaka sasa hivi havijafikiwa umeme, lakini kwa uhakika kwamba kufikia mwezi wa nane mwaka huu tutakuwa na umeme wa kutosha, wanataraji kwamba REA III sasa iweze kugusa vijiji vyote na vitongoji vyote takribani 240 ambavyo vimebaki ili kusudi umeme huu uweze kuleta tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye upande wa madini. Mheshimiwa Waziri anatambua kwamba Wilaya ya Ngara ni Wilaya ambayo ina madini mengi ambayo yanaweza yakaleta mabadiliko makubwa katika uchumi wa Tanzania. Wilaya ya Ngara ina madini ya nickel na ndiyo maana hata katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ile reli ya kati wameelekeza kwenda Keza. Keza iko Ngara ambapo kuna madini ya nickel. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, madini haya ni madini ambayo kwa Tanzania yanaifanya Tanzania i-rank nafasi ya tatu duniani kwa kuwa na deposit kubwa ikitanguliwa na Russia pamoja na Canada. Kumekuwepo na vikwazo ambavyo vimepelekea mgodi huu wa nickel usianze, mgodi ambao umeanza utafiti tangu miaka 1973. Nina uhakika wengi wetu humu walikuwa hawajazaliwa, lakini mpaka leo mgodi huo haujaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu miaka 2002 kumekuwepo na ahadi kwamba mwaka kesho tutafungua, mwaka kesho tutafungua mgodi, lakini mpaka sasa hivi bado mgodi huo haujafunguliwa. Kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano umeeleza vikwazo vitatu ambavyo vilikuwa vinaonesha kwamba mgodi huu ili uweze kufunguliwa ni lazima vikwazo hivyo viwe vimeondolewa. Ni pamoja na kikwazo cha umeme, kikwazo cha miundombinu ya usafiri na kikwazo cha bei kwenye Soko la Dunia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vikwazo hivyo viwili naweza kusema kwamba vimeondoka kwa sababu umeme sasa ambao tunategemea kuwa nao katika Wilaya hii ya Ngara ni umeme wa kutosha kuendesha mgodi huo na wananchi vijiji vyote wakapata umeme kwa matumizi ya majumbani na hata kwa matumizi ya viwanda vidogo vidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mawasiliano kulingana na bajeti kwamba reli ya kati sasa kwa standard gauge ndani ya miaka mitatu, minne ijayo kwa maana kufikia mwaka 2019 yawezekana tayari reli hii ikawepo.
Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri kwamba madini haya muhimu na ambayo yanaweza yakaleta mabadiliko ya uchumi katika nchi yetu, inaonekana kama vile inasahaulika sahaulika kwamba madini hayo yapo na mradi huu upo. Kwa sababu hata kwenye kitabu hiki cha bajeti haikuonesha kwamba mradi huo unafikiriwa. Ndiyo maana hata wawekezaji katika mgodi huo (Barrick) leo ukiangalia hakuna shughuli zozote zinazoendelea pale mgodini, pamoja na kuomba retention ya miaka mitano kwa maana ya mwaka 2015 kwenda 2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgodi haujengwi kwa siku moja, haujengwi kwa miaka miwili au miaka mitatu; tunahitaji kuona kwamba kunakuwepo na msukumo na kampuni hii ambayo inahusika pale iweze kuweka nguvu tuone jitihada. Sasa hivi wame-abandon site, hakuna kinachoendelea. Tunahitaji kuona jitihada zinazofanywa na Wizara hii kwa maana ya Serikali kuhakikisha kwamba wanapeleka miundombinu inayotakiwa, iende sambamba na jitihada zao katika kufanya maandalizi. Tunajua kufanya fidia siyo chini ya miaka miwili, wananchi hawajafidiwa.
Kwa hiyo, naomba Wizara iweze kusukuma kampuni hiyo ianze maandalizi ya ujenzi wa mgodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia katika Wilaya ya Ngara kuna madini ya manganese. Ipo kampuni ambayo sasa inafanya utafiti na uchimbaji pale. Nilikuwa najaribu kuteta na Naibu Waziri wa Nishati na Madini kwamba mazingira yalivyo ya shughuli inavyofanyika, inahitaji wakajiridhishe. Tuna mashaka kwamba pengine hawakufuata taratibu na sheria za utafiti na uchimbaji. Barua ambayo mwekezaji huyu ameandikiwa na Wizara ya Nishati na Madini kupitia Kanda Maalum, ni kwamba ni lazima awasiliane na Halmashauri na afuate taratibu na sheria za Halmashauri. Hakuripoti Halmashauri