Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Alex Raphael Gashaza (8 total)

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona na kunipa nafasi. Napenda kumuuliza swali la nyongeza Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa umwagiliajii wa Bonde la Bigombo ambao ulianza 2012 na ulitakiwa kukamilika 2013, ulifadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika chini ya ASDP, mpaka sasa mradi huo haujakamilika. Mradi huu ilikuwa ni tegemeo kwa wananchi wa Jimbo la Ngara hususani wananchi wa Kata ya Rulenge, Keza na Nyakisasa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Ni lini sasa mradi huu utaweza kukamilika?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilisema kwamba miradi yote ya umwagiliaji inasimamiwa na Tume ya Umwagiliaji. Nikasema katika bajeti ya mwaka huu wa 2015/2016, tumepanga fedha kiasi cha shilingi bilioni 53 katika kuendeleza sekta hii ya umwagiliaji. Miradi hii ilikuwa imeanzishwa chini ya programu ya ASDP ambapo wafadhili ni African Development Bank na mingi ilikuwa haijakamilika. Kwa sababu tumeunda Tume, tutakwenda kufuatilia tuone tunaweza kukamilisha kwa namna gani mradi ambao tayari ulikuwa umeshaanza.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Naitwa Alex Raphael Gashaza, Mbunge wa Jimbo la Ngara.
Kwa kuwa barabara ya Murugarama – Rulenge – Nyakahura yenye kilometa 85 ni barabara ambayo iliahidiwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2008 kwamba itaweza kujengwa kwa kiwango cha lami na miaka miwili iliyopita wananchi wa Jimbo la Ngara walikuwa wakielezwa kwamba tayari upembuzi yakinifu wa barabara hii umeanza.
Naomba kumuuliza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ni lini mkandarasi atakuwepo site kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata taarifa kutoka kwa Waziri mwenyewe wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano juu ya upatikanaji wa fedha za kulipa madeni ya wakandarasi, kama jana mlimsikia alisema ni karibu shilingi bilioni 419 zimeshatolewa. Kwa hiyo, katika lile deni la shilingi trilioni 1.268 sasa tumeshuka tuko kwenye shilingi bilioni 800 na zaidi. Naomba kuchukua nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mara fedha zitakapopatikana kwa mradi huo, barabara yake itashughulikiwa kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, barabara ya Mrugarama – Rulenge kwenda mpaka Mzani iko kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kujengwa kwa kiwango cha lami, lakini kwa mwaka wa fedha 2016/2017 haiko kwenye bajeti, badala yake ni Kilometa tatu na nusu tu ambazo zimewekwa kwenye bajeti kwa ajili ya kiwango cha changarawe chini ya TANROAD; na barabara hii imekuwa mbaya sana kwa kipindi kilichopita cha mvua na mwaka mzima maana yake hakuna bajeti nyingine itakayotengeneza barabara hii:-
Je, Waziri haoni umuhimu wa kuongeza fungu ili kwa kipindi cha mwaka wa 2016/2017, barabara hii iweze kupitika kwa wepesi japo itakuwa imetengenezwa kwa kiwango cha changarawe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Gashaza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uwezo wa kuongeza bajeti sina kwa sababu nina uhakika huu mwaka ndiyo tumemaliza, mmetupa kazi, mmepitisha bajeti yatu na tunawahakikishia sisi tutaisimamia kwa nguvu zetu zote. Kitu ambacho ninamhakikishia, tutahakikisha hii barabara aliyoiongelea, inapitika mwaka mzima. Kama itatokea mahitaji makubwa ya fedha kutokana labda na kuharibika kwa kiwango ambacho hakitegemewi, namhakikishia kwamba tutatafuta fungu la dharura ili kuweza kurudisha mawasilino kama yatakatika.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba mawasiliano yatakuwepo katika kipindi chote cha mwaka wakati tukijiandaa na bajeti ya miaka inayokuja.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa mgogoro uliopo katika Pori la Kagera Nkanda unataka kufanana na matatizo yaliyopo katika Pori la Burigi na Kimisi hususan maeneo yaliyopo katika Jimbo la Ngara; kama ambavyo tangu mkutano wa pili wa Bunge niliweza kueleza na hata katika mchango wangu wa bajeti ya maliasili; kwamba tangu mwaka 1959 mrahaba ule wa asilimia 25 ambao unatakiwa kurudishwa kwenye Halmashauri kutokana na vitalu vya uwindaji haijawahi kupelekwa kwenye Jimbo la Ngara.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, Waziri wa Maliasili na Utalii anaweza kuwaeleza wananchi wa Jimbo la Ngara na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, ni lini pesa hizo zitapelekwa, ambazo tangu mwaka 1959 mpaka leo hazijapelekwa?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la mrabaha likilinganishwa na swali la msingi ambalo nimelijibu ni mahususi kidogo na bila shaka linahitaji takwimu na linahitaji taarifa ambayo ni mahususi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimuahidi Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hiki cha asubuhi, mchana awasiliane na mimi nitaweza kumpa jibu sahihi kwa swali lake ambalo ni mahususi.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, naitwa Alex Raphael Gashaza, ni Mbunge wa Jimbo la Ngara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa barabara ya Murugarama Lulenge mpaka Mzani kilomita 85 iliahidiwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne mwaka 2012, lakini barabara hiyo imeahidiwa tena na Rais wa Awamu ya Tano wakati wa Kampeni mwaka 2015 na ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, lakini katika bajeti hii ya 2016/2017 haipo kwenye bajeti, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge tumeongea naye kwa muda mrefu, tulikutana na Waziri wa Ujenzi na baadaye tukaomba twende tukakutane na Katibu Mkuu. Kwa kweli anafuatilia sana ujenzi wa hii barabara. Namshukuru sana na naomba aendelee na juhudi hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho tulikuwa tumemwambia na naomba kurudia ni kwamba ahadi zote za Mheshimiwa Rais na ahadi za Viongozi wengine wote zilizotolewa na zile ambazo zimewekwa katika Kitabu cha Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa mwaka 2015 hadi 2020, Serikali hii ya Awamu ya Tano itazitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichotekea, kwa nini mwaka huu fedha hazikutengwa, ni kwa sababu tu tulitoa kipaumbele kwa zile barabara ambazo zilishaanza kujengwa na Wakandarasi wako site na Serikali inapoteza fedha kuwalipa watu ambao hawafanyi kazi. Tulitaka barabara hizi kwanza zikamilike, halafu kuanzia mwaka ujao wa fedha tutaanza kuingia katika maeneo mapya ambayo viongozi wetu wakuu waliahidi.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo ni majibu ya Serikali. Lakini kwa kuzingatia kwamba Ngara ni miongoni mwa Wilaya za Mkoa wa Kagera, Wilaya inayopakana na nchi mbili, Rwanda na Burundi imekuwa ni waathirika wakubwa sana wa hali ya usalama katika eneo hilo. Sasa swali langu, je, ni lini sasa Serikali itaanzisha Kanda Maalum ya kipolisi kwa Wilaya hii ya Ngara ambayo kwa muda mrefu wamekuwa ni waathirika wa hali ya usalama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumekuwa tukiangalia maeneo ambayo yamekuwa na changamoto kubwa sana za kiusalama nchini mwetu na maamuzi ya kuongeza Wilaya katika maeneo hayo yanatokana na wingi wa matukio ya uhalifu. Ngara ni moja kati ya sehemu ambayo kuna matukio ya uhalifu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema, hasa kutokana na kupakana na nchi jirani. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge atuachie hili tunalifanyia kazi na baadaye pale ambapo hatua itakapofikiwa, tutamjulisha.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ambayo yamejielekeza kwenye sehemu ndogo tu ya swali langu la msingi; kwa sababu ameelezea juu ya mpango wa maji kwenye miji sita ya Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kwamba Wilaya yangu ya Ngara, takriban asilimia 50 ya maeneo ya vijijini kuna tatizo kubwa hili la maji; na bahati nzuri tarehe 30 mwezi Desemba mwaka jana, 2016, Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo alifika akaona mito hiyo na mlima huo ninaousema; na kwa kutumia vyanzo hivi maana yake ni kwamba tutaondoa kabisa kero ya maji katika vijiji vyote vya Wilaya ya Ngara na hizi nyingine ambazo nimezitaja; na huu ndiyo utakuwa ni mwarobaini:-
Sasa swali langu namba moja: Je, Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI wako tayari kutuma wataalam ili waweze kufika maeneo yale na kuweza kuweka mkakati wa kuandaa mradi mkubwa ambao unaweza ukaondoa kero hii ya maji kwenye Vijiji vya Wilaya ya Ngara, Karagwe, Kyerwa, Biharamulo na Chato kama ilivyoelezwa kwenye swali la msingi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; mwaka 2016 mwezi wa Pili Halmashauri yangu ya Wilaya ya Ngara ilipeleka barua kwenye Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa ajili ya kuomba mitambo miwili ya kusukuma maji kwenye eneo la K9 ambapo kuna taasisi za Serikali na wananchi kwa maana Kambi ya Jeshi, Shule mbili za Sekondari na wananchi wa Kijiji cha Kasharazi; na pampu ya pili kwenye eneo la Mamlaka ya Mji wa Ngara Mjini, ambayo pamoja mamlaka kushugulikia usambazaji wa maji mjini, bado kulingana na umuhimu wa taasisi zilizopo pembezoni kama Shule ya Sekondari Ishunga walikuwa wakipeleka maji kule, lakini baada ya mtambo kuharibika uliokuwa unasukuma maji, imekuwa ni tatizo.
Je, Wizara kwa sababu tayari ilishaji-commit tangu tarehe 25 mwezi wa Pili kwamba itapeleka pampu hizi mbili mwaka jana…
SPIKA: Mheshimiwa Gashaza, sasa si uulize swali!
Mheshimiwa Spika, swali langu je, ni lini sasa Wizara itapeleka fedha hizi ambazo ni takriban shilingi milioni 50 kwa ajili ya kununua pampu hizi za kusukuma maji katika maeneo haya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Gashaza amezungumzia matatizo ya maji ya Ngara na Wilaya zote Mkoa wa Kagera akihusisha pia na vijiji vya wilaya hizo; na ameomba kwamba tupeleke wataalam.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa yupo mtaalam mshauri ambaye anaangalia uwezekano wa kutumia mito hiyo miwili ambayo ni mikubwa ili kuweza kupeleka maji kwa wananchi. Miradi hii ambayo itatekelezwa chini ya Wizara ya Maji, itahakikisha inapeleka maji kwenye miji mikuu ya hizo Wilaya na vijiji vinavyopitiwa na bomba kuu kuelekea kwenye hizo Wilaya.
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Vijijini, katika bajeti ya mwaka huu tumehakikisha kwamba kila Wilaya imepewa bajeti ili waweze kushughulikia kupeleka maji kwenye Kata na Vijiji vinavyozunguka hizo Halmashauri. Mheshimiwa Waziri ametoka kuzungumza sasa hivi kwamba tayari baada ya kuona kwamba utekelezaji unasuasua tuliamua kuandika mwongozo kupeleka kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maji kupitia bajeti ambayo imetengwa na Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Spika, pia nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba tupo tayari na tumekuwa tunafanya hivyo. Kama Halmashauri zinahitaji wataalam, basi tunaweza tukashirikiana kutoa wataalam ili kwenda kuangalia hilo tatizo kwa pamoja tuone jinsi ya kulishughulikia.
Mheshimiwa Spika, nikiri katika swali lake la pili, ni kweli na mimi mwenyewe waliniambia na aliniletea nakala ya barua kuhusiana na maombi ya pampu kwa ajili ya kufufua zile pampu ambazo zimeharibika.
Mheshimiwa Spika, nizungumze suala moja. Waheshimiwa Wabunge, ikishakuwa Mamlaka, maana yake, inajitegemea kwenye running. Serikali inasaidia katika uwekezaji. Sasa inawezekana barua hizo baada ya kwenda kule kwenye Wizara zilikutana na tatizo hilo. Mara nyingi kwenye uwekezaji ndiyo tunasaidia mamlaka, lakini kwenye yale matumizi ya kila siku huwa tuaachia wao wenyewe wafanye kazi hiyo kwa kutumia mapato yao. Inategemea sasa, Mamlaka kama ipo chini ya Wilaya, kama kuna matatizo inabidi waripoti kwenye Wilaya. Mamlaka zilizopo chini ya Mikoa, kama kuna tatizo, wanaripoti kwenye Mikoa.
Mheshimiwa Spika, namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hili suala kwa sababu nalifahamu, nitajaribu kuwasiliana na Wizara kuona limefikia wapi.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna asiyetambua kwamba mabadiliko ya tabianchi ni janga la kitaifa na kimataifa. Kwa kutambua hilo binafsi kama Mbunge wa Jimbo la Ngara kwa kushirikiana na wataalam wangu katika Halmashauri yangu ya Ngara tumejipanga kuanzisha programu ya kuwa na vikosi kazi vya kupambana na moto kama kisababishi kikuu cha uharibifu wa mazingira. Programu hiyo ambayo tutaiita Community Fire Brigade kuanzia kwenye ngazi ya vijiji na kata.
Sasa swali, Serikali kupitia Wizara ya Muungano na Mazingira wako tayari ku-support programu hii kwa kutoa fedha kwa sababu lengo ni kuanzisha vitalu, kupanda miti katika maeneo ambayo yameathirika na moto lakini pia
kuanzisha miradi ambayo ni rafiki wa mazingira kwa maana ufugaji wa nyuki kwa malengo matatu, moja, kulinda mazingira; lakini pili, kuinua kipato cha wananchi na tatu, kutoa ajira.
MWENYEKITI: Naomba swali kwa ufupi Mheshimiwa.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Tayari nimeshauliza swali…Serikali ipo tayari…
MWENYEKITI: Basi naomba ukae upate majibu!
MHE. ALEX R. GASHAZA: Haya!
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS-MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuanzisha mkakati huo katika Jimbo lake na Wabunge wengine waige mfano wa Wabunge kama mtazamo alionao Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kabisa kwamba ofisi yangu haina tatizo lolote, tunaomba huo mkakati wake atuandikie ili tuweze kuona jinsi ya kuuingiza katika mipango ya Serikali tuweze ku-support mpango huo ili kuweze kuhakikisha kwamba mazingira yanalindwa kwa gharama zote kuhakikisha kwamba mazingira yako salama lakini tunapambana nahii hali ya mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa kweli inahitaji wadau mbalimbali wote wa Tanzania wote kwa ujumla kuunga mkono jitihada hizi.