Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Esther Edwin Maleko (2 total)

MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kumuuliza Waziri Mkuu swali.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, mikoa takribani 15 ya Tanzania ikiwemo Kilimanjaro, Kagera, Tanga, Ruvuma na mingineyo uchumi wake unategemea sana zao la kahawa, lakini zao hili halina ruzuku.

Ni nini msimamo wa Serikali kuhakikisha zao hili linapata ruzuku kama ilivyo kwa mazao mengine ya kimkakati? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Malleko, Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kahawa ni miongoni mwa mazao yanayotegemea kupandisha uchumi kwenye maeneo mbalimbali hasa kwenye mikoa ambayo Mheshimiwa ameitaja; na mimi juzi nilikuwa Mkoani Kagera kushughulikia zao hilo hilo, lakini pia jana tumekamilisha bajeti ya Wizara ya Kilimo na limechangiwa sana na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hapa juu ya ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upo mkakati wa Serikali kutoa ruzuku kwenye mazao mbalimbali ikiwemo kahawa na ruzuku inategemea sana kwenye zao hilo mahitaji yake makubwa kwa sababu kila zao lina mahitaji yake, lakini tunajua tuna suala la mbegu au miche wakati mwingine, lakini pia tuna madawa kwa maana ya pembejeo madawa, mbolea lakini pia namna bora ya kulisimamia zao hili hata maghala nayo pia tunaweza kuweka ruzuku kama alivyosema Waziri wa Kilimo jana. Zao la kahawa linalolimwa Kagera na kule Kilimanjaro kila eneo linategemea na mahitaji yao na hayo mahitaji ndio tunayoyafanyia ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano juzi nilipokuwa Kagera Vyama Vikuu vya Ushirika vilikuwa vinazungumzia wakulima wao kwamba kuna umuhimu wa kuongeza ruzuku kupata miche, lakini pia kuna tatizo la upungufu maghala na wanahitaji ruzuku kwa ajili ya maghala. Kwa hiyo unaweza ukaenda Mbinga nilishakwenda Mbinga wakati tunasimamia zao hili kule sehemu kubwa ilikuwa ni kupata ruzuku ya kupata mbolea kwa sababu Mbinga bila mbolea huwezi kukuza zao hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ruzuku inategemea na mahitaji ya zao na eneo hilo kwa hiyo Serikali imeweka utaratibu wa kutoa ruzuku na kwenye kahawa kama kule Kagera tumetoa ruzuku kwenye miche kupitia taasisi ya utafiti ya TACRI. Lakini pia tumeshakubaliana na Waziri na Waziri ameshaahidi kule Kagera kujenga maghala ambako pia tunaanza na mfumo wa masoko kupitia stakabadhi ghalani ambayo inahitaji kuwa na maghala. (Makofi)

Kwa hiyo ruzuku huko Mkoani Kilimanjaro na maeneo mengine tutakapokuja tutajua mahitaji ni nini na tutaona uwezo wa Serikali na mpango ambao tumeweka ruzuku basi tutatoa ruzuku kutegemea na eneo hilo na mahitaji ya zao hilo; huo ndio utaratibu ambao tunautumia kwenye mazao yetu karibu yote. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTHER E. MALLEKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu. Wanawake wengi wamekuwa wakijihusisha na biashara za mazao ya kilimo kandokando ya barabara kuu hapa nchini. Je, ni upi mkakati wa Serikali sasa kuhakikisha kwamba wanawake hawa wanatengenezewa mazingira bora ikiwa ni kujengewa mabanda ili waweze kufanya biashara zao katika hali nzuri zaidi? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Esther Malleko Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumeshuhudia akinamama sasa hivi wamekuwa na mwamko mzuri tu wa kufanya shughuli za ujasiriamali na kufanya biashara kando kando ya barabara zetu. Unapokwenda Dar es Salaam tunawakuta hapo Gairo, lakini pale mbele kidogo Dumila hata Mikese unakuta wamejipanga wanafanya biashara zao na barabara zote nchini utakuta akinamama wengi na vijana wengine wa kiume wakifanya biashara zao. Zipo baadhi ya halmashauri zimekuwa na maono na zimeendelea kusimamia wajasiriamali hawa kwa kuwajengea mazingira mazuri ya kufanya biashara zao kwa kuwajengea vibanda vya kibiashara kama pale Dumila palivyo, lakini na eneo la Mikese kwa Halmashauri ya Morogoro Vijijini. Mheshimiwa Taletale ameshiriki pia kuwajengea vibanda wafanyabiashara, wananchi wake eneo la Mikese, Mbunge wa Morogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utaratibu huu ni utaratibu ambao unawahamasisha hawa wafanyabiashara kufanya biashara zao vizuri, lakini pia wanakingwa na mvua na jua wanapofika kwenye msimu huo wakiwa wanaendelea kufanya biashara zao, lakini hata bidhaa inayouzwa inabaki kuwa salama na inafaa kwa kuendelea kuliwa pale ambapo inakaa kwenye kivuli na mahali sahihi pa kutunzwa.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua mipango ya Serikali, nitoe maelekezo kwa halmashauri zote nchini zihakikishe zinaendelea kutambua wajasariamali wanawake na vijana wanaouza biashara zao kandokando ya barabara kwa ajili ya wasafiri wanaosafiri ili watengenezewe mazingira mazuri ya kufanya biashara hiyo kwa kuwajengea vibanda vinavyowakinga na jua na mvua, lakini vinavyokinga pia bidhaa zile kwa jua na mvua ili bado mlaji apate bidhaa iliyo safi na salama ambayo bado ina mng’aro unaovutia kununuliwa. Hili litasaidia sana wajasiriamali hawa kupata kipato chao kwa uhakika na kufanya biashara kwenye maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tunalichukua hili na kama ambavyo nimeiagiza Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia halmashauri zote wasimamie jambo hili ili wajasiriamali hawa wafanye biashara kwenye maeneo haya na wapate manufaa ya biashara zao. Ahsante sana. (Makofi)