na mpaka sasa hivi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara imebidi kumwandikia barua kusitisha ili tuweze kupata ufafanuzi. Ninaamini kwamba hilo wataweza kulifuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye gesi. Baada ya kugundua gesi nchini Tanzania, imeonekana kwamba sasa ni tumaini la Watanzania wengi kwamba gesi hii itaweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi na gesi hii maeneo mengi ndani ya nchi hii tunaitegemea ili iweze kusaidia kwa kuzalisha nishati ya umeme lakini pia hata kwa matumizi ya kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kuishauri Wizara hii ni kwamba tujaribu kuangalia ni namna gani ambavyo tunaweza ku-establish substations ambazo zitatumika kwa ajili ya kusambaza gesi hii katika maeneo mbalimbali ikiwezekana kutenga substations hizi kikanda ili kusudi wananchi wote waweze kunufaika na gesi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba yapo makampuni kadha wa kadha ambayo yako tayari kuja kuwekeza kwa maana ya kutumia gesi hii na kufanya uzalishaji wa umeme. Kuna kampuni kutoka Uturuki, kuna kampuni kutoka maeneo mbalimbali ambao wanatamani waingie Tanzania kwa ajili ya kutumia gesi hii. Tunapoweza kukaribisha makampuni hayo, nina uhakika kwamba yataweza kutusaidia katika kuzalisha umeme wa kutosha kutokana na gesi na kusambaza kwa wepesi zaidi na kuweza kuleta mabadiliko mazuri ya kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye madini ambayo ni unique, madini ya Tanzanite. Kwa muda mrefu tumekuwa tukipiga kelele kwamba inakuwaje Tanzanite ambayo ni madini yanayozalishwa Tanzania peke yetu tunakuja kujikuta kwenye Soko la Dunia Tanzania tuko nyuma; eti nchi kama Kenya na South Africa ndio ambao wanaonekana kuuza na kuteka soko la Tanzanite! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inatutia aibu. Hebu niombe Wizara husika iweze kujikita na kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukawa na umiliki wa Tanzanite kama fahari ya Tanzania na madini ambayo yanaweza yakainua uchumi wa Tanzania na kuleta manufaa kwa watanzania walio wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika hili, hata kama ni kutafuta wataalam wa kufanya utafiti ili kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukarejesha heshima ya madini haya, kama nembo ya Taifa hata kwa jina lenyewe kwamba ni Tanzanite kwa maana ya kwamba ni madini yanayopatikana Tanzania tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika kwamba Wizara hii imejipanga na ndiyo maana hata katika bajeti yake imeonesha jinsi ambavyo matumizi kuelekea kwenye bajeti ya maendeleo imepewa kipaumbele kikubwa, asilimia 94. Zaidi ni pale ambapo nimefarijika kwamba katika fungu hili la maendeleo takribani asilimia 68 ni bajeti ya ndani ni fedha za ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaonesha kwamba ni rahisi na tutaweza kufanikiwa kutekeleza miradi hii ambayo tumeipanga kwa sababu ya own source kwa maana ya kwamba ni pesa za ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimtie moyo Mheshimiwa Profesa Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini; unajua wakati mwingine unapoenda kufanya kitu kizuri wengine hawakubali, ndiyo maana mtu mmoja akasema kwamba don’t focus on barriers or obstacles, always focus on your destiny.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kwamba Wizara hii chini ya Profesa Muhongo, mmeamua kuleta mabadiliko makubwa ndani ya nchi hii kwa sababu viwanda vitapatikana kutokana na nishati ya umeme, huduma bora za afya zitapatikana kutokana na nishati ya umeme kwa maana ya kutumia mitambo, Ultra Sound na CT-Scan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ubora wa huduma ya afya kwa Mtanzania inatokana na nishati ya umeme. Just keep on, usibabaike, songa mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba Wizara hii ni Wizara Mtambuka, ni Wizara nyeti, ni Wizara inayolitangaza Taifa, ni Wizara inayotangaza fahari za Taifa, ni Wizara ambayo ina umuhimu wake. Najua wachangiaji waliotangulia wamechangia mambo mengi na nitasisitiza katika mambo kadha wa kadha. Nianze tu kwa kujikita kwenye bajeti yenyewe, nikimpongeza Waziri Mwenye dhamana kwa hotuba nzuri aliyoitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii kulingana na umuhimu wa Wizara hii naweza nikasema kwamba upo upungufu hususan katika bajeti ile ya maendeleo kulinganisha na changamoto ambazo zinakabili Wizara hii. Ningeomba na ningeshauri kwamba kiasi kilichotengwa kwa ajili ya maendeleo kiongezwe ili kuweza kukabiliana na changamoto ambazo Wizara hii inakabiliana nazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwanza kwenye upande wa utalii. Waliotangulia pia wamesema juu ya promotion katika sehemu hii ya utalii. Naweza nikasema kwamba promotion bado haijafanyika kwa kiasi cha kutosha, hasa promotion kwa utalii wa ndani. Ukijaribu kuangalia Watanzania walio wengi leo ambao angalau wana ufahamu, zaidi ya milioni 30 hawajui fahari, hawajui rasilimali za utalii ambazo tunazo sisi Watanzania. Kwa maana ya kwamba ni wengi ambao hawapati access kuingia kwenye vile vivutio vya utalii. kwa hiyo tunayo kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba tuna-promote utalii wa ndani ili kuweza kuongeza pato katika sekta hii ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia tunavyo vyanzo vingi ambavyo hatujavitumia vizuri ili kuweza kuongeza utalii. Vyanzo hivyo ni pamoja na fukwe ambazo tunazo katika bahari kuu, ukianzia Tanga, Dar es Salaam ukashuka mpaka Mtwara zipo fukwe nzuri ambazo tungezitumia vizuri zingeweza kuongeza utalii na kuongeza pato la Taifa. Kwa mfano, ukienda Maputo Msumbiji unaweza kuona jinsi ambavyo wamejaribu kutumia fukwe zao na zinaingiza pato kubwa la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia bado yapo maeneo ya asili ambayo hatujayatumia vizuri. Ukienda kwa mfano, Iringa kwenye zile palace za Ki-chief kwa Chief Mkwawa, leo inatumika kama kituo cha utalii. Kuna aliye-raise hoja ya mjusi mrefu duniani ambaye alitoka Tanzania na akapelekwa Ujerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niwakumbushe Watanzania pia kwamba katika harakati kama mnakumbuka wakati ule wa Vita vya Maji Maji hata Chief Mwenyewe Mkwawa mnakumbuka kwamba baada ya kuuawa kichwa chake kilichukuliwa kikapelekwa Ujerumani. Lakini tarehe 9 Julai, 1954, Kichwa chake kilirudishwa Tanzania na kikawekwa mahali maalum kama makumbusho kwenye palace ya Chief Mkwawa pale Iringa Kalenga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali kupitia Wizara hii, kichwa cha Chief Songea ambacho nacho pia kilipelekwa Ujerumani ni wakati sasa wa kupaza sauti na kukirudisha, ili kusudi kiwekwe kwenye museum na hatimaye kiweze kuwa kituo cha utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna miundombinu pia ambayo haitoshelezi, haikidhi hususani katika maeneo ya utalii kwenye Wizara hii. Kwenye kitabu cha bajeti wameeleza juu ya kuongeza vifaa kwa ajili ya (patrol) ya doria kupambana na majangili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kutokana na miundombinu kutokuwa rafiki wakati mwingine kufika kwenye maeneo ya utalii ni ngumu; niombe pia waweze kuongeza ndege kwa ajili ya shughuli yenyewe ya utalii, kwa sababu mahali pengine barabara hazipitiki, huwezi kwenda kwa magari. Kwa hiyo, wajaribu kuongeza pia ndege kwa ajili ya shughuli hizo za kitalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi Jimboni kwangu, kwa sababu muda siyo rafiki. Jimbo la Ngara ni Jimbo ambalo lina takribani game reserve mbili. Kuna Game Reserve ya Burigi yenye hekta 13500 na kuna Game Reserve ya Kimisi ambayo ina takribani hekta 35,000. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri kwamba katika hifadhi hizi Jimbo langu la Ngara na Halmashauri yangu ya Ngara hainufaiki na chochote. Burigi Game reserve iliingizwa kwenye gazeti la Serikali tangu mwaka 1959, lakini mpaka leo ile tozo ambayo inatakiwa kurudishwa Halmashauri ya asilimia 25 kutokana na shughuli za uwindaji zinazofanyika haijawahi kutumwa hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Game Reserve ya Kimisi vivyo hivyo imekuwa gazetted tangu mwaka 2005, mpaka leo haijawahi kutolewa hata senti tano. Mbaya zaidi Kimisi Game Reserve sasa imekuwa ni kama kichaka cha majangili, wanaonufaika katika Kimisi Game Reserve ni wageni kabisa tofauti na Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa hii Kimisi Game Reserve unaanzia Rusumo boda unashuka kwenda Karagwe jirani kwa ndugu yangu Innocent Bashungwa. Kuna Kijiji cha Kashasha kule ni mpakani na Rwanda, upande wa Rwanda ni wananchi wanaishi pale. Game reserve yao ya Kagera iko ndani na ndiyo game ambayo wanaitegemea sana kwa upande wa Rwanda kwa ajili ya kuingiza kipato kama utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa Tanzania unapovuka mto tu unaanza na pori na kule kuna wanyama, kule kuna ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo, kuna maziwa kama Ziwa Ngoma ambalo ziwa lile nafikiri halijawahi kufanyiwa utaratibu wa uvuvi au wa uwindaji mzuri. Kuna viboko wanaibiwa mle, tena wanaibiwa na watu kutoka Rwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kambi moja ya Wanyamapori iko Rusumo pale lakini nashindwa kuelewa wanafanya nini? Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri pamoja na changamoto iliyoko ya mifugo iliyoko mle ndani, lakini niseme kwamba changamoto ni usalama wa maeneo yale na mipaka yetu ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba kama ambavyo upande wa Rwanda wamefanya kutengeneza kama Buffer Zone ambayo wananchi wanakaa wanaendesha shughuli za kilimo, basi na upande huu mwingine kwa ajili ya kuimarisha usalama, tuweze kuangalia namna gani tunaweza kuitumia ardhi ile kwa ufasaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ngara ni Jimbo ambalo lina vivutio vingi vya kitalii. Tuna maporomoko ya Mto Rusumo, mto unaotenganisha Rwanda na Tanzania. Maporomoko yale ni maporomoko ambayo tukiyatumia vizuri ni kivutio kizuri sana cha kitalii. Bahati nzuri eneo lile ni eneo ambalo sasa lina miradi mikubwa. Kuna mradi wa umeme unaozalishwa pale, kuna daraja kubwa la Kimataifa ambalo limefunguliwa juzi na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, kuna maeneo ambayo tukiyatumia tunaweza tukainua pato hususani katika sekta hii ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna vilima vinaitwa vilima vitatu. Hivi vilima vitatu vinaunganisha nchi tatu ambazo ni washirika wa Afrika Mashariki, Tanzania, Rwanda na Burundi. Vilima vile ni kituo kizuri kinachoweza kuwa kituo cha kitalii kama Wizara hii inaweza ikawekeza katika eneo lile. Pia bado tuna pango ambalo lilikuwa linatumika kama root ya kupitishia watumwa wakati wa utumwa. Pango ambalo ni underground, unatembea kilomita tano uko ndani ya pango. Lile limegeuka kuwa ni pango kwa ajili ya maficho ya majambazi. Hili likiandaliwa vizuri, likatunzwa vizuri ni eneo ambalo linaweza likawa ni zuri sana kwa ajili ya kivutio cha utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo kadha wa kadha ambayo ningeweza kushauri. Kama nilivyotangulia kusema kwamba, Wizara hii ina changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na changamoto ya ujangili, naomba Serikali sasa ifanye mipango mikakati ya dhati kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inadhibiti hali hii ya ujangili, pia migogoro inayojitokeza ya wakulima na wafugaji. Pamoja na kwamba tumeshauri kuwa Wizara zote ambazo zinaingiliana ziweze kukaa pamoja na kuweka mipango ya pamoja, naomba ufanyike utafiti wa kuona ni namna gani ambavyo ardhi hizi, misitu hii, reserve hizi…
Mheshimiwa Mwenyekiti naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenijalia kuiona jioni hii ya leo. Pia, nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya kusimamia Kanuni na Sheria za Uendeshaji wa Bunge. Mungu akutie nguvu na akupe afya ili uendelee kukalia Kiti hicho mpaka tunapomaliza Bunge hili la Bajeti, tarehe Mosi, Mwezi wa Saba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha Mheshimiwa Mpango, Naibu Waziri wa Fedha na timu yao kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika kuandaa mpango huu wa Bajeti ya Mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii iliyofanyika ni kubwa na hii kazi imefanywa na binadamu. Yamkini kukawepo na upungufu sehemu, lakini kwa sehemu kubwa, mambo makubwa yamefanyika na ambayo kwa hakika yanatupa dira na mwelekeo wa kuwa na Tanzania ya tofauti, Tanzania ya viwanda, Tanzania ya uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na eneo la maji na umwagiliaji, sehemu ambapo wachangiaji wengi waliotangulia kama si Wabunge wote wanagusia eneo hilo kwa sababu ndilo eneo ambalo sasa linamgusa kila Mtanzania na ndilo eneo ambalo lina kero kubwa kwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wamejitahidi sana katika kuweka bajeti kwa ajili ya kutekeleza miradi hii kama ambavyo hata wakati wa uwasilishaji wa Waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji alisema kwamba, tunahitaji sasa kwa miaka mitano ijayo kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukamwondolea adha huyu mwana mama Mtanzania anayeishi kijijini kubeba ndoo ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili niseme bado ipo kazi kubwa ya kufanya na niungane mkono na waliotangulia kuchangia kwamba, katika kuondoa kero hii au tatizo hili, lazima tufanye maamuzi, sisemi kwamba, ni maamuzi magumu, lakini tuzingatie ushauri ule ambao kila mmoja anaposimama anajaribu kuutoa. Ili kuondoa kero hii, lazima tujibane na tutafute ni mahali gani ambapo tunaweza tukapata fedha kwa ajili ya kuongeza kwenye Mfuko huu wa Maji hususan maji vijijini na si kwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane mkono na waliotangulia kwamba tozo ya sh.i 50/= kwa kila lita kwenye mafuta, hebu tujaribu kufanya uamuzi huo tuipeleke kule ili tuongeze Mfuko huu na tuweze kutatua kero hii. Nasema hivi kwa sababu mifano iko hai, ukiangalia hata katika bajeti iliyotengwa nina uhakika kwa maka wa fedha 2016/2017, hata viporo ambavyo bado havijakamilika hatuwezi kuvikamilisha kwa bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kwenye Jimbo langu la Ngara, kwa miradi ile ya vijiji 10 tu, mkataba ulikuwa ni bilioni tano nukta, mpaka sasa hivi Wakandarasi wameshalipwa bilioni mbili nukta sita, maana yake bado bilioni mbili nukta tano. Kwenye Bajeti hii, Fungu la Maji lililoenda kule ni bilioni mbili tu ambayo haitoshelezi hata kuwalipa Wakandarasi kama watamaliza miradi ile. Kwa maana hiyo, mwaka 2016/2017 hakuna miradi mingine itakayofanyika pamoja na kwamba kuna Kata nyingi ambazo zina tatizo la maji ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Ngara Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana nasema kwamba, lazima tuzingatie tuone ni namna gani tunavyoweza kuongeza kwenye Mfuko huu wa Maji hususan maji vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kwa sababu kauli mbiu ni kuwa na Tanzania ya Viwanda, lazima kuwe na uzalishaji na uzalishaji huo unatoka mashambani na huko ndiko waliko Watanzania, wananchi walio wengi takribani asilimia 70, ambao wanafanya shughuli hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri hata Mheshimiwa Waziri mwenyewe kwenye hotuba yake ya Bajeti amekiri kwamba, hapo kuna changamoto kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna namna ambavyo tunaweza tukaleta mabadiliko ya viwanda kama hatutajikita na kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji ili tuweze kulisha viwanda vyetu na ili tuongeze uzalishaji, ni lazima tuingie kwenye kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo langu kuna mabonde makubwa takribani hekta 5,000 na zaidi. Wizara ilishafanya survey ikaonekana yapo mabonde matano makubwa ambayo yakifanyiwa kilimo cha umwagiliaji yanaweza kubadilisha uchumi wa wana Ngara, lakini kuongeza pia pato la Taifa. Kwa sababu kundi hili linapokuwa maskini, linapokuwa halizalishi, maana yake halilipi kodi, kwa maana hiyo inazidi kuvuta hata wale wachache wanaolipa kodi, GDP ya Taifa inashuka kwa sababu ya kundi hili ambalo halijaangaliwa kwa umakini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wa Bigombo - mradi wa umwagiliaji, ambao ulikuwa ukamilike tangu mwaka 2013. Mradi ule kama ungekuwa umekamilika ungeweza kuzalisha tani nyingi sana za mazao kutoka kwenye kilimo cha umwagiliaji, lakini kwenye Bajeti hii bado haikutengewa fedha pamoja na kwamba mradi ule umefikia kwenye asilimia 80. Badala yake zimetengwa bilioni karibu mbili kwa ajili ya mabonde mengine mawili kwa kufanya upembuzi yakinifu na detailed design kwa ajili ya kuja kuanzisha haya mabonde mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri Mheshimiwa Waziri kwamba katika eneo hili, kwa sababu tayari lipo bonde ambalo mradi ulishaanza na uko kwenye asilimia 80 basi, kiasi cha fedha ambacho kimetengwa kwa ajili ya kwenda kwenye upembuzi yakinifu kwa mabonde mengine kiweze kuhamishiwa hapo ili kumalizia huo mradi na wananchi wa Ngara waweze kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Sheria ile ya Kodi, imejaribu kueleza juu ya kuondoa msamaha wa kodi hususan kwa ile Pay As You Earn kwa wafanyakazi. Ukijaribu kuangalia dhamira ya Serikali ni njema kuhakikisha kwamba, inapunguza ile kodi kutoka kwenye digit mbili na kubakia kwenye digit moja. Ukiangalia kwenye Bajeti hii…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia taarifa za Kamati hizi mbili, Kamati ya UKIMWI na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze kwa kupongeza Kamati hizi kwa kazi nzuri walioifanya na niwapongeze waliotangulia kuchangia. Mengi wameyagusa, mimi nijielekeze tu kwanza kwenye suala la elimu.
Mheshimiwa Mwenekiti, kama wengine walivyotangulia kusema hakuna namna ambavyo Taifa lolote lile linaweza kuendelea kama bado halijaweza kuelimisha watu wake. Kwa kutambua kwamba kupitia elimu ndipo unapoweza kuwa na rasilimali watu iliyo bora na zaidi hasa katika kujenga msingi. Ukijaribu kuangalia rasilimali hii muhimu tunaanza kuipoteza kuanzia darasa la saba, tunakuja sekondari kwa maana kidato cha nne pale ambapo tunajikuta tumehamasisha, tumejenga shule nyingi za kata tukitegemea watoto wetu waweze kupate elimu hii na waweze kuendelea hadi vyuo vikuu lakini kwa matokeo kwanza ya mwaka huu ya kidato cha nne unaweza ukaona ni rasilimali kiasi gani ambayo itabaki nyuma huku vijijini ambayo ni nguvu kazi vijana kama hatukuweka mpango mahsusi kwa ajili ya kuona ni namna gani ambavyo rasilimali hii tunaweza tukaiboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wamejaribu kuweka mpango wa kuanzisha vyuo vya VETA. Niombe mpango huu usiwe katika karatasi tu, uwe ni mpango unaotekelezeka, vinginevyo kama tutaendelea kupoteza rasilimali hii muhimu, kila mwaka vijana wetu wanamaliza kidato cha nne, zaidi ya 60%, 70% wanabaki vijijini, hawana ujuzi wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoteza rasilimali hii muhimu na hasa ukizingatia tunajipanga sasa Taifa hili liweze kuwa linajenga uchumi kuelekea kwenye uchumi wa kati kupitia viwanda. Hakuna namna tunaweza kufaulu kama tusipoweza kuiandaa hii rasilimali muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na huduma zinazotolewa katika shule zetu, kuna kitu ambacho napenda Kamati wajaribu kuangalia. Sijui maeneo mengine lakini katika Jimbo langu la Ngara mara kadhaa kumekuwepo na tatizo la radi hususani katika maeneo ya shule. Mwaka jana tulipoteza wanafunzi watatu katika shule ya sekondari Kanazi kwa kupigwa na radi, lakini pia katika Kata ya Nyamagoma tulipoteza wananchi watatu kwenye familia moja ambao wako karibu na shule ya msingi na maeneo kadha wa kadha. Kwa hiyo, niombe…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja za Kamati zote mbili